Kristo Hufanya Kazi ya Hukumu kwa Ukweli
Kazi ya siku za mwisho ni kuainisha wote kulingana na aina zao, na kuhitimisha mpango wa usimamizi wa Mungu, kwa maana wakati uko karibu na siku ya Mungu imewadia. Mungu huwaleta wote wanaoingia katika ufalme Wake—wote ambao ni waaminifu Kwake hadi mwisho kabisa—katika enzi ya Mungu Mwenyewe. Hata hivyo kabla ya kuwasili kwa enzi ya Mungu Mwenyewe, kazi ya Mungu si kukagua matendo ya mwanadamu, au kuchunguza maisha ya mwanadamu, bali ni kuhukumu uasi wa mwanadamu, kwa maana Mungu atawatakasa wale wote wanaokuja mbele ya kiti Chake cha enzi. Wote ambao wamefuata hatua za Mungu hadi leo ni wale wanaokuja mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, na hili likiwa hivi, kila mtu anayekubali kazi ya Mungu katika awamu yake ya mwisho ni mlengwa wa utakaso wa Mungu. Kwa maneno mengine, kila mtu anayekubali kazi ya Mungu katika awamu yake ya mwisho ni mlengwa wa hukumu ya Mungu.
Katika hukumu inayoanza katika nyumba ya Mungu iliyozungumziwa nyakati za zamani, neno “hukumu” katika maneno haya linarejelea hukumu ambayo Mungu leo anatekeleza kwa wale wanaokuja mbele ya kiti Chake cha enzi katika siku za mwisho. Pengine kuna wale wanaoamini kwamba siku za mwisho zitakapofika, Mungu ataweka meza kubwa mbinguni, ambayo juu yake kitambaa cheupe kitatandikwa, na kisha, Akiketi juu ya kiti kikuu cha enzi huku watu wote wakiwa wamepiga magoti chini, Yeye atafichua dhambi za kila mtu na hivyo kuamua iwapo watapaa mbinguni au kutumwa chini katika ziwa la moto na kiberiti, miongoni mwa mawazo mengine kama hayo yasiyo ya ulimwengu. Haijalishi mwanadamu anawazia nini, jambo hilo haliwezi kubadilisha kiini cha kazi ya Mungu. Mawazo ya mwanadamu si chochote bali na ubunifu wa fikira za mwanadamu; yanatoka katika ubongo wa mwanadamu, yakijumlishwa na kuunganishwa kutoka katika kile ambacho mwanadamu ameona na kusikia. Kwa hivyo Ninasema, haijalishi mawazo ya watu ni mazuri kiasi gani, hayo ni michoro ya katuni tu, na hayawezi kuchukua nafasi ya mpango wa kazi ya Mungu. Mwanadamu, baada ya yote, amepotoshwa na Shetani, kwa hivyo anawezaje kufahamu fikira za Mungu? Mwanadamu huwazia kazi ya hukumu ya Mungu kama kitu cha ajabu sana. Anaamini kwamba kwa kuwa ni Mungu Mwenyewe anayefanya kazi ya hukumu, basi kazi hii lazima iwe ya kiwango kikubwa sana, na isiyoeleweka kwa wanadamu, na lazima ivume kote mbinguni na kuitikisa ardhi; kama sivyo, inawezaje kuwa kazi ya hukumu ya Mungu? Anaamini kwamba, kwa kuwa hii ni kazi ya hukumu, basi Mungu lazima awe mwenye kuogofya na mwadhimu hasa Anapofanya kazi, na wale wanaohukumiwa lazima wawe wakiomboleza kwa machozi na wakiwa wamepiga magoti wakiomba rehema. Mandhari kama hayo hakika yangekuwa ya kustaajabisha, na yenye kusisimua sana…. Kila mtu anawazia kazi ya hukumu ya Mungu kuwa ya kimuujiza. Hata hivyo, je, unajua kwamba, wakati ambapo Mungu ameanza kazi Yake ya hukumu miongoni mwa wanadamu tangu kitambo, wewe unasalia umezama katika usingizi mzito? Kwamba wakati unapofikiri kazi ya hukumu ya Mungu imeanza rasmi, Mungu atakuwa tayari amefanya mbingu na ardhi kuwa mpya? Wakati huo, labda, utakuwa ndio kwanza umeelewa maana ya maisha, lakini kazi ya Mungu ya adhabu isiyo na huruma itakupeleka wewe, ukiwa bado katika usingizi mzito, katika jahanamu. Hapo tu ndipo utakapopata utambuzi wa ghafla, na kuelewa kwamba kazi ya hukumu ya Mungu tayari imehitimishwa.
Tusipoteze wakati wetu wa thamani, na tusizungumze tena kuhusu mada hizi za kuchukiza na zenye kinyaa. Badala yake hebu tuzungumze kuhusu hukumu ni nini. Linapotajwa neno “hukumu,” kuna uwezekano wa wewe kufikiria maneno ambayo Yehova alizungumza ili kuwaagiza watu katika kila eneo na maneno ambayo Yesu alinena ili kuwakemea Mafarisayo. Licha ya ukali wa maneno hayo, hayakuwa hukumu ya Mungu kwa mwanadamu; yalikuwa tu maneno yaliyonenwa na Mungu ndani ya mazingira tofauti, yaani, katika miktadha tofauti. Maneno haya ni tofauti na maneno yanayonenwa na Kristo wa siku za mwisho Anapomhukumu mwanadamu. Kristo wa siku za mwisho hutumia aina mbalimbali za ukweli kumfundisha mwanadamu, kufichua kiini cha mwanadamu, na kuchanganua maneno na matendo ya mwanadamu. Maneno haya yanajumuisha ukweli mbalimbali, kama vile wajibu wa mwanadamu, jinsi mwanadamu anavyopaswa kumtii Mungu, jinsi mwanadamu anavyopaswa kuwa mwaminifu kwa Mungu, jinsi mwanadamu anavyopaswa kuishi kwa kudhihirisha ubinadamu wa kawaida, na vilevile hekima na tabia ya Mungu. Maneno haya yote yanaelekezwa kwa kiini cha mwanadamu na tabia zake potovu. Hasa, maneno yanayofichua jinsi mwanadamu humkataa Mungu yanaelekezwa hata zaidi kwa jinsi mwanadamu kimsingi alivyo mfano halisi wa Shetani, na jinsi mwanadamu kimsingi alivyo nguvu ya uhasama dhidi ya Mungu. Katika kufanya kazi Yake ya hukumu, Mungu haelezi kwa ukamilifu asili ya mwanadamu kwa maneno machache tu; Anafichua na kupogoa kwa muda mrefu. Mbinu hizi zote tofauti za kufichua na kupogoa haziwezi kubadilishwa na maneno ya kawaida; badala yake, ukweli ambao mwanadamu hana kabisa hutumiwa kutekeleza kazi hii ya ufichuzi na upogoaji. Ni mbinu kama hizi pekee ndizo zinazoweza kuitwa hukumu; ni hukumu ya aina hii pekee ndiyo inayoweza kumtiisha mwanadamu na kumsadikisha kikamilifu kumhusu Mungu, na zaidi ya hayo kumwezesha kupata maarifa ya kweli ya Mungu. Kile ambacho kazi ya hukumu huleta ni maarifa ya mwanadamu ya uso wa kweli wa Mungu; kile inacholeta ni uelewa wa mwanadamu wa ukweli kuhusu uasi wake mwenyewe. Kazi ya hukumu imemwezesha mwanadamu kupata uwazi mwingi sana kuhusu nia za Mungu, uwazi mwingi sana kuhusu kusudi la kazi ya Mungu, na ufahamu mwingi wa siri ambazo hawezi kuzing’amua. Pia imemwezesha mwanadamu kujua na kupata ufahamu wa kiini chake kipotovu na chanzo cha upotovu wake, na imemwezesha mwanadamu kugundua uso wake mbaya. Matokeo haya yote ya kazi yanaletwa na kazi ya hukumu, kwani kiini cha kazi ya hukumu kwa kweli ni kazi ya kufungua ukweli, njia, na uzima wa Mungu kwa wale wote wanaomwamini Yeye. Kazi hii ni kazi ya hukumu inayofanywa na Mungu. Usipouchukulia kweli hizi kuwa muhimu, ikiwa kila mara unajaribu kuepuka kweli hizi, na kila mara unajaribu kutafuta njia mpya ya kutokea nje ya kweli hizi, basi Ninasema wewe ni mtenda dhambi mwovu sana. Kama unamwamini Mungu, lakini hutafuti ukweli au kutafuta nia za Mungu, wala huipendi njia inayokuleta karibu na Mungu, basi Ninakwambia kuwa wewe ni yule anayejaribu kuepuka hukumu, na kwamba wewe ni kibaraka na msaliti anayekikimbia kiti kikuu cheupe cha enzi. Mungu hatakosa kuwaadhibu waasi wowote ambao wanatoroka kutoka machoni Pake. Watu wa aina hii watapokea adhabu kali zaidi. Wale wanaokuja mbele za Mungu ili wapokee hukumu Yake, na ambao zaidi ya hayo wametakaswa, wataishi milele katika ufalme wa Mungu. Bila shaka, hili ni jambo ambalo ni la siku za usoni.
Kazi ya hukumu ni kazi ya Mungu Mwenyewe, kwa hivyo bila shaka lazima ifanywe na Mungu Mwenyewe; haiwezi kufanywa na mwanadamu badala Yake. Kwa sababu hukumu ni matumizi ya ukweli kuwashinda binadamu, ni jambo lisilopingika kwamba Mungu bado anaonekana miongoni mwa watu katika mfano wa umwilisho ili kutekeleza kazi hii. Yaani, Kristo wa siku za mwisho atatumia ukweli kuwafundisha watu kutoka kila mahali na kuwatajia wazi ukweli wote. Hii ndiyo kazi ya hukumu ya Mungu. Wengi hawana raha kuhusu Mungu kupata mwili mara ya pili, kwa maana watu wote wanaona ni vigumu kuamini kwamba Mungu angepata mwili ili kufanya kazi ya hukumu. Hata hivyo, lazima Nikuambie kwamba kazi ya Mungu mara nyingi inazidi sana matarajio ya mwanadamu, na ni vigumu kwa akili za binadamu kukubali. Kwa maana watu si chochote ila ni funza juu ya ardhi, huku Mungu ndiye Yule mkuu anayejaza ulimwengu; akili ya mwanadamu ni kama shimo la maji machafu, na inazalisha funza tu, ilhali kila hatua ya kazi inayoongozwa na fikira za Mungu ni zao la mwisho la hekima ya Mungu. Mwanadamu kila mara hujaribu kushindana na Mungu, na kwa hili Ninasema, ni dhahiri ni nani atakayepoteza mwishowe. Ninawahimiza ninyi nyote msijione kuwa wa thamani zaidi kuliko dhahabu. Ikiwa wengine wanaweza kukubali hukumu ya Mungu, kwa nini wewe usiweze? Uko juu kiasi gani kuliko wengine? Ikiwa wengine wanaweza kuinamisha vichwa vyao mbele ya ukweli, kwa nini wewe usiweze pia? Kazi ya Mungu haizuiliki. Yeye hatarudia kazi ya hukumu kwa sababu tu ya “mchango” ambao umetoa, na utapitia majuto yaumizayo moyo kwa kuacha fursa nzuri kama hiyo ikupite. Ikiwa huamini maneno Yangu, basi ngoja tu kile kiti kikuu cheupe cha enzi angani “kikuhukumu”! Lazima ujue kwamba Waisraeli wote walimkataa Yesu na walimkana Yesu, na bado ukweli wa ukombozi wa Yesu kwa wanadamu ulienea kote ulimwenguni na hadi miisho ya ardhi. Je, huu si ukweli ambao Mungu alikamilisha kitambo? Ikiwa bado unangoja Yesu akuchukue hadi mbinguni, basi Ninasema kwamba wewe ni gogo lenye ukaidi la mti uliokufa. Yesu hatamtambua muumini wa uongo kama wewe, ambaye si mwaminifu kwa ukweli na anatafuta baraka pekee. Kinyume chake, Yeye hataonyesha huruma katika kukutupa katika ziwa la moto ili uteketee kwa makumi ya maelfu ya miaka.
Je, sasa unaelewa hukumu ni nini na ukweli ni nini? Ikiwa unaelewa, basi nakushauri ujitiishe chini ya kuhukumiwa kwa unyenyekevu, la sivyo hutaweza kamwe kupata nafasi ya kukubaliwa na Mungu au kuletwa na Yeye katika ufalme Wake. Wale wanaokubali hukumu tu lakini hawawezi kutakaswa, yaani, wale wanaokimbia katikati ya kazi ya hukumu, watakataliwa na Mungu milele. Dhambi zao ni za kusikitisha zaidi na nyingi zaidi kuliko zile za Mafarisayo, kwa maana wamemsaliti Mungu na ni waasi dhidi ya Mungu. Watu hawa ambao hawastahili hata kufanya kazi watapata adhabu kali zaidi, adhabu ambayo, zaidi ya hayo, ni ya milele. Mungu hatamsamehe msaliti yeyote ambaye aliwahi kudhihirisha uaminifu kwa maneno lakini baadaye akamsaliti. Watu wa namna hiyo watapata adhabu kupitia adhabu ya roho, nafsi, na mwili. Je, huu si ufunuo halisi wa tabia ya haki ya Mungu? Je, hili si kusudi hasa la Mungu kumhukumu na kumfichua mwanadamu? Mungu anawakabidhi wale wanaotenda maovu ya kila aina wakati wa kipindi cha hukumu mahali palipojaa pepo wabaya, na anawaacha pepo hao wabaya waziharibu nyama zao za kimwili wapendavyo, na miili ya watu hao hunuka uvundo wa maiti. Hiyo ndiyo adhabu wanayostahili. Mungu huandika kila mojawapo ya dhambi za waumini wa uongo wasio waaminifu, mitume wa uongo, na wafanyakazi wa uongo katika vitabu vyao vya kumbukumbu, na ifikapo wakati unaofaa, Anawatupa katikati ya roho wachafu, akiwaacha roho hao wachafu wachafue miili yao yote wapendavyo, na kuwafanya wasiweze kamwe kuzaliwa upya wala kuona nuru tena. Mungu huwahesabu miongoni mwa waovu wale wanafiki wanaotoa huduma kwa muda fulani lakini hawakai waaminifu hadi mwisho, Akiwaacha watumbukie matopeni pamoja na waovu na kuunda pamoja na wao genge la wahalifu wenye tabia mbalimbali, na mwishowe Mungu atawaangamiza. Mungu huwatupa kando na hawatilii maanani wale ambao hawajawahi kuwa waaminifu kwa Kristo au hawajawahi kutoa nguvu zao zozote, na wakati wa mabadiliko ya enzi Atawaangamiza wote. Hawatakuwapo tena duniani, sembuse kupata njia ya kuingia katika ufalme wa Mungu. Mungu humhesabu yeyote ambaye hajawahi kuwa mwaminifu kwa Mungu miongoni mwa wale wanaowatumikia watu Wake, bali hana budi tu kumshughulikia kwa njia isiyo ya dhati. Ni wachache tu kati ya watu hao watakaosalia, huku wengi wataangamizwa pamoja na wale ambao kazi yao haifikiii kiwango kinachohitajika. Mwishowe, Mungu atawaleta katika ufalme Wake wote walio na moyo na nia moja na Mungu, watu na wana wa Mungu, na wale walioamuliwa kabla na Mungu kuwa makuhani. Ni udhihirisho wa kazi za Mungu. Kuhusu wale ambao hawawezi kuainishwa katika mojawapo ya makundi yaliyotenganishwa na Mungu, wataorodheshwa miongoni mwa safu za wasioamini, na hakika mnaweza kuwazia matokeo yao yatakuwaje. Tayari Nimewaambia yote ambayo Ninapaswa kusema; njia mnayochagua ni chaguo lenu pekee. Kile mnachopaswa kuelewa ni hiki: Kazi ya Mungu kamwe haimsubiri mtu yeyote ambaye hawezi kwenda sambamba na Yeye, na tabia ya haki ya Mungu haionyeshi huruma kwa mwanadamu yeyote.