Kuhusu Uzoefu
Katika uzoefu wote wa Petro, alikumbana na mamia ya majaribio. Ingawa watu wa leo wanafahamu neno “jaribio,” wao huchanganyikiwa kuhusiana na maana yake ya kweli na hali. Mungu hutuliza azimio la watu, husafisha imani yao, na hukamilisha kila sehemu yao—na hii hufanikishwa kimsingi kupitia majaribio, ambayo pia ni kazi ya Roho Mtakatifu iliyofichwa. Inaonekana kama kwamba Mungu amewaacha watu, na kwa hivyo wasipokuwa waangalifu, watayaona majaribio haya kama majaribu ya Shetani. Kwa kweli, majaribio mengi yanaweza kufikiriwa kuwa majaribu, na hii ni kanuni na sheria ambazo Mungu hufanya kazi kupitia kwazo. Watu wakiishi mbele ya Mungu kwa kweli, wataona vitu vile kama majaribio kutoka kwa Mungu, na hawataviruhusu viponyoke. Mtu akisema kwamba kwa sababu Mungu yu pamoja naye Shetani hakika hatamwendea, hii siyo sahihi kabisa; je, basi inaweza kuelezwa vipi kwamba Yesu alikabiliwa na majaribu baada ya Yeye kufunga jangwani kwa siku arobaini? Kwa hivyo watu wakirekebisha maoni yao juu ya imani katika Mungu, wataona mambo mengi kwa uwazi zaidi, na ufahamu wao hautakuwa wa upogoupogo na wa uongo. Ikiwa mtu kwa kweli ameamua kukamilishwa na Mungu, anapaswa kuyakabili masuala yanayomkabili toka kwa mitazamo mingi tofauti, bila kuyumbayumba upande wa kushoto wala kulia. Ikiwa huna maarifa ya kazi ya Mungu, hutajua jinsi ya kushirikiana na Mungu. Ikiwa hujui kanuni za kazi ya Mungu, na hujui jinsi Shetani anavyofanya kazi kwa mwanadamu, hutakuwa na njia ya kutenda. Ufuatiliaji wenye ari pekee hautakuruhusu ufikie matokeo yanayohitajiwa na Mungu. Mbinu kama hiyo ya kupitia ni sawa na ile ya Lawrence: kutotofautisha hali yoyote kabisa na kusisitiza uzoefu tu, kutojua kabisa kazi ya Shetani ni nini, kutojua kazi ya Roho Mtakatifu ni nini, jinsi mwanadamu alivyo bila kuwepo kwa Mungu, na ni watu wa aina gani ambao Mungu anataka kuwakamilisha. Ni kanuni gani zinapaswa kukubaliwa wakati wa kushughulikia aina tofauti za watu, jinsi ya kuelewa vizuri mapenzi ya Mungu sasa, jinsi ya kujua tabia ya Mungu, na ni kwa watu, mazingira, na enzi gani ndiyo huruma, uadhama, na haki ya Mungu huelekezwa—hana utambuzi wowote kuhusu yoyote kati ya haya. Ikiwa watu hawana maono mengi kama msingi wa uzoefu wao, basi uzima haupo, sembuse uzoefu; wanaweza kuendelea kutii na kuvumilia kila kitu kwa upumbavu. Watu kama hawa ni vigumu sana kuwakamilisha. Inaweza kusemwa kuwa ikiwa huna maono yoyote yaliyotajwa hapo juu, hili ni thibitisho tosha kwamba wewe ni mpumbavu, wewe ni kama nguzo ya chumvi ambayo husimama daima katika Israeli. Watu kama hawa ni bure, vinyangarika! Watu wengine hutii kila mara bila kufikiri, wao daima hujitambua na hutumia njia zao wenyewe za kutenda wanaposhughulikia masuala mapya, au wanatumia “hekima” kushughulikia mambo madogo na yasiyofaa kutajwa. Watu kama hao hawana utambuzi, ni kama kwamba asili yao ni kukubali kuonewa bila kulalamika, na wao daima huwa vilevile, hawabadiliki kamwe. Watu kama hawa ni wapumbavu ambao hawana utambuzi hata kidogo. Kamwe hawajaribu kulinganisha matendo kwa hali au watu tofauti. Watu kama hawa hawana uzoefu. Nimewaona watu fulani ambao hushughulika sana katika ujuzi wao wenyewe kiasi kwamba wanapokabiliwa na watu walio na kazi ya pepo waovu, huinamisha vichwa vyao na kukiri dhambi zao, bila kuthubutu kusimama na kuwashutumu. Na wanapokabiliwa na kazi dhahiri ya Roho Mtakatifu, hawathubutu kutii. Wanaamini kwamba pepo hawa waovu pia wako mikononi mwa Mungu, na hawana ujasiri hata kidogo wa kusimama na kuwapinga. Watu kama hawa wanamwaibisha Mungu, na hawawezi kabisa kubeba mzigo mzito kwa ajili ya Mungu. Wapumbavu kama hawa hawaleti tofauti ya aina yoyote. Kwa hivyo, mbinu kama hiyo ya kupata uzoefu, inapaswa kusafishwa, kwani haiwezi kuthibitishwa machoni pa Mungu.
Hakika Mungu hufanya kazi nyingi kwa watu, wakati mwingine kuwajaribu, wakati mwingine kusababisha mazingira ya kuwatuliza, na wakati mwingine kuzungumza maneno ili kuwaongoza na kurekebisha upungufu wao. Wakati mwingine Roho Mtakatifu huwaongoza watu kwenye mazingira yaliyotayarishwa na Mungu kwao ili wagundue mambo mengi ambayo hawana. Kupitia kile ambacho watu husema na kufanya, jinsi ambavyo watu huwatendea wengine na kuvishughulikia vitu, bila wao kujua, Roho Mtakatifu huwapa nuru kuhusu vitu vingi ambavyo hawakuvielewa hapo zamani, Akiwaruhusu waone mambo mengi na watu kwa uwazi zaidi, Akiwaruhusu wabaini mengi kuhusu yale ambayo hawakuyajua hapo zamani. Unapojishughulisha na ulimwengu, unaanza kutambua mambo ya ulimwengu hatua kwa hatua, na kabla ya kufikia mwisho wako, unaweza kufikia uamuzi: “Ni vigumu kweli kuwa mtu.” Ukitumia muda kiasi kupata uzoefu mbele ya Mungu, na kuja kuelewa kazi ya Mungu na tabia Yake, utapata umaizi zaidi bila kufahamu, na kimo chako kitakua polepole. Utaelewa mambo mengi ya kiroho vizuri zaidi, na utakuwa na hakika zaidi kuhusu kazi ya Mungu hasa. Utakubali maneno ya Mungu, kazi ya Mungu, kila tendo la Mungu, tabia ya Mungu, na kile Mungu alicho na kile Anacho kama uzima wako mwenyewe. Ikiwa yote unayofanya ni kuzurura ulimwenguni, mabawa yako yatakua magumu zaidi, na upinzani wako dhidi ya Mungu utakuwa mkubwa zaidi; hivyo basi Mungu anawezaje kukutumia? Kwa sababu kuna “kwa maoni yangu” kwa wingi sana ndani yako, Mungu hawezi kukutumia. Kadiri unavyozidi kuwa mbele ya Mungu, ndivyo utakavyokuwa na uzoefu zaidi. Ikiwa wewe bado unaishi ulimwenguni kama mnyama, kinywa chako kikitangaza imani katika Mungu lakini moyo wako ukiwa mahali pengine, na kama bado unazichunguza falsafa za kidunia za kuishi, basi si kazi zako zote za awali zitakuwa bure? Kwa hiyo, kadiri watu wanavyozidi kuwa mbele ya Mungu, ndivyo inavyokuwa rahisi zaidi kwao kukamilishwa na Mungu. Hii ndiyo njia ambayo kwayo Roho Mtakatifu hufanya kazi Yake. Usipoelewa hili, haitawezekana wewe kuingia kwenye njia sahihi, na kukamilishwa na Mungu hakutawezekana. Hutaweza kuwa na maisha ya kawaida ya kiroho, itakuwa kama kwamba wewe ni mlemavu, utakuwa tu na bidii yako na bila kazi yoyote ya Mungu. Je, si hili ni kosa katika uzoefu wako? Si lazima uombe ili uwe mbele ya Mungu; wakati mwingine ni katika kufikiri kwako juu ya Mungu au kutafakari kazi Yake, wakati mwingine katika kushughulikia kwako suala fulani, na wakati mwingine kwa njia ya kufichuliwa kwako katika tukio, ndipo wewe huja mbele ya Mungu. Watu wengi husema, “Je, siko mbele ya Mungu, kwa kuwa mimi mara nyingi huomba?” Watu wengi huomba bila kukoma “mbele ya Mungu.” Sala zinaweza kuwa daima kwenye midomo yao, lakini hawaishi kwa kweli mbele ya Mungu. Hii ndiyo njia pekee ambayo watu hao wanaweza kudumisha hali zao mbele ya Mungu; hawawezi kabisa kutumia mioyo yao kushirikiana na Mungu wakati wote, wala hawawezi kuja mbele ya Mungu kwa njia ya kupata uzoefu, iwe kwa njia ya kuwaza, kutafakari kwa kimya, au kutumia mawazo yao kushirikiana na Mungu ndani ya mioyo yao kwa kuzingatia mzigo wa Mungu. Wao hutoa tu sala kwa Mungu mbinguni wakitumia vinywa vyao. Mioyo ya watu wengi haina Mungu, Mungu yuko pale tu wakati ambapo wanamkaribia; mara nyingi, Mungu hayupo kabisa. Je, si hili ni dhihirisho la kutokuwa na Mungu katika moyo wa mtu? Kama kweli wangekuwa na Mungu mioyoni mwao, je, wangefanya mambo ambayo wezi na wanyama hufanya? Ikiwa mtu anamcha Mungu kwa kweli, ataleta moyo wake wa kweli kuwa karibu na Mungu, na mawazo na dhana zao daima zitamilikiwa na maneno ya Mungu. Hatafanya makosa katika usemi au vitendo, na hatafanya chochote kinachompinga Mungu waziwazi. Hicho ndicho kiwango cha kuwa muumini.