Majukumu ya Viongozi na Wafanyakazi (29)
Kipengele cha Kumi na Tano: Kulinda wafanyakazi muhimu wa kila aina, kuwalinda kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje, na kuwaweka salama ili kuhakikisha vipengele mbalimbali muhimu vya kazi vinaweza kuendelea kwa utaratibu
Tuliachia wapi wakati uliopita katika kushiriki juu ya mada ya majukumu ya viongozi na wafanyakazi? (Wakati uliopita, tulishiriki hasa juu ya dhihirisho tatu za mwisho katika jukumu la kumi na nne la viongozi na wafanyakazi kuhusiana na kutambua aina mbalimbali za watu kulingana na ubinadamu wao. Dhihirisho hizi tatu ni: kuwa mwoga na mwenye kushukiwa, kuelekea kukaribisha shida, na kuwa na maisha ya nyuma yasiyo wazi.) Tulimaliza kushiriki juu ya mada tatu za mwisho katika jukumu la kumi na nne la viongozi na wafanyakazi wakati uliopita, kwa hivyo leo tutashiriki juu ya jukumu la kumi na tano. Jukumu la kumi na tano ni lipi? (“Kipengele cha Kumi na Tano: Kulinda wafanyakazi muhimu wa kila aina, kuwalinda kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje, na kuwaweka salama ili kuhakikisha vipengele mbalimbali muhimu vya kazi vinaweza kuendelea kwa utaratibu.”) “Kulinda wafanyakazi muhimu wa kila aina, kuwalinda kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje, na kuwaweka salama.” Jukumu hili linahusisha kipengele kingine cha majukumu ya viongozi na wafanyakazi; pia ni kipengele mahususi cha kazi ambacho viongozi na wafanyakazi lazima wafanye vizuri. Kipengele hiki cha kazi kinafungamana na nini? (Kinafungamana kuwaweka watu wateule wa Mungu salama.) Kinahusisha masuala ya usalama wa kibinafsi. Je, si mada hii hujitokeza mara kwa mara katika kazi ya kanisa? Je, hamuifahamu mada hii? (La.) Mada hii si ngeni kwa ndugu Wachina, kwa sababu katika mazingira ya kijamii ya Uchina, waumini huteswa na kukamatwa, na wanahitaji hakikisho la usalama katika kutekeleza wajibu wao na katika vipengele vyote vya maisha. Kwa hivyo, kazi hii iko ndani ya upeo wa majukumu ya viongozi na wafanyakazi; si jambo la hiari. Bila kujali kama nchi ina uhuru wa dini, kuwapangia wafanyakazi wanaotekeleza wajibu mbalimbali muhimu makazi na maisha ipasavyo ni kipengele mahususi cha kazi ambacho viongozi na wafanyakazi lazima watekeleze. Lengo au mahitaji mahususi ya kazi hii yanaweza kutofautiana, lakini kimsingi yote inahusu iwapo akina ndugu wanaweza kutekeleza wajibu wao kwa usalama na uthabiti, na iwapo matokeo ya wajibu wao yanaweza kuhakikishwa. Kwa hivyo, usipuuze kazi hii au kuichukulia kuwa haikuhusu kwa sababu unaishi katika nchi ya kidemokrasia. Bila kujali mfumo wa utawala katika nchi unamoishi au iwapo waumini wanateswa huko, kazi hii imo ndani ya upeo wa majukumu ya viongozi na wafanyakazi; ni kazi ambayo viongozi na wafanyakazi lazima watekeleze—hakuna anayeachwa nje, na haipaswi kuchukuliwa kama kazi ya “ziada.” Basi leo, hebu tushiriki juu ya masuala yote mbalimbali yanayohusika katika mada hii.
Upeo wa Wafanyakazi Muhimu wa Kazi
Kwanza, hebu tuangalie maana ya “wafanyakazi muhimu wa kila aina” waliotajwa katika jukumu la kumi na tano. Je, si hii ni mada tunayopaswa kushiriki juu yake? (Ndiyo.) Basi, “wafanyakazi muhimu wa kila aina” inarejelea nini? Hebu kwanza tuanzishe mawanda ya walengwa wa kazi hii. Nani anaweza kuzungumzia hili? (Wafanyakazi muhimu wa kila aina wanajumuisha ndugu katika timu za video, timu za utengenezaji filamu, timu za usahihishaji, na timu za nyimbo za sifa, na wale wanaotekeleza wajibu mwingine muhimu. Zaidi ya hayo, inajumuisha ndugu fulani wanaotimiza majukumu muhimu katika vipengele mbalimbali muhimu vya kazi, pamoja na wasimamizi wa kila timu.) Nani mwingine angependa kuongezea juu hili? (Pia inajumuisha viongozi na wafanyakazi.) Viongozi na wafanyakazi lazima kwa kweli walindwe vizuri. Nani mwingine? (Pia kuna wafanyakazi muhimu wanaoshughulikia mambo ya jumla, kama vile wafanyakazi wa fedha.) (Na ndugu ambao, kwa sababu wanamwamini Mungu na wanatekeleza wajibu, wanatafutwa au wana rekodi ya polisi pia wanahitaji ulinzi.) Hiki ni kitengo kingine, na ni kundi maalum. Hebu tufanye muhtasari wa ni vitengo vingapi vilivyopo. Kitengo cha kwanza kinajumuisha viongozi na wafanyakazi. Kitengo cha pili kinajumuisha wafanyakazi ambao hawawezi kukosekana katika vipengele mbalimbali vya kazi katika nyumba ya Mungu, hasa viongozi wa timu na wasimamizi wa vipengele mbalimbali vya kazi na wafanyakazi wenye ubora mzuri wa tabia, ufahamu wa kiroho, na uwezo wa kufahamu kanuni na kubeba kazi muhimu kwa kujitegemea. Kuna wafanyakazi wa aina nyingi wanaoshughulikia vipengele mbalimbali vya kazi, kama vile wale walio katika kazi ya maandishi, kazi ya nyimbo za sifa, kazi ya utengenezaji filamu, na kadhalika, pamoja na wale wanaohubiri injili, kushuhudia, au kutumika kama waelekezi wa injili, miongoni mwa wengine. Zaidi ya hayo, hii inajumuisha wafanyakazi wanaoshughulikia kazi ya fedha, utunzaji, na mambo ya nje. Watu hawa hutimiza jukumu la usaidizi katika kazi ya kanisa na ni wa msingi; wote wanajumuishwa kama sehemu ya wafanyakazi wanaoshughulikia vipengele mbalimbali vya kazi. Hiki ni kitengo kikuu cha pili. Kitengo kikuu cha tatu kinajumuisha wale wanaojihusisha na kazi iliyo hatari ya kanisa. Hasa, katika nchi zenye serikali za kimabavu ambapo hakuna uhuru wa dini, kuna vipengele fulani vya kazi vya hatari sana, kama vile kuchapisha vitabu, kusafirisha vitabu, kutunza mali ya kanisa, pamoja na kuwa wenyeji na kuwapangia makazi wafanyakazi wanaotekeleza wajibu muhimu. Nani mwingine amejumuishwa? (Pia kuna wafanyakazi fulani wa mambo ya jumla wanaowasilisha taarifa nje; wajibu wanaoutekeleza pia ni wa hatari kwa ulinganisho.) Watu hawa pia wanachukuliwa kuwa wanajihusisha katika kazi ya hatari. Hata hivyo, watu hawa hakika hawafanyi kazi hii mara kwa mara; bali, wao hujikita katika kutekeleza kazi hizi muhimu na za hatari, kama vile kuwasilisha taarifa, kusambaza mipangilio ya kazi, kusambaza video, filamu, au rekodi zote za mahubiri za nyumba ya Mungu, na kadhalika. Katika nchi za kimabavu zisizo na uhuru wa dini, viongozi na wafanyakazi lazima wawe wazi kuhusu ni wepi kati ya watu wateule wa Mungu wanaotekeleza wajibu muhimu na kufanya kazi ya hatari. Kwa ufupi, watu hawa pia ni kitengo mojawapo cha wafanyakazi muhimu, na viongozi na wafanyakazi lazima wazingatie usalama wao kwa namna ya kipekee; haiwezi kupuuzwa. Hiki ni kitengo cha tatu. Kitengo cha nne ni kundi lingine la msingi katika kazi ya kanisa. Watu hawa wana ujuzi maalum na karama, kama vile kuwa hodari katika kuhubiri injili, kutoa mahubiri, kulinyunyizia kanisa, au kuchukua jukumu la kupanga vipengele maalum vya kazi. Watu hawa wanaweza kuwa viongozi na wafanyakazi, wasimamizi wa vipengele mbalimbali vya kazi, au watu wanaojihusisha na kazi ya hatari. Bila watu kama hao, kungekuwa na pengo katika kazi muhimu wanayoshughulikia, na hakuna mtu mwingine ambaye angeweza kujaza nafasi yao. Kwa hivyo, watu hawa wanapaswa kulindwa, na usalama wao unapaswa kuhakikishwa. Hiki ni kitengo mojawapo cha watu. Kitengo kingine ni wale ambao, katika nchi ambapo dini zinateswa, wanatafutwa au rekodi zao zipo katika vituo vya polisi kwa sababu ya imani yao katika Mungu. Bila kujali upeo wa hati ya kukamatwa au kazi mahususi wanayofanya kanisani, maadamu wanatafutwa kwa sababu ya imani yao katika Mungu na kwa kutekeleza wajibu wao, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kutafuta njia za kuwalinda, wakiwapangia wawekwe katika makazi yaliyo katika maeneo salama kwa ulinganisho ili watekeleze wajibu wao. Kati ya nchi zote zinazotesa imani ya kidini, mateso ya China ndiyo makali zaidi. Katika mikoa na maeneo mbalimbali kote nchini China, watu wengi wamekamatwa au wanatafutwa, hawawezi kurudi nyumbani. Kuna nchi kama hii kote ulimwenguni na katika kila bara ambazo zinatesa imani ya kidini kama China, na katika nchi hizi, pia kuna wale ambao, kwa sababu ya kumkubali Mwenyezi Mungu, wanakabiliwa na mateso na hawawezi kurudi nyumbani. Kwa wale wanaoteswa na hawawezi kurudi nyumbani, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuwapangia makazi katika kanisa la wajibu wa wakati wote haraka iwezekanavyo. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuwapa makazi katika mazingira salama kiasi kulingana na hali za mahali hapo ili waweze kufanya wajibu wao. Hiki ni kipengele cha kipaumbele cha kazi ambacho lazima kifanywe vizuri. Watu hawa ambao wamekamatwa au wanatafutwa wanaunda kitengo cha tano cha wafanyakazi wanaohitaji ulinzi. Kuna kitengo kingine miongoni mwa wafanyakazi wanaoshughulikia vipengele mbalimbali vya kazi muhimu ambacho ni cha kipekee. Watu hawa wanaweza kuwa si viongozi au wafanyakazi kwa sasa, wala hawajihusishi na kazi ya hatari, lakini hapo awali wamefanya wajibu mwingi na kazi yao imejumlisha eneo pana. Wanazijua familia nyingi za wenyeji na pia wanajua kuhusu wafanyakazi fulani wanaotekeleza wajibu muhimu. Kwa hivyo, watu kama hao wakikamatwa, italeta pia maafa kwa kazi ya kanisa. Watu hawa wanapaswa kurejelewa kama “watu wanaojua mambo,” na wanapaswa pia kujumuishwa miongoni mwa wafanyakazi muhimu wa kila aina. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuhakikisha usalama wao, kwa kusudi la kulinda usalama wa watu wote wateule wa Mungu na kuhakikisha kwamba kazi ya kanisa inaweza kuendelea kwa kawaida. Watu fulani katika kundi hili hasa ni wasiojali kabisa; hawajui kutahadhari, na hawana hekima nyingi. Daima wana mwelekeo wa kutenda kutokana na shauku, wakifanya mambo bila kujali huko nje. Kwa kuwa hawajawahi kukamatwa au kuteswa, hawafahamu hatari iliyopo na matokeo yanayoweza kutokea ikiwa jambo fulani litakwenda mrama, sembuse kuelewa uzito wa matokeo hayo ungekuwaje. Kwa sababu wanaamini kwamba wanamwamini Mungu tu, na hawafanyi chochote kibaya, hawaogopi chochote. Matokeo yake, baada ya kufanya kazi katika eneo hilo kwa muda, wanaweza kujulikana sana na kuwa chini ya ufuatiliaji wa serikali. Je, hilo halisababishi hatari? Mara wanapokamatwa, ikiwa hawawezi kuhimili kuhojiwa kwa kuteswa, wanaweza kuwa wasaliti kama Yuda, na kuwasaliti akina ndugu. Hili litaleta hasara kubwa kwa kanisa na kuwahusisha ndugu wengine, likiwaweka katika hatari ya kukamatwa na kufungwa jela, jambo ambalo litaathiri pakubwa vipengele mbalimbali vya kazi ya kanisa. Kwa hivyo, kanisa linapaswa pia kuupa kipaumbele ulinzi wa watu kama hao. Ikiwa hakuna mahali salama panapoweza kupatikana katika eneo la karibu pa kuwaficha, wanapaswa kuhamishiwa mahali salama kiasi kwingineko ili wafanye wajibu wao. Hiki bado ni kitengo kingine cha watu. Kwa sababu ya ubora maalum ya hali yao, viongozi na wafanyakazi wanahitaji kuwapangia sehemu za kazi, kwa hivyo wao pia wamejumuishwa miongoni mwa wafanyakazi muhimu wa kila aina. Kuna vitengo vingapi vya watu kwa jumla? (Vitengo sita. Kitengo cha kwanza ni viongozi na wafanyakazi. Cha pili kinajumuisha wafanyakazi wasioweza kukosekana wanaoshughulikia vipengele mbalimbali vya kazi katika nyumba ya Mungu; wasimamizi, viongozi wa timu, na waelekezi wa injili; na wale wanaoweza kubeba kazi. Kitengo cha tatu ni wafanyakazi wanaojihusisha na kazi ya hatari ya kanisa. Cha nne ni wale walio na ujuzi maalum na karama. Kitengo cha tano kina watu wenye rekodi za polisi, wale wanaosakwa, na wale wanaotafutwa. Na Kitengo cha sita ni watu wanaojua mambo.) Tumepitia kimsingi wafanyakazi wote muhimu wanaohusika katika vipengele mbalimbali vya kazi, lakini kuna kitengo kimoja cha kuongezea: Ikiwa ndugu wowote kanisani, kwa sababu ya kwenda nje kutekeleza wajibu wao, kukamatwa, au kukabiliwa na hali nyingine yoyote isiyotarajiwa, hawawezi kuwatunza watoto wao wenye umri mdogo, basi viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuwapangia watoto hawa waishi katika nyumba inayofaa ili wawe na namna ya kuishi. Hiki pia ni kipengele maalum cha kazi. Ingawa kipengele hiki cha kazi hakihusiani na kazi ya kanisa, na kinatokana tu na hali maalum, viongozi na wafanyakazi lazima wachukue jukumu la kuwapangia makazi na maisha yanayofaa watoto hawa wenye umri mdogo. Ikiwa hawana jamaa wanaofaa, au ikiwa jamaa zao ni wasioamini na hawako radhi kuwapokea, basi kanisa linapaswa kuwapokea. Kanisa halipaswi tu kuwapangia nyumba ya wenyeji inayofaa bali pia kuwapangia ndugu watakaowajibika kwa ajili ya kuwatunza. Punde makazi yanayofaa yakiisha kupangwa kwa ajili yao, ikiwa wanamwamini Mungu, hilo bila shaka ni bora, na wanapofikia utu uzima, wanaweza kutekeleza wajibu wao kanisani. Ikiwa hawamwamini Mungu, basi wanapofikia utu uzima na kuingia katika jamii, hawatahusiana tena na kanisa, na jukumu letu litakuwa limetimizwa. Hatutahitaji kujishughulisha na mambo yao baada ya hapo. Je, hili linafaa? (Ndiyo.) Ingawa kazi hii haihusishi vipengele mbalimbali vya kazi ya kanisa, bado inapaswa kujumuishwa ndani ya upeo wa majukumu ya viongozi na wafanyakazi. Ikiwa kuna watoto wa wale wanaotekeleza wajibu kanisani wanaohitaji kupangiwa makazi, isipokuwa kama viongozi na wafanyakazi hawajui kuhusu hali hiyo, hawawezi kuipuuza. Wakijua kuihusu, wanapaswa kuuliza maswali, kuishughulikia, na kuchukua jukumu hili la kuwapangia makazi yanayofaa. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuhakikisha kwamba ndugu wanaotekeleza wajibu wao—hasa wale wanaofanya kazi muhimu—hawana wasiwasi linapokuja suala hili. Kutekeleza kipengele hiki cha kazi vizuri si vigumu, sivyo? (La, si vigumu.) Kuna angalau vitengo sita vya wafanyakazi muhimu. Kitengo cha saba ni cha ziada, kinawakilisha aina maalum sana ya hali. Wafanyakazi mbalimbali walioainishwa katika vitengo sita vya kwanza huenda wasiwepo wote katika kila eneo la uchungaji au nchi. Hata hivyo, bila kujali nchi, kuwalinda viongozi na wafanyakazi na wale wanaotekeleza wajibu muhimu ni kipengele muhimu cha kazi. Hiki ni kipengele cha kazi ambacho viongozi na wafanyakazi wote wa kanisa lazima wakitilie maanani, na ni jukumu ambalo lazima walitimize vizuri.
Kuwakinga Wafanyakazi wa Kazi Muhimu Dhidi ya Kuingiliwa na Ulimwengu wa Nje
I. Masharti ya Usalama kwa Familia za Wenyeji
Sasa kwa kuwa tumebainisha wafanyakazi muhimu ni kina nani, hebu tuangalie kazi mahususi ambayo viongozi na wafanyakazi lazima wafanye—yaani, kulinda wafanyakazi muhimu wa kila aina, kuwalinda kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje, na kuwaweka salama. Hivyo, ni kazi gani mahususi inayohitajika kufanywa ili kuwalinda kwa ufanisi kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje, ili viongozi na wafanyakazi wachukuliwe kuwa wametimiza majukumu yao? Linapokuja suala la kutekeleza kazi mahususi, baadhi ya viongozi na wafanyakazi wanahisi wamekwama, wakijikuna vichwa na kuhangaika sana, wasijue la kufanya. Kuna kanuni muhimu katika kuwapangia makazi wafanyakazi hawa muhimu: Lazima walindwe kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje ili kuhakikisha usalama wao. Iwe wafanyakazi muhimu wamewekwa katika nyumba za ndugu au katika nyumba za kukodi, jambo la msingi ni kwamba usalama wao lazima uhakikishwe. Kuhakikisha usalama wao kunamaanisha kuwalinda kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje. Basi, viongozi na wafanyakazi lazima wafanye nini ili kuwalinda kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje? Inahitaji kuwapangia makazi wale wanaotekeleza wajibu muhimu katika maeneo yanayofaa. Hebu tuliangalie hili kutoka kwa vipengele viwili: Kimoja ni mazingira ya ndani ya familia ya wenyeji, na kingine ni mazingira ya nje. Kwa upande wa mazingira ya ndani, kwanza, mwenyeji lazima awe muumini wa kweli, aliye tayari kuwa mwenyeji, anayeweza kuweka siri, kutenda kwa tahadhari, na kushughulika na ulimwengu wa nje kwa hekima. Hali yoyote maalum ikitokea, wanapaswa kujua jinsi ya kuishughulikia; wanapaswa kuweza kuishughulikia na kuitatua kwa kuchukua hatua badala ya kungoja tu. Zaidi ya hayo, wanapaswa kuwa na sifa nzuri katika eneo hilo, au labda hadhi na mahusiano fulani katika eneo hilo. Hata kama hawana ushawishi, wanapaswa angalau kuwa watu wenye kujiheshimu na kuishi maisha ya heshima na ambao hawakaribishi shida kamwe au kuvutia watu wenye hila nyumbani kwao. Hawapaswi kuwa na marafiki wanaokusanyika kucheza mahjong au kunywa pombe. Zaidi ya hayo, mahusiano yao na ulimwengu wa nje na majirani zao yanapaswa kuwa ya kawaida kiasi. Hawapaswi kujihusisha na mizozo yoyote juu ya madeni na hawapaswi kuwa na ugomvi na majirani zao. Kwa maneno mengine, mazingira ya nyumbani kwao yanapaswa kuwa tulivu kiasi, mwenyeji anapaswa kuwa na mahusiano yasiyo na utata, na watu wa nje wachache sana wanapaswa kuwa wakija nyumbani kwake kusababisha usumbufu, na kadhalika—vipengele vyote vinapaswa kuwa vinafaa. Zaidi ya hayo, watoto au jamaa wa mwenyeji wanapaswa kuunga mkono imani yake katika Mungu, au angalau wasimpinge kuwakaribisha ndugu, na hakika wasiende huku na kule wakizungumza juu ya mambo haya ovyoovyo. Wengine wanaweza kusema, “Si rahisi kupata familia ya wenyeji inayotimiza vigezo hivi vyote!” Hili linamaanisha kutafuta mahali panapofaa kiasi; ukamilifu kabisa hauhitajiki. Angalau, mazingira ya kuishi yanapaswa kuwa yanayofaa—matulivu na yasiyo na kuingiliwa kutoka nje—jambo ambalo linatimiza hitaji la kuwalinda wafanyakazi muhimu kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje. Katika familia fulani za wenyeji, ingawa si kila mshiriki wa familia ni muumini, mtu anayewakaribisha ana hadhi ndani ya nyumba na hufanya maamuzi. Watoto au jamaa zake wasioamini hawathubutu kuingilia imani yao katika Mungu au kuwakaribisha ndugu; hata kama hawakubaliani moyoni, hawathubutu kutoa habari hii kwa watu wa nje ya familia. Jambo fulani likitokea kweli, wanaweza hata kusaidia kutoa ulinzi. Kwa namna hii, ndugu wanaokaa katika nyumba hii ya wenyeji wanaweza pia kubaki bila kuathiriwa na kuingiliwa na ulimwengu wa nje. Katika hali fulani, mwenyeji ni mwoga, akiogopa kwamba watoto wake wanaweza kufichua imani yake katika Mungu, kwamba majirani wake wanaweza kugundua kuhusu imani yake na kumripoti, na hasa kwamba mambo yanaweza kuharibika na akamatwe. Punde anapoanza kuwakaribisha ndugu, anakuwa na wasiwasi mwingi kila siku, hawezi kula mchana au kulala usiku, akishinda kutwa nzima akiwa na hofu na woga, kama mwizi. Kila anaposikia kwamba kuna jambo, kama vile serikali kupanga kukagua usajili wa kaya au wafanyakazi wa serikali kuja nyumbani kwake kufanya kitu kwa visingizio mbalimbali, anaogopa sana na kutaka kila mara ndugu waondoke mara moja ili yeye mwenyewe asihusishwe. Ndugu wanapoona hili, wanapaswa kuhama mara moja, kwani mahali kama hapo hapafai kwa ajili ya kuwa wenyeji; panaweza kutumiwa tu kama kituo cha muda kwa siku chache. Ikiwa watoto, jamaa, au marafiki wa familia ya wenyeji ni watu waovu ambao, baada ya kujua kwamba mwenyeji anawapokea waumini, wanaweza kuja kusumbua au hata kuwakabidhi ndugu kwa polisi, basi hili ni jambo hatari sana. Familia ya wenyeji kama hiyo haifai kukaa nayo. Wazazi wengine hutenda kama watumwa mbele ya watoto wao; wanaweza kusema, “Ni sawa, watoto wangu hunisikiliza,” lakini kwa uhalisi, utii wa watoto wao unategemea hali. Masilahi yao wenyewe yanapohusika, watoto hawatawasikiliza. Mtu kama huyo hawezi kuthubutu kuwaruhusu watoto wake wajue kwamba anawakaribisha ndugu. Watoto au jamaa zake wakijua, hakika watawafukuza ndugu, na mwenyeji hataweza kuwazuia—hana mamlaka nyumbani kwake mwenyewe. Mtu kama huyo hafai kuwa mwenyeji; anaweza kuwa na shauku lakini anakosa ujasiri wa kuwa mwenyeji. Je, mtu mwoga anaweza kuthubutu kweli kuwa mwenyeji? Ikiwa huwezi kuhakikisha usalama wa ndugu, basi hufai kwa wajibu huu—hupaswi kujitolea kuufanya na hupaswi kutoa ahadi tupu kwa viongozi na wafanyakazi, wala hupaswi kuukubali wajibu huu. Viongozi na wafanyakazi wakiwapangia ndugu makazi katika nyumba kama hiyo ili wakaribishwe, je, mnafikiri inafaa? (La.) Haifai kabisa. Msiwapeleke ndugu kwenye meno ya hatari. Inawezekana kuwa ndugu walikuwa salama kabisa wakiishi mahali pengine; ikiwa unawapangia makazi katika nyumba ya mtu huyu, ambapo watoto au jamaa ni wasioamini na wanaweza kuwaripoti na kuwakabidhi kwa polisi punde wanapogundua waumini wanaishi hapo, hivyo kuhatarisha maisha yao, je, si hiyo itakuwa ole kwa mwenyeji huyo? Ikiwa mwenyeji yuko tayari kuhatarisha maisha yake ili kuwalinda ndugu katika hali kama hizo na anaweza kuhakikisha usalama wao kwa ufanisi, na ikiwa kwa kawaida anaonyesha hekima kubwa, basi familia hii ya wenyeji bado inaweza kuwa chaguo linalofaa. Hata hivyo, ikiwa hawezi kuhatarisha maisha yake ili kuwalinda ndugu, na, wasioamini katika familia yake wanapotishia kuwaripoti ndugu na kuwakabidhi kwa polisi, hana suluhisho na anaweza tu kurudi nyuma kama kobe anayeingiza kichwa chake ndani ya ganda lake, bila kuwalinda ndugu na kuwaruhusu tu wasioamini wawakabidhi kwa polisi, basi nyumba hii haifai kwa ajili ya kuwa wenyeji kwa akina ndugu. Ikiwa ndugu wanakaa hapo kwa muda kwa siku chache, na kisha wahame mara moja hadi mahali panapofaa punde panapopatikana, hilo linavumilika kidogo tu. Haifai kukaa kwa muda mrefu katika nyumba kama hiyo ili kutekeleza wajibu wao. Mwenyeji lazima angalau aweze kulinda usalama wa ndugu—hili ni hitaji moja kwa mwenyeji. Kwa wale wanaotekeleza wajibu wao ili kuepuka kuingiliwa na ulimwengu wa nje, kwanza, mazingira yao ya kuishi lazima yawe yanafaa; zaidi ya hayo, sifa za mwenyeji mwenyewe lazima pia ziwe zinafaa katika kila namna—yaani, lazima aweze kuwalinda wafanyakazi muhimu kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje. Ni wanapoweza tu kutimiza hili ndiyo viongozi na wafanyakazi wanaweza kuwapangia wafanyakazi muhimu makazi na maisha katika nyumba yao. Ikiwa mwenyeji ana imani haba na hana uwezo na ni mwoga, asiyeweza kuwa na kauli ya mwisho katika nyumba yake mwenyewe, na mtoto au jamaa yake yeyote asiyeamini anaweza kuingia na kuchukua mamlaka juu yake, basi hili ni tatizo kubwa. Mahali kama hapo hapafai kabisa kwa ajili ya kuwa wenyeji kwa akina ndugu. Hata kama nyumba ni kubwa, yenye vyumba vingi, mazingira ya starehe, na hali nzuri vinginevyo, bado haifai kwa ajili ya kuwa wenyeji kwa ndugu. Mazingira yanayofaa ya kuishi pekee hayatoshi; mwenyeji lazima pia awe anayefaa. Jambo la msingi hapa ni kwamba mwenyeji lazima kwanza aweze kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanaotekeleza wajibu wao ambao yeye ni mwenyeji wao wanalindwa kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje. Hapo tu ndipo mazingira ya kuishi yanapaswa kuzingatiwa. Mazingira duni kidogo bado yanakubalika—iwe ni nafasi ndogo, intaneti finyu, chakula sahili zaidi, au kupatika kwa maji si rahisi sana. Maadamu mwenyeji anafaa, anayeweza kukabiliana na hatari inapotokea, kudhibiti hali mbalimbali tata, na hasa kushughulikia ipasavyo hali zozote maalum zinazoweza kutokea ili kulinda usalama wa ndugu, basi anafikia kiwango kinachostahili kama mwenyeji. Mahitaji yetu kwa mazingira ya kuishi ya familia ya wenyeji si ya juu; jambo muhimu zaidi ni kwamba inaweza kuhakikisha usalama. Hakuna haja ya kuingia kwa undani juu ya hoja hii.
II. Mahitaji ya Mazingira Katika Eneo la Makazi
Kuhusu mazingira ya nje karibu na makazi ya familia ya wenyeji, iwapo ni salama ndilo jambo la kwanza ambalo viongozi na wafanyakazi lazima wazingatie. Bila kujali hali ya familia ya wenyeji au iwapo makazi ni nyumba ya ndugu au nyumba ya kukodi, ni lazima kuzingatia iwapo mazingira ya nje ya makazi ni salama; hili ndilo jambo muhimu zaidi. Kwanza kabisa, inafaa tu ikiwa imani ya familia hii ya wenyeji katika Mungu haijulikani sana na hakuna rekodi kuhusu imani yao katika Ofisi ya Usalama wa Umma. Ikiwa, hapo awali, akina ndugu walipokusanyika hapo, majirani waliripoti hili kwa serikali, na serikali tayari inafahamu kwamba familia hii mara nyingi huwa na mikutano na wageni, basi eneo hili halifai kwa ajili ya kuwa mwenyeji. Ikiwa ni kukodi, pia haifai kukodi nyumba ya familia kama hiyo. Hiki ni kipengele kimoja. Zaidi ya hayo, katika maeneo fulani, usalama wa umma ni duni, kukiwa na matukio ya mara kwa mara ya wizi, mauaji, na visa vingine mbalimbali. Wakazi pia ni watu tata kiasi, na polisi huenda huko mara nyingi kukagua usajili wa kaya na vitambulisho, na kuchunguza washukiwa wa uhalifu, miongoni mwa mambo mengine. Niambieni, kama mngekaa mahali kama hapo, hamngesumbuliwa mara kwa mara? (Ndiyo.) Maeneo kama hayo pia hayafai kwa kuishi. Polisi huja kubisha hodi kila baada ya siku chache, wakisema kwamba kumekuwa na wizi au mauaji karibu na kuomba ushirikiano katika uchunguzi, wakiwaambia watu waripoti mara moja wakimwona mhalifu. Polisi huja kubisha hodi kila mara chini ya kisingizio cha kila aina ya udhuru, wakidai kuwa wanachunguza kesi, lakini kwa uhalisi, wanawachunguza watu wa nje na wageni—kwa usahihi zaidi, wanawatafuta watu wanaomwamini Mungu. Je, utakuwa na hisia yoyote ya usalama ukikaa katika nyumba ya wenyeji kama hiyo? (La.) Bila shaka, utakuwa na wasiwasi mwingi siku nzima. Hata ingawa matukio haya ya uhalifu nje hayahusiani na familia ya wenyeji, bado hutahisi amani. Kuishi katika mazingira kama hayo mara nyingi hukufanya uhisi kwamba usalama wako wa kibinafsi uko hatarini. Huenda siku moja polisi, wanapowaona akina ndugu, wanaweza kuanza kuwahoji wageni hawa, na kuishia kuwakamata. Je, huwezi kusema hii ni hali ya kutisha? (Ndiyo.) Zaidi ya hayo, Wachina wengi wanakosa ufahamu wa usalama; punde wanaposikia mtu akibisha hodi, wanafungua mlango, na pia kwa kawaida hawafungi milango yao, jambo ambalo husababisha matukio kwa urahisi. Katika nchi za Magharibi zenye uhuru na demokrasia, makazi ya kibinafsi yanachukuliwa kuwa miliki za kibinafsi. Mtu wa nje akiingia katika miliki ya kibinafsi bila ruhusa, inachukuliwa kuwa kinyume cha sheria, na watu wanaoishi huko wataita polisi. Mvamizi huyo basi anawajibishwa kisheria. Kwa hivyo, mgeni akibisha hodi, si lazima ufungue mlango—unaweza kukataa. Hata kama mtu amepanga kukutembelea, ikiwa huko tayari au umebadilisha mawazo yako, bado si lazima ufungue mlango; unaweza kupanga naye wakati mwingine. Watu katika nchi za Magharibi wana haki hii, wana ufahamu huu wa kisheria. Hata hivyo, Wachina wanakosa ufahamu huu wa kisheria. Kila wanaposikia hodi mlangoni, wao hukimbia kuufungua. Hili linaonyesha ukosefu wa kuwa macho, ukosefu wa ufahamu wa kujilinda, na kutozifahamu sheria zinazohusika. Ni kwa sababu China ni nchi ya kidikteta, na utawala wa chama kimoja kilichowekwa juu ya sheria, kiasi kwamba mfumo wake wa kisheria ni pambo tu. Joka kubwa jekundu hutenda bila kujali sheria na utaratibu kabisa nchini China, likitenda maovu bila kujali, na watu hawana haki zozote za binadamu. Wachina hawazingatii haki za binadamu, wala hawajakuza hisia ya kufuata kanuni za nidhamu na kutii sheria; hasa, wanakosa ufahamu wa kujilinda, na watu wengi hawajui kutumia sheria kujilinda. Matokeo yake, hakuna hakikisho la usalama. Kwa muhtasari, katika mahali popote penye usalama duni wa umma, wakazi wenye maisha ya nyuma na utambulisho tata, ukaguzi wa mara kwa mara, au matukio ya mara kwa mara ya kesi mbalimbali za uhalifu, ni rahisi kwa watu kuathiriwa na uingiliaji wa ulimwengu wa nje. Mahali kama hapo hapafai kwa kuishi. Hiki ni kipengele cha usalama wa umma cha kuzingatia wakati wa kuwapangia makazi wafanyakazi wa kazi muhimu.
Mazingira ya kuishi kwa wale wanaotekeleza wajibu wao lazima yachaguliwe kwa uangalifu; ni bora kuepuka maeneo ya mijini yenye shughuli nyingi na maeneo ya hatari. Tunarejelea maeneo yapi kama maeneo ya mijini yenye shughuli nyingi? Haya yanajumuisha maeneo kama vile yale yaliyo karibu na reli, barabara kuu, makutano ya barabara, na masoko. Hasa kando ya njia kuu za reli, ambapo treni nyingi hupita kila siku, na sakafu za nyumba zilizo karibu hutetemeka kila treni inapopita. Katika mazingira kama hayo, haiwezekani kabisa kupata amani wakati wa kutekeleza wajibu wa mtu. Zaidi ya hayo, watu wengine ambao wametumia miaka mingi wakitekeleza wajibu wao mbali na nyumbani wanaishi na wasiwasi wa mara kwa mara, na mioyo yao haiko katika hali nzuri, na kuifanya isifae hata zaidi kwao kuishi katika maeneo kama hayo. Ikiwa kazi fulani inahitaji mazingira tulivu, kama vile kazi ya kurekodi au kazi ya maandishi, lazima angalau kusiwe na usumbufu wa kelele, na usalama lazima pia uhakikishwe—hili lingekuwa bora. Ikiwa hakuna mahali salama kabisa, mahali salama kiasi lazima papatikane. Katika hali hii, kelele kidogo inakubalika, na hatupaswi kuweka mahitaji yawe ya juu sana; mradi tu mazingira ya kuishi ni salama, yatatosha. Zaidi ya hayo, ikiwa nyumba iko katika eneo linalopita magari mengi, kama vile karibu na taa zinazongoza magari au makutano ya barabara, kutakuwa na watembea kwa miguu na magari mengi yanayopita kila siku. Nyumba kama hiyo iko wazi kwa mtazamo wa wapita njia wengi, na kwa kutazama tu, watu wanaopita wanaweza kuona kwa urahisi wale walio ndani. Hasa taa zinapowashwa usiku, hali ndani ya nyumba inaonekana wazi. Je, ungesema nyumba kama hiyo bado inakubalika kwa kuishi? Je, mazingira haya yanafaa? (La, hayafai.) Kwa kweli hayafai. Watu wanaokaa mahali kama hapo mara nyingi hupata usumbufu, mara nyingi wakiwaona wageni wakiwatazama. Macho yao yanapokutana na yale ya mgeni, wanashtuka, wakihisi wasiwasi kila siku, wakihisi kila mara wanatazamwa—huenda ikiwa kuna mtu aayefanya hili, anayeelekeza na kudhibiti mambo. Je, unafikiri mtu anaweza kuhisi amani akiishi katika mazingira kama hayo? Pia, nyumba nyingine ni za ubora duni na hazizuii sauti vizuri, kwa hivyo mnapozungumza kwa sauti kubwa au kucheza nyimbo za sifa ndani, watu wa nje wanaweza kusikia kila kitu. Zaidi ya hayo, nyumba zingine ziko katika sehemu ya juu zaidi katika jamii, ambapo mbali na kuwepo kwa uwezekano wa kupigwa na radi kwa urahisi pia huruhusu majirani walio karibu kuwaona akina ndugu wakati wowote wanapotoka nje. Ni vigumu kwao hata kufungua dirisha mara kwa mara ili kupata hewa safi au kupunguza joto; madirisha lazima yabaki yakiwa yamefungwa vizuri na mapazia yakiwa yamefungwa, kwa hivyo hakuna mwanga unaoingia, na kwenda nje kutembea ni vigumu hata zaidi. Kuna wasiwasi daima kuhusu kutazamwa na kutambuliwa na watu wa nje. Ingawa akina ndugu hawaingii na kutoka wote kwa wakati mmoja, kila wakati mtu anapoingia au kutoka, watu wa nje wanaweza kuona wazi. Mwishowe, watakuwa na wazo la jumla kuhusu ni wageni wangapi wanaoishi katika nyumba hii. Je, mnaweza kusema kwamba usalama wa watu bado unaweza kuhakikishwa wakikaa hapa? (La, hauwezi.) Watu wengine wanafikiri, “Wakati mwingi tunatekeleza wajibu wetu ndani ya nyumba, na hata tukienda nje, tunabadilishana na hatutoki wote kwa wakati mmoja. Kwa kutenda kwa njia hii, majirani walio karibu hawatafahamu chochote.” Lakini hata ukibadilishana kwenda nje, bado hili litasababisha shida ikiwa mtu atatambua kwamba wewe ni mgeni. Wasioamini wengi hawaishi maisha mazuri sana wao wenyewe lakini hupata furaha ya kipekee katika kutazama na kuchunguza mambo ya watu wengine. Wengine wanaweza hata kutumia darubini kukupeleleza, wakitazama unachofanya ndani. Wakigundua kwamba waumini wanakusanyika, wanakimbia kuripoti kwa serikali ili wapate zawadi. Punde tu mtu kama huyo anapokukazia macho, je, hii si hali ya hatari? (Ndiyo.) Punde tu anapokukazia macho, kuna chochote kizuri kinachoweza kutokea? Hakika utaishia kukamatwa! Bila kujali nchi au eneo, hakuna uhaba wa watu wanaojishughulisha na mambo ya wengine. Hata kama hawapati senti kwa kukufuatilia, wako radhi kabisa kufanya hivyo—wanaweza hata kulipia wao wao wenyewe na kuchelewesha kazi yao wenyewe ili kutumia muda kukuangalia. Na ikiwa kuna zawadi ya kukuripoti, watakuwa na hamu zaidi ya kufanya hivyo. Hasa katika udikteta kama China, kuna watu wengi sana wanaowafuatilia wale wanaomwamini Mungu. Kwa sababu wanachukia ukweli na kuhisi chuki kuelekea wale wanaomwamini Mungu, punde tu wanapogundua waumini wakiingiliana pamoja au kukusanyika, wanaripoti. Ikiwa kuna zawadi ya kuripoti, wanapata ridhaa isiyochoka katika kufanya hivyo. Je, hili halililetei kanisa taabu kwa urahisi? (Ndiyo.) Ikiwa unaingiliwa kwa njia hii, je, si kwa sababu viongozi na wafanyakazi hawakupanga makazi vizuri? Ikiwa eneo na mazingira ya kuwapangia wafanyakazi wa kazi muhimu hayafai kwa sababu viongozi na wafanyakazi hawakuzingatia mambo kikamilifu, haya ndiyo matokeo yanayotokea. Ikiwa mahali ambapo mtu anaishi panavutia umakini mwingi, hili linaweza kusababisha mambo kwenda mrama kwa urahisi. Punde tu jambo linapokwenda mrama na hapo ndipo unapotambua kwamba mahali hapa hapafai kwa kuishi, tayari ni kuchelewa mno. Kwa hivyo, kuchagua eneo linalofaa la kuishi kwa wale wanaotekeleza wajibu wao pia ni kazi muhimu, na uteuzi mbaya unaweza kusababisha hatari kwa urahisi.
III. Jinsi Viongozi na Wafanyakazi Wanavyopaswa Kufanya Kazi ya Kupanga Nafasi za Wafanyakazi
Kuhusu mazingira ya kuishi ya wafanyakazi wa kazi muhimu, iwe inahusu mazingira ya ndani au ya nje, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuzingatia vipengele vyote kikamilifu. Hawapaswi kuwa na mawazo rahisi, wakidhani kila mara kwamba tusipoingiliana na ulimwengu wa nje, hakuna kitakachotokea. Jamii ya leo ni tata sana, imejaa pepo wa kila aina, na bila kujali mahali, daima kuna watu wanaojishughulisha na mambo ya wengine wanaokutazama, na kuifanya isiwezekane kuepuka uchunguzi wao. Unaweza kufikiri, “Sijavunja sheria yoyote au kufanya chochote kibaya kwa kumwamini Mungu. Ninatimiza tu wajibu wangu; hakuna kinachopaswa kunitendekea, sivyo?” Lakini ukweli wa mambo si rahisi kama unavyowazia. Kwa nini CCP kinatumia nguvu kazi na rasilimali nyingi sana kumpinga Mungu na kulikandamiza kanisa la Mungu? Je, unaweza kuelewa hili? Hutaweza kamwe. Unaweza kung’amua kiini cha maibilisi na Mashetani kwa kiasi gani? Unaelewa kidogo sana kuhusu maibilisi na Mashetani. Jamii hii ni tata sana, na maibilisi na Mashetani ni viumbe duni wanaotenda matendo maovu. Wanachotaka zaidi ni kuwakamata watu wateule wa Mungu na kuvuruga kazi ya kanisa. Ikiwa kila mara unawachukulia Mashetani kama watu wa kawaida tu, basi wewe ni mjinga kweli; inaonyesha kwamba hujang’amua uovu wa jamii hii, na hakika hujaona chuki ya maibilisi na Mashetani. Kwa hivyo, ili viongozi na wafanyakazi wafanye kazi ya kanisa vizuri, lazima wahakikishe usalama wa wale wanaotekeleza wajibu wao—hili ni la umuhimu mkubwa zaidi. Katika nchi iliyo chini ya utawala wa kidikteta, ambapo hakuna uhuru wa imani, kuhakikisha usalama wa wale wanaotekeleza wajibu wao ni jambo gumu kiasi. Hata hivyo, haijalishi ni vigumu kiasi gani, maeneo yanayofaa ya kuishi lazima yachaguliwe kwa uangalifu; hakuwezi kuwa na uzembe katika suala hili. Mipangilio ya kazi ya nyumba ya Mungu imejumuisha ushirika juu ya mambo haya. Lazima viongozi na wafanyakazi wahakikishe kwamba akina ndugu wanaweza kutekeleza wajibu wao bila usumbufu na bila kuingiliwa na ulimwengu wa nje—maadamu wanaiweka mioyo yao katika hilo, wanaweza kutimiza hili. Wasiwasi pekee ni wanapotenda kwa juujuu na bila kuwajibika, wakijali tu usalama wao wenyewe huku wakipuuza usalama wa akina ndugu. Hili linafanya isiwezekane kufanya kazi ya kanisa vizuri. Ikiwa, kwa sababu ya uzembe wako, ukosefu wa umakini, kutowajibika, au kuogopa mazingira na shida, unashindwa kufanya mambo haya, na kusababisha kukamatwa kwa wafanyakazi wanaotekeleza wajibu muhimu na kutishia maisha ya akina ndugu—jambo ambalo huchelewesha kazi ya kanisa na kuwaletea akina ndugu madhara—basi, kama kiongozi au mfanyakazi, unapaswa kubeba jukumu. Jukumu hili haliwezi kutatuliwa tu kwa kutumia pesa fulani kama fidia au kwa kukiri kupitia maombi; si rahisi hivyo. Basi, asili ya jambo hili ni nini? Ni doa lisilofutika, kosa la milele—umeandikiwa dosari. “Dosari” hii haionyeshi kosa la kawaida; machoni pa Mungu, ni makosa. Ikiwa makosa yako ni mengi sana—ukiwa umetenda makosa hapo awali, bado unayatenda leo, na kisha kutenda zaidi katika siku zijazo—pamoja na makosa makuu kadhaa yakiunganishwa, utapata mateso ya milele na maangamizi. Mungu hatakuokoa tena, na imani yako katika Mungu itakuwa imekuwa ya bure. Sio tu kwamba hutakuwa na tumaini la wokovu, bali pia utakabiliwa na adhabu. Kwa hivyo, ni muhimu sana kwamba viongozi na wafanyakazi wafanye kazi yao kulingana na kanuni! Je, mmekariri hili? (Ndiyo.) Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kutimiza majukumu yao, na haijalishi mazingira ni mabaya au ya hatari kiasi gani, lazima wafanye kila linalowezekana kulingana na hali za mahali hapo ili kulinda usalama wa wafanyakazi wa kazi muhimu na kuwapangia makazi ipasavyo. Lengo ni kuhakikisha kwamba kazi ya kanisa inaweza kuendelea kwa kawaida.
Ili viongozi na wafanyakazi wahakikishe kwamba maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya wafanyakazi wa kazi muhimu hayako chini ya kuingiliwa na ulimwengu wa nje, mbali na kuwa na mahitaji na kanuni kwa ajili ya makazi na mazingira yake, pia kuna mahitaji na kanuni kwa ajili ya vipengele mbalimbali vya hali ya familia ya wenyeji. Viongozi na wafanyakazi wanapopata familia ya wenyeji tarajiwa, wanapaswa kwanza kuuliza kuhusu mazingira na hali ya familia hiyo ikoje, hali ya washiriki wake, kama wana migogoro yoyote na wengine, maadui wowote, matatizo yoyote na serikali, kama wanahusika mara kwa mara katika mashtaka, kama wana mahusiano tata ya kijamii, na kadhalika. Hali hizi zote za msingi zinapaswa kuuliziwa na kujulikana kikamilifu. Ikiwa mwenyeji au watoto wake na washiriki wengine wa familia wana mahusiano tata ya kijamii, na familia inakosa amani daima—mara nyingi ikitembelewa na watu wasioeleweka wanaokuja kutafuta matata au kudai madeni, au kupata barua za vitisho kutoka kwa majambazi au wezi, pamoja na wito kutoka kwa serikali au mahakama—haya yote ni mambo ya taabu sana. Kama ungekuwa unakutana au kutekeleza wajibu wako katika nyumba hii, je, haya hayangekuwa usumbufu? Kwa hivyo, unapopata familia hii ya wenyeji, unapaswa kwanza kuuliza maswali na kujua kuhusu hali yao ya msingi. Ni bora ikiwa masuala haya hayapo, lakini yakiwepo na kwa sasa huwezi kupata mahali panapofaa zaidi, basi zingatia kama mwenyeji anaweza kushughulikia matatizo haya kwa ufanisi. Ikiwa mwenyeji hawezi kuyashughulikia kwa ufanisi na hawezi kuondokana na masuala haya ya vurugu, basi nyumba hii haifai kwa ajili ya kuwa wenyeji wa akina ndugu, kwani kuishi hapa kunamaanisha kwamba wanaweza kuteseka wakati wowote kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje na watu, matukio, na vitu vya nje. Mazingira haya hayawalengi moja kwa moja watu wanaomwamini Mungu. Hata hivyo, waumini ni kundi nyeti hasa katika nchi ambapo dini inateswa, na, zaidi ya hayo, baada ya juhudi za serikali za kueneza propaganda, kupotosha akili, kutunga uvumi, na kashfa, wasioamini hawawezi tu kukosa kuwaelewa watu wanaomwamini Mungu bali hata kufikia kuamini maneno ya CCP, wakikuza chuki na uhasama maalum kuelekea waumini. Kwa hivyo, wakigundua kwamba nyumba fulani ni wenyeji wa waumini, inakuwa hatari sana kwa familia ya wenyeji na kwa akina ndugu pia. Akina ndugu wanapoishi katika mazingira kama hayo, sio tu kwamba wanateseka mara kwa mara kutokana na kuingiliwa bali pia usalama wao hauwezi kuhakikishwa. Basi, kwa nini kuendelea kuwaacha waishi huko? Ni wazi kuwa ni mahali pa hatari, pasipofaa kuishi—wanapaswa kuhamishwa haraka. Viongozi na wafanyakazi hawapaswi tu kuwapangia makazi na maisha akina ndugu na kisha kujiondoa katika jambo hilo, wakifikiri, “Maadamu kuna mahali pa wao kula na kulala, pa kujikinga kutokana na hali ya hewa, ni sawa. Maadamu wanaweza kutekeleza wajibu wao, hakuna tatizo. Tutapata wapi maeneo mengi yanayofaa hivyo?” Huku ni kutowajibika sana! Ikiwa hakuna mahali panapofaa wakati huo, wanaweza kukaa huko kwa muda, lakini unapaswa kutafuta mara moja eneo linalofaa la kuwahamishia haraka iwezekanavyo; usipachukulie hapa kama makazi ya muda mrefu.
Viongozi na wafanyakazi wengine hawafanyi kazi halisi. Wanawapangia makazi na maisha wafanyakazi wa kazi muhimu mahali fulani, wanauliza jinsi chakula kilivyo na mahali pa mapumziko yalivyo, na kuuliza kama wasioamini wowote wamekuwa wakiwachunguza. Wanaposikia kwamba hakuna kitu kisicho cha kawaida kilichogunduliwa kwa siku kadhaa, wanaliacha jambo hilo, bila kuwajulia hali tena kwa nusu mwaka au zaidi. Wanaamini kwamba wamewapangia makazi vizuri na kutimiza jukumu lao, wakichukulia kila kitu kimekamilika na kiko sawa. Kuhusu kama mazingira yatapata pigo kwa sababu ya kuingiliwa baadaye au kama kuna hatari zozote za usalama zinazoweza kutokea, hawazingatii zaidi. Je, hili linafaa? (La.) Kwa nini halifai? (Baada ya kuwapangia makazi, viongozi na wafanyakazi wanahitaji kufuatilia. Wasipofanya hivyo, na akina ndugu wajipate katika hali ya hatari na washindwe kuhama, wanaweza kuishia kukamatwa.) Lakini viongozi na wafanyakazi wengine wanafikiri, “Nyote ni watu wazima—je, ninahitaji kweli kufuatilia? Je, huwezi kuona kama kuna hatari? Ikiwa huwezi, basi ubongo wako lazima uwe haufanyi kazi! Ukigundua hatari, hama tu wewe mwenyewe—je, ninahitaji kweli kukuambia?” Wanafikiri kwa namna hii. Je, mnafikiri sababu hii ina maana? (Haina.) Kwa nini haina? (Kwa sababu kuhakikisha usalama wa wale wanaotekeleza wajibu muhimu kimsingi ni jukumu la viongozi na wafanyakazi; ni kazi iliyojumuishwa katika jukumu lao ambayo wanapaswa kuitekeleza.) Hawaoni hili kama sehemu ya kazi ambayo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufanya; wanafikiri ni kusaidia tu akina ndugu, kama kufuata mfano wa Lei Feng wa kufanya mambo mema. Pia hawalichukulii kama linafanywa ili kuitetea kazi ya kanisa, wakiiona badala yake kama mpangilio tu wa makazi kwa ajili ya wafanyakazi, usiohusiana na kazi ya kanisa. Je, hutasema huu ni upumbavu? Ni mtu wa aina gani ambaye angefikiri hivi? (Mtu asiye na hisia ya kuwajibika.) Viongozi hao wa uwongo wavivu, wasio waaminifu, na wasiowajibika hufikiri hivi. Hawaitetei kazi ya nyumba ya Mungu; baada ya kuwapangia mahali akina ndugu, wanafikiri, “Niliwapangia makazi katika eneo zuri sana—ni upendeleo mkubwa ulioje ambao nimewafanyia!” Hawaoni hili kama kuitetea kazi ya kanisa. Kama viongozi na wafanyakazi, msipowapangia makazi ipasavyo wafanyakazi wa kazi muhimu na msipohakikisha usalama wao kwa ufanisi, basi wakikumbana na hatari na wasiweze kutekeleza wajibu wao kama kawaida, je, kazi ya kanisa haitacheleweshwa? Lazima kwanza muwapangie makazi ipasavyo ili usalama wao uhakikishwe, na hapo tu ndipo wanaweza kuendelea kufanya kazi kama kawaida. Lakini viongozi hao wa uwongo hawafikirii hivyo; wanawaacha watu hawa katika sehemu fulani na kisha kuwapuuza, na hawawajulii hali kwa muda mrefu. Hali ya hatari inapotokea na hawawezi kumpata kiongozi wao, hawana budi ila kuhama wao wenyewe. Kufikia wakati kiongozi wao anapogundua na hatimaye kwenda kuangalia, watu wameondoka muda mrefu, na kiongozi hajui walikokwenda. Huyu ni mtu wa aina gani? Huyu ni kiongozi au mfanyakazi wa aina gani? Kiongozi wa uwongo. Hasa kwa akina ndugu ambao wametoka maeneo mengine na hawajazoea mazingira ya huko, viongozi na wafanyakazi wanahitaji hata zaidi kuwatembelea na kuwafuatilia mara kwa mara. Viongozi na wafanyakazi hawapaswi kudhani kwamba kuwapangia tu makazi mara moja kunatatua kila kitu kabisa; kwa uhalisi, kazi hii haijakamilika hata kidogo. Wanahitaji kuwatembelea na kuwafuatilia mara kwa mara. Ikiwa haifai kwa viongozi na wafanyakazi kuonekana katika eneo hilo, wanapaswa kuwaagiza wengine kuwajulia hali. Angalau, wanahitaji kufuatilia kazi hii—kutathmini mazingira ya kuishi ya wafanyakazi hawa wa kazi muhimu, wakiangalia kama kuna hatari yoyote au kitu chochote kisicho cha kawaida, au kama hali zozote maalum zimetokea, na kama kuhama kunahitajika. Haya yote lazima yajulikane na kufuatiliwa. Ikiwa, kwa muda mfupi, mahali hapa panaonekana kuwa panapofaa zaidi, hiyo ni sawa, lakini baada ya muda, wanapaswa kurudi kuangalia mazingira na usalama wao, na kama wana chakula na vifaa vya kutosha—maelezo haya yote yanapaswa kuuliziwa. Inawezekana kwamba viongozi na wafanyakazi huenda wasielewe kazi ya wafanyakazi wa kazi muhimu, ambapo hawapaswi kuingilia kipengele hicho, lakini kuwapangia makazi ipasavyo ni jukumu la viongozi na wafanyakazi—kushindwa kufanya hivyo ni kupuuza jukumu lao na kunaonyesha kwamba wao ni viongozi wa uwongo wasiofanya kazi halisi. Hasa kwa akina ndugu wanaotoka maeneo mengine, wanahitaji hata zaidi umakini wa ziada, wa karibu na hawapaswi kuchukuliwa kwa uzembe. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuwajulia hali mara kwa mara, wakiona kama wana matatizo yoyote yanayohitaji kutatuliwa, na kama kumekuwa na masuala yoyote au hali maalum katika mazingira wanapofanyia wajibu wao wakati huu, kwa mfano, kama kumekuwa na shughuli yoyote isiyo ya kawaida inayohusisha serikali ya mtaa, kamati ya mtaa, au kituo cha polisi. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuuliza na kuuliza kuhusu mambo haya ili waweze kuwa na habari za kutosha. Kisha, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kushiriki na mwenyeji juu ya kanuni na njia za utendaji za kuwakaribisha na kuwalinda ipasavyo wale wanaotekeleza wajibu wao, ili mwenyeji aelewe kikamilifu kanuni na njia hizi za utendaji. Huu bado si mwisho wa jambo hilo. Viongozi na wafanyakazi lazima pia watembelee na kuuliza kuhusu hali ya familia ya wenyeji mara kwa mara. Masuala yoyote wanayoyagundua yanapaswa kutatuliwa mara moja ili kuhakikisha kwamba hakuna matatizo yanayotokea. Hapo tu ndipo kazi inafanywa vizuri kweli. Mwenyeji akikumbana na matatizo ya kuwa mwenyeji, kama vile uwezo mdogo wa kifedha au ukosefu wa hekima unaomfanya ashindwe kuitikia au kushughulikia hali zinazotokea, basi viongozi na wafanyakazi lazima wasaidie kutatua masuala haya. Uwezo mdogo wa kifedha ni rahisi kutatua—nyumba ya Mungu inaweza kutoa fedha kwa ajili ya kuwa wenyeji, huku familia ya wenyeji ikihitaji tu kutoa nguvu kazi. Mwenyeji akikosa hekima, hili ni suala kubwa. Viongozi na wafanyakazi lazima waeleze wazi hekima inayohitajika na kanuni chache za utendaji kuhusu eneo hili. Ikiwa mwenyeji bado anapungukiwa, basi viongozi na wafanyakazi wanapaswa kutafuta ndugu mwenye hekima aliye karibu ili kushirikiana na mwenyeji katika kutekeleza kazi hii vizuri. Ikiwa suala liko upande wa mwenyeji mwenyewe—kama vile kuwa mwoga au kuogopa kukamatwa—basi viongozi na wafanyakazi wanapaswa kushiriki juu ya ukweli ili kutoa msaada na usaidizi, wakishiriki nia za Mungu pamoja na thamani na umuhimu wa kutekeleza wajibu huu. Ikiwa ni suala la mazingira halisi, halipaswi kucheleweshwa au kukubaliwa tu, na hakika halipaswi kuchukuliwa kwa uzembe; linapaswa kutatuliwa mara moja. Kwa mfano, ikiwa watu tayari wamegundua mahali hapa, wageni wanaoshukiwa mara nyingi huingia na kutoka katika eneo hilo, na inawezekana mtu anafuatilia eneo hilo, basi hili linasababisha hatari iliyofichika. Basi, wahamishe akina ndugu mara moja—kungoja hadi jambo liende mrama itakuwa kuchelewa mno. Ikiwa hali ni ya muda mfupi tu na ni utaratibu tu wa kawaida, wa kila siku, basi inaweza kuvumiliwa kwa shida: Waagize akina ndugu waondoke kwa muda ili kuiepuka kwa siku moja au mbili, na wanaweza kurudi baadaye. Ikiwa watu tayari wamegundua, basi kukaa huko si chaguo tena, na uhamisho wa kudumu unahitajika. Haya ni baadhi ya masuala ya kina ambayo viongozi na wafanyakazi wanahitaji kushughulikia na kutatua katika kazi hii. Kazi hii si tu kuwaweka watu wachache katika eneo lenye chakula na makazi na kusema imekamilika; kuna maelezo mengi yanayohusika. Hasa katika nchi kama China, ambapo mazingira ni ya uhasama hasa na mateso ya kidini ni makali, viongozi na wafanyakazi lazima hata zaidi wawe makini sana na kufuatilia kwa karibu mazingira ya kuishi na masuala ya usalama ya wafanyakazi wa kazi muhimu. Hawawezi kuwa wazembe. Vipengele vyote vya kazi mahususi lazima vifanywe vizuri ili kuhakikisha kwamba usalama wa wa wafanyakazi hawa wa kazi muhimu unahakikishwa na wanaweza kutekeleza wajibu wao kwa amani ya akili. Kwa njia hii, kazi inafanywa vizuri. Hii ndiyo kazi ambayo viongozi na wafanyakazi lazima wafanye kuhusu familia za wenyeji, na kuna maelezo mengi kiasi yanayohusika hapa.
Viongozi na wafanyakazi wengine, baada ya kuwapangia makazi wafanyakazi wa kazi muhimu katika familia za wenyeji zinazofaa, wanawapuuza kabisa na hawafuatilii hali ya familia za wenyeji mara kwa mara. Wanasema, “Mimi huwa na shughuli nyingi na kazi ya kanisa kila siku—ningepata wapi muda wa kuwatembelea watu hawa? Isitoshe, kuna kazi nyingine nyingi, na pia ni hatari sana. Kufanya kazi yetu si rahisi!” Wanasisitiza daima sababu za kisingizio, lakini hawataki kutimiza wajibu wao wenyewe. Mnaonaje—je, kauli yao hii inaleta maana? (La.) Kwa nini? (Kwa kweli, kufanya kazi hii hakuhitaji muda na nguvu nyingi sana za viongozi na wafanyakazi. Wanaweza kuwatembelea kwa kupita tu wakiwa nje. Na ikiwa hawana muda, wanaweza pia kupanga ndugu wa karibu waende kuwatembelea.) Ikiwa viongozi na wafanyakazi wanataka kufanya kazi hii vizuri, hata kama kazi yao ya msingi inawafanya wawe na shughuli nyingi kiasi, bado watatenga muda wa kuangazia kazi hii. Ikiwa hawana muda wa kwenda wao wenyewe, wanaweza kupanga wengine waende. Iwe wanapanga wengine au wanaenda wao wenyewe, hatimaye, kazi hii imo ndani ya upeo wa wajibu wa viongozi na wafanyakazi. Kufanya kazi hii vizuri ni jukumu muhimu kwa viongozi na wafanyakazi, na haiwezi kupuuzwa. Ikiwa viongozi na wafanyakazi wana shughuli nyingi sana na hawana muda wao wenyewe, na pia hawawapangi wengine waende, basi hakuna atakayeshughulikia jambo hili. Jambo fulani likienda mrama, huku kutakuwa kupuuza jukumu kwa upande wa viongozi na wafanyakazi. Ili kuzuia wale wanaotekeleza wajibu muhimu wasiteseke kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje, viongozi na wafanyakazi lazima wazingatie vipengele vyote vya masuala, wakihakikisha kwa kiwango kikubwa zaidi iwezekanavyo kwamba wanaweza kutekeleza wajibu wao kwa amani na kutekeleza kazi iliyo mikononi mwao kwa utaratibu. Ikiwa wafanyakazi wa kazi muhimu wamelindwa vizuri, ni sawa na kulinda kazi muhimu yenyewe. Wafanyakazi wa kazi muhimu wanapoweza kufanya kazi kama kawaida, kazi muhimu inaweza pia kuendelea kwa utaratibu. Kwa hivyo, lengo la viongozi na wafanyakazi kulinda wafanyakazi wa kazi muhimu ni, kwa kweli, kulinda kila kipengele muhimu cha kazi. Viongozi na wafanyakazi wengine husema, “Unatekeleza wajibu muhimu na ninaombwa kukulinda, lakini niko katika nafasi ya uongozi, na siko salama pia. Siwezi hata kuhakikisha usalama wangu mwenyewe, kwa hivyo ninawezaje kuwalinda?”—je, kauli hii ni sahihi? (Si sahihi.) Viongozi na wafanyakazi kama hao wana ufahamu wa aina gani? (Ufahamu wao ni duni; watu kama hao ni wabinafsi na wenye kuelekea upotovu.) Wao ni watu wenye kuelekea upotovu. Je, watu wenye kuelekea upotovu wanakosa urazini? (Ndiyo.) Kama ndugu hawa hawangekuwa wakitekeleza wajibu wao katika nyumba ya Mungu bali badala yake wawe walikuwa wanafanya kazi za kuajiriwa na kuishi maisha yao ulimwenguni, je, bado wangehitaji kulindwa? Hasa kwa sababu wanafanya kazi ya kanisa na wajibu muhimu katika nyumba ya Mungu, na kwa sababu wakikamatwa wanaweza kuhukumiwa kifungo gerezani au kupigwa hadi kujeruhiwa au kupata ulemavu, kukiathiri sana kazi ya kanisa, wafanyakazi wa kazi muhimu lazima walindwe vizuri. Ni kwa njia hii tu ndiyo kazi ya kanisa inaweza kuendelea kwa utaratibu. Ikiwa wako katika nchi fulani za kidemokrasia ambapo kuna uhuru wa imani ya kidini na waumini katika Mungu hawateswi, basi kazi hii inakuwa rahisi kwa viongozi na wafanyakazi. Kimsingi wanahitaji tu kupata nyumba inayofaa na, kulingana na sheria na kanuni za mahali hapo, kuwapangia makazi ipasavyo wale wanaotekeleza wajibu wao. Kwa kiwango cha juu kabisa, wanahitaji tu kuuliza jinsi mambo yanavyoendelea katika maisha yao ya kila siku hivi karibuni na kama mazingira ya kuishi yanakiuka kanuni zozote za serikali. Ikiwa kuna ukiukaji, ni lazima kufafanua suala ni nini, pamoja na jinsi linavyopaswa kurekebishwa na kutatuliwa. Ikiwa hakuna ukiukaji wowote, lakini serikali inasababisha shida, au watu waovu au watu wasiojulikana wanasababisha unyanyasaji, basi ni muhimu kushauriana na wakili ili kushughulikia mambo haya ipasavyo. Katika baadhi ya nchi huru, za kidemokrasia, kwa juu zaidi ni kazi ya aina hii tu inayohitajika. Hata hivyo, katika udikteta ambapo hakuna uhuru wa imani ya kidini, mahitaji kwa ajili ya mazingira na hali ya familia za wenyeji lazima yawe makali zaidi, na kazi zaidi—pamoja na kazi ya kina zaidi—inahitaji kufanywa kuhusiana na usalama. Bila shaka, ugumu unaohusika katika kazi kama hiyo pia ni mkubwa zaidi. Kwa ajili ya kazi ya kuwalinda wafanyakazi wa kazi muhimu kutokana na kuingiliwa na ulimwengu wa nje, ikiwa kila kipengele cha mazingira kinazingatiwa kikamilifu, kuingiliwa kunakotokana na mazingira kutapunguzwa kiasi. Ikiwa mazingira ya nje na mazingira ya ndani yanazingatiwa kikamilifu, basi njia yenye uhalisi na inayowezekana inaweza kupatikana. Kwa njia hii, mazingira yanaweza kuboreshwa kwa kiwango fulani, na kuingiliwa kunaweza kupunguzwa. Mbinu hii inafaa kiasi.
Kuweka Usalama wa Wafanyakazi Muhimu
I. Jinsi ya Kuhakikisha Usalama wa Watu Wateule wa Mungu Katika Nchi Ambazo Imani Inateswa
Jukumu la kumi na tano la viongozi na wafanyakazi ni, kwanza kabisa, kuwalinda wafanyakazi muhimu kwa kuwakinga dhidi ya uingiliaji wa ulimwengu wa nje; zaidi ya hayo, viongozi na wafanyakazi lazima pia waweke usalama kwa ajili ya watu hawa. Mahitaji ya kuwaweka salama ni makali hata zaidi. Hebu kwanza tuangalie ni vipengele vipi vinavyohusisha usalama—ni masuala gani yanayohusiana na usalama mnayoweza kufikiria? Ili kuhakikisha usalama wa wale wanaofanyaa wajibu muhimu, ni muhimu kwanza kuhakikisha kwamba hawaathiriwi na uingiliaji wa ulimwengu wa nje—hiki ndicho kiwango cha chini kabisa ambacho ni lazima kifikiwe, na ni kwa msingi huu tu ndiyo usalama wao unaweza kuhakikishwa hatimaye. Usalama tunaouzungumzia hapa unamaanisha tu kuweza kuhakikisha kwamba wale wanaofanya wajibu wao hawasumbuliwi wala hawakamatwi na wanaweza kufanya wajibu wao kwa kawaida. Ni rahisi hivyo tu. Ikiwa viongozi na wafanyakazi hawawezi kuhakikisha kwamba wale wanaofanya wajibu wao watakingwa dhidi ya uingiliaji na ukamataji, basi hakuna njia ya kuhakikisha usalama wao. Fikiria kuhusu hili—viongozi na wafanyakazi wanapaswa kutilia maanani kitu gani ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa kazi muhimu? Kwanza, lazima wapange ili wafanyakazi wa kazi muhimu wawekwe katika eneo linalofaa. Eneo linalofaa linamaanisha nini? Lazima litimize angalau masharti mawili. Kwanza, eneo hili lazima lisiwe na usumbufu wowote kutoka kwa mazingira. Pili, lazima lisivutie uangalifu; ni akina ndugu wachache tu wa eneo hilo wanaojua kwamba familia hii inamwamini Mungu na inakuwa mwenyeji wa wengine, huku hakuna mtu mwingine anayejua. Ni mahali kama hapo tu ndipo panapofaa kwa kuwa wenyeji wa wale wanaofanya wajibu muhimu. Baada ya wafanyakazi hawa wa kazi muhimu kuhamia hapo, taarifa za kibinafsi kama vile jina la kila mtu na mahali anapotoka, pamoja na hali mahususi kama vile aina ya kazi ya kanisa anayojihusisha nayo na iwapo amewahi kukamatwa hapo awali au anasakwa na serikali, hazipaswi kufichuliwa kwa wengine kiholela. Kadiri watu wanaojua wanavyokuwa wachache zaidi, ndivyo inavyokuwa bora zaidi. Kwa sababu kimo cha watu ni kidogo sana na haijulikani iwapo wangeweza kusimama imara ikiwa wangekamatwa na kufungwa gerezani, wanapaswa kujitambua na kujizuia kuulizia kiholela kuhusu taarifa za kibinafsi za akina ndugu, ili kuepuka kujiletea shida za baadaye. Kanuni na hekima katika suala hili zinapaswa kufanyiwa ushirika mara kwa mara ili kila mtu azielewe. Mbali na hili kuwa na manufaa kwa kazi ya nyumba ya Mungu pia lina manufaa kwa kila mtu binafsi. Kwa hivyo, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuwaagiza akina ndugu wa familia za wenyeji wachunge ndimi zao na wasifichue taarifa za kibinafsi za wale wanaofanya wajibu muhimu kwa akina ndugu wengine au kwa wanafamilia wao wasio na dini. Je, ni lazima kufanya kazi hii? (Ndiyo.) Baadhi ya akina ndugu wa familia za wenyeji hawawezi kuchunga ndimi zao. Kwa mfano, mtu fulani alikuwa mwenyeji wa viongozi na wafanyakazi wachache, na akafahamu hali za kibinafsi za watu hawa, historia za familia zao, na wajibu waliokuwa wakifanya. Kisha, akawaambia watoto wake, “Tazama, yeye ana umri sawa na wewe. Amemwamini Mungu kwa miaka kumi na hata aliacha kazi yake ili afanye wajibu wake. Alikuwa akifanya kazi katika idara ya serikali katika jiji fulani, akiwa na mapato ya kila mwaka ya makumi ya maelfu ya yuani!” Unaona, kana kwamba alikuwa akipiga gumzo tu, alifichua hali ya watu hawa wanaofanya wajibu muhimu kwa wanafamilia wake wasio na dini. Kuna hata baadhi ambao, wanapokuwa wenyeji wa akina ndugu ambao wamewahi kukamatwa na kufungwa gerezani hapo awali, wao huwaambia wanafamilia wao, “Tazama, walikuwa gerezani kwa miaka na hawakuwahi kugeuka kuwa Yuda. Baada ya kuachiliwa, wanaendelea kutekeleza wajibu wao. Sasa serikali inataka kuwakamata tena, kwa hivyo hawawezi kwenda nyumbani kuungana tena na familia zao, lakini wao si hasi. Unaona jinsi imani yao ilivyo kuu? Kwa nini wewe huwezi kuamini ipasavyo?” Kwa njia hii, wanafichua kiholela taarifa muhimu kuhusu akina ndugu kupitia mbinu ya kuwafundisha watoto wao. Je, hili linaweza kusababisha shida za baadaye? (Ndiyo.) Je, hili ni tatizo? (Ndiyo.) Kitu kisipotendeka kwa sababu ya hili, ni sawa; lakini punde tu joka kubwa jekundu linapofanya ukamataji, wanafamilia wao wasio na dini ndio wa kwanza kujitokeza na kuwaripoti akina ndugu: “Afisa! Fulani ni kiongozi—yeye ndiye unayemtaka.” Mtu aliyesalitiwa kisha anakamatwa na joka kubwa jekundu na kupigwa karibu kufa, na kuacha maswali kuhusu iwapo ataweza kuendelea kufanya wajibu wake au kuishi maisha ya kawaida. Haya ni matokeo ya usaliti. Je, hili halisababishwi na usemi wa kiholela wa mwenyeji? (Ndiyo.) Ikiwa wafanyakazi wa kazi muhimu wanakabiliwa na hatari kama hizo za usalama, je, hiyo haimaanishi kwamba viongozi na wafanyakazi hawajafanya kazi zao kikamilifu? (Ndiyo.) Mwenyeji anawaza, “Wanafamilia wetu wote ni watu wazuri; hawatawasaliti. Wanaunga mkono imani kwa Mungu—hata wananunua mboga na nyama mnapokuja!” Wanawatendea wanafamilia wao wasio na dini kana kwamba ni akina ndugu, wakishindwa kuona wazi kile ambacho familia yao inaweza kufanya au jinsi matokeo yangekuwa mabaya sana ikiwa wangewasaliti akina ndugu. Pia ni wadadisi sana kuhusu hali za akina ndugu, wakiuliza, “Umekuwa ukifanya wajibu huu kwa miaka mingapi? Umewahi kutekeleza wajibu wowote wa hatari? Je, wewe unajulikana sana hapa kama muumini wa Mungu? Umewahi kukamatwa?” Hasa linapokuja suala la wale wanaosakwa au walio na rekodi ya polisi kwa sababu ya imani yao katika Mungu na wanahubiri injili katika eneo au nchi nyingine, mwenyeji daima huulizia kuhusu habari zao, akiuliza, “Unasakwa? Je, ni hati ya kukamatwa ya eneo hili, hati ya mkoa, au hati ya kitaifa?” “Una rekodi—je, umekamatwa mara ngapi? Ulihukumiwa kifungo cha miaka mingapi gerezani?” Anauliza kuhusu mambo haya kwa maelezo ya kina sana. Akina ndugu wanaokaa nyumbani kwa wenyeji wanaona kwamba wao ni wenye shauku sana katika kuwa wenyeji na kwamba wao si watu wabaya. Wasiposhiriki nao taarifa hizi, wanahisi inaweza kuonekana kama ukosefu wa adabu, jambo ambalo linawaweka katika hali ngumu. Watu wengine huhisi kulazimika waseme mambo machache, na baada ya kuzungumza, wakati mwingine bila shaka husababisha matokeo mabaya sana. Kwa hivyo, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kumwagiza mwenyeji moja kwa moja: “Kuna masharti machache unayopaswa kufuata unapokuwa mwenyeji wa akina ndugu. Usidadisi wala kuuliza maswali kiholela—kujua mengi sana kuwahusu hakutakufaidi. Ikiwa jambo fulani litatokea na huwezi kustahimili mateso, unaweza kuishia kugeuka kuwa Yuda. Katika hali hiyo, taarifa ulizopata na kufahamu kimsingi zinakuandalia njia ya kuwa Yuda. Hilo likitokea, litakuacha na majuto ya maisha yako yote, na hatimaye utakabiliwa na adhabu. Ikiwa hujui maelezo haya, hutakuwa Yuda. Kwa hivyo, hupaswi kabisa kuulizia au kujaribu kujua kuhusu mambo haya. Kutojua kunakulinda na hakuathiri wewe kuwa mwenyeji au kupata kwako ukweli katika imani yako katika Mungu. Ni bora ikiwa hujui. Unaelewa wazi kwamba akina ndugu hawa wako hapa kufanya wajibu wao na kwamba wao si watu wabaya au watu waovu, kwa hivyo hakuna haja ya kuulizia zaidi. Kutimiza wajibu wako wa kuwa mwenyeji wao ndilo jambo muhimu kabisa, na kuhakikisha usalama wao kunatosha.” Hiki ni kipengele cha kazi ambacho viongozi na wafanyakazi lazima wafanye. Zaidi ya hayo, wale waumini wa eneo hilo ambao hawana msingi katika imani yao na ni waumini kwa jina tu, wale ambao hawawezi kuchunga ndimi zao na wana mwelekeo wa kuulizia mambo, wale wanaodumisha uhusiano wa karibu na wafanyakazi wa serikali, na wale ambao hujificha mara moja kama kobe wanaoingiza vichwa vyao ndani ya maganda yao shida inapotokea—na ambao wanaweza hata kulisaliti kanisa na kugeuka kuwa Yuda—hawapaswi kuruhusiwa kabisa kujua kwamba familia za wenyeji zinakuwa wenyeji wa akina ndugu. Ikiwa baadhi ya akina ndugu na dada wanahitajika kusaidia katika kazi ya kuwa wenyeji wa wafanyakazi wa kazi muhimu, basi ni wale tu walio na msingi katika imani yao katika Mungu na walio na hekima ndio wanaopaswa kuchaguliwa ili kushirikiana. Wale wasio na msingi wala hekima hawafai kabisa. Kwa hivyo usaidizi unapaswa kutolewaje hasa? Akina ndugu na dada wa familia za wenyeji wanazingatia kuwa wenyeji katika nyumba zao, huku akina ndugu na dada wa eneo hilo walio na hekima na imani wakisaidia kutoka nje kwa kutoa ulinzi na kulinda mazingira. Wanapaswa kushirikiana na watu wenye ushawishi, kufuatilia sera za serikali, mienendo, na operesheni zinazoweza kutokea, na wawajulishe mara moja akina ndugu na dada wa familia za wenyeji. Kwa njia hii, serikali ikianzisha operesheni zozote za ukamataji, hatua za kuzuia zinaweza kuchukuliwa mara moja, na bado kutakuwa na muda wa kuondoka na kuhamishwa, au kujificha, na hivyo kuepuka hatari yoyote. Ni kwa njia hii tu ndiyo usalama wa wale wanaofanya wajibu muhimu unaweza kuhakikishwa kimsingi. Kwa ufupi, si sawa kwa viongozi na wafanyakazi kushughulikia kazi hii kwa mtazamo rahisi; kufikiri kwa namna tata katika suala hili daima ni bora kuliko kufikiri kwa urahisi, kwa sababu masuala ya usalama hayawezi kupuuzwa—jambo likienda mrama, halitakuwa suala dogo!
Pia kuna hali mahususi za kutilia maanani katika kazi ya kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa kazi muhimu. Watu wengine huchukua wajibu wa hatari, kama vile kusafirisha vitabu vya maneno ya Mungu, au, katika maeneo yenye hatari, kufikisha maagizo ya kazi au kushughulikia hali baada ya tukio. Wale wanaofanya kazi hiyo ya hatari hawapaswi kamwe kuishi na wale wanaofanya wajibu muhimu, wala hawapaswi kujua mahali ambako watu hao wanaishi au ni familia gani inayokuwa mwenyeji wao. Hii ni kwa sababu wale wanaofanya kazi ya hatari wako katika hatari ya kufuatiliwa na kukamatwa wakati wowote. Wakikamatwa na kuteswa, wanaweza kulisaliti kanisa, jambo ambalo kwa sababu hiyo linaweza kuwahusisha wale wanaofanya wajibu muhimu na familia za wenyeji. Je, hili halihusishi suala la usalama? Ikiwa baadhi ya wafanyakazi wanaofanya wajibu muhimu watatoka nje kushughulikia mambo na wamekubaliana kurudi baada ya siku tatu, lakini hawajarudi baada ya siku tatu, je, mnaweza kusema hali hii ni ya hatari? Je, wafanyakazi wengine wanaofanya wajibu wao wanapaswa kuondoka? (Ndiyo.) Katika hali kama hizo, kuondoka mara moja ni muhimu; lazima kusiwe na ucheleweshaji na wasiingie katika hatari yoyote—hawawezi kuwa na mtazamo wa kutegemea bahati. Watu wengine ni wavivu, wanahisi kwamba hili linasumbua, na wanasita kuondoka, wakisema, “Kuna madhara gani kusubiri siku moja zaidi? Pengine walicheleweshwa tu na hali fulani maalum.” Kusubiri siku moja zaidi kunaongeza tu hatari. Ukiondoka na chochote kisitokee, unaweza kurudi wakati wowote, na hilo halitakuwa kosa. Lakini usipoondoka na usubiri siku moja zaidi, tukio linaweza kutokea, na wakati linapotokea, utajuta wakati ambapo itakuwa imechelewa mno. Kwa hivyo, ikiwa akina ndugu na dada waliotoka nje kushughulikia mambo hawatarudi ndani ya muda uliokubaliwa, inawezekana kwamba jambo fulani lilienda mrama. Ili kujilinda dhidi ya tukio lolote, akina ndugu na dada wanaohusika wanapaswa kuondoka mara moja na wahamie mahali salama kiasi. Punde tu eneo linalofaa linapopatikana, wanaweza kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa kawaida, bila kuchelewa mno. Hali nyingine ni wakati mtu katika kanisa la eneo hilo ambaye anahusika na kazi ya kuwapangia makazi akina ndugu na dada wanaofanya wajibu wao anakamatwa na joka kubwa jekundu. Ni kitu gani kinachopaswa kufanywa katika hali kama hizo? (Kuwahamisha wafanyakazi wa kazi muhimu mara moja.) Kipaumbele cha kwanza kwa viongozi na wafanyakazi ni kuwahamisha wafanyakazi hawa wa kazi muhimu mara moja hadi mahali salama kiasi. Zaidi ya yote, usalama wao lazima uhakikishwe. Hawapaswi kuwekwa katika hatari yoyote. Baada ya kuwahamisha, ndipo kazi inayofuata inaweza kutekelezwa. Baadhi ya watu waliokanganyika vichwa daima wana mtazamo wa kutegemea bahati: “Fulani alikamatwa, lakini ni sawa; imani yake ni thabiti sana, na amekuwa imara hasa katika hali ngumu. Yeye hawezi kujihusisha na usaliti kamwe. Kwa hivyo, ninaweza kuhakikisha hakuna hatari kabisa—hakuna haja ya mtu yeyote kuhamishwa.” Je, maneno haya ni sahihi? (La.) Pia kuna watu wanaosema, “Hata akijihusisha na usaliti, atachagua mambo ya kusema—atasaliti tu taarifa kuhusu mambo yasiyo muhimu, jambo ambalo hakika halitaathiri usalama wenu.” Je, maneno haya ni sahihi? (La.) Maneno haya hayana msingi! Je, watu wanaweza kuwang’amua watu wengine waziwazi? Hata kama mtu huyo ana kimo, tunapaswa kuepuka kuzungumza kwa ujasiri kupita kiasi, kwa kuwa hakuna anayeweza kustahimili matokeo jambo fulani likienda mrama. Ni kazi gani nyingine inayohitajika ili kulinda usalama wa wafanyakazi wanaofanya wajibu muhimu? Wanapoanza wajibu wao, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufanya ushirika waziwazi kuhusu kanuni za ukweli zinazohusiana na kufanya wajibu wao, pamoja na ni kanuni na hekima gani za kutumia hali zinapotokea. Zaidi ya hayo, wanapotoka nje kufanya wajibu wao, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuwapangia mtu mmoja au wawili walio na uzoefu wa kijamii na hekima ili kushirikiana nao. Ni mbinu hii tu ndiyo iliyo salama na ya kutegemewa. Kutenda kwa njia hii kunaweza, kwa upande mmoja, kulinda usalama wao wa kibinafsi. Kwa upande mwingine, kunaweza kuwasaidia kutatua baadhi ya masuala ambayo hawawezi kuyatatua wenyewe. Hili litazuia matatizo fulani na kuhakikisha kwamba wale wanaotoka nje kutekeleza wajibu wao wanaweza kufanya kazi yao kwa kawaida. Kwa viongozi na wafanyakazi, kuhakikisha usalama wa wale wanaofanya wajibu wao ni kipengele muhimu sana cha kazi, hasa katika nchi zisizo na uhuru wa imani. Ili kufanya kazi ya kanisa vizuri, kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wanaofanya wajibu wao, bila kujali kama wanafanya wajibu wao katika eneo hilo au wanatoka nje kuufanya. Ni viongozi na wafanyakazi tu wanaoweza kushughulikia kazi ya usalama vizuri ndio wanaofaa kutumiwa na Mungu. Wale wasioweza kufanya kazi hii ni watu ambao ubinadamu wao haujakomaa, na wasio na umaizi na hekima. Itakuwa vigumu kwao kuwa wanaofaa kutumiwa na Mungu.
II. Jinsi ya Kuhakikisha Usalama wa Watu Wateule wa Mungu Katika Nchi Mbalimbali Ng’ambo
A. Kushughulikia Hali za Kisheria za Watu Wateule wa Mungu
Katika kuendesha kazi ya kanisa katika nchi mbalimbali ng’ambo, kipaumbele cha kwanza kinapaswa kuwa kuwapangia makazi ipasavyo wafanyakazi wanaofanya wajibu wao, kuhakikisha usalama wao ili waweze kufanya wajibu wao kwa kawaida. Jambo lingine muhimu ni kushughulikia suala la hali ya kisheria, ambalo lazima lishughulikiwe punde tu watu wateule wa Mungu wanapowasili katika nchi mpya. Bila hali ya kisheria au ikiwa hali yao si halali, daima kuna hatari ya kufukuzwa nchini, bila kujali mazingira yao ya kuishi yanaweza kuwa mazuri kiasi gani. Watu ambao hali yao si halali wanachukuliwa kuwa wakaazi haramu, na usalama wa watu hawa uko hatarini; kama usalama wao haujahakikishwa, hawawezi kufanya wajibu wao kwa muda mrefu. Kwa hivyo, katika nchi za ng’ambo, kuwapangia makazi ipasavyo wafanyakazi wanaofanya wajibu wao ndiyo kazi ya kwanza kwa viongozi na wafanyakazi. Punde tu makazi yao yanapopangwa ipasavyo, hatua inayofuata ni kuwapangia waanze kushughulikia hali yao ya kisheria. Katika nchi yoyote, angalau, lengo la kushughulikia hali ya kisheria linapaswa kuwa kuwawezesha akina ndugu na dada kuishi huko kisheria. Hiki pia ni kipengele muhimu cha kazi katika kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa kazi muhimu. Ili kufikia ukaaji kulingana na sheria, hitaji la kwanza ni kwamba hali ya mtu lazima iwe halali; hawezi kuwa anaishi mahali fulani kinyume cha sheria. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufanya kadiri iwezekanavyo kuwapangia makazi akina ndugu na dada kulingana na kanuni za serikali za ukaaji kulingana na sheria. Viongozi na wafanyakazi wanaweza kuhusika moja kwa moja katika kazi hii ya kupanga makazi au kuifuatilia. Ikiwa kuna mambo ambayo hawawezi kuyang’amua, wanapaswa kutafuta ushauri mara moja kutoka kwa viongozi na wafanyakazi wa ngazi za juu. Pasipokuwa na hali maalum, wanapaswa kutenda kulingana na sheria za awali za kanisa. Viongozi na wafanyakazi wanahitaji kuulizia mara kwa mara, na wakigundua kwamba mtu fulani ana matatizo na hali yake ya kisheria au hali yoyote maalum, wanapaswa kuwapangia wafanyakazi wanaoshughulikia mambo ya nje kutatua masuala ya ushughulikiaji wa hali ya kisheria ya watu wateule wa Mungu. Bila shaka, hatua ya kwanza ni kutafuta mawakili wachache waliobobea ili washughulikie mchakato wa kupata hali ya kisheria. Katika kuajiri mawakili, tahadhari lazima zichukuliwe ili kuepuka kudanganywa—mawakili wa uongo au wale ambao hawajabobea katika kushughulikia hali ya kisheria hawapaswi kuajiriwa. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kwanza kabisa kuzingatia vipengele hivi vinavyohusiana na ushughulikiaji wa hali ya kisheria, na mambo haya lazima yapangwe vizuri. Kazi hii pia ni sehemu ya kuwalinda wafanyakazi wa kazi muhimu na kuhakikisha usalama wao, kwa hivyo linapokuja suala la kufanya kazi hii, viongozi na wafanyakazi hawapaswi kusimama tu bila kufanya chochote. Watu wengine husema, “Kuwapangia makazi wafanyakazi wanaofanya wajibu wao ni kazi ya nyumba ya Mungu; tunahitaji tu kuifanya baada ya kupokea mipango ya moja kwa moja kutoka kwa Aliye juu. Aliye juu asipopanga hilo, hatuhitaji kujisumbua nalo, na hata jambo likienda mrama, halituhusu. Isitoshe, kila nchi ina kanuni tofauti kuhusu uhamiaji na hali ya kisheria; hatuwezi kushughulikia suala kubwa kama hilo! Kila mtu anapaswa kujitegemea mwenyewe na kutumaini mambo yatakuwa sawa—ikiwa anaweza kubaki katika nchi, anabaki; asipoweza, anajerea alikotoka.” Je, maneno haya ni sahihi? (La.) Mnafikiria nini kuhusu mtazamo huu? (Ni wa kutowajibika.) Kwa upande mmoja, ni wa kutowajibika; kwa upande mwingine, ni udhihirisho wa viongozi wa uwongo kutofanya kazi halisi na kukwepa majukumu. Kwa viongozi na wafanyakazi, kuwapangia makazi wafanyakazi wa kazi muhimu ng’ambo pia ni kipengele muhimu cha kazi. Punde tu makazi yao yanapopangwa ipasavyo na wanapoweza kufanya wajibu wao kwa kawaida, hatua inayofuata mara moja ni kuwapangia wafanyakazi wanaoshughulikia mambo ya nje kuwaongoza katika kushughulikia hali yao ya kisheria. Hasa wakati hali maalum zinapotokea wakati wa ushughulikiaji ambazo akina ndugu na dada hawawezi kuzishughulikia, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufikiria njia za kupata suluhu, na wasipuuze suala hilo. Ikiwa kuna tatizo lolote katika kushughulikia hali ya kisheria, si jambo dogo na linapaswa kushughulikiwa na kutatuliwa mapema na haraka iwezekanavyo. Msicheleweshe—kile kinachoweza kufanywa leo hakipaswi kuahirishwa hadi kesho; kukiahirisha hadi kesho kunaweza kusababisha matokeo ambayo huenda yakawa mabaya sana kiasi cha kutofikirika. Ikiwa viongozi na wafanyakazi ni wazembe na wanapuuza majukumu yao, bila kulichukulia suala hilo kwa dharura na kuchelewesha wakati bora wa kushughulikia hali ya kisheria, na hivyo kusababisha wafanyakazi wanaofanya wajibu wao kushindwa kufanya hivyo kwa kawaida, ni nani anayebeba jukumu? Watu hawa waliwasilisha maombi yao kwa viongozi wa kanisa na wafanyakazi wanaoshughulikia mambo hayo, na viongozi na wafanyakazi walikuwa wakijua, lakini kwa sababu hawakulichukulia suala hilo kwa uzito au walitoa visingizio vya kutolishughulikia, ushughulikiaji wa hali ya kisheria wa baadhi ya wafanyakazi wa kazi muhimu ulicheleweshwa, jambo ambalo liliathiri vipengele fulani muhimu vya kazi ya kanisa kwa kiasi fulani. Kwa hivyo, mnafikiri ni nani anayepaswa kubeba jukumu hapa? (Ni viongozi na wafanyakazi.) Nyumba ya Mungu imesisitiza suala hili mara kwa mara. Viongozi na wafanyakazi si kwamba hawalijui, wala si kwamba hawana taarifa au wanakosa uelewa; badala yake, wanajua kulihusu lakini hawalichukulii kwa uzito. Mradi tu halihusu mambo yao wenyewe, mradi tu ni masuala ya mtu mwingine, wanaliahirisha kila inapowezekana, na hatimaye wanachelewesha jambo muhimu kama ushughulikiaji wa hali ya kisheria ya watu wateule wa Mungu. Matokeo mabaya yanapotokea, viongozi na wafanyakazi lazima wabebe jukumu. Jukumu hili si maneno tu—ikiwa linaathiri kazi ya kanisa, hasa kazi muhimu ya nyumba ya Mungu, basi jukumu linalobebwa na viongozi na wafanyakazi linakuwa kubwa. Angalau, wataandikiwa dosari na Mungu, litakuwa kosa—hayo ndiyo matokeo. Ikiwa ni jambo ambalo ni jukumu lako kufanya, jambo lililo ndani ya upeo wa majukumu yako, na hulifanyi au unalipuuza, au unalichelewesha kwa sababu fulani za kibinafsi, basi lazima ubebe jukumu. Watu wengine husema, “Sikujua jinsi ya kulitatua; sikuwa na njia yoyote ya kusonga mbele.” Lakini, je, ulilichukulia kwa uzito na kutafuta ushauri kutoka kwa viongozi na wafanyakazi wa ngazi za juu punde ulipopata fursa? Wengine husema walilisahau kwa sababu walikuwa na shughuli nyingi na kazi nyingine. Hata kama kwa kweli walilisahau kwa sababu ya kuwa na shughuli nyingi, wanawezaje kuendelea kusahau baada ya mtu fulani kuzungumza nao kuhusu suala hilo na kuwakumbusha mara kwa mara? Hili linaonyesha tatizo gani? (Hawajaweka suala la kushughulikia hali ya kisheria ya akina ndugu na dada mioyoni mwao; hawana hisia yoyote ya mzigo.) Ukweli kwamba wanaweza kusahau jambo muhimu kama hilo unaonyesha kwamba wanakosa hisia ya wajibu na sio wa kuaminika. Unaweza kusahau jambo muhimu kama kushughulikia hali ya kisheria ya watu wateule wa Mungu—je, unaweza kusahau ushughulikiaji wa hali yako mwenyewe ya kisheria? Ikiwa huwezi kusahau mambo yako mwenyewe lakini unaweza kusahau ya wengine, hilo linathibitisha kwamba wewe una hulka duni, unakosa upendo, na wewe ni mbinafsi na mwenye kudharauliwa. Umekamilisha ushughulikiaji wa hali yako mwenyewe ya kisheria, lakini unachukulia ushughulikiaji wa hali ya kisheria ya akina ndugu na dada kama jambo dogo, la kawaida—au hata unalipuuza jambo hilo kabisa—na mwishowe unachelewesha ushughulikiaji wa hali yao ya kisheria, jambo hili muhimu. Je, unaweza kubeba jukumu hilo? Je, si viongozi na wafanyakazi kama hao wanakosa kabisa dhamiri na busara? Wao ni wabinafsi na wenye kudharauliwa sana! Wanajijali wenyewe tu na kuwapuuza wengine—hili linaonyesha tatizo gani? Je, si wao ni viongozi wa uwongo? (Ndiyo.) Kiini cha tatizo lao hivyo kinafichuliwa kikamilifu. Hawataki tu kushughulikia hali ya kisheria ya akina ndugu na dada; wanaona inasumbua. Mioyoni mwao, wanawaza, “Kushughulikia hali ya kisheria ya akina ndugu na dada kunanihusu nini?” Huu ndio mtazamo wanaokuwa nao wanaposhughulikia suala la ushughulikiaji wa hali ya kisheria ya akina ndugu na dada, na hatimaye wanachelewesha jambo hili muhimu, wanaathiri utekelezaji wa wajibu wa akina ndugu na dada, na wanaathiri kazi ya kanisa. Je, unaweza kusema kwamba viongozi wa uwongo kama hao wanastahili adhabu? (Ndiyo.) Wanapaswa kuwajibishwa kwa sababu hili lilikuwa jambo la makusudi; hakika halikuwa ucheleweshaji wa bahati mbaya uliosababishwa na mambo ya nje. Ikiwa kungekuwa na janga la asili, kama vile tetemeko la ardhi, mafuriko, au tukio fulani kubwa la kisiasa ambalo lilitatiza usafiri na mawasiliano, na kufanya isiwezekane kushughulikia mambo haya, hilo lingeeleweka. Lakini ikiwa hakuna hata moja ya matukio haya yaliyotokea, na bado walisahau au walipuuza ushughulikiaji wa hali ya kisheria ya akina ndugu na dada, na wakachelewesha jambo muhimu kama hilo—hali ya kisheria ya watu hawa—basi kiongozi au mfanyakazi kama huyo anapuuza majukumu yake. Ataandikiwa dosari na atawajibishwa. Je, mnaelewa? (Ndiyo.) Kwa kuwa wewe ni kiongozi au mfanyakazi, wewe una jukumu la kufanya kazi unayopaswa kuwa ukifanya. Kwa kila kitu kilicho ndani ya upeo wa jukumu lako, lazima ukishughulikie ipasavyo na ukikamilishe kulingana na mahitaji ya nyumba ya Mungu. Lakini ukiepuka kwa makusudi kukifanya au ukicheleweshe, huku ni kutelekeza majukumu yako, na utelekezaji huu ni kosa. Ukichelewesha jambo kwa makusudi na usilishughulikie, kushindwa kwako hatimaye kutakuwa kosa, na utaandikiwa dosari na Mungu. Utawajibishwa kwa ajili ya jambo hili.
Katika nchi za ng’ambo, kukiwa na matatizo fulani na hali ya kisheria ya watu wateule wa Mungu, au majirani wao au watu wasiowajua wakiwasilisha malalamiko kuwahusu au kuwaripoti, wanaweza kukabiliwa na hatari ya kufukuzwa nchini. Inaweza pia kutokea kwamba baadhi ya watu wateule wa Mungu katika nchi za ng’ambo wanazuiliwa na kuadhibiwa au kukamatwa na kufungwa gerezani na serikali za nchi fulani kwa mashtaka ghushi. Bila kujali hali, viongozi na wafanyakazi wanapojua kuhusu hilo, hawapaswi kutenda kama kobe wanaoingiza vichwa vyao ndani magamba yao; wanapaswa kushughulikia jambo hili mara moja, lengo kuu likiwa ni kuhakikisha usalama wa akina ndugu, wasiwaruhusu waanguke mikononi mwa watu waovu. Ikiwa viongozi na wafanyakazi wanajali tu kupanga kazi ya kanisa, lakini hawaliwekei umakinifu suala la ushughulikiaji wa hali ya kisheria ya akina ndugu, jambo ambalo linasababisha akina ndugu kukamatwa au kufukuzwa nchini kwa sababu ya kukosa hali ya kisheria, haya ni madhara gani? Je, si viongozi na wafanyakazi kama hao wameharibu fursa ya akina ndugu ya kufanya wajibu wao? Je, si hili linaiathiri kazi ya kanisa moja kwa moja? Asili ya tatizo hili basi ni zito sana. Ikiwa viongozi na wafanyakazi hawajashughulikia jambo hili hapo awali, wanaweza kutafuta miongoni mwa akina ndugu na dada mtu aliye na ustadi wa kushughulikia mambo ya nje ambaye atashauriana na wakili ili kushughulikia jambo hili, wakijitahidi kufikia lengo la kuwalinda akina ndugu na dada na kulinda usalama wa wafanyakazi wa kazi muhimu. Hiki pia ni kipengele muhimu cha kazi ambacho viongozi na wafanyakazi lazima watekeleze ng’ambo; viongozi na wafanyakazi wa eneo hilo lazima wachukue hatua ya kulishughulikia jambo hili. Mbali na kulinda usalama wa akina ndugu na dada wa eneo hilo, lazima walinde usalama wa akina ndugu na dada wa kigeni hata zaidi; ni kwa njia hii tu ndiyo kuna uhakikisho kwa kazi ya kanisa. Hili ndilo jukumu ambalo viongozi na wafanyakazi katika kila nchi wanapaswa kutimiza kwa akina ndugu na dada wa eneo hilo na wafanyakazi wa kazi muhimu wa kigeni; hawapaswi kusimama tu bila kufanya chochote. Baadhi ya viongozi na wafanyakazi husema, “Wao ni akina ndugu na dada wa kigeni, na hatuwafahamu; hakuna uhusiano wa kibinafsi kati yetu. Walitumwa na nyumba ya Mungu kuhubiri injili hapa—hilo linatuhusu nini? Mkasa huu ni jambo walilojiletea wenyewe; hawakuulizia hali kikamilifu kabla ya kuja na hawakushughulikia mambo haya vizuri. Hatuna njia ya kuingilia kati mkasa huu; ni nani ajuaye kile ambacho serikali itawafanyia.” Wanatumia tu visingizio mbalimbali kukwepa na kuepuka mambo haya, na hawajaribu kutafuta njia za kuchukua hatua ili kuyatatua. Je, kutenda kwa namna hii ni sahihi? (La.) Kwa nini sivyo? (Viongozi na wafanyakazi wasipochukua hatua za kutatua matatizo haya, na akina ndugu na dada, wakati huo huo, hawana njia ya kutatua matatizo hayo, basi hakika shida itatokea. Viongozi na wafanyakazi hawajatimiza jukumu lao la kuwalinda akina ndugu na dada—huku ni kutelekeza majukumu yao.) Wajibu wa viongozi na wafanyakazi ni kutimiza kila jukumu ambalo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kutimiza katika nyumba ya Mungu. Upeo wa nyumba ya Mungu haukomei katika eneo la mahali hapo, mkoa wa eneo hilo, au nchi fulani; nyumba ya Mungu haina mipaka ya kitaifa, haina mipaka ya kikanda. Je, kuna mipaka ya rangi Mungu anapowachagua watu na kuwaokoa watu? (Hakuna.) Je, kuna mipaka ya utaifa au kanda? (Pia hakuna.) Hakuna. Hii ndiyo kanuni ambayo kwayo Mungu anafanya kazi Yake; hivyo, kanuni hii ni ukweli! Haijalishi akina ndugu na dada wanatoka katika nchi gani, wote wanamwamini Mungu mmoja, wanamfuata Mungu mmoja, na pia wanakula na kunywa ukweli ambao Mungu mmoja anashiriki na kuruzuku. Wanapitia kazi anayofanya Mungu mmoja, na kumwabudu Mungu mmoja. Bila kujali rangi ya ngozi wala kabila, katika nyumba ya Mungu na mbele za Mungu, wao ni kitu kimoja—wao ni familia moja. Kwa kuwa wao ni familia moja, hakupaswi kuwa na tofauti miongoni mwao; hakupaswi kuwa na mipaka ya rangi wala ya kikanda; hakupaswi kuwa na migawanyiko ya “wewe ni Mwasia, mimi ni Mwulaya,” au “wewe ni Mweupe, mimi ni mtu asiye mweupe”—hakupaswi kuwa na tofauti hizi. Ikiwa bado unaweka tofauti hizi katika nyumba ya Mungu, basi ni wazi kwamba huichukulii nyumba ya Mungu kama nyumba ya Mungu, na hujichukulii kama mshiriki wa nyumba ya Mungu. Kwa hivyo, wakati akina ndugu na dada wa kigeni wanakumbana na matatizo kama vile kufukuzwa nchini au kukamatwa kinyume cha sheria, bila kujali wanatoka wapi, utaifa wao ni upi, au wana rangi gani ya ngozi, wao ni akina ndugu na dada—kwa kuwa wao ni akina ndugu na dada, wanapokabiliwa na matatizo, viongozi na wafanyakazi wa eneo hilo wanapaswa kuchukua hatua na kushughulikia jambo hili kama wajibu wao, na hawapaswi kuweka tofauti miongoni mwa watu. Hili linakubaliana na kanuni, linaendana kikamilifu na nia za Mungu, na ndio ukweli ambao watu wanapaswa kutenda.
Kwa sasa, wengi wa watu wateule wa Mungu kutoka nchini China wanaenda katika nchi mbalimbali ng’ambo kuhubiri injili na kumshuhudia Mungu. Baada ya kuwasili katika nchi hizi, jambo la kwanza wanalopaswa kufanya ni kushughulikia hali yao ya kisheria kabla ya kuweza kufanya kazi kwa amani moyoni. Kushughulikia hali ya kisheria si jambo rahisi; kunahitaji ushirikiano wa watu kutoka kanisa la eneo hilo. Wale wanaosimamia makanisa katika nchi mbalimbali wanapaswa kutafuta baadhi ya akina ndugu na dada wanaoelewa sera za nchi yao na wanaojua sheria za nchi hiyo ili wawasaidie watu wateule wa Mungu kutoka China kutatua suala la kushughulikia hali ya kisheria. Kutatua suala hili ni jambo la umuhimu mkubwa. Viongozi na wafanyakazi wa makanisa ya nchi mbalimbali wanapaswa kufanya kila juhudi kulifanyia kazi, kwani ni kwa kutatua kikamilifu suala la hali ya kisheria ya watu tu ndiyo kazi ya kanisa inaweza kuendelea kwa kawaida; la sivyo, kazi ya kanisa itaathirika. Wale wanaosimamia makanisa katika nchi mbalimbali wanapaswa kuwa wameandaa watu wenye uwezo wa kushughulikia mambo kama hayo. Kufanya hivi kunaifaidi kazi ya kanisa na pia ni udhihirisho wa kuzijali nia za Mungu. Huenda baadhi ya viongozi na wafanyakazi waseme, “Hatujawahi kushughulikia jambo la aina hii, na hatujui la kufanya pia.” Katika hali hii, wanapaswa kuwatafuta watu wanaoelewa mambo ya aina hii. Miongoni mwa watu wateule wa Mungu katika kila nchi, kuna wale walio na elimu na maarifa, na pia kuna wale wanaoelewa sheria na sera za kitaifa. Kwao, kushughulikia mambo haya kunahitaji tu mashauriano kidogo ili kupata njia—je, si hivyo ndivyo ilivyo? Katika kushughulikia jambo la aina hii, hupaswi kuwa mtu asiyechukua hatua na asiyetenda; ikiwa huelewi jambo fulani, unapaswa kutafuta wakili wa kushauriana na yeye. Mradi tu wakili anayefaa anapatikana, bila shaka kutakuwa na njia. Huenda hatuelewi jambo hili, lakini wakili ataelewa. Kuwa na moyo unaotafuta ndio mtazamo sahihi; kuwa na moyo unaotafuta ni udhihirisho wa kuwa na hisia ya uwajibikaji. Matatizo fulani yakitokea, mnapaswa kuomba, kutafuta, na kufanya ushirika pamoja kwa moyo na nia moja, na baada ya kupata kanuni na njia ya kutatua tatizo, mnapaswa kulitatua kikamilifu. Ni hapo tu ndipo kazi ya kanisa inaweza kuendelea vizuri. Ikiwa, wanapogundua tatizo, viongozi na wafanyakazi wanaweza kupata habari kulihusu mara moja, kulifuatilia, na kulitatua, je, si wao ni viongozi na wafanyakazi wanaowajibika? (Ndiyo.) Si kwamba viongozi na wafanyakazi kama hao wana hisia ya wajibu tu bali pia wanaweza kutatua matatizo mara moja, jambo ambalo linamaanisha kwamba wana tumaini la kuwa viongozi na wafanyakazi wanaofikia kiwango kinachostahili. Bila kujali kina cha uelewa wao wa ukweli, ikiwa wanazingatia kutatua matatizo, basi wanaweza kufanya kazi halisi. Angalau, wanaweza kufanikiwa kufanya makosa machache au kutofanya makosa; na hata wakifanya makosa fulani, wanaweza kuyarekebisha mara moja ili kufidia hasara fulani, na hatimaye wanaweza kufikia lengo la kulinda kazi ya nyumba ya Mungu. Je, mnafikiri kutimiza jukumu hili ni jambo gumu? (La.) Kwa kweli, si jambo gumu; linategemea iwapo watu wana uaminifu katika kufanya wajibu wao na iwapo wanaweza kutimiza jukumu lao katika kazi yao. Unahitaji tu kufikiri kidogo, kutumia muda kidogo, na kuwekeza nguvu kidogo; halikuhitaji wewe utumie pesa au kuchukua hatari yoyote. Unahitaji tu kuchukua hatua ili kusaidia kutatua matatizo na kushughulikia mambo vizuri, na kwa namna hii, unaweza kufikia kiwango kinachostahili. Kwa hivyo, hili si jambo gumu, na kwa viongozi na wafanyakazi, linapaswa kuwa rahisi kufikiwa. Lakini kuna baadhi ya watu ambao hawawezi kutimiza hata jambo rahisi hivi, na ni wazi sana kwamba hili halisababishwi na ubora wa tabia au uwezo usiotosha, au kwa sababu ya hali au mazingira kutoruhusu, bali badala yake ni kwa sababu hawako tayari kulifanya. Wakati hali maalum zinapotokea zinazohusisha hali ya kisheria au ukaazi wa wafanyakazi wa kazi muhimu, au mambo yanayohusu kupangwa kwao, viongozi na wafanyakazi wana jukumu la kufanya kazi hii. Haijalishi ni nani unayempangia makazi, au utaifa wake au kabila lake; kile unachohitaji kufanya ni kukubali hili kutoka kwa Mungu. Kazi hii imekabidhiwa kwako na Mungu; ni jukumu na wajibu wako, pamoja na utume wako. Kazi hii unayoikubali inatoka kwa Mungu, si kutoka kwa mtu yeyote, kwa hivyo hupaswi kutilia maanani watu hawa unaowapangia makazi ni akina nani. Watu wengine wanaweza kusema, “Kuwalinda akina ndugu na dada wa eneo hilo kunakubalika, lakini si jukumu letu akina ndugu na dada wa kigeni wakija hapa.” Je, watu wanaosema hivi wana hisia ya uwajibikaji au ya ubinadamu? (Hawana.) Wao wanawachukulia akina ndugu na dada wa eneo hilo kama akina ndugu na dada, lakini hawawachukulii akina ndugu na dada wa kigeni kama akina ndugu na dada—je, hili lina msingi? (Halina.) Je, hili linakubaliana na ukweli? (Halikubaliani.) Kwa nini halikubaliani na ukweli? (Viongozi wa uwongo hawazijali nia za Mungu; wanawapuuza akina ndugu na dada wa kigeni, na hawachukui hatua kushughulikia masuala matatizo yanapotokea—hawailindi kazi ya nyumba ya Mungu.) Viongozi wa uwongo hukwepa majukumu kwa visingizio mbalimbali na hawafanyi kazi halisi. Wao hudai kwamba wako tayari kujitumia kwa ajili ya Mungu na wako tayari kutenda ukweli, lakini linapokuja hasa suala la mambo muhimu ya kazi ya kanisa, wao hujificha. Huku ni kutowajibika. Kwa masuala yote yanayohusiana na kulinda usalama wa akina ndugu na dada ng’ambo, viongozi na wafanyakazi lazima wayashughulikie mara moja, wakiyachukulia kama jukumu na kazi inayopaswa kukamilishwa. Hawapaswi kutoa visingizio ili kuyaepuka, wala kuruhusu kupuuza kwao kazi hii kuathiri maendeleo ya vipengele mbalimbali vya kazi ya nyumba ya Mungu.
B. Kuwapa Akina ndugu na dada Wote Maarifa ya Msingi ya Kisheria
Ni vipengele vingine vipi vya kazi vinavyohusiana na usalama wa akina ndugu na dada ng’ambo mnavyoweza kufikiria? (Katika nchi za ng’ambo, viongozi na wafanyakazi pia lazima wawape akina ndugu na dada wote maarifa fulani ya msingi ya kisheria, ili wakuze ufahamu wa sheria na waepuke kujihusisha na shughuli zinazokiuka sheria.) Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuwapa akina ndugu na dada wote maarifa ya msingi ya kisheria na uelewa wa kanuni mbalimbali za serikali. Wanapaswa kufahamu zaidi kuhusu nyanja hizi kutoka kwa akina ndugu na dada wa eneo hilo katika nchi waliyomo, kama vile sera za uhamiaji na sera zinazohusiana na maisha ya kila siku, na kisha waratibu mpango wa akina ndugu na dada kujifunza haya ili wafuate kikamilifu kanuni za serikali ya kitaifa na wajizuie kufanya chochote kinachokiuka sheria. Hasa, watu wateule wa Mungu kutoka China, ambao wamekuwa chini ya utawala wa kidikteta kwa miaka mingi sana, hawana maarifa ya kisheria na hawaelewi umuhimu wa sheria. Matokeo yake, wao hutenda kiholela na bila uangalifu, kama watu wasiostaarabika. Wanapokuja kuishi ng’ambo, wao huonekana wasio na ufahamu sana na mara nyingi wao hufanya mambo yanayoonyesha ukosefu wa uelewa wa taratibu. Kwa mfano, katika baadhi ya nchi za kidemokrasia za Magharibi, utaratibu wa kijamii unasimamiwa vizuri sana, kukiwa na taratibu zinazokataza kelele kuanzia saa nne usiku hadi saa mbili asubuhi—hakuna sauti kama vile mbwa kubweka au mngurumo wa mitambo ya ujenzi zinazoruhusiwa. Mtu yeyote akikiuka taratibu hizi na aripotiwe, polisi watalishughulikia. Katika China bara, hakuna anayesimamia mambo haya; popote ambapo kuna watu wanaoishi kutakuwa na kelele kiholela, kukiwa na sauti za muziki wa sauti ya juu, kucheza dansi, kunywa, na kufanya sherehe, na hakuna anayeingilia kati. Mtu yeyote akijaribu kuingilia kati, anaweza kukabiliwa na ulipizaji kisasi, kwa hivyo watu wa China hawana budi ila kuvumilia jambo hilo. Nchi za Magharibi ni tofauti; kila mtu analindwa na sheria. Mbwa wako akibweka mara kwa mara katikati ya usiku, na kusumbua mapumziko ya majirani wako, watawasilisha malalamiko dhidi yako. Kile unachofanya kinaathiri maisha ya kawaida ya wengine, umekiuka taratibu za kisheria—ni halali kwao kutumia sheria kama silaha kuwasilisha malalamiko dhidi yako. Pia kuna watu wanaoendelea na kazi ya ujenzi hadi saa tano au saa sita usiku, na kuathiri mapumziko ya majirani wao, jambo ambalo husababisha malalamiko. Kisha polisi huja kuwatoza faini na kuwaonya wasipige kelele wakati wa saa zilizopangwa. Watu wengine hata hawana ufahamu wa usafi wa mazingira, wakitupa taka na kuziacha zimetapakaa barabarani kote. Nchi za kidemokrasia za Magharibi zina utaratibu hasa. Wakaazi wana nyakati zilizopangwa za kutupa taka, na malori ya kukusanya taka huja katika siku zilizopangwa kuzikusanya. Baada ya ukusanyaji, mitaa hubaki ikiwa safi. Wale wasioelewa hili wanaweza kutupa taka ovyo, jambo ambalo pia linachukuliwa kuwa ukiukaji wa taratibu. Hili linaathiri usafi wa umma na mwonekano wa jiji, kwa hivyo malalamiko yanaweza kuwasilishwa dhidi yao. Kwa sababu watu wa China kutofuata sheria, mara nyingi malalamiko huwasilishwa dhidi yao wanapoishi ng’ambo. Baada ya kuripotiwa mara nyingi, wao huanza kuwa na maoni kuwahusu watu wa Magharibi, wakisema, “Watu wa Magharibi wanapenda tu kuwasilisha malalamiko; wanawasilisha malalamiko kuhusu kila jambo dogo,” ambapo mimi husema, “Waliwasilisha malalamiko dhidi yako kwa mambo mengi sana, na hujajitafakari bali unawalaumu kwa kuwasilisha malalamiko. Basi, je, walikuwa sahihi kuwasilisha malalamiko? Je, mambo uliyofanya yalikuwa sahihi au la?” Wao walikuwa sahihi kabisa kuwasilisha malalamiko hayo; ulidhuru masilahi yao na uliyaathiri maisha yao, kwa hivyo kwa nini wasiwasilishe malalamiko dhidi yako? Hili linafanywa ili kulinda utaratibu wa kijamii na linaonyesha kwamba nchi hii inatawaliwa na sheria; kila mtu analindwa na sheria, na sheria katika nchi hii si ya maonyesho tu—kila mtu anaweza kutumia sheria kama silaha kulinda haki na masilahi yake mwenyewe. Wao wanawasilisha malalamiko dhidi yako kwa sababu wewe huelewi sheria na umekiuka taratibu za eneo hilo. Unapaswa kwanza kujifunza taratibu za eneo hilo na utende kulingana na sheria na taratibu—basi, je, unafikiri bado wangewasilisha malalamiko dhidi yako? (Hawangewasilisha malalamiko tena.) Hivyo, kwa nini watu wa China huwa hawawasilishi malalamiko kamwe, bila kujali jambo lilivyo zito? (Wamekandamizwa na serikali kwa muda mrefu sana. Hawathubutu kuwasilisha malalamiko. Watu wa China pia hawana dhana yoyote ya kutetea haki zao.) China si nchi inayotawaliwa na sheria. Haitawaliwi kulingana na sheria. Sheria za China ni za maonyesho tu, na kuwasilisha malalamiko huko ni bure tu. Ukiwasilisha malalamiko, na ule upande mwingine uwe na mamlaka na ushawishi, wanaweza kukulipiza kisasi. Ikiwa huna ushawishi, huwezi kuthubutu hata kuwasilisha malalamiko; kuwasilisha malalamiko kunaweza kukuletea shida kwa urahisi. Kwa hivyo watu wa China wanapokumbana na mateso—hasa katika visa ambapo mtu ameuawa—haijalishi kifo hicho ni dhalimu kiasi gani, jambo hilo husuluhishwa tu kwa faragha mhusika akilipa pesa kiasi. Kwa nini wanafamilia wa mwathiriwa hawawasilishi kesi mahakamani? Wanajua kwamba hawatashinda kamwe; itagharimu pesa nyingi, lakini bado hawatapata haki, wala mhusika hatachukuliwa hatua za kisheria, kwa hivyo wanachagua kutolifuatilia kisheria na badala yake kulisuluhisha kwa faragha. Sheria za China ni za maonyesho tu; China si nchi inayotawaliwa na sheria, isiyo na uwanja wa kutafuta haki. Kuwasilisha kesi mahakamani hakuna maana. Hivyo, haijalishi ni hali gani za ukiukaji wa sheria ambazo watu wa China wanakumbana nazo, hawathubutu kuwasilisha malalamiko. Hii ni kwa sababu Chama cha Kikomunisti hakifanyi chochote ila kutenda maovu, hakina busara, na hakitawali kulingana na sheria. Nchini China, mradi tu mtu ni mtu wa kawaida, haijalishi suala analokabiliana nalo ni zito kiasi gani, halihesabiwi kama jambo la maana machoni pa Chama cha Kikomunisti—hakuna atakayelishughulikia. Mambo kama vile kuathiri mapumziko ya wengine, au hata visa vya wizi, unyang’anyi, na wizi wa uvunjaji nyumba, hayachukuliwi kabisa kama matatizo na Chama cha Kikomunisti. Hata hivyo, katika nchi za Magharibi, ni tofauti. Nchi za Magharibi zina mfumo wa kidemokrasia na ni jamii inayotawaliwa na sheria; mradi mapumziko ya mtu yanaathiriwa, malalamiko yatawasilishwa, na polisi watakuja kulichunguza na kulishughulikia jambo hilo. Watu wa Nchi za Magharibi wana ufahamu huu wa sheria na hawafanyi mambo ya kijinga kama hayo; ni wale tu wanaotoka ng’ambo na wasioelewa kanuni ndio wanaofanya mambo haya ya kijinga. Watu wa China wanapoanza kuishi ng’ambo kwa mara ya kwanza, mara nyingi malalamiko huwasilishwa dhidi yao. Kadiri muda unavyopita, wao hujifunza kuhusu sheria na taratibu za eneo hilo na hawathubutu tena kufanya mambo yanayokiuka sheria au kuwasumbua wengine. Kwa hivyo, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuratibu mpango wa akina ndugu na dada kujifunza kuhusu sheria na kanuni mbalimbali za nchi waliyomo. Haijalishi kile wanchokusudia kufanya, lazima kwanza warejelee sheria—hata kama wanafuga kuku au nguruwe katika uga wao wenyewe, wanapaswa kwanza kuangalia taratibu za serikali. Wanaweza kutafuta habari mtandaoni au kushauriana na akina ndugu na dada wa eneo hilo na kwa njia hii kupata majibu sahihi. Katika mambo yote katika nchi mbalimbali za Magharibi, serikali ina taratibu mahususi. Kwa mfano, katika ujenzi, kuna kanuni kuhusu urefu wa soketi za umeme kutoka sakafuni na umbali kati ya kila soketi. Pia kuna viwango mahususi vya unene wa vitau vya ngazi na upana wa nguzo za ngazi. Kila hatua ya ujenzi hukaguliwa na wafanyakazi wa serikali, kwa hivyo visa vya majengo yanayokiuka kanuni za ujenzi au ujenzi usiodhibitiwa ni nadra. Wakaazi wakitaka kujenga nyumba, kibanda cha zana, au kibanda kidogo cha kuhifadhia vitu katika uga wao, lazima wapate idhini ya serikali. Ikiwa wanataka kufuga kuku au bata, kuna taratibu kuhusu umbali unaopaswa kuwepo kati ya zizi na eneo la majirani wao. Hata kama viongozi na wafanyakazi hawaelewi sheria na kanuni hizi, ikiwa kazi ya kanisa inahusisha mambo haya, basi viongozi na wafanyakazi lazima wayatilie maanani. Wanapaswa kwanza kurejelea sheria za eneo hilo na taratibu za serikali; kuelewa mambo haya waziwazi kuna manufaa kwa utendaji wetu wa wajibu. Ingawa masuala ya kisheria hayahusiani moja kwa moja na kazi ya ndani ya kanisa, kuwapa wote maarifa ya msingi ya kisheria bado kuna manufaa. Angalau, wanaweza kupata maarifa fulani, wanaweza kuelewa sheria fulani, wanaweza kujifunza jinsi ya kuishi ipasavyo, na wanaweza kufikia sura fulani ya ubinadamu. Zaidi ya hayo, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufanya ushirika na wale wanaohusika na mambo ya nje, wakiwasaidia kukuza ufahamu wa sheria. Kwa mambo madogomadogo, si lazima kushauriana na wakili—wanahitaji tu kuelewa taratibu za eneo hilo na kuzifuata kikamilifu. Hata hivyo, kuhusiana na mambo makubwa, wanapaswa kushauriana na wakili ili kupata uelewa wa sheria za eneo hilo. Kwa muhtasari, haijalishi kile kinachofanywa, matendo yote lazima yafuate sheria na taratibu. Kutenda kwa njia hii kwa kipindi cha muda kutawaruhusu watu kutambua umuhimu wa kufuata sheria na taratibu, na watafuata masharti wanapofanya mambo. Hili pia ni la manufaa kwa kazi ya kanisa.
C. Kanuni za Kufuata Wakati wa Kuwatuma Watu Kuhubiri Injili
Kuhusiana na kulinda usalama wa wale wanaotekeleza wajibu muhimu, kuna kipengele kingine cha kazi ambacho viongozi na wafanyakazi lazima wakishughulikie, ambacho ni kulinda usalama wa wale wanaotoka nje kufanya wajibu wao. Ni kanuni zipi zinazopaswa kufuatwa wakati wa kuwatuma watu watoke nje kufanya wajibu wao? Kwanza, umri na jinsia ya watu vinapaswa kuzingatiwa, pamoja na umaizi wao na uzoefu wao wa maisha—viongozi na wafanyakazi hawapaswi kuwa waliokanganyika vichwa au wasiojali katika suala hili. Kwa mfano, ukiwa unawatuma wafanyakazi wa injili kuhubiri injili katika mahali wasipopafahamu, ni watu wa aina gani ambao wanafaa kutumwa? (Watu walio na umaizi na hekima kiasi.) Ikiwa kanisa fulani halina watu wengi wanaofaa, huku wengi wakiwa vijana wasio na uzoefu wa maisha na umaizi, ambao hawajui jinsi ya kushughulikia hali—hasa matatizo magumu—wanapokumbana nazo, wanaozungumza bila kanuni, na wasio pia na hekima, basi hawataweza kufanya kazi hiyo. Watu kama hao wakitumwa, si tu kwamba hawataweza kutatua matatizo, bali pia wana uwezekano wa kuathiri na kuchelewesha kazi. Kwa hivyo, wakati wa kuwatuma watu watoke nje kufanya wajibu wao, ni lazima kuwachagua wale walio na ubinadamu uliokomaa na hekima komavu—ni watu kama hao tu ndio wanaofaa. Ikiwa hakuna watu wa kutosha wanaofaa, basi waruhusu vijana washirikiane na watu wazee kwenda kufanya wajibu wao. Kwa mfano, tuseme kuna dada kijana mwenye umri wa karibu miaka 25 au 26 ambaye, licha ya kumwamini Mungu kwa muda mrefu kiasi, kuwa na imani na kimo, na kufanya wajibu wake kwa muda mrefu, hangejua jinsi ya kulinda usalama wake mwenyewe ikiwa angetumwa kufanya wajibu wake katika mahali asipopafahamu—katika hali kama hiyo, ingekuwa lazima kutafuta ndugu wa eneo hilo aliye na uzoefu wa kijamii ili kushirikiana na yeye kufanya wajibu huo. Bila shaka, ikiwa eneo la wajibu ni mahali panapofahamika au mahali ambapo tayari kuna kanisa, basi akina ndugu na dada vijana wanaweza kwenda. Hata hivyo, watu wakienda mahali wasipopafahamu, hasa penye usalama duni wa umma, kuhubiri injili au kufanya kazi nyingine, basi usalama wao binafsi lazima utiliwe maanani. Kwa viongozi na wafanyakazi, haijalishi ni nani wanayemtuma atoke nje kufanya kazi, usalama ndio jambo la kwanza kuzingatiwa. Ikiwa haijulikani wapokeaji watarajiwa wa injili ni watu wa aina gani, au iwapo watu hawa wanaweza kufanya mambo yasiyofaa, basi tahadhari inapaswa kuchukuliwa wakati wa kuwatuma watu kuhubiri injili. Hapo awali, nilisikia kwamba baadhi ya viongozi na wafanyakazi mara nyingi walikuwa wakiwatuma akina dada vijana—wenye umri wa karibu miaka 18 au 19, au mwanzoni mwa miaka yao ya 20—waende kwenye maeneo wasiyoyafahamu ili wahubiri injili, na inasemekana, baadhi ya matukio ya kusikitisha yalitokea. Bila kujali kile kilichotokea kwa kweli, hatimaye ilihusiana na viongozi na wafanyakazi kutofikiria kwa kina katika mazingatio yao wakati wa kufanya kazi. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuzingatia mambo haya kwa kina katika kazi yao na hawapaswi kuwapangia kiholela akina dada au akina ndugu vijana sana kwenda katika maeneo wasiyoyafahamu na ya hatari kufanya wajibu wao. Kulikuwa na kiongozi ambaye wakati mmoja aliwapangia akina dada wawili, wenye umri wa miaka 18 au 19, kwenda kuhubiri injili. Mtu fulani aliposema kwamba walikuwa vijana sana na hawakufaa kwa hili, kiongozi huyo kisha alimpata dada wa miaka 21 aende badala yao, akiwaza, “Ulisema miaka 19 ni mdogo sana, kwa hivyo nimepata mtu wa miaka 21. Huyo ni mkubwa zaidi, sivyo?” Ubora wa tabia wa kiongozi huyu ulikuwaje? Alikuwa na fikira potofu, sivyo? (Ndiyo.) Akiwa mkubwa kwa miaka miwili tu kuliko 19—je, angeweza kuwa na uzoefu wa maisha? Je, angeweza kuwa na uzoefu katika jamii? Kama angekabiliwa na matatizo au hali za hatari, je, angeishia kulia? Ingawa alikuwa mkubwa kwa miaka miwili, kwa upande wa umri, bado alikuwa mdogo sana na hakuwa na uwezo wa kuchukua kazi hii. Angalau, ni lazima kutafuta ndugu aliye katika miaka yake ya 30 au 40, au miaka yake ya 50 au 60—yeye ni mkubwa na ana uzoefu katika jamii; anapokumbana na hali, ana hekima ya kuzishughulikia, akizuia hali zozote za hatari kutokea. Vijana hawajaona au kupitia mambo mengi na hawajui jinsi ya kuyashughulikia; wanapokumbana na hatari, huenda hata wasiyatambue, jambo ambalo hufanya iwe rahisi kwa matukio kutokea. Watu wazee, kwa kuwa wameona uovu zaidi katika jamii hii na binadamu hawa, huwa na mwelekeo wa kuwa makinifu zaidi kwa watu. Kulingana na uzoefu wao wa kijamii na maarifa kutoka kwa maisha halisi, wanaweza kufanya tathmini fulani za busara kuhusu ni aina gani ya hatari inayoweza kutokea katika hali fulani, kiwango cha hatari kiko juu kiasi gani, ni watu gani ndio watu waovu, na ni mambo ya aina gani ambayo watu fulani wanaweza kufanya. Wanapokumbana na hali za hatari, pia wana hekima ya kuepuka hatari. Kwa upande mwingine, vijana hawana uzoefu. Wanapokumbana na hali, hawawezi kutambua madhara ya hatari yanayoweza kutokea. Kwa hivyo, linapokuja suala la usalama, watu wazee hufikiria kwa kina zaidi katika mazingatio yao kuliko vijana. Viongozi na wafanyakazi wanapowapangia watu watoke nje kufanya wajibu wao, wanapaswa kuzingatia hali za eneo hilo na kuwapangia watu wakubwa kiasi walio na hekima na uzoefu fulani ili washirikiane na vijana kufanya wajibu wao. Viongozi na wafanyakazi lazima wazingatie mambo haya kwa ukamilifu.
Haijalishi kazi ya kanisa inafanywa katika nchi gani, kuhakikisha usalama wa wale wanaofanya wajibu wao ni kipengele cha kazi ambacho viongozi na wafanyakazi lazima wakitilie maanani sana. Haijalishi ni nani anayetumwa kufanya kazi gani, lazima awe na ubora fulani wa tabia na awe na uwezo kiasi ili aweze kuwa na ustadi katika kazi hiyo na ili usalama wake uweze kuhakikishwa; hasa, hili ni muhimu hata zaidi katika maeneo au nchi zenye usalama duni wa umma. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuchukulia usalama wa wale wanaofanya wajibu wao kama jambo la kwanza la kuzingatia, na wasiupuuze kiholela. Watu wengine wanasema, “Ni sawa. Tunachofanya ni kufanya wajibu katika nyumba ya Mungu—tuna ulinzi wa Mungu, kwa hivyo hakuna atakayekufa. Ni kitu gani kinachoweza kwenda mrama?” Je, ni sawa kwao kusema hivi? (La.) Kwa nini si sawa? (Kuzungumza kwa namna hii ni kutowajibika, na mtazamo huu pia uko mbali sana na uhalisi.) Watu wanapaswa kufanya juu chini kutimiza majukumu wanayoweza kutimiza na kushughulikia yale wanayoweza kuzingatia; hawapaswi kumjaribu Mungu, wala kucheza kamari na usalama wa akina ndugu na dada. Mungu anaweza kuwalinda watu, lakini ikiwa wewe huzingatii matatizo unayoweza kuzingatia, na unatumia usalama wa akina ndugu na dada kama rehani ili kumjaribu Mungu, Mungu atakufunua—ni nani aliyekufanya uwe mpumbavu mno kiasi hicho, ukifanya mambo ya kijinga kama hayo! Kwa hivyo, viongozi na wafanyakazi hawapaswi kutumia mazungumzo ya aina hii kama kisingizio cha kufanya mambo ya kutowajibika; kuhakikisha usalama wa wale wanaofanya wajibu wao ni jukumu lako, na unapaswa kutimiza jukumu lako mwenyewe. Baada ya kushughulikia kila kitu unachoweza kuzingatia na unachoweza kufanya, basi kuhusu kile ambacho hujazingatia, jinsi Mungu atatenda katika suala hilo ni jambo la Mungu Mwenyewe na halikuhusu wewe. Watu wengine kiholela humsukumia Mungu majukumu yote, wakisema, “Mungu anawajibikia usalama wa watu, hatuhitaji kuogopa; tunaweza kuhubiri vyovyote tunavyotaka. Tukiwa na Mungu, kila kitu ni huru na kilichombolewa; hatuhitaji kuwa na wasiwasi kuhusu mambo hayo!” Je, kauli ya aina hii ni sahihi? (La.) Kulingana na kauli ya aina hii, watu hawahitaji kutafuta kanuni wakati mambo yanapotokea; kama ingekuwa hivyo, ukweli ambao Mungu ameonyesha ungekuwa na manuaa gani? Haungekuwa na maana. Katika miaka hii, Mungu amezungumza maneno mengi sana kwa subira na kwa juhudi kubwa ili kuwafunza watu, kwa lengo la kuwawezesha watu Wake wateule kujua jinsi ya kuendelea kuishi, jinsi ya kufuatilia ukweli, na jinsi ya kujiendesha katika ulimwengu huu mwovu na miongoni mwa binadamu hawa waovu, ili walingane na nia ya Mungu. Hupaswi kumjaribu Mungu, wala hupaswi kutenda vyovyote unavyotaka kulingana na maneno na mafundisho na bila kanuni. Ili viongozi na wafanyakazi wafanye kazi nzuri katika kazi ya kuhubiri injili, kwanza kabisa lazima wahakikishe usalama wa watu. Ili kufanya hivyo, lazima kwanza wajue na wafahamu hali mahususi za wale wanaofanya wajibu wao, wawatume watu wanaofaa, na pia waelewe la kufanya katika hali mbalimbali ili wahakikishe usalama wa watu. Ikiwa eneo lina machafuko hasa, hakuna mtu aliye na watu anaowajua huko, na usalama wa yeyote anayeenda huko kuhubiri injili hauwezi kuhakikishwa, basi msiwatume watu huko kwa wakati huu; msijiweke hatarini, msifanye dhabihu zisizo za lazima. Haijalishi ni wajibu gani unaofanywa au ni kazi gani inayotekelezwa, haikuhitaji wewe ujitose ulimwenguni au uhatarishe maisha yako, wala haikuhitaji wewe uweke rehani usalama wako au maisha yako. Bila shaka, katika mazingira ya China, kujiweka hatarini ili kufanya wajibu wa mtu hakuepukiki. Serikali inawatesa wale wanaomwamini Mungu, na hata ukijua fika kwamba kuna hatari, bado lazima umwamini Mungu, umfuate Mungu, na ufanye wajibu wako; huwezi kuutelekeza wajibu wako, na hakuna kazi inayoweza kusimamishwa. Hali katika nchi za ng’ambo zote ni tofauti—baadhi yazo ni nchi za kimabavu sawa na China, huku nyingine zikiwa na mifumo ya kidemokrasia. Katika nchi zilizo na mifumo ya kidemokrasia, kazi ya kuhubiri injili inaweza kuendelea vizuri, na vipengele mbalimbali vya kazi vinaweza pia kutekelezwa kwa wepesi zaidi. Lakini katika baadhi ya nchi zenye sifa za kimabavu, watu ni wakatili na wa nyuma kimaendeleo, na si rahisi kwao kuikubali njia ya kweli. Injili inapohubiriwa kwao, si tu kwamba hawaichunguzi, bali wanaweza kuishutumu kwa upofu, na hata wanaweza kuripoti hali hiyo kwa polisi. Katika hali kama hizo, msiwatume watu kuhubiri injili huko; badala yake, chagueni maeneo ambapo usalama unaweza kuhakikishwa ili kufanya kazi hiyo. Haya yote ni mambo ambayo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuzingatia kwa makini. Kwa mfano, katika nchi kama Malaysia, Indonesia, au India, ambazo zina mazingira tata sana ya kidini, madhehebu fulani ya kidini yana ushawishi mkubwa na yanadhibiti jamii nzima, kiasi kwamba hata serikali zinatii ushawishi wa dini hizi. Katika nchi kama hizo, basi, msiwatume watu wa ziada kuhubiri injili huko; inatosha kwa makanisa ya eneo hilo pekee kuhubiri injili. Katika baadhi ya nchi, hali inatofautiana katika majimbo au mikoa tofauti, na sheria na taratibu za eneo hilo zinatofautiana na sheria na taratibu za kitaifa. Kwa mfano, maeneo fulani yana mazingira maalum ya kidini, na katika maeneo hayo, kanisa na serikali vimeunganishwa. Katika baadhi ya hali, viongozi wa kidini wana mamlaka makubwa hata zaidi kuliko maafisa wa serikali ya eneo hilo na wanaweza kukiuka baadhi ya sera za kitaifa waziwazi. Ukihubiri injili katika maeneo kama hayo, kutakuwa na hatari zinazoweza kutokea za kiusalama. Hatari hizi zinazoweza kutokea haziishii tu katika kutunga uvumi kukuhusu au kukufukuza—wanaweza pia kukukamata, kukufungia gerezani bila mashtaka, na hata kukutesa, kukulemaza au kukuua, na serikali haitaingilia kati. Kwa kweli, viongozi wa madhehebu mengi ya kidini wanachukia dini za nje. Kwa sababu ushawishi wao ni mkubwa mno na hawazuiliwi na sheria kwa vyovyote vile, hakuna anayethubutu kuwawajibisha haijalishi wanawatesa wafanyakazi wa injili kikatili kiasi gani, na hata maafisa wa serikali ya eneo hilo hawataki kuwaudhi. Punde tu unapoanza kuhubiri injili katika eneo lao, wanaweza kukutesa kwa namna yoyote wanayotaka. Kwa hivyo, viongozi na wafanyakazi lazima wawe waangalifu hasa wanapowatuma watu kuhubiri injili mahali fulani. Kwanza, lazima wachunguze na wafahamu hali katika eneo hilo—kama kuna uhuru wa imani, jinsi nguvu za kidini zilivyo na ushawishi, na ni madhara gani yanayoweza kutokea watu wanaohubiri injili huko wakiripotiwa. Mambo haya lazima yaeleweke wazi kabla ya kuamua iwapo wawatume watu huko au la. Ikiwa, baada ya kufahamu kuhusu eneo fulani, itaamuliwa kwamba halifai kwa kuhubiri injili, basi hakuna anayeruhusiwa kuwatuma watu kuhubiri huko. Hii pia ni sehemu ya kazi inayopaswa kufanywa ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa injili. Baadhi ya viongozi na wafanyakazi wana ufahamu potofu, na wanasema, “Ni sawa; Mungu atatulinda. Kadiri changamoto inavyokuwa ngumu, ndivyo tunavyopaswa kuikabili zaidi. Kuna watu wengi sana wanaomwamini Bwana katika eneo hilo, kwa hivyo kwa nini tusiende kuhubiri injili huko?” Mtu fulani anawaambia, “Kuna magereza ya kibinafsi huko. Tukienda huko kuhubiri injili, si tu kwamba tutazuiliwa, bali tunaweza hata kufia huko. Hatuwezi kwenda!” Viongozi hao wa uwongo wapumbavu wanawaza kuhusu hili, “Joka kubwa jekundu lina magereza mengi sana, lakini hatuliogopi—hivyo kwa nini tuogope kundi la magereza ya kibinafsi huko? Magereza yanaweza kuifunga miili yetu lakini hayawezi kuifunga mioyo yetu! Msiogope—nendeni tu!” Kisha wanatuma wimbi baada ya wimbi la watu, na hatimaye, hakuna hata mmoja wao anayerudi; wote wanazuiliwa. Viongozi wa uwongo wanapigwa na butwaa. Tatizo ni gani hapa? (Viongozi wa uwongo kama hao ni wajinga.) Viongozi wa uwongo kama hao ni wahuni; ni wasiojukumika, wakiwatumbukiza watu kwenye meno ya hatari. Kwa nini hawaendi wenyewe? Kwa kuwa wao hawaogopi hatari, basi wanapaswa kwenda kwanza. Wakienda, warudi salama, na wawapate watu, basi wengine wanaweza kwenda baada yao. Bila kujali chochote, usalama wa watu lazima uhakikishwe katika kuhubiri injili. Msijiweke hatarini kabisa katika maeneo ambayo ni ya hatari na hayafai kwa kuhubiri injili. Msidhani kwamba mahali popote nje ya China bara ni salama; hii ni njozi, ufahamu potofu. Ni watu wajinga pekee ndio wanaofikiri namna hii—ni watu kama hao wanaelewa kiasi kidogo mno kuihusu dunia hii! Usidhani kwamba kwa sababu nchi nyingi sana za Magharibi zina uhuru wa imani na kuna watu wengi kwa ulinganisho wanaomwamini Bwana, unaweza kuhubiri injili waziwazi na kutoa kauli mbalimbali waziwazi zinazofichua jinsi ulimwengu wa kidini ulivyo na giza na ulivyo mwovu; ukifanya hivi, madhara yatakuwa yasiyofikirika. Lazima uelewe kwamba unapohubiri injili, iwe kwa watu wa dini au kwa wasio na dini, unawakabili binadamu wapotovu, binadamu wanaompinga Mungu. Usilifikirie suala hili kwa urahisi mno.
Viongozi na wafanyakazi wakitaka kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa injili, lazima wazingatie kikamilifu vipengele vyote vya suala hilo, na endapo tatizo lolote litatokea, linapaswa kushughulikiwa mara moja. Baadaye, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kupata uzoefu na mafunzo ili kupata kanuni na njia ya utendaji, wakiamua jinsi ya kutenda kwa siku za usoni—hiki pia ni kipengele muhimu cha kazi ambacho lazima kifanywe. Kuna baadhi ya mambo ambayo viongozi na wafanyakazi hawajayazingatia au kukumbana nayo hapo awali; baada ya matatizo kutokea, wanapaswa kufanya hitimisho: “Je, bado tunapaswa kwenda mahali pa aina hiyo? Je, njia hii ya kuwatuma watu ni sahihi? Je, tunapaswa kurekebisha mipango, mikakati, au mwelekeo kwa ajili ya hatua zinazofuata katika kuhubiri injili au kufanya kazi nyingine yoyote muhimu?” Katika mchakato endelevu wa kufanya mahitimisho, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuamua hatua kwa hatua mbinu na kanuni za kazi, ili kadiri wanavyozidi kufanya kazi hiyo, ndivyo inavyozidi kuwa mahususi na ndivyo inavyozidi kufikia kiwango kinachotarajiwa, kukiwa na matukio machache yasiyotarajiwa yanayotokea, au hakuna matukio yasiyotarajiwa yanayotokea, au hata, bila kuwaweka wafanyakazi wa kazi muhimu hatarini kwa namna yoyote ile. Ili kufikia matokeo haya, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kupata uzoefu mara kwa mara na kupata ufahamu wa mazingira na hali mbalimbali zinazokabiliwa katika mikoa mbalimbali wakati wa kuhubiri injili. Kadiri wanavyopata taarifa nyingi na kadiri zinavyokuwa sahihi, ndivyo kanuni na mipango ya kushughulikia mambo itakavyokuwa sahihi zaidi, na hatimaye kufikia matokeo ya kuhakikisha usalama wa watu. Kwa njia hii, inaweza kuhakikishwa kwamba kazi ya kuhubiri injili inaendelea kwa njia ya mfuatano.
III. Jinsi ya Kuwashughulikia Viongozi na Wafanyakazi Ambao Hawazingatii Kazi ya Usalama
Baadhi ya viongozi na wafanyakazi wana ubora duni wa tabia na wanakosa hisia ya kujukumika; hawawezi kufanya kazi halisi na pia ni wavivu mno kufanya kazi halisi. Katika maeneo wanayoyajukumikia, wale wanaofanya wajibu muhimu mara kwa mara hukumbana na hatari za kiusalama, zikiwahitaji kuhama au kuhamishwa, na kuwafanya washindwe kufanya wajibu wao kwa utulivu. Hata mambo ambayo hayapaswi kutokea hutokea mara kwa mara. Kwa mfano, kiongozi au mfanyakazi fulani anapata nyumba ya wenyeji ambayo iko katika eneo la bondeni. Mvua kubwa na mafuriko yanapotarajiwa, kwa kuhofia kwamba nyumba itazama, akina ndugu na dada wanaokaa hapo wanahitaji kuhama mapema—wakichukua vifaa vya kazi, vyungu, sufuria, na kila kitu kingine, wakihama kwa siku mbili mfululizo. Hili linamfanya kila mmoja achoke kabisa, huku vichwa vyao vikiwa vimeinama chini kwa kukata tamaa. Wanasema, “Tunahama kila baada ya siku chache, daima tukiwa mafichoni. Hili litaisha lini? Je, hatuwezi kupata nyumba salama na ya kutegemewa ambapo tunaweza kufanya wajibu wetu kwa kawaida?” Viongozi na wafanyakazi kama hao hawawezi hata kubeba kazi hii ndogo; akina ndugu na dada walio chini yao hawawezi kula wala kulala vizuri, wala hawana makazi ya kutosha. Hali zao za kuishi daima ni za muda, huku kila mtu akiwa tayari kukimbia janga wakati wowote. Punde tu wanapomaliza kutumia vitu vyao vya kila siku, wanavifunga haraka, kwa kuwa wakati wowote hali inaweza kutokea ambapo ukaguzi wa usajili wa kaya unatangazwa. Kwa kweli, kila mtu anajua hili linamaanisha kuchunguza kama kuna wale wanaomwamini Mungu, kwa hivyo lazima wawe tayari kuhamishwa wakati wowote. Kwa hivyo, wale wanaofanya wajibu wao daima wana hofu na hawana hisia ya usalama. Je, hili haliathiri matokeo ya wajibu wao? Je, si hili linahusiana na kazi ambayo viongozi na wafanyakazi wanafanya? (Ndiyo.) Wanafanyaje kazi hii? (Wanaifanya vibaya, hawatimizi jukumu lao.) Baadhi ya viongozi na wafanyakazi hawawajibiki na wanakosa kujitolea. Wao wenyewe hawana viwango vya juu vya hali za kuishi; mradi tu kuna mahali pa kuwakinga dhidi ya upepo na mvua, inatosha. Kwa hivyo, wao pia hawafanyi kila juhudi kutafuta mahali salama na tulivu kwa ajili ya akina ndugu na dada kuishi. Baadhi ya viongozi na wafanyakazi wana ubora duni wa tabia; hawajui ni mazingira ya aina gani yaliyo tulivu na yanayofaa kwa kuishi, au yanayofaa kwa akina ndugu na dada kufanya wajibu wao. Wanakodisha nyumba iliyo bondeni ambayo hakuna mtu mwingine anayetaka kuikodisha, na baada ya akina ndugu na dada kuhamia, ndani ya siku chache wanapata ukurutu, wakiwashwa mwili mzima. Ni kitu gani kinachoendelea? Nyumba ina unyevunyevu mno, huku maji yakipenya kutoka sakafuni. Je, kuna yeyote anayeweza kuishi mahali kama hapo? Viongozi na wafanyakazi kama hao hawawezi hata kutatua tatizo hili, hawawezi kupata nyumba inayofaa kwa kufanya wajibu—huu ni ubora wa tabia wa aina gani? Baadhi ya viongozi na wafanyakazi wengine hukodisha nyumba ambazo daima zinavuja mvua, zinaingiza upepo, hazizuii sauti, au hazina muunganisho wa mtandao, maji, wala umeme—mtu yeyote anawezaje kuishi huko? Wanapuuza nyumba nzuri na kusisitiza kukodisha hizi zenye kasoro—je, hili halikwamishi mambo? Ingawa akina ndugu na dada hawalali nje, huduma nyingi za msingi za nyumba hazipo; ingekuwa bora kwao kuishi hemani. Hata kama akina ndugu na dada wengi wamezoea ugumu, hata kama wanahisi kwamba kuvumilia kiwango hiki cha ugumu si jambo kubwa, na wanaweza kustahimili, je, kuteswa daima namna hii kila baada ya siku chache hakuathiri utendaji wao wa wajibu? Kwa hivyo, ikiwa viongozi na wafanyakazi wana ubora duni wa tabia na wanakosa hisia ya kujukumika, hawawezi kubeba kazi hii; wanapaswa kujiuzulu mara moja na wampendekeze mtu anayeweza kufanya kazi hii vizuri achukue nafasi, ili wasiathiri maisha na utendaji wa wajibu wa idadi kubwa ya wafanyakazi muhimu. Kuwapangia makazi wale wanaofanya wajibu muhimu hakuhitaji kuzingatia kila kipengele kimoja, lakini angalau mazingira ya msingi ya kuishi lazima yahakikishwe. Ni wakati tu kunapokuwa na uhakika katika suala hili ndipo kazi ya kanisa haitaathiriwa. Je, kazi hii ni rahisi kufanya? (Ndiyo.) Ni rahisi tu kusema ni rahisi kufanya, lakini ikiwa viongozi na wafanyakazi ni watu waliokanganyika vichwa walio na ubora duni wa tabia na wanakosa hisia yoyote ya kujukumika, hawawezi kuifanya kabisa. Wakati viongozi na wafanyakazi hawawezi kufanya kazi hii au hawawezi kuifanya vizuri, watu wengi sana huishia kuteseka sana matokeo ya jambo hili, wakiishi kila siku kana kwamba wanakimbia njaa—wanawezaje kufanya wajibu wao namna hii? Baadhi ya viongozi wa uwongo hawaelewi kanuni za ukweli lakini bado wanapenda kujionyesha. Hawawezi kufanya kazi vizuri lakini wanakataa kujiuzulu, waking’ang’ania nafasi yao na hawaondoki. Viongozi kama hao wanapaswa kushughulikiwaje? (Wanapaswa kuvuliwa wadhifa.) Kuwavua wadhifa ni rahisi; tatizo ni iwapo kuna mtu bora wa kuchukua kazi yao. Kama hakuna, je, ninyi mnaweza kubeba kazi hii? Je, mnaweza kuhakikisha kwamba wafanyakazi wa kazi muhimu wana mazingira tulivu ya kuishi? Ikiwa mtu mmoja hawezi kuimudu, je, ninyi watatu au watano mnaweza kushirikiana pamoja kubeba kazi hii? Ikiwa ninyi pia hamwezi kuimudu kazi hii—ikiwa hamwezi hata kufanya kazi rahisi kama hiyo, mkishindwa hata kuhakikisha mazingira ya msingi ya kuishi—basi lazima mvumilie kwa muda ugumu na mateso zaidi kidogo. Ikiwa bado mnaweza kushikilia kufanya wajibu wenu, na Mungu, akiona kwamba azimio lenu la kuvumilia ugumu ni thabiti vya kutosha, anamtuma mtu anayeshughulikia mambo kwa kutegemewa na anayeweza kutatua matatizo afanye kazi hiyo, basi siku zenu za mateso zitaisha na zitabadilishwa na nyakati nzuri. Ikiwa hakuna mtu kama huyu anayekuja kutatua matatizo haya, basi lazima mkubali hatima yenu—ninyi mmekusudiwa kuvumilia ugumu, mnapaswa kuuvumilia; lazima muitulize mioyo yenu na muuvumilie. Kwa kweli, kuvumilia ugumu huu kidogo kunafaa; ni bora zaidi kuliko kuwa gerezani na kupitia mateso. Angalau hamteswi wala kuhojiwa; bado mnaweza kusoma maneno ya Mungu, kufanya wajibu wenu, na kuishi maisha ya kanisa pamoja na akina ndugu na dada. Ingawa kuna hofu, vikwazo, na matatizo fulani njiani, na mara kwa mara mnalazimika kuhama, huu bado ni uzoefu wa kipekee katika maisha yenu, ambapo mnaweza kujifunza mafunzo na kupata kitu. Je, si hili ni jambo zuri kabisa? (Ndiyo.) Watu wanapaswa kuwa na azimio la kuvumilia ugumu, na kumwacha Mungu apange jinsi Apendavyo. Ikiwa kwa kweli hamwezi kuvumilia ugumu huu, mnaweza kumwomba Mungu kwa dhati mioyoni mwenu: “Mungu, tunakuomba Wewe ututazame sisi tunaoteseka—jinsi tulivyo wa kuhurumiwa! Tunakufuata Wewe bila malalamiko wala majuto! Tunakuomba Wewe, kwa kuzingatia uaminifu wetu usioyumbayumba Kwako, ukomeshe maisha haya ya ugumu! Tunakuomba Wewe utume kiongozi au mfanyakazi anayefaa ili atutafutie mahali panapofaa! Daima tunahangaika nje, tukihama kutoka mahali pamoja hadi pengine kila siku, na hatujui hili litaendelea kwa muda gani. Hatutaki kuhama-hama tena—tafadhali tutafutie makazi tulivu!” Je, inafaa kuomba kwa namna hii? Mnaweza kuomba kwa namna hii; kulingana na mahitaji ya mazingira, mnapaswa kuomba kwa namna hii.
Kuvumilia ugumu, kunapotazamwa kutoka pembe nyingine, si jambo baya sana; kuvumilia ugumu kiasi kunaweza kunoa utashi wako. Kunoa utashi wako kunamaanisha nini? Kunamaanisha kwamba kupitia kuvumilia ugumu huu daima, unakuwa usiyejali kuelekea ugumu huo na huutambui tena kama ugumu; haijalishi unavumilia ugumu kiasi gani, wewe huhisi maumivu tena. Hata hivyo, unapokabiliwa na hali, lazima ujifunze mafunzo fulani, upate umaizi fulani, na ujifunze jinsi ya kuwatambua watu. Ikiwa kiongozi au mfanyakazi ana ubora duni sana wa tabia na hawezi hata kufanya kazi ya kupanga makazi ipasavyo, anawezaje kuwaruzuku na kuwaongoza watu wateule wa Mungu? Watu kama hao hawafai kuwa viongozi au wafanyakazi. Nyumba ya Mungu haikosi pesa za kukodisha nyumba, na haiko tayari kuona akina ndugu na dada daima wakiwa hawana mahali maalum pa kuishi. Nyumba ya Mungu haitetei watu kuvumilia ugumu daima au kuishi maisha magumu kila siku, ingawa bila shaka haikwepi watu kuvumilia ugumu wowote pia. Lakini ikiwa viongozi na wafanyakazi hawawezi hata kushughulikia kazi ya kupanga makazi, na kufanya jambo lolote linalofaa kwa kweli ni kitu kigumu sana kwao, basi kuna kitu gani kilichobaki cha wao kujisifu? Kila mmoja wao anaonekana kuwa nadhifu, ana diploma, na ni mtu wa hadhi, lakini kushughulikia jambo hili dogo ni kitu kigumu sana kwao. Katika hali hiyo, hakuna kinachoweza kufanywa—unaweza tu kukikubali kutoka kwa Mungu. Huu ndio ugumu ambao watu wanapaswa kuvumilia; unapaswa kumwacha Mungu apange jinsi Apendavyo. Hili ni sahihi. Pengine siku moja, ugumu huu utafuatiwa na siku bora, na maisha ya aina hii hayataendelea tena. Haijalishi uko katika mazingira ya aina gani, unapaswa kudumisha mtazamo wa utii na kuepuka kulalamika. Ikiwa kiongozi au mfanyakazi fulani si wa kutegemewa na hafanyi kazi vizuri, usiruhusu hilo liathiri udhati na uaminifu wako kwa Mungu, na usiruhusu hilo liathiri utii wako kwa Mungu na mtazamo wako wa utii kwa Mungu. Kwa njia hii, utakuwa umesimama imara katika suala hili. Viongozi na wafanyakazi ni watu wa kawaida tu. Ikiwa wana ubora duni wa tabia na hawawezi kufanya kazi, au ikiwa wao ni viongozi wa uwongo ambao hawatimizi jukumu lao, hilo ni tatizo lao la kibinafsi na halihusiani na nyumba ya Mungu. Si nyumba ya Mungu iliyowaagiza watende kwa namna hii; ni kwamba tu wamefunuliwa kwa sababu ya kutojukumika kwao. Hawawezi kukamilisha kazi waliyokabidhiwa na nyumba ya Mungu, na hivyo wanaweza tu kuvuliwa wadhifa na kuondoshwa. Katika hali kama hizo, watu wateule wa Mungu wanapovumilia ugumu huu, lazima waukubali kutoka kwa Mungu na wamwache Mungu apange jinsi Apendavyo. Hata kama viongozi na wafanyakazi hawajafanya kazi vizuri au wana matatizo yoyote, ukweli kwamba Mungu ndiye ukweli, njia, na uzima haubadiliki milele. Kumfuata kwako Mungu, kumtii kwako Mungu, na kukubali kwako maneno ya Mungu hakupaswi kubadilika kamwe. Hizi ni kweli za milele. Unapokuwa ukifanya wajibu wako, haijalishi ni mambo gani yasiyopendeza yanayotokea, unapaswa kuyakubali kutoka kwa Mungu na ujifunze mafunzo yaliyo ndani ya hayo. Unapaswa kujituliza mbele za Mungu na kumwomba Yeye, na usijiruhusu uathiriwe na ulimwengu wa nje. Lazima ujifunze kuzoea mazingira mbalimbali na ujifunze kupitia kazi ya Mungu katika mazingira ya kila aina. Ni kwa njia hii tu ndiyo unaweza kufikia kuingia katika uzima. Watu wengine wana kimo kidogo; ugumu unapotokea, wanalalamika na kuwa na wasiwasi, wakihisi kufadhaika na kupoteza imani katika Mungu—huu ni upumbavu na ujinga uliokithiri! Viongozi na wafanyakazi ambao hawafanyi kazi halisi wamefichuliwa na kuondoshwa, lakini hilo linakuhusu nini? Kwa nini wewe uwe hasi na ujitenge na Mungu kwa sababu tu walipanga mambo kwa namna isiyofaa? Je, si huu ni uasi kabisa? (Ndiyo.) Watu wanapofanya jambo baya, unaweza kuwatambua na kuwakataa, lakini usimkatae Mungu wala kuukataa ukweli. Ukweli haukosei, Mungu hakosei. Nia ya asili ya Mungu si kwamba watu wavumilie ugumu kama huo; lakini kwa binadamu wapotovu, kuvumilia ugumu kiasi kwa kweli ni jambo muhimu. Kuvumilia ugumu kidogo kuna manufaa kwako; manufaa ni kwamba wewe unajifunza mafunzo na unajifunza kutafuta ukweli ili utatue matatizo. Ikiwa unaweza kuvumilia ugumu mbalimbali, unapata uvumilivu kiasi, na unakuwa na uwezo wa kusimama imara katika ushuhuda wako katika mazingira ya kila aina. Kuweza kuvumilia ugumu kunanoa azimio lako la kumtii Mungu. Hii ndiyo nia ya asili ya Mungu na matokeo ambayo Mungu anataka kuona ndani yako. Ikiwa unaweza kuelewa nia ya Mungu na kutenda kulingana na nia ya Mungu; ikiwa unaweza kujizuia kumtelekeza Mungu bila kujali unakumbana na watu au mazingira ya aina gani; na ikiwa unaweza kujifunza kutenda ukweli, kuwa na utii kwa Mungu, kuwa na ufahamu na mtazamo sahihi, kudumisha imani isiyobadilika katika Mungu, na kujizuia kumlalamikia Mungu au kujitenga na Yeye moyoni mwako, bila kujali mwili wako unavumilia mateso kiasi gani; basi wewe una kimo.
Viongozi na wafanyakazi lazima walinde usalama wa wale wanaofanya wajibu muhimu, wakiwakinga dhidi ya uingiliaji wa dunia ya nje. Kazi hii inahusisha vipengele vingi. Kwanza kabisa, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuelewa jinsi ya kutekeleza kazi hizi za kina kwa namna mahususi. Zaidi ya hayo, wanapokumbana na hali fulani maalum, lazima wafanye maamuzi sahihi, kisha watafute kanuni zinazofaa na waunde mipango mahususi ya kushughulikia hali hizo. Lengo kuu ni kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa kazi muhimu wa kila aina. Ni kwa njia hii tu ndiyo inaweza kuhakikishwa kwamba kazi ya kuhubiri injili inaendelea kwa namna ya mfuatano. Kuzingatia kanuni hii ni sahihi; hili ndilo lengo na kanuni ya viongozi na wafanyakazi katika kufanya kazi hii. Viongozi na wafanyakazi wakizingatia lengo na kanuni hii kwa usahihi, basi kimsingi wao wanafikia kiwango kinachohitajika katika kufanya kazi hii. Ni matatizo gani mengine yanayohusika katika kazi hii? Watu wengine husema, “Sijawahi kuwa kiongozi wala mfanyakazi hapo awali, wala sijakumbana na mambo ya aina hii. Sijui ninachopaswa kufanya katika kazi hii, na sijui jinsi ya kuifanya. Kwa hivyo, sihitaji kuifanya—nani anajali kama ninyi mko salama au la? Ninyi lishughulikieni wenyewe.” Je, inakubalika kwao kujiepusha tu na jambo hilo? (La, haikubaliki.) Viongozi na wafanyakazi kama hao wanapaswa kuondolewa. Ikiwa hufanyi kazi halisi, wewe una faida gani? Je, tunakuweka karibu kama pambo kwa sababu wewe unaonekana mzuri? Viongozi na wafanyakazi kama hawa lazima wavuliwe wadhifa na waondoshwe; hawapaswi kuruhusiwa kuchukua nafasi bila kufanya kazi yoyote. Viongozi wa uwongo hawafanyi kazi halisi—hawana dhamiri wala busara, sivyo? Ikiwa kwa kweli wangekuwa na dhamiri na busara, kwa nini wasingetafuta ukweli ili watatue matatizo yanapotokea? Hakuna mtu anayezaliwa akijua kila kitu; kila mtu anajifunza kadiri anavyoendelea. Ikiwa unaweza kutafuta ukweli, utapata njia ya kuifanya kazi hiyo vizuri. Ikiwa una hisia ya kujukumika, utafikiria njia ya kuifanya kazi hiyo vizuri. Kufanya kazi ya uongozi kwa kweli si jambo gumu; mradi tu mtu anaweza kutafuta ukweli, ni rahisi kufanya kazi vizuri. Zaidi ya hayo, viongozi na wafanyakazi wana wenzi; maadamu watu wawili au watatu wana moyo na nia moja, kazi yoyote ni rahisi kukamilisha. Kwa sasa, viongozi na wafanyakazi wengi wanajifundisha; wanajifundisha katika kutafuta ukweli katika mambo yote ili kutatua matatizo. Katika hatua hii, angalau baadhi ya viongozi na wafanyakazi wana uwezo katika kazi ya uongozi na wana uwezo kamili wa kufanya kazi ya kueneza injili vizuri, sivyo? (Ndiyo.) Kwa hivyo, tutafanya ushirika hadi kufikia hapa kwa leo. Kwaheri!
Julai 20, 2024