Kufikia Wakati Utakapouona Mwili wa Kiroho wa Yesu, Mungu Atakuwa Amefanya Mbingu na Ardhi Kuwa Mpya
Je, unatamani kumwona Yesu? Je, unatamani kuishi na Yesu? Je, unatamani kusikia maneno yaliyonenwa na Yesu? Ikiwa ndivyo, basi utakaribishaje kurudi kwa Yesu? Je, umejitayarisha kikamilifu? Utakaribisha kurudi kwa Yesu kwa namna gani? Nadhani kwamba kila ndugu na dada anayemfuata Yesu angependa kumkaribisha vizuri. Lakini, je, mmefikiria hili: Je, utamjua Yesu kweli Atakaporudi? Je, mtafahamu kweli kila kitu Anachosema? Je, mtakubali kweli, bila masharti, kazi yote Anayofanya? Wale wote ambao wamesoma Biblia wanajua kuhusu kurudi kwa Yesu, na wanangoja kwa hamu kuja Kwake. Ninyi nyote mmekazia fikira kuwasili kwa wakati huo, na unyofu wenu unastahili sifa, imani yenu ni ya kutamanika kweli, lakini, je, mnatambua mmefanya kosa kubwa? Yesu atarudi kwa namna gani? Mnaamini kwamba Yesu atarudi juu ya wingu jeupe, lakini Mimi ninawauliza: wingu hili jeupe linarejelea nini? Kukiwa na wafuasi wengi sana wa Yesu wanaongoja kurudi Kwake, atashuka miongoni mwa watu gani? Ikiwa ninyi ndio wa kwanza ambao Yesu anashuka miongoni mwao, je, hili halitakuwa jambo lisilo la haki kabisa kwa watu wengine? Mimi ninajua kwamba mna unyofu na uaminifu mkubwa kwa Yesu, lakini, je, mmewahi kukutana na Yesu? Je, mnaijua tabia Yake? Je, mmewahi kuishi na Yeye? Mnamwelewa kiasi gani kweli? Wengine watasema kwamba maneno haya yanawaweka taabani. Watasema, "Nimesoma Biblia kuanzia mwanzo hadi mwisho mara nyingi sana. Ningekosaje kumwelewa Yesu? Achilia mbali tabia ya Yesu—ninajua hata rangi ya nguo ambazo Yeye alipenda kuvaa. Je, Wewe hunidharau Unaposema simwelewi?" Mimi ninapendekeza kwamba usibishane dhidi ya masuala haya; hebu tutulie na tushiriki kuhusu maswali yafuatayo: Kwanza, je, unajua uhalisi ni nini, na nadharia ni nini? Pili, je, unajua mawazo ni nini, na ukweli ni nini? Tatu, je, unajua kile kinachodhaniwa ni nini, na kile kilicho halisi ni nini?
Watu wengine hukana ukweli kwamba hawamwelewi Yesu. Na bado Mimi ninasema ninyi hammwelewi hata kidogo, na hamwelewi hata neno moja la Yesu. Hiyo ni kwa sababu kila mmoja wenu anamfuata kwa sababu ya masimulizi ya Biblia, kwa sababu ya kile ambacho mmesikia kutoka kwa watu wengine. Ninyi hamjawahi kumwona Yesu, sembuse kuishi na Yeye, na hata hamjatangamana naye kwa muda mfupi. Je, uelewa wenu kumhusu Yesu ni nadharia tu? Je, si unakosa uhalisi? Pengine watu wengine wameona picha ya Yesu, au wengine wametembelea nyumba ya Yesu wao binafsi. Pengine wengine wamegusa nguo za Yesu. Hata hivyo uelewa wako kumhusu Yeye bado ni wa kinadharia na si wa vitendo, hata kama umeonja binafsi chakula kilicholiwa na Yesu. Bila kujali haya yote, wewe hujawahi kumwona Yesu, na hujawahi kutangamana na Yeye katika umbo la mwili, na hivyo uelewa wako kumhusu Yesu daima utakuwa nadharia tupu isiyo na uhalisi. Pengine maneno Yangu hayakuvutii sana, lakini Mimi ninakuuliza hili: Ingawa unaweza kuwa umesoma kazi nyingi za mwandishi ambaye unavutiwa naye zaidi, je, unaweza kumwelewa kikamilifu bila kuwahi kushinda na yeye? Je, unajua haiba yake ikoje? Je, unajua anaishi maisha ya aina gani? Je, unajua chochote kuhusu hali yake ya kihisia? Huwezi hata kumwelewa kikamilifu mtu ambaye unavutiwa naye, kwa hivyo unawezaje kumwelewa Yesu Kristo? Kila kitu unachoelewa kumhusu Yesu kimejaa mawazo bunifu na fikira na hakina ukweli au uhalisi. Kinanuka na kimejaa mwili. Uelewa kama huo ungewezaje kukupa sifa za kukaribisha kurudi kwa Yesu? Yesu hatawapokea wale waliojaa njozi na mawazo ya mwili. Wale wasiomwelewa Yesu wanafaaje kuwa waumini Wake?
Je, mngependa kujua chanzo cha kwa nini Mafarisayo walimpinga Yesu? Je, mngependa kujua kiini cha Mafarisayo? Walikuwa wamejaa njozi kumhusu Masihi. Zaidi ya hayo, waliamini tu kwamba Masihi angekuja, lakini hawakufuatilia ukweli wa maisha. Na hivyo, hata leo bado wanamngoja Masihi, kwa maana hawana maarifa ya njia ya uzima, na hawajui njia ya ukweli ni nini. Mnasemaje, watu wapumbavu, wakaidi na wajinga kama hao wangewezaje kupata baraka ya Mungu? Je, wangeweza kumwona Masihi? Walimpinga Yesu kwa sababu hawakujua mwelekeo wa kazi ya Roho Mtakatifu, kwa sababu hawakujua njia ya ukweli iliyonenwa na Yesu, na, zaidi ya hayo, kwa sababu hawakumwelewa Masihi. Na kwa kuwa hawakuwa wamewahi kumwona Masihi na hawakuwa wamewahi kutangamana na Masihi, walifanya kosa la kung'ang'ania jina tu la Masihi huku wakipinga kiini cha Masihi kwa njia yoyote iwezekanavyo. Mafarisayo hawa katika kiini walikuwa wakaidi, wenye kiburi, na hawakutii ukweli. Kanuni ya imani yao kwa Mungu ilikuwa: Haijalishi mahubiri yako ni ya kina kiasi gani, haijalishi mamlaka yako ni ya juu kiasi gani, wewe si Kristo isipokuwa kama unaitwa Masihi. Je, imani hii si ya kipumbavu na ya kuchekesha? Ninawauliza ninyi zaidi: Je, si rahisi sana kwenu kufanya makosa ya Mafarisayo wa wakati huo, kwa kuwa hammwelewi Yesu hata kidogo? Je, unaweza kutambua njia ya ukweli? Je, unaweza kuhakikisha kweli kwamba hutampinga Kristo? Je, unaweza kufuata kazi ya Roho Mtakatifu? Ikiwa hujui kama utampinga Kristo, basi Ninasema kwamba tayari unaishi ukingoni mwa kifo. Wale ambao hawakumjua Masihi wote waliweza kutenda matendo ya kumpinga Yesu, ya kumkataa Yesu, ya kumkashifu. Watu ambao hawamwelewi Yesu wote wanaweza kumkataa na kumtukana. Zaidi ya hayo, wanaweza kuona kurudi kwa Yesu kama upotoshaji wa Shetani, na idadi kubwa ya watu hawa watamhukumu Yesu aliyerudi katika mwili. Je, haya yote hayawatii ninyi hofu? Kile mtakachokabili kitakuwa kufuru dhidi ya Roho Mtakatifu, kuchana maneno ya Roho Mtakatifu kwa makanisa, na kubeua kwa maneno yote yaliyoonyeshwa na Yesu. Mnaweza kupata nini kutoka kwa Yesu ikiwa mmechanganyikiwa kabisa? Mtawezaje kuelewa kazi ambayo Yesu anafanya Anaporudi katika mwili juu ya wingu jeupe, ikiwa mnakataa kwa ukaidi kuzinduka? Mimi ninawaambia ninyi hili: Watu ambao hawakubali ukweli, lakini wanangoja kwa upofu kuwasili kwa Yesu juu ya mawingu meupe, hakika ni wale wanaokufuru dhidi ya Roho Mtakatifu, na hakika wao ni kundi ambalo litaangamizwa. Ninyi mnatamani tu neema ya Yesu, na mnataka tu kufurahia eneo la mbinguni lenye furaha tele, lakini hamjawahi kutii maneno yaliyonenwa na Yesu, na hamjawahi kukubali ukweli ulioonyeshwa na Yesu anaporudi katika mwili. Mtashikilia nini kama mabadilishano ya ukweli wa kurudi kwa Yesu juu ya wingu jeupe? Je, ni unyofu ambao kwao mnatenda dhambi tena na tena, na kisha kutoa ungamo lenu, tena na tena? Mtatoa nini kama dhabihu kwa Yesu anayerudi juu ya wingu jeupe? Je, ni mtaji wa miaka mingi ya kazi ambao kwao mnajikweza? Mtatoa nini ili kumfanya Yesu aliyerudi awaamini ninyi? Je, ni hiyo asili yenu ya kiburi, ambayo haitii ukweli wowote?
Uaminifu wenu ni kwa neno tu, maarifa yenu ni yale ya kufikiri na mawazo, kumenyeka kwenu ni kwa ajili ya kupata baraka za mbinguni, na hivyo imani yenu lazima iweje? Hata leo, bado mnaziba masikio yenu kwa kila neno la ukweli. Ninyi hamjui kile Mungu alicho, hamjui kile Kristo alicho, hamjui jinsi ya kumcha Yehova, hamjui jinsi ya kuingia katika kazi ya Roho Mtakatifu, na hamjui jinsi ya kutofautisha kati ya kazi ya Mungu Mwenyewe na upotoshaji wa mwanadamu. Mnajua tu kuhukumu neno lolote la ukweli lililoonyeshwa na Mungu ambalo halilingani na mawazo yenu wenyewe. Uko wapi unyenyekevu wako? Uko wapi utii wako? Uko wapi uaminifu wako? Uko wapi mtazamo wako wa kutafuta ukweli? Uko wapi moyo wako umwogopao Mungu? Mimi ninawaambia ninyi, wale wanaomwamini Mungu kwa sababu ya ishara hakika ni kundi ambalo litaangamizwa. Wale wasioweza kukubali maneno ya Yesu ambaye amerudi katika mwili hakika ni uzao wa jahanamu, wazao wa malaika mkuu, kundi ambalo litaangamizwa milele. Watu wengi wanaweza kukosa kujali kile Ninachosema, lakini bado Ninataka kumwambia kila anayejiita mtakatifu anayemfuata Yesu kwamba, mnapomwona Yesu akishuka kutoka mbinguni juu ya wingu jeupe kwa macho yenu wenyewe, huu utakuwa wakati wa kuonekana hadharani kwa Jua la haki. Pengine huo utakuwa wakati wa msisimko mkubwa kwako. Hata hivyo, unapaswa kujua kwamba wakati unaposhuhudia Yesu akishuka kutoka mbinguni pia utakuwa wakati unaposhuka kwenda jahanamu ili kuadhibiwa, wakati ambapo mwisho wa mpango wa usimamizi wa Mungu umetangazwa, na wakati Mungu anapowatuza wema na kuwaadhibu waovu. Kwa maana hukumu ya Mungu itakuwa imeisha kabla ya mwanadamu kuona ishara, wakati ambapo kuna maonyesho ya ukweli tu. Wale wanaokubali ukweli na hawatafuti ishara, na hivyo wametakaswa, watakuwa wameletwa mbele ya kiti cha enzi cha Mungu na kuingia katika kumbatio la Muumba. Ni wale tu wanaoshikilia imani kwamba "Yesu asiyepanda juu ya wingu jeupe ni kristo wa uongo" ndio watakaopewa adhabu ya milele, kwa maana wanaamini tu katika Yesu anayefanya ishara, lakini hawamkiri Yesu anayeonyesha hukumu kali na kutoa uzima na njia ya kweli. Na hivyo inaweza tu kuwa kwamba Yesu anawashughulikia Anaporudi hadharani juu ya wingu jeupe. Wao ni wakaidi mno, wanajiamini mno, wenye kiburi mno. Watu duni kama hao wangewezaje kutuzwa na Yesu? Kurudi kwa Yesu ni wokovu mkuu kwa wale wanaoweza kukubali ukweli, lakini kwa wale wasioweza kukubali ukweli ni ishara ya hukumu. Ninyi mnapaswa kuchagua njia yenu wenyewe, na hampaswi kukufuru dhidi ya Roho Mtakatifu na kukataa ukweli. Hampaswi kuwa watu wajinga na wenye kiburi, bali watu wanaotii mwongozo wa Roho Mtakatifu na kuonea kiu na kutafuta ukweli; kwa namna hii tu ndipo mtakapofaidika. Mimi ninawashauri ninyi mtembee katika njia ya imani kwa Mungu kwa uangalifu. Msifanye hitimisho kiholela; zaidi ya hayo, msiwe wa kijuujuu na wazembe katika imani yenu kwa Mungu. Ninyi mnapaswa kujua kwamba, angalau, wale wanaomwamini Mungu wanapaswa kuwa na mioyo ya unyenyekevu na imwogopayo Mungu. Wale ambao wamesikia ukweli na bado wanautazama kwa dharau ni wapumbavu na wajinga. Wale ambao wamesikia ukweli na bado wanafanya hitimisho kiholela au kuuhukumu ni watu wenye kiburi. Hakuna anayemwamini Yesu aliye na sifa za kuwalaani au kuwahukumu wengine. Ninyi nyote mnapaswa kuwa watu walio na busara na wanaokubali ukweli. Pengine, baada ya kusikia njia ya ukweli na kusoma neno la uzima, unaamini kwamba ni neno moja tu kati ya 10,000 ya maneno haya ndilo linalolingana na uelewa wako na Biblia, na kisha unapaswa kuendelea kutafuta katika hilo neno moja kati ya 10,000 ya maneno haya. Mimi pia ninakushauri uwe mnyenyekevu, usiwe mwenye kujiamini kupita kiasi, na usiwe mwenye kujikweza mno. Kwa chembe ya moyo umwogopao Mungu ulio nao, utapata nuru kuu zaidi. Ukichunguza kwa uangalifu na kutafakari maneno haya tena na tena, utaelewa kama ni ukweli au la, na kama ni uzima au la. Pengine, baada ya kusoma sentensi chache tu, watu wengine watahukumu maneno haya kwa upofu, wakisema, "Haya si chochote ila nuru fulani ya Roho Mtakatifu," au, "Huyu ni kristo wa uongo aliyekuja kuwapotosha watu." Wale wanaosema mambo kama hayo ni wajinga mno! Unaelewa machache mno kuhusu kazi na hekima ya Mungu, na Mimi ninakushauri uanze tena kutoka mwanzo! Ninyi hampaswi kuhukumu kwa upofu maneno yaliyoonyeshwa na Mungu kwa sababu makristo wa uongo watatokea katika siku za mwisho, na hampaswi kuwa watu mnaokufuru dhidi ya Roho Mtakatifu kwa sababu mnaogopa kupotoshwa. Je, hilo halitakuwa jambo la kusikitisha sana? Ikiwa, baada ya uchunguzi wa mara kwa mara, bado unaamini kwamba maneno haya si ukweli, si njia, na si maonyesho ya Mungu, basi hatimaye utaadhibiwa, na utakuwa bila baraka. Ikiwa huwezi kukubali ukweli kama huo ulionenwa waziwazi na kwa uwazi sana, basi, je, hufai kwa wokovu wa Mungu? Je, wewe si mtu anayekosa baraka ya kurudi mbele ya kiti cha enzi cha Mungu? Fikiria hilo! Usiwe mwenye haraka na msukumo, na usichukulie imani kwa Mungu kama mchezo. Fikiri kwa ajili ya hatima yako, kwa ajili ya matarajio yako mema, kwa ajili ya maisha yako, na usijidanganye. Je, unaweza kuyakubali maneno haya?