Maono ya Kazi ya Mungu (3)

Mara ya kwanza ambapo Mungu alipata mwili ilikuwa kupitia kutungwa mimba kwa Roho Mtakatifu, na hili lilikuwa muhimu kwa kazi Aliyokusudia kufanya. Enzi ya Neema ilianza na Jina la Yesu. Wakati Yesu Alianza kufanya huduma Yake, Roho Mtakatifu Alianza kutoa ushuhuda kwa jina la Yesu, na jina la Yehova halikuzungumziwa tena, na badala yake Roho Mtakatifu Alianza kazi mpya hasa kwa jina la Yesu. Ushuhuda wa wale waliomwamini Yeye ulitolewa kwa ajili ya Yesu Kristo, na kazi waliyoifanya walifanya pia kwa ajili ya Yesu Kristo. Hitimisho Enzi ya Sheria ya Agano la Kale lilimaanisha kuwa kazi iliyofanywa hasa kutumia jina la Yehova ilikuwa imefikia kikomo. Baada ya hii, jina la Mungu halikuwa Yehova tena; badala yake Yeye Aliitwa Yesu, na kutoka hapa Roho Mtakatifu Alianza kazi hasa kwa kutumia jina la Yesu. Kwa hiyo leo, watu ambao leo bado hula na kunywa maneno ya Yehova, na bado hutumia kazi ya Enzi ya Sheria—je, hufuati masharti bila kufikiria? Je! Hujakwama katika siku za zamani? Leo, unajua kwamba siku za mwisho zimefika. Wakati Yesu atakapokuja, bado Ataitwa Yesu? Yehova aliwaambia watu wa Israeli kwamba Masihi angekuja, lakini alipofika, hakuitwa Masihi bali Yesu. Yesu alisema kwamba Angekuja tena, na kwamba Angekuja kama Alivyoondoka. Haya yalikuwa maneno ya Yesu, lakini je, ulishuhudia jinsi Yesu alivyoondoka? Yesu aliondoka akiwa juu ya wingu jeupe, lakini je, Yeye Mwenyewe angerudi kati ya binadamu juu ya wingu jeupe? Ingekuwa hivyo, je, si bado angeitwa Yesu? Wakati Yesu Atakuja tena, enzi itakuwa tayari imebadilika, je, hivyo bado Ataweza kuitwa Yesu? Je, Mungu Anajulikana tu kwa jina la Yesu? Je, hangeweza kuitwa kwa jina jipya katika enzi mpya? Je, sura ya mtu mmoja na hasa jina moja vinaweza kumwakilisha Mungu katika ukamilifu wake? Katika kila enzi, Mungu Anafanya kazi mpya na huitwa kwa jina jipya; Je, anawezaje kufanya kazi sawa katika enzi tofauti? Itakuwaje Yeye kugandamana na yale ya zamani? Jina la Yesu lilichukuliwa kuwa la kazi ya ukombozi, hivyo bado Yeye Anaweza kuitwa kwa jina moja wakati Atarudi katika siku za mwisho? Je, bado Yeye Atafanya kazi ya ukombozi? Ni kwa nini Yehova na Yesu ni kitu kimoja, ilhali wanaitwa kwa majina tofauti katika enzi hizi tofauti? Je, si kwa sababu enzi za kazi Yao ni tofauti? Jina moja linawezaje kumwakilisha Mungu kwa ukamilifu wake? Kwa njia hii, lazima Mungu aitwe kwa jina tofauti katika enzi tofauti, lazima Atumie jina kubadilisha enzi na kuwakilisha hiyo enzi, kwa kuwa hakuna jina moja linaweza kumwakilisha Mungu mwenyewe kikamilifu. Na kila jina linaweza tu kuwakilisha kipengele cha wakati cha tabia ya Mungu katika enzi fulani; yote linahitaji kufanya ni kuwakilisha kazi Yake. Kwa hivyo, Mungu Anaweza kuchagua jina lolote ambalo linafaa tabia yake kuwakilisha enzi nzima. Bila kujali iwapo ni enzi ya Yehova, au ni enzi ya Yesu, kila enzi inawakilishwa kwa jina. Baada ya Enzi ya Neema, enzi ya mwisho imewadia na Yesu Amekwisha kuja. Itakuwaje awe bado anaitwa Yesu? Itakuwaje awe bado anachukua umbo la Yesu miongoni mwa watu? Je, umesahau kuwa Yesu Alikuwa tu sura ya Mnazareti? Je, umesahau kuwa Yesu Alikuwa tu mkombozi wa wanadamu? Itakuwaje achukue kazi ya kushinda na kurekebisha mwanadamu katika siku za mwisho? Yesu aliondoka akiwa juu ya wingu jeupe, huu ni ukweli, lakini Angewezaje kurudi juu ya wingu jeupe kati ya wanadamu na bado aitwe Yesu? Ikiwa Yeye kweli alikuja juu ya wingu, si Angetambuliwa na mwanadamu? Je, si watu ulimwenguni kote wangemtambua Yeye? Katika hali hiyo, je, si Yesu peke Yake ndiye angekuwa Mungu? Katika hali hiyo, sura ya Mungu ingekuwa ni sura ya Myahudi, na ingekuwa vilevile milele. Yesu alisema kwamba Angewasili kama Alivyoondoka, lakini unajua maana halisi ya maneno Yake? Je, angeweza kwa kweli kuwaambia ninyi kundi la watu? Unajua tu kwamba Atawasili kama Alivyoondoka juu ya wingu, lakini unajua hasa jinsi Mungu Mwenyewe hufanya kazi Yake? Ikiwa ungeweza kuona kweli, basi maneno ya Yesu yanapaswa kuelezwa vipi? Alisema: Wakati Mwana wa Adamu atakapokuja katika siku za mwisho, Yeye Mwenyewe hatajua, malaika hawatajua, wajumbe wa mbinguni hawatajua, na watu wote hawatajua. Baba tu ndiye atakayejua, yaani, Roho pekee ndiye atajua Hata Mwana wa Adamu Mwenyewe hajui, lakini wewe unaweza kuona na kujua? Ikiwa ungekuwa na uwezo wa kujua na kuona kwa macho yako mwenyewe, je, si maneno haya yatakuwa yalisemwa bure? Na Yesu alisema nini wakati huo? “Lakini juu ya hiyo siku na saa hiyo hakuna mtu anayejua, wala malaika wa mbinguni, isipokuwa Baba yangu tu. Lakini kama jinsi zilivyokuwa zile siku za Nuhu, ndivyo pia kuja kwa Mwana wa Adamu kutakuwa. … Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo atakapokuja Mwana wa Adamu.” Wakati siku hiyo itakapofika, Mwana wa Adamu Mwenyewe hataijua. Mwana wa Adamu inahusu umbo la Mungu lililopata mwili wa Mungu, ambaye atakuwa mtu wa kawaida. Hata Mwana wa Adamu mwenyewe hajui, kwa hiyo wewe ungejuaje? Yesu alisema kwamba Angewasili kama Alivyoondoka. Wakati Atakapowasili, hata Yeye Mwenyewe hajui, kwa hiyo Angekujulisha mapema? Je, unaweza kuona kuwasili kwake? Je, huo sio utani? Kila wakati ambao Mungu Atawasili hapa duniani, Yeye Atabadilisha jina lake, jinsia yake, mfano wake, na kazi yake; Yeye harudii kazi yake, na Yeye daima yu mpya na kamwe si wa zamani. Wakati Alikuja hapo awali, Aliitwa Yesu; Je, anaweza bado kuitwa Yesu anapokuja tena wakati huu? Alipokuja hapo awali, Alikuwa wa kiume, Ataweza kuwa wa kiume tena wakati huu? Kazi Yake Alipokuja wakati wa Enzi ya Neema ilikuwa ya kusulubishwa msalabani; Atakapokuja tena, je, bado Atawakomboa wanadamu kutoka kwenye dhambi? Je, bado Atasulubishwa msalabani? Je, huko hakutakuwa kurudia kazi Yake? Je, hukujua kwamba Mungu daima ni mpya na kamwe si wa zamani? Kuna wale ambao wanasema kuwa Mungu habadiliki. Hiyo ni sahihi, lakini inaashiria kutobadilika kwa tabia ya Mungu na kiini Chake. Mabadiliko ya jina lake na kazi hayathibitishi ya kuwa kiini chake kimebadilika; kwa maneno mengine, Mungu siku zote Atakuwa Mungu, na hii kamwe haitabadilika. Iwapo utasema kuwa kazi ya Mungu daima inabaki vile vile, basi Angekuwa na uwezo wa kumaliza mpango wake wa usimamizi wa miaka elfu sita? Wewe hujua tu kwamba Mungu habadiliki milele, lakini je, unajua kuwa Mungu ni mpya milele na kamwe si wa zamani? Kama kazi ya Mungu kamwe haikubadilika, basi Angeweza kulea mwanadamu hadi leo? Kama Mungu habadiliki, basi mbona Yeye tayari Amefanya kazi ya nyakati mbili? Kazi yake daima inaendelea mbele, na hivyo pia ndivyo tabia yake inafichuliwa kwa binadamu hatua kwa hatua, na kile ambacho kinafichuliwa ni tabia yake ya asilia. Hapo mwanzo, tabia ya Mungu ilikuwa siri kwa mwanadamu, na kamwe Yeye hadharani hakumfichulia mwanadamu tabia yake, na mwanadamu hakuwa na ufahamu kuhusu Yeye, na hivyo hatua kwa hatua Alitumia kazi Yake kumfichulia mwanadamu tabia Yake, lakini hii haina maana kuwa tabia Yake inabadilika katika kila enzi. Sio kweli kuwa tabia ya Mungu kila wakati inabadilika kwa ajili mapenzi Yake daima hubadilika. Bali, kwa kuwa enzi za kazi Yake ni tofauti, asili ya tabia Yake kwa ujumla hufichuliwa kwa binadamu hatua kwa hatua, ili mwanadamu aweze kumjua Yeye. Lakini hii si kwa njia yoyote ushahidi kuwa Mungu hapo awali hakuwa na tabia fulani na tabia Yake imebadilika hatua kwa hatua kwenye enzi zinazopita—ufahamu kama huo ni wenye kosa. Mungu humfichulia mwanadamu tabia yake fulani ya asili, kile Alicho, kwa mujibu wa enzi zinazopita. Kazi ya enzi moja haiwezi kueleza tabia nzima ya Mungu. Na kwa hivyo, maneno haya “Mungu daima ni mpya na kamwe si wa zamani” yanarejelea kazi yake, na maneno haya “Mungu habadiliki” kinarejelea kile ambacho Mungu anacho na alicho kiasili. Bila kujali, huwezi kubaini kazi ya miaka elfu sita kwa mtazamo mmoja, ama kwa kuielezea tu kwa maneno ambayo hayabadiliki. Huo ni ujinga wa mwanadamu. Mungu si wazi kama mwanadamu anavyofikiria, na kazi yake haitasimama katika enzi moja. Yehova, kwa mfano, haliwezi daima kusimamia jina la Mungu; Mungu pia hufanya kazi yake kwa kutumia Jina la Yesu, ambayo ni ishara ya vile ambavyo kazi ya Mungu daima husonga kwenda mbele.

Mungu siku zote huwa Mungu, na kamwe Yeye hatakuwa Shetani; Shetani daima ni Shetani, na yeye hawezi kuwa Mungu. Hekima ya Mungu, ajabu ya Mungu, haki ya Mungu, na adhama ya Mungu kamwe hayatabadilika. Kiini chake na anachomiliki na kile Anacho na alicho kamwe hakitabadilika. Kazi yake, hata hivyo, daima inaendelea mbele, daima inaenda ndani zaidi, kwa kuwa Mungu daima ni mpya na kamwe si wa zamani. Katika kila enzi Mungu huchukua jina jipya, katika kila enzi anafanya kazi mpya, na katika kila enzi Yeye huwaruhusu viumbe Wake kuona mapenzi Yake mapya na tabia Yake mpya. Ikiwa watu hawaoni dhihirisho la tabia mpya ya Mungu katika enzi mpya, wao si watamsulubisha msalabani milele? Na kwa kufanya hivyo, si watakuwa wamebaini Mungu? Ikiwa Angepata mwili tu kama mume, watu wangemfafanua kama mume, kama Mungu wa wanaume, na kamwe hawangemwamini kuwa Mungu wa wanawake. Kisha, wanaume wangeamini kwamba Mungu ni wa jinsia sawa na wanaume, kwamba Mungu ni kichwa cha wanaume na je, wanawake? Hii si haki; je, huu sio utendeaji wa upendeleo? Ikiwa ingekuwa hivi, basi wale wote ambao Mungu aliwaokoa wangekuwa wanaume kama Yeye, na hakungekuwa na wokovu wa wanawake. Wakati ambapo Mungu aliumba wanadamu, Alimuumba Adamu na Akamuumba Hawa. Hakumuumba tu Adamu, lakini Aliwafanya wote mume na mke kwa mfano Wake. Mungu sio tu Mungu wa wanaume—Yeye pia ni Mungu wa wanawake. Mungu anafanya kazi mpya katika siku za mwisho. Atafichua tabia Yake zaidi, na haitakuwa huruma na upendo wa wakati wa Yesu. Kwa kuwa Ana kazi mpya, kazi hii mpya itaandamana na tabia mpya. Kwa hiyo kama kazi hii ingefanywa na Roho—kama Mungu hangepata mwili, na badala yake Roho angenena moja kwa moja kupitia radi ili mwanadamu hangekuwa na njia ya kuwasiliana na Yeye, je, mwanadamu angejua tabia yake? Kama Roho tu Angefanya kazi, basi mtu hangekuwa na njia yoyote ya kujua tabia Yake. Watu wanaweza tu kuona tabia ya Mungu kwa macho yao wenyewe wakati Anapopata mwili, wakati ambapo Neno laonekana katika mwili, na Anaonyesha tabia Yake yote kupitia mwili. Mungu kweli huishi kati ya wanadamu. Anaonekana; mwanadamu anaweza kweli kujihusisha na tabia Yake na kile Anacho na Alicho; ni kwa njia hii tu ndiyo mwanadamu anaweza kumjua kweli. Wakati huo huo, Mungu pia Amekamilisha kazi ya Mungu kuwa Mungu wa wanaume na wanawake, na Ametimiza ukamilifu wa kazi Yake katika mwili. Mungu harudii kazi yake katika kila enzi mpya. Kwa kuwa siku za mwisho zimewadia, Yeye Atafanya kazi ya siku za mwisho na kufichua tabia yake yote siku za mwisho. Siku za mwisho ni enzi tofauti, enzi ambayo Yesu Alisema lazima mteseke kwa maafa, na ukabiliwe na mitetemeko ya ardhi, njaa, na baa, ambavyo vitaonyesha kuwa hii ni enzi mpya, na sio tena Enzi ya Neema ya zamani. Kama, watu wanavyosema, Mungu daima habadiliki, tabia yake daima ni ya huruma na ya upendo, kwamba Yeye anampenda mwanadamu jinsi Anavyojipenda, na Anampa kila mwanadamu wokovu na kamwe hamchukii mwanadamu, basi Angekuwa na uwezo wa kukamilisha kazi yake? Wakati Yesu Alikuja, Alisulubishwa msalabani, na Yeye Alijitoa kama sadaka kwa sababu ya wote wenye dhambi na kwa kujitoa Yeye mwenyewe madhabahuni. Yeye tayari Alikuwa Amemaliza kazi ya ukombozi na tayari Alikuwa Ametamatisha Enzi ya Neema, na hivyo ni nini kiini cha kurudia kazi ya enzi hiyo katika siku za mwisho? Je, kufanya kitu kimoja haitakuwa kukana kazi ya Yesu? Iwapo Mungu hatafanya kazi ya kusulubiwa awamu hii itakapofika, lakini Yeye Asalie mwenye mapenzi na Mungu wa huruma, je, anaweza kufikisha enzi hii mwisho? Je, Mungu mwenye upendo na mwenye huruma, si Angeweza kuhitimisha enzi hii? Katika kazi yake ya kuhitimisha enzi, tabia ya Mungu ni ile ya kuadibu na hukumu, ambayo inafichua yote ambayo si ya haki, na kuhukumu wanadamu hadharani, na kukamilisha wale ambao wanampenda kwa ukweli. Ni tabia tu kama hii ndiyo ambayo inaweza kufikisha enzi hii mwisho. Siku za mwisho tayari zimewadia. Kila kitu kitatengashwa kulingana na aina, na kitagawanywa katika makundi tofauti kulingana na asili yake. Huu ni wakati ambapo Mungu Atafichua matokeo na hatima ya binadamu. Kama mwanadamu hatashuhudia kuadibu na hukumu yake, basi hakutakuwepo na mbinu ya kufichua uasi na udhalimu wao mwanadamu. Ni kwa njia ya kuadibu na hukumu ndipo mwisho wa mambo yote yatafunuliwa. Mwanadamu huonyesha tu ukweli ulio ndani yake anapoadibiwa na kuhukumiwa. Mabaya yataekwa na mabaya, mema na mema, na wanadamu watatenganishwa kulingana na aina. Kupitia kuadibu na hukumu, mwisho wa mambo yote utafichuliwa, ili mabaya yaadhibiwe na mazuri yatunukiwe zawadi, na watu wote watakuwa wakunyenyekea chini ya utawala wa Mungu. Kazi hii yote inapaswa kutimizwa kupitia kuadibu kwa haki adhibu na hukumu. Kwa sababu upotovu wa mwanadamu umefika upeo wake na uasi wake umekua mbaya mno, ni haki ya tabia ya Mungu tu, ambayo hasa ni ya kuadibu na hukumu, na imefichuliwa kwa kipindi cha siku za mwisho, inayoweza kubadilisha na kukamilisha mwanadamu. Ni tabia hii pekee ambayo itafichua maovu na hivyo kuwaadhibu watu wote dhalimu. Kwa hivyo, tabia kama hii imejazwa umuhimu wa enzi, na ufunuo na maonyesho ya tabia yake ni kwa ajili ya kazi ya kila enzi mpya. Mungu hafichui tabia yake kiholela na bila umuhimu. Kama, wakati wa mwisho wa mwanadamu umefichuliwa katika kipindi cha siku za mwisho, Mungu bado anamfadhili binadamu kwa huruma na upendo usioisha, kama yeye bado ni wa kupenda mwanadamu, na kutompitisha mwanadamu katika hukumu ya haki, bali anamwonyesha stahamala, uvumilivu, na msamaha, kama bado Yeye anamsamehe mwanadamu bila kujali ubaya wa makosa anayofanya, bila hukumu yoyote ya haki: basi usimamizi wa Mungu ungetamatishwa lini? Ni wakati gani tabia kama hii itaweza kuwaongoza wanadamu katika hatima inayofaa? Chukua, kwa mfano, hakimu ambaye daima ni mwenye upendo, mwenye roho safi na mpole. Anawapenda watu bila kujali dhambi wanazozifanya, na ni mwenye upendo na stahamala kwa watu bila kujali hao ni nani. Kisha ni lini ambapo ataweza kufikia uamuzi wa haki? Katika siku za mwisho, ni hukumu ya haki tu inaweza kumtenganisha mwanadamu kulingana na aina yake na kumleta mwanadamu katika ufalme mpya. Kwa njia hii, enzi nzima inafikishwa mwisho kupitia kwa tabia ya Mungu iliyo ya haki ya hukumu na kuadibu.

Kazi ya Mungu kokote katika usimamizi wake ni wazi kabisa: Enzi ya Neema ni Enzi ya Neema, na siku za mwisho ni siku za mwisho. Kuna tofauti baina ya kila enzi, kwa kuwa katika kila enzi Mungu Anafanya kazi ambayo inawakilisha enzi hiyo. Ili kazi ya siku za mwisho iweze kufanywa, lazima kuwe na kuungua, hukumu, kuadibu, ghadhabu, na uharibifu wa kuleta enzi kwenye kikomo. Siku za mwisho zinaashiria enzi ya mwisho. Wakati wa enzi ya mwisho, je, Mungu si Ataleta enzi kwenye kikomo? Na ni kwa njia tu ya kuadibu na hukumu ndio inaweza kuleta enzi kwenye kikomo. Ni kwa njia hii tu ndiyo Anaweza kuitamatisha enzi hiyo. Madhumuni ya Yesu yalikuwa kwamba mwanadamu aweze kuendelea kuwepo, kuishi, na kuweza kuwepo kwa njia bora zaidi. Alimwokoa mwanadamu kutoka kwa dhambi ili mwanadamu akome upotovu wa kudumu na kamwe asiishi katika Kuzimu na jehanamu, na kwa kumwokoa mwanadamu kutoka kwa Kuzimu na jehanamu, Yesu alimwezesha mwanadamu kuendelea kuishi. Sasa, siku za mwisho zimewadia. Mungu atamwangamiza mwanadamu, Atamharibu mwanadamu kabisa, ambayo ina maana kuwa Atageuza uasi wa binadamu. Kwa hivyo, huruma ya Mungu na tabia yake ya hapo zamani ya kupenda haitakuwa na uwezo wa kuhitimisha enzi hiyo, na haitakuwa na uwezo wa kukamilisha usimamizi wa Mungu wa miaka elfu sita. Kila enzi inaonyesha uwakilishi maalum wa tabia ya Mungu, na kila enzi ina kazi ambayo inafaa kufanywa na Mungu. Kwa hivyo, kazi iliyofanywa na Mungu mwenyewe kwa kila enzi ina dhihirisho la tabia Yake ya ukweli, na jina Lake na kazi anaofanya hubadilika na enzi—zote ni mpya. Wakati wa Enzi ya Sheria, kazi ya kumwelekeza mwanadamu ilifanyika katika Jina la Yehova, na awamu ya kwanza ya kazi ilifanyika duniani. Kazi ya awamu hii ilikuwa ni kujenga hekalu na madhabahu, na kutumia sheria kuwaongoza watu wa Israeli na kufanya kazi miongoni mwao. Kwa kuongoza watu wa Israeli, Alizindua kituo cha kazi Yake hapa duniani. Kwa msingi huu, Yeye Alipanua kazi yake nje ya Israeli, ambayo ni kusema kwamba, kuanzia Israeli, Aliendeleza kazi yake nje, ili vizazi vya baadaye walikuja kujua polepole kwamba Yehova Alikuwa Mungu, na kuwa Yehova Alikuwa Ameumba mbingu na nchi na vitu vyote, Alitengeneza viumbe vyote. Yeye Alieneza kazi yake kupitia kwa watu wa Israeli. Nchi ya Israeli ilikuwa ya mahali takatifu pa kwanza pa kazi ya Yehova hapa duniani, na kazi ya Mungu ya hapo mwanzoni ilikuwa kote katika nchi ya Israeli. Hiyo ilikuwa kazi ya Enzi ya Sheria. Wakati wa Enzi ya Neema, Yesu Alikuwa Mungu ambaye Alimwokoa mwanadamu. Alichokuwa nacho na Aliyekuwa ni neema, upendo, huruma, uvumilivu, subira, unyenyekevu, huduma, na stahamala, na nyingi ya kazi ambayo Alifanya ilikuwa kwa ajili ya kumwokoa mwanadamu. Tabia Yake ilikuwa ya huruma na upendo, na kwa sababu Yeye Alikuwa na huruma na upendo, ilikuwa sharti asulubishwe msalabani kwa ajili ya mwanadamu, ili kuonyesha kwamba Mungu Alimpenda mwanadamu jinsi anavyojipenda, kwa kiasi kwamba Yeye mwenyewe Alijitoa kama kafara na kwa ukamilifu Wake. Wakati wa Enzi ya Neema, jina la Mungu lilikuwa ni Yesu, ambalo lina maana kuwa Mungu Alikuwa Mungu ambaye Alimwokoa mwanadamu, na ya kwamba Alikuwa Mungu wa rehema na wa upendo. Mungu Alikuwa na mwanadamu. Upendo wake, huruma yake, na wokovu wake uliandamana na kila mtu. Mwanadamu angeweza tu kupata amani na furaha, kupokea baraka zake, kupokea neema yake kubwa na nyingi, na kupokea wokovu wake iwapo mwanadamu angekubali jina lake na akubali uwepo wake. Kupitia kusulubiwa kwa Yesu, wale wote ambao walimfuata Yeye walipokea wokovu na walisamehewa dhambi zao. Wakati wa Enzi ya Neema, jina la Mungu lilikuwa ni Yesu. Kwa maneno mengine, kazi ya Enzi ya Neema ilifanywa hasa katika Jina la Yesu. Wakati wa Enzi ya Neema, Mungu Aliitwa Yesu. Yeye Alifanya kazi mpya zaidi ya Agano la Kale, na kazi yake ilimalizika kwa kusulubiwa, na ya kwamba huo ulikuwa ukamilifu wa kazi yake. Kwa hivyo, wakati wa Enzi ya Sheria Yehova ndilo lilikuwa jina la Mungu, na katika Enzi ya Neema jina la Yesu lilimwakilisha Mungu. Katika siku za mwisho, jina lake ni Mwenyezi Mungu—mwenye uweza, na yeye hutumia nguvu zake kumwongoza mwanadamu, kumshinda mwanadamu, kumtwaa mwanadamu, na mwishowe, kuhitimisha enzi hiyo. Katika kila enzi, katika awamu yote ya kazi yake, tabia ya Mungu ni dhahiri.

Hapo mwanzo, kumwongoza mwanadamu wakati wa Enzi ya Sheria ya Agano la Kale ilikuwa kama kuyaongoza maisha ya mtoto. Wanadamu wa mwanzoni sana walikuwa wazaliwa wapya wa Yehova, ambao walikuwa Waisraeli. Hawakuelewa jinsi ya kumcha Mungu au kuishi duniani. Ambayo ni kusema, Yehova aliwaumba wanadamu, yaani, Yeye aliwaumba Adamu na Hawa, lakini Hakuwapa uwezo wa kuelewa jinsi ya kumcha Yehova au kufuata sheria za Yehova duniani. Bila mwongozo wa moja kwa moja wa Yehova, hakuna ambaye angeweza kulijua hili moja kwa moja, kwani mwanzoni mwanadamu hakuwa na uwezo huo wa kuelewa. Mwanadamu alijua tu kwamba Yehova alikuwa Mungu, na hakuwa na habari ya namna ya kumcha Yeye, nini cha kufanya ili kumcha Yeye, kumcha Yeye na akili gani, na nini cha kutoa katika kumcha Yeye, mwanadamu alijua tu jinsi ya kufurahia kile ambacho kingeweza kufurahiwa kati ya viumbe wa Yehova, lakini mwanadamu hakuwa na fununu ya aina gani ya maisha duniani yalifaa yale ya kiumbe cha Mungu. Bila mtu wa kuwaelekeza, bila mtu wa kuwaongoza binafsi, wanadamu kama hao hawangeweza kamwe kuishi maisha ya kufaa wanadamu, na wangeweza tu kutekwa na Shetani kwa siri. Yehova aliwaumba wanadamu, ambayo ni kusema kwamba Yeye aliumba babu za wanadamu: Hawa na Adamu. Lakini hakuwapa akili zaidi au hekima. Ingawa walikuwa tayari wanaishi duniani, hawakuelewa takriban chochote. Na kwa hiyo, kazi ya Yehova ya kuwaumba wanadamu ilikuwa imefanyika nusu tu, haikuwa imekaribia kukamilika. Alikuwa ameumba tu mfano wa mwanadamu kutoka kwa udongo na kumpa pumzi Yake, lakini Hakuwa amempa mwanadamu radhi ya kutosha kumcha Yeye. Hapo mwanzo, mwanadamu hakuwa na akili ya kumcha Yeye, au kumwogopa Yeye. Mwanadamu alijua tu jinsi ya kuyasikiliza maneno Yake lakini hakujua ujuzi wa msingi wa maisha duniani na sheria za kawaida za maisha. Na kwa hiyo, ingawa Yehova aliumba mwanamume na mwanamke na kumaliza siku saba za shughuli, Hakukamilisha uumbaji wa mwanadamu hata kidogo, kwa maana mwanadamu alikuwa ganda tu, na hakuwa na uhalisi wa kuwa mwanadamu. Mwanadamu alijua tu kwamba ni Yehova aliyeumba wanadamu, lakini mwanadamu hakuwa na fununu ya jinsi ya kutii maneno na sheria za Yehova. Na kwa hiyo, baada ya kuumbwa kwa wanadamu, kazi ya Yehova ilikuwa mbali sana kumalizika. Pia alitakiwa kuwaongoza wanadamu kabisa mbele Yake ili wanadamu waweze kuishi pamoja duniani na kumcha Yeye, na ili wanadamu waweze kwa mwongozo Wake kuingia katika njia sahihi ya maisha ya kawaida ya binadamu duniani baada ya kuongozwa na Yeye. Kwa njia hii tu ndiyo kazi ambayo ilikuwa imeendeshwa kwa kiasi kikubwa kupitia jina la Yehova ilimalizika kabisa; yaani, kwa njia hii tu ndiyo kazi ya Yehova ya kuumba ulimwengu ilihitimishwa kabisa. Na kwa hiyo, kwa vile Alimuumba mwanadamu, Alipaswa kuongoza maisha ya wanadamu duniani kwa miaka elfu kadhaa, ili wanadamu waweze kutii amri na sheria Zake, na kushiriki katika shughuli zote za maisha ya kufaa ya binadamu duniani. Wakati huo tu ndio kazi ya Yehova ilikamilika kabisa. Alianza kazi hii baada ya kuumba wanadamu, na kazi Yake iliendelea mpaka wakati wa Yakobo, wakati wana kumi na wawili wa Yakobo walipokuwa makabila kumi na mbili ya Israeli. Tangu wakati huo na kuendelea, kila mtu katika Israeli akawa watu walioongozwa rasmi na Yeye duniani, na Israeli ikawa mahali maalumu duniani ambapo Alifanya kazi Yake. Yehova aliwafanya watu hawa kundi la kwanza kati ya watu ambalo kwalo Alifanya kazi Yake rasmi duniani, na kuifanya nchi nzima ya Israeli kuwa kiwango cha kuanzia kazi Yake. Aliwatumia kama mwanzo wa hata kazi kubwa zaidi, ili watu wote waliozaliwa kutoka Kwake duniani wangejua jinsi ya kumcha Yeye na kuishi duniani. Na kwa hiyo, matendo ya Waisraeli yakawa mfano wa kufuatwa na Mataifa, na kile kilichosemwa kati ya watu wa Israeli kikawa maneno ya kusikizwa na Mataifa. Kwa kuwa walikuwa wa kwanza kupokea sheria na amri za Yehova, na vivyo hivyo pia walikuwa wa kwanza kujua jinsi ya kuzicha njia za Yehova. Wao walikuwa mababu wa binadamu ambao walijua njia za Yehova, na walikuwa wawakilishi wa wanadamu waliochaguliwa na Yehova. Enzi ya Neema ilipofika, Yehova hakuwaongoza wanadamu kwa namna hii tena. Mwanadamu alikuwa amefanya dhambi na kujiachia mwenyewe kwa dhambi, na kwa hiyo Akaanza kumwokoa mwanadamu kutoka kwa dhambi. Kwa njia hii, alimshutumu mwanadamu mpaka mwanadamu akakombolewa kabisa kutoka kwa dhambi. Katika siku za mwisho, mwanadamu ameshuka kwenye kiasi hicho cha upotovu mpaka kazi ya hatua hii inaweza kutelezwa tu kupitia hukumu na kuadibu. Ni kwa njia hii tu ndiyo kazi inaweza kufanikishwa. Hii imekuwa kazi ya enzi kadhaa. Kwa maneno mengine, Mungu hutumia jina Lake, kazi Yake, na taswira tofauti za Mungu kugawanya na kuhamisha enzi; jina la Mungu na kazi Yake vinawakilisha enzi Yake na kuwakilisha kazi Yake katika kila enzi. Kama kazi ya Mungu katika kila enzi ni sawa daima, naye daima anaitwa kwa jina sawa, ni jinsi gani basi mwanadamu atamjua Yeye? Mungu lazima aitwe Yehova, na mbali na Mungu kuitwa Yehova, yeyote ambaye ataitwa jina jingine si Mungu. Ama kwa njia nyingine Mungu Anaweza tu kuitwa Yesu, na Mungu hawezi kuitwa jina lingine isipokuwa Yesu; na mbali na Yesu, Yehova si Mungu, na wala Mwenyezi Mungu si Mungu. Mwanadamu anaamini kuwa ni ukweli Mungu ni mwenye uweza, lakini Mungu ni Mungu pamoja na mwanadamu; Sharti aitwe Yesu, kwa kuwa Mungu yu pamoja na mwanadamu. Kufanya hili ni kufuata mafundisho, na kumshurutisha Mungu kwenye eneo fulani. Kwa hivyo, kazi ambayo Mungu hufanya katika kila enzi, jina ambalo Yeye huitwa, na mfano ambao Yeye hutwaa—kazi ambayo Yeye hufanya katika kila hatua mpaka leo—hivi havifuati kanuni hata moja, na hayakabiliwi na kikwazo chochote. Yeye ni Yehova lakini pia ni Yesu, na vile vile ni Masihi, na Mwenyezi Mungu. Kazi yake inaweza kubadilika polepole, na kuna mabadiliko sambamba katika jina lake. Hamna jina moja ambalo linaweza kumwakilisha Yeye kikamilifu, lakini majina yote ambayo Yeye huitwa yanaweza kumwakilisha Yeye, na kazi ambayo Amefanya katika kila enzi inawakilisha tabia yake. Tuseme, siku za mwisho zikifika, Mungu ambaye unamtazamia bado ni Yesu, na bado anaendesha wingu jeupe, na bado ana sura ya Yesu, na maneno ambayo Yeye anayasema ni bado maneno ya Yesu: “Mnapaswa kuwapenda jirani zenu kama mnavyojipenda nyinyi wenyewe, mnapaswa kufunga na kuomba, wapende adui zenu kama mnavyopenda maisha yenu wenyewe, stahimili wengine, na muwe na uvumilivu na unyenyekevu. Lazima mfanye haya yote. Hapo tu ndipo mtaweza kuwa wafuasi Wangu. Mkifanya haya yote, mtaweza kuingia katika Ufalme Wangu.” Je, hii haitakuwa kazi ya Enzi ya Neema? Je, hii haitakuwa njia ambayo ilizungumziwa katika Enzi ya Neema? Mnajisikiaje mnaposikia maneno haya. Je, hamhisi kuwa bado hii ni kazi ya Yesu? Je, hayo hayatakuwa marudio ya kazi Yake? Je, hii inaweza kumpendeza mwanadamu? Mnaweza kuhisi kuwa kazi ya Mungu inaweza kubaki tu kama ilivyo sasa, na haiwezi kuendelea zaidi. Yeye ana nguvu kubwa kiasi hiki pekee, na hana kazi mpya ya kutekeleza, na Amefikia upeo wake. Miaka elfu mbili iliyopita ilikuwa ni Enzi ya Neema, na miaka elfu mbili baadaye, Yeye bado anahubiri kwa njia ya Enzi ya Neema, na bado anawafanya wanadamu watubu. Watu watasema “Mungu, una nguvu kubwa kiasi hiki pekee. Niliamini kuwa wewe ni mwenye busara sana, ilhali unajua tu uvumilivu na unashughulika na subira tu. Unajua tu jinsi ya kupenda adui yako na bila chochote kingine.” Katika akili ya mwanadamu, Mungu milele Atakuwa Alivyokuwa katika Enzi ya Neema, na mwanadamu daima ataamini ya kwamba Mungu ni wa upendo na rehema. Je, unafikiri kuwa kazi ya Mungu daima itapitia kwenye ardhi ile ile ya zamani? Na hivyo, katika awamu hii ya kazi yake Yeye hawezi kusulubishwa, na kila kitu mnachoona na kugusa kitakuwa tofauti na chochote ambacho mmewahi kufikiri na kusikia. Leo, Mungu hashiriki na Mafarisayo, Anauweka ulimwengu katika ujinga, na ninyi wafuasi tu ndio mnamjua Yeye, kwa maana Yeye hatasulubiwa tena. Wakati wa enzi ya Neema, Yesu alihubiri waziwazi kote katika nchi kwa ajili ya kazi Yake ya injili. Alijishughulisha na Mafarisayo kwa ajili ya kusulubiwa; kama Hangejishughulisha na Mafarisayo na wale waliokuwa mamlakani hawangejua kamwe juu Yake, Angewezaje kushutumiwa, na kisha kusalitiwa na kupigiliwa misumari msalabani? Na kwa hiyo, Alijishughulisha na Mafarisayo kwa ajili ya kusulubiwa. Leo, Yeye hufanya kazi Yake kwa siri ili kuepuka majaribu. Kazi, umuhimu, na mandhari ya kupata mwili kwa Mungu kuwili vyote vilikuwa tofauti, kwa hiyo kazi Aliyoifanya ingewezaje kuwa sawa kabisa?

Je, Jina la Yesu—“Mungu pamoja nasi,”—linaweza kuwakilisha tabia ya Mungu kwa ukamilifu wake? Je, linaweza kueleza Mungu kwa ukamilifu? Kama mwanadamu atasema ya kwamba Mungu Ataitwa tu Yesu, na hawezi kuwa na jina lingine kwa sababu Mungu hawezi kubadilisha tabia yake, basi maneno hayo ni kufuru! Je, unaamini kwamba jina la Yesu, Mungu pamoja nasi, linaweza kumwakilisha Mungu kikamilifu? Mungu Anaweza kuitwa majina mengi, lakini baina ya majina haya mengi, hamna moja ambalo linaweza kujumlisha yote ambayo Mungu Anamiliki, na hamna jina moja ambalo linaweza kumwakilisha Mungu kikamilifu. Na hivyo Mungu Ana majina mengi, lakini majina haya mengi hayawezi kuelezea tabia ya Mungu kikamilifu, kwa kuwa tabia ya Mungu ni tajiri sana, na yanazidi uwezo wa mwanadamu kumjua Yeye. Lugha ya mwanadamu haina uwezo wa kumfafanua Mungu kwa ukamilifu. Mwanadamu ana msamiati finyu tu ambao anaweza kufafanua yote anayojua kuhusu tabia ya Mungu: kubwa, yenye heshima, ya ajabu, isiyoeleweka, kuu, takatifu, yenye haki, yenye hekima, na kadhalika. Maneno mengi sana! Msamiati kama huo finyu hauwezi kuelezea kile kidogo mtu ameshuhudia juu ya tabia ya Mungu. Baadaye, watu wengi waliongeza maneno zaidi ili kueleza vizuri zaidi ari ndani ya mioyo yao: Mungu ni mkuu sana! Mungu ni mtakatifu sana! Mungu ni wa kupendeza sana! Leo, maneno kama haya yamefikia kilele chake, lakini bado mwanadamu hawezi kujieleza wazi wazi. Na kwa hiyo, kwa mwanadamu, Mungu ana majina mengi, lakini Hana jina moja, na hilo ni kwa sababu nafsi ya Mungu ni ya ukarimu sana, na lugha ya mwanadamu haitoshi sana. Neno au jina moja maalum halina uwezo wa kumwakilisha Mungu kwa ukamilifu wake. Kwa hivyo, je, Mungu Anaweza kuchukua jina moja lisilobadilika? Mungu ni mkuu sana na mtakatifu sana, kwa hivyo mbona wewe huwezi kumruhusu Yeye abadili jina Lake katika kila enzi mpya? Kwa hivyo, katika kila enzi ambayo Mungu binafsi hufanya kazi yake mwenyewe, Yeye hutumia jina ambalo linafaa enzi hiyo ili kujumlisha kazi ambayo anaifanya. Yeye hutumia hili jina haswa, ambalo linamiliki umuhimu wa wakati, kuwakilisha tabia yake katika enzi hiyo. Mungu hutumia lugha ya mwanadamu kuelezea tabia yake mwenyewe. Hata hivyo, watu wengi ambao wamepata uzoefu wa kiroho na wamemuona Mungu binafsi bado wanahisi kuwa jina moja maalumu haliwezi kumwakilisha Mungu kwa ukamilifu wake—ole wetu, hili linasikitisha, hivyo mwanadamu hamwiti Mungu kwa jina lolote, lakini humwita tu “Mungu.” Moyo wa mwanadamu unaonekana kujawa na upendo, lakini pia unaonekana kuzongwa na ukinzani, kwa maana mwanadamu hajui jinsi ya kumueleza Mungu. Kile Mungu alicho ni cha ukarimu sana kiasi kwamba hakuna kabisa njia ya kukieleza. Hakuna jina moja ambalo linaweza kutoa muhtasari wa tabia Ya Mungu, na hakuna jina moja ambalo linaweza kuelezea yote ambayo Mungu anacho na Alicho. Kama mtu ataniuliza, “Ni jina gani hasa unalotumia?” Nitamwambia, “Mungu ni Mungu!” Je, hilo silo jina bora zaidi la Mungu? Je, huko sio kufafanua bora zaidi kuhusu tabia ya Mungu? Hali ikiwa hivi, kwa nini mnatumia juhudi nyingi sana kutafuta jina la Mungu? Kwa nini ufikirie sana, kukaa bila kula na kulala, kwa ajili ya jina? Siku itawadia ambapo Mungu hataitwa Yehova, Yesu, au Masihi—Yeye Ataitwa tu Muumba. Wakati huo, majina yote ambayo Alichukua hapa duniani yatafikia kikomo, kwa kuwa kazi yake hapa duniani itakuwa imefika mwisho, na baada ya hapo Mungu hatakuwa na jina. Wakati mambo yote yatakuja kuwa chini ya utawala wa Muumba, kwa nini umwite kwa jina sahihi ila bado halijakamilika? Je, bado unatafuta jina la Mungu sasa? Je, bado unathubutu kusema kuwa Mungu Anaitwa tu Yehova? Je, bado unathubutu kusema kuwa Mungu Anaweza tu kuitwa Yesu? Je, unaweza kubeba dhambi ya kumkufuru Mungu? Unapaswa kujua kuwa Mungu mwanzoni hakuwa na jina. Yeye Alichukua tu jina moja, au majina mawili, ama majina mengi kwa sababu Alikuwa na kazi ya kufanya na Alikuwa na jukumu la kumsimamia mwanadamu. Jina lolote ambalo anaitwa Yeye, je, si lile analolichagua kwa hiari yake? Je, Yeye atakuhitaji wewe, mmoja wa viumbe wake Wake, kuliamua? Jina ambalo Mungu Anaitwa ni kwa mujibu wa kile ambacho mwanadamu anaweza kufahamu na lugha ya mwanadamu, lakini hili jina haliwezi kujumlishwa na mwanadamu. Wewe unaweza kusema tu kuwa mbinguni kuna Mungu, ya kwamba Yeye anaitwa Mungu, na kwamba Yeye mwenyewe ni Mungu mwenye nguvu nyingi, busara tele, wakuinuliwa sana, wa ajabu kuu, mwenye siri kuu, mwenye uweza mkuu sana, na huwezi kusema mengi zaidi; hayo ndiyo yote unayoyajua. Kwa njia hii, je, jina la Yesu tu linaweza kumwakilisha Mungu mwenyewe? Wakati siku za mwisho zitawadia, ingawa ni Mungu ndiye anafanya kazi yake, ni sharti jina lake libadilike, kwa kuwa ni enzi tofauti.

Mungu akiwa mkuu zaidi katika ulimwengu wote, na katika ulimwengu wa juu, Angeweza kujieleza Mwenyewe kwa ukamilifu kwa kutumia mfano wa mwili? Mungu hujivika Mwenyewe mwili ili kufanya hatua ya kazi Yake. Hakuna umuhimu mahsusi kwa sura ya mwili, na haina uhusiano na kupita kwa enzi, na haina uhusiano wowote na tabia ya Mungu. Kwa nini Yesu hakuruhusu sura Yake kubaki? Kwa nini hakumruhusu mtu kuchora sura Yake, ili iweze kupitishwa kwa vizazi vya baadaye? Kwa nini Hakuruhusu watu kukubali kwamba sura yake ilikuwa sura ya Mungu? Ingawa sura ya mwanadamu iliumbwa kwa mfano wa Mungu, ni kwa jinsi gani sura ya mwanadamu ingewakilisha mfano wa Mungu aliyeinuliwa? Mungu anapopata mwili, Yeye anashuka tu kutoka mbinguni na kuingia ndani ya mwili maalumu. Roho Wake ashuka kingia ndani ya mwili, kwa njia ambayo Yeye hufanya kazi ya Roho. Roho huonyeshwa katika mwili, na Roho hufanya kazi Yake katika mwili. Kazi iliyofanyika katika mwili inawakilisha Roho kwa ukamilifu, na mwili ni kwa ajili ya kazi, lakini hilo halimaanishi kwamba sura ya mwili ni mbadala wa sura halisi ya Mungu Mwenyewe; hili silo kusudi na umuhimu wa Mungu kupata mwili. Anapata mwili tu ili Roho apate mahali pa kuishi Akifanya kazi Yake, ili Apate kufanikisha kazi Yake katika mwili, ili watu waweze kuona matendo Yake, waelewe tabia Yake, kusikia maneno Yake, na kujua ajabu ya kazi Yake. Jina Lake linawakilisha tabia Yake, kazi Yake inawakilisha utambulisho Wake, lakini Hajawahi kusema kuwa kuonekana Kwake katika mwili kunawakilisha sura Yake; hiyo ni fikira tu ya mwanadamu. Na kwa hiyo, hoja muhimu za kupata mwili kwa Mungu ni jina Lake, kazi Yake, tabia Yake, na jinsia Yake. Yeye hutumia hivi kuwakilisha usimamizi wake katika enzi hii. Kuonekana Kwake katika mwili hakuna uhusiano na usimamizi Wake, na ni kwa ajili tu ya kazi Yake wakati huo. Hata hivyo haiwezekani kwa Mungu mwenye mwili kutokuwa na kuonekana maalumu, na kwa hiyo Anachagua jamii inayofaa ili kuamua kuonekana Kwake. Ikiwa kuonekana kwa Mungu kuna umuhimu wa uwakilishi, basi wale wote ambao wana sifa muhimu za uso sawa na Zake pia wanawakilisha Mungu. Hilo silo kosa la kupita kiasi? Picha ya Yesu ilichorwa na mwanadamu ili mwanadamu angeweza kumwabudu. Wakati huo, hakuna maagizo maalum yaliyotolewa na Roho Mtakatifu, na kwa hiyo mwanadamu alipitisha picha hiyo iliyodhaniwa hadi leo. Kwa kweli, kulingana na kusudi la Mungu, mwanadamu hakupaswa kufanya hivyo. Ni ari tu ya mwanadamu ambayo imesababisha picha ya Yesu kubaki hadi siku hii. Mungu ni Roho, na mwanadamu hataweza kamwe kuwa na uwezo wa kutoa muhtasari wa hasa sura Yake ni nini. Sura Yake inaweza tu kuwakilishwa na tabia Yake. Huwezi kufafanua kuonekana kwa pua Lake, kwa mdomo Wake, kwa macho Yake, na kwa nywele Zake. Wakati ufunuo ulipofika kwa Yohana, aliona sura ya Mwana wa Adamu: Kutoka mdomoni mwake ulikuwa upanga mkali ukatao kuwili, macho Yake yalikuwa kama miale ya moto, kichwa Chake na nywele vilikuwa vyeupe kama sufu, miguu Yake ilikuwa kama shaba iliyong’arishwa, na kulikuwa na mshipi wa dhahabu unaozunguka kifua Chake. Ingawa maneno yake yalikuwa wazi sana, sura ya Mungu aliyoieleza haikuwa sura ya kiumbe. Aliyoona ni maono tu, na sio sura ya mtu kutoka ulimwengu yakinifu. Yohana alikuwa ameona maono, lakini hakuwa ameshuhudia kuonekana kwa kweli kwa Mungu. Sura ya mwili wa Mungu uliopata mwili ni sura ya uumbaji, na haiwezi kuwakilisha tabia ya Mungu kwa ukamilifu wake. Wakati Yehova alipoumba wanadamu, Alisema kuwa Alifanya hivyo kwa mfano Wake na Akaumba mume na mke. Wakati huo, Alisema Alifanya mume na mke katika mfano wa Mungu. Ingawa sura ya mwanadamu inafanana na sura ya Mungu, haimaanishi kuwa kuonekana kwa mwanadamu ni sura ya Mungu. Huwezi kutumia lugha ya mwanadamu kufanya muhtasari wa sura ya Mungu kwa ukamilifu, kwa maana Mungu ameinuliwa sana, ni mkubwa sana, wa ajabu sana na Asiyeeleweka!

Wakati Yesu Alikuja kufanya kazi yake, ilikuwa ni kwa uongozi wa Roho Mtakatifu; Yeye Alitenda vile ambavyo Roho Mtakatifu Alitaka, na haikuwa kwa mujibu wa Enzi ya sheria ya Agano la Kale ama kwa mujibu wa kazi ya Yehova. Ingawa kazi ambayo Yesu Alikuja kufanya haikuambatana na sheria za Yehova ama amri za Yehova, chanzo chao kilikuwa sawa. Kazi ambayo Yesu Alifanya iliwakilisha jina la Yesu, na iliwakilisha Enzi ya Neema; kazi iliyofanywa na Yehova, iliwakilisha Yehova, na iliwakilisha Enzi ya Sheria. Kazi yao ilikuwa kazi ya Roho mmoja katika enzi tofauti. Kazi ambayo Yesu Alifanya ingeweza tu kuwakilisha Enzi ya Neema, na kazi ambayo Yehova Alifanya ingeweza tu kuwakilisha Enzi ya Sheria ya Agano la Kale. Yehova Aliwaongoza tu watu wa Israeli na Misri, na mataifa yote nje ya Israeli. Kazi ya Yesu katika Enzi ya Neema ya Agano Jipya ilikuwa kazi ya Mungu katika jina la Yesu kwa kuwa Yesu ndiye Aliongoza enzi hii. Iwapo utasema kuwa kazi ya Yesu ilikuwa kwa msingi wa kazi ya Yehova, na kuwa hakufanya kazi yoyote mpya, na kuwa yote Aliyofanya ilikuwa kwa mujibu wa maneno ya Yehova, kulingana na kazi ya Yehova na unabii wa Isaya, basi Yesu hakuwa Mungu Aliyekuwa katika mwili. Kama Alitekeleza kazi yake kwa njia hii, basi Yeye Alikuwa mtume au mfanyikazi wa Enzi ya Sheria. Iwapo ni kama unavyosema, basi Yesu hangeweza kuzindua enzi, wala hangeweza kufanya kazi nyingine. Kwa njia hiyo hiyo, Roho Mtakatifu ni sharti afanye kazi Yake hasa kupitia kwa Yehova, na isipokuwa kupitia kwa Yehova Roho Mtakatifu hangeweza kufanya kazi yoyote mpya. Mwanadamu amekosea kwa kuona kazi ya Yesu kwa njia hii. Kama mwanadamu anaamini kwamba kazi iliyofanywa na Yesu ilifanywa inaambatana na maneno ya Yehova na unabii wa Isaya, basi, je, Yesu Alikuwa Mungu Aliyepata mwili, au Yeye Alikuwa nabii? Kwa mujibu wa mtazamo huu, hakukuwa na Enzi ya Neema, na Yesu hakuwa Mungu Aliyepata mwili, kwa kuwa kazi ambayo Alifanya haingeweza kuwakilisha Enzi ya Neema na ingewakilisha tu Enzi ya Sheria ya Agano la Kale. Kungekuwepo tu na enzi mpya wakati Yesu Alikuja kufanya kazi mpya, Alipozindua enzi mpya, na kupenya katika kazi iliyokuwa imefanyika hapo awali katika nchi ya Israeli, na hakufanya kazi yake kwa mujibu wa kazi iliyofanywa na Yehova huko Israeli, hakuzingatia sheria Yake ya zamani, na hakufuata kanuni zozote, na Alifanya kazi mpya ambayo Alitakiwa kufanya. Mungu Mwenyewe anakuja kuzindua enzi, na Mungu mwenyewe huja kuleta enzi kwenye kikomo. Mwanadamu hana uwezo wa kufanya kazi ya kuanzisha enzi hiyo na kuhitimisha enzi. Kama Yesu hakuleta kazi ya Yehova kwenye kikomo baada ya Yeye kuja, basi hio inadhihirisha ya kwamba Yeye Alikuwa tu mwanadamu, na hakuwakilisha Mungu. Kwa usahihi kwa sababu Yesu Alikuja na kuhitimisha kazi ya Yehova, Akaendeleza kazi ya Yehova na, aidha, Akatekeleza kazi Yake, kazi mpya, inathibitisha kuwa hii ilikuwa enzi mpya, na kwamba Yesu alikuwa Mungu Mwenyewe. Walifanya kazi katika awamu mbili zinazotofautiana. Awamu moja ilifanyika katika hekalu, na hiyo nyingine ilifanyika nje ya hekalu. Awamu moja ilikuwa ya kuongoza maisha ya mwanadamu kwa mujibu wa sheria, na awamu nyingine ilikuwa ya kutoa kafara ya dhambi. Awamu hizi mbili za kazi bila shaka zilikuwa tofauti; huu ni mgawanyiko wa enzi ya zamani na enzi mpya, na hakuna kosa kusema kuwa hizo ni enzi mbili! Maeneo ya kazi yao yalikuwa tofauti, na kiini cha kazi yao kilikuwa tofauti, na lengo la kazi yao lilikuwa tofauti. Kwa hivyo, enzi hizi zinaweza kugawanywa kwa awamu mbili: Agano la Kale na Jipya, ambayo ni kusema, enzi mpya na ya zamani. Yesu alipokuja hakuenda katika hekalu, ambayo inathibitisha kwamba enzi ya Yehova ilikuwa imeisha. Hakuingia hekaluni kwa sababu kazi ya Yehova katika hekalu ilikuwa imekamilika, na haikuhitajika kufanywa tena, na kwa hiyo kuifanya tena kungekuwa kuirudia. Kwa kuondoka tu hekaluni, kuanza kazi mpya na kuzindua njia mpya nje ya hekalu, ndio Aliweza kuifikisha kazi ya Mungu kwa upeo wake. Kama Hangeenda nje ya hekalu kufanya kazi Yake, kazi ya Mungu haingeweza kamwe kuendelea mbele kupita hekalu, na hakungekuwa na mabadiliko yoyote mapya. Na kwa hiyo, Yesu Alipokuja, Hakuingia hekaluni, na Hakufanya kazi Yake hekaluni. Alifanya kazi Yake nje ya hekalu, na Akafanya kazi Yake kwa uhuru Akiandamana na wanafunzi. Kuondoka kwa Mungu katika hekalu kufanya kazi Yake kulikuwa na maana kwamba Mungu alikuwa na mpango mpya. Kazi Yake ilikuwa ifanyike nje ya hekalu, na ilikuwa iwe kazi mpya ambayo haingezuiliwa kwa njia ya utekelezaji wake. Kuwasili kwa Yesu kulimaliza kazi ya Yehova ya wakati wa Agano la Kale. Ingawa ziliitwa kwa majina mawili tofauti, awamu zote mbili za kazi zilifanywa na Roho mmoja, na kazi ya pili ilikuwa mwendelezo wa kazi ya kwanza. Kwa kuwa jina lilikuwa tofauti, na kiini cha kazi kilikuwa tofauti, basi enzi ilikuwa tofauti. Wakati Yehova Alikuja, hiyo ilikuwa enzi ya Yehova, na wakati Yesu Alikuja, hiyo ilikuwa enzi ya Yesu. Na kwa hivyo, kila wakati Mungu Anapokuja, anaitwa kwa jina moja, Yeye anawakilisha enzi moja, na Yeye anazindua njia mpya; na kwa kila njia mpya, Yeye huchukua jina jipya, ambalo inaonyesha kuwa Mungu daima ni mpya na wala si wa zamani, na ya kwamba kazi yake daima inasonga mbele. Historia inasonga mbele daima, na kazi ya Mungu inasonga mbele daima. Ili mpango wa usimamizi wa Mungu wa miaka elfu sita ufike upeo wake, lazima uendelee kusonga mbele. Kila siku ni sharti Yeye afanye kazi mpya, kila mwaka lazima Yeye afanye kazi mpya, ni sharti Yeye azindue njia mpya, azindue enzi mpya, aanzishe kazi mpya na kubwa zaidi, na ni sharti alete majina mapya na kazi mpya. Roho wa Mungu daima hufanya kazi mpya, na kamwe Hashikilii njia za zamani au masharti. Kazi Yake pia kamwe haikomi, na inatendeka wakati wote. Ukisema kwamba kazi ya Roho Mtakatifu ni isiyobadilika, basi kwa nini Yehova aliwaruhusu makuhani kumhudumia Yeye hekaluni, lakini Yesu hakuingia hekaluni licha ya ukweli kwamba Alipokuja watu pia walisema kwamba Alikuwa kuhani mkuu, na kwamba Alikuwa wa nyumba ya Daudi na pia kuhani mkuu, na Mfalme mkuu? Na kwa nini Hakutoa dhabihu? Kuingia hekaluni au la—hii yote sio kazi ya Mungu Mwenyewe? Iwapo, kama mwanadamu anavyofikiria, Yesu Atakuja, akiwa anaitwa Yesu wakati wa siku za mwisho, na bado juu ya wingu jeupe, akishuka miongoni mwa wanadamu kwa mfano wa Yesu: huko hakutakuwa kurudia kazi yake? Je, si Roho Mtakatifu Atakuwa Ameshikamana na ya kale? Yote yale ambayo mwanadamu anaamini ni mawazo, na yote ambayo mwanadamu anakubali ni kulingana na maana halisi, na ni kwa mujibu wa mawazo yale; yanakinzana na kanuni za kazi ya Roho Mtakatifu, na hayafuatani na nia ya Mungu. Mungu pia hawezi kufanya hivyo; Mungu si mpumbavu na mjinga kiasi hicho, na kazi Yake si rahisi kama unavyofikiria. Kwa kutegemeza mambo yote yanayofikiriwa na mwanadamu, Yesu Atarejea juu ya wingu na Atateremka kati yenu. Mtamwona Yeye ambaye, akiwa amepaa juu ya wingu, atawaambia kwamba yeye ni Yesu. Nanyi pia mtatazama alama za misumari katika mikono yake, na mtamjua Yeye ni Yesu. Naye ndiye Atakayewaokoa tena, na Atakuwa Mungu wenu Mwenye nguvu. Yeye ndiye Atakayewaokoa, na kuwakabidhi ninyi jina jipya, na kumpa kila mtu jiwe jeupe, ambapo baadaye mtakubaliwa kuingia katika ufalme wa mbinguni na kulakiwa kwenye paradiso. Je, imani kama hizo si fikira za mwanadamu? Je, Mungu hufanya kazi kulingana na fikira za mwanadamu, au, je, Yeye hufanya kazi kinyume cha fikira za mwanadamu? Je, si fikira zote za mwanadamu zatoka kwa Shetani? Je, mwanadamu hajapotoshwa na Shetani? Kama Mungu Alifanya kazi yake kulingana na fikira ya mwanadamu, je, si Mungu Angekuwa Shetani? Je, si Angekuwa wa aina sawa na viumbe Wake wenyewe? Kwa kuwa viumbe Wake wamepotoshwa na Shetani hadi mwanadamu amekuwa mfano halisi ya Shetani, kama Mungu Angefanya kazi kwa mujibu wa vitu vya Shetani, si angekuwa katika ligi ya Shetani. Mwanadamu anawezaje kupima kina cha kazi ya Mungu? Na kwa hivyo, Mungu hafanyi kazi kwa mujibu wa fikira ya mwanadamu, na hangefanya kazi kwa njia unazofikiria. Kuna wale ambao husema kwamba Mungu mwenyewe Alisema kuwa Atawasili kwa wingu. Ni ukweli kuwa Mungu mwenyewe Alisema hivyo, lakini, je, hujui kuwa siri za Mungu haziwezi kueleweka na mwanadamu? Je, unajua kuwa maneno ya Mungu hayawezi kuelezwa na mwanadamu? Na wewe una hakika, bila tashwishi yoyote, kuwa ulipewa nuru na kuangaziwa na Roho Mtakatifu? Je, si Roho Mtakatifu Aliyekuonyesha moja kwa moja kwa namna hii? Je, haya ni maelekezo ya Roho Mtakatifu, au ni fikira zako? Ulisema, “Haya yalisemwa na Mungu mwenyewe.” Lakini hatuwezi kutumia fikira zetu na akili zetu kupima maneno ya Mungu. Na kuhusu maneno ya Isaya, je, unaweza kueleza maneno yake kwa kujiamini kikamilifu? Je, wewe unathubutu kueleza maneno yake? Kwa sababu huthubutu kueleza maneno ya Isaya, mbona unathubutu kueleza maneno ya Yesu? Nani ameinuliwa kuliko mwingine, Yesu au Isaya? Kwa vile jibu ni Yesu, kwa nini unaeleza maneno yaliyosemwa na Yesu? Je, Mungu Angeweza kukwambia kuhusu kazi yake mapema? Hakuna kiumbe kinachoweza kufahamu, wala hata wajumbe walio mbinguni, wala hata Mwana wa Adamu, kwa hivyo wewe ungejuaje? Mwanadamu ana upungufu mkuu. Kilicho muhimu kwenu sasa ni kufahamu awamu tatu za kazi. Kutoka kwa kazi ya Yehova mpaka ile ya Yesu, na kutoka kwa kazi ya Yesu hadi kwa kazi iliyoko kwa awamu hii ya sasa, awamu hizi tatu zinajumlisha upana wote wa usimamizi wa Mungu, na zote ni kazi za Roho mmoja. Kutoka Alipoumba ulimwengu, Mungu Amekuwa Akisimamia wanadamu. Yeye ndiye Mwanzo na ndiye Mwisho; Yeye ndiye wa Kwanza na wa Mwisho, na Yeye ndiye mwanzilishi wa enzi na Yeye ndiye huleta enzi kwenye kikomo. Awamu tatu za kazi, katika enzi tofauti na maeneo mbalimbali, hakika yanafanywa na Roho mmoja. Wote ambao wanatenganisha awamu hizi tatu wanampinga Mungu. Sasa, lazima uelewe kwamba kazi yote kutoka awamu ya kwanza hadi leo ni kazi ya Mungu mmoja, ni kazi ya Roho mmoja, ambapo hakuna shaka.

Iliyotangulia: Maono ya Kazi ya Mungu (2)

Inayofuata: Kuhusu Biblia (1)

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp