Ni Wale tu Wanaoijua Kazi ya Sasa ya Mungu Ndio Wanaoweza Kumtumikia Mungu

Ili kuwa na ushuhuda kwa Mungu na kuliaibisha joka kuu jekundu, mtu lazima awe na kanuni, na mtu lazima atimize sharti: Lazima mtu ampende Mungu moyoni mwake na aingie katika maneno Yake. Usipoingia katika maneno ya Mungu, basi hutakuwa na njia ya kumwaibisha Shetani. Kupitia ukuaji katika maisha yako, unaliasi joka kuu jekundu na kuliletea aibu kamili—hii ndiyo maana ya kuliaibisha joka kuu jekundu kwa kweli. Kadiri unavyokuwa radhi kutia maneno ya Mungu katika vitendo, ndivyo uthibitisho wa upendo wako kwa Mungu na chuki yako kwa joka kuu jekundu unavyokuwa mkubwa zaidi; kadiri unavyotii maneno ya Mungu, ndivyo uthibitisho wa kiu yako ya ukweli unavyokuwa mkubwa zaidi. Watu ambao hawana kiu ya maneno ya Mungu ni watu wasio na uzima. Watu kama hao ni wale walio nje ya maneno ya Mungu, ambao ni wa dini. Watu wanaomwamini Mungu kweli wana ufahamu wa kina zaidi wa maneno ya Mungu kupitia kula na kunywa maneno Yake. Usipoyaonea kiu maneno ya Mungu, basi haitawezekana kwako kula na kunywa maneno Yake kwa dhati, na ikiwa huna ufahamu wa maneno ya Mungu, basi huna njia ya kuwa na ushuhuda kwa Mungu au kumridhisha Mungu.

Katika kumwamini Mungu, mtu anapaswa kumjuaje Mungu? Mtu anapaswa kumjua Mungu kulingana na maneno na kazi ya sasa ya Mungu, bila mkengeuko au uwongo, na, kabla ya yote mengine, mtu anapaswa kuijua kazi ya Mungu, ambayo ndiyo msingi wa kumjua Mungu Mwenyewe. Hoja zote mbalimbali za uwongo ambazo hazina ufahamu safi wa maneno ya Mungu ni dhana za kidini; ni ufahamu uliopotoka. Ustadi mkubwa kabisa wa watu wa kidini ni kuchukua maneno ya Mungu yaliyoeleweka zamani na kuyapima maneno ya Mungu ya leo na kuyalinganisha na hayo. Ikiwa, unapomtumikia Mungu wa leo, unashikilia mambo yaliyofunuliwa na nuru ya Roho Mtakatifu zamani, basi huduma yako itasababisha vurugu, na kuwa aina ya utendaji uliopitwa na wakati, si chochote zaidi ya mila za kidini. Ukiamini kwamba wale wanaomtumikia Mungu lazima kwa nje wawe wanyenyekevu na wavumilivu, miongoni mwa sifa nyingine, na ukitia maarifa ya aina hii katika vitendo leo, basi maarifa kama hayo ni dhana ya kidini; kutenda kwa njia hii ni sawa na kuonyesha unafiki. Fungu la maneno "dhana za kidini" linarejelea mambo yaliyopitwa na wakati (ikiwa ni pamoja na ufahamu wa maneno yaliyonenwa na Mungu hapo awali na nuru ya moja kwa moja ya Roho Mtakatifu), na yakitiwa katika vitendo leo, basi yanavuruga kazi ya Mungu na hayaleti faida yoyote kwa mwanadamu. Ikiwa watu hawawezi kujiondolea mambo hayo ambayo ni ya dhana za kidini, basi mambo haya yatakuwa kizuizi kikubwa kwao katika kumtumikia Mungu. Watu walio na dhana za kidini hawana njia ya kwenda sambamba na hatua za kazi ya Roho Mtakatifu—punde tu wanapoachwa nyuma kidogo, wanaendelea kuachwa nyuma zaidi na zaidi. Hii ni kwa sababu dhana hizi za kidini humfanya mwanadamu awe mwenye kujihesabia haki na mwenye kiburi kupita kiasi. Mungu hahisi hamu yoyote juu ya kile Alichosema na kufanya zamani; ikiwa kitu kimepitwa na wakati, Yeye hukiondosha. Je, kwa kweli huwezi kuachilia dhana zako? Ukishikilia maneno ambayo Mungu Alinena zamani, je, hili linathibitisha kwamba unaijua kazi ya Mungu? Ikiwa huwezi kukubali nuru ya sasa ya Roho Mtakatifu, na badala yake unashikilia nuru ya zamani, je, hili linaweza kuthibitisha kwamba unafuata hatua za Mungu? Je, bado huwezi kuachilia dhana za kidini? Ikiwa hivyo ndivyo ilivyo, basi utakuwa mtu anayempinga Mungu.

Ikiwa watu wanaweza kuachana na dhana za kidini, hawatatumia akili zao kupima maneno na kazi ya Mungu ya leo, na badala yake watatii moja kwa moja. Ingawa kazi ya Mungu leo ni tofauti dhahiri na ile ya zamani, bado unaweza kuiachilia mitazamo ya zamani na kutii kazi ya Mungu ya leo moja kwa moja. Ikiwa una uwezo wa kuelewa kwamba lazima uipe kipaumbele kazi ya Mungu ya leo, bila kujali jinsi Mungu Alivyofanya kazi zamani, basi wewe ni mtu ambaye ameachilia dhana zake, anayemtii Mungu, na ambaye anaweza kutii kazi na maneno ya Mungu na kufuata hatua Zake. Katika hili, utakuwa mtu anayemtii Mungu kwa kweli. Huchambui wala huchunguzi kazi ya Mungu; ni kana kwamba Mungu amesahau kazi Yake ya awali, na wewe, pia, umeisahau. Sasa ni sasa, na zamani ni zamani, na kwa kuwa leo, Mungu Ameweka kando kile Alichokifanya zamani, hupaswi kukikazia fikira. Mtu kama huyo pekee ndiye anayemtii Mungu kikamilifu na ameachilia dhana zake za kidini kikamilifu.

Kwa sababu daima kuna maendeleo mapya katika kazi ya Mungu, kuna kazi ambayo hupitwa na wakati na kuwa ya zamani kazi mpya inapoibuka. Aina hizi tofauti za kazi, za zamani na mpya, hazipingani, bali zinakamilishana; kila hatua inafuata kutoka kwa ile iliyotangulia. Kwa sababu kuna kazi mpya, mambo ya zamani lazima, bila shaka, yaondoshwe. Kwa mfano, baadhi ya desturi za muda mrefu na misemo ya kawaida ya mwanadamu, pamoja na miaka mingi ya uzoefu wa mwanadamu na mafunzo aliyojifunza vimeunda kila namna na aina ya dhana katika akili ya mwanadamu. Kwamba Mungu bado Hajafunua kikamilifu uso Wake wa kweli na tabia Yake asili kwa mwanadamu—katika muungano na kuenea, kunakofanyika kwa miaka mingi, kwa nadharia za kitamaduni kuanzia zamani hadi sasa—kumechangia hata zaidi mwanadamu kuunda dhana kama hizo. Inaweza kusemwa kwamba, katika kipindi kizima cha imani ya mwanadamu katika Mungu, ushawishi wa dhana mbalimbali umesababisha kuundwa na kubadilika kwa kuendelea kwa kila aina ya ufahamu wa kidhana wa Mungu ndani ya watu, jambo ambalo limesababisha watu wengi wa kidini wanaomtumikia Mungu kuwa maadui Zake. Kwa hivyo, kadiri dhana za kidini za watu zinavyokuwa na nguvu zaidi, ndivyo wanavyompinga Mungu zaidi, na ndivyo wanavyokuwa maadui wa Mungu zaidi. Kazi ya Mungu daima ni mpya na si ya zamani kamwe—haiundi kanuni kamwe; badala yake, inapitia viwango mbalimbali vya mabadiliko na kufanywa upya kila wakati. Mungu kufanya kazi kwa namna hii ni onyesho la tabia Yake ya asili. Pia ni kanuni asili ya kazi ya Mungu, na mojawapo ya njia za kufanya kazi ambazo kwazo Mungu hutimiza usimamizi Wake. Mungu asingefanya kazi kwa njia hii, mwanadamu asingebadilika au kuweza kumjua Mungu, na Shetani asingeshindwa. Kwa hivyo, katika kazi Yake, mabadiliko hutokea kila wakati ambayo yanaonekana kutokuwa na utaratibu, lakini ambayo kwa kweli ni yenye kutokea kwa vipindi. Hata hivyo, namna ambavyo mwanadamu anamwamini Mungu ni tofauti kabisa. Yeye hushikilia kanuni na mifumo ya zamani anayoifahamu, na kadiri inavyokuwa ya zamani, ndivyo inavyompendeza zaidi. Akili ya kipumbavu ya mwanadamu, akili ambayo ni ngumu kama jiwe, ingewezaje kukubali kazi na maneno mengi mapya ya Mungu yasiyoweza kueleweka? Mwanadamu hampendi Mungu ambaye daima ni mpya na si mzee kamwe; anampenda tu Mungu mzee, ambaye ni mzee sana, mwenye nywele nyeupe, na asiyeweza kutembea. Kwa hivyo, kwa sababu Mungu na mwanadamu kila mmoja ana "mapendeleo" yake, mwanadamu amekuwa adui wa Mungu. Mengi ya mambo haya yanayopingana bado yapo hata leo, wakati ambapo Mungu amekuwa akifanya kazi mpya kwa karibu miaka elfu sita. Basi, hayawezi kurekebishwa. Pengine kwa sababu ya ukaidi wa mwanadamu, au pengine kutokana na kutoweza kukiukwa kwa amri za utawala za Mungu na mwanadamu yeyote, makasisi hao wa kiume na wa kike bado wanashikilia vitabu na karatasi za zamani zilizooza, huku Mungu akiendelea na kazi Yake ya usimamizi ambayo haijakamilika kana kwamba hakuna anayeona. Ingawa kuna mambo kama haya ya uhasama yanayopingana, ambayo hata haiwezekani kuyasuluhisha, Mungu hayatilii maanani, kana kwamba yalikuwepo na wakati huohuo hayakuwepo. Hata hivyo, mwanadamu bado anashikilia imani na dhana zake, na haachani nazo kamwe. Lakini jambo moja ni dhahiri: Ingawa mwanadamu hakengeuki kutoka katika msimamo wake, "miguu" ya Mungu daima inasonga, na Yeye daima Anabadilisha msimamo Wake kulingana na mazingira. Mwishowe, ni mwanadamu ndiye atakayeshindwa bila kupigana. Wakati huohuo, Mungu ndiye "adui mkubwa kabisa" wa maadui Zake wote walioshindwa, na pia ndiye "bingwa" wa binadamu, walioshindwa na wasioshindwa vilevile. Ni nani anayeweza kushindana na Mungu na kuwa mshindi? Dhana za mwanadamu zinaonekana kutoka kwa Mungu kwa sababu nyingi za hizo zilitokea kidogo kidogo kufuatia kazi ya Mungu. Hata hivyo, Mungu hamsamehei mwanadamu kwa sababu ya hili, sembuse kumlimbikizia sifa mwanadamu kwa kuzalisha kundi baada ya kundi la bidhaa "kwa ajili ya Mungu" kufuatia kazi Yake ambazo ziko nje ya kazi Yake. Badala yake, Yeye anachukizwa sana na dhana za mwanadamu na imani ya zamani, ya ucha Mungu, na hata Hana nia ya kuzipa dhana hizi uangalifu wowote kuhusu tarehe ambayo ziliibuka kwa mara ya kwanza. Yeye hakubali hata kidogo kwamba dhana hizi zinasababishwa na kazi Yake, kwa maana dhana za mwanadamu zinatokana na maambukizi ya kibinadamu; chanzo cha dhana hizo ni mawazo na akili ya mwanadamu—sio Mungu, bali Shetani. Nia ya Mungu daima imekuwa kwamba kazi Yake iwe mpya na hai, si ya zamani na iliyokufa, na kile Anachomfanya mwanadamu ashikilie kinatofautiana kulingana na enzi na kipindi, na si cha milele na kisichobadilika. Hii ni kwa sababu Yeye ni Mungu anayemfanya mwanadamu aishi na awe mpya, badala ya ibilisi anayemfanya mwanadamu afe na awe wa zamani. Je, bado hamwelewi hili? Kwamba una dhana kumhusu Mungu na huwezi kuachana nazo ni kwa sababu ya kushindwa kwako kuelewa mambo—si kwa sababu kuna busara kidogo sana katika kazi ya Mungu, wala si kwa sababu kazi Yake haijali hisia za mwanadamu, sembuse kwamba ni kwa sababu Mungu hashughulikii kazi Yake ifaayo kamwe. Huwezi kuachana na dhana zako kwa sababu unapungukiwa sana na utii, na kwa sababu huna mfano wa kiumbe aliyeumbwa hata kidogo; si kwa sababu Mungu anafanya mambo yawe magumu kwako. Wewe ulisababisha haya yote, na hayana uhusiano wowote na Mungu; mateso na maafa yote yanaundwa na mwanadamu. Mawazo ya Mungu daima ni mema: Yeye hataki kukusababisha uunde dhana, bali Anataka ufanywe upya na upitie mabadiliko kadiri enzi zinavyopita. Hata hivyo, hujui kile kilicho chema kwako, na daima unachunguza au unachambua. Si kwamba Mungu anafanya mambo kuwa magumu kwako, bali ni kwamba unakosa moyo umwogopao Mungu, na uasi wako ni mkubwa mno. Kiumbe mdogo aliyeumbwa, anayethubutu kuchukua sehemu ndogo isiyo na maana ya kile ambacho Mungu alitoa hapo awali, na kugeuka na kukitumia kumshambulia Mungu—je, huu si uasi wa mwanadamu? Wanadamu, ni sawa kusema, hawastahili kabisa kutoa maoni yao mbele za Mungu, na hawastahili hata kidogo kujionyesha kwa maneno yao yasiyo na thamani, yanayonuka, yaliyooza, na ya kale wapendavyo—sembuse dhana hizo zilizooza. Je, hazikosi thamani hata zaidi?

Mtu anayemtumikia Mungu kwa kweli ni mtu anayelingana na nia za Mungu, anayestahili kutumiwa na Mungu, na anayeweza kuachilia dhana za kidini. Ukitaka kula na kunywa kwako maneno ya Mungu kuwe na matokeo, basi lazima uachilie dhana zako za kidini. Ukitaka kumtumikia Mungu, basi ni muhimu hata zaidi kwanza kuachilia dhana za kidini na kutii maneno ya Mungu katika kila kitu. Hiki ndicho kinachopaswa kumilikiwa na mtu anayemtumikia Mungu. Ukikosa maarifa haya, basi punde tu unapotumikia, utasababisha vurugu na usumbufu, na ukishikilia dhana zako, basi bila shaka "utaangushwa" na Mungu, na hutainuka tena kamwe. Chukua wakati wa sasa, kwa mfano: Misemo mingi na kazi nyingi hazilingani na Biblia na kazi iliyofanywa na Mungu hapo awali, na usipokuwa na moyo wa utii, basi utaanguka wakati wowote. Kama ungependa kutumikia kulingana na nia za Mungu, basi lazima kwanza uachilie dhana za kidini na urekebishe mitazamo yako mwenyewe. Katika siku zijazo, misemo mingi haitalingana na ile ya zamani, na ikiwa sasa huna azimio la kutii, hutaweza kutembea katika njia iliyo mbele yako. Ikiwa mojawapo ya mbinu za Mungu za kufanya kazi imekita mizizi ndani yako na huiachilii kamwe, basi mbinu hii itakuwa dhana yako ya kidini. Ikiwa kile Mungu alicho kimekita mizizi ndani yako, basi umepata ukweli, na ikiwa maneno na ukweli wa Mungu vinakuwa uzima wako, hutakuwa tena na dhana kumhusu Mungu. Wale walio na ufahamu wa kweli wa Mungu hawatakuwa na dhana na hawatafuata taratibu.

Uliza maswali haya ili uwe macho wewe mwenyewe:

1. Je, maarifa yaliyo ndani yako yanasumbua huduma yako kwa Mungu?

2. Kuna matendo mangapi ya kidini katika maisha yako ya kila siku? Ikiwa unaonyesha tu mwonekano wa ucha Mungu, je, hili linamaanisha kwamba maisha yako yamekua na kukomaa?

3. Unapokula na kunywa maneno ya Mungu, je, unaweza kuachilia dhana zako za kidini?

4. Unapoomba, je, unaweza kuachana na mila za kidini?

5. Je, wewe ni mtu anayestahili kutumiwa na Mungu?

6. Ni kiasi gani cha ufahamu wako wa Mungu kina dhana za kidini?

Iliyotangulia: Katika Imani, Mtu Anapaswa Kuzingatia Uhalisi—Kujihusisha na Taratibu za Kidini Sio Imani

Inayofuata: Jua Kazi Mpya Zaidi ya Mungu na Ufuate Nyayo Zake

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp