Mungu na Mwanadamu Wataingia Rahani Pamoja
Mwanzoni, Mungu alikuwa anapumzika. Hakukuwa na binadamu ama kitu chochote kingine duniani wakati huo, na Mungu hakuwa amefanya kazi yoyote ile. Mungu alianza tu kazi Yake ya usimamizi baada ya binadamu kuwepo na baada ya binadamu kupotoshwa. Kutoka hapa kuendelea, Mungu hakupumzika tena lakini badala yake Alianza kufanya kazi miongoni mwa binadamu. Ilikuwa kwa sababu ya upotovu wa binadamu ndipo Mungu alichukuliwa kutoka kwa pumziko Lake, na ilikuwa pia kwa sababu ya uasi wa malaika mkuu ndipo Mungu alichukuliwa kutoka kwa pumziko Lake. Iwapo Mungu hatamshinda Shetani na kuokoa binadamu, ambao wamepotoshwa, Mungu hatawahi tena kuweza kuingia rahani. Mungu anakosa pumziko akosavyo mwanadamu. Wakati Mungu ataingia rahani tena, mwanadamu pia ataingia rahani. Maisha ya pumziko ni yale bila vita, bila uchafu, bila udhalimu unaoendelea. Hii ni kusema kwamba hayana unyanyasaji wa Shetani (hapa “Shetani” inamaanisha nguvu za uhasama), upotovu wa Shetani, na pia uvamizi wa nguvu yoyote inayompinga Mungu. Kila kitu kinafuata aina yake na kuabudu Bwana wa uumbaji. Mbingu na dunia ni shwari kabisa. Haya ni maisha matulivu ya binadamu. Mungu aingiapo rahani, hakuna udhalimu wowote utakaoendelea duniani, na hakutakuwa na uvamizi wowote wa nguvu za uhasama. Binadamu pia wataingia ulimwengu mpya; hawatakuwa tena binadamu waliopotoshwa na Shetani, lakini badala yake binadamu ambao wameokolewa baada ya kupotoshwa na Shetani. Siku ya pumziko ya binadamu pia ni siku ya pumziko ya Mungu. Mungu alipoteza pumziko Lake kwa sababu wanadamu hawakuweza kuingia rahani; haikuwa kwamba Hakuweza awali kupumzika. Kuingia rahani hakumaanishi kwamba mambo yote yatakoma kusonga, ama kwamba mambo yote yatakoma kuendelea, wala hakumaanishi kwamba Mungu atakoma kufanya kazi ama mwanadamu atakoma kuishi. Ishara ya kuingia rahani ni kama hii: Shetani ameangamizwa; wale watu waovu wanaomuunga mkono Shetani kwa kufanya maovu wameadhibiwa na kuondolewa; nguvu zote za uhasama kwa Mungu zimekoma kuwepo. Mungu kuingia rahani kunamaanisha kwamba Hatafanya tena kazi Yake ya wokovu wa binadamu. Binadamu kuingia rahani kunamaanisha kwamba binadamu wote wataishi ndani ya mwangaza wa Mungu na chini ya baraka Zake; hakutakuwa na upotovu wowote wa Shetani, wala maovu yoyote kutokea. Binadamu wataishi kama kawaida duniani, na wataishi chini ya ulinzi wa Mungu. Mungu na mwanadamu waingiapo rahani pamoja, kutamaanisha kwamba binadamu wameokolewa na kwamba Shetani ameangamizwa, kwamba kazi ya Mungu ndani ya mwanadamu imemalizika kabisa. Mungu hataendelea tena kufanya kazi ndani ya mwanadamu, na mwanadamu hataendelea tena kumilikiwa na Shetani. Kwa hivyo, Mungu hatakuwa shughulini tena, na mwanadamu hatakimbiakimbia tena; Mungu na mwanadamu wataingia rahani wakati huo huo. Mungu atarudia nafasi yake ya awali, na kila mtu atarudia nafasi yake husika. Hizi ndizo hatima ambazo Mungu na mwanadamu wataishi ndani kwa utaratibu huu baada ya mwisho wa usimamizi wote wa Mungu. Mungu ana hatima ya Mungu na mwanadamu ana hatima ya mwanadamu. Apumzikapo, Mungu ataendelea kuwaongoza binadamu wote kwa maisha yao duniani. Akiwa kwa mwangaza wa Mungu, mwanadamu atamwabudu Mungu wa kweli aliye mbinguni. Mungu hataishi tena miongoni mwa binadamu, na mwanadamu pia hataweza kuishi na Mungu katika hitimisho la Mungu. Mungu na mwanadamu hawawezi kuishi ndani ya ulimwengu sawa; badala yake, wote wawili wana njia zao binafsi za kuishi. Mungu ndiye anayeongoza binadamu wote, wakati binadamu wote ni matokeo ya kazi ya Mungu ya usimamizi. Ni binadamu wanaoongozwa; kuhusu kiini, binadamu si sawa na Mungu. Kuingia rahani kunamaanisha kurudi pahali pa awali pa mtu. Kwa hivyo, Mungu aingiapo rahani, kunamaanisha kwamba Mungu amerudi pahali Pake pa awali. Mungu hataishi tena duniani ama kushiriki kwa furaha na mateso ya binadamu wakati yupo miongoni mwa binadamu. Binadamu wanapoingia rahani, kunamaanisha kwamba mwanadamu amekuwa kiumbe halisi; binadamu watamwabudu Mungu wakiwa duniani na kuwa na maisha ya kawaida ya wanadamu. Watu hawatakuwa tena wasiomtii Mungu ama kumpinga Mungu; watarudia maisha asili ya Adamu na Hawa. Haya ndiyo maisha na hatima binafsi ya Mungu na binadamu baada ya kuingia rahani. Kushindwa kwa Shetani ni mwelekeo usioepukika katika vita kati ya Mungu na Shetani. Kwa njia hii, kuingia kwa Mungu rahani baada ya kukamilika kwa kazi Yake ya usimamizi na wokovu kamili wa mwanadamu na kuingia rahani pia kunakuwa mielekeo isiyoepukika. Pahali pa pumziko pa mwanadamu ni duniani, na pahali pa Mungu pa pumziko ni mbinguni. Wakati binadamu wanamwabudu Mungu katika pumziko, wataishi duniani, na wakati Mungu anaongoza sehemu iliyobaki ya binadamu katika pumziko, Atawaongoza kutoka mbinguni, sio kutoka duniani. Mungu bado atakuwa Roho, wakati mwanadamu bado atakuwa mwili. Mungu na mwanadamu wote wawili wana njia zao tofauti za kupumzika. Mungu anapopumzika, Atakuja na kujitokeza miongoni mwa mwanadamu, mwanadamu anapopumzika, ataongozwa na Mungu kutembea mbinguni na pia kufurahia maisha mbinguni. Baada ya Mungu na mwanadamu kuingia rahani, Shetani hatakuweko tena, na kama Shetani, wale watu waovu pia hawatakuweko tena. Kabla ya Mungu na mwanadamu kuingia rahani, wale watu waovu waliomtesa Mungu wakati mmoja duniani na adui waliokuwa hawamtii duniani watakuwa tayari wameangamizwa; watakuwa wameangamizwa na majanga makubwa ya siku za mwisho. Baada ya hao watu waovu kuangamizwa kabisa, dunia haitajua tena unyanyasaji wa Shetani. Binadamu watapata wokovu kamili, na hapo tu ndipo kazi ya Mungu itaisha kabisa. Haya ndiyo masharti ya Mungu na mwanadamu kuingia rahani.
Kukaribia kwa mwisho wa kila kitu kunaonyesha mwisho wa kazi ya Mungu na kunaonyesha mwisho wa maendeleo ya binadamu. Hii inamaanisha kwamba binadamu kama walivyopotoshwa na Shetani wamefika mwisho wao wa maendeleo, na kwamba vizazi vya Adamu na Hawa vitakuwa vimekamilisha uenezi wake. Na pia inamaanisha ya kwamba itawezekana kwa binadamu kama hawa, baada ya kupotoshwa na Shetani, kuendelea kustawi. Adamu na Hawa wa mwanzoni hawakuwa wamepotoshwa, lakini Adamu na Hawa waliofukuzwa kutoka Bustani ya Edeni walivurugwa na Shetani. Wakati Mungu na mwanadamu wanaingia rahani pamoja, Adamu na Hawa—waliofukuzwa kutoka Bustani ya Edeni—na vizazi vyao hatimaye watafika mwisho; binadamu wa baadaye bado watakuwa na vizazi vya Adamu na Hawa, lakini hawatakuwa watu wanaomilikiwa na Shetani. Badala yake, watakuwa watu waliookolewa na kutakaswa. Hawa watakuwa binadamu ambao wamehukumiwa na kuadibiwa, na walio watakatifu. Hawa watu hawatakuwa sawa na jamii ya binadamu kama ilivyokuwa awali; mtu anaweza kusema kwamba hao ni watu wa aina tofauti kabisa na Adamu na Hawa wa awali. Hawa watu watakuwa wamechaguliwa kutoka miongoni mwa wote waliopotoshwa na Shetani, na watakuwa ndio watu ambao hatimaye wamesimama imara wakati wa hukumu na kuadibu kwa Mungu, watakuwa kundi la mwisho la watu miongoni mwa wanadamu potovu. Kundi hili la watu ndilo tu litaweza kuingia katika raha ya mwisho pamoja na Mungu. Wanaoweza kusimama imara wakati wa kazi ya Mungu ya hukumu na kuadibu siku za mwisho—yaani, wakati wa kazi ya mwisho ya utakaso—watakuwa wale watakaoingia katika raha ya mwisho na Mungu; kwa hivyo, wanaoingia rahani wote watakuwa wametoka katika ushawishi wa shetani na kupokewa na Mungu baada tu ya kupitia kazi Yake ya mwisho ya utakaso. Hawa watu ambao hatimaye wamepokewa na Mungu wataingia katika raha ya mwisho. Kiini cha kazi ya Mungu ya kuadibu na hukumu ni kutakasa binadamu, na ni ya siku ya raha ya mwisho. Vinginevyo, binadamu wote hawataweza kufuata aina yao ama kuingia katika raha. Hii kazi ni njia ya pekee ya binadamu kuingia rahani. Kazi ya Mungu ya utakaso pekee ndiyo itatakasa udhalimu wa binadamu, na kazi Yake ya kuadibu na hukumu pekee ndiyo itadhihirisha hayo mambo yasiyotii miongoni mwa binadamu, hivyo kutenga wanaoweza kuokolewa kutoka wale wasioweza, na wale watakaobaki kutoka wale ambao hawatabaki. Kazi Yake itakapoisha, wale watu watakaoruhusiwa kubaki wote watatakaswa na kuingia katika hali ya juu zaidi ya ubinadamu ambapo watafurahia maisha ya pili ya binadamu ya ajabu zaidi duniani; kwa maneno mengine, wataingia katika siku ya binadamu ya raha na kuishi pamoja na Mungu. Baada ya wasioweza kubaki kupitia kuadibu na hukumu, umbo zao halisi zitafichuliwa kabisa; baada ya haya wote wataangamizwa na, kama Shetani, hawatakubaliwa tena kuishi duniani. Binadamu wa baadaye hawatakuwa tena na aina yoyote ya watu hawa; watu hawa hawafai kuingia eneo la raha ya mwisho, wala hawafai kuingia siku ya raha ambayo Mungu na mwanadamu watashiriki, kwani ni walengwa wa adhabu na ni waovu, na si watu wenye haki. Walikuwa wamekombolewa wakati mmoja, na pia walikuwa wamehukumiwa na kuadibiwa; walikuwa pia wamemhudumia Mungu wakati mmoja, lakini siku ya mwisho itakapofika, bado wataondolewa na kuangamizwa kwa sababu ya uovu wao na kwa sababu ya kutotii na kutokombolewa kwao. Hawatakuwa tena katika ulimwengu wa baadaye, na hawatakuweko tena miongoni mwa jamii ya binadamu ya baadaye. Watenda maovu wote na yeyote na wote ambao hawajaokolewa wataangamizwa wakati watakatifu miongoni mwa binadamu wataingia rahani, bila kujali kama wao ni roho za wafu ama wale wanaoishi bado katika mwili. Bila kujali enzi ya hizi roho zitendazo maovu na watu watenda maovu, ama roho za watu wenye haki na watu wanaofanya haki wako, mtenda maovu yeyote ataangamizwa, na yeyote mwenye haki ataishi. Iwapo mtu ama roho inapokea wokovu haiamuliwi kabisa kulingana na kazi ya enzi ya mwisho, lakini inaamuliwa kulingana na iwapo wamempinga ama kutomtii Mungu. Kama watu wa enzi ya awali walifanya maovu na hawangeweza kuokolewa, bila shaka wangekuwa walengwa wa adhabu. Kama watu wa enzi hii wanafanya maovu na hawawezi kuokolewa, hakika wao pia ni walengwa wa adhabu. Watu wanatengwa kwa msingi wa mema na mabaya, sio kwa msingi wa enzi. Baada ya kutengwa kwa msingi wa mema na mabaya, watu hawaadhibiwi ama kutuzwa mara moja; badala yake, Mungu atafanya tu kazi Yake ya kuwaadhibu waovu na kuwatuza wema baada ya Yeye kumaliza kutekeleza kazi Yake ya ushindi katika siku za mwisho. Kwa kweli, Amekuwa akitumia mema na mabaya kutenga binadamu tangu Afanye kazi Yake miongoni mwa binadamu. Atawatuza tu wenye haki na kuwaadhibu waovu baada ya kukamilika kwa kazi Yake, badala ya kuwatenga waovu na wenye haki baada ya kukamilika kwa kazi Yake mwishowe na kisha kufanya kazi Yake ya kuwaadhibu waovu na kuwatuza wazuri mara moja. Kazi Yake ya mwisho ya kuadhibu waovu na kuwatuza wazuri inafanywa kabisa ili kutakasa kabisa binadamu wote, ili Aweze kuleta binadamu watakatifu mno katika pumziko la milele. Hatua hii ya kazi Yake ni kazi Yake muhimu zaidi. Ni hatua ya mwisho ya kazi Yake yote ya usimamizi. Kama Mungu hangewaangamiza waovu lakini badala yake kuwaacha wabakie, basi binadamu wote bado hawangeweza kuingia rahani, na Mungu hangeweza kuleta binadamu katika ulimwengu bora. Kazi ya aina hii haingekuwa imekamilika kabisa. Atakapomaliza kazi Yake, binadamu wote watakuwa watakatifu kabisa. Mungu anaweza kuishi kwa amani rahani kwa namna hii pekee.
Watu leo hawawezi kutengana na mambo ya mwili; hawawezi kuacha starehe za mwili, wala hawawezi kuiacha dunia, pesa, ama tabia yao potovu. Watu wengi wanaendelea na shughuli zao kwa hali ya uzembe. Kwa kweli, hawa watu hawana Mungu mioyoni mwao hata kidogo; zaidi ya hayo, hawamchi Mungu. Hawana Mungu mioyoni mwao, na hivyo hawawezi kutambua yote anayofanya Mungu, na hawawezi kabisa kuamini maneno Azungumzayo kwa mdomo Wake. Watu hawa ni wa mwili sana, wamepotoshwa sana na hawana ukweli wowote, zaidi ya hayo, hawaamini kwamba Mungu anaweza kuwa mwili. Yeyote asiyemwamini Mungu wa mwili—yaani, yeyote asiyeamini kazi na hotuba ya Mungu anayeonekana na haamini Mungu anayeonekana lakini badala yake anaabudu Mungu asiyeonekana mbinguni—hana Mungu katika moyo wake. Ni watu wasiomtii na wanaompinga Mungu. Watu hawa hawana ubinadamu na fahamu, kusema chochote kuhusu ukweli. Kwa watu hawa Mungu anayeonekana na kushikika hawezi kuaminika zaidi, lakini Mungu asiyeonekana wala kushikika ni Mungu wa kuaminika na pia Anayefurahisha nyoyo zao. Wanachotafuta si ukweli wa uhalisi, wala si kiini cha kweli cha uhai, wala nia za Mungu; badala yake, wanatafuta msisimko. Mambo yoyote yanayoweza kuwaruhusu kufikia tamaa zao ni, bila shaka, imani na shughuli zao. Wamwamini Mungu tu ili kuridhisha tamaa zao, si kutafuta ukweli. Hawa watu si watenda maovu? Wanajiamini sana, na hawaamini kwamba Mungu aliye mbinguni atawaangamiza, hawa “watu wazuri.” Badala yake, wanaamini kwamba Mungu atawaruhusu kubaki na, zaidi ya hayo, Atawatuza vizuri sana, kwani wamemfanyia Mungu mambo mengi na kuonyesha kiwango kikubwa cha “uaminifu” Kwake. Kama wangemtafuta Mungu anayeonekana, wangelipiza kisasi mara moja dhidi ya Mungu na kukasirika wakati hawatapata tamaa zao. Hawa ni watu waovu wanaotaka kuridhisha tamaa zao; si watu wa uadilifu wanaosaka ukweli. Watu kama hao ni wale wanaojulikana kama waovu wanaomfuata Kristo. Wale watu wasioutafuta ukweli hawawezi kuamini ukweli. Hawawezi kabisa kutambua matokeo ya baadaye ya binadamu, kwani hawaamini kazi ama hotuba yoyote ya Mungu anayeonekana, na hawawezi kuamini hitimisho la baadaye la binadamu. Hivyo, hata wakimfuata Mungu anayeonekana, bado wanatenda maovu na hawatafuti ukweli, wala hawatendi ukweli Ninaohitaji. Wale watu wasioamini kwamba wataangamizwa kinyume ni kwamba ni wale watu watakaoangamizwa. Wote wanajiamini kuwa wajanja sana, na wanaamini kwamba wao wenyewe ndio wanaotenda ukweli. Wanafikiria mwenendo wao mbovu kuwa ukweli na hivyo wanauthamini. Hawa watu waovu wanajiamini sana; wanachukua ukweli kuwa mafundisho ya dini, na kuchukua vitendo vyao vibovu kuwa ukweli, na mwishowe watavuna tu walichopanda. Watu wanapojiamini zaidi na wanapokuwa na kiburi zaidi, ndipo hawawezi zaidi kupata ukweli; watu wanapomwamini Mungu wa mbinguni zaidi, ndipo wanampinga Mungu zaidi. Hawa ndio watu watakaoadhibiwa. Kabla ya binadamu kuingia rahani, iwapo kila aina ya mtu ataadhibiwa ama kutuzwa kutaamuliwa kulingana na iwapo wanatafuta ukweli, iwapo wanamjua Mungu, iwapo wanaweza kumtii Mungu anayeonekana. Waliomhudumia Mungu anayeonekana lakini bado hawamjui wala kumtii hawana ukweli. Watu hawa ni watenda maovu, na watenda maovu bila shaka wataadhibiwa; zaidi ya hapo, wataadhibiwa kulingana na mienendo yao mibovu. Mungu ni wa mwanadamu kumwamini, na pia Anastahili utii wa mwanadamu. Wale wanaomwamini tu Mungu asiye yakini na asiyeonekana ni wale wasiomwamini Mungu; zaidi ya hapo, hawawezi kumtii Mungu. Kama hawa watu bado hawawezi kumwamini Mungu anayeonekana wakati kazi Yake ya ushindi inakamilika, na pia wanaendelea kutomtii na kumpinga Mungu anayeonekana katika mwili, hawa wanaoamini isiyo yakini bila shaka, wataangamizwa. Ni kama ilivyo na wale miongoni mwenu—yeyote anayemtambua Mungu Aliyepata mwili kwa maneno lakini bado hatendi ukweli wa utii kwa Mungu Aliyepata mwili hatimaye ataondolewa na kuangamizwa, na yeyote anayemtambua Mungu anayeonekana na pia kula na kunywa ukweli ulioonyeshwa na Mungu anayeonekana lakini bado anamtafuta Mungu asiye yakini na asiyeonekana pia yeye ataangamizwa baadaye. Hakuna hata mmoja wa watu hawa anayeweza kubaki hadi wakati wa pumziko baada ya kazi ya Mungu kukamilika; hakuwezi kuwa yeyote kama watu hawa atakayebakia hadi wakati wa pumziko. Watu wenye pepo ni wale wasiotenda ukweli; asili yao ni ile inayompinga na kutomtii Mungu, na hawana nia hata kidogo za kumtii Mungu. Watu wote kama hao wataangamizwa. Iwapo una ukweli na iwapo unampinga Mungu hayo yanaamuliwa kulingana na asili yako, si kulingana na sura yako ama hotuba na mwenendo wako wa mara kwa mara. Asili ya kila mtu inaamua iwapo ataangamizwa; hii inaamuliwa kulingana na asili iliyofichuliwa na mienendo yao na kutafuta kwao ukweli. Miongoni mwa watu wanaofanya kazi sawa na pia kufanya kiasi sawa cha kazi, wale ambao asili yao ni nzuri na wanaomiliki ukweli ni watu wanaoweza kubaki, lakini wale ambao asili yao ya ubinadamu ni mbovu na wasiomtii Mungu anayeonekana ni wale watakaoangamizwa. Kazi ama maneno yoyote ya Mungu yanayoelekezwa kwa hatima ya binadamu yanahusiana na binadamu ipasavyo kulingana na asili ya kila mtu; hakuna kosa lolote litakalotokea, na hakutakuwa na kosa hata moja litakalofanywa. Ni pale tu ambapo watu wanafanya kazi ndipo hisia za binadamu ama maana itaingilia. Kazi anayofanya Mungu ndiyo inayofaa zaidi; hakika Hataleta madai ya uongo dhidi ya kiumbe yeyote. Sasa kuna watu wengi wasioweza kutambua hatima ya baadaye ya binadamu na ambao pia hawaamini maneno Nisemayo; wote wasioamini, pamoja na wasiotenda ukweli, ni mapepo!
Wanaotafuta na wasiotafuta sasa ni aina mbili tofauti ya watu, na wao ni aina mbili ya watu na hatima mbili tofauti. Wanaotafuta maarifa ya ukweli na kutenda ukweli ni watu ambao Mungu ataokoa. Wale wasiojua njia ya ukweli ni mapepo na adui; ni vizazi vya malaika mkuu na wataangamizwa. Hata wacha Mungu wanaomwamini Mungu asiye yakini—je, si mapepo pia? Watu wanaomiliki dhamiri nzuri lakini hawakubali njia ya ukweli ni mapepo; asili yao ni ile inayompinga Mungu. Wale wasiokubali njia ya ukweli ni wale wanaompinga Mungu, na hata kama watu hawa wanavumilia taabu nyingi, bado wataangamizwa. Wasio tayari kuiwacha dunia, wasioweza kuvumilia kutengana na wazazi wao, wasioweza kuvumilia kujiondolea raha zao za mwili, wote hawamtii Mungu na wote wataangamizwa. Yeyote asiyemwamini Mungu aliyepata mwili ni pepo; zaidi ya hayo, wataangamizwa. Wanaoamini lakini hawatendi ukweli, wasiomwamini Mungu aliyepata mwili, na wale ambao hawaamini kabisa kuwepo kwa Mungu wataangamizwa. Yeyote anayeweza kubaki ni mtu ambaye amepitia uchungu wa usafishaji na kusimama imara; huyu ni mtu ambaye kweli amepitia majaribio. Yeyote asiyemtambua Mungu ni adui; yaani, yeyote aliye ndani ama nje ya mkondo huu ambaye hamtambui Mungu aliyepata mwili ni adui wa Kristo! Shetani ni nani, mapepo ni nani, na nani ni maadui wa Mungu kama si wapinzani wasiomwamini Mungu? Wao si watu wasiomtii Mungu? Wao si watu wanaodai kwa maneno kuamini lakini hawana ukweli? Wao si wale watu wanaofuata tu kupata kwa baraka lakini hawawezi kumshuhudia Mungu? Bado unachanganyika na wale mapepo leo na kuwa na dhamiri na mapenzi kwao, lakini kwa hali hii huenezi nia nzuri kuelekea kwa Shetani? Je, huchukuliwi kuwa unashiriki na mapepo? Kama watu siku hizi bado hawawezi kutofautisha kati ya mema na maovu, na wanaendelea kuwa wenye kupenda na kuhurumia bila kufikiri na bila nia yoyote ya kutafuta mapenzi ya Mungu au kuweza kwa njia yoyote kushikilia nia za Mungu kama zao wenyewe, basi miisho wao utakuwa dhalili zaidi. Yeyote asiyemwamini Mungu wa mwili ni adui wa Mungu. Kama unaweza kushikilia dhamiri na mapenzi kuelekea kwa adui, je, hujakosa hisia ya haki? Kama unalingana na wale Ninaowachukia na wale Nisiokubaliana nao, na bado unashikilia mapenzi na hisia za binafsi kwao, basi wewe si asiyetii? Humpingi Mungu kimakusudi? Je, mtu kama huyu anamiliki ukweli? Ikiwa watu wako na dhamiri kwa maadui, wana upendo kwa mapepo na wana huruma kwa Shetani, basi hawaikatizi kazi ya Mungu kimakusudi? Wale watu wanaomwamini Yesu tu na hawamwamini Mungu aliyepata mwili wakati wa siku za mwisho na wale wanaodai kwa maneno kumwamini Mungu aliyepata mwili lakini wanafanya maovu wote ni adui wa Kristo, sembuse wale watu wasiomwamini Mungu. Hawa watu wote wataangamizwa. Kiwango ambacho mwanadamu anamhukumu mwanadamu kinatokana na tabia zake; aliye na mwenendo mzuri ni mtu mwenye haki, na aliye na mwenendo wa kuchukiza ni mwovu. Kiwango ambacho Mungu anamhukumu mwanadamu kinatokana na iwapo asili ya mtu inamtii Yeye; anayemtii Mungu ni mtu mwenye haki, na asiyemtii Mungu ni adui na mtu mwovu, bila kujali iwapo tabia ya mtu huyu ni nzuri ama mbaya, na bila kujali iwapo hotuba ya mtu huyu ni sahihi ama si sahihi. Watu wengine wanatamani kutumia matendo mazuri kupata hatima nzuri ya baadaye, na watu wengine wanataka kutumia hotuba nzuri kununua hatima nzuri. Watu wanaamini kimakosa kwamba Mungu anaamua matokeo ya mwanadamu kulingana na tabia ama hotuba yake, na kwa hivyo watu wengi watataka kutumia haya kupata fadhila ya muda mfupi kupitia udanganyifu. Watu ambao baadaye watasalimika kupitia pumziko wote watakuwa wamevumilia siku ya dhiki na pia kumshuhudia Mungu; wote watakuwa watu ambao wamefanya jukumu lao na wana nia ya kumtii Mungu. Wanaotaka tu kutumia fursa kufanya huduma ili kuepuka kutenda ukweli hawataweza kubaki. Mungu ana viwango sahihi vya mipangilio ya matokeo ya kila mtu; Hafanyi tu maamuzi haya kulingana na maneno na mwenendo wa mtu, wala Hayafanyi kulingana na tabia zao wakati wa kipindi kimoja cha muda. Hakika Hatakuwa na huruma na mwenendo wowote mbaya wa mtu kwa sababu ya huduma ya mtu ya zamani kwa Mungu, wala Hatamnusuru mtu kutokana na kifo kwa sababu ya gharama kwa Mungu ya mara moja. Hakuna anayeweza kuepuka adhabu ya uovu wake, na hakuna anayeweza kuficha tabia zake mbovu na hivyo kuepuka adhabu ya maangamizi. Kama mtu anaweza kweli kufanya jukumu lake, basi inamaanisha kwamba ni mwaminifu milele kwa Mungu na hatafuti tuzo, bila kujali iwapo anapokea baraka ama bahati mbaya. Kama watu wana uaminifu kwa Mungu waonapo baraka lakini wanapoteza uaminifu wao wasipoweza kuona baraka na mwishowe bado wasiweze kumshuhudia Mungu na bado wasiweze kufanya jukumu lao kama wapasavyo, hawa watu waliomhudumia Mungu wakati mmoja kwa uaminifu bado wataangamizwa. Kwa ufupi, watu waovu hawawezi kuishi milele, wala hawawezi kuingia rahani; watu wenye haki tu ndio mabwana wa pumziko. Baada ya binadamu kuingia katika njia sawa, watu watakuwa na maisha ya kawaida ya binadamu. Wote watafanya jukumu lao husika na kuwa waaminifu kabisa kwa Mungu. Watatoa kabisa kutotii kwao na tabia yao iliyopotoshwa, na wataishi kwa ajili ya Mungu na kwa sababu ya Mungu. Watakosa uasi na upinzani. Wataweza kabisa kumtii Mungu. Haya ndiyo maisha ya Mungu na mwanadamu na maisha ya ufalme, na ni maisha ya pumziko.
Wanaopeleka watoto na jamaa zao wasioamini kabisa kanisani ni wachoyo sana na wanaonyesha ukarimu wao. Watu hawa wanalenga tu kuwa wenye upendo, bila kujali iwapo wanaamini au la na iwapo ni mapenzi ya Mungu. Wengine wanaleta wake zao mbele ya Mungu, ama kuleta wazazi wao mbele ya Mungu, na bila kujali iwapo Roho Mtakatifu anakubali ama anafanya kazi Yake, kwa upofu “wanawachukua watu wenye vipaji” kwa ajili ya Mungu. Kuna faida gani inayoweza kupatikana kutokana na kueneza ukarimu huu kwa watu hawa wasioamini? Hata kama hawa wasioamini wasio na uwepo wa Roho Mtakatifu wanapambana kumfuata Mungu, bado hawawezi kuokolewa kama mtu anavyodhani wanaweza. Wanaopokea wokovu kwa kweli si rahisi hivyo kuwapata. Wale ambao hawajapitia kazi ya Roho Mtakatifu na majaribio na hawajakamilishwa na Mungu aliyepata mwili hawawezi kukamilika kabisa. Kwa hivyo, watu hawa hawana uwepo wa Roho Mtakatifu kutoka wakati wanaanza kumfuata Mungu kwa jina. Kulingana na hali yao halisi, hawawezi tu kufanywa kamili. Hivyo, Roho Mtakatifu Haamui kutumia nguvu nyingi kwao, wala Hawapatii nuru yoyote ama kuwaongoza kwa njia yoyote; Anawaruhusu tu kufuata na hatimaye kufichua matokeo yao—haya yametosha. Shauku na nia za mwanadamu zinatoka kwa Shetani, na hakuna vile zinaweza kukamilisha kazi ya Roho Mtakatifu. Bila kujali mtu ni mtu wa aina gani, mtu lazima awe na kazi ya Roho Mtakatifu—je, mtu anaweza kumkamilisha mtu? Mbona mume anampenda mke wake? Na mbona mke anampenda mume wake? Mbona watoto ni watiifu kwa wazazi wao? Na mbona wazazi wanawapenda sana watoto wao? Watu kweli wana nia za aina gani? Je, si kuweza kukidhi mipango na tamaa zao za ubinafsi? Kweli ni ya mpango wa usimamizi wa Mungu? Ni ya kazi ya Mungu? Ni ya kutimiza wajibu wa kiumbe? Waliomwamini Mungu kwanza na hawangepata uwepo wa Roho Mtakatifu hawawezi kupata kazi ya Roho Mtakatifu; imeamuliwa kwamba watu hawa wataangamizwa. Bila kujali kiasi cha upendo ambao mtu anao kwao, hauwezi kuchukua nafasi ya kazi ya Roho Mtakatifu. Shauku na upendo wa mwanadamu unawakilisha nia za mwanadamu, lakini haviwezi kuwakilisha nia za Mungu na haviwezi kuchukua nafasi ya kazi ya Mungu. Hata mtu akieneza kiasi kikubwa zaidi cha upendo ama huruma kwa hao watu wanaomwamini Mungu kwa jina na kujifanya kumfuata Yeye lakini hawajui ni nini maana ya kumwamini Mungu, bado hawatapata huruma ya Mungu ama kupata kazi ya Roho Mtakatifu. Hata kama watu wanaomfuata Mungu kwa dhati ni wenye akili ndogo na hawawezi kuelewa kweli nyingi, bado wanaweza kupata kazi ya Roho Mtakatifu mara kwa mara, lakini wale walio wa akili nzuri kidogo, lakini hawaamini kwa dhati hawawezi kabisa kupata uwepo wa Roho Mtakatifu. Hakuna kabisa uwezekano wowote wa wokovu na watu hawa. Hata wakisoma maneno ya Mungu au wasikilize mahubiri mara kwa mara ama hata kumwimbia Mungu sifa, mwishowe hawataweza kubaki mpaka wakati wa pumziko. Iwapo mtu anatafuta kwa dhati hakuamuliwi na jinsi wengine wanamhukumu ama jinsi wengine karibu wanamwona, lakini kunaamuliwa na iwapo Roho Mtakatifu anamfanyia kazi na iwapo ana uwepo wa Roho Mtakatifu, na kunaamuliwa zaidi na iwapo tabia yake inabadilika na iwapo ana maarifa ya Mungu baada ya kupitia kazi ya Roho Mtakatifu kwa muda fulani; ikiwa Roho Mtakatifu anamfanyia mtu kazi, tabia ya mtu huyu itabadilika polepole, na mtazamo wake wa kumwamini Mungu utakua safi polepole. Bila kujali muda gani mtu anamfuata Mungu, kama wamebadilika, hii inamaanisha kwamba Roho Mtakatifu anafanya kazi kwake. Kama hawajabadilika, inamaanisha kwamba Roho Mtakatifu hafanyi kazi kwake. Hata kama hawa watu wanatoa huduma fulani, wanachochewa na nia zao za kupata bahati nzuri. Huduma ya mara kwa mara haiwezi kuchukua nafasi ya mabadiliko katika tabia yao. Hatimaye, bado wataangamizwa, kwani hakuna haja ya wale wanaotoa Huduma ndani ya ufalme, wala hakuna haja ya yeyote ambaye tabia yake haijabadilika kuwahudumia wale watu ambao wamekamilishwa na walio waaminifu kwa Mungu. Hayo maneno kutoka zamani, “Wakati mtu anamwamini Bwana, bahati inatabasamu kwa familia yake nzima,” yanafaa kwa Enzi ya Neema lakini hayana uhusiano na hatima ya mwanadamu. Yalifaa tu kwa hatua ya wakati wa Enzi ya Neema. Maana iliyokusudiwa ya maneno haya inaelekezwa kwa amani na baraka yakinifu ambazo watu wanafurahia; hayamaanishi kwamba familia nzima ya anayemwamini Bwana itaokolewa, wala hayamaanishi kwamba wakati mtu anapata bahati nzuri, familia yake nzima pia itaingia rahani. Iwapo mtu anapokea baraka ama kupata bahati mbaya inaamuliwa kulingana na kiini cha mtu, na haiamuliwi kulingana na asili ya kawaida ambayo mtu anashiriki na wengine. Ufalme hauna kabisa usemi kama huu ama kanuni kama hii. Kama mtu anaweza kusalimika hatimaye, ni kwa sababu amefikia mahitaji ya Mungu, na kama mtu hawezi hatimaye kubaki katika kipindi cha pumziko, ni kwa sababu mtu huyu hamtii Mungu na hajakidhi mahitaji ya Mungu. Kila mtu ana hatima inayofaa. Hatima hizi zinaamuliwa kulingana na asili ya kila mtu na hazihusiani kabisa. Mwenendo ovu wa mtoto hauwezi kuhamishwa kwa wazazi wake, na haki ya mtoto haiwezi kushirikishwa wazazi wake. Mwenendo ovu wa mzazi huwezi kuhamishwa kwa watoto wake, na haki ya mzazi haiwezi kushirikishwa watoto wake. Kila mtu anabeba dhambi zake husika, na kila mtu anafurahia bahati yake husika. Hakuna anayeweza kuchukua ya mwingine. Hii ni haki. Kwa mtazamo wa mwanadamu, iwapo wazazi wanapata bahati nzuri, watoto wao pia wanaweza, na watoto wakifanya maovu, wazazi wao lazima walipie dhambi zao. Huu ni mtazamo wa mwanadamu na njia ya mwanadamu ya kufanya vitu. Si mtazamo wa Mungu. Matokeo ya kila mtu yanaamuliwa kulingana na asili inayotoka kwa mwenendo wao, na daima yanaamuliwa inavyofaa. Hakuna awezaye kubeba dhambi za mwingine; hata zaidi ya hayo, hakuna anayeweza kupokea adhabu badala ya mwingine. Hii ni thabiti. Malezi ya upendo ya mzazi kwa watoto wake hayamaanishi kwamba anaweza kufanya matendo ya haki badala ya watoto wake, wala upendo wenye utiifu wa mtoto kwa wazazi wake haumaanishi kwamba anaweza kufanya matendo ya haki badala ya wazazi wake. Hiyo ndiyo maana ya kweli ya maneno haya, “Basi kutakuwa na watu wawili shambani; mmoja wao atachukuliwa, na mwingine kuachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga katika kisiagi; mmoja atachukuliwa, na mwingine kuachwa.” Hakuna anayeweza kuwaingiza watoto wake watenda maovu rahani kwa msingi wa upendo wao wa kina kwa watoto wao, wala hakuna anayeweza kumwingiza mke wake (ama mume) rahani kwa sababu ya mwenendo wao wa haki. Hii ni kanuni ya utawala; hakuwezi kuwa na ubaguzi kwa mtu yeyote. Wanaotenda haki ni wanaotenda haki, na watenda maovu ni watenda maovu. Watenda haki watasalimika, na watenda maovu wataangamizwa. Watakatifu ni watakatifu; wao si wachafu. Wachafu ni wachafu, na hawana sehemu yoyote takatifu. Watu wote waovu wataangamizwa, na watu wote wa haki watasalimika, hata kama watoto wa watenda maovu wanafanya matendo ya haki, na hata kama wazazi wa mtu wa haki wanafanya matendo maovu. Hakuna uhusiano kati ya mume anayeamini na mke asiyeamini, na hakuna uhusiano kati ya watoto wanaoamini na wazazi wasioamini. Ni aina mbili zisizolingana. Kabla ya kuingia rahani, mtu ana jamaa wa kimwili, lakini baada ya mtu kuingia rahani, mtu hana jamaa wa kimwili tena wa kuzungumzia. Wanaofanya wajibu wao na wasiofanya ni adui, wanaompenda Mungu na wanaomchukia Mungu ni wapinzani. Wanaoingia rahani na wale ambao wameangamizwa ni aina mbili ya viumbe wasiolingana. Viumbe wanaotimiza wajibu wao watasalimika, na viumbe wasiotimiza wajibu wao wataangamizwa; zaidi ya hayo, hii itadumu milele. Je, unampenda mume wako ili kutimiza wajibu wako kama kiumbe? Je, unampenda mke wako ili kutimiza wajibu wako kama kiumbe? Je, wewe ni mtiifu kwa wazazi wako wasioamini ili kutimiza wajibu wako kama kiumbe? Mtazamo wa mwanadamu wa kumwamini Mungu ni sahihi ama la? Mbona unamwamini Mungu? Unataka kupata nini? Unampenda Mungu jinsi gani? Wasioweza kutimiza wajibu wao kama viumbe na hawawezi kufanya juhudi nzima wataangamizwa. Watu leo wana mahusiano ya kimwili miongoni mwao, na pia ushirikiano wa damu, lakini baadaye hii yote itavunjwa. Waumini na wasioamini hawalingani ila wanapingana. Walio rahani wanaamini kwamba kuna Mungu na wanamtii Mungu. Wasiomtii Mungu wote watakuwa wameangamizwa. Familia hazitakuwa tena duniani; kunawezaje kuwa na wazazi na watoto ama mahusiano kati ya waume na wake? Kutoambatana kati ya imani na kutoamini kutakuwa kumevunja haya mahusiano ya kimwili!
Awali hakukuwa na familia miongoni mwa binadamu; mwanamume na mwanamke tu walikuwepo—aina mbili tofauti za wanadamu. Hakukuwa na nchi, sembuse familia, lakini kwa sababu ya upotovu wa mwanadamu, watu wa aina yote walijipanga katika koo binafsi, baadaye kukua kwa nchi na mataifa. Nchi na mataifa haya yalikuwa na familia ndogo binafsi, na kwa namna hii watu wa aina yote walisambazwa miongoni mwa jamii mbalimbali kulingana na tofauti ya lugha na mipaka igawayo. Kwa kweli, bila kujali idadi ya jamii zilizo duniani, binadamu wana babu mmoja pekee. Mwanzoni, kulikuwa na watu wa aina mbili tu, na aina hizi mbili zilikuwa mwanamume na mwanamke. Hata hivyo, kwa sababu ya maendeleo ya kazi ya Mungu, kupita kwa historia na mabadiliko ya kijiografia, kwa viwango mbalimbali aina hizi mbili za watu ziliendelezwa kuwa watu wa aina nyingine zaidi. Mwishowe, bila kujali idadi ya jamii zilizo katika binadamu, binadamu wote bado ni viumbe wa Mungu. Bila kujali jamii ambayo watu wako ndani, wote ni viumbe Wake; wote ni vizazi vya Adamu na Hawa. Hata kama hawajatengenezwa na mikono ya Mungu, ni vizazi vya Adamu na Hawa, ambao Mungu Mwenyewe aliumba. Bila kujali aina ambayo watu wako ndani, wote ni viumbe Wake; kwa sababu ni wa binadamu, ambao uliumbwa na Mungu, hatima yao ni hiyo ambayo binadamu wanapaswa kuwa nayo, na wamegawanywa kulingana na kanuni zinazopanga binadamu. Hiyo ni kusema kwamba, watenda maovu na wenye haki, hata hivyo, ni viumbe. Viumbe wafanyao maovu wataangamizwa hatimaye, na viumbe wafanyao matendo ya haki watasalimika. Huu ni mpangilio unaofaa sana wa viumbe wa aina hizi mbili. Watenda maovu hawawezi, kwa sababu ya kutotii kwao, kukataa kwamba ni viumbe wa Mungu lakini wameporwa na Shetani na hivyo hawawezi kuokolewa. Viumbe wa mwenendo wa haki hawawezi kutegemea ukweli kwamba watasalimika kukataa kwamba wameumbwa na Mungu na bado wamepokea wokovu baada ya kupotoshwa na Shetani. Watenda maovu ni viumbe wasiomtii Mungu; ni viumbe ambao hawawezi kuokolewa na tayari wameporwa na Shetani. Watu wanaotenda maovu ni watu pia; ni watu waliopotoshwa mno na watu wasioweza kuokolewa. Jinsi walivyo viumbe pia, watu wa mwenendo wa haki pia wamepotoshwa, lakini ni watu walio tayari kuacha tabia yao potovu na wanaweza kumtii Mungu. Watu wa mwenendo wa haki hawajajaa haki; badala yake, wamepokea wokovu na kuacha tabia yao potovu kumtii Mungu; watashikilia msimamo huo mwishowe, lakini hii si kusema kwamba hawajapotoshwa na Shetani. Baada ya kazi ya Mungu kuisha, miongoni mwa viumbe Wake wote, kutakuwa na wale watakaoangamizwa na wale watakaosalimika. Huu ni mwelekeo usioepukika wa kazi Yake ya usimamizi. Hakuna anayeweza kuyakataa haya. Watenda maovu hawawezi kusalimika; wanaomtii na kumfuata Mungu hadi mwishowe hakika watasalimika. Kwa sababu kazi hii ni ya usimamizi wa binadamu, kutakuwa na wale watakaobaki na wale watakaoondolewa. Haya ni matokeo tofauti ya watu wa aina tofauti, na hii ndiyo mipango inayofaa zaidi ya viumbe Wake. Mpango wa mwisho wa Mungu kwa mwanadamu ni kugawa kwa kuzivunja familia, kuyavunja mataifa na kuivunja mipaka ya kitaifa. Ni moja isiyo na familia na mipaka ya kitaifa, kwani mwanadamu, hata hivyo, ni wa babu mmoja na ni kiumbe wa Mungu. Kwa ufupi, viumbe wafanyao maovu wataangamizwa, na viumbe wanaomtii Mungu watasalimika. Kwa njia hii, hakutakuwa na familia, hakutakuwa na nchi na hasa hakutakuwa na mataifa katika pumziko la baadaye; binadamu wa aina hii ni aina takatifu kabisa ya binadamu. Adamu na Hawa waliumbwa awali ili mwanadamu aweze kutunza mambo yote duniani; mwanadamu awali alikuwa bwana wa vitu vyote. Nia ya Yehova ya kumuumba mwanadamu ilikuwa kumruhusu mwanadamu kuwa duniani na pia kutunza vitu vyote duniani, kwani mwanadamu awali hakuwa amepotoshwa na pia hakuweza kutenda maovu. Hata hivyo, baada ya mwanadamu kupotoshwa, hakuwa mtunzaji wa vitu vyote tena, na madhumuni ya wokovu wa Mungu ni kurejesha kazi hii ya mwanadamu, kurejesha ufahamu wa awali wa mwanadamu na utii wake wa awali; binadamu rahani watakuwa picha halisi ya matokeo ambayo kazi ya Mungu ya wokovu inatarajia kufikia. Ingawa hayatakuwa tena maisha kama yale ya bustani ya Edeni, kiini chake kitakuwa sawa; binadamu hawatakuwa tu nafsi yake ya awali isiyo potovu, lakini badala yake binadamu waliopotoshwa na kisha kupata wokovu. Watu hawa waliopata wokovu hatimaye (yaani, baada ya kazi Yake kuisha) wataingia rahani. Vivyo hivyo, matokeo ya wale walioadhibiwa pia yote yatafichuliwa mwishowe, na wataangamizwa tu baada ya kazi Yake kuisha. Hii ni kusema kwamba baada ya kazi Yake kuisha, watendao maovu na wale waliookolewa wote watafichuliwa, kwani kazi ya kufichua watu wa aina zote (bila kujali iwapo ni watenda maovu ama waliookolewa) itatekelezwa kwa watu wote wakati huo huo. Watenda maovu wataondolewa, na wale wanaoweza kubaki watafichuliwa wakati huo huo. Kwa hivyo, matokeo ya watu wa aina zote yatafichuliwa wakati huo huo. Hataliruhusu kwanza kundi la watu waliookolewa kuingia rahani kabla ya kuweka kando watenda maovu na kuwahukumu au kuwaadhibu kidogo kidogo; ukweli kwa kweli si hivyo. Wakati watenda maovu wanaangamizwa na waliosalimika wanaingia rahani, kazi Yake katika ulimwengu mzima itakuwa imemalizika. Hakutakuwa na utaratibu wa kipaumbele miongoni mwa wale wanaopata baraka na wale wanaopata taabu; wanaopokea baraka wataishi milele, na wanaopata taabu wataangamia milele. Hizi hatua mbili za kazi zitakamilika wakati huo huo. Ni hasa kwa sababu kuna watu wasiotii ndiyo maana haki ya watu wanaotii itafichuliwa, na ni hasa kwa sababu kuna wale waliopokea baraka ndiyo maana taabu ya wale wanaotenda maovu kwa sababu ya mwenendo wao mbovu itafichuliwa. Kama Mungu hakufichua watenda maovu, hao watu wanaomtii Mungu kwa dhati hawangeona jua; kama Mungu hangewapelekea wanaomtii katika hatima inayofaa, wasiomtii Mungu hawangeweza kupata adhabu wanayostahili. Huu ndio mwendo wa kazi Yake. Kama hangefanya kazi hii ya kuadhibu maovu na kutuza mazuri, viumbe Wake hawangeweza kuingia hatima zao husika. Mwanadamu aingiapo rahani, watenda maovu wataangamizwa, binadamu wote wataingia katika njia sahihi, na watu wa kila aina watakuwa na aina yao kulingana na kazi wanayopaswa kufanya. Hii tu ndiyo itakuwa siku ya binadamu kupumzika na mwenendo usioepukika wa maendeleo ya binadamu, na wakati tu binadamu wataingia rahani ndipo utimilifu mkubwa na wa mwisho wa Mungu utamalizika; hii itakuwa tamati ya kazi Yake. Hii kazi itamaliza maisha ya uharibifu ya kimwili ya binadamu, na itamaliza maisha ya binadamu potovu. Kutoka hapa binadamu wataingia katika ulimwengu mpya. Ingawa mwanadamu anaishi kimwili, kuna tofauti kubwa kati ya kiini cha maisha yake na kiini cha maisha ya binadamu wapotovu. Maana ya kuwepo kwake na maana ya kuwepo kwa binadamu wapotovu pia ni tofauti. Ingawa haya si maisha ya mtu wa aina mpya, inaweza kusemwa kuwa maisha ya binadamu ambao wamepata wokovu na maisha yenye ubinadamu na busara kurejeshwa. Hawa ni watu ambao hawakumtii Mungu wakati mmoja, na ambao walishindwa na Mungu wakati mmoja na baadaye kuokolewa na Yeye; hawa ni watu waliomwaibisha Mungu na baadaye wakamshuhudia. Uwepo wao, baada ya kupitia na kuendelea kuishi baada ya jaribio Lake, ni uwepo wa maana kubwa zaidi; ni watu waliomshuhudia Mungu mbele ya Shetani; ni watu wanaofaa kuishi. Watakaoangamizwa ni watu wasioweza kumshuhudia Mungu na hawafai kuishi. Maangamizo yao yatakuwa kwa sababu ya mwenendo wao mwovu, na maangamizo ni hatima yao bora zaidi. Mwanadamu aingiapo baadaye katika ulimwengu mzuri, hakutakuwa na mahusiano kati ya mume na mke, kati ya baba na binti ama kati ya mama na mwana wa kiume ambayo mwanadamu anafikiria atapata. Wakati huo, mwanadamu atafuata aina yake, na familia itakuwa tayari imevunjwa. Baada ya kushindwa kabisa, Shetani hatawasumbua binadamu tena, na mwanadamu hatakuwa tena na tabia potovu ya kishetani. Wale watu wasiotii watakuwa wameangamizwa tayari, na wale watu wanaotii pekee ndio wataishi. Na basi familia chache sana zitasalimika bila kuharibika; mahusiano ya kimwili yatawezaje kuweko? Maisha ya kimwili ya zamani ya mwanadamu yatapigwa marufuku kabisa; mahusiano ya kimwili yatawezaje kuweko kati ya watu? Bila tabia potovu ya kishetani, maisha ya watu hayatakuwa tena maisha ya zamani ya siku zilizopita, lakini badala yake maisha mapya. Wazazi watapoteza watoto, na watoto watapoteza wazazi. Waume watapoteza wake, na wake watapoteza waume. Watu sasa wana mahusiano ya kimwili miongoni mwao. Wakati wote watakuwa wameingia rahani hakutakuwa na mahusiano ya kimwili tena. Binadamu kama hawa tu ndio watakuwa wa haki na watakatifu, binadamu kama hawa tu ndio watamwabudu Mungu.
Mungu aliumba binadamu na Akawaweka duniani, ambao Amewaongoza mpaka siku ya leo. Kisha Akaokoa binadamu na kuhudumu kama sadaka ya dhambi kwa binadamu. Mwishowe lazima bado ashinde binadamu, aokoe binadamu kabisa na kuwarejesha kwa mfano wao wa awali. Hii ndiyo kazi Amekuwa akifanya kutoka mwanzo hadi mwisho—kurejesha mwanadamu kwa sura yake halisi na kwa mfano wake wa awali. Ataanzisha ufalme Wake na kurejesha mfano wa awali wa mwanadamu, kumaanisha kwamba Atarejesha mamlaka Yake duniani na kurejesha mamlaka Yake miongoni mwa viumbe vyote. Mwanadamu alipoteza moyo wake wa kumcha Mungu baada ya kupotoshwa na Shetani na kupoteza kazi ambayo kiumbe mmoja wa Mungu anapaswa kuwa nayo, kuwa adui asiyemtii Mungu. Mwanadamu alimilikiwa na Shetani na kufuata amri za Shetani; hivyo Mungu hakuwa na njia ya kufanya kazi miongoni mwa viumbe Wake, na hakuweza zaidi kuwafanya viumbe Wake kumcha. Mwanadamu aliumbwa na Mungu, na anapaswa kumwabudu Mungu, lakini mwanadamu kwa kweli alimpuuza Mungu na kumwabudu Shetani. Shetani alikuwa sanamu katika moyo wa mwanadamu. Hivyo Mungu alipoteza nafasi yake katika moyo wa mwanadamu, kusema kwamba Alipoteza maana ya uumbaji Wake wa mwanadamu, na ili kurejesha maana ya uumbaji Wake wa mwanadamu lazima arejeshe mfano wa awali wa mwanadamu na kumtoa mwanadamu tabia yake potovu. Ili kumrejesha mwanadamu kutoka kwa Shetani, lazima Amwokoe mwanadamu kutoka kwa dhambi. Kwa njia hii tu ndiyo Anaweza kurejesha mfano wa awali wa mwanadamu polepole na kurejesha kazi halisi ya mwanadamu, na mwishowe kurejesha ufalme Wake. Maangamizo ya mwisho ya wale wana wa uasi pia yatafanywa ili kumruhusu mwanadamu kumwabudu Mungu vizuri zaidi na kuishi duniani vizuri zaidi. Kwa sababu Mungu alimuumba mwanadamu, Atamfanya mwanadamu amwabudu; kwa sababu Anataka kurejesha kazi halisi ya mwanadamu, Atairejesha kabisa, na bila ughushi wowote. Kurudisha mamlaka Yake kunamaanisha kumfanya mwanadamu amwabudu na kumfanya mwanadamu amtii; kunamaanisha kwamba Atamfanya mwanadamu aishi kwa sababu Yake na kufanya adui zake waangamie kwa sababu ya mamlaka Yake; kunamaanisha kwamba Atafanya kila sehemu Yake kuendelea miongoni mwa binadamu na bila upinzani wowote wa mwanadamu. Ufalme Anaotaka kuanzisha ni ufalme Wake Mwenyewe. Binadamu Anaotaka ni wale wanaomwabudu, wale wanaomtii kabisa na wana utukufu Wake. Asipookoa binadamu wapotovu, maana ya uumbaji Wake wa mwanadamu hautakuwa chochote; Hatakuwa na mamlaka yoyote miongoni mwa mwanadamu, na ufalme Wake hautaweza kuweko tena duniani. Asipoangamiza wale adui wasiomtii, Hataweza kupata utukufu Wake wote, wala Hataweza kuanzisha ufalme Wake duniani. Hizi ndizo ishara za ukamilishaji wa kazi Yake na ishara za ukamilishaji wa utimilifu Wake mkubwa; kuangamiza kabisa wale miongoni mwa binadamu wasiomtii, na kuwaleta wale waliokamilika rahani. Wakati binadamu wamerejeshwa katika mfano wake wa awali, wakati binadamu wanaweza kutimiza kazi yao husika, kuwa na nafasi zao wenyewe na kutii mipango yote ya Mungu, Mungu atakuwa amepata kundi la watu duniani wanaomwabudu, na Atakuwa pia Ameanzisha ufalme duniani unaomwabudu. Atakuwa na ushindi wa milele duniani, na wale wanaompinga wataangamia milele. Hii itarejesha nia Yake ya asili ya kumuumba mwanadamu; itarejesha nia Yake ya kuumba vitu vyote, na pia itarejesha mamlaka Yake duniani, mamlaka Yake miongoni mwa vitu vyote na mamlaka yake miongoni mwa adui Zake. Hizi ni ishara za ushindi Wake wote. Tangu sasa na kwendelea binadamu wataingia katika raha na kuingia katika maisha yafuatayo njia sahihi. Mungu pia ataingia katika raha ya milele na mwanadamu na kuingia katika maisha ya milele yanayoshirikisha Mungu na mwanadamu. Uchafu na kutotii duniani vitatoweka, na pia maombolezo duniani. Wote walio duniani wanaompinga Mungu hawatakuweko. Mungu na wale Aliowaokoa pekee ndio watabaki; viumbe Wake tu ndio watabaki.