75. Hili Jaribu Langu

Na Zhongxin, Uchina

Mwenyezi Mungu anasema, “Matendo Yangu ni mengi zaidi kwa kuhesabiwa kuliko chembechembe za changarawe kwenye ufuo na hekima Yangu kubwa zaidi kuliko ile ya watoto wote wa kiume wa Suleimani, ilhali binadamu wanafikiria kwamba Mimi ni daktari tu asiye na mengi kumhusu na mwalimu wa binadamu asiyejulikana! Ni wangapi wanaoniamini Mimi ili waweze tu kupata uponyaji? Ni wangapi wanaoniamini Mimi hili tu niweze kutumia nguvu Zangu kupunga roho chafu kutoka kwenye miili yao? Na ni wangapi wanaoniamini Mimi ili tu waweze kupokea amani na furaha kutoka Kwangu? Ni wangapi wanaoniamini Mimi ili kuhitaji kutoka Kwangu utajiri mwingi zaidi wa dunia, na ni wangapi wanaoniamini Mimi ili waweze kuishi maisha hayo kwa usalama na kuwa salama salimini katika maisha yajayo? Ni wangapi wanaoniamini Mimi ili waweze kuepuka tu mateso ya kuzimu na kupokea baraka za mbinguni? Ni wangapi wanaoniamini Mimi ili wapate tulizo lakini hawatafuti kupata chochote kutoka kwa ulimwengu ujao? Niliposhushia hasira Zangu binadamu na kuchukua furaha na amani yote aliyokuwa nayo mwanzo, binadamu akaanza kuwa na shaka. Nilipomkabidhi binadamu mateso ya kuzimu na kuchukua tena baraka za mbinguni, aibu ya binadamu iligeuka na kuwa hasira. Wakati binadamu aliponiomba Mimi kumponya, bado Sikumsikiza na aidha nilimchukia pakubwa, binadamu alienda mbali sana na Mimi na akatafuta njia za dawa ovu na uchawi. Nilipochukua kila kitu ambacho binadamu walitaka kutoka Kwangu, walitoweka bila kuonekana tena. Kwa hivyo, Ninasema kwamba mwnadamu ana imani Kwangu kwa sababu Nampa neema nyingi kupindukia, na mambo yapo mengi sana ya kupata(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Unajua Nini Kuhusu Imani?). Niliposoma haya hapo awali, nilisema tu kwamba kila kitu ambacho Mungu anasema hapa ni ukweli, lakini sikuwahi kuyaelewa kwa kweli. Nilidhani kwamba kwa kuwa nilikuwa nimemwamini Mungu kwa miaka mingi, nikaacha kazi na familia yangu, nikajitumia, na kuteseka sana kwa ajili ya wajibu wangu, majaribu yatakapokuja sitamlaumu Mungu au kumsaliti. Lakini nilipopitia jaribu la ugonjwa, nilimwelewa Mungu visivyo na kumlaumu. Motisha yangu ya kubarikiwa na kufanya mapatano na Mungu ilifunuliwa waziwazi. Wakati huo tu ndipo niliridhishwa kabisa kuhusu maneno ya Mungu ambayo huwafichua watu na maoni yangu juu ya ufuatiliaji katika imani yangu yalipitia mabadiliko.

Siku moja mnamo Julai 2018, nilipata uvimbe mdogo na mgumu kwenye titi langu la kushoto. Sikufikiria sana juu ya huo uvimbe na nikadhani kwamba dawa za kupambana na uvimbe zingeumaliza. Lakini katika miezi miwili iliyofuata, ulizidi tu kuwa mbaya. Nilitokwa na jasho usiku na sikuwa na nguvu, na eneo lililozunguka uvimbe ule liliuma sana. Nilianza kujiuliza iwapo kweli kulikuwa na tatizo, lakini nilijituliza tena kwa kufikiri kwamba halikuwa tatizo kubwa. Nilimwamini Mungu na nilikuwa na shughuli nyingi kila siku kanisani ya kufanya wajibu wangu. Nilifikiri kwamba Mungu angenilinda. Usiku mmoja, niliamshwa na maumivu makali. Uowevu wa manjano ulikuwa ukivuja kutoka katika titi langu, na nilijua kwamba kulikuwa na tatizo. Mimi na mume wangu tulikwenda hospitalini upesi ili likaguliwe. Matokeo yalirudi: Nilikuwa na saratani ya matiti. Moyo wangu ulipapa nilipomsikia daktari akisema hivyo. “Saratani ya matiti?” Niliwaza. “Nina umri wa miaka 30 tu! Hiyo inawezekanaje?” Niliendelea tu kujiambia, “Haiwezekani. Hii haiwezi kunifanyikia. Mimi ni muumini, na nimekuwa nikifanya wajibu wangu kanisani kwa miaka mingi. Mungu atanitunza na kunilinda. Hakika daktari amekosea.” Nilitumaini sana hiyo isiwe kweli. Hata sikumbuki jinsi nilivyofika nyumbani kutoka hospitalini siku hiyo. Mume wangu aliona jinsi nilivyoonekana kuchanganyikiwa na akajaribu kunifariji, akisema, “Hii ni hospitali ndogo na madaktari si stadi vile. Yawezekana kwamba wamekosea. Hebu twende katika hospitali kubwa ili uchunguzwe.” Niliona dalili ya matumaini aliposema hivyo. Kwa bahati mbaya, daktari katika hospitali kubwa alithibitisha kupatikana kwa ugonjwa ule: Ulikuwa saratani ya matiti. Alisema pia kwamba ilikuwa katika hatua ya katikati hadi ya mwisho, na kwamba sikuwa na budi kulazwa kwa ajili ya tibakemikali na upasuaji, vinginevyo huenda inifishe. Nilichanganyikiwa kabisa na kupigwa na butwaa. Niliwaza, “Je, haya yote yatagharimu kiasi gani cha fedha? Je, itakuwaje nikifa ninapokuwa nikipokea tibakemikali? Je, familia yangu itawezaje kukabiliana na deni hilo lote?” Nilikata tamaa na nikahisi kwamba sikujiweza kabisa.

Baada ya raundi yangu ya kwanza ya tibakemikali, mwili wangu wote ulijawa na maumivu. Sikutaka kufanya lolote na nilikuwa dhaifu kila wakati. Ilikuwa tu baada ya dawa hizo kuisha mwilini siku chache baadaye ndipo nilianza kupata nafuu. Nilikuwa nimemwamini Mungu kwa miaka mingi, nilikuwa nimejitolea na kujitumia kwa ajili ya wajibu wangu. Nilifanya wajibu wangu sikuzote, kwa heri na kwa shari, na sikukosa kamwe kuhudhuria mkutano wowote. Niliwasaidia ndugu zangu kutatua shida zao kila wakati. Nilikuwa nimetia bidii sana, na yote kwa sababu gani? Kwa nini Mungu hakuwa Akinilinda? Sasa sikuweza kufanya wajibu wowote. Nilichungulia kaburi. Je, Mungu alitaka kuniondoa? Nilipitia raundi nyingine tano za tibakemikali na kisha upasuaji. Je, nilipaswa kukabiliana vipi na hayo? Mbali na maumivu na mateso hayo yote, nikifa, hiyo itamaanisha kwamba miaka yangu yote ya kuwa na imani imekuwa bure? Nililia nilipofikiria hayo. Niliteseka sana katika siku hizo chache. Nilisoma maneno ya Mungu lakini sikuyaelewa kikamilifu, na nikaacha kuomba. Roho yangu ilikuwa na giza sana na nilizidi kuwa mbali na Mungu.

Siku moja, Dada Li kutoka kanisani alinitembelea na akaulizia hali yangu kwa huruma. Aliponiona nikiumia sana na nikiwa na huzuni sana, alinipa ushirika. Alisema, “Mungu huruhusu ugonjwa utupate na ni jaribu. Lazima tuombe na kutafuta zaidi na hakika Mungu atatuongoza kuelewa mapenzi Yake …” Kumsikia akisema neno “jaribu” kulichochea moyo wangu. Labda Mungu hakutaka kuniondoa bali Alitaka tu nipitie jaribu hili! Baada ya yeye kuondoka, nilikwenda mbele za Mungu kuomba, nikisema, “Mungu, nimekuwa nikiishi kwa uchungu tangu nilipougua, nikikuelewa visivyo na kukulaumu. Leo, dada yangu amenikumbusha kuwa hili ni jaribu Lako, lakini bado sijui jinsi ya kushinda hali hii. Tafadhali niongoze nijue mapenzi Yako.”

Baada ya hayo, nilienda mbele za Mungu na nikamwomba kwa namna hii kila siku. Siku moja, nilisoma maneno haya ya Mungu: “Kuingia katika majaribio hukuacha bila upendo au imani, huna sala, na huwezi kuimba nyimbo—na, bila kulitambua, katikati ya hili unakuja kujijua. Mungu ana njia nyingi za kumkamilisha mwanadamu. Yeye hutumia mazingira ya kila aina ili shughulikia tabia potovu ya mwanadamu, na hutumia vitu mbalimbali ili kumuweka mwanadamu wazi; katika suala moja Yeye humshughulikia mwanadamu, katika jingine Yeye humuweka mwanadamu wazi, na katika jingine Yeye humfichua mwanadamu, kuzichimbua na kuzifichua ‘siri’ katika vina vya moyo wa mwanadamu, na kumwonyesha mwanadamu asili yake kwa kuzifichua hali zake nyingi. Mungu humkamilisha mwanadamu kupitia mbinu nyingi—kupitia ufunuo, ushughulikiaji, usafishwaji, na kuadibu—ili mwanadamu aweze kujua kwamba Mungu ni wa vitendo(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Ni Wale Wanaolenga Kutenda tu Ndio Wanaoweza Kukamilishwa). Nilipokuwa nikitafakari maneno ya Mungu, nilianza kuelewa mapenzi Yake hatimaye. Mungu anafanya kazi katika siku za mwisho ili Awakamilishe watu kwa kufunua tabia zetu potovu kupitia hali za kila aina, na kwa kutumia hukumu na ufunuo wa maneno Yake kutufanya tuelewe tabia zetu za kishetani, tutafute na tutende ukweli, na mwishowe kufanya tabia zetu potovu zitakaswe na zibadilishwe. Nilielewa kwamba Mungu alikuwa Ameniruhusu niwe mgonjwa na haikuwa ili Aniondoe au kuniumiza kwa makusudi, bali ili Anitakase na kunibadilisha. Sikupaswa kumuelewa Mungu visivyo au kugaagaa tena. Ilibidi nitii, nitafute ukweli katika ugonjwa wangu, na kutafakari juu yangu mwenyewe na kujijua. Mara nilipoelewa mapenzi ya Mungu sikuhisi tena huzuni au kuwa na maumivu sana. Niliomba sala ya kumtii Mungu.

Na punde nilipomaliza, nilikumbuka mstari kutoka katika maneno ya Mungu: “Harakati yako ni kuishi kwa starehe, ili ajali isipate familia yako, ili upepo ukupite, ili uso wako usiguswe na changarawe….” Niliutafuta haraka katika kitabu changu cha maneno ya Mungu na nikapata kifungu hiki: “Unatumai kwamba imani yako kwa Mungu haitakuwa na changamoto ama dhiki, ama mateso yoyote. Unafuata vile vitu ambavyo havina maana, na huambatanishi faida yoyote kwa maisha, badala yake kuweka mawazo ya fujo kabla ya ukweli. Huna maana! … Unachofuata ni cha kukuwezesha kupata amani baada ya kumwamini Mungu—watoto wako wawe huru kutokana na magonjwa, ili mme wako apate kazi nzuri, ili mwana wako apate mke mwema, binti wako apate mme anayeheshimika, ili ndume na farasi wako walime shamba vizuri, kwa mwaka wa hali ya anga nzuri kwa mimea yako. Hili ndilo unalolitafuta. Harakati yako ni kuishi kwa starehe, ili ajali isipate familia yako, ili upepo ukupite, ili uso wako usiguswe na changarawe, ili mazao ya familia yako yasipate mafuriko, ili usiguswe na majanga yoyote, kuishi katika mikono ya Mungu, kuishi kwenye kiota chenye joto. Mwoga kama wewe, anafuata mwili kila wakati—je, una moyo, una roho? … Ukiendelea kuwa na uzoefu wa haya, je, si utakosa kupata chochote? Umepewa njia ya ukweli, lakini kama utaipata ama hapana inategemea na kutafuta kwako(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Matukio Aliyopitia Petro: Ufahamu Wake wa Adabu na Hukumu). Maneno ya Mungu yalifunua kwa usahihi tamaa yangu ya kubarikiwa katika imani yangu. Nilikumbuka miaka yangu yote ya kuwa na imani, wakati ambapo mambo yote yalikuwa sawa nyumbani, nilikuwa na afya, na kila kitu kilikuwa kizuri, nilikuwa nimejishughulisha kikamilifu na wajibu wangu na nilionekana kuwa na nguvu isiyoisha. Lakini mara nilipopata saratani, nilianza kuwa hasi na nilimwelewa Mungu visivyo, na kumlaumu kwa kutonilinda. Nilitumia kazi niliyokuwa nimefanya kwa manufaa yangu na kubishana na Mungu. Hata nilijutia miaka yangu yote ya kujitolea. Niliishi katika hali ya kujitenga na Mungu na kumsaliti. Ni wakati tu ambapo nilisafishwa na kufunuliwa kupitia kuwa ugonjwa ndipo niliona kwamba sikuwa nikifanya wajibu wangu wala kujitolea ili kufuatilia ukweli au kufanya wajibu wa kiumbe aliyeumbwa, lakini nilikuwa nikifanya mambo hayo ili nipate amani na baraka. Nilikuwa nikifanya mapatano na Mungu ili nibarikiwe kama malipo ya kujitolea kwangu. Nilitaka kila kitu katika maisha haya na uzima wa milele katika maisha yafuatayo. Sasa nilikuwa na saratani, na wakati ambapo ilionekana kama kwamba nitakufa na sitabarikiwa, nilimlaumu Mungu kwa kutokuwa wenye haki—sikuwa na ubinadamu hata kidogo. Nilifikiri juu ya miaka yangu yote ya kuwa na imani. Nilikuwa nimepokea neema na baraka nyingi sana kutoka kwa Mungu na nilikuwa nimenyunyiziwa na kudumishwa sana na ukweli. Mungu alikuwa Amenipa mengi sana, lakini sikuwahi kufikiria kulipa upendo Wake. Nilipougua, sikumtii Mungu hata kidogo. Nilimwelewa visivyo na kumlaumu tu. Sikuwa na dhamiri wala busara hata kidogo! Mwishowe nilielewa kuwa Mungu alikuwa Ameniruhusu niwe mgonjwa ili Afunue na kutakasa motisha yangu ya kubarikiwa katika imani yangu na maoni yangu mabaya juu ya ufuatiliaji, na kunifanya nilenge kufuatilia ukweli na kutafuta mabadiliko katika tabia yangu. Nilijuta sana na kujilaumu baada ya kuelewa nia njema za Mungu. Nilifanya azimio hili kwa ukimya: “Iwapo nitapata afueni au la, sitatarajia zaidi yasiyo ya maana kutoka kwa Mungu. Nataka tu kukabidhi maisha na kifo changu mikononi mwa Mungu na kutii mipango Yake.” Nilitulia sana baada ya hapo. Sikuona wasiwasi sana wala kuhangaika tena, na niliweza kujituliza ili kusoma maneno ya Mungu, kuomba, na kutafuta pamoja na Mungu.

Mara nilipotii, kupokea tena tibakemikali hakukuwa kuchungu kama awali. Ingawa bado nilihisi kichefuchefu kiasi, kila kitu kilikuwa sawa. Wagonjwa wengine walishangaa na walinionea wivu. Nilijua moyoni mwangu kwamba hii ilikuwa tu huruma na ulinzi wa Mungu. Nilimshukuru Mungu sana. Baada ya raundi kadhaa za tibakemikali, uvimbe ule wenye ukubwa sawa na yai ulikuwa umepungua. Haukuuma sana na titi halikuvuja tena. Daktari alisema kwamba niliendelea kupata afueni kwangu vizuri, na kwamba mambo yakiendelea hivyo basi baada ya raundi sita za tibakemikali huenda hata nisihitaji upasuaji. Nilifurahi sana niliposikia haya, na nikaendelea kumshukuru Mungu. Imani yangu katika Mungu ilizidi kuongezeka na nilidhani kwamba kama ningetafakari juu yangu mwenyewe na kujaribu kujijua kwa dhati basi labda ningepata nafuu bila kuhitaji upasuaji.

Siku moja mnamo Machi, nilipokea tibakemikali yangu ya mwisho. Nilikuwa na wasiwasi na pia matumaini. Ilipomalizika, daktari alisema kwamba bado nilihitaji upasuaji, kisha raundi nyingine mbili za tibakemikali, na kisha tibaredio. Nilipigwa na bumbuazi na nikachanganyikiwa. Niliwaza, “Hii inawezekanaje? Nimetafakari kama ninavyopaswa na kuelewa kile ninachopaswa kuelewa. Kwa nini sijapata nafuu sasa? Ni upasuaji mkubwa, na mbali na kupata makovu, tibakemikali na tibaredio nitakazohitaji zitakuwa chungu sana. Bado naweza kufa …” Nilizidi kuhisi huzuni na mwili wangu wote haukuwa na nguvu. Nilianza kulia kwa sababu ya udhalimu wa hayo yote. Usiku uliofuata upasuaji wangu, mara nusukaputi ilipoisha mwilini, maumivu yaliyotokana na mkato yalikuwa mabaya sana kiasi kwamba yalinifanya nilie. Sikuweza hata kupumua kwa kina sana. Nilihisi kwamba sikujiweza kabisa na nilikosewa sana, na nikaanza kumlaumu Mungu tena. Hali hii ilikuwa mbaya sana kwangu—maumivu yangeisha lini? Katika mateso yangu, nilisoma maneno haya ya Mungu: “Kwa watu wote, usafishaji ni wa kutesa sana na ni mgumu sana kukubali—ilhali ni katika usafishaji ndipo Mungu huweka wazi tabia Yake ya haki kwa mwanadamu, na Huweka hadharani mahitaji Yake kwa mwanadamu, na Hutoa nuru zaidi, na upogoaji na ushughulikiaji halisi zaidi; kwa kulinganisha mambo ya hakika na ukweli, Yeye humpa mwanadamu ufahamu mkubwa zaidi kujihusu na ukweli, na Humpa mwanadamu ufahamu mkubwa zaidi wa mapenzi ya Mungu, hivyo kumruhusu mwanadamu kuwa na upendo wa kweli zaidi na safi zaidi wa Mungu. Haya ndiyo malengo ya Mungu katika kutekeleza usafishaji. Kazi yote Afanyayo Mungu kwa mwanadamu ina malengo yake na maana yake; Mungu hafanyi kazi isiyo na maana, wala Hafanyi kazi isiyo na manufaa kwa mwanadamu. Usafishaji haumaanishi kuondoa watu kutoka mbele ya Mungu, wala haumaanishi kuwaangamiza katika kuzimu. Unamaanisha kubadilisha tabia ya mwanadamu wakati wa usafishaji, kubadilisha motisha zake, mitazamo yake ya kale, kubadilisha upendo wake kwa Mungu, na kubadilisha maisha yake yote. Usafishaji ni jaribio la kweli la mwanadamu, na aina ya mafunzo halisi na ni wakati wa usafishaji tu ndipo upendo wake unaweza kutimiza wajibu wake wa asili(“Kusudi la Kazi ya Mungu ya Usafishaji” Mfuateni Mwanakondoo na Kuimba Nyimbo Mpya). Kila neno la Mungu liliingia moyoni mwangu na niliguswa sana. Nilijua kwamba mapenzi ya Mungu katika kunisafisha kwa njia hii yalikuwa kunifanya nipate kujijua kidogo kwa kweli, kuniwezesha nitafute ukweli, na kufanya tabia zangu potovu zitakaswe na kubadilishwa. Hapo awali, ingawa nilitambua kwamba sikupaswa kufuatilia baraka katika imani yangu, sikuwa nimeachilia kikamilifu motisha yangu ya kubariki. Bado moyoni mwangu nilitaka mambo yaliyopita kiasi kutoka kwa Mungu. Nilidhani, kwa kuwa nilikuwa nimetafakari juu yangu na kujijua kidogo, Mungu alipaswa basi kuondoa ugonjwa wangu. Kutafakari juu yangu na kujijua kwangu kulitiwa doa na nia za kibinafsi na vilificha tu tamaa yangu ya kufanya mapatano na Mungu. Sikuwa nimetubu hata kidogo kwa kweli! Mungu alikuwa Amechunguza mawazo yangu na kutumia ugonjwa wangu kunifunua, kunifanya nitafakari juu yangu zaidi na kutubu kwa kweli. Huu ulikuwa upendo wa Mungu kwangu. Baadaye, nilimwomba Mungu, nikisema, “Mungu wangu, sasa ninaelewa mapenzi Yako. Natamani kuacha chaguo na matakwa yangu yote ya kibinafsi na kutafuta ukweli katika hali ambazo Umepanga. Tafadhali niongoze.”

Siku chache baadaye, nilisoma haya katika maneno ya Mungu: “Watu wanapoanza kumwamini Mungu, ni yupi kati yao asiyekuwa na nia, motisha na tabia yake binafsi ya makuu? Ingawa sehemu moja yao inaamini uwepo wa Mungu, na imeona uwepo wa Mungu, imani yao katika Mungu bado ina hiyo motisha, na nia yao kuu ya kumwamini Mungu ni kupokea baraka Zake na vitu wanavyotaka. … Kila mtu kila wakati hufanya hesabu kama hizi ndani ya moyo wake, na yeye hutoa madai yake kwa Mungu yanayoonyesha motisha yake, malengo na mawazo ya mabadilishano. Hii ni kusema, ndani ya moyo wake mwanadamu siku zote humweka Mungu majaribuni, siku zote anaunda njama kumhusu Mungu, akijitetea kwa Mungu kila wakati kwa sababu ya mwisho wake binafsi na kujaribu kumfanya Mungu atoe kauli, aweze kuona kama Mungu anaweza kumpa kile anachotaka au la. Wakati huohuo akimfuata Mungu, binadamu hamchukulii Mungu kama Mungu. Siku zote mwanadamu amejaribu kufanya mipango na Mungu, akitoa madai bila kusita kwake Yeye na hata akimsukuma Yeye katika kila hatua, akijaribu kupiga hatua ya maili licha ya kupewa inchi moja. Wakati huohuo akijaribu kufanya mabadilishano na Mungu, binadamu pia anabishana na Yeye, na wapo hata watu ambao, wakati majaribu yanawapata au wanapojipata katika hali ya kuteketea, mara nyingi wanakuwa wanyonge, wananyamaza na kuzembea katika kazi yao, na wanajaa malalamiko kumhusu Mungu. Tangu wakati ambapo mwanadamu alianza kumwamini Mungu, amemchukulia Mungu kama alama ya pembe inayoonyesha wingi wa neema, kisu cha Kijeshi cha Uswisi, na amejichukulia yeye mwenyewe kuwa mdaiwa mkubwa zaidi wa Mungu, ni kana kwamba kujaribu kupata baraka na ahadi kutoka kwa Mungu ni haki na jukumu lake la asili, huku jukumu la Mungu likiwa ni kumlinda na kumtunza mwananadamu na kumruzuku. Huu ndio ufahamu wa kimsingi wa ‘imani katika Mungu’ wa wale wote wanaomwamini Mungu, na ufahamu wao wa kina zaidi wa dhana ya imani katika Mungu. Kutoka katika kiini cha asili ya mwanadamu hadi katika ufuatiliaji wake wa kibinafsi, hakuna kitu chochote kinachohusiana na kumcha Mungu. Nia ya mwanadamu katika kumwamini Mungu huenda isiwe na uhusiano na kumwabudu Mungu. Hivi ni kusema kwamba, mwanadamu hajawahi kufikiria wala kuelewa kwamba imani katika Mungu inahitaji kumcha Mungu, na kumwabudu Mungu. Kwa mujibu wa haya yote, kiini cha mwanadamu kiko wazi. Kiini hiki ni kipi? Ni kwamba moyo wa mwanadamu ni mwovu, unaficha udanganyifu na ujanja, haupendi mambo ya kutopendelea na haki na kile kilicho chanya, nao ni wenye kustahili dharau na ulafi. Moyo wa mwanadamu umemfungia Mungu nje sana, hajampa Mungu moyo wake kabisa. Mungu hajawahi kuona moyo wa kweli wa mwanadamu, wala hajawahi kuabudiwa na mwanadamu(Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe II). Nilihisi aibu sana niliposoma haya. Maneno ya Mungu yalifichua kabisa hali yangu ya kweli. Nilikuwa nimemwamini Mungu kwa miaka mingi sana na nilitaka kila mara kubarikiwa, nikifanya mapatano na Mungu kila wakati. Nilihisi kwamba kwa kuwa nilimwamini Mungu na nilikuwa nikifanya wajibu wangu na kujitumia kanisani kila wakati, Mungu alipaswa kunitunza na kunilinda, na kunikinga dhidi ya magonjwa na madhara yote. Nilidhani kwamba hilo lilikuwa jambo lililofaa zaidi. Nilipogundua kwamba nilikuwa na saratani, nilianza kumlalamikia Mungu mara moja na nikataka kutumia miaka yangu ya kuteseka na kujitolea kwa faida yangu ili kubishana na Yeye. Nilipoanza kupata nafuu, nilisema “Asante Mungu” kwa kinywa changu, lakini moyoni mwangu, nilitaka mengi hata zaidi. Nilitaka Mungu auondoe ugonjwa wangu kabisa ili nisiteseke tena. Wakati ambapo tamaa yangu iliyopita kiasi haikutoshelezwa, asili yangu ya kishetani ilijitokeza tena, na kwa mara nyingine nilimlaumu Mungu na kujaribu kubishana na Yeye. Tabia yangu ilikuwa kama tu Mungu anavyofichua katika maneno Yake: “Wale wasiokuwa na ubinadamu, hawawezi kumpenda Mungu kwa kweli. Wakati mazingira ni mema na salama, au kama kuna faida inayoweza kupatwa, wao ni watiifu kabisa kwa Mungu, lakini wakati walilokuwa wanataka limepatikana au hatimaye kukataliwa, wanageuka mara moja. Hata kama ni kwa muda wa usiku mmoja tu, wao watatoka katika hali ya tabasamu, watu wenye ‘mioyo mikunjufu’ hadi wenye sura mbovu na wauaji wakatili, ghafla wakiwatendea wafadhili wao wa jana kana kwamba ni adui wa milele, bila chanzo wala sababu . Ikiwa mapepo haya hayatarushwa nje, mapepo haya ambayo yanaweza kuua bila kusita, je, hayatakuwa hatari iliyofichika?(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Kazi ya Mungu na Utendaji wa Mwanadamu). Nilivunjika moyo sana. Ingawa nilikuwa nimemwamini Mungu kwa miaka mingi, sikuwa nikimwabudu au kumtii kama nilivyopaswa. Badala yake, nilikuwa nikimchukulia kama daktari mwenye uwezo, kama kimbilio. Nilikuwa nikimtumia Mungu kufanikisha malengo yangu mwenyewe, nikijaribu kupata amani katika maisha haya na baraka za baadaye kutoka Kwake. Niliona kwamba imani yangu katika Mungu ilikuwa tu kufanya mapatano ya wazi kabisa na nilikuwa nikimtumia Mungu kupata neema na baraka kutoka Kwake. Je, sikuwa nikimdanganya na kumpinga Mungu? Niliona jinsi nilivyokuwa mbinafsi na mdanganyifu sana, bila ubinadamu hata kidogo, nikiishi kwa kudhihirisha tu tabia ya kisheteni. Hakika Mungu alinidharau na kunichukia!

Kisha nilisoma haya katika maneno ya Mungu: “Ayubu hakuzungumzia mabadilishano na Mungu, na wala hakutoa ombi lolote au madai yoyote kwa Mungu. Kulisifu kwake jina la Mungu kulikuwa kwa sababu ya nguvu kuu na mamlaka ya Mungu katika kutawala mambo yote, na haikutegemea kama alipata baraka au alipigwa na janga. Aliamini kwamba haijalishi kama Mungu anawabariki watu au analeta janga kwao, mamlaka na nguvu vyote havitabadilika, na hivyo, haikujalisha hali za mtu, jina la Mungu linafaa kusifiwa. Kwamba binadamu amebarikiwa na Mungu ni kwa sababu ya ukuu wa Mungu, na janga linapompata mwanadamu, hivyo, pia ni kwa sababu ya ukuu wa Mungu. Nguvu na mamlaka ya Mungu vyote vinatawala na kupangilia kila kitu kumhusu mwanadamu; matukio yasiyo ya kawaida kuhusu utajiri wa binadamu ni maonyesho ya nguvu na mamlaka ya Mungu, na licha ya maoni yake mtu, jina la Mungu linafaa kusifiwa. Haya ndiyo ambayo Ayubu alipitia na kuishia kujua katika miaka ya maisha yake. Fikira na matendo yote ya Ayubu vyote vilifikia masikio ya Mungu na vikawasili mbele ya Mungu, na vikaonekana kuwa muhimu na Mungu. Mungu aliyapenda sana maarifa haya ya Ayubu na akamthamini sana Ayubu kwa kuwa na moyo kama huo. Moyo huu ulisubiria amri ya Mungu siku zote, na pahali pote, na haijalishi ni muda au mahali gani palipokaribisha chochote kile kilichomsibu. Ayubu hakutoa mahitaji yoyote kwa Mungu. Kile alichohitaji kutoka kwake kilikuwa kusubiria, kukubali, kukabiliana na kutii mipangilio yote iliyotoka kwa Mungu; Ayubu aliamini hili kuwa wajibu wake, na ndicho hasa kile ambacho Mungu Alitaka(Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe II). Niliguswa sana nilipotafakari maneno ya Mungu. Niliwaza, “Mungu ndiye Muumba. Mungu anaweza kutupa neema na baraka, na Anaweza kutuhukumu, kutuadibu, kutujaribu na kutusafisha. Je, Mungu hawezi kutupa majaribu kwa sababu tu Anatupenda?” Nilimkumbuka Ayubu. Mungu alimpa utajiri mkubwa na alimshukuru na kumsifu Mungu, lakini hakutamani utajiri yakinifu. Mungu alipochukua kila kitu kutoka kwake, bado aliweza kutukuza jina la Mungu hadi mwisho wa jaribu lake, akisema, “Tupokee mema kutoka mkononi mwa Mungu, nasi tusipokee mabaya?” (Ayubu 2:10). Ayubu alijua kwamba kila kitu alichokuwa nacho kilitoka kwa Mungu na kwamba Mungu alikuwa mwenye haki, iwe kwamba Mungu alimpa vitu au kuvichukua. Imani ya Ayubu katika Mungu haikutiwa doa na nia za binafsi na hakufikiria iwapo atabarikiwa au kukabiliwa na maafa. Hakulalamika bila kujali Mungu alifanya nini. Aliweza kuchukua nafasi yake kama kiumbe aliyeumbwa kumwabudu na kumtii Mungu. Nilipoona ubinadamu na mantiki ya Ayubu, nilihisi aibu sana. Niliangalia kila kitu nilichokuwa nacho. Mungu alikuwa Amenipa vyote, hata pumzi yangu. Lakini sikuwa nimeshukuru hata kidogo, badala yake nilimlaumu Mungu nilipokuwa mgonjwa. Sikuwa na dhamiri au mantiki hata kidogo! Nilimwamini Mungu lakini sikumjua, na sikujua nafasi yangu sahihi mbele Yake au jinsi nilivyopaswa kumtii Muumba. Nilipomwamini Mungu kwa fikira, mawazo, na nia zangu kuhusu kufanya mapatano, nilimlalamikia Mungu na kumpinga wakati wa majaribu. Hata hivyo, nilitaka baraka na neema kutoka kwa Mungu kila wakati, na nilitaka kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa kweli sikuwa na aibu! Niliona kwamba, hata kama ningekufa wakati huo, hiyo ingekuwa haki ya Mungu kwa ajili ya uasi na upotovu wangu. Nilipata njia ya utendaji katika uzoefu wa Ayubu. Bila kujali ningekuwa mgonjwa kwa muda gani, au iwapo ningepata nafuu au la, nilitamani tu kutii utawala na mipango ya Mungu. Hii ndiyo mantiki niliyopaswa kuwa nayo kama kiumbe aliyeumbwa. Wazo hili liliniletea hisia nzuri ya kuachiwa huru.

Kufumba na kufumbua, wakati wa tibaredio uliwadia. Wagonjwa wengine wa saratani walisema kwamba tibaredio ilisababishia mwili dhiki nyingi na kwamba itauchoma mwili wangu. Walisema kwamba nitapata kizunguzungu na kuwa na kichefuchefu kila wakati, na kwamba sitaweza kuonja chochote. Niliposikia haya yote, nilianza kumwomba Mungu anisaidie kukwepa hali hii tena, lakini niligundua haraka kuwa hali yangu haikuwa sahihi na nikamwomba Mungu. Kisha nilikumbuka baadhi ya mistari kutoka kwa wimbo wa maneno ya Mungu: “Kwa kuwa uliumbwa, unapaswa kumtii Bwana aliyekuumba, kwa kuwa wewe huna mamlaka kiasili juu yako mwenyewe, na huna uwezo wa kudhibiti hatima yako. Kwa kuwa wewe ni mtu ambaye anamwamini Mungu, inapaswa utafute utakatifu na mabadiliko(Mfuateni Mwanakondoo na Kuimba Nyimbo Mpya). Nilijua kwamba ni Mungu aliyekuwa akinijaribu katika hali hii na kwamba sikupaswa kumwomba Mungu vitu au kumuumiza tena kipumbavu. Nilijua kwamba sikuwa na budi kutii mipango Yake. Mara nilipotii, ingawa ilibidi nipate tibaredio kila siku na sehemu fulani za mwili wangu ziliuma, haikuwa mbaya kama wagonjwa wengine walivyokuwa wamesema. Nilijua kwamba ni Mungu aliyekuwa Akinihurumia na kunijali. Nilipomaliza tibaredio yangu, mwili wangu ulipata nafuu haraka sana. Nilionekana mwenye afya na nilihisi vizuri sana. Ndugu zangu kanisani walisema kwamba sikuonekana kama mgonjwa wa saratani hata kidogo. Wakati fulani baadaye, nilianza kufanya wajibu wangu tena. Imani yangu katika Mungu iliongezeka kupitia tukio hili na nilianza kuthamini fursa ya kufanya wajibu wangu hata zaidi.

Miaka hii miwili imepita upesi, lakini kila ninapokumbuka ile miezi kumi ambapo nilikuwa mgonjwa, nahisi kama kwamba hilo lilitokea jana tu. Ingawa mwili wangu uliteseka kidogo, nilikuja kuelewa motisha yangu ya baraka na maoni yangu yenye makosa kuhusu kile cha kufuatilia. Najua sasa kwamba sina budi kufuatilia ukweli na kutafuta kumtii Mungu katika imani yangu. Iwe ninabarikiwa au kukumbana na maafa, ni sharti nitii utaratibu, sheria, na mipango ya Mungu kila wakati. Kiumbe aliyeumbwa anapaswa kuwa na hisia hii ya mantiki. Kila kitu maishani kingekwenda vizuri, kamwe singepata haya yote. Huu ni utajiri wa maisha ambao Mungu amenipa. Shukrani kwa Mwenyezi Mungu!

Iliyotangulia: 73. Wokovu wa Mungu

Inayofuata: 80. Kutumikia Wakati wa Upeo wa Ujana Gerezani

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Maudhui Yanayohusiana

68. Ulinzi wa Mungu

Mwenyezi Mungu anasema: “Watu hawawezi kubadilisha tabia yao wenyewe; lazima wapitie hukumu na kuadibu, mateso na usafishaji wa maneno ya...

40. Tiba ya Wivu

Na Xunqiu, UchinaMwenyezi Mungu anasema, “Mwili wa mwanadamu ni wa Shetani, umejaa tabia za uasi, ni mchafu kiasi cha kusikitisha, na ni...

32. Roho Yangu Yakombolewa

Na Mibu, Uhispania“Katika maisha yake, kama mwanadamu anatamani kutakaswa na kufikia mabadiliko katika tabia yake, kama anatamani kuishi...

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp