Uhusiano Wako na Mungu Ukoje?

Katika kumwamini Mungu, angalau lazima utatue suala la kuwa na uhusiano wa kawaida na Mungu. Ikiwa huna uhusiano wa kawaida na Mungu, basi maana ya imani yako katika Mungu imepotea. Kuanzishwa kwa uhusiano wa kawaida na Mungu kunaweza kufikiwa kabisa kwa moyo ulio kimya katika uwepo wa Mungu. Kuwa na uhusiano wa kawaida na Mungu kunamaanisha kuweza kutokuwa na shaka na kutoikana kazi yoyote Yake na kuweza kuitii kazi Yake. Kunamaanisha kuwa na nia zisizo na makosa katika uwepo wa Mungu, kutofanya mipango kwa ajili yako mwenyewe, na kuzingatia masilahi ya familia ya Mungu kwanza katika mambo yote; kunamaanisha kukubali uchunguzi wa Mungu na kuitii mipango ya Mungu. Lazima uweze kuutuliza moyo wako katika uwepo wa Mungu katika yote ufanyayo. Hata kama huyaelewi mapenzi ya Mungu, bado unapaswa kutekeleza wajibu na majukumu yako kadiri uwezavyo. Mara tu mapenzi ya Mungu yanapofichuliwa kwako, lichukulie hatua, na hutakuwa umechelewa mno. Wakati ambapo uhusiano wako na Mungu umekuwa wa kawaida, basi pia utakuwa na uhusiano wa kawaida na watu. Kila kitu kimejengwa kwa msingi wa maneno ya Mungu. Kula na unywe maneno ya Mungu, kisha uyatie matakwa ya Mungu katika vitendo, rekebisha maoni yako, na uepuke kufanya chochote ili kumpinga Mungu au kulivuruga kanisa. Usifanye chochote ambacho hakifaidi maisha ya ndugu zako, usiseme chochote kisichowasidia wengine, na usifanye jambo lolote la aibu. Kuwa mwenye haki na mwenye heshima katika jambo unalotenda na uhakikishe kuwa kila kitendo chako kinapendeza mbele za Mungu. Ingawa wakati mwingine mwili unaweza kuwa dhaifu, lazima uweze kuweka masilahi ya familia ya Mungu kwanza, bila tamaa ya kupata faida ya kibinafsi, na lazima uweze kutenda kwa haki. Ikiwa unaweza kutenda kwa namna hii, basi uhusiano wako na Mungu utakuwa wa kawaida.

Katika kila jambo unalofanya, sharti uchunguze ikiwa nia zako hazina makosa. Ikiwa unaweza kutenda kulingana na matakwa ya Mungu, basi uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida. Hiki ndicho kiwango cha chini kabisa. Chunguza nia zako, na ukiona kwamba nia mbaya zimejitokeza, uweze kuziacha na kutenda kulingana na maneno ya Mungu; hivyo utakuwa mtu aliye sawa mbele za Mungu, ambayo inaonyesha kwamba uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida, na kwamba yote unayoyafanya ni kwa ajili ya Mungu, si kwa ajili yako. Katika yote unayofanya na yote unayosema, uweze kuuweka moyo wako uwe sawa na uwe mwenye haki katika matendo yako, na usiongozwe na hisia zako, wala kutenda kulingana na mapenzi yako mwenyewe. Hizi ni kanuni ambazowaumini katika Mungu wanapaswa kutenda. Mambo madogo yanaweza kufichua nia na kimo cha mtu, na kwa hivyo, ili mtu aweze kuingia kwenye njia ya kukamilishwa na Mungu, lazima kwanza arekebishe nia zake na uhusiano wake na Mungu. Ni wakati tu uhusiano wako na Mungu unapokuwa wa kawaida ndipo unaweza kukamilishwa na Yeye; ni wakati huo tu ndipo ushughulikiaji, upogoaji, ufundishaji nidhamu, na usafishaji wa Mungu vifanikisha athari zake zilizokusudiwa ndani yako. Hiyo ni kusema, ikiwa wanadamu wanaweza kumweka Mungu mioyoni mwao na wasifuatilie faida ya kibinafsi au kufikiria matarajio yao wenyewe (kwa njia ya mwili), lakini badala yake wabebe mzigo wa kuingia katika uzima, wajitahidi kabisa kuufuatilia ukweli, na kuitii kazi ya Mungu—ikiwa unaweza kufanya hivi, basi malengo unayoyafuatilia yatakuwa sawa, na uhusiano wako na Mungu utakuwa wa kawaida. Kuufanya uhusiano wa mtu na Mungu uwe muwafaka kunaweza kuitwa hatua ya kwanza ya kuingia katika safari ya kiroho ya mtu. Ingawa hatima ya mwanadamu iko mikononi mwa Mungu na imeamuliwa kabla na Mungu, na haiwezi kubadilishwa na mwanadamu, kama unaweza kukamilishwa na Mungu au kupatwa na Yeye kunategemea ikiwa uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida. Kunaweza kuwa na sehemu fulani ndani yako ambazo ni dhaifu au zisizotii—lakini mradi maoni yako na nia zako ni sawa, na mradi uhusiano wako na Mungu uko sawa na wa kawaida, basi unastahili kukamilishwa na Mungu. Ikiwa huna uhusiano muwafaka na Mungu, na unatenda kwa ajili ya mwili au familia yako, basi bila kujali jinsi unavyotia bidii, itakuwa bure. Ikiwa uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida, basi kila kitu kingine kitakuwa sawa. Mungu haangalii kitu kingine chochote, lakini tu ikiwa maoni yako katika imani yako katika Mungu yako sawa: unamwamini nani, unaamini kwa ajili ya nani, na kwa nini unaamini. Ikiwa unaweza kuona mambo haya waziwazi na kutenda wakati maoni yako yakiwa na mwelekeo mzuri, basi utaendelea katika maisha yako, na pia utahakikishiwa kuingia kwenye njia muwafaka. Ikiwa uhusiano wako na Mungu si wa kawaida, na maoni ya imani yako katika Mungu yamepotoka, basi mengine yote ni bure, na haijalishi kadiri unavyoamini, hutapokea chochote. Ni baada tu ya uhusiano wako na Mungu kuwa wa kawaida ndipo utakapopata sifa kutoka Kwake unapoukana mwili, uombe, uteseke, uvumilie, utii, uwasaidie ndugu zako, ujitumie zaidi kwa ajili ya Mungu, na kadhalika. Kama kile unachofanya kina thamani na umuhimu inategemea ikiwa nia zako ni sawa na maoni yako hazina makosa. Siku hizi, watu wengi wanamwamini Mungu kana kwamba wanageuza vichwa vyao ili kutazama saa—mitazamo yao imepotoka, na lazima irekebishwe kwa mafanikio mapya. Ikiwa shida hii itatatuliwa, kila kitu kitakuwa sawa; la sivyo, kila kitu kitakuwa bure. Watu wengine ni wenye tabia nzuri mbele Zangu, lakini bila Mimi kujua, wananipinga tu. Hili ni onyesho la upotovu na udanganyifu, na mtu wa aina hii ni mtumishi wa Shetani; yeye ni mfano halisi wa Shetani, aliyekuja kumjaribu Mungu. Wewe ni mtu sahihi tu ikiwa unaweza kuitii kazi Yangu na maneno Yangu. Mradi unaweza kula na kunywa maneno ya Mungu; mradi kila kitu unachofanya kinapendeza mbele za Mungu na unaenenda kwa njia ya haki na kwa heshima katika yote unayofanya; mradi hufanyi mambo ya aibu, au mambo ambayo yanaweza kuyadhuru maisha ya wengine; na mradi unaishi katika nuru na hujiruhusu kudhulumiwa na Shetani, basi uhusiano wako na Mungu uko katika mpangilio unaofaa.

Kumwamini Mungu kunakuhitaji uweke nia na maoni yako katika mpangilio unaofaa; unapaswa kuwa na ufahamu muwafaka wa, na njia muwafaka ya kuyachukulia maneno ya Mungu na kazi ya Mungu, mazingira yote ambayo Mungu hupanga, mtu ambaye Mungu humshuhudia, na Mungu wa vitendo. Hupaswi kutenda kulingana na dhana zako mwenyewe au kubuni miradi yako mwenyewe iliyo midogomidogo. Chochote unachofanya, sharti uweze kuutafuta ukweli na, katika nafasi yako kama kiumbe aliyeumbwa, uitii kazi yote ya Mungu. Ikiwa unataka kufuatilia kukamilishwa na Mungu na kuingia kwenye njia muwafaka ya maisha, basi lazima moyo wako uishi katika uwepo wa Mungu daima. Usiwe mwovu, usimfuate Shetani, usimpe Shetani fursa zozote za kutekeleza kazi yake, na usimruhusu Shetani akutumie. Lazima ujitolee kwa Mungu kabisa na umruhusu Mungu akutawale.

Je, uko tayari kuwa mtumishi wa Shetani? Uko tayari kutumiwa vibaya na Shetani? Unamwamini Mungu na kumfuatilia ili uweze kukamilishwa na Yeye, au ili uweze kuwa foili[a] kwa ajili ya kazi Mungu? Ungependa maisha yenye kusudi ambayo unapatwa na Mungu, au maisha yasiyofaa na matupu? Ungependa kutumiwa na Mungu, au kudhulumiwa na Shetani? Ungependa kuruhusu maneno na ukweli wa Mungu vikujaze, au uruhusu kujazwa na dhambi na Shetani? Zingatia mambo haya kwa uangalifu. Katika maisha yako ya kila siku, lazima uelewe ni maneno gani unayoyasema na ni mambo gani unayoyafanya ndiyo yanaweza kusababisha hitilafu katika uhusiano wako na Mungu, na kisha ujibadilishe ili uingie katika njia muwafaka. Wakati wote, yachunguze maneno yako, matendo yako, kila harakati yako, na mawazo na maoni yako yote. Pata ufahamu muwafaka kuhusu hali yako halisi na uingie katika njia ya kazi ya Roho Mtakatifu. Hii ndiyo njia ya pekee ya kuwa na uhusiano wa kawaida na Mungu. Kwa kutathmini kama uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida, utaweza kurekebisha nia zako, kuelewa asili na kiini cha mwanadamu, na kujielewa kwa kweli, na kwa kufanya hivyo, utaweza kuingia katika matukio halisi, ujikane kwa njia halisi, na kutii kwa kusudi. Unapopitia mambo haya kuhusu ikiwa uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida au la, utapata fursa za kukamilishwa na Mungu na kuweza kufahamu hali nyingi za kazi ya Roho Mtakatifu. Pia utaweza kubaini hila nyingi za Shetani na kufahamu njama zake. Njia hii tu ndiyo inayosababisha kukamilishwa na Mungu. Rekebisha uhusiano wako na Mungu, ili uweze kutii mpangilio Wake kwa ukamilifu, na ili uweze kuingia kwa undani hata zaidi katika matukio halisi na kupokea kazi zaidi ya Roho Mtakatifu. Ukijizoeza kuwa na uhusiano wa kawaida na Mungu, mara nyingi, mafanikio yatapatikana kwa kuukana mwili na kupitia kwa ushirikiano wa kweli na Mungu. Unapaswa kuelewa kwamba “bila moyo wa kushirikiana, ni vigumu kuipokea kazi ya Mungu; ikiwa mwili hautateseka, hakutakuwa na baraka kutoka kwa Mungu; ikiwa roho haijitahidi sana, Shetani hataaibishwa.” Ukifuata kanuni hizi na uzielewe kabisa, maoni ya imani yako katika Mungu yatarekebishwa. Katika kutenda kwako kwa sasa, lazima uache fikira ya “kutafuta mkate ili kukidhi njaa”; lazima uache fikira ya “kila kitu kinafanywa na Roho Mtakatifu, na watu hawawezi kuingilia kati.” Kila mtu asemaye hivyo hufikiria, “Watu wanaweza kufanya chochote watakacho, na wakati ufikapo, Roho Mtakatifu atafanya kazi Yake. Watu hawana haja ya kuuzuia mwili au kushirikiana; jambo la maana ni kwamba waguswe na Roho Mtakatifu.” Maoni haya yote ni ya kipumbavu. Katika hali kama hizo, Roho Mtakatifu hawezi kufanya kazi. Ni mtazamo wa aina hii ndio unaoizuia sana kazi ya Roho Mtakatifu. Mara nyingi, kazi ya Roho Mtakatifu hufikiwa kupitia ushirikiano wa binadamu. Wale ambao hawashirikiani na hawajaamua, ilhali wanataka kupata mabadiliko katika tabia yao na kuipokea kazi ya Roho Mtakatifu na nuru na mwangaza kutoka kwa Mungu, wana mawazo ya kupita kiasi kweli. Hii inaitwa “kujifurahisha na kumsamehe Shetani.” Watu kama hao hawana uhusiano wa kawaida na Mungu. Unapaswa kuona ufunuo na udhihirisho mwingi wa tabia ya kishetani ndani yako mwenyewe na uone mazoea yoyote ambayo unayo yaliyo kinyume na kile ambacho Mungu anahitaji sasa. Je, sasa utaweza kumkana Shetani? Unapaswa kufikia uhusiano wa kawaida na Mungu, kutenda kulingana na nia ya Mungu, na kuwa mtu mpya aliye na maisha mpya. Usifikiri sana kuhusu makosa ya zamani; usiwe mwenye kujuta mno; uweze kusimama na kushirikiana na Mungu, na utimize wajibu unaopaswa kutimiza. Kwa njia hii, uhusiano wako na Mungu utakuwa wa kawaida.

Ikiwa baada ya kusoma makala haya, unadai tu kukubali maneno haya, ilhali moyo wako hauguswi, na hutafuti kufanya uhusiano wako na Mungu uwe wa kawaida, inathibitisha kwamba hutilii maanani uhusiano wako na Mungu. Inathibitisha kwamba maoni yako bado hayajarekebishwa, kwamba nia zako bado hazijadhamiria kupatwa na Mungu na kumletea Yeye utukufu, lakini badala yake zimedhamiria kuruhusu njama za Shetani zitawale na kufanikisha malengo yako mwenyewe. Watu kama hao wanahodhi nia mbaya na maoni yaliyo na makosa. Haijalishi lile analosema Mungu au jinsi Anavyolisema, watu kama hao hubaki wasiojali kabisa na hawabadiliki hata kidogo. Mioyo yao haihisi woga na wao hawaoni haya. Mtu kama huyo ni mjinga aliyekata tamaa. Soma matamko yote ya Mungu na uyatie katika vitendo mara tu utakapoyaelewa. Labda kulikuwa na nyakati ambapo mwili wako ulikuwa dhaifu, au ulikuwa mwasi, au ulipinga; bila kujali jinsi ulivyotenda zamani, si muhimu, na haiwezi kuyazuia maisha yako kukomaa leo. Mradi unao uhusiano wa kawaida na Mungu leo, kuna matumaini. Ikiwa kuna mabadiliko ndani yako kila wakati unapoyasoma maneno ya Mungu, na wengine wanaweza kukuambia kuwa maisha yako yamebadilika na kuwa bora, inaonyesha kuwa uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida sasa, kwamba umerekebishwa. Mungu hawatendei watu kulingana na makosa yao. Mara tu unapoelewa na kufahamu, mradi unaweza kuacha kuasi au kupinga, basi bado Mungu atakuonea huruma. Unapokuwa na ufahamu na azimio la kufuatilia kukamilishwa na Mungu, basi hali yako katika uwepo wa Mungu itakuwa ya kawaida. Haijalishi unachofanya, fikiria yafuatayo wakati unapofanya jambo hilo: Je, Mungu atafikiria nini nikifanya hili? Litawafaidi ndugu zangu? Litaifaidi kazi katika nyumba ya Mungu? Iwe ni katika sala, ushirika, hotuba, kazi, au kuwasiliana na wengine, zichunguze nia zako, na uchunguze ikiwa uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida. Ikiwa huwezi kutambua nia na mawazo yako mwenyewe, hii inamaanisha kuwa huna upambanuzi, ambayo inathibitisha kwamba unaelewa ukweli kidogo sana. Ikiwa unaweza kuelewa vizuri kila kitu ambacho Mungu hufanya, na unaweza kuyatazama mambo kupitia katika maneno Yake, ukisimama upande Wake, basi maoni yako yatakuwa yamekuwa yasiyo na makosa. Kwa hivyo, kuanzisha uhusiano mzuri na Mungu ni muhimu sana kwa mtu yeyote anayemwamini Mungu; kila mtu anapaswa kuliona kama kazi muhimu sana na tukio kubwa kabisa katika maisha yake. Kila kitu unachofanya kinapimwa na kama una uhusiano wa kawaida na Mungu. Ikiwa uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida na nia zako ni zisizo na makosa, basi chukua hatua. Ili kudumisha uhusiano wa kawaida na Mungu, hupaswi kuogopa kupata hasara kwa masilahi yako ya kibinafsi; huwezi kumruhusu Shetani atawale, huwezi kumruhusu Shetani akununue, na huwezi kumruhusu Shetani akufanye uwe kichekesho. Kuwa na nia kama hiyo ni ishara kwamba uhusiano wako na Mungu ni wa kawaida—si kwa ajili ya mwili, bali ni kwa ajili ya amani ya roho, kwa ajili ya kuipata kazi ya Roho Mtakatifu, na kwa ajili ya kuyaridhisha mapenzi ya Mungu. Ili kuingia katika hali inayofaa, lazima uimarishe uhusiano mzuri na Mungu na urekebishe maoni ya imani yako katika Mungu. Hii ni ili Mungu aweze kukupata, na ili Aweze kudhihirisha matunda ya maneno Yake ndani yako na kukupa nuru na kukuangazia hata zaidi. Kwa njia hii, utakuwa umeingia katika njia inayofaa. Endelea kula na kunywa maneno ya Mungu ya leo, ingia katika njia ya sasa ya Roho Mtakatifu ya kufanya kazi, tenda kulingana na matakwa ya Mungu ya leo, usifuate mbinu za zamani za kutenda, usishikilie njia za zamani za kufanya mambo, na uingie katika njia ya leo ya kufanya kazi haraka iwezekanavyo. Hivyo, uhusiano wako na Mungu utakuwa wa kawaida kabisa na utakuwa umeanza kutembea katika njia muwafaka ya imani katika Mungu.

Tanbihi:

a. Mtu/kitu kinachodhihirisha uzuri/ubora wa kingine kwa kuvilinganisha

Iliyotangulia: Ufalme wa Milenia Umewasili

Inayofuata: Sisitiza Uhalisi Zaidi

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp