Radi Saba Zinanguruma—Kutabiri Kwamba Injili ya Ufalme Itaenea Katika Ulimwengu Mzima

Ninaeneza kazi Yangu miongoni mwa Mataifa. Nuru Yangu ya utukufu inamulika katika ulimwengu mzima; watu wote walio kama nyota na vitone wanabeba nia Zangu ndani yao, na wote wanaongozwa na mkono Wangu na kuanza kazi ambazo Nimewapa. Kuanzia wakati huu na kuendelea, Nimeingia katika enzi mpya, Nikiwaleta watu wote katika ulimwengu mwingine. Niliporudi katika "nchi Yangu ya asili," Nilianza sehemu nyingine tena ya kazi katika mpango Wangu wa asili, ili mwanadamu apate maarifa zaidi kunihusu. Ninautazama ulimwengu kwa ukamilifu wake na kuona kwamba[a] ni wakati mwafaka kwa ajili ya kazi Yangu, kwa hivyo Ninaharakisha huku na kule, Nikifanya kazi Yangu mpya juu ya mwanadamu. Baada ya yote, hii ni enzi mpya, na Nimeleta kazi mpya, Nikiwachukua watu zaidi wapya katika enzi mpya na kuwatupa zaidi wa wale ambao Nitawaondosha. Katika nchi ya joka kuu jekundu, Nimefanya hatua ya kazi isiyoweza kueleweka kwa wanadamu, Nikiwafanya wayumbe katika upepo, na baada ya hapo wengi wanapeperushwa kimyakimya na uvumaji wa upepo. Kwa kweli, huu ni "uwanja wa kupuria" ambao Ninakaribia kuusafisha; ndicho Ninachotamani sana na pia ndio mpango Wangu. Kwa maana waovu wengi wameingia kisirisiri wakati Ninafanya kazi, lakini Sina haraka ya kuwafukuza. Badala yake, Nitawatawanya wakati utakapokuwa mwafaka. Ni baada tu ya hapo ndipo Nitakuwa chemchemi ya uzima, nikiwaruhusu wale wanaonipenda Mimi kwa kweli kupokea kutoka Kwangu tunda la mtini na harufu nzuri ya yungiyungi. Katika nchi ambayo Shetani anashinda kwa muda, nchi ya vumbi, hakuna dhahabu safi inayosalia, ni mchanga tu, na hivyo, ninapokumbana na hali hizi, Ninafanya hatua kama hiyo ya kazi. Mnapaswa kujua kwamba kile Ninachopata ni dhahabu safi, iliyosafishwa, si mchanga. Waovu wanawezaje kusalia katika nyumba Yangu? Ninawezaje kuvumilia mbweha wanaoishi kama vimelea katika paradiso Yangu? Ninatumia kila mbinu kuwafukuza. Kabla ya nia Zangu kufunuliwa, hakuna anayejua kile Ninachokaribia kufanya. Nikichukua fursa hii, Ninawafukuza hao waovu, na wanalazimishwa kuondoka mbele Zangu. Hivi ndivyo Ninavyowatendea waovu, lakini bado kutakuwa na siku ya wao kutumika kwa ajili Yangu. Tamaa ya watu ya baraka ni kali mno; kwa hivyo, Ninaugeuza mwili Wangu na kuonyesha uso Wangu mtukufu kwa watu wa mataifa, ili watu wote waweze kuishi katika ulimwengu wao wenyewe na wajihukumu wenyewe, huku Nikiendelea kunena maneno ambayo Ninapaswa kunena, na kuwapa kile wanachohitaji. Watu watakapopata fahamu zao, Nitakuwa nimeshaeneza kazi Yangu kitambo. Kisha Nitaonyesha nia Zangu kwao, na kuanza sehemu ya pili ya kazi Yangu juu yao, Nikiwaruhusu watu wote wanifuate kwa karibu ili washirikiane na kazi Yangu, na kuwaruhusu wafanye kila kitu kulingana na uwezo wao ili kutekeleza pamoja na Mimi kazi ambayo ni lazima Nifanye.

Hakuna aliye na imani kwamba atauona utukufu Wangu, na Mimi siwalazimishi, lakini badala yake Ninaondoa utukufu Wangu kutoka miongoni mwa wanadamu na kuupeleka katika ulimwengu mwingine. Watu watakapohisi majuto kwa mara nyingine tena, ndipo Nitakapochukua utukufu Wangu na kuuonyesha kwa watu wengi zaidi walio na imani. Hii ndiyo kanuni ambayo kwayo Ninafanya kazi. Kwa maana kuna wakati ambapo utukufu Wangu unaondoka Kanaani, na pia kuna wakati ambapo utukufu Wangu unawaacha watu wateule. Zaidi ya hayo, kuna wakati ambapo utukufu Wangu unaondoka katika dunia nzima, ukiifanya ififie na kuitumbukiza gizani. Hata nchi ya Kanaani haitaona mwanga wa jua; watu wote watapoteza imani yao, lakini hakuna anayeweza kustahimili kuiacha harufu nzuri ya nchi ya Kanaani. Ni wakati tu Ninapoingia katika mbingu na nchi mpya ndipo Ninachukua sehemu nyingine ya utukufu Wangu na kuufunua kwanza katika nchi ya Kanaani, Nikisababisha mwali wa nuru kuangaza kote katika dunia nzima yenye giza totoro. Hii ni ili dunia nzima iweze kuja kwenye nuru. Ni ili watu kote duniani waweze kuja kutumia nguvu ya nuru, na kuruhusu utukufu Wangu uongezeke zaidi na uonekane upya kwa kila taifa, na ili wanadamu wote waweze kutambua kwamba Nimekuja katika ulimwengu wa mwanadamu tangu zamani na tangu zamani Nimeleta utukufu Wangu kutoka Israeli hadi Mashariki, kwa maana utukufu Wangu unang'aa kutoka Mashariki na uliletwa kutoka Enzi ya Neema hadi leo. Lakini ilikuwa kutoka Israeli ndipo Niliondoka na kutoka huko ndipo Niliwasili Mashariki. Ni wakati tu nuru ya Mashariki inapogeuka kuwa nyeupe polepole ndipo giza kote duniani litaanza kugeuka kuwa nuru, na ni wakati huo tu ndipo mwanadamu atagundua kwamba Nimeondoka Israeli tangu zamani na Ninachomoza upya Mashariki. Haiwezekani kwamba Mimi, baada ya kushuka Israeli wakati mmoja na baadaye kuondoka huko, Ningezaliwa tena Israeli kwa mara nyingine, kwa sababu kazi Yangu inaongoza ulimwengu mzima na, zaidi ya hayo, umeme unatoka Mashariki na kumulika hadi Magharibi. Kwa sababu hii Nimeshuka Mashariki na kuleta Kanaani kwa watu Wangu wateule Mashariki. Nitawaleta watu Wangu wateule kutoka kote duniani hadi katika nchi ya Kanaani, na hivyo Ninaendelea kutoa matamko katika nchi ya Kanaani ili kuudhibiti ulimwengu mzima. Wakati huu, hakuna nuru katika dunia nzima. Mbali na wale walio Kanaani, watu wote wanahatarishwa na njaa na baridi. Niliipa Israeli utukufu Wangu na kisha nikautwaa, na hivyo kuwaleta Waisraeli Mashariki, na pia kuwaleta watu wote Mashariki, Nikiwaleta wote kwenye nuru ili waweze kuunganishwa nayo tena, na kuwa na ushirika nayo, na wasitafute tena. Nitawafanya wote wanaotafuta waweze kuiona nuru tena, waone utukufu Niliokuwa nao huko Israeli, waone kwamba Nimeshuka tangu zamani juu ya wingu jeupe miongoni mwa wanadamu, na waone makundi ya mawingu meupe na matunda katika vicha vingi. Zaidi ya hayo, Nitawafanya waweze kumwona Yehova Mungu wa Israeli, wamwone "Mwalimu" wa Wayahudi, wamwone Masihi aliyengojewa kwa hamu, na waone kuonekana Kwangu kikamilifu, Yeye ambaye ameteswa na wafalme katika enzi zote. Nitafanya kazi juu ya ulimwengu mzima na Nitafanya kazi kuu, Nikifunua utukufu Wangu wote na matendo Yangu yote kwa mwanadamu katika siku za mwisho, na kufunua uso Wangu wote wenye utukufu kwa wale ambao wamenisubiria kwa miaka mingi, kwa wale ambao wametamani Mimi nije juu ya wingu jeupe, kwa Israeli ambayo imetamani Mimi nionekane kwa mara nyingine tena, na kwa wanadamu wote wanaonitesa, ili wote wajue kwamba Nimechukua utukufu Wangu tangu zamani na kuuleta Mashariki, na kwamba hauko Yudea tena, kwa maana siku za mwisho tayari zimefika!

Katika ulimwengu mzima Ninafanya kazi Yangu, na Mashariki, mvumo wa ngurumo unatoka bila kikomo, ukitikisa mataifa na madhehebu yote. Ni matamko Yangu ndiyo yamewaongoza watu wote hadi leo. Ninawafanya watu wote washindwe na matamko Yangu, waingie katika mkondo huu, na wajisalimishe mbele Zangu, kwa maana Nimeuondoa utukufu Wangu kutoka katika dunia nzima tangu zamani na kuutoa upya Mashariki. Ni nani asiyetamani kuuona utukufu Wangu? Ni nani asiyetazamia kwa hamu kurudi Kwangu? Ni nani asiyeonea kiu kuonekana Kwangu tena? Ni nani asiyetamani kupendeza Kwangu? Ni nani ambaye hangekuja kwenye nuru? Ni nani ambaye hangetazama utajiri wa Kanaani? Ni nani asiyetamani kurejea kwa Mkombozi? Ni nani asiyemstahi Yeye aliye na uwezo mkuu? Matamko Yangu yatapandwa kote duniani na Nitatoa matamko na kunena maneno zaidi kwa watu Wangu wateule, kama ngurumo kuu inavyotikisa milima na mito. Ninanena maneno Yangu kwa ulimwengu mzima na kwa binadamu. Kwa hivyo maneno kutoka kinywani Mwangu yamekuwa hazina ya mwanadamu, na watu wote wanathamini maneno Yangu. Umeme unamulika kutoka Mashariki hadi Magharibi. Maneno Yangu ni ya namna ambayo mwanadamu hawezi kutaka kuachana nayo, na pia hayawezi kueleweka kwa mwanadamu, na zaidi ya hayo yanamfanya mwanadamu ahisi furaha. Kama watoto wachanga, watu wote wanahisi furaha na shangwe, na wanasherehekea kuja Kwangu. Kwa njia ya matamko Yangu, Nitawaleta watu wote mbele Zangu. Kuanzia hapo, Nitaingia rasmi miongoni mwa wanadamu, na kuwafanya waje kunitolea heshima kuu. Kwa utukufu Ninaoutoa na maneno kutoka kinywani Mwangu, watu wote wanakuja mbele Zangu, na kuona kwamba umeme unamulika kutoka Mashariki, kwamba Nimeshuka pia juu ya "Mlima wa Mizeituni" katika Mashariki, na Nimekuja duniani tangu zamani, na kwamba Mimi si Mwana wa Wayahudi tena, bali Umeme wa Mashariki. Kwa maana Nilishafufuka zamani, na kuondoka miongoni mwa binadamu, na kisha kuonekana tena na utukufu miongoni mwao. Mimi ndimi Niliyeabudiwa kwa enzi zisizohesabika zilizopita, na Mimi pia ndimi mtoto mchanga aliyetelekezwa na Waisraeli enzi zisizohesabika zilizopita. Zaidi ya hayo, Mimi ni Mwenyezi Mungu mwenye utukufu wote wa enzi ya sasa! Wote na waje mbele ya kiti Changu cha enzi waone uso Wangu mtukufu, wasikie matamko Yangu, na watazame matendo Yangu. Huu ndio ukamilifu wa nia Yangu; ni mwisho na kilele cha mpango Wangu, na vilevile lengo la usimamizi Wangu: kuyafanya mataifa yasiyohesabika yanitolee heshima, vinywa visivyohesabika vinikiri, watu wasiohesabika waweke tumaini lao Kwangu, na watu Wangu wateule wasiohesabika wajisalimishe Kwangu!

Maelezo ya chini:

a. Nakala ya asili haina kirai "kuona kwamba."

Iliyotangulia: Unapaswa Kuishi kwa Ajili ya Ukweli Kwa Kuwa Unamwamini Mungu

Inayofuata: Tofauti Muhimu Kati ya Mungu Mwenye Mwili na Watu Wanaotumiwa na Mungu

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp