Kazi na Kuingia (1)
Tangu watu waanze kuikanyaga njia sahihi ya kumwamini Mungu, kumekuwa na mambo mengi ambayo bado hayajaeleweka vizuri. Bado wapo kwenye mkanganyiko kabisa kuhusu kazi ya Mungu, na kuhusu kiasi gani cha kazi wanapaswa kufanya. Hii, kwa upande mmoja, ni kwa sababu ya kuwa na uelekeo tofauti wa uzoefu wao na mipaka katika uwezo wao wa kupokea; kwa upande mwingine, ni kwa sababu kazi ya Mungu bado haijawaleta watu katika hatua hii. Kwa hiyo, kila mtu anapata utata kuhusu masuala mengi ya kiroho. Sio tu kwamba hamna uhakika kuhusu kile ambacho mnapaswa kuingia kwacho; bali pia ni wajinga kuhusu kazi ya Mungu. Hili ni zaidi ya suala la hasara kwenu. Ni dosari kubwa iliyopo kwa wale walio katika ulimwengu wa dini. Hii ndiyo sababu kuu ya watu kutomjua Mungu, na hivyo dosari hii ni kasoro ya kawaida miongoni mwa wale wote wanaomtafuta. Hakuna mtu hata mmoja aliyewahi kumjua Mungu, au amekwishawahi kuuona uso Wake halisi. Ni kwa sababu hii ndipo kazi ya Mungu inakuwa ngumu kama kazi ya kuhamisha mlima au kukausha bahari. Ni watu wangapi ambao wameyatoa maisha yao kwa ajili ya kazi ya Mungu; ni wangapi wametengwa kwa sababu ya kazi Yake; ni wangapi wameteswa hadi kufa kwa ajili ya kazi Yake; ni wangapi wamelia kwa ajili ya upendo wao kwa Mungu, wamekufa pasipo haki; ni wangapi wamekutana na mateso katili na ya kinyama…? Kwamba majanga haya yatapita—hii sio kwa sababu ya watu kutokuwa na maarifa juu ya Mungu? Inawezekanaje mtu ambaye hamjui Mungu awe na ujasiri wa kusimama mbele Yake? Inawezekanaje mtu anayemwamini Mungu na bado anamtesa awe na ujasiri wa kusimama mbele Yake? Haya si makosa kwa wale walio katika ulimwengu wa kidini pekee, bali ni makosa ya kawaida kwenu na kwao. Watu wanamwamini Mungu bila kumfahamu, ni kwa sababu hii ndio watu hawamheshimu Mungu kwa dhati, na hawamchi Yeye kwa dhati. Hata kuna wale ambao, kwa uwazi na bila haya, kwa majivuno makuu na hali, wanafanya kazi ambayo wanafikiria kichwani wenyewe katika mkondo huu, na wanaifanya kazi iliyoagizwa na Mungu kulingana na matakwa yao wenyewe na tamaa zao zisizo na kadiri. Watu wengi wanafanya ovyoovyo, hawamtukuzi Mungu bali wanafuata mapenzi yao wenyewe. Je, hii si mifano mizuri ya mioyo ya watu iliyo na ubinafsi? Je, haya hayaonyeshi dalili nyingi zaidi za udanganyifu walionao watu? Watu wanaweza kuwa wenye akili sana, lakini inawezekanaje karama zao zichukue nafasi ya kazi ya Mungu? Watu wanaweza kujali mzigo wa Mungu, lakini hawawezi kufanya mambo kwa ubinafsi sana. Je, matendo ya watu ni ya kiungu kweli? Je, mtu yeyote anaweza kuhakikishwa kwa namna chanya? Kutoa ushuhuda kuhusu Mungu kurithi utukufu Wake—huyu ni Mungu anayewatenga na kuwainua watu; kwa nafsi yao hawawezi kustahili. Kazi ya Mungu ndio kwanza imeanza, maneno Yake ndio kwanza yameanza kuzungumzwa. Katika hatua hii, watu wanajisikia vizuri katika nafsi yao wenyewe; hii haiwezi kuwa ni kujitafutia fedheha? Wanaelewa kidogo sana. Hata mwanafalsafa mwenye karama ya juu sana, mzungumzaji mzuri kabisa, hawezi kuelezea yote kuhusu uteule wa Mungu—sembuse nyinyi? Ni vyema msijione wakubwa kabisa kupita viwango vya mbinguni, badala yake jioneni kuwa watu wa chini kabisa kuliko watu razini wengine wanaotafuta kumpenda Mungu. Hii ndiyo njia ambayo mnapaswa kutumia kuingia: kujiona wadogo kuliko wengine wote. Kwa nini mjiweke katika viwango vya juu? Kwa nini mjiweke katika heshima hiyo ya juu? Katika safari ndefu ya maisha, mmepiga hatua chache tu za kwanza. Mnachokiona ni mkono wa Mungu tu, si mwili mzima wa Mungu. Ni wajibu wenu kuiona kazi ya Mungu zaidi, kugundua zaidi juu ya kile mnachopaswa kuingia ndani, kwa sababu mmebadilika kidogo sana.
Huku Mungu anapomkamilisha mwanadamu na kuigeuza tabia yake, kazi Yake kamwe haikomi, kwa kuwa wanakosa katika njia nyingi sana na wao wamepungukiwa na viwango vilivyowekwa na Yeye. Na kwa hiyo inaweza kusemwa kwamba, machoni pa Mungu, milele mtakuwa watoto waliozaliwa karibuni, wenye sifa muhimu chache sana zinazompendeza Yeye, kwa sababu ninyi ni viumbe tu mikononi mwa Mungu. Kama mtu angeingia katika ridhaa, hangechukiwa sana na Mungu? Kusema kwamba mnaweza kumridhisha Mungu leo ni kuzungumza kutoka kwa mtazamo mdogo wa miili yenu; ikiwa kweli mngelinganishwa dhidi ya Mungu, ninyi daima mngeshindwa uwanjani. Mwili wa mwanadamu haujawahi kupata ushindi. Ni kupitia tu kazi ya Roho Mtakatifu ndio inawezekana kwa mwanadamu kuwa na sifa muhimu za kukomboa. Kwa kweli, kati ya vitu vingi katika uumbaji wa Mungu, mwanadamu ni wa kiwango cha chini sana. Ingawa ni mtawala wa vitu vyote, mwanadamu ni kiumbe pekee ambaye yupo chini ya hila za Shetani, ni kiumbe pekee ambaye anashikwa kwa namna nyingi katika uharibifu wake. Mwanadamu hajawahi kuwa na ukuu juu yake mwenyewe. Watu wengi wanaishi katika uovu wa Shetani, na kuumizwa na dhihaka zake; anawaudhi kwa njia hii hata hapo watakapokuwa wamelemewa kabisa, wakistahimili kila badiliko, kila ugumu katika ulimwengu wa kibinadamu. Baada ya kuwachezea, Shetani huimaliza hatima yao. Na hivyo watu wanapita katika maisha yao yote wakiwa na mkanganyiko, wala hawajawahi kufurahia hata siku moja vitu vizuri ambavyo Mungu amewaandalia, badala yake wanajeruhiwa na Shetani na kuachwa wakiwa wameharibika kabisa. Leo wamekuwa wadhoofu na walegevu sana kiasi kwamba hawana mwelekeo wa kuzingatia kazi ya Mungu. Ikiwa watu hawana mwelekeo wa kuzingatia kazi ya Mungu, uzoefu wao utabakia kuwa vipandevipande na kutokamilika milele, na kuingia kwao kutabakia sehemu tupu milele. Katika Miaka elfu kadhaa tangu Mungu alipokuja duniani, idadi yoyote ya watu wenye mawazo ya kiburi wamekuwa wakitumiwa na Mungu kumfanyia Yeye kazikwa miaka mingi; lakini wale wanaoijua kazi Yake ni wachache sana takribani hawapo kabisa. Kwa sababu hii, idadi kubwa ya watu ambao hawajatajwa wanachukua jukumu la kumpinga Mungu wakati huo huo wanapomfanyia kazi, kwa sababu, badala ya kufanya kazi Yake, kimsingi wanafanya kazi ya mwanadamu katika nafasi waliyopewa na Mungu. Je, hii inaweza kuitwa kazi? Wanawezaje kuingia? Mwanadamu amechukua neema ya Mungu na kuizika. Kwa sababu hii, kwa karne nyingi zilizopita wale wanaofanya kazi Yake wana kuingia kwa kiwango kidogo. Hawazungumzi juu ya kuijua kazi ya Mungu kwa sababu wana ufahamu kiasi kidogo wa hekima ya Mungu. Inaweza kusemwa kwamba, ingawa kuna watu wengi wanaomtumikia Mungu, wameshindwa kuona jinsi Alivyoinuliwa, na hii ndiyo sababu watu wamejifanya wao ndio Mungu wa kuabudiwa na watu.
Kwa miaka mingi sana Mungu amebakia sirini katika uumbaji; Ameangalia katika misimu yote ya machipuko na kipupwe nyuma ya umande ufunikao; Ametazama chini kutoka mbingu ya tatu kwa siku nyingi sana; Ametembea miongoni mwa wanadamu kwa miezi na miaka mingi sana. Amekaa juu ya wanadamu wote Akisubiri kwa utulivu katika vipindi vingi vya baridi. Hajawahi kujionyesha wazi kwa mtu yeyote yule, wala kutoa sauti hata kidogo, Anaondoka bila ishara na kurudi kimyakimya. Nani anaweza kuujua uso wake halisi? Hajawahi kuzungumza na mwanadamu hata mara moja, Hajawahi kuonekana kwa mwanadamu hata mara moja. Ni rahisi kiasi gani kwa watu kufanya kazi iliyoagizwa na Mungu? Wanatambua kidogo tu kwamba kumjua Yeye ni kitu kigumu sana kuliko vitu vyote. Leo Mungu amezungumza na mwanadamu, lakini mwanadamu hajawahi kumfahamu, kwa sababu kuingia kwake katika maisha ni finyu sana na hakuna kina. Kwa mtazamo Wake, watu hawastahili kabisa kuonekana mbele za Mungu. Wana ufahamu kiasi kidogo sana juu ya Mungu na wametanga mbali Naye sana. Aidha, mioyo inayomwamini Mungu ni tatanishi sana, na hawana taswira ya Mungu ndani ya mioyo yao. Na matokeo yake ni, juhudi za Mungu zenye kubeba maumivu, na kazi Yake, kama vipande vya dhahabu vilivyofunikwa mchangani, haviwezi kutoa mwanga. Kwa Mungu, tabia, nia, na mitazamo ya watu hawa ni machukizo sana. Ni dhaifu katika uwezo wao wa kupokea, hawana hisia kiasi cha kufa ganzi, wamejishusha thamani na kuharibika, wametumikishwa kupita kiasi, ni dhaifu wasiokuwa na dhamiri, ni lazima waongozwe kama vile ng'ombe na farasi huongozwa. Kama ilivyo kuingia kwao katika roho, au kuingia katika kazi ya Mungu, hawachukui tahadhari yoyote, hawajizatiti hata kidogo kuteseka kwa ajili ya ukweli. Kwa mtu kama huyu kufanywa mkamilifu na Mungu haitakuwa rahisi. Hivyo ni muhimu kwamba mnapanga kuingia kwenu katika pembe hii—kwamba kupitia kazi yenu na kuingia kwenu ndipo mnakaribia kuijua kazi ya Mungu.