Majukumu ya Viongozi na Wafanyakazi (3)

Kipengele cha Tatu: Kushiriki kanuni za ukweli zinazopaswa kueleweka ili kutekeleza kila wajibu ipasavyo (Sehemu ya Pili)

Katika mkutano uliopita, tulifanya ushirika wa ziada kuhusu jukumu la pili la viongozi na wafanyakazi, tukizungumzia matatizo ya kuingia katika uzima yaliyopo, na kufichua matendo na udhihirisho fulani wa viongozi wa uwongo. Kisha, tulijadili mambo kadhaa kuhusu jukumu la tatu la viongozi na wafanyakazi—kushiriki kanuni za ukweli zinazopaswa kueleweka ili kutekeleza kila wajibu ipasavyo—na tukafichua na kuchanganua ni wapi "uwongo" wa viongozi wa uwongo hudhihirika kupitia mitazamo, matendo, na udhihirisho wa viongozi wa uwongo kuelekea mambo haya, kwa maneno mengine, udhihirisho wa jinsi viongozi wa uwongo wanavyoshindwa kutekeleza majukumu yao kama viongozi. Tafadhali orodhesheni mambo haya. (Jambo moja lilihusu uchapishaji wa vitabu vya maneno ya Mungu. Kiongozi huyo wa uwongo hakufanya kazi halisi, alinena tu mafundisho kwa njia tupu. Pia hakushiriki mahususi juu ya kanuni za ukweli au kufanya hata chembe ya kazi halisi.) Katika jambo hili, kiongozi huyo wa uwongo hakufanya kazi halisi, alishindwa kutimiza majukumu yake kama kiongozi na mfanyakazi, na hakuyafanyia ushirika waziwazi mahitaji ya kitaalamu, kanuni mahususi, na mambo ya kuzingatia yaliyohusika katika kazi hiyo. Alitoa kauli mbiu fulani tu kwa kupiga kelele na kusema maneno matupu, kisha akafikiri amefanya kazi nzuri. Tulijadili nini kingine? (Kulikuwa pia na tukio la kumnunulia Mungu koti la manyoya.) Tukio hili lilifichua tatizo gani kuwahusu viongozi wa uwongo? (Lilifichua kwamba viongozi wa uwongo hawafanyi kazi halisi, na kwamba wanakosa kabisa ubinadamu na busara.) Mtu fulani aliponinunulia Mimi nguo, viongozi hao walisaidia kuikagua—je, hii ni sehemu ya kazi ambayo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufanya? (La, siyo.) Walifanya kazi ambayo hawakupaswa kufanya—kuna shida gani na hili? (Hawakuwa wakishughulikia kazi yao inayofaa.) Huu ni udhihirisho mmoja wa viongozi wa uwongo. Kwanza, lilifichua kwamba viongozi wa uwongo hawashughulikii kazi yao inayofaa, na pili, lilifichua kwamba wanakosa busara na wanafanya tu mambo ya kuchukiza ambayo yanakosa busara na ubinadamu. Ninyi mnakumbuka tu mifano hiyo, lakini hamjang’amua masuala ambayo mifano hii inakusudiwa kuonyesha, au kiini cha masuala haya ambayo mifano hii inakusudiwa kuchanganua. Nilitoa mifano gani mingine kuhusu viongozi wa uwongo kutoshughulikia kazi yao inayofaa? (Kulikuwa na yule mwoka vitobosha ambaye aliendelea kumwokea Mungu vitobosha. Mungu alimwambia asifanye hivyo, lakini viongozi na wafanyakazi waliendelea kumruhusu afanye hivyo, na hata wakaonja vitobosha hivyo wao wenyewe.) Mfano huu ulifichua matatizo gani ya viongozi wa uwongo? (Kwamba hawashughulikii kazi yao inayofaa, au kufanya kazi wanayopaswa kufanya, na wanasisitiza kufanya kazi wasiyopaswa kufanya.) Kimsingi, lilifichua kwamba viongozi wa uwongo hawashughulikii kazi yao inayofaa na wanashindwa kufahamu kiini na lengo kuu la kazi yao. Zaidi ya hayo, viongozi wa uwongo wana tatizo zito. Ni lipi? (Hawayatii maneno ya Mungu au kutekeleza kazi kulingana na mahitaji ya Mungu.) Je, kuna mtu mwingine anayetaka kuongeza kitu? (Wanajifanya kuwa wa kiroho na kuonyesha kuujali mzigo wa Mungu, lakini kwa uhakika, wanafanya mambo kiholela.) Hilo ni tatizo lao lingine. Mtu mwingine yeyote? (Kabla ya kutenda, hawajaribu kuelewa mahitaji ya Mungu; badala yake, wanatumia mawazo yao wenyewe kuchukua nafasi ya mapenzi ya Mungu.) Hili linaingia katika kundi la kukosa busara. Mtu mwingine yeyote? (Jinsi viongozi wa uwongo walivyoshughulikia jambo la mtu kumnunulia Mungu nguo ilifichua ukosefu wao wa ubinadamu wa kawaida.) Wanakosa kipengele gani cha ubinadamu wa kawaida? Hawaelewi kanuni za jinsi ya kuwa na mwenendo mzuri na hawana adabu. Je, si hivyo ndivyo ilivyo? (Ndiyo.) Kwa kweli, mambo haya mliyotaja si ya msingi; suala kuu ni lipi? Pindi watu hawa wanapokuwa viongozi, wanataka kufurahia manufaa ya hadhi na makaribisho maalum, na kutamani starehe. Kwa mfano, wanataka kula vitobosha vichache, na wanapoona kwamba mtu fulani ni hodari wa kupika, wanafikiria kuonja chakula chake ili watosheleze tamaa zao. Tayari inakera kwamba hawashughulikii kazi yao inayofaa au kufanya kazi halisi, lakini juu ya hayo, wanatamani starehe na anasa za ulafi. Wanatumia kisingizio cha kuonja na kukagua kwa niaba ya Mungu ili kutosheleza tamaa zao za ulafi, wakijifurahisha kwa manufaa ya hadhi yao. Huu wote ni udhihirisho wa viongozi wa uwongo. Ingawa udhihirisho huu hauwezi kuitwa wa kikatili au mwovu unapolinganishwa na kiini cha tabia ya wapinga Kristo, ubinadamu wa viongozi wa uwongo unatosha kuwachukiza watu. Kwa upande wa sifa zao, wamepungukiwa kuwa na dhamiri na busara; ubinadamu wao ni duni na mchafu sana, na wana uadilifu wa chini. Kutokana na mifano hii, inaweza kuonekana kwamba viongozi wa uwongo hawawezi kufanya kazi halisi. Huu ni ukweli.

Viongozi wa Uwongo Hawawezi Kushiriki Kanuni za Kutenda Kazi

Leo, tutaendelea kufichua udhihirisho mbalimbali wa viongozi wa uwongo kulingana na majukumu ya viongozi na wafanyakazi. Viongozi wa uwongo kimsingi hawawezi kufanya kazi muhimu, na ya maana ya kanisa. Wao hushughulikia tu mambo rahisi, ya kawaida; kazi yao haitekelezi jukumu muhimu au la kuamua katika kazi ya kanisa kwa ujumla, na haitoi matokeo halisi. Ushirika wao kimsingi unahusu tu mada chache zisizo mpya na za kawaida kabisa, yote ni maneno na mafundisho yanayorudiwarudiwa mara nyingi na ni matupu sana, mapana, na kukosa maelezo mahususi. Ushirika wao una mambo tu ambayo watu wanaweza kuelewa kwa kusoma kitu kwa maana ya neno kwa neno. Viongozi hawa wa uwongo hawawezi kutatua matatizo halisi ambayo watu wateule wa Mungu wanayo katika kuingia kwao katika uzima hata kidogo; hasa, wana uwezo mdogo hata zaidi wa kutatua dhana, mawazo, na ufichuzi wa tabia potovu za watu. Jambo kuu ni kwamba viongozi wa uwongo hawawezi kabisa kubeba kazi muhimu iliyopangwa na nyumba ya Mungu, kama vile kazi ya injili, kazi ya utengenezaji filamu, au kazi ya maandishi. Hasa, linapokuja suala la kazi inayohusisha maarifa ya kitaalamu, ingawa viongozi wa uwongo wanaweza kujua wazi kabisa kwamba wao si wataalamu katika nyanja hizi, hawajifunzi kuzihusu, wala hawafanyi utafiti, na sembuse kuweza kuwapa wengine mwelekeo mahususi au kutatua matatizo yoyote yanayohusiana nazo. Na bado wanaendelea bila aibu kufanya mikutano, wakiongea bila kikomo kuhusu nadharia tupu, na kusema maneno na mafundisho. Viongozi wa uwongo wanajua vizuri sana kwamba hawawezi kufanya kazi ya aina hii, lakini wanajifanya kuwa wataalamu, wanatenda kwa majivuno, na daima wanatumia mafundisho makuu kuwakaripia wengine. Hawawezi kujibu maswali ya mtu yeyote, lakini wanatafuta visingizio na udhuru wa kuwakaripia wengine, wakiuliza kwa nini hawajifunzi taaluma hiyo, kwa nini hawatafuti ukweli, na kwa nini hawawezi kutatua matatizo yao wenyewe. Viongozi hawa wa uwongo, ambao si wataalamu katika nyanja hizi na hawawezi kutatua matatizo yoyote, bado wanawakaripia wengine kwa dharau. Kwa nje, wanaonekana kuwa na shughuli nyingi sana kwa watu wengine, kana kwamba wanaweza kufanya kazi nyingi na wana uwezo sana, lakini kwa kweli, wao si kitu. Ni wazi kuwa viongozi wa uwongo hawawezi kufanya kazi halisi, lakini wanajishughulisha kwa shauku, na kila mara wanasema maneno yale yale yaliyochakaa katika mikutano, wakijirudiarudia tena na tena, bila kuweza kutatua tatizo halisi hata moja. Watu wanachoshwa sana na hili, na hawawezi kuadilishwa hata kidogo kutokana na hilo. Kazi ya aina hii ya kazi haina ufanisi hata kidogo, na haitoi matokeo yoyote. Hivi ndivyo viongozi wa uwongo wanavyofanya kazi, na kazi ya kanisa inacheleweshwa kwa sababu hiyo. Lakini bado viongozi wa uwongo wanahisi wanafanya kazi kubwa na kwamba wana uwezo sana, ilhali ukweli ni kwamba hawajafanya kipengele hata kimoja cha kazi ya kanisa vizuri. Hawajui kama viongozi na wafanyakazi walio chini ya upeo wa wajibu wao wanafikia kiwango kinachostahili, wala hawajui kama viongozi na wasimamizi wa timu mbalimbali wanaweza kubeba kazi yao, na hawajali wala kuuliza kama matatizo yametokea katika utekelezaji wa wajibu wa akina ndugu. Kwa ufupi, viongozi wa uwongo hawawezi kutatua matatizo yoyote katika kazi yao, lakini wanaendelea kujishughulisha kwa bidii. Kutoka katika mtazamo wa watu wengine, viongozi wa uwongo wanaweza kuvumilia taabu, wako tayari kulipa gharama, na wanashinda kila siku wakihangaika. Unapofika wakati wa kula, wanahitaji kuitwa mezani, na wanachelewa sana kulala. Lakini matokeo ya kazi yao si mazuri. Kwa juu juu, usipoangalia kwa makini, itaonekana kwamba kila kipengele cha kazi kinafanywa, na kwamba kila mtu ana shughuli nyingi akitekeleza wajibu wake, lakini ukichunguza kwa karibu na uwe makini, na ukague kazi kwa dhati, hali halisi itafichuka. Kila kipengele cha kazi kilicho ndani ya upeo wa wajibu wao ni shaghalabaghala, hakina muundo au utaratibu hata kidogo. Kuna matatizo—au hata mapengo—katika kila kipengele cha kazi. Kutokea kwa matatizo haya kunahusiana na viongozi wa uwongo kutoelewa kanuni za ukweli, na kutenda kulingana na dhana, mawazo, na shauku yao. Viongozi wa uwongo hawashiriki kamwe kuhusu kanuni za ukweli, wala hawatafuti kamwe ukweli ili kutatua matatizo. Ni wazi kwamba wanakosa ufahamu wa kiroho na hawawezi kufanya kazi ya uongozi, na wanaweza tu kufoka maneno na mafundisho na hawaelewi ukweli hata kidogo, lakini wanajifanya kujua mambo wasiyoyajua na kujaribu kujifanya wataalamu. Kazi wanayofanya ni ya kijuujuu tu. Tatizo linapotokea, wao hutumia kanuni kulitatua kiupofu. Wanahangaika tu bila mwelekeo na bila kutoa matokeo yoyote halisi. Kwa sababu viongozi hawa wa uwongo hawaelewi kanuni za ukweli, na wanafoka tu maneno na mafundisho na kuwashauri wengine watii kanuni, maendeleo ya kila kipengele cha kazi ya kanisa yanacheleweshwa na hakuna matokeo ya wazi yanayopatikana. Matokeo dhahiri zaidi ya kiongozi wa uwongo kuwa kazini kwa muda fulani ni kwamba watu wengi hawawezi kuelewa ukweli, hawajui jinsi ya kutambua wakati wowote ambapo mtu anafichua upotovu au kuwa na dhana, na hakika hawaelewi kanuni za ukweli zinazopaswa kushikiliwa katika kutekeleza wajibu wao. Wale wanaotekeleza wajibu wao na wale wasiotekeleza wote ni wazembe, wasiozuiwa na wasio na nidhamu, na waliovurugika kama mchanga uliotawanyika. Wengi wao wanaweza kusema maneno na mafundisho machache, lakini wanapokuwa wakifanya wajibu wao, wanashikilia tu kanuni; hawajui jinsi ya kutafuta ukweli ili kutatua matatizo. Kwa kuwa viongozi wa uwongo wenyewe hawajui jinsi ya kutafuta ukweli ili kutatua matatizo, wanawezaje kuwaongoza wengine kufanya hivyo? Haijalishi ni kitu gani kinachowapata watu wengine, viongozi wa uwongo wanaweza tu kuwahimiza kwa kusema, "Lazima tuzifikirie nia za Mungu!" "Lazima tuwe na uaminifu katika utekelezaji wa wajibu wetu!" "Jambo fulani linapotupata, lazima tujue jinsi ya kuomba, na lazima tutafute kanuni za ukweli!" Viongozi wa uwongo mara nyingi hutoa kauli mbiu kwa kupiga kelele na mafundisho haya, na hili halitoi matokeo yoyote hata kidogo. Baada ya watu kuyasikia, bado hawaelewi kanuni za ukweli ni zipi, na wanakosa njia ya utendaji. Kwa nje, watu huomba mambo yanapowapata, na wanataka kuwa waaminifu katika kufanya wajibu wao—lakini wote wanakosa uelewa wa masuala kama vile kile wanachopaswa kufanya ili kuwa waaminifu, jinsi wanavyopaswa kuomba ili kuelewa nia za Mungu, na jinsi wanavyopaswa kutafuta wanapokumbana na tatizo ili kupata uelewa wa kanuni za ukweli. Watu wanapowauliza viongozi wa uwongo, wao husema, "Jambo linapokupata, soma maneno ya Mungu zaidi, omba zaidi, na ufanye ushirika zaidi juu ya ukweli." Watu huuliza, "Kazi hii inagusa kanuni zipi?" na wao husema, "Maneno ya Mungu hayasemi chochote kuhusu mambo ya kazi ya kitaalamu, na sielewi sehemu hiyo ya kazi pia. Fanyeni utafiti wenu wenyewe mkitaka kuelewa—msiniulize. Ninawaongoza katika kuelewa ukweli, si katika mambo ya kazi ya kitaalamu." Viongozi wa uwongo hutumia maneno ya aina hii kukwepa maswali. Na matokeo yake, ingawa watu wengi wana shauku kubwa ya kufanya wajibu wao, hawajui jinsi ya kutenda kulingana na kanuni za ukweli, wala hawajui jinsi ya kushikilia kanuni wanapokuwa wakitekeleza wajibu wao. Kuyaangalia matokeo ya kila kipengele cha kazi ndani ya mawanda ya wajibu wa viongozi wa uwongo, watu wengi wanategemea maarifa, elimu, na karama zao kufanya kazi yao, na hawajui kuhusu masuala kama vile mahitaji mahususi ya Mungu ni yapi, kanuni za kufanya wajibu ni zipi, na jinsi ya kutenda ili kufikia matokeo ya kumshuhudia Mungu na jinsi ya kueneza injili kwa ufanisi zaidi ili wote wanaotamani kuonekana kwa Mungu waisikie sauti Yake, wachunguze njia ya kweli, na kumrudia Mungu haraka iwezekanavyo. Kwa nini hawajui mambo haya? Hili linahusiana moja kwa moja na kushindwa kwa viongozi wa uwongo kufanya kazi halisi. Sababu kuu ya hili ni kwamba viongozi wa uwongo wenyewe hawajui kanuni za ukweli ni zipi, au ni kanuni zipi ambazo watu wanapaswa kuelewa na kufuata. Wanatenda bila kanuni, na hawawaongozi watu kamwe kutafuta kanuni za utendaji na njia katika wajibu wao. Kiongozi wa uwongo anapopata tatizo, hawezi kulitatua mwenyewe, na hashiriki wala kutafuta na wengine, jambo ambalo husababisha kazi kuhitaji kufanywa upya mara kwa mara katika kila kipengele cha kazi. Huu si ufujaji wa rasilimali za kifedha na mali tu, bali pia wa nguvu na wakati wa watu. Matokeo kama haya yanahusiana moja kwa moja na ubora duni wa tabia na kutowajibika kwa viongozi wa uwongo. Ingawa haiwezi kusemwa kwamba viongozi wa uwongo hutenda maovu kimakusudi na kusababisha usumbufu, inaweza kusemwa kwamba huwa hawatafuti kanuni za ukweli hata kidogo katika kazi yao, kwamba daima wao hutenda kulingana na mapenzi yao wenyewe. Hili ni hakika. Viongozi wa uwongo hawaelewi kanuni za ukweli, wala hawawezi kushiriki waziwazi kuzihusu na wengine; badala yake, wanawapa watu uhuru wa kufanya wanavyotaka. Bila kukusudia hili husababisha baadhi ya watu wanaosimamia kazi fulani kutenda kiholela na kwa ukaidi, wakitenda wanavyotaka na kufanya chochote wanachopenda. Matokeo yake, siyo tu kwamba kuna matokeo machache halisi, bali pia kazi ya kanisa inavurugwa kabisa. Kiongozi wa uwongo anapotimuliwa, sio tu kwamba hajitafakari au kujijua, pia anajihusisha na ujanja wa maneno na kujitetea, na hakubali ukweli hata kidogo, na hana nia kabisa ya kutubu. Anaweza hata kuomba kwamba nyumba ya Mungu impe nafasi nyingine, akisema kwamba anaweza kufanya kazi vizuri. Je, mnamwamini? Hajijui hata kidogo, wala hakubali ukweli. Je, hivyo anaweza kubadilisha njia zake? Hana uhalisi wa ukweli, kwa hivyo anaweza kufanya kazi vizuri? Je, hilo linawezekana? Hakufanya kazi vizuri wakati huu—je, aataweza kuifanya vizuri akipewa nafasi nyingine? Hilo haliwezekani. Inaweza kusemwa kwa uhakika kwamba viongozi wa uwongo hawana uwezo wa kazi; wakati mwingine, wanaweza kumenyeka sana na kuwa na shughuli nyingi, lakini ni kuhangaika kwa upofu, na hazizai matunda. Hili linatosha kuonyesha kwamba viongozi wa uwongo wana ubora duni sana wa tabia, kwamba hawaelewi ukweli hata kidogo, na kwamba hawawezi kufanya kazi halisi. Hili husababisha matatizo mengi kutokea katika kazi, lakini hawawezi kuyatatua kwa kushiriki juu ya ukweli, na wanatumia tu mafundisho machache matupu kuwahimiza watu kutii kanuni, na kwa hivyo wao huvuruga kazi na kuiacha ikiwa shaghalabaghala. Hii ndiyo namna viongozi wa uwongo wanavyofanya kazi na matokeo yanayoletwa na hilo. Viongozi na wafanyakazi wote wanapaswa kulichukulia hili kama onyo.

Matatizo mbalimbali yasiyoridhisha ambayo hutokea ndani ya kanisa yanahusiana moja kwa moja na viongozi wa uwongo—hili ni tatizo lisiloepukika. Viongozi hawa wa uwongo wanakosa uwezo wa kufahamu ukweli, lakini wanafikiri kwamba wanaelewa na kufahamu kila kitu, na kisha wanatenda kulingana na mawazo na dhana zao wenyewe. Hawatafuti kamwe ukweli ili kushughulikia ukosefu wao wa uelewa wa kanuni za ukweli au wa viwango vinavyohitajika na Mungu. Nimetangamana na viongozi na wafanyakazi wengi, na Ninakutana nao mara kwa mara. Tunapokutana, Mimi huwauliza, "Je, mna masuala yoyote? Je, mumeweka rekodi ya matatizo yaliyopo katika kazi? Je, kuna matatizo yoyote ambayo hamwezi kuyatatua wenyewe?" Baada ya kumaliza, wanakodoa macho bila kusema kitu, na mioyoni mwao wana mashaka: "Sisi ni viongozi; tunaweza kuwa na masuala yoyote? Kama tungekuwa nayo, je, kazi ya kanisa isingekuwa imepooza zamani? Hili ni swali la aina gani? Sisi husikiliza mahubiri na kufanya ushirika, na kushikilia maneno ya Mungu mikononi mwetu. Kanisa lina watu wengi sana kama sisi tunaoliongoza, unawezaje bado kuwa na wasiwasi? Kwa kuuliza swali hili, ni wazi kwamba Wewe unatudharau. Tungekuwaje na matatizo? Kama tungekuwa na matatizo, tusingekuwa viongozi. Swali lako halifai kabisa!" Kila Ninapowauliza kama wana masuala yoyote, hii ndiyo aina ya hali waliyo nayo—kila mmoja wao ni picha ya kufa ganzi na ujuha. Kuna matatizo mengi sana katika vipengele mbalimbali vya kazi ya kanisa, lakini watu hawa hawayaoni wala kuyagundua. Hawawezi kuibua masuala yanayohusiana na kuingia katika uzima kwao binafsi, au masuala yaliyopo katika kazi yanayohusisha kanuni za ukweli. Kwa kuwa hawawezi kuibua masuala haya, Ninawauliza, "Je, kazi ya kutafsiri maneno ya Mungu inaendeleaje? Je, mnajua ni lugha ngapi zinazopaswa kutafsiriwa sasa? Ni lugha zipi zinazopaswa kutafsiriwa kwanza, na zipi zitafsiriwe baadaye? Ni nakala ngapi za maneno ya Mungu zinazopaswa kuchapishwa kwa lugha fulani?" Wanajibu, "Ah, zinatafsiriwa." Ninawauliza, "Tafsiri imefikia kiwango gani? Je, kuna masuala yoyote?" Wanajibu, "Sijui; nahitaji kwenda kuuliza." Lazima Niwaulize kuhusu mambo haya, na bado hawajui majibu. Kwa hiyo wamekuwa wakifanya kazi gani muda huu wote? Ninawauliza, "Je, ulitatua masuala ambayo akina ndugu waliuliza wakati uliopita?" Wanajibu, "Nilifanya mkutano nao—mkutano wa siku nzima." Ninawauliza, "Je, masuala yalitatuliwa baada ya mkutano?" Wanajibu, "Je, Unamaanisha kwamba ikiwa bado kuna masuala, tunapaswa kuwa na mkutano mwingine?" Ninasema, "Siulizi kama ulifanya mkutano au la. Ninauliza kama masuala ya kitaalamu yametatuliwa. Je, watu hawa wanaelewa kanuni? Je, wamekiuka kanuni zozote katika utekelezaji wa wajibu wao? Je, umegundua matatizo yoyote?" Wanajibu, "Ah, matatizo? Niliyatatua. Niliwafanyia akina ndugu mkutano." Je, mazungumzo haya yanaweza kuendelea? (Hapana, hayawezi.) Je, kusikiliza mazungumzo haya hakuwafanyi mkasirike? (Ndiyo.) Viongozi hawa wakoje? Je, hawa si wajinga wanaojifanya kuwa wa kiroho tu? Wanakosa ubora wa tabia wa viongozi na wafanyakazi; ni vipofu, hawaelewi jinsi ya kufanya kazi, na wanajibu "Sijui" kwa kila swali, na mnapoendelea kuwauliza maswali, wanajibu, "Hata hivyo, nilifanya mkutano; achana na hilo!" Je, viongozi hawa wamefanya kazi halisi? Je, wanafikia kiwango kinachohitajika kama viongozi? (Hapana.) Hawa ni viongozi wa uwongo. Je, mnawapenda viongozi wa aina hii? Mkiwakuta viongozi kama hawa, mnapaswa kufanya nini? Baadhi ya viongozi wanapokutana na akina ndugu, wao husema, “Bila kujali mna masuala gani leo, hebu kwanza tushiriki kuhusu jinsi ya kutekeleza wajibu vizuri.” Kisha baadhi ya watu husema, “Tumekumbana na suala la mbinu za kitaalamu katika wajibu wetu: Je, tunapaswa kutumia mbinu za kitaalamu ambazo ni maarufu kwa wasioamini?” Je, hili si tatizo ambalo viongozi wanahitaji kulitatua? Ikiwa masuala fulani hayawezi kutatuliwa kupitia ushirika miongoni mwa ndugu, viongozi wanapaswa kuingilia kati ili kuyatatua—hili linagusia majukumu ya viongozi. Viongozi wa uwongo hufanya nini wanapokumbana na matatizo haya? Wao husema, “Hili ni suala la kitaalamu; ni tatizo lenu, linanihusu nini mimi? Fanyeni ushirika kuhusu suala hili ninyi wenyewe, lakini kwanza, nitawafanyia mkutano. Katika mkutano wa leo, tutafanya ushirika kuhusu kushirikiana kwa maelewano. Swali mlilouliza hivi punde linahusiana na kushirikiana kwa maelewano. Mnapaswa kuweza kujadili mambo na kushiriki pamoja, na kufanya utafiti zaidi; hakuna anayepaswa kujihesabia haki, na kila mtu anapaswa kukubali uamuzi wowote unaoungwa mkono na wengi—je, hili si suala la kushirikiana kwa maelewano? Inaonekana hamjui jinsi ya kushirikiana kwa maelewano, au jinsi ya kujadili matatizo yanapotokea. Mnaniuliza kuhusu kila tatizo. Kwa nini mnaniuliza mimi? Je, mimi nayaelewa mambo haya? Kama ningeyaelewa, je, si ninyi mngekosa cha kufanya? Mnaniuliza kuhusu kila kitu. Je, hili ni tatizo ambalo ninapaswa kulishughulikia? Mimi ninawajibikia tu kufanya ushirika juu ya ukweli; tatueni masuala ya kitaalamu ninyi wenyewe. Yananihusu nini? Hata hivyo, tayari nimefanya ushirika nanyi na kuwaambia mshirikiane kwa maelewano—kama hamwezi kufanya hivyo, basi msitekeleze wajibu huu. Nimemaliza ushirika wangu; nendeni mkatatue tatizo ninyi wenyewe.” Je, viongozi hawa wanajua jinsi ya kutatua matatizo? (Hapana, hawajui.) Licha ya kutojua jinsi ya kufanya hivi, wanajiona wako kwamba sahihi kabisa, na ni hodari wa kukwepa wajibu. Kwa nje, wamefanya kazi yao, wamefika kwenye eneo la kazi kufanya ukaguzi, na hawazembei. Hata hivyo, hawawezi kufanya kazi halisi au kutatua matatizo halisi, jambo ambalo linamaanisha kwamba wao ni viongozi wa uwongo. Je, mnaweza kumtambua kiongozi wa uwongo wa aina hii? Wanapokabiliwa na tatizo lolote, hawawezi kufanya ushirika juu ya ukweli unaohusika: wao husema tu mafundisho na nadharia tupu ambazo wanazifanya zisikike kuwa za juu na za kina sana, na baada ya watu kuzisikia, sio tu kwamba hawaelewi ukweli, pia wanahisi kuchanganyikiwa na kukosa mwelekeo. Hii ndiyo kazi ambayo viongozi wa uwongo hufanya.

Katika kazi ya kufanya ushirika juu ya kanuni za ukweli zinazopaswa kueleweka ili kutekeleza kila wajibu ipasavyo, viongozi wa uwongo wanafichuliwa kabisa. Hawawezi kufanya ushirika juu ya kanuni za ukweli, au kuwaongoza watu kutii na kutenda kanuni za ukweli katika utekelezaji wa wajibu wao, au kuwaongoza kuelewa na kuingia katika uhalisi wa ukweli—hawawezi kutimiza majukumu ambayo viongozi wanapaswa kutimiza. Na si hayo tu, pia hawawezi kufahamu hali ya wasimamizi wa kazi mbalimbali na wafanyakazi wanaohusika na kazi mbalimbali muhimu, na hata kama wana ufahamu kiasi kuhusu hili, si sahihi. Hili husababisha usumbufu mkubwa na madhara kwa vipengele mbalimbali vya kazi. Huu ndio udhihirisho mbalimbali wa viongozi wa uwongo tutakaoufichua leo kuhusu jukumu la nne la viongozi na wafanyakazi.

Kipengele cha Nne: Kufahamu hali ya wasimamizi wa kazi mbalimbali na wafanyakazi wanaohusika na kazi mbalimbali muhimu, na kurekebisha mara moja kazi zao au kuwatimua inapobidi, ili kuzuia au kupunguza hasara zinazosababishwa na kutumia watu wasiofaa, na kuhakikisha ufanisi na maendeleo sambamba ya kazi

Viongozi na Wafanyakazi Lazima Wafahamu Hali za Wasimamizi wa Kazi Tofauti

Jukumu la nne la viongozi na wafanyakazi ni lipi? (“Kufahamu hali ya wasimamizi wa kazi mbalimbali na wafanyakazi wanaohusika na kazi mbalimbali muhimu, na kurekebisha mara moja kazi zao au kuwatimua inapobidi, ili kuzuia au kupunguza hasara zinazosababishwa na kutumia watu wasiofaa, na kuhakikisha ufanisi na maendeleo sambamba ya kazi.”) Hiyo ni sahihi, hiki ndicho kiwango cha chini kabisa ambacho viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuweza kufikia wanapofanya kazi. Je, nyote mnaelewa wazi majukumu makuu ya viongozi na wafanyakazi kuhusu kipengele hiki cha nne? Viongozi na wafanyakazi lazima wawaelewe vizuri wasimamizi wa kazi mbalimbali na wafanyakazi wanaohusika na kazi mbalimbali muhimu. Kufahamu hali za wasimamizi wa kazi mbalimbali na wafanyakazi wanaohusika na kazi mbalimbali muhimu kuko ndani ya upeo wa majukumu ya viongozi na wafanyakazi. Basi, wafanyakazi hawa ni akina nani? Kimsingi, kuna viongozi wa kanisa, wakifuatiwa na wasimamizi wa timu na viongozi wa vikundi mbalimbali. Je, si ni jambo muhimu sana na la maana kubwa kuelewa na kufahamu hali kama vile iwapo wasimamizi wa kazi mbalimbali na wafanyakazi wanaohusika na kazi mbalimbali muhimu wanamiliki uhalisi wa ukweli, wana kanuni katika matendo yao, na wanaweza kufanya kazi ya kanisa vizuri? Ikiwa viongozi na wafanyakazi watafahamu kwa kina hali za wasimamizi wakuu wa kazi mbalimbali, na kufanya mabadiliko yanayofaa kwa wafanyakazi, hilo ni sawa na wao kufanya uchunguzi ufaao kwa kila kipengele cha kazi, na ni sawa na wao kutimiza majukumu na wajibu wao. Ikiwa mabadiliko sahihi hayatafanywa kuhusu wafanyakazi hawa na tatizo litokee, kazi ya kanisa itaathirika sana. Ikiwa wafanyakazi hawa wana ubinadamu mzuri, wanamiliki msingi katika imani yao kwa Mungu, wanawajibika katika kushughulikia mambo, na wanaweza kutafuta ukweli ili kutatua matatizo, basi kuwaweka wasimamie kazi kutaepusha shida nyingi, na la muhimu zaidi kutaruhusu kazi iendelee vizuri. Lakini ikiwa wasimamizi wa timu mbalimbali si wa kutegemewa, wana ubinadamu duni, hawana mwenendo mzuri, na hawaweki ukweli katika vitendo, na, zaidi ya hayo, wana uwezekano wa kusababisha vurugu na usumbufu, basi hili litakuwa na athari kwa kazi wanayowajibikia na kwa kuingia katika uzima kwa akina ndugu wanaowaongoza. Bila shaka, athari hiyo inaweza kuwa kubwa au ndogo. Ikiwa wasimamizi ni wazembe tu katika wajibu wao na hawashughulikii kazi yao inayofaa, hili pengine litasababisha tu ucheleweshaji fulani katika kazi; maendeleo yatakuwa ya polepole kidogo, na kazi itakosa ufanisi kidogo. Ikiwa ni wapinga Kristo, hata hivyo, tatizo litakuwa kubwa: Hili halitakuwa suala la kazi kukosa ufanisi au matokeo kidogo—watavuruga na kuharibu kazi ya kanisa wanayowajibikia, wakisababisha madhara makubwa. Na kwa hivyo, kufahamu hali za wasimamizi wa kazi mbalimbali na wafanyakazi wanaohusika na kazi mbalimbali muhimu, na kufanya marekebisho au kuwatimua kwa wakati baada ya kugundua kwamba mtu fulani hafanyi kazi halisi si wajibu ambao viongozi na wafanyakazi wanaweza kuukwepa—ni kazi nzito sana, muhimu sana. Ikiwa viongozi na wafanyakazi wanaweza kupata kujua mara moja tabia ya wasimamizi wa kazi mbalimbali na wafanyakazi wanaohusika na kazi mbalimbali muhimu, na mtazamo wao kuelekea ukweli na wajibu wao, pamoja na hali zao na utendaji wao wakati wa kila kipindi na katika kila hatua, na kufanya marekebisho mara moja na kuwashughulikia watu hao kulingana na hali, basi kazi inaweza kuendelea kwa uthabiti. Kinyume chake, ikiwa watu hao wanafanya mambo kiholela na kutenda mabaya na hawafanyi kazi halisi kanisani, na viongozi na wafanyakazi hawawezi kutambua hili mara moja na kufanya marekebisho kwa wakati, lakini wanasubiri hadi matatizo makubwa ya kila aina yatokee, yakileta hasara kubwa kwa kazi ya kanisa, kabla ya kujaribu kuyashughulikia kwa kutoijali, kufanya marekebisho, na kurekebisha na kuokoa hali hiyo, basi viongozi na wafanyakazi hao ni takataka. Wao ni viongozi wa uwongo halisi ambao lazima watimuliwe na kuondoshwa.

Hivi punde, tumefanya ushirika kwa njia pana juu ya umuhimu wa kuelewa na kuwa na ufahamu wa hali halisi za wasimamizi wa kazi mbalimbali na ufanisi wa kazi yao, tukitumia hali hizi halisi kutathmini kama viongozi na wafanyakazi wametimiza majukumu yao, na kufichua ni madhihirisho gani wanayoonyesha ambayo yanathibitisha kwamba wao ni viongozi wa uwongo, na hivyo kuchanganua kiini cha viongozi wa uwongo. Matatizo makubwa yanapotokea katika kazi ya kanisa, viongozi wa uwongo hushindwa kutimiza majukumu yao. Hawawezi kugundua masuala haya mara moja, sembuse kuyashughulikia na kuyatatua kwa wakati. Hili husababisha masuala hayo kuendelea kwa muda mrefu, jambo ambalo pia husababisha ucheleweshaji na madhara kwa kazi ya kanisa, na linaweza hata kusababisha kazi ya kanisa kupooza au kuwa shaghalabaghala. Ni pindi tu hili linapotokea ndipo viongozi wa uwongo huenda shingo upande kuangalia eneo la kazi ya kanisa, lakini bado hawawezi kutambua suluhu zinazolingana au zinazofaa kutatua matatizo, na hatimaye wanayaacha tu bila kutatuliwa. Huu ndio udhihirisho wa msingi wa viongozi wa uwongo.

Viwango vya Kuchagua Wasimamizi wa Kazi Tofauti

Je, watu wengi kabisa wanaelewa kiasi kuhusu viwango vya kuchagua wasimamizi wa kazi tofauti na wafanyakazi wanaowajibikia kazi mbalimbali muhimu? Kwa mfano, msimamizi wa kazi ya sanaa anapaswa kuwa na nini kwanza kabisa? (Anapaswa kuwa na ujuzi wa kitaalamu katika nyanja hii na aweze kuimudu kazi hiyo.) Kuwa na ujuzi wa kitaalamu ni nadharia moja. Basi, ujuzi huu wa kitaalamu unarejelea nini hasa? Hebu tufafanue hili. Ikiwa mtu anafurahia kuchora na anavutiwa na kufanya sanaa, lakini si taaluma yake, na hana maarifa katika eneo hili, na analipenda tu, je, inafaa kumchagua mtu wa aina hiyo kama msimamizi wa timu ya sanaa? (Hapana, haifai.) Wengine husema, “Ikiwa anapenda kutengeneza sanaa, anaweza kufanya kazi hiyo na ajifunze kuihusu polepole.” Je, kauli hii ni sahihi? (Hapana.) Kuna hali moja ya kipekee kuhusu hili, ambao ni ikiwa kila mtu mwingine kwenye timu ya sanaa pia hafahamu taaluma hiyo, na mtu huyu anajua zaidi kidogo na anajifunza haraka kuwashinda wengine. Je, kumchagua lingekuwa jambo la kufaa kwa kiasi fulani basi? (Ndiyo.) Mbali na hali hili, tuseme kwamba kati ya wale wote wanaohusika katika kuunda sanaa, ni mtu huyu tu asiyejua taaluma hiyo, lakini anachaguliwa kwa sababu anaelewa ukweli na anapenda kufanya sanaa—je, hilo linafaa? (Hapana, halifai.) Kwa nini halifai? Kwa sababu yeye si chaguo la kwanza au la pekee. Basi, msimamizi wa aina hii anapaswa kuchaguliwaje? Anapaswa kuchaguliwa kutoka miongoni mwa wale ambao ni mahiri zaidi na wenye uzoefu zaidi katika taaluma hiyo; yaani, ni lazima awe mtaalamu, aliye na ujuzi wa kitaalamu na uwezo wa kazi—usichague mtu asiye na ujuzi. Hiki ni kipengele kimoja. Zaidi ya hayo, lazima abebe mzigo, awe na ufahamu wa kiroho, na aweze kuelewa ukweli. Lazima pia awe na angalau msingi katika imani yake kwa Mungu. Kanuni kuu ni: Kwanza, lazima awe na uwezo wa kazi; pili, lazima aelewe taaluma hiyo; na tatu, lazima awe na ufahamu wa kiroho na aweze kuelewa ukweli. Tumia vigezo hivi vitatu kuwachagua wasimamizi wa kazi tofauti.

Udhihirisho wa Viongozi wa Uwongo Kuhusiana na Wasimamizi wa Kazi Tofauti

Baada ya kuwachagua wasimamizi wa vipengele mbalimbali mahususi vya kazi, viongozi na wafanyakazi hawapaswi tu kukaa kando na kutofanya chochote; wanapaswa pia kuwafundisha na kuwakuza wasimamizi hawa kwa muda, ili kuona ikiwa watu waliochaguliwa wanaweza kweli kuimudu kazi hiyo na kuiweka kwenye njia sahihi. Hiyo ndiyo maana ya kutimiza majukumu yao. Tuseme kwamba, wakati wa uteuzi, unaona kwamba watahiniwa wako wanaelewa taaluma zao, wana uwezo wa kazi, wanabeba mzigo kiasi, na wana ufahamu wa kiroho na uwezo wa kuelewa ukweli, na unadhani kwamba kila kitu kitakuwa sawa kwa sababu wanastahili katika nyanja hizi, na useme, “Mnaweza kuanza kufanya kazi; nimewaambia kanuni zote. Kuanzia sasa, fanyeni tu kile ambacho nyumba ya Mungu inawaagiza mfanye ninyi wenyewe.” Je, hii ni njia inayokubalika ya kutekeleza kazi? Mara tu unapowapanga wasimamizi, je, hili linamaanisha kwamba unaweza kuachia hapo tu? (Hapana, halimaanishi hivyo.) Basi ni kitu gani kinachopaswa kufanywa? Tuseme kiongozi anakutana na wasimamizi mara mbili kwa wiki, anafanya ushirika wa ukweli nao, na kuishia hapo, akiamini kwamba kwa sababu wasimamizi hao wote wanajituma, ni wa kutegemewa, na wana uwezo wa kuelewa kile ambacho watu wengine wanasema, kwa hiyo wanaweza kutenda kulingana na ukweli. Kiongozi huyu anadhani kwamba hawahitaji kuchunguza au kufuatilia jinsi wasimamizi hawa wanavyofanya kazi yao hasa, ikiwa wanashirikiana kwa amani na wengine, ikiwa wameufahamu ujuzi wa kitaalamu katika kipindi hiki, au ni kiasi gani wamekamilisha kazi waliyopewa na nyumba ya Mungu. Je, hii ndiyo njia ambayo kiongozi na mfanyakazi anapaswa kushughulikia kazi? (Hapana, siyo.) Hivi ndivyo viongozi wa uwongo wanavyofanya kazi yao. Hujaribu kumaliza kazi yote mara moja, wanawapanga wasimamizi na kuunda timu yenye washiriki wachache, na kisha wanasema, “Anzeni kazi. Mkihitaji kifaa chochote, nijulisheni, na nyumba ya Mungu itawanunulia. Mkishindwa na jambo lolote katika maisha yenu ya kila siku au mkikumbana na matatizo yoyote, kuweni huru kuyataja, na nyumba ya Mungu itayatatua kila wakati kwa ajili yenu. Ikiwa hamna matatizo yoyote, basi zingatieni kazi yenu. Msisababishe vurugu au usumbufu, na msitoe mawazo yoyote ya majivuno.” Viongozi wa uwongo huwapanga watu hawa kufanya kazi pamoja, na kufikiri kwamba mradi tu wana chakula, vinywaji, na mahali pa kuishi, hiyo inatosha, na hakuna haja ya kuwajali. Aliye juu anapouliza, “Ni muda gani umepita tangu wasimamizi wa kazi hii walipochaguliwa? Kazi inaendeleaje?” wao hujibu, “Imepita miezi sita. Tumefanya mikutano karibu 10 kwa ajili yao, na wanaonekana kuwa na ari nzuri, na kazi inafanywa.” Aliye juu anapouliza, “Basi uwezo wa kazi wa wasimamizi ukoje?” wanasema, “Ni mzuri tu; tulipowachagua, walikuwa bora zaidi.” Aliye juu anawauliza, “Wanaendeleaje sasa? Je, wanaweza kufanya kazi halisi?” Wanajibu, “Nilifanya mkutano kwa ajili yao.” Aliye juu anajibu, “Sikuuliza ikiwa ulifanya mkutano; niliuliza kazi yao inaendeleaje.” Wanasema, “Pengine ni nzuri; hakuna aliyeripoti chochote kibaya kuwahusu.” Aliye juu anajibu, “Kutokuwepo kwa mtu anayeripoti chochote kibaya kuwahusu si kigezo. Unahitaji kuangalia jinsi uwezo wao wa kazi na ujuzi wao wa kitaalamu ulivyo, na uone kama wana ufahamu wa kiroho, na ikiwa wanafanya kazi halisi.” Wanajibu, “Wakati wa uteuzi, walionekana kuwa sawa. Sijaulizia maelezo haya kwa muda. Kama unataka kujua, nitauliza tena.” Hivi ndivyo viongozi wa uwongo wanavyofanya kazi. Wanaendelea kufanya mikutano na ushirika bila kikomo na wale walio chini yao, lakini linapokuja suala la Aliye juu, wanaepa kusema ukweli wote na kutoa majibu ya kijuujuu tu. Jibu lao bora la kijuujuu ni kusema, “Nilifanya mkutano kwa ajili yao. Mara ya mwisho, niliuliza kuhusu kazi, kwa kina sana.” Hivi ndivyo wanavyomjibu Aliye juu. Je, viongozi hawa wa uwongo wanafanya kazi halisi? Je, wamebaini masuala halisi? Je, wameyatatua? Baada ya kuwapanga wasimamizi, viongozi wa uwongo hawajui kabisa ikiwa wasimamizi wametimiza majukumu yao au wamekuwa waaminifu, jinsi kazi inavyofanywa, ikiwa matokeo ni mazuri au mabaya, jinsi ndugu wanavyotoa ripoti kuwahusu, au ikiwa kuna watu wanaofaa zaidi kwa kazi hiyo. Kwa nini hawajui mambo haya? Kwa sababu hawafanyi kazi hii halisi; wanajishughulisha tu na mambo yasiyo na maana. Wanadhani si lazima kusimamia na kukagua kazi kila wakati namna hii, kwamba hilo lingemaanisha walikosa imani na wasimamizi hao. Akilini mwao, kufanya mikutano ni kutimiza majukumu yao na kuonyesha uaminifu. Huu ndio udhihirisho mkuu wa viongozi wa uwongo kutofanya kazi halisi.

I. Jinsi Viongozi wa Uwongo Wanavyowatendea Wasimamizi Wasiofanya Kazi Halisi

Viongozi wa uwongo hufumbia macho hali mbalimbali za wasimamizi wa kila aina ya kazi kanisani; hawana ufahamu wa hali hizi, au kuzichunguza, au kuzishughulikia, au kuzitatua. Kuna hali gani mahususi za wasimamizi? Ya kwanza ni wakati wasimamizi hawabebi mzigo, na wanakula, kunywa, na kutafuta burudani, bila kujali kazi yao inayofaa au kufanya kazi halisi. Je, si hili ni tatizo zito? (Ndiyo.) Watu wengine wana uwezo wa kazi, ni mahiri katika taaluma fulani, na wao ndio bora zaidi; wana ufasaha wa kuongea na wana akili, na wakiulizwa warudie maagizo wanaweza kufanya hivyo bila kukosa neno, wana akili ya kutosha; wanapokea tathmini nzuri sana kutoka kwa kila mtu, na wamekuwa waumini kwa muda mrefu. Kwa hiyo, wanachaguliwa kuwa wasimamizi. Hata hivyo, hakuna anayejua ikiwa watu hawa wanajali uhalisi wa mambo, wanaweza kulipa gharama, au wana uwezo wa kufanya kazi halisi. Kwa kuwa watu waliwachagua, mwanzoni wanapandishwa cheo ili kukuzwa na kutumiwa katika nafasi ya majaribio. Hata hivyo, baada ya kufanya kazi kwa muda, inagundulika kuwa licha ya ujuzi wao wa kitaalamu na uzoefu, ni walafi na wavivu, na hawako tayari kulipa gharama. Wanaacha kufanya kazi mara tu inapochosha kidogo, na hawataki kumshughulikia mtu yeyote aliye na matatizo au shida anayehitaji mwongozo wao. Asubuhi, mara tu wanapofungua macho yao wanafikiri, “Nitakula nini leo? Imepita siku nyingi tangu jikoni walipopika nyama ya nguruwe ya kukaangwa.” Kwa kawaida, wao huwaambia wengine kila mara, “Kumbwe katika mji wangu wa nyumbani ni tamu sana; tulikuwa tukienda kula wakati wa kila tamasha. Nilipokuwa shuleni, wikendi nilikuwa nikilala hadi niamke kawaida, na kisha ningeenda kula bila kujisumbua kunawa uso au kuchana nywele zangu. Alasiri, ningecheza michezo ya video ndani ya nyumba nikiwa nimevaa nguo za kulala, wakati mwingine hadi saa 11 alfajiri siku inayofuata. Sasa, kazi katika nyumba ya Mungu imenilazimisha kufika hatua hii, na kama msimamizi, lazima nifanye mambo fulani. Angalieni jinsi ninyi nyote mlivyo na maisha mazuri; hamhitaji kulipa gharama hii. Kama msimamizi, lazima niweze kuvumilia ugumu.” Wanasema hivi, lakini, je, wanauasi mwili? Je, wanalipa gharama? Wamejaa malalamiko, na hawako tayari kufanya kazi yoyote halisi. Wanasonga tu wakisukumwa, na bila usimamizi, wanatenda kwa njia ya kijuujuu tu. Katika utekelezaji wa wajibu wao, wametulia na hawana nidhamu, mara nyingi wao ni wajanja na wanazembea, na hawana uwajibikaji hata kidogo. Linapokuja suala la matatizo ya kitaalamu ambayo wanayaona, hawawarekebishii watu wengine, na wanafurahi wakati kila mtu mwingine anatenda kwa njia ya kijuujuu tu kama wao. Hawataki mtu yeyote achukulie kazi kwa uzito. Wasimamizi wengine hukamilisha kazi chache walizo nazo mkononi kwa njia ya kawaida na ya kijuujuu tu, kisha wanaanza kutazama vipindi vya mfululizo bila kikomo. Sababu yao ya kutazama vipindi vya mfululizo ni nini? “Nimekamilisha kazi zangu; sili chakula cha nyumba ya Mungu bure. Ninastarehe tu ili kuburudisha akili yangu. Vinginevyo, nitachoka sana, na ufanisi wangu wa kazi utapungua. Acha nistarehe kwa muda, ili kuboresha ufanisi wangu wa kazi.” Wanaendelea kutazama vipindi vya mfululizo hadi saa nane au saa tisa usiku. Kila mtu anapokuwa amemaliza kiamsha kinywa siku inayofuata saa mbili asubuhi na kuanza kufanya wajibu wao, wasimamizi hawa bado wamelala, na hawatoki kitandani hata jua linapokuwa juu angani. Baadaye, wanaamka shingo upande, wakivuta miili yao iliyojaa uvivu mbele, wakinyoosha viungo na kupiga miayo, na wanapoona kwamba kila mtu mwingine ameanza kazi, wanaogopa kwamba wengine wataona uvivu wao, na huanza kutafuta visingizio, “Nilichelewa kulala jana usiku, nilikuwa na mengi ya kufanya, mzigo wa kazi ulikuwa mzito sana. Nimechoka kidogo. Hata niliota jana usiku kwamba kulikuwa na tatizo katika kazi fulani. Nilipoamka asubuhi ya leo, mikono yangu ilikuwa katika hali ya kupiga chapa kwenye kompyuta. Akili yangu imechanganyikiwa sana, na ninahitaji kulala kidogo mchana huu.” Wanaamka wakiwa wamechelewa sana na wanahitaji kulala kidogo mchana pia—je, hawajageuka kuwa nguruwe? Walikuwa wakizembea waziwazi, lakini wanatoa visingizio ili kuhalalisha na kujitetea, wakidai kwamba wamechoka kwa sababu walikuwa wakifanya wajibu wao hadi usiku sana. Walikuwa wakitazama vipindi vya mfululizo waziwazi, wakijishughulisha na starehe ya mwili, na kuishi katika hali ya anasa, lakini hatimaye wanapata hata kisingizio kizuri cha kuwadanganya wengine. Je, si huku ni kutofanya kazi yao ipasavyo? (Ndiyo.) Watu kama hawa wanaweza kuwa na uwezo wa kazi na ujuzi wa kitaalamu, lakini, je, wanafikia kiwango kinachohitajika kama wasimamizi? Bila shaka hawafikii. Hawafai kuwa wasimamizi kwa sababu ni wavivu sana, wanajishughulisha na starehe ya mwili, ni walafi wa chakula, kulala, na burudani, na hawawezi kubeba au kutimiza majukumu ya msimamizi.

Wanawake wengine mara nyingi huangalia nguo, viatu, vipodozi, na vyakula mtandaoni, na baada ya kumaliza, wanaanza kutazama vipindi vya mfululizo bila kikomo. Watu husema, “Kwa nini unatazama vipindi vya mfululizo bila kikomo ilhali hujamaliza kazi yako? Zaidi ya hayo, watu wengine bado wana matatizo mengi. Kama msimamizi, unapaswa kuwapa mwongozo. Kwa nini hutimizi majukumu yako?” Wanawake hawa husema, “Kutazama vipindi vya mfululizo bila kikomo pia ni sehemu ya kazi yangu. Video na filamu za nyumba ya Mungu zinahitaji kuendelezwa, na lazima nitafute msukumo katika vipindi hivi!” Je, hayo si maneno ya udanganyifu? Ikiwa unajihusisha na taaluma hii, kutazama vipindi mara kwa mara kwa ajili ya kupata msukumo kunakubalika, lakini, je, kutazama bila kikomo usiku na mchana ni kutafuta msukumo? Je, si huo ni udanganyifu? (Ndiyo.) Kila mtu anajua kinachoendelea, kwa hiyo kusema mambo kama hayo ni kuisaliti heshima na uadilifu wako. Watu wengine tayari wana tabia ya kucheza michezo ya video, na imekuwa sehemu ya kawaida ya maisha yao. Hata hivyo, baada ya kuchaguliwa kama wasimamizi, je, si kubadilisha kubadilisha tabia hizi mbaya na maovu haya? (Ndiyo.) Ikiwa huwezi kuasi dhidi ya haya, unapochaguliwa kama msimamizi, unapaswa kusema, “Siwezi kuimudu kazi hii. Nina uraibu wa kucheza michezo ya video. Ninapoicheza, ninafikia hali ya kujisahau kabisa, na hakuna anayeweza kuniingilia au kunishawishi. Mkinichagua, hakika itachelewesha kazi. Kwa hiyo chukueni hatua mapema na msiniruhusu niwe msimamizi.” Usipotangaza hili mapema na ufurahi na kujivuna unapochaguliwa, ukithamini hadhi hii, lakini uendelee kucheza michezo ya video upendavyo kama ulivyofanya hapo awali ukiwa msimamizi, hili halifai, na hakika litachelewesha kazi.

Wasimamizi wengine wana tabia fulani mbaya. Ndugu wanapowachagua, wengine hawaelewi hali yao, huku wengine wakiamini kwamba watu hawa wanaweza kujitumia kwa ajili ya Mungu muda wote, na kufikiri kwamba tabia mbaya na maovu ya vijana huenda yakabadilika polepole kadiri umri unavyosonga na kadiri wanavyoendelea kuelewa ukweli. Watu wengi wana mtazamo na mwelekeo huu wanapowachagua watu hawa kuwa wasimamizi. Baada ya watu hawa kuchaguliwa, wanafanya kazi kiasi, lakini hawadumu muda mrefu kabla ya kuwa hasi na wao huwaza, “Kuwa msimamizi si jambo rahisi. Lazima niamke mapema na nilale nikiwa nimechelewa, na lazima nifanye mengi zaidi na kuchunguza mengi zaidi kuliko watu wengine kila wakati. Pia lazima nihangaike zaidi, na kutumia muda na nguvu zangu nyingi zaidi. Kazi hii ni ngumu; inachosha sana!” Kwa hivyo, wanafikiria kuacha. Ikiwa hubebi mzigo, huwezi kufanya kazi ya msimamizi. Ikiwa unabeba mzigo moyoni mwako, utakuwa tayari kuhangaikia kazi, na hata ukiwa umechoka kidogo kuliko wengine, hutahisi kwamba unateseka. Hata wakati wa kupumzika, bado utakuwa ukiwaza, “Kazi ya leo iliendaje?” Ukikumbuka ghafla suala ambalo halijatatuliwa, hutaweza kulala. Ikiwa unabeba mzigo moyoni mwako, utakuwa ukiwaza kuhusu kazi kila wakati, na hutajali hata unakula au kupumzika vizuri kiasi gani. Ikiwa watu wanabeba mzigo mdogo sana kama wasimamizi, shauku yao kidogo inaweza kudumu kwa siku chache tu, na baada ya muda, baadhi yao hawawezi kuvumilia tena. Watawaza, “Kazi hii inachosha sana. Kuna njia gani ya mimi kujiburudisha na kustarehe kidogo? Nitacheza michezo ya video.” Wanafanya kazi vizuri kwa muda mfupi, lakini ghafla wanahisi hamu ya kucheza michezo ya video. Mara tu wanapoanza, hawawezi kuacha; mzigo mdogo waliokuwa wamebeba utapotea wanapocheza, pamoja na msukumo wao wa shauku wa kujitumia, azimio lao, na mtazamo wao chanya katika kufanya wajibu wao. Mtu anapowauliza jambo, wanakosa subira. Wao huwapogoa watu, au kuwafokea na kuwakejeli, au kufanya mambo kwa njia ya kijuujuu na kutelekeza kazi yao. Je, si kuna tatizo na wasimamizi hawa? (Ndiyo.) Wakati wa mchana, wanajikokota tu kazini kwa hali ya kusinzia na kuchanganyikiwa, na usiku, wakati hakuna anayetazama, wanacheza michezo ya video kwa siri, bila kulala usiku kucha. Mwanzoni, wanajihisi sawa kuhusu hilo, wakiwaza, “Sikuchelewesha kazi wakati wa mchana. Nimefanya kazi yote niliyopaswa kufanya. Nimetatua matatizo yote ambayo wengine wameniuliza. Hata nisipolala usiku ili kutenga muda wa kucheza michezo ya video, je, si huku kunanihesabia kuwa mwaminifu?” Matokeo yake, mara tu wanapoanza kucheza michezo ya video, hawawezi kuacha, na hawamsikilizi yeyote. Ingawa haliathiri kupumzika kwa watu wengine au mazingira ya kazi, je, wasimamizi kama hawa bado wanaweza kuimudu kazi yao? Wanaweza kuifanya vizuri? (Hapana.) Kwa nini? Mara nyingi wanacheza michezo ya video usiku kucha bila kulala na lazima wafanye kazi wakati wa mchana—mtu mmoja anaweza kuwa na nguvu kiasi gani? Je, ufanisi wao wa kazi utakuwa wa juu wakishikilia kucheza michezo ya video hivi? Hakika hapana. Kwa hivyo, wasimamizi kama hawa hawawezi kutimiza wajibu wao au kuimudu kazi yao hata kidogo. Ingawa wana ujuzi wa kitaalamu na ubora wa tabia kiasi, wanapenda kucheza na hawazingatii kazi yao inayofaa. Je, si wasimamizi hawa wanapaswa kutimuliwa? Wasipotimuliwa, kazi itacheleweshwa. Watu wengine husema, “Wakitimuliwa, hatutaweza kupata mtu mwingine yeyote aliye na ujuzi wa kitaalamu walio nao. Lazima tuwaruhusu wafanye kazi hii—bado wanaweza kuimudu kazi hata kama wanacheza michezo ya video.” Je, kauli hii ni sahihi? (Hapana.) Mtu hawezi kuzingatia mambo mawili kwa wakati mmoja; nguvu za mwanadamu zina kikomo. Ukielekeza nguvu zako nyingi katika kucheza, kujitolea kwako katika kutekeleza wajibu kutaathirika, na ufanisi wako katika kutekeleza wajibu utapungua sana. Huu ni mtazamo usio wa kuwajibika katika kutekeleza wajibu. Hata kama mtu ataweka moyo wake wote na nguvu zake zote katika wajibu wake, matokeo si lazima yafikie kiwango kinachohitajika kwa asilimia mia moja. Itakuwa mbaya zaidi ukiuelekeza moyo wako na nguvu zako nyingi katika kucheza—hutabaki na nguvu na mawazo mengi ya kutumia katika utekelezaji wa wajibu wako, na ufanisi wako katika kutekeleza wajibu utaathirika. Kusema kwamba utaathirika ni kusema kwa kiasi tu; katika uhalisi, ufanisi wako katika kutekeleza wajibu utaharibiwa vibaya sana. Wasimamizi kama hao wakitambuliwa, wajibu wao unapaswa kubadilishwa mara moja, na wanapaswa kutimuliwa, kwa sababu tayari wameharibika. Si tu kwamba utekelezaji wa wajibu wao haufikii kiwango kinachohitajika—tayari hawawezi kuimudu kazi yao na hawawezi kuwa na matokeo yoyote chanya katika kazi yao. Kwa hiyo, kutafuta mtu wa kuchukua kazi yao aliye makini na anayewajibika licha ya kuwa na ujuzi wa chini kidogo wa kitaalamu lingekuwa chaguo bora zaidi kuliko wao.

Hivi punde, Nimeshiriki juu ya aina mbalimbali za watu ambao ni walafi wa chakula, kulala, na burudani. Kuna mtu wa aina nyingine. Mwanzoni, wasimamizi wanapochaguliwa, mtu wa aina hii anaonekana kufaa kwa kila njia kwa ajili ya jukumu hilo, na ndugu wote wako tayari kumchagua. Wanafikiri kwamba mtu huyu ana ubinadamu mzuri, kwamba ana shauku, na ni mahiri katika taaluma yake, na pia ndiye bora na mwenye nguvu zaidi kwenye timu katika kila kipengele, jambo linalomfanya awe chaguo la wazi kwa nafasi ya msimamizi. Hata hivyo, muda fulani baada ya kuchaguliwa, mtu huyu anaanza kuhisi kusinzia mara kwa mara, hata wakati wa mikutano. Wengine wanapozungumza naye, yeye huchanganyikiwa kila wakati na kutoa majibu yasiyohusiana na maswali. Hakuwa hivi hapo awali, kwa nini ghafla inaonekana kama amekuwa mtu tofauti? Baadaye, mtu fulani anagundua bila kukusudia kwamba mazungumzo ya msimamizi huyu na mtu fulani yanasikika kama wawili hao wako katika uhusiano wa kimapenzi, na dhana zinaibuka kuhusu iwapo kweli wanajihusisha kimapenzi. Jambo hili linapozidi kuwa dhahiri, msimamizi huyu anazidi kuchanganyikiwa. Kila anapoulizwa maswali au kuzungumziwa kuhusu jambo fulani, majibu yake hayawi ya haraka kama hapo awali, na hasikiki kwa uwazi na kueleweka kama zamani. Anaanza kufanya kazi kidogo na kidogo ambayo msimamizi anapaswa kufanya, na anakuwa na shauku kidogo zaidi na zaidi katika kutekeleza wajibu wake. Ni kana kwamba amekuwa mtu tofauti; anavutiwa zaidi na nguo zake na mapambo ya kibinafsi kuliko hapo awali. Kuna tatizo hapa. Zamani, wakati wa vipindi vya kazi nyingi, alioga mara chache sana, lakini sasa ananawa uso wake mara mbili kwa siku, na kuchana nywele zake na kujiangalia kwenye kioo kila apatapo fursa, na kuwauliza wengine kila mara, “Je, unafikiri ngozi yangu imekuwa nyeupe au nyeusi hivi karibuni? Kwa nini inaonekana kama nimekuwa mweusi?” Watu hujibu, “Ni upuzi sana kwako, msimamizi, kuzungumzia mambo haya—kuwa mweupe au mweusi kunaathiri nini?” Anazungumzia mada hizi za upuuzi kila wakati, na hana hisia ya kufanya kazi yake. Kila anapopata nafasi, anajadili nguo, wanawake, wanaume, mapenzi, na aina gani ya wenzi ambao watu wangechagua, lakini hajadili kamwe ni masuala gani yaliyopo katika utekelezaji wa wajibu wao au jinsi ya kuyatatua. Je, si kuna tatizo hapa? Je, bado anaweza kufanya kazi? (Hapana, hawezi.) Mtazamo wake umebadilika, na masuala ya kutekeleza wajibu hayamo tena katika mawazo yake. Badala yake, akili zake zimejaa siku nzima mawazo ya jinsi ya kujihusisha katika mahusiano ya kimapenzi, jinsi ya kuvaa, na jinsi ya kuvutia jinsia tofauti. Kuna msemo miongoni mwa wasioamini: “kutumbukia katika mapenzi.” Je, hayo ni mapenzi? Hapana, ni shimo ndefu! Mara tu unapoingia, huwezi kutoka. Je, kuna watu kama hawa miongoni mwa wafanyakazi wanaotekeleza wajibu wao? (Ndiyo.) Ingawa nyumba ya Mungu haiingilii watu kutafuta wenzi wa kimapenzi, ikiwa watavuruga maisha ya kanisa na kuathiri kazi ya kanisa kwa kufanya hivyo, watu hao wanahitaji kuondolewa. Wapenzi hao wanapaswa kwenda na kuchumbiana peke yao na wasiathiri watu wengine. Ikiwa wewe ni mtu ambaye amejitolea kutumia maisha yake yote kujitumia kwa ajili ya Mungu, na umeazimia kutojihusisha katika mahusiano ya kimapenzi, basi zingatia kujitumia kwa ajili ya Mungu. Ikiwa umeingia katika uhusiano wa kimapenzi na huhisi tena kufanya kazi yako, basi hupaswi kutekeleza wajibu wa msimamizi, na nyumba ya Mungu itamchagua mtu mwingine achukue nafasi hiyo. Kazi ya nyumba ya Mungu haipaswi kucheleweshwa au kuathiriwa na uhusiano wako wa kimapenzi. Kazi lazima iendelee. Inawezaje kuendelea? Kwa kumchagua msimamizi mwingine ambaye hajihusishi kimapenzi, ambaye ana ujuzi mkubwa wa kitaalamu na anaweza kuimudu kazi, ili akabidhiwe kazi yako. Nyumba ya Mungu hufanya kazi kwa njia hii kila wakati, na kanuni hii inabaki bila kubadilika. Wasimamizi wengine husema, “Uhusiano wangu wa kimapenzi hauathiri kazi yangu; niache niendelee kusimamia.” Je, tunaweza kuamini kauli hii? (Hapana, hatuwezi.) Kwa nini tusiweze kuiamini? Kwa sababu ukweli wa mambo uko wazi kwa wote kuona! Mtu anapokuwa katika uhusiano wa kimapenzi, anachofikiria tu ni mwenzi wake wa kimapenzi, na moyo wake unashughulishwa na mambo haya, na hivyo mara nyingi yeye huhisi kusinzia wakati wa mikutano na hawezi kutekeleza wajibu wake. Kwa hiyo, jinsi nyumba ya Mungu inavyowashughulikia watu kama hawa inafaa na inalingana na kanuni. Nyumba ya Mungu haikuzuii wewe kuwa na uhusiano wa kimapenzi, wala haikunyang'anyi uhuru wako wa kuwa na uhusiano. Unaweza kuwa na uhusiano na mtu kwa kadiri ya kuridhika kwa moyo wako: huo ni uamuzi wako mwenyewe, mradi tu usijute, na usilie juu yake baadaye. Wasimamizi wengine wametimuliwa kwa sababu ya uhusiano wa kimapenzi. Watu wengine huuliza, “Je, mtu haruhusiwi kumwamini Mungu mara tu anapokuwa katika uhusiano wa kimapenzi?” Nyumba ya Mungu haijawahi kusema hivyo. Je, ni kweli kwamba nyumba ya Mungu inawakataa au kuwafukuza wale wote wanaojihusisha na uhusiano wa kimapenzi? (Hapana.) Ikiwa uko katika uhusiano wa kimapenzi, basi huwezi kuwa msimamizi au kiongozi au mfanyakazi, na ikiwa hujitolei katika kutekeleza wajibu wako, basi unapaswa kuondoka katika kanisa la wajibu wa wakati wote. Je, kuna mtu yeyote aliyesema kwamba huruhusiwi kumwamini Mungu tena, au kwamba utafukuzwa? Je, kuna mtu yeyote aliyetoa uamuzi akisema kwamba huwezi kuokolewa, au kwamba utalaaniwa? (Hapana.) Nyumba ya Mungu haijawahi kusema mambo kama hayo. Nyumba ya Mungu haiingilii chaguzi na uhuru wako wa kibinafsi hata kidogo; haikunyang'anyi uhuru wowote hata kidogo—inakupa uhuru. Hata hivyo, linapokuja suala la msimamizi wa aina hii, kanuni ya nyumba ya Mungu ya kumshughulikia ni kumtimua na kutafuta mtu anayefaa achukue nafasi yake. Ikiwa anafaa kuendelea kutekeleza wajibu, anaweza kubakizwa. Ikiwa sivyo, ataambiwa aende zake. Hakutakuwa na kupigwa au matusi au udhalilishaji wowote. Sio jambo la aibu; ni jambo la kawaida sana. Kwa hiyo wakati watu wengine wanaondolewa katika nafasi zao au kutumwa kwa makanisa ya kawaida kwa sababu ya uhusiano wao wa kimapenzi, je, hili linaaibisha? Linaweza kuonyesha tu kwamba wanakosa uaminifu katika kutekeleza wajibu wao, kwamba hawapendezwi na ukweli, na hawabebi mzigo wowote kwa ajili ya kuingia kwao katika uzima. Msimamizi wa aina hii hazingatii kazi yake inayofaa—anazingatia tu uhusiano wa kimapenzi, jambo ambalo huchelewesha kazi ya kanisa, na tayari limeathiri maendeleo ya kazi ya kanisa—je, si hili ni tatizo kubwa? (Ndiyo.) Kwa hiyo, msimamizi wa aina hii hafai kubakizwa na anapaswa kuondolewa katika nafasi yake. Wengine husema, “Je, si haraka sana kuwaondoa?” Ikiwa, tangu kuanza kwa uhusiano wao wa kimapenzi hadi wakati wa kuondolewa kwao, siku moja au mbili tu zimepita, hilo linaweza kuchukuliwa kuwa haraka. Lakini ikiwa miezi mitatu hadi mitano imepita, je, hilo bado lingechukuliwa kuwa haraka? (Hapana.) Hatua imechukuliwa polepole vya kutosha, kazi tayari imecheleweshwa sana—mbona wewe huna wasiwasi kuhusu hilo? Je, si hili ni tatizo? (Ndiyo, ni tatizo.)

Viongozi wa uwongo kamwe hawaulizi kuhusu wasimamizi ambao hawafanyi kazi halisi, au ambao hawashughulikii kazi yao inayofaa. Wanafikiri wanahitaji tu kumchagua msimamizi na hilo linatosha, na kwamba baadaye msimamizi huyo anaweza kushughulikia masuala yote ya kazi yeye mwenyewe. Kwa hiyo viongozi wa uwongo hufanya mikutano tu mara kwa mara, na hawasimamii kazi au kuuliza inavyoendelea, na kutenda kama mabosi wasiojishughulisha. Mtu akiripoti tatizo kuhusu msimamizi, kiongozi wa uwongo atasema, “Ni tatizo dogo tu, hakuna shida. Ninyi mnaweza kulishughulikia wenyewe. Msiniulize.” Mtu aliyeripoti suala hilo anasema, “Msimamizi huyo ni mlafi mvivu. Analenga tu chakula na burudani, na ni mvivu sana. Hataki kuteseka hata kidogo katika wajibu wake, na daima yeye huzembea kwa hila na kutoa visingizio ili kukwepa kazi yake na kukwepa majukumu yake. Hafai kuwa msimamizi.” Kiongozi wa uwongo atajibu, “Alikuwa mzuri sana alipochaguliwa kama msimamizi. Unachosema si kweli, au hata kama ni kweli, ni dhihirisho la muda tu.” Kiongozi wa uwongo hatajaribu kujua zaidi kuhusu hali ya msimamizi huyo, badala yake ataamua na kutoa maamuzi juu ya jambo hilo kulingana na maoni yake ya zamani kuhusu msimamizi huyo. Bila kujali ni nani anayeripoti matatizo kuhusu msimamizi, kiongozi wa uwongo atampuuza. Msimamizi hafanyi kazi halisi, na kazi ya kanisa inakaribia kusimama, lakini kiongozi wa uwongo hajali, ni kana kwamba hata hahusiki. Inachefua vya kutosha kwamba mtu anaporipoti masuala ya msimamizi, anajifanya haoni. Lakini ni nini kinachochukiza zaidi kuliko yote? Watu wanaporipoti masuala mazito sana kuhusu msimamizi kwake, hajaribu kuyatatua, na hata atatoa visingizio vya kila aina: “Ninamjua msimamizi huyu, anaamini katika Mungu kweli, hawezi kuwa na matatizo yoyote kamwe. Hata kama angekuwa na suala dogo, Mungu angemlinda na kumtia adabu. Akifanya makosa yoyote, hilo ni kati yake na Mungu—hatuhitaji kujishughulisha nalo.” Viongozi wa uwongo hufanya kazi kulingana na mawazo na fikira zao wenyewe kwa njia hii. Wanajifanya kuelewa ukweli na kuwa na imani, lakini wanavuruga tu kazi ya kanisa—kazi ya kanisa inaweza hata kusimama na bado watajifanya kutojua hili. Je, viongozi wa uwongo hawatendi kama warasimu sana? Hawana uwezo wa kufanya kazi halisi wao wenyewe, na wala hawako makini kuhusu kazi ya viongozi wa timu na wasimamizi—hawaifuatilii au kuuliza kuihusu. Mtazamo wao kuhusu watu unategemea tu maoni na mawazo yao wenyewe. Wanapomwona mtu akifanya vizuri kwa muda, wanafikiri kwamba mtu huyu atakuwa mwema milele, kwamba hatabadilika; hawamwamini mtu yeyote anayesema kuna tatizo na mtu huyu, na wanapuuza mtu anapowaonya kumhusu mtu huyo. Je, ninyi mnafikiri viongozi wa uwongo ni wajinga? Ni wajinga na wapumbavu. Ni nini kinachowafanya wawe wajinga? Wanamwamini mtu kiholela, wakiamini kwamba kwa sababu mtu huyu alipochaguliwa, aliapa, na kuweka nadhiri, na kuomba huku machozi yakimtiririka usoni, hilo linamaanisha kwamba ni mwenye kutegemewa, na hakutawahi kuwa na masuala yoyote naye kusimamia kazi. Viongozi wa uwongo hawana uelewa wa asili ya watu; hawajui hali halisi ya wanadamu wapotovu. Wanasema, “Mtu anawezaje kubadilika na kuwa mbaya wakati amechaguliwa kuwa msimamizi? Mtu anayeonekana kuwa makini sana na mwenye kutegemewa anawezaje kukwepa kazi yake? Hawezi, sivyo? Ana uadilifu mwingi.” Kwa sababu viongozi wa uwongo wameweka imani kubwa sana katika mawazo na hisia zao wenyewe, hatimaye hili huwafanya washindwe kutatua kwa wakati matatizo mengi yanayotokea katika kazi ya kanisa, na kuwazuia kumtimua msimamizi anayehusika mara moja na kubadilisha kupeanwa kwa wajibu wake. Wao ni viongozi halisi wa uwongo. Na tatizo hapa ni lipi hasa? Je, mtazamo wa viongozi wa uwongo kwa kazi yao una uhusiano wowote na kufanya mambo kwa kijuujuu tu? Kwa upande mmoja, wanaliona joka kuu jekundu likitekeleza ukamataji wa watu wateule wa Mungu kwa ukali sana, kwa hiyo ili kujiweka salama, wanapanga mtu asimamie kazi bila kufikiria, wakiamini kwamba hili litatatua tatizo, na kwamba hawahitaji kulizingatia tena. Wanafikiri nini mioyoni mwao? “Mazingira haya ni ya uhasama sana, ninapaswa kujificha kwa muda.” Huku ni kutamani starehe za mwili, sio? Kwa upande mwingine, viongozi wa uwongo wana udhaifu mkuu: Wao ni wepesi wa kuwaamini watu kulingana na mawazo yao wenyewe. Na hili linasababishwa na kutoelewa ukweli, sio? Neno la Mungu linafichuaje kiini cha wanadamu wapotovu? Kwa nini wawaamini watu wakati Mungu hawaamini? Viongozi wa uwongo ni wenye kiburi na wenye kujihesabia haki sana, sio? Wanachofikiria ni, “Siwezi kuwa nimekosea kumhusu mtu huyu, hakupaswi kuwa na matatizo yoyote na mtu huyu ambaye nimemwona kuwa anafaa; hakika yeye si mtu anayefurahia kula, kunywa na burudani, au anayependa starehe na kuchukia kazi ngumu. Yeye ni mtu mwenye kutegemewa kabisa na anayeaminika. Hatabadilika; kama akibadilika, hilo litamaanisha kwamba nilikosea kumhusu, sivyo?” Haya ni mantiki ya aina gani? Je, wewe ni aina fulani ya mtaalamu? Je, una macho yenye uwezo wa kupenya? Je, una ujuzi huo maalum? Unaweza kuishi na mtu kwa mwaka mmoja au miwili, lakini je, utaweza kuona yeye ni nani hasa bila mazingira yanayofaa ili kuweka kiini chake cha asili wazi kabisa? Asipofunuliwa na Mungu, unaweza kuishi naye bega kwa bega kwa miaka mitatu, au hata mitano, na bado uhangaike kuona ana kiini cha asili cha aina gani hasa. Na ni kweli kiasi gani zaidi wakati humwoni mara kwa mara, na huko naye mara kwa mara? Viongozi wa uwongo wanamwamini mtu kwa wepesi wa moyo kulingana na maoni ya muda au tathmini nzuri ya mtu mwingine kumhusu, na wanathubutu kumkabidhi kazi ya kanisa mtu kama huyo. Katika hili, je, si wao wanakuwa vipofu kupindukia? Je, hawatendi kiholela? Na wanapofanya kazi hivi, je, viongozi wa uwongo si wanakosa kuwajibika mno? Viongozi na wafanyakazi wa juu wanawauliza, “Je, umekagua kazi ya msimamizi huyo? Sifa na ubora wa tabia yake ukoje? Je, anajukumika katika kazi yake? Je, anaweza kubeba kazi hiyo?” Viongozi wa uwongo wanajibu, “Hakika anaweza! Alipochaguliwa, aliweka nadhiri na azimio. Bado nina kiapo chake kilichoandikwa. Anapaswa kuwa na uwezo wa kubeba kazi hiyo.” Unaonaje maneno ya viongozi wa uwongo? Wanaamini kwamba kwa kuwa mtu huyu aliweka nadhiri ili kuonyesha kujitolea kwake, hakika ataweza kutimiza hilo. Je, kauli hii ni ya kweli? Ni watu wangapi siku hizi wanaweza kutimiza nadhiri zao kweli? Kuna watu wangapi waaminifu ambao hutekeleza mambo kulingana na maazimio yao? Kwa sababu tu mtu anaweka nadhiri haimaanishi anaweza kuitimiza kweli. Tuseme umwulize, “Je, unaweza kuhakikisha kwamba msimamizi hatabadilika? Je, unaweza kuhakikisha uaminifu wake wa maisha? Mungu anapotaka kuwafunua watu lazima Aweke mazingira mbalimbali ili kuwajaribu. Unasema kwamba ni mwenye tegemewa kwa msingi gani? Je, umemchunguza?” Viongozi wa uwongo wanajibu, “Hakuna haja ya kufanya hivyo. Ndugu wote wameripoti kwamba ni mwenye kutegemewa.” Kauli hii pia si sahihi. Je, mtu ni mzuri kweli kwa sababu tu ndugu wanaripoti kwamba yuko hivyo? Je, ndugu wote wanamiliki ukweli? Je, wote wanaweza kung’amua mambo? Je, ndugu wote wanamfahamu mtu huyu? Kauli hii inachefua hata zaidi! Kwa kweli, mtu huyo amefunuliwa kwa muda mrefu sasa. Amepoteza kazi ya Roho Mtakatifu, na sifa zake za uduni za kupenda starehe na kuchukia kazi ngumu, kuwa mlafi na mvivu, na kutoshughulikia kazi yake ipasavyo, tayari zimefichuliwa. Mbali na viongozi wa uwongo, ambao bado hawajui kabisa, kila mtu amemng’amua kitambo—ni viongozi wa uwongo pekee ndio bado wanamwamini kiasi hiki. Viongozi hawa wa uwongo wana faida gani? Je, si wao ni nyangarika? Kuna hata baadhi ya visa ambapo Aliye juu huja kujua kuhusu dhihirisho mbalimbali za wasimamizi fulani kwa kwenda kwenye eneo la kazi ili kuchunguza na kuuliza kuwahusu, na bado viongozi bado wako gizani kabisa. Je, hili si tatizo? Viongozi hawa ni viongozi halisi wa uwongo. Hawafanyi kazi halisi, wao ni warasimu tu, na kama mabosi wasiojishughulisha, wanafanya kazi kidogo tu na kisha wanaishi kwa kutegemea hayo na kufikiria kwamba wana haki ya kujifurahisha, bila hata kujisumbua kunyoosha kidole kusaidia mambo yanapoharibika. Una haki gani ya kufurahia manufaa ya hadhi? Kwa kweli huna aibu! Viongozi wa uwongo wanapofanya kazi, hawakagui kazi yoyote kamwe, hawaulizi kuhusu maendeleo ya kazi, na hakika hawachunguzi hali za wasimamizi wa timu mbalimbali. Wao hupanga tu kazi na kupanga wasimamizi, na kisha wanafikiri kwamba wamemaliza, kwamba kazi yao imeisha na kukamilika, kabisa. Wanaamini, “Kuna mtu anayeshughulikia kazi hii, kwa hiyo si shughuli yangu tena. Ninaweza kujifurahisha.” Je, huku ni kufanya kazi? Bila shaka, mtu yeyote anayefanya kazi hivi ni kiongozi wa uwongo—kiongozi wa uwongo anayechelewesha kazi ya kanisa na kuwadhuru watu wateule wa Mungu.

Viongozi wa uwongo huwa hawaulizi au kufuatilia hali za kazi za wasimamizi wa timu mbalimbali. Pia hawaulizi, hawafuatilii, au kuwa na ufahamu juu ya kuingia katika uzima kwa wasimamizi wa timu tofauti na wafanyakazi wanaowajibika kwa kazi mbalimbali muhimu, pamoja na mitazamo yao kwa kazi ya kanisa na wajibu wao, na kwa imani katika Mungu, ukweli, na Mungu Mwenyewe. Hawajui kama watu hawa wamepitia mabadiliko au ukuaji wowote, wala hawajui kuhusu masuala mbalimbali yanayoweza kuwepo katika kazi yao; hasa, hawajui kuhusu athari za makosa na mikengeuko inayotokea katika hatua mbalimbali za kazi juu ya kazi ya kanisa na kuingia katika uzima kwa watu wateule wa Mungu, pamoja na kama makosa na mikengeuko hii imewahi kurekebishwa. Hawajui kabisa mambo haya yote. Ikiwa hawajui chochote kuhusu hali hizi za kina, wanakuwa baridi matatizo yanapotokea. Hata hivyo, viongozi wa uwongo hawajishughulishi na masuala haya ya utondoti hata kidogo wanapofanya kazi yao. Wanaamini kwamba baada ya kupanga wasimamizi wa timu mbalimbali na kugawa kazi, kazi yao imeisha—inahesabika kuwa wamefanya kazi hiyo vizuri, na matatizo mengine yakitokea hayawahusu. Kwa sababu viongozi wa uwongo wanashindwa kusimamia, kuelekeza, na kufuatilia wasimamizi wa timu mbalimbali, na hawatimizi majukumu yao katika maeneo haya, hili husababisha kazi ya kanisa kuvurugika kabisa. Huku ni kutowajibika kwa viongozi na wafanyakazi katika majukumu yao. Mungu anaweza kuchunguza vina vya moyo wa mwanadamu; huu ni uwezo ambao wanadamu wanakosa. Kwa hiyo, wanapofanya kazi, watu wanahitaji kuwa wenye bidii na makini zaidi, wakienda mara kwa mara kwenye eneo la kazi ili kufuatilia, kusimamia, na kuelekeza kazi ili kuhakikisha maendeleo ya kawaida ya kazi ya kanisa. Ni wazi kwamba, viongozi wa uwongo hawawajibiki kabisa katika kazi yao, na kamwe hawasimamii, hawafuatilii, au kuelekeza kazi mbalimbali. Matokeo yake, baadhi ya wasimamizi hawajui jinsi ya kutatua masuala mbalimbali yanayotokea katika kazi, na hubakia katika majukumu yao kama wasimamizi licha ya kutokuwa na uwezo wa kutosha hata kidogo wa kufanya kazi hiyo. Hatimaye, kazi inacheleweshwa tena na tena na wanaivuruga kabisa. Haya ni matokeo ya viongozi wa uwongo kutouliza, kutosimamia, au kutofuatilia hali za wasimamizi, matokeo ambayo yanasababishwa kabisa na kutowajibika kwa viongozi wa uwongo. Kwa sababu viongozi wa uwongo hawakagui, hawafuatilii, au hawaulizi kuhusu kazi, na hawawezi kuelewa hali hiyo mara moja, wanabaki bila kujua mambo kama vile iwapo wasimamizi wanafanya kazi halisi, jinsi kazi inavyoendelea, na kama imeleta matokeo halisi. Wanapoulizwa wasimamizi wanashughulika na nini au wanashughulikia kazi gani mahususi, viongozi wa uwongo hujibu, “Sijui, lakini wanahudhuria kila mkutano, na kila ninapowasiliana nao kuhusu kazi, hawataji kamwe masuala au matatizo yoyote.” Viongozi wa uwongo wanaamini kwamba mradi tu wasimamizi hawajaacha kazi yao na wapo kila wanapowatafuta, hawana tatizo lolote hata kidogo. Hivi ndivyo viongozi wa uwongo wanavyofanya kazi. Je, hili si dhihirisho la “uwongo”? Je, huku si kushindwa kutimiza majukumu yao? Huku ni kutowajibika kwa kiasi kibubwa! Katika kazi yao, viongozi wa uwongo huzingatia tu kufanya mambo kwa kijuujuu, na hawatafuti matokeo halisi. Kwa juu juu, wao hufanya mikutano mara kwa mara, wakionekana kuwa na shughuli nyingi kuliko mtu wa kawaida. Hata hivyo, bado haijulikani ni matatizo gani ambayo wametatua hasa, ni kazi gani mahususi ambazo wameshughulikia kwa namna inayofaa, na ni matokeo gani ambayo wamefikia. Hakuna anayeweza kutoa jibu la wazi kuhusu mambo haya, ikiwa ni pamoja na viongozi wa uwongo wenyewe. Lakini jambo moja ni la hakika: Bila kujali watu wana matatizo gani kwenye eneo la kazi, viongozi hawa wa uwongo hawapatikani popote; hakuna aliyewahi kuwaona kwenye eneo la kazi wakitatua matatizo ya watu. Basi, viongozi wa uwongo wanafanya kazi gani siku nzima? Mikutano yao hutatua matatizo gani? Hakuna anayejua kwa hakika, na rundo la masuala yaliyolimbikizwa na ambayo hayajatatuliwa hugunduliwa tu hatimaye wakati kazi yao inapokaguliwa. Kwa juu juu, viongozi wa uwongo kwa kweli wanaonekana kuwa na shughuli nyingi sana—wao “wanashughulikia mambo yasiyohesabika”. Hata hivyo, mtu anapochunguza matokeo ya kazi yao, ni vurugu tupu; ni machafuko, hakuna kitu cha thamani ndani yake hata kidogo, na ni dhahiri kwamba viongozi hawa wa uwongo hawajafanya hata chembe ya kazi halisi. Licha ya wingi wa matatizo halisi ambayo wameyaacha bila kutatuliwa, viongozi wa uwongo wanaonekana kutokuwa na hisia ya dhamiri na kutohisi kujilaumu. Zaidi ya hayo, wameridhika sana na wao wenyewe na kufikiria kwamba wao ni wazuri sana; kwa kweli hawana busara. Watu kama hawa hawastahili kuwa viongozi au wafanyakazi katika kanisa.

Msimamizi wa aina ambayo tumeshiriki kumhusu hivi punde anajua taaluma yake na ana uwezo wa kazi, lakini habebi mzigo tu, na anajishughulisha na kula, kunywa, na burudani siku nzima bila kushughulikia kazi yake ipasavyo au kufanya kazi yoyote halisi. Viongozi wa uwongo hawawezi kubadilisha wajibu wa msimamizi wa aina hii mara moja au kumtimua, na hili huzuia na kusumbua kazi, na kuifanya isiendelee vizuri. Je, hili halisababishwi na viongozi wa uwongo? Ingawa viongozi wa uwongo hawawajibikii hili moja kwa moja, kuacha kwao kujumika, kushindwa kwao kutimiza jukumu lao kama waangalizi, kunawafanya wawajibike kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa hasara iliyosababishwa kwa kazi. Viongozi hawa wa uwongo hawatimizi wajibu wao kama waangalizi, hawawajibikii majukumu yao, na hatimaye kusababisha kazi ya kanisa kupata hasara. Kazi fulani hata hufikia hatua ya kusimama na kuachwa zikiwa zimesambaratika kwa sababu ya kutokuwepo kwa msimamizi anayefaa wa kuongoza, kufanya ukaguzi, na kusimamia na kuendeleza kazi mbele. Matumizi yasiyofaa ya wafanyakazi yatasababisha hasara za aina hii kwa kazi. Ingawa msimamizi wa aina hii ana ubora wa tabia kidogo na anaelewa taaluma hiyo kidogo, hashughulikii kazi yake inayofaa, mara nyingi hufuata njia yake mwenyewe, na hafuati njia sahihi. Hata kama viongozi wa uwongo watasikia kwamba mtu fulani ameripoti matatizo kuhusu msimamizi wa aina hii, hawayachunguzi au kuyashughulikia mara moja, na hatimaye hili hulemaza kazi ya kanisa. Je, hili halisababishwi na kutowajibika kwa viongozi wa uwongo? Hata wanajaribu kukwepa wajibu, wakidai kwamba hawakuelewa hali ya msimamizi, kwamba walikuwa wajinga na wasiojua, wakifikiri kwamba kusema hivi kutakuwa mwisho wa jambo hilo, kwamba hawatahitaji kuwajibika. Katika kazi yao, viongozi wa uwongo daima hutenda kwa njia ya kijuujuu tu. Hata watu wanaporipoti matatizo, hawaulizi wala hawayashughulikii, na mambo yanapoharibika, wanajaribu kukwepa wajibu. Hili ni dhihirisho moja la viongozi wa uwongo.

II. Jinsi Viongozi wa Uwongo Wanavyowatendea Wasimamizi Wenye Ubora Duni wa Tabia na Wasio na Uwezo wa Kufanya Kazi

Viongozi wa uwongo wanapokuwa wakifanya kazi, matatizo wanayokutana nayo hayakomei kwenye hali hii tu—kuna hali nyingine ambapo wasimamizi wana ubora duni wa tabia na hawana uwezo wa kazi na hawawezi kubeba kazi hiyo. Katika visa kama hivyo, viongozi wa uwongo pia hushindwa kuuliza na kushughulikia suala hilo mara moja. Kwa nini iko hivyo? Viongozi wa uwongo wanakosa uwezo wa kazi, wana ubora duni wa tabia, na hawana ufahamu wa kiroho. Hawajali kamwe kuhusu au kuchukua hatua ya kuuliza kuhusu ubora wa tabia wa wasimamizi wa timu mbalimbali, uwezo wao wa kubeba kazi, au hali za kazi yao. Hawawezi kung’amua wasimamizi ambao wana ubora duni wa tabia na hawawezi kubeba kazi yao, wala hawajui kuhusu mambo haya. Akilini mwao, mara tu mtu yeyote anapochukua nafasi ya msimamizi, mtu huyo atabaki katika nafasi yake kwa muda mrefu, isipokuwa akitenda maovu ya kila aina, achochee hasira ya wengi na aondolewe na ndugu, au isipokuwa mtu aripoti masuala yake kwa Aliye juu na Aliye juu amtimue mtu huyo moja kwa moja. Vinginevyo, viongozi wa uwongo hawatamtimua mtu huyo kamwe. Wanaamini kwamba kwa kuwa ndugu walisema mtu huyo alikuwa mzuri na kumchagua, mtu huyo lazima awe chaguo bora zaidi. Viongozi wa uwongo daima hutegemea mawazo na maoni ili kuamua kama mtu anaweza kufanya kazi na kama anafaa kutenda kama msimamizi. Kwa mfano, kulikuwa na msimamizi wa timu ya densi ambaye hakujua kucheza densi, na hakuelewa kanuni za kuchagua densi. Wakati akitunga densi, hakujua kama achague mtindo wa kisasa au wa kiasili. Kusema kweli kabisa, hakuwa na maarifa ya densi. Hata hivyo, kiongozi wa uwongo hakuweza kuona hili. Alimchagua mtu huyo kama msimamizi kwa sababu alikuwa na shauku na alikuwa tayari kujionyesha, akidhani kwamba alielewa kila kitu na kumwacha awaongoze ndugu. Baadaye, kiongozi wa uwongo hakufuatilia, hakuchunguza kazi yake, au kuona jinsi alivyokuwa akiwaongoza ndugu vizuri, kama alikuwa mtaalamu au mtu asiye na ujuzi, kama alichofundisha kilifaa, au kama kililingana na mahitaji ya nyumba ya Mungu. Hakuweza kung’amua mambo haya, na hakuenda kuuliza kuyahusu. Matokeo yake, wote walifanya kazi kwa muda mrefu bila kutoa matokeo yoyote, na hatimaye iligundulika kwamba msimamizi aliyechaguliwa na kiongozi wa uwongo hakuweza kucheza densi kabisa, na bado alikuwa akijifanya kuwa mtaalamu na kuwaelekeza wengine. Je, hili halikuchelewesha kazi? Lakini kiongozi wa uwongo hakuweza kubaini tatizo hili na bado aliamini kwamba alikuwa akifanya kazi nzuri. Katika akili za viongozi wa uwongo, bila kujali mtu ni nani, mradi tu ana ujasiri na anathubutu kusema, kutenda, na kuchukua kazi, hili linathibitisha kwamba ana ubora wa tabia na anaweza kuibeba, ilhali asipothubutu kufanya mambo hayo, inathibitisha kwamba ubora wake wa tabia hautoshi kuibeba kazi hiyo. Watu wengine ni wapumbavu au watu wa kukurupuka ambao wana ujasiri wa kutosha kufanya chochote. Watu hawa hawajui kama wana ubora wa tabia unaofaa au kama wanaweza kuibeba kazi hiyo lakini bado wanathubutu kuwa wasimamizi. Na inatukia kuwa baada ya kuchukua nafasi hiyo, hakuna kazi yoyote inayoendelea, na bila kujali wanafanya kazi gani, hawana mwelekeo wa wazi, au hatua, au mawazo sahihi. Mtu yeyote anaweza kutoa maoni yoyote na hawatajua kama ni sahihi au la. Mtu mmoja akisema wafanye mambo kwa njia fulani, wanasema ni sawa, huku mtu mwingine akisema wafanye mambo kwa njia nyingine, wanasema ni sawa pia. Na linapokuja suala la mbinu gani ya kuchukua hasa, wanamruhusu kila mtu atoe maoni yake, na yeyote anayepaza sauti zaidi ndiye maoni yake hutekelezwa. Watu wa aina hii hawana ubora wowote wa tabia, hawawezi kung’amua chochote, na wanavuruga tu kazi yao, lakini viongozi wa uwongo bado hawawezi kuwang’amua wasimamizi kama hawa. Watu wengine wanasema, “Msimamizi huyo ana ubora duni sana wa tabia; anahitaji kutimuliwa mara moja!” Lakini viongozi wa uwongo wanajibu, “Nimezungumza naye, na alisema yuko tayari kushirikiana. Tumpe nafasi nyingine.” Unaonaje kauli hii? Je, hili si jambo ambalo mpumbavu annaweza kusema? Kuna tatizo gani na kauli hii? (Si suala la iwapo yuko tayari kufanya wajibu wake au la; anakosa ubora wa tabia na hawezi tu kuibeba kazi hiyo hata kidogo.) Hiyo ni kweli, si suala la kama yuko tayari kuufanya; ni kuhusiana na yeye kuwa na ubora duni mno wa tabia na kutojua jinsi ya kuufanya—hiki ndicho kiini cha tatizo. Hiyo ndiyo sababu viongozi wao wanahitaji kuwa na akili na kuweza kuwatathmini watu, ili kuona kama wasimamizi hawa wana ubora wa tabia unaohitajika. Viongozi hawa wanahitaji kufanya tathmini ya kina kuwahusu kulingana na usemi na ushirika wao, kwa kuangalia kama kwa kawaida wanatenda kwa mpangilio sahihi na kwa njia na hatua za utaratibu, na kwa majibu kutoka kwa ndugu. Ikiwa ubora wao wa tabia ni duni sana na wanakosa uwezo wa kazi unaohitajika, kama wanavuruga kila kitu wanachofanya, na kama wao ni nyangarika, basi wasimamizi hawa wanahitaji kutimuliwa mara moja.

Kulikuwa na msimamizi fulani wa shamba aliyeivuruga kazi ya ukulima. Hakujua ni mazao gani anayopaswa kupanda katika kipande gani cha ardhi, au ni kipande gani cha ardhi kilichofaa kukuza mboga, na hakutafuta na kushiriki na kila mtu—hakujua jinsi ya kushiriki kuhusu mambo haya, kwa hiyo aliacha tu. Alipanda mazao jinsi alivyopenda, akitupa kanuni za nyumba ya Mungu nyuma ya mawazo yake. Matokeo yake, alitekeleza upandaji wa kila kipande cha ardhi ya shamba kwa njia ya vurugu, huku mazao yaliyopaswa kupandwa kwa kiasi kidogo yakipandwa kwa wingi, na mazao yaliyopaswa kupandwa kwa wingi yakipandwa kwa kiasi kidogo. Aliye juu alipompogoa, bado alikuwa kaidi, na alihisi kwamba hakukuwa na kosa lolote kwake kupanda mazao kwa njia hii. Niambieni, je, wasimamizi wa aina hii si wagumu sana? Hakujua jinsi ya kushughulikia mambo kulingana na kanuni zilizowekwa na nyumba ya Mungu, au kwamba alipaswa kuamua ni mashamba mangapi ya nafaka na mashamba mangapi ya mboga yaliyopaswa kupandwa kulingana na idadi ya watu wanaofanya wajibu wao katika kanisa la wajibu wa wakati wote. Badala yake, aliamua kupanda mazao fulani kwa wingi na mengine kwa uchache kulingana na mapendeleo yake mwenyewe, na aliamini kwamba kufanya hivi kulifaa kabisa. Hatimaye, alipanda mazao hayo kwa njia ya kuchanganyikiwa. Baadaye, miche ilichipuka. Baadhi yake ilikuwa imebadilika na kuwa ya manjano na kuhitaji mbolea, lakini hakujua ni kiasi gani cha kuweka au ni lini inapaswa kuwekwa. Baadhi ya mazao yalishambuliwa na wadudu, na hakujua kama anapaswa kupiga dawa za kuua wadudu au la. Baadhi ya watu walipendekeza kuzitumia, na wengine walipendekeza kutozitumia, naye alichanganyikiwa, na hakujua la kufanya kuhusu dawa hizo. Kwa njia hii, aliboronga tu hadi ulipofika wakati wa msimu wa mavuno. Pia hakujua msimu wa ukuaji wa kila zao ulichukua muda gani au ni lini kila zao lingekomaa. Matokeo yake, nafaka zilizovunwa mapema bado zilikuwa za kijani kibichi kiasi, huku zile zilizovunwa zikiwa zimechelewa zilianguka ardhini. Mwishowe, licha ya hayo yote, mazao yalivunwa, nafaka hatimaye ziliwekwa ghalani, na shughuli za kilimo za mwaka huo zilikuwa zimekamilika. Msimamizi wa shamba alifanyaje kazi yake? (Aliivuruga.) Kwa nini ilivurugika kiasi hicho? Tafuteni chanzo cha suala hili. (Ubora wake wa tabia ni duni mno.) Msimamizi huyu ana ubora duni mno wa tabia! Alipokabiliwa na mambo, hakuwa na upambanuzi sahihi, hakuweza kupata kanuni, na hakuwa na njia au mbinu ya kushughulikia mambo. Hili lilimfanya ashughulikie kazi rahisi kama kupanda mazao kwa njia ya vurugu ajabu, na kuivuruga sana kazi hii. Maonyesho makuu ya ubora duni wa tabia ni yapi? (Kukosa uamuzi sahihi na kutoweza kupata kanuni.) Je, maneno haya si muhimu? Je, mtayakumbuka? Mtu anapokabiliwa na mambo, kukosa upambanuzi sahihi na kutoweza kupata kanuni kunaashiria ubora duni mno wa tabia. Kadiri watu wengine walivyotoa mapendekezo na vidokezo vingi, ndivyo msimamizi huyu alivyozidi kuchanganyikiwa. Alifikiri ingekuwa vyema kama kungekuwa na pendekezo moja tu, kisha angeweza kulichukulia kama kanuni na kulitii, jambo ambalo lingefanya mambo kuwa rahisi sana na kumaanisha kwamba hakuhitaji kufikiri au kutumia uamuzi. Aliogopa watu wengi kutoa mapendekezo kwa sababu alipoyasikia, hakujua jinsi ya kuyashughulikia. Kwa kweli, watu wenye akili na ubora mzuri wa tabia hawaogopi watu wengine wakitoa mapendekezo. Wanafikiri kwamba uamuzi wao unakuwa sahihi zaidi na kiwango cha makosa kinapungua wakati watu wengi wanapotoa mapendekezo. Watu wasio na akili au ubora wa tabia wanaogopa maoni na mapendekezo mbalimbali kutoka kwa watu wengi; wanachanganyikiwa wanapokabiliwa na ushauri kutoka vyanzo vingi. Je, yule msimamizi wa shamba Niliyemtaja hivi punde hakuwa na ubora duni mno wa tabia—je, hakukosa sifa za kutosha kuibeba kazi hii? (Ndiyo.) Wengine wanatoa hoja kwamba, “Labda hajawahi kulima hapo awali. Wewe ulisisitiza afanye kazi ya ukulima—je, huko hakukuwa kama kumlazimisha samaki kuishi nchi kavu?” Je, kutokuwa na uzoefu wa awali wa ukulima kunamaanisha kwamba mtu hawezi kulima? Nani aliye na uwezo wa asili wa kulima? Je, inawezekana kwamba wakulima wanazaliwa na uwezo huu? (Hapana.) Je, kumewahi kuwa na wakulima wowote ambao, kwa kukosa uzoefu na kutojua jinsi ya kulima, hawakuvuna mavuno na hawakuwa na nafaka yoyote ya kula mara ya kwanza walipopanda mazao, na kusababisha mwaka wa njaa? Je, jambo la aina hii hutokea? (Hapana.) Kama ingekuwa hivyo kweli, lingekuwa janga la asili, si matokeo ya matendo ya wanadamu. Hali kama hizo ni adimu sana! Wakulima hujipatia riziki kwa kulima, na hata wale ambao wamelima kwa mwaka mmoja au miwili hujifunza kuifanya. Watu wenye ubora mzuri wa tabia wanaweza kuvuna zaidi kidogo kutokana na kulima shamba, huku wale wenye ubora duni wa tabia wanaweza kuwa na mavuno kidogo. Zaidi ya hayo, kukiwa na maendeleo ya sasa na wingi wa habari, ikiwa mtu ana ubora wa tabia, habari hizi zinatosha kutumika kama marejeleo ya kufanya uamuzi na maamuzi sahihi. Kadiri habari zinavyokuwa pana na sahihi, ndivyo uamuzi na maamuzi yao yanavyokuwa sahihi zaidi, na ndivyo wanavyofanya makosa machache zaidi. Hata hivyo, watu wenye ubora duni wa tabia ni kinyume chake; kadiri kunavyokuwa na habari nyingi, ndivyo wanavyozidi kuchanganyikiwa. Mwishowe, kila hatua inakuwa ya taabu na ngumu sana kwao. Ukulima ni kukimbizana na muda; haitafaa ukifanya mambo mapema sana au ukiwa umechelewa sana. Ukichelewa na kukosa wakati sahihi, mavuno ya mwisho yataathirika. Katika kipindi cha kufanya ukulima, msimamizi huyu alilemewa, alikimbizwa na kupita kwa muda, na alilazimishwa katika kila hatua. Hata ingawa bado alifaulu kupiga kila hatua, ilikuwa ngumu sana kwake, na mwishowe, ilimsababisha kuivuruga kazi hiyo. Watu kama hao wana ubora duni mno wa tabia!

Watu walio na ubora duni mno wa tabia hawawezi hata kufanya kazi moja, moja tu vizuri; bila kujali ni kazi gani wanayofanya, wanaivuruga kabisa. Ikiwa viongozi wa wasimamizi hawa wana ubora mzuri wa tabia na wanaweza kutimiza majukumu yao, wanapaswa kuweza kuona mambo haya. Wanapaswa kuwasaidia wasimamizi walio na ubora duni wa tabia kwa maelekezo, uwekaji wa viwango, na ukaguzi. Hata hivyo, viongozi wa uwongo hushindwa kufanya hivi; pia hawawezi kufanya mambo ambayo wasimamizi hawawezi kufanya, na wasimamizi wanapoiona kazi yao kuwa ngumu au wanapohisi kutokuwa na uhakika na kusita katika kazi yao, viongozi wa uwongo husitasita pamoja nao. Hata hawajui jinsi wasimamizi wanavyoendelea katika kazi yao, wamefikia kiwango gani na kazi hiyo, ni changamoto gani ambazo zimeibuka, au wana mkanganyiko gani. Mtu fulani alipomwuliza kiongozi huyo kuhusu ukulima, alisema, "Mimi ni kiongozi, mimi sisimamii ukulima." Akajibu, "Wewe ni kiongozi, kwa hivyo kuna tatizo gani kukuuliza kuhusu ukulima? Kazi hii iko ndani ya upeo wa majukumu yako." Akasema, "Acha nikuulizie kuhusu hilo." Baada ya kuuliza, akajibu, "Kwa sasa tunapanda viazi." Akauliza, "Mnapanda viazi vingapi?" Akajibu, "Sikuuliza hilo, acha niende nikuangalilie." Baada ya kuuliza tena, akajibu, "Tulipanda ekari mbili." Akauliza: "Mlipanda aina gani? Je, shamba hilo linafaa kwa kupanda viazi? Je, mlitia mbolea mlipovipanda? Mbegu za viazi zilipandwa kwa kina gani?" Hakujua lolote kati ya haya. Hujui mambo haya, lakini huulizii kuyahusu wala hutafuti mtu wa kumwuliza kuyahusu—je, si hili linachelewesha mambo? Je, wewe ni kiongozi kweli? Unafanya kazi gani kama kiongozi? Ikiwa huwezi hata kuwaongoza watu kufanya kazi hii ndogo ya nje, kuna faida gani ya wewe kuwa kiongozi? Ingawa ubora wa tabia wa msimamizi ulikuwa duni namna hii, kiongozi huyu wa uwongo alishindwa kugundua hilo, na alipoulizwa ubora wa tabia wa msimamizi ulikuwaje, mimea ilikuwa ikiendeleaje, na iwapo kutakuwa na mavuno hakika, aliamini: "Si lazima wewe uulize kuhusu mambo haya; ukulima ni kazi rahisi sana! Tayari tumepanda mimea shambani, sivyo? Inawezekanaje kusiwe na mavuno?" Hakuzingatia chochote, hakuulizia kuhusu chochote, na hakuwa na akili hata kidogo. Huyu alikuwa kiongozi wa aina gani? (Kiongozi wa uwongo.) Kila alipokabiliwa na jambo lolote, msimamizi alikuwa amechanganyikiwa kabisa kama kuku aliyekatwa kichwa. Hakujua amwulize nani, au jinsi ya kupata habari, au achague upande upi wakati vyanzo tofauti vya habari vilipotoa mawazo mengi tofauti. Kiongozi huyu hakuchunguza hali hizi. Alifikiri kwamba kazi ilikuwa imekabidhiwa kwa mtu huyu, na kwa hivyo hakujishughulisha nayo hata kidogo. Je, mnafikiri kwamba msimamizi kuwa na ubora duni wa tabia kama huo kungekuwa na athari kwa matokeo ya kazi? (Ndiyo.) Basi, je, kiongozi alipaswa kufanya nini ili kutatua tatizo hili? Kupitia kuchunguza hili na kuulizia kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kupitia matukio yaliyofanyika karibu na yeye, na kupitia upandaji wa mimea ya msimu huo, alipaswa kugundua kwamba msimamizi alikuwa mwenye ubora duni mno wa tabia, kwamba hakuweza kufanya chochote. Hakuweza kupata maarifa yoyote kutokana na uzoefu wake hata baada ya miaka mingi ya ukulima—kufikia wakati huo hakuwa hata na uhakika kuhusu jinsi ya kupanda mimea—ilipasa kuwa wazi kwake kwamba alikuwa na ubora duni wa tabia na hakufaa kwa kazi hiyo, na mtu kama huyo alipaswa kuvuliwa wadhifa! Alipasa kuulizia kuhusu ni nani aliyefaa kuwa msimamizi, ni nani angeweza kujitwika kazi hii na kuifanya vizuri, na hivyo kuhakikisha kwamba kazi ya nyumba ya Mungu haikudhurika. Je, kiongozi huyo wa uwongo alikuwa na mtazamo huu? Je, angeweza kuona masuala haya? (La.) Yeye hakuwa na ufahamu wa kiroho na alikuwa kipofu; alikuwa kipofu kabisa. Huu ni udhihirisho wa viongozi wa uwongo. Linapokuja suala la watu walio na ubora duni wa tabia, hawajui jinsi ya kuwaelekeza katika kazi yao, hawajui jinsi ya kuwasaidia kwa kufanya ukaguzi au jinsi ya kutatua matatizo yao mara moja, na hakika hawajui kwamba mtu aliye na ubora duni wa tabia hawezi kujitwika kazi hiyo na anapaswa kubadilishwa haraka na mtu anayefaa. Viongozi wa uwongo hawafanyi kazi yoyote kati ya hizi; hawafai kwa kazi hiyo, na hawawezi kuona lolote kati ya haya. Je, si hawa ni vipofu? Watu wengine husema, "Pengine wana shughuli nyingi na kazi zingine. Kwa nini Unaendelea kuwataka washughulikie kazi hizi ndogondogo, zisizo na maana?" Hizi ni kazi ambazo viongozi lazima wafanye, zinawezaje kuchukuliwa kuwa ndogondogo? Mambo haya yako ndani ya upeo wa majukumu ya viongozi—je, ingekuwa sawa ikiwa wangeyapuuza? Ikiwa wangefanya hivyo, huko kungekuwa kutelekeza majukumu. Matatizo na shida katika kazi yao huibuka kila siku mbele ya macho ya viongozi, na watu huyaibua kila siku. Hata hivyo, viongozi wa uwongo hawana ufahamu wa kiroho. Hawawezi kuona, kuhisi, wala kung'amua kwamba haya ni matatizo, kwa hivyo, bila shaka, hawawezi kuyatatua. Kiongozi huyo wa uwongo hakuweza kugundua kwamba ubora wa tabia wa msimamizi ulikuwa duni mno. Pia hakuweza kutambua matatizo mbalimbali yaliyoibuka katika kazi yake. Msimamizi huyu hakuweza kushughulikia masuala na jambo wakati lilipotokea, alitenda kwa njia ya vurugu kama siafu kwenye sufuria moto, akikosa kanuni, na akivuruga kazi, na kiongozi huyo wa uwongo hakuweza kuona wala kugundua lolote kati ya haya. Kuna kanuni moja ya jinsi viongozi wa uwongo wanavyofanya kazi yao: Mradi tu wamempangia mtu kuwajibikia kila kazi, wanaichukulia kuwa imekamilika, na bila kujali iwapo ubora wa tabia wa msimamizi ni mzuri au mbaya, iwapo anaweza kufanya kazi vizuri, au ni matatizo mangapi yanaibuka katika kazi, wanahisi kwamba haiwahusu. Je, kiongozi kama huyo bado anaweza kufanya kazi? Je, anaelewa jinsi ya kufanya kazi? (La.) Ikiwa huelewi jinsi ya kufanya kazi, basi kwa nini wewe unatenda kama kiongozi? Ikiwa unatumikia kama kiongozi licha ya hili, basi wewe ni kiongozi wa uwongo. Viongozi wa uwongo hawawezi kuona wala kugundua udhihirisho mbalimbali wa watu walio na ubora duni wa tabia au matatizo mbalimbali yanayoibuka wanapotekeleza wajibu wao. Mioyo yao imekufa ganzi kabisa. Je, si wao wamekosa ufahamu wa kiroho? Huenda wengine waseme, "Wao si vipofu. Wewe huwakashifu na kuwasingizia kila mara." Matatizo ya msimamizi huyu wa ukulima yalikuwa makubwa mno; kiongozi huyo wa uwongo aliishi pamoja na yeye kila siku, na angeweza kusikia na kuona kila kitu kilichofanyika. Basi iliwezekanaje ashindwe kugundua au kutambua kwamba haya yalikuwa matatizo? Kwa nini hakushughulikia au kutatua matatizo haya? Je, si yeye amekosa ufahamu wa kiroho? Je, tatizo hili lilikuwa kubwa? (Ndiyo, lilikuwa kubwa.) Huu ni udhihirisho mwingine wa viongozi wa uwongo—kukosa ufahamu wa kiroho.

Unapompangia kazi mtu aliye na ubora duni wa tabia, unaweza kutambua kutokana na jinsi anavyozungumza kwa kawaida, mtazamo na maoni yake anapojadili kazi, na jinsi anavyoshughulikia kazi, kwamba ubora wake wa tabia ni duni mno, kwamba kufikiri kwake kumevurugika, na kwamba anashughulikia kila kitu kwa upofu na na namna ya kutojali kiasi, na hana malengo yoyote. Unaweza amua kwamba mtu huyu ana ubora duni mno wa tabia kwa kuangalia tu jinsi anavyofanya mambo, kwa hivyo, je, unahitaji hata kumchunguza kwa muda mrefu hivyo? La, huhitaji kufanya hivyo. Hata hivyo, viongozi wa uwongo wana tatizo la kufisha; yaani, wao huamini kwamba kwa kuwa mtu ameendelea kufanya kazi kwa muda huu wote bila kuacha, na hawajasikia mtu yeyote akimripoti kwa kufanya jambo baya, au kwa kusababisha vurugu au usumbufu, au kwa kuwa hasi au mvivu, inamaanisha kwamba mtu huyu bado anaweza kufanya kazi. Hawajui jinsi ya kupima ubora wa tabia wa mtu wala uwezo wake wa kufanya kazi nzuri kulingana na usemi wake, mtazamo wake na maoni yake kuhusu mambo, au jinsi anavyofanya mambo. Hawana ufahamu huu; wamekufa ganzi na hawana utambuzi wowote kuhusu jambo hili. Wao wana mtazamo mmoja: Mradi tu mtu hakai tu bila kufanya chochote, kila kitu kiko sawa na kazi inaweza kuendelea. Je, ninyi mnafikiri kiongozi aliye na mtazamo wa aina hii anaweza kufanya kazi nzuri? Je, anafaa kwa kazi hiyo? (La.) Kumruhusu mtu kama huyo awe kiongozi kunavuruga kazi, sivyo? Mtu anapojiingiza katika kula, kunywa, na burudani, na anautelekeza wajibu wake, viongozi wa uwongo hawajishughulishi kuchunguza wala kushughulikia hili, na hawawezi kuona kama ubora wa tabia au hulka ya mtu ni nzuri au mbaya, haijalishi wamekuwa wakihusiana na yeye kwa muda gani. Je, viongozi hawa wana uwezo wa kazi wa kiongozi? (La.) Hawa ni viongozi wa uwongo. Viongozi wa uwongo hawawezi kutambua kama mtu ana ubora mzuri wa tabia au la, na hawawezi kufanya kazi hizi mahususi. Wao hufikiri hii si sehemu ya kazi yao. Je, huku si kutelekeza majukumu? Ninyi mnaonaje, je, mtu aliye na ubora duni wa tabia anaweza kujitwika kazi, au mtu aliye na ubora kiasi wa tabia? (Mtu aliye na ubora kiasi wa tabia.) Kwa hivyo, kutathmini ubora wa tabia wa mtu na uwezo wake kwa kazi hiyo ni suala ambalo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kujali na kulifahamu, na pia ni kazi ambayo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kutekeleza. Lakini viongozi wa uwongo hawaelewi kwamba hii ni sehemu ya kazi yao, hawana ufahamu huu, na hawawezi kutimiza sehemu hii ya majukumu yao. Hapa ndipo viongozi wa uwongo wanapoyatelekeza majukumu yao, na pia ni udhihirisho wa viongozi wa uwongo kutofaa kwa kazi hiyo. Hii ni aina ya pili ya hali: wasimamizi kuwa na ubora duni wa tabia, kukosa uwezo wa kazi, na kutoweza kujitwika kazi yao, ambalo ni suala linalohusu ubora wao wa tabia. Katika hali hii, viongozi wa uwongo vivyo hivyo hushindwa kutekeleza jukumu la kiongozi na hawawezi kuwavua wadhifa mara moja wasimamizi walio na ubora duni wa tabia.

III. Jinsi Viongozi wa Uwongo Wanavyowatendea Wasimamizi Wanaowatesa Wengine na Kuvuruga Kazi ya Kanisa

Aina ya tatu ya hali inahusisha wasimamizi wanaowatesa na kuwabana wengine, wakivuruga kazi ya kanisa. Hali ya kwanza tuliyozungumzia hapo awali ilikuwa pale ambapo baadhi ya wasimamizi, licha ya kuwa na ubora mzuri kiasi wa tabia na kuweza kujitwika kazi yao, hawaichukulii kazi kwa uzito, na wanatenda tu kwa kijuujuu, huku viongozi wa uwongo wakiwa hawajui hili na hawawavui wadhifa mara moja. Hali ya pili inahusisha baadhi ya wasimamizi kuwa na ubora duni wa tabia na kutoweza kujitwika kazi, lakini viongozi wa uwongo wanashindwa kutambua hili au kuwabadilisha mara moja. Hali hii ya tatu inahusu wasimamizi ambao, bila kujali kama ubora wao wa tabia ni mzuri au mbaya, hawashughulikii kazi yao inayofaa, na wanawatesa na kuwabana wengine tu, wakivuruga kazi ya kanisa. Tangu wakati wanapochaguliwa kama wasimamizi, hawajaribu kujifunza au kuichunguza nyanja yao, wala hawatafuti kanuni za ukweli, na hakika hawawaelekezi wengine kufanya wajibu wao ipasavyo. Badala yake, kila nafasi wanayopata, wanamwonea mtu fulani, na kumdhihaki na kumdharau mtu mwingine; mradi tu wana fursa, wao wanajionyesha, na na bila kujali kile wanachokifanya, hawafanyi mambo kwa namna halisi. Siku moja wanawaambia watu wafanye mambo kwa njia moja, na siku inayofuata wanawaambia wafanye mambo kwa njia nyingine; wanabuni tu mbinu mpya, wakitaka kujitokeza daima. Hili lote linawaweka watu katika hali ya wasiwasi. Kila wanapozungumza, watu wengine wanahisi mioyo yao ikitetemeka. Wanapokuwa wamemtiisha kila mmoja, na kumfanya kila mmoja awaogope na awatii, watahisi furaha tele. Bila kujali kama wao ni viongozi wa uwongo au wapinga Kristo, na bila kujali kama wako madarakani au la, watu wa aina hii huharibu utulivu wa kanisa. Si tu kwamba hawawezi kufanya kazi halisi au kutekeleza wajibu wao kwa kawaida, pia wanachochea mafarakano na kusababisha mapigano kati ya watu, wakivuruga maisha ya kanisa. Si tu kwamba hawawezi kuwasaidia wengine kuelewa ukweli, pia mara nyingi wanawahukumu na kuwashutumu watu, na kuwafanya watu wawatii katika kila kitu, wakiwabana kiasi kwamba hawajui jinsi ya kutenda ipasavyo. Hasa kuhusu jinsi wanavyoishi, watu hawawezi kulala mapema kidogo au wakiwa wamechelewa kulala kidogo. Chochote wanachofanya, lazima waangalie sura za watu hawa, jambo linalofanya maisha yachoshe sana. Ikiwa watu kama hawa watakuwa wasimamizi, kila mtu mwingine atakuwa na wakati mgumu. Ukizungumza nao kwa uaminifu na ufichue masuala yao, watasema kwamba unawalenga na kuwafichua kwa makusudi. Usipozungumza nao kuhusu matatizo yao, watasema kwamba unawadharau. Ukiwa makini na mwenye kuwajibika kuhusu kazi na uwape ushauri, watakuwa wakaidi, na watasema kwamba unawashambulia na kukuita mwenye kiburi. Kwa vyovyote vile, haijalishi kile unachofanya, watakiona kuwa kisichopendeza. Siku zote wanafikiria kuhusu kuwatesa watu, na wanawabana watu kiasi kwamba wanafungwa mikono na miguu na kuhisi kwamba hakuna wanachofanya kilicho sawa. Wasimamizi kama hao wanavuruga kazi ya kanisa.

Viongozi wa uwongo ni hodari katika kazi ya kijuujuu, lakini kamwe hawafanyi kazi halisi. Hawaendi kukagua, kusimamia, wala kuelekeza kazi mbalimbali za kitaaluma, au kujua kinachoendelea katika timu tofauti kwa wakati unaofaa, wakikagua jinsi kazi inavyoendelea, kuna matatizo gani, kama wasimamizi wa timu wana uwezo katika kazi yao, na jinsi akina ndugu wanavyoripoti au kuwatathmini wasimamizi. Hawachunguzi ili kuona kama kuna mtu yeyote anayebanwa na viongozi wa timu au wasimamizi, iwapo mapendekezo sahihi ambayo watu hutoa yanakubalika, kama mtu yeyote aliye na talanta au anayefuatilia ukweli anakandamizwa au kutengwa, kama watu wowote wasio na hila wanaonewa, kama watu wanaowafichua na kuwaripoti viongozi wa uwongo wanashambuliwa, wanalipizwa kisasi, wanaondolewa, au wanafukuzwa, kama viongozi wa timu au wasimamizi ni watu waovu, na kama kuna mtu yeyote anayeteswa. Viongozi wa uwongo wasipofanya kazi yoyote kati ya hizi mahususi, wanapaswa kuvuliwa wadhifa. Tuseme, kwa mfano, mtu fulani anaripoti kwa kiongozi wa uwongo kwamba kuna msimamizi ambaye mara nyingi huwabana na kuwakandamiza watu. Msimamizi amefanya mambo fulani vibaya lakini hawaruhusu akina ndugu watoe mapendekezo yoyote, na hata anatafuta visingizio vya kujitetea na kujilinda, bila kukubali makosa yake kamwe. Je, msimamizi kama huyo hapaswi kuvuliwa wadhifa mara moja? Haya ni matatizo ambayo viongozi wanapaswa kutatua kwa wakati unaofaa. Baadhi ya viongozi wa uwongo hawaruhusu wasimamizi waliowateua wafichuliwe, haijalishi ni masuala gani yameibuka katika kazi yao, na hakika hawawaruhusu waripotiwe kwa wale walio juu—hata wao huwaambia watu wajifunze kutii. Mtu fulani akifichua masuala ya msimamizi, viongozi hawa wa uwongo hujaribu kumkinga au kuficha ukweli halisi, wakisema, "Hili ni tatizo katika kuingia katika uzima kwa msimamizi. Ni kawaida kwake kuwa na tabia ya kiburi—kila mtu aliye na ubora kiasi wa tabia ni mwenye kiburi. Si jambo kubwa, ninahitaji tu kufanya ushirika naye kidogo." Kupitia ushirika huo, msimamizi anaonyesha msimamo wake, akisema, "Ninakubali mimi ni mwenye kiburi. Ninakubali kuna nyakati ambapo ninajali ubatili, fahari, na hadhi yangu mwenyewe, na sikubali mapendekezo ya watu wengine. Lakini watu wengine si hodari katika taaluma hii, mara nyingi wao huleta mapendekezo yasiyo na thamani, kwa hivyo kuna sababu kwa nini siwasikilizi." Viongozi wa uwongo hawajaribu kuelewa hali hiyo kikamilifu, hawaangalii matokeo ya kazi ya msimamizi, sembuse namna ubinadamu, tabia, na ufuatiliaji wake vilivyo. Wanachofanya tu ni kupunguza uzito wa mambo, wakisema, "Hili liliripotiwa kwangu kwa hivyo ninakufuatilia. Ninakupa fursa nyingine." Baada ya mazungumzo yao, msimamizi anasema kwamba yuko tayari kutubu, lakini kuhusu kama kwa kweli anatubu baadaye, au anasema uwongo na kudanganya tu, viongozi wa uwongo hawasikizi hili. Mtu fulani akiibua maswali kuhusu jambo hili, viongozi wa uwongo wanasema, "Nimeshazungumza naye na hata nimefanya ushirika juu ya vifungu vingi vya maneno ya Mungu na yeye. Yuko tayari kutubu, na tatizo limeshatatuliwa." Mtu huyo anapouliza, "Ubinadamu wa msimamizi huyo ukoje? Je, yeye ni mtu anayekubali ukweli? Umempa nafasi, lakini, je, ataweza kutubu na kubadilika kweli?" Viongozi wa uwongo, wakiwa hawawezi kung'amua hili, hujibu, "Bado ninamchunguza." Mtu huyo anajibu: "Umekuwa ukimchunguza kwa muda gani? Umefikia hitimisho lolote?" Viongozi wa uwongo wanasema: "Imekuwa zaidi ya miezi sita, na bado sijafikia hitimisho lolote." Ikiwa hawajapata matokeo yoyote baada ya zaidi ya miezi sita ya uchunguzi, huo ni ufanisi gani wa kazi? Viongozi wa uwongo huamini kwamba kuwa na mazungumzo mara moja na msimamizi ni jambo la kufaa na linatatua suala hilo. Je, wazo hili ni halali? Wanafikiri kwamba punde tu wanapomaliza kuzungumza na mtu, mtu huyo ataweza kubadilika, na mtu akitekeleza azimio lake la kutofanya hivyo tena, wanamwamini kabisa bila kufanya uchunguzi wowote zaidi au kuiangalia hali hiyo tena. Ikiwa hakuna anayefuatilia jambo hilo, huenda hata wasijishughulishe kuchunguza au kufuatilia kazi kwa nusu mwaka. Viongozi wa uwongo wanaendelea kutojua hata wakati msimamizi huyo anapovuruga kazi. Hawawezi kutambua jinsi msimamizi anavyowahadaa na kuwachezea. Kinachochukiza hata zaidi ni kwamba mtu anaporipoti matatizo ya msimamizi, viongozi wa uwongo wanayapuuza na hawachunguzi kwa kweli kama matatizo hayo yapo au kama matatizo wanayoripoti ni ya kweli. Hawazingatii masuala haya—kwa kweli wanajiamini kupita kiasi! Bila kujali ni hali gani zinaibuka katika kazi ya kanisa, viongozi wa uwongo hawafanyi haraka kuzishughulikia; wanafikiri kwamba haziwahusu kwa vyovyote vile. Mwitikio wa viongozi wa uwongo kwa matatizo haya ni goigoi mno, wanachukua hatua na kusonga polepole sana, wanaendelea kukwepa kusema ukweli wote, na kuendelea kuwapa watu nafasi nyingine ya kutubu, kana kwamba nafasi wanazowapa watu ni za thamani na muhimu sana, kana kwamba zinaweza kubadilisha majaliwa yao. Viongozi wa uwongo hawajui jinsi ya kuona kiini cha asili cha mtu kupitia kile kinachodhihirishwa ndani yake, au kuamua ni njia gani ambayo mtu anaitembea kulingana na kiini chake cha asili, au kuona kama mtu anafaa kuwa msimamizi au kufanya kazi ya uongozi kulingana na njia anayoitembea. Hawawezi kuona mambo kwa njia hiyo. Viongozi wa uwongo wana uwezo wa kufanya mambo mawili tu katika kazi yao: kwanza, kuwavuta watu katika upigaji gumzi na kufanya mambo kwa kijuujuu tu; pili, kuwapa watu fursa, kuwafurahisha wengine, na kutomkosea mtu yeyote. Je, wanafanya kazi halisi? Bila shaka hawafanyi kazi halisi. Lakini viongozi wa uwongo wanaamini kwamba kumvuta mtu katika kupiga gumzo ni kazi halisi. Wanachukulia mazungumzo haya kuwa ya thamani sana na muhimu, na kuona maneno matupu na mafundisho wanayoropoka kuwa muhimu sana. Wanafikiri kwamba wametatua matatizo makubwa kupitia mazungumzo haya na kwamba wamefanya kazi halisi. Hawajui kwa nini Mungu anahukumu na anaadibu, kupogoa, au kuwajaribu na kuwasafisha watu. Hawajui kwamba ni maneno ya Mungu na ukweli pekee ndivyo vinavyoweza kutatua tabia potovu za mwanadamu. Wanarahisisha mno kazi ya Mungu na wokovu wa Mungu kwa binadamu! Wanaamini kwamba kuzungumza maneno na mafundisho machache ni mbadala wa kazi ya Mungu, kwamba kunaweza kutatua tatizo la upotovu wa mwanadamu. Je, huu si upumbavu na ujinga wa viongozi wa uwongo? Viongozi wa uwongo hawana hata chembe ya uhalisi wa ukweli, kwa hivyo kwa nini wanajiamini sana? Je, kuropoka mafundisho machache kutawafanya watu wajijue? Je, kutawawezesha wavue tabia zao potovu? Viongozi hawa wa uwongo wanawezaje kuwa wajinga na wasio na ufahamu kiasi hiki? Je, kutatua matendo yenye makosa na mwenendo mpotovu wa mtu ni rahisi hivyo kweli? Je, suala la tabia potovu za mwanadamu ni rahisi sana kutatua? Viongozi wa uwongo ni wapumbavu na wa juujuu sana! Mungu hatumii mbinu moja tu kutatua suala la upotovu wa mwanadamu. Yeye hutumia mbinu nyingi na huweka mazingira tofauti ili kuwafunua, kuwatakasa, na kuwakamilisha watu. Viongozi wa uwongo, kinyume chake, wanafanya kazi kwa njia isiyobadilika na ya kijuujuu sana: Wanawavuta watu kwa ajili ya kupiga gumzo, wanafanya kazi kidogo ya kuwashauri watu kuhusu jinsi wanavyofikiri, wanawahimiza watu kidogo, na wanaamini kwamba huku ni kufanya kazi halisi. Haya ni mambo ya kijuujuu, sivyo? Na ni suala gani ambalo limefichwa nyuma ya hali hii ya kijuujuu? Je, si ukosefu wa ufahamu? Viongozi wa uwongo hawana ufahamu kabisa, na pia wao huwatazama watu na mambo kwa njia isiyo na ufahamu kabisa. Hakuna kitu kigumu zaidi kutatua kuliko tabia potovu za watu—chui hawezi kubadili madoa yake. Viongozi wa uwongo hawawezi kung'amua tatizo hili hata kidogo. Kwa hivyo, linapokuja suala la aina ya wasimamizi kanisani ambao daima wanasababisha usumbufu, ambao daima wanawabana na kuwatesa watu, viongozi wa uwongo hawafanyi chochote isipokuwa kuzungumza nao, na kuwapogoa kwa maneno machache, basi. Hawabadilishi wajibu wao mara moja au kuwavua wadhifa. Mbinu hii ya viongozi wa uwongo husababisha madhara makubwa kwa kazi ya kanisa, na mara nyingi husababisha kazi ya kanisa kuzuiwa, kucheleweshwa, kuharibiwa, na kuzuiwa kuendelea kwa kawaida, vizuri, na kwa ufanisi kwa sababu ya usumbufu wa baadhi ya watu waovu—ambalo lote ni tokeo la kudhuru la viongozi wa uwongo kutenda kulingana na hisia zao, kukiuka kanuni za ukweli, na kuwatumia watu wasio sahihi. Kwa kuangalia kwa nje, viongozi wa uwongo hawafanyi maovu mengi kwa makusudi, au kufanya mambo kwa njia yao wenyewe na kuanzisha falme zao wenyewe huru, kama wapinga Kristo wanavyofanya. Lakini viongozi wa uwongo hawawezi kutatua mara moja matatizo mbalimbali yanayoibuka katika kazi ya kanisa, na matatizo yanapotokea kwa wasimamizi wa timu mbalimbali, na wasimamizi hao wanaposhindwa kujitwika kazi yao, viongozi wa uwongo hawawezi kubadilisha wajibu wao au kuwavua wadhifa mara moja, wakileta hasara kubwa kwa kazi ya kanisa. Na hili lote linasababishwa na viongozi wa uwongo kutelekeza majukumu yao. Je, si viongozi wa uwongo ni wa kuchukiza sana? (Ndiyo.)

IV. Jinsi Viongozi wa Uwongo Wanavyowatendea Wasimamizi Wanaokiuka Mipangilio ya Kazi na Kufanya Mambo Kwa Njia Yao Wenyewe

Viongozi wa uwongo hawawezi kushughulikia mara moja matendo maovu yanayotokea kanisani kama vile wasimamizi kuwatesa wengine, wakiwabana, na kuisumbua kazi ya kanisa. Vivyo hivyo, baadhi ya wasimamizi wanapokiuka mipangilio ya kazi ya nyumba ya Mungu na kufanya mambo kwa njia yao wenyewe, viongozi wa uwongo hawawezi kupata masuluhisho yanayofaa ili kutatua masuala haya mara moja. Hili husababisha hasara kwa kazi ya kanisa na rasilimali za kimaada na za kifedha za nyumba ya Mungu. Viongozi wa uwongo ni wajinga na wa kijuujuu, wasioweza kuelewa kanuni za ukweli, na hasa wasioweza kung'amua viini vya asili vya watu. Kwa sababu hiyo, mara nyingi wao hufanya kazi yao kwa njia ya kijuujuu, wanafanya mambo kwa namna isiyo ya dhati, wanashikilia taratibu, na kuimba kaulimbiu, lakini hawaendi kwenye eneo la kazi ili kukagua kazi, kumtazama na kuulizia kuhusu kila msimamizi, au kuuliza kwa wakati ufaao kuhusu kile ambacho wasimamizi hawa wamefanya, kanuni zinazoongoza matendo yao ni zipi, na matokeo ya baadaye ni yapi. Matokeo yake, hawajui kabisa watu wanaowatumia ni akina nani kwa kweli na wamefanya nini. Kwa hivyo, wasimamizi hawa wanapokiuka kwa siri mipangilio ya kazi ya nyumba ya Mungu na kufanya mambo kwa njia yao wenyewe, si kwamba tu viongozi wa uwongo hawajui kuhusu hili, bali hata wanajaribu kuwatetea wasimamizi hao. Hata wakisikia kuhusu jambo hilo, wao hawachunguzi na hawalishughulikii mara moja. Viongozi wa uwongo kwa upande mmoja hawana uwezo katika kazi yao, na kwa upande mwingine, ni wazembe katika wajibu wao. Hebu tutoe mfano. Kiongozi fulani alimchagua mtu ambaye alikuwa ameondoshwa kutoka kwenye timu nyingine awe fundi wa upanzi. Hakuchunguza iwapo mtu huyu alikuwa na uzoefu na utaalamu unaofaa, kama angeweza kufanya kazi hiyo vizuri, au kama alikuwa na mtazamo makini na wa kuwajibika, na baada ya kumweka katika jukumu hilo, alimwacha bila kumchunguza kabisa, akisema, "Endelea na uanze kupanda mboga. Unaweza kuchagua mbegu, na mimi nitaidhinisha kiasi chochote unachotumia. Fanya tu kazi hii kwa namna yoyote unayoona inafaa!" Kiongozi alisema hili, na hivyo msimamizi huyu alianza kufanya kazi kwa namna yoyote aliyoona inafaa. Kazi yake ya kwanza ilikuwa kuchagua mbegu. Alipoangalia mtandaoni, aligundua, "Kuna aina nyingi sana tofauti za mboga—dunia hii kubwa imejaa mambo ya ajabu! Kuchagua mbegu kunafurahisha sana. Sijawahi kufanya kazi hii hapo awali, na sikujua ningevutiwa nayo sana. Kwa kuwa ninavutiwa nayo sana, nitafanya bila kujizuia!" Alifungua sehemu ya mbegu za nyanya kwanza, na alishangazwa sana. Kulikuwa na aina za kila namna na ukubwa wa kila aina, na kwa upande wa rangi kulikuwa na nyekundu, za njano, na za kijani. Aina moja hata ilikuwa na rangi nyingi—hakuwa amewahi kuona kitu kama hicho, na hili kwa kweli lilipanua upeo wake! Lakini angechaguaje mbegu sahihi? Aliamua kupanda kiasi cha kila aina, hasa ile ya rangi nyingi iliyoonekana ya kipekee sana. Msimamizi huyo alichagua zaidi ya aina 10 za nyanya za ukubwa, rangi, na maumbo tofauti. Baada ya kuchagua mbegu za nyanya, ulikuwa wakati wa kuchagua biringanya. Kwa kawaida, aina za biringanya ambazo watu hula ni biringanya ndefu na za zambarau au biringanya nyeupe, lakini aliwaza, "Biringanya hazipaswi kuwekewa mipaka kwa aina hizi mbili tu. Kuna aina za kijani, zenye michoro, ndefu, za mviringo, na za duaradufu. Nitachagua kiasi kidogo cha kila aina, ili kila mtu aweze kupanua mawazo yake na kula aina zote tofauti za biringanya. Kama msimamizi, tazama jinsi nilivyo stadi na jasiri katika kuchagua mbegu, jinsi ninavyowajali akina ndugu, nikiridhisha tamaa ya kila mtu." Kisha, alichagua mbegu za vitunguu. Kulikuwa na jumla ya aina 14 za vitunguu katika eneo hilo, na alivichagua vyote, na alipomaliza, alihisi kuridhika sana. Je, msimamizi huyu ni "jasiri"? Ni nani angethubutu kuchagua aina nyingi hivyo? Baadaye, Niliendelea kuchanganua jambo hili, na hata mtu mmoja akasema, "Hakuna aina 14 tu katika eneo hili; bado kuna aina chache zaidi ambazo hakuchagua!" Kile alichomaanisha ni kwamba aina 14 hazikuwa nyingi sana, na kwamba bado kulikuwa na aina nyingine ambazo msimamizi hakuchagua, kwa hivyo hakufanya kosa lolote. Je, si mtu aliyesema hili bozibozi? Huku ni kuwa mzito wa kuelewa, kutoelewa lugha ya binadamu, na kutojua kwa nini Nilikuwa nikichanganua jambo hilo. Baada ya kuchagua mbegu za vitunguu, msimamizi huyo pia alichagua angalau aina nane za viazi. Lengo lake katika kuchagua aina nyingi hivyo lilikuwa lipi? Kupanua upeo wa kila mtu na kuwaruhusu waonje ladha mbalimbali tofauti. Msimamizi huyo aliamini kwamba uteuzi wa mbegu unapaswa kutegemea kanuni ya kuwanufaisha akina ndugu. Mnafikiria nini kuhusu motisha yake? Je, kutenda kwa msingi wa mtazamo wa kufikiria kwa niaba ya kila mtu na kumhudumia kila mtu ndiyo kanuni inayotakiwa na nyumba ya Mungu? (La.) Basi, kanuni ya nyumba ya Mungu ya kuchagua mbegu ni ipi? Msipande aina fulani za ajabu na adimu ambazo hatuli kwa kawaida. Kuhusu aina ambazo huliwa kwa kawaida, ikiwa hatujazipanda hapo awali na hatujui kama zinafaa kwa udongo na hali ya hewa ya eneo hilo, chagueni aina moja au mbili, tatu au nne kwa kiwango cha juu kabisa. Kwanza, lazima zifae kwa udongo na hali ya hewa ya eneo hilo; pili, lazima ziwe rahisi kukuza na zisizoathiriwa na magonjwa na wadudu; tatu, zinapaswa kutoa mbegu kwa ajili ya mwaka unaofuata; mwisho, zinapaswa kutoa mavuno mazuri. Ikiwa ni tamu lakini mavuno ambayo zinatoa ni duni, hazifai. Kwa kuangalia suala la kuchagua mbegu, je, msimamizi huyu alitenda kulingana na kanuni? Je, alitafuta? Je, alitii? Je, aliijali nyumba ya Mungu? Je, alitenda kwa mtazamo anaopaswa kuwa nao katika utendaji wa wajibu? (La.) Ni wazi kwamba, alikuwa akifanya mambo mabaya kiholela, akikiuka waziwazi mipangilio ya kazi ya nyumba ya Mungu na kufanya mambo kwa namna yake mwenyewe! Alifuja sadaka za Mungu kwa njia hii ili kutosheleza udadisi wake binafsi na tamaa ya kujifurahisha, na alichukulia kazi muhimu kama hiyo kama mchezo, lakini kiongozi wake wa uwongo alimwacha afanye apendavyo bila kumwuliza maswali au kuingilia kati. Alipoulizwa, "Je, msimamizi uliyemchagua alifanya kazi yoyote kwa kweli? Matokeo yalikuwa yapi? Je, ulimsaidia kwa kufanya uchunguzi ilipokuja kwa suala la kuchagua mbegu?" Hakuzingatia mambo haya, na alisema tu, "Mbegu zimepandwa; tulitembelea eneo hilo wakati wa upanzi." Hakujali kuhusu masuala mengine yoyote. Suala la msimamizi huyu liligunduliwaje mwishowe? Alipanda baadhi ya stroberi, na kulingana na maelezo husika ya kiufundi, mimea ya stroberi haipaswi kufunikwa au kuruhusiwa kuzaa matunda katika mwaka wa kwanza, na maua yote yanapaswa kuondolewa; la sivyo, hakutakuwa na matunda yoyote mwaka wa pili, na hata kama kuna matunda mwaka wa kwanza, yatakuwa madogo sana. Hata ingawa wataalamu walimwambia msimamizi hili, alikataa kusikiliza. Kufikiri kwake kulitegemea habari mtandaoni iliyosema kwamba ilikubalika kufunika mimea ya stroberi kwa karatasi ya plastiki katika mwaka wa kwanza na kuiacha izae matunda. Matokeo ya hili yalikuwa kwamba ilizaa stroberi ndogo mbalimbali zilizoharibika umbo zikiwa zimefunikwa kwa mbegu—baadhi zikiwa kali, baadhi zikiwa tamu, na baadhi zisizo na ladha—kulikuwa na kila aina. Tatizo lilikuwa limekuwa baya kiasi hicho, lakini viongozi wa uwongo hapo walilipuuza kabisa. Kwa nini? Kwa sababu walifikiri kwamba hawangepata kula stroberi hizo hata hivyo, kwa hivyo waliamua kupuuza suala hilo. Je, kutopata kula kitu kunamaanisha hawapaswi kukijali? Vipi kuhusu viazi na vitunguu ambavyo wangepata kula—je, walivijali? Hakuna hata mmoja kati ya viongozi hawa wa uwongo aliyejali; walitazama tu huku msimamizi akifanya apendavyo. Siku moja, Niliwatembelea, na mtu mmoja akaripoti kwamba letasi ilikuwa imekomaa sana, na iwapo hawangeivuna hivi karibuni, hakuna mtu ambaye angeweza kuila na ingeharibika. Hata hivyo, msimamizi alisisitiza kuiacha, na akasema kwamba ikiwa wangeivuna wangelazimika kupanda mboga nyingine, jambo ambalo aliliona kuwa la kusumbua. Licha ya kujua kuhusu jambo hili, viongozi wa uwongo hawakufanya chochote. Hatimaye, Aliye juu alilazimika kuwaamuru wavune letasi haraka na washughulikie hali hiyo; la sivyo, letasi ingechukua ardhi na kuzuia mboga za majira ya joto kupandwa. Licha ya tatizo kubwa kama hilo kutokea katika kazi, hakuna hata mmoja wa viongozi wa uwongo aliyefanya chochote kulihusu, waliogopa sana kuwaudhi watu. Kwa sababu msimamizi alipandishwa cheo na kiongozi wa uwongo, na hakuwahi kukagua kazi yake baada ya kumpandisha cheo, alimruhusu atende kwa uhuru, na akampa msaada na kumuunga mkono, na viongozi wengine hawakuthubutu kuingilia kati, na walishirikiana nao kwa karibu, kwa hivyo matatizo mengi yaliibuka hatimaye. Hii ndiyo kazi ambayo viongozi walifanya. Je, bado wanaweza kuitwa viongozi? Licha ya suala zito kama hilo kufanyika mbele ya macho yao, walishindwa kulitambua kama tatizo, sembuse kulitatua. Je, si hawa ni viongozi wa uwongo? (Ndiyo, wao ni viongozi wa uwongo.) Kwa upande mmoja, walikuwa wenye kutaka kuwafurahisha wengine na waliogopa kuwaudhi wengine. Kwa upande mwingine, hawakujua jinsi tatizo lilivyokuwa zito, hawakuwa na uamuzi sahihi, hawakujua lilikuwa tatizo, na hawakujua kwamba kazi hii ilikuwa ndani ya upeo wa majukumu yao. Je, si wao nyangarika na wafujaji? Je, si huu ni utelekezaji wa wajibu? (Ndiyo.) Hii ni hali ya nne: wasimamizi kukiuka mipangilio ya kazi ya nyumba ya Mungu na kufanya mambo kwa namna yao wenyewe. Tumetoa mfano, ambao unafichua udhihirisho wa viongozi wa uwongo wa kutelekeza majukumu yao katika jambo hili na kuweka wazi kiini cha asili cha viongozi wa uwongo.

V. Jinsi Viongozi wa Uwongo Wanavyowatendea Wasimamizi Ambao Ni Wapinga Kristo na Kuanzisha Falme Zinazojitegemea

Hali nyingine ni wakati wasimamizi wanapoasi dhidi ya wakubwa wao na kuanzisha falme zinazojitegemea—wasimamizi hawa ni wapinga Kristo. Viongozi wa uwongo hawawezi kutekeleza jukumu la wasimamizi linapokuja suala la mambo kama vile wasimamizi kuwa na ubora duni wa tabia, kuwa na ubinadamu mbaya, au kufanya mambo mabaya kiholela. Pia wanashindwa kukagua na kuulizia mara moja kuhusu kazi ambayo wasimamizi wa aina hii wanafanya na matatizo yao ili kubaini kufaa kwao. Vivyo hivyo, viongozi wa uwongo wanashindwa hata zaidi kung'amua kiini cha asili cha wapinga Kristo, ambao ni watu waovu na wakatili. Si tu kwamba wanashindwa kung'amua hili, wakati huo huo wanawaogopa watu hawa kiasi, na hawana msaada na ni dhaifu kiasi, kiasi kwamba, mara nyingi, wanaburutwa na wapinga Kristo. Hili linaweza kuwa zito kiasi gani? Wapinga Kristo wanaweza kuunda makundi ndani ya maeneo ya kazi ya viongozi wa uwongo, wakikusanya nguvu zao wenyewe na kuanzisha falme zinazojitegemea, na hatimaye, wanaweza kuchukua usukani, waanze kutoa amri, na wawafanye viongozi wa uwongo wawe viongozi wa jina tu. Viongozi hawa wa uwongo kwa namna fulani hawajui mambo ambayo wapinga Kristo wanaamua na kujua kuyahusu, na wako gizani kuyahusu. Wao hutambua mambo haya tu baada ya jambo kutokea na mtu kuwaripotia, lakini kufikia wakati huo, inakuwa imechelewa sana. Viongozi wa uwongo hata huwauliza wapinga Kristo kwa nini hawakujulishwa, na jibu lao ni, "Kuna faida gani ya kukwambia? Huwezi kufanya maamuzi kuhusu chochote, kwa hivyo hakukuwa na haja ya kujadili hili na wewe, tulifanya uamuzi wenyewe. Hata kama tungalikujulisha, hakika ungalikubali. Ungalikuwa na maoni gani?" Viongozi wa uwongo hawana uwezo wa kufanya lolote katika mambo kama hayo. Ikiwa huwezi kuwang'amua, kuwashughulikia, au kutatua tatizo la wapinga Kristo hawa, unapaswa kuwaripoti kwa Aliye juu, lakini wewe huthubutu hata kufanya hivyo—je, si wewe ni nyangarika? (Ndiyo.) Wanapokabiliwa na mambo kama haya, nyangarika hawa wakubwa huja Kwangu tu kulalamika wakitokwa na machozi, wakinung'unika, "Si kosa langu; mimi sikufanya uamuzi huo. Iwe uamuzi walioufanya ulikuwa sahihi au la haunihusu, kwa sababu hawakunijulisha au kuniambia kuuhusu walipoufanya." Wanamaanisha nini kwa hili? (Wanakwepa kujukumika.) Kama kiongozi, unapaswa kujua na kufahamu mambo haya; wapinga Kristo wasipokujulisha kuhusu mambo, kwa nini huchukui hatua ya kwenda na uulize wewe mwenyewe? Kama kiongozi, unapaswa kupanga, kusimamia, na kufanya maamuzi kuhusu kila jambo; wasipokujulisha kuhusu chochote na wanafanya maamuzi wao wenyewe, wakikutumia ankara baadaye ili utie saini, je, hawakunyang’nyi mamlaka yako? Punde tu viongozi wa uwongo wanapokutana na wapinga Kristo wakiisumbua kazi ya kanisa, wanapigwa na butwaa; hawana uwezo wa kufanya lolote kama wapumbavu wanaokabiliwa na mbwa mwitu, na wanasimama tu bila uwezo huku wakifanywa kuwa viongozi wa jina tu na kunyang’anywa mamlaka yao. Hawawezi kufanya hata jambo moja kulihusu—kundi la watu wasio na maana walioje! Hawawezi kutatua masuala, hawawezi kuwang'amua au kuwafichua wapinga Kristo, na hakika hawawezi kuwazuia kufanya matendo yoyote maovu. Wakati huo huo, hawaripoti masuala haya kwa Aliye juu. Je, si hawa ni nyangarika? Kuna faida gani ya kukuchagua wewe kuwa kiongozi? Wapinga Kristo wanafanya mambo mabaya kiholela, wanafuja sadaka waziwazi, na wanaunda nguvu ambazo wanaziongoza na kuanzisha falme zinazojitegemea ndani ya kanisa; wakati huo huo, unashindwa kabisa kuwasimamia, kuwafichua, kuwazuia, au kuwashughulikia, lakini unakuja Kwangu kulalamika. Wewe ni kiongozi wa aina gani? Wewe kwa kweli ni nyangarika! Haijalishi kile wanachokifanya, magenge haya yanayoongozwa na wapinga Kristo hufanya majadiliano kwa siri miongoni mwao na kisha kufanya maamuzi bila idhini. Hata hawawapi viongozi haki ya kujua kinachoendelea, sembuse haki ya kufanya maamuzi. Wanawapuuza viongozi moja kwa moja, wakitumia mamlaka yote wao wenyewe na kufanya maamuzi yote. Viongozi waliopewa jukumu la kuwasimamia wanafanya nini katikati ya haya yote? Wanashindwa kabisa kukagua, kusimamia, kuongoza, au kufanya maamuzi kuhusu kazi hii. Mwishowe, wanawaacha wapinga Kristo wachukue usukani na wawasimamie kutoka juu. Je, si tatizo hili linatokana na kazi ya viongozi wa uwongo? Kiini cha tatizo hili ni nini? Linatokana na nini? Linatokana na viongozi wa uwongo kuwa na ubora duni wa tabia, kukosa uwezo wa kazi, na wapinga Kristo kutowajali kabisa. Wapinga Kristo huwaza, "Unaweza kufanya nini kama kiongozi? Bado sitakusikiliza, na nitaendelea kukupita na kufanya mambo. Ukiripoti hili kwa Aliye juu, tutakutesa!" Viongozi wa uwongo huwa hawathubutu kuripoti mambo kama hayo. Si tu kwamba viongozi wa uwongo wanakosa uwezo wa kazi, pia wanakosa ujasiri wa kushikilia kanuni, wanaogopa kuwaudhi watu, na hawana uaminifu kabisa—je, hili si tatizo zito? Kama kwa kweli wangekuwa na ubora kiasi wa tabia na wangekuwa wanaelewa ukweli, basi baada ya kuona kwamba watu hawa walikuwa wabaya, wangesema, "Sithubutu kuwafichua peke yangu, kwa hivyo nitafanya ushirika na akina ndugu na dada kadhaa wanaofuatilia na kuelewa ukweli zaidi ili kutatua masuala haya. Ikiwa, baada ya kufanya ushirika nao, bado hatuwezi kuwashughulikia wapinga Kristo, nitaripoti tatizo hilo kwa Aliye juu na nimwache alitatue. Siwezi kufanya chochote kingine, lakini lazima kwanza nilinde masilahi ya nyumba ya Mungu; masuala ambayo nimeyang'amua na matatizo ambayo nimeyagundua hayapaswi yaruhusiwe kabisa yaendelee kukua." Je, si hii ni njia ya kushughulikia tatizo? Je, haiwezi pia kuhesabiwa kama kutimiza wajibu wa mtu? Ukiweza kufanya hili, basi Aliye juu hatasema kwamba una ubora duni wa tabia na unakosa uwezo wa kazi. Hata hivyo, huwezi hata kuripoti matatizo kwa Aliye juu, kwa hivyo unaainishwa kama nyangarika na kiongozi wa uwongo. Si kwamba tu una ubora duni wa tabia na unakosa uwezo wa kazi, huna hata imani na ujasiri wa kumtegemea Mungu ili kuwafichua na kupambana na wapinga Kristo. Je, si wewe ni nyangarika? Je, wale ambao wamenyang’anywa mamlaka na wapinga Kristo ni wa kuhurumiwa? Wanaweza kusikika kuwa wa kuhurumiwa; hawajafanya chochote kibaya, na katika kazi yao wao ni waangalifu sana, wanaogopa sana kufanya makosa, kupogolewa, na kudharauliwa na akina ndugu. Lakini wanaishia kunyang’anywa mamlaka kabisa na wapinga Kristo mbele ya macho yao, hakuna wanachosema kilicho na athari yoyote, na haijalishi sana kama wapo au la. Wanaweza kuonekana wa kuhurumiwa kwa nje, lakini kwa kweli wanachukiza sana. Hebu Niambie, je, nyumba ya Mungu inaweza kutatua matatizo ambayo watu hawawezi? Je, watu wanapaswa kuripoti matatizo kwa Aliye juu? (Ndiyo, wanapaswa kuripoti.) Katika nyumba ya Mungu, hakuna matatizo ambayo hayawezi kutatuliwa, na maneno ya Mungu yanaweza kutatua suala lolote. Je, una imani ya kweli katika Mungu? Ikiwa huna hata imani hii kidogo, unastahilije kuwa kiongozi? Je, si wewe ni mtu asiye na maana? Hili si tu kuhusu kuwa kiongozi wa uwongo; unakosa hata imani ya msingi kabisa katika Mungu. Wewe ni asiyeamini na hustahili kuwa kiongozi!

Kuhusu jukumu la nne la viongozi na wafanyakazi, tumeorodhesha hali tano ili kufichua jinsi viongozi wa uwongo wanavyoshughulikia vipengele mbalimbali vya kazi na wasimamizi. Kwa kuzingatia hali hizi tano, tulichanganua udhihirisho mbalimbali wa ubora duni mno wa tabia wa viongozi wa uwongo, ukosefu wao wa uwezo, na kutoweza kwao kufanya kazi halisi. Kwa kufanya ushirika kwa njia hii, je, mmeelewa wazi zaidi jinsi ya kuwang'amua viongozi wa uwongo? (Ndiyo.) Sawa basi, hebu tuhitimishe ushirika wetu hapa leo. Kwaherini!

Tarehe 23 Januari 2021

Iliyotangulia: Majukumu ya Viongozi na Wafanyakazi (2)

Inayofuata: Majukumu ya Viongozi na Wafanyakazi (4)

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp