Ufalme wa Milenia Umewadia

Je, mmeona ni kazi gani ambayo Mungu atatimiza katika kundi hili la watu? Mungu alisema wakati mmoja, hata katika Ufalme wa Milenia bado lazima watu wafuate matamko Yake kusonga mbele, na katika siku za usoni matamko ya Mungu bado yataelekeza moja kwa moja maisha ya mwanadamu katika nchi nzuri ya Kanaani. Musa alipokuwa nyikani, Mungu alimpa maagizo na kuzungumza na yeye moja kwa moja. Kutoka mbinguni Mungu alituma chakula, maji na mana ili watu wafurahie, na leo bado ni vivyo hivyo: Mungu binafsi ameshusha vitu vya kula na kunywa ili watu wafurahie, na Yeye binafsi ametuma laana ili kuwaadibu watu. Na hivyo, kila hatua ya kazi Yake inatekelezwa na Mungu binafsi. Leo, watu wanatafuta kutokea kwa ukweli, wanatafuta kuona ishara na maajabu, na inawezekana kwamba watu wote kama hao wataachwa, kwa kuwa kazi ya Mungu inazidi kuwa ya utendaji. Hakuna anayejua kwamba Mungu ameshuka kutoka mbinguni, pia hawajui kwamba Mungu ametuma chakula na virutubisho kutoka mbinguni—hata hivyo Mungu yupo kweli, na hali ya kusisimua ya Ufalme wa Milenia ambayo watu wanawazia pia ni Mungu binafsi akitoa matamko. Huu ni ukweli, na hili pekee ndilo linaloitwa kutawala pamoja na Mungu duniani. Kutawala pamoja na Mungu duniani kunarejelea mwili. Kile ambacho si cha mwili hakipo duniani, na hivyo wale wote wanaozingatia kwenda katika mbingu ya tatu wanafanya hivyo bure. Siku moja, ulimwengu mzima utakapomrudia Mungu, kitovu cha kazi Yake katika ulimwengu kitafuata matamko Yake. Kwingineko, watu wengine watatumia simu, wengine watapanda ndege, wengine watapanda boti kuvuka bahari, na wengine watatumia leza kupokea matamko ya Mungu. Kila mtu atajawa na kustaajabu na kutamani sana. Wote watamkaribia Mungu, na watakusanyika kumwelekea Mungu, na wote watamwabudu Mungu. Na haya yote yatakuwa matendo ya Mungu. Kumbukeni hili! Hakika Mungu hataanza tena mahali pengine. Mungu atatimiza ukweli huu: Atawafanya watu wote katika ulimwengu waje mbele Zake na wamwabudu Mungu duniani. Kazi Yake katika maeneo mengine itakoma, na watu watalazimika kutafuta njia ya kweli. Itakuwa kama Yusufu: Kila mtu alimjia kwa ajili ya chakula, na alimsujudia, kwa maana alikuwa na vitu vya kula. Ili kuepuka janga la njaa, watu watalazimika kutafuta njia ya kweli. Ulimwengu mzima wa kidini utateseka kwa njaa kali, na Mungu wa leo pekee ndiye chemchemi ya maji ya uzima, Aliye na chemchemi inayotiririka daima iliyotolewa kwa ajili ya kufurahia kwa mwanadamu, na watu watakuja na kumtegemea Yeye. Huo ndio utakuwa wakati ambapo matendo ya Mungu yatafunuliwa na ambapo Mungu atapata utukufu; watu wote katika ulimwengu watakuja kutoa heshima kwa “mwanadamu” huyu wa kawaida. Je, si hii itakuwa siku ambayo Mungu anapata utukufu? Siku moja, wachungaji wazee watatuma telegramu wakitafuta maji kutoka katika chemchemi ya maji ya uzima. Watakuwa wazee, lakini bado watakuja kumwabudu mtu huyu, ambaye walimdharau. Watamkiri kwa vinywa vyao na watamwamini mioyoni mwao—je, si hii ni ishara na maajabu? Siku ambayo ufalme mzima utashangilia itakuwa siku ambayo Mungu atapata utukufu, na yeyote atakayekuja kwenu na kupokea habari njema ya Mungu atabarikiwa na Mungu, na nchi na watu wanaofanya hivyo watabarikiwa na kutunzwa na Mungu. Mwelekeo wa siku za usoni utakuwa huu: Wale wanaopokea matamko ya Mungu watakuwa na njia ya kuendelea mbele duniani, na iwe wanajihusisha na biashara, utafiti wa kisayansi, elimu, au viwanda, wale ambao hawana matamko ya Mungu watashindwa kupiga hata hatua moja, na watalazimika kutafuta njia ya kweli. Hii ndiyo maana ya, “Ukiwa na ukweli utatembea ulimwengu mzima; bila ukweli, hutafanikiwa katika lolote.” Huu ni ukweli. Mungu anatumia Njia (ambayo inamaanisha maneno Yake yote) kudhibiti ulimwengu mzima na kuwa bwana wa wanadamu na kuwashinda. Watu daima wanatumaini mabadiliko makubwa katika njia anazotumia Mungu kufanya kazi. Kusema kweli, ni kupitia maneno ndiyo Mungu huwadhibiti watu, na lazima ufanye kile Anachosema iwe unataka au la; huu ni ukweli usiopingika, na ni sharti ukubaliwe na wote, na hivyo, pia, hauepukiki, na unajulikana na wote.

Roho Mtakatifu huwapa watu hisia: Baada ya kusoma maneno ya Mungu, mioyoni mwao watu huhisi uthabiti na wenye amani, huku wale ambao hawapati maneno ya Mungu wakihisi utupu. Hivyo ndivyo ulivyo uweza wa maneno ya Mungu; ni sharti watu wayasome, na baada ya kuyasoma wanarutubishwa, na hawawezi kuishi bila kuyasoma. Ni kama wakati watu wanatumia afyuni: Inawapa nguvu, na bila hiyo wanahisi mvuto wake wenye nguvu, na wanakosa nguvu. Hivyo ndivyo ulivyo mwelekeo miongoni mwa watu leo. Kusoma maneno ya Mungu huwapa watu nguvu. Wasipoyasoma, wanahisi dhaifu kimwili, lakini baada ya kuyasoma, mara moja wanainuka kutoka kwenye “vitanda vyao vya wagonjwa.” Hili kwa kweli ni neno la Mungu likitumia mamlaka duniani na Mungu akitawala kama Mfalme duniani. Watu wengine wanataka kuondoka, au wameichukia kazi ya Mungu. Licha ya hayo, hawawezi kujitenga na maneno ya Mungu; haijalishi mtu ni dhaifu kiasi gani, lazima bado aishi kwa kuyategemea maneno ya Mungu, na haijalishi yeye ni mwasi kiasi gani, bado hathubutu kuyaacha maneno ya Mungu. Wakati maneno ya Mungu yanafunua uweza wayo kweli ndio wakati ambapo Mungu anatawala kama Mfalme na kutumia mamlaka; hivi ndivyo Mungu anavyofanya kazi. Kwa ufupi, hii ndiyo njia ambayo kwayo Mungu anafanya kazi, na hakuna anayeweza kuwa bila maneno ya Mungu. Maneno ya Mungu yataenea miongoni mwa nyumba zisizohesabika, yakijulikana na wote, na hapo tu ndipo kazi Yake itakuwa imeenea katika ulimwengu mzima. Yaani, ili kazi ya Mungu ienee katika ulimwengu mzima, basi maneno Yake lazima yaenezwe. Siku ambayo Mungu atapata utukufu, maneno ya Mungu yataonyesha mamlaka na uweza wa maneno hayo. Kila moja ya maneno Yake tangu kabla ya enzi hadi leo litatimizwa na litatimia. Kwa njia hii, Mungu atakuwa amepata utukufu duniani—yaani, maneno Yake yatatumia mamlaka duniani. Watu wote waovu wataadibiwa kama matokeo ya maneno yaliyonenwa kutoka kinywani mwa Mungu, wote walio wenye haki watabarikiwa kama matokeo ya maneno yaliyonenwa kutoka kinywani Mwake, na yote yataanzishwa na kufanikishwa kwa maneno yaliyonenwa kutoka kinywani Mwake. Yeye hataonyesha ishara au maajabu yoyote; yote yatafanikishwa kwa maneno Yake, na maneno Yake yataleta ukweli. Kila mtu duniani atatangaza na kusifu sana maneno ya Mungu; iwe ni watu wazima au watoto, mwanamume, mwanamke, mzee au kijana, watu wote watajisalimisha chini ya maneno ya Mungu. Maneno ya Mungu yanaonekana katika mwili, na pia yanawaruhusu watu kuyaona duniani, yakiwa na nguvu na yakiwa hai. Hii ndiyo maana ya Neno kuwa mwili. Mungu amekuja duniani kimsingi kutimiza ukweli wa “Neno kuwa mwili,” yaani, Amekuja ili maneno Yake yaweze kutolewa kutoka katika mwili (sio kama wakati wa Musa katika Agano la Kale, wakati sauti ya Mungu ilitoka moja kwa moja angani). Baada ya hapo, maneno Yake yote yatatimizwa wakati wa Enzi ya Ufalme wa Milenia, yatakuwa ukweli unaoonekana mbele ya macho ya mwanadamu, na watu watayatazama kwa kutumia macho yao wenyewe bila tofauti hata kidogo. Huu ndio umuhimu mkubwa wa Mungu kupata mwili. Yaani, kazi ya Roho inatimizwa kupitia mwili, na kupitia maneno. Hii ndiyo maana ya kweli ya “Neno kuwa mwili” na “kuonekana kwa Neno katika mwili.” Mungu pekee ndiye anayeweza kunena nia za Roho, na Mungu katika mwili pekee ndiye anayeweza kuzungumza kwa niaba ya Roho; maneno ya Mungu yanadhihirishwa katika Mungu mwenye mwili, na kila mtu mwingine anaongozwa nayo. Hakuna anayeweza kukwepa hili; wote wapo ndani ya upeo huu. Kutokana na matamko haya pekee ndiyo watu wanaweza kufahamu; bila hayo, watu wanaota ndoto ikiwa wanafikiri wanaweza kupata matamko kutoka mbinguni. Haya ndiyo mamlaka yanayodhihirishwa katika mwili wa Mungu aliyepata mwili, yakiwasababisha wote kuamini katika hilo kwa usadikisho kamili. Hata wataalamu wanaoheshimika kabisa na wachungaji wa kidini hawawezi kunena maneno haya. Wote lazima wajisalimishe chini ya maneno hayo, na hakuna atakayeweza kuanza upya. Mungu atatumia maneno kuushinda ulimwengu. Yeye hatafanya hili kwa mwili Wake alioupata, bali kwa kutumia matamko kutoka kinywani mwa Mungu aliyekuwa mwili kuwashinda watu wote katika ulimwengu mzima; hili pekee ndilo Neno kuwa mwili, na hili pekee ndilo kuonekana kwa Neno katika mwili. Pengine, kwa binadamu, inaonekana kana kwamba Mungu hajafanya kazi yoyote kuu—lakini punde tu Mungu anapotoa matamko Yake, watasadikishwa kikamilifu na kubaki vinywa wazi. Bila mambo ya hakika, watu hupiga kelele na kupiga mayowe; wakiwa na maneno ya Mungu, wananyamaza kimya. Hakika Mungu atatimiza ukweli huu, kwani huu ni mpango wa Mungu uliowekwa tangu zamani: kutimiza ukweli wa kuwasili kwa Neno duniani. Kwa kweli, hakuna haja ya Mimi kulifafanua—kuwasili kwa Ufalme wa Milenia duniani ni kuwasili kwa maneno ya Mungu duniani. Kushuka kwa Yerusalemu Mpya kutoka mbinguni ni kuwasili kwa maneno ya Mungu ili kuishi miongoni mwa binadamu, kuandamana na kila kitendo cha binadamu, kila wazo na fikira yake. Huu pia ni ukweli ambao Mungu atautimiza; huu ndio uzuri wa Ufalme wa Milenia. Huu ndio mpango uliowekwa na Mungu: Maneno Yake yataonekana duniani kwa miaka elfu moja, na yatafunua matendo Yake yote, na kukamilisha kazi Yake yote duniani, na baada ya hilo hatua hii ya binadamu itafikia kikomo.

Iliyotangulia: Amri za Enzi Mpya

Inayofuata: Uhusiano Wako na Mungu Ukoje?

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp