D. Kuhusu Mungu kama Chanzo cha Uzima wa Vitu Vyote
583. Njia ya maisha si kitu ambacho mtu yeyote anaweza kumiliki, wala si kitu ambacho mtu yeyote anaweza kufikia kwa urahisi. Hii ni kwa sababu maisha yanaweza kuja tu kutoka kwa Mungu, ambayo ni kusema, Mungu Mwenyewe tu ndiye Anamiliki mali ya maisha, hakuna njia ya maisha bila Mungu Mwenyewe, na hivyo Mungu tu ndiye chanzo cha uzima, na kijito cha maji ya uzima kinachotiririka nyakati zote. Kutoka Alipoumba dunia, Mungu amefanya kazi kubwa inayoshirikisha uhai wa maisha, Amefanya kazi kubwa ambayo huletea mwanadamu maisha, na Amelipa gharama kubwa ili mtu aweze kupata uzima, kwa kuwa Mungu Mwenyewe ni uzima wa milele, na Mungu Mwenyewe ni njia ambayo kwayo mtu hufufuliwa. Mungu kamwe hajawahi kosa kwa moyo wa mwanadamu, na Anaishi miongoni mwa binadamu wakati wote. Amekuwa nguvu ya kuendesha maisha ya mwanadamu, chanzo cha kuwepo kwa binadamu, na amana ya fahari ya kuwepo kwa binadamu baada ya kuzaliwa. Husababisha binadamu kuzaliwa upya, na kumwezesha kwa ushupavu kuishi kwa kila jukumu lake. Kwa sababu ya uwezo Wake, na nguvu ya maisha Yake yasiyopungua, binadamu ameishi kwa kizazi baada ya kizazi, ambapo nguvu ya uhai wa Mungu umekuwa uti wa mgongo wa kuwepo kwa binadamu, na ambayo Mungu amelipia gharama ambayo hakuna mtu wa kawaida amewahi kulipa. Nguvu za Mungu za maisha zinaweza kutawala juu ya nguvu zozote; zaidi ya hayo, inazidi mamlaka yoyote. Maisha Yake ni ya milele, nguvu zake za ajabu, na nguvu Zake za maisha haziwezi kuzidiwa na kiumbe yeyote au nguvu za adui. Nguvu za maisha ya Mungu zipo, na hung’aa mwangaza wake ulio mzuri sana, bila ya kujali muda au mahali. Mbingu na dunia zinaweza kupitia mabadiliko makubwa, lakini uzima wa Mungu ni ule ule daima. Mambo yote hupita, lakini maisha ya Mungu hubaki, kwa maana Mungu ni chanzo cha kuwepo kwa mambo yote, na mizizi ya kuwepo kwao. Asili ya maisha ya mwanadamu hutoka kwa Mungu, kuwepo kwa mbingu ni kwa sababu ya Mungu, na kuwepo kwa ardhi kunatokana na nguvu ya uhai wa Mungu. Hakuna kitu kinachomiliki nguvu kinachoweza kuzidi ukuu wa Mungu, na hakuna kitu chenye nguvu kinachoweza kuvunja mipaka ya mamlaka ya Mungu. Kwa njia hii, bila kujali wao ni nani, kila mtu lazima ajiwasilishe kwa utawala wa Mungu, kila mtu lazima aishi chini ya amri za Mungu, na hakuna mtu anayeweza kutoroka kutoka katika utawala Wake.
Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Ni Kristo wa Siku za Mwisho Pekee Ndiye Anayeweza Kumpa Mwanadamu Njia ya Uzima wa Milele
584. Tangu Mungu alipoviumba, kulingana na sheria ambazo Aliziamua, vitu vyote vimekuwa vikitenda kazi na vimekuwa vikiendelea kukua kwa kawaida. Chini ya uangalizi Wake, chini ya kanuni Yake, vitu vyote vimekuwa vikiendelea kwa kawaida sambamba na kuendelea kuishi kwa binadamu. Hakuna kitu hata kimoja kinaweza kubadilisha sheria hizi, na hakuna hata kitu kimoja kinachoweza kuziharibu sheria hizi. Ni kwa sababu ya kanuni ya Mungu ndipo viumbe vyote vinaweza kuongezeka, na kwa sababu ya kanuni na usimamizi Wake ndipo vitu vyote vinaweza kuendelea kuishi. Hii ni kusema kwamba chini ya kanuni ya Mungu, viumbe vyote vinakuwepo, vinastawi, vinatoweka, na kuzaliwa upya kwa namna ya mpangilio. Msimu wa machipuo unapowadia, mvua ya manyunyu huleta hisia hiyo ya machipuo na kuipatia nchi unyevunyevu. Ardhi huanza kuyeyuka, na majani huota na kujipenyeza juu ya udongo na kuanza kuchipuka, ilihali miti kwa utaratibu hubadilika kuwa ya kijani. Viumbe hai hivi vyote vinaleta uzima mpya katika dunia. Hii ndiyo picha ya viumbe vyote kuwepo na kustawi. Wanyama wa kila aina pia hutoka matunduni mwao ili kupata uvuguvugu wa msimu wa machipuo na kuanza mwaka mpya. Viumbe vyote vinaota jua kwenye joto wakati wa kiangazi na kufurahia uvuguvugu unaoletwa na msimu huu. Vinakua haraka; miti, nyasi, na aina zote za mimea inakua haraka sana, kisha inachanua na kuzaa matunda. Viumbe vyote vinakuwa vimetingwa sana wakati wa kiangazi, binadamu wakiwemo. Katika msimu wa majani kupukutika, mvua inaleta utulivu wa msimu wa majani kupukutika, na aina zote za viumbe hai vinaanza kuhisi majilio ya msimu wa kiangazi. Viumbe vyote vinazaa matunda, na binadamu wanaanza kuvuna matunda haya ya aina mbalimbali ili kuwa na chakula kwa ajili ya msimu wa baridi. Katika msimu wa baridi viumbe vyote taratibu vinaanza kupumzika katika ubaridi, kuwa kimya, na watu pia wanachukua pumziko wakati wa msimu huu. Mabadiliko haya kutoka msimu wa machipuo kwenda msimu wa kiangazi kwenda msimu wa mapukutiko na kwenda msimu wa baridi—mabadiliko haya yote yanatokea kulingana na sheria zilizoanzishwa na Mungu. Anaongoza vitu vyote na wanadamu kwa kutumia sheria hizi na amebuni maisha yenye utajiri na ya kupendeza kwa ajili ya mwanadamu, akiandaa mazingira kwa ajili ya kuendelea kuishi ambayo yana halijoto tofautitofauti na misimu tofautitofauti. Chini ya mazingira haya yaliyopangiliwa kwa ajili ya kuendelea kuishi, binadamu wanaweza kuendelea kuishi na kuongezeka kwa namna ya mpangilio. Wanadamu hawawezi kuzibadilisha sheria hizi, na hakuna mtu hata mmoja au kiumbe ambacho kinaweza kuzivunja. Ingawa mabadiliko yasiyohesabika yametokea—bahari zimekuwa mbuga, ilhali mbuga zimekuwa bahari—sheria hizi zinaendelea kuwepo. Sheria hizi zipo kwa sababu Mungu yupo, na kwa sababu ya sheria na usimamizi Wake. Kwa aina hii ya mpangilio, mazingira makubwa, maisha ya watu yanaendelea ndani ya sheria na kanuni hizi. Sheria hizi ziliendeleza kizazi baada ya kizazi cha watu na kizazi baada ya kizazi cha watu wameendelea kuishi ndani ya sheria hizi. Watu wamefurahia mazingira haya ya mpangilio kwa ajili ya kuendelea kuishi vilevile vyote miongoni mwa vingi vilivyoumbwa na Mungu kwa ajili ya kizazi baada ya kizazi cha binadamu. Ingawa watu wanahisi kwamba aina hii ya sheria ni za kiasili, ingawa wanazipuuza kabisa sheria hizo, na ingawa hawawezi kuhisi kuwa Mungu ndiye anaweka utaratibu wa sheria hizi, kwamba Mungu anatawala sheria hizi, haijalishi, Mungu siku zote anajihusisha katika kazi hii isiyobadilika. Kusudi lake katika kazi hii isiyobadilika ni kwa ajili ya binadamu kuendelea kuishi, na ili binadamu waweze kuendelea.
Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee IX
585. Mungu anaamuru sheria zinazoongoza uendeshaji wa vitu vyote; Anaamuru sheria zinazoongoza uwepo wa vitu vyote; Yeye hudhibiti vitu vyote, na huviweka kutiana nguvu na kutegemeana, ili visiangamie au kutoweka. Hivi tu ndivyo wanadamu wanaweza kuendela kuishi; ni hivyo tu ndivyo wanaweza kuishi chini ya mwongozo wa Mungu katika mazingira kama hayo. Mungu ndiye bwana wa sheria hizi za uendeshaji, na binadamu hawawezi kuingilia na hawawezi kuzibadilisha; ni Mungu Mwenyewe pekee ndiye Anajua kanuni hizi na ni Yeye pekee ndiye anazisimamia. Ni lini miti itachipuka, ni lini mvua itanyesha, ni maji kiasi gani na virutubisho kiasi gani ardhi itaipatia mimea, ni katika msimu gani majani yatapukutika, ni katika msimu gani miti itazaa matunda, jua litaipa miti virutubisho vingapi; kile ambacho miti itatoa nje baada ya kulishwa na jua—vitu hivi vyote viliamuliwa kabla na Mungu alipoumba vitu vyote, kama sheria ambazo hakuna mtu anayeweza kuvunja. Vitu vilivyoumbwa na Mungu—ama ni hai au vinaonekana kwa watu si hai—vyote vipo mikononi mwa Mungu na chini ya utawala Wake. Hakuna mtu anayeweza kubadilisha au kuvunja kanuni hii. Hii ni kusema, Mungu alipoviumba vitu vyote Aliweka kanuni ya jinsi vinavyopaswa kuwa. Miti isingeweza kuzamisha mizizi, kuchipua na kukua bila ardhi. Ardhi isingekuwa na miti, ingekauka. Pia, mti ni makazi ya chiriku, ni sehemu ambapo wanapata kujikinga dhidi ya upepo. Je, ingekuwa sawa ikiwa miti ingekuwa bila mwanga wa jua? (Isingekuwa sawa.) Ikiwa miti ingekuwa na ardhi peke yake hiyo isingefanya kazi. Hii yote ni kwa ajili ya mwanadamu na kuendelea kuishi kwa mwanadamu. Mwanadamu anapokea hewa safi kutoka kwenye miti, na anaishi katika ardhi inayomlinda. Mwanadamu hawezi kuishi bila mwanga wa jua, mwanadamu hawezi kuishi bila viumbe hai mbalimbali. Ingawa uhusiano baina ya vitu hivi ni changamani, mnapaswa kukumbuka kwamba Mungu alitengeneza kanuni ambazo zinaongoza vitu vyote ili kwamba viweze kuimarishana, kutegemeana na kuwepo pamoja. Kwa maneno mengine, kila kitu alichokiumba kina thamani na umuhimu. Ikiwa Mungu aliumba kitu bila kuwa na umuhimu, Mungu angeacha kipotee. Hii ni njia mojawapo Aliyoitumia katika kuvikimu vitu vyote.
Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee VII
586. Mungu alipoumba vitu vyote, alitumia aina zote za mbinu na njia za kuziwekea uwiano, kuweka uwiano katika mazingira ya kuishi kwa ajili ya milima na maziwa, kuweka uwiano katika mazingira ya kuishi kwa ajili ya mimea na aina zote za wanyama, ndege, wadudu—lengo Lake lilikuwa ni kuruhusu aina zote za viumbe hai kuishi na kuongezeka ndani ya sheria ambazo alikuwa Amezianzisha. Hakuna hata kimoja katika viumbe wote kinachoweza kwenda nje ya sheria, na sheria haziwezi kuvunjwa. Ni ndani ya aina hii tu ya mazingira ya msingi ndipo binadamu wanaweza kuendelea kuishi kwa usalama na kuongezeka, kizazi baada ya kizazi. Ikiwa kiumbe yeyote anakwenda zaidi ya ukubwa au mawanda yaliyoanzishwa na Mungu, au ikiwa anazidi kiwango cha ukuaji, marudio, au idadi chini ya utawala Wake, mazingira ya binadamu kwa ajili ya kuendelea kuishi yangepata uharibifu wa viwango vinavyotofautiana. Na wakati uo huo, kuendelea kuishi kwa binadamu kungetishiwa. … Ikiwa kuna aina moja au aina kadhaa za viumbe hai ambavyo vinazidi idadi yao inayofaa, hewa, halijoto, unyevunyevu, na hata vijenzi vya hewa ndani ya eneo la binadamu kwa ajili ya kuendelea kuishi litakuwa na sumu na kuharibiwa kwa viwango vinavyotofautiana. Hali kadhalika, chini ya mazingira haya, kuendelea kuishi kwa binadamu na hatma bado vitakuwa chini ya tishio la aina hiyo ya mazingira. Kwa hiyo, ikiwa watu watapoteza uwiano huu, hewa wanayovuta itaharibiwa, maji wanayokunywa yatachafuliwa, na halijoto ambayo wanahitaji pia itabadilika, itaathiriwa kwa viwango tofautitofauti. Ikiwa hiyo itatokea, mazingira kwa ajili ya kuendelea kuishi ambayo kiasili ni ya wanadamu yataandamwa na madhara na changamoto kubwa. Chini ya aina hii ya mazingira ambapo mazingira ya msingi ya binadamu kwa ajili ya kuendelea kuishi yameharibiwa, hatma na matarajio ya binadamu yatakuwa ni nini? Ni tatizo kubwa sana! Kwa sababu Mungu anajua vitu vyote ni nini kwa binadamu, wajibu wa kila aina ya kitu Alichokiumba, aina gani ya athari kinacho kwa watu, na faida kubwa kiasi gani kinaleta kwa binadamu—katika moyo wa Mungu kuna mpango kwa ajili ya haya yote na Anasimamia kila kipengele cha vitu vyote alivyoviumba, kwa hiyo kwa binadamu, kila kitu Anachofanya ni muhimu sana—vyote ni lazima. Kwa hiyo wakati unaona baadhi ya matukio ya kiikolojia miongoni mwa vitu vyote, au baadhi ya sheria za asili miongoni mwa vitu vyote, hutashuku tena ulazima wa kila kitu ambacho kiliumbwa na Mungu. Hutatumia tena maneno ya kijinga kufanya hukumu zisizokuwa na msingi juu ya mipangilio ya Mungu juu ya vitu vyote na njia zake mbalimbali za kuwakimu binadamu. Pia hutafanya mahitimisho yasiyokuwa na msingi juu ya sheria za Mungu kwa ajili ya vitu vyote ambavyo Aliviumba.
Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee IX
587. Ikiwa vitu vyote vya uumbaji vingepoteza sheria zao, visingeishi tena; ikiwa sheria za vitu vyote zingekuwa zimepotea, basi viumbe hai miongoni mwa vitu vyote visingeweza kuendelea. Wanadamu pia wangepoteza mazingira yao kwa ajili ya kuendelea kuishi ambayo wanayategemea kwa ajili ya kuendelea kuishi. Ikiwa binadamu wangepoteza hayo yote, wasingeweza kuendelea kuishi na kuongezeka kizazi baada ya kizazi. Sababu ya wanadamu kuendelea kuishi mpaka sasa ni kwa sababu Mungu amewapatia wanadamu viumbe vyote vya uumbaji kuvilea, kuwalea wanadamu kwa namna tofauti. Ni kwa sababu tu Mungu anawalea binadamu kwa namna tofauti ndio maana wameendelea kuishi mpaka sasa, kwamba wameendelea kuishi hadi siku ya leo. Kwa aina hiyo ya mazingira yasiyobadilika kwa ajili ya kuendelea kuishi ambayo ni ya kufaa na yapo katika mpangilio, aina zote za watu duniani, aina zote za jamii zinaweza kuishi ndani ya mawanda yao husika. Hakuna anayeweza kwenda zaidi ya mawanda haya au mipaka hii kwa sababu ni Mungu ambaye ameichora.
Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee IX
588. Ulimwengu wa kiroho ni sehemu muhimu, ambayo ni tofauti na ulimwengu yakinifu. Na mbona Ninasema kwamba ni muhimu? Tutalizungumzia hili kwa kina. Uwepo wa huu ulimwengu wa kiroho umeungana na ulimwengu yakinifu wa mwanadamu kwa njia isiyoweza kufumbulika. Una jukumu katika mzunguko wa uhai na mauti wa mwanadamu katika utawala wa Mungu juu ya vitu vyote; hili ndilo jukumu lake, na sababu mojawapo inayofanya uwepo wake kuwa muhimu. Kwa sababu ni mahali ambapo hapawezi kutambuliwa kwa milango mitano ya fahamu ya mwanadamu, hakuna anayeweza kubaini kwa hakika kuwepo au kutokuwepo kwake. Shughuli za ulimwengu wa kiroho zimeunganika kikamilifu na uwepo wa mwanadamu, na kwa sababu hiyo mpango wa maisha ya wanadamu pia unaathiriwa kwa kiwango kikubwa na ulimwengu wa kiroho. Je, hili linahusiana na ukuu wa Mungu? Linahusiana. Nisemapo hili, unaelewa ni kwa nini Ninajadili mada hii; Kwa sababu inahusu ukuu wa Mungu, na utawala Wake. Katika ulimwengu kama huu—ulimwengu ambao hauonekani kwa watu—kila sheria yake ya peponi, amri na mfumo wake wa utawala ni wa juu zaidi kuliko sheria na mifumo ya nchi yoyote katika ulimwengu yakinifu, na hakuna kiumbe aishiye katika ulimwengu huu anaweza kuzivunja au kujitwalia bila haki. Je, hili linahusiana na ukuu na utawala wa Mungu? Katika ulimwengu huu kuna amri wazi za utawala, sheria wazi za mbinguni, na masharti wazi. Katika viwango tofauti na katika mawanda tofauti, wasimamizi huzingatia kikamilifu katika wajibu wao na kufuata sheria na masharti, kwa kuwa wanajua matokeo ya kukiuka sheria ya mbinguni ni yapi, wanafahamu wazi jinsi ambavyo Mungu anaadhibu maovu na kutuza mazuri, na kuhusu jinsi Anavyoviendesha vitu vyote, jinsi Anavyotawala vitu vyote, na zaidi, wanaona wazi ni jinsi gani Mungu anaendesha sheria za mbinguni na masharti Yake. Je, hizi ni tofauti na ulimwengu yakinifu unaokaliwa na wanadamu? Ni tofauti kwa kiasi kikubwa. Ni ulimwengu ambao ni tofauti kabisa na ulimwengu yakinifu. Kwa kuwa kuna sheria na masharti ya mbinguni, inahusu ukuu wa Mungu, utawala, aidha, tabia ya Mungu ya kile Anacho na alicho.
Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee X
589. Mungu ameweka sheria mbalimbali za mbinguni, amri, na mifumo katika milki ya kiroho, na baada ya kutangazwa kwa hizi sheria za mbinguni, amri na mifumo, ambazo zinatekelezwa kabisa, kama zilivyopangwa na Mungu, na viumbe wenye nyadhifa rasmi mbalimbali katika ulimwengu wa kiroho, na hakuna anayethubutu kuzikiuka. Na kwa hivyo, katika Mzunguko wa uhai na mauti wa wanadamu katika dunia ya mwanadamu, mtu awe amepata mwili kama mwanadamu au mnyama, kuna sheria kwa yote mawili. Kwa kuwa sheria hizi zinatoka kwa Mungu, hakuna anayethubutu kuzivunja, wala hakuna awezaye kuzivunja. Ni kwa sababu tu ya huo ukuu wa Mungu, na kwa sababu kuna sheria hizo, ndiyo ulimwengu yakinifu uonekanao kwa mwanadamu ni wa kawaida na wenye mpangilio; ni kwa sababu tu ya ukuu wa Mungu ndipo mwanadamu anaweza kuishi kwa amani pamoja na ulimwengu mwingine ambao hauonekani kabisa kwa mwanadamu, na kuweza kuishi nao kwa amani—vitu ambavyo vyote haviwezi kutenganishwa na mamlaka ya Mungu. Baada ya maisha ya mtu ya kimwili kufa, roho bado huwa na uhai, basi ni nini kingetendeka ikiwa roho ingekosa utawala wa Mungu? Roho ingezurura kila mahali, ikiingia kila sehemu, na hata kudhuru viumbe hai katika ulimwengu wa wanadamu. Madhara hayo hayangekuwa tu kwa mwanadamu bali pia kwa mimea na wanyama—ila wa kwanza kudhuriwa wangekuwa watu. Kama hili lingetukia—roho kama hiyo ingekosa uendeshaji, na kuwadhuru watu kwa hakika, na kufanya mambo maovu kwa hakika—basi pia kungekuwa na ushughulikiaji ufaao wa roho hii katika ulimwengu wa kiroho: Ikiwa mambo yangekuwa mabaya, roho haingeendelea kuwepo, ingeangamizwa; ikiwezekana, ingewekwa mahali fulani halafu ipatiwe mwili. Yaani, utawala wa ulimwengu wa kiroho kwa roho mbalimbali umepangiliwa, na kutekelezwa kulingana na hatua na sheria. Ni kwa sababu tu ya utawala huo ndiyo ulimwengu yakinifu wa mwanadamu haujatumbukia kwenye machafuko, ndiyo mwanadamu wa ulimwengu wa kuonekana ana akili ya kawaida, urazini wa kawaida, na maisha ya kimwili yenye mpangilio. Ni baada tu ya mwanadamu kuwa na maisha ya kawaida ndiyo wale wanaoishi katika mwili wanaweza kuendelea kufanikiwa na kuzaana katika vizazi vyote.
Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee X
590. Kifo cha kiumbe hai—kuondokewa na uhai wa kimwili—kinaashiria kwamba kiumbe hai huyu ametoka katika ulimwengu yakinifu hadi ulimwengu wa kiroho, ilhali kuzaliwa kimwili kunaashiria kwamba kiumbe hai ametoka ulimwengu wa kiroho na kuja ulimwengu yakinifu kuanza kufanya kazi yake, kuchukua nafasi yake. Iwe ni kuondoka au kuwasili kwa kiumbe, vyote havitenganishwi na kazi ya ulimwengu wa kiroho. Mtu akija katika ulimwengu yakinifu, mipango kabambe na fafanuzi huwa tayari imetengenezwa na Mungu katika ulimwengu wa kiroho kuhusu atakwenda katika familia gani, atafikia enzi gani, atawasili saa ngapi, na nafasi yake. Hivyo basi, maisha yote ya mtu huyu—mambo afanyayo, na njia azichukuazo—yanasonga kulingana na mipango ya ulimwengu wa kiroho, bila hitilafu hata kidogo. Wakati ambapo maisha ya kiroho yanaisha, wakati huo, na namna na mahali ambapo yanaishia, ni wazi na yanaonekana katika ulimwengu wa kiroho. Mungu anatawala ulimwengu yakinifu, na Anatawala ulimwengu wa kiroho, na Hawezi kuchelewesha mzunguko wa kawaida wa uhai na mauti wa roho, wala Hawezi kufanya makosa katika mpangilio wa mzunguko wa uhai na mauti wa roho. Kila msimamizi katika nyadhifa rasmi katika ulimwengu wa kiroho anafanya majukumu yake na kufanya ambacho anapaswa kufanya, kulingana na maelezo na sheria za Mungu. Na kwa hiyo, katika ulimwengu wa wanadamu, kila tukio la kuonekana lishuhudiwalo na binadamu lina utaratibu, na halina vurugu yoyote. Haya yote ni kwa sababu ya utawala uliopangiliwa wa Mungu juu ya vitu vyote, hali kadhalika kwa sababu mamlaka ya Mungu yanatawala kila kitu, na kila kitu Anachokitawala kinajumuisha ulimwengu yakinifu ambamo mwanadamu anaishi, aidha, ulimwengu wa kiroho usioonekana nyuma ya mwanadamu. Na kwa hiyo, ikiwa mwanadamu anataka kuwa na maisha mazuri, na anataka kuishi katika mazingira mazuri, hali kadhalika kupewa ulimwengu yakinifu mzima, mwanadamu sharti pia apatiwe ulimwengu wa kiroho, ambao hauwezi kuonekana kwa yeyote, ambao unaongoza kila kiumbe hai kwa niaba ya mwanadamu, na ambao una utaratibu.
Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee X
591. Tangu unapoingia katika dunia hii ukilia, unaanza kutekeleza wajibu wako. Kwa kuchukua jukumu lako katika mpango wa Mungu na katika utaratibu Wake, unaanza safari yako katika maisha. Licha ya asili yako na licha ya safari iliyoko mbele yako, hakuna kitakachoepuka mpango na utaratibu ambao mbingu imeunda, na hakuna aliye na udhibiti wa hatima yake mwenyewe, kwa maana yule Anayetawala kila kitu ndiye tu Aliye na uwezo wa kazi hiyo. Tangu siku aliyoumbwa binadamu, Mungu amekuwa akitenda kazi Yake kwa njia hii, kusimamia ulimwengu huu na kuelekeza mifuatano ya mabadiliko katika mambo yote na njia ambazo yanasongea. Pamoja na vitu vyote vingine, mwanadamu polepole na bila kujua anastawishwa na utamu na mvua na umande kutoka kwa Mungu. Kama vitu vyote vingine, mwanadamu bila kujua, anaishi chini ya mpango wa mkono wa Mungu. Moyo na roho ya mwanadamu vimeshikwa katika mkono wa Mungu, na maisha yake yote yanatazamwa machoni mwa Mungu. Haijalishi kama unayaamini mambo haya au la, vitu vyote, viwe hai au vilivyokufa, vitahamishwa, vitabadilika, kufanywa vipya, na kutoweka kulingana na mawazo ya Mungu. Hii ndiyo njia ambayo Mungu huongoza vitu vyote.
Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Mungu Ndiye Chanzo cha Uhai wa Mwanadamu
592. Mungu aliumba dunia hii na kuleta mwanadamu, kiumbe hai ambaye alitia uhai ndani yake. Kisha, mwanadamu akaja kuwa na wazazi na jamaa na hakuwa mpweke tena. Tangu mwanadamu alipotua macho kwa mara ya kwanza katika dunia hii ya mali, ilibainika kuwa angeishi ndani ya utaratibu wa Mungu. Ni pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu ndiyo hustawisha kila kiumbe hai katika ukuaji wake hadi kinapokomaa. Wakati wa mchakato huu, hakuna anayehisi kwamba mwanadamu anakua chini ya uangalizi wa Mungu, bali badala yake anaamini kwamba mwanadamu anafanya hivyo chini ya utunzaji wa upendo wa wazazi wake, na kwamba ni silika yake mwenyewe ya maisha ambayo inaongoza mchakato huu wa kukua kwake. Hii ni kwa sababu mwanadamu hajui aliyeleta maisha au yalikotoka maisha hayo, sembuse jinsi silika ya maisha husababisha miujiza. Anajua tu kwamba chakula ndicho msingi wa kuendelea kwa maisha yake, kwamba uvumilivu ndio chanzo cha kuwepo kwake, na kwamba imani zilizomo akilini mwake ndizo raslimali ambazo kwazo kuendelea kuishi kwake kunategemea. Mwanadamu hajui kabisa kuhusu neema na riziki zitokazo kwa Mungu, na kwa njia hii yeye hupoteza. uzima aliopewa na Mungu bila azma…. Hakuna hata mmoja wa wanadamu hawa ambaye Mungu anamwangazia usiku na mchana huchukua jukumu la kumwabudu. Mungu anaendelea tu kufanya kazi juu ya mwanadamu, akiwa hana matarajio yoyote kutoka kwake, kama jinsi ambavyo Amepanga. Anafanya hivyo kwa matumaini kwamba siku moja, mwanadamu ataamka kutoka katika ndoto yake na ghafla kuelewa thamani na maana ya maisha, gharama aliyolipa Mungu kwa yote ambayo Amempa, na wasiwasi wa hamu ambao kwao Mungu anangoja mwanadamu amgeukie. …
Wote wanaokuja duniani humu lazima wapitie maisha na kifo, na wengi wao walipitia mzunguko wa kifo na kuzaliwa upya. Wale wanaoishi watakufa hivi karibuni na wafu watarejea karibuni. Yote haya ni mwendo wa maisha uliopangwa na Mungu kwa kila kiumbe hai. Hata hivyo, njia hii na mzunguko huu hasa ni ukweli ambao Mungu anataka binadamu aone: kwamba uzima aliopewa mwanadamu na Mungu hauna mipaka, na hauzuiliwi na maumbile ya nje, wakati, au nafasi. Hili ndilo fumbo la uzima aliopewa binadamu na Mungu, na dhihirisho kwamba maisha yalikuja kutoka Kwake. Ingawa watu wengi wanaweza kukosa kuamini kwamba maisha yalitoka kwa Mungu, binadamu bila ya kufahamu hufurahia yote yatokayo kwa Mungu, iwe wanaamini au wanakana uwepo Wake. Iwapo siku moja Mungu kwa ghafla Atabadili moyo na Atake kurudisha yote yaliyomo duniani na kuchukua maisha Aliyotoa, basi yote duniani yataisha. Mungu hutumia maisha Yake kukimu vitu vyote vilivyo hai na visivyo na uhai, na kuleta yote kwa utaratibu mzuri kwa mujibu wa uwezo na mamlaka Yake. Huu ni ukweli ambao hauwezi kuwazika au kueleweka na yeyote, na kweli hizi zisizoeleweka kwa fikira zetu ni dhihirisho halisi na ushahidi wa nguvu za Mungu katika maisha. Sasa hebu nikupe siri: Ukuu wa uzima wa Mungu na nguvu ya uzima Wake haziwezi kueleweka na kiumbe yeyote. Hivi ndivyo hali ilivyo sasa, kama ilivyokuwa awali, na itakuwa hivyo wakati ujao. Siri ya pili Nitakayotoa ni hii: Chanzo cha uhai hutoka kwa Mungu, kwa viumbe wote, bila kujali jinsi wanavyoweza kuwa tofauti katika maumbile au muundo. Hata uwe kiumbe hai wa aina gani, huwezi kwenda kinyume na njia ya maisha ambayo Mungu ameweka. Katika hali yoyote, kile Napenda ni kuwa mwanadamu kuelewa hili: Bila ulinzi, utunzaji, na utoaji wa Mungu, mwanadamu hawezi kupokea yote aliyokusudiwa kupokea, haijalishi anajaribu kwa juhudi au kupambana kwa bidii namna gani. Bila ruzuku ya uhai kutoka kwa Mungu, mwanadamu hupoteza maana ya thamani ya kuishi na madhumuni ya maana katika maisha. Mungu angewezaje kumruhusu mwanadamu, ambaye bila umakini hupoteza thamani ya uhai wake, kuishi hivyo bila ya kujali? Kama vile nimesema awali: Usisahau kwamba Mungu Ndiye chanzo cha maisha yako.
Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Mungu Ndiye Chanzo cha Uhai wa Mwanadamu
593. Mungu ndiye mtawala wa vitu vyote, na anayeendesha vitu vyote. Aliumba vitu vyote, Anaendesha vitu vyote, na pia Anatawala vitu vyote na kukimu vitu vyote. Hii ndiyo hadhi ya Mungu, na utambulisho wa Mungu. Kwa vitu vyote na vyote vilivyopo, utambulisho wa kweli wa Mungu ni Muumbaji, na Mtawala wa vitu vyote. Huo ni utambulisho unaomilikiwa na Mungu, na ni wa kipekee miongoni mwa vitu vyote. Hakuna Kati ya viumbe wa Mungu—wawe miongoni mwa wanadamu, au katika ulimwengu wa kiroho—ambao wanaweza kutumia namna yoyote au kisingizio kuiga au kuchukua nafasi ya utambulisho wa Mungu na hadhi Yake, kwa kuwa kuna mmoja tu kati ya vitu vyote anayemiliki huu utambulisho, nguvu, mamlaka, na uwezo wa kutawala vitu vyote: Mungu wetu wa kipekee Mwenyewe. Anaishi na kutembea miongoni mwa vitu vyote; Anaweza kufikia palipo mbali zaidi, juu ya vitu vyote; Anaweza kunyenyekea kwa kuwa mwanadamu, kuwa mmoja wa wenye mwili na damu, kuonana ana kwa ana na watu na kushiriki na wao dhiki na faraja; wakati huo huo, Anaamuru vitu vyote, na Huamua hatima ya vitu vyote, na njia itakayofuata, zaidi na hayo, Anaongoza hatima za wanadamu wote, na njia za wanadamu. Mungu kama huyu anastahili kuabudiwa, kuheshimiwa, na kujulikana na viumbe wote. Na hivyo, pasipo kujali uko katika kundi na aina gani ya wanadamu, kumwamini Mungu, kumfuata Mungu, kumheshimu Mungu sana, kukubali utawala wa Mungu, na kukubali mipango ya Mungu katika hatima yako ndio uamuzi wa pekee, na uamuzi unaofaa, kwa mtu yeyote, kwa kiumbe chochote kinachoishi. Katika upekee wa Mungu, watu huona kwamba mamlaka Yake, tabia Yake ya haki, kiini Chake, na namna ambazo Anakirimia vitu vyote ni za kipekee; upekee Wake unabainisha utambulisho wa kweli wa Mungu Mwenyewe, na unabaini hadhi Yake. Na kwa hivyo, miongoni mwa viumbe vyote, kama kuna kiumbe anayeishi katika ulimwengu wa kiroho au miongoni mwa wanadamu angetamani kusimama badala ya Mungu, haingewezekana, sawa na kujaribu kumuiga Mungu. Huu ni ukweli.
Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee X
594. Kazi Yangu ya mwisho si kwa ajili ya kumwadhibu mwanadamu tu bali pia kwa ajili ya kupanga hatima ya mwanadamu. Aidha, ni kwa ajili ya kupokea shukrani kutoka kwa kila mtu kwa yale yote ambayo Nimefanya. Ninataka kila mtu aone kwamba yale yote ambayo Nimefanya ni sahihi na kwamba yote ambayo Nimefanya ni dhihirisho la tabia Yangu; si kwa uwezo wa mwanadamu, sembuse ulimwengu, ambao uliwaleta wanadamu. Kinyume na hili, mimi Ndiye Ninalisha kila kiumbe miongoni mwa vitu vyote. Bila uwepo Wangu, wanadamu wataangamia tu na kusumbuka kutokana na mashambulizi ya misiba. Hamna mwanadamu atakayeona uzuri wa jua na mwezi au dunia ya kijani kibichi; wanadamu watakumbana tu na usiku wenye baridi na bonde kali la uvuli wa mauti. Mimi tu Ndiye wokovu wa wanadamu. Mimi tu ndiye tumaini la wanadamu na zaidi ya hayo; Mimi tu Ndiye mwamba wa uwepo wa wanadamu wote. Bila Mimi, wanadamu watasimama kabisa mara moja. Bila mimi, wanadamu watakumbana na msiba mkuu na kukanyagwa na mapepo wa aina yote, hata kama hamna anayenisikiliza. Nimefanya kazi ambayo haiwezi kufanywa na yeyote yule ila mimi. tumaini Langu la pekee ni kwamba mwanadamu anaweza kunilipa kwa kutenda matendo kiasi mema. Ingawa wanaoweza kunilipa ni wachache, bado Nitahitimisha safari Yangu duniani na Nianze hatua ifuatayo ya kazi Yangu inayotokea, kwa sababu kukimbia kimbia Kwangu miongoni mwa wanadamu kwa miaka hii mingi imekuwa na matokeo mazuri, na Nimefurahishwa sana. Sijali kuhusu idadi ya watu ila kuhusu matendo yao mazuri. Kwa hali yoyote ile, Ninatumaini kwamba mtatayarisha matendo mema ya kutosha kwa ajili ya hatima yenu wenyewe. Huo ndio wakati Nitakaporidhika; la sivyo, hakuna yeyote miongoni mwenu atakayepuka maafa yatakayowafikia. Maafa haya hutoka Kwangu na bila shaka Mimi ndiye Niliyeyapanga. Ikiwa hamwezi kuonekana kuwa wema mbele Yangu, basi hamtaweza kuyaepuka maafa.
Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Tayarisha Matendo Mema ya Kutosha kwa ajili ya Hatima Yako