Kazi ya Kueneza Injili Pia Ni Kazi ya Kumwokoa Mwanadamu

Watu wote wanahitaji kuelewa makusudi ya kazi Yangu duniani, yaani, kile Ninachokusudia kupata hatimaye, na ni kiwango gani Ninachopaswa kufikia katika kazi hii kabla haijakamilika. Ikiwa, baada ya kutembea na Mimi hadi leo, watu hawaelewi kazi Yangu inahusu nini hasa, basi, je, hawajatembea na Mimi bure? Watu wakinifuata, wanapaswa kujua nia Zangu. Nimekuwa nikifanya kazi duniani kwa maelfu ya miaka, na hadi leo, Ninaendelea kutekeleza kazi Yangu namna hii. Ingawa kazi Yangu iko na miradi mingi, makusudi yake bado hayajabadilika; ingawa Nimejawa na hukumu na kuadibu kuelekea mwanadamu, kwa mfano, kile Ninachofanya bado ni kwa ajili ya kumwokoa, na kwa ajili ya kueneza injili Yangu vizuri zaidi na kupanua kazi Yangu vizuri zaidi miongoni mwa Mataifa yote punde tu mwanadamu anapofanywa kuwa kamili. Kwa hivyo leo, wakati ambapo watu wengi wamevunjika moyo sana kwa muda mrefu, bado Ninaendelea na kazi Yangu, Ninaendelea na kazi Ninayopaswa kufanya ya kumhukumu na kumwadibu mwanadamu. Licha ya ukweli kwamba mwanadamu amechoshwa na kile Ninachosema, na hana hamu ya kujihusisha na kazi Yangu, bado Ninatekeleza kazi ambayo ni wajibu Wangu, kwa kuwa makusudi ya kazi Yangu hayajabadilika, na mpango Wangu wa asili hautavunjwa. Makusudi ya hukumu Yangu ni kumwezesha mwanadamu anitii vyema zaidi, na makusudi ya kuadibu Kwangu ni kumwezesha mwanadamu afikie mabadiliko vyema zaidi. Ingawa kila kitu Ninachofanya ni kwa ajili ya usimamizi Wangu, Sijawahi kufanya kazi yoyote ambayo haikuwa na manufaa kwa mwanadamu, kwa maana Ninakusudia kuyafanya mataifa yote yaliyo nje ya Israeli yawe matiifu kama Waisraeli, kuwafanya wawe wanadamu halisi, ili Niweze kuwa na mahali pa kuweka mguu katika nchi zilizo nje ya Israeli. Huu ndio usimamizi Wangu; ni kazi Yangu miongoni mwa Mataifa. Hata sasa, watu wengi bado hawaelewi usimamizi Wangu, kwa sababu hawajali kuhusu mambo kama hayo, na badala yake wanajali kuhusu mustakabali na hatima zao wenyewe. Haijalishi Ninasema nini, watu wanabaki wasiojali kazi Ninayofanya, badala yake wakizingatia kwa moyo wote hatima zao za baadaye. Mambo yakiendelea kwa njia hii, kazi Yangu inaweza kueneaje? Injili Yangu inaweza kuhubiriwaje ulimwenguni kote? Ninyi mnapaswa kujua kwamba kazi Yangu inapoenea, Nitawatawanya ninyi, na kuwapiga ninyi kama vile Yehova alivyopiga kila mojawapo ya makabila ya Israeli. Haya yote yatafanywa ili injili Yangu iweze kuenea duniani kote, ili kazi Yangu iweze kuenea katika Mataifa, hivyo kuliwezesha jina Langu litukuzwe kama kuu miongoni mwa watu wazima na watoto pia, na jina Langu takatifu lisifiwe vinywani mwa watu kutoka makabila na mataifa yote. Katika enzi hii ya mwisho, acha jina Langu litukuzwe kama kuu miongoni mwa Mataifa, acha matendo Yangu yaonekane na watu wa Mataifa, na waniite Mwenyezi kwa sababu ya matendo Yangu, na acha maneno Yangu yatimie hivi karibuni. Nitawafanya watu wote wajue kwamba Mimi si Mungu wa Waisraeli tu, bali pia Mungu wa watu wa Mataifa yote, hata yale mataifa ambayo Nimeyalaani. Nitawafanya watu wote waone kwamba Mimi ndimi Mungu wa viumbe wote walioumbwa. Hii ndiyo kazi Yangu kuu zaidi, makusudi ya mpango Wangu wa kazi kwa ajili ya siku za mwisho, na kazi pekee Ninayokusudia kuitimiza katika siku za mwisho.

Ni wakati wa siku za mwisho tu ambapo kazi ambayo Nimekuwa nikiisimamia kwa maelfu ya miaka inafunuliwa kikamilifu kwa mwanadamu. Ni sasa tu ndipo Nimefichua siri kamili ya usimamizi Wangu kwa mwanadamu, na mwanadamu amejifunza makusudi ya kazi Yangu na, zaidi ya hayo, amefikia kuelewa siri Zangu zote. Tayari Nimemwambia mwanadamu kila kitu kuhusu hatima anayojali kuhusu. Tayari Nimemfunulia mwanadamu siri Zangu zote, siri ambazo zilikuwa zimefichwa kwa zaidi ya miaka 5,900. Yehova ni nani? Masihi ni nani? Yesu ni nani? Ninyi mnapaswa kujua haya yote. Majina haya ni hatua za mabadiliko makuu ya kazi Yangu. Je, ninyi mmeelewa hilo? Jina Langu takatifu linapaswa kutangazwaje? Jina Langu linapaswa kuhubiriwaje kwa taifa lolote ambalo limeniitia kwa jina Langu lolote? Kazi Yangu inaenea, na Nitaeneza yote kwa taifa lolote na mataifa yote. Kwa kuwa kazi Yangu imetekelezwa kwenu, Nitawapiga ninyi kama vile Yehova alivyowapiga wachungaji wa nyumba ya Daudi katika Israeli, nikiwafanya mtawanywe miongoni mwa kila taifa. Kwa maana katika siku za mwisho, Nitaiponda kila nchi vipandevipande na kuwafanya watu waliomo wagawanywe upya miongoni mwa makabila na mataifa. Nitakaporudi tena, nchi zote zitakuwa tayari zimegawanywa kwa kufuata mipaka iliyowekwa na miali Yangu inayowaka. Wakati huo, Nitawatokea wanadamu upya kama jua linalochoma na Nitajionyesha waziwazi kwao katika mfano wa Mtakatifu ambao hawajawahi kuuona hapo awali, Nikitembea miongoni mwa mataifa mengi, kama vile Mimi, Yehova, nilivyowahi kutembea miongoni mwa makabila mbalimbali ya Kiyahudi. Kuanzia wakati huo na kuendelea, Nitawaongoza wanadamu katika maisha yao duniani, na hakika wataona kwamba utukufu Wangu uko juu yao, na kwamba nguzo ya wingu angani inawaongoza katika maisha yao, kwa maana Nitaonekana katika mahali patakatifu. Mwanadamu ataona siku Yangu ya haki, na pia kuonekana kwa utukufu Wangu. Huo ndio wakati ambapo Nitatawala kama Mfalme juu ya dunia nzima na kuwaleta wana Wangu wengi katika utukufu. Watu watasujudu kote duniani, na hema Langu litasimamishwa imara miongoni mwa wanadamu, likijengwa juu ya mwamba wa kazi Yangu ya leo. Watu wote pia watanitumikia hekaluni. Madhabahu, iliyojaa kwa vitu vichafu na vya kuchukiza, itavunjwa vipandevipande na kujengwa upya na Mimi. Wanakondoo na ndama wachanga watarundikwa juu ya madhabahu hiyo takatifu. Nitabomoa hekalu la leo na hakika Nitajenga jipya. Hekalu ambalo limesimama sasa, ambalo limejaa watu wa kuchukiza, litaporomoka, na lile Ninalolijenga litajazwa na watumishi waliojitolea Kwangu. Watasimama kwa mara nyingine tena na Kunitumikia kwa ajili ya utukufu wa hekalu Langu. Hakika ninyi mtaona siku Ninapopata utukufu mkuu, pamoja na siku Ninapobomoa hekalu na kujenga jipya. Hakika ninyi pia mtaona siku ya kuja kwa hema Langu miongoni mwa wanadamu. Kwa namna ileile Ninavyovunja hekalu, Nitaleta hema Langu miongoni mwa wanadamu, kama vile tu wanavyotazama kushuka Kwangu. Baada ya kuiponda kila nchi, Nitazikusanya pamoja upya, kuanzia hapo Nikijenga hekalu Langu na kuanzisha madhabahu Yangu, na hivyo watu wote wanaweza kunitolea dhabihu, kunitumikia katika hekalu Langu, na kuonyesha kujitoa kwao kwa kazi Ninayofanya katika Mataifa. Watakuwa kama Waisraeli wa siku hizi, wakiwa wamevalia mavazi ya kikuhani na taji za kifahari, wakiwa na utukufu Wangu, Yehova, katikati yao, na uadhama Wangu ukiwa pamoja nao katika anga za juu. Kazi Yangu katika Mataifa pia itakuwa vivyo hivyo. Kama vile kazi Yangu katika Israeli ilivyokuwa, ndivyo kazi Yangu katika Mataifa itakavyokuwa, kwa sababu Nitaeneza kazi Yangu katika Israeli na kuipanua kwa nchi za Mataifa.

Sasa ndio wakati ambapo Roho Wangu anafanya kazi kuu, na wakati ambapo Ninaanza kazi Yangu miongoni mwa Mataifa. Zaidi ya hayo, ni wakati ambapo Ninawaainisha viumbe wote walioumbwa, Nikimweka kila mmoja katika kundi lake husika, ili kazi Yangu iweze kuendelea kwa haraka zaidi na iwe na uwezo zaidi wa kupata matokeo. Na hivyo, kile Ninachotaka kwako bado ni kwamba utoe nafsi yako yote kwa kazi Yangu yote, na, hata zaidi, kwamba utambue waziwazi na uone kwa usahihi kazi yote ambayo Nimefanya kwako, na utumie nguvu zako zote ili kazi Yangu iweze kupata matokeo makubwa zaidi. Hiki ndicho unachopaswa kuelewa. Acha kushindana na wengine, kutafuta mpango wa mambo yasiyotarajiwa, au kutafuta faraja kwa ajili ya mwili wako, ili kuepuka kuchelewesha kazi Yangu, na kuzuia mustakabali wako mzuri. Badala ya kukulinda, kufanya hivyo kunaweza tu kuleta maangamizi juu yako. Je, huu hautakuwa upumbavu kwa upande wako? Kile unachokifurahia leo ndicho hasa kinachoharibu mustakabali wako, ilhali maumivu unayovumilia leo ndiyo hasa yanayokulinda. Lazima ufahamu mambo haya waziwazi, ili uepuke kuanguka katika vishawishi ambavyo utapata ugumu kujinasua kutoka kwavyo, na kuepuka kutumbukia katika ukungu mzito na kutoweza kulipata jua tena kamwe. Ukungu mzito unapoisha, utajikuta katikati ya hukumu ya siku kuu. Kufikia wakati huo, siku Yangu itakuwa imewakaribia wanadamu. Utaepukaje hukumu Yangu? Utawezaje kuvumilia joto kali la jua linalochoma? Ninapompa mwanadamu utele Wangu, yeye hauhifadhi kifuani mwake, bali anautupa kando mahali ambapo hakuna mtu atakayeutambua. Siku Yangu inapomshukia mwanadamu, hataweza tena kugundua utele Wangu, au kupata maneno machungu ya ukweli Niliyomnenea zamani. Ataomboleza na kulia, kwa sababu amepoteza mwangaza wa nuru na kuanguka gizani. Kile mnachokiona leo ni upanga mkali wa kinywa Changu tu; hamjaona fimbo mkononi Mwangu au mwali wa moto Ninaomchoma nao mwanadamu. Hiyo ndiyo maana ninyi bado ni wenye majivuno na msio na kadiri mbele Zangu, na kwa nini bado mnapigana na Mimi katika nyumba Yangu, mkipinga kwa ulimi wenu wa binadamu kile ambacho Nimenena kwa kinywa Changu. Mwanadamu haniogopi, na hadi leo anaendelea kujiweka katika uadui na Mimi, bado hahisi hofu hata kidogo. Mna ulimi na meno ya wasio haki vinywani mwenu. Maneno na matendo yenu ni kama yale ya nyoka aliyemshawishi Hawa kutenda dhambi. Mnadaiana jicho kwa jicho na jino kwa jino, na mnang'ang'ana mbele Zangu ili kujinyakulia hadhi, umaarufu, na faida, lakini hamjui kwamba Ninatazama maneno na matendo yenu kwa siri. Hata kabla hamjaingia katika mkazo wa macho Yangu, Nimechunguza kilindi cha mioyo yenu. Mwanadamu daima hutamani kuepuka mshiko wa mkono Wangu na kukwepa uchunguzi wa macho Yangu, lakini Sijawahi kuepuka maneno au matendo yake. Badala yake, kwa makusudi, Ninaruhusu maneno na matendo hayo yaingie machoni Mwangu, ili Niweze kuadibu ukosefu wa haki wa mwanadamu na kutekeleza hukumu juu ya uasi wake. Hivyo, maneno na matendo ya mwanadamu kwa siri hubaki daima mbele ya kiti Changu cha hukumu, na hukumu Yangu haijawahi kumwacha mwanadamu, kwa maana uasi wake umekithiri. Kazi Yangu ni kuchoma na kutakasa maneno na matendo yote ya mwanadamu yaliyotamkwa na kufanywa mbele ya Roho Wangu. Kwa njia hii,[a] Ninapoondoka duniani, watu bado watadumisha uaminifu wao Kwangu, na bado wataweza kuitendea kazi Yangu kama watumishi Wangu watakatifu wafanyavyo katika kunitumikia, wakiruhusu kazi Yangu duniani iendelee hadi siku itakapokamilika.

Maelezo ya Chini:

a. Nakala ya asili haina kirai “Kwa njia hii.”

Iliyotangulia: Mwokozi Amerudi Tayari Juu ya “Wingu Jeupe”

Inayofuata: Kazi katika Enzi ya Sheria

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp