Wale Wasiolingana na Kristo Hakika ni Wapinzani wa Mungu
Watu wote wanatamani kuona sura ya kweli ya Yesu, na wote wanatamani kuwa pamoja na Yeye. Sifikiri kwamba ndugu yeyote angesema kwamba hatamani kumwona au kuwa pamoja na Yesu. Kabla hamjamwona Yesu—kabla hamjamwona Mungu mwenye mwili—mnakuwa na mawazo ya kila aina, kwa mfano, kuhusu mwonekano wa Yesu, njia Yake ya kuzungumza, njia Yake ya kuishi, na kadhalika. Lakini punde tu mnapomwona Yeye kweli, mawazo yenu yatabadilika haraka. Kwa nini inakuwa hivi? Je, mngependa kujua? Kufikiri kwa mwanadamu hakuwezi kupuuzwa, jambo ambalo ni kweli—lakini zaidi ya hayo, kiini cha Kristo hakistahimili kubadilishwa na mwanadamu. Ninyi mnamfikiria Kristo kama mtu asiyekufa au mwenye hekima, lakini hakuna anayemchukulia Yeye kama mtu wa kawaida aliye na kiini cha uungu. Kwa hivyo, wengi wa wale wanaotamani sana mchana na usiku kumwona Mungu kwa kweli wako katika uadui na Mungu, na hawalingani na Yeye. Je, hili si kosa kwa upande wa mwanadamu? Hata sasa bado mnafikiri kwamba imani na uaminifu wenu vinatosha kuwafanya mstahili kuiona sura ya Kristo, lakini Ninawahimiza mjizatiti na mambo mengi zaidi yaliyo ya vitendo! Kwa maana katika wakati uliopita, wa sasa, na ujao, wengi wa wale wanaokutana na Kristo wameshindwa au watashindwa; wote wanatenda kama Mafarisayo. Sababu ya kushindwa kwenu ni ipi? Ni kwa sababu hasa kila mmoja wenu katika fikira zake ana mungu aliye mkuu na anayestahili kustaajabiwa. Lakini ukweli wa mambo si kama mwanadamu anavyotamani. Sio tu kwamba Kristo si mkuu, bali Yeye ni mdogo hasa; sio tu kwamba Yeye ni mtu, bali Yeye ni mtu wa kawaida; sio tu kwamba hawezi kupaa mbinguni, bali hawezi hata kutembea kwa uhuru duniani. Na hili likiwa hivi, watu wanamtendea Yeye kama wangemtendea mtu wa kawaida; wanamtendea Yeye bila heshima wanapokuwa na Yeye, na kuzungumza na Yeye kiholela, wakati huo wote bado wakisubiria kuja kwa “Kristo wa kweli.” Ninyi mnamchukulia Kristo ambaye tayari amekuja kama mtu wa kawaida, na maneno Yake kama ya mtu wa kawaida. Kwa sababu hii, hamjapokea chochote kutoka kwa Kristo, na badala yake mmefichua kabisa ubaya wenu wenyewe kwenye nuru.
Kabla ya kukutana na Kristo, unaweza kuamini kwamba tabia yako imebadilishwa kabisa, kwamba wewe ni mfuasi mwaminifu wa Kristo, na kwamba hakuna anayestahili zaidi kupokea baraka za Kristo kuliko wewe, kwa sababu umesafiri katika barabara nyingi, umefanya kazi nyingi, na kuzaa matunda mengi, na hivyo unafikiri kwamba mwishowe hakika utakuwa mmoja wa wale wanaopokea taji. Lakini, je, unajua ukweli ufuatao, ambao ni kwamba tabia potovu ya mwanadamu na uasi na upinzani wake hufichuliwa anapomwona Kristo, na kwamba wakati huu uasi na upinzani wake unafichuliwa kabisa na kwa ukamilifu zaidi kuliko wakati mwingine wowote? Ni kwa sababu Kristo ni Mwana wa Adamu—Mwana wa Adamu aliye na ubinadamu wa kawaida—ndiyo maana mwanadamu hamheshimu wala kumstahi Yeye. Ni kwa sababu Mungu anaishi katika mwili ndiyo maana uasi wa mwanadamu unaletwa katika nuru kwa kina sana na kwa maelezo dhahiri sana. Kwa hivyo Ninasema kwamba kuja kwa Kristo kumefichua uasi wote wa wanadamu na kuweka asili ya wanadamu wazi kabisa. Huku kunaitwa “kumshawishi simbamarara ashuke mlimani” na “kumshawishi mbwa mwitu atoke pangoni mwake.” Je, unathubutu kusema kwamba wewe ni mwaminifu kwa Mungu? Je, unathubutu kusema kwamba unaonyesha utii kamili kwa Mungu? Je, unathubutu kusema kwamba wewe si mwasi? Wengine watasema: “Wakati wowote Mungu anaponipangia mazingira, mimi silalamiki kamwe na kila mara ninaweza kutii, na zaidi ya hayo sina fikira zozote kuhusu Mungu.” Wengine watasema: “Chochote ambacho Mungu ananiagiza mimi hukikamilisha kadiri ya uwezo wangu na sifanyi kwa juujuu tu kamwe.” Katika hali hiyo, Ninawauliza ninyi hili: Je, mnaweza kulingana na Kristo mnapoishi na Yeye? Na mtalingana na Yeye kwa muda gani? Siku moja? Siku mbili? Saa moja? Saa mbili? Imani yenu bila shaka inaweza kuwa ya kupongezwa, lakini hamna ustahimilivu mwingi. Punde tu unapokuwa unaishi na Kristo kweli, kujihesabia haki kwako na kujikweza kwako kutafunuliwa kupitia maneno na matendo yako, kidogo kidogo, na vivyo hivyo matamanio yako ya kupita kiasi, mtazamo wako wa uasi na kutoridhika vitafichuliwa kiasili. Hatimaye, kiburi chako kitazidi kuwa kikubwa, hadi usipatane na Kristo kama yalivyo maji na moto, na kisha asili yako itafichuliwa kabisa. Wakati huo, fikira zako hazitaweza kufunikwa tena, malalamiko yako, pia, yatajitokeza kiasili, na ubinadamu wako wenye kudharauliwa utafichuliwa kabisa. Hata hivyo, hata wakati huo, bado utakataa kukubali uasi wako mwenyewe, ukiamini badala yake kwamba Kristo kama huyu si rahisi kwa mwanadamu kumkubali, kwamba Yeye anadai mengi mno kutoka kwa mwanadamu, na kwamba ungetii kikamilifu kama Angekuwa Kristo bora zaidi. Ninyi mnaamini kwamba uasi wenu unatetewa, kwamba ninyi humwasi Yeye tu Anapowasukuma mno. Hamjawahi kufikiria hata mara moja kwamba hamumchukulii Kristo kama Mungu, kwamba mnakosa nia ya kumtii Yeye. Badala yake, unasisitiza kwa ukaidi kwamba Kristo atende kulingana na matakwa yako mwenyewe, na punde tu Anapofanya jambo moja ambalo halikubaliani na namna yako mwenyewe ya kufikiri, unaamini kwamba Yeye si Mungu bali ni mtu. Je, si kuna wengi miongoni mwenu ambao wamebishana na Yeye kwa njia hii? Je, ni nani, hasa, ambaye ninyi mnamwamini? Na mnafuatilia kwa njia gani?
Ninyi hutamani kila mara kumwona Kristo, lakini Ninawahimiza msijikweze sana; mtu yeyote anaweza kumwona Kristo, lakini Ninasema hakuna anayestahili kumwona Kristo. Kwa sababu asili ya mwanadamu imejaa uovu, kiburi, na uasi, katika wakati unapomwona Kristo, asili yako itakuangamiza na kukuhukumu kifo. Kushirikiana kwako na ndugu (au dada) kunaweza kusifichue mengi kukuhusu, lakini si rahisi hivyo unaposhirikiana na Kristo. Wakati wowote, fikira zako zinaweza kukita mizizi, kiburi chako kikaanza kuchipua, na uasi wako ukazaa tini. Unawezaje wewe uliye na ubinadamu kama huo kustahili kushirikiana na Kristo? Je, unaweza kweli kumtendea Yeye kama Mungu kila wakati wa kila siku? Je, una uhalisi wa utii kwa Mungu kweli? Ninyi nyote mnamwabudu mungu aliye mkuu ndani ya mioyo yenu kama Yehova huku mkimchukulia Kristo anayeonekana kama mtu. Busara yenu ni duni mno na ubinadamu wenu ni wa chini mno! Hamna uwezo wa kumchukulia Kristo kama Mungu kila wakati; mara kwa mara tu, mnapokuwa na furaha, ndipo mnamshika na kumwabudu kama Mungu. Hii ndiyo maana Ninasema ninyi si waumini wa Mungu, bali ni kundi la washirika wanaompinga Kristo. Hata watu wanaoonyesha wema kwa wengine hulipwa, lakini Kristo, ambaye amefanya kazi kama hiyo miongoni mwenu, hajapokea upendo wa mwanadamu wala fidia wala utii wake. Je, hili si jambo la kuhuzunisha sana?
Inaweza kuwa kwamba katika miaka yako yote ya imani katika Mungu, hujawahi kumlaani yeyote au kutenda tendo baya, lakini katika kushirikiana kwako na Kristo, huwezi kusema ukweli, kutenda kwa uaminifu, au kutii neno la Kristo; katika hali hiyo, Ninasema kwamba wewe ni mtu mdanganyifu na mwenye kudhuru zaidi duniani. Unaweza kuwa mpole na aliyejitoa kwa namna ya kipekee kwa jamaa, marafiki, mke (au mume), wanao na mabinti wako, na wazazi wako, na usiwahi kuwatumia wengine vibaya, lakini ikiwa huwezi kulingana na Kristo, ikiwa huwezi kuingiliana na Yeye kwa upatano, basi hata kama utajitumia kikamilifu kutoa msaada kwa majirani wako au kuwatunza kwa uangalifu baba yako, mama yako, na washiriki wa nyumba yako, Ninasema kwamba wewe bado ni mtu mwovu, na zaidi ya hayo aliyejaa hila za ujanja. Usifikiri kwamba unalingana na Kristo kwa sababu tu unapatana na wengine au unafanya mambo machache mazuri. Je, unafikiri kwamba nia yako ya kutoa msaada inaweza kupata baraka za Mbinguni kwa hila? Je, unafikiri kwamba kufanya mambo machache mazuri ni mbadala wa utii wako? Hakuna hata mmoja wenu anayeweza kukubali kupogolewa, ninyi nyote mnaona ni vigumu kuukubali ubinadamu wa kawaida wa Kristo, na juu ya hili, mnatangaza utii wenu kwa Mungu daima. Imani kama yenu italeta malipo yanayostahili. Acheni kujiingiza katika mawazo potovu na kutamani kumwona Kristo, kwa maana ninyi ni wadogo mno katika kimo, kiasi kwamba hata hamstahili kumwona Yeye. Unapokuwa umetupa mbali uasi wako kabisa, na unapoweza kuingiliana kwa upatano na Kristo, wakati huo Mungu atajionyesha kwako kiasili. Ukienda kumwona Mungu bila kupitia upogoaji au hukumu, basi hakika utakuwa mpinzani wa Mungu na hakika utakuwa mlengwa wa maangamizo. Asili ya mwanadamu ni yenye uhasama kwa Mungu kiasili, kwa maana watu wote wamepitia upotovu mkubwa zaidi wa Shetani. Mwanadamu akijaribu kuingiliana na Mungu kutoka katikati ya upotovu wake mwenyewe, ni hakika kwamba hakuna jambo zuri linaloweza kutokana na hili; matendo na maneno yake hakika yatafunua upotovu wake kila wakati, na katika kushirikiana na Mungu uasi wake utafunuliwa kila wakati. Bila kujua, mwanadamu huja kumpinga Kristo, kumdanganya Kristo, na kumkataa Kristo; hili linapofanyika, mwanadamu atakuwa katika hali ya hatari zaidi na, hili likiendelea, atakuwa mlengwa wa kuadhibiwa.
Wengine wanaweza kuamini kwamba, ikiwa ushirikiano na Mungu ni hatari sana, basi inaweza kuwa jambo la hekima zaidi kumweka Mungu mbali. Watu kama hawa wanaweza kupata nini? Je, wanaweza kuwa waaminifu kwa Mungu? Hakika, ushirikiano na Mungu ni mgumu sana—lakini hiyo ni kwa sababu mwanadamu amepotoshwa, sio kwa sababu Mungu hawezi kushirikiana na yeye. Ingekuwa bora kwenu kutia bidii kiasi kwa ukweli wa kujijua. Kwa nini Mungu hawathamini ninyi? Kwa nini tabia yenu ni yenye kuchukiza Kwake? Kwa nini usemi wenu unaibua chuki Yake? Wakati ambapo mmeonyesha uaminifu kidogo, mnajisifu; mnapotoa mchango mdogo, mnadai thawabu; mnawadharau wengine mnapoonyesha utii kiasi, na mnamdharau Mungu mnapotimiza kazi fulani ndogo. Kwa kumkaribisha Mungu, mnaitisha pesa, vitu vya kimwili, na sifa. Mnaumia moyo kutoa sarafu mbili; mnapotoa kumi, mnaomba baraka na mnaomba kutofautishwa na wengine. Aina yenu ya ubinadamu inachukiza kabisa kuzungumziwa au kusikiwa. Je, kuna chochote kinachostahili sifa katika maneno na matendo yenu? Wale wanaotekeleza wajibu wao na wale wasiotekeleza; wale wanaoongoza na wale wanaofuata; wale wanaokuwa wenyeji wa Mungu na wale wasiokuwa; wale wanaotoa matoleo na wale wasiotoa; wale wanaohubiri na wale wanaopokea Neno, na kadhalika: watu wote kama hao hujisifu wenyewe. Je, hamwoni hili kuwa la kuchekesha? Mkijua fika kwamba mnamwamini Mungu, hata hivyo hamwezi kulingana na Mungu. Mkijua fika kwamba hamna sifa yoyote nzuri, bado mnasisitiza kujisifu. Je, hamhisi busara yenu imefikia hatua ambapo haiwezi kudhibitiwa? Mkiwa na busara kama hii, mnastahilije kukutana na Mungu? Je, hamna wasiwasi kujihusu wakati huu? Tabia yenu tayari imedhoofika hadi kufikia hatua ambapo hamwezi kulingana na Mungu. Hili likiwa hivi, je, imani yenu si ya kuchekesha? Je, imani yenu si ya upuuzi? Utakabilianaje na mustakabali wako? Utaichaguaje njia unayochukua?