Kutanafusi kwa Mwenyezi

Kuna siri kubwa sana moyoni mwako, ambayo hujawahi kuifahamu kamwe, kwa kuwa umekuwa ukiishi katika ulimwengu bila mwanga. Moyo wako na roho yako vimepokonywa na yule mwovu. Macho yako yamezuiwa kwa giza yasione, na huwezi kuliona jua angani wala ile nyota ya usiku imetametayo. Masikio yako yamezibwa na maneno ya udanganyifu, na husikii sauti ya Yehova ingurumayo kama radi, wala sauti ya maji mengi yanayotiririka kutoka katika kiti cha enzi. Umepoteza kila kitu ambacho ni chako kwa haki, kila kitu ambacho Mwenyezi alikupa. Umeingia katika bahari ya mateso isiyokuwa na mwisho, bila nguvu ya kuweza kukuokoa wewe, bila matumaini ya kuendelea kuishi, na yote unayofanya ni kupambana na kukimbia huku na kule.… Kuanzia wakati huo na kuendelea, umehukumiwa kuteswa na yule mwovu, mbali sana na baraka za Mwenyezi, mbali sana na riziki ya Mwenyezi, ukiitembea njia ambayo huwezi kurudi nyuma tena. Kuitwa mara milioni hakuwezi kuamsha moyo wako na roho yako. Unalala fofofo mikononi mwa yule mwovu, ambaye amekushawishi uingie katika ulimwengu usio na mipaka, ambao hauna mwelekeo, na hauna alama za barabarani. Kuanzia hapo, umepoteza asili ya unyofu na utakatifu wako, na ukaanza kukwepa utunzaji wa Mwenyezi. Ndani ya moyo wako, yule mwovu anakuelekeza katika kila jambo na anakuwa uhai wako. Humwogopi tena, humwepuki, au kumshuku; badala yake, unamchukulia kama Mungu aliye moyoni mwako. Unaanza kumtukuza na kumwabudu, na nyinyi wawili mnakuwa msiotengana kama mwili na kivuli chake, kila mmoja akijitoa kwa mwingine katika uzima na mauti. Hujui chochote kabisa kuhusu mahali ulikotoka, kwa nini ulizaliwa, au kwa nini utakufa. Unamwona Mwenyezi kama mgeni; hujui asili Yake, sembuse yale yote ambayo Amekutendea. Kila kitu kitokacho Kwake kimekuwa cha kuchukiza kwako. Huvithamini wala hujui thamani yao. Unatembea pamoja na yule mwovu, kuanzia siku ile uliyoanza kupokea riziki ya Mwenyezi. Wewe na yule mwovu mmepitia maelfu ya miaka ya dhoruba na tufani pamoja, na pamoja naye, mnampinga Mungu ambaye alikuwa chanzo cha uhai wako. Hujui chochote kuhusu kutubu, sembuse kujua kwamba umefikia ukingo wa kuangamia. Unasahau kwamba yule mwovu amekudanganya na kukutesa; umesahau asili yako. Kwa njia hii, yule mwovu amekuwa akikuharibu, hatua kwa hatua, hata mpaka leo. Moyo wako na roho yako vimekufa ganzi na vimeoza. Umeacha kulalamika juu ya machukizo ya dunia ya wanadamu, na huamini tena kwamba dunia si ya haki. Bado hujali sana kama Mwenyezi yupo. Hii ni kwa sababu ulimchukulia yule mwovu kuwa baba yako wa kweli kitambo, na huwezi tena kutengana naye. Hii ndiyo siri iliyo moyoni mwako.

Alfajiri inapofika, nyota ya asubuhi inaanza kuangaza mashariki. Hii ni nyota ambayo haijawahi kuwepo hapo awali. Inaliangazia anga tulivu, na nyota, ikileta nuru iliyozimwa katika mioyo ya wanadamu. Binadamu si wapweke tena, kwa sababu ya mwanga huu, ambao unakuangazia wewe pamoja na wengine. Lakini ni wewe tu unayebaki ukiwa umelala fofofo katika usiku wa giza. Huwezi kuisikia sauti, wala kuiona nuru, hujui kuhusu ujio wa mbingu mpya na nchi mpya, enzi mpya, kwa sababu baba yako anakwambia, “Mwanangu, usiamke, bado ni mapema. Hali ya hewa ni baridi, kwa hivyo usiende nje, usije ukachomwa machoni kwa mkuki na upanga.” Unaamini tu maonyo ya baba yako, maana unaamini kwamba baba yako tu ndiye aliye sahihi, kwa sababu baba yako ana umri mkubwa kuliko wewe na kwamba baba yako anakupenda sana. Maonyo kama hayo na upendo kama huo unakufanya uache kuamini hekaya kwamba kuna nuru ulimwenguni, na uache kujali kama ukweli bado upo ulimwenguni humu. Huthubutu tena kutumainia ukombozi kutoka kwa Mwenyezi. Umeridhika kuwa katika hali hiyo, hutumainii tena ujio wa nuru, na hutazamii tena ujio wa Mwenyezi kama inavyosimuliwa katika hekaya. Kwa maoni yako, yote ambayo ni mazuri hayawezi kufufuliwa, wala hayawezi kuendelea kuwepo. Machoni pako, kesho ya wanadamu, siku za baadaye za wanadamu zinapotea, zinaharibika kabisa. Unashikilia sana mavazi ya baba yako kwa nguvu zako zote, ukifurahia kushiriki taabu zake, ukihofu sana kumpoteza mwenzako wa kusafiri na mwelekeo wa safari yako ya mbali. Ulimwengu huu mpana na wenye giza wa wanadamu umewafanya wengi wenu, kuwa majasiri na watu wa kujitahidi sana katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya ulimwengu huu. Umewafanya “mashujaa” wengi ambao hawaogopi kifo kabisa. Zaidi ya hayo, umetengeneza kundi baada ya kundi la watu waliokufa ganzi na wanadamu waliopooza ambao hawajui kusudi la kuumbwa kwao. Macho ya Mwenyezi yanamchunguza kila mmoja wa jamii ya wanadamu walio katika mateso makali. Anachosikia ni vilio vya wale wanaoteseka, Anachoona ni kutokua na aibu kwa wale wanaoteseka, na Anachohisi ni kutojiweza na hofu ya jamii ya wanadamu ambayo imepoteza neema ya wokovu. Wanadamu wanakataa utunzaji Wake, wakichagua kutembea katika njia yao wenyewe, na wakijaribu kukwepa macho Yake yanayochunguza kwa karibu, wakiona ni afadhali waonje uchungu wa bahari yenye kina hadi mwisho, pamoja na adui. Kutanafusi kwa Mwenyezi hakusikiki tena na binadamu. Mikono ya Mwenyezi haiko tayari tena kuwabembeleza wanadamu hawa wa kusikitisha. Anarudia kazi Yake, muda baada ya muda Anawakamata tena, na muda baada ya muda Anawapoteza tena, na kuanzia wakati huo, Anaanza kuchoka, Anahisi uchovu, na hivyo Anasitisha kazi inayofanyika, na kuacha kutembea kati ya wanadamu…. Wanadamu hawana ufahamu kabisa kuhusu mabadiliko haya, hawajui kuhusu kuja na kuondoka, huzuni na majonzi ya Mwenyezi.

Kila kitu cha ulimwengu huu kinabadilika haraka sawasawa na mawazo ya Mwenyezi, na chini ya macho Yake. Mambo ambayo wanadamu hawajawahi kuyasikia yanaweza kuja kwa ghafla, ilhali vitu ambavyo wanadamu wamevimiliki kwa muda mrefu vinaweza kutoweka bila wao kujua. Hakuna anayeweza kutambua mahali alipo Mwenyezi, sembuse mtu yeyote anayeweza kuhisi kule kwenda zaidi ya uwezo wa binadamu na ukuu wa nguvu za maisha za Mwenyezi. Yeye ni Mkuu kwa kuwa Anaweza kutambua kile ambacho wanadamu hawawezi. Yeye ni Mkuu kwa kuwani Yeye anayekataliwa na wanadamu na bado Anawaokoa wanadamu. Yeye anajua maana ya uzima na mauti na, isitoshe, Anajua sheria za kuishi ambazo wanadamu, ambao wameumbwa, wanapaswa kuzifuata. Yeye ndiye msingi wa kuwepo kwa mwanadamu, na Yeye ndiye Mkombozi anayewafufua wanadamu tena. Anailemea mioyo yenye furaha kwa huzuni, na kuiinua mioyo yenye huzuni kwa furaha, yote ni kwa ajili ya kazi Yake, na kwa ajili ya mpango Wake.

Wanadamu, baada ya kuacha uzima unaotolewa na Mwenyezi, hawajui kusudi la kuishi, lakini hata hivyo wanaogopa kifo. Hawana usaidizi wala msaada, lakini bado wanasita kufumba macho yao, na wanajitia nguvu ili kutegemeza magunia ya miili, ambayo haina hisia yoyote katika nafsi zao, huku wakiendeleza uwepo wa aibu katika ulimwengu huu. Unaishi kwa njia hii, bila tumaini, kama wengine wafanyavyo, bila malengo. Kuna mmoja tu aliye Mtakatifu katika hekaya Atakayewaokoa watu ambao, wakiwa wanaomboleza katikati ya mateso yao, wanatamani sana kuwasili Kwake. Imani kama hiyo kwa muda mrefu imebaki bila kutambuliwa kwa wale ambao hawana ufahamu. Hata hivyo, bado watu wanatamani iwe hivyo. Mwenyezi ana huruma kwa watu hawa ambao wameteseka sana; wakati huo huo, Anawachukia watu hawa ambao hawana ufahamu hata kidogo, kwani Amelazimika kusubiri kwa muda mrefu sana ili kupata jibu kutoka kwa wanadamu. Anatamani kutafuta, kuutafuta moyo wako na roho yako, na kukuletea maji na chakula, ili uamke usiwe na kiu na kuhisi njaa tena. Unapokuwa umechoka na unapoanza kuhisi huzuni kubwa ya ulimwengu huu, usipotee, usilie. Mwenyezi Mungu, Mlinzi, atakaribisha kuwasili kwako wakati wowote. Yuko kando yako Akikutazama, Akikusubiri urudi. Anasubiri siku ambayo utarudisha ghafla kumbukumbu zako: ukitambua ukweli kwamba ulitoka kwa Mungu, lakini wakati fulani usiojulikana ukapoteza mwelekeo wako, wakati fulani usiojulikana ukaanguka barabarani ukiwa hujitambui na tena wakati fulani usiojulikana ukampata “baba.” Zaidi ya hayo, ukatambua kwamba daima Mwenyezi amekuwa hapo Akikutazama, Akisubiri kurudi kwako, kwa muda mrefu sana. Amekuwa akitazama kwa shauku kubwa, Akisubiri mwitikio pasipo jibu. Kutazama na kusubiri Kwake kunazidi gharama yoyote ile, na ni kwa ajili ya moyo na roho ya mwanadamu. Pengine kutazama na kusubiri huku hakuna mwisho, na pengine kumefika mwisho. Lakini unapaswa kujua moyo wako na roho yako hasa viko wapi sasa hivi.

Mei 28, 2003

Iliyotangulia: Mungu Ndiye Chanzo cha Uhai wa Mwanadamu

Inayofuata: Kuonekana kwa Mungu Kumeleta Enzi Mpya

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp