Unapaswa Kuishi kwa Ajili ya Ukweli Kwa Kuwa Unamwamini Mungu
Tatizo la kawaida ambalo lipo ndani ya watu wote ni kwamba wanaelewa ukweli lakini wanashindwa kuutia katika vitendo. Hii ni kwa sababu, kwa upande mmoja, hawako tayari kulipa gharama, na kwa upande mwingine, kwa sababu utambuzi wao ni duni sana; hawawezi kuona matatizo mengi ya maisha ya kila siku jinsi yalivyo, na hawajui jinsi ya kutenda ipasavyo. Kwa sababu upitiaji wa watu ni wa juujuu sana, ubora wao wa tabia ni duni sana, na kiwango ambacho wanaelewa ukweli ni finyu, hawana njia ya kusuluhisha matatizo wanayokumbana nayo katika maisha yao ya kila siku. Wanamwamini Mungu kwa maneno tu, na hawawezi kumleta Mungu katika maisha yao ya kila siku. Yaani, Mungu ni Mungu, maisha ni maisha, na ni kana kwamba watu hawana uhusiano na Mungu katika maisha yao. Hivyo ndivyo kila mtu anavyofikiri. Kwa kumwamini Mungu namna hii, watu hawawezi, katika uhalisi, kupatwa na kufanywa kuwa watimilifu na Yeye. Kwa kweli, si kwamba neno la Mungu halijaonyeshwa waziwazi, bali ni kwamba uwezo wa watu wa kufahamu ni duni mno. Inaweza kusemwa kwamba karibu hakuna mtu anayetenda kulingana na nia asili za Mungu, na badala yake kila mtu anatenda kulingana na mapenzi yake mwenyewe. Kila mtu anamwamini Mungu kulingana na dhana za kidini alizokuwa nazo zamani, na mbinu zake mwenyewe. Ni wachache wanaopitia mabadiliko kufuatia kukubali neno la Mungu na kuanza kutenda kulingana na nia Zake. Badala yake, wanakataa kurudiwa na fahamu zao. Watu wanapoanza kumwamini Mungu, wanafanya hivyo kwa msingi wa kanuni za kawaida za dini, na wanaishi na kujiendesha na kushughulika na ulimwengu kikamilifu kwa msingi wa falsafa zao wenyewe za shughuli za kidunia. Mtu anaweza kusema kwamba hivi ndivyo ilivyo kwa watu tisa kati ya kila watu kumi. Kuna wachache sana ambao huunda mpango mwingine na kuanza maisha mapya baada ya kuanza kumwamini Mungu. Binadamu ameshindwa kulichukulia neno la Mungu kama ukweli, au kulitenda kama ukweli.
Chukua, kwa mfano, imani katika Yesu. Iwe mtu alikuwa ameanza kuamini hivi punde au alikuwa amefanya hivyo kwa muda mrefu sana, wote walitumia tu talanta zozote walizokuwa nazo na kuonyesha ustadi wowote waliokuwa nao. Watu waliongeza tu “imani katika Mungu,” maneno haya matatu, katika maisha yao ya kawaida, lakini hawakufanya mabadiliko yoyote kwenye tabia yao, na imani yao katika Mungu haikukua hata kidogo. Ufuatiliaji wao haukuwa moto wala baridi. Hawakusema kwamba wangeacha imani yao, lakini pia hawakumtolea Mungu kila kitu. Hawakuwa wamewahi kumpenda Mungu kweli au kumtii. Imani yao katika Mungu ilikuwa mchanganyiko wa ukweli na uwongo, waliishughulikia kwa jicho moja wazi na jicho moja limefumbwa, na hawakuichukulia kwa uzito. Waliendelea katika hali kama hiyo ya kuchanganyikiwa, na hatimaye walikufa kifo cha kukanganyika. Kuna maana gani katika hayo yote? Leo, kama muumini wa Mungu wa vitendo, lazima uingie katika njia sahihi. Katika imani yako katika Mungu, hupaswi kutafuta baraka tu; badala yake, unapaswa kufuatilia kumpenda Mungu na kumjua Mungu. Kupitia nuru Yake, kupitia ufuatiliaji wako binafsi, unapaswa kuweza kula na kunywa neno Lake, kukuza uelewa wa kweli wa Mungu, na kuwa na upendo wa kweli kwa Mungu unaotoka ndani kabisa ya moyo wako. Yaani, wakati upendo wako kwa Mungu ni wa kweli kabisa, na hakuna anayeweza kuharibu au kuzuia upendo wako Kwake, hapo ndipo unapokuwa kwenye njia sahihi katika imani yako katika Mungu. Hili linathibitisha kwamba uko upande wa Mungu, kwa maana moyo wako tayari unamilikiwa na Mungu na hakuna kitu kingine kinachoweza kukumiliki wewe. Kwa njia ya upitiaji wako, kwa njia ya gharama ambayo umelipa, na kwa njia ya kazi ya Mungu, unaweza kukuza upendo wa hiari kwa Mungu—na unapofanya hivyo, utawekwa huru kutokana na ushawishi wa Shetani na utakuja kuishi katika nuru ya neno la Mungu. Ni wakati tu ambapo umejinasua kutokana na ushawishi wa giza ndipo inaweza kusemwa kwamba umempata Mungu. Katika imani yako katika Mungu, lazima ujaribu kufuatilia lengo hili. Hili ni jukumu la kila mmoja wenu. Hakuna hata mmoja wenu anayepaswa kuridhika na hali ya mambo ya sasa. Hamwezi kuwa wenye mawazo yaliyogawanyika kuelekea kazi ya Mungu, wala hamwezi kuichukulia kwa urahisi. Mnapaswa kumfikiria Mungu katika vipengele vyote na nyakati zote, na kufanya kila kitu kwa ajili Yake. Na katika usemi na matendo yenu, mnapaswa kuweka masilahi ya nyumba ya Mungu kwanza. Ni kwa njia hii tu ndiyo mnaweza kulingana na nia za Mungu.
Katika imani yao katika Mungu, kosa kubwa kabisa la watu ni kwamba wanaamini kwa maneno tu, na Mungu hayupo kabisa katika maisha yao ya kila siku. Watu wote, kwa kweli, wanaamini katika uwepo wa Mungu, lakini Mungu si sehemu ya maisha yao ya kila siku. Vinywa vya watu hunena maombi mengi kwa Mungu, lakini Mungu ana nafasi ndogo mioyoni mwao, na hivyo Mungu huwajaribu tena na tena. Ni kwa sababu watu si safi ndiyo maana Mungu hana budi ila kuwajaribu, ili waweze kuona aibu na kuja kujijua katikati ya majaribu haya. La sivyo, binadamu wangegeuka kuwa dhuria ya malaika mkuu, na kuzidi kuwa wapotovu. Katika mchakato wa imani yao katika Mungu, kila mtu hutupa mbali nia na malengo yake mengi binafsi chini ya utakaso wa Mungu usio na kikomo. La sivyo, Mungu hangekuwa na njia ya kumtumia mtu yeyote, na hangekuwa na njia ya kufanya ndani ya watu kazi ambayo Yeye anapaswa kufanya. Mungu kwanza huwatakasa watu, na kupitia mchakato huu, wanaweza kuja kujijua na Mungu anaweza kuwabadilisha. Hapo tu ndipo Mungu anaweza kufanya uzima Wake uingie ndani yao, na kwa njia hii tu ndiyo mioyo yao inaweza kugeuzwa kikamilifu kwa Mungu. Na hivyo, kumwamini Mungu si rahisi kama watu wanavyosema. Mungu anavyoona, ikiwa una maarifa tu lakini huna neno Lake kama uzima, na ikiwa umewekewa mipaka kwa maarifa yako mwenyewe tu lakini huwezi kutenda ukweli au kuishi kwa kudhihirisha neno la Mungu, basi huu bado ni ushahidi kwamba huna moyo umpendao Mungu, na inaonyesha kwamba moyo wako hauko upande wa Mungu. Mtu anaweza kuja kumjua Mungu kwa kumwamini Yeye: Hili ndilo lengo la mwisho, na ni lengo la ufuatiliaji wa mwanadamu. Lazima utie bidii katika kuishi kwa kudhihirisha maneno ya Mungu ili yaweze kutimizwa katika utendaji wako. Ukiwa na maarifa ya mafundisho tu, basi imani yako katika Mungu itaambulia patupu. Ni ikiwa tu wewe pia unatenda na kuishi kwa kudhihirisha neno Lake ndiyo imani yako inaweza kuchukuliwa kuwa kamili na kulingana na nia za Mungu. Kwenye njia hii, watu wengi wanaweza kuzungumza kuhusu maarifa mengi, lakini wakati wao wa kufa, macho yao hujaa machozi, na wanajichukia kwa kupoteza maisha yao yote na kuishi hadi uzee bure. Wanaelewa tu mafundisho, lakini hawawezi kutia ukweli katika vitendo au kumshuhudia Mungu; wanakimbia huku na kule tu, wakiwa wamezama katika kazi, na wakiwa ukingoni mwa kifo tu ndipo hatimaye wanaona kwamba hawana ushuhuda wa kweli, kwamba hawamjui Mungu hata kidogo. Na, je, si huku ni kuchelewa mno? Kwa nini hutumii fursa ya leo na kufuatilia ukweli unaoupenda? Kwa nini usubiri hadi kesho? Ikiwa unapokuwa hai huteseki kwa ajili ya ukweli au kutafuta kuupata, inaweza kuwa kwamba unataka kuhisi majuto katika saa yako ya kufa? Ikiwa ni hivyo, basi kwa nini umwamini Mungu? Katika uhalisi, kuna mambo mengi ambayo kwayo watu wanaweza kutia ukweli katika vitendo na kumridhisha Mungu, ikiwa wataweka bidii kidogo tu. Ni kwa sababu tu akili za watu daima zimegubikwa ndiyo maana hawawezi kutenda kwa ajili ya Mungu, na kila mara wanakimbia huku na kule kwa ajili ya miili yao, bila kupata chochote mwishowe. Kwa sababu hii, watu kila mara wana shida na matatizo. Je, haya si mateso kutoka kwa Shetani? Je, huu si upotovu wa mwili? Hupaswi kujaribu kumdanganya Mungu kwa maneno matupu—lazima utende kwa kweli. Usijidanganye—hilo litakuwa na maana gani? Unaweza kupata nini kwa kuishi kwa ajili ya mwili wako na kupigania umaarufu na faida?