Jinsi ya Kujua Tabia ya Mungu na Matokeo Ambayo Kazi Yake Itafanikisha

Kwanza, hebu tuuimbe wimbo wa kumsifu Mungu: Wimbo wa Ufalme (I) Ufalme Unashuka Duniani.

Kiambata: Umati unanishangilia Mimi, umati wananisifu Mimi; vinywa vyote vinamtaja Mungu mmoja wa kweli. Ufalme unashuka juu ya ulimwengu wa wanadamu.

1  Umati unanishangilia, umati unanisifu; watu wote wanalitaja jina la Mungu mmoja wa kweli, watu wote wanayainua macho yao Kuyatazama matendo Yangu. Ufalme unashuka juu ya ulimwengu wa wanadamu, nafsi Yangu ni yenye utele na wingi. Nani asingesherehekea kwa ajili ya hili? Ni nani asingecheza kwa furaha? Ee Sayuni! Inua bendera yako ya ushindi unisherehekee! Imba wimbo wako wa ushindi ili ulieneze jina Langu takatifu!

2  Viumbe vyote mpaka miisho ya dunia! Harakisheni kujitakasa ili muweze kufanywa kuwa sadaka Kwangu! Makundi ya nyota juu angani! Rudini kwa haraka kwenye maeneo yenu ili muonyeshe nguvu Zangu kuu katika anga! Nazisikiliza sauti za watu duniani, wanaomimina upendo na uchaji wao mwingi kwa ajili Yangu katika wimbo! Katika siku hii, wakati viumbe wote wanarudishiwa uhai, Ninashuka katika ulimwengi wa wanadamu. Kwa wakati huu, mambo yalivyo, maua yanachanua kwa wingi, ndege wote wanaimba kwa sauti moja, vitu vyote vinajawa na furaha! Kwa sauti ya saluti ya ufalme, ufalme wa Shetani unaanguka, ukiangamizwa katika mngurumo wa wimbo wa ufalme, usiinuke tena!

3  Ni nani duniani anayethubutu kuinuka na kupinga? Ninaposhuka duniani, Ninaleta mwako, Nashusha ghadhabu, Naleta maafa ya kila aina. Falme za dunia sasa ni ufalme Wangu! Juu angani, mawingu yanagaagaa na kuvuma; chini ya anga, maziwa na mito huchangamka na kutoa sauti za kusisimua. Wanyama wanaopumzika wanaibuka kutoka kwenye matundu yao, na watu wote ambao wamelala wanaamshwa kutoka katika usingizi wao na Mimi. Siku ambayo watu wengi wameingojea hatimaye imefika! Wananiimbia nyimbo nzuri sana!

Mfuateni Mwanakondoo na Kuimba Nyimbo Mpya

Ni nini mnachofikiria kila wakati mnapouimba wimbo huu? (Tunajisikia uchangamfu na kusisimkwa sana, na tunafikiria jinsi uzuri wa ufalme ulivyo mtukufu, jinsi wanadamu na Mungu watakavyounganishwa milele.) Je, yupo yeyote aliyefikiria kuhusu umbo ambalo binadamu lazima achukue ili kuweza kuwa na Mungu? Katika mawazo yenu, mtu anapaswa kuwa vipi ili aweze kuungana na Mungu na kufurahia maisha yenye utukufu yanayofuata katika ufalme? (Tabia zake zinapaswa kuwa zimebadilishwa.) Anapaswa kuwa na tabia iliyobadilika, lakini, je, kubadilika hadi kiwango gani? Je, atakuwa vipi baada ya kubadilishwa tabia? (Atakuwa mtakatifu.) Je, kiwango cha utakatifu ni kipi? (Fikira zake zote na yote anayozingatia ni lazima yalingane na Kristo.) Je, ulinganifu huo unaonyeshwaje? (Mtu hampingi Mungu, wala kumsaliti Mungu, bali anatoa utiifu kamili kwa Mungu, na kumcha Mungu katika moyo wake.) Baadhi ya majibu yenu yapo sahihi. Fungueni mioyo yenu, ninyi nyote, na mshiriki kile ambacho mioyo yenu inawaambia. (Watu wanaoishi na Mungu katika ufalme wanaweza kutekeleza wajibu wao, kutekeleza kwa uaminifu wajibu wao, kwa kutafuta ukweli na kutozuiliwa na mtu, tukio, au kitu chochote. Kisha inakuja kuwezekana kwao kujitenga na ushawishi wa giza, kuilinganisha mioyo yao na Mungu, na kumcha Mungu na kujiepusha na uovu.) (Mtazamo wetu wa kuangalia mambo unaweza kulingana na ule wa Mungu, na tunaweza kujitenga na ushawishi wa giza. Kiwango cha chini zaidi ni kutotumiwa vibaya na Shetani, kutupilia mbali tabia zozote potovu, na kutimiza utiifu wa Mungu. Tunasadiki kwamba kuwa huru dhidi ya ushawishi wa giza ndiyo jambo la msingi. Kama mtu hawezi kujitenga na ushawishi wa giza, hawezi kujipa uhuru kutoka kwenye minyororo ya Shetani, basi hajapata wokovu wa Mungu.) (Ili kufikia kiwango cha kukamilishwa na Mungu, ni lazima watu wawe na moyo mmoja na akili moja na Yeye, na wasimpinge tena. Ni lazima waweze kujijua wenyewe, kuuweka ukweli katika vitendo, kupata ufahamu wa Mungu, kumpenda Mungu, na kupatana na Mungu. Hayo ndiyo yote ambayo mtu anahitaji kufanya.)

Uzito wa Matokeo katika Mioyo ya Watu

Inaonekana kuwa mna mawazo fulani katika mioyo yenu kuhusu jinsi mnavyopaswa kufuata, na mmepata uelewa fulani juu yake au ufahamu fulani kuihusu. Hata hivyo, iwapo maneno yote ambayo mmeyatamka yatageuka kuwa matupu au halisi, itategemea umakini wako katika utendaji wako wa kila siku. Kwa miaka mingi, nyote mmevuna matunda fulani kutoka kwa kila kipengele cha ukweli, katika suala la mafundisho na katika suala la maudhui halisi ya ukweli. Hii inathibitisha kwamba, watu siku hizi wanatilia mkazo sana katika kujitahidi kupata ukweli, na kwa sababu hiyo, kila kipengele na kila sehemu yà ukweli hakika imeweka mizizi katika mioyo ya baadhi ya watu. Hata hivyo, ni nini hasa Ninachoogopa sana? Ni kwamba, licha ya ukweli kwamba mada hizi za ukweli, na nadharia hizi zimekita mizizi ndani ya mioyo yenu, maudhui halisi bado hayana uzito mkubwa katika mioyo yenu. Wakati mnapokumbana na masuala, mnapopitia majaribio, mnapokabiliwa na uchaguzi—je, ni kwa kiwango kipi utumiaji wa kivitendo wa ukweli huu utakuwa kwenu? Je, itaweza kuwasaidia kuyashinda magumu yenu na kuibuka kutoka kwenye majaribu yenu, ili kuweza kutosheleza nia za Mungu? Je, mtasimama imara katika majaribio yenu na kutoa ushuhuda thabiti kwa Mungu? Je, mmewahi kutamani masuala haya hapo awali? Mniruhusu Niwaulize: Katika mioyo yenu, katika fikira na tafakari zenu zote za kila siku, ni nini ambacho ni muhimu zaidi kwenu? Je, mmewahi kufikia hitimisho? Ni nini mnachosadiki kuwa kitu muhimu zaidi? Baadhi ya watu husema “ni kuweka ukweli katika vitendo, bila shaka”; baadhi ya watu husema “bila shaka ni kusoma neno la Mungu kila siku”; baadhi ya watu husema “ni kujiweka mbele za Mungu na kumwomba Mungu kila siku, bila shaka”; na kisha kuna wale wanaosema “bila shaka ni kutekeleza wajibu wangu kwa njia bora kila siku”; kuna baadhi ya watu pia ambao wanasema wanafikiria wakati wote tu kuhusu namna ya kumtosheleza Mungu, namna ya kumtii Yeye katika mambo yote, na namna ya kutenda kulingana na mapenzi Yake. Je, hivi ndivyo ilivyo? Je, hivi ndivyo vitu vyote vinavyohitajika kufanywa? Kwa mfano, kuna baadhi wanaosema: “Mimi nataka tu kumtii Mungu, lakini jambo linapotokea, nashindwa kumtii Yeye.” Wengine wanasema, “Mimi nataka tu kumridhisha Mungu, hata kama ningeweza kumridhisha mara moja tu, hio ingekua sawa—lakini kamwe siwezi kumridhisha Yeye.” Wengine wanasema, “Mimi nataka tu kunyenyekea kwa Mungu. Wakati wa majaribu nataka tu kujitiisha katika mipango Yake, na kujisalimisha katika ukuu na mipangilio Yake, bila malalamiko au maombi yoyote. Lakini bado nashindwa kujisalimisha karibu kila wakati.” Baadhi ya watu wengine husema, “Ninapokabiliwa na uchaguzi, siwezi kamwe kuchagua kuweka ukweli katika vitendo. Siku zote ninataka kuuridhisha mwili, siku zote nataka kutimiza matamanio yangu binafsi.” Je, ni nini sababu ya hili? Kabla ya majaribio ya Mungu kufika, je, tayari mmejipima mara nyingi, mkijijaribu na kujipima ninyi wenyewe tena na tena? Kuona kama unaweza kweli kumtii na kumridhisha Mungu, na kama unaweza kuhakikisha kwamba hutamsaliti Mungu. Kuona kama hutaweza kujiridhisha wewe mwenyewe, na kutotimiza matamanio yako binafsi, bali umridhishe Mungu tu, bila kufanya uchaguzi wowote wa kibinafsi. Je, kuna mtu yeyote anayefanya hivi? Kwa hakika, kuna ukweli mmoja tu ambao umewekwa mbele ya macho yenu nyinyi wenyewe. Ni kile ambacho kila mmoja wenu anavutiwa nacho, kile mnachotaka kujua zaidi, na hilo ni suala la matokeo na hatima ya kila mmoja wenu. Huenda msitambue, lakini hili ni jambo ambalo hakuna anayeweza kulikataa. Inapokuja kwa ukweli wa matokeo ya watu, ahadi ya Mungu kwa wanadamu, na ni aina gani ya hatima ambayo Mungu anakusudia kuwaleta watu ndani yake, Najua kuna baadhi ambao tayari wamesoma maneno ya Mungu kuhusu mada hizi mara kadhaa. Kisha kuna wale ambao mara kwa mara wanatafuta jibu na kutafakari juu yake katika akili zao, lakini bado hawajapata chochote, au labda wameishia kufikia hitimisho fulani lisiloeleweka. Mwishowe, wanabaki kutokuwa na uhakika kuhusu ni aina gani ya matokeo yanayowangojea. Wakati wa kutekeleza wajibu wao, watu wengi huwa na mwelekeo wa kutaka kujua majibu yenye uhakika kwa maswali yafuatayo: “Matokeo yangu yatakuwa ni yapi? Je, naweza kuitembea njia hii hadi mwisho wake? Je, mtazamo wa Mungu kwa mwanadamu ni upi?” Wengine hata wana wasiwasi kama huu: “Katika siku zilizopita, nimesema baadhi ya mambo, sikumtii Mungu, nimefanya mambo fulani ambayo yamemsaliti Mungu, kulikuwa na masuala fulani ambayo sikumtosheleza Mungu, niliuumiza moyo wa Mungu, na nilimkatisha tamaa na kumfanya Anichukie na kunikataa, hivyo basi pengine matokeo yangu hayajulikani. Ni sahihi kusema kwamba watu wengi zaidi wanahisi wasiwasi kuhusu matokeo yao wenyewe. Hakuna anayethubutu kusema: “Nahisi kwa uhakika wa asilimia mia moja kwamba nitanusurika; Nina uhakika wa asilimia mia moja kwamba ninaweza kutosheleza nia za Mungu; mimi ni mtu ambaye nafuata mapenzi ya Mungu; mimi ni mtu anayesifiwa na Mungu.” Baadhi ya watu wanafikiria ni vigumu kufuata njia ya Mungu, na kwamba kuweka ukweli katika vitendo ndilo jambo gumu zaidi la kufanya. Kwa hivyo, watu hawa wanafikiria hawawezi kusaidika, na hawathubutu kuwa na matumaini ya kuwa na matokeo mazuri. Au pengine wanasadiki kwamba hawawezi kutosheleza nia za Mungu, na kuweza kunusurika; na kwa sababu ya haya watasema kwamba hawana matokeo, na hawawezi kufikia hatima nzuri. Haijalishi jinsi watu wanavyofikiri hasa, wote wamewahi kujiuliza kuhusu matokeo yao mara nyingi. Kuhusu masuala ya siku zao za usoni, kuhusu maswali ya kile watakachopata wakati Mungu atakapomaliza kazi Yake, watu hawa siku zote wanapiga hesabu, siku zote wanapanga. Baadhi ya watu wanalipa gharama mara dufu; baadhi ya watu wanaacha familia zao na kazi zao; baadhi wanaacha ndoa zao; baadhi yao wanajiuzulu ili kujitoa kwa ajili ya Mungu; baadhi ya watu wanaacha nyumba zao ili kufanya wajibu wao; baadhi ya watu wanachagua ugumu, na kuanza kufanya kazi ambazo zinaumiza zaidi na zinazochosha zaidi; baadhi ya watu wanachagua kutoa mali zao, kujitolea kila kitu chao; na bado baadhi ya watu wanachagua kufuatilia ukweli na kufuatilia kumjua Mungu. Haijalishi namna mnavyochagua kutenda, je, namna mnavyotenda ndiyo muhimu zaidi? (Si muhimu.) Ni vipi tunavyoelezea kwamba si muhimu, basi? Kama namna hiyo si muhimu, basi ni nini ambacho ni muhimu? (Tabia nzuri za nje haziwakilishi kuweka ukweli katika vitendo.) (Kile ambacho kila mmoja anafikiria si muhimu. Cha msingi hapa ni kama tumeweza kuweka ukweli katika vitendo au la, na kama tunampenda Mungu au la.) (Anguko la wapinga Kristo na viongozi wa uongo hutusaidia kuelewa kwamba tabia ya nje si jambo la muhimu zaidi. Kwa nje wanaonekana kuwa wamejinyima mengi, na wanaonekana kuwa wapo tayari kulipa gharama, lakini kwa kuchambua tunaweza kuona kwamba hawana moyo kabisa unaomcha Mungu; lakini badala yake wanampinga Yeye katika mambo yote. Katika nyakati muhimu sana, wao daima wanakuwa upande wa Shetani na kuvuruga kazi ya Mungu. Kwa hivyo, mambo ya msingi ya kuzingatia hapa ni upande gani tunasimama wakati utakapofika, na maoni yetu kuhusu mambo ni yapi.) Ninyi nyote mmezungumza vyema, na mnaonekana kuwa tayari mnaufahamu wa msingi, na kiwango cha kuishi wakati utakapofika wa kuweka ukweli katika vitendo, nia za Mungu, na kile ambacho Mungu anahitaji kwa wanadamu. Kwamba mnaweza kuongea hivi inatia moyo sana. Ingawa baadhi ya yale mliyosema si sahihi sana, tayari yamekaribia kuwa na maelezo sahihi ya ukweli—na hii inathibitisha kwamba mmekuza ufahamu wenu halisi wa watu, matukio, na vitu vinavyowazunguka, na mazingira yenu yote ambayo yamepangwa na Mungu, na kwa kila kitu ambacho mnaweza kuona. Huu ni ufahamu ambao uko karibu na ukweli. Hata ingawa kile mlichosema si cha kina kabisa, na maneno machache hayafai sana, uelewa wenu tayari unakaribia uhalisi wa ukweli. Kuwasikiliza mkiongea kwa njia hii kunanifanya Mimi kuhisi vizuri sana.

Imani za Watu Haziwezi Kubadilishwa na Ukweli

Kuna baadhi ya watu wanaoweza kuvumilia magumu; wanaoweza kulipa gharama; tabia yao ya nje ni nzuri sana; wanaheshimika sana; na wanaheshimiwa na wengine. Mnaonaje: Je, tabia kama hii ya nje inaweza kuchukuliwa kama kuweka ukweli katika vitendo? Je, unaweza kusema kwamba mtu huyu anatosheleza nia za Mungu? Kwa nini mara kwa mara watu wanamwona mtu wa aina hii na kufikiria kwamba wao wanamtosheleza Mungu, wanafikiria kwamba wanatembea katika njia kuweka ukweli katika vitendo, kwamba wanatembea katika njia ya Mungu? Kwa nini baadhi ya watu wanafikiria kwa njia hii? Upo ufafanuzi mmoja tu kwa haya. Na ufafanuzi huo ni upi? Sababu ni kwamba kwa watu wengi, maswali kama vile; kuweka ukweli katika vitendo ni nini, kumridhisha Mungu ni nini, ni nini maana ya kuwa na uhalisi wa ukweli—maswali haya hayako wazi sana. Kwa hivyo, kuna baadhi ya watu ambao mara nyingi wanadanganywa na wale ambao kwa nje wanaonekana kuwa wa kiroho, wanaonekana waungwana, wanaonekana kuwa na taswira za ukuu. Kuhusiana na watu hao ambao wanaweza kuzungumza maneno kwa ufasaha na mafundisho, na ambao maneno na matendo yao yanaonekana yanastahili kusifiwa, wale wanaodanganywa nao hawajawahi kuangalia kiini cha matendo yao, kanuni zilizo nyuma ya matendo yao, au malengo yao ni nini. Na hawajawahi kuangalia kama watu hawa wanamtii Mungu kwa kweli, na kama wao ni watu wanaomcha Mungu kwa kweli na kujiepusha na maovu au la. Hawajawahi kutambua kiini cha ubinadamu wa watu hawa. Badala yake, kutoka kwenye hatua ya kwanza ya kuanza kufahamiana nao, kidogo kidogo, wanaanza kuvutiwa na watu hawa, wanawaheshimu watu hawa, na hatimaye watu hawa wanakuwa sanamu zao. Zaidi ya hayo, katika akili za baadhi ya watu, watu hao wanaowaabudu—na ambao wanaamini wanaweza kuziacha familia zao na kazi zao, na wanaoonekana kuwa na uwezo wa juu juu wa kulipa gharama—ndio wanaomridhisha Mungu kwa kweli, na ambao wanaweza kupata matokeo mazuri na hatima nzuri. Katika akili zao, sanamu hizi ndizo ambazo Mungu anazisifu. Ni nini kinachowafanya watu waamini jambo kama hilo? Ni nini kiini cha suala hili? Je, inaweza kusababisha matokeo gani? Hebu kwanza tujadili suala la kiini chake.

Kimsingi, masuala haya kuhusu mitazamo ya watu, mbinu zao za utendaji, ni kanuni zipi za utendaji wanazochagua kufuata, na kile ambacho kwa kawaida kila mmoja anazingatia, hazina uhusiano na mahitaji ya Mungu kwa mwanadamu hata kidogo. Bila kujali kama watu wanazingatia masuala ya juujuu au yale ya kina, au maneno na mafundisho, au uhalisi, watu hawashikilii yale ambayo wanapaswa kushikamana nayo zaidi, wala hawayajui yale ambayo wanapaswa kuyajua zaidi. Sababu ya hili ni kwamba, watu hawaupendi ukweli hata kidogo; kwa hivyo, hawako tayari kutumia muda na juhudi zao katika kutafuta na kuweka katika vitendo kanuni za utendaji zinazopatikana katika matamshi ya Mungu. Badala yake, wanapendelea kutumia njia za mkato, wakihitimisha kile wanachoelewa na kujua kuwa ni utendaji mzuri na tabia njema; muhtasari huu unakuwa lengo lao wenyewe la kufuata, ambalo wanalichukulia kama ukweli wa kutekelezwa. Athari ya moja kwa moja ya haya yote ni kwamba watu wanatumia tabia nzuri ya kibinadamu kama mbadala wa kuweka ukweli katika matendo yao, ambayo pia inatosheleza matamanio yao ya kutaka kupata kibali cha Mungu. Hii inawapa watu mtaji wa kushindana na ukweli, ambao wao pia wanautumia kutoa sababu na kushindana na Mungu. Wakati huo huo, watu pia wanamweka Mungu kando bila uadilifu, wakiwaweka watu wanaowapenda katika nafasi ya Mungu. Kuna sababu moja tu ya msingi ambayo inawafanya watu wawe na vitendo na mitazamo ya kijinga kama hii, au maoni na utendaji wa upande mmoja—na leo Nitawaambia kuhusu hilo. Sababu ni kwamba ingawa watu wengi wanaweza kumfuata Mungu, kumwomba Yeye kila siku, na kusoma neno la Mungu kila siku, hawaelewi kwa hakika nia za Mungu. Hiki ndicho chanzo cha tatizo. Kama mtu aliuelewa moyo wa Mungu, na alijua kile ambacho Mungu anapenda, kile ambacho Anachukia, kile Anachotaka, kile Anachokataa, ni mtu wa aina gani ambaye Mungu anampenda, ni mtu wa aina gani ambaye Mungu hampendi, ni kiwango gani ambacho Mungu anatumia katika kutoa mahitaji Yake kwa watu, na ni mbinu gani Anazotumia ili kuwakamilisha watu, je, bado mtu kama huyo angeweza kuwa na maoni yake binafsi? Je, watu kama hao wangeweza tu kwenda na kumwabudu mtu mwingine? Je, mwanadamu wa kawaida angeweza kuwa sanamu yao? Watu wanaoelewa nia za Mungu, wana maoni yenye busara zaidi kuliko hayo. Hawataweza kumwabudu mtu mpotovu kiholela, wala, wanapotembea katika njia ya kuweka ukweli katika vitendo, kuamini kwamba kufuata kwa upofu sheria au kanuni chache rahisi ni sawa na kuweka ukweli katika vitendo.

Kuna Maoni Mengi Kuhusu Kiwango Ambacho Mungu Hutumia Kuamua Matokeo ya Mwanadamu

Hebu turejee katika mada hii na tuendelee kuzungumzia suala la matokeo.

Kwa sababu kila mmoja anajali matokeo yake, je, mnajua namna ambavyo Mungu huamua matokeo hayo? Na ni kwa njia gani ambayo Mungu huamua matokeo ya mtu? Na je, ni kiwango gani ambacho Mungu anatumia kuamua matokeo ya mtu? Na kwa wakati ambao matokeo ya mtu bado hayajaamuliwa, ni nini ambacho Mungu anafanya ili kufichua matokeo haya? Je, yupo anayejua haya? Kama Nilivyosema muda mfupi uliopita, kuna baadhi ambao tayari wametumia muda mrefu sana kutafiti maneno ya Mungu katika jitihada za kutafuta vidokezo kuhusu matokeo ya watu, kuhusu vipengele ambavyo matokeo hayo yamegawanywa, na kuhusu matokeo mbalimbali yanayowasubiri aina tofauti za watu. Pia wanataka kujua jinsi neno la Mungu linavyoamua matokeo ya watu, ni kiwango cha aina gani ambacho Mungu anatumia, na jinsi hasa Anavyoamua matokeo ya mtu. Mwishowe, hata hivyo, watu hawa hawajaweza kupata majibu yoyote. Kwa hakika, kuna machache ya muhimu yaliyosemwa kuhusu jambo hilo katika matamshi ya Mungu. Kwa nini ni hivyo? Ilimradi matokeo ya watu bado hayajafichuliwa, Mungu hataki kumwambia yeyote kuhusu kile kitakachotokea mwishowe, wala Hataki kumfahamisha yeyote kuhusu hatima yake kabla ya wakati kufika. Sababu ya kufanya hivi ni kwamba Mungu kufanya hivyo hakutaleta manufaa yoyote kwa binadamu. Sasa hivi, Nataka kuwaambia tu kuhusu jinsi ambavyo Mungu anaamua matokeo ya binadamu, kuhusu kanuni Anazotumia katika kazi Yake ili kuamua matokeo ya binadamu, na kuonyesha matokeo hayo, pamoja na kiwango Anachotumia ili kuamua kama mtu ataweza kuishi au la. Je, hiki sicho kile ambacho mnajali zaidi kuhusu? Hivyo basi, ni vipi ambavyo watu wanaamini kuhusu njia ambayo Mungu anaamua matokeo ya binadamu? Mlizungumzia kidogo kuhusu suala hili muda mfupi uliopita. Baadhi yenu mlisema kwamba inahusiana na kufanya wajibu wa mtu kwa uaminifu, kujitumia kwa ajili ya Mungu; baadhi ya watu walisema kumtii Mungu na kumridhisha Mungu; baadhi ya watu walisema kumwacha Mungu akudhibiti; na baadhi ya watu walisema kua na hadhi ya chini…. Mnapoweka ukweli huu katika vitendo, mnapotenda kanuni za kufikiria kwenu, je, mnajua kile ambacho Mungu anafikiria? Je, mmewahi kufikiria kama kuendelea hivi ni kutosheleza nia za Mungu au la? Kama kunakidhi kiwango cha Mungu? Kama kunakidhi mahitaji ya Mungu? Ninaamini kwamba watu wengi hawafikirii sana maswali haya. Wao wanatumia tu sehemu ya neno la Mungu, au sehemu ya mahubiri, au viwango vya watu fulani wa kiroho ambao wanawaabudu, na kujilazimisha kufanya hivi na vile. Wanasadiki kwamba hii ndiyo njia sahihi, kwa hiyo wanaendelea kushikamana nayo na kuifanya, bila kujali kile kitakachowatokea mwishoni. Baadhi ya watu wanafikiri, “Nimeamini kwa miaka mingi sana; nimekuwa nikitenda kwa njia hii siku zote; ninahisi kama nimemridhisha Mungu kabisa; ninahisi pia kuwa nimejifunza mengi kutoka kwa haya. Kwani nimekwishaelewa ukweli mwingi katika kipindi hiki, na nimeelewa mambo mengi ambayo sikuyaelewa awali—hasa, mawazo na mitazamo yangu mingi imebadilika, maadili ya maisha yangu yamebadilika sana, na sasa nina ufahamu mzuri wa ulimwengu huu.” Watu kama hao wanaamini kwamba haya ni mavuno, na kwamba ni matokeo ya mwisho ya kazi ya Mungu kwa binadamu. Kwa maoni yenu, kwa viwango hivi na vitendo vyenu vyote vikiwekwa pamoja—je, mnatosheleza nia za Mungu? Baadhi ya watu watasema kwa uhakika wote, “Bila shaka! Tunatenda kulingana na neno la Mungu; tunatenda kulingana na kile ambacho Aliye juu Alihubiri na kuwasilisha. Sisi siku zote tunafanya wajibu wetu na tunamfuata Mungu bila kukoma, hatujawahi kumwacha Mungu. Hivyo basi tunaweza kusema kwa uhakika kabisa kwamba tunamtosheleza Mungu. Haijalishi ni kiasi gani tunaelewa nia za Mungu, na haijalishi ni kiasi gani tunaelewa neno Lake, daima tumekuwa kwenye njia ya kutafuta kupatana na Mungu. Mradi tu tunachukua hatua sahihi, na kutenda kwa usahihi, basi matokeo yatakuwa sahihi.” Je, mnafikiria nini kuhusu mtazamo huu? Je, ni sahihi? Pengine wapo wale wanaosema: “Sijawahi kufikiria kuhusu mambo haya hapo awali. Mimi nafikiria, mradi tu nikiendelea kufanya wajibu wangu na kutenda kulingana na matakwa ya maneno ya Mungu, basi nitanusurika. Sijawahi kufikiria swali la kama ninaweza kutosheleza moyo wa Mungu, na sijawahi kufikiria kama ninatimiza kiwango kinachohitajika na Yeye. Kwa sababu Mungu hajawahi kuniambia, wala kunipatia maagizo yoyote kwa uwazi, ninaamini kwamba mradi tu nikiendelea kufanya kazi na nisiache, Mungu atatosheka na Yeye hapaswi kuwa na mahitaji yoyote ya ziada kwangu.” Je, kuamini hivi ni sahihi? Kwa maoni Yangu, njia hii ya kutenda, njia hii ya kufikiri, na mitazamo hii—yote yanajumuisha dhana, pamoja na upofu kidogo. Ninaposema hivi, pengine wapo baadhi yenu wanaohisi kuvunjika moyo: “Ni upofu? Kama huu ni ‘upofu,’ basi tumaini letu la wokovu, tumaini letu la kubaki ni dogo sana, na halina uhakika, je, si hivyo? Je, Unaposema hivyo, si sawa na kutumwagia maji ya baridi?” Haijalishi kile mnachoamini, mambo Ninayoyasema na kuyafanya hayanuii kuwafanya ninyi mhisi kama mnamwagiwa maji baridi. Badala yake, yananuia kuboresha uelewa wenu wa nia za Mungu, na kuboresha ufahamu wenu kuhusu kile ambacho Mungu anafikiria, kile ambacho Mungu anataka kutimiza, ni ni watu wa aina gani ambao Anawapenda, kile ambacho Anachukia, kile ambacho Anadharau, ni mtu wa aina gani ambaye Mungu anataka kumpata, na ni mtu wa aina gani ambaye Mungu anamkataa. Yananuia kupatia akili zako uwazi, na kukupa kufahamu kwa uwazi kuhusu jinsi matendo na mawazo ya kila mmoja wenu yamepotoka kutoka kwenye kiwango kinachohitajika na Mungu. Je, ni muhimu sana kujadili mada hizi? Kwa sababu Ninajua mmeamini kwa muda mrefu, na mmesikiliza mahubiri mengi, lakini kwa hakika haya ndiyo mambo mnayokosa zaidi. Ingawa mmeandika kila ukweli katika daftari zenu, na mmekariri na kuandika katika mioyo yenu baadhi ya mambo ambayo ninyi wenyewe mnaamini kuwa ni ya muhimu, na hata ingawa mmepanga kutumia mambo haya ili kumridhisha Mungu wakati wa kutenda kwenu, kuyatumia wakati mnaona kuwa mnahitaji msaada, kuyatumia ili kupitia nyakati ngumu zilizo mbele yenu, au kuruhusu tu mambo haya yaambatane nanyi mnapoishi maisha yenu. Lakini kulingana na maoni Yangu, haijalishi jinsi mnavyotenda, jinsi mnavyotenda hasa si muhimu sana. Ni nini, basi, kilicho muhimu zaidi? Ni kwamba wakati unatenda, ni lazima ujue moyoni mwako, kwa uhakika kabisa, kama kila kitu unachofanya, kila kitendo, ndicho kile ambacho Mungu anataka au la; na kama matendo yako yote, mawazo yako yote, na matokeo na lengo unalotaka kufikia vinakidhi nia za Mungu na kukidhi matakwa Yake ama la, na vilevile kama Anayakubali ama la. Haya ndiyo mambo ya muhimu zaidi.

Tembea katika Njia ya Mungu: Mche Mungu na Kujiepusha na Maovu

Kuna msemo ambao mnapaswa kuzingatia. Ninaamini msemo huu ni muhimu sana, kwa sababu Kwangu, unanijia akilini mara nyingi kila siku. Kwa ni nini hivyo? Kwa sababu kila wakati Ninapokumbana na mtu, kila wakati Ninaposikia hadithi ya mtu fulani, na kila wakati Ninaposikia uzoefu wa mtu au ushuhuda wa kumwamini Mungu, kila wakati Ninatumia msemo huu ili kubainisha moyoni Mwangu kama mtu huyu ni aina ya mtu ambaye Mungu anamtaka au la, na kama ni aina ya mtu ambaye Mungu anampenda. Kwa hivyo msemo huu ni upi, basi? Sasa nyinyi nyote mnasubiri kwa hamu. Nitakapoufichua msemo huu, pengine mtakasirika kwa sababu wapo baadhi yenu ambao mmekuwa mkijifanya kuwa mnakubaliana nao kwa miaka mingi. Lakini Kwangu Mimi, Sijawahi kujifanya kuwa nakubaliana nao tu. Msemo huu upo moyoni Mwangu. Hivyo basi msemo huu ni upi? Msemo huuni “tembea katika njia ya Mungu: mche Mungu na kujiepusha na maovu.” Je, hili si neon rahisi sana? Hata ingawa msemo huu unaweza kuwa rahisi, mtu ambaye ana uelewa wa ndani na wa kweli wa msemo huu atahisi kwamba ni wenye uzito mkubwa; kwamba usemi huu ni wa thamani sana kwa utendaji wa mtu; kwamba ni usemi katika lugha ya maisha yenye uhalisi wa ukweli; kwamba inawakilisha lengo la maisha yote kwa wale wanaotafuta kumridhisha Mungu, na kwamba ni njia ya maisha yote ambayo mtu yeyote anayefikiria nia za Mungu anapaswa kufuata. Kwa hivyo mnafikiria nini: Je, msemo huu sio ukweli? Je, una umuhimu kama huo ama la? Vile vile, pengine baadhi yenu wanafikiria kuhusu msemo huu, wakijaribu kuuelewa, na wapo baadhi ambao bado wanautilia shaka. Je, msemo huu ni muhimu sana? Je, ni muhimu zaidi? Je, ni muhimu na unastahili kusisitizwa sana? Pengine wapo baadhi ya watu ambao hawaupendi sana msemo huu kwa sababu wanafikiria kwamba kuchukua njia ya Mungu na kuiweka katika msemo huu mmoja ni kurahisisha kupita kiasi. Kuyachukua yale yote ambayo Mungu aliyasema na kuyafanya yawe msemo mmoja—je, hivi si kumfanya Mungu kuwa yule asiyekuwa na umuhimu sana? Je, hivi ndivyo ilivyo? Huenda ikawa kwamba wengi wenu hamwelewi kikamilifu umuhimu wa kina wa maneno haya. Ingawa ninyi nyote mmeuandika mahali, hamna nia ya kuuhifadhi msemo huu katika mioyo yenu; umeuandika tu kwa urahisi katika daftari lako ili kurejelea na kutafakari katika muda wako wa ziada. Kuna watu wengine ambao hawatajisumbua hata kukariri msemo huu, sembuse hata kujaribu kuutumia vizuri. Lakini kwa nini Nikauzungumzia msemo huu? Licha ya mtazamo wenu, au kile mtakachofikiria, ni lazima Nizungumzie msemo huu, kwa kuwa una uhusiano mkubwa wa jinsi Mungu anavyoamua matokeo ya watu. Haijalishi kama ufahamu wako wa sasa wa msemo huu ni nini, au jinsi mnavyouchukulia, bado Nitawaeleza: kama watu wanaweza kuyaweka maneno ya msemo huu katika vitendo na kuyapitia, na kutimiza kiwango cha kumcha Mungu na kujiepusha na maovu, basi atahakikishiwa kuishi, kisha atahakikishiwa kuwa mtu mwenye matokeo mazuri. Kama huwezi kutimiza kiwango kilichowekwa wazi katika msemo huu, basi inaweza kusemwa kwamba matokeo yako hayajulikani. Hivyo, Ninazungumza kwenu kuhusu msemo huu kwa ajili ya matayarisho yenu ya kiakili, na ili muweze kujua ni kiwango cha aina gani ambacho Mungu anatumia kukupima. Kama Nilivyowaambia hivi punde, msemo huu unahusiana sana na wokovu wa Mungu kwa mwanadamu, na vile vile jinsi Anavyoamua matokeo ya watu. Je, uhusiano huu upo wapi? Mngependa kweli kujua, kwa hivyo tutazungumzia kuhusu hilo leo.

Mungu Anatumia Majaribio Tofauti ili Kupima Kama Watu Wanamcha Mungu na Kujiepusha na Maovu

Katika kila enzi ya kazi ya Mungu, Yeye huwapa watu baadhi ya maneno Anapofanya kazi ulimwenguni, na kuwaambia kuhusu ukweli fulani. Kweli hizi zinatumika kama njia ambayo watu wanapaswa kuifuata, njia ambayo wanapaswa kuitembea, njia inayowawezesha kumcha Mungu na kujiepusha na maovu, na njia ambayo watu wanapaswa kuiweka katika vitendo na kuitii katika maisha yao na kwenye mkondo wa safari zao za maisha. Ni kwa sababu hizi ambapo Mungu anampa binadamu maneno haya. Binadamu anapaswa kuyatii maneno haya yanayotoka kwa Mungu, na kuyatii ni kupokea uzima. Kama mtu hataweza kuyatii, na hayaweki kwenye matendo, na haishi kwa kudhihirisha maneno ya Mungu katika maisha yake, basi mtu huyo hauweki ukweli katika matendo. Na kama hawaweki ukweli katika matendo, basi hawamchi Mungu na hawaepuki maovu, wala hawawezi kumtosheleza Mungu. Kama mtu hawezi kumtosheleza Mungu, basi hawezi kupokea sifa ya Mungu; mtu wa aina hii hana matokeo. Kwa hivyo, ni kwa jinsi gani, basi, katika mkondo wa kazi Yake, Mungu anaamua matokeo ya mtu? Je, Mungu anatumia njia gani ili kuamua matokeo ya mtu? Pengine bado hamlielewi suala hili kwa sasa, lakini Nitakapowaambia kuhusu mchakato huo, itakuwa wazi kabisa. Hii ni kwa sababu watu wengi tayari wamepitia suala hili wao wenyewe.

Katika mkondo wa kazi ya Mungu, kuanzia mwanzo hadi sasa, Mungu Amepanga majaribio kwa kila mtu—au mnaweza kusema, kila mtu anayemfuata Yeye—na majaribio haya yanakuja kwa ukubwa tofauti. Wapo wale ambao wamepitia jaribio la kukataliwa na familia zao; wapo wale ambao wamepitia jaribio la mazingira mabaya; wapo wale ambao wamepitia majaribio ya kukamatwa na kuteswa; wapo wale ambao wamepitia majaribio ya kukabiliwa na uchaguzi; na wapo wale ambao wamekumbwa na majaribio ya pesa na hadhi. Nikizungumza kwa ujumla, kila moja wenu amekabiliwa na aina zote za majaribio. Kwa nini Mungu anafanya kazi hivyo? Kwa nini Mungu Anamtendea hivi kila mtu? Je, ni matokeo ya aina gani Anayotaka kuyaona? Hii ndiyo hoja muhimu kuhusu kile Ninachotaka kuwaambia: Mungu anataka kuona kama mtu huyu ni yule anayemcha Mungu na kujiepusha na maovu. Maana ya haya ni kwamba wakati Mungu anakupa jaribio, na kukufanya ukabiliwe na baadhi ya hali, Anataka kukupima na kujua kama wewe ndiye yule mtu anayemcha Mungu, mtu anayejiepusha na maovu au la. Kama mtu amekumbwa na wajibu wa kutunza sadaka, na anakutana na sadaka ya Mungu, basi unadhani kwamba hiki ni kitu ambacho Mungu amepanga? Bila shaka! Kila kitu unachokumbana nacho ni kitu ambacho Mungu amepanga. Unapokumbwa na suala hili, Mungu atakuangalia kwa siri, namna unavyochagua, namna unavyotenda, na kile unachofikiria. Matokeo ya mwisho ndiyo ambayo Mungu anayajali zaidi, sababu ni matokeo ambayo yatamruhusu Yeye kupima kama umetimiza kiwango cha Mungu katika jaribio hilo au la. Hata hivyo, wakati watu wanakabiliwa na baadhi ya masuala haya, mara nyingi hawafikirii ni kwa nini wanakumbwa na mambo hayo, au kile kiwango ambacho kinahitajika na Mungu. Hawafikirii kuhusu kile Mungu anachotaka kutoka kwao, kile Anachotaka kupata kutoka kwao. Wanapokumbwa na suala hili, mtu wa aina hii anafikiria tu: “Hili ni jambo ambalo nimekumbwa nalo; lazima niwe makini, nisiwe mzembe! Hata iweje, hii ni sadaka ya Mungu na siwezi kuigusa.” Mtu huyo anaamini kwamba anaweza kutimiza jukumu lake kwa mawazo rahisi kama haya. Je, Mungu ataweza kutosheka na matokeo ya jaribio hili? Au Hatatosheka? Mnaweza kuzungumzia suala hili. (Kama mtu anamcha Mungu katika moyo wake, anapokumbwa na wajibu unaomruhusu kukutana na sadaka ya Mungu, anaweza kufikiria jinsi ilivyo rahisi kuikosea tabia ya Mungu, na hilo litamfanya awe na uhakika wa kuendelea kwa tahadhari.) Jibu lako lipo katika njia sahihi, lakini bado haujafika. Kutembea katika njia ya Mungu hakuhusu kuangalia sharia kwa juujuu. Badala yake, kunamaanisha kwamba unapokabiliwa na suala, kwanza kabisa, unaliangalia kama ni hali ambayo imepangwa na Mungu, wajibu uliopewa wewe na Yeye, au kitu ambacho Amekuaminia wewe, na kwamba unapokabiliana na suala hili, unapaswa kuliona kama jaribio kutoka kwa Mungu. Wakati unapokabiliwa na suala hili, lazima uwe na kiwango, lazima ufikirie kwamba suala hilo limetoka kwa Mungu. Lazima ufikirie ni vipi ambavyo utashughulikia suala hili kiasi cha kwamba utaweza kutimiza wajibu wako, na kuwa mwaminifu kwa Mungu; namna ya kuifanya bila kumkasirisha Mungu; au kuikosea tabia Yake. Tumetoka tu kuzungumzia kuhusu kutunza sadaka. Swala hili linahusu sadaka, na linahusisha pia wajibu wako, jukumu lako. Unahitajika kuwajibikia jukumu hili. Hata hivyo, unapokabiliwa na suala hili, je, kuna jaribio lolote? Lipo! Jaribio hilo linatoka wapi? Jaribio hilo linatoka kwa Shetani, na pia linatokana na tabia ovu na potovu za mwandamu. Kwa sababu kuna jaribio, hili linahusisha kuwa shahidi; kuwa shahidi ni jukumu na wajibu wako pia. Baadhi ya watu husema: “Hili ni suala dogo sana; je, kuna umuhimu wa kufanya suala hili dogo kuwa kubwa hivyo?” Ndiyo pana haja! Kwa sababu ili kutembea katika njia ya Mungu, hatuwezi kuachilia chochote kinachotuhusu sisi wenyewe, au kinachofanyika karibu nasi, hata yale mambo madogo madogo. Haijalishi kama tunadhani tunapaswa kuyazingatia au la, maadamu jambo lolote linatukabili, tusiliache litupite. Mambo yote yanayotutokea yanapaswa kuonwa kama majaribio ya Mungu kwetu. Je, una maoni gani kuhusu mtazamo huu? Kama una mtazamo wa aina hii, basi inathibitisha ukweli mmoja kwamba: Moyo wako unamcha Mungu, na moyo wako upo tayari kujiepusha na maovu. Kama una shauku kama hii ya kumridhisha Mungu, basi kile ambacho unaweka katika vitendo hakiko mbali na kiwango cha kumcha Mungu na kujiepusha na maovu.

Mara nyingi wale wanaoamini kwamba masuala ambayo hayatiliwi maanani na watu, masuala ambayo kwa kawaida hayatajwi—haya ni mambo madogo tu, na hayana chochote kuhusiana na kuweka ukweli katika matendo. Wakati watu hawa wanakabiliwa na suala kama hilo, hawalifikirii sana na wanaliachilia tu. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba, suala hili ni somo ambalo unapaswa kujifunza, somo kuhusu namna ya kumcha Mungu, na namna ya kujiepusha na maovu. Zaidi ya hayo, kile unachopaswa kuzingatia zaidi ni kujua kile ambacho Mungu anafanya wakati suala hili linapokukabili. Mungu yuko kando yako, Anatazama kila neno na tendo lako, na Anatazama kila kitu unachofanya, na ni mabadiliko gani yanayotokea katika mawazo yako—hii ni kazi ya Mungu. Baadhi ya watu wanasema: “Ikiwa hiyo ni kweli, basi ni kwa nini siihisi?” Huihisi kwa sababu jinsi ya kumcha Mungu na kujiepusha na maovu haijawa ndiyo njia ya muhimu zaidi kwako kuishikilia. Kwa hivyo, huwezi kuihisi kazi ya Mungu isiyoeleweka kwa binadamu, ambayo inajidhihirisha kulingana na fikira tofauti na vitendo tofauti vya watu. Wewe upo makini! Suala kubwa ni lipi? Swala dogo ni lipi? Masuala yanayohusu kutembea katika njia ya Mungu hayagawanywi katika masuala makubwa au madogo, yote ni yenye umuhimu—je, mnaweza kulikubali hilo? (Tunaweza kulikubali). Kuhusiana na masuala ya kila siku, kuna yale ambayo watu wanayaona kuwa makubwa sana na muhimu, na mengine yanaonekana kuwa mambo madogo madogo tu. Mara nyingi watu wanayaona masuala haya makubwa kuwa ndiyo ya muhimu zaidi, na wanayachukulia kwamba yametumwa na Mungu. Hata hivyo, kwenye mkondo wa masuala haya makubwa yanayojitokeza, kutokana na kimo kidogo cha watu, na kutokana na kiwango duni cha watu, mara nyingi binadamu haendani sawa na nia za Mungu, hawezi kupata ufunuo wowote, na hawezi kufaidi maarifa yoyote halisi yenye thamani. Kuhusu masuala madogo, haya yanapuuzwa tu na watu, na kuachwa yaondoke moja kwa moja. Kwa hivyo, watu wamepoteza fursa nyingi sana za kuchunguzwa na kujaribiwa mbele za Mungu. Je, inamaanisha nini ikiwa kila mara unapuuza watu, matukio, masuala, na hali ambazo Mungu amekuandalia? Inamaanisha kwamba kila siku, hata kila wakati, unakana ukamilishaji wa Mungu kwako, na uongozi wa Mungu. Kila Mungu anapopanga hali hizi kwako, Yeye anakuangalia kwa siri, Anauchunguza moyo wako, Anaziangalia fikira na hali zako, Anaangalia namna unavyofikiria, Anaangalia namna unavyochukua hatua. Kama wewe ni mtu asiyejali—mtu ambaye hajawahi kujali kuhusu njia ya Mungu, neno la Mungu, au ukweli—basi hutajali, hutatilia maanani kile ambacho Mungu anataka kukamilisha, na yale ambayo Mungu anakuhitaji wewe uyafanye wakati Anapopanga hali hizi kwako. Wala hutajua jinsi watu, matukio na vitu ambavyo unakumbana navyo vinavyohusiana na ukweli au mapenzi ya Mungu. Baada ya kukabiliana na hali nyingi kama hizi na majaribio mengi kama haya, ikiwa Mungu haoni matokeo yoyote ndani yako, je, Atafanyaje? Baada ya kukabiliwa na majaribio mara kwa mara, hujamheshimu Mungu kama Aliye mkuu moyoni mwako, wala hujachukulia zile hali ambazo Mungu amekuandalia kwa uzito—na hujazichukulia kama majaribio au mitihani kutoka kwa Mungu. Badala yake unakataa fursa ambazo Mungu amekupa wewe moja baada ya nyingine, na unaziacha zitokomee mara kwa mara. Je, huku si kutokutii kwa hali ya juu ambako watu wanaonyesha? (Ndiyo, ni kutokutii.) Je, Mungu atahuzunika kwa mambo haya? (Ndiyo, Atahuzunika). Sivyo, Mungu hatahuzunika! Mnaposikia Nikiongea hivi mnashtuka kwa mara nyingine tena. Huenda ukawa unafikiria: “Je, haikusemwa hapo awali kwamba Mungu anahuzunika siku zote? Je, Mungu hatahuzunika? Ni lini basi Mungu atahuzunika? Kwa ufupi, Mungu hatahuzunika kuhusu jambo hili. Kwa hivyo, mtazamo wa Mungu ni upi katika aina hii ya tabia iliyoelezwa hapo juu? Wakati watu wanakataa majaribio na mitihani ambayo Mungu anawapa, wakati wanapoikwepa, kuna mtazamo mmoja tu ambao Mungu anao kwa watu kama hao. Je, mtazamo huo ni upi? Mungu anawadharau watu wa aina hio kutoka kwenye kina cha moyo Wake. Kuna safu mbili za maana ya neno “kudharau.” Je, Ninaelezeaje hilo kutoka kwa mtazamo Wangu? Neno “dharau” linabeba maana ya kukataa na kuchukia. Na je, safu ya pili ya maana ni ipi? Hiyo ndiyo sehemu inayomaanisha kukata tamaa juu ya kitu fulani. Ninyi nyote mnajua maana ya “kukata tamaa”, sivyo? Kwa ufupi, “kudharau” ni neno ambalo linawakilisha mwitikio na mtazamo wa mwisho wa Mungu kwa wale watu ambao wana tabia kama hiyo; ni chuki na karaha ya hali ya juu kwao, na hivyo inapelekea uamuzi wa kukata tamaa juu yao. Huu ndio uamuzi wa mwisho wa Mungu kwa mtu ambaye hajawahi kutembea katika njia ya Mungu, ambaye hajawahi kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Je, nyote mnaweza kuona sasa umuhimu wa msemo huu Niliouzungumzia?

Je, sasa mnaelewa njia ambayo Mungu anatumia katika kuamua matokeo ya watu? (Anapanga hali tofauti kila siku.) Anapanga hali tofauti—hili ni jambo ambalo watu wanaweza kuhisi na kugusa. Kwa hivyo, nia ya Mungu katika kufanya hivi ni nini? Dhumuni ni kwamba Mungu anataka kumpa kila mmoja wetu majaribio katika njia tofauti, katika nyakati tofauti, na katika sehemu tofauti. Ni vipengele vipi vya watu vinavyopimwa katika jaribio? Jaribio huamua kama wewe ni aina ya mtu ambaye anamcha Mungu na kujiepusha na maovu ama la, katika kila suala unalokabiliana nalo, unalosikia kuhusu, unaloliona, na unalolipitia wewe mwenyewe. Kila mtu atakabiliwa na aina hii ya majaribio, kwa sababu Mungu ni mwenye haki kwa watu wote. Baadhi ya watu husema: “Nimemwamini Mungu kwa miaka mingi; inakuaje kwamba sijawahi kukabiliwa na majaribu yoyote?” Unahisi kwamba hujawahi kukabiliwa na jaribio lolote kwa sababu, kila wakati Mungu alipopanga hali kwa ajili yako, hukuzichukulia hali hizo kwa uzito, na hukutaka kufuata njia ya Mungu. Kwa hivyo, huna hisia yoyote ya majaribio ya Mungu. Baadhi ya watu husema: “Nimekabiliwa na majaribio machache, lakini sijui njia bora ya kutenda. Hata ingawa nilitenda, bado sijajua kama nilisimama imara wakati huo wa majaribio.” Watu walioko katika hali ya aina hii bila shaka hawamo katika kundi la wale wachache. Kwa hivyo je, ni kiwango gani ambacho Mungu anawapima watu? Ni kama tu Nilivyosema muda mfupi uliopita: Ni ikiwa unamcha Mungu na kujiepusha na maovu au la, katika kila jambo unalofanya, unalofikiri na kueleza. Hivi ndivyo jinsi inavyoamuliwa kama wewe ni mtu anayemcha Mungu na kujiepusha na maovu. Je, kipengele hiki ni rahisi, au la? Ni rahisi mno kwa kusema, lakini je, ni rahisi kutekeleza? (Si rahisi mno.) Kwa nini si rahisi mno? (Kwa sababu watu hawamjui Mungu, hawajui namna ambavyo Mungu anamfanya binadamu kuwa mkamilifu, na hivyo basi wanapokabiliwa na masuala hawajui namna ya kutafuta ukweli ili kutatua tatizo lao; watu lazima wapitie majaribio mbalimbali, usafishaji, kuadibu, na hukumu kabla ya kuwa na uhalisi wa kumcha Mungu.) Mnasema hivyo, lakini kulingana na vile mnavyojua, kumcha Mungu na kujiepusha na maovu kunaonekana kuwa rahisi kufanywa kwa sasa. Kwa nini Nasema hivi? Kwa sababu mmesikiliza mahubiri mengi, na mmepokea kiwango kikubwa cha kunyunyiziwa kwa uhalisi wa ukweli. Hii imewaruhusu kuelewa namna ya kumcha Mungu na kujiepusha na maovu kwa mujibu wa nadharia na kufikiria. Kuhusiana na jinsi ya kuweza kumcha Mungu na kujiepusha na maovu katika vitendo, maarifa haya yote yamekuwa yenye manufaa na yamewafanya mhisi kwamba kitu kama hicho kinaweza kufanyika kwa urahisi. Basi ni kwa nini katika uhalisia wa mambo watu hawajawahi kukitimiza? Hii ni kwa sababu kiini cha asili ya binadamu hakimchi Mungu na kinapenda maovu. Hiyo ndiyo sababu halisi.

Kutomcha Mungu na Kutojiepusha na Maovu ni Kumpinga Mungu

Hebu tuanze kwa kuangazia ni wapi ambapo msemo huu “kumcha Mungu na kujiepusha na maovu” ulitokea. (Kitabu cha Ayubu.) Sasa kwa vile mmemtaja Ayubu, hebu tumzungumzie. Katika nyakati za Ayubu, je, Mungu alikuwa akifanya kazi kwa ajili ya wokovu na ushindi wa wanadamu? Hakufanya hivyo, sivyo? Na kuhusiana na Ayubu, ni maarifa ya kiwango gani aliyokuwa nayo kumhusu Mungu kwa wakati huo? (Si mengi.) Je, Ayubu alikuwa na maarifa mengi au kidogo kuhusu Mungu kuliko mliyo nayo ninyi sasa hivi? Kwa nini hamwezi kuthubutu kujibu? Hili ni swali rahisi sana kujibu. Ni kidogo! Hilo halina shaka! Sasa hivi mpo uso kwa uso na Mungu, uso kwa uso na neno la Mungu. Maarifa yenu ya Mungu ni mengi zaidi kuliko yale ya Ayubu. Kwa nini Naleta suala hili? Kwa nini Ninaongea hivi? Ningependa kuwaeleza ukweli mmoja, lakini kabla Sijafanya hivyo, Ningependa kuwauliza swali: Ayubu alijua machache sana kumhusu Mungu, lakini bado aliweza kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Kwa hivyo, ni kwa nini watu siku hizi wanashindwa kufanya hivyo? (Wamepotoka sana.) “Wamepotoka sana”—hili ni jambo la kijuujuu linalosababisha tatizo hili, lakini siwezi kulitazama kwa namna hiyo kamwe. Mara nyingi mnachukua mafundisho na maneno yanayotumiwa mara kwa mara, kama vile “upotovu mkubwa,” “kuasi dhidi ya Mungu,” “kutokuwa mwaminifu kwa Mungu,” “kukosa utiifu,” “kutopenda ukweli,” na kadhalika, mmetumia maneno kama haya katika kuelezea kiini cha kila swali. Hii ni njia isiyofaa ya kufanya mazoezi. Kutumia jibu moja katika kuelezea maswali yaliyo na asili tofauti, bila shaka, inaibua mashaka ya kuukufuru ukweli na Mungu. Sipendi kusikia jibu la aina hii. Hebu fikiria! Hakuna yeyote kati yenu ambaye amefikiria kuhusu suala hili, lakini kila siku Mimi Ninaliona, na kila siku Mimi Ninalihisi. Kwa hivyo, mnapolifanya, Mimi Ninatazama. Wakati mnapolifanya, hamwezi kuhisi kiini halisi cha suala hili. Lakini wakati Ninapoliona, Ninaweza kuona kiini chake, na Ninaweza kuhisi kiini chake. Kwa hivyo, kiini hiki ni kipi basi? Kwa nini watu siku hizi hawawezi kumcha Mungu na kujiepusha na maovu? Majibu yenu yako mbali na kuweza kuelezea kiini cha swali hili, wala hayawezi kulitatua. Hiyo ni kwa sababu ina chanzo ambacho ninyi hamkijui. Je, chanzo hicho ni nini? Ninajua mnataka kusikia kuhusu hilo, kwa hivyo Nitawaambia kuhusu chanzo cha swali hili.

Tangu Mungu Alipoanza kufanya kazi, je, Amewachukuliaje wanadamu? Mungu amewaokoa; Amewaona wanadamu kama washiriki wa familia Yake, kama walengwa wa kazi Yake, kama wale Aliotaka kuwashinda na kuwaokoa, na kama wale Aliotaka kuwakamilisha. Huu ndio ulikuwa mtazamo wa Mungu kwa binadamu mwanzoni mwa kazi Yake. Hata hivyo, je, mtazamo wa wanadamu kwa Mungu ulikuwa ni upi kwa wakati huo? Mungu alikuwa hafahamiki kwa wanadamu, na watu walimwona Mungu kama mgeni. Inaweza kusemwa kwamba, mtazamo wao kwa Mungu haukuleta matokeo sahihi, na kwamba hawakuwa na ufahamu wa wazi kuhusu jinsi wanavyopaswa kumtendea Mungu. Kwa hivyo, walimtendea Yeye jinsi wapendavyo, na wakafanya chochote walichopenda. Je, walikuwa na maoni yoyote kumhusu Mungu? Hapo mwanzo, binadamu hawakuwa na maoni yoyote kumhusu Mungu. Maoni ya binadamu kama yalivyojulikana, yalikuwa tu na baadhi ya dhana na fikira kumhusu Mungu. Kile ambacho kiliendana na dhana za watu kilikubalika; na kile ambacho hakikuendana na dhana zao, walitii kijuujuu, lakini ndani kabisa walihisi kuwa na mgongano mkubwa na waliipinga. Huu ndio ulikuwa uhusiano kati ya mwanadamu na Mungu hapo mwanzo: Mungu alimwona mwandamu kama mshiriki wa familia, lakini binadamu alimchukulia Mungu kama mgeni. Lakini baada ya kipindi cha kazi ya Mungu, binadamu alielewa hatimaye kile ambacho Mungu alikuwa akijaribu kutimiza. Wanadamu walikuja kuelewa kwamba Mungu ndiye aliyekuwa Mungu wa kweli, na hatimaye wakajua kile ambacho binadamu angeweza kupata kutoka kwa Mungu. Je, binadamu alimchukuliaje Mungu kwa wakati huu? Alimchukulia Mungu kama tegemeo kuu, akitumai kupokea neema, kupokea baraka, na kupokea ahadi Zake. Je, kwa wakati huu, Mungu alimchukuliaje binadamu? Mungu alimchukulia binadamu kuwa mlengwa wa ushindi Wake. Mungu alitaka kuyatumia maneno ili kumhukumu binadamu, kumpima binadamu, kumpa majaribio binadamu. Lakini kwa wanadamu wakati huu hasa, Mungu alikuwa kifaa ambacho wangeweza kutumia ili kutimiza malengo yao wenyewe. Watu waliona kwamba ukweli uliotolewa na Mungu ungeweza kuwashinda na kuwaokoa, kwamba walikuwa na fursa ya kupata vitu walivyotaka kutoka Kwake, na pia kufikia malengo waliyotaka. Kwa sababu ya hili, uaminifu mdogo ulijitokeza katika mioyo yao, na wakawa tayari kumfuata Mungu huyu. Muda ulipita, na kwa sababu watu walipata maarifa ya juujuu na ya kimafundisho kuhusu Mungu, inaweza hata kusemwa kwamba wanadamu walikuwa wameanza “kumfahamu” Mungu na maneno Aliyoyasema, mahubiri Yake, kweli Alizotoa, na kazi Yake. Kwa hivyo, watu walifikiria kimakosa kwamba Mungu hakuwa mgeni tena, na kwamba walikuwa tayari wakitembea katika njia ya kupatana na Mungu. Mpaka sasa, watu wamesikiliza mahubiri mengi ya ukweli, na wamepitia kazi nyingi ya Mungu. Hata hivyo, kwa sababu ya maingiliano na vizuizi vinavyosababishwa na mambo na hali nyingi tofauti, watu wengi hawawezi kufanikisha kuweka ukweli katika vitendo, wala hawawezi kumridhisha Mungu. Watu wanazidi kua walegevu na wanazidi kukosa ujasiri. Wanazidi kua na hisia kwamba matokeo yao wenyewe hayajulikani. Hawathubutu kuja na mawazo yoyote ya kupita kiasi, na hawatafuti kufanya maendeleo; wanafuata tu kwa kusita, kwenda mbele, hatua kwa hatua. Kuhusiana na hali ya sasa ya wanadamu, je, Mungu ana mtazamo gani kwao? Anatamani tu kuwapa kweli hizi, na kuwaweka hatua kwa hatua katika njia Yake, na kisha kupanga hali mbalimbali ili kuwajaribu kwa njia tofauti. Lengo Lake ni kuchukua maneno haya, ukweli huu, na kazi Yake, na kuleta matokeo, ambapo wanadamu wataweza kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Watu wengi ambao Nimewaona wanachukua maneno ya Mungu na kuyachukulia tu kama mafundisho, kama barua tu, wanayachukulia kama kanuni zinazopaswa kufuatwa. Katika matendo na usemi wao, au wanapokabiliwa na majaribu, hawachukulii njia ya Mungu kama njia ambayo wanapaswa kuifuata. Hii ni kweli hasa wakati watu wanapokabiliwa na majaribu makubwa; Sijaona mtu yeyote ambaye amekuwa akitenda katika mwelekeo wa kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Kwa sababu ya hili, mtazamo wa Mungu kwa wanadamu umejaa chuki na chuki kubwa! Ijapokuwa Mungu amewapa watu majaribio kadhaa, hata mara mia moja, bado hawana mtazamo wowote wa wazi wa kuonyesha azimio lao kwamba: “Nataka kumcha Mungu na kujiepusha na maovu!” Kwa kuwa watu hawana azimio hili na hawaonyeshi ishara kama hii, mtazamo wa sasa wa Mungu kwao, sio sawa na ulivyokuwa hapo zamani, Alipowapa rehema, uvumilivu, ustahimilivu, na subira Yake. Badala yake, Amekatishwa tamaa sana na binadamu. Je, ni nani aliyesababisha kukata tamaa huku? Je, mtazamo ambao Mungu anao kwa binadamu, unamtegemea nani? Unamtegemea kila mtu anayemfuata Mungu. Kwenye mkondo wa miaka Yake mingi ya kazi, Mungu ametoa mahitaji mengi kwa binadamu, na kupangilia hali nyingi kwa binadamu. Lakini haijalishi jinsi ambavyo binadamu ametenda, na haijalishi ni mtazamo upi ambao binadamu anao kwa Mungu, binadamu hawezi kutenda kwa njia sawa kulingana na malengo ya kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Kwa hivyo, Nitajumuisha yote haya kwa msemo mmoja, na kuweza kutumia msemo huu kuelezea kila kitu ambacho tumeweza kuzungumzia kuhusiana na ni kwa nini watu hawawezi kutembea katika njia ya Mungu—ya kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Msemo huu ni upi? Msemo huu ni: Mungu huwachukulia wanadamu kama walengwa wa wokovu Wake, na walengwa wa kazi Yake; wanadamu wanamchukulia Mungu kama adui yao, na kama Aliye kinyume nao. Je, unalielewa suala hili sasa? Kile ambacho ni mtazamo wa binadamu; kile ambacho ni mtazamo wa Mungu; kile ambacho ni uhusiano wa binadamu na Mungu—hivi vyote viko wazi sana kwa sasa. Haijalishi ni mahubiri mengi kiasi gani umesikiliza, yale mambo ambayo umefikia hitimisho lako mwenyewe, kama vile kuwa mwaminifu kwa Mungu, kumtii Mungu, kutafuta njia ya kupatana na Mungu, kutaka kutumia maisha yote kwa ajili ya Mungu, na kutaka kuishi kwa ajili ya Mungu—Kwangu, mambo hayo si mifano ya kufuata njia ya Mungu kwa uangalifu, ambayo ni kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Badala yake, ni njia mbalimbali ambazo mnaweza kufikia malengo fulani. Ili kufikia malengo hayo, unafuata kanuni fulani bila kupenda. Na ni kanuni hizi hasa ambazo huwapeleka watu mbali zaidi kutoka katika njia ile ya kumcha Mungu na kujiepusha na maovu, na kumweka Mungu katika upinzani na binadamu kwa mara nyingine tena.

Mada ya leo ni nzito kidogo, lakini haijalishi ni nini, bado Ninatumai kwamba wakati unapitia uzoefu ujao, na nyakati zijazo, utaweza kufanya kile ambacho Nimekuambia hivi punde. Usimchukulie Mungu kama hewa tupu-kana kwamba Anakuwepo tu wakati Yeye ni wa manufaa kwako, lakini wakatiambao humhitaji unahisi kwamba Yeye hayupo. Mara tu unapokuwa na wazo kama hilo katika ufahamu wako bila kujua, tayari umemkasirisha Mungu. Pengine kuna watu wanaosema, “Simchukulii Mungu kama hewa tupu. Mimi namwomba Yeye kila mara na ninajaribu kumridhisha Yeye, na kila kitu ninachofanya kipo ndani ya upeo, kiwango, na kanuni ambazo Mungu anahitaji. Bila shaka sifanyi kulingana na mawazo yangu mwenyewe.” Ndio, njia hii ambayo unafanya mazoezi ni sahihi. Hata hivyo, je, unafikiria nini unapokutana ana kwa ana na tatizo? Je, unatenda vipi unapokabiliwa na suala? Baadhi ya watu huhisi kwamba Mungu yupo wakati wanapomwomba Yeye, na kumsihi awasikilizea. Lakini wakati wanapokabiliwa na suala wanakuja na mawazo yao wenyewe na wanataka kuyatii. Hapa Mungu anachukuliwa kama hewa tupu. Hali ya aina hii inamfanya Mungu kutokuwepo katika akili zao. Watu wanafikiri kwamba Mungu anafaa kuwepo wakati wanapomhitaji Yeye, na wakati hawamhitaji Mungu hafai kuwepo. Watu wanafikiri kwamba kutenda kulingana na mawazo yao wenyewe inatosha. Wanaamini kuwa wanaweza kufanya chochote wanachopenda; hawaamini kwamba wanahitaji kutafuta njia ya Mungu. Watu ambao kwa sasa wamo katika hali ya aina hii, na wamekwama katika hali ya aina hii—je, hawaoni kwamba karibu wataingia hatarini? Baadhi ya watu husema: “Haijalishi kama karibu nitaingia hatarini au la, nimeamini kwa miaka mingi sana, na ninaamini kwamba Mungu hataniacha, kwa sababu Asingeweza kustahimili kuniacha mimi.” Watu wengine husema: “Nimemwamini Bwana tangu nilipokuwa tumboni mwa mama yangu. Imekuwa takriban miaka arobaini au hamsini, kwa hiyo katika suala la muda, ninastahili zaidi kuokolewa na Mungu, na ninastahili zaidi kuishi. Katika kipindi cha miongo hii minne au mitano, niliiacha familia yangu na kazi yangu. Nilijitolea kila kitu nilichokuwa nacho kwa Mungu, vitu kama vile pesa, hadhi, starehe, na wakati wa kuwa na familia yangu. Sijala vyakula vingi vitamu, sijafurahia burudani nyingi; sijatembelea sehemu nyingi za kuvutia; nimeweza hata kupitia mateso ambayo hata watu wa kawaida wasingevumilia. Kama Mungu hawezi kuniokoa mimi kwa sababu ya haya yote, basi mimi natendewa kwa njia isiyo ya haki, na siwezi kuamini katika Mungu wa aina hii.” Je, kuna watu wengi walio na mtazamo wa aina hii? (Wapo wengi sana.) Basi leo Nitawasaidia kuelewa ukweli mmoja: Kila mmoja wa hao anayeshikilia mtazamo wa aina hii, anachukua hatua zitakazomdhuru yeye mwenyewe. Hii ni kwa sababu wanatumia maoni yao binafsi katika kuyafunika macho yao. Ni fikira hizi hasa, pamoja na hitimisho zao binafsi, zinazochukua nafasi ya kiwango cha kile ambacho Mungu anahitaji kutoka kwa binadamu, ndizo zinazowazuia kukubali nia za kweli za Mungu, na kuwafanya wasiweze kuhisi uwepo wa kweli wa Mungu, na kuwafanya pia wapoteze fursa yao ya kukamilishwa na Mungu, na kutokuwa na sehemu au ushiriki katika ahadi ya Mungu.

Jinsi Mungu Anavyoamua Matokeo Ya Mwanadamu na Viwango Ambavyo Anatumia Kuamua Matokeo ya Mwanadamu

Kabla ya kuwa na mitazamo au hitimisho zako binafsi, unapaswa kwanza kuelewa mtazamo wa Mungu kwako ni upi, na kile Anachofikiria, kisha unaweza kuamua kama mawazo yako mwenyewe ni sahihi au la. Mungu hajawahi kutumia vipimo vya muda katika kuasisi matokeo ya mtu, na Hajawahi kutumia kiwango cha mateso yaliyovumiliwa na mtu katika kuamua matokeo yake. Kwa hivyo, basi, Mungu anatumia kiwango gani katika kuamua matokeo ya mtu? Kutumia kipimo cha wakati katika kuamua matokeo ya mtu—hii ndiyo inalingana zaidi na dhana za watu. Na pia kuna wale watu ambao mara nyingi mnawaona, wale ambao kwa wakati fulani walijitolea sana, wakatumia muda mwingi sana, wakagharamika sana, wakateseka sana. Hawa ndio, kwa maoni yenu, wanaweza kuokolewa na Mungu. Kile tu ambacho watu hawa wanaonyesha, yote wanayoishi kwa kudhihirisha, ndiyo hasa dhana ya wanadamu kuhusu kiwango ambacho Mungu anatumia kuamua matokeo ya binadamu. Haijalishi kile unachoamini, Sitaorodhesha mifano hii moja baada ya nyingine. Ili kuiweka kwa ufupi, chochote kile ambacho si kiwango kilicho ndani ya mawazo ya Mungu mwenyewe kinatokana na mawazo ya mwanadamu, na mambo hayo yote ni mawazo ya kibinadamu. Ikiwa unasisitiza kwa upofu dhana na matamanio yako mwenyewe, je, matokeo yatakuwa ni yapi? Ni dhahiri kabisa kwamba matokeo ya hili yanaweza tu kuwa Mungu atakukataa. Hii ni kwa sababu kila mara unajivunia sifa zako mbele za Mungu, unashindana na Yeye, na kubishana Naye, na hujaribu kuelewa kwa kweli mawazo Yake, wala hujaribu kuelewa nia Zake au mtazamo Wake kwa wanadamu. Unapoendelea kwa namna hii, unajiheshimu wewe mwenyewe kama mkuu; inakua humheshimu Mungu kama mkuu. Unajiamini wewe mwenyewe; humwamini Mungu. Mungu hamtaki mtu wa aina hii, na Mungu hatamwokoa mtu wa aina hii. Kama utaweza kuachilia mtazamo wa aina hii, na zaidi ya hayo, urekebishe maoni hayo yasiyo sahihi uliyokuwa nayo hapo awali, ikiwa utaweza kuendelea kulingana na matakwa ya Mungu; ikiwa utaweza kutenda kwa njia ya kumcha Mungu na kujiepusha na maovu kuanzia sasa na kuendelea; ikiwa utaweza kumheshimu Mungu na kumwona kama mkuu katika mambo yote; na usitumie matamanio yako binafsi, mitazamo, au imani ili kujifafanua nwenyewe na kumfafanua Mungu. Na kama, badala yake, unatafuta nia za Mungu katika hali zote, kama utafikia utambuzi na uelewa wa mtazamo wa Mungu kwa wanadamu, na kama utamridhisha Yeye kwa kufikia viwango Vyake—kufanya hivyo kutapendeza! Hii itamaanisha kwamba upo karibu kuingia katika njia ya kumcha Mungu na kujiepusha na maovu.

Kwa kuwa Mungu hatumii fikira, mawazo, na mitazamo mbalimbali ya watu, kama viwango vya kuamua matokeo yao, basi ni kiwango cha aina gani ambacho Anatumia katika kuamua matokeo ya watu? Mungu anatumia majaribio kuamua matokeo ya watu. Kuna viwango viwili vya kutumia majaribio ili kuamua matokeo ya watu: Kiwango cha kwanza ni idadi ya majaribio ambayo watu wanapitia, na kiwango cha pili ni matokeo ya watu katika majaribio hayo. Ni viashiria hivi viwili vinavyoamua matokeo ya mtu. Sasa, hebu tufafanue viwango hivi viwili.

Kwanza kabisa, unapokabiliwa na jaribio kutoka kwa Mungu (Inawezekana kwamba katika macho yako jaribio hili ni dogo sana na halifai kutajwa), Mungu atakufanya uwe na ufahamu kabisa kwamba huu ni mkono wa Mungu juu yako, na kwamba ni Mungu ambaye amepangilia hali hizi zote kwako. Wakati kimo chako hakijakomaa, Mungu atapanga majaribio ili kuweza kukupima. Majaribio haya yatalingana na kimo chako, yale ambayo unaweza kuelewa, na yale ambayo unaweza kustahimili. Ni sehemu gani kwako inayojaribiwa? Ni mtazamo wako kwa Mungu. Je, mtazamo huu ni muhimu sana? Bila shaka ni muhimu! Ina umuhimu maalumu! Kwa sababu mtazamo huu wa binadamu ndiyo matokeo ambayo Mungu anayataka, ndicho kitu cha muhimu zaidi kuliko vyote kwa Mungu. Vinginevyo, Mungu asingetumia juhudi Zake kwa watu kwa kushiriki katika kazi ya aina hiyo. Mungu anataka kuona mtazamo wako Kwake, kupitia kwa majaribio haya; Anataka kujua kama uko kwenye njia sahihi na Anataka kujua kama unamcha Mungu na kujiepusha na maovu. Hivyo basi, bila kujali kama unaelewa ukweli mwingi au kidogo kwa wakati huo, bado utakabiliwa na majaribio ya Mungu, na kufuatia ongezeko lolote katika kiwango chochote cha ukweli unaouelewa, Mungu ataendelea kupangilia majaribio sawa na hayo kwako. Wakati unapokabiliwa kwa mara nyingine tena na jaribio, Mungu anataka kuona iwapo maoni yako, mawazo yako, na mtazamo wako Kwake umepata ukuaji wowote katika kipindi cha muda. Baadhi ya watu husema: “Kwa nini siku zote Mungu anataka kuona mitazamo ya watu? Kwani Mungu hajaona namna wanavyouweka ukweli katika matendo? Kwa nini Atake tena kuona mitazamo ya watu?” Huku ni kupayuka kipuuzi! Ikizingatiwa kwamba Mungu anafanya kazi kwa namna hii, nia Yake lazima iwe humo. Siku zote Mungu anawaangalia watu Akiwa kando yao, Akiangalia kila neno na tendo lao, kila tendo na kusonga kwao, na hata kila fikira na wazo lao. Kila kitu kinachotokea kwa watu: matendo yao mema, makosa yao, dhambi zao, na hata kuasi na kusaliti kwao, Mungu atazirekodi hizizote kama ushahidi wa kuamua matokeo yao. Kadiri kazi ya Mungu inavyoendelea kuimarika hatua kwa hatua, unasikia ukweli zaidi na zaidi, unakubali mambo mazuri zaidi na zaidi, taarifa nzuri, na uhalisia wa kweli. Kwenye mkondo wa mchakato huu, mahitaji ya Mungu kwako yataongezeka pia. Wakati huo huo, Mungu atapanga majaribio makubwa zaidi kwako. Lengo Lake ni kuchunguza kama mtazamo wako kwa Mungu umekomaa mpaka sasa. Bila shaka, kwenye kipindi hiki, mtazamo ambao Mungu anahitaji kwako unaingiliana na uelewa wako wa uhalisi wa ukweli.

Kadiri kimo chako kinavyoongezeka polepole, kile kiwango ambacho Mungu atahitaji kutoka kwako kitaendelea kuongezeka taratibu pia. Ikiwa bado hujakomaa, Mungu atakupa kiwango kidogo sana; wakati kimo chako kitakapokuwa kikubwa kidogo, Mungu atakupa kiwango cha juu zaidi kidogo. Lakini Mungu atafanya nini baada ya kuwa umeelewa ukweli wote? Mungu atahakikisha kuwa unakabiliana na hata majaribio makubwa zaidi. Katikati ya majaribio haya, kile Mungu anachotaka kupata, kile Mungu anachotaka kuona, ni maarifa yako ya kina zaidi ya Mungu na uchaji wa kweli Kwake. Kwa wakati huu, mahitaji ya Mungu kwako yatakuwa ya juu zaidi “makali zaidi” kuliko wakati ambapo kimo chako kilikuwa kidogo zaidi (watu wanaona kwamba hali hii ni kali, lakini kwa hakika Mungu Anaiona kama inayostahimilika). Wakati Mungu anawapa watu majaribio, ni uhalisia wa aina gani ambao Mungu anataka kuunda? Mungu anauliza kila mara kwamba watu wampe Yeye mioyo yao. Baadhi ya watu watasema: “Mtu anawezaje kufanya hivyo? Natekeleza wajibu wangu, niliacha nyumba yangu na riziki yangu, niligharamika kwa sababu ya Mungu. Hii yote si mifano ya kuutoa moyo wangu kwa Mungu? Ni kwa namna gani tena ningeweza kuutoa moyo wangu kwa Mungu? Yaweza kuwa kwamba, hii si mifano ya kuutoa moyo wangu kwa Mungu? Mahitaji mahususi ya Mungu ni yapi?” Mahitaji haya ni mepesi mno. Kwa hakika, kuna baadhi ya watu ambao tayari wameitoa mioyo yao kwa Mungu katika viwango tofauti na awamu mbalimbali za majaribio yao. Lakini idadi kubwa ya watu hawaikabidhi mioyo yao kwa Mungu. Wakati Mungu anakupa jaribio, Mungu anataka kujua kama moyo wako uko pamoja na Yeye, pamoja na mwili au pamoja na Shetani. Mungu anapokupa jaribio, Mungu anataka kujua kama unasimama kinyume na Yeye au kama unasimama katika hali ambayo inalingana na Yeye, na kutaka kuona pia kama moyo wako uko upande Wake. Wakati haujakomaa na unakabiliwa na majaribio, kiwango cha imani yako kiko chini, na huwezi kujua hasa ni nini ambacho unahitaji kufanya ili kutosheleza nia za Mungu kwa sababu una uelewa mdogo wa ukweli. Licha ya haya yote, bado unaweza kumwomba Mungu kwa dhati na kwa unyofu, kuwa radhi kuutoa moyo wako kwa Mungu, na kumwacha Yeye akutawale, na kuwa radhi kumpa Mungu yale mambo unayosadiki kuwa yenye thamani zaidi. Hii ndiyo maana ya wewe kuwa tayari umempa Mungu moyo wako. Unaposikiliza mahubiri mengi zaidi na zaidi, na kuelewa ukweli zaidi na zaidi kimo chako kitaanza kukomaa kwa utaratibu. Kiwango ambacho Mungu anahitaji kutoka kwako si sawa na kile ambacho ulikuwemo wakati ulikuwa hujakomaa; Anahitaji kiwango cha juu zaidi kuliko hicho. Watu wanapotoa mioyo yao polepole kwa Mungu, mioyo yao inaanza kuwa karibu zaidi na zaidi kwa Mungu; kadri watu wanavyoweza kumkaribia Mungu kwa kweli, ndivyo wanavyozidi kuwa na mioyo inayomcha Mungu. Mungu anahitaji moyo wa aina hiyo.

Wakati Mungu anataka kuumiliki moyo wa mtu, Atawapa majaribio mengi. Kwenye majaribio haya, kama Mungu hatauchukua moyo wa mtu huyu, wala Haoni kama mtu huyu ana mwelekeo wowote—hiyo ni kusema Haoni kwamba mtu huyu anafanya mambo au anatenda kwa njia ya kumcha Mungu, na haoni mtazamo na azimio ambalo huepuka uovu kutoka kwa mtu huyu. Kama hivi ndivyo ilivyo, basi baada ya majaribio mengi, subira ya Mungu kwa mtu huyu binafsi itaondolewa, na Hatamvumilia mtu huyu tena. Hataweza kuwapa watu kama hawa majaribio, na Hataweza tena kuwashughulikia. Basi hiyo inamaanisha nini kwa matokeo ya mtu huyu? Inamaanisha kwamba hawatakuwa na matokeo. Yawezekana kwamba mtu huyu hajafanya maovu yoyote. Yawezekana pia kwamba watu hawa hawajafanya chochote cha kuvuruga au kutatiza. Yawezekana kuwa watu hawa hawajampinga Mungu waziwazi. Hata hivyo, moyo wa mtu huyu umefichwa kutoka kwa Mungu. Hawajawahi kuwa na mwelekeo na mtazamo wa wazi kwa Mungu, na Mungu hawezi kuona waziwazi kwamba moyo wake umekabidhiwa Kwake, na Yeye Hawezi kuona waziwazi kwamba mtu huyu anatafuta kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Mungu hana subira tena kwa watu hawa, Hatawagharamikia tena, Hatatoa tena rehema Yake kwao, na Hatafanya kazi kwao tena. Maisha ya imani ya mtu huyu katika Mungu tayari hayapo tena. Hii ni kwa sababu katika majaribio yote mengi ambayo Mungu amempa mtu huyu, Mungu hajapata matokeo Anayotaka. Kwa hivyo, kuna idadi ya watu ambao Sijawahi kuona mwangaza na nuru ya Roho Mtakatifu. Je, inawezekanaje kuona hili? Mtu wa aina hii anaweza kuwa amemwamini Mungu kwa miaka mingi, na kwa juu juu amekuwa na bidii sana. Wamesoma vitabu vingi, wameshughulikia mambo mengi, wamejaza zaidi ya madaftari 10 na maelezo, na wamefahamu barua na mafundisho mengi. Hata hivyo, hakuna ukuaji wowote unaoonekana, na kamwe hakuna mtazamo wowote unaoonekana kwa Mungu kutoka kwa mtu huyu, wala hakuna mwelekeo wowote wa wazi. Hiyo ni kusema kwamba huwezi kuona moyo wa mtu huyu. Mioyo yao daima imefungwa, mioyo yao imetiwa muhuri—imefungwa kwa Mungu, kwa hivyo Mungu hajauona moyo wa kweli wa mtu huyu, Hajaona hofu ya kweli ya mtu huyu kwa Mungu, na hata zaidi, Hajaona jinsi mtu huyu anatembea katika njia ya Mungu. Kama mpaka sasa Mungu hajampata mtu wa aina hii, je,Anaweza kuwapata katika siku za usoni? Hawezi! Je, Mungu ataendelea kusukumiza mbele mambo ambayo hayawezi kupatikana? Hatafanya hivyo! Mwelekeo wa Mungu kwa watu kama hawa, hivyo basi ni nini? (Anawasukumia mbali, Hawasikilizi.) Yeye hawasikilizi! Mungu hasikilizi mtu wa aina hii; Anawasukumia mbali. Mmetia kwenye kumbukumbu maneno haya kwa haraka sana, kwa usahihi sana. Inaonekana mmeelewa kile mlichosikia!

Kuna baadhi ya watu ambao, punde wanapoanza kumfuata Mungu, hawajakomaa na hawajui chochote; hawaelewi nia za Mungu; pia hawajui maana ya kuamini katika Mungu, huchukua njia iliyobuniwa na mwanadamu na potofu ya kuamini katika Mungu, kumfuata Mungu. Wakati mtu wa aina hii anapokabiliwa na majaribio hana habari na hajali kuhusu mwongozo na nuru ya Mungu. Hajui maana ya kuutoa moyo wake kwa Mungu na maana ya kusimama imara wakati wa jaribio. Mungu atampa mtu huyu kiasi cha muda, na katika wakati huu, Atawaruhusu kuelewa jaribu la Mungu ni nini, nia za Mungu ni nini. Baadaye, mtu huyu anahitaji kuonyesha maoni yake. Kuhusiana na watu wale walio katika awamu hii, Mungu angali anasubiri. Kuhusu wale watu ambao wana maoni fulani lakini bado wanayumba-yumba, wanaotaka kutoa mioyo yao kwa Mungu lakini hawajapatanishwa na kufanya hivyo, ambao, ingawa wameweka ukweli fulani wa kimsingi katika vitendo, wanapokabiliwa na jaribu kuu, wanalikwepa na kutaka kukata tamaa—ni nini mtazamo wa Mungu kuelekea watu hawa? Mungu angali bado ana matarajio kidogo kwa watu kama hawa. Matokeo hutegemea mitazamo na maonyesho yao. Je, Mungu huitikiaje ikiwa watu hawana bidii ili kufanya maendeleo? Anakata tamaa. Hii ni kwa sababu kabla Mungu hajakata tamaa juu yako, tayari wewe umekata tamaa juu yako. Kwa hivyo, huwezi kumlaumu Mungu kwa kufanya hivyo. Ni makosa kwako kuwa na malalamiko dhidi ya Mungu.

Swali la Kiutendaji Huleta Aina Zote za Aibu kwa Watu

Kuna aina nyingine ya mtu aliye na matokeo mabaya zaidi ya yote. Hawa ndio Nisiopenda kutaja sana. Hali si mbaya kwa sababu mtu huyu hupokea adhabu ya Mungu, au kwamba mahitaji ya Mungu kwao ni makali na wana matokeo mabaya. Badala yake, hali ni mbaya kwa sababu wanajifanyia wenyewe, kama inavyosemwa mara kwa mara: Wanajichimbia kaburi lao. Huyu ni mtu wa aina gani? Mtu huyu hatembei kwenye njia inayofaa, na matokeo yake yanafichuliwa mapema. Mungu humwona mtu wa aina hii kama lengo Lake kubwa zaidi la chuki Yake. Kama watu wanavyosema hawa ndio wa huzuni kuliko wote. Mtu wa aina hii ni mwenye shauku sana mwanzoni mwa kumfuata Mungu; wanalipa bei nyingi; wana maoni mazuri juu ya mtazamo wa kazi ya Mungu; wamejaa mawazo juu ya maisha yao ya baadaye; wana uhakika hasa katika Mungu, wakiamini kwamba Mungu anaweza kumfanya mwanadamu kuwa kamili, na kumfanya huyo mwanadamu kufikia hatima tukufu. Ilhali kwa sababu isiyoeleweka, mtu huyu kisha hukimbia akiwa katika harakati ya kazi ya Mungu. Ni nini maana ya mtu huyu kukimbia? Maana yake ni kwamba wanatoweka bila kwaheri, bila sauti yoyote. Wanaondoka bila kutaja neno lolote. Ingawa mtu wa aina hii anadai kumwamini Mungu, kamwe haweki mizizi yoyote kwenye njia ya kumwamini Mungu. Hivyo, haijalishi wameamini kwa muda gani, bado wanaweza kumwacha Mungu. Watu wengine wanaondoka kwenda kufanya biashara, wengine wanaondoka kwenda kuishi maisha yao, wengine wanaondoka ili kutajirika, wengine wanaondoka kwenda kuoa au kuolewa, kupata watoto…. Miongoni mwa wale wanaoondoka, kuna wengine ambao wana shambulio la dhamiri na wanataka kurudi, na wengine wanaoendelea vibaya sana kimaisha, wanaishi maisha tu na kuyasukuma kwa miaka na miaka. Wasukuma maisha hawa wamepitia mateso mengi, na wanasadiki kwamba kuwa ulimwenguni kuna maumivu mno, na hawawezi kutenganishwa na Mungu. Wanataka kurudi katika nyumba ya Mungu ili kupokea faraja, amani, shangwe, na kuendelea kumwamini Mungu ili kuepuka msiba, au kuokolewa na kupata hatima nzuri. Hii ni kwa sababu watu hawa wanasadiki kwamba upendo wa Mungu hauna mipaka, kwamba neema ya Mungu haiwezi kuisha na kwamba haiwezi kutumika yote. Wanasadiki kwamba haijalishi ni nini mtu amefanya, Mungu anafaa kumsamehe na kuvumilia maisha yao ya kale. Watu hawa wanasema mara kwa mara ya kwamba wanataka kurudi na kufanya wajibu wao. Kuna wale ambao hata hutoa baadhi ya mali zao kwa kanisa, wakitumaini kwamba hii ndiyo njia yao ya kurudi katika nyumba ya Mungu. Mtazamo wa Mungu kwa watu aina hii ni upi? Mungu anafaa kuanzisha vipi matokeo yao? Kuwa huru kuongea. (Nilidhani kwamba Mungu angewakaribisha watu wa aina hii, lakini baada ya kusikia hivyo sasa hivi, labda hawatakaribishwa tena.) Na wewe unafikiria vipi? (Mtu wa aina hii huja mbele za Mungu ili matokeo yake yasiwe ya kifo. Hawarudi kwa unyofu wa kweli. Badala yake, kutokana na maarifa kwamba kazi ya Mungu itakamilika hivi karibuni, wanakuja chini ya udanganyifu wa kupokea baraka.) Unasema kwamba mtu huyu hamwamini Mungu kwa dhati, hivyo Mungu hawezi kumkubali? Je, ndivyo ilivyo? (Ndiyo.) (Uelewa wangu ni kwamba mtu wa aina hii ni yule wa kujali maslahi yake kuliko uhaki wa jambo, na kwamba hamsadiki Mungu kwa dhati.) Hajapata kumsadiki Mungu; yeye ni mtu mwenye kuangalia maslahi yake kuliko haki. Yamesemwa vizuri! Watu hawa wanaojali maslahi yao ni wale ambao kila mmoja anawachukia. Wanaenda na mkondo tu, na hawawezi kusumbuliwa ili kufanya kitu isipokuwa kama watafaidi kwa jambo hilo. Bila shaka wanastahili dharau! Je, kuna kaka au dada mwingine yeyote mwenye maoni mengine? (Mungu hatawakubali tena kwa sababu kazi ya Mungu karibu inakamilika na sasa ndipo matokeo ya watu yanaandaliwa. Ni wakati huu ambapo watu hawa wanataka kurudi. Si kwa sababu kwa kweli wanataka kufuata ukweli; wanataka kurudi kwa sababu wanayaona majanga yakishushwa, au wanashawishiwa na mambo ya nje. Kama kweli walikuwa na moyo uliokuwa ukifuatilia ukweli, wasingewahi kukimbia wakiwa katikati ya safari.) Je, yapo maoni mengine? (Hawatakubaliwa. Kwa kweli Mungu aliwapa fursa lakini mtazamo wao kwa Mungu siku zote ulikuwa wa kutokumsikiliza. Bila kujali nia za mtu huyu ni zipi, na hata kama atatubu, Mungu bado hatamkubali. Hii ni kwa sababu Mungu tayari aliwapa fursa nyingi sana lakini wao walionyesha mtazamo wao: Walitaka kumwacha Mungu. Hivyo basi, wanapojaribu kurudi sasa, Mungu hatawakaribisha.) (Ninakubali pia kwamba Mungu hatamkaribisha mtu wa aina hii, kwa sababu kama mtu ameona njia ya kweli, akapitia kazi ya Mungu kwa kipindi kirefu kama hicho, na bado anaweza kurudi kwa ulimwengu, kurudi kwa kumbatio la Shetani, basi huu ni usaliti mkubwa kwa Mungu. Licha ya ukweli kwamba kiini cha Mungu ni rehema, na upendo, inategemea ni mtu wa aina gani ambaye kiini hicho kinaelekezwa kwake. Kama mtu huyu atakuja mbele ya Mungu akitafuta faraja, kitu cha kuwekea tumaini lake, basi mtu wa aina hii kwa kweli si mtu anayemwamini Mungu kwa dhati, na rehema za Mungu kwake zinaishia hapo.) Kiini cha Mungu ni rehema, kwa hivyo ni kwa nini Hampatii mtu wa aina hii rehema zaidi kidogo tu? Kwa rehema kidogo zaidi, je, mtu huyu hangepata fursa? Hapo awali, watu walisema mara kwa mara kwamba, Mungu anataka kila mtu aokolewe na Hataki mtu yeyote apotee. Kama kondoo mmoja miongoni mwa kondoo mia moja atapotea, Mungu atawaacha wale kondoo tisini na tisa kumtafuta yule kondoo aliyepotea. Sasa, inapokuja kwa watu wa aina hii, je, Mungu anapaswa kuwakubali na kuwapa nafasi ya pili kwa sababu ya imani yao ya kweli kwa Mungu? Kwa kweli hili si swali gumu; ni rahisi sana! Ikiwa unamtambua Mungu kwa kweli, na una maarifa halisi Kwake, basi hakuna maelezo mengi yanayohitajika—na hakuna ufafanuzi mwingi unaohitajika, sivyo? Majibu yenu yapo kwenye njia sahihi, lakini bado yana umbali na ule mtazamo wa Mungu.

Sasa hivi tu kulikuwepo na baadhi yenu mliokuwa na uhakika kwamba Mungu asingeweza kumkubali mtu wa aina hii. Wengine hawakuwa na uhakika sana kuwa Mungu anaweza kuwakubali, na huenda asiwakubali—mtazamo huu ndio ule wa wastani; na kisha kulikuwa na wale ambao mtazamo wao ulikuwa kwamba wanatumai kwamba Mungu atamkaribisha mtu wa aina hii—huu ndio ule mtazamo usioeleweka. Wale walio na mtazamo wenye uhakika wanaamini kuwa Mungu amefanya kazi mpaka sasa, na kazi Yake imekamilika, hivyo basi Mungu hahitaji kuwa mvumilivu kwa watu hawa, na kwamba Hatawakaribisha tena. Wale watu wa wastani wanasadiki kwamba masuala haya yanafaa kushughulikiwa kulingana na hali inayowazunguka: Kama moyo wa mtu huyu hauwezi kutenganishwa na wa Mungu, na bado wao ni watu wanaomsadiki Mungu kwa kweli, mtu anayefuatilia ukweli, basi Mungu hafai kukumbuka udhaifu na makosa yao ya awali; Anafaa kuwasamehe, na kuwapa fursa nyingine, kuwaruhusu kurudi katika nyumba ya Mungu, na kukubali wokovu wa Mungu. Hata hivyo, kama mtu huyu atatoroka kwa mara nyingine, hapo ndipo Mungu hatamtaka mtu huyu na kitendo hiki hakitachukuliwa kuwa cha ukiukaji wa haki. Kuna kundi jingine ambalo linatumaini kwamba Mungu anaweza kumkaribisha mtu huyu. Kundi hili halina uhakika sana kama Mungu anawakaribisha au la. Kama wanaamini kwamba Mungu anafaa kuwakaribisha, lakini Mungu asiwakaribishe, basi yaonekana kwamba wamepotoka kidogo na mtazamo wa Mungu. Kama watasadiki kwamba Mungu hafai kuwakaribisha, naye Mungu atokee kusema kwamba upendo Wake kwa binadamu hauna kikomo na kwamba Yuko radhi kumpa mtu fursa nyingine, basi huu si mfano wa kutojua kwa binadamu ukiwekwa wazi? Kwa vyovyote vile, nyinyi nyote mna mitazamo yenu binafsi. Mitazamo hii ni maarifa katika fikira zenu binafsi; ni onyesho pia la kina cha uelewa wenu wa kweli na uelewa wenu wa nia za Mungu. Imesemwa vyema, sivyo? Ni jambo la kupendeza kwamba mna maoni katika suala hili! Lakini suala kuhusu kama maoni yenu ni sahihi au si sahihi, kuna alama ya kiulizo. Je, nyinyi nyote hamna wasiwasi kidogo? “Ni nini kilicho sahihi basi? Siwezi kuona kwa uwazi, na sijui hasa kile anachofikiria Mungu. Mungu hakuniambia chochote. Nawezaje kujua anachofikiria Mungu? Mtazamo wa Mungu kwa binadamu ni upendo. Kulingana na mtazamo wa kale wa Mungu, Anafaa kumkubali mtu huyu. Lakini sina uhakika kuhusu mtazamo wa sasa wa Mungu—ninaweza kusema tu kwamba pengine Atamkaribisha mtu huyu na pengine Hatamkaribisha.” Je, huu si ujinga? Jambo hili limewachanganya sana. Kama hamna msimamo bora wa suala hili basi ni nini mtakachofanya endapo kanisa lenu litakumbana kwa kweli na mtu wa aina hii? Kama hamtalishughulikia kwa njia bora, basi pengine mtamkosea Mungu. Je, hamuoni kwamba suala hili ni hatari mno?

Kwa nini Ninataka kuulizia maoni yenu kuhusu kile Nilichokuwa Nazungumzia? Nataka kupima mitazamo yenu, kupima ni maarifa kiasi kipi ya Mungu mliyo nayo, ni uelewa kiasi kipi mlio nao katika nia za Mungu na mtazamo wa Mungu. Jibu ni lipi? Jibu limo kwenye mitazamo yenu. Baadhi yenu mnashikilia sana ukale, na baadhi yenu mnatumia kufikiria kwenu katika kukisia. “Kukisia” ni nini? Ni wakati ambapo hamjui jinsi Mungu anavyofikiri, kwa hivyo mnakuja na mawazo yasiyo na msingi kuhusu jinsi Mungu anavyopaswa kufikiria kwa njia hii au ile. Hamna uhakika kama kukisia kwenu ni sahihi au si sahihi, na hivyo basi mnatoa mtazamo usioleweka. Mnapokabiliwa na ukweli huu mnaona nini? Wakati wakimfuata Mungu, ni nadra sana kwa watu kutilia maanani makusudi ya Mungu, na ni nadra wao kutilia maanani mawazo ya Mungu na mtazamo Wake kwa wanadamu. Watu hawaelewi fikira za Mungu, kwa hivyo mnapoulizwa maswali yanayohusisha nia za Mungu, yanayohusisha tabia ya Mungu, mnaingia katika hali ya kutokuwa na uhakika; mnakuwa kwa kweli hamna uhakika, na mnakisia au kubahatisha. Mtazamo huu ni upi? Inathibitisha ukweli huu: kwamba watu wengi wanaomwamini Mungu wanamwona kama kundi la hewa tupu na kama kitu kinachoonekana kuwapo dakika moja na sio ijayo. Kwa nini Nasema hivyo? Kwa sababu kila wakati mnapokumbwa na suala, hamzijui nia za Mungu. Kwa nini hamzijui? Si kwamba hamzijui tu kwa sasa. Badala yake kuanzia mwanzo hadi mwisho hamjui mtazamo wa Mungu katika suala hili. Katika nyakati zile ambazo huwezi kuona na hujui mtazamo wa Mungu, je, umewahi kuifikiria sana? Je, umetafuta kuijua? Je, umeshiriki kuhusu hilo? La! Hii inathibitisha ukwei: Mungu wa imani yako na Mungu wa kweli hawana uhusiano. Wewe, unayeamini katika Mungu, unafikiria tu mapenzi yako mwenyewe, unafikiria tu mapenzi ya viongozi wako, na unafikiria tu maana ya juu juu na ya kimafundisho ya neno la Mungu, lakini hufanyi kwa dhati kujaribu kujua na kutafuta mapenzi ya Mungu hata kidogo. Sivyo ndivyo hali ilivyo? Kiini cha suala hili hakipendezi! Kwa miaka mingi Nimeona watu wanaomsadiki Mungu. Kusadiki huku kunachukua mfumo gani? Baadhi ya watu wanamwamini Mungu kana kwamba Yeye ni hewa tupu. Watu hawa hawana jibu kwa maswali ya kuwepo kwa Mungu kwa sababu hawawezi kuhisi au kufahamu uwepo au kutokuwepo kwa Mungu, sembuse kuona au kuelewa kwa uwazi. Kwa nadharia yao, watu hawa wanafikiria kwamba Mungu hayupo. Baadhi wanasadiki katika Mungu ni kana kwamba Yeye ni binadamu. Watu hawa wanasadiki kwamba Mungu hawezi kufanya mambo yale ambayo wao hawawezi kufanya, na kwamba Mungu anafaa kufikiria namna wanavyofikiria. Ufafanuzi wa mtu huyu kuhusu Mungu ni “mtu asiyeonekana na asiyegusika.” Kunalo pia kundi la watu wanaosadiki katika Mungu kana kwamba Yeye ni kikaragosi; watu hawa wanasadiki kwamba Mungu hana hisia. Wanafikiria kwamba Mungu ni sanamu ya matope, na kwamba wanapokabiliwa na jambo, Mungu hana mwelekeo, hana mtazamo, hana mawazo; Anatawaliwa na binadamu. Watu wanasadiki tu wanavyotaka kusadiki. Wakimfanya kuwa mkubwa, Yeye ni mkubwa; wakimfanya kuwa mdogo, Yeye ni mdogo. Wakati wanapotenda dhambi na wanahitaji rehema za Mungu, wanapohitaji uvumilivu wa Mungu, wanapohitaji upendo wa Mungu, basi Mungu anafaa kutoa rehema Zake. Watu hawa wanamuunda “Mungu” katika akili zao wenyewe, na kisha wanamfanya “Mungu” huyu atimize mahitaji yao na kutosheleza matamanio yao yote. Haijalishi ni lini na ni wapi, na haijalishi watu kama hao wanafanya nini, watachukua dhana hii katika kumtendea Mungu, na katika imani yao kwa Mungu. Kuna hata wale wanaosadiki katika Mungu kuweza kuwaokoa baada kuikera tabia ya Mungu. Hii ni kwa sababu wanasadiki kuwa upendo wa Mungu hauna mipaka, tabia ya Mungu ni ya haki, na kwamba bila kujali ni vipi ambavyo watu wanamkosea Mungu, Hatakumbuka chochote. Wanafikiri kwamba kwa sababu makosa ya binadamu, dhambi za binadamu na kutotii kwa binadamu ni maonyesho ya mara moja ya tabia ya mtu huyo, Mungu atawapatia watu fursa, kuvumilia na kuwa na subira nao. Mungu angali atawapenda kama awali. Kwa hivyo tumaini la wokovu wao lingali kubwa. Kwa hakika, haijalishi jinsi mtu anavyomwamini Mungu, mradi tu hafuatilii ukweli, basi Mungu ana mtazamo hasi kwake. Hii ni sababu wakati unamsadiki Mungu, labda unakithamini kitabu cha neno la Mungu unakichambua kila siku, unakisoma kila siku, lakini unamweka Mungu halisi pembeni, unamchukulia kama hewa tupu, unamchukulia Yeye kama mtu, na baadhi yenu mnamchukulia kuwa kikaragosi. Kwa nini Nasema hivi? Kwa sababu kutokana na jinsi Ninavyoiona, bila kujali kama unakabiliwa na jambo au hali fulani, mambo yale ambayo yapo katika ufahamu wako mdogo, mambo yale ambayo yamekuzwa ndani—hakuna hata moja kati ya hayo yenye uhusiano wowote na neno la Mungu au kufuatilia ukweli. Unajua tu kile ambacho wewe mwenyewe unafikiria, maoni yako mwenyewe ni nini, na kisha unalazimishia mawazo yako na maoni yako mwenyewe kwa Mungu. Katika akili yako yanakuwa maoni ya Mungu, nawe unaweka viwango hivi vya maoni ambavyo unashikilia bila kuyumbayumba. Baada ya muda, kuendelea hivi kunakupeleka mbali zaidi na Mungu.

Elewa Mtazamo wa Mungu na Utupilie Mbali Dhana zote Potovu Kumhusu Mungu

Mungu huyu ambaye kwa sasa mnamwamini, je, mmewahi kufikiria Yeye ni Mungu wa aina gani? Anapomwona mtu mwovu akifanya mambo maovu, je Anayachukia? (Anayachukia.) Anapoona makosa ya watu wajinga, mtazamo Wake ni upi? (Huzuni.) Anapowaona watu wakiiba matoleo Yake, je, mtazamo Wake ni upi? (Anawachukia.) Haya yote yako wazi sana, sivyo? Anapoona mtu akiwa mzembe katika imani yake kwa Mungu, na kwa njia yoyote asifuatilie ukweli, ni nini mtazamo wa Mungu? Hamko wazi kabisa juu ya hili, sivyo? Uzembe ni tabia ambayo si dhambi, na si kumkosea Mungu. Watu wanaamini kuwa haupaswi kuzingatiwa kama kosa. Basi mnafikiria mtazamo wa Mungu ni nini? (Hayuko tayari kuitikia.) Kutotaka kuitikia—huu ni mtazamo gani? Ni kwamba Mungu anawadharau watu hawa, anawachukia watu hawa! Mungu hushughulika na watu hawa kwa kutowathamini. Mtazamo Wake ni kuwaweka kando, bila kujihusisha katika kazi yoyote juu yao, ikiwemo kuwapa nuru, mwangaza, kuwarudi, au kuwaadibu. Mtu wa aina hii hahesabiwi katika kazi ya Mungu. Je, mtazamo wa Mungu kwa watu wanaoikera sana tabia Yake, na kuzikosea amri Zake za kiutawala ni upi? Chuki kupindukia! Kwa kweli Mungu anakasirishwa sana na watu ambao hawatubu kwa kuikera sana tabia Yake! “Hasira Kali” ni hisia tu, hali ya moyo; haiwezi kuwakilisha mtazamo kamili. Lakini hisia hii, hali hii ya moyo, itasababisha matokeo kwa mtu huyu: Itamjaza Mungu chuki kali! Je, ni nini matokeo ya chuki hii iliyokithiri? Ni kwamba Mungu atamweka pembeni mtu huyu, na kutomwitikia kwa sasa. Kisha atasubiri kuwashughulikia “baada ya msimu wa kupukutika kwa majani.” Je, hii inaashiria nini? Je, mtu huyu bado ana matokeo? Mungu hakuwahi kunuia kumpa mtu wa aina hii matokeo! Hivyo basi si jambo la kawaida endapo Mungu kwa sasa hamwitikii mtu wa aina hii? (Ndiyo.) Je, mtu wa aina hii anapaswa kujiandaa kufanya nini? Anapaswa kujitayarisha kukabiliana na zile athari mbaya zilizosababishwa na tabia zao na maovu waliofanya. Huu ndio mwitikio wa Mungu kwa mtu wa aina hii. Hivyo basi Nasema waziwazi kwa mtu wa aina hii: Usishikilie imani za uwongo tena, na usijihusishe katika kufikiria makuu tena. Mungu hatawavumilia watu siku zote bila kikomo; Hatastahimili dhambi zao au kutotii kwao bila kukoma. Baadhi ya watu watasema: “Pia nimeona watu wachache kama hawa. Wanapoomba wanaguswa hasa na Mungu, na wanalia kwa uchungu. Kwa kawaida wao pia wana furaha sana; wanaonekana kuwa na uwepo wa Mungu, na mwongozo wa Mungu.” Usiseme huo upuzi! Kulia kwa uchungu si lazima iwe kwamba mtu ameguswa na Mungu au kuwa na uwepo wa Mungu, achilia mbali mwongozo wa Mungu. Kama watu watamghadhabisha Mungu, je, bado Mungu atawaongoza? Nikiongea kwa ujumla, wakati Mungu ameamua kumwondoa mtu, kuwaacha watu hao, tayari mtu huyo hana matokeo. Haijalishi ni vipi wanavyohisi kutosheka kujihusu wao wenyewe wakati wanapoomba, na imani kiwango kipi walichonacho katika Mungu mioyoni mwao; tayari hii si muhimu. Kitu cha muhimu ni kwamba Mungu hahitaji aina hii ya Imani, kwamba Mungu tayari amemsukumia mbali mtu huyu. Jinsi ya kukabiliana nao baadaye pia sio muhimu. Kilicho muhimu ni kwamba wakati mtu huyu anamghadhabisha Mungu, matokeo yake tayari yameamuliwa. Ikiwa Mungu ameamua kutomwokoa mtu wa aina hii, basi ataachwa nyuma ili kuadhibiwa. Huu ni mtazamo wa Mungu.

Ingawa sehemu ya kiini cha Mungu ni upendo, na Anaitoa rehema yake kwa kila mtu, watu hupuuza na kusahau ukweli kwamba kiini Chake halisi ni heshima vilevile. Kwamba Ana upendo haimaanishi kwamba watu wanaweza kumkosea Yeye wapendavyo na Hana hisia zozote, au miitikio yoyote. Kwamba Ana rehema haimaanishi kwamba Hana kanuni zozote katika jinsi Anavyowatendea watu. Mungu yu hai; kwa kweli Yupo. Yeye si kikaragosi kilichofikiriwa au kitu kingine tu. Kwa kuwa Yeye yuko, tunapaswa kusikiliza kwa makini sauti ya moyo Wake wakati wote, kuzingatia makini mtazamo Wake, na kuzielewa hisia Zake. Hatupaswi kutumia mawazo ya watu kumfafanua Mungu, na hatupaswi kulazimisha mawazo na matamanio ya watu kwa Mungu, na kumfanya Mungu atumie mtindo na kufikiri kwa mwanadamu katika jinsi Anavyowatendea wanadamu. Ukifanya hivyo, basi unamghadhabisha Mungu, unaijaribu hasira ya Mungu, na unapinga heshima ya Mungu! Hivyo basi, baada ya kuelewa ukali na uzito wa suala hili, Ninasihi kila mmoja wenu aliye hapa kuwa makini na wenye busara katika vitendo vyenu. Kuwa makini na wenye busara katika kuongea kwenu. Na kuhusu jinsi mnavyomtendea Mungu, kadiri mnavyokuwa waangalifu na wenye busara zaidi, ndivyo ilivyo bora! Wakati huelewi mtazamo wa Mungu ni nini, usizungumze kwa uzembe, usiwe mzembe katika vitendo vyako, na usipachike majina ovyo ovyo. Na hata zaidi, usikimbilie kufanya hitimisho kiholela. Badala yake, unafaa kusubiri na kutafuta; hili pia ndilo dhihirisho la kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Ikiwa wewe unaweza kufikia kiwango hiki zaidi ya yote, na kuwa na mtazamo huu zaidi ya yote, basi Mungu hatakulaumu kwa upumbavu wako, ujinga wako, na ukosefu wa kuelewa sababu za mambo. Badala yake, kwa sababu ya hofu yako ya kumkosea Mungu, heshima yako kwa mapenzi ya Mungu, na mtazamo wako wa kutaka kumtii, Mungu atakukumbuka, atakuongoza na kukupa mwanga, au kuvumilia uchanga na ujinga wako. Kinyume chake, endapo mtazamo wako Kwake utakuwa usio na heshima—kumhukumu Mungu kiholela, kukisia kiholela, na kufafanua mawazo ya Mungu—Mungu atakupa hukumu, nidhamu, au hata adhabu; au Atakupa kauli. Pengine kauli hii inahusisha matokeo yako. Hivyo basi, Ningali bado nataka kutilia mkazo jambo hili kwa mara nyingine tena: Unapaswa uwe makini na mwenye busara katika kila kitu kinachotoka kwa Mungu. Usiongee kwa uzembe, na usiwe mzembe katika matendo yako. Kabla ya kusema chochote, unafaa kufikiria: Je, kufanya hivi kutamghadhabisha Mungu? Je, kufanya hivi ni kumcha Mungu? Hata katika masuala mepesi, bado unafaa kujaribu kuelewa hakika maswali haya, yafikirie kwa kweli. Ikiwa unaweza kwa kweli kutenda kulingana na kanuni hizi katika nyanja zote, katika mambo yote, kila wakati, na kukubali mtazamo kama huu hasa wakati huelewi kitu, basi Mungu atakuongoza daima na kukupatia njia ya kufuata. Bila kujali ni nini ambacho watu wanaonyesha, Mungu anaona yote waziwazi, dhahiri, na Atakupa utathmini sahihi na unaofaa kwa maonyesho haya. Baada ya kupitia jaribio la mwisho, Mungu atachukua tabia yako yote na kuijumlisha ili kuamua matokeo yako. Matokeo haya yatamshawishi kila mmoja bila shaka lolote. Kile ambacho Ningependa kuwaambia ni kwamba kila kitendo chenu, kila hatua yenu, na kila fikira yenu vyote vitaamua majaliwa yenu.

Ni Nani Hupanga Matokeo ya Binadamu

Kuna jambo lingine muhimu zaidi, na hilo ni mtazamo wenu kwa Mungu. Mtazamo huu ni muhimu sana! Unaamua kama hatimaye mtatembea katika maangamizo, au kwenye hatima nzuri na ya kupendeza ambayo Mungu amewatayarishia. Katika Enzi ya Ufalme, Mungu tayari amefanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 na kwenye kipindi cha miaka hii 20 pengine mioyo yenu imekuwa na tashwishi kuhusu utendakazi wenu. Hata hivyo, katika moyo wa Mungu, Ameweka rekodi halisi na ya kweli kwa kila mmoja wenu. Kuanzia wakati kila mtu anapoanza kumfuata na kusikiliza mahubiri Yake, kuelewa zaidi na zaidi ukweli, hadi wakati wanatekeleza wajibu wao—Mungu ana rekodi ya kila moja ya maonyesho haya. Wakati mtu anapofanya wajibu wake, wakati anapokabiliwa na kila aina ya hali, kila aina ya majaribio, mtazamo wa mtu huyo ni upi? Wanatenda kazi vipi? Je, wanajisikiaje kumwelekea Mungu mioyoni mwao? … Mungu anayo maelezo ya haya yote, rekodi yake yote. Pengine kutokana na mtazamo wenu, masuala haya yanakanganya. Hata hivyo, kutoka pale ambapo Mungu yupo, yote yako wazi kabisa, na hakuna hata dalili yoyote ya kutokuwa wazi. Hili ni suala linahusisha matokeo ya kila mmoja, na hatima zao na matarajio ya siku zijazo pia. Hata zaidi, hapa ndipo ambapo Mungu anatumia jitihada Zake zote alizomakinikia. Hivyo basi Mungu hathubutu kuipuuza hata kidogo, na Hatavumilia kutomakinika kokote. Mungu anarekodi haya yote kuhusu mwanadamu, akirekodi historia ya mwenendo mzima wa mwanadamu kumfuata Mungu, kutoka mwanzo hadi mwisho. Mtazamo wako kwa Mungu wakati huu utaamua hatima yako. Je, haya si kweli? Sasa, mnaamini kwamba Mungu ni mwenye haki? Je, matendo ya Mungu yanafaa? Je, bado mna picha nyingine yoyote ya Mungu vichwani mwenu? (La.) Kisha mnasema kwamba matokeo ya mwanadamu ni kwa ajili ya Mungu kuweza kupanga au kwa mwanadamu mwenyewe kupanga? (Ni kwa Mungu kupanga.) Je, ni nani basi anayeyapanga? (Mungu.) Hamna hakika, sivyo? Ndugu kutoka makanisa ya Hong Kong, ongeeni—ni nani anayeyapanga? (Binadamu anayapanga mwenyewe.) Mwanadamu anayapanga? Hivyo basi haimaanishi kwamba haina chochote kuhusu Mungu? Ndugu kutoka Korea Kusini, ongeeni. (Mungu anaamua matokeo ya binadamu kutokana na hatua na vitendo vyake vyote na kutokana pia na njia wanayoitembea.) Hili ni jibu halisi sana. Kuna ukweli hapa ambao ni lazima Niwafahamishe nyinyi: Kwenye mkondo wa kazi ya wokovu wa Mungu, Yeye huweka kiwango kwa binadamu. Kiwango hiki ni kwamba binadamu anaweza kutii neno la Mungu, na kutembea katika njia ya Mungu. Ndicho kiwango kinachotumika kupima matokeo ya binadamu. Kama utatenda kwa mujibu wa kiwango hiki cha Mungu, basi unaweza kupata matokeo mazuri; kama hutafanya hivyo, basi huwezi kupokea matokeo mazuri. Basi ni nani unayesema kwamba anayapanga matokeo haya? Si Mungu pekee anayeyapanga, lakini badala yake Mungu na binadamu pamoja. Hiyo ni sahihi? (Ndiyo.) Kwa nini ipo hivyo? Kwa sababu ni Mungu ambaye anataka kujishughulisha na kujihusisha katika kazi ya wokovu wa wanadamu, na kutayarisha hatima nzuri kwa ajili ya binadamu; binadamu ndiye mlengwa wa kazi ya Mungu, na matokeo haya, hatima hii, ndiyo ambayo Mungu humtayarishia binadamu. Kama kusingekuwa na mlengwa wa kazi Yake, basi Mungu asingehitaji kazi hii; kama Mungu asingefanya kazi hii, basi binadamu asingekuwa na fursa ya wokovu. Binadamu ndiye mlengwa wa wokovu, na ingawa binadamu yumo kwenye upande wa kimya katika mchakato huu, ni mwelekeo wa upande huu ambao unaamua kama Mungu atafanikiwa katika kazi Yake ya kuwaokoa wanadamu au la. Kama si mwongozo ambao Mungu anakupa wewe, basi usingejua kiwango Chake, na usingekuwa na lengo lolote. Kama unacho kiwango hiki, lengo hili, ilhali hushirikiani, huliweki katika vitendo, hulipii gharama, basi bado hutapokea matokeo haya. Kwa sababu hii, Ninasema kwamba matokeo haya hayawezi kutenganishwa na Mungu, na pia hayawezi kutenganishwa na binadamu. Na sasa unaweza kujua ni nani anayepanga matokeo ya binadamu.

Watu Huishia Kumfafanua Mungu Kutokana na Uzoefu Wao

Wakati wa kuwasilisha mada ya kumjua Mungu, je, mmegundua kitu? Je, mmegundua kwamba mtazamo wa sasa wa Mungu umepitia mabadiliko? Je, mtazamo wa Mungu kwa wanadamu hauwezi kubadilika? Je, siku zote Mungu atavumilia hivi, huku Akitoa upendo Wake wote na rehema kwa binadamu bila kikomo? Suala hili pia linahusu kiini halisi cha Mungu. Hebu turudi kwenye swali la yule anayeitwa mwana mpotevu kutoka hapo awali. Baada ya swali hili kuulizwa, majibu yenu hayakuwa wazi sana. Kwa maneno mengine, bado hamwelewi vyema nia za Mungu. Punde tu watu wanapojua kwamba Mungu anawapenda wanadamu, wanamfafanua Mungu kama ishara ya upendo: Haijalishi kile wanachofanya watu, haijalishi namna wanavyotenda mambo, haijalishi jinsi wanavyomtendea Mungu na haijalishi ni vipi wasivyotii, hakuna chochote kinachojalisha kwa sababu Mungu ni upendo na upendo wa Mungu hauna mipaka na haupimiki. Mungu ana upendo, hivyo Anaweza kuwa mvumilivu kwa watu; Mungu ana upendo, hivyo anaweza kuwa na huruma kwa watu, Mwenye rehema kwa kutokomaa kwao, Mwenye rehema kwa ujinga wao, na Mwenye rehema kwa kutotii kwao. Je, hivi ndivyo ilivyo kweli? Kwa watu wengine, wanapokuwa wamepitia subira ya Mungu mara moja, au mara chache, watashughulikia suala hili kama mtaji katika uelewa wao wenyewe wa Mungu, wakiamini kwamba Mungu atakuwa mvumilivu kwao milele, kuwa na huruma kwao, na katika maisha yao yote watachukua subira ya Mungu na kuiona kama kiwango cha jinsi Mungu anavyowatendea. Pia kuna wale watu ambao, wakati wamepitia uvumilivu wa Mungu mara moja, watamfafanua Mungu milele kama mvumilivu, na uvumilivu huu hauna kikomo, hauna masharti, na hata hauna kanuni kabisa. Je, imani hizi ni sahihi? Kila wakati mambo kuhusu kiini cha Mungu au tabia ya Mungu yanapozungumziwa, mwaonekana mmechanganyikiwa mno. Kuwaona mkiwa hivi kunanifanya Mimi kuwa na wasiwasi. Mmesikia mambo mengi ya ukweli kuhusiana na kiini cha Mungu; mmeweza pia kusikiliza mada nyingi kuhusiana na tabia ya Mungu. Hata hivyo, katika akili zenu masuala haya, na ukweli wa vipengele hivi, ni kumbukumbu tu kulingana na nadharia na maneno yaliyoandikwa. Hakuna kati yenu anayeweza kupitia kile ambacho tabia ya Mungu inamaanisha katika maisha yenu halisi, wala hamwezi kuona tu tabia ya Mungu ni nini. Kwa hivyo, ninyi nyote mmechanganyikiwa katika imani zenu, nyote mnaamini kwa upofu, hadi kwamba mna mtazamo usio na heshima kwa Mungu, na kwamba mnamweka kando. Mtazamo kama huu kwa Mungu unawaongoza wapi? Mnaongozwa katika hali ya kutoa hitimisho siku zote kuhusu Mungu. Mara tu unapopata maarifa kidogo, unahisi kutosheka sana, unahisi kama umempata Mungu katika ukamilifu Wake. Baadaye unahitimisha kwamba hivi ndivyo Mungu Alivyo, na humruhusu kuendelea mbele na shughuli Zake kwa furaha zaidi. Na kila Mungu anapofanya jambo jipya, hukubali kwamba Yeye ni Mungu. Siku moja, wakati Mungu atakaposema: “Simpendi binadamu tena; Sitoi rehema kwa binadamu tena; Sina uvumilivu au subira yoyote kwa binadamu tena; Nimejaa chuki na uhasama kupindukia kwa binadamu,” watu watakinzana na aina hii ya taarifa kutoka ndani ya mioyo yao. Baadhi yao wataweza hata kusema: “Wewe si Mungu wangu tena; Wewe si Mungu ninayetaka kumfuata tena. Kama hivi ndivyo Unavyosema, basi Hustahili tena kuwa Mungu wangu, na sihitaji kuendelea kukufuata Wewe. Kama Hunipi rehema, hunipi upendo, hunipi uvumilivu, basi nami sitakufuata Wewe tena. Kama Utakuwa mvumilivu tu kwangu bila kikomo, utakuwa mwenye subira kwangu, na kuniruhusu mimi kuona kwamba Wewe ni upendo, kwamba Wewe ni subira, kwamba Wewe ni uvumilivu, hapo tu ndipo nitakapoweza kukufuata Wewe, na hapo tu ndipo nitakapoweza kuwa na ujasiri wa kukufuata mpaka mwisho. Kwa sababu ninapata subira na rehema Zako, kutotii kwangu na dhambi zangu zinaweza kusamehewa bila kikomo, kuondolewa bila kikomo, na ninaweza kutenda dhambi wakati wowote na mahali popote, kutubu na kusamehewa wakati wowote na mahali popote, na kukughadhabisha wakati wowote na mahali popote. Hufai kuwa na fikira au hitimisho Zako binafsi kuhusiana na mimi.” Ingawa unaweza usifikirie juu ya swali la aina hii kwa namna hiyo ya ubinafsi na ufahamu, wakati wowote unapomchukulia Mungu kama chombo cha kupata kusamehe dhambi zako na kitu cha kutumika kupata hatima nzuri, tayari umemweka Mungu aliye hai katika hali ya kukupinga wewe, kuwa adui yako. Hivi ndivyo Ninavyoona. Unaweza kuendelea kusema, “Ninaamini katika Mungu”; “Ninafuatilia ukweli”; “Ninataka kubadilisha tabia yangu”; “Nataka kujitenga na ushawishi wa giza”; “Nataka kumridhisha Mungu”; “Nataka kumtii Mungu”; “Nataka kuwa mwaminifu kwa Mungu, na kufanya wajibu wangu vyema”; na kadhalika. Hata hivyo; haijalishi chochote unachosema kinasikika jinsi gani, haijalishi ni nadharia kiasi gani unajua, haijalishi nadharia hiyo ni ya nguvu kiasi gani, ni ya heshima kiasi gani, ukweli wa mambo ni kwamba sasa kuna wengi wenu ambao tayari mmejifunza jinsi ya kutumia kanuni, mafundisho, nadharia ambayo mmeifahamu ili kuhitimisha mambo kuhusu Mungu, na kujiweka katika upinzani kamili kwa njia ya asili kabisa. Ingawa umejifunza barua na kujifunza falsafa, bado hujaingia kwa hakika katika uhalisia wa ukweli, kwa hivyo, ni vigumu sana kwako kuwa karibu na Mungu, kumjua Mungu, na kumwelewa Mungu. Hali hii inasikitisha!

Niliiona tukio hili kwenye video: Akina dada wachache walikuwa wameshikilia kitabu cha Neno Laonekana katika Mwili, na walikuwa wamekishikilia juu sana. Walikuwa wamekishikilia kitabu hiki kikiwa katikati yao, na juu zaidi kuliko vichwa vyao. Ingawa hii ni picha tu, kile kilichoamshwa ndani Yangu si picha. Badala yake, hiyo picha ilinifanya kufikiria kwamba kile ambacho kila mtu hushikilia juu angani kwenye mioyo yao si neno la Mungu, lakini ni kitabu cha neno la Mungu. Hili ni suala la kusikitisha sana. Njia hii ya kufanya mambo si njia ya kweli ya kumshikilia Mungu kwa heshima. Ni kwa sababu hammwelewi Mungu kiasi cha kwamba swali la wazi, swali dogo sana, linawafanya kuja na mawazo yenu binafsi. Wakati Ninapowauliza maswali, wakati Ninapomakinika na ninyi, mnajibu kwa kubahatisha na kwa kutumia mawazo yenu wenyewe; baadhi yenu hata mnakua na sauti ya mashaka na mnauliza tena swali hilo Kwangu. Hii inathibitisha hata waziwazi Kwangu, kwamba huyo Mungu mnayemsadiki si Mungu wa kweli. Baada ya kusoma neno la Mungu kwa miaka mingi, mnatumia neno la Mungu, mnatumia kazi ya Mungu, na mafundisho zaidi kufanya hitimisho kuhusu Mungu kwa mara nyingine tena. Zaidi ya hayo, hamjawahi kujaribu kumwelewa Mungu; hamjawahi kujaribu kujua nia za Mungu; hamjaribu kuelewa mtazamo wa Mungu kwa mwanadamu ni upi; au jinsi Mungu anavyofikiri, kwa nini Ana huzuni, kwa nini Ana ghadhabu, kwa nini Anawadharau watu, na maswali mengine kama hayo. Na kwa kuongezea hayo, watu wengi zaidi wanasadiki kwamba Mungu siku zote amekuwa kimya kwa sababu Anaangalia tu vitendo vya wanadamu, kwa sababu Hana mtazamo wowote kwao, wala Hana Hana mawazo Yke Mwenyewe. Kundi jingine linasukumiza mbali zaidi suala hili. Watu hawa wanaamini kwamba Mungu hatamki neno kwa sababu Amekubali, Mungu hatamki neno kwa sababu Anasubiria, Mungu hatamki neno kwa sababu Hana mtazamo, kwa sababu mtazamo wa Mungu tayari umefafanuliwa kwa kina ndani ya vitabu, tayari umeelezewa kwa ukamilifu wake kwa wanadamu, na hauhitajiki kurudiwa kwa watu mara kwa mara. Ingawa Mungu yuko kimya, bado Ana mwelekeo, ana mtazamo, na anacho kiwango ambacho Anahitaji kutoka kwa watu. Ingawa watu hawajaribu kumwelewa Yeye, na hawajaribu kumtafuta Yeye, mwelekeo Wake uko wazi sana. Fikiria mtu ambaye aliwahi kumfuata Mungu kwa shauku, lakini wakati fulani akaacha kumfuata Yeye na akaondoka. Mtu huyu akitaka kurudi sasa, jambo la kushangaza ni kwamba, hamjui mtazamo wa Mungu utakuwa ni upi, na mwelekeo wa Mungu utakuwa ni upi. Hili si jambo ovyo? Kwa hakika, hili ni suala ambalo kwa kiasi fulani ni la juujuu. Kama kweli mngeelewa moyo wa Mungu, mngejua mtazamo Wake kwa mtu wa aina hii, na msingelitoa jibu la juujuu. Kwa sababu hamjui, mniruhusu Niwafafanulia pale msipoelewa.

Mtazamo wa Mungu kwa Wale Wanaotoroka Wakati Kazi Yake Inaendelea

Kuna watu kama hawa kila mahali: Baada ya kuwa na uhakika kuhusu njia ya Mungu, kwa sababu mbalimbali, wanaondoka kimyakimya bila kuaga, kwenda na kufanya chochote kile ambacho mioyo yao inatamani. Kwa wakati huu, hatutaangalia kwa nini mtu huyu anaondoka. Kwanza tutaangalia mtazamo wa Mungu ni upi kwa mtu wa aina hii. Iko wazi sana! Kuanzia wakati ambao mtu huyu anaondoka, machoni pa Mungu, muda wa imani yao umekwisha. Sio mtu huyu aliyemaliza, lakini ni Mungu. Kwamba mtu huyu alimwacha Mungu inamaanisha kwamba tayari amemkataa Mungu, kwamba tayari hamtaki Mungu. Inamaanisha kwamba tayari hakubali wokovu wa Mungu. Kwa sababu mtu huyu hamtaki Mungu, Mungu naye anaweza bado kumtaka? Zaidi ya hayo, wakati mtu huyu ana mwelekeo huu, mtazamo huu, na kuazimia kumwacha Mungu, tayari ameikera tabia ya Mungu. Hata ingawa hawakupandwa na hasira na wakamlaani Mungu, hata ingawa hawakujihusisha na tabia yoyote mbaya au ya kupita kiasi, na hata ingawa mtu huyu anafikiria: Kama kutawahi kuwepo na siku nitakapokuwa nimeshiba anasa zangu kwa nje, au nitakapokuwa bado nahitaji kitu kutoka kwa Mungu, nitarudi. Au kama Mungu ataniita, nitarudi. Au wanasema: Kama nitajeruhiwa kwa nje, nikiuona ulimwengu wa nje una giza sana na una maovu sana na sitaki tena kujishirikisha nao, nitarudi kwa Mungu. Hata ingawa mtu huyu amepiga hesabu katika akili zake ni wakati gani anarudi, hata ingawa wanauacha mlango ukiwa wazi wa kurudi kwao, hawatambui kwamba bila kujali ni namna gani wanavyofikiria na ni jinsi gani wanavyopanga, hii ni ndoto tu. Kosa lao kubwa zaidi ni kutokuwa wazi kuhusu namna ambavyo Mungu anahisi wakati wanapotaka kuondoka. Kuanzia muda huo ambao mtu huyu anaamua kumwacha Mungu, Mungu amemwacha kabisa; tayari Mungu ameamua matokeo yao katika moyo Wake. Matokeo hayo ni yapi? Ni kwamba mtu huyu atakuwa mmoja wa panya, na ataangamia pamoja nao. Hivyo basi, watu mara nyingi huona aina hii ya hali: Mtu anamwacha Mungu, lakini hapokei adhabu yoyote. Mungu hufanya kazi kulingana na kanuni Zake binafsi. Watu wanaweza kuona baadhi ya mambo, na baadhi ya mambo yanahitimishwa tu katika moyo wa Mungu, kwa hivyo watu hawawezi kuyaona matokeo. Kile ambacho watu wanaona si lazima kiwe ndio upande wa ukweli wa mambo; lakini upande ule mwingine, ule upande usiouona—haya ndiyo mawazo ya kweli na hitimisho la moyo wa Mungu.

Watu Wanaotoroka Wakati wa Kazi ya Mungu ni Wale Wanaoiacha Njia ya Kweli

Kwa nini Mungu anawapa watu wanaomkimbia wakati wa kazi Yake adhabu kali namna hii? Kwa nini Mungu anakuwa na hasira kali kwao? Kwanza kabisa tunajua kwamba tabia ya Mungu ni ukuu, ni ghadhabu. Yeye si kondoowa kuchinjwa na yeyote; na hata zaidi Yeye si kikaragosiwa kudhibitiwa na watu watakavyo. Yeye pia si hewa tupu ya kuamrishwa huku na kule na watu. Kama kweli unasadiki kwamba Mungu yupo, unapaswa kuwa na moyo unaomcha Mungu, na unapaswa kujua kwamba kiini cha Mungu hakipaswi kughadhabishwa. Ghadhabu hii inaweza kusababishwa na neno; pengine fikira; pengine aina fulani ya tabia mbaya; pengine tabia ya upole, tabia inayoweza kuruhusiwa machoni pake na maadili ya mwanadamu; au pengine inasababishwa na mafundisho, aunadharia. Hata hivyo, punde unapomghadhabisha Mungu, fursa yako inapotea na siku zako za mwisho zinakuwa zimewasili. Hili ni jambo baya sana! Kama huelewi kwamba Mungu hawezi kukosewa, basi pengine humchi Mungu, na pengine unamkosea Yeye kila wakati. Kama hujui jinsi ya kumcha Mungu, basi huwezi kumcha Mungu, na hutaweza kujua namna ya kujiweka kwenye njia ya kutembea katika njia ya Mungu—kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Punde unapofahamu, unaweza kuwa na ufahamu kwamba Mungu hawezi kukosewa, kisha utajua ni nini maana ya kumcha Mungu na kujiepusha na maovu.

Kutembea katika njia ya kumcha Mungu na kujiepusha na maovu si lazima iwe kuhusu ukweli mwingi unaoujua, ni majaribu mangapi ambayo umepitia, au ni kiasi gani umeadhibiwa. Badala yake, kunategemea aina ya mtazamo ulio nao kwa Mungu moyoni mwako, na kiini unachokionyesha. Kiini halisi cha watu na mitazamo yao wenyewe—mambo haya ni muhimu sana, ni muhimu kabisa. Kuhusiana na wale watu ambao wamemkana na kumwacha Mungu, mtazamo wao wa dharau kwa Mungu na mioyo yao inayodharau ukweli ilikera tabia ya Mungu, hivyo basi kulingana na Mungu hawatawahi kusamehewa. Wamejua kuhusu uwepo wa Mungu, wamekuwa na taarifa kwamba Mungu tayari amewasili, wameweza hata kupitia kazi mpya ya Mungu. Kuondoka kwao si kutokana na kudanganywa, wala si suala kwamba wao wamechanganyikiwa kulihusu. Hata zaidi ni suala la wao kulazimishwa kuondoka. Lakini kwa nadhari yao, na kwa akili iliyo wazi, wamechagua kumwacha Mungu. Kuondoka kwao si kupotea njia; si hata kutupwa kwao nje. Kwa hiyo, machoni pa Mungu, wao si mwana-kondoo aliyepotea kutoka katika kundi, sembuse mwana mpotevu aliyepotea njia. Waliondoka bila hofu ya kuadhibiwa, na hali kama hiyo, mfano kama huo unaikera tabia ya Mungu na ni kutokana na kero hii ambapo Yeye anawapa matokeo yasiyo na matumaini. Je, aina hii ya matokeo si ya kutisha? Kwa hivyo, kama watu hawamjui Mungu, wanaweza kumkosea Mungu. Hilo si suala dogo! Kama mtu hatachukulia mtazamo wa Mungu kwa umakinifu, na bado anasadiki kwamba Mungu angali anatarajia kurudi kwake—kwa sababu wao ni mojawapo wa kondoo wa Mungu waliopotea na kwamba Mungu angali anawasubiria kubadilisha mioyo yao—basi hawako mbali na siku zao za adhabu. Mungu hatakataa tu kumkubali—ikizingatiwa kwamba hii ni mara yake ya pili ya kuikera tabia ya Mungu; hivyo basi suala hili ni baya zaidi! Mtazamo wa mtu huyu usioheshimu vitu vitakatifu tayari umekosea agizo la kiutawala la Mungu. Je, bado Mungu atawakaribisha? Katika moyo Wake, kanuni za Mungu kuhusiana na suala hili ni kwamba mtu fulani amepata uhakika kuhusu ni ipi ndiyo njia ya kweli, lakini bado ameweza kwa kufahamu na kwa akili ya wazi kumkataa Mungu, na kuondoka kutoka kwa Mungu, basi Mungu atazuia kabisa barabara iendayo katika wokovu wake, na hata lango la kuingia kwenye ufalme watafungiwa. Wakati mtu huyu atakapokuja kubisha kwa mara nyingine, Mungu hatamfungulia lango. Mtu huyu atafungiwa milele. Labda baadhi yenu mmeisoma hadithi ya Musa katika Biblia. Baada ya Musa kupakwa mafuta na Mungu, viongozi 250 walionyesha kutomtii Musa kwa sababu ya matendo yake na kwa sababu nyinginezo mbalimbali. Walikataa kumtii nani? Haikuwa Musa. Walikataa kutii mipango ya Mungu; walikataa kutii kazi ya Mungu katika suala hili. Walisema yafuatayo: “Ninyi mnachukua mengi kwenu, kwa sababu mkusanyiko wote ni mtakatifu, kila mmoja wao, naye Yehova yuko miongoni mwao….” Katika macho yenu, maneno haya ni mazito? Si mazito! Angalau maana ya juu juu ya maneno haya sio mbaya. Katika mkondo wa kisheria, hawavunji sheria zozote, kwa juujuu kabisa si lugha katili, au msamiati, isitoshe, hayana maana yoyote ya kukufuru. Sentensi ya kawaida ndiyo iliyoko hapo, hamna cha ziada. Ilhali inakuwaje kwamba maneno haya yanaweza kuanzisha hasira kali kama hiyo kutoka kwa Mungu? Ni kwa sababu hayasemwi kwa watu, bali kwa Mungu. Mtazamo na tabia inayoonyeshwa na wao ndicho hasa kinachoikera tabia ya Mungu, na wao wanaikosea tabia ya Mungu ambayo haipaswi kukosewa. Sote tunajua matokeo yao hatimaye yalikuwa ni yapi. Kuhusiana na wale waliomwacha Mungu, mtazamo wao ni upi? Mwelekeo wao ni upi? Na ni kwa nini mtazamo na mwelekeo wao unasababisha Mungu kuwashughulikia kwa njia hiyo? Sababu ni kwamba wanajua waziwazi Yeye ni Mungu ilhali bado wanachagua kumsaliti Yeye. Na ndiyo maana wanaondolewa kabisa fursa yao ya wokovu. Kama vile Biblia inavyosema: “Kwa sababu tukitenda dhambi makusudi baada ya sisi kupokea maarifa ya ukweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi” (Waebrania 10:26). Je, mmelielewa suala hili sasa?

Hatima ya Mwanadamu Huamuliwa na Mtazamo Wake Kwa Mungu

Mungu ni Mungu aliye hai, na kama vile watu hutenda tofauti katika hali tofauti, mtazamo wa Mungu kuelekea maonyesho haya hutofautiana kwa sababu Yeye si kikaragosi, wala Yeye si hewa tupu. Kupata kuujua mtazamo wa Mungu ni jambo lenye thamani kwa wanadamu. Watu wanapaswa kujifunza jinsi, kwa kuujua mtazamo wa Mungu, wanaweza kujua tabia ya Mungu na kuuelewa moyo Wake kidogo kidogo. Wakati unapokuja kuuelewa moyo wa Mungu kidogo kidogo, hutahisi kwamba kumcha Mungu na kuepuka maovu ni jambo gumu kutimiza. Kilicho zaidi ni kwamba, unapomwelewa Mungu, hakuna uwezekano wa wewe kufanya hitimisho kuhusu Yeye. Unapoacha kufanya hitimisho kuhusu Mungu, hakuna uwezekano wa wewe kumkosea Yeye, na bila kujua Mungu atakuongoza kuwa na maarifa Yake, na hivyo basi utamcha Mungu katika moyo wako. Utaacha kumfafanua Mungu kwa kutumia mafundisho, zile barua, na nadharia ambazo umejifunza. Badala yake, kwa kutafuta nia za Mungu katika mambo yote na siku zote utaweza bila kufahamu kuwa mtu anayefuata moyo wa Mungu.

Kazi ya Mungu haionekani na haiwezi kuguswa na wanadamu, lakini kwa jinsi Mungu anavyohusika, matendo ya kila mtu, pamoja na mtazamo wao Kwake—haya hayatambuliki tu na Mungu, lakini yanaonekana pia. Hili ni jambo ambalo kila mmoja anafaa kutambua na kuwa wazi kulihusu. Unaweza kuwa ukijiuliza siku zote: “Je, Mungu anajua kile ninachofanya hapa? Je, Mungu anajua kile ninachofikiria sasa hivi? Pengine Anajua, pengine Hajui.” Kama utakuwa na mtazamo wa aina hii, kumfuata na kumwamini Mungu ilhali unatilia shaka kazi Yake na uwepo Wake, basi hivi karibuni au baadaye siku itawadia ambapo utamghadhabisha, kwa sababu tayari unaelea kwenye ukingo wa mteremko wa hatari. Nimeona watu ambao wamemwamini Mungu kwa miaka mingi, lakini bado hawajapata uhalisi wa ukweli, wala hata hawaelewi mapenzi ya Mungu. Maisha yao na kimo chao havipigi hatua yoyote, wakishikilia tu mafundisho duni kabisa. Hii ni kwa sababu watu hawa hawajawahi kuchukulia neno la Mungu kama maisha yao binafsi, na hawajawahi kukabiliana na kukubali uwepo Wake. Je, unafikiri kwamba Mungu anapowaona watu kama hao, Anajawa na furaha? Je, wanamfariji Yeye? Katika hali hiyo, ni njia ya imani ya watu kwa Mungu ambayo huamua hatima yao. Kuhusu jinsi watu wanavyomwamini Mungu ndivyo inavyoamua hatima yao. Kuhusu jinsi watu wanavyotafuta na jinsi watu wanavyomkaribia Mungu, mitazamo ya watu ni ya muhimu sana. Usimpuuze Mungu kama vile Yeye ni rundo la hewa tupu linalozunguka nyuma ya kichwa chako. Daima mfikirie Mungu wa imani yako kama Mungu aliye hai, Mungu halisi. Yeye hayupo kule juu kwenye mbingu ya tatu bila chochote cha kufanya. Badala yake, Yeye hutazama kila mara ndani ya moyo wa kila mtu, Akiangalia kile unachotaka kufanya, katika kila neno dogo na kila tendo dogo, Akiangalia jinsi unavyotenda na mtazamo wako kwa Mungu ni upi. Iwe uko radhi kujitolea kwa Mungu au la, tabia yako yote na fikira zako na mawazo yako ya ndani zaidi yako mbele za Mungu, na yanaangaliwa na Yeye. Ni kulingana na tabia yako, kulingana na vitendo vyako, na kulingana na mwelekeo wako kwa Mungu, ambapo maoni Yake kwako, na mwenendo Wake kwako, vinaendelea kubadilika. Mimi Ningependa kutoa ushauri fulani kwa baadhi ya watu. Msijiweke kwenye mikono ya Mungu kama watoto wachanga, kana kwamba Yeye Anapaswa kukupenda sana, kana kwamba Hawezi kamwe kukuacha, na kana kwamba mwelekeo Wake kwako ni imara na usingeweza kubadilika, na Ninawashauri muache kuota ndoto! Mungu ni mwenye haki katika kumtendea kila mtu, na Yeye ni mwaminifu katika mtazamo Wake kwa kazi ya kuwashinda na kuwaokoa watu. Huu ndio usimamizi Wake. Anamtendea kila mmoja kwa umakinifu, na wala si kama kiumbe cha kufugwa cha kucheza nacho. Upendo wa Mungu kwa binadamu si ule wa kudekeza au kupotosha; rehema na uvumilivu Wake kwa wanadamu si wa kuendekeza au kutojali. Kinyume cha mambo, upendo wa Mungu kwa wanadamu ni wa kutunza, kuhurumia, na kuheshimu maisha; rehema na uvumilivu Wake vyote vinaonyesha matarajio Yake kwa binadamu; rehema na uvumilivu Wake ndivyo ambavyo binadamu anahitaji ili kuishi. Mungu yuko hai, na kwa hakika Mungu yupo; Mtazamo Wake kwa wanadamu ni wa kanuni, sio sheria ya kiitikadi hata kidogo, na unaweza kubadilika. Mapenzi Yake kwa ubinadamu yanabadilika polepole na kurekebishwa kulingana na wakati, na hali, na mtazamo wa kila mtu. Kwa hiyo, unapaswa kujua ndani ya moyo wako kwa uwazi kabisa kwamba kiini cha Mungu hakibadiliki, na kwamba tabia Yake itajidhihirisha kwa nyakati tofauti na katika mazingira tofauti. Huenda usifikirie kwamba hili si suala zito, na unatumia mawazo yako binafsi kufikiria jinsi Mungu anapaswa kufanya mambo. Lakini kuna nyakati ambapo kinyume kabisa cha mtazamo wako ni kweli, na kwamba kwa kutumia mawazo yako binafsi katika kumjaribu na kumpima Mungu, tayari umemghadhabisha. Hii ni kwa sababu Mungu hafanyi kazi kama unavyofikiria wewe, Naye Mungu hatalishughulikia suala hili kama vile unavyosema Atalishughulikia. Kwa hivyo, Ninakukumbusha uwe makini na mwenye hekima katika mtazamo wako kwa kila kitu, na ujifunze namna ya kufuata kanuni ya kutembea kwenye njia ya Mungu katika mambo yote—kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Lazima uimarishe uelewa thabiti katika masuala ya mapenzi ya Mungu na mtazamo wa Mungu; lazima utafute watu walio na nuru ili wakujulishe mambo haya, na ni lazima utafute kwa bidii. Usimwone Mungu wa imani yako kama kikaragosi—ukimhukumu upendavyo, ukifanya hitimisho kiholela kuhusu Yeye, na kumtendea kwa mtazamo usio na heshima. Katika mchakato wa wokovu wa Mungu, Anapoamua matokeo yako, bila kujali kama Yeye atakupa rehema, au uvumilivu, au hukumu na kuadibu, kwa vyovyote vile, mtazamo Wake kwako unabadilika. Inategemea mtazamo wako kwa Mungu, na uelewa wako kuhusu Mungu. Usiruhusu kipengele kimoja cha kupita cha maarifa yako au uelewa wako katika Mungu kumfafanua Yeye milele. Usiamini katika Mungu aliyekufa; amini katika Aliye hai. Kumbuka hili! Ingawa Nimezungumza ukweli fulani hapa, ukweli mliohitaji kusikia, kwa kuzingatia hali yenu ya sasa na kimo chenu cha sasa, Sitatoa madai yoyote makubwa zaidi ili Nisipunguze shauku yenu. Kufanya hivyo kunaweza kuijaza mioyo yenu na huzuni na simanzi, na kuwafanya mhisi kuvunjika moyo sana kumwelekea Mungu. Badala yake Natumai kwamba mnaweza kutumia upendo wa Mungu katika mioyo yenu, na kutumia mtazamo ambao ni wa heshima kwa Mungu wakati mnapotembea katika njia iliyo mbele. Usichukulie imani katika Mungu kwa njia iliyochanganyikiwa, lakini ichukulie kama jambo muhimu zaidi, iweke moyoni, iweke katika vitendo na iunganishe na maisha halisi, na usizungumze tu maneno matupu. Kwani hili ni suala la uzima na mauti, na ndilo ambalo litaamua hatima yako. Usilichukulie kama mzaha, kama mchezo wa mtoto! Baada ya kuwaambia maneno haya leo, Najiuliza ni uelewa wa kiwango gani ambao akili yako imeweza kupata. Je, kuna maswali yoyote ambayo ungependa kuuliza kuhusu kile Nilichokisema leo?

Ingawa mada hizi ni mpya kidogo, na zimeondolewa kidogo kutoka kwenye mitazamo yenu na kile ambacho kwa kawaida mnafuatilia na kutilia maanani, Nafikiria kwamba baada ya mada hizi kuwasilishwa kwa kipindi cha muda, mtaimarisha uelewa mzuri wa kila kitu Nilichosema hapa. Kwa sababu hizi ni mada mpya, mada ambazo hujawahi kuzifikiria hapo awali, Ninatumai kwamba hazitaongezea mzigo kwako. Ninaongea maneno haya leo si kwa sababu ya kuwatishia nyinyi, wala Sijaribu kukushughulikia wewe; badala yake, nia Yangu ni kukusaidia kuelewa ukweli halisi kuhusu ukweli. Kwa vyovyote vile, kunao umbali kati ya wanadamu na Mungu. Ingawa binadamu anaamini katika Mungu, hajawahi kumwelewa Mungu; hajawahi kujua mitazamo ya Mungu.Mwanadamu pia hajawahi kuwa na shauku katika kujali kwake mtazamo wa Mungu. Badala yake, ameamini kwa upofu, ameendelea kwa upofu, na amekuwa mzembe katika maarifa na uelewa wake wa Mungu. Kwa hivyo Ninahisi kulazimishwa kuwafafanulia masuala haya, na kuwasaidia kuelewa ni Mungu wa aina gani huyu mnayemwamini; kile Anachofikiri; mtazamo Wake ulivyo katika kuwatendea watu wa aina mbalimbali; uko mbali kiasi gani na kutimiza matakwa Yake; na tofauti kati ya matendo yako na kiwango Anachohitaji Yeye. Lengo la kuwajulisha juu ya mambo haya, ni ili kuwapa kigezo cha kujipimia kwenye mioyo yenu, na ili ujue ni aina gani ya mavuno ambayo njia unayoitembea inasababisha, kile ambacho hamjapata kwenye njia hii, na ni katika maeneo gani bado hamjajihusisha. Mnaposhiriki ninyi wenyewe, kwa kawaida mnazungumza juu ya mada chache zinazojadiliwa mara kwa mara, ambazo zina upeo finyu, na maudhui ni ya juujuu sana. Kuna umbali, pengo, kati ya kile ambacho mnazungumzia na nia za Mungu, katikati ya mazungumzo yenu na upana na kiwango cha mahitaji ya Mungu. Kuendelea hivi baada ya muda kutawafanya kupotoka zaidi na zaidi kutoka kwenye njia ya Mungu. Mnayachukua tu maneno yaliyopo kutoka kwa Mungu na kuyageuza kuwa vitu vya kuabudu, kuwa kaida za dini na kanuni. Hayo tu ndiyo maana yake! Kwa hakika, Mungu hana nafasi kamwe katika mioyo yenu, na Mungu hajawahi kuipata mioyo yenu. Baadhi ya watu hufikiria kwamba kumjua Mungu ni vigumu sana—huu ndio ukweli. Ni vigumu! Kama watu wataambiwa kutekeleza wajibu wao na kuhakikisha kwamba mambo yanatendeka kwa nje, kama wataulizwa kutia bidii, basi watu watafikiria kwamba kumwamini Mungu ni jambo rahisi sana, kwa sababu haya yote yanapatikana katika ule upana wa uwezo wa binadamu. Ilhali punde tu mada hizo zinaposonga kuelekea kwenye maeneo ya nia za Mungu na mtazamo wa Mungu kwa binadamu, basi mambo yanapata kuwa magumu zaidi kwa watu wote. Hiyo ni kwa sababu yote haya yanahusisha uelewa wa ukweli na kuingia kwao katika uhalisia; bila shaka kuna kiwango cha ugumu. Lakini baada ya wewe kuingia kupitia mlango wa kwanza, baada ya wewe kuanza kuingia ndani yake, mambo yataanza kuwa mepesi polepole.

Mahali pa Kuanzia Kumcha Mungu ni Kumchukulia Yeye kama Mungu

Mtu fulani ameuliza swali muda mfupi uliopita: Inakuwaje kwamba, ingawa tunamjua Mungu zaidi ya Ayubu, lakini bado hatuwezi kumcha Mungu? Tuliligusia kidogo suala hili hapo awali, sivyo? Kwa hakika, kiini halisi cha swali hili kimeweza pia kuzungumziwa awali kwamba ingawa Ayubu hakumjua Mungu kwa wakati huo, alimchukulia Yeye kama Mungu, na kumchukulia kama Bwana wa vitu vyote mbinguni na duniani. Ayubu hakumchukulia Mungu kuwa adui. Badala yake, alimwabudu Yeye kama Muumba wa vitu vyote. Watu siku hizi wanampinga Mungu sana kwa nini? Kwa nini hawawezi kumcha Mungu? Sababu moja ni kwamba wamepotoshwa sana na Shetani. Wakiwa na asili hiyo ya kishetani iliyokita mizizi ndani, watu wanageuka na kuwa adui wa Mungu. Hivyo basi, hata ingawa wanasadiki katika Mungu na kumtambua Mungu, bado wanaweza kumpinga Mungu na kujiweka katika nafasi ya upinzani na Yeye. Hili linaamuliwa na asili ya binadamu. Sababu nyingine ni kwamba ingawa watu wanamwamini Mungu, hawamchukulii Yeye kama Mungu. Badala yake, wanamchukulia Mungu kuwa ndiye anayempinga binadamu, wakimwona Yeye kuwa adui wa binadamu, na hawawezi kupatanishwa na Mungu. Ni rahisi hivyo. Je, jambo hili halikuzungumziwa kwenye kikao cha awali? Hebu fikiria: Je, hiyo ndio sababu? Ingawa unaweza kuwa na maarifa kidogo ya Mungu, lakini maarifa haya yanahusisha nini? Je, hayo siyo yale ambayo kila mtu anazungumzia juu yake? Je, hayo si yale ambayo Mungu alikuambia? Unajua tu vipengele vya kinadharia na mafundisho; je umewahi kupitia kipengele halisi cha Mungu? Je, unayo maarifa ya kibinafsi? Je, unayo maarifa na uzoefu wa vitendo? Kama Mungu asingekuambia, ungelijua hili? Maarifa yako ya nadharia hayawakilishi maarifa halisi. Kwa ufupi, bila kujali ni kiwango kipi unachojua na ni vipi ulivyokijua hatimaye, kabla ya wewe kufikia uelewa halisi wa Mungu, Mungu ni adui yako, na mpaka utakapoanza kumchukulia Mungu kama Mungu, Amewekwa kuwa mpinzani wako, kwani wewe ni mfano halisi wa Shetani.

Unapokuwa pamoja na Kristo, labda unaweza kumhudumia milo mitatu kwa siku, labda kumhudumia Yeye chai, kuhudumia mahitaji Yake ya maisha, ni kana kwamba unamchukulia Kristo kama Mungu. Kila wakati jambo linapofanyika, mitazamo ya watu siku zote inakuwa kinyume cha mtazamo wa Mungu. Siku zote wanashindwa kuelewa mtazamo wa Mungu, na wanashindwa kuukubali. Ingawa watu wanaweza kupatana na Mungu kwa juujuu, hii haimaanishi kwamba wanalingana na Yeye. Mara tu jambo linapotokea, ukweli wa kutotii kwa mwanadamu hujitokeza, kuthibitisha uhasama uliopo kati ya mwanadamu na Mungu. Uhasama huu sio Mungu anayempinga mwanadamu; sio Mungu kutaka kuwa na uadui kwa mwanadamu, na sio Mungu kumweka mwanadamu katika upinzani na kumtendea mwanadamu hivyo. Badala yake, ni suala la kiini hiki cha upinzani dhidi ya Mungu kinachonyemelea katika utashi wa mwanadamu, na katika akili ya kutofahamu ya mwanadamu. Kwa sababu binadamu anachukulia kila kitu kinachotoka kwa Mungu kama kitu cha utafiti wake, mwitikio wake kwa hiki ambacho kinatoka kwa Mungu na kile ambacho kinamhusisha Mungu ni, zaidi ya yote, kukisia, na kushuku, na kisha kuchukua kwa haraka sana mtazamo ambao unakinzana na Mungu, na unapingana na Mungu. Baada ya hapo, binadamu atachukua hali hizi za moyo za kimyakimya na kuzua mjadala na Mungu au kushindana na Mungu hadi kufikia kiwango ambacho atatia shaka kama Mungu wa aina hii anastahili kufuatwa. Licha ya ukweli kwamba urazini wa binadamu unamwambia asiendelee hivi, bado atachagua kufanya hivyo licha ya kutotaka kufanya hivyo, kiasi kwamba ataendelea bila kusita hadi mwisho. Kwa mfano, ni nini mwitikio wa kwanza kwa baadhi ya watu wanaposikia uvumi fulani au kashfa fulani kumhusu Mungu? Mwitikio wa kwanza ni: Sijui kama uvumi huu ni kweli au la, kama upo ama haupo, hivyo basi nitasubiri na kuona. Kisha wanaanza kutafakari: Hakuna njia ya kuthibitisha haya; je, hilo lilifanyika kweli? Je, uvumi huu ni wa kweli au la? Ingawa mtu huyu haonyeshi kwa juujuu, mioyo yao tayari imeanza kuwa na shaka, tayari imeanza kumkana Mungu. Ni nini kiini cha aina hii ya mwelekeo, aina hii ya mtazamo? Je, si usaliti? Kabla ya wao kukumbwa na suala, huwezi kuona mtazamo wa mtu huyu ni nini—inaonekana ni kana kwamba wao hawakinzani na Mungu, ni kama hawamchukulii Mungu kuwa adui. Hata hivyo, punde wanapokumbwa na suala hilo, wanasimama mara moja na Shetani na kumpinga Mungu. Hali hii inapendekeza nini? Inapendekeza kwamba binadamu na Mungu wanapingana! Si kwamba Mungu anamchukulia binadamu kama adui, lakini kwamba kile kiini chenyewe cha binadamu kina uadui kwa Mungu. Haijalishi ni kwa muda mrefu kiasi gani ambapo mtu amemfuata Mungu, au ni kiwango kipi anacholipa; bila kujali jinsi mtu anavyomsifu Mungu, jinsi wanavyojizuia kumpinga Mungu, hata kujihimiza kumpenda Mungu, hawawezi kamwe kumchukulia Mungu kama Mungu. Je, hii si inaamuliwa na kiini halisi cha mwanadamu? Ikiwa unamchukulia Yeye kama Mungu, na kuamini kwa kweli kwamba Yeye ni Mungu, je, bado unaweza kuwa na mashaka yoyote Kwake? Je, bado kunaweza kuwa na alama zozote za maswali kuhusu Yeye katika moyo wako? Hakuwezi. Mitindo ya ulimwengu huu ni miovu kweli, na wanadamu wa kizazi hiki pia, hivyo, inawezekanaje kwamba huna fikira zozote kuzihusu? Wewe mwenyewe umejaa uovu, hivyo inakuwaje kwamba huna fikira zozote kuhusu hayo? Na bado, uvumi kidogo tu, kashfa fulani zinaweza kusababisha dhana kubwa mno kumhusu Mungu, zinaweza kuleta mawazo mengi mno, hali inayoonyesha vile ambavyo kimo chako kilivyo bado kichanga! “Mnong’ono” tu wa mbu wachache, nzi wachache wabaya, hilo tu ndilo linalokupotosha? Huyu ni mtu wa aina gani? Je, unajua anachofikiria Mungu kuhusu mtu wa aina hii? Mtazamo wa Mungu kwa hakika uko wazi sana kuhusiana na jinsi Anavyowatendea watu kama hawa. Ni kwamba tu Mungu anavyowatendea watu hawa ni kuwapuuza—mtazamo Wake ni kutowatilia maanani, na kutomakinikia watu hawa wajinga. Kwa nini ni hivyo? Ni kwa sababu katika moyo Wake Hakuwahi kupangilia kuhusu kupata watu kama hao ambao wameahidi kuwa na uadui Kwake hadi mwisho kabisa, na ambao hawajawahi kamwe kupanga kutafuta njia ya kupatana na Yeye. Pengine maneno haya Niliyoyaongea yamewaumiza watu wachache. Kwa kweli, mko radhi kuniruhusu Mimi niwaumize siku zote namna hii? Bila kujali kama mko radhi au la, kila kitu Ninachosema ni ukweli! Kama siku zote Ninawaumiza namna hii, siku zote Nafichua makovu yenu, je, itaathirisura ya juu ya Mungu mioyoni mwenu? (Haitaathiri.) Ninakubali kwamba haitaathiri kwani kwa ufupi hakuna Mungu katika mioyo yenu. Yule Mungu wa juu anayepatikana ndani ya mioyo yenu, yule mnayemtetea kwa dhati na kumlinda, kwa ufupi si Mungu. Badala yake ni mfano wa mawazo ya mwanadamu; kwa ufupi hayupo. Kwa hivyo, ni bora zaidi kama Nitafichua jibu la kitendawili hiki. Je, huu si ukweli wote? Mungu halisi hatokani na mawazo ya mwanadamu Natumai kwamba nyote mnaweza kukabiliana na uhalisia huu, na utawasaidia katika maarifa yenu ya Mungu.

Wale Watu Wasiotambuliwa na Mungu

Kuna baadhi ya watu ambao imani yao haijawahi kutambuliwa katika moyo wa Mungu. Kwa maneno mengine, Mungu hatambui kwamba watu hawa ni wafuasi Wake, kwa sababu Mungu haisifu imani yao. Kwa watu hawa, haijalishi wamemfuata Mungu kwa miaka mingapi, mawazo na mitazamo yao haijawahi kubadilika. Wao ni kama wasioamini, wanatii kanuni na njia ambayo wasioamini wanafanya mambo yao, kutii sheria zao za kunusurika na imani. Hawajawahi kukubali neno la Mungu kama maisha yao, hawajawahi kuamini kwamba neno la Mungu ni ukweli, hawajawahi kunuia kukubali wokovu wa Mungu, na hawajawahi kumtambua Mungu kama Mungu wao. Wanachukulia kuamini katika Mungu kama aina fulani ya burudani ya kielimu, wakimchukulia Mungu kama riziki ya kiroho tu, kwa hivyo hawafikirii kuwa ipo thamani ya kujaribu na kuelewa tabia ya Mungu, au kiini cha Mungu. Unaweza kusema kwamba kila kitu kinacholingana na Mungu wa kweli hakihusiani kwa vyovyote vile na watu hawa. Hawana hamu yoyote, na hawawezi kusumbuliwa kutilia maanani. Hii ni kwa sababu ndani kabisa ya mioyo yao ipo sauti ya nguvu ambayo siku zote inawaambia: Mungu haonekani na hagusiki, na Mungu hayupo. Wanasadiki kwamba kujaribu kumwelewa Mungu wa aina hii hakutastahili jitihada zao; itakuwa sawa na wao kujidanganya. Wao wanaamini tu kwa kumtambua Mungu kwa maneno tu bila kuchukua msimamo wowote halisi au kujiweka ndani yao kupitia vitendo halisi, wao wanakuwa werevu sana. Je, Mungu anawachukuliaje watu hawa? Anawachukulia kuwa wasioamini. Baadhi ya watu huuliza: “Je, wasioamini wanaweza kulisoma neno la Mungu? Je, wanaweza kutekeleza wajibu wao? Je, wanaweza kuyasema maneno haya: ‘Nitaishi kwa ajili ya Mungu’?” Kile ambacho binadamu wanaona mara nyingi ni maonyesho ya juujuu tu ya watu, na wala si kiini chao halisi. Ilhali Mungu haangalii maonyesho haya ya juujuu; Yeye anaona tu kiini chao halisi cha ndani. Kwa hivyo, hii ndiyo aina ya mtazamo na ufafanuzi ambao Mungu anao, kwa watu kama hawa. Kuhusiana na kile ambacho watu hawa husema: “Kwa nini Mungu hufanya hivi? Kwa nini Mungu hufanya vile? Siwezi kuelewa haya; siwezi kuelewa yale; haya hayaingiliani na mawazo ya mwanadamu; Lazima unielezee haya; …” Katika kujibu hili, Nauliza: Je, ni muhimu kweli kukuelezea mambo haya? Je, mambo haya yana uhusiano wowote na wewe? Je, unafikiri wewe ni nani? Ulitokea wapi? Je, umehitimu kumwelekeza Mungu? Je, unamwamini Yeye? Je, Anatambua imani yako? Kwa sababu imani yako haina chochote kuhusiana na Mungu, matendo Yake yana uhusiano gani na wewe? Hujui pale ulipo katika moyo wa Mungu, kwa hivyo, je, umehitimu kuzungumza na Mungu?

Maneno ya Maonyo

Je, hamhisi vibaya baada ya kusikia matamshi haya? Ingawa huenda msiwe radhi kusikiliza maneno haya, au msiwe radhi kuyakubali, yote ni ukweli. Kwa sababu awamu hii ya kazi ni ya Mungu kutenda, kama hujali nia za Mungu, hujali mtazamo wa Mungu na huelewi kiini halisi na tabia ya Mungu, basi hatimaye wewe ndiwe utakayekosa kufaidi. Msiyalaumu maneno Yangu kwa kuwa magumu kuyasikiliza, na msiyalaumu kwa kufifisha shauku yenu. Mimi naongea ukweli; na wala Sinuii kuwavunja moyo. Haijalishi ni nini Ninachowaomba, na haijalishi jinsi mnavyotakiwa kukifanya, Ninatumai kwamba mtatembea katika njia sahihi, na Ninatumai kwamba mtafuata njia ya Mungu na hamtakengeuka kutoka kwa njia hii. Ikiwa hutaendelea kwa mujibu wa neno la Mungu, na hufuati njia Yake, basi hapawezi kuwa na shaka kwamba unamuasi Mungu na umepotoka kutoka kwenye njia sahihi. Hivyo Ninahisi kuna baadhi ya mambo ambayo ni lazima Niwafafanulie, na kuwafanya muamini bila shaka, kwa uwazi, bila hata chembe ya kutokuwa na uhakika, na kuwasaidia kujua kwa uwazi mtazamo wa Mungu, nia za Mungu, jinsi Mungu humkamilisha mwanadamu, na ni kwa njia gani Anapanga matokeo ya mwanadamu. Endapo kutakuwa na siku ambayo hutaweza kuanza katika njia hii, basi Sitahitajika kuwajibika kwa vyovyote vile kwa sababu maneno haya tayari yamezungumzwa kwako waziwazi. Kuhusu matokeo ya aina mbalimbali za watu Mungu ana mitazamo tofauti. Ana njia Zake mwenyewe za kuwapima, pamoja na kiwango Chake mwenyewe cha mahitaji kwao. Kiwango Chake cha kupima matokeo ya watu ni kile ambacho ni chenye haki kwa kila mmoja—hakuna shaka kuhusu hilo. Hivyo basi, woga wa watu fulani hauhitajiki. Je, umepata tulizo la moyo sasa? Ni hayo kwa leo. Kwaheri!

Oktoba 17, 2013

Iliyotangulia: Dibaji

Inayofuata: Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe I

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp