Kuonekana kwa Mungu Kumeleta Enzi Mpya

Mpango wa Mungu wa miaka elfu sita ya usimamizi unakariba kuisha, na lango la ufalme limefunguliwa kwa wale ambao wanatafuta kuonekana kwa Mungu. Ndugu wapendwa, mnasubiri nini? Ni nini mnachotafuta? Mnasubiri kuonekana kwa Mungu? Mnazitafuta nyayo za Mungu? Ni jinsi gani kuonekana kwa Mungu kunavyotamaniwa sana! Na ni jinsi gani kulivyo kugumu kupata nyayo za Mungu! Katika enzi kama hii, katika ulimwengu kama huu, tunapaswa kufanya nini ili tushuhudie kuonekana kwa Mungu? Tunapaswa kufanya nini ili tufuate nyayo za Mungu? Wale wote wanaosubiri kuonekana kwa Mungu wanakumbana na maswali kama haya. Nyinyi nyote mmewahi kuyafikiria zaidi ya mara moja—lakini matokeo ni yapi? Je, Mungu anaonekana wapi? Nyayo za Mungu zipo wapi? Je, mmepata jibu? Watu wengi wangejibu kwa njia hii: “Mungu anaonekana miongoni mwa wale wote wanaomfuata na nyayo Zake zipo miongoni mwetu; ni rahisi hivyo! Mtu yeyote anaweza kutoa jibu kwa kutumia mbinu fulani, lakini je, mnafahamu kuonekana kwa Mungu ni nini, na nyayo za Mungu ni nini? Kuonekana kwa Mungu kunarejelea kuwasili Kwake duniani kufanya kazi Yake. Akiwa na utambulisho na tabia Yake, na katika njia ambayo ni ya asili Kwake, Anashuka miongoni mwa wanadamu kufanya kazi ya kuanzisha enzi mpya na kuhitimisha enzi nyingine. Kuonekana kwa aina hii si aina fulani ya sherehe. Si ishara, picha, muujiza, au aina fulani ya maono makubwa, na hata zaidi si mchakato fulani wa kidini. Ni ukweli halisi ambao unaweza kushikwa na kuonekana. Kuonekana kama huku si kwa ajili ya kufuata taratibu, au kwa ajili ya shughuli ya muda mfupi; badala yake, ni kwa ajili ya hatua ya kazi ya mpango Wake wa usimamizi. Kuonekana kwa Mungu daima ni kwenye maana na daima kuna uhusiano fulani na mpango Wake wa usimamizi. Kinachoitwa kuonekana hapa ni tofauti kabisa na aina ya “kuonekana” ambako Mungu anamwongoza, Anamtawala, na kumpa nuru mwanadamu. Mungu anafanya hatua kubwa ya kazi Yake kila wakati Anapojidhihirisha Mwenyewe. Kazi hii ni tofauti na ile ya enzi nyingine yoyote. Ni jambo lisiloweza kufikiriwa na mwanadamu, na halijawahi kushuhudiwa na mwanadamu. Ni kazi inayoanzisha enzi mpya na kuhitimisha enzi ya zamani, na ni aina ya kazi mpya na iliyoboreshwa kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu; zaidi ya hayo, ni kazi inayowaleta wanadamu katika enzi mpya. Hivi ndivyo inavyomaanisha kuonekana kwa Mungu.

Mara tu unapoelewa kuonekana kwa Mungu kunamaanisha nini, je, unapaswa kutafuta vipi nyayo za Mungu? Swali hili si gumu kuelezea: Palipo na kuonekana kwa Mungu, hapo utapata nyayo Zake. Ufafanuzi kama huo unaonekana kuwa wazi sana, lakini si rahisi sana kuutekeleza, kwa kuwa watu wengi hawafahamu ni wapi ambapo Mungu anajidhirisha, sembuse ni wapi ambapo Angependa, au mahali Anapopaswa kuonekana. Wengine kwa msukumo wanaamini kwamba popote palipo na kazi ya Roho Mtakatifu, pana kuonekana kwa Mungu. Ama pia wanaamini kwamba popote palipo na watu wa kiroho, hapo ndipo Mungu anaonekana. Ama pia wanaamini kwamba popote palipo na watu mashuhuri, hapo ndipo Mungu anapoonekana. Kwa sasa, tuweke kando ikiwa imani hizo ni sahihi au si sahihi. Ili kufafanua swali kama hilo, ni lazima kwanza tuwe na lengo la wazi: Tunatafuta nyayo za Mungu. Hatutafuti viongozi wa kiroho, wala kutafuta watu mashuhuri; tunafuata nyayo za Mungu. Kwa sababu hii, kwa kuwa tunatafuta hatua za Mungu, inatulazimu tutafute nia ya Mungu, maneno ya Mungu, na matamko Yake. Hii ni kwa sababu popote palipo na maneno mapya yanayonenwa na Mungu, sauti ya Mungu ipo hapo, na popote palipo na hatua za Mungu, matendo ya Mungu yapo hapo; popote palipo na maonyesho ya Mungu, Mungu anaonekana hapo, na popote anapoonekana Mungu, ukweli, njia, na uzima vipo hapo. Katika kutafuta hatua za Mungu, ninyi mmeyapuuza maneno “Mungu ni ukweli, njia, na uzima.” Na hivyo, watu wengi, hata wanapoupata ukweli, hawaamini kuwa wamepata hatua za Mungu, na sembuse kukiri kuonekana kwa Mungu. Hili ni kosa zito kiasi gani! Kuonekana kwa Mungu hakuwezi kulingana na mawazo ya mwanadamu, sembuse Mungu kuonekana kwa jinsi mwanadamu anavyodai Yeye aonekane. Mungu anafanya uamuzi Wake mwenyewe na Ana mipango Yake mwenyewe Anapofanya kazi Yake; zaidi ya hayo, Ana malengo Yake, na mbinu Zake mwenyewe. Si lazima Ajadiliane kazi Azifanyazo na mwanadamu au Atafute ushauri wa mwanadamu, sembuse kumfahamisha kila mtu kuhusu kazi Yake. Hii ndiyo tabia ya Mungu na, zaidi ya hayo, inafaa kutambuliwa na kila mmoja. Ikiwa unatamani kushuhudia kuonekana kwa Mungu, kama unatamani kufuata nyayo za Mungu, basi ni sharti kwanza uzishinde dhana zako mwenyewe. Haupaswi kudai kwamba Mungu afanye hiki au kile, sembuse kumweka Yeye ndani ya mipaka yako mwenyewe na kumzuia kwa dhana zako mwenyewe. Badala yake, unapaswa kujua jinsi utakavyotafuta nyayo za Mungu, na jinsi unavyopaswa kukubali kuonekana kwa Mungu, na jinsi unavyopaswa kutii kazi mpya ya Mungu; hiki ndicho kinapaswa kufanywa na mwanadamu. Kwa kuwa mwanadamu si ukweli, na hamiliki ukweli, mwanadamu anapaswa kutafuta, kukubali na kutii.

Bila kujali kama wewe ni Mmarekani, Mwingereza, au mtu wa taifa jingine, ni lazima utoke nje ya mipaka ya utaifa wako, ni lazima ujivuke mwenyewe, na unapaswa kuitazama kazi ya Mungu kutoka kwa utambulisho wa kiumbe aliyeumbwa. Kwa njia hii, hutaweka mipaka katika nyayo za Mungu kwa upeo wowote ule. Hii ni kwa sababu, siku hizi, watu wengi wanafikiri kuwa haiwezekani Mungu kutokea katika taifa fulani au miongoni mwa watu fulani. Ni jinsi gani umuhimu wa kazi ya Mungu ulivyo wa kina, na ni jinsi gani kuonekana kwa Mungu kulivyo muhimu! Inawezekanaje hii iweze kupimwa kwa dhana na mawazo ya mwanadamu? Na ndio maana Ninasema kwamba, unapaswa kuvuka dhana zako za utaifa na kabila ili kutafuta kuonekana kwa Mungu. Ni kwa njia hii tu hautafungwa na dhana zako mwenyewe; kwa njia hii, utahitimu kukaribisha kuonekana kwa Mungu. Vinginevyo, daima utakuwa gizani na hutapata kibali cha Mungu.

Mungu ni Mungu wa jamii yote ya wanadamu. Hajichukulii kuwa mali binafsi ya taifa lolote au watu, bali Anaenda huku na huko kufanya kazi Yake jinsi Alivyoipanga, bila kuzuiliwa na mfumo wowote, taifa, au watu. Labda hujawahi kuufikiria mfumo huu, au pengine mtazamo wako kwa mfumo huu ni wa kukana, au pengine taifa ambalo Mungu anajidhihirisha Mwenyewe na watu ambao Anajidhihirisha miongoni mwao inatokea kuwa wanabaguliwa na kila mtu na inatokea kuwa ni watu walio nyuma sana duniani. Hata hivyo Mungu ana hekima Yake. Kwa uwezo Wake, kupitia ukweli Wake, na tabia Yake, kwa hakika Amepata kundi la watu ambao wana mawazo sawa na Yeye, na Amepata kundi la watu Aliotaka kuwakamilisha—kundi lililoshindwa na Yeye, ambao, wamevumilia kila aina ya majaribio na dhiki, na kila aina ya mateso, na wanaweza kumfuata Yeye mpaka mwisho. Lengo la kuonekana kwa Mungu, ambako hakuzuiliwi na mfumo au taifa lolote, ni ili kumwezesha Yeye akamilishe kazi Yake jinsi Alivyoipanga. Kwa mfano, Mungu alipopata mwili kule Uyahudi, lengo Lake lilikuwa kukamilisha kazi ya msalaba na kuwakomboa wanadamu wote. Na bado Wayahudi waliamini kuwa Mungu asingeweza kulifanya hili, na wakafikiri kuwa Mungu asingeweza kufanyika mwili na kuchukua umbo la Bwana Yesu. “Kutowezekana” kwao kukawa msingi wa kumshutumu na kumpinga Mungu, na hatimaye kupelekea kuangamizwa kwa Israeli. Leo hii, watu wengi wamefanya kosa lile lile. Wanatangaza kwa nguvu zao zote kuonekana kwa Mungu ambako kumekaribia, lakini wakati huo huo wanashutumu kuonekana Kwake; “haiwezekani” yao kwa mara nyingine tena inaweka kuonekana kwa Mungu ndani ya mipaka ya dhana zao. Na kwa hivyo Nimeona watu wengi wakiangua kicheko baada ya kuyasikia maneno ya Mungu. Lakini je, kicheko hiki kinatofautianaje na shutuma na kufuru za Wayahudi? Huna heshima mbele ya ukweli, sembuse kuutamani ukweli. Nyinyi mnachunguza tu kama vipofu na kungoja bila kujali. Je, mtafaidi. Je, mtafaidi nini kwa kutafiti na kusubiri kwa njia hii? Je, mnaweza kupata uongozi binafsi wa Mungu? Kama huwezi kutambua matamshi ya Mungu, ni kwa njia gani unastahili kushuhudia kuonekana kwa Mungu? Mahali ambapo Mungu anaonekana, pana maonyesho ya ukweli, na pana sauti ya Mungu. Ni wale tu wanaoukubali ukweli ndio watakaoisikia sauti ya Mungu, na ni watu kama hao tu ndio waliohitimu kushuhudia kuonekana kwa Mungu. Weka dhana zako kando. Tafakari na kusoma maneno haya kwa makini. Ukitamani ukweli, Mungu atakupa nuru ya kuyafahamu mapenzi Yake na maneno Yake. Wekeni kando mitazamo yenu ya “haiwezekani”! Kadiri watu wanavyozidi kuamini kuwa jambo fulani haliwezekani, ndivyo kulivyo zaidi na uwezekano wake wa kutokea, kwa kuwa hekima za Mungu ziko juu zaidi kuliko mbingu, mawazo ya Mungu ni ya juu zaidi kuliko mawazo ya mwanadamu, na kazi ya Mungu inavuka mipaka ya fikira za mwanadamu. Kadiri kitu kinavyokuwa hakiwezekani, ndivyo kinavyokuwa zaidi na ukweli wa kutafutwa; kadiri kitu kinavyokuwa nje ya mipaka ya dhana na fikira za mwanaadamu, ndivyo kinavyozidi kuwa na mapenzi ya Mungu. Hii ni kwa sababu, haijalishi ni wapi ambapo Anaonekana, Mungu bado ni Mungu, na kiini Chake hakitawahi kubadilika kwa sababu ya mahali au jinsi ya kuonekana Kwake. Tabia ya Mungu hubaki kuwa vilevile bila kujali nyayo Zake ziko wapi. Bila kujali ni wapi nyayo za Mungu zilipo, Yeye ndiye Mungu wa wanadamu wote. Kwa mfano, Bwana Yesu si Mungu tu wa Waisraeli, lakini vilevile ni Mungu wa watu wote wa Asia, Ulaya, na Marekani, na hata zaidi, ndiye Mungu pekee wa ulimwengu mzima. Hivyo basi, tutafute mapenzi ya Mungu na tugundue kuonekana Kwake kutoka kwa matamshi Yake na tufuate nyayo Zake. Mungu ndiye ukweli, njia na uzima. Maneno Yake na kuonekana Kwake vipo kwa wakati mmoja, na tabia na nyayo Zake huonyeshwa hadharani kwa wanadamu kila wakati. Akina kaka na dada wapendwa, Natumaini kwamba mnaweza kuona kuonekana kwa Mungu katika maneno haya, na kwamba mnaweza kuanza kufuata nyayo Zake na kupiga hatua kuelekea enzi mpya, na kuingia katika mbingu mpya na dunia mpya nzuri ambayo Mungu ametayarisha kwa ajili ya wale wanaosubiri kuonekana kwa Mungu.

Iliyotangulia: Kutanafusi kwa Mwenyezi

Inayofuata: Mungu Anaongoza Majaliwa ya Wanadamu Wote

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp