Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe I
Leo tunashiriki kuhusu mada muhimu. Hii ni mada ambayo imezungumziwa tangu kuanza kwa kazi ya Mungu mpaka sasa, na ina umuhimu mkubwa sana kwa kila mtu. Kwa maneno mengine, hili ni suala ambalo kila mmoja atakutana nalo katika njia ya kumwamini Mungu; ni suala ambalo lazima lizungumziwe. Ni suala muhimu, lisiloepukika ambalo mwanadamu hawezi kujitenganisha nalo. Tukizungumzia umuhimu, ni kitu gani cha muhimu zaidi kwa kila muumini katika Mungu? Baadhi ya watu wanafikiri kwamba kitu cha muhimu zaidi ni kuyaelewa mapenzi ya Mungu; wengine wanaamini kwamba ni muhimu zaidi kula na kunywa maneno ya Mungu; katika njia ya kumwamini Mungu; ni suala ambalo lazima lizungumziwe muhimu zaidi ni kujua namna ya kupata wokovu kupitia kwa Mungu, namna ya kumfuata Mungu, na namna ya kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Tutayaweka masuala haya yote pembeni kwa leo. Hivyo basi ni nini tunachozungumzia? Tunazungumzia mada kuhusu Mungu. Je, hii ndiyo mada muhimu zaidi kwa kila mtu? Maudhui ya mada kuhusu Mungu ni yapi? Bila shaka, mada hii haiwezi kamwe kutenganishwa na tabia ya Mungu, kiini cha Mungu na kazi ya Mungu. Hivyo leo, hebu tuzungumzie “Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe.”
Tangu wakati wanadamu walipoanza kumwamini Mungu, wamekuwa wakikutana na mada kama vile kazi ya Mungu, tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe. Inapokuja kwa suala la kazi ya Mungu, baadhi ya watu watasema: “Kazi ya Mungu imefanywa juu yetu; tunaipitia kila siku, kwa hivyo tunaifahamu.” Wanapozungumzia kuhusu tabia ya Mungu, wengine watasema: “Tabia ya Mungu ni mada tunayojifunza, tunayoichunguza, na kuizingatia katika maisha yetu yote, kwa hivyo ni lazima tuwe tunaifahamu.” Na kuhusu Mungu Mwenyewe, wengine watasema: “Mungu Mwenyewe ndiye tunayemfuata, ambaye tunamwamini, na ndiye tunayemshikilia; hivyo tumejuzwa kuhusu Yeye.” Mungu hajawahi kusitisha kazi Yake tangu uumbaji, wakati wote huu Ameendelea kuonyesha tabia Yake na kutumia njia mbalimbali kuonyesha neno Lake. Wakati huohuo, hajawahi kuacha kujionyesha Yeye Mwenyewe na kiini Chake kwa mwanadamu, akionyesha mapenzi Yake kwa binadamu na kile Anachohitaji kutoka kwa mwanadamu. Kwa hivyo, kwa mtazamo halisi, hakuna mtu mgeni kwa mada hizi. Kwa watu wanaomfuata Mungu leo, hata hivyo, Kazi ya Mungu, tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe kwa hakika ni mambo ambayo hayajulikani kwao. Kwa nini hali iko hivi? Kadri wanadamu wanavyoipitia kazi ya Mungu, wanakuja pia karibu na Mungu, na inawafanya wahisi ni kana kwamba wanaielewa tabia ya Mungu, au wana ujuzi fulani kuhusu jinsi ilivyo. Kutokana na hayo, mwanadamu hafikirii kuwa yeye ni mgeni katika kazi ya Mungu au tabia ya Mungu. Badala yake, mwanadamu anafikiria kwamba anamfahamu sana Mungu na anaelewa mengi kuhusu Mungu. Lakini kulingana na hali ya sasa, uelewa wa watu wengi kumhusu Mungu, umezuiliwa katika yale waliyoyasoma vitabuni, una ufinyu wa uzoefu binafsi, umezuiliwa na mawazo yao, na zaidi ya yote, umefungiwa katika kweli ambazo wanaweza kuziona kwa macho yao wenyewe. Haya yote yapo mbali sana na Mungu Mwenyewe wa kweli. Na je, umbali huu upo “mbali” kiasi gani? Pengine mwanadamu hana uhakika mwenyewe, au pengine mwanadamu ana hisia kidogo, ana fununu kiasi—lakini inapokuja kuhusu Mungu Mwenyewe, uelewa wa binadamu kumhusu Yeye u mbali sana na kiini cha Mungu Mwenyewe wa kweli. Hii ndiyo maana tunahitajika kutumia mada kama “Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe” ili kuwasilisha ujumbe huu hatua kwa hatua na kwa njia mahususi.
Kwa hakika, tabia ya Mungu iko wazi kwa kila mmoja na haijafichwa, kwa sababu Mungu hajawahi kumwepuka kimakusudi mtu yeyote na Hajawahi kudhamiria kujaribu kujificha Mwenyewe ili watu wasiweze kumjua Yeye au kumwelewa Yeye. Tabia ya Mungu siku zote imekuwa wazi na siku zote imekuwa ikikabiliana na kila mtu kwa uwazi. Katika usimamizi wa Mungu, Mungu hufanya kazi Yake, akimtazama kila mmoja; na kazi Yake inafanywa kwa kila mtu. Anapoifanya kazi hii, Anazidi kuifichua tabia Yake na kuendelea kutumia kiini Chake, na kile ambacho Anacho na Alicho, ili kumuongoza na kumkimu kila mmoja. Katika kila enzi na kwa kila hatua, haijalishi kama hali ni nzuri au ni mbaya, tabia ya Mungu siku zote iko wazi kwa kila mmoja, na vyote Anavyomiliki na uwepo Wake siku zote viko wazi kwa kila mtu, kama vile tu uhai Wake unavyomtosheleza na kumsaidia mwanadamu kila wakati na bila kukoma. Licha ya haya yote, tabia ya Mungu imebakia kufichwa kwa baadhi ya watu. Kwa nini iko hivyo? Ni kwa sababu ingawa watu hawa wanaishi ndani ya kazi ya Mungu na wanamfuata Mungu, hawajawahi kutafuta kumwelewa Mungu au kutaka kumjua Mungu, sembuse hata kumkaribia Mungu. Kwa watu hawa, kuelewa tabia ya Mungu kunamaanisha mwisho wao umekaribia; inamaanisha wako karibu kuhukumiwa na kushtakiwa na tabia ya Mungu. Hivyo basi, watu hawa hawajawahi kutamani kumwelewa Mungu au tabia Yake, na hawatamani uelewa au maarifa ya kina ya mapenzi ya Mungu. Hawanuii kufahamu mapenzi ya Mungu kwa ushirikiano wa hiari—wanafurahia tu milele na hawachoki kufanya mambo wanayotaka kuyafanya; kumwamini Mungu wanayetaka kumwamini; kumwamini Mungu aliyepo tu katika fikira zao, Mungu aliyepo tu katika dhana zao; na kumwamini Mungu asiyeweza kutenganishwa na wao katika maisha yao ya kila siku. Inapokuja kwa suala la Mungu Mwenyewe wa kweli, wanapuuza kabisa, hawataki kusikia mambo ya Mungu na hawana tamanio la kumwelewa Yeye, kumtilia maanani Yeye, sembuse kuwa na tamanio la kuwa karibu zaidi na Yeye. Wanayatumia tu maneno ambayo Mungu anayaonyesha ili kuweza kujipamba, kujiweka kwa namna fulani wao wenyewe. Kwao, hilo tayari linawafanya kuwa waumini wenye mafanikio na watu walio na imani kwa Mungu ndani ya mioyo yao. Katika mioyo yao, wanaongozwa na mawazo yao, dhana zao, na hata ufafanuzi wao binafsi wa Mungu. Mungu Mwenyewe wa kweli, kwa upande mwingine, Hana uhusiano wowote na wao. Kwa sababu pindi wanapomwelewa Mungu Mwenyewe wa kweli, kuelewa tabia ya Mungu ya kweli, na kuelewa kile Mungu anacho na alicho, hii inamaanisha kwamba matendo ya, imani yao, na yale yote wanayoyafuatilia yatashutumiwa. Na ndiyo maana wanachukia kuelewa kiini cha Mungu, ndiyo maana wanasitasita na hawako tayari kutafuta kwa bidii au kuomba ili wamwelewe Mungu zaidi, wapate kujua zaidi kuhusu mapenzi ya Mungu, na kuielewa vizuri zaidi tabia ya Mungu. Ni Afadhali kwao Mungu awe kitu kilichotungwa, kitu kisicho wazi na kisichoeleweka. Afadhali kwao Mungu awe ni mtu ambaye anafanana kabisa na vile ambavyo wamemfikiria Yeye, mtu ambaye Anaweza kutii matakwa yao, Asiyepunguka kutoa na Anayepatikana kila wakati. Wakati wanapotaka kuifurahia neema ya Mungu, wanamwomba Mungu awe neema hiyo. Wanapohitaji baraka za Mungu, wanamwomba Mungu awe baraka hiyo. Wanapokabiliwa na magumu, wanamwomba Mungu awatie moyo, ili Awe ngao yao. Maarifa ya watu hawa juu ya Mungu yamebakia ndani ya upeo wa neema na baraka. Uelewa wao wa kazi ya Mungu, tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe umezuiliwa pia kwa mawazo yao na vilevile barua na mafundisho ya kidini tu. Lakini wapo baadhi ya watu walio na shauku ya kuielewa tabia ya Mungu, wanaotaka kumwona Mungu Mwenyewe kwa kweli, na kuielewa tabia ya Mungu kwa kweli na kile Anacho na alicho. Watu hawa wanautafuta uhalisia wa ukweli na wokovu wa Mungu na wanatafuta kupokea ushindi, wokovu, na ukamilishaji wa Mungu. Watu hawa wanaitumia mioyo yao kusoma neno la Mungu, wanaitumia mioyo yao kuthamini kila hali na kila mtu, tukio, au kitu ambacho Mungu amewapangia, na kuomba na kutafuta kwa uaminifu. Kile wanachotaka zaidi ni kuyajua mapenzi ya Mungu na kuielewa tabia ya kweli na kiini cha Mungu. Hivi ndivyo ilivyo ili wasiweze tena kumkosea Mungu, na kupitia kwa mambo waliyoyapitia, waweze kuona zaidi uzuri wa Mungu na upande Wake wa kweli. Ni ili pia kwamba Mungu halisi na wa kweli aweze kuwepo ndani ya mioyo yao, na ili Mungu awe na nafasi katika mioyo yao, kiasi cha kwamba hawatakuwa wakiishi tena katikati ya fikira, dhana, au hali ya kutokuwa dhahiri. Kwa watu hawa, sababu inayowafanya kuwa na shauku kubwa ya kuielewa tabia ya Mungu na kiini Chake ni kwa sababu tabia ya Mungu na kiini Chake ni mambo ambayo mwanadamu anaweza kuyahitaji wakati wowote katika uzoefu wao, ni tabia Yake na kiini Chake ambavyo hutoa uhai katika maisha yao yote walioishi. Pindi wanapoielewa tabia ya Mungu, wataweza kumcha Mungu kwa njia bora zaidi, kushirikiana kwa njia bora zaidi na kazi ya Mungu, na kujali zaidi mapenzi ya Mungu na kutekeleza wajibu wao kwa njia bora zaidi wakitumia uwezo wao. Hawa ndio watu wa aina mbili inapokuja katika mitazamo yao kwa tabia ya Mungu. Watu wa aina ya kwanza hawataki kuielewa tabia ya Mungu. Ingawa wanasema wanataka kuielewa tabia ya Mungu, waweze kumjua Mungu Mwenyewe, kuona kile Mungu anacho na alicho, na kufahamu kwa kweli mapenzi ya Mungu, ndani yao kabisa wanaona afadhali Mungu asikuwepo. Ni kwa sababu watu wa aina hii wanakosa kumtii Mungu kila wakati na wanampinga; wanashindana na Mungu kwa ajili ya nafasi ndani ya mioyo yao na mara nyingi wanashuku na hata kukataa uwepo wa Mungu. Hawataki kuiruhusu tabia ya Mungu au kumuacha Mungu mwenyewe wa kweli aimiliki mioyo yao. Wanataka tu kutosheleza matamanio, mawazo, na maono yao binafsi. Kwa hivyo, watu hawa wanaweza kumwamini Mungu, kumfuata Mungu, na wanaweza pia kuacha familia zao na kazi kwa ajili Yake, lakini hawaachi njia zao mbaya. Wengine hata wanaiba au kutapanya sadaka, au kumlaani Mungu kisirisiri, ilhali wengine wanaweza kutumia nyadhifa zao mara kwa mara ili kujishuhudia, kujitukuza, na kushindana na Mungu kwa ajili ya watu na hadhi. Wanatumia mbinu na njia mbalimbali kuwafanya watu wawaabudu, wakijaribu daimaa kuwa na ufuasi mkubwa wa watu na kutaka kuwadhibiti watu hao. Baadhi hata wanawapotosha watu kwa kudhamiria na wanawafanya wafikirie kwamba wao ni Mungu ili waweze kutendewa kama Mungu. Hawawezi katu kuwaambia watu kwamba wamepotoshwa, kwamba wao pia ni wapotovu na wenye kiburi, na hivyo wasiwaabudu, na kwamba haijalishi wanafanya vizuri kiasi gani, yote ni kwa sababu ya kuinuliwa na Mungu na kwamba, hata hivyo, wanafanya yale wanayopaswa kufanya. Je, ni kwa nini hawasemi mambo haya? Ni kwa sababu wanaogopa sana kupoteza nafasi zao katika mioyo ya watu. Hii ndiyo maana watu kama hao hawamtukuzi Mungu katu na katu hawamshuhudii Mungu, kwani hawajawahi kujaribu kumwelewa Mungu. Je, wanaweza kumjua Mungu kama hawamwelewi? Haiwezekani! Hivyo, ingawa maneno katika mada “Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe” yanaweza kuwa rahisi, yana maana tofauti kwa kila mtu. Kwa mtu ambaye mara nyingi anamwasi Mungu, anampinga Mungu, na ana chuki dhidi ya Mungu, maneno hayo yanaashiria shutuma; ilhali mtu anayefuatilia uhalisi wa kweli na mara nyingi anakuja mbele za Mungu kutafuta mapenzi ya Mungu atayachukulia maneno hayo kama kawaida yake. Kwa hivyo kuna wale miongoni mwenu ambao, wanaposikia mazungumzo kuhusu tabia ya Mungu na kazi ya Mungu, wanaanza kuumwa na kichwa, mioyo yao inajaa upinzani, na wanakuwa katika hali isiyo na utulivu kabisa. Lakini kuna wengine miongoni mwenu wanaofikiria: Mada hii ndiyo hasa ninayohitaji, kwa sababu mada hii ni yenye manufaa sana kwangu. Ni sehemu ambayo haiwezi kukosekana katika uzoefu wangu wa maisha; ni kiini cha msingi, msingi wa imani kwa Mungu, na jambo ambalo mwanadamu hawezi kufikiria kuliacha. Kwenu nyote, mada hii inaweza kuonekana kuwa ya karibu na ya mbali, isiyojulikana ilhali inayozoeleka. Lakini haijalishi ni nini, hii ni mada ambayo kila mmoja lazima aisikilize, aijue, na lazima aielewe. Haijalishi ni vipi utakavyoishughulikia, haijalishi haijalishi jinsi unavyoitazama, au jinsi unavyoielewa, lakini umuhimu wa mada hii hauwezi kupuuzwa.
Mungu amekuwa akifanya kazi Yake tangu Alipowaumba wanadamu. Hapo mwanzo, ilikuwa kazi rahisi sana, lakini licha ya urahisi wake, ingali ilikuwa na maonyesho ya kiini na tabia ya Mungu. Ingawa kazi ya Mungu kwa sasa imepandishwa viwango, na kazi hii kwa kila mtu anayemfuata Yeye imekuwa kubwa mno na thabiti, yenye maonyesho makubwa ya neno Lake, nafsi ya Mungu imekuwa ikifichwa kutoka kwa wanadamu. Ingawa Amefanyika mwili mara mbili, kuanzia wakati wa simulizi za biblia hadi kwa siku za kisasa, ni nani amewahi kuona nafsi halisi ya Mungu? Kutokana na uelewa wenu, je, kuna mtu yeyote aliyewahi kuona nafsi halisi ya Mungu? La. Hakuna aliyewahi kuona nafsi halisi ya Mungu, kumaanisha kwamba hakuna aliyewahi kuona nafsi ya kweli ya Mungu. Hili ni jambo ambalo kila mmoja anakubaliana nalo. Hivi ni kusema, nafsi halisi ya Mungu, au Roho wa Mungu, amefichwa kutoka kwa wanadamu wote, wakiwemo Adamu na hawa, ambao Aliwaumba, na akiwemo Ayubu mwenye haki, ambaye alikuwa Amemkubali. Hata wao hawakuona nafsi halisi ya Mungu. Lakini ni kwa nini Mungu amedhamiria kuificha nafsi Yake halisi? Baadhi ya watu husema: “Mungu anaogopa kuwatisha watu.” Wengine husema: “Mungu huficha nafsi Yake halisi kwa sababu binadamu ni mdogo sana na Mungu ni mkuu sana; wanadamu hawaruhusiwi kumwona Yeye, la sivyo watakufa.” Wapo pia wale wanaosema: “Mungu amekua akishughulika sana na usimamizi wa kazi Yake kila siku, huenda Asiwe na muda wa kuonekana na kuwaruhusu watu kumwona Yeye.” Haijalishi ni nini mnachoamini, Nina hitimisho hapa. Hitimisho hilo ni nini? Ni kwamba tu Mungu hataki watu waione nafsi Yake halisi. Akiwa amefichwa kutoka kwa binadamu ni kitu ambacho Mungu anafanya kimakusudi. Kwa maneno mengine, ni nia ya Mungu kwa watu kutoona nafsi Yake halisi. Hii inapaswa kuwa wazi kwa wote sasa. Kama Mungu hajawahi kuonyesha nafsi Yake kwa yeyote, je, mnafikiria nafsi ya Mungu ipo? (Ipo.) Bila shaka ipo. Uwepo wa nafsi ya Mungu haupingiki. Lakini kuhusu nafsi ya Mungu ni kubwa vipi au inafanana vipi, je, ni maswali ambayo mwanadamu anafaa kuchunguza? La. Jibu ni hapana. Kama nafsi ya Mungu si mada ambayo tunafaa kuchunguza, basi ni swali lipi ambalo tunafaa kuchunguza? (Tabia ya Mungu.) (Kazi ya Mungu.) Kabla hatujaanza kushiriki kuhusu mada hii rasmi, hata hivyo, hebu turudi katika kile tulichokuwa tukikizungumzia muda mfupi uliopita: Kwa nini Mungu hajawahi kuonyesha nafsi Yake kwa wanadamu? Kwa nini Mungu anaficha kimakusudi nafsi Yake kutoka kwa wanadamu? Kuna sababu moja tu, nayo ni hii: Ingawa mwanadamu ambaye Mungu alimuumba, amepitia maelfuya miaka ya kazi ya Mungu, hakuna hata mtu mmoja anayejua kazi ya Mungu, tabia ya Mungu, na kiini cha Mungu. Watu kama hao, machoni pa Mungu, wako kinyume na Mungu, na Mungu asingejionyesha mwenyewe kwa watu walio na uadui na Yeye. Hii ndiyo sababu ya pekee kwa nini Mungu hajawahi kuwaonyesha wanadamu nafsi Yake na ndiyo sababu Anaificha kwa makusudi nafsi Yake dhidi yao. Je, sasa mnaelewa kuhusu umuhimu wa kuijua tabia ya Mungu?
Tangu kuwepo kwa usimamizi wa Mungu, siku zote Amejitolea kikamilifu katika kutekeleza kazi Yake. Licha ya kuficha nafsi Yake kutoka kwao, siku zote Amekuwa upande wa mwanadamu, Akifanya kazi kwa mwanadamu, Akionyesha tabia Yake, Akiwaongoza wanadamu wote kwa kiini Chake, na kufanya kazi Yake kwa kila mmoja kupitia nguvu Zake, hekima Yake, na mamlaka Yake, hivyo akiileta Enzi ya Sheria, Enzi ya Neema, na sasa Enzi ya Ufalme. Ingawa Mungu huificha nafsi Yake kutoka kwa binadamu, tabia Yake, uwepo Wake na miliki Yake, na mapenzi Yake kwa binadamu yanafichuliwa kikamilifu kwa mwanadamu, ili mwanadamu aweze kuona na kupitia. Kwa maneno mengine, ingawa binadamu hawawezi kumwona au kumgusa Mungu, tabia na kiini cha Mungu ambacho binadamu wamekuwa wakikutana nacho ni maonyesho kabisa ya Mungu Mwenyewe. Je, hayo si kweli? Bila kujali ni mbinu gani au ni mtazamo gani ambao Mungu anachagua kwa ajili ya kazi Yake, Yeye huwatendea watu siku zote kupitia utambulisho Wake wa kweli, Akifanya kazi Anayopaswa kufanya, na kunena maneno ambayo Anapaswa kunena. Haijalishi ni nafasi gani ambayo Mungu anazungumza kutoka—Anaweza kuwa amesimama kwenye mbingu ya tatu, au Amesimama akiwa katika mwili, au hata kama mtu wa kawaida—siku zote Anaongea kwa binadamu kwa moyo Wake wote na kwa akili Zake zote, bila udanganyifu wowote au kuficha chochote Anapotekeleza kazi Yake, Mungu huonyesha neno Lake na tabia Yake, na huonyesha kile Anacho na Alicho, bila kuficha chochote. Anawaongoza wanadamu kwa uhai Wake na nafsi Yake na miliki yake. Hivi ndivyo binadamu alivyoishi katika Enzi ya Sheria—enzi asilia ya binadamu—akiongozwa na Mungu asiyeonekana na asiyegusika.
Mungu alifanyika mwili kwa mara ya kwanza baada ya Enzi ya Sheria, kupata mwili ambako kulidumu kwa miaka thelathini na tatu na nusu. Kwa mwanadamu, je, miaka thelathini na mitatu na nusu ni muda mrefu? (Si muda mrefu.) Kwa sababu urefu wa maisha ya mwanadamu kwa kawaida ni mirefu zaidi kuliko miaka thelathini na kitu, huu si muda mrefu kwa mwanadamu. Lakini kwa Mungu mwenye mwili, miaka hii thelathini na mitatu na nusu ilikuwa mirefu mno. Aligeuka na kuwa mtu—mtu wa kawaida aliyetekeleza kazi na agizo la Mungu. Hii ilimaanisha kwamba Alipaswa kufanya kazi ambayo mtu wa kawaida asingeweza kuifanya, huku Akivumilia mateso ambayo binadamu wa kawaida hawezi kuvumilia. Kiwango cha mateso aliyovumilia Bwana Yesu katika Enzi ya Neema, kuanzia mwanzo wa kazi Yake hadi wakati Aliposulubishwa msalabani, huenda isiwe ni kitu ambacho watu wa leo wanaweza kushuhudia wao binafsi, lakini je, mnaweza kutambua angalau kwa kiasi kidogo kupitia hadithi zilizo kwenye Biblia? Haijalishi ni maelezo mangapi yaliyopo kwenye ukweli huu uliorekodiwa, kwa ujumla, kazi ya Mungu katika kipindi hiki ilijaa ugumu na mateso. Kwa mwanadamu aliyepotoka muda wa miaka thelathini na mitatu na nusu si mrefu; mateso kidogo si jambo la kutisha. Lakini kwa Mungu mtakatifu asiye na doa, ambaye lazima Avumilie dhambi zote za binadamu, na kula, kulala na kuishi na watenda dhambi, maumivu haya ni makubwa mno. Yeye ndiye Muumba, Bwana wa viumbe vyote na Mtawala wa vitu vyote, lakini Alipokuja duniani alilazimika kuvumilia unyanyasaji na ukatili wa wanadamu waliopotoka. Ili kuikamilisha kazi Yake na kuwaokoa binadamu kutoka kwa taabu, Alilazimika kushutumiwa na binadamu, na kuvumilia dhambi za wanadamu wote. Kiwango cha mateso Aliyoyapitia hakiwezi kwa kweli kueleweka au kutambulika na watu wa kawaida. Je, mateso haya yanawakilisha nini? Yanawakilisha kujitoa kwa Mungu kwa ajili ya wanadamu. Yanawakilisha fedheha Aliyoipata na gharama Aliyolipa kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu, kukomboa dhambi zao, na kukamilisha hatua hii ya kazi Yake. Pia yanamaanisha kwamba mwanadamu angekombolewa kutoka msalabani na Mungu. Hii ndiyo gharama iliyolipwa kwa damu, kwa maisha, gharama ambayo viumbe walioumbwa hawawezi kumudu. Ni kwa sababu Anacho kiini cha Mungu na Ana kile Mungu anacho na alicho, ndiyo maana Anaweza kuvumilia aina hii ya mateso na aina hii ya kazi. Hili ni jambo ambalo hakuna kiumbe aliyeumbwa ambaye angeweza kufanya badala Yake. Hii ni kazi ya Mungu katika Enzi ya Neema na ufunuo wa tabia Yake. Je, hii inafichua chochote kuhusu kile Mungu anacho na alicho? Je, wanadamu wanastahili kuijua? Katika enzi hiyo, japokuwa mwanadamu hakuiona nafsi ya Mungu, alipokea sadaka ya Mungu dhidi ya dhambi zake na akakombolewa kutoka msalabani na Mungu. Huenda wanadamu wasiijue kazi ambayo Mungu alifanya wakati wa Enzi ya Neema, lakini je, kuna yeyote anayefahamu tabia na nia zilizoonyeshwa na Mungu katika kipindi hiki? Binadamu anajua tu kuhusu maudhui ya kazi ya Mungu katika enzi tofauti na kupitia njia mbalimbali, au anajua hadithi zinazohusiana na Mungu ambazo zilifanyika kwa wakati huo huo ambao Mungu alikuwa akitekeleza kazi Yake. Maelezo haya na hadithi hizi kwa kiasi kikubwa ni taarifa fulani tu au hekaya kuhusu Mungu na hazina uhusiano wowote na tabia na kiini cha Mungu. Hivyo haijalishi ni hadithi ngapi watu wanazojua kuhusu Mungu, haimaanishi kwamba wanao uelewa wa kina na maarifa kuhusu tabia ya Mungu au kiini Chake. Kama vile katika Enzi ya Sheria, ingawaje watu kutoka Enzi ya Neema walikuwa wameweza kupitia kukutana kwa karibu na kwa karibu zaidi na Mungu katika mwili, maarifa yao kuhusu tabia ya Mungu na kiini cha Mungu kwa hakika hayakuwepo.
Katika Enzi ya Ufalme, Mungu akafanyika mwili tena, kwa njia sawa na ile Aliyotumia mara ya kwanza. Katika kipindi hiki cha kazi, bado Mungu anaonyesha neno Lake kikamilifu, Anafanya kazi Anayopaswa kufanya, na kueleza kile Anacho na Alicho. Kwa wakati huohuo, Anaendelea kuvumilia na kustahimili kutotii na kutojua kwa binadamu. Je, Mungu hafichui kila wakati tabia Yake na kuonyesha mapenzi yake katika kipindi hiki cha kazi pia? Hivyo basi, tangu kuumbwa kwa mwanadamu hadi sasa, tabia ya Mungu, nafsi Yake na miliki Zake, na mapenzi Yake, siku zote yamekuwa wazi kwa kila mmoja. Mungu hajawahi kuficha kimakusudi kiini Chake, tabia Yake au mapenzi Yake. Ni vile tu mwanadamu hajali kuhusu kile ambacho Mungu anafanya, mapenzi Yake ni yapi—ndio maana uelewa wa binadamu kumhusu Mungu ni finyu mno. Kwa maneno mengine, wakati Mungu anaficha nafsi Yake, Yeye pia Anasimama kando ya mwanadamu kila wakati, akionyesha waziwazi mapenzi Yake, tabia Yake na kiini chake halisi siku zote. Kimsingi, nafsi ya Mungu pia iko wazi kwa watu lakini kutokana na upofu na kutotii kwa binadamu, siku zote hawawezi kuona kuonekana kwa Mungu. Kwa hivyo ikiwa hivyo ndivyo, si inawezekana kuielewa tabia ya Mungu na Mungu Mwenyewe isiwe ni jambo rahisi kwa kila mmoja? Hili ni swali gumu sana kujibu, sivyo? Mnaweza kusema ni rahisi, lakini wakati watu wengine wanatafuta kumjua Mungu, hatimaye hawamjui Yeye au kupata uelewa wa wazi kumhusu Yeye—siku zote ni jambo lililojaa ukungu na lisiloeleweka. Lakini mkisema si rahisi, hilo si sahihi vilevile. Baada ya kuwa mlengwa wa kazi ya Mungu kwa muda mrefu, kila mmoja anapaswa, kupitia uzoefu wake, kuwa amepitia kwa kweli mambo mbalimbali na Mungu. Angalau wanapaswa kumhisi Mungu kwa kiwango fulani katika mioyo yao au wawe na mguso wa kiroho na Mungu, na angalau wanapaswa kuwa na uwezo fulani wa kutambua kuhusu tabia ya Mungu au kupata uelewa fulani kumhusu Yeye. Kuanzia wakati ambao mwanadamu alianza kumfuata Mungu hadi sasa, mwanadamu amepokea mengi mno, lakini kutokana na kila aina ya sababu—uwezo duni wa mwanadamu, ujinga, uasi, na nia mbalimbali—wanadamu pia wamepoteza mengi sana. Je, Mungu bado hajawapatia wanadamu vya kutosha? Ingawa Mungu huficha nafsi Yake kutoka kwa wanadamu, Anawatosheleza mahitaji yao kwa kile Anacho na alicho, na hata uzima Wake; maarifa ya wanadamu kumhusu Mungu hayafai kuwa vile yalivyo tu sasa. Ndiyo maana Nafikiri inahitajika kuwa na ushirika zaidi na nyinyi kuhusu mada ya kazi ya Mungu, kuhusu tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe. Dhumuni ni ili kwamba maelfu ya miaka ya utunzaji na fikira ambayo Mungu ameweka kwa mwanadamu isiishie kuwa bure, na ili wanadamu waweze kuelewa na kutambua kwa kweli mapenzi ya Mungu kwao. Ni ili watu waweze kusonga mbele kwenye hatua mpya ya maarifa yao kumhusu Mungu. Itaweza pia kumrudisha Mungu katika nafasi Yake iliyo sahihi katika mioyo ya watu; yaani, kumtendea Yeye haki.
Ili kuelewa tabia ya Mungu na Mungu Mwenyewe lazima muanzie na jambo dogo sana. Jambo hilo dogo sana mnalopaswa kuanzia ni lipi? Kwanza kabisa, Nimezikusanya baadhi ya sura kutoka kwenye Biblia. Taarifa iliyo hapa chini inayo mistari ya Biblia, ambayo yote inahusiana na mada ya tabia ya Mungu, kazi ya Mungu na Mungu Mwenyewe. Nilipata dondoo hizi mahususi kama nyenzo za marejeleo ili kuwasaidia kujua kazi ya Mungu, tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe. Hapa Nitashiriki nanyi ili muweze kuona ni aina gani ya tabia na kiini cha Mungu ambacho kimefichuliwa kupitia kwa kazi Yake iliyopita lakini watu hawajui kuihusu. Sura hizi zinaweza kuwa nzee, lakini mada tunayowasiliana ni kitu kipya ambacho watu hawana na hawajawahi kusikia. Baadhi yenu huenda mkaona kuwa jambo hilo haliwezekani—je, kule kuwataja Adamu na Hawa na kumrejelea Nuhu si kurudia hatua zilezile tena? Haijalishi ni nini mnafikiria, sura hizi ni zenye manufaa sana kwa ushirika kuhusu mada hii na zinaweza kutumika kama vifungu vya kufundishia au nyenzo za matumizi ya kwanza katika ushirika wa leo. Mtaelewa nia Zangu za kuchagua sehemu hizi kufikia wakati Nitakapoumaliza ushirika huu. Wale ambao wamesoma Biblia hapo awali huenda wameona mistari hii michache, lakini huenda hawakuielewa kwa kweli. Hebu kwanza tuangalie kwa haraka kabla ya kuipitia mistari hii moja baada ya nyingine kwa kina zaidi.
Adamu na Hawa ni mababu wa wanadamu. Ikiwa tutataja wahusika kutoka kwenye Biblia, basi lazima tuanzie na wawili hawa. Kisha Nuhu, babu wa pili wa mwanadamu. Mhusika wa tatu ni nani? (Ibrahimu.) Je, nyote mnaijua hadithi ya Ibrahimu? Baadhi yenu mnaweza kuijua, lakini kwa baadhi yenu huenda isiwe wazi sana. Nani ndiye mhusika wa nne? Ni nani anayetajwa kwenye hadithi ya kuangamizwa kwa Sodoma? (Lutu.) Lakini Lutu hajarejelewa hapa. Ni nani anayerejelewa? (Ibrahimu.) Jambo kubwa lililotajwa katika hadithi ya Ibrahimu ni kile ambacho Yehova Mungu alichokuwa amesema. Je, mnaona haya? Ni nani ndiye mhusika wa tano? (Ayubu.) Je, Mungu hataji hadithi nyingi za Ayubu katika hatua hii ya sasa ya kazi Yake? Basi je, mnajali sana kuhusu hadithi hii? Kama mnajali sana, je mmeisoma hadithi ya Ayubu kwenye Biblia kwa umakinifu? Je, mnajua ni mambo gani Ayubu aliyoyasema, ni mambo gani aliyofanya? Wale ambao wameisoma hadithi hiyo sana, ni mara ngapi mmeisoma? Je, mnaisoma mara kwa mara? Akina dada kutoka Hong Kong, tafadhali tuambieni. (Mimi niliisoma mara kadhaa hapo awali tulipokuwa katika Enzi ya Neema.) Hamjawahi kuisoma tena tangu hapo? Kama ni hivyo, basi hiyo ni aibu kubwa. Wacha Niwaambie: Katika hatua hii ya kazi ya Mungu Alimtaja Ayubu mara nyingi, na hilo ni onyesho la nia Zake. Kwamba Alimtaja Ayubu mara nyingi lakini umakini wenu haukuzinduliwa ni uthibitisho wa ukweli kwamba: Hamna haja ya kuwa watu ambao ni wazuri na watu wanaomcha Mungu na kujiepusha na maovu. Hii ni kwa sababu mnatosheka tu na kuwa na wazo la juujuu kuhusu hadithi ya Ayubu iliotajwa na Mungu. Mnatosheka na uelewa wa juujuu wa hadithi yenyewe, lakini hamjali kuihusu na hamtaki kufahamu maelezo yanayohusu Ayubu ni nani na dhumuni la kwa nini Mungu anamrejelea Ayubu mara nyingi. Ikiwa mtu kama huyo anayesifiwa na Mungu hakupendezi wewe, basi je, ni nini hasa unachozingatia? Ikiwa hujali au kujaribu kumwelewa mtu muhimu kama huyo ambaye Mungu amemtaja, basi hilo linaweza kuashiria nini kuhusu mtazamo wako kwa neno la Mungu? Je, hilo si jambo baya? Je, hiyo haithibitishi kwamba wengi wenu hawajihusishi katika mambo ya kivitendo na nyinyi nyote hamfuatilii ukweli? Kama unafuatilia ukweli, utaweka umakinifu unaohitajika kwa watu ambao Mungu anawakubali na hadithi za wahusika ambazo Mungu amezungumzia juu yao. Bila kujali kama unaweza kuishi kulingana nazo au kuona hadithi zao kuwa za kueleweka, utaenda haraka na kuzisoma, utajaribu kuzielewa, kutafuta njia za kufuata mfano wao, na kufanya vile uwezavyo kwa kadiri ya uwezo wako. Hiyo ndiyo tabia ya mtu anayetamani ukweli. Lakini ukweli ni kwamba wengi wenu mlioketi hapa hamjawahi kuisoma hadithi ya Ayubu. Hii kwa kweli inaniambia kitu.
Hebu turudi katika mada niliyokuwa Nikizungumzia muda mfupi uliopita. Sehemu hii ya maandiko inayohusu Enzi ya Sheria ya Agano la Kale ndio haswa hadithi za wahusika ambao Nilikuwa nimewachagua. Hizi ni hadithi zinazofahamika kwa watu wengi ambao wamesoma Biblia. Wahusika hawa ni wawakilishi sana. Wale waliosoma hadithi hizi wataweza kuhisi kwamba kazi ambayo Mungu ameifanya juu yao na maneno ambayo Mungu amewazungumzia yanaeleweka na yanafikika kwa watu wa leo. Unaposoma hadithi hizi na rekodi hizi kutoka kwenye Biblia, utaweza kuelewa namna ambavyo Mungu alifanya kazi Yake na jinsi alivyowatendea watu wa wakati huo. Lakini dhumuni la Mimi kushiriki sura hizi leo sio kwamba ujaribu kuzingatia hadithi zenyewe au wahusika ndani yake. Badala yake, ni ili uweze—kupitia hadithi za wahusika hawa—uje uone matendo ya Mungu na tabia Yake, na hivyo itakuwezesha kupata kumjua na kumwelewa Mungu kwa urahisi zaidi, kuona upande Wake halisi; itasitisha fikira zako, na kukomesha dhana zako kumhusu Yeye, na kukusaidia kuiweka mbali imani isiyokuwa na uhakika. Kujaribu kuifahamu tabia ya Mungu na kuielewa na kupata kumjua Mungu mwenyewe bila ya msingi, kunaweza mara nyingi kukufanya ujihisi kama mtu usiye na msaada, usiye na nguvu, na usiye na uhakika ni wapi utaanzia. Na ndiyo maana Nilifikiria ni wazo zuri kutumia mbinu kama hii na mtazamo ili kukufanya kumwelewa Mungu kwa njia bora zaidi, kufahamu mapenzi ya Mungu kwa uhalisi zaidi, na kupata kuijua tabia ya Mungu na Mungu Mwenyewe, na kukufanya uhisi kwa kweli uwepo wa Mungu na kufahamu mapenzi Yake kwa wanadamu. Je, haya si yenye manufaa kwenu? Sasa mnahisi vipi ndani ya mioyo yenu mnapoziangalia hadithi hizi na maandiko haya tena? Je, mnafikiria maandiko haya Niliyoyachukua yamepita kiasi? Lazima Nitilie mkazo tena kile Nimetoka tu kuwaambia. Nia ya kuwaruhusu kusoma hadithi za wahusika hawa ni ili kuwasaidia kuelewa namna ambavyo Mungu anafanya kazi Yake kwa watu na mtazamo Wake kwa wanadamu. Ni kupitia nini ndipo mtaweza kuelewa haya? Ni kwa kupitia kazi ambayo Mungu ameifanya hapo awali, na ikiunganishwa pamoja na kazi ambayo Mungu anaifanya kwa sasa itawasaidia kuelewa mambo mbalimbali kuhusu Yeye. Mambo haya mbalimbali ni ya kweli, na lazima yajulikane na yatambulike na wote wanaotaka kumjua Mungu.
Tutaanza sasa na hadithi ya Adamu na Hawa. Kwanza, hebu tuyasome maandiko.
A. Adamu na Hawa
1. Amri ya Mungu kwa Adamu
Mwa 2:15-17 Naye Yehova Mungu akamchukua mtu huyo, na kumweka ndani ya bustani ya Edeni ili ailime na kuihifadhi. Yehova Mungu akamwamrisha mtu huyo, akisema, Unaweza kula kwa uhuru matunda kutoka miti yote ya bustani: Lakini kutoka mti wa maarifa ya mema na maovu, usiyale: kwa kuwa katika siku ambapo utakula matunda kutoka mti huo bila shaka utakufa.
Je, mlielewa chochote kutoka kwenye mistari hii? Je, sehemu hii ya maandiko inakufanya ujihisi vipi? Ni kwa nini Nimeamua kuzungumzia kuhusu “Amri ya Mungu kwa Adamu”? Je, kila mmoja wenu sasa anayo picha ya Mungu na Adamu katika akili yake? Unaweza kujaribu kufikiria: Kama ungekuwa ni wewe katika tukio hilo, je, Mungu katika moyo wako angekuwa vipi? Je, ni hisia gani ambazo picha hii inakupatia? Hii ni picha ya kusisimua na ya kutia moyo. Ingawa kuna Mungu tu na mwanadamu ndani yake, ule ukaribu kati yao unajaza hisia za kupendeza: Upendo wa Mungu ulio tele umetolewa bure kwa mwanadamu, unamzunguka mwanadamu; mwanadamu ni mnyofu na asiye na hatia, aliye huru kabisa na asiye na wasiwasi wowote, anaishi kwa furaha chini ya uangalizi wa jicho la Mungu; Mungu anaonyesha hali ya kumjali mwanadamu, huku naye mwanadamu anaishi katika ulinzi na baraka za Mungu; kila kitu mwanadamu anachofanya na kusema kinaunganishwa kwa karibu na Mungu na hakiwezi kutenganishwa na Mungu.
Mnaweza kusema kwamba hii ndiyo amri ya kwanza ya Mungu aliyoitoa kwa mwanadamu baada ya kumuumba. Je, amri hii inabeba nini? Amri hii ina mapenzi ya Mungu, lakini pia ina wasiwasi Wake kwa wanadamu. Hii ndiyo amri ya kwanza ya Mungu na pia ndio mara ya kwanza Mungu anakuwa na wasiwasi kuhusu binadamu. Hivi ni kusema, Mungu analo jukumu kwa mwanadamu tangu wakati ule Alipomuumba. Jukumu Lake ni lipi? Anapaswa kumlinda mwanadamu, kumwangalia mwanadamu. Anatumaini kwamba mwanadamu ataweza kuamini na kutii maneno Yake. Hili pia ndilo tarajio la kwanza la Mungu kwa binadamu. Na ni kwa tarajio hili kwamba Mungu anasema yafuatayo: “Unaweza kula kwa uhuru matunda kutoka miti yote ya bustani: Lakini kutoka mti wa maarifa ya mema na maovu, usiyale: kwa kuwa katika siku ambapo utakula matunda kutoka mti huo bila shaka utakufa.” Maneno haya rahisi yanawakilisha mapenzi ya Mungu. Yanafichua pia kwamba moyo wa Mungu tayari umeanza kuonyesha hali ya kumjali mwanadamu. Kati ya vitu vyote, ni Adamu pekee aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu; Adamu alikuwa kiumbe hai pekee mwenye pumzi ya uhai wa Mungu; angeweza kutembea na Mungu, kuzungumza na Mungu. Na ndiyo maana Mungu alimpa amri kama hiyo. Mungu aliweka wazi katika amri hii kile binadamu anachoweza kufanya, na vilevile Akaweka wazi kile asichoweza kufanya.
Katika maneno haya machache rahisi, tunauona moyo wa Mungu. Lakini ni moyo wa aina gani tunaouona? Je, kuna upendo katika moyo wa Mungu? Je, upendo huo unao hali yoyote ya kujali ndani yake? Katika mistari hii, upendo na kujali kwa Mungu sio tu kwamba vinaweza kufahamika, bali pia kuhisiwa kwa karibu. Je, hayo ni kweli? Sasa kwa kuwa Nimesema mambo haya, je, bado unafikiri haya ni maneno machache tu yaliyo rahisi? Si rahisi sana, sivyo? Je, mgeweza kuona hili hapo kabla? Kama Mungu mwenyewe angekuambia maneno hayo machache, ungehisi vipi ndani? Kama wewe si mtu mwenye utu, kama moyo wako ni baridi kama barafu, basi usingehisi chochote, usingethamini upendo wa Mungu, na usingejaribu kuuelewa moyo wa Mungu. Lakini kama wewe ni mtu mwenye dhamiri, mwenye ubinadamu, basi utahisi tofauti. Utahisi joto, utahisi kuwa umetunzwa na umependwa, na utahisi furaha. Je, hayo ni kweli? Unapohisi mambo haya, utatenda vipi kwa Mungu? Je, ungehisi kuunganishwa na Mungu? Je, ungempenda na kumheshimu Mungu kutoka ndani kabisa ya moyo wako? Je, moyo wako ungekua karibu zaidi na Mungu? Unaweza kuona kutoka kwa haya jinsi ambavyo upendo wa Mungu ulivyo muhimu kwa binadamu. Lakini kile kilicho muhimu zaidi ni kuthamini na kufahamu kwa binadamu upendo huu wa Mungu. Kwa hakika, je, Mungu hasemi mambo mengi yanayofanana kwenye awamu hii ya kazi Yake? Lakini je, watu wa leo wanauthamini moyo wa Mungu? Je, mnaweza kung’amua mapenzi ya Mungu Niliyoyazungumzia muda mfupi uliopita? Hamwezi hata kutambua mapenzi ya Mungu wakati yanaonekana waziwazi, yanaweza kuonekana na ni halisi. Na ndiyo maana Nasema hamna maarifa na uelewa halisi wa Mungu. Je, haya si kweli? Hayo tu ndiyo yote tutakayoshiriki katika sehemu hii.
2. Mungu Amuumba Hawa
Mwa 2:18-20 Yehova Mungu akasema, Si vizuri kuwa mtu huyo akuwe peke yake; nitamuumbia msaidizi anayefanana na yeye. Na kutoka kwa ardhi Yehova Mungu akaumba wanyama wote wa msituni, na ndege wote wa angani; na akawaletea kwa Adamu ndiyo aone majina ambayo angewapa: na chochote ambacho Adamu alikiita kiumbe hai, hilo ndilo likawa jina lake kuanzia hapo. Naye Adamu akawapa wanyama wote wa kufugwa majina, na ndege wa hewani, na wanyama wote wa mwituni; lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi ambaye alifanana na yeye.
Mwa 2:22-23 Nao ubavu, ambao Yehova Mungu aliuchukua kutoka kwa Adamu, Yeye akaufanya uwe mwanamke, na akampeleka kwa Adamu. Naye Adamu akasema, Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu, na nyama ya nyama zangu: ataitwa Mwanamke, kwa kuwa amechukuliwa kutoka kwa Mwanamume.
Kuna msitari mmoja muhimu katika sehemu hii ya Maandiko: “chochote ambacho Adamu alikiita kiumbe hai, hilo ndilo likawa jina lake kuanzia hapo.” Kwa hivyo, ni nani aliyewapatia viumbe hai wote majina yao? Ilikuwa Adamu, si Mungu. Msitari huu unamwambia mwanadamu ukweli: Mungu alimpa binadamu werevu Alipomuumba. Hivi ni kusema kwamba, werevu wa binadamu ulitoka kwa Mungu. Hili ni kweli. Lakini kwa nini? Baada ya Mungu kumuumba Adamu, je, Adamu alienda shuleni? Je, alijua namna ya kusoma? Baada ya Mungu kuwaumba viumbe hai mbalimbali, je, Adamu aliwatambua viumbe hawa wote? Je, Mungu alimwambia majina ya viumbe hao? Bila shaka, Mungu pia hakumfunza namna ya kutunga majina ya viumbe hawa. Huo ndio ukweli! Basi alijua vipi namna ya kuwapa viumbe hao hai majina yao na aina gani ya majina ya kuwapatia? Haya yote yanahusiana na swali kuhusu ni nini ambacho Mungu aliongezea kwa Adamu Alipomuumba. Ukweli unathibitisha kwamba wakati Mungu alipomuumba mwanadamu, Alimwongezea akili. Huu ni ukweli muhimu sana. Je, nyinyi nyote mmesikiliza kwa makini? Kuna ukweli mwingine wa muhimu ambao unapaswa kuwa wazi kwenu? Baada ya Adamu kuwapatia viumbe hai majina yao, majina haya yalipangwa kwenye msamiati wa Mungu. Kwa nini Ninasema hivyo? Hii pia inahusisha tabia ya Mungu, na lazima Niielezee.
Mungu alimuumba mwanadamu, Alimpulizia uhai ndani yake, na pia akampa sehemu ya akili Zake, uwezo Wake, na kile Anacho na Alicho. Baada ya Mungu kumpa mwanadamu vitu hivi vyote, mwanadamu aliweza kufanya baadhi ya mambo kwa kujitegemea na kwa kufikiria peke yake. Ikiwa kile ambacho mwanadamu anaunda na kufanya ni kizuri machoni mwa Mungu, basi Mungu anakikubali na haingilii kati. Kama kile mwanadamu anachofanya ni sahihi, basi Mungu atakiacha tu kiwe hivyo milele. Kwa hivyo kauli hii “chochote ambacho Adamu alikiita kiumbe hai, hilo ndilo likawa jina lake kuanzia hapo” inaonyesha nini? Hiyo inaonyesha kwamba Mungu hakufanya marekebisho yoyote kwa majina ya wale viumbe hiyo mbalimbali. Jina lolote lile ambalo Adamu aliliita kwa kiumbe, Mungu alisema “Ndiyo” na akasajili jina hilo kama ilivyo. Je, Mungu alitoa maoni yoyote? La, hilo ni hakika. Kwa hivyo, mnaona nini hapa? Mungu Alimpa mwanadamu akili na mwanadamu akatumia akili zake alizopewa na Mungu kufanya mambo. Ikiwa kile mwanadamu anachofanya ni chanya machoni pa Mungu, basi kinathibitishwa, kutambulika, na kukubalika na Mungu bila ya utathmini au ukosoaji wowote. Hili ni jambo ambalo hakuna mtu au roho mwovu, au Shetani, anaeweza kulifanya. Je, mnauona ufunuo wa tabia ya Mungu hapa? Je, mwanadamu, mtu aliyepotoshwa, au Shetani anaweza kuwaruhusu watu wengine katika kuwawakilisha kufanya mambo huku wakitazama? Bila shaka sivyo! Je, wanaweza kupigania cheo na yule mtu mwingine au nguvu nyingine ambayo ni tofauti na wao? Bila shaka wangefanya hivyo! Na kwa muda huo, kama angekuwa ni mtu aliyepotoshwa au Shetani aliyekuwa na Adamu, bila shaka wangekataa kile ambacho Adamu alikuwa akifanya. Ili kuthibitisha kwamba wanao uwezo wa kufikiria kwa kujitegemea na wana ujuzi wao binafsi wa kipekee, wangekataa kabisa kila kitu alichofanya Adamu: “Unataka kukiita hivyo? Kwa kweli, sitakiita hivyo, nitakiita hivi; ulikiita Tom lakini mimi nitakiita Harry. Lazima nionyeshe jinsi nilivyo mwerevu.” Hii ni asili ya aina gani? Je, hiki si kiburi kilichopitiliza? Lakini je, Mungu ana tabia kama hiyo? Je, Mungu alikuwa na upinzani wowote usiokuwa wa kawaida kwa mambo haya ambayo Adamu alifanya? Bila shaka, jibu ni hapana! Kuhusu tabia ambayo Mungu anaifichua, hakuna kidokezo chochote cha mabishano, kiburi, au kujigamba. Hilo liko wazi kabisa hapa. Hili linaweza kuonekana kuwa jambo dogo tu, lakini kama huelewi kiini cha Mungu, kama moyo wako hautajaribu kujua namna ambavyo Mungu anatenda na mtazamo wa Mungu ni upi, basi hutaijua tabia ya Mungu au kuona udhihirisho na ufunuo wa tabia ya Mungu. Je, hayo si kweli? Je, unakubali kile Nimetoka tu kukuelezea? Kwa mujibu wa matendo ya Adamu, Mungu hakutangaza kwa sauti kwamba, “Umefanya vyema. Umefanya sahihi Ninakubali.” Katika Moyo Wake, hata hivyo, Mungu aliidhinisha, Akathamini, na Akashangilia kile ambacho Adamu alikuwa amefanya. Hili ndilo jambo la kwanza tangu uumbaji ambalo binadamu alikuwa amemfanyia Mungu akifuata maagizo Yake. Ni jambo ambalo binadamu alilifanya badala ya Mungu na kwa niaba ya Mungu. Machoni pa Mungu, hili lilitokana na werevu Aliokuwa amempa mwanadamu. Mungu aliliona kama jambo jema, jambo chanya. Kile ambacho Adamu alikifanya kwa wakati huo kilikuwa ni udhihirisho wa kwanza wa werevu wa Mungu kwa binadamu. Huu ulikuwa ni udhihirisho mzuri kutoka kwa maoni ya Mungu. Kile Ninachotaka kuwaambia ninyi hapa ni kwamba nia za Mungu katika kuongezea sehemu ya kile Anacho na Alicho na werevu wake kwa mwanadamu ilikuwa ni ili mwanadamu aweze kuwa kiumbe hai anayemdhihirisha Yeye. Kwa kiumbe hai kama huyo kufanya mambo hayo kwa niaba Yake, ilikuwa ndicho hasa kile ambacho Mungu alikuwa akitamani kuona.
3. Mungu Awatengenezea Adamu na Hawa Nguo za Ngozi
Mwa 3:20-21 Adamu akampa mke wake jina la Hawa; kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa mama ya wote wenye uhai. Pia Yehova Mungu akawatengenezea Adamu na mke wake nguo za ngozi; na akawavisha.
Hebu tuangalie kifungu hiki cha tatu, kinachosema kwamba, kuna maana katika jina ambalo Adamu alimpa Hawa, sivyo? Hii inaonyesha kwamba baada ya kuumbwa, Adamu alikuwa na fikira zake na alielewa mambo mengi. Lakini kwa sasa, hatutasoma na kuchunguza kile alichoelewa au kwa kiwango kipi alielewa kwa sababu hiyo si hoja kuu Ninayotaka kuzungumzia kwenye kifungu hiki cha tatu. Kwa hivyo, ni hoja gani iliyo kuu Ninayotaka kuzungumzia? Hebu tuangalie mstari huu, “Pia Yehova Mungu akawatengenezea Adamu na mke wake nguo za ngozi; na akawavisha.” Kama hatutakuwa na ushirika kuhusu mstari huu wa maandiko ya leo, huenda hamtawahi kutambua uzito uliopo katika maneno haya. Kwanza, hebu niwape vidokezo fulani. Jaribu kufikiria na uvute picha ya Bustani ya Edeni, Adamu na Hawa wakiwa wanaishi ndani yake. Mungu anaenda kuwatembelea lakini wanajificha kwa sababu wako uchi. Mungu hawezi kuwaona, na baada ya kuwaita wao, wanasema, “Hatuwezi kuthubutu kukuona kwa sababu tuko uchi.” Hawathubutu kumwona Mungu kwa sababu wako uchi. Kwa hivyo, Yehova Mungu anawafanyia nini? Maandishi ya awali yanasema: “Yehova Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, na Akawavisha.” Kutokana na hili, je, mnaelewa kile ambacho Mungu alitumia kuwatengenezea nguo zao? Mungu alitumia ngozi za wanyama kutengeneza nguo zao. Hivyo ni kusema, nguo ambazo Mungu aliwatengenezea binadamu zilikuwa za koti la manyoya. Hizi zilikuwa ndizo nguo za kwanza ambazo Mungu alizitengeneza kwa ajili ya mwanadamu. Koti la manyoya ni mavazi ya bei ghali kwa viwango vya leo, kitu ambacho si kila mtu anaweza kumudu kuvaa. Kama mtu atakuuliza: Kipande cha kwanza cha nguo zilizovaliwa na mababu wa wanadamu kilikuwa ni kipi? Unaweza kujibu: Kilikuwa ni koti la manyoya. Ni nani aliyetengeneza koti hilo la manyoya? Unaweza kujibu zaidi: Ni Mungu ndiye Aliyetengeneza! Hilo ndilo jambo kuu hapa: Nguo hii ilitengenezwa na Mungu. Je, hilo si jambo linalofaa kujadiliwa? Baada ya kusikia maelezo Yangu, je, umepata picha akilini mwako? Unapaswa angalau kuwa na ufahamu wa juujuu kuihusu. Dhumuni la kuwaambia haya leo si kuwafahamisha kuhusu kipande cha kwanza cha nguo ya mwanadamu ilikuwa ni nini. Kwa hivyo, lengo ni lipi? Lengo kuu si lile koti la manyoya, lakini ni jinsi watu wanavyoweza kuja kujua—kama ilivyofichuliwa na Mungu katika kile Alichokifanya hapa—tabia Yake, kile Anacho, na Alicho.
“Pia Yehova Mungu akawatengenezea Adamu na mke wake nguo za ngozi; na akawavisha.” Katika tukio hili, ni nafasi ya aina gani ambayo tunamwona Mungu akiichukua Anapokuwa na Adamu na Hawa? Na je,ni kwa njia gani Mungu anajidhihirisha Mwenyewe katika ulimwengu huu, akiwa na wanadamu wawili tu? Je, Anasimama Mwenyewe katika nafasi ya Mungu? Kaka na dada kutoka Hong Kong, tafadhali jibuni. (Anasimama kama mzazi.) Kaka na dada kutoka Korea Kusini, je, ni nafasi ya aina gani ambayo mnafikiria kwamba Mungu anaichukua hapa? (Kiongozi wa familia.) Kaka na dada kutoka Taiwan, je, mnafikiria nini? (Anasimama nafasi ya mtu aliyepo katika familia ya Adamu na Hawa, nafasi ya mwanafamilia.) Baadhi yenu mnafikiria kuwa Mungu anasimama kama mwanafamilia wa Adamu na Hawa, huku wengine wanasema kwamba Mungu anasimama kama kiongozi wa familia na wengine wanasema kwamba Anasimama kama mzazi. Haya yote yanafaa sana. Lakini ni nini hasa Ninachotilia mkazo hapa? Mungu aliwaumba watu hawa wawili na Aliwachukulia kama wandani Wake. Akiwa kama mwanafamilia wao wa pekee, Mungu aliyaangalia maisha yao, na pia Alikidhi mahitaji yao ya msingi. Hapa, Mungu anasimama kama mzazi wa Adamu na Hawa. Wakati Mungu akifanya haya, binadamu haoni jinsi ambavyo Mungu ni mkuu; haoni mamlaka ya juu zaidi ya Mungu, uajabu Wake, na hata zaidi haoni hasira au uadhama Wake. Kile anachoona tu ni unyenyekevu wa Mungu, upendo Wake, Anavyowajali wanadamu, na jukumu Lake na utunzaji Wake kwake. Mtazamo na njia ambayo Mungu aliwatendea Adamu na Hawa ni sawa na jinsi ambavyo wazazi wanawajali watoto wao. Ni kama pia jinsi wazazi wanavyowapenda, kuwaangalia, na kuwatunza watoto wao wenyewe wa kiume na wa kike—kiuhalisia, kwa namna ya kuonekana, na kushikika. Badala ya kujiweka katika nafasi Yake ya juu na ya ukuu, Mungu mwenyewe alitumia ngozi kutengeneza vazi la binadamu. Haijalishi kama koti hili la manyoya lilitumika kufunika utupu wao au wao kujikinga dhidi ya baridi. Kilicho muhimu ni kwamba, vazi hili lililotumika kuufunika mwili wa binadamu lilitengenezwa na Mungu binafsi kwa mikono Yake mwenyewe. Badala ya kuitengeneza tu kupitia fikira au kwa mbinu za kimiujiza kama watu wanavyofikiria, Mungu kwa halali alikuwa Amefanya jambo ambalo mwanadamu anafikiria kwamba Mungu hawezi na hapaswi kufanya. Hili linaweza kuwa jambo rahisi—ambalo hata baadhi ya watu wanaweza wasifikirie kwamba linastahili kutajwa—lakini linamruhusu mfuasi yeyote wa Mungu ambaye alikuwa amejawa na mawazo yasiyoeleweka kumhusu Yeye, kuweza kupata utambuzi wa uhalisi na uzuri Wake, na kuona uaminifu na unyenyekevu Wake. Inawafanya watu wenye kiburi kupindukia wanaofikiri kuwa wako juu na wana nguvu, kuinamisha vichwa vyao vya majivuno kwa aibu mbele ya ukweli na unyenyekevu wa Mungu. Hapa, ukweli na unyenyekevu wa Mungu unawawezesha zaidi watu kuona jinsi ambavyo Anapendeza. Kinyume chake, yule Mungu “mkuu sana”, Mungu “anayependwa” na Mungu “mwenye nguvu zote” ambaye watu wanamshikilia katika mioyo yao, amekuwa mdogo sana, asiyevutia, na mdhaifu. Unapoona sentensi hii na kusikia hadithi hii, je, unamdharau Mungu kwa sababu Alifanya jambo kama hilo? Baadhi ya watu wanaweza kufanya hivyo, lakini wengine watakuwa na mwitikio tofauti. Watafikiri kwamba Mungu ni wa kweli na wa kupendwa, na hasa ni ule ukweli na uzuri wa Mungu ndio unaowasukuma. Kadiri wanavyoona upande halisi wa Mungu, ndivyo wanavyoweza kuthamini zaidi uwepo wa kweli wa upendo wa Mungu, umuhimu wa Mungu mioyoni mwao, na jinsi ambavyo Anasimama kando yao kila wakati.
Kwa sasa, wacha tuhusishe mazungumzo yetu na ya wakati huu. Kama Mungu aliweza kufanya mambo haya madogo tofauti kwa binadamu Aliowaumba hapo mwanzo kabisa, hata vitu vingine ambavyo watu hawangethubutu kamwe kuvifikiria ama kuvitarajia, basi je, Mungu anaweza kuwafanyia watu wa leo mambo kama hayo? Baadhi ya watu wanasema, “Ndiyo!” Kwa nini ni hivyo? Kwa sababu kiini cha Mungu si bandia, uzuri Wake si bandia. Kwa sababu kiini cha Mungu kwa kweli kipo, na si kitu kilichoongezwa tu na wengine, na bila shaka si kitu ambacho kinabadilika kulingana na wakati, mahali, na enzi. Ukweli na uzuri wa Mungu unaweza kwa kweli kuonyeshwa kupitia kufanya jambo ambalo watu wanafikiria si la kipekee na ni dogo, jambo ambalo ni dogo sana kiasi cha kwamba watu hawawezi hata kufikiria kama Angeweza kulifanya. Mungu si mnafiki. Hakuna kutia chumvi, kufunika ukweli, majivuno au kiburi katika tabia na kiini Chake. Siku zote Hajigambi, lakini badala yake Anawapenda, Anaonyesha hali ya kuwajali, Anawaangalia, na kuwaongoza wanadamu Aliowaumba kwa uaminifu na kwa dhati. Haijalishi ni kiwango kipi ambacho watu wanaweza kuthamini, kuhisi, au kuona, Mungu kwa hakika anafanya mambo haya. Je, kujua kwamba Mungu anacho kiini kama hicho kutaweza kuathiri upendo wa watu Kwake? Je, kutaweza kushawishi namna wanavyomcha Mungu? Ninatumai utakapoelewa upande halisi wa Mungu utaweza kuwa hata karibu zaidi na Yeye na kuweza kuthamini hata zaidi na kwa kweli upendo Wake na utunzaji Wake kwa wanadamu, huku wakati huohuo pia ukimpa moyo wako na kutowahi tena kuwa na shaka au wasiwasi wowote Kwake. Mungu anafanya kimyakimya kila kitu kwa ajili ya binadamu, akifanya kimyakimya kupitia ukweli, uaminifu, na upendo Wake. Lakini siku zote Hana hofu au majuto yoyote kwa yale yote Anayofanya, wala hahitaji mtu yeyote amlipe Yeye kwa njia yoyote au kuwa na nia za kuwahi kupokea kitu kutoka kwa wanadamu. Dhumuni tu la kila kitu Alichowahi kufanya ni ili Aweze kupokea imani na upendo wa kweli kutoka kwa wanadamu. Hebu tuhitimishe mada hii ya kwanza hapa.
Je, mazungumzo haya yamewasaidia? Yamewasaidia kwa kiasi gani? (Tuna uelewa na maarifa zaidi kuhusu upendo wa Mungu.) (Mbinu hii ya ushirika inaweza kutusaidia katika siku zijazo kuthamini vyema neno la Mungu, kufahamu hisia Alizokuwa nazo na maana ya mambo Aliyoyasema wakati Alipoyasema, na kuhisi kile Alichohisi kwa wakati huo.) Je, yupo yeyote kati yenu anayehisi hata zaidi uwepo halisi wa Mungu baada ya kuyasoma maneno haya? Je, mnahisi uwepo wa Mungu si mtupu wala wa kutiliwa mashaka tena? Mara tu unapokuwa na hisia hii, je, utaweza kuhisi kwamba Mungu yupo kando yako? Pengine hisia hiyo si dhahiri kwa sasa au huenda bado hutaweza kuihisi kwa sasa. Lakini siku moja, utakapokuwa na ufahamu wa kina na wakweli na maarifa halisi kuhusu tabia na kiini cha Mungu ndani ya moyo wako, utahisi kwamba Mungu yupo kando yako—ni vile tu kwamba haujawahi kumkubali Mungu kwa kweli ndani ya moyo wako. Haya ni halisi.
Je, mna maoni gani kuhusu mbinu hii ya ushirika? Je, mnaweza kuendana nayo? Je, mnafikiri ushirika wa aina hii kuhusu mada ya kazi ya Mungu na tabia ya Mungu ni nzito sana? Je, mnajisikiaje? (Vizuri sana, kusisimka.) Ni nini kilichokufanya ujisikie vizuri? Kwa nini ulisisimka? (Ilikuwa ni sawa na kurudi kwenye Bustani ya Edeni, kurudi kuwa kando na Mungu.) “Tabia ya Mungu” kwa kweli ni mada ambayo haijazoeleka sana na kila mmoja, kwa sababu kile ambacho unafikiria kwa kawaida, kile unachosoma kwenye vitabu au kusikia kwenye ushirika, siku zote inakufanya ujihisi kama mtu asiyeona akimgusa ndovu—unahisi tu kila mahali kwa kutumia mikono yako, lakini kwa hakika huoni chochote kwa macho yako. “Kupapasa-papasa” hakuwezi kukupa hata uelewa wa juu juu kuhusu Mungu, licha ya maudhui ya wazi kuhusu Yeye. Kile ambacho itakupatia zaidi ni mawazo, yatakayokuzuia kufafanua kwa usahihi tabia na kiini cha Mungu ni nini, na kutokuwa na uhakika kunakotokana na mawazo yako daima kutaujaza moyo wako na mashaka. Wakati ambapo huwezi kuwa na uhakika kuhusu kitu na ilhali bado unajaribu kukielewa, ndani ya moyo wako bado siku zote kutaendelea kuwa na mambo yanayopingana na kukinzana, na hata hali ya kusumbuliwa, ukiachwa ukiwa umepotea na kuchanganyikiwa. Je, si jambo la kusikitisha sana unapotaka kumtafuta Mungu, kumjua Mungu, na kumwona Yeye waziwazi, lakini siku zote huwezi kupata majibu? Bila shaka, maneno haya yanalengwa kwa wale wanaotamani kutafuta kumcha Mungu na kumridhisha Mungu. Kwa wale watu ambao hawatilii maanani mambo kama haya, hili kwa hakika si muhimu, kwa sababu kile wanachotumaini zaidi ni kwamba uhalisi na uwepo wa Mungu ni hadithi za kale au ni dhana tu, ili waweze kufanya chochote wanachotaka, ili waweze kuwa wakubwa zaidi na wenye umuhimu zaidi, ili waweze kufanya vitendo viovu bila kujali matokeo yake, ili wasilazimike kukabiliana na adhabu au kupata kuwajibishwa kokote, na ili hata mambo ambayo Mungu anasema kuhusu watu waovu hayataweza kuwahusu wao. Watu hawa hawako tayari kuifahamu tabia ya Mungu. Wanachukia kujaribu kumjua Mungu na kila kitu kuhusu Yeye. Wanapendelea kwamba Mungu asingekuwepo. Watu hawa wanampinga Mungu, na wao ni miongoni mwa wale ambao wataondolewa.
Kisha, tutazungumzia hadithi ya Nuhu na namna ambavyo inahusiana na mada ya kazi ya Mungu, tabia ya Mungu na Mungu Mwenyewe.
Mnaona Mungu akimfanyia nini Nuhu kwenye sehemu hii ya maandiko? Pengine kila mmoja aliyeketi hapa anajua kitu kuhusu hayo baada ya kusoma maandiko: Mungu alimfanya Nuhu ajenge safina, kisha Mungu akatumia gharika kuuangamiza ulimwengu. Mungu alimgiza Nuhu ajenge safina ili kuokoa familia yake ya watu wanane, ambayo iliwawaruhusu waweze kunusurika, ili wawe mababu wa kizazi kifuatacho cha wanadamu. Sasa hebu tuyasome maandiko.
B. Nuhu
1. Mungu Anuia Kuuangamiza Ulimwengu kwa Gharika na Amwagiza Nuhu Kuijenga Safina
Mwa 6:9-14 Hivi ni vizazi vyake Nuhu: Nuhu alikuwa mtu mwenye haki na mtimilifu katika vizazi vyake, naye Nuhu alitembea na Mungu. Naye Nuhu akapata watoto watatu wa kiume, Shemu, Hamu, na Yafethi. Dunia pia ilikuwa potovu mbele za Mungu, nayo dunia ilijaa vurugu. Naye Mungu akaiangalia dunia, na, tazama, ilikuwa imepotoka; kwa sababu kila aliye na mwili alikuwa amejipotoshea njia yake duniani. Naye Mungu akasema kwake Nuhu, Mwisho wa wote walio na mwili umefika mbele Zangu; kwa kuwa dunia imejawa na vurugu kupitia kwao; na, tazama, nitawaangamiza pamoja na dunia. Ujitengenezee safina ya mbao wa mvinje; utatengeneza vyumba ndani ya safina, na uipake lami ndani na nje.
Mwa 6:18-22 Lakini na wewe nitaliimarisha agano Langu; na utaingia ndani ya safina, wewe, na wana wako, na mke wako, na wake zao wana wako pamoja na wewe. Na kwa kila kilicho na uhai chenye mwili, utawaleta wawili wa kila aina katika safina, kuwaweka hai pamoja nawe; watakuwa wa kiume na wa kike. Kila ndege arukaye kwa aina yake, na mifugo kwa aina yake, kila kinachotambaa duniani kwa aina yake, wawili wa aina yote watakuja kwa wewe, ili uwaweke hai. Na ujichukulie chakula cha kila aina kinacholika, nawe ukikusanye kwako; na kitakuwa kwa ajili ya chakula cha ninyi, na cha wao. Nuhu alifanya hivyo; kulingana na vyote ambavyo Mungu alimwamrisha, alifanya hivyo.
Je, sasa mna uelewa wa jumla kuhusu Nuhu ni nani baada ya kusoma vifungu hivi viwili? Je, Nuhu ni mtu wa aina gani? Maandiko asili yanasema: “Nuhu alikuwa mtu mwenye haki na mtimilifu katika vizazi vyake.” Kulingana na uelewa wa watu wa sasa, ni mtu wa aina gani aliyekuwa “mtu mwenye haki” kwa siku hizo? Mtu mwenye haki anapaswa kuwa mtu mkamilifu. Je, mnajua kama mtu huyu mkamilifu alikuwa ni mkamilifu machoni pa mwanadamu au ni mkamilifu machoni pa Mungu? Bila shaka, mtu huyu mkamilifu alikuwa mtu mkamilifu machoni pa Mungu na wala si machoni pa mwanadamu. Haya yote ni kweli! Hii ni kwa sababu binadamu ni kipofu na hawezi kuona, ni Mungu tu ndiye Anayeitazama dunia yote na kila mmoja, na ni Mungu tu ndiye Aliyejua Nuhu alikuwa ni mtu mkamilifu. Kwa hivyo, mpango wa Mungu wa kuuangamiza ulimwengu kwa gharika ulianza pindi tu Alipomuita Nuhu.
Katika enzi hiyo, Mungu alinuia kumuita Nuhu ili afanye kitu cha muhimu sana. Kwa nini ilikuwa lazima Afanye hivyo? Kwa sababu Mungu alikuwa na mpango katika moyo Wake kwa wakati huo. Mpango Wake ulikuwa ni kuuangamiza ulimwengu kwa gharika. Kwa nini Auangamize ulimwengu? Maandiko yanasema hivi: “Dunia pia ilikuwa potovu mbele za Mungu, nayo dunia ilijaa vurugu.” Je, mnaona nini kutoka kwenye kauli “dunia ilijaa vurugu”? Ni ajabu duniani wakati ulimwengu na watu wake wanapotoka kupindukia, kwa hivyo: “dunia ilijaa vurugu.” Katika lugha ya leo, “ilijaa vurugu” inamaanisha kila kitu hakiko katika mpangilio. Kwa binadamu, inamaanisha kwamba katika nyanja zote za maisha hakuna mpangilio, na kwamba kila kitu kilikuwa kimechafuka na kisichoweza kudhibitiwa. Machoni pa Mungu, inamaanisha watu wa ulimwengu wamepotoka sana. Je, wamepotoka hadi kiwango gani? Wamepotoka hadi kiwango ambacho Mungu hawezi tena kuvumilia kuangalia na Hawezi tena kuwa na subira kuhusu hali hiyo. Wamepotoka hadi kiwango ambacho Mungu anaamua kuwaangamiza. Wakati Mungu alipoamua kuuangamiza ulimwengu, Alipanga kupata mtu wa kuijenga safina. Kisha Mungu akamchagua Nuhu kufanya kitu hicho, ambacho ni kumruhusu Nuhu aijenge safina. Kwa nini Mungu alimchagua Nuhu? Machoni pa Mungu, Nuhu alikuwa ni mtu mwenye haki, na haijalishi kile ambacho Mungu alimwagiza afanye, Nuhu alifanya vile inavyotakiwa. Hio inamaanisha kwamba, Nuhu alikuwa tayari kufanya chochote ambacho Mungu alimwambia afanye. Mungu alitaka kumpata mtu kama huyu ili afanye kazi pamoja na Yeye, ili akamilishe kile alichokuwa Amemwaminia afanye, ili akamilishe kazi Yake hapa duniani. Hapo kabla, je, kulikuwa na mtu mwingine mbali na Nuhu ambaye angeweza kuikamilisha kazi hiyo? Bila shaka hakuna! Nuhu pekee ndiye aliyekuwa mtu ambaye angeweza kukamilisha kile ambacho Mungu alikuwa amemwaminia afanye, na hivyo Mungu alimchagua yeye. Lakini, je, mipaka na viwango vya Mungu vya kuwaokoa watu kwa wakati huo ni sawa na vilivyoko kwa wakati huu? Jibu ni, hakika kuna utofauti! Na kwa nini Nauliza hili? Nuhu pekee ndiye aliyekuwa mwanadamu mwenye haki machoni pa Mungu kwa wakati huo, ambayo inadokeza kwamba watoto wake, mke wake, na wakwe zake wote hawakuwa watu wenye haki, lakini bado Mungu aliwaokoa kwa sababu ya Nuhu. Mungu hakuwawekea matakwa kama Anavyofanya sasa, na badala yake Aliwaacha hai wanachama wote wanane wa familia ya Nuhu. Walipata baraka za Mungu kwa sababu ya Nuhu kuwa mwenye haki. Kama Nuhu asingekuwepo, hakuna yeyote kati yao ambaye angekamilisha kile ambacho Mungu alikuwa Amemwaminia afanye. Kwa hivyo, Nuhu alikuwa ndiye mtu pekee ambaye alipaswa kubaki hai baada ya ulimwengu kuangamizwa kwa wakati huo, na wale wengine walikuwa tu wanufaika wa ziada. Hii inaonyesha kwamba, katika enzi kabla ya Mungu kuanza rasmi kazi Yake ya usimamizi, kanuni na viwango ambavyo Aliwatendea watu na kuwawekea mahitaji vilikuwa vimelegezwa kidogo. Kwa watu wa leo, jinsi ambavyo Mungu aliitendea familia ya Nuhu ya watu wanane inaonekana kuwa haina “haki.” Lakini ikilinganisha na kiwango kikubwa cha kazi ambayo Yeye anaifanya sasa kwa watu, na kiwango kikubwa cha neno Lake analowasilisha sasa, jinsi Mungu alivyoitendea familia ya Nuhu ya watu wanane ilikuwa tu ni kanuni ya kazi Yake kutokana na usuli wa kazi Yake kwa wakati huo. Kwa kulinganisha, je, ni familia ya Nuhu ya watu wanane ndio iliyopokea mengi zaidi kutoka kwa Mungu, au ni watu wa leo?
Kwamba Nuhu aliitwa ni ukweli rahisi, lakini jambo kuu la kile tunachozungumzia—tabia ya Mungu, mapenzi Yake, na kiini Chake katika rekodi hii—si rahisi sana. Ili kuelewa vipengele hivi kadhaa vya Mungu, ni lazima kwanza tuelewe ni mtu wa aina gani ambaye Mungu anatamani kumwita, na kupitia hili, tutaweza kuelewa tabia Yake, mapenzi Yake na kiini Chake. Hili ni muhimu. Kwa hivyo, machoni pa Mungu, huyu mtu ambaye Anamwita ni mtu wa aina gani? Huyu ni lazima awe mtu ambaye anaweza kusikiliza maneno Yake na ambaye anaweza kufuata maagizo Yake. Wakati huo huo, ni lazima pia mtu huyu awe na hisia ya uwajibikaji, mtu ambaye atatekeleza neno la Mungu kwa kulichukulia kama jukumu na wajibu ambao anahitajika kutimiza. Basi je, mtu huyu anahitajika kuwa mtu anayemjua Mungu? Hapana. Kwa wakati huo, Nuhu hakuwa amesikia mafundisho mengi ya Mungu au kupitia kazi yoyote ile ya Mungu. Kwa hivyo, maarifa ya Nuhu kumhusu Mungu yalikuwa kidogo sana. Ingawa imerekodiwa hapa kwamba Nuhu alitembea na Mungu, je, aliwahi kuiona nafsi ya Mungu? Jibu ni bila shaka hapana! Kwa sababu katika siku hizo, ni wajumbe wa Mungu tu ndio waliokuja kati ya watu. Ingawa waliweza kumwakilisha Mungu katika kunena na kufanya mambo, walikuwa tu wakiwasilisha mapenzi Yake na nia Zake. Nafsi ya Mungu haikufichuliwa kwa binadamu uso kwa uso. Katika sehemu hii ya maandiko, yote tunayoona kimsingi ni kile ambacho Nuhu alipaswa kufanya na maagizo ya Mungu kwake yalikuwa ni yapi. Kwa hivyo ni kiini kipi kilichoonyeshwa na Mungu hapa? Kila kitu anachofanya Mungu kimepangiliwa kwa uhakika. Anapoona jambo au hali inapotokea, kutakuwa na kiwango cha kulipima jambo hilo katika macho Yake, na kiwango hiki kitaamua kama Ataanza mpango wa kulishughulikia au namna ya kuchukulia jambo na hali hiyo. Yeye si asiyejali au Asiye na hisia kwa kila kitu. Kwa hakika ni kinyume kabisa. Kuna mstari hapa ambao Mungu alimwambia Nuhu: “Mwisho wa wote walio na mwili umefika mbele Zangu; kwa kuwa dunia imejawa na vurugu kupitia kwao; na, tazama, nitawaangamiza pamoja na dunia.” Mungu aliposema hivi, je, Alimaanisha kuwa angewaangamiza wanadamu pekee? La! Mungu Alisema kwamba Angeangamiza viumbe vyote vilivyo hai vyenye mwili. Ni kwa nini Mungu alitaka kuviangamiza? Kuna ufunuo mwingine wa tabia ya Mungu hapa: Machoni pa Mungu, kuna kikomo cha uvumilivu Wake kwa upotovu wa mwanadamu, kwa uchafu, dhuluma, na uasi wa kila mwenye mwili. Je, ukomo Wake ni upi? Ni kama vile Mungu alivyosema: “Mungu akaiangalia dunia, na, tazama, ilikuwa imepotoka; kwa sababu kila aliye na mwili alikuwa amejipotoshea njia yake duniani.” Je, kauli hii “kwa sababu kila aliye na mwili alikuwa amejipotoshea njia yake duniani” inamaanisha nini? Inamaanisha kwamba viumbe vyote vilivyo hai, ikiwa ni pamoja na wale waliomfuata Mungu, wale walioliita jina la Mungu, wale waliowahi kutoa sadaka za kuteketezwa kwa Mungu, wale waliomtambua Mungu kwa vinywa vyao na hata kumsifu Mungu—mara tu tabia zao zilipojaa upotovu na kufikia macho ya Mungu, basi Angelazimika kuwaangamiza. Huo ulikuwa ukomo wa Mungu. Kwa hivyo, ni hadi kiwango gani ambapo Mungu alibaki kuwa mvumilivu kwa mwanadamu na kwa upotovu wa wenye mwili wote? Hadi kufikia kiwango ambacho watu wote, wawe wafuasi wa Mungu au wasioamini, walikuwa hawatembei katika njia sahihi. Hadi kiwango ambacho binadamu alikuwa hajapotoshwa tu katika maadili na kujawa na maovu, lakini hadi pale ambapo hapakuwa na mtu yeyote ambaye aliamini kuwa Mungu yupo, achilia mbali mtu yeyote ambaye aliamini kuwa ulimwengu unatawaliwa na Mungu na kwamba Mungu anaweza kuwaletea watu nuru na njia sahihi. Hadi kiwango ambacho binadamu aliudharau uwepo wa Mungu, na hakumruhusu Mungu kuwepo. Mara tu upotovu wa mwanadamu ulipofikia kiwango hiki, Mungu asingeweza tena kuvumilia. Je, ni nini ambacho kingechukua nafasi ya hilo? Kuja kwa ghadhabu ya Mungu na adhabu ya Mungu. Je, huo haukuwa ufunuo kiasi wa tabia ya Mungu? Katika enzi hii ya sasa, je, bado yupo binadamu mwenye haki machoni pa Mungu? Je, bado yupo binadamu mkamilifu machoni pa Mungu? Je, enzi hii ndiyo ile ambayo tabia ya wenye mwili wote duniani imepotoka machoni pa Mungu? Katika siku na enzi hii, mbali na wale ambao Mungu anataka kuwakamilisha, wale wanaoweza kumfuata Mungu na kuukubali wokovu Wake, je, hawapimi kikomo cha uvumilivu wa Mungu? Je, kila kitu kinachotokea kando yenu, kila mnachokiona kwa macho yenu, na kusikia kwa masikio yenu, na kupitia ninyi wenyewe kila siku katika ulimwengu huu—si kimejaa vurugu? Machoni pa Mungu, je, ulimwengu kama huu, enzi kama hii, haipaswi kukomeshwa? Ingawa usuli wa enzi ya sasa ni tofauti kabisa na usuli wa enzi ya Nuhu, hisia na ghadhabu Aliyo nayo Mungu kwa kupotoka kwa binadamu inabakia vilevile sawa na ilivyokuwa kwa wakati huo. Mungu anaweza kuwa mvumilivu kwa sababu ya kazi Yake, lakini kulingana na mambo na hali, ulimwengu huu ulipaswa kuangamizwa zamani sana machoni pa Mungu. Hali imepitiliza zaidi ya vile ilivyokuwa wakati ulimwengu ulipoangamizwa kwa gharika. Lakini tofauti ni ipi? Hili ndilo jambo jingine linalohuzunisha moyo wa Mungu zaidi, na pengine kitu ambacho hakuna yeyote kati yenu anayeweza kutambua.
Wakati alipokuwa Akiuangamiza ulimwengu kwa gharika, Mungu aliweza kumwita Nuhu ili aijenge safina na kufanya baadhi ya kazi za matayarisho. Mungu aliweza kumwita mtu mmoja—Nuhu—ili afanye mfululizo wa mambo kwa ajili Yake. Lakini katika enzi hii ya sasa, Mungu hana mtu yeyote wa kumuita. Kwa nini ipo hivyo? Kila mmoja aliyeketi hapa pengine anaweza kuelewa na kujua sababu vizuri sana. Je, mngependa Niweze kuiweka wazi? Kuitaja kwa sauti huenda ikawafanya mhisi aibu na kumfanya kila mmoja akasirike. Baadhi ya watu wanaweza kusema: “Ingawa sisi si watu wenye haki na wala sisi si watu wakamilifu machoni pa Mungu, kama Mungu atatuelekeza sisi kufanya kitu, bado tutaweza kukifanya. Hapo awali, Aliposema maafa makubwa yanakuja, tulianza kuandaa chakula na vitu ambavyo vingehitajika wakati wa maafa. Je, haya yote hayakufanywa kulingana na matakwa ya Mungu? Je, kwa kweli hatukuwa tukishirikiana na kazi ya Mungu? Je, mambo haya tuliyofanya hayawezi kulinganishwa na yale aliyofanya Nuhu? Je, kufanya kile tulichofanya si utiifu wa kweli? Je, hatukuwa tunafuata maagizo ya Mungu? Je, hatukufanya kile ambacho Mungu alisema kwa sababu tuna imani katika maneno ya Mungu? Basi ni kwa nini Mungu bado ana huzuni? Kwa nini Mungu anasema Hana mtu wa kumwita?” Je, kuna tofauti yoyote kati ya vitendo vyenu na vile vya Nuhu? Tofauti ni nini? (Kutayarisha chakula leo kwa ajili ya janga kulikuwa nia yetu wenyewe.) (Matendo yetu hayawezi kufikia yale ya “haki,” ilhali Nuhu alikuwa ni mtu mwenye haki machoni pa Mungu.) Kile mlichosema hakiko mbali sana na ukweli. Kile alichofanya Nuhu ni tofauti sana kulingana na kile ambacho watu wanafanya sasa. Wakati Nuhu alipofanya kama vile Mungu alivyomwagiza hakujua nia za Mungu zilikuwa ni nini. Hakujua ni nini ambacho Mungu Alitaka kukamilisha. Mungu alikuwa amempa tu amri, Akamwagiza afanye kitu, na bila ya maelezo mengi, Nuhu aliendelea mbele na kukifanya. Hakujaribu kuelewa kwa siri nia za Mungu zilikuwa ni nini, wala hakumpinga Mungu au kukosa uaminifu. Alienda tu na kuifanya ipasavyo kwa moyo safi na rahisi. Chochote ambacho Mungu alimruhusu afanye alifanya, na kutii na kusikiliza neno la Mungu vyote vilikuwa ni imani yake ya kufanya mambo. Hivyo ndivyo alivyoshughulika moja kwa moja na kwa urahisi na kile ambacho Mungu alimwaminia kufanya. Kiini chake—kiini cha vitendo vyake kilikuwa ni utiifu, si kubahatisha, si kupinga, na zaidi ya hayo, si kufikiria kuhusu maslahi yake binafsi na faida zake na hasara zake. Zaidi ya hayo, wakati Mungu aliposema Angeuangamiza ulimwengu kwa gharika, Nuhu hakuuliza ni lini au kuuliza jinsi mambo yatakavyokuwa, na bila shaka hakumwuliza Mungu jinsi ambavyo Angeuangamiza ulimwengu. Alifanya tu kama Mungu alivyomwagiza. Njia yoyote ile ambayo Mungu alitaka safina hiyo iweze kujengwa na hasa ijengwe na nini, alifanya vile ambavyo Mungu alimwambia, na pia alianza kazi mara moja. Alifanya kulingana na maagizo ya Mungu kwa mtazamo wa kutaka kumridhisha Mungu. Je, alikuwa akifanya hivyo ili kujisaidia yeye mwenyewe kuepuka janga? La. Je, alimwuliza Mungu itachukua muda gani zaidi kabla ya ulimwengu kuangamizwa? Hakuuliza. Je, alimwuliza Mungu au alijua ingechukua muda gani kuijenga safina? Hakujua hilo pia. Alitii tu, akasikiliza, na kufanya hivyo inavyohitajika. Watu wa sasa si sawa: Mara tu taarifa fulani inapojitokeza kupitia kwa neno la Mungu, mara tu watu wanapohisi ishara ya kutatizwa au matatizo, wote watachukua hatua mara moja, haijalishi ni nini, au bila kujali gharama, ili kutayarisha kile ambacho watakula, kunywa, na kutumia baada ya janga kupita, hata kupanga njia za wao kutoroka wakati janga litakapotokea. La kuvutia hata zaidi ni kwamba, wakati huu muhimu, akili za binadamu ni nzuri sana katika “kukamilisha kazi.” Katika hali ambazo Mungu hajatoa maagizo yoyote, binadamu anaweza kupanga kila kitu kwa njia inayofaa. Mnaweza kutumia neno “sahihi” ili kuielezea. Na kuhusiana na kile ambacho Mungu anasema, nia za Mungu ni nini, au kile ambacho Mungu anataka ni nini, hakuna anayejali na hakuna anayejaribu kuzitambua. Je, hii siyo tofauti kubwa zaidi kati ya watu wa leo na Nuhu?
Katika rekodi hii ya hadithi ya Nuhu, je, mnaona sehemu ya tabia ya Mungu? Kuna ukomo kwa subira ya Mungu kwa upotovu, uchafu, na dhuluma ya mwanadamu. Anapofikia kikomo hicho, Hatawahi tena kuwa na subira na badala yake Ataanza usimamizi Wake mpya na mpango mpya, kuanza kufanya kile ambacho lazima Afanye, kufichua matendo Yake na upande ule mwingine wa tabia Yake. Hiki kitendo Chake si cha kuonyesha kwamba lazima Asiwahi kamwe kukosewa na binadamu au kwamba Amejawa na mamlaka na ghadhabu, na wala si kuonyesha kwamba Anaweza kuwaangamiza binadamu. Ni kwamba tabia Yake na kiini Chake kitakatifu hakiwezi tena kuruhusu zaidi, hakiwezi tena kuwavumilia zaidi binadamu wa aina hii waishi mbele Zake, kuishi chini ya utawala Wake. Hivyo ni kusema, wakati wanadamu wote wako dhidi Yake, wakati hakuna mtu yeyote Anayeweza kumwokoa katika ulimwengu mzima, Hatakuwa tena na subira kwa binadamu kama hawa, na Ataweza, bila mashaka yoyote, kutekeleza mpango Wake—kuangamiza binadamu wa aina hii. Kitendo kama hicho cha Mungu kinaamuliwa na tabia Yake. Haya ni matokeo ya lazima, na matokeo ambayo kila kiumbe aliyeumbwa chini ya utawala wa Mungu lazima ayachukue. Je, haya hayaonyeshi kwamba katika enzi ya sasa, Mungu hawezi kusubiri kuukamilisha mpango Wake na kuwaokoa watu Anaotaka kuwaokoa? Katika hali hizi, je, Mungu anajali kuhusu nini zaidi? Sio jinsi wale wasiomfuata Yeye kabisa au wale wanaompinga Yeye, wanavyomtendea au kumpinga Yeye, au jinsi ambavyo mwanadamu anamkashfu Yeye. Anajali tu kuhusu kama wale wanaomfuata Yeye, walengwa wa wokovu Wake katika mpango Wake wa usimamizi, wamekamilishwa na Yeye, na kama wamestahili kuridhika Kwake. Na kuhusiana na wale watu wengine mbali na wale wanaomfuata Yeye, Anawatolea tu adhabu kidogo mara kwa mara ili kuonyesha ghadhabu Yake. Kwa mfano; tsunami, matetemeko ya ardhi, milipuko ya volkano, na kadhalika. Wakati huo huo, pia Anawalinda na kuwaangalia kwa dhati wale wanaomfuata Yeye na ambao wako karibu kuokolewa na Yeye. Tabia ya Mungu ni hii: Kwa upande mmoja, Anaweza kuwa na subira na uvumilivu mwingi kwa watu Anaokusudia kuwakamilisha, na Anaweza kuwasubiria kwa muda mrefu Anavyoweza; kwa upande mwingine, Mungu anawachukia na kuchukizwa kwa dhati na watu wa aina ya Shetani ambao hawamfuati na wanampinga Yeye. Ingawa Hajali kama hawa watu wa aina ya Shetani wanamfuata au wanamwabudu Yeye, bado Anawachukia huku Akiwa na subira kwao katika moyo Wake, na huku Akiamua mwisho wa watu hawa wa aina ya Shetani, Yeye pia anasubiria kufika kwa hatua za mpango Wake wa usimamizi.
Hebu tuangalie kifungu kinachofuata.
2. Baraka za Mungu kwa Nuhu Baada ya Gharika
Mwa 9:1-6 Naye Mungu akawabariki Nuhu na wana wake, na akasema kwao, Ninyi Zaeni, na muongezeke, na muijaze tena dunia. Na wanyama wote wa dunia watawaogopa na kuwa na hofu nanyi, na ndege wote wa angani, na vyote vitembeavyo duniani, na kila samaki wa baharini; wamewekwa katika mikono yenu. Kila kisongacho kilicho na uhai kitakuwa chakula chenu, jinsi ambavyo nimewapa mboga ndivyo ninavyowapa vitu vyote. Lakini nyama iliyo na uhai, ambayo ni damu yake, ninyi msiile. Na bila shaka nitahitaji damu yenu ya uhai wenu, nitaihitaji kwa mkono wa kila mnyama, na kwa mkono wa mwanadamu, nitahitaji uhai wa mwanadamu kwa mkono wa ndugu wa kila mwanadamu. Yeyote ambaye atamwaga damu ya mwanadamu, damu yake itamwagika na mwanadamu: kwa kuwa Mungu alimfanya mwanadamu kwa mfano Wake.
Ni nini mnachoona katika kifungu hiki? Kwa nini Nikachagua mistari hii? Kwa nini Sikuchukua dondoo kuhusu Nuhu na maisha ya familia yake kwenye safina? Kwa sababu maelezo hayo hayana uhusiano mwingi na mada ambayo tunashiriki leo. Kile tunachozingatia hasa ni tabia ya Mungu. Kama mnataka kujua kuhusu maelezo hayo, basi mnaweza kuchukua Biblia ili muweze kujisomea wenyewe. Hatutazungumzia hilo hapa. Kitu kikuu tunachozungumzia leo ni kuhusu namna ya kujua matendo ya Mungu.
Baada ya Nuhu kukubali maagizo ya Mungu na kujenga safina na kuishi katika siku zile ambazo Mungu alitumia gharika ili kuangamiza ulimwengu, familia yake yote ya watu wanane ilinusurika. Mbali na familia ya Nuhu ya watu wanane, wanadamu wote waliangamizwa, na viumbe vyote vilivyokuwa hai duniani viliangamizwa. Kwa Nuhu, Mungu alimpa baraka, na Akasema baadhi ya mambo kwake na kwa watoto wake. Mambo haya yalikuwa yale ambayo Mungu alikuwa amempa na pia ni baraka Zake kwake. Hizi ndizo baraka na ahadi ambazo Mungu anampa yule ambaye anaweza kumsikiliza Yeye na kuyakubali maagizo Yake, na pia namna Anavyowathawabisha watu. Hivi ni kusema, haijalishi kama Nuhu alikuwa binadamu mkamilifu au alikuwa binadamu mwenye haki machoni pa Mungu, na haijalishi ni kiwango kipi alichomjua Mungu, kwa ufupi, Nuhu na watoto wake wa kiume watatu wote waliyasikiliza maneno ya Mungu, walishirikiana na kazi ya Mungu, na kufanya kile ambacho walipaswa kufanya kulingana na maagizo ya Mungu. Kutokana na hayo, walimsaidia Mungu kuweza kubakiza binadamu na aina mbalimbali za viumbe walio na uhai baada ya kuangamizwa kwa ulimwengu na gharika, na hivyo wakawa wamefanya mchango mkubwa kwa hatua iliyofuata ya mpango wa usimamizi wa Mungu. Kwa sababu ya kila kitu alichokuwa amefanya, Mungu alimbariki. Pengine kwa watu wa leo, kile alichofanya Nuhu hakikuwa sana na thamani ya kutajwa. Wengine wanaweza hata kufikiria: “Nuhu hakufanya chochote; Mungu alikuwa ameamua akilini Mwake kumwacha, kwa hivyo bila shaka angeokolewa. Kubaki kwake si kwa sababu ya mambo aliyokamilisha mwenyewe. Hili ndilo jambo ambalo Mungu alitaka lifanyike, kwa sababu mwanadamu hafanyi chochote.” Lakini hicho sicho ambacho Mungu alikuwa anafikiria. Kwa Mungu, haijalishi kama mtu ni mkubwa au asiye wa maana, mradi tu aweze kumsikiliza Yeye, kutii maagizo Yake na kile anachomwaminia na aweze kushirikiana na kazi Yake, mapenzi Yake, na mpango Wake, ili mapenzi Yake na Mpango Wake viweze kukamilika vizuri, basi mwenendo wake unastahili kukumbukwa na Yeye na kustahili kupokea baraka Zake. Mungu huwathamini watu kama hao; Anathamini matendo yao, na Anathamini uaminifu huu na moyo huu wanaouonyesha Kwake. Huu ndio mtazamo wa Mungu. Hivyo kwa nini Mungu alimbariki Nuhu? Kwa sababu hivi ndivyo Mungu anavyoshughulikia vitendo kama hivyo na utiifu wa mwanadamu.
Kuhusiana na baraka za Mungu kwa Nuhu, baadhi ya watu watasema: “Kama binadamu atamsikiliza Mungu na kumtosheleza Mungu, basi Mungu anapaswa kumbariki mwanadamu.” Je, tunaweza kusema hivyo? Watu wengine wanasema: “Hapana.” Kwa nini hatuwezi kusema hivyo? Baadhi ya watu watasema: “Binadamu hastahili kufurahia baraka za Mungu.” Hilo si sahihi kabisa. Kwa sababu wakati mtu anapokubali kile ambacho Mungu amemwaminia, Mungu anacho kiwango cha kuhukumu kama vitendo vya mtu huyu ni vizuri au vibaya na kama mtu huyu amemtii, na kama mtu huyu ametosheleza mapenzi ya Mungu na kama kile anachofanya kinastahili. Kile anachojali Mungu ni kuhusu moyo wa mtu huyu, si vitendo vyake vya juujuu. Siyo kwamba Mungu anapaswa kumbariki mtu ilimradi tu anafanya jambo fulani, bila kujali jinsi wanavyolifanya. Huku ni kutoelewa kwa watu kumhusu Mungu. Mungu haangalii tu mwisho wa matokeo ya mambo, lakini Anazingatia zaidi kuhusu jinsi moyo wa mtu ulivyo na jinsi mtazamo wa mtu ulivyo wakati wa maendeleo ya mambo, na Anaangalia kama kuna utiifu, uzingatiaji, na tamanio la kumtosheleza Mungu katika mioyo yao. Je, ni kiwango gani ambacho Nuhu alijua kuhusu Mungu kwa wakati huo? Je, kiwango hicho kilikuwa ni kikubwa kama mafundisho ya dini mnayojua sasa? Kuhusu vipengele vya ukweli kama vile dhana na maarifa ya Mungu, je, alipokea unyunyiziaji na uchungaji kama ninyi? La, hakupokea! Lakini kuna ukweli mmoja ambao haupingiki: Katika fahamu, akili, na hata kina cha mioyo ya watu wa leo, dhana zao na mtazamo wao kwa Mungu ni usioeleweka na usio na uhakika. Mnaweza hata kusema kwamba sehemu fulani ya watu inashikilia mtazamo hasi kwa uwepo wa Mungu. Lakini katika moyo wa Nuhu na ufahamu wake, uwepo wa Mungu ulikuwa ni halisi na usio na shaka hata kidogo, na hivyo utiifu wake kwa Mungu ulikuwa haujatiwa doa na ungeweza kustahimili majaribio. Moyo wake ulikuwa safi na wazi kwa Mungu. Hakuhitaji maarifa mengi ya mafundisho ili ajishawishi kufuata kila neno la Mungu, wala hakuhitaji ukweli mwingi kuthibitisha uwepo wa Mungu, ili akubali kile ambacho Mungu alimwaminia na kuweza kufanya chochote kile ambacho Mungu angemruhusu kufanya. Hii ni tofauti muhimu kati ya Nuhu na watu wa leo, na pia ndio ufafanuzi wa kweli wa jinsi mtu mkamilifu alivyo machoni pa Mungu. Kile anachotaka Mungu ni watu kama Nuhu. Yeye ni aina ya mtu anayesifiwa na Mungu, na pia hasa mtu wa aina ile ambaye Mungu anambariki. Je, umepata nuru yoyote kutoka kwa hili? Watu wanawatazama watu kutoka kwa nje, ilhali kile ambacho Mungu anatazama ni mioyo ya watu na kiini chao. Mungu hamruhusu mtu yeyote kuwa na moyo usio na ari au wenye mashaka Kwake, wala Hawaruhusu watu wamshuku au kumjaribu kwa njia yoyote ile. Kwa hivyo, ijapokuwa watu wa leo wako uso kwa uso na neno la Mungu—unaweza hata kusema kwamba wako uso kwa uso na Mungu—kutokana na kitu fulani kilicho ndani ya mioyo yao, kuwepo kwa kiini chao potovu, na mtazamo wao wenye uadui Kwake, watu wamezuiwa kuwa na imani ya kweli kwa Mungu na kuzuiwa kutoka kwa utiifu wao Kwake. Kwa sababu hii, ni vigumu sana kwao kupata baraka ile ile ambayo Mungu alimpa Nuhu.
Kisha, hebu tuangalie sehemu hii ya maandiko kuhusu jinsi Mungu alivyounda upinde wa mvua kama ishara ya Agano lake na binadamu.
3. Mungu Aufanya Upinde wa Mvua Kama Ishara ya Agano Lake na Mwanadamu
Mwa 9:11-13 Na nitaweka agano Langu na ninyi, wala miili yote haitaondolewa tena na maji ya gharika; wala hakutakuwa na gharika tena kuiharibu dunia. Naye Mungu akasema, Hii ni alama ya agano ambayo naifanya kati ya Mimi na ninyi na viumbe vyote vyenye uhai vilivyo nanyi, kwa vizazi vya kudumu: naweka upinde Wangu mawinguni, na utakuwa alama ya agano kati ya Mimi na dunia.
Watu wengi zaidi wanajua upinde wa mvua ni nini na wamesikia baadhi ya hadithi zinazohusiana na upinde wa mvua. Kuhusiana na hadithi ile ya upinde wa mvua kwenye biblia, baadhi wa watu wanaisadiki, baadhi wanaichukulia tu kama hadithi ya kale, huku wengine hawaisadiki kabisa. Haijalishi ni nini, kila kitu kilichofanyika kuhusiana na upinde wa mvua ndicho kila kitu ambacho Mungu Alifanya hapo awali, na mambo yaliyofanyika katika mchakato wa usimamizi wa Mungu wa binadamu. Mambo haya yamerekodiwa vivyo hivyo katika Biblia. Rekodi hizi hazituelezi kama Mungu alikuwa katika hali gani kwa wakati huo au nia zilizokuwepo katika maneno haya ambayo Mungu aliyasema. Zaidi ya hayo, hakuna anayeweza kutambua kile ambacho Mungu alikuwa akihisi Aliposema maneno hayo. Hata hivyo, hali ya akili ya Mungu kuhusiana na tukio hili lote imefunuliwa katikati ya mistari ya maandiko. Ni kana kwamba fikira Zake kwa wakati huo zimeandikwa katika kurasa kupitia kila neno na sentensi ya neno la Mungu.
Mawazo ya Mungu ndiyo ambayo watu wanapaswa kuyajali na ndiyo ambayo wanapaswa kuwa wakijaribu kujua zaidi. Hii ni kwa sababu mawazo ya Mungu yana uhusiano wa karibu na uelewa wa mwanadamu kuhusu Mungu, na uelewa wa mwanadamu kuhusu Mungu ni kiungo kisichoweza kukosekana katika kuingia kwa mwanadamu katika maisha. Sasa, Mungu alikuwa akifikiria nini wakati mambo haya yalitokea?
Hapo mwanzo, Mungu aliumba binadamu ambao katika macho Yake walikuwa wazuri sana na karibu na Yeye, lakini waliangamizwa kwa gharika baada ya kuasi dhidi Yake. Je, ilimwumiza Mungu kwamba binadamu kama hao walitoweka tu papo hapo hivyo? Bila shaka Aliumizwa! Kwa hivyo, maonyesho Yake kwa maumivu haya yalikuwa nini? Ilirekodiwaje kwenye Biblia? Ilirekodiwa kwenye Biblia hivi: “Na nitaweka agano langu na ninyi, wala miili yote haitaondolewa tena na maji ya gharika; wala hakutakuwa na gharika tena kuiharibu dunia.” Sentensi hii rahisi inafichuamawazo ya Mungu. Kuangamizwa huku kwa ulimwengu kulimpa Yeye maumivu sana. Kwa maneno ya binadamu, Alikuwa na huzuni sana. Tunaweza kufikiria: Dunia ambayo ilikuwa imejaa maisha ilionekana vipi baada ya kuangamizwa na gharika? Dunia ambayo ilikuwa imejaa wanadamu ilionekana vipi sasa? Hakuna makazi ya kibinadamu, hakuna viumbe hai, maji kila mahali na machafuko kabisa juu ya uso wa maji. Hilo ndilo lililokuwa onyesho la kusudio la asili la Mungu wakati alipoumba ulimwengu? Bila shaka la! Kusudi la awali la Mungu lilikuwa ni kuyaona maisha katika maeneo yote, kuwaona wanadamu Aliowaumba wakimwabudu Yeye, si tu kwa Nuhu kuwa mtu pekee anayemwabudu, au kuwa wa pekee ambaye angeweza kujibu wito Wake wa kukamilisha kile alichoaminiwa kufanya. Ubinadamu ulipotoweka, Mungu hakuona kile Alichokuwa amekusudia awali bali kinyume kabisa cha mambo. Ni vipi ambavyo moyo Wake usingekuwa katika maumivu? Hivyo Alipokuwa akifichua tabia Yake na kuelezea hisia Zake, Mungu alifanya uamuzi. Ni aina gani ya uamuzi Aliofanya? Kuunda upinde mawinguni (upinde wa mvua tunaouona) kama agano na binadamu, ahadi kwamba Mungu hangemwangamiza mwanadamu kwa gharika tena. Wakati huohuo, ilikuwa pia ni kuwaambia watu kwamba Mungu aliwahi kuangamiza ulimwengu kwa gharika, kumfanya mwanadamu akumbuke milele ni kwa nini Mungu alifanya kitu kama hicho.
Je, kuangamizwa kwa ulimwengu wakati huu kulikuwa ni jambo alilotaka Mungu? Bila shaka halikuwa ni jambo ambalo Mungu alitaka. Huenda tukaweza kufikiria sehemu ndogo ya picha ile ya kusikitisha ya ulimwengu baada ya kuangamizwa kwa ulimwengu, lakini hatuwezi kukaribia kufikiria namna hali ilivyokuwa wakati huo machoni pa Mungu. Tunaweza kusema kwamba, haijalishi kama ni watu wa sasa au wa wakati huo, hakuna yeyote anayeweza kufikiria au kutambua ni vipi Mungu alikuwa akihisi Aliposhuhudia tukio hilo, picha hiyo ya ulimwengu baada ya kuangamizwa kwake kwa gharika. Mungu alilazimishwa kufanya haya kutokana na kutotii kwa binadamu, lakini maumivu ambayo moyo wa Mungu ulipitia kutokana na maangamizo haya ya ulimwengu kwa gharika ni uhalisia ambao hakuna anayeweza kuufikiria au kuutambua. Ndiyo maana Mungu aliweka agano na mwanadamu, ambalo kupitia hilo Alilenga kuwaambia watu wakumbuke kwamba Mungu aliwahi kufanya kitu kama hiki, na kuapa kwamba Mungu asingewahi kuangamiza ulimwengu kwa njia hii tena. Katika agano hili, tunauona moyo wa Mungu—tunaona kwamba moyo wa Mungu ulikuwa katika maumivu Alipoangamiza binadamu hawa. Katika lugha ya binadamu, wakati Mungu alipomwangamiza mwanadamu na Akaona mwanadamu akitoweka, moyo Wake ulikuwa ukiomboleza na kuvuja damu. Je, hivyo sivyo tunavyoweza kuifafanua kwa njia bora zaidi? Maneno haya yanatumika na binadamu kuonyesha hisia za kibinadamu, lakini kwa sababu lugha ya binadamu ina upungufu mwingi, kuitumia kufafanua hisia za Mungu haionekani kuwa mbaya sana Kwangu. Sasa mtafikiria nini mtakapouona upinde wa mvua tena? Angalau mtakumbuka namna ambavyo Mungu aliwahi kuwa katika huzuni kwa sababu ya kuuangamiza ulimwengu kwa gharika. Mtakumbuka namna, hata kama Mungu aliuchukia ulimwengu huu na kuudharau ubinadamu huu, Alipowaangamiza wanadamu Aliowaumba kwa mikono Yake mwenyewe, moyo Wake ulikuwa ukisononeka, ukipambana kuachilia, Akihisi kwamba Hakuwa na chaguo lingine, na kupata ugumu kustahimili. Faraja Yake pekee ilikuwa katika familia ya Nuhu ya watu wanane. Ulikuwa ni ushirikiano wa Nuhu uliofanya jitihada Zake za kipekee za kuumba viumbe wote wawe wa thamani. Wakati ambapo Mungu alikuwa akiteseka, hili ndilo jambo pekee ambalo lingeweza kufidia uchungu Wake. Kuanzia hapo, Mungu aliweka matarajio Yake yote ya binadamu kwa familia ya Nuhu, Wakati ambapo Mungu alikuwa akiteseka, hili ndilo jambo pekee ambalo lingeweza kufidia uchungu Wake kwamba wasingeangamizwa.
Ni sehemu gani ya tabia ya Mungu tunayopaswa kujifunza kutokana na hili? Mungu alikuwa amemdharau binadamu kwa sababu binadamu alikuwa na uadui na Yeye, lakini ndani ya moyo Wake, utunzaji Wake, kujali Kwake, na huruma Yake kwa binadamu vilibakia vilevile. Hata wakati alipowaangamiza wanadamu, moyo Wake haukubadilika. Wakati binadamu walikuwa wamejaa upotovu na kutomtii Mungu hadi katika kiwango cha kuhuzunisha, Mungu alilazimika, kwa sababu ya tabia Yake na kiini Chake, na kulingana na kanuni Zake, kuwaangamiza binadamu hao. Lakini kwa sababu ya kiini cha Mungu, bado Aliwahurumia binadamu, hata Akataka kutumia njia mbalimbali za kuwakomboa wanadamu ili waweze kuendelea kuishi. Badala yake, binadamu alimpinga Mungu, akaendelea kumwasi Mungu, na akataa kukubali wokovu wa Mungu, yaani, alikataa kukubali nia Zake nzuri. Haijalishi jinsi ambavyo Mungu aliwaita, kuwakumbusha, kukidhi haja zao, kuwasaidia, au Alivyowavumilia, binadamu hakutambua haya, wala hakutilia maanani. Katika maumivu Yake, Mungu bado hakusahau kumpa binadamu uvumilivu Wake wa kiwango cha juu zaidi, Akimsubiria binadamu ageuke na kubadilika. Baada ya Yeye kufikia kikomo Chake, Alifanya kile Alicholazimika kufanya bila ya kusita. Kwa maneno mengine, kulikuwa na kipindi cha muda mahususi na mchakato kutoka pale ambapo Mungu alipanga kuwaangamiza wanadamu hadi katika mwanzo rasmi wa kazi Yake ya kuwaangamiza wanadamu. Mchakato huu ulikuwepo kwa madhumuni ya kumwezesha mwanadamu kugeuka, na ilikuwa nafasi ya mwisho ambayo Mungu alimpa mwanadamu. Hivyo ni nini ambacho Mungu alifanya kwenye kipindi hiki kabla ya kuwaangamiza wanadamu? Mungu alifanya kiwango kikubwa cha kazi ya kukumbusha na kazi ya kusihi. Haijalishi ni maumivu na huzuni ya kiwango gani yaliyokuwa ndani ya moyo wa Mungu, Aliendelea kutumia utunzaji Wake, kujali, na rehema nyingi kwa wanadamu. Tunaona nini kutoka kwa haya? Bila shaka, tunaona kwamba upendo wa Mungu kwa wanadamu ni wa kweli na si tu jambo ambalo Analizungumzia bila matendo. Ni jambo halisi, linaloweza kushikika na kutambulika, si bandia, hauna dosari, haudanganyi wala haujifanyi. Mungu kamwe hatumii uongo au kuunda taswira za bandia ili Awafanye watu waone kwamba Yeye anapendeka. Kamwe hatumii ushuhuda wa uongo ili kuwafanya watu wauone uzuri Wake, au kuringia uzuri wake na utakatifu Wake. Je, vipengele hivi vya tabia ya Mungu havistahili kupendwa na mwanadamu? Kwani navyo havistahili kuabudiwa? Kwani navyo havistahili kupendwa sana? Kwa sasa, Ningependa kuwauliza: Baada ya kuyasikia maneno haya, mnafikiri kwamba ukuu wa Mungu ni maneno matupu tu kwenye kipande cha karatasi? Je, uzuri wa Mungu ni maneno matupu tu? La! Bila shaka sivyo! Mamlaka ya juu, ukuu, utakatifu, uvumilivu, upendo wa Mungu na kadhalika—kila undani wa kila mojawapo ya vipengele mbalimbali vya tabia na kiini cha Mungu hupata maonyesho ya kivitendo kila wakati Anapofanya kazi Yake, ikijumuishwa katika mapenzi Yake kwa mwanadamu, na pia kutimizwa na kuakisiwa kwa kila mtu. Licha ya kama umewahi kuihisi hapo awali, Mungu anamtunza kila mtu katika kila njia inayowezekana, kwa kutumia moyo Wake wa dhati, hekima, na mbinu mbalimbali ili kuuchangamsha moyo wa kila mtu, na kuamsha roho ya kila mtu. Huu ni ukweli usiopingika. Haijalishi ni watu wangapi wameketi hapa, kila mtu amekuwa na uzoefu tofauti na hisia tofauti kwa ustahimilivu, uvumilivu, na uzuri wa Mungu. Uzoefu huu wa Mungu na hisia hizi au mtazamo Wake—kwa ufupi, mambo haya yote chanya yanatoka kwa Mungu. Kwa hivyo kwa kuunganisha uzoefu wa kila mtu na maarifa ya Mungu na kuyachanganya na usomaji wetu wa vifungu hivi vya Biblia leo, je, sasa una uelewa wa kweli na sahihi zaidi kumhusu Mungu?
Baada ya kuisoma hadithi hii na kuelewa baadhi ya tabia za Mungu iliyofichuliwa kupitia tukio hili, ni aina gani ya maarifa mapya mliyo nayo kwa Mungu? Je, imewapa uelewa wa kina zaidi wa Mungu na moyo Wake? Je, mnahisi utofauti sasa mnapoiangalia hadithi ya Nuhu tena? Kulingana na maoni yenu, je, hapakuwa na umuhimu wa kufanya ushirika kwa mistari hii ya Biblia? Kwa vile tumeshiriki kuihusu, je, mnafikiria kwamba haikuwa na umuhimu? Ilikuwa na umuhimu, sivyo? Ingawa kile tulichosoma ni hadithi, ni rekodi ya kweli ya kazi ya Mungu ambayo aliwahi kuifanya. Nia yangu haikuwa kuwawezesha kufahamu maelezo ya hadithi hizi au mhusika huyu, wala haikuwa kwamba mweze kwenda kusoma kuhusu mhusika huyu, na bila shaka si eti mweze kurudi kujifunza Biblia tena. Je, mnaelewa? Kwa hivyo, je, hadithi hizi zimesaidia maarifa yenu ya Mungu? Hadithi hii imeongezea nini katika uelewa wenu wa Mungu? Twambieni, akina kaka na dada kutoka Hong Kong. (Tuliona kwamba upendo wa Mungu ni kitu ambacho hakuna yeyote kati yetu sisi wanadamu wapotovu anayemiliki.) Twambieni, akina kaka na dada kutoka Korea Kusini. (Upendo wa Mungu kwa binadamu ni wa kweli. Upendo wa Mungu kwa binadamu umebeba tabia Yake na unabeba ukuu Wake, utakatifu, uongozi, na ustahimilivu Wake. Inastahili sisi tujaribu kupata ufahamu wa kina zaidi juu yake.) (Kupitia ushirika ambao tumetoka kuwa nao, kwa upande mmoja ninaweza kuona tabia ya Mungu ya haki na kitakatifu, na ninaweza pia kuona wasiwasi alionao Mungu kwa mwanadamu, rehema za Mungu kwa mwanadamu, na kwamba kila kitu anachofanya Mungu na kila fikira na wazo Alilonalo linafichua upendo na kujali Kwake kwa binadamu.) (Uelewa wangu katika siku zilizopita ulikuwa kwamba Mungu alitumia gharika kuangamiza ulimwengu kwa sababu mwanadamu alikuwa amekuwa mwovu kwa kiwango fulani, na ilikuwa kana kwamba Mungu aliwaangamiza binadamu hawa kwa sababu Aliwachukia. Ilikuwa tu baada ya Mungu kuzungumza kuhusu hadithi ya Nuhu leo na kusema ya kwamba moyo wa Mungu ulikuwa unavuja damu ndipo nilipogundua kwamba Mungu kwa kweli alikuwa Anasita kuwaachilia wanadamu hawa. Ilikuwa tu ni kwa sababu mwanadamu alikuwa mwasi sana kiasi cha kwamba Mungu alikuwa hana chaguo ila kumwangamiza. Kwa hakika, moyo wa Mungu wakati huo ulikuwa na huzuni sana. Kutokana na hili, ninaweza kuona katika tabia ya Mungu utunzaji na kujali Kwake kwa mwanadamu. Hili ni jambo ambalo Sikulijua awali.) Vizuri sana! Unaweza kufuata. (Niliguswa sana baada ya kusikiliza. Nimeisoma Biblia hapo awali, lakini sijawahi kuwa na uzoefu kama wa leo ambapo Mungu anachambua kwa njia ya moja kwa moja mambo haya ili tuweze kumjua Yeye. Kwa Mungu kutushika mkono ili tuweze kuona Biblia inanifanya nijue kwamba kiini cha Mungu kabla ya kupotoshwa kwa binadamu kilikuwa ni upendo na utunzaji kwa mwanadamu. Tangu wakati ule binadamu alipopotoka hadi katika siku za mwisho, ingawa Mungu ana tabia ya haki, upendo na utunzaji Wake unabakia vilevile, haubadiliki. Hii inaonyesha kwamba kiini cha upendo wa Mungu, kuanzia uumbaji hadi sasa, licha ya kama binadamu amepotoka, haubadiliki.) (Leo niliona kwamba kiini cha Mungu hakitabadilika kutokana na mabadiliko ya muda au mahali pa kazi Yake. Niliona pia kwamba, haijalishi kama Mungu anauumba ulimwengu au Anauangamiza baada ya binadamu kupotoka, kila kitu Anachofanya kina maana na kuna tabia Yake. Pia niliona kwamba upendo wa Mungu hauna kikomo na haupimiki. Pia niliona, kama vile ambavyo kaka na dada wengine, utunzaji na huruma ya Mungu kwa wanadamu Alipouangamiza ulimwengu.) (Haya ni mambo ambayo kwa hakika sikujua kuyahusu hapo awali. Baada ya kusikiliza leo, nahisi kwamba Mungu ni wa ajabu kwa kweli, wa kuaminika kwa kweli, Anayestahili kuaminiwa, na kwamba kwa kweli Yupo. Ninaweza kutambua kwa dhati ndani ya moyo wangu kwamba tabia ya Mungu na upendo wa Mungu kwa kweli ni vitu vinavyoonekana. Hii ndiyo hisia niliyo nayo baada ya kusikiliza leo.) Safi kabisa! Yaonekana nyote mmechukua kile mlichosikia na kukitia moyoni.
Je, mmetambua ukweli fulani kutoka kwa mistari yote ya Biblia, ikiwa ni pamoja na hadithi zote za Biblia tulizowasiliana nazo leo? Je, Mungu amewahi kutumia lugha Yake Mwenyewe kueleza mawazo Yake mwenyewe au kueleza upendo Wake na utunzaji Wake kwa wanadamu? Je, kuna rekodi ya Yeye kutumia lugha nyepesi kueleza ni kiasi gani Anajali au Anawapenda wanadamu? Hapana! Si hivyo? Kuna wengi sana miongoni mwenu ambao wamesoma Biblia au vitabu vingine mbali na Biblia. Je, yupo yeyote kati yenu aliyeyaona maneno kama hayo? Jibu bila shaka ni hapana! Yaani, kwenye rekodi za Biblia, yakiwemo maneno ya Mungu au rekodi za kazi Yake, Mungu hajawahi katika enzi yoyote au kipindi chochote kile kutumia mbinu Zake mwenyewe kufafanua hisia Zake au kuelezea upendo na utunzaji Wake kwa mwanadamu wala Mungu hajawahi kutumia matamshi au vitendo kufikisha hisia na mawazo Yake—je, huo si ukweli? Kwa nini Ninasema hivyo? Kwa nini lazima Nitaje hii? Ni kwa sababu hii pia ina uzuri wa Mungu na tabia Yake.
Mungu alimuumba mwanadamu; bila kujali kama wamepotoshwa au kama wanamfuata Yeye, Mungu huwachukulia wanadamu kama wapendwa Wake zaidi—au kama vile wanadamu wangesema, watu wanaopendwa sana Naye—na si kama vikaragosi Wake. Ingawa Mungu anasema Yeye ndiye muumba na kwamba binadamu ni uumbaji Wake, hali ambayo inaweza kuonekana ni kana kwamba kuna tofauti kiasi katika mpangilio wa cheo, uhalisia ni kwamba kila kitu ambacho Mungu amefanya kwa mwanadamu kinazidi kabisa uhusiano wa asili hii. Mungu anampenda mwanadamu, Anamtunza mwanadamu, na anaonyesha kwamba anamjali mwanadamu, pamoja na kumkimu mwanadamu bila kuacha na bila ya kusita. Wala Hahisi katika moyo Wake kwamba hii ni kazi ya ziada au ni kitu kinachostahili sifa nyingi. Wala Hahisi kwamba kuwaokoa wanadamu, kuwatosheleza, na kuwapatia kila kitu, ni kutoa mchango mkubwa kwa binadamu. Anamkimu tu mwanadamu kimyakimya na kwa utulivu, kwa njia Yake mwenyewe na kupitia kwa kiini Chake na kileAnacho na alicho. Haijalishi ni kiasi gani cha utoaji na msaada kiasi gani mwanadamu anapokea kutoka Kwake, Mungu kamwe hafikirii wala hajaribu kujipatia sifa. Hii inaamuliwa na kiini cha Mungu, na pia hasa ni maonyesho ya kweli ya tabia ya Mungu. Hii ndiyo sababu, bila kujali ikiwa ni katika Biblia au vitabu vingine vyovyote, hatupati kamwe Mungu akieleza mawazo Yake, na hatupati kamwe Mungu akieleza au kutangaza kwa wanadamu kwa nini Anafanya mambo haya, au kwa nini Anawajali sana wanadamu, ili kuwafanya wanadamu wawe na shukrani Kwake au kumsifu. Hata Anapoumizwa, wakati moyo Wake ukiwa katika maumivu makali, Hasahau kamwe wajibu Wake kwa wanadamu au kujali Kwake kwa wanadamu, wakati wote Anabeba uchungu na maumivu haya peke yake kwa ukimya. Kinyume cha mambo ni kwamba, Mungu anaendelea kumkimu mwanadamu kama Anavyofanya siku zote. Ingawa mwanadamu mara nyingi humsifia Mungu au huwa na ushuhuda Kwake, hakuna kati ya tabia hii ambayo imedaiwa na Mungu. Hii ni kwa sababu Mungu hajawahi kunuia kwa kitu chochote kizuri Anachofanya kwa wanadamu kibadilishwe kwa shukrani au kiweze kulipwa. Kwa upande mwingine, wale wanaomcha Mungu na kujiepusha na maovu, wale wanaomfuata Mungu kwa kweli, wanaomsikiliza Yeye, na walio waaminifu Kwake, na wale wanaomtii Yeye—hawa ndio watu ambao mara nyingi watapokea baraka za Mungu, na Mungu atawakabidhi baraka hizo bila kusita. Zaidi ya hayo, baraka ambazo watu hupokea kutoka kwa Mungu mara nyingi huwa zaidi ya mawazo yao, na pia zaidi ya chochote ambacho wanadamu wanaweza kubadilishana kwa kile ambacho wamefanya au gharama ambayo wamelipa. Wakati wanadamu wanafurahia baraka za Mungu, je, kuna yeyote anayejali kuhusu kile ambacho Mungu anafanya? Je, yupo yeyote anayeonyesha wasiwasi wowote kuhusu vile ambavyo Mungu anahisi? Je, yupo yeyote anayejaribu kutambua maumivu ya Mungu? Jibu la uhakika la maswali haya ni: Hapana! Je, mwanadamu yeyote, akiwemo Nuhu, anaweza kutambua yale maumivu ambayo Mungu alikuwa akihisi wakati huo? Je, kuna yeyote anayeweza kufahamu ni kwa nini Mungu alianzisha agano kama hilo? Hakuna anayeweza! Mwanadamu hafahamu maumivu ya Mungu si kwa sababu hawezi kuelewa maumivu ya Mungu, na si kwa sababu ya umbali uliopo kati ya Mungu na mwanadamu au tofauti kati ya hadhi zao; badala yake, ni kwa sababu mwanadamu hata hajali kuhusu hisia zozote za Mungu. Mwanadamu anafikiria Mungu yuko huru—Mungu hahitaji watu wa kujali kuhusu Yeye, kumwelewa au kumwonyesha namna anavyomfikiria. Mungu ni Mungu, hivyo Hana maumivu, Hana hisia; Hatakasirika, Hahisi huzuni, hata Halii. Mungu ni Mungu, hivyo Hahitaji maonyesho yoyote ya kihisia na Hahitaji faraja yoyote ya kihisia. Ikiwa, chini ya hali fulani, Atahitaji vitu hivi, basi Atatatua mwenyewe na Hatahitaji usaidizi wowote kutoka kwa mwanadamu. Lakini kinyume chake ni kwamba, ni wale binadamu wanyonge, ambao hawajakomaa ndio wanaohitaji faraja ya Mungu, utoaji, himizo, na hata kwa Yeye kuweza kufariji hisia zao wakati wowote na mahali popote. Fikira kama hiyo inajificha ndani kabisa ya mioyo ya wanadamu: Binadamu ndiye mnyonge; wanamhitaji Mungu ili awatunze kwa kila njia, wanastahili utunzaji wote wanaopokea kutoka kwa Mungu, na wanapaswa kudai kutoka kwa Mungu chochote kile wanachohisi kinafaa kuwa chao. Mungu ndiye mwenye Nguvu; Ana kila kitu, na Anahitaji kuwa mlezi wa mwanadamu na Anayetoa baraka. Kwa sababu Yeye tayari ni Mungu, Yeye ni Muweza wa yote na Hahitaji kamwe chochote kutoka kwa mwanadamu.
Kwa vile binadamu hatilii maanani ufunuo wowote wa Mungu, hajawahi kuhisi huzuni, maumivu au furaha ya Mungu. Lakini kinyume chake ni kwamba, Mungu anajua maonyesho yote ya binadamu kama vile anavyojua sehemu ya kiganja cha mkono Wake. Mungu hutosheleza mahitaji ya kila mtu wakati wote na mahali popote, Akitazama mawazo yanayobadilika ya kila mtu na hivyo Anawafariji na kuwahimiza, na kuwaongoza na kuwaangazia. Kuhusu mambo yote ambayo Mungu amemfanyia mwanadamu, na gharama zote Alizolipa kwa sababu yao, je, watu wanaweza kupata kifungu kutoka kwenye Biblia au kutoka kwa chochote ambacho Mungu amesema mpaka sasa kinachoelezea waziwazi kwamba Mungu atadai kitu kutoka kwa binadamu? La! Kinyume cha mambo, haijalishi jinsi watu wanavyopuuza fikira za Mungu, bado Anawaongoza wanadamu mara kwa mara, Anawakimu na kuwasaidia mara kwa mara, Akiwaruhusu wafuate njia ya Mungu ili waweze kupokea hatima nzuri ambayo Amewatayarishia. Inapokuja kwa Mungu, kile Anacho na alicho, neema Yake, rehema Yake, na thawabu Zake zote, zitatotelewa bila ya kusalia kwa wale wanaompenda na kumfuata Yeye. Lakini hajawahi kufichua kwa mtu yeyote maumivu aliyopitia Yeye au hali ya akili Yake, na katu halalamiki kuhusu yeyote ambaye hamtilii Yeye maanani au hajui mapenzi Yake. Anavumilia tu haya yote kimyakimya, Akisubiria siku ambayo mwanadamu ataweza kuelewa.
Kwa nini Nasema mambo haya hapa? Ni nini mnachoona kutoka kwa mambo haya Niliyosema? Kuna kitu katika kiini na tabia ya Mungu ambacho ni rahisi kupuuza, kitu ambacho kinamilikiwa na Mungu pekee na si mtu yeyote, ikiwa ni pamoja na wale wengine wanaofikiri kuwa watu wakuu, watu wema, au Mungu wa mawazo yao. Kitu gani hiki? Ni kutokuwa na ubinafsi kwa Mungu. Tunapozungumza juu ya kutokuwa na ubinafsi, unaweza kufikiria wewe pia ni mtu asiye na ubinafsi, kwa sababu inapokuja kwa watoto wako, hautawahi kujadiliana nao na wewe ni mkarimu kwao, au unafikiri wewe pia hujitolea sana inapokuja kwa wazazi wako. Haijalishi unafikiria nini, angalau una dhana ya neno “kutokuwa na ubinafsi” na unalifikiria kama neno chanya, na kwamba kuwa mtu asiye na ubinafsi ni jambo la heshima sana. Wakati huna ubinafsi, unajiona wewe ni mkuu. Lakini hakuna anayeweza kuona kutojitolea kwa Mungu kati ya vitu vyote, miongoni mwa watu, matukio, na vitu, na kupitia kazi ya Mungu. Kwa nini ni hivyo? Kwa sababu mwanadamu ni mbinafsi sana! Kwa nini Ninasema hivyo? Mwanadamu anaishi katika ulimwengu yakinifu. Unaweza kumfuata Mungu, lakini huoni wala hufahamu jinsi ambavyo Mungu anakukimu, Anavyokupenda na Anavyoonyesha kwamba Anakujali. Kwa hivyo unaona nini? Unawaona watu wa ukoo wako wanaokupenda au kukujali sana. Unayaona mambo ambayo ni ya manufaa kwa mwili wako, unajali kuhusu watu na vitu unavyopenda. Huku ndiko kutokuwa na ubinafsi kwa binadamu kunakodaiwa. Watu kama hao “wasiokuwa na ubinafsi” hata hivyo, huwa hawajali kamwe kuhusu Mungu anayewapa uzima. Tofauti na ile ya Mungu, kutokuwa na ubinafsi kwa binadamu kunakuwa ubinafsi na kudharauliwa. Kutokuwa na ubinafsi ambako binadamu anaamini ndani yake, ni ule ulio mtupu na usio halisi, ulio na dosari, usiolingana na Mungu, na usiohusika na Mungu. Kutokuwa na ubinafsi kwa binadamu ni kwa ajili yake, huku kutokuwa na ubinafsi kwa Mungu ni ufunuo wa kweli wa kiini Chake. Ni kutokana na kutokuwa na ubinafsi kwa Mungu kwamba mwanadamu anapata mkondo thabiti wa msaada kutoka Kwake. Huenda usiathiriwe sana na mada hii Ninayozungumzia leo na unaweza kuwa tu unatikisa kichwa chako kwa kukubaliana na Mimi, lakini wakati unapojaribu kuuelewa moyo wa Mungu katika moyo wako, bila kujua utaweza kugundua hili: Miongoni mwa watu wote, masuala, na vitu utaweza kuhisi katika ulimwengu huu ni kutokuwa na ubinafsi tu kwa Mungu ambako ni kweli na thabiti, kwa sababu ni upendo wa Mungu tu kwako ndio ambao hauna masharti na hauna dosari. Mbali na Mungu, kutokuwa na kile kinachodaiwa kutokuwa na ubinafsi wa mtu mwingine yeyote ni kwa kujifanya, kwa juu juu, kuna hila; kuna madhumuni, nia fulani, kunabeba mabadilishano, na hakuwezi kusimama ili kupimwa. Unaweza hata kusema kwamba ni wenye uchafu na wa kudharauliwa. Je, unakubaliana na maneno haya?
Ninajua hamfahamu mada hizi na mnahitaji muda kidogo ili ziweze kuingia ndani yenu kabla hamjaweza kuzielewa kwa kweli. Kadri mnavyokosa kufahamu masuala na mada hizi, ndivyo inavyothibitisha zaidi kwamba mada hizi zinakosekana katika mioyo yenu. Kama Nisingewahi kuzitaja mada hizi, je, kuna yeyote kati yenu ambaye angeweza kujua chochote kuzihusu? Ninaamini hamgewahi kuweza kuzijua. Hiyo ni kwa hakika. Haijalishi ni kiasi kipi mnachoweza kufahamu au kuelewa, kwa ufupi, mada hizi Ninazozungumzia ndizo ambazo watu wanakosa sanasana na ndizo wanazopaswa kuzijua zaidi. Mada hizi ni muhimu kwa kila mmoja—ni zenye thamani na ndiyo maisha, na ni mambo ambayo lazima mmiliki vizuri kwa safari ijayo. Bila ya maneno haya kama mwongozo, bila ya uelewa wako wa tabia na kii cha Mungu, siku zote utabakia na alama ya kiulizo inapokuja kwa Mungu. Unawezaje kumwamini Mungu ipasavyo kama hata humwelewi Yeye? Hujui chochote kuhusu hisia Zake, mapenzi Yake, hali ya akili Yake, kile Anachofikiria, nini kinachomfanya Yeye kuwa na huzuni, na nini kinachomfanya Yeye kuwa na furaha, hivyo unawezaje kuujali moyo wa Mungu?
Kila wakati Mungu anapokuwa amekasirika, Anakumbana na mwanadamu ambaye hamtilii maanani kamwe, mwanadamu anayemfuata Yeye na anayedai kumpenda Yeye hata hivyo anapuuza kabisa hisia Zake. Moyo Wake utakosaje kuumia? Katika kazi ya usimamizi ya Mungu, Anaitekeleza kwa dhati kazi Yake na Anaongea na kila mmoja, na Anakabiliana nao bila kusita au kujificha, lakini kinyume chake ni kuwa, kila mtu anayemfuata Yeye anatenganishwa na Yeye, na hakuna aliye tayari kumkaribia Yeye kikamilifu, kuuelewa moyo Wake, au kutilia maanani hisia Zake. Hata wale wanaotaka kuwa wandani wa Mungu hawataki kuwa karibu na Yeye, hawatilii maanani moyo Wake, au kujaribu kumwelewa Yeye. Wakati Mungu anashangilia na Ana furaha, hakuna yeyote yule wa kushiriki katika furaha hiyo na Yeye. Wakati Mungu anakosa kueleweka na watu, hakuna mtu wa kuufariji moyo Wake ulio na majeraha. Wakati moyo Wake unaumia, hakuna hata mtu mmoja aliye tayari kumsikiliza Yeye na kuwa mwandani Wake. Katika maelfu ya miaka hii ya usimamizi wa kazi ya Mungu, hakuna mtu anayeelewa hisia za Mungu, hakuna hata mtu anayefahamu au kutambua hisia Zake, licha ya hata yeyote ambaye angesimama kando ya Mungu ili kushiriki katika furaha na huzuni Zake. Mungu ni mpweke. Yeye ni pweke! Mungu ni mpweke si tu kwa sababu wanadamu waliopotoka wanampinga Yeye, lakini zaidi kwa sababu wale wanaofuatilia kuwa wa kiroho, wale wanaotafuta kumjua Mungu na kumwelewa Yeye, na hata wale walio tayari kujitolea maisha yao yote Kwake, pia hawajui fikira Zake, na hawaielewi tabia Yake na hisia Zake.
Mwishoni mwa hadithi ya Nuhu, tunaona kwamba Mungu alitumia mbinu isiyo ya kawaida kuelezea hisia Zake wakati huo. Mbinu hii ni maalumu sana, na ni kuweka agano na mwanadamu ambalo lilitangaza mwisho wa uharibifu wa Mungu wa ulimwengu kwa gharika. Kwa juu juu, kuweka agano kunaonekana kuwa jambo lililo la kawaida sana. Si jambo lolote zaidi ya kutumia maneno kufunga wahusika ili wasitende vitendo vitakavyokiuka agano, ili kusaidia kutimiza kusudio la kulinda maslahi ya pande zote mbili. Kwa nje, ni jambo la kawaida sana, lakini kutokana na motisha zilizopo na dhamira ya Mungu kufanya kitu hiki, ni ufunuo wa kweli wa tabia ya Mungu na hali Yake ya akili. Endapo utayaweka maneno haya kando na kuyapuuza, kama Sitawahi kukuambia ukweli wa mambo, basi binadamu hawatawahi kwa hakika kujua mawazo ya Mungu. Pengine katika kufikiria kwako Mungu alikuwa akitabasamu wakati Alipofanya agano hili, au pengine maonyesho Yake yalikuwa mazito, lakini haijalishi ni maonyesho gani ya kawaida kabisa ambayo watu wanafikiria Mungu alikuwa nayo, hakuna ambaye angeweza kuuona moyo wa Mungu au maumivu Yake, na hata upweke Wake. Hakuna mtu anayeweza kumfanya Mungu amwamini au anayestahili kuaminiwa na Mungu, au kuwa mtu Anayeweza kumweleza mawazo Yake au kuwa mwandani Wake wa kumwambia maumivu Yake. Ndiyo maana Mungu hakuwa na chaguo ila kufanya kitu kama hicho. Kwa juujuu, Mungu alifanya jambo rahisi la kuwaaga binadamu wale wa awali, kuhitimisha hali ya kale ilivyokuwa na kuleta mwisho kamili wa uharibifu Wake wa ulimwengu kwa gharika. Hata hivyo, Mungu alikuwa ameyazika maumivu kuanzia wakati huu ndani kabisa ya moyo Wake. Kwa wakati ambao Mungu hakuwa na yeyote wa kumwita mwandani, Alifanya agano na wanadamu, Akiwaambia kwamba Asingeuangamiza ulimwengu kwa gharika tena. Wakati upinde wa mvua unapojitokeza ni ili kuwakumbusha watu kwamba, kitu kama hicho kiliwahi kufanyika, ni ili kuwapa watu onyo dhidi ya kufanya maovu. Hata katika hali hiyo ya maumivu, Mungu hakusahau kuhusu wanadamu na bado Alionyesha kujali kwingi sana juu yao. Je, huu si upendo na kutokuwa na ubinafsi kwa Mungu? Lakini watu wanafikiria nini wakati wanapoteseka? Je, huu si wakati ambao wanamhitaji Mungu zaidi? Katika nyakati kama hizi, siku zote watu wanamkokota Mungu katika mambo yao ili Mungu aweze kuwapa faraja. Haijalishi ni lini, Mungu hatawahi kuwavunja moyo watu, na siku zote Atawaruhusu watu kutoka katika changamoto zao na kuishi katika mwangaza. Ingawa Mungu anawakimu wanadamu, ndani ya moyo wa mwanadamu, Mungu si chochote ila kidonge cha kutuliza, dawa ya tulizo. Wakati Mungu anateseka, wakati moyo Wake una majeraha, kuwa na kiumbe aliyeumba au mtu yeyote wa kuwa pamoja Naye au wa kumfariji Yeye, bila shaka kungekuwa ni tamanio la kupita kiasi kwa Mungu. Siku zote binadamu hatilii maanani hisia za Mungu, hivyo Mungu siku zote Haulizii wala Hatarajii kuwa kuna mtu anayeweza kumfariji Yeye. Anatumia mbinu Zake mwenyewe kueleza hali Yake. Watu hawafikirii kwamba ni jambo kubwa kwa Mungu kupitia mateso fulani, lakini unapojaribu tu kumwelewa Mungu kwa kweli, unapoweza kufahamu kwa dhati, nia nzuri za Mungu katika kila kitu Anachofanya, ndipo utakapoweza kuuhisi ukuu wa Mungu na kutokuwa na ubinafsi Kwake. Ingawa Mungu alifanya agano na wanadamu kwa kutumia upinde wa mvua, Hakuwahi kumwambia yeyote ni kwa nini Alifanya hivyo, ni kwa nini Alianzisha agano hili, kumaanisha kwamba Hakuwahi kumwambia mtu yeyote fikira Zake halisi. Hii ni kwa sababu hakuna mtu anayeweza kufahamu kina cha upendo ambao Mungu anao kwa wanadamu Aliowaumba kwa mikono Yake mwenyewe, na hakuna pia mtu anayeweza kutambua ni kiwango kipi cha maumivu ambayo moyo Wake uliteseka wakati Alipowaangamiza binadamu. Hivyo basi, hata kama Angewaambia watu jinsi Anavyohisi, wasingeweza kumwamini. Licha ya kuwa katika maumivu, bado Anaendelea na hatua inayofuata ya kazi Yake. Siku zote Mungu Anatoa upande Wake ulio bora zaidi na vitu bora zaidi kwa wanadamu wakati Yeye mwenyewe Akistahimili kimyakimya mateso yote. Mungu kamwe hafichui mateso haya. Badala yake, Anayavumilia na kusubiri kwa ukimya. Ustahimilivu wa Mungu si wa ukimya tu, usio na hisia, au usio na suluhu, wala si ishara ya unyonge. Ni kwamba upendo na kiini cha Mungu siku zote umekuwa usio na ubinafsi. Huu ni ufunuo wa kiasili wa kiini na tabia Yake na maonyesho halisi ya utambulisho wa Mungu kama Muumba wa kweli.
Baada ya kusema hayo, wengine wanaweza kutafsiri kimakosa kile Ninachomaanisha, na kufikiria, “Je, kuelezea hisia za Mungu kwa undani sana, kwa hali ya hisia nyingi sana, kulikusudiwa kuwafanya watu wamuonee Mungu huruma?” Je, hilo ndilo dhumuni hapa? (La.) Dhumuni pekee la Mimi kusema maneno haya ni ili kukufanya umjue Mungu vyema zaidi, uelewe kila kipengele Chake, uelewe hisia Zake, ili ufahamu kwamba kiini na tabia ya Mungu, kwa uthabiti na hatua kwa hatua, vinaonyeshwa kupitia kwa kazi Yake, kinyume na vile inavyoonyeshwa kupitia kwa maneno matupu ya mwanadamu, barua na mafundisho yao, au mawazo yao. Hiyo ni kusema, Mungu na kiini cha Mungu kwa kweli vipo—sio michoro, si mawazo ya kufikirika, havijaundwa na mwanadamu, na kwa hakika hazijabuniwa na mwanadamu. Je, unatambua hili sasa? Kama unatambua, basi maneno Yangu leo yamefanikisha lengo lao.
Tulijadili mada tatu leo. Ninaamini kwamba kila mtu amepata mengi kutokana na ushirika wetu juu ya mada hizi tatu. Ninaweza kusema kwa uhakika kwamba, kupitia kwa mada hizi tatu, fikira za Mungu Nilizofafanua au tabia na kiini cha Mungu Nilizotaja vyote vimebadili mawazo na ufahamu wa watu kuhusu Mungu, hata kubadili imani za kila mmoja kwa Mungu, na zaidi, kubadili picha ya Mungu inayopendwa na kila mmoja katika mioyo yao. Haijalishi chochote, Natumai kwamba kile ambacho mmejifunza kuhusu tabia ya Mungu katika sehemu hizi mbili za Biblia ni cha manufaa kwenu, na Natumai kwamba baada ya nyinyi kurudi mtajaribu kuzitafakari zaidi. Kikao cha leo kinahitimishwa hapa. Kwaheri!
Novemba 4, 2013