Jinsi ya Kutumikia Kulingana na Nia Za Mungu

Mnapaswa kuwa wazi kuhusu jinsi mtu anavyopaswa kumtumikia Mungu katika imani yake, kuhusu masharti yanayopaswa kutimizwa na ukweli unaopaswa kueleweka na wale wanaomtumikia Mungu, na kuhusu kupotoka kwenu katika kutumikia kwenu. Masuala haya yanahusisha jinsi mnavyomwamini Mungu, na jinsi mnavyotembea kwenye njia ambayo inaongozwa na Roho Mtakatifu na kumruhusu Mungu awapange namna ambavyo Anataka katika vitu vyote, hivyo kuwaruhusu mwelewe kila hatua ya kazi ya Mungu juu yenu. Mnapofikia hatua hiyo, mtaelewa imani katika Mungu ni nini hasa, mtaelewa namna ya kumwamini Mungu ipasavyo, na kile mnachopaswa kufanya ili kutenda kulingana na nia za Mungu. Hili litawafanya muwe watiifu kabisa kwa kazi ya Mungu; hamtakuwa na malalamiko na hamtahukumu, wala kuchambua, sembuse kuichunguza kazi ya Mungu, kwa kiwango kwamba nyote mtakuwa na uwezo wa kumtii Mungu hadi kufa, mkimruhusu Mungu awaongoze na kuwachinja kama kondoo, na kwamba kila mmoja wenu anaweza kuwa Petro wa miaka ya 1990, akimpenda Mungu kwa kiwango kikubwa kabisa hata msalabani, bila lalamiko hata kidogo. Ni hapo tu ndipo mtakapoweza kuishi kwa kudhihirisha mtindo wa Petro katika miaka ya 1990.

Kila mtu mwenye azimio anaweza kumtumikia Mungu—lakini ni wale tu wanaoonyesha kujali na kuzifahamyu nia za Mungu ndio wenye sifa na wanaostahili kumtumikia Mungu. Nimegundua jambo hili miongoni mwenu: Watu wengi wanaamini kwamba mradi tu wanaihubiri njia ya Mungu kwa bidii, wanaenda barabarani kwa ajili ya Mungu, wanajituma na kuacha vitu kwa ajili ya Mungu, na kadhalika, basi huku ni kumtumikia Mungu. Watu wengi wa kidini wanaamini kwamba kumtumikia Mungu kunamaanisha kukimbia huku na huko wakiwa na Biblia mikononi mwao, wakihubiri injili ya ufalme wa mbinguni na kuwaokoa watu kwa kuwafanya watubu na wakiri. Pia kuna maafisa wengi wa kidini wanaofikiri kwamba kumtumikia Mungu kunahusisha kuhubiri katika makanisa baada ya kufuatilia masomo ya juu na kupata mafunzo katika seminari, na kuwafundisha watu kupitia usomaji wa mistari ya Biblia. Zaidi ya hayo, kuna watu katika maeneo yenye umaskini ambao wanaamini kumtumikia Mungu kunamaanisha kuwaponya wagonjwa na kutoa mapepo miongoni mwa akina ndugu na dada zao, kuwaombea, na kuwahudumia. Miongoni mwenu, kuna wengi ambao wanaamini kwamba kumtumikia Mungu kunamaanisha kula na kunywa maneno ya Mungu na kumwomba Mungu kila siku, pamoja na kuyatembelea makanisa na kufanya kazi makanisani kila mahali. Kuna akina ndugu na dada wengine ambao wanaamini kwamba kumtumikia Mungu kunamaanisha kutooa au kutoanzisha familia na kujitolea nafsi yao yote kwa Mungu. Lakini ni watu wachache wanaojua kile kinachomaanishwa na kumtumikia Mungu. Ingawa kuna watu wengi mithili ya nyota angani wanaomtumikia Mungu, idadi ya wale wanaoweza kumtumikia moja kwa moja, na ambao wanaweza kutumikia kulingana na nia za Mungu, ni ndogo sana—ni ndogo sana isiyo na maana. Kwa nini Ninasema hivi? Ninasema hivi kwa sababu nyinyi hamwelewi kiini cha msemo "kumtumikia Mungu," na mnaelewa kidogo sana jinsi ya kutumikia kulingana na nia za Mungu. Kuna haja ya haraka kwa watu kuelewa hasa utumishi wa aina gani kwa Mungu ndio unaolingana na nia Zake.

Mkitaka kutumikia kulingana na nia za Mungu, lazima kwanza mwelewe ni watu wa aina gani ndio wanaompendeza Mungu, ni watu wa aina gani ndio wanaochukiwa na Mungu, ni watu wa aina gani ndio wanaofanywa kuwa watimilifu na Mungu, na ni watu wa aina gani ndio wanaostahili kumtumikia Mungu. Angalau, mnapaswa kuwa na maarifa haya. Jambo la muhimu zaidi, mnapaswa kujua kusudi la kazi ya Mungu, na kazi ambayo Mungu atafanya katika wakati wa sasa. Baada ya kuelewa hili, na kupitia maelekezo ya maneno ya Mungu, mnapaswa kwanza kuingia, na kwanza kukubali agizo la Mungu. Punde tu mnapokuwa na upitiaji wa vitendo wa maneno ya Mungu, na mnapoijua kazi ya Mungu kweli, mtakuwa na sifa za kumtumikia Mungu. Na Mungu atayafungua macho yenu ya kiroho mnapomtumikia na kuwaruhusu muwe na ufahamu mkubwa wa kazi Yake na muione kwa uwazi zaidi. Unapoingia katika uhalisi huu, upitiaji wako utakuwa wa kina na wa vitendo zaidi, na wale wote kati yenu ambao mmepitia uzoefu kama huo wataweza kutembea miongoni mwa makanisa na kutoa riziki kwa akina ndugu na dada zenu, ili kwamba kila mmoja wenu aweze kutumia nguvu za mwenzake ili kufidia mapungufu yake mwenyewe, na kupata maarifa mengi zaidi katika roho zenu. Ni baada tu ya kufikia athari hii ndipo mtaweza kutumikia kulingana na nia za Mungu na kufanywa kuwa watimilifu na Mungu katika mchakato wa utumishi wenu.

Wale wanaomtumikia Mungu wanapaswa kuwa wandani wa Mungu, wanapaswa kumpendeza Mungu, na wanapaswa kuwa na uwezo wa kuwa waaminifu kabisa kwa Mungu. Iwe ni faraghani au hadharani, mbele ya Mungu matendo yako yanapaswa kuweza kumpendeza Yeye, na wote wanapaswa kuweza kusimama imara mbele Zake; bila kujali jinsi watu wengine wanavyokutendea, wewe unapaswa kutembea kila wakati katika njia unayopaswa kuitembea ili uonyeshe unaujali mzigo wa Mungu. Ni watu kama hawa pekee ndio wandani wa Mungu. Kwamba wandani wa Mungu wanaweza kumtumikia Yeye moja kwa moja ni kwa sababu wamepewa agizo kubwa la Mungu na mzigo wa Mungu, wanaweza kuufanya moyo wa Mungu kuwa wao wenyewe, na kuuchukulia mzigo wa Mungu kama wao wenyewe, na hawazingatii faida au hasara ya matarajio yao ya baadaye—hata wakati matarajio yao ni kwamba hawatakuwa na chochote, na hawatapata chochote, watamwamini Mungu kila wakati kwa moyo unaompenda Mungu. Na kwa hivyo, mtu wa aina hii ni mwandani wa Mungu. Wandani wa Mungu pia ni wasiri Wake; ni wasiri wa Mungu pekee ndio wanaoweza kushiriki dharura Yake, na mawazo Yake, na ingawa miili yao ni yenye uchungu na dhaifu, wanaweza kustahimili uchungu na kuacha kile wanachopenda ili kumridhisha Mungu. Mungu huwapa watu kama hao mizigo zaidi, na kile ambacho Mungu anatamani kufanya kinabebwa katika ushuhuda wa watu kama hao. Hivyo, watu hawa wanampendeza Mungu, ni watu wanaomtumikia Mungu na wanaolingana na nia Zake, na ni watu kama hawa tu wanaoweza kutumia mamlaka kama wafalme pamoja na Mungu. Wakati ambapo kweli umekuwa mwandani wa Mungu ndio wakati hasa utakapotumia mamlaka kama mfalme pamoja na Mungu.

Yesu aliweza kukamilisha agizo la Mungu—kazi ya ukombozi wa binadamu wote—hasa kwa sababu aliweza kuonyesha kuzijali nia za Mungu, bila kujifanyia mipango au mipangilio yoyote. Alikuwa mwandani wa Mungu mnayemwelewa vizuri—Mungu Mwenyewe. (Kwa kweli, alikuwa Mungu Mwenyewe aliyeshuhudiwa na Mungu. Ninataja hili hapa ili kutumia ukweli wa Yesu kuelezea suala hilo.) Aliweza kuweka mpango wa usimamizi wa Mungu katikati kabisa, na kila mara aliomba kwa Baba wa mbinguni na kutafuta mapenzi ya Baba wa mbinguni. Aliomba na kusema, “Mungu Baba! Timiza kile ambacho ni mapenzi Yako, na Usitende kulingana na matamanio Yangu bali kulingana na mpango Wako. Mwanadamu huenda akawa dhaifu, lakini kwa nini Wewe umjali? Mwanadamu anawezaje kustahili kujali Kwako, mwanadamu ambaye ni kama chungu mkononi Mwako? Moyoni Mwangu, Ninatamani tu kutimiza mapenzi Yako, na Ningependa Wewe utimize kile ambacho Wewe ungefanya ndani Yangu kulingana na nia Zako mwenyewe.” Akiwa njiani kuelekea Yerusalemu, Yesu alikuwa katika uchungu, kana kwamba kisu kilikuwa kinazungushwa moyoni Mwake, hata hivyo Yeye hakuwa na nia hata kidogo ya kurudi nyuma; sikuzote kulikuwa na nguvu yenye uwezo ikimsukuma kuelekea mahali ambapo Angesulubiwa. Hatimaye, Alisulubiwa msalabani na akawa mfano wa mwili wenye dhambi, akikamilisha kazi ya ukombozi wa binadamu. Alivuka mipaka ya vikwazo vyote vya kifo na Kuzimu. Mbele Yake, kifo, jahanamu, na Kuzimu vyote vilipoteza nguvu zao, na vikashindwa na Yeye. Aliishi kwa miaka thelathini na mitatu, ambayo katika hiyo wakati Alifanya kila Alichoweza ili kuziridhisha nia za Mungu kulingana na kazi ya Mungu wakati huo, bila kufikiria faida au hasara Yake binafsi, na kila wakati kufanya mipango kwa ajili ya nia za Mungu Baba. Hivyo, baada ya kubatizwa, Mungu alisema, “Huyu ni Mwana Wangu mpendwa, ambaye Ninapendezwa naye.” Kwa sababu ya utumishi Wake mbele za Mungu ambayo ilikuwa kulingana na nia za Mungu, Mungu aliweka mzigo mzito wa kuwakomboa binadamu wote mabegani Mwake na kumfanya Yeye autimize, na Yeye alikuwa na sifa na haki ya kukamilisha kazi hii muhimu. Katika maisha Yake yote, Alivumilia mateso yasiyopimika kwa ajili ya Mungu, na Alishawishiwa na Shetani mara nyingi, lakini Yeye hakukata tamaa kamwe. Mungu alimpa kazi muhimu sana kwa sababu Alimwamini, na Alimpenda, na hivyo Mungu mwenyewe alisema, “Huyu ni Mwana Wangu mpendwa, ambaye Ninapendezwa na Yeye.” Wakati huo, ni Yesu pekee ndiye angeweza kukamilisha agizo hili, na hii ilikuwa sehemu moja ya hali halisi ya Mungu kukamilisja kazi Yake ya kuwakomboa binadamu wote katika Enzi ya Neema.

Iwapo, kama Yesu, ninyi mnaweza kuijali mizigo ya Mungu, na kuasi dhidi ya miili yenu, Mungu atawakabidhi jukumu Lake zito, ili ninyi mpate kutimiza masharti yanayohitajika ili kumtumikia Mungu. Ni katika hali kama hizo tu ndiyo mtathubutu kusema kwamba nyinyi ni watu mnaofuata mapenzi ya Mungu, watu wanaokamilisha agizo la Mungu, na watu wanaomtumikia Mungu kweli. Ikilinganishwa na mfano wa Yesu, je, unathubutu kusema kwamba wewe ni mwandani wa Mungu? Je, unathubutu kusema kwamba wewe ni mtu anayefuata mapenzi ya Mungu? Je, unathubutu kusema kwamba wewe ni mtu anayemtumikia Mungu kweli? Leo, wewe huelewi jinsi ya kumtumikia Mungu, je, unathubutu kusema kwamba wewe ni mwandani wa Mungu? Ukisema kwamba wewe ni mtu anayemtumikia Mungu, je, wewe hukufuru dhidi yake? Fikiria kuhusu hilo: Je, unamtumikia Mungu, au unajitumikia wewe mwenyewe? Wewe unamtumikia Shetani, lakini unasema kwa ukaidi kwamba unamtumikia Mungu—katika hili, je, humkufuru Mungu? Watu wengi—nyuma Yangu—wanafurahia faida za hadhi; wanajiingiza katika kufurahia chakula, wanapenda kulala, na wanajali sana mwili, wakiogopa kila wakati kwamba hakuna njia ya kutoka kwa mwili. Hawatimizi kazi yao ipasavyo kanisani, wanalidoea kanisa, au vinginevyo wanawakaripia akina ndugu na dada kwa maneno Yangu, wakiwazuia wengine kutoka nafasi za juu. Watu hawa huendelea kusema kwamba wao ni watu wanaofuata mapenzi ya Mungu na daima husema wao ni wandani wa Mungu—je, hili si jambo la kipuuzi? Ikiwa wewe una motisha sahihi, lakini huwezi kutumikia kulingana na nia za Mungu, basi wewe ni mpumbavu; lakini ikiwa motisha yako si sahihi, na bado unasema kwamba wewe ni mtu anayemtumikia Mungu, basi wewe ni mtu anayempinga Mungu, na unapaswa kuadhibiwa na Mungu! Sina huruma kwa watu kama hao! Katika nyumba ya Mungu, wao wanadoea, wanajiingiza katika kufurahia starehe za mwili kila wakati, na hawayajali kabisa maslahi ya Mungu. Wao daima hutafuta faida za kibinafsi, na hawazingatii nia za Mungu. Hawawezi kukubali uchunguzi wa Roho wa Mungu katika chochote wanachofanya. Wao daima wanawalaghai akina ndugu na dada zao kwa kutokuwa waaminifu na wadanganyifu, na wao ni wanafiki. Wao ni kama mbweha katika shamba la mizabibu, kila mara wanaiba zabibu na kuharibu shamba la mizabibu. Je, watu kama hao wanaweza kuwa wandani wa Mungu? Je, wewe unastahili kurithi baraka za Mungu? Hubebi mzigo wowote kwa ajili ya maisha yako na kanisa, je, wewe unastahili kupokea agizo la Mungu? Ni nani anayeweza kuthubutu kumwamini mtu kama wewe? Unapotumikia kwa namna hii, je, Mungu anaweza kukukabidhi kazi kubwa zaidi? Je, hili halitasababisha kucheleweshwa kwa kazi?

Ninasema hivi ili ninyi muweze kujua ni masharti gani ambayo lazima yatimizwe ili kutumikia kulingana na nia za Mungu. Msipoitoa mioyo yenu kwa Mungu, ikiwa hamtazingatia nia za Mungu kama Yesu alivyofanya, basi itakuwa vigumu kwenu kupata uaminifu wa Mungu, na nyinyi mtaishia kuhukumiwa na Mungu. Pengine leo, katika utumishi wako kwa Mungu, daima unaweka nia ya kumdanganya Mungu kila wakati na unashughulika na Yeye kwa njia ya kijuujuu tu. Kwa ufupi, bila kujali chochote, ukimdanganya Mungu, hukumu isiyo na huruma itakujia. Sasa hivi, ingawa mmeingia tu kwenye njia sahihi ya kumtumikia Mungu, kwanza mpeni Mungu mioyo yenu; huwezi kuwa na moyo uliogawanyika. Bila kujali kama uko mbele za Mungu, au mbele za watu wengine, moyo wako daima unapaswa kuelekezwa kwa Mungu, na unapaswa kuwa na azimio la kumpenda Mungu kama Yesu alivyofanya. Kwa namna hii, Mungu atakufanya kuwa mtimilifu, ili uwe mtu anayemtumikia Mungu na anayelingana na nia Zake. Ikiwa kweli ungependa kufanywa kuwa mtimilifu na Mungu, na ili utumishi wako ulingane na nia Zake, basi unapaswa kubadilisha mitazamo yako ya awali kuhusu imani katika Mungu, na ubadilishe desturi zako za zamani za kumtumikia Mungu, ili kiasi kikubwa cha nafsi yako kifanywe kuwa timilifu na Mungu. Kwa njia hii, Mungu hatakuacha, na, kama Petro, utakuwa katika mstari wa mbele wa wale wanaompenda Mungu. Ukisalia bila kutubu, basi utakutana na matokeo sawa na Yuda. Hili linapaswa kueleweka na wote wanaomwamini Mungu.

Iliyotangulia: Jinsi ya Kuingia Katika Hali ya Kawaida

Inayofuata: Jinsi ya Kujua Uhalisi

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp