Wale Wanaomtii Mungu kwa Moyo wa Kweli Hakika Watapatwa na Mungu
Kazi ya Roho Mtakatifu inabadilika siku hadi siku. Inainuka juu zaidi kwa kila hatua, ufunuo wa kesho ukiwa wa juu zaidi kuliko wa leo, ikipanda juu zaidi daima, hatua baada ya hatua. Hii ndiyo kazi ambayo kwayo Mungu humfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Ikiwa watu hawawezi kwenda sambamba na hatua, basi wanaweza kuondoshwa wakati wowote. Ikiwa hawana moyo wa utii, hawataweza kufuata hadi mwisho kabisa. Enzi iliyotangulia imepita; hii ni enzi mpya. Na katika enzi mpya, kazi mpya lazima ifanywe. Hasa katika enzi ya mwisho ambapo watu wanafanywa kuwa watimilifu, Mungu atafanya kazi mpya zaidi, kwa haraka zaidi, kwa hivyo ikiwa watu hawatii kwa makusudi, wataona ugumu kufuata hatua za Mungu. Mungu hafuati kanuni zozote, wala Hachukulii hatua yoyote ya kazi Yake kama isiyobadilika milele. Badala yake, Yeye hufanya kazi ambayo ni mpya zaidi na ya juu zaidi daima. Kwa kila hatua, kazi Yake inazidi kuwa ya vitendo zaidi na zaidi, na inazidi kulingana na mahitaji halisi ya mwanadamu. Ni kwa kupitia kazi kama hiyo tu ndiyo watu wanaweza kufikia mabadiliko ya mwisho ya tabia zao. Maarifa ya mwanadamu kuhusu maisha yanafika viwango vya juu zaidi daima, na hivyo, vivyo hivyo, kazi ya Mungu inafika viwango vya juu zaidi daima. Ni kwa njia hii tu ndiyo mwanadamu anaweza kufanywa kuwa mtimilifu na kustahili kutumiwa na Mungu. Mungu hufanya kazi kwa njia hii kwa upande mmoja ili kukabiliana na kubadilisha fikira za mwanadamu, na kwa upande mwingine kumwongoza mwanadamu kuingia katika hali ya juu zaidi na ya vitendo zaidi, katika upeo wa juu zaidi wa imani kwa Mungu, ili mwishowe, mapenzi ya Mungu yaweze kutimizwa. Wale wote wenye asili ya uasi ambao wanapinga kwa ukaidi wataondoshwa na hatua hii ya kazi ya Mungu ya haraka na yenye nguvu; ni wale tu wanaotii kwa makusudi na ambao wanajinyenyekeza kwa furaha ndio wanaoweza kusonga mbele hadi mwisho wa njia. Katika kazi ya aina hii, ninyi nyote mnapaswa kujifunza jinsi ya kutii na jinsi ya kuweka kando fikira zenu. Mnapaswa kuwa waangalifu katika kila hatua mnayochukua. Kama mtakuwa wazembe, hakika mtakuwa watu wanaochukiwa na Roho Mtakatifu, watu wanaovuruga kazi ya Mungu. Kabla ya kupitia hatua hii ya kazi, kanuni na sheria za zamani za mwanadamu zilikuwa nyingi sana kiasi kwamba alijisahau, na akawa mwenye majivuno na kujisahau. Hivi vyote ni vizuizi vinavyomzuia mwanadamu kuikubali kazi mpya ya Mungu; ni maadui wa maarifa ya mwanadamu kuhusu Mungu. Ni hatari kwa watu kutokuwa na utii mioyoni mwao wala kiu ya ukweli. Ukitii tu kazi na maneno ambayo ni rahisi, na usiweze kukubali chochote cha kina zaidi, basi wewe ni mtu anayeng'ang'ania njia za zamani na asiyeweza kwenda sambamba na kazi ya Roho Mtakatifu. Kazi inayofanywa na Mungu inatofautiana kutoka enzi hadi enzi. Ukitii vizuri kazi ya Mungu katika awamu moja, lakini katika awamu inayofuata utii wako kwa kazi Yake ni duni, au huna uwezo wa kutii, basi Mungu atakuacha. Unaenda sambamba na Mungu Anapochukua hatua hii, na lazima uendelee kwenda sambamba Anaposonga kwenye hatua inayofuata; ni hapo tu ndipo utakuwa mtu ambaye ni mtiifu kwa Roho Mtakatifu. Kwa kuwa unamwamini Mungu, lazima ubakikuwa thabiti katika utii wako. Huwezi tu kutii unapopenda na kutotii usipopenda. Utii wa aina hii haukubaliwi na Mungu. Ikiwa huwezi kwenda sambamba na ushirika Wangu wa kazi mpya, na unaendelea kushikilia misemo ya zamani, basi kunawezaje kuwa na maendeleo katika maisha yako? Kazi ya Mungu ni kukuruzuku kupitia maneno Yake. Unapotii na kukubali maneno Yake, hakika Roho Mtakatifu atafanya kazi ndani yako. Roho Mtakatifu hufanya kazi sawasawa na Ninavyonena; ukifanya kama Nilivyosema, Roho Mtakatifu atafanya kazi ndani yako mara moja. Ninatoa nuru mpya ili muitazame, Nikiwaleta katika nuru ya sasa, na wakati unatembea katika nuru hii, Roho Mtakatifu atafanya kazi ndani yako mara moja. Kuna baadhi ambao wanaweza kuwa wakaidi, wakisema, "sitatenda kile Unachosema." Katika hali hiyo, Ninakuambia kwamba sasa umefika mwisho wa njia; umekauka, na huna uzima. Hivyo, katika kupitia mabadiliko ya tabia yako, hakuna kitu ambacho ni muhimu zaidi kuliko kwenda sambamba na nuru ya sasa. Roho Mtakatifu hafanyi kazi ndani ya watu fulani wanaotumiwa na Mungu tu, bali, zaidi ya hayo, Anafanya ndani ya kanisa. Anaweza kuwa anafanya kazi ndani ya mtu yeyote. Anaweza kufanya kazi ndani yako wakati wa sasa, na utapitia kazi hii. Katika kipindi kinachofuata, Anaweza kufanya kazi ndani ya mtu mwingine, katika hali ambayo lazima ufanye haraka kufuata; kadiri unavyofuata nuru ya sasa kwa karibu zaidi, ndivyo maisha yako yanavyoweza kukua zaidi. Haijalishi mtu ni wa aina gani, Roho Mtakatifu akifanya kazi ndani yake, basi lazima ufuate. Kadiri wewe mwenyewe unavyopitia mambo, pata upitiaji halisi wa kile walichopitia, na utapokea mambo ya juu zaidi. Kupitia utendaji wa aina hii, utasonga mbele kwa haraka zaidi. Hii ndiyo njia ya ukamilifu kwa mwanadamu na njia ambayo kwayo maisha hukua. Njia ya kufanywa kuwa mtimilifu inafikiwa kupitia utii wako kwa kazi ya Roho Mtakatifu. Hujui ni kupitia mtu wa aina gani ndiyo Mungu atafanya kazi ili kukufanya uwe mtimilifu, wala ni kupitia mtu, tukio, au kitu gani ndiyo Atakuruhusu upate na kuona mambo. Ikiwa unaweza kuweka mguu kwenye njia hii sahihi, hilo linaonyesha kwamba kuna tumaini kubwa kwako kufanywa kuwa mtimilifu na Mungu. Ikiwa huwezi, hilo linaonyesha kwamba mustakabali wako ni wa giza, usio na nuru. Punde tu unapoanza safari katika njia sahihi, utapata ufunuo katika mambo yote. Haijalishi kile ambacho Roho Mtakatifu anawafunulia wengine, ikiwa unaendelea kwa msingi wa maarifa yao ili kupitia mambo wewe mwenyewe, basi itakuwa sehemu ya maisha yako, na utaweza kuwaruzuku wengine kutokana na uzoefu huu. Wale wanaowaruzuku wengine kwa kurudia maneno kama kasuku ni watu ambao hawajapata uzoefu wowote; lazima ujifunze kupata njia ya utendaji kupitia nuru na mwangaza wa wengine kabla ya kuweza kuanza kuzungumza kuhusu upitiaji na maarifa yako mwenyewe halisi. Hili litakuwa la manufaa makubwa zaidi kwa maisha yako mwenyewe. Unapaswa kupitia kwa namna hii, ukitii yote yanayotoka kwa Mungu. Unapaswa kutafuta nia za Mungu katika mambo yote na ujifunze mafunzo katika mambo yote, ili maisha yako yaweze kukua. Utendaji kama huo huleta maendeleo ya haraka zaidi.
Roho Mtakatifu hukutia nuru kwa njia ya upitiaji wako halisi, na kukufanya kuwa mtimilifu kupitia imani yako. Je, uko radhi kweli kufanywa kuwa mtimilifu? Ikiwa uko radhi kweli kufanywa kuwa mtimilifu na Mungu, basi utakuwa na ujasiri wa kuutelekeza mwili wako, utaweza kutenda maneno ya Mungu, na hutakuwa hasi au dhaifu. Utaweza kuyatii yote yatokayo kwa Mungu, na utaweza kuwasilisha matendo yako yote—yawe yalifanywa mbele ya wengine au nyuma yao—kwa Mungu. Ukitenda kama mtu mwaminifu, na utende ukweli katika mambo yote, basi utakuwa mtu anayefanywa kuwa mtimilifu. Wale watu wadanganyifu ambao hutenda kwa namna moja mbele ya wengine na kwa namna nyingine nyuma yao hawako radhi kufanywa kuwa watimilifu. Wote ni wana wa mateso ya milele na wana wa maangamizo; wao ni wa Shetani, na hawajachaguliwa na Mungu. Mungu hawachagui watu kama hao! Ikiwa matendo na tabia yako haiwezi kuwasilishwa mbele ya Mungu au kuchunguzwa na Roho wa Mungu, huu ni ushahidi kwamba wewe una tatizo. Lazima ukubali hukumu na kuadibu kwa Mungu, na uzingatie mabadiliko ya tabia yako; hapo tu ndipo utaweza kuanza kuitembea njia ya kufanywa kuwa mtimilifu. Ikiwa uko tayari kweli kufanywa kuwa mtimilifu na Mungu na kufuata mapenzi ya Mungu, basi unapaswa kuitii kazi yote ya Mungu, bila neno hata moja la malalamiko, bila kutoa hukumu za kiholela au hitimisho kuhusu kazi ya Mungu. Haya ni mahitaji ya chini kabisa ya kufanywa kuwa mtimilifu na Mungu. Hitaji la lazima kwa wale wanaotafuta kufanywa kuwa watimilifu na Mungu ni hili: Tenda kwa moyo umpendao Mungu katika mambo yote. Inamaanisha nini kutenda kwa moyo umpendao Mungu? Inamaanisha kwamba matendo yako na tabia yako yote yanaweza kuwasilishwa mbele ya Mungu. Na kwa sababu una nia sahihi, iwe matendo yako ni sahihi au si sahihi, huogopi kuyaonyesha kwa Mungu au kwa akina ndugu, na unathubutu kula kiapo mbele ya Mungu. Lazima uwasilishe kila nia, wazo, na fikira yako mbele ya Mungu ili Yeye achunguze; ukitenda na kuingia kwa njia hii, basi maendeleo katika maisha yako yatakuwa mepesi.
Kwa kuwa unamwamini Mungu, lazima uweke imani katika maneno yote ya Mungu na katika kazi Yake yote. Ambayo ni kusema, kwa kuwa unamwamini Mungu, lazima umtii. Ikiwa huwezi kufanya hili, basi hakuna tofauti iwe unaamini au la. Ikiwa umemwamini Mungu kwa miaka mingi, na bado hujawahi kumtii, na hukubali ukamilifu wa maneno Yake, na badala yake unaomba kwamba Mungu akutii na atende kulingana na fikira zako, basi wewe ni mwasi zaidi ya wote, wewe ni asiyeamini. Watu kama hao wanawezaje kutii kazi na maneno ya Mungu ambayo hayalingani na fikira za mwanadamu? Waasi zaidi ya wote ni wale ambao kwa makusudi wanakataa kukubali kushindwa na Mungu na wanampinga Mungu. Wao ni maadui wa Mungu, wapinga Kristo. Daima wanaweka mtazamo wa uhasama kuelekea kazi mpya ya Mungu; hawana kamwe mwelekeo hata mdogo kabisa wa kutii, wala hawajawahi kutii kwa furaha au kujinyenyekeza. Mbele ya wengine, wao ndio wenye kujikweza zaidi, na hawamtii mtu yeyote kamwe. Mbele ya Mungu, wanajiona kuwa bora kabisa katika kuhubiri "mahubiri," na walio stadi kabisa katika kufanya kazi kwa wengine. Kamwe hawaachilii "hazina" walizo nazo; badala yake wanazichukulia kama urithi wa familia wa kuabudiwa na kuhubiriwa kwa wengine, na wanazitumia kuwakaripia wale wajinga wanaowaabudu. Kwa kweli kuna idadi fulani ya watu kama hawa kanisani. Inaweza kusemwa kwamba wao ni "nasaba ya mashujaa wasioshindwa," kizazi baada ya kizazi wakikaa katika nyumba ya Mungu kwa muda. Wanachukulia kuhubiri "mahubiri" (mafundisho) kuwa wajibu wao wa juu kabisa. Mwaka baada ya mwaka, kizazi baada ya kizazi, wanaendelea kutekeleza kwa ukali wajibu wao "mtakatifu na usiokaidiwa". Hakuna anayethubutu kuwagusa; hakuna hata mtu mmoja anayethubutu kuwakemea waziwazi. Wanakuwa "wafalme" katika nyumba ya Mungu, wakifanya watakavyo huku wakiwadhulumu wengine kutoka enzi hadi enzi. Kundi hili la mapepo waovu linatafuta kuungana mikono ili kubomoa kazi Yangu; Ninawezaje kuruhusu ibilisi hawa wanaoishi kuwepo mbele ya macho Yangu? Hata wale ambao ni watiifu nusu tu hawawezi kuendelea hadi mwisho, sembuse madhalimu hawa wasio na utii hata kidogo mioyoni mwao! Kazi ya Mungu haipatwi kwa urahisi na mwanadamu. Hata wakitumia nguvu zote walizo nazo, watu wanaweza tu kupata sehemu yake, hatimaye kuwaruhusu wafanywe kuwa watimilifu. Vipi, basi, kuhusu watoto wa malaika mkuu, ambao wanatafuta kuharibu kazi ya Mungu? Je, si wao wana tumaini dogo hata zaidi la kupatwa na Mungu? Kusudi Langu katika kufanya kazi ya ushindi si tu kushinda kwa ajili ya ushindi pekee, bali kushinda ili kufunua haki na ukosefu wa haki, kupata ushahidi kwa ajili ya adhabu ya mwanadamu, kuhukumu uovu, na, zaidi ya hayo, kushinda kwa ajili ya kuwafanya kuwa watimilifu wale wanaotii kwa makusudi. Mwishowe, wote wataainishwa kulingana na aina zao, na mawazo na fikira za wale watakaofanywa kuwa watimilifu zitajazwa na utii. Hii ndiyo kazi ambayo hatimaye itatimizwa. Wale waliojaa matendo ya uasi, wakati huo huo, wataadhibiwa na kutupwa katika moto unaowaka, na kuwa walengwa wa laana ya milele. Wakati huo utakapofika, ile "nasaba ya mashujaa wakuu na wasioshindwa," ambayo imekuwepo katika enzi zote, itakuwa "nasaba ya waoga dhaifu na wasio na uwezo" duni kabisa na inayotengwa zaidi. Hili pekee ndilo linaweza kufunua haki yote ya Mungu, na tabia Yake ambayo haivumilii kukosewa na mwanadamu, na hili pekee ndilo linaweza kutuliza chuki iliyo moyoni Mwangu. Je, si mnakubali kwamba hili ni jambo la busara kabisa?
Sio wale wote wanaopitia kazi ya Roho Mtakatifu, wala wale walio katika mkondo huu, wanaweza kupata uzima. Uzima si mali ya umma inayoshirikiwa na watu wote, na mabadiliko katika tabia hayafikiwi kwa urahisi na wote. Utii kwa kazi ya Mungu lazima uwe na uhalisi na uishiwe kwa kudhihirishwa. Utii wa juujuu pekee hauwezi kupata kibali cha Mungu, na kutii tu vipengele vya juujuu vya neno la Mungu, bila kufuatilia mabadiliko katika tabia ya mtu, hakulingani na nia za Mungu. Utii kwa Mungu na utii kwa kazi ya Mungu vinafanana. Wale wanaomtii Mungu tu lakini hawaitii kazi Yake hawawezi kuhesabiwa kuwa watiifu, sembuse wale ambao hawatii kweli lakini ni wenye kujipendekeza kwa nje. Wale wanaomtii Mungu kweli wote wanaweza kupata faida kutokana na kazi hiyo na kufikia ufahamu wa tabia na kazi ya Mungu. Ni watu kama hao pekee ndio wanaomtii Mungu kweli. Watu kama hao wanaweza kupata maarifa mapya, na kupitia mabadiliko mapya, kupitia kazi mpya. Ni watu hawa pekee ndio wanaokubaliwa na Mungu, watu hawa pekee ndio wanaofanywa kuwa watimilifu, na ni hawa pekee ndio wale ambao tabia zao zimebadilika. Wale wanaokubaliwa na Mungu ni wale wanaomtii Mungu, na wanaotii neno na kazi Yake kwa furaha. Ni watu kama hao pekee ndio watu wenye haki, ni watu kama hao pekee ndio wanaomtaka Mungu kwa dhati, na ndio wanaomtafuta Mungu kwa dhati. Kuhusu wale wanaozungumza tu kuhusu imani yao katika Mungu kwa vinywa vyao, lakini katika kiini wanamtupia matusi, wao ni watu wanaojificha kwa vinyago, wanaobeba sumu ya nyoka; wao ndio wadanganyifu zaidi ya wote. Ipo siku, magenge haya ya wahalifu yatavuliwa barakoa zao mbovu. Je, hii siyo kazi inayofanywa leo? Watu waovu daima watakuwa waovu, na hawatawahi kuiepuka siku ya adhabu. Watu wema daima watakuwa wema, na watafunuliwa kazi ya Mungu itakapofika mwisho. Hakuna hata mmoja wa waovu atakayehesabiwa kuwa mwenye haki, wala yeyote kati ya wenye haki atakayehesabiwa kuwa mwovu. Je, Nitamwacha mtu yeyote ashtakiwe isivyo haki?
Maisha yako yanavyoendelea, lazima daima uwe na kuingia kupya na umaizi mpya, wa juu zaidi, ambao unakua wa kina zaidi katika kila hatua. Hiki ndicho ambacho kila mtu anapaswa kuingia kwacho. Ikiwa, kupitia kufanya ushirika, kusikiliza mahubiri, kusoma neno la Mungu, au kushughulikia jambo fulani, unapata ufahamu mpya na nuru mpya, huishi kamwe ndani ya kanuni za zamani na nyakati za zamani, na daima unaishi katika nuru mpya, bila kupotoka kutoka kwa neno la Mungu, hii ndiyo maana ya kuanza kuitembea njia sahihi. Kulipa gharama tu kwa kiwango fulani cha juujuu hakutatosha; siku baada ya siku, neno la Mungu linafika viwango vya juu zaidi, na mambo mapya yanaonekana kila siku, na mwanadamu, pia, lazima aingie upya kila siku. Kama Mungu anavyonena, ndivyo Anavyofanikisha yale yote ambayo Amenena, na ikiwa huwezi kwenda sambamba, basi utabaki nyuma. Lazima uende kwa kina zaidi katika maombi yako; kula na kunywa neno la Mungu hakuwezi kufanywa katika vipindi. Fanya nuru na mwangaza unaopokea uwe wa kina zaidi, na dhana na mawazo yako yote lazima yapungue taratibu. Lazima pia uimarishe uamuzi wako, na chochote unachokumbana nacho, lazima uwe na mawazo yako mwenyewe kukihusu na uwe na mitazamo yako mwenyewe. Kwa kuelewa mambo fulani ya roho, lazima upate utambuzi katika mambo ya nje na kufahamu kiini cha masuala haya. Usipojizatiti na mambo haya, utawezaje kuliongoza kanisa? Ukizungumza tu kuhusu maneno na mafundisho bila uhalisi wowote na bila njia ya utendaji, utaweza tu kusonga mbele kwa kipindi kifupi cha muda. Inaweza kukubalika kidogo unapozungumza na waumini wapya, lakini baada ya muda, wakati waumini wapya wamepata upitiaji halisi kiasi, hutaweza tena kuwaruzuku. Basi unastahilije kutumiwa na Mungu? Bila nuru mpya, huwezi kufanya kazi. Wale wasio na nuru mpya ni wale wasiojua jinsi ya kupitia, na watu kama hao hawapati kamwe maarifa mapya au uzoefu mpya. Na, katika suala la kuruzuku uzima, hawawezi kamwe kutekeleza kazi yao, wala hawawezi kustahili kutumiwa na Mungu. Mtu wa aina hii ni nyangarika, ni mtu bure tu. Kwa kweli, watu kama hao hawana uwezo kabisa wa kutekeleza shughuli yao katika kazi, wote ni nyangarika. Sio tu kwamba wanashindwa kutekeleza shughuli yao, bali kwa kweli wanaleta shida nyingi zisizo za lazima kwa kanisa. Ninawahimiza hawa "wazee waheshimiwa" wafanye hima na waondoke kanisani, ili wengine wasilazimike tena kukutazama. Watu kama hao hawana ufahamu wa kazi mpya na wamejawa na dhana. Hawatekelezi kazi yoyote ile kanisani; badala yake, wanapanda mfarakano na kueneza matamshi hasi kila mahali, na hata kufanya matendo mabaya bila kujali na kuamsha vurugu kanisani, na hivyo kuwatupa wale wasio na utambuzi katika mkanganyiko na machafuko. Ibilisi hawa walio hai, roho hawa waovu wanapaswa kuondoka kanisani haraka iwezekanavyo, isije kanisa likapata hasara kwa sababu yako. Huenda usiogope kazi ya leo, lakini, je, huogopi adhabu ya haki ya kesho? Kuna idadi kubwa ya watu kanisani ambao ni wadoezi, na idadi kubwa ya mbwa mwitu wanaotafuta kuharibu kazi ya kawaida ya Mungu. Vitu hivi vyote ni pepo waliotumwa na pepo mkuu, mbwa mwitu wakatili wanaotafuta kuwameza wanakondoo wajinga. Watu hawa waliotajwa wasipotimuliwa, watakuwa vimelea kanisani, nondo wanaoteketeza matoleo. Ipo siku inakuja ambapo funza hawa wa kudharauliwa, wajinga, waovu, na wa hali ya chini wataadhibiwa!