Je, Ufahamu Wenu Kuhusu Baraka Ni Upi?

Ingawa watu waliozaliwa katika enzi hii wamepotoshwa na Shetani na roho wachafu, ni kwa sababu ya upotovu huu ndiyo pia wamepata wokovu mkuu kabisa, wokovu mkuu hata zaidi ya utele wa mifugo na utajiri mkubwa alioupata Ayubu, na mkuu hata zaidi kuliko baraka ya kumwona Yehova ambayo Ayubu alipokea kufuatia majaribu yake. Ni baada tu ya Ayubu kupitia jaribu la kifo ndipo alimsikia Yehova akizungumza, akiisikia sauti Yake katika kimbunga. Hata hivyo hakuuona uso wa Yehova, na hakuijua tabia Yake. Kile ambacho Ayubu alipata kilikuwa tu utajiri wa kimaada uliotoa raha za kimwili na watoto wazuri kabisa kuliko wote katika miji yote iliyokuwa karibu, pamoja na ulinzi wa malaika wa mbinguni. Hakumwona Yehova kamwe, na ingawa aliitwa mwenye haki, hakuwahi kuijua tabia ya Yehova. Na ingawa raha za kimaada za watu wa leo, inaweza kusemwa, ni za kiwango cha chini kwa muda, au mazingira ya ulimwengu wa nje ni ya uhasama, Mimi hata hivyo Ninafunua tabia Yangu, ambayo Sijawahi kuijulisha kwa mwanadamu tangu zamani za kale na ambayo imefichika daima—pamoja na siri za enzi zilizopita—kwa watu hawa, ambao ni wa hali ya chini kabisa kuliko wote lakini ambao wamepokea wokovu Wangu mkuu zaidi. Zaidi ya hayo, hii ndiyo mara ya kwanza ambayo Nimefunua mambo haya; Sijawahi kufanya kazi kama hiyo hapo awali. Ingawa ninyi ni duni sana kuliko Ayubu, kile ambacho mmepata na kile ambacho mmeona vimepita vyake kwa mbali. Ingawa ninyi mmepitia mateso ya kila aina na mmepitia kila namna ya kuteswa, kile ambacho mmevumilia si kama majaribu ya Ayubu hata kidogo; badala yake, ni hukumu na kuadibu kunakopokewa na watu kwa sababu ya uasi wao, kwa sababu ya upinzani wao, na kwa sababu ya tabia Yangu ya haki; ni hukumu, kuadibu, na laana ya haki. Ayubu, kwa upande mwingine, alikuwa mtu mwenye haki miongoni mwa Waisraeli aliyepokea upendo mkuu na huruma ya Yehova. Hakuwa amefanya matendo yoyote maovu, na hakumpinga Yehova; badala yake, alikuwa mwaminifu katika kujitoa kwake kwa Yehova. Kwa sababu ya haki yake, alikabiliwa na majaribu, na alipitia majaribu ya moto kwa sababu alikuwa mtumishi mwaminifu wa Yehova. Watu wa leo wanakabiliwa na hukumu na laana Yangu kwa sababu ya uchafu na udhalimu wao. Ingawa kuteseka kwao si kama kule alikopitia Ayubu alipopoteza mifugo yake, mali yake, watumishi wake, watoto wake, na wale wote aliowapenda, mateso wanayopitia ni usafishaji wa moto na kuteketezwa. Na kile kinachoyafanya kuwa makali zaidi kuliko yale aliyopitia Ayubu ni kwamba majaribu kama hayo hayapunguzwi wala kuondolewa kwa sababu watu ni dhaifu; badala yake, ni ya kudumu, na yanaendelea hadi siku ya mwisho ya maisha ya watu. Hii ni adhabu, hukumu, na laana; ni kuteketezwa kusiko na huruma, na hata zaidi, ni "urithi" halali wa wanadamu. Ndicho kile ambacho watu wanastahili, na ndipo pale ambapo tabia Yangu ya haki inaonyeshwa. Huu ni ukweli unaojulikana. Hata hivyo, kile ambacho watu wamepata kimepita kwa mbali mateso wanayovumilia leo. Mateso mnayovumilia ni kikwazo tu kinachotokana na upumbavu wenu, huku kile ambacho mmepata ni kikubwa mara mia zaidi ya mateso yenu. Kulingana na sheria za Israeli katika Agano la Kale, wale wote wanaonipinga Mimi, wale wote wanaonihukumu Mimi waziwazi, na wale wote wasiofuata njia Yangu, na badala yake wananitolea dhabihu yenye kufuru kwa ujasiri, hakika wataangamizwa kwa moto hekaluni au kupigwa mawe hadi kufa na baadhi ya watu wateule, na hata dhuria ya koo zao wenyewe na jamaa wengine wa karibu watapata laana Yangu. Katika maisha yajayo, hawatakuwa huru, bali watakuwa watumwa wa watumwa Wangu, na Nitawafukuza uhamishoni miongoni mwa watu wa mataifa, na hawataweza kurudi katika nchi yao ya nyumbani. Kulingana na matendo na tabia zao, mateso yanayovumiliwa na watu wa leo hayakaribii kuwa makali kama adhabu waliyopata Waisraeli. Kusema kwamba mateso mnayopitia sasa ni malipo si bila sababu, kwa sababu ninyi kwa kweli mmevuka mipaka. Mngelikuwa Israeli, ninyi mngelikuwa wenye dhambi wa milele, na mngelikatwakatwa vipande vipande na Waisraeli kitambo na kuteketezwa kwa moto kutoka mbinguni katika hekalu la Yehova. Ni nini ambacho mmepata sasa? Mmepokea nini, na mmefurahia nini? Nimefunua tabia Yangu ya haki ndani yenu, lakini jambo muhimu kabisa ni kwamba Nimefunua uvumilivu Wangu kwa ajili ya kuwakomboa binadamu. Inaweza kusemwa kwamba kazi Niliyofanya ndani yenu ni kazi ya uvumilivu tu; inafanywa kwa ajili ya usimamizi Wangu na, hata zaidi, kwa ajili ya kufurahia kwa wanadamu.

Ingawa Ayubu alipitia majaribu ya Yehova, alikuwa tu mtu mwenye haki aliyemwabudu Yehova. Licha ya kupitia majaribu hayo, hakumlalamikia Yehova, na alithamini kukutana kwake na Yeye. Sio tu kwamba watu wa leo hawathamini uwepo wa Yehova, bali wanakataa, wanachukia, wanalalamikia, na wanadhihaki kuonekana Kwake. Je, hamjapata mengi sana? Je, mateso yenu kwa kweli yamekuwa makubwa hivyo? Je, hamjabarikiwa zaidi ya Mariamu na Yakobo? Na, je, upinzani wenu kwa kweli umekuwa mdogo hivyo? Je, inawezekana kwamba matakwa Yangu kwenu ni ya juu mno, na Nimehitaji mengi mno kutoka kwenu? Ghadhabu Yangu iliachiliwa tu juu ya wale Waisraeli walionipinga Mimi, si moja kwa moja juu yenu; kile ambacho mmepata kimekuwa tu hukumu na ufichuzi Wangu usio na huruma, pamoja na usafishaji wa moto usio na kikomo. Bila kujali haya, watu bado wananipinga na kunikanusha, na hawana hata chembe ya utii. Kuna hata baadhi ambao hujitenga na Mimi na kunikana; watu kama hao ni wabaya hata zaidi ya kundi la Kora na Dathani waliompinga Musa. Mioyo ya watu ni migumu sana, na asili zao ni za ukaidi mno. Hawabadilishi kamwe asili zao za zamani. Ninasema wamewekwa wazi kama makahaba mchana kweupe, na maneno Yangu ni makali kiasi kwamba yanaweza hata "kuudhi masikio," yakifichua asili za watu waziwazi—hata hivyo wao huitikia kwa vichwa vyao tu, humwaga machozi machache, na kujilazimisha kuhisi huzuni kidogo. Punde tu haya yanapopita, wao wanakuwa wakali kama mfalme wa wanyama wa mwituni milimani, na hawana utambuzi hata kidogo. Watu wenye tabia kama hiyo wanawezaje kujua kwamba wamebarikiwa mara mia zaidi ya Ayubu kitambo? Wanawezaje kutambua kwamba yale wanayofurahia ni baraka ambazo zimeonekana kwa nadra sana katika enzi zote, na ambazo hakuna mtu amewahi kuzifurahia hapo awali? Dhamiri za watu zinawezaje kuhisi baraka kama hizo, baraka ambazo zina adhabu ndani yazo? Kusema kweli, yote Ninayohitaji kutoka kwenu ni kwamba mweze kuwa mifano kwa ajili ya kazi Yangu, na mashahidi kwa ajili ya tabia Yangu nzima na matendo Yangu yote, na ili mweze kuwekwa huru kutokana na mateso ya Shetani. Hata hivyo watu daima huchukizwa na kazi Yangu na wanakuwa wenye uhasama kwa kazi hiyo kwa makusudi. Watu kama hao wanawezaje kukosa kunichochea Mimi nirudishe sheria za Israeli, na kuwaletea ghadhabu Niliyoileta juu ya Israeli? Ingawa kuna wengi miongoni mwenu ambao ni "wasikivu na watiifu" Kwangu, kuna wengi hata zaidi ambao ni wa aina ya kundi la Kora. Punde tu Nitakapokuwa nimepata utukufu Wangu kamili, Nitatumia moto kutoka mbinguni kuwateketeza wawe majivu. Mnapaswa kujua kwamba Sitawaadibu watu tena kwa maneno Yangu; badala yake, kabla ya kufanya kazi ya Israeli, Nitawateketeza kabisa "kundi la Kora" wanaonipinga Mimi na ambao Niliwaondosha kitambo. Binadamu hawatakuwa tena na fursa ya kunifurahia Mimi; badala yake, yote watakayoona yatakuwa ghadhabu Yangu na miali ya moto kutoka mbinguni. Nitafunua matokeo mbalimbali ya kila aina ya watu, na Nitawagawa wote katika makundi. Nitaweka kwenye kumbukumbu kila tendo lao la uasi na kisha kumaliza kazi Yangu, ili matokeo ya watu yaamuliwe kulingana na uamuzi Wangu nikiwa duniani pamoja na mitazamo yao Kwangu. Wakati huo utakapofika, hakutakuwa na chochote kinachoweza kubadilisha matokeo yao. Acha watu wafunue matokeo yao wenyewe! Kwa njia hiyo Ninaweza kukabidhi matokeo ya watu kwa Baba wa mbinguni.

Iliyotangulia: Watu Waliochaguliwa wa China Hawana Uwezo wa Kuwakilisha Kabila Lolote la Israeli

Inayofuata: Ufahamu Wako Kumhusu Mungu Ni Upi?

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp