Mafanikio au Kushindwa Kunategemea Njia Ambayo Mwanadamu Hutembea
Watu wengi wanamwamini Mungu kwa ajili ya hatima yao ya baadaye au kwa ajili ya starehe ya muda mfupi. Kwa wale ambao hawajapitia ushughulikiaji wowote, imani kwa Mungu ni kwa ajili ya kuingia mbinguni, ili kupata tuzo. Si ili kufanywa mkamilifu, au kutekeleza wajibu wa kiumbe wa Mungu. Ambayo ni kusema kwamba watu wengi hawamwamini Mungu ili watimize majukumu yao, au kukamilisha wajibu wao. Ni mara chache sana watu humwamini Mungu ili kuishi maisha yenye maana, wala hakuna wale wanaoamini kwamba kwa kuwa mwanadamu yu hai, anapaswa kumpenda Mungu kwa sababu ni sheria ya Mbinguni na kanuni ya dunia kufanya hivyo, na ni wito wa asili wa mwanadamu. Kwa njia hii, ingawa watu tofauti kila mmoja hufuatilia malengo yao binafsi, lengo la harakati zao na motisha yao yote ni sawa, na, zaidi ya hayo, kwa wengi wao, malengo yao ya ibada kwa kiasi kikubwa ni sawa. Zaidi ya miaka elfu kadhaa iliyopita, waumini wengi wamekufa, na wengi wamekufa na kuzaliwa tena. Sio tu mtu mmoja au wawili wanaomtafuta Mungu, wala hata elfu moja au mbili, lakini ufuatiliaji wa wengi wa watu hawa ni kwa ajili ya matazamio yao wenyewe au matumaini yao matukufu ya siku zijazo. Wale ambao ni waaminifu kwa Kristo ni wachache na nadra. Waumini wengi wacha Mungu bado wamekufa wakiwa wamenaswa katika nyavu zao wenyewe, na idadi ya watu ambao wamekuwa washindi, zaidi ya hayo, ni ndogo sana. Hadi siku ya leo, sababu za watu kushindwa, au siri ya ushindi wao, bado hazijulikani kwao. Wale ambao wamejawa na hamu ya kumtafuta Kristo bado hawajapata wakati wao wa ufahamu wa ghafla, hawajafikia kina cha mafumbo haya, kwa sababu hawajui. Ingawa wanafanya juhudi kubwa katika harakati zao, njia wanayoifuata ni njia ya kushindwa iliyowahi kupitiwa na watangulizi wao, na sio ile ya mafanikio. Kwa njia hii, bila kujali jinsi wanavyotafuta, je, si wao wanatembea katika njia ambayo inaelekea gizani? Je, si wanachopata ni matunda machungu? Ni vigumu vya kutosha kutabiri ikiwa watu wanaoiga wale waliofaulu zamani hatimaye watapata bahati au balaa. Uwezekano ni mbaya kiasi gani, basi, kwa watu ambao hutafuta kwa kufuata nyayo za wale ambao hawakufaulu? Je, si wao wana uwezekano mkubwa zaidi wa kutofaulu? Ni thamani gani iliyoko katika njia wanayoipitia? Je, wao si wanapoteza wakati wao? Bila kujali iwapo mtu hufaulu ama hufeli katika harakati yake, kuna, kwa kifupi, sababu kwa nini wao wanafanya hivyo, na si kweli kuwa kufaulu kwao ama kushindwa kwao kunaamuliwa na kutafuta vyovyote watakavyo.
Mahitaji ya msingi ya imani ya mtu kwa Mungu ni kuwa ni sharti awe na moyo mwaminifu, na kwamba ajitolee mwenyewe, na kutii kwa kweli. Kile kigumu sana kwa mwanadamu ni kutoa mwili wake ili abadilishe na imani ya kweli, ambapo kupitia hii anaweza kupata ukweli wote, na kutimiza wajibu wake kama kiumbe wa Mungu. Hili haliwezi kufikiwa na wale ambao wanafeli, na hata zaidi haliwezi kufikiwa na wale ambao hawawezi kumpata Kristo. Kwa sababu mwanadamu si hodari kwa kujitolea mwenyewe kwa Mungu kabisa, kwa sababu mwanadamu hayuko tayari kutekeleza wajibu wake kwa Muumba, kwa sababu mwanadamu ameona ukweli lakini anauepuka na kutembea katika njia yake mwenyewe, kwa sababu mwanadamu daima anatafuta kwa kufuata njia ya wale walioshindwa, kwa sababu mwanadamu daima anaasi Mbingu, hivyo, mwanadamu daima hushindwa, daima hunaswa na hila ya Shetani, na kunaswa katika mtego wake mwenyewe. Kwa sababu mwanadamu hamjui Kristo, kwa sababu mwanadamu hana ustadi wa kuelewa na kuupitia ukweli, kwa sababu mwanadamu anamwabudu Paulo kupita kiasi na ana tamaa ya mbinguni, kwa sababu mwanadamu daima anadai kwamba Kristo amtii na kuamuru kuhusu Mungu, kwa hivyo wale watu wakuu na wale ambao wamepitia mabadiliko ya ulimwengu bado ni watu wa kufa, na bado wanakufa kati ya kuadibu kwa Mungu. Ninachoweza kusema tu kuhusu watu kama hao ni kwamba wanakufa kifo cha kusikitisha, na kwamba matokeo yao—kifo chao—si hakina haki. Je, si kushindwa kwao hakuvumiliki hata zaidi kwa sheria ya Mbinguni? Ukweli unatoka katika ulimwengu wa mwanadamu, lakini ukweli kati ya wanadamu hupitishwa na Kristo. Unaanzia kwa Kristo, yaani, kutoka kwa Mungu mwenyewe, na hiki si kitu ambacho mwanadamu anaweza kufanya. Ilhali Kristo hutoa ukweli tu; Yeye haji kuamua ikiwa mwanadamu atafanikiwa katika harakati yake ya kufuata ukweli. Hivyo, kinachofuata ni kuwa mafanikio au kushindwa kwa kweli yote yanategemea harakati ya mwanadamu. Mafanikio au kushindwa kwa mwanadamu katika ukweli hakujawahi kuwa na uhusiano wowote na Kristo, lakini badala yake kunaamuliwa na ufuatiliaji wake. Hatima ya mwanadamu na mafanikio yake ama kushindwa hakuwezi kurundikwa kichwani pa Mungu, ili Mungu mwenyewe afanywe wa kuibeba, kwa sababu sio jambo la Mungu mwenyewe, lakini linahusiana moja kwa moja na wajibu ambao viumbe wa Mungu wanapaswa kutekeleza. Watu wengi wana ufahamu mdogo wa ufuatiliaji na hatima ya Paulo na Petro, ilhali watu hawajui chochote zaidi ya matokeo ya Petro na Paulo, na hawajui siri ya mafanikio ya Petro, au mapungufu ambayo yalisababisha kushindwa kwa Paulo. Na kwa hivyo, kama ninyi hamwezi kabisa kuelewa kiini cha harakati zao basi harakati ya wengi wenu bila shaka haitafaulu, na hata kama wachache wenu watafaulu, bado hawatakuwa sawa na Petro. Ikiwa njia ya ufuatiliaji wako ndiyo sahihi, basi una matumaini ya mafanikio. Ikiwa njia unayotembea katika kufuatilia ukweli ni ile mbaya, basi hutakuwa na uwezo wa kufaulu milele, na utakuwa na hatima sawa na Paulo.
Petro alikuwa mtu aliyefanywa mkamilifu. Ni baada tu ya kupitia kuadibu na hukumu, na hivyo kupata upendo safi kwa Mungu, ndipo alifanywa mkamilifu kabisa; njia ambayo alipitia ilikuwa ni njia ya kukamilishwa. Ambayo ni kusema kuwa, tangu hapo mwanzo kabisa, njia ambayo Petro alipitia ilikuwa ya haki, na motisha yake ya kumwamini Mungu ilikuwa sahihi, na kwa hivyo akawa mtu aliyekuwa amefanywa mkamilifu na alifuata njia mpya ambayo mwanadamu hajawahi kupitia hapo awali. Hata hivyo, njia ambayo Paulo alitembea tangu mwanzo ilikuwa njia ya upinzani kwa Kristo, na ni kwa sababu tu Roho Mtakatifu alitaka kumtumia, na kufaidika na vipaji vyake na ustahili wake wote kwa kazi yake, kwamba alifanya kazi kwa ajili ya Kristo kwa miongo mingi. Alikuwa mtu tu ambaye alitumiwa na Roho Mtakatifu, na hakutumika kwa sababu Yesu alitazama ubinadamu wake kwa mapendeleo, lakini ni kwa sababu ya vipaji vyake. Aliweza kufanya kazi ya Yesu kwa sababu alipigwa, na sio kwa sababu alifurahia kufanya hivyo. Aliweza kufanya kazi kama hiyo kwa sababu ya kupata nuru na uongozi wa Roho Mtakatifu, na kazi aliyoifanya haikuwakilisha ufuatiliaji wake kwa njia yeyote, au ubinadamu wake. Kazi ya Paulo iliwakilisha kazi ya mtumishi, ambayo ni kusema kuwa yeye alifanya kazi ya mtume. Petro, hata hivyo, alikuwa tofauti: Yeye pia alifanya baadhi ya kazi; haikuwa kuu kama kazi ya Paulo, lakini alifanya kazi huku akiwa na harakati ya kuingia kwake mwenyewe, na kazi yake ilikuwa tofauti na kazi ya Paulo. Kazi ya Petro ilikuwa utekelezaji wa wajibu wa kiumbe wa Mungu. Yeye hakufanya kazi katika nafasi ya mtume, lakini alifanya kazi huku akifuatilia upendo kwa Mungu. Mwenendo wa kazi ya Paulo pia ulikuwa na ufuatiliaji wake wa kibinafsi: Ufuatiliaji wake haukuwa kwa ajili ya chochote zaidi ya matumaini yake ya siku zijazo, na hamu yake ya hatima njema. Yeye hakukubali usafishaji wakati wa kazi yake, wala hakukubali upogoaji na ushughulikaji. Yeye aliamini kuwa alimradi kazi aliyoifanya iliridhisha mapenzi ya Mungu, na yote aliyofanya yalimpendeza Mungu, basi tuzo hatimaye ilikuwa inamsubiri. Hakukuwa na uzoefu wa kibinafsi katika kazi yake—yote yalikuwa kwa ajili yake, na hayakutekelezwa katikati ya harakati za mabadiliko. Kila kitu katika kazi yake kilikuwa ni shughuli, hakikuwa na wajibu wowote au kujisalimisha kwa kiumbe cha Mungu. Wakati wa safari ya kazi yake, hakukuwa na mabadiliko yaliyotokea katika tabia ya zamani ya Paulo. Kazi yake ilikuwa tu ya kufanya huduma kwa ajili ya wengine, na haikuwa na uwezo wa kuleta mabadiliko katika tabia yake. Paulo alifanya kazi yake moja kwa moja, bila ya kufanywa mkamilifu ama kushughulikiwa, na alivutiwa na thawabu. Petro alikuwa tofauti: alikuwa mtu ambaye alikuwa amepitia upogoaji na ushughulikiaji na alikuwa amepitia usafishaji. Lengo na motisha za kazi ya Petro zilikuwa tofauti kimsingi na zile za Paulo. Ingawa Petro hakufanya sehemu kubwa ya kazi, tabia yake ilipitia mabadiliko mengi, na alichotafuta ni ukweli, na mabadiliko ya kweli. Kazi yake haikufanyika tu kwa ajili ya kazi yenyewe. Ingawa Paulo alifanya kazi nyingi, yote ilikuwa kazi ya Roho Mtakatifu, na ingawa Paulo alishirikiana katika kazi hii, yeye, hakuipitia. Kwamba Petro alifanya kazi ndogo ilikuwa tu kwa ajili Roho Mtakatifu hakufanya kazi kubwa kupitia yeye. Wingi wa kazi zao haukuamua kama walifanywa wakamilifu; harakati ya mmoja ilikuwa ili kupokea tuzo, na ile ya mwingine ilikuwa ili kufikia upendo wa mwisho kwa Mungu na kutimiza wajibu wake kama kiumbe cha Mungu, kwa kiasi kwamba angeweza kuishi kwa kudhihirisha picha inayopendeza ili kukidhi mapenzi ya Mungu. Kwa nje walikuwa tofauti, na pia vile vile viini vyao vilikuwa tofauti. Huwezi kuamua ni nani kati yao alifanywa mkamilifu kwa msingi wa kazi waliyofanya. Petro alitafuta kuishi kwa kudhihirisha picha ya mtu anayempenda Mungu, kuwa mtu anayemtii Mungu, kuwa mtu anayekubali kushughulikiwa na kupogolewa, na kuwa mtu ambaye alitimiza wajibu wake kama kiumbe wa Mungu. Aliweza kujitolea kwa Mungu, kuweka nafsi yake kamilifu katika mikono ya Mungu, na kumtii hadi kifo. Hilo ndilo alilokuwa ameamua kufanya na, zaidi ya hayo, hilo ndilo alilotimiza. Hii ndiyo sababu ya msingi kwa nini hatimaye hatima yake ilikuwa tofauti na ile ya Paulo. Kazi ambayo Roho Mtakatifu alifanya ndani ya Petro ilikuwa kumfanya mkamilifu, na kazi ambayo Roho Mtakatifu alifanya ndani ya Paulo ilikuwa kumtumia. Hii ni kwa sababu asili zao na mitazamo yao kuhusu harakati hazikuwa sawa. Wote walikuwa na kazi ya Roho Mtakatifu. Petro alitumia kazi hii kwake mwenyewe, na pia aliitoa kwa wengine; Paulo, kwa upande mwingine, aliwapa wengine kazi nzima ya Roho Mtakatifu, na mwenyewe hakufaidika na chochote kutoka kwa kazi hiyo. Kwa njia hii, baada ya yeye kushuhudia kazi ya Roho Mtakatifu kwa miaka mingi, mabadiliko ndani ya Paulo yalikuwa karibu na kutokuwepo. Bado alibaki karibu katika hali yake ya asili, na bado alikuwa Paulo wa hapo awali. Ilikuwa tu kwamba baada ya kuvumilia ugumu wa miaka mingi ya kazi, alikuwa amejifunza jinsi ya “kufanya kazi,” na alikuwa amejifunza uvumilivu, lakini asili yake ya zamani—asili yake ya ushindani mkubwa na mamluki—bado ilibaki. Baada ya kufanya kazi kwa miaka mingi, hakufahamu asili yake potovu, wala hakuwa amejiondoa mwenyewe kutoka kwa asili yake ya zamani, na bado ilikuwa inaonekana katika kazi yake. Ndani yake kulikuwa na uzoefu zaidi wa kazi, lakini uzoefu mdogo kama huo peke yake haukuweza kumbadilisha na haungeweza kubadilisha maoni yake juu ya uwepo au umuhimu wa harakati yake. Ingawa alimfanyia Kristo kazi kwa miaka mingi, na hakumtesa tena Bwana Yesu, ndani ya Moyo wake hakukuwa na mabadiliko katika elimu kuhusu Mungu. Hii ina maana kuwa hakufanya kazi ili awe mwaminifu kwa Mungu, lakini badala yake, alilazimika kufanya kazi kwa ajili ya hatima yake ya siku zijazo. Kwa kuwa, hapo mwanzo, alimtesa Kristo, na hakumtii Kristo; kiasili yeye alikuwa mwasi ambaye alimpinga Kristo kimakusudi, na mtu ambaye hakuwa na elimu kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu. Kazi yake ilipokuwa inakaribia kukamilika, yeye bado hakujua kazi ya Roho Mtakatifu, na yeye tu alitenda kwa hiari yake mwenyewe kwa mujibu wa hulka yake mwenyewe, bila hata kidogo kutilia maanani mapenzi ya Roho Mtakatifu. Na hivyo asili yake ilikuwa katika uhasama na Kristo na haikutii ukweli. Mtu kama huyu, ambaye alikuwa ameachwa na kazi ya Roho Mtakatifu, ambaye hakujua kazi ya Roho Mtakatifu, na ambaye pia alimpinga Kristo—je, ni jinsi gani mtu kama huyu angeokolewa? Iwapo mtu ataweza kuokolewa au la haitegemei kiasi cha kazi anayoifanya, au ni kiasi gani anajitolea, lakini badala yake kunaamuliwa na iwapo anajua au hajui kazi ya Roho Mtakatifu, iwapo anaweza kuweka ukweli kwenye vitendo au la, na iwapo maoni yake kuhusu harakati yanalingana na ukweli au la.
Ingawa ufunuo wa asilia ulitokea baada ya Petro kuanza kumfuata Yesu, katika asili alikuwa, tangu mwanzo kabisa, mtu ambaye alikuwa tayari kujiwasilisha kwa Roho Mtakatifu na kumtafuta Kristo. Utiifu wake kwa Roho Mtakatifu ulikuwa safi: hakutafuta umaarufu na mali, lakini badala yake alisukumwa na utii kwa ukweli. Ingawa kuna nyakati tatu ambapo Petro alikana kumjua Kristo, na ingawa alimjaribu Bwana Yesu, udhaifu kidogo kama huu wa kibinadamu haukubeba uhusiano wa asilia yake, na haukuathiri harakati zake za mbeleni, na huwezi kuthibitisha kikamilifu ya kuwa majaribu yake yalikuwa kitendo cha mpinga Kristo. Udhaifu wa kawaida wa kibinadamu ni kitu ambacho kimo kwa watu wote duniani—je, unatarajia Petro kuwa tofauti? Je, si watu wana mtazamo fulani kuhusu Petro kwa sababu alifanya makosa mengi ya kijinga? Na je, si watu wanampenda Paulo kwa sababu ya kazi yote aliyoifanya, na nyaraka zote alizoandika? Itakuwaje mtu kuwa na uwezo wa kuona kupitia kiini cha mwanadamu? Hakika, je, wale walio na akili kweli wanaweza kuona jambo lisilo la maana kama hilo? Ingawa miaka mingi ya matukio ya uchungu ya Petro hayajanakiliwa katika Biblia, hii haithibitishi kuwa Petro hakuwa na matukio halisi, au kwamba Petro hakufanywa mkamilifu. Ni jinsi gani kazi ya Mungu inaweza kueleweka na mwanadamu? Kumbukumbu katika Biblia hazikuchaguliwa binafsi na Yesu, bali zilikusanywa na vizazi vya baadaye. Kwa njia hii, je, yote yaliyoandikwa katika Biblia hayakuchaguliwa kulingana na mawazo ya mwanadamu? Zaidi ya hayo, hatima ya Petro na Paulo hazijaelezwa kwa dhati katika nyaraka, kwa hivyo mwanadamu anawahukumu Petro na Paulo kulingana na mtazamo wake mwenyewe, na kulingana na matakwa yake mwenyewe. Na kwa sababu Paulo alifanya kazi nyingi sana, kwa sababu “michango” yake ilikuwa mikubwa sana, alipata imani ya watu wengi. Je, mwanadamu hazingatii mambo ya juu juu tu? Mwanadamu angewezaje kuwa na uwezo wa kuona hadi kiini cha mwanadamu? Bila kusahau, ikizingatiwa kwamba Paulo amekuwa kitu cha kuabudiwa kwa maelfu ya miaka, ni nani ambaye angethubutu kukana kazi yake kwa haraka? Petro alikuwa mvuvi tu, hivyo ni jinsi gani mchango wake ungekuwa mkubwa kama ule wa Paulo? Kwa msingi wa mchango, Paulo angepaswa kuzawadiwa kabla ya Petro, na inapaswa kuwa yeye ndiye angekuwa amehitimu vyema zaidi kupata kibali cha Mungu. Nani angeweza kufikiri kuwa, katika kumtendea Paulo, Mungu alimfanya tu afanye kazi kupitia vipawa vyake, ilhali Mungu alimfanya Petro kuwa mkamilifu. Si kwa vyovyote vile kwamba Bwana Yesu alikuwa amefanya mpango kwa ajili ya Petro na Paulo tangu mwanzo kabisa: Badala yake, walifanywa wakamilifu au kuwekwa kazini kulingana na tabia zao za kiasili. Na kwa hivyo, kile ambacho wanadamu huona kama michango ya nje ya mwanadamu tu, ilhali anachoona Mungu ni kiini cha mwanadamu, na vile vile njia ambayo mwanadamu hufuatilia tangu mwanzo, na motisha inayosukuma harakati ya mwanadamu. Watu hupima mwanadamu kulingana na dhana zao, na kulingana na mitazamo yao wenyewe, lakimi hatima ya mwisho ya mwanadamu haiamuliwi kulingana na mambo ya nje ya mwanadamu. Na kwa hivyo Ninasema kwamba ikiwa njia unayochukua tangu mwanzo ni njia ya mafanikio, na mtazamo wako kuelekea ufuatiliaji ni sahihi tangu mwanzo, basi wewe ni kama Petro; kama njia ambayo unatembea ni njia ya kushindwa, basi gharama yoyote ambayo unalipa, hatima yako itakuwa sawa na ile ya Paulo. Vyovyote iwavyo, hatima yako, na kama utafaulu au utafeli, vyote viwili vinaamuliwa na kama njia unayotafuta ni sahihi au la, badala ya kujitolea kwenu, au gharama unayolipa. Kiini cha Petro na kiini cha Paulo, na malengo ambayo walifuatilia, yalikuwa tofauti; mwanadamu hana uwezo wa kugundua vitu hivi, na ni Mungu pekee ndiye anayeweza kuvijua kwa ukamilifu. Kwa kuwa kitu ambacho Mungu huona ni kiini cha mwanadamu, ilhali mwanadamu hajui chochote kuhusu kiini chake mwenyewe. Mwanadamu hana uwezo wa kukitazama kiini ndani ya mwanadamu ama kimo chake halisi, na hivyo hana uwezo wa kutambua sababu za kutofaulu ama kufaulu kwa Paulo na Petro. Sababu ya wanadamu wengi kumuabudu Paulo na wala si Petro ni kuwa Paulo alitumika katika kazi ya umma, na mwanadamu anaweza kutambua kazi hii, na hivyo watu wanakiri “mafanikio” ya Paulo. Matukio ya Petro, wakati huo huo, hayaonekani kwa mwanadamu, na kile alichotafuta hakiwezi kufikiwa na mwanadamu, na hivyo mwanadamu hana hamu na Petro.
Petro alifanywa mkamilifu kwa kupitia ushughulishaji na usafishaji. Alisema, “Mimi ni lazima nikidhi mapenzi ya Mungu wakati wote. Kwa yote nifanyayo mimi natafuta tu kukidhi mapenzi ya Mungu, na kama mimi ninaadibiwa, au kuhukumiwa, bado nina furaha kufanya hivyo.” Petro alimpa Mungu kila kitu chake, na kazi yake, maneno, na maisha yote yalikuwa yote kwa ajili ya kumpenda Mungu. Alikuwa mtu aliyetafuta utakatifu, na kadiri alivyokuwa na uzoefu zaidi, ndivyo upendo wake kwa Mungu ulivyokuwa mkubwa ndani ya moyo wake. Paulo, wakati huo huo, alifanya tu kazi ya nje, na ingawa alitia bidii katika kazi yake, juhudi zake zilikuwa kwa ajili ya kufanya kazi yake vizuri na hivyo kupata tuzo. Angalijua kuwa hatapokea tuzo, yeye angalikata tamaa katika kazi yake. Kitu ambacho Petro alijali mno ni upendo wa kweli moyoni mwake, na ule ambao ulikuwa wa vitendo na ungeweza kutimizika. Yeye hakujali kuhusu iwapo angepokea tuzo, lakini kuhusu iwapo tabia yake ingebadilishwa. Paulo alijali kuhusu kufanya kazi kwa bidii hata zaidi, alijali kuhusu kazi ya nje na kujitolea, na kuhusu mafundisho ambayo watu wa kawaida hawakuwa nayo. Yeye hakujali chochote kuhusu mabadiliko ndani yake wala kwa ajili ya upendo wa kweli kwa Mungu. Uzoefu wa Petro ulikuwa kwa ajili ya kupata upendo wa kweli na maarifa ya kweli kuhusu Mungu. Uzoefu wake ulikuwa ili kupata uhusiano wa karibu na Mungu, na kwa kuishi kwa kudhihirisha kwa vitendo. Kazi ya Paulo ilifanywa kwa sababu ya kile alichoaminiwa na Yesu, na ili apate vitu ambavyo alitamani, lakini haya hayakuwa na uhusiano na maarifa yake mwenyewe na Mungu. Kazi yake ilikuwa tu kwa ajili ya kuepuka kuadibu na hukumu. Petro alichotafuta ni upendo safi, na Paulo alichotafuta ni taji ya haki. Petro alishuhudia miaka mingi ya kazi ya Roho Mtakatifu, na alikuwa na ujuzi wa vitendo wa Kristo, pamoja na ujuzi wa kina juu yake mwenyewe. Na hivyo, upendo wake kwa Mungu ulikuwa safi. Miaka mingi ya usafishaji ilikuwa imeinua ujuzi wake wa Yesu na maisha, na upendo wake ulikuwa upendo usio na masharti, ulikuwa upendo wa hiari, na hakuomba malipo yoyote, wala hakutarajia manufaa yoyote. Paulo alifanya kazi kwa miaka mingi, lakini hakuwa na ujuzi mwingi wa Kristo, na ujuzi wake mwenyewe pia ulikuwa mdogo sana. Yeye kwa kifupi hakuwa na upendo kwa Kristo, na kazi yake na njia ambayo alikimbia ilikuwa ili apate heshima na taji la mwisho. Kitu ambacho alitafuta kilikuwa ni taji zuri kabisa, wala si upendo safi. Yeye hakutafuta kikamilifu, lakini kwa kutoonyesha hisia; hakuwa anatekeleza majukumu yake, lakini alilazimika katika harakati yake baada ya kukamatwa na kazi ya Roho Mtakatifu. Kwa hivyo, harakati yake haithibitishi kuwa yeye alikuwa kiumbe wa Mungu kilichokuwa na sifa zinazostahili; ilikuwa ni Petro ambaye alikuwa kiumbe wa Mungu aliyekuwa na sifa zilizostahili na ambaye alitekeleza wajibu wake. Mwanadamu anafikiri kuwa wale wote wanaotoa mchango kwa Mungu wanapaswa kupokea tuzo, na kwamba mchango unavyokuwa mkubwa zaidi, ndivyo mwanadamu anavyosadiki zaidi kuwa atapokea fadhila za Mungu. Kiini cha mtazamo wa mwanadamu ni wa shughuli, na hatafuti kikamilifu kutekeleza wajibu wake kama kiumbe wa Mungu. Kwa Mungu, watu wanavyozidi kutafuta upendo kwa Mungu wa kweli na utii mkamilifu kwa Mungu, ambayo pia ina maana kutafuta kutekeleza wajibu wao kama viumbe wa Mungu, ndivyo zaidi wanaweza kupata kibali cha Mungu. Mtazamo wa Mungu ni kudai kwamba mwanadamu arejeshe hadhi na wajibu wake wa awali. Mwanadamu ni kiumbe wa Mungu, na kwa hivyo mwanadamu hapaswi kuvuka mpaka mwenyewe kwa kutoa madai yoyote kwa Mungu, na anapaswa asifanye lolote zaidi ya kutekeleza wajibu wake kama kiumbe wa Mungu. Hatima ya Paulo na hatima ya Petro ilipimwa kulingana na iwapo wangeweza kutekeleza wajibu wao kama viumbe wa Mungu, na wala si kulingana na ukubwa wa michango yao; hatima zao ziliamuliwa kulingana na kile ambacho walitafuta tangu mwanzo, wala si kulingana na kiasi cha kazi waliyofanya, au makadirio ya watu wengine kuwahusu. Kwa hivyo, kutafuta kutekeleza kikamilifu wajibu wa mtu kama kiumbe wa Mungu ndiyo njia ya mafanikio; kutafuta njia ya upendo wa kweli kwa Mungu ndiyo njia sahihi kabisa; kutafuta mabadiliko katika tabia ya zamani ya mtu, na kutafuta upendo safi kwa Mungu, ndiyo njia ya mafanikio. Njia kama hiyo ya mafanikio ndiyo njia ya urejesho wa jukumu la asili na vile vile mwonekano wa asili wa kiumbe wa Mungu. Hiyo ndiyo njia ya kurejeshwa, na pia ni lengo la kazi yote ya Mungu kuanzia mwanzo hadi mwisho. Kama harakati ya mwanadamu inatiwa doa na madai badhirifu ya kibinafsi na tamaa isiyo ya akili, basi athari ambayo inatimizwa haitakuwa mabadiliko katika tabia ya mwanadamu. Hii ni kinyume na kazi ya kurejeshwa. Bila shaka siyo kazi inayofanywa na Roho Mtakatifu, na hivyo hii inathibitisha kuwa harakati ya aina hii haikubaliki na Mungu. Harakati ambayo haijakubalika na Mungu ina umuhimu gani?
Kazi iliyofanywa na Paulo ilionyeshwa mbele ya mwanadamu, lakini jinsi upendo wake kwa Mungu ulivyokuwa safi, ni kiasi gani upendo wake kwa Mungu ulikuwa ndani kabisa ya moyo wake—haya hayaonekani na mwanadamu. Mwanadamu anaweza tu kutazama kazi ambayo aliifanya, ambapo mwanadamu hujua kuwa kwa hakika alitumiwa na Roho Mtakatifu, na hivyo mwanadamu hudhani kwamba Paulo alikuwa bora kuliko Petro, ya kwamba kazi yake ilikuwa kubwa zaidi, kwa kuwa alikuwa na uwezo wa kutoa kwa makanisa. Petro alitazama tu matukio yake binafsi, na akapata watu wachache wakati wa kazi yake ya mara kwa mara. Kutoka kwake kuna barua chache tu zisizojulikana, lakini ni nani ajuaye jinsi upendo wake kwa Mungu ulivyokuwa mkubwa ndani ya moyo wake? Siku zote, usiku na mchana, Paulo alimfanyia Mungu kazi: alimradi kulikuwepo na kazi ya kufanywa, yeye aliifanya. Yeye alihisi kuwa kwa njia hii angeweza kupata taji, na angemridhisha Mungu, lakini hakutafuta njia za kujibadilisha mwenyewe kupitia kazi hii. Chochote katika maisha ya Petro ambacho hakikukimu mapenzi ya Mungu kilimfanya ahisi wasiwasi. Kama hakikukidhi mapenzi ya Mungu, basi angehisi kujuta, na angetafuta njia mwafaka ambayo angejitahidi kuridhisha moyo wa Mungu. Hata katika masuala madogo kabisa maishani mwake yasiyokuwa na maana, bado alijishurutisha mwenyewe kukidhi mapenzi ya Mungu. Alikuwa makini sana ilipokuja kwa tabia yake ya asili, daima alikuwa mwenye bidii sana katika matakwa yake mwenyewe ili aendelee kwa kina zaidi katika ukweli. Paulo alitafuta sifa na hadhi ya juujuu tu. Alitafuta kujionyesha mbele ya mwanadamu, na hakutafuta kufanya maendeleo yoyote zaidi katika kuingia maishani. Alichojali ni mafundisho, sio uhalisi. Baadhi ya watu husema, “Paulo alimfanyia Mungu kazi nyingi, kwa nini yeye hakukumbukwa na Mungu? Petro alimfanyia Mungu kazi kidogo, na hakufanya mchango mkubwa katika makanisa, je, kwa nini yeye alifanywa mkamilifu?” Petro alimpenda Mungu mpaka kufikia kiwango fulani, ambacho kilitakiwa na Mungu; ni watu kama hawa pekee wana ushuhuda. Na kuhusu Paulo? Ni kiwango gani ambacho Paulo alimpenda Mungu, je, wewe wajua? Kazi ya Paulo ilikuwa kwa ajili ya nini? Na kazi ya Petro ilikuwa kwa ajili ya nini? Petro hakufanya kazi kubwa, lakini, je, wafahamu ni nini kilikuwa moyoni mwake? Kazi ya Paulo inahusiana na utoaji kwamakanisa, na msaada kwa makanisa. Kile ambacho Petro alishuhudia ni mabadiliko ya tabia ya maisha yake; alishuhudia upendo kwa Mungu. Kwa kuwa sasa unajua tofauti katika kiini cha kila mmoja wao, unaweza kuona ni nani, hatimaye, kwa kweli alimwamini Mungu, na ni nani ambaye kwa kweli hakumwamini Mungu. Mmoja wao alimpenda Mungu kweli, na mwingine hakumpenda Mungu kikweli; mmoja alipitia mabadiliko katika tabia yake, na mwingine hakupitia; mmoja alitumikia kwa unyenyekevu, na hakuonekana kwa urahisi na watu, na mwingine aliabudiwa na watu, na alikuwa wa sanamu kuu; mmoja alitafuta utakatifu, na mwingine hakufanya hivyo, na ingawa hakuwa mchafu, hakuwa na upendo safi; mmoja alikuwa na ubinadamu wa kweli, na mwingine hakuwa nao; mmoja alikuwa na hisia ya kiumbe wa Mungu, na mwingine hakuwa nayo. Hizo ndizo tofauti zilizokuwa katika kiini cha Paulo na Petro. Njia ambayo Petro alitembea ni njia ya mafanikio, ambayo pia ni njia ya kutimiza kurejesha ubinadamu wa kawaida na wajibu wa kiumbe wa Mungu. Petro anawakilisha wote hao waliofaulu. Njia aliyoipitia Paulo ndiyo njia ya kushindwa, na anawakilisha wale wote wanaonyenyekea tu na kujituma kijuujuu tu, na hawampendi Mungu kwa dhati. Paulo anawakilisha wote ambao hawana ukweli. Katika imani yake kwa Mungu, Petro alitafuta kumridhisha Mungu katika kila kitu, na alitafuta kutii yote yaliyotoka kwa Mungu. Bila malalamiko hata kidogo, aliweza kukubali kuadibu na hukumu, na vile vile usafishaji, dhiki na kuwa bila kitu maishani, yote ambayo hayangeweza kubadilisha upendo wake kwa Mungu. Je, huu haukuwa upendo mkamilifu kwa Mungu? Je, huku hakukuwa ni kutimiza wajibu wa kiumbe wa Mungu? Kuadibu, hukumu, dhiki—una uwezo wa kufikia utii hadi kifo, na hili ndilo linafaa kutimizwa na kiumbe wa Mungu, huu ni usafi wa upendo kwa Mungu. Kama mwanadamu anaweza kutimiza kiasi hiki, basi yeye ni kiumbe wa Mungu mwenye sifa inayostahili, na hakuna kitu kinachokidhi mapenzi ya Muumba bora zaidi ya hiki. Fikiria kwamba wewe unaweza kumfanyia Mungu kazi, ilhali wewe humtii Mungu, na huna uwezo wa kumpenda Mungu kwa kweli. Kwa njia hii, wewe hutakuwa tu umekosa kutimiza wajibu wa kiumbe cha Mungu, lakini pia utalaaniwa na Mungu, kwa kuwa wewe ni mtu ambaye hana ukweli, ambaye hana uwezo wa kumtii Mungu, na ambaye si mtiifu kwa Mungu. Wewe unajali tu kuhusu kumfanyia Mungu kazi, na hujali kuhusu kuweka ukweli katika vitendo, ama kujifahamu. Wewe humfahamu ama kumjua Muumba, na humtii ama kumpenda Muumba. Wewe ni mtu ambaye asilia si mtiifu kwa Mungu, na hivyo watu kama hawa hawapendwi na Muumba.
Baadhi ya watu husema, “Paulo alifanya kazi sana, na alibeba mizigo mikubwa kwa ajili ya makanisa na alitoa mchango mkubwa sana kwao. Nyaraka kumi na tatu za Paulo zilishikilia miaka 2,000 ya Enzi ya Neema, na ni za pili tu baada ya Injili Nne. Ni nani anayeweza kulinganishwa naye? Hakuna anayeweza kufafanua Ufunuo wa Yohana, ilhali nyaraka za Paulo zinatoa maisha, na kazi ambayo aliifanya ilikuwa na manufaa kwa makanisa. Ni nani mwingine ambaye angeweza kutimiza mambo kama hayo? Na ni kazi gani ambayo Petro aliifanya?” Mwanadamu anapowapima wengine, ni kwa mujibu wa michango yao. Mungu anapompima mwanadamu, ni kwa mujibu wa asili yake. Miongoni mwa wale ambao wanatafuta uzima, Paulo alikuwa mtu ambaye hakujua kiini chake mwenyewe. Hakuwa kwa njia yoyote mnyenyekevu ama mtiifu, wala hakujua kiini chake, ambacho kilikuwa kinyume na Mungu. Na hivyo, alikuwa mtu ambaye hakuwa amepitia uzoefu wa kina, na alikuwa mtu ambaye hakuweka ukweli katika vitendo. Petro alikuwa tofauti. Yeye alijua mapungufu yake, udhaifu, na tabia yake potovu kama kiumbe wa Mungu, na hivyo alikuwa na njia ya kivitendo ambayo angeweza kubadilisha tabia yake; hakuwa mmoja wa wale ambao walikuwa tu na mafundisho ya kidini lakini hawakuwa na uhalisi. Wale ambao hubadilika ni watu wapya ambao wameokolewa, ni wale ambao wana sifa za kufuatilia ukweli. Watu ambao hawabadiliki wapo miongoni mwa wale ambao kiasili hawahitajiki; ni wale ambao hawajaokolewa, yaani, ni wale ambao wamechukiwa na kukataliwa na Mungu. Hawatakumbukwa na Mungu bila kujali jinsi kazi zao zilivyo kubwa. Wakati unapolinganisha haya na kile unachofuatilia mwenyewe, kama wewe hatimaye ni mtu wa aina sawa na Petro au Paulo inapaswa kuwa wazi. Kama bado hakuna ukweli kwa yale unayotafuta, na kama hata leo bado wewe ni mwenye kiburi na jeuri kama Paulo, na bado wewe ni mwepesi wa kusema maneno matupu na mwenye kujisifu kama yeye, basi bila shaka wewe ni mtu mpotovu aliyeshindwa. Ikiwa unatafuta kwa njia sawa kama Petro, ikiwa unatafuta kufanya mazoezi na mabadiliko ya kweli, na usiwe mwenye kiburi au mkaidi, bali utafute kutekeleza majukumu yako, basi utakuwa kiumbe wa Mungu ambaye anaweza kufikia ushindi. Paulo hakujua kiini chake mwenyewe ama upotovu, vile vile hakujua kutotii kwake. Hakuwahi kutaja uasi wake wa kudharauliwa kwa Kristo, wala hakuwa na majuto kupita kiasi. Alitoa tu maelezo mafupi, na ndani ya moyo wake kabisa, hakujitiisha kwa Mungu kikamilifu. Ingawa alianguka barabarani akielekea Dameski, hakujitazama ndani yake kwa kina. Aliridhika tu kwa kuendelea kufanya kazi, na hakuzingatia kujijua mwenyewe na kubadilisha tabia yake ya zamani kuwa jambo la muhimu zaidi ya masuala yote. Yeye aliridhika tu kwa kusema ukweli, na kuwakimu wengine kama dawa ya dhamiri yake mwenyewe, na kwa kutowatesa tena wanafunzi wa Yesu ili ajifariji na kujisamehe mwenyewe kwa dhambi zake za zamani. Lengo ambalo alifuatilia halikuwa chochote zaidi ya taji la wakati ujao na kazi ya muda tu, lengo ambalo alifuatilia lilikuwa neema tele. Yeye hakutafuta ukweli wa kutosha, wala hakutafuta kuendelea kwa kina katika ukweli ambao hapo awali hakuwa ameuelewa. Na kwa hivyo kujijua kwake mwenyewe kunaweza kusemwa kuwa ni uwongo, na hakukubali kuadibu au hukumu. Kwamba aliweza kufanya kazi haina maana alikuwa na ufahamu wa asili au kiini chake; kile alichozingatia ni matendo ya nje pekee. Zaidi ya hayo, kile ambacho alijitahidi juu yake, hakikuwa mabadiliko, bali maarifa. Kazi yake kwa ujumla ilikuwa ni matokeo ya kutokewa na Yesu akiwa njiani kuelekea Dameski. Haikuwa kitu ambacho alikuwa ameamua kukifanya hapo awali, wala haikuwa kazi ambayo ilikuwa imetokea baada ya yeye kukubali upogoaji wa tabia yake ya zamani. Bila kujali jinsi ambavyo alifanya kazi, tabia yake ya zamani haikubadilika, na hivyo kazi yake haikufidia dhambi zake za zamani bali ilikuwa tu na wajibu fulani kwenye makanisa ya wakati huo. Kwa mtu kama huyu, ambaye tabia yake ya zamani haikubadilika—hivyo ni kusema, ambaye hakupata wokovu, na hata zaidi hakuwa na ukweli—hakuweza kabisa kuwa mmoja wa wale waliokubaliwa na Bwana Yesu. Hakuwa mtu ambaye alikuwa amejawa na upendo na heshima kwa Yesu Kristo, wala hakuwa mtu ambaye alikuwa na ustadi katika kutafuta ukweli, na wala hakuwa mtu ambaye alitafuta fumbo la kupata mwili. Alikuwa tu mtu ambaye alikuwa na ustadi katika kutumia maneno ya kupotosha, na ambaye hangeweza kusalimu amri kwa yeyote ambaye alikuwa mkuu kwake au aliyekuwa na ukweli. Aliwaonea kijicho watu ama ukweli ambao ulikuwa tofauti naye, ama wenye uadui naye, na kupendelea watu wenye vipawa ambao walionyesha picha nzuri na kumiliki maarifa makubwa. Hakupenda kuingiliana na watu maskini ambao walitafuta njia ya kweli na waliojali kuhusu ukweli pekee, na badala yake alijihusisha na viongozi mashuhuri kutoka mashirika ya kidini ambao walizungumza kuhusu mafundisho ya dini pekee, na walikuwa na maarifa mengi. Hakukupenda kazi mpya ya Roho Mtakatifu, na hakujali kuhusu harakati za kazi mpya ya Roho Mtakatifu. Badala yake, yeye alipendelea kanuni hizo na mafundisho ya dini ambayo yalikuwa juu kuliko ukweli wa ujumla. Katika kiini chake cha asili na yote ambayo aliyatafuta, hastahili kuitwa Mkristo ambaye alifuatilia ukweli, wala mtumishi mwaminifu katika nyumba ya Mungu, kwa kuwa unafiki wake ulikuwa mwingi sana, na uasi wake ulikuwa mkubwa sana. Ingawa anajulikana kama mtumishi wa Bwana Yesu, hakustahili kamwe kuingia kwenye lango la ufalme wa mbinguni, kwa kuwa matendo yake tangu mwanzo hadi mwisho hayawezi kuitwa yenye haki. Anaweza tu kuonekana kama mtu ambaye alikuwa mnafiki, na aliyefanya udhalimu, lakini ambaye pia alimfanyia Kristo kazi. Ingawa hawezi kuitwa mwovu, yeye anaweza ipasavyo kuitwa mtu ambaye alifanya udhalimu. Alifanya kazi nyingi, ilhali ni lazima asihukumiwe juu ya wingi wa kazi aliyofanya, lakini tu kwa ubora na kiini cha kazi hiyo. Ni kwa njia hii tu ndiyo inawezekana kufikia kwenye kiini cha suala hili. Yeye siku zote aliamini: “Mimi nina uwezo wa kufanya kazi, mimi ni bora kuliko watu wengi; mimi ni mwenye kujali kuhusu mzigo wa Bwana kuliko mtu yeyote, na hakuna anayetubu sana kama ninavyotubu, kwa kuwa nuru kuu iliniangazia, na nimeona nuru kuu, na hivyo toba yangu ni ya kina kuliko ya mwingine yeyote.” Wakati huo, hivi ndivyo alivyofikiria moyoni mwake. Mwishoni mwa kazi yake, Paulo alisema: “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki.” Mapambano yake, kazi, na mwendo wake ulikuwa kwa ajili ya taji la haki, na hakusonga mbele kwa bidii. Ingawa hakuwa mzembe katika kazi yake, inaweza kusemwa kwamba kazi yake ilifanywa kwa ajili tu ya kufidia makosa yake, na kufidia mashtaka ya dhamiri yake. Alitumaini tu kumaliza kazi yake, kumaliza mwendo wake, na kupigana vita vyake haraka iwezekanavyo, ili apate taji yake ya haki ambayo aliitamani sana mapema zaidi. Alichotamani si kukutana na Bwana Yesu pamoja na uzoefu wake na ujuzi wa kweli, bali ni kukamilisha kazi yake haraka iwezekanavyo, ili kwamba aweze kupokea tuzo ambayo kazi yake ilikuwa imemwezesha kupata wakati alipokutana na Bwana Yesu. Alitumia kazi yake kujifariji, na kufanya makubaliano kwa ajili ya mabadilishano ya taji la baadaye. Alichotafuta si ukweli au Mungu, bali ni taji tu. Je, ufuatiliaji kama huo unawezaje kufikia kiwango? Motisha yake, kazi yake, gharama aliyolipa, na juhudi zake zote—ndoto zake za ajabu zilienea kote, na alifanya kazi kabisa kulingana na mapenzi yake. Katika kazi yake yote, hakukuwa na uhiari hata kidogo katika gharama aliyolipa; alikuwa anashiriki kwenye mapatano tu. Juhudi zake hazikufanywa kwa hiari ili kutimiza wajibu wake, bali zilifanywa kwa hiari ili kufikia lengo la mapatano. Je, kuna thamani yoyote kwa jitihada kama hizo? Ni nani ambaye angeweza kupongeza jitihada zake chafu? Ni nani anayeweza kupendezwa na juhudi kama hizo? Kazi yake ilikuwa imejaa ndoto za siku za baadaye, ilijawa na mipango ya ajabu, na haikuwa na njia ya kubadilisha tabia ya mwanadamu. Ukarimu wake mwingi ulikuwa wa kinafiki; kazi yake haikutoa maisha, bali ilikuwa ni unyenyekevu bandia; ilikuwa ni kufanya makubaliano. Je, kazi kama hii inawezaje kumwongoza mwanadamu kwenye njia ya kurejesha wajibu wake wa awali?
Yote ambayo Petro alitafuta yalikuwa ni kulingana na niza za Mungu. Alitaka kutimiza mapenzi ya Mungu, na licha ya taabu na dhiki, bado yeye alikuwa tayari kutimiza mapenzi ya Mungu. Hakuna ufuatiliaji mkubwa zaidi wa muumini katika Mungu. Kile ambacho Paulo alitafuta kilitiwa doa na mwili wake, na dhana zake mwenyewe, na mipango na mipangilio yake mwenyewe. Hakuwa kwa njia yeyote kiumbe wa Mungu aliyehitimu, hakuwa mtu ambaye alitaka kutimiza mapenzi ya Mungu. Petro alitaka kujitiisha kwenye mipango ya Mungu, na ingawa kazi aliyofanya haikuwa kubwa, motisha za ufuatiliaji wake na njia aliyotembea ilikuwa ni sahihi; ingawa hakuweza kupata watu wengi, aliweza kufuata njia ya ukweli. Kwa hivyo inaweza kusemwa kwamba alikuwa kiumbe wa Mungu aliyehitimu. Leo, hata kama wewe si mfanyakazi, unapaswa kuwa na uwezo wa kutekeleza wajibu wa kiumbe wa Mungu, na kutafuta kutii mipango yote ya Mungu. Unapaswa kuwa na uwezo wa kutii chochote ambacho Mungu anasema, na upitie kila aina ya dhiki na usafishaji, na ingawa wewe ni dhaifu, moyoni mwako unapaswa bado uwe na uwezo wa kumpenda Mungu. Wale ambao huchukua jukumu kwa ajili ya maisha yao wenyewe wako tayari kutekeleza wajibu wa kiumbe wa Mungu, na mtazamo wa watu kama hawa kuhusu ufuatiliaji ni ule ulio sahihi. Hawa ndio watu ambao Mungu anawahitaji. Ikiwa ulifanya kazi nyingi, na watu wengine walipata mafundisho yako, lakini wewe mwenyewe hukubadilika, na hukuwa na ushuhuda wowote, au kuwa na uzoefu wowote wa kweli, kiasi kwamba mwisho wa maisha yako, bado hakuna hata moja kati ya yale uliyofanya yanayotoa ushuhuda, basi je, wewe ni mtu ambaye umebadilika? Je, wewe ni mtu ambaye unafuatilia ukweli? Wakati huo, Roho Mtakatifu alikutumia, lakini alipokutumia, alitumia sehemu yako ambayo ingeweza kutumika kufanya kazi, na wala hakutumia sehemu yako ambayo haingeweza kutumika kufanya kazi. Kama wewe ulitafuta kubadilika, basi ungeweza kufanywa mkamilifu hatua kwa hatua wakati wa mchakato wa kutumiwa. Hata hivyo Roho Mtakatifu hachukui jukumu la iwapo hatimaye utapatwa au la, na hii inategemea na namna ya ufuatiliaji wako. Ikiwa hakuna mabadiliko katika tabia yako binafsi, basi hiyo ni kwa sababu mtazamo wako katika kufuatilia ni mbaya. Kama hutatunukiwa tuzo, basi hilo ni tatizo lako, na kwa sababu wewe mwenyewe hujaweka ukweli katika vitendo, na huwezi kutimiza mapenzi ya Mungu. Na hivyo, hakuna kitu cha muhimu zaidi kama uzoefu wako binafsi, na hakuna chenye maana zaidi kuliko kuingia kwako binafsi. Baadhi ya watu wataishia kusema, “Nimefanya kazi nyingi kwa ajili Yako, na ingawa kunaweza kuwa hakuna mafanikio ya kufurahiwa, bado nimekuwa na bidii katika jitihada zangu. Je, Huwezi tu kuniruhusu niingie mbinguni ili nile tunda la uzima?” Ni lazima ujue aina ya watu ambao Ninataka; wale walio najisi hawaruhusiwi kuingia katika ufalme, wale walio najisi hawaruhusiwi kuchafua nchi takatifu. Ingawa unaweza kuwa umefanya kazi nyingi, na umefanya kazi kwa miaka mingi, mwishowe kama bado wewe ni mwovu kupindukia—hakuvumiliki kwa sheria ya Mbinguni kwamba wewe unataka kuingia katika ufalme Wangu! Tangu mwanzo wa dunia hadi leo, kamwe Sijawahi kutoa njia rahisi ya kuingia katika ufalme Wangu kwa wale wenye neema Yangu. Hii ni sheria ya Mbinguni, na hakuna awezaye kuivunja. Ni lazima utafute uzima. Leo, wale watakaofanywa wakamilifu ni wa aina sawa na Petro: ni wale ambao wanatafuta mabadiliko katika tabia zao wenyewe, na wako tayari kuwa na ushuhuda kwa Mungu na kutekeleza wajibu wao kama kiumbe wa Mungu. Ni watu kama hawa pekee ndio watakaofanywa wakamilifu. Kama wewe unatazamia tu tuzo, na hutafuti kubadilisha tabia ya maisha yako mwenyewe, basi juhudi zako zote zitakuwa za bure—na huu ni ukweli usiobadilika!
Kutoka kwa tofauti katika kiini cha Paulo na kiini cha Petro unapaswa kufahamu kuwa wale wote ambao hawafuati uzima wanafanya kazi ya bure! Unamwamini Mungu na unamfuata Mungu, na kwa hivyo moyoni mwako ni lazima umpende Mungu. Ni lazima uache tabia yako potovu, lazima utafute kutimiza mapenzi ya Mungu, na ni lazima utekeleze wajibu wako kama kiumbe wa Mungu. Kwa kuwa unamwamini na kumfuata Mungu, unapaswa kutoa kila kitu kwake, na hupaswi kufanya uamuzi au madai ya kibinafsi, na unapaswa kufikia kuridhisha mapenzi ya Mungu. Kwa kuwa uliumbwa, unapaswa kumtii Bwana aliyekuumba, kwa kuwa wewe huna mamlaka kiasili juu yako mwenyewe, na huna uwezo wa kudhibiti hatima yako. Kwa kuwa wewe ni mtu ambaye unamwamini Mungu, unapaswa utafute utakatifu na mabadiliko. Kwa kuwa wewe ni kiumbe wa Mungu, unapaswa kushika wajibu wako, na ushike nafasi yako, na ni lazima usivuke mpaka wa wajibu wako. Hii si kwa ajili ya kukuzuia, ama kukukandamiza kupitia mafundisho, bali ndiyo njia ambayo utaweza kutekeleza wajibu wako, na inaweza kufikiwa—na inapaswa kufikiwa—na wote wanaotenda haki. Ukilinganisha kiini cha Petro na kiini cha Paulo, basi utajua jinsi unavyopaswa kutafuta. Kati ya njia ambazo Petro na Paulo walitembea, njia moja ni ya kufanywa mkamilifu, na nyingine ni njia ya kuondolewa; Petro na Paulo wanawakilisha njia mbili tofauti. Ingawa kila mmoja wao alipokea kazi ya Roho Mtakatifu, na kila mmoja alipata nuru na mwangaza wa Roho Mtakatifu, na kila mmoja alikubali kile alichokuwa ameaminiwa na Bwana Yesu, tunda lililozaliwa katika kila mmoja wao halikuwa sawa. Mmoja kwa kweli alizaa tunda, na mwingine hukuzaa tunda. Kutokana na kiini cha kila mmoja wao, kazi waliyofanya, ile ambayo walionyesha kwa upande wa nje, na hatima yao ya mwisho, unapaswa kuelewa ni njia gani unayopaswa kuchukua, njia ambayo unapaswa kuchagua kuitembea. Walitembea njia mbili tofauti kabisa. Paulo na Petro, walikuwa ni mifano halisi ya kila njia, na kwa hivyo tangu mwanzo walionekana kuwakilisha njia hizi mbili. Je, ni mambo gani muhimu katika uzoefu wa Paulo, na ni kwa nini yeye hakufaulu? Je, ni mambo gani muhimu katika matukio ya Petro, na ni jinsi gani aliweza kupitia kufanywa mkamilifu? Ukilinganisha kile ambacho kila mmoja alikijali, basi utajua hasa ni mtu wa aina gani ambaye Mungu anamtaka, mapenzi ya Mungu ni yapi, tabia ya Mungu ni ipi, ni mtu wa aina gani ambaye hatimaye atafanywa mkamilifu, na pia ni mtu wa aina gani ambaye hawezi kufanywa mkamilifu, ni tabia gani za wale ambao watafanywa kuwa wakamilifu, na ni tabia gani za wale ambao hawatafanywa wakamilifu—masuala haya ya kiini yanaweza kuonekana katika uzoefu wa Petro na Paulo. Mungu aliumba vitu vyote, na hivyo Yeye huvifanya viumbe vyote vije chini ya utawala Wake, na kunyenyekea chini ya utawala Wake; Ataamuru vitu vyote, ili kwamba kila kitu kiwe mikononi Mwake. Vitu vyote vilivyoumbwa na Mungu, pamoja na wanyama, mimea, wanadamu, milima na mito, na maziwa—vyote ni lazima vije chini ya utawala Wake. Vitu vyote vilivyo mbinguni na ardhini lazima viwe chini ya utawala Wake. Haviwezi kuwa na uchaguzi wowote na vyote ni lazima vitii mipango Yake. Hii iliamuliwa na Mungu, na ni mamlaka ya Mungu. Mungu huamuru kila kitu, na Anaagiza na kupangilia kila kitu, ambapo kila kimoja kinapangwa kulingana na aina, na kutengewa nafasi zao zenyewe, kulingana na mapenzi ya Mungu. Bila kujali kitu ni kikubwa namna gani, hakuna kitu kinachoweza kumpita Mungu, na vitu vyote vinawatumikia wanadamu walioumbwa na Mungu, na hakuna kitu kinachothubutu kumwasi Mungu au kutoa madai yoyote kwa Mungu. Na kwa hivyo mwanadamu, kama kiumbe wa Mungu, ni lazima atekeleze wajibu wa mwanadamu. Bila kujali kama yeye ni bwana au mtunzaji wa vitu vyote, bila kujali jinsi ambavyo hadhi ya mwanadamu ni ya juu miongoni mwa vitu vyote, yeye bado ni mwanadamu mdogo chini ya utawala wa Mungu; yeye si zaidi ya mwanadamu mdogo, kiumbe wa Mungu, na kamwe hatawahi kuwa juu ya Mungu. Kama kiumbe wa Mungu, mwanadamu anapaswa kutafuta kutekeleza wajibu wa kiumbe wa Mungu, na kutafuta kumpenda Mungu bila kufanya chaguo lingine kwa kuwa Mungu anastahiki upendo wa mwanadamu. Wale ambao wanatafuta kumpenda Mungu hawapaswi kutafuta faida zozote za kibinafsi au lile ambalo wanatamani binafsi; hii ndiyo njia sahihi kabisa ya ufuatiliaji. Kama kile ambacho unatafuta ni ukweli, kile ambacho unatenda ni ukweli, na kile ambacho unafikia ni badiliko katika tabia yako, basi njia unayoitembea ni sahihi. Ikiwa kile unachotafuta ni baraka za kimwili, na kile unachoweka katika vitendo ni ukweli wa dhana zako mwenyewe, na iwapo hakuna mabadiliko katika tabia yako, na wewe si mtiifu kabisa kwa Mungu kwenye mwili, na bado unaishi kwenye mashaka, basi unachotafuta bila shaka kitakupeleka kuzimu, kwa kuwa njia unayoitembea ni njia ya kushindwa. Ikiwa utafanywa kuwa mkamilifu ama utaondolewa, inategemea na yale unayofuatilia mwenyewe, ambayo pia ni kusema kuwa kufanikiwa au kushindwa kunategemea njia ambayo mwanadamu anaitembea.