Kubaki Bila Kubadilika katika Tabia Ni Kuwa katika Uhasama na Mungu

Katika miaka elfu kadhaa ya upotovu, watu wote wamekufa ganzi na kuwa bozibozi; wote wamekuwa mapepo waovu wanaompinga Mungu, kiasi kwamba uasi wao dhidi ya Mungu umeandikwa katika rekodi za kihistoria, na kwamba hata watu wenyewe hawana uwezo wa kutoa maelezo kamili ya matendo yao ya uasi—kwa maana wamepotoshwa sana na Shetani, na wamepotezwa na Shetani kiasi kwamba hawajui waelekee wapi. Hata leo, watu bado wanamsaliti Mungu. Wanapomwona Mungu, wanamsaliti, na wakati hawawezi kumwona Mungu, vivyo hivyo wanamsaliti. Hata kuna wale ambao, baada ya kushuhudia laana za Mungu na ghadhabu ya Mungu, bado wanamsaliti. Na hivyo Ninasema kwamba busara ya mwanadamu imepoteza kazi yake ya asili, na kwamba dhamiri ya mwanadamu, pia, imepoteza kazi yake ya asili. Machoni Pangu, watu wote ni wanyama waliovalia mavazi ya binadamu na nyoka wenye sumu. Haijalishi wanajaribu kuonekana wa kuhurumiwa kiasi gani mbele ya macho Yangu, Sitawahi kuwa na rehema kwao, kwa maana hawana ufahamu kabisa wa tofauti kati ya weusi na weupe, na hakuna hata mmoja wao anayeelewa tofauti kati ya ukweli na yasiyo ya kweli. Busara yao imekufa ganzi sana, lakini bado wanatamani kupata baraka; ubinadamu wao ni duni sana, lakini bado wanatamani kutawala kama wafalme na kushikilia mamlaka. Wanaweza kuwa wafalme wa nani, wakiwa na busara kama hiyo? Wanawezaje kuketi kwenye viti vya enzi wakiwa na ubinadamu kama huo? Watu kwa kweli hawana aibu! Wao ni watu duni wanaojikadiria kupita kiasi! Ninapendekeza kwamba ninyi mnaotamani kupata baraka kwanza mtafute kioo na mtazame taswira yenu wenyewe mbaya. Je, una kile kinachohitajika kuwa mfalme? Je, una sura ya mtu anayeweza kupokea baraka? Hakujakuwa na mabadiliko hata kidogo katika tabia yako na hujaweza kutia ukweli wowote katika vitendo, lakini bado unatamani kesho nzuri. Huku ni kujidanganya kabisa! Mwanadamu, ambaye alizaliwa katika nchi chafu kama hii, ameambukizwa na jamii kwa kiwango kikubwa, ameshawishiwa na maadili ya kikabaila, na amepokea elimu ya “taasisi za elimu ya juu.” Fikira duni, maadili potovu, mtazamo ulioshushwa hadhi kuhusu maisha, falsafa za shughuli za kidunia zinazostahili dharau, uwepo usio na thamani kabisa, na desturi duni na maisha ya kila siku—mambo haya yote yamekuwa yakiingilia sana moyo wa mwanadamu, na yamekuwa yakiiharibu na kuishambulia sana dhamiri yake. Kama matokeo, mwanadamu anazidi kuwa mbali na Mungu, na anazidi kumpinga. Tabia ya mwanadamu inazidi kuwa katili siku baada ya siku, na hakuna hata mtu mmoja ambaye anajinyima chochote kwa hiari kwa ajili ya Mungu, hakuna hata mtu mmoja ambaye anamtii Mungu kwa hiari, sembuse mtu mmoja ambaye anatafuta kuonekana kwa Mungu kwa hiari. Badala yake, mwanadamu anafuatilia anasa kadiri ya matamanio ya moyo wake chini ya nguvu za Shetani, na kuupotosha mwili wake matopeni bila kujali. Hata wanaposikia ukweli, wale wanaoishi gizani hawana hamu ya kuutenda, na hawana mwelekeo wa kutafuta hata wanapoona kwamba Mungu tayari ameonekana. Mwanadamu aliyeharibika tabia kama huyu angeweza vipi kuwa na nafasi yoyote ya wokovu? Mwanadamu aliyeoza kama huyu angeweza vipi kuishi katika nuru?

Kubadilisha tabia ya mwanadamu kunapaswa kuanza na maarifa ya kiini chake na kupitia mabadiliko katika fikira zake, asili, na mtazamo wa kiakili—kupitia mabadiliko ya kimsingi. Ni kwa njia hii tu ndiyo mabadiliko ya kweli yatafikiwa katika tabia ya mwanadamu. Chanzo cha tabia potovu kuibuka ndani ya mwanadamu ni upotoshaji, upotovu, na utiaji sumu wa Shetani. Mwanadamu amefungwa na kudhibitiwa na Shetani, na fikira, maadili, umaizi, na busara yake vyote vimeharibiwa sana na Shetani. Ni kwa sababu hasa vitu vya kimsingi vya mwanadamu vimepotoshwa na Shetani, na ni tofauti kabisa na jinsi Mungu alivyoviumba hapo awali, ndiyo maana mwanadamu anampinga Mungu na hawezi kuukubali ukweli. Hivyo, ili kuwe na mabadiliko katika tabia ya mwanadamu, kile kinachopaswa kufanywa kwanza ni kubadilisha maarifa yake kumhusu Mungu na maarifa yake kuhusu ukweli katika nyanja za fikira, umaizi, na busara yake. Wale waliozaliwa katika nchi zilizopotoshwa zaidi kuliko zote ni wajinga hata zaidi kuhusu kile Mungu alicho, au maana ya kumwamini Mungu. Kadiri watu wanavyokuwa wapotovu zaidi, ndivyo wanavyojua kidogo zaidi kuhusu uwepo wa Mungu, na ndivyo busara na umaizi wao unavyokuwa duni zaidi. Chanzo cha upinzani na uasi wa mwanadamu dhidi ya Mungu ni kupotoshwa kwake na Shetani. Kwa sababu ya kupotoshwa na Shetani, dhamiri ya mwanadamu imekufa ganzi, yeye ni mpotovu kimaadili, fikira zake zimepotoka, na ana mtazamo duni wa kiakili. Kabla hajapotoshwa na Shetani, mwanadamu hapo awali alimtii Mungu na kuyatii maneno Yake baada ya kuyasikia. Hapo awali alikuwa na busara na dhamiri timamu, na ubinadamu wa kawaida. Baada ya mwanadamu kupotoshwa na Shetani, busara, dhamiri, na ubinadamu wake wa asili vyote vilikufa ganzi na vikaharibiwa na Shetani. Hivyo, amepoteza utii na upendo wake kwa Mungu. Busara ya mwanadamu imekuwa isiyo ya kawaida, tabia yake imekuwa sawa na ile ya mnyama, na uasi wake dhidi ya Mungu unazidi kuongezeka na kuwa mbaya zaidi. Lakini bado mwanadamu hajui wala haelewi hili, na anapinga na kuasi tu bila kukoma. Ufichuzi wa tabia ya mwanadamu ni maonyesho ya busara, umaizi, na dhamiri yake. Kwa sababu busara na umaizi wake si timamu, na dhamiri yake imekufa ganzi kupindukia, tabia yake ni ya uasi dhidi ya Mungu. Ikiwa busara na umaizi wa mwanadamu haviwezi kubadilika, basi mabadiliko katika tabia yake hayawezekani, na vilevile kulingana na nia za Mungu hakuwezekani. Ikiwa busara ya mwanadamu si timamu, basi hawezi kumtumikia Mungu na si mwenye kustahili kutumiwa na Mungu. “Busara ya kawaida” inarejelea kumtii na kuwa mwaminifu kwa Mungu, kumtamani Mungu, kujitoa kikamilifu kwa Mungu, na kuwa na dhamiri kumwelekea Mungu. Inarejelea kuwa na moyo na nia moja kumwelekea Mungu, na kutompinga Mungu kwa makusudi. Kuwa na busara isiyo ya kawaida si hivi. Baada ya kupotoshwa na Shetani, mwanadamu amekuwa na fikira kuhusu Mungu, na hana uaminifu kwa Mungu au kumtamani, sembuse kuwa na dhamiri kumwelekea Mungu. Mwanadamu anampinga Mungu kwa makusudi na kumhukumu, na, zaidi ya hayo, anamtukana kisogoni Mwake. Mwanadamu anamhukumu Mungu kisogoni Mwake, akijua fika kwamba Yeye ni Mungu; mwanadamu hana nia kabisa ya kumtii Mungu, bali anaendelea tu kutoa matakwa na maombi Kwake. Watu kama hao—watu walio na busara isiyo ya kawaida—hawawezi kujua matendo yao wenyewe ya kudharauliwa au kujutia matendo yao ya uasi. Watu wakiweza kujijua, basi wamepata tena busara yao kidogo; kadiri watu wanavyokuwa waasi dhidi ya Mungu na bado hawajijui, ndivyo busara yao inavyokuwa si timamu.

Ufichuzi wa tabia potovu ya mwanadamu ina chanzo chake katika dhamiri iliyokufa ganzi ya mwanadamu, asili yake ya kudhuru, na busara yake isiyo timamu; ikiwa dhamiri na busara za mwanadamu zinaweza kuwa za kawaida tena, basi atakuwa mtu anayefaa kutumiwa mbele za Mungu. Ni kwa sababu tu dhamiri ya mwanadamu imekufa ganzi sikuzote, na kwa sababu busara ya mwanadamu haijawahi kuwa timamu na inazidi kufa ganzi, ndiyo maana matendo ya uasi ya mwanadamu dhidi ya Mungu yanaongezeka, kiasi kwamba hata alimsulubisha Yesu msalabani na anaufungia mlango mwili wa Mungu mwenye mwili katika siku za mwisho, na anauhukumu mwili wa Mungu, na kuuona mwili wa Mungu kama duni. Kama mwanadamu angekuwa na ubinadamu kidogo tu, hangekuwa katili sana katika kuutendea mwili wa Mungu mwenye mwili; kama angekuwa na busara kidogo tu, hangekuwa na ukatili sana katika kuutendea mwili wa Mungu mwenye mwili; kama angekuwa na dhamiri kidogo tu, hangetoa “shukrani” kwa Mungu mwenye mwili kwa njia hii. Mwanadamu anaishi katika enzi ya Mungu kupata mwili, lakini hamshukuru Mungu kwa kumpa fursa nzuri kama hiyo, na badala yake analaani kuja kwa Mungu, au anapuuza kabisa ukweli wa Mungu kupata mwili, akionekana kuupinga na kuuchukia. Haijalishi jinsi mwanadamu anavyochukulia kuja kwa Mungu, Mungu amekuwa akifanya kazi Yake sikuzote, bila kuchoka kuifanya kamwe—ingawa mwanadamu hajamkaribisha hata kidogo, na anaendelea kutoa maombi Kwake. Tabia ya mwanadamu imekuwa yenye uovu kupindukia, busara yake imekufa ganzi kupindukia, na dhamiri yake imekanyagwa kabisa na yule mwovu na iliacha kuwa dhamiri ya asili ya mwanadamu kitambo. Mwanadamu si tu kwamba hana shukrani kwa Mungu mwenye mwili kwa kumkirimia binadamu uzima na neema nyingi sana, bali hata anamchukia Mungu kwa sababu ya ukweli anaomkirimu; kwa sababu mwanadamu hapendezwi na ukweli, anamchukia Mungu. Si tu kwamba mwanadamu hawezi kuyatoa maisha yake kwa ajili ya Mungu mwenye mwili, bali badala yake anajaribu kupata upendeleo kutoka Kwake, na anadai malipo ambayo ni dazeni mara kadhaa zaidi ya kile ambacho mwanadamu amempa Mungu. Hivi ndivyo dhamiri na busara ya mwanadamu ilivyo, lakini bado anafikiri hili si jambo kubwa, bado akiamini kwamba amejitumia mno kwa ajili ya Mungu, na kwamba Mungu amempa kidogo mno. Kuna watu ambao, baada ya kunipa bakuli la maji, wananyoosha mikono yao na kudai Niwalipe kwa mabakuli mawili ya maziwa, au, baada ya kunipa chumba kwa usiku mmoja, wanadai Nilipe ada za malazi mara nyingi zaidi. Kwa ubinadamu kama huo na dhamiri kama hiyo, mnawezaje bado kutamani kupata uzima? Ninyi ni watu duni wa kudharauliwa kama nini! Ubinadamu wa aina hii ndani ya mwanadamu na dhamiri ya aina hii ndani ya mwanadamu ndivyo vinavyosababisha Mungu mwenye mwili atangatange kote nchini, bila mahali pa kupata hifadhi. Sembuse ukweli kwamba Mungu mwenye mwili amefanya kazi nyingi sana, hata kama Hangefanya kazi yoyote kabisa, wale walio na dhamiri na ubinadamu kweli wanapasa kumwabudu na kumtumikia kwa moyo wote. Hiki ndicho kinachopaswa kufanywa na wale walio na busara timamu, na ni wajibu wa mwanadamu. Watu walio wengi hata wanazungumzia masharti katika utumishi wao kwa Mungu. Hawajali kama Yeye ni Mungu au mwanadamu, na wanazungumzia tu masharti yao wenyewe, na wanatafuta tu kuridhisha matamanio yao wenyewe. Mnaponipikia, mnadai ada ya huduma, mnaponifanyia shughuli, mnaomba ada za kushughulika, mnaponifanyia kazi mnadai ada za kazi, mnaponifulia nguo Zangu mnadai ada za dobi, mnapotoa mahitaji kwa ajili ya kanisa mnadai gharama za kujijenga kiafya, mnapozungumza mnadai ada za mzungumzaji, mnapogawa vitabu mnadai ada za usambazaji, na mnapoandika mnadai ada za uandishi. Wale ambao Nimewapogoa hata wanadai fidia kutoka Kwangu, huku wale ambao wametumwa nyumbani wakidai fidia kwa uharibifu wa jina lao; wale wasio na ndoa wanadai mahari, au fidia kwa ujana wao uliopotea; wale wanaochinja kuku wanadai ada za mchinjaji, wale wanaokaanga chakula wanadai ada za kukaanga, na wale wanaotengeneza supu wanadai malipo kwa hilo, pia…. Huu ni ubinadamu wenu wa juu sana na mkuu, na haya ni matendo ambayo dhamiri yenu kunjufu inaamuru. Iko wapi busara yenu? Uko wapi ubinadamu wenu? Acheni niwaambie! Mkiendelea hivi, Nitaacha kufanya kazi kati yenu. Sitafanya kazi kati ya kundi la wanyama waliovalia mavazi ya kibinadamu, Sitateseka hivi kwa ajili ya kikundi cha watu kama hicho ambao nyuso zao nzuri zinaficha mioyo ya kinyama, Sitavumilia kwa ajili ya kundi la wanyama kama hilo ambalo halina uwezekano hata kidogo wa wokovu. Siku Nitakapowapa kisogo ni siku mtakayokufa, ni siku ambayo giza litawajia, na siku ambayo mtaachwa na nuru. Acheni Niwaambie! Sitawahi kuwa mwema kwa kikundi kama chenu, kikundi ambacho ni duni hata kuliko wanyama! Kuna mipaka kwa maneno na matendo Yangu, na jinsi ubinadamu na dhamiri yenu ilivyo, Sitafanya kazi zaidi tena, kwa maana mmekosa dhamiri mno, mmenisababishia maumivu mengi mno, na matendo yenu ya kudharauliwa yananichukiza mno. Watu kama hao ambao hawana ubinadamu na dhamiri hawatakuwa na nafasi ya wokovu kamwe; Siwezi kamwe kuwaokoa watu wasio na moyo na wasio na shukrani namna hii. Siku Yangu itakapofika, Nitanyesha miali Yangu ya moto mkali kwa umilele wote juu ya wana wa uasi ambao wakati mmoja walichokoza ghadhabu Yangu kali, Nitaweka adhabu Yangu ya milele juu ya wanyama hao ambao wakati mmoja walinitukana na kuniacha, Nitawateketeza kwa wakati wote kwa moto wa hasira Yangu wana wa uasi ambao wakati mmoja walikula na kuishi pamoja na Mimi lakini hawakuniamini, ambao walinitukana na kunisaliti. Nitawaweka wale wote waliochokoza hasira Yangu chini ya adhabu Yangu, nitanyesha hasira Yangu yote juu ya wanyama hao ambao wakati mmoja walitamani kusimama kando Yangu kama walio sawa na Mimi lakini hawajawahi kuniabudu au kunitii; fimbo ambayo kwayo Ninampiga mwanadamu itawaangukia wanyama hao ambao wakati mmoja walifurahia utunzaji Wangu na wakati mmoja walifurahia siri Nilizozinena, na ambao wakati mmoja walijaribu kuchukua starehe za kimaada kutoka Kwangu. Sitakuwa na msamaha kwa mtu yeyote anayejaribu kuchukua nafasi Yangu; Sitamhurumia yeyote kati ya wale wanaojaribu kuninyang'anya chakula na nguo. Kwa sasa, mnabaki salama salimini na mnaendelea kupita mipaka katika matakwa mnayotoa Kwangu. Siku ya ghadhabu itakapofika, hamtatoa matakwa yoyote tena Kwangu; wakati huo, Nitawaacha “mfurahie” kadiri ya matamanio ya mioyo yenu, Nitazilazimisha kwa nguvu nyuso zenu ardhini, na hamtaweza kuinuka tena kamwe! Ipo siku, “Nitawalipa” deni hili—na Ninatumai mtasubiri kwa uvumilivu kuwasili kwa siku hii.

Ikiwa watu hawa wa kudharauliwa wanaweza kweli kuweka kando matamanio yao ya kupita kiasi na kumrudia Mungu, basi bado wana nafasi ya wokovu; mwanadamu akiwa na moyo unaomtamani Mungu kweli, basi hataachwa na Mungu. Mwanadamu anashindwa kumpata Mungu si kwa sababu Mungu ana hisia za nyama, au kwa sababu Mungu hataki kupatwa na mwanadamu, bali ni kwa sababu mwanadamu hataki kumpata Mungu, na kwa sababu mwanadamu hana moyo unaomtafuta Mungu kwa dharura. Mmoja wa wale wanaomtafuta Mungu kweli angewezaje kulaaniwa na Mungu? Mtu aliye na busara timamu na dhamiri nyeti angewezaje kulaaniwa na Mungu? Mtu anayemwabudu na kumtumikia Mungu kweli anawezaje kuteketezwa na moto wa ghadhabu Yake? Mtu aliye tayari kumtii Mungu anawezaje kufukuzwa kutoka katika nyumba ya Mungu? Mtu anayehisi kwamba hawezi kumpenda Mungu vya kutosha kamwe anawezaje kuishi katika adhabu ya Mungu? Mtu aliye tayari kuacha kila kitu kwa ajili ya Mungu anawezaje kuachwa bila chochote? Mwanadamu hayuko tayari kumfuatilia Mungu, hayuko tayari kutumia mali yake kwa ajili ya Mungu, na hayuko tayari kutoa juhudi za maisha yake yote kwa Mungu; badala yake, anasema kwamba Mungu amevuka mipaka, kwamba mambo mengi mno kumhusu Mungu yanapingana na fikira za mwanadamu. Kukiwa na ubinadamu kama huu, hata kama mnafanya juhudi bila kujibakiza bado hamwezi kupata kibali cha Mungu, sembuse ukweli kwamba hamumtafuti Mungu. Je, hamjui kwamba ninyi ni bidhaa zenye kasoro za wanadamu? Je, hamjui kwamba hakuna ubinadamu ulio duni zaidi kuliko wenu? Je, hamjui kile ambacho wengine wanawaita ili “wawaheshimu”? Wale wanaompenda Mungu kweli wanawaita baba wa mbwa mwitu, mama wa mbwa mwitu, mwana wa mbwa mwitu, na mjukuu wa mbwa mwitu; ninyi ni wazao wa mbwa mwitu, watu wa mbwa mwitu, na mnapasa kujua utambulisho wenu wenyewe na msiusahau kamwe. Msifikiri kwamba ninyi ni watu fulani wakuu: Ninyi ni kikundi kikatili zaidi cha wasio binadamu miongoni mwa wanadamu. Je, hamjui lolote kati ya haya? Je, mnajua Nimejiweka hatarini kiasi gani kwa kufanya kazi kati yenu? Ikiwa busara yenu haiwezi kuwa ya kawaida tena, na dhamiri yenu haiwezi kufanya kazi kwa kawaida, basi hamtawahi kuwa huru kutoka kwa jina “mbwa mwitu,” hamtawahi kuepuka siku ya laana na hamtawahi kuepuka siku ya adhabu yenu. Mlizaliwa duni, kitu kisicho na thamani yoyote. Kwa asili ninyi ni kundi la mbwa mwitu wenye njaa, rundo la vifusi na takataka, na, tofauti nanyi, Sifanyi kazi ndani yenu kwa ajili ya faida ya kibinafsi, bali kwa sababu ya hitaji la kazi. Kama mtaendelea kuwa waasi kwa njia hii, basi Nitaacha kazi Yangu, na Sitafanya kazi ndani yenu tena kamwe; kinyume na hilo, Nitahamishia kazi Yangu kwa kikundi Ninachokipenda, na kwa njia hii Nitawaacha milele, kwa sababu siko tayari kuwaona wale walio katika uhasama na Mimi. Hivyo basi, je, mnatamani kulingana na Mimi, au kuwa katika uhasama dhidi Yangu?

Iliyotangulia: Je, Wewe ni Mtu Ambaye Amekuja katika Uzima?

Inayofuata: Watu Wote Wasiomjua Mungu Ni Watu Wanaompinga Mungu

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp