Masumbuko Makali ya Milele

05/11/2020

Roho zote ambazo zimepotoshwa na Shetani ziko chini ya udhibiti wa miliki ya Shetani. Ni wale tu wanaomwamini Kristo ndio waliotengwa kando, wakiokolewa kutoka katika kambi ya Shetani, na kuletwa katika ufalme wa leo. Watu hawa kamwe hawaishi chini ya ushawishi wa Shetani. Hata hivyo, asili ya mwanadamu bado imekita mizizi katika mwili wa mwanadamu. Hiyo ni kusema kwamba ijapokuwa roho zenu zimeokolewa, asili yenu bado ni ya mwonekano wake wa zamani na uwezekano kuwa mtanisaliti unabakia asilimia mia moja. Ndiyo maana kazi Yangu ni ya kudumu muda mrefu sana, kwa kuwa asili yenu ni isiyotikiswa kabisa. Sasa hivi nyote mnateseka jinsi mnavyoweza katika kutimiza wajibu wenu, lakini ukweli usiopingika ni huu: Kila mmoja wenu ana uwezo wa kunisaliti Mimi na kuirudia miliki ya Shetani, katika kambi yake, na kuyarudia maisha yenu ya zamani. Wakati huo haitawezekana kwenu kuwa hata na chembe ya utu au mwonekano wa binadamu kama mlionao sasa. Katika hali nzito, mtateketezwa, na zaidi mtalaaniwa milele, msipate mwili tena lakini muadhibiwe vikali. Hili ni tatizo lililowekwa mbele yenu(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Tatizo Zito Sana: Usaliti (2)). Nilikuwa nikifikiri kwamba nilikuwa nimemwamini Mungu kwa zaidi ya muongo mmoja, ningeweza kuacha kila kitu ili kumfuata Mungu, kuteseka kwa ajili ya wajibu wangu, na sikujikunyata licha ya ukandamizaji wa CCP, kwa hivyo nilidhani kuwa nilikuwa mwaminifu kwa Mungu na kamwe singemsaliti. Kitu ambacho sikuwahi kufikiria ni kwamba wakati ambapo ningekamatwa na kuteswa kikatili na polisi wa CCP, ningepoteza heshima yangu na kukubali kushindwa na Shetani. Asili yangu ya kumsaliti Mungu ilifunuliwa kabisa. Kufikiria kuhusu ushinde huo mbaya kunaumiza vibaya sana, na kutakuwa majuto ya maisha.

Ilikuwa mnamo mwaka wa 2008 wakati ambapo CCP ilianza raundi nyingine ya ukandamizaji mkubwa na kukamatwa kwa Wakristo katika taifa zima. Nakumbuka siku moja mnamo Agosti niliarifiwa kwamba viongozi wa kanisa na ndugu wengi katika maeneo mengi walikuwa wamekamatwa. Nilifanya hima kuwasiliana na kina ndugu fulani ili kujaribu kushughulikia athari za baadaye za mambo hayo na kuhamisha mali ya kanisa. Kupanga mambo yote ya kanisa kwa utaratibu kulichukua zaidi ya wiki mbili. Niliridhika sana wakati huo, nikifikiri kwamba, wakati ambapo CCP ilikuwa ikiwakamata watu kwa hasira, ningeweza kuikabili kwa ujasiri na kutetea kazi ya kanisa, kwamba nilikuwa mwaminifu sana kwa Mungu na nilizingatia mapenzi Yake zaidi. Niliposikia kwamba baadhi ya wale waliokamatwa walikuwa Yuda, na kumsaliti Mungu na kuwasaliti ndugu, niliwadharau sana na niliamua kimyakimya: “Siku ikiwadia ambapo mimi pia nitakamatwa, nitakufa kabla ya kuwa Yuda!” Nilidhani kwamba nilikuwa na imani kubwa sana. Ajabu ni kwamba, baada tu ya Mwaka Mpya mnano 2009, CCP ilianza operesheni nyingine ya ukamataji katika taifa zima iliyoitwa “Thunder III” ambayo ililenga Kanisa la Mungu Mwenyezi. Siku moja nilipokuwa katika mkutano na baadhi ya kina ndugu, zaidi ya maafisa 30 wa polisi waliingia kwa kishindo ghafla. Walitupeleka katika kituo cha polisi cha manispaa na kututenganisha ili watuhoji. Walidai kujua mambo mawili: Majina na anwani za viongozi na wafanyakazi wenzetu, na kiasi cha pesa ambazo kanisa lilikuwa nazo na zilikuwa zimefichwa nyumbani kwa nani. Walisema kwa tishio, “Usipozungumza, utakufa!” Wakati huo sikuogopa sana. Nilihisi kwamba nilikuwa nimeteseka kiasi cha kutosha tangu nilipokuwa mchanga, kwa hivyo hata wangenitesa, ningeweza kuvumilia. Na kwa vyovyote vile, nilifanya wajibu wangu na nilikuwa mwaminifu kwa Mungu, kwa hivyo bila shaka Angenilinda. Walipoona kwamba sikuzungumza, polisi walileta video ya uchunguzi na picha za kuingia na kutoka kwangu nyumbani kwa wenyeji wangu na wakaorodhesha mahali pote nilipokuwa miezi michache iliyopita, kisha wakaniambia nikiri. Kuona ushahidi kama huo wa kuthibitika kulinitia wasiwasi. Nilifikiri kwamba hata ningekanusha hayo, bado hawangeniamini, kwa hivyo nilimwomba Mungu na kumsihi Anizuie ili nisiwe Yuda. Walipoona kwamba bado sikuzungumza, ofisa mmoja alisema kwa hasira, “Inaonekana kwamba unatulazimisha tuwe wakali kwako!” huku akisukuma kiti cha chuma nilichokuwa nimefungiwa kwacho, na akiniacha nikilala chali. Kisha wakachukua sirinji iliyokuwa na mchanganyiko wa mafuta ya haradali na maji ya mronge na wakaanza kuingiza ndani ya pua yangu na kuyasugua kwenye macho yangu. Yalikuwa machungu sana. Nilihisi kana kwamba sikuweza kupumua. Macho yangu yalikuwa yakiuma sana kiasi kwamba sikuweza kuyafungua na tumbo langu lilikuwa likiuma. Kisha wakanivua nguo hadi kiunoni, wakaifungia mikono yangu kwenye mgongo wangu na kuivuta ghafla kwa nguvu. Walipochoka, walitumia kidawati kuitegemeza. Nilivumilia tu maumivu hayo na sikusema lolote. Walipoona mbinu yao haikufaulu, walijaribu mbinu nyingine mbaya. Walinitia pingu na kunifungia kwenye kiti cha chuma tena, wakachukua nyaya kadhaa za umeme, wakafungia mwisho mmoja kwenye vidole vyangu viwili vya gumba vya mguu huku mwisho mwingine ukiunganishwa na kirungu cha umeme, kisha wakaanza kunirashia maji baridi huku wakinishtua kwa umeme tena na tena. Mwili wangu wote ulitukutika kutokana na kutiwa umeme na nilihisi moyo wangu ukitukutika. Nilihisi kwa kweli kana kwamba nilikuwa karibu kufa. Waliendelea kuniumiza vibaya hadi saa nane usiku

Siku iliyofuata, polisi walinipeleka katika eneo la siri la mahojiano. Mara tu nilipoingia kule, niliweza kuona madoa ya damu kila mahali. Kulitisha. Nilihisi hofu sana, nikishangaa iwapo watanipiga hadi nifie humo. Wakati huo huo, afisa mmoja alivuta mikono yangu bila kusema neno, na kunifanya nikumbatie kiti cha chuma, kisha akanisukuma mimi na kile kiti sakafuni. Tayari kulikuwa na vidonda vya kina kwenye vifundo vya mikono yangu mahali nilipotiwa pingu ambavyo vilikuwa vikivuja damu na mikono yangu ilikuwa imevimba kama baluni. Niliposukumwa sakafuni nilihilisi uchungu mno, na nilichoweza tu kufanya ni kumwomba Mungu tena na tena. Baadaye polisi walisema upesi uwongo kadhaa wakilikashifu kanisa. Kusikia uwongo huu kulinichafua moyo na kunikasirisha. Walipoona kwamba bado sikuongea, mmoja wao alichukua kirungu cha umeme kwa ghadhabu na akendelea kunitia umeme kwenye mwili wangu wote, usoni, na hata kinywani mwangu. Kulikuwa na mwanga wa bluu uliowaka na sikuthubutu kuyafungua macho yangu, lakini niliweza tu kusikia mlio wa kirungu kile na kunusa harufu ya mwili wangu uliokuwa ukiungua. Kisha afisa mmoja alionekana kupata wazimu. Alichukua mfuko wa plastiki na kunivisha kichwani, huku akiuondoa wakati tu ambapo nilikaribia kukosa hewa. Mwingine alianza kuupiga teke upande wa chini wa mwili wangu wakati mwingine alichukua kirungu cha mbao cha unene wa takribani sentimita 4 na kuanza kunigonga, wakati wote wakisema kwa sauti kubwa na kwa hasira, “Tuna vifaa zaidi ya 100 vya mateso hapa ambavyo tutatumia kwako kimojakimoja. Yeyote ambaye hufia hapa hutupwa ndani ya shimo, hamna shida! Usipozungumza kabisa utafungwa kwa miaka minane hadi kumi, na hata ukipigwa hadi kulemazwa, bado utahukumiwa kifungo. Utakapotoka gerezani, maisha yako yote hayatakuwa ya maana!” Nilikuwa na wasiwasi sana niliposikia haya, nikiwaza, “Je, nikipigwa vibaya sana hadi nilemazwe nitaendeleaje na maisha? Askari walisema kwamba wamepata data yote kutoka katika kompyuta yangu, kwa hivyo nisipozungumza, watakapoenda kuwakamata watu wengine watasema kwamba niliwasaliti. Kila mtu kanisani atanichukia na sitaweza kutokea mbele za watu.” Polisi walipopumzika niliweza kuhisi kwamba uso wangu wote ulikuwa umevimba sana, macho yangu yalikuwa yamevimba karibu yafungike na sikuweza kuona chochote. Vifundo vya mikono yangu vilikuwa vikivuja damu na nilikuwa na vidonda vya kuungua mwilini kote. Niliweza kuhisi moyo wangu ukibana na nilikuwa nikijitahidi sana kupumua. Nilihisi kana kwamba nilikuwa karibu kufa. Kisha nikasikia afisa mmoja akisema kwamba mtaalamu wa kompyuta alikuwa amekuja na alikuwa amepata kila kitu kwenye kompyuta yangu. Nilijawa na woga ghafla. Niliwaza, “Basi hamna lingine. Kuna habari kuhusu viongozi na wafanyakazi wenzangu humo, pamoja na orodha ya washiriki wa kanisa na vitabu vya hesabu vya kanisa.” Nilihisi hofu kuu na sikujua nifanye nini baada ya hapo. Jioni hiyo, maafisa waliandaa kiweko chenye miguu mitatu chumbani, wakafungia mikono yangu mgongoni pangu na kunining’iniza kwenye kiweko kile cha miguu mitatu. Nilikuwa nikining’inia futi mbili kutoka ardhini na waliendelea kunibembeza mbele na nyuma. Kila walipofanya hivyo mikono yangu iliuma sana na matone makubwa ya jasho yalitiririka usoni pangu. Kisha nikafikiria yale ambayo askari huyo alikuwa amesema, kwamba kunipiga hadi nife hakutakuwa tatizo, na nitahukumiwa hata kama nitakuwa mlemavu. Nilianza kuhisi kana kwamba singeweza kuvumilia na niliwaza, “Je, itakuwa vipi nikifia hapa? Nina umri wa miaka 30 tu. Nikipigwa hadi kufa, hiyo itakuwa bure sana! Nikilemazwa na nishindwe kufanya kazi, nitawezaje kuishi? Kwa kuwa wamepata data yote kwenye kompyuta yangu, haijalishi ikiwa nitakiri au la. Nikiwaambia habari kidogo, labda hawataniua.” Lakini nikawaza baadaye, “Hapana, siwezi kufanya hivyo. Je, hiyo haitanifanya niwe Yuda?” Vita hivi vya ndani viliendelea na kuendelea. Hata ingawa nilikuwa nimemwomba Mungu na kusema kwamba ni afadhili nife kuliko kuwa Yuda, kadiri muda ulivyozidi kupita ndivyo maumivu yalivyozidi kuwa mabaya zaidi, na kufikia mnamo saa nane au saa tisa usiku huo sikuweza kabisa kuvumilia mateso hayo ya polisi tena na nilivurugikiwa kabisa. Nilikubali kuwapa habari juu ya kanisa. Halafu mwishowe wakanishusha chini. Walipofanya hivyo, nililala tu sakafuni, na nikashindwa kusonga na sikuwa na hisia mikononi mwangu. Maafisa waliniamuru nithibitishe ghorofa na nambari za nyumba za ndugu wawili wenyeji, na nikakubali. Pindi nilipowasaliti ndugu zangu, nilikuwa nimechanganyikiwa kabisa. Nilishikwa na hofu kuu, na nilihisi kwamba jambo baya lilikaribia kutokea. Nilikumbuka maneno haya ya Mungu, “Yeyote atakayeuhuzunisha moyo Wangu hatapokea huruma kutoka Kwangu mara ya pili.” Nilijua wazi kuwa nilikuwa nimemsaliti Mungu na kuikosea tabia Yake, na Yeye hangenisamehe tena. Nilihisi uchungu sana na nilijichukia kabisa. Niliwaza, “Kwa nini niliwasaliti? Laiti ningevumilia na kuteseka kwa muda zaidi, labda ningefaulu.” Nilijawa na hatia na majuto. Baada ya hapo, bila kujali polisi walichojaribu kufanya, nilikataa kusema neno lingine. Baadaye, kila nilipofikiria kumsaliti Mungu na ndugu zangu, kuwa Yuda, kufanya kitu ambacho hakiwezi kabisa kusamehewa, niliteseka sana. Nilihisi kana kwamba njia yangu ya imani ilikuwa imefika mwisho, kana kwamba nilikuwa nimehukumiwa kifo, na ningefia gerezani wakati wowote.

Kisha kitu kisichotarajiwa kilitokea. Muda mfupi baada ya saa tano asubuhi siku ya nne baada ya kukamatwa kwangu wakati ambapo maafisa waliokuwa wakinichunga walikuwa katika usingizi mzito, nilifungua kamba niliyokuwa nimefungwa nayo na kuruka nje ya dirisha kimyakimya kabisa. Baada ya matatizo mengi, nilifika nyumbani kwa ndugu mmoja na nikaandika barua bila kupoteza wakati ili kumwambia kiongozi wa kanisa kuhusu jinsi nilivyokuwa nimewasaliti ndugu wale wawili wenyeji na nikawaambia kwamba walihitaji kutahadhari mara moja. Vizuri. Baadaye kiongozi alinipangia kwamba nipewe makao mahali palipokuwa salama. Nilihisi vibaya sana nilipoona mshiriki mwingine wa kanisa akiwa tayari kujiweka hatarini ili kunipa makao. Nilikuwa nimemsaliti Mungu na kina ndugu. Nilikuwa Yuda. Sikufaa kabisa kupewa makao na mtu yeyote na sikuweza kutokea mbele ya ndugu wengine. Nilisoma maneno haya ya Mungu: “Sitawahurumia tena wale ambao hawakuwa waaminifu Kwangu kabisa wakati wa majonzi, kwa sababu huruma Yangu ina mipaka. Zaidi ya hayo, Simpendi yeyote yule ambaye amewahi kunisaliti Mimi, wala Sipendi kujihusisha na wale ambao hawawajali wenzao. Bila kujali huyo mtu ni nani, hii ndiyo tabia Yangu. Ni lazima Niwaambie hili: Yeyote atakayeuhuzunisha moyo Wangu hatapokea huruma kutoka Kwangu mara ya pili, na yeyote ambaye amekuwa mwaminifu Kwangu atadumu moyoni Mwangu milele(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Tayarisha Matendo Mema ya Kutosha kwa ajili ya Hatima Yako). Maneno haya yalinitikisa sana. Kila neno lilikuwa pigo chungu. Mimi ndimi niliyekuwa mtu huyo asiyekuwa mwaminifu kwa Mungu wakati wa dhiki. Mimi ndimi niliyekuwa mtu huyo aliyemsaliti Mungu na kusaliti masilahi ya marafiki zake. Mimi ndimi niliyekuwa mtu huyo aliyevunja moyo wa Mungu. Nilikuwa mwoga, nilikuwa nimemsaliti Mungu na kuwasaliti kina ndugu, na nilikuwa nimeikosea sana tabia ya Mungu. Singepokea tena huruma ya Mungu, bali sikuwa na budi kuadhibiwa na Mungu. Kadiri nilivyozidi kufikiria hilo ndivyo nilivyozidi kufadhaika, na sikuweza kuzia machozi yangu tena.

Siku chache baadaye, nilisikia kwamba dada mmoja mkubwa kwa umri katika mojawapo ya makao niliyokuwa nimesaliti alikamatwa na nyumba yake kupekuliwa. Alikuwa amefanya jambo la hatari kunipa makao na kunijali, lakini nilimsaliti. Nilijua vyema kabisa kuhusu jinsi CCP ilivyokuwa katili kwa Wakristo, na mimi mwenyewe nilikuwa nimepitia mateso hayo, lakini ili kuokoa maisha yangu, nilikuwa nimemkabidhi mikononi mwa pepo. Kufanya hivyo ni vibaya mno! Nilijizaba vikali sana kofi usoni mwangu mara kadhaa na nikasujudu mbele za Mungu kwa kuomba: “Ee Mungu, nimekusaliti na nimewasaliti kina ndugu. Mimi hata si binadamu, na sistahili kuishi. Napaswa kulaaniwa na kuadhibiwa. Hata kifo changu kitakuwa haki Yako.” Sikuweza kupata amani hata kidogo na niliteseka kila wakati. Niligutushwa usiku na majinamizi mara kwa mara na niliendelea kuwaza, “Niliwezaje kumsaliti Mungu na kuwa Yuda? Katika miaka yangu ya kuamini nimeacha familia na kazi yangu kwa ajili Mungu, na sijawahi kukubali kushindwa bila kujali wajibu wangu ulikuwa hatari kiasi gani. Niliwezaje kumsaliti Mungu na kuwa Yuda ghafla? Kwa nini nilifanya hivyo?” Mara tu baada ya kukamatwa nilitaka kuwa shahidi, lakini nilipoteswa kikatili na maisha yangu yakawa hatarini, nilisita kwa hofu, na niliposikia askari wakisema kwamba wangewauwa waumini wa Mwenyezi Mungu bila hofu ya kuadhibiwa, na kwamba ningehukumiwa hata kama ningekuwa mlemavu, nilionea wasiwasi jinsi ambavyo ningeishi maisha yangu kama mtu mlemavu. Nilikuwa mwenye umri wa miaka 30 tu, na ingekuwa bure sana iwapo ningeuawa! Waliposema kwamba tayari walikuwa wamepata nenosiri la kompyuta yangu na walipata habari yote ya kanisa humo, nilikufa moyo na nilihisi kwamba kukiri au kutokiri kwangu hakungebadili hali, na ningeweza kuyaokoa maisha yangu kwa kuwapa habari kidogo. Nilipoteza heshima yangu na kuwa Yuda. Niliona kuwa sababu kuu ya mimi kumsaliti Mungu ni kwamba nilitaka kujiokoa, na kwamba niliyathamini sana maisha yangu. Nilikuwa nikifikiri kwamba ningeweza kuvumilia mateso na kwamba nilikuwa mwaminifu kwa Mungu, na singemsaliti Mungu kamwe. Lakini pindi nilipokamatwa na kuteswa, nilionyesha tabia yangu halisi ilivyo. Kisha nikaona kwamba sikuwa kabisa na uhalisi wa ukweli na sikuwa na imani ya kweli katika Mungu. Nikikabiliwa na majaribio na dhiki, na maisha yangu yawe hatarini, ninaweza kumsaliti Mungu wakati wowote. Nilianza kusoma maneno ya Mungu ili kusuluhisha tatizo langu la kuogopa kifo. Nilisoma haya: “Je, nani kati ya wanadamu wote hatunzwi mbele ya macho ya Mwenyezi? Nani haishi maisha kati ya majaaliwa ya Mwenyezi? Uhai na kifo cha nani kilitokana na kuchagua kwake? Je, mwanadamu anadhibiti hatima yake? Wanadamu wengi wanalilia kifo, lakini kiko mbali nao; watu wengi wanataka kuwa watu wenye nguvu maishani na wanahofia kifo, lakini bila kujua kwao, siku ya kufa kwao inasongea karibu, ikiwatumbukiza ndani ya dimbwi la kifo(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Maneno ya Mungu kwa Ulimwengu Mzima, Sura ya 11). “Watu wanapokuwa tayari kuyatoa maisha yao, kila kitu huwa hafifu, na hakuna anayeweza kuwashinda. Ni nini kingekuwa muhimu zaidi kuliko uzima? Hivyo, Shetani anakuwa hawezi kufanya chochote zaidi ndani ya watu, hakuna anachoweza kufanya na mwanadamu. Ingawa, katika ufafanuzi wa ‘mwili’ inasemekana kwamba mwili hupotoshwa na Shetani, kama watu watajitoa kweli, na wasiendeshwe na Shetani, basi hakuna anayeweza kuwashinda….(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Ufafanuzi wa Mafumbo ya “Maneno ya Mungu kwa Ulimwengu Mzima”, Sura ya 36). Maneno ya Mungu yalinifanya nitambue kwamba vitu vyote viko mikononi Mwake, pamoja na maisha na kifo chetu. Nitakapokufa, ikiwa nitapigwa na kulemazwa, bila kujali maisha yangu yatakuwa vipi, yote yaliamuliwa na Mungu kabla. Kila kitu hutoka kwa Mungu, na ikiwa nitaishi au kufa, napaswa kutii mipango ya Mungu. Hata nikiteswa na Shetani hadi kufa, ikiwa nitaweza kumshuhudia Mungu, kitakuwa kifo cha thamani na cha maana. Nilikumbuka kwamba Bwana Yesu alisema, “Kwa maana atakayeyaokoa maisha yake atayapoteza: lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa sababu Yangu, yeye atayaokoa(Luka 9:24). Nilifikiri juu ya mitume na wanafunzi wa Bwana Yesu, na kwamba wengi wao waliuawa ili kueneza injili ya Mungu na kufanya mapenzi Yake. Vifo vyao vilikumbukwa na Mungu. Ingawa walikufa kimwili, roho zao hazikufa. Lakini mimi kumsaliti Mungu, kuwasaliti wengine, na kuwa Yuda ni aibu ya milele. Nilikuwa kama mfu aliye hai na maiti anayetembea bila roho. Nilijutia usaliti wangu na nilichukia upumbavu wangu. Nilifikiria jinsi ambavyo, nilipoamini kwamba polisi tayari walikuwa na habari ya kanisa, nilidhani kukiri kwangu hakungebadili hali ya mambo. Lakini nilikosea kabisa. Nilipokuwa nikiteswa na joka kubwa jekundu, kile ambacho Mungu aliangalia ni mtazamo wangu na iwapo nilishuhudia mbele za Shetani. Ikiwa kwa kweli walikuwa na habari au la, bado sikupaswa kunena. Kuzungumza kwangu na polisi kulikuwa kumwinania Shetani, na kulikuwa ishara ya aibu. Nilichukia kwamba sikufuatilia ukweli na sikuwa na imani ya kweli katika Mungu. Nilichukia tamaa yangu ya maisha, ukosefu wa heshima, na ukosefu wa uaminifu. Hata zaidi, nilichukia huyo pepo, joka kubwa jekundu. Linamchukia Mungu na ukweli kupita kiasi, na huwakamata na kuwatesa wateule Wake kwa hasira. Huwalazimisha watu wamkane na kumsaliti Mungu, na huharibu nafasi zao za kuokolewa. Niliamua kuvunja uhusiano wangu na joka kubwa jekundu na kuahidi maisha yangu kumfuata Mungu.

Wakati mmoja, nilisoma makala za ushuhuda juu ya uzoefu wa washindi na nikaona kwamba walipokuwa wakiteswa na joka kubwa jekundu, wote walitegemea maneno ya Mungu kumshinda Shetani na kuwa mashahidi. Niliaibika hata zaidi. Walikuwa waumini walioteswa kama mimi, kwa hivyo waliwezaje kuvumilia uchungu na kuwa mashahidi? Kwa nini nilikuwa mbinafsi sana, mwenye kustahili dharau, na mwenye tamaa ya maisha kiasi kwamba nikawa Yuda msaliti? Kufikiria jinsi usaliti wangu ulivyokuwa kitu cha kuchekwa na Shetani kulikuwa kama kisu kilichonichoma moyoni. Kuliumiza sana, na sikuweza kujisamehe. Nilikuwa hasi sana. Ni wakati huo tu ndipo nilisoma maneno haya kutoka kwa Mungu: “Watu wengi wametenda makosa, kwa mfano, wengine waliwahi kumpinga Mungu, wengine walimwasi Mungu, wengine walilalamika dhidi ya Mungu, au wengine walifanya vitendo dhidi ya kanisa au walifanya vitu ambavyo viliiletea nyumba ya Mungu hasara. Je, watu hawa wanapaswa kutendewa vipi? Matokeo yao yataamuliwa kulingana na asili yao na tabia yao isiyokoma. … Mungu humshughulikia kila mtu kulingana na mazingira na muktadha wa wakati huo, hali halisi, matendo ya watu, na tabia na maneno yao. Mungu hatawahi kumkosea mtu yeyote. Hii ni haki ya Mungu(“Msingi wa Jinsi Mungu Anavyomtendea Mwanadamu” katika Kumbukumbu za Hotuba za Kristo). Baada ya hapo nilisoma haya kutoka katika mahubiri fulani: “Kuna watu wengine ambao, kwa sababu ya udhaifu, husaliti kidogo baada ya kukamatwa. Hata hivyo, hawamhudumii Shetani na mioyoni mwao, bado wanamwamini Mungu na bado wanamwomba Mungu. Sababu ya kusaliti kidogo ni kwamba wana kimo kichanga na mwili wao ni dhaifu sana. Hata hivyo, hawasaliti kabisa, wala hawamhudumii Shetani; hii ni sawa na wao kuwa mashahidi. Wale ambao husaliti kanisa na ndugu zao kabisa wanapokamatwa, na wanaoshirikiana na joka kubwa jekundu kufuatilia na kuwakamata ndugu zao, na ambao hata hutia saini taarifa ambamo wameahidi kwamba hawatamwamini tena Mungu— watu hawa wataondolewa kabisa na hawana budi kulaaniwa na Mungu. … Hapo zamani kumekuwa na ndugu wengine ambao walisaliti kidogo, kwa sababu ya udhaifu, walipokuwa wamefungwa gerezani. Baadaye, walijuta baada ya mchomo wa dhamira, na wakatumbukia katika kilio na kujichukia. Walifanya nadhiri mbele za Mungu ya kumfanya Awaadhibu, na wakamsihi Awaruhusu wakabiliane na hali mbaya kwa mara nyingine ili wapate nafasi ya kutoa ushuhuda mzuri wa kumridhisha Mungu. Kwa njia hiyo walimwomba Mungu mara kwa mara, hadi mwishowe, wakapata uwezo wa kufuatilia ukweli na kutekeleza wajibu wao kama kawaida, na hata walikuja kumiliki kazi ya Roho Mtakatifu. Watu kama hao wametubu kwa kweli, na ni waaminifu. Mungu atawarehemu.” Maneno haya yalinigusa sana na sikuweza kuacha kulia. Uamuzi wa Mungu juu ya mtu hutegemea asili na kiwango cha dhambi zake, na ikiwa atatubu kwa kweli. Yeye haamui matokeo yao kwa kutegemea kosa moja tu. Niliona jinsi tabia ya Mungu ilivyo ya haki, na kwamba haki Yake ina hukumu na huruma kwa watu. Nilikuwa nimetenda dhambi kubwa sana ya kumsaliti Mungu na kuwasaliti ndugu, lakini Mungu hakuniondoa. Alinipa nafasi ya kutubu. Alinipa nuru na kunielekeza na Akaniwezesha nielewe mapenzi Yake. Nilishukuru sana kwamba Mungu huleta wokovu mkubwa zaidi kwa kila mmoja wetu, na jinsi Mungu alivyo mkarimu sana. Majuto na hatia yangu vilizidi na nilihisi kwamba nilikuwa na deni kubwa kwa Mungu. Niliamua ndani ya moyo wangu: “Nikikamatwa tena na CCP, niko tayari kutoa maisha yangu. Hata polisi wakinitesa hadi nife, nitakuwa shahidi na kumwaibisha Shetani!”

Miezi michache baadaye kanisa lilinipangia nichukue wajibu mwingine. Niliguswa sana. Mungu alihuzunishwa sana na usaliti wangu Kwake, lakini kwa uvumilivu na rehema Yake kuu, Alinipa nafasi ya kutubu. Nilijua kwamba nilipaswa kuthamini nafasi hiyo na kutia bidii katika wajibu wangu ili kulipa upendo Wake.

Desemba ya 2012 iliwadia kufumba na kufumbua, na CCP ikaanza operesheni nyingine kubwa ya kukamata na kulikandamiza Kanisa la Mwenyezi Mungu. Walikuwa wakitumia ufuatiliaji wa simu na kuwafuata watu ili kuwakamata ndugu wengi. Mnamo Desemba 18, dada wawili ambao walifanya wajibu wao nami walikamatwa baada ya simu zao kufuatiwa, na kisha viongozi wawili wakakamatwa baadaye kidogo. Niliposikia habari hiyo nilianza kuhisi wasiwasi sana. Nilijua kulikuwa na uwezekano mkubwa kwamba nilikuwa tayari nikichunguzwa na CCP na ningekamatwa wakati wowote. Sikujua iwapo ningeendelea kuishi kama ningekamatwa tena. Wazo hilo liliniacha na woga sana, lakini pia nilijua kuwa kila kitu hufanyika kwa idhini ya Mungu. Nilimwomba Mungu, nikisema kwamba sikutaka kufikiria hatari yangu ya binafsi tena, lakini kwamba nilitaka tu kushughulika halio hiyo ya hatari na kutekeleza wajibu wangu vizuri kadiri nilivyoweza. Hata kama ningekamatwa, ningekuwa shahidi ili kumwaibisha Shetani, hata kwa gharama ya maisha yangu. Nilihisi utulivu na raha zaidi baada ya maombi hayo, na kisha nilianza kupanga kazi ya kanisa. Kwa msaada wa Mungu, zaidi ya mwezi mmoja baadaye, kazi ya kanisa ilirejelea hali ya kawaida. Kupitia tukio hili niliona kwamba wakati ambapo watu hawaishi kwa ajili ya maslahi yao, na wanaweza kufanya wajibu wao, wanahisi amani na utulivu ndani yao kwa kweli, na dhamiri zao zinaweza kuwa na amani.

Kila ninapofikiria kuwa Yuda wa aibu, na kumsaliti Mungu, nahisi vibaya kabisa. Hata hivyo, ni kushindwa na kufunuliwa kwa njia hiyo kulikonipa ufahamu kiasi tu juu ya tabia ya Mungu ya haki na kumcha Mungu kidogo. Niliona jinsi Mungu alivyo na busara. Niliona kwamba Mungu alitumia ukamataji na mateso ya joka kubwa jekundu kuyafunua makosa yangu, na wakati huo tu ndipo nilijijua na kujichukia, na kuanza kufuatilia ukweli. Niliona pia jinsi kazi ya Mungu ya kuwakoa wanadamu ilivyo ya vitendo kwa kweli!

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Maudhui Yanayohusiana

Ukombozi wa Moyo

Na Zheng Xin, Marekani Mnamo Oktoba ya 2016, mimi na mume wangu tulikubali kazi ya Mungu katika siku za mwisho wakati tulikuwa ughaibuni....

Pingu za Umaarufu na Faida

Na Jieli, Uhispania Mwenyezi Mungu anasema, “Kwa hivyo Shetani hutumia umaarufu na faida kudhibiti fikira za mwanadamu hadi anachofikiria...

Leave a Reply

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp