Majukumu ya Viongozi na Wafanyakazi (12)

Katika mkutano wetu uliopita, tulishiriki juu ya kipengele cha kumi cha majukumu ya viongozi na wafanyakazi: “Kulinda vizuri na kutenga kwa busara vitu mbalimbali vya nyumba ya Mungu (vitabu, vifaa mbalimbali, nafaka, na kadhalika), na kufanya ukaguzi, matengenezo, na ukarabati wa mara kwa mara ili kupunguza uharibifu na hasara; pia kuzuia watu waovu wasivimiliki.” Ushirika wa kipengele cha kumi ulihusu kazi ambayo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufanya na majukumu wanayopaswa kutimiza kuhusu vitu mbalimbali vya nyumba ya Mungu, na wakati huo huo, ulifichua udhihirisho mbalimbali wa viongozi wa uongo kwa ulinganishi. Viongozi na wafanyakazi wakitimiza majukumu wanayopaswa na wanayoweza kutimiza katika kila kipengele cha kazi ya nyumba ya Mungu, basi watakuwa wamefikia kiwango kinachohitajika kama viongozi na wafanyakazi; wasipotimiza majukumu yao na kufanya kazi yoyote halisi, basi ni dhahiri shahiri kuwa wao ni viongozi wa uwongo. Kuhusiana na kipengele cha kumi, viongozi wa uongo bila shaka hawafanyi vyema kazi ya kulinda wala kugawa kwa busara vitu yakinifu mbalimbali vya nyumba ya Mungu—vitu hivyo yakinifu havilindwi vizuri, au huenda visilindwe kabisa, na viongozi hao wa uwongo wanaweza kuchezea fungu lao. Huenda hata wasichukulie kazi hii kwa uzito hata kidogo. Ingawa ni kazi ya masuala ya jumla, bado ni jukumu ambalo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kulitimiza na kazi ambayo wanapaswa kuifanya. Bila kujali kama wanafanya kazi hiyo wao wenyewe, au kuwapangia watu wanaofaa kuifanya, na pia kuisimamia, kukagua, kufuatilia, na kadhalika, kwa vyovyote vile, kazi hii haiwezi kutenganishwa na majukumu ya viongozi na wafanyakazi—vinahusiana moja kwa moja. Kwa hivyo, inapofikia kazi hii, ikiwa viongozi na wafanyakazi hawalindi vizuri na kutenga kwa busara vifaa mbalimbali vya nyumba ya Mungu, basi hawatimizi majukumu yao na hawafanyi kazi yao vizuri. Hii ni mojawapo ya udhihirisho wa viongozi wa uwongo. Kwenye mkutano wetu uliopita, tulifichua na kufanya uchanganuzi wa kawaida wa udhihirisho ambao viongozi wa uongo huonyesha wanaposhughulikia kipengele hiki cha masuala ya jumla, na tukatoa mifano kadhaa. Iwapo mtu ni kiongozi wa uongo, basi hajatimiza kabisa majukumu yake katika kazi hii, na kazi anayoifanya haijafikia kiwango kinachohitajika. Hii ni kwa sababu viongozi wa uongo kamwe hawajitahidi katika kazi halisi—pindi tu inapopangwa, na kumaliza, hawaifuatilii kamwe wala kushiriki katika kazi hiyo. Sababu nyingine kuu ni kuwa viongozi wa uongo hawaelewi kanuni za kazi yoyote wanayofanya. Hata kama si walegevu katika kazi yao, wanachokifanya kinakinzana na kanuni na sheria ambayo nyumba ya Mungu inahitaji, au hata hakikubaliani kabisa na kanuni hizo. Je, kutokubaliana na kanuni kunamaanisha nini? Maana yake ni kwamba wanatenda kwa kutojali, wanatenda bila mpango, kulingana na mawazo yao, mapenzi yao, hisia zao, na kadhalika. Kwa hivyo, bila kujali chochote, kuna dhihirisho mbili kuu za viongozi wa uongo inapofikia kipengele hiki cha majukumu ya viongozi na wafanyakazi: La kwanza ni kwamba hawafanyi kazi halisi, la pili ni kwamba hawawezi kuelewa kanuni, kwa hivyo hawawezi kufanya kazi halisi. Huu ndio udhihirisho wa msingi. Kwenye mkutano wetu uliopita, tulishiriki na kufichua jinsi ubinadamu wa viongozi wa uongo hudhihirika wanaposhughulikia masuala ya jumla ya aina hii. Hata kwa kipande hiki rahisi cha kazi, viongozi wa uongo hawawezi kutimiza majukumu yao. Wana uwezo wa kuifanya kazi hii, lakini hawaifanyi. Hii inahusiana na tabia na ubinadamu wa watu wa aina hii. Je, ubinadamu wao una tatizo gani? Wao si wakweli na tabia yao ni mbaya. Kimsingi, tumemaliza ushirika wetu kuhusu majukumu ya viongozi na wafanyakazi, kanuni za jumla, na maonyesho mbalimbali ya viongozi wa uongo chini ya kipengele cha kumi. Leo, tutashiriki juu ya kipengele cha kumi na moja cha majukumu ya viongozi na wafanyakazi.

Kipengele cha Kumi na Moja: Kuwachagua watu wanaotegemewa ambao ubinadamu wao unafikia kiwango kinachostahili kwa ajili ya kazi ya kusajili, kujumlisha na kulinda matoleo kwa utaratibu; kupitia mara kwa mara na kuangalia mapato na matumizi ili visa vya ubadhirifu au uharibifu, pamoja na matumizi yasiyo ya busara, viweze kutambuliwa mara moja—kukomesha mambo kama hayo na kudai fidia inayofaa; zaidi ya hayo, kuzuia, kwa njia yoyote ile, matoleo yanayoanguka mikononi mwa watu waovu na kumilikiwa na wao

Sadaka Ni Nini

Maudhui ya kipengele cha kumi na moja cha majukumu ya viongozi na wafanyakazi ni: “Kuwachagua watu wanaotegemewa ambao ubinadamu wao unafikia kiwango kinachostahili kwa ajili ya kazi ya kusajili, kujumlisha na kulinda matoleo kwa utaratibu; kupitia mara kwa mara na kuangalia mapato na matumizi ili visa vya ubadhirifu au uharibifu, pamoja na matumizi yasiyo ya busara, viweze kutambuliwa mara moja—kukomesha mambo kama hayo na kudai fidia inayofaa; zaidi ya hayo, kuzuia, kwa njia yoyote ile, matoleo yanayoanguka mikononi mwa watu waovu na kumilikiwa na wao.” Majukumu ya viongozi na wafanyakazi katika kazi hii ni gani? Wanapaswa kufanya kazi gani kuu? (Kulinda sadaka vizuri). Kipengele cha kumi kilikuwa kuhusu kulinda vizuri na ugawaji wa busara vifaa mbalimbali vya nyumba ya Mungu; hiki kinahusu kulinda sadaka vizuri. Vitu mbalimbali vya nyumba ya Mungu na sadaka zake zinafanana kwa kiasi fulani—lakini, je, ni vitu sawa? (Hapana.) Tofauti ni nini? (Sadaka hasa zinahusu pesa.) Pesa ni kipengele kimoja cha sadaka. Vitu mbalimbali vya nyumba ya Mungu na sadaka vinatofautiana kwa namna gani kwa asili? Je, vitabu vya maneno ya Mungu ni sadaka? Je, mashine mbalimbali zinazotumika kwa kazi ni sadaka? Je, mahitaji mbalimbali ya kila siku ambayo nyumba ya Mungu hununua ni sadaka? (Hapana). Hivyo, vitu hivi ni nini, basi? Katika nyumba ya Mungu, vitabu vyote vya maneno ya Mungu, na aina zote za vitu vinavyohitajika kwa kazi yake ambayo inanunua kwa fedha zilizotolewa na wateule wa Mungu, vikiwemo vitu mbalimbali kama vile kamera, virekodi vya sauti, kompyuta, na simu za rununu—vyote hivi ni vitu vya nyumba ya Mungu. Zaidi ya hayo, meza, viti, benchi, vyakula, na mahitaji mengine ya kila siku kama hayo pia ni vitu vya nyumba ya Mungu. Baadhi ya vitu hivi hununuliwa na kina ndugu, na vingine, nyumba ya Mungu hununua kwa kutumia sadaka; vyote hivyo vinaainishwa kama vitu vya nyumba ya Mungu. Tulishiriki kuhusu mada hii kwenye mkutano wetu uliopita. Sasa tutaendelea na jambo muhimu ambalo tutalishiriki chini ya kipengele cha kumi na moja: sadaka. Sadaka ni nini hasa? Mawanda yake yanaelezwaje? Kabla ya kushiriki kuhusu majukumu ya viongozi na wafanyakazi, ni lazima tufafanue swali la, je, sadaka ni nini? Ingawa watu wengi walimwamini Yesu hapo zamani na wamekubali hatua hii ya kazi kwa miaka kadhaa, bado dhana zao kuhusu sadaka hazibainiki. Hawajaelewa vyema sadaka ni nini hasa. Wengine watasema kwamba sadaka ni pesa na mali zinazotolewa kwa Mungu, ilhali wengine watasema kwamba sadaka hasa zinamaanisha pesa. Maelezo gani kati ya haya ndiyo sahihi? (Almradi kitu kimetolewa kwa Mungu, bila kujali ni pesa au kitu chochote, kikubwa au kidogo, hicho ni sadaka). Huo ni muhtasari sahihi kwa kiasi fulani. Sasa kwa kuwa mawanda na mipaka ya sadaka vimeeleweka, hebu tuelezee sawasawa sadaka ni nini hasa, ili kila mtu aweze kufahamu waziwazi dhana hiyo.

Kuhusu suala la sadaka, Biblia inarekodi kwamba hapo mwanzo Mungu alimwambia mwanadamu atoe fungu la kumi kwa Mungu—hii ni sadaka. Bila kujali kiasi kilichotolewa kilikuwa kikubwa au kidogo, na bila kujali ni nini kilichotolewa—kiwe ni pesa au vitu—almradi kilikuwa ni sehemu ya kumi ya mapato ya mtu ambayo ilipaswa kutolewa, bila shaka hiyo ilikuwa sadaka. Hili ndilo jambo ambalo Mungu alitaka kwa mwanadamu, na ndilo waumini wa Mungu walipaswa kumtolea Mungu. Fungu hili la kumi ni kipengele kimoja cha sadaka. Watu wengine huuliza, “Je, fungu hilo la kumi linamaanisha tu pesa?” Si lazima. Kwa mfano, mtu akivuna nafaka kutoka ekari kumi, basi bila kujali kiasi cha nafaka kilichopatikana, thamani ya nafaka ya ekari moja inapaswa hatimaye kutolewa kwa Mungu—fungu hili la kumi ndilo watu wanapaswa kutoa. Kwa hivyo, dhana ya “fungu la kumi” haimaanishi pesa pekee—haimaanishi tu kuwa mtu akipata yuani elfu moja lazima amtolee Mungu mia moja—bali inamaanisha kila kitu ambacho watu hupata, ambacho kinajumuisha mambo mengi zaidi, yakiwemo mali na pesa. Hii ndiyo Biblia inazungumzia. Bila shaka, siku hizi nyumba ya Mungu haifuati Biblia kabisa katika kuwalazimu watu kutoa sehemu ya kumi ya kila kitu wanachokipata. Hapa ninashiriki tu na kueneza dhana na ufafanuzi wa “sehemu ya kumi,” ili watu wafahamu kwamba fungu la kumi ni kipengele kimoja cha sadaka. Siwashurutishi watu watoe sehemu ya kumi; kiasi ambacho watu watatoa kitategemea ufahamu na mapenzi yao binafsi, na nyumba ya Mungu haina masharti yoyote ya ziada kuhusu jambo hili.

Kipengele kingine cha sadaka ni vitu ambavyo watu humtolea Mungu. Kwa upana, bila shaka hii pia inajumuisha fungu la kumi; hasa, kando na fungu la kumi, kitu chochote ambacho watu humtolea Mungu kipo katika kundi la sadaka. Mawanda makubwa yanajumuisha vitu vinavyotolewa kwa Mungu, kwa mfano, vyakula, vitu vya nyumbani, mahitaji ya kila siku, virutubisho vya afya, pamoja na ng’ombe, kondoo, na kadhalika vilivyotolewa kwenye madhabahu katika nyakati za Agano la Kale. Hizi zote ni sadaka. Kitu fulani kuwa sadaka hutegemea nia ya yule anayekitoa; ikiwa mtu anayekitoa anasema kitu hiki kimetolewa kwa Mungu, basi bila kujali iwapo kimetolewa moja kwa moja kwa Mungu au kimewekwa katika nyumba ya Mungu kwa ajili ya kulindwa, kitu hicho kinaingia katika kundi la sadaka, na hakiwezi kuguswa kiholela na watu. Kwa njia ya mfano: mtu anaponunua kompyuta ya hali ya juu na kumtolea Mungu, inakuwa sadaka; mtu anapomnunulia Mungu gari, linakuwa sadaka; mtu anaponunua chupa mbili za virutubisho vya afya na kumtolea Mungu, basi chupa hizo zinakuwa sadaka. Hakuna ufafanuzi mahsusi na wenye mipaka wa vitu vinavyotolewa kwa Mungu. Kwa jumla, mawanda yake ni mpana sana—ni vitu vinavyotolewa kwa Mungu na wale wanaomfuata. Wengine huenda wakasema, “Sasa Mungu amepata mwili duniani, na vitu vinavyotolewa Kwake ni mali Yake—lakini ingekuwa vipi kama Asingekuwa duniani? Wakati Mungu yuko mbinguni, je, vitu vinavyotolewa Kwake si sadaka tena?” Je, hili ni sahihi? (Hapana). Hili halitegemei kama Mungu yuko katika kipindi cha kupata mwili au la. Kwa vyovyote vile, mradi kitu kinatolewa kwa Mungu, basi ni sadaka. Wengine huenda wakasema, “Kuna vitu vingi sana vinavyotolewa kwa Mungu. Anaweza kuvitumia? Anaweza kuvitumia vyote?” (Jambo hilo halimhusu mwanadamu). Hiyo ni njia sahihi na yenye busara ya kuieleza. Vitu hivi vinatolewa kwa Mungu na wanadamu; jinsi Anavyovitumia, kama Anaweza kuvitumia vyote au la, na jinsi Anavyovitenga na kuvishughulikia, haimhusu mwanadamu. Hakuna haja ya kuhangaika au kujisumbua kuhusu jambo hilo. Kwa ufupi, mara tu mtu anapomtolea Mungu kitu, kitu hicho kinaingia katika mawanda yamawanda ya sadaka. Ni cha Mungu, na hakina uhusiano wowote na mtu yeyote. Wengine huenda wakasema, “Kwa namna unavyosema, inaonekana kwamba Mungu anadai umiliki wa kitu hicho kwa nguvu.” Je, ni hivyo ndivyo ilivyo? (Hapana). Kitu hicho ni cha Mungu, hivyo kinaitwa sadaka. Watu hawawezi kukigusa au kukigawa kwa mapenzi yao. Wengine huenda wakauliza, “Je, hiyo si hasara?” Hata kama ni hivyo, hilo halikuhusu. Wengine huenda wakasema, “Wakati Mungu yuko mbinguni na hajapata mwili, Hawezi kufurahia au kutumia vitu ambavyo watu wanamtolea. Basi itafanywaje?” Jambo hilo hushughulikiwa kwa urahisi: Nyumba ya Mungu pamoja na kanisa vipo ili kushughulikia vitu hivi kulingana na kanuni; hakuuna haja ya kujisumbua au kuhangaika kuhusu jambo hilo. Kwa jumla, bila kujali kitu kinashughulikiwaje, mara tu kinapoingia katika kundi la sadaka, mara tu kinapoainishwa kama sadaka, hakina tena uhusiano na mwanadamu. Na kwa sababu kitu hicho ni cha Mungu, watu hawawezi kukifanyia watakavyo—kuna athari ya kufanya hivyo. Katika enzi ya Agano la Kale, wakati wa mavuno katika msimu wa vuli, watu walitoa aina mbalimbali za vitu kwenye madhabahu. Wengine walitoa nafaka, matunda, na mazao mengine mbalimbali, huku wengine wakitoa ng’ombe na kondoo. Je, Mungu alifurahia vitu hivyo? Anakula vitu hivyo? (Hapana). Unajuaje Hali vitu hivyo? Je, uliona? Hilo ni wazo lako tu. Unasema Mungu havili—haya, kama Angeonja kidogo, jambo hilo lingekufanya uhisi vipi? Je, jambo hilo lingekuwa kinyume na mawazo na fikra zako? Je, watu wengine hawaamini kwamba kwa kuwa Mungu hali wala kufurahia vitu hivyo, basi hakuna haja ya kuvitoa? Mnawezaje kuwa na hakika hivyo? Mnasema “Mungu hali vitu hivyo” kwa sababu mnafikiri kuwa Yeye ni mwili wa kiroho na hawezi kula, au kwa sababu mnafikiri kwamba Mungu ana utambulisho Wake kama Mungu, Yeye si wa mwili wala wa kufa, na kwa hivyo Hapaswi kufurahia vitu hivi? Je, ni aibu kwa Mungu kufurahia sadaka ambazo watu wanamtolea? (Hapana.) Basi, je, hilo ni kinyume na mawazo ya watu, au ni kinyume na utambulisho wa Mungu? Ni lipi hasa? (Watu hawapaswi kujadili jambo hili.) Hiyo ni kweli—hilo si jambo ambalo watu wanapaswa kujishughulisha nalo. Huhitaji kuamua kwamba Mungu lazima afurahie vitu hivyo, au kwamba hapaswi kuvifurahia. Fanya unachopaswa kufanya, timiza wajibu wako na majukumu yako, na utekeleze wajibu wako—hayo yanatosha. Utakuwa basi umekamilisha kazi yako. Kuhusu jinsi Mungu atakavyoshughulikia hivyo vitu, hiyo ni kazi Yake. Kama Mungu atashiriki vitu hivyo na watu, au kuviacha viharibike, kama Atafurahia sehemu ya hivyo vitu, au kuviona tu, jambo hilo si la kuhakikiwa, na ni halali. Mungu ana uhuru Wake kuhusiana na jinsi Anavyoshughulikia mambo haya. Si jambo ambalo watu wanapaswa kujihusisha nalo, wala si jambo ambalo wanapaswa kutoa maoni kulihusu. Watu hawapaswi kuwaza kiholela kuhusu mambo haya, sembuse kutoa maoni au uamuzi kuyahusu. Sasa mmeelewa? Mungu anapaswa kushughulikiaje sadaka ambazo watu wanamtolea? (Atazishughulikia jinsi Atakavyo.) Hiyo ni kweli. Watu wanaoelewa jambo hili kwa namna hiyo wana mantiki ya kawaida. Mungu atashughulikia vitu hivi kwa namna yoyote Atakayo. Anaweza kuviangalia tu kidogo, au Asivitazame wala kuvijali hata kidogo. Jishughulishe tu na kutoa sadaka wakati wa jambo hilo unapofika, na kutoa sadaka unapotaka, kulingana na mahitaji ya Mungu, na kutimiza majukumu ya mwanadamu. Usijihusishe na jinsi Mungu anavyoshughulikia au kutendea mambo kama hayo. Kwa ufupi, inatosha kama kile unachokifanya kiko ndani ya mawanda ya mahitaji ya Mungu, kinaendana na kiwango cha dhamiri, na kinaambatana na wajibu, masharti, na majukumu ya mwanadamu. Kuhusu jinsi Mungu anavyosimamia na kushughulikia vitu hivi, hilo ni shauri Yake Mwenyewe, na watu hawapaswi kabisa kutoa maoni au maamuzi kuhusu jambo hilo. Mlifanya kosa kubwa ndani ya sekunde chache tu. Niliwauliza ikiwa Mungu hufurahia au hula vitu hivi, nanyi mkasema Yeye hali wala kuvirufahia. Kosa lenu lilikuwa lipi? (Kumhukumu Mungu.) Lilikuwa kuweka mipaka na kutoa hukumu kwa pupa, na jambo hilo linathibitisha kwamba bado watu wana madai moyoni mwao dhidi ya Mungu. Kwao, ni kosa Mungu kufurahia hivi vitu, na pia ni kosa Asipovifurahia. Akivifurahia, watasema, “Wewe ni mwili wa kiroho, si mwenye mwili wala kiumbe cha kufa. Kwa nini Ufurahie hivi vitu? Hilo ni jambo lisilowazika kabisa!” Na ikiwa Mungu hatilii maanani hivi vitu, basi watu watasema, “Tumejitahidi kwa bidii kukutolea mioyo yetu, ila vitu tulivyokutolea Huwezi hata kuvitazama. Je, Unatujali kweli?” Hapa, pia, watu wana jambo la kusema. Huku ni kukosa mantiki. Kwa muhtasari, watu wanapaswa kuchukulia jambo hili kwa mtazamo gani? (Watu wanapaswa kumtolea Mungu kile wanachopaswa kumtolea, na kuhusu jinsi Mungu atakavyoshughulikia vitu hivyo, watu hawapaswi kuwa na mawazo wala fikira zozote kuhusu jambo hilo hata kidogo, wala hawapaswi kutoa maoni juu yake). Ndiyo—hiyo ndiyo mantiki ambayo watu wanapaswa kumiliki. Hii inahusiana na vitu vinavyotolewa kwa Mungu, ambavyo pia ni kipengele kimoja cha sadaka. Vitu vinavyotolewa kwa Mungu vinajumuisha mambo anuwai. Hii ni kwa sababu watu wanaishi katika ulimwengu wa vitu yakinifu, na kando na pesa, dhahabu, fedha, na vito, kuna vitu vingi zaidi wanavyodhania kuwa vizuri sana na vya thamani, na watu fulani wanapomkumbuka Mungu au kufikiria kuhusu upendo wa Mungu, wako tayari kutoa kile wanachoona kuwa ghali na cha thamani kwa Mungu. Vitu hivi vinapotolewa kwa Mungu, vinaingia katika mawanda ya sadaka; vinakuwa sadaka. Na wakati huo huo vinapokuwa sadaka, ni juu ya Mungu kuvishughulikia—watu hawawezi kuvigusa, haviko chini ya madaraka ya watu, wala haviwezi kuwa mali ya watu. Mara tu unapomtolea Mungu kitu, kinakuwa mali ya Mungu, si juu yako kukishughulikia, na huwezi tena kuingilia kitu hicho. Bila kujali jinsi Mungu anavyokisimamia au kukishughulikia, hakihusiani na mwanadamu. Vitu vilivyotolewa kwa Mungu pia ni kipengele cha sadaka. Watu wengine huuliza, “Je, ni pesa pekee pamoja na dhahabu, fedha, na vito vya thamani tu ndivyo vinaweza kuwa sadaka? Tuseme mtu ametoa jozi ya viatu, jozi ya soksi, au jozi ya pedi za viatu kwa Mungu—je, vitahesabiwa kama sadaka?” Tukifuata ufafanuzi wa sadaka, haijalishi kitu hicho ni kikubwa au kidogo, au ni ghali au ni cha bei nafuu—hata kama ni kalamu au kipande cha karatasi—almradi kimetolewa kwa Mungu, ni sadaka.

Kuna kipengele kingine cha sadaka: vitu yakinifu vinavyotolewa kwa nyumba ya Mungu na kanisa. Vitu hivi pia vinaingia katika kundi la sadaka. Vitu hivi vya mali vinajumuisha nini? Tuseme, kwa mfano, mtu alinunua gari, na baada ya kuliendesha kwa muda, alihisi limezeeka kidogo, kisha akanunua jingine jipya, na kutolea nyumba ya Mungu gari la zamani, ili nyumba ya Mungu ilitumie katika kazi yake. Gari hilo basi ni mali ya nyumba ya Mungu. Vitu vinavyomilikiwa na nyumba ya Mungu vinapaswa kuainishwa kama sadaka—hii ni kweli. Bila shaka, vyombo na vitu yakinifu sivyo vitu pekee vinavyotolewa kwa kanisa na nyumba ya Mungu; kuna vitu vingine pia, na wigo huu ni mpana kiasi. Watu wengine husema, “Sehemu ya kumi ya kila kitu wanachopata ambayo watu hutoa ni sadaka, sawia na pesa na vitu vinavyotolewa kwa Mungu; hatuna pingamizi hivi vitu vikiainishwa kama sadaka, hakuna kitu chochote chenye shaka kuhusu jambo hili. Lakini ni kwa nini vitu vinavyotolewa kwa kanisa na nyumba ya Mungu pia vinaingia katika kundi la sadaka? Hilo halieleweki.” Niambie, je, kuanishwa kwao kama sadaka kunaleta maana? (Ndiyo.) Na mbona mnasema hivyo? (Kanisa lipo tu kwa sababu Mungu yupo, na kwa hivyo chochote kinachotolewa kwa kanisa pia ni sadaka). Kwa hakika. Kanisa na nyumba ya Mungu ni mali ya Mungu, na vipo tu kwa sababu Mungu yupo; kuna mahali pa kina ndugu kukusanyika na kuishi kwa sababu tu kanisa lipo, na matatizo yote ya kina ndugu yana pahali yanaweza kutatuliwa, na kina ndugu wana nyumbani ya kweli pekee, kwa sababu kuna nyumba ya Mungu. Yote haya yapo tu kwa msingi wa uwepo wa Mungu. Watu hawatoi vitu kwa kanisa na kwa nyumba ya Mungu kwa sababu watu kanisani wanamwamini Mungu na ni washirika wa nyumba ya Mungu—hiyo si sababu sahihi. Ni kwa sababu ya Mungu ndiyo watu hutoa vitu kwa kanisa na nyumba ya Mungu. Hii ina maana gani? Nani angetoa vitu kwa kanisa kwa urahisi isipokuwa kwa sababu ya Mungu? Bila Mungu, kanisa halingekuwepo. Watu wanapokuwa na vitu ambavyo hawavihitaji au ambavyo vimezidi mahitaji, wangevitupa au kuviacha visitumike; baadhi ya vitu pia vingeuzwa. Njia hizi zote zinaweza kutumika kushughulikia vitu hivi, sivyo? Basi kwa nini watu hawavishughulikii kwa njia hizi—kwa nini, badala yake, wanavitoa kwa kanisa? Je, si kwa sababu ya Mungu? (Ndiyo). Watu hulipa kanisa vitu hasa kwa sababu Mungu yupo. Kwa hivyo, chochote kinachotolewa kwa kanisa au nyumba ya Mungu kinapaswa kuainishwa kama sadaka. Watu wengine husema, “Ninatoa kitu hiki changu kwa kanisa.” Kutoa kitu hicho kwa kanisa ni sawa na kukitoa kwa Mungu, na kanisa pamoja na nyumba ya Mungu vina mamlaka kamili juu ya usimamizi wa vitu kama hivyo. Unapotolea kanisa kitu chochote, huwezi tena kuwa na uhusiano wowote nacho. Nyumba ya Mungu na kanisa itatenga, itatumia, na kushughulikia vitu hivi kwa busara kulingana na kanuni zilizowekwa na nyumba ya Mungu. Basi, kanuni hizi hutoka wapi? Zinatoka kwa Mungu. Kimsingi, kanuni ya matumizi ya vitu hivi ni kwamba vinapaswa kutumika kwa mpango wa usimamizi wa Mungu, na kwa ajili ya kueneza injili ya kazi ya Mungu. Havikusudiwi kwa matumizi ya mtu yeyote binafsi, sembuse kundi lolote la watu, bali ni vya kutumika kwa ajili ya kazi ya kueneza injili na kwa vitu mbalimbali ya kazi ya nyumba ya Mungu. Kwa hivyo, hakuna mtu aliye na haki ya kutumia vitu hivi; kanuni na msingi pekee wa matumizi na ugavi ni kuvitumia kulingana na kanuni za nyumba ya Mungu. Hili ni jambo la mantiki na linalofaa.

Hizi ndizo sehemu tatu za ufafanuzi wa sadaka, ambazo kila moja ni ufafanuzi wa kipengele kimoja cha sadaka, na kipengele kimoja cha mawanda yake. Sasa nyote mmeelewa sadaka ni nini, sivyo? (Ndiyo). Hapo awali kulikuwepo baadhi waliokuwa wakisema, “Kitu hiki si pesa, na yule mtu aliyekitoa hakusema ni cha Mungu. Alisema tu kuwa alikitoa. Kwa hivyo, hakiwezi kuwa cha matumizi ya nyumba ya Mungu, wala kukitoa kwa Mungu.” Na kwa hivyo, hawakukiandika na walikitumia kisiri jinsi wapendavyo. Je, hilo ni jambo lenye mantiki? (Hapana). Walilolisema lenyewe si la busara; walisema pia, “Sadaka zinazotolewa kwa kanisa na nyumba ya Mungu ni mali ya pamoja—mtu yeyote anaweza kuzitumia,” jambo ambalo bila shaka si lenye mantiki. Baadhi ya watu waovu na wenye mioyo yenye tamaa na shauku isiyo sahihi huchukua fursa hiyo na kufikiria kujitwalia vitu hivyo hasa kwa sababu watu wengi hawana ufahamu uliowazi na sahihi kuhusu ufafanuzi na dhana ya sadaka. Sasa kwa kuwa mmeelewa vizuri ufafanuzi halisi na dhana ya sadaka, mtakuwa na utambuzi wa kutosha mtakapokutana na matukio na watu wa aina hiyo katika siku zijazo.

Majukumu ya Viongozi na Wafanyakazi Kuhusu Kulinda Sadaka

I. Kulinda Sadaka Ipasavyo

La kufuata, hebu tuangalie ni majukumu gani hasa ambayo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kutimiza inapofikia kulinda sadaka. Kuhusu sadaka, lazima kwanza viongozi na wafanyakazi waelewe sadaka ni nini. Watu wanapotoa sehemu ya kumi ya mapato yao, hiyo ni sadaka; wanaposema wazi kwamba wanamtolea Mungu pesa au vitu, hizo ni sadaka; wanaposema wazi kwamba wanalitolea kanisa na nyumba ya Mungu kitu, hicho pia ni sadaka. Pindi wanapoelewa maana na dhana ya sadaka, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufahamu vyema kabisa sadaka zinazotolewa na watu na kuzisimamia, na kuhakiki suala hili. Kwanza, wanapaswa kuwatafuta watu wa kutegemewa ambao ubinadamu wao umefikia kiwango kinachostahili ili wafanye kazi ya waangalizi ili kuhifadhi kumbukumbu za sadaka kwa utaratibu na kulinda sadaka. Hili ndilo jukumu la kwanza katika kazi ambayo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufanya. Wasimamizi hawa wa sadaka huenda wakawa watu wenye ubora wa tabia wa wastani na wasioweza kuwa viongozi wala wafanyakazi, lakini watakuwa wa kutegemewa; na hawatabadhiri chochote, kikiwa mikononi mwao, sadaka hazitapotea wala kuchanganyika, bali zitalindwa ipasavyo. Kuna kanuni katika mipango kuhusiana na jambo hili. Ni lazima mtu atakayeifanya awe mtu wa kutegemewa ambaye ubinadamu wake ni wa kiwango kinachostahili. Watu wenye ubinadamu duni wanapokiona kitu kizuri, wanakitamani, na daima hutafuta nafasi ya kujipatia. Liwe liwalo, wao kila mara hutafuta namna ya kujinufaisha. Watu wa aina hii hawawezi kutumika. Mtu ambaye ubinadamu wake ni wa kiwango kinachostahili lazima angalau awe mtu mwaminifu, mtu anayeaminiwa na watu. Akipewa jukumu la kulinda sadaka au kusimamia mali za kanisa, atalitekeleza vyema, kwa umakini, kwa bidii, na kwa uangalifu mkubwa. Ana moyo wa kumcha Mungu, na hatavitumia vibaya vitu hivyo, wala kuvikopesha, na kadhalika. Kwa ufupi, unaweza kuwa na hakika kwamba ukimkabidhi sadaka, hakuna hata senti moja itakayopotea na hakuna kitu chochote kitakachopotea. Ni lazima mtu wa aina hii atafutwe. Zaidi ya hayo, nyumba ya Mungu ina amri kwamba si mtu mmoja tu wa aina hiyo anayepaswa kutafutwa; ni bora wawe wawili au watatu—wengine wao wahifadhi kumbukumbu, na wengine wafanye ulinzi. Pindi watu hawa wanapopatikana, sadaka zinapaswa kuainishwa, na kumbukumbu za mfumo zinazoonyesha ni nani anayehifadhi kundi gani la kitu zinapaswa kutengenezwa, na ni kiasi gani wanachohifadhi. Pindi watu wanaofaa wanapopatikana na vitu kuhifadhiwa na kusajiliwa katika makundi, je, huo ndio mwisho wa kazi? (Hapana.) Basi ni nini kinapaswa kufanywa baada ya hapo? Akaunti za mapato na matumizi lazima zikaguliwe kila baada ya miezi mitatu hadi mitano ili kuona kama ziko sahihi—yaani, kama mhifadhi wa kumbukumbu ameziandika kwa usahihi, kama kuna kitu kilichosahaulika kiliposajiliwa, kama idadi kwa jumla inalingana na akaunti za mapato na matumizi, na kadhalika. Kazi kama hii ya uhasibu lazima ifanywe kwa uangalifu sana. Viongozi na wafanyakazi ambao hawaelewi vyema kazi kama hii wanapaswa kumpa mtu aliye na ujuzi kiasi kazi hiyo ili aifanye, kisha wafanye ukaguzi wa mara kwa mara na kusikiliza ripoti zake. Kwa jumla, iwe wanaelewa au hawaelewi kazi ya uhasibu na upangaji wa jumla, hawawezi kuacha kazi ya kulinda sadaka bila anayeiangalia, wala hawawezi kuipuuza na kutoiulizia. Badala yake, ni lazima wafanye ukaguzi wa mara kwa mara, wakiuliza jinsi akaunti zilizokaguliwa zilivyo na kama zinalingana, kisha wakague kwa ghafla baadhi ya kumbukumbu za matumizi ili kuona hali ya matumizi ya hivi karibuni imekuwaje, kama kumekuwa na ufujaji wowote, hali ya uwekaji wa hesabu, na kama mapato yanalingana na matumizi. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuwa na usimamizi thabiti wa hali hizi zote. Hili ni mojawapo ya majukumu yanayohusiana na kulinda sadaka. Je, unaweza kusema jukumu hili ni rahisi? Je, lina changamoto kiwango fulani? Baadhi ya viongozi na wafanyakazi husema, “Sipendi hesabu; kichwa changu huuma ninapoziona.” Basi, tafuta mtu anayestahili akusaidie katika ukaguzi na usimamizi; mwambie akusaidie kuchunguza haya masuala. Huenda usipende au usiwe na ustadi katika kazi hii, lakini ukijua jinsi ya kuwatumia watu na kufanya hivyo kwa usahihi, bado utaweza kufanya kazi hii vizuri. Watumie watu wanaostahili kufanya kazi hiyo, na usukilize tu ripoti zao. Hilo pia linakubalika. Shikilia kanuni hii: Fanya ukaguzi wa mara kwa mara na ulinganishe mali zote zilizohifadhiwa pamoja na mtu anayepewa jukumu la kazi hiyo, kisha uliize maswali machache kuhusu matumizi muhimu—je, unaweza kutimiza hayo? (Ndiyo.) Kwa nini viongozi na wafanyakazi lazima wafanye kazi hii? Kwa sababu ni kulinda sadaka—na hilo ni jukumu lako.

Sadaka ambazo watu humtolea Mungu ni ya kufurahiwa na Mungu, lakini, je, Mungu huzitumia? Je, Mungu ana matumizi ya pesa hizi au vitu hivi? Je, sadaka hizi kwa Mungu hazikusudiwi kutumika kusambaza kazi ya injili? Je, hazikusudiwi kugharamia gharama zote za kazi ya nyumba ya Mungu? Kwa kuwa zinahusiana na kazi ya nyumba ya Mungu, usimamizi na matumizi ya sadaka hizo zote vinahusisha majukumu ya viongozi na wafanyakazi. Haijalishi ni nani anayetoa pesa hii au vitu hivi vinatoka wapi, almradi vinamilikiwa na nyumba ya Mungu, unapaswa uvisimamie vizuri, na ufuatilie kazi hii, uikague na kuijali. Ikiwa sadaka zinazotolewa kwa Mungu haziwezi kutumika ipasavyo kueneza kazi ya injili ya Mungu, bali zinafujwa kwa utukutu na kutumiwa vibaya, au hata kutwaliwa na kuchukuliwa na watu waovu, je, hilo linafaa? Je, hilo ni kosa la kutelekeza majukumu kwa upande wa viongozi na wafanyakazi? (Ndiyo.) Ni kutelekeza majukumu kwa upande wao. Kwa hivyo, viongozi na wafanyakazi lazima wafanye kazi hii. Hawana budi. Kusimamia vizuri sadaka, na kuwezesha zitumike ipasavyo katika kueneza kazi ya injili na katika kazi yoyote inayohusiana na usimamizi wa Mungu, ni jukumu la viongozi na wafanyakazi, na ni jambo lisilopaswa kupuuzwa. Ndugu huweza kujitahidi sana kuweka akiba kiasi kidogo cha pesa ili wamtolee Mungu. Tuseme kwamba, kwa sababu ya viongozi na wafanyakazi kuwa wazembe na wavivu katika kutekeleza wajibu wao, pesa hizi zianguke mikononi mwa watu waovu—itabadhiriwa na kufujwa bila kujali na watu hao waovu, au hata kuziteka kabisa. Kwa hivyo, viongozi na wafanyakazi hawatakuwa na pesa za kutosha gharama za kusafiri au za kujikimu, na hata hakuna pesa za kutosha ifikapo wakati wa kuchapisha vitabu vya maneno ya Mungu au kununua vifaa na zana muhimu. Je, huku si kuchelewesha kazi? Pesa zinapotolewa na ndugu na kuchukuliwa na watu waovu badala ya kutumiwa ipasavyo, na pesa zinahitajika kutumika kwa kazi ya nyumba ya Mungu, lakini hazitoshi, je, kazi hiyo haijazuiwa? Je, viongozi na wafanyakazi wameshindwa kutimiza jukumu lao? (Ndiyo.) Kwa sababu viongozi na wafanyakazi wameshindwa kutimiza jukumu lao na hawajasimamia sadaka vizuri, na hawajakuwa watumishi wazuri au kuwa na shauku ya kutimiza jukumu lao, hasara imepatikana kwenye sadaka na baadhi ya kazi za kanisa zimetumbukia katika hali ya kupooza au kusitishwa kwa muda. Je, si viongozi na wafanyakazi waliosababisha haya wenyewe? Huu ni uovu. Huenda ikawa hujanyakua, kufuja, au kutumia vibaya hizi sadaka, na huenda hujaziweka mfukoni mwako, lakini hali hii imetokea kwa sababu ya uzembe wako na kutelekeza wajibu wako. Je, unapaswa kuwajibikia jambo hili? (Ndiyo.) Huu ni wajibu mkubwa sana kuwajibikia!

II. Kukagua Hesabu

Katika kazi yao, mbali na kutekeleza mipango mbalimbali ya kazi ipasavyo na kuweza kushiriki ukweli ili kutatua matatizo, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kulinda sadaka vizuri. Wanapaswa kuwatafuta watu wanaostahili, kulingana na masharti ya nyumba ya Mungu, kufanya usimamizi wa kimfumo wa sadaka, na mara kwa mara, wanapaswa kukagua akaunti. Wengine huuliza, “Nitawezaje kuzikagua wakati hali ya mambo hairuhusu?” “Hali ya mambo hairuhusu”—je, hiyo ni sababu ya kutokagua akaunti? Unaweza kuzikagua hata kama hali ya mambo hairuhusu; kama huwezi kwenda mwenyewe, ni lazima umtume mtu anayeaminika na anayefaa kufanya usimamizi, na kuona kama msimamizi analinda sadaka kwa njia inayofaa, kama kuna tofauti zozote katika akaunti hizo, kama msimamizi huyo ni wa kutegemewa, hali yake imekuwaje hivi karibuni na kama amekuwa na hali ya uhasi, kama aliwahi kuhisi hofu alipokabiliana na hali fulani, na kama kuna uwezekano wa usaliti. Tuseme kwamba umesikia kuwa familia yake imekuwa na ugumu wa kupata pesa—je, inawezekana kwamba anaweza kuiba sadaka? Kupitia ushirika na kuchunguza hali hiyo, unaweza kuona kwamba msimamizi huyo ni mwaminifu kabisa, kwamba anajua sadaka hazipaswi kuguswa, na kwamba, bila kujali familia yake imekuwa na ugumu kiasi gani wa kupata pesa, hajawahi kugusa sadaka hizo, na baada ya kipindi kirefu cha uangalizi, inaweza kuthibitishwa kwamba msimamizi huyo anaaminika kabisa. Zaidi ya hayo, ni lazima ichunguzwe kama mazingira yanayozunguka nyumba ambako sadaka zinahifadhiwa ni hatari, kama kuna ndugu ambao wamekamatwa humo na joka kubwa jekundu, kama msimamizi wa sadaka amekumbana na hatari yoyote, kama sadaka zinahifadhiwa katika sehemu inayofaa, na kama zinapaswa kuhamishwa au la. Mazingira na hali za nyumba za wasimamizi wa sadaka lazima zichunguzwe mara kwa mara, ili majibu na mipango inayofaa iweze kufanywa wakati wowote. Unapokuwa ukifanya hili, pia unapaswa kufanya uchunguzi mara kwa mara kuhusu timu ambazo zimepata vifaa vipya hivi karibuni, na jinsi vifaa hivyo vilipatikana. Iwapo vilinunuliwa, lazima uulize kama mtu yeyote alihakiki maombi na kuyaidhinisha kabla ya kununuliwa, kama vilinunuliwa kwa bei ghali au bei ya kawaida ya sokoni, kama pesa zisizo za lazima zimetumika, na kadhalika. Tuseme kwamba, hakuna matatizo yaliyopatikana kwenye vitabu baada ya kukagua na kuhakiki akaunti, lakini imegunduliwa kwamba baadhi ya wanunuzi wamekuwa wakitumia vibaya sadaka mara kwa mara kwa ubadhirifu. Haijalishi kitu ni cha bei ghali kiasi gani, watakinunua; zaidi ya hayo, wanapojua vyema kwamba bidhaa fulani itauzwa kwa bei nafuu, kwamba bei yake itapunguzwa, hawasubiri, badala yake wanainunua papo hapo, na watanunua bidhaa bora, ya hali ya juu, na ya mifumo ya kisasa zaidi. Wanunuzi hawa hutumia pesa bila maadili na kwa njia ya ubadhirifu, na wanatumia sadaka kuinunulia nyumba ya Mungu vitu kana kwamba wanamfanyia adui wao mambo. Hawanunui kamwe vitu vya utendaji kulingana na kanuni, bali wanatafuta duka lolote na kununua vitu papo hapo bila kujali gharama au ubora wake. Mara tu vifaa vinapoletwa, vinaharibika baada ya kutumiwa kwa siku chache, na wanunuzi hawa hawavitengenezeshi pale vinapoharibika—wao hununua vipya. Wakati wa kukagua akaunti na kupitia upya matumizi ya kifedha, ikigunduliwa kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakifuja sadaka na kuzitumia vibaya sana, jambo hili linapaswa kushughulikiwa vipi? Je, watu hao wanapaswa kupewa onyo la kinidhamu, au wanapaswa kulazimishwa kulipa fidia? Bila shaka, vyote viwili ni muhimu. Ikigunduliwa kwamba si wakweli, kwamba wao hasa si waumini, kwamba hawana imani, ni mapepo, basi tatizo haliwezi kutatuliwa tu kwa kuwapa onyo la kinidhamu au kuwapogoa. Haijalishi ukweli utashirikishwa vipi, hawataukubali; haijalishi watapogolewa vipi, hawatakuchukulia jambo hilo kwa uzito. Wakiambiwa walipe fidia, watafanya hivyo, lakini wataendelea kutenda vivyo hivyo katika siku za usoni, na hawatabadilika. Hakika hawatatenda kulingana na masharti ya nyumba ya Mungu; badala yake, watatenda kwa ukaidi, bila kujali, na kwa njia isiyo na maadili. Mtu wa aina hii anapaswa kushughulikiwa vipi? Je, anaweza kutumika baada ya hapa? Hapana, hapaswi; ikiwa atatumika, basi viongozi na wafanyakazi ni wapumbavu sana—ni wapuuzi kupita kiasi! Watu kama hao wasioamini wakigunduliwa, wanapaswa kutimuliwa, kuondolewa, na kusafishwa kutoka kanisani mara moja. Hata hawastahili kutoa huduma—hawafai kufanya hivyo!

Viongozi na wafanyakazi wanapokagua akaunti na matumizi, huenda wasigundue visa vya ufujaji na matumizi mabaya au matumizi yasiyo na busara pekee—huenda pia wakagundua kwamba baadhi ya watu wanaofanya kazi hiyo wana tabia potovu, ni waovu na wabinafsi, na kwamba wamesababisha hasara katika kazi ya kanisa. Ukigundua hali kama hii, unapaswa kuishughulikia vipi? Ni rahisi kuishughulikia: ni lazima uishughulikie na kuitatua papo hapo—watimue watu hao, kisha uchague watu wanaostahili kufanya kazi hiyo. Watu wanaofaa inamaanisha wale ambao ubinadamu wao ni wa kiwango kinachostahili, ambao wana dhamiri na mantiki, na ambao wanaweza kushughulikia mambo kulingana na kanuni za nyumba ya Mungu. Wanapofanyia nyumba ya Mungu ununuzi, wao hununua vitu vya bei rahisi ambavyo pia ni vya utendaji na vinadumu kiasi, vitu ambavyo ni muhimu kununua. Sio kwamba lazima wadhamirie kununua vitu vya bei nafuu, lakini pia hawaoni haja ya kununua vitu vya bei ghali mno, au; miongoni mwa bidhaa zinazofanana, watachagua zile zenye uhakiki na sifa nzuri, pamoja na kibandiko cha bei inayostahili, na bila shaka, ikiwa zina hati ya kubadilishwa au kutengenezwa, ya muda mrefu zaidi, ni bora zaidi. Unapaswa kumtafuta mtu wa namna hii ili afanye ununuzi kwa niaba ya nyumba ya Mungu. Anapaswa kuwa mkweli, na ni lazima azingatie nyumba ya Mungu katika matendo yake, na kufikiria mambo kwa makini; pia ni lazima ashughulikie mambo kulingana na masharti ya nyumba ya Mungu, akifanya na kutenda kwa njia yenye nidhamu, bila kuwapotosha watu, na kwa uwazi. Ukishampata mtu wa aina hii, mwache ashughulikie mambo machache ya nyumba ya Mungu na umwangalie kwa makini. Ikiwa ataonekana mwenye kufaa kiasi, anaweza kutumika. Lakini, pindi unapofanya hivyo, sio mwisho wa mambo—kuanzia hapo kuendelea mbele, lazima ukutane naye, ushiriki naye, na ukague kazi yake. Wengine huuliza, “Je, hivyo ni kwa sababu hawezi kuaminiwa?” Si kwa sababu ya kutokuaminika pekee—wakati mwingine, hata kama anafaa kuaminika, bado ni lazima ukaguzi ufanywe. Na ni nini kinachopaswa kukaguliwa? Angalia kama kumekuwa na michepuko katika utendaji wake katika hali ambayo hajaelewa kanuni au kama amekuwa na ufahamu uliopotoka. Ni lazima umsadie kwa kufanya uchunguzi wa makini. Kwa mfano, tuseme kwamba anasema kuna kitu maarufu sana sokoni, lakini hajui kama nyumba ya Mungu inakihitaji, na ana wasiwasi kwamba ikiwa hatakinunua sasa, huenda kisipatikane tena baadaye sokoni. Atakuuliza jinsi ya kushughulikia jambo hilo. Ikiwa hujui, basi unapaswa kumwacha amuulize mtu anayehusika na kazi hiyo ya utaalamu. Mtaalamu huyo kisha atasema kwamba kitu hicho ni kipya lakini hakitakuwa na matumizi wakati mwingi, na kwamba hakuna haja ya kutumia pesa kukinunua. Kwa kuzingatia maoni ya mtaalamu huyo kama marejeo, inaamuliwa kwamba hakuna haja ya kukinunua, kwamba kukinunua kutakuwa hasara, na kutokinunua sasa hakutaleta hasara. Viongozi na wafanyakazi lazima wafanye kazi yao kwa kadiri hii. Haijalishi jambo ni kubwa au dogo kiasi gani, ikiwa wanaweza kuliona, kulifikiria, au kuligundua, ni lazima walifuatilie na kulikagua kwa umoja, na wafanye hivyo kwa utaratibu uliowekwa kulingana na masharti ya nyumba ya Mungu. Hii ndiyo maana ya mtu kutimiza wajibu wake.

Watu wengine mara nyingi huomba kununua vitu fulani, wakiisihi nyumba ya Mungu inunue bidhaa hizi, na baada ya uhakiki na uchambuzi wa makini, kwa kawaida hupatikana kwamba kati ya vitu vitano vilivyotakikana, kimoja tu ndicho kinachohitajika kununuliwa, na hakuna haja ya kununua vile vingine vinne. Ni kitu gani kinachopaswa kufanywa katika hali kama hii? Vitu wanavyoomba vinunuliwe lazima vihakikiwe na kuzingatiwa kwa kweli, havipaswi kununuliwa kwa pupa. Havipaswi kununuliwa tu kwa sababu watu hao wanasema kazi inavihitaji—watu hao hawapaswi kuruhusiwa kuomba vitu kiholela wakitumia kisingizio kuwa ni kwa ajili ya kazi yao. Bila kujali watu hawa watatumia kisingizio gani, na bila kujali haraka yao, viongozi na wafanyakazi au watu wenye jukumu la kusimamia sadaka lazima wawe thabiti moyoni. Ni lazima wakague na kuchunguza hivi vitu kwa makini; hakupaswi kuwe na kosa hata dogo. Vitu ambavyo ni lazima kabisa vinunuliwe lazima vifanyiwe utafiti na kuidhinishwa na viongozi, na kama si lazima vinunuliwe, vinapaswa kukataliwa, wala si kuviidhinisha. Ikiwa viongozi na wafanyakazi watafanya kazi hii kwa uangalifu, kwa uthabiti, na kwa undani, visa vya ufujaji na matumizi mabaya ya sadaka vitapungua, na zaidi ya hayo, bila shaka, matumizi yasiyo na mantiki yatapungua. Kufanya kazi hii hakuhitaji tu kuangalia kwa makini mapato na matumizi yaliyorekodiwa kwenye vitabu, au hesabu. Hiyo ni ya baadaye. Cha muhimu zaidi ni kwamba sharti uwe mnyofu, na ushughulikie matumizi yote na kila ingizo kana kwamba ni ingizo katika akaunti yako binafsi ya benki. Kisha utaziangalia kwa undani, utaweza kuyakumbuka, na utaweza kuyaelewa—na ikiwa kutakuwa na kosa au tatizo, utaweza kulitambua. Ukiziangalia kama akaunti za mtu mwingine au za umma, hakika hutaweza kuona wala kufikiria mambo, wala hutagundua matatizo yoyote. Watu wengine huweka kiasi kidogo cha pesa kwenye benki, na kila mwezi, wao husoma taarifa zao na kuangalia riba, kisha wao hukagua akaunti—wao hukagua kiasi cha pesa wanachotumia kila mwezi, wao hutoa pesa mara ngapi, na kiasi cha pesa wanachohifadhi. Kila ingizo linarekodiwa akilini mwao, wanajua hesabu zote kama wanavyojua anuani yao wenyewe, na wanazikumbuka waziwazi. Tatizo likitokea mahali fulani, wanaweza kuliona mara moja, na hawapuuzi hata kosa dogo kabisa. Watu wanaweza kuwa makini sana kwa pesa zao wenyewe, lakini, je, wao hushughulikia sadaka za Mungu vivyo hivyo? Kwa maoni yangu, asilimia 99.9 ya watu hawafanyi hivyo, kwa hivyo watu wanapopewa sadaka za Mungu ili kuzilinda, mara nyingi visa vya ufujaji na matumizi mabaya na aina mbalimbali za matumizi yasiyo na mantiki hutokea, na bado hakuna anayehisi kwamba ni tatizo, na pia wale wanaohusika na kazi hii kamwe hawahisi wasiwasi kwa ajili ya matendo yao. Hata wapoteze yuani mia moja, sembuse elfu moja, elfu kumi, hawahisi hatia, deni, au lawama moyoni. Kwa nini watu huchanganyikiwa sana ifikiapo jambo hili? Je, hili halionyeshi kwamba watu wengi sana si wanyofu? Ni vipi kwamba unajua kwa uwazi umehifadhi pesa ngapi kwenye benki? Pesa za nyumba ya Mungu zinapowekwa kwa muda mfupi katika akaunti yako ili uzilinde, huchukulii jambo hilo kwa uzito au kulijali. Je, hii ni akili gani? Wewe hata si mwaminifu ifikiapo kulinda sadaka za Mungu, hivyo bado wewe ni muumini wa Mungu? Mwelekeo wa watu kuhusu sadaka ni ushahidi wa mwelekeo wao kumhusu Mungu—mwelekeo wao kuhusu sadaka unadhihirisha mengi. Watu hawajali kuhusu sadaka na hawajihusishi nazo. Kupotea kwa sadaka hakuwahuzunishi; hawawajibiki wala kujali. Basi, je, wana mwelekeo huo huo kwa Mungu? (Ndiyo.) Je, kuna yeyote ambaye husema, “Sadaka za Mungu ni Zake. Mradi sizitamani au kuzitwaa, kila kitu ni sawa. Yeyote atakayezitwaa ataadhibiwa—hiyo ni shauri yake, na anastahili. Hainihusu. Sina wajibu wowote kujihusisha na jambo hilo?” Je, kauli hii ni sahihi? Hakika si sahihi. Tatizo liko wapi basi? (Mtu huyo si mkweli; hatetei kazi ya nyumba ya Mungu, wala kulinda sadaka.) Ubinadamu wa mtu wa namna hii ni upi? (Ni wa kibinafsi na wa chini. Anajali sana kuhusu mali yake mwenyewe na kuilinda vizuri sana, lakini hajali wala kuulizia hali ya sadaka za Mungu. Ubinadamu wa watu kama hao ni duni sana.) Kimsingi, ni wa ubinafsi na wa chini. Je, watu wa aina hii si wakatili? Wao wabinafsi na wabaya, wakatili, na hawana hisia za kibinadamu. Je, watu kama hawa wanaweza kumpenda Mungu? Je, wanaweza kumtii? Je, wanaweza kuwa na moyo wa kumcha Mungu? (Hapana.) Basi watu kama hawa humfuata Mungu kwa sababu gani? (Ili kupata baraka.) Je, huku si kutoona haya? Jinsi mtu anavyochukulia sadaka za Mungu ni udhihirisho mkuu zaidi wa asili yake. Kwa kweli, watu hawawezi kumfanyia Mungu lolote. Hata kama wanaweza kutekeleza sehemu kidogo ya wajibu, hiyo ni finyu. Ikiwa huwezi hata kuchukulia sadaka—ambazo ni za Mungu—ipasavyo, au kuzilinda vizuri, ikiwa una mtazamo na tabia ya aina hiyo, basi, je, si wewe ni mtu ambaye amepungukiwa na ubinadamu kabisa? Je, si uongo kwako kusema unampenda Mungu? Je, si udanganyifu? Ni udanganyifu mkubwa! Hakuna ubinadamu wowote ndani ya mtu wa aina hii—je, Mungu atamwokoa mtu mbaya wa aina hii?

III. Kufuatilia, Kuchunguza, na Kukagua Matumizi ya Kila Aina, Kufanya Uhakiki Mkali

Ili viongozi na wafanyakazi wawe watumishi wazuri wa nyumba ya Mungu, kazi ya kwanza wanayopaswa kuifanya vizuri ni kusimamia sadaka vizuri. Zaidi ya kulinda sadaka vizuri, wanapaswa pia kufanya uhakiki mkali kuhusu matumizi ya sadaka. Kufanya uhakiki mkali kunamaanisha nini? Kimsingi, kunamaanisha kuondosha kabisa matumizi yasiyo ya busara, na kujitahidi kuyafanya matumizi yote ya sadaka kuwa ya busara na ya kufaa, badala ya sadaka kufujwa na kutumiwa vibaya. Matukio ya uharibifu au ufujaji yakigunduliwa, viongozi na wafanyakazi hawapaswi tu kuzikomesha mara moja, bali pia wawajibishe waliohusika, na pia kutafuta watu wanaostahili kufanya kazi hiyo. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kujua ni wapi hasa matumizi yote yanakwenda na yanatumiwa kwa ajili ya nini, ndani ya mawanda yao ya usimamizi—wanapaswa kuangalia upya mambo haya kwa akali. Kwa mfano, ikiwa chumba kinakosa feni, wanapaswa kuweka vigezo kuhusu ni nani atakayeinunua, pesa ngapi zitatumika, na itakuwa ya kazi gani inayofaa zaidi. Baadhi ya viongozi na wafanyakazi husema, “Tuna shughuli nyingi; hatuwezi kupata muda wa kwenda kuinunua.” Hujaagizwa uinunue mwenyewe. Unapaswa kumleta mtu mzuri, mwenye ubora mzuri wa tabia ashughulikie jukumu hili. Usimlete mtu mpumbavu au mtu mbaya asiye mkweli ainunue. Watu wenye ubinadamu wa kawaida wanajua kuwa wanapaswa kununua vitu vyenye matumizi yanayofaa na vya bei inayostahili—vitu vyenye matumizi mengi kupita kiasi havina maana, na hupatikana kwa bei ya juu zaidi. Watu wanaopenda anasa na ambao wana nia mbaya, kwa upande mwingine, hununua vitu visivyoweza kutumika vilivyo na mchanganyiko wa matumizi mengi, na ambavyo hugharimu pesa nyingi zaidi. Wanunuzi lazima wawe na mantiki; lazima waelewe kanuni. Vitu vinavyonunuliwa lazima viweze kutumika bila kuwa ghali, na vionekane na watu wote kuwa vinastahili. Iwapo utamleta mtu asiyewajibika na anayependa kutumia pesa bila mpango na kufuja pesa afanye ununuzi huu, atalipia tu bei ghali kiyoyozi cha hali ya juu, kwa gharama ya mara kumi ya bei ya feni. Anaamini kuwa ingawa inagharimu pesa nyingi zaidi, watu lazima wawe kipaumbele chetu cha kwanza—kiyoyozi hicho hakisafishi tu hewa, bali pia kinarekebisha unyevunyevu na halijoto, na kina vipimo vya wakati na mipangilio mbalimbali. Je, huo si uharibifu? Huo ni ubadhirifu na ufujaji. Mtu huyo ana nia ya kujifurahisha, na anatumia pesa kwa raha na kujionyesha, si kwa kununua vitu vya utendaji. Watu kama hao si wakweli. Wakijinunulia bidhaa, wao hutafuta njia za kuokoa pesa, hutafuta vitu vyenye bei nafuu, na hujaribu kujadiliana juu ya bei. Wao huokoa pesa wanapoweza—ni bora kitu kinapokuwa cha bei rahisi mno. Lakini wanapofanyia nyumba ya Mungu ununuzi, hawajali wanatumia pesa ngapi. Hata hawajisumbui kuangalia vitu vya bei nafuu; wanataka tu kununua vitu vya bei ghali, vya hali ya juu na vya kisasa. Hii inaonyesha kwamba hawana nia nzuri. Je, watu ambao si wakweli wanaweza kutumika? (Hapana.) Watu wenye nia mbaya wanaposhughulikia kazi ya nyumba ya Mungu, hufanya tu mambo ya kipumbavu na yasiyo na thamani. Hawatumii pesa kwa mambo yanayofaa; wao hutumia tu sadaka vibaya na kuifuja, na matumizi yao yote si ya busara.

Watu wengine wana mawazo ya umaskini, na wanaamini kwamba lazima wanunue vitu vya bei ya chini kabisa wanapoifanyia nyumba ya Mungu ununuzi, kadiri vilivyo vya bei ya chini zaidi ndivyo bora zaidi. Wanafikiri kwamba kufanya hivyo kunasaidia kuokoa pesa za nyumba ya Mungu, kwa hivyo wananunua tu vitu vya kizamani na vya bei ya kutupa. Matokeo yake, wananunua mashine za bei nafuu ambazo ni za bandia. Mashine hizi huharibika mara tu zinapotumika, na haziwezi kutengenezwa wala kutumika tena. Kisha inalazimu mashine zingine zenye ubora wa kutosha, ambazo zinaweza kutumika kawaida zinunuliwe, na hivyo pesa nyingine hutumika. Je, jambo hilo si upumbavu? Watu wa namna hiyo wanapaswa kuitwa wachoyo, na wenye mawazo ya umaskini. Daima wanataka kuokoa pesa za nyumba ya Mungu, lakini, je, matokeo ya ubahili wao na uokoaji wao wa pesa ni nini? Yote yanaishia kupotea bure, na kuwa ubadhirifu wa pesa. Wao hata hujisingizia kwa kusema, “Sikufanya makusudi. Nilikuwa na nia nzuri—nilikuwa tu nikijaribu kuokoa pesa za nyumba ya Mungu—sikutaka kutumia pesa bila mpango.” Je, wao kutotaka kufanya hivyo kunasaidia chochote? Kwa kweli, wanatumia pesa bila mpango, wanasababisha hasara, na jambo hili linatumia pesa na wafanyakazi. Watu wa namna hiyo pia hawawezi kutumika—ni watu wapumbavu, au wasio na ujuzi wa kutosha. Kwa ufupi, watu ambao wana nia mbaya hawapaswi kutumika kuifanyia nyumba ya Mungu ununuzi, na wala wapumbavu. Wanaopaswa kutumika ni wale wenye ujuzi, wenye uzoefu fulani wa kufanya ununuzi, na wa kimo fulani, na wanaoona mambo kwa mtazamo usiopotoka. Chochote kinachonunuliwa, lazima kiwe cha kutumika, na kiwe cha bei adili, na hata kikiharibika, lazima kiwe rahisi kutengenezwa, na lazima vipuri vyake viwe rahisi kununuliwa. Hilo ndilo jambo la busara. Baada ya watu wengine kununua kitu, wanaona kwamba kina muda wa kurudishwa wa mwezi mmoja, wanaharakisha kukijaribu, na wanapata matokeo ndani ya mwezi huo mmoja. Kikionekana kina kasoro au hakifanyi kazi vizuri, wanakirudisha mara moja na kuchagua kitu kingine, hivyo kupunguza hasara. Watu hao wana ubinadamu mzuri kiasi. Watu wasio na ubinadamu hununua kitu, kisha wanakitupa tu. Hawakijaribu kuona kama kina shida au kama kinadumu, wala hawaangalii hati ya kubadilisha kitu hicho ni ya muda gani au wana muda gani kukirudisha—hawajali kabisa kuhusu chochote kuhusu mambo hayo. Siku moja wanapokitaka ghafla, wanakichukua na kukijaribu, na hapo ndipo wanagundua kuwa kimeharibika. Wanakagua risiti na kuona muda wa kurudisha umepita, na kitu hicho hakiwezi kurudishwa tena. Kisha wanasema, “Hebu tununue kingine basi.” Je, hiyo si hasara? “Hebu tununue kingine”—kauli hiyo inamaanisha nyumba ya Mungu inapaswa kutoa pesa nyingine tena. Kijuujuu, inaonekana kwamba maombi ya kununua kingine ni kwa ajili ya kazi ya kanisa, na ni matumizi ya busara, lakini kwa kweli, kwa undani, ni kwa sababu ya uzembe wao wa kutotekeleza wajibu wao, kwa kutokikagua kitu papohapo baaada ya kukinunua. Sehemu moja ya sadaka inapotezwa, na ingine inalipia, na kitu hicho kipya bado hakina mtu wa kukilinda, hivyo, hicho pia, kinatumika kwa muda mfupi tu kabla hakijaharibika. Cha kushangaza ni kwamba hakuna mtu wa kusimamia hivi vitu, hakuna anayeshughulikia matatizo yanayotokea—viongozi na wafanyakazi wanafanya nini? Wamezembea kabisa katika majukumu yao kuhusiana na kazi hii—hawajatekeleza wajibu wao wa kusimamia, kukagua, na kuchunguza kwa makini, na kwa hivyo sadaka zinafujwa na kutumiwa vibaya namna hii. Ikiwa wanunuzi ni watu wa kuwajibika, watakirudisha haraka kitu walichokinunua wakiona hakitumiki. Hii inapunguza hasara na uharibifu. Ikiwa ni watu wasiowajibika na hawana nia nzuri, watanunua vitu bandia, hivyo basi kutumia sadaka vibaya. Hivyo basi, hasara hii ya pesa inasababishwa na nani? Je, si mnunuzi pamoja na viongozi na wafanyakazi wote wanawajibikia suala hili? Kama viongozi na wafanyakazi wangeshughulikia jambo hili kwa makini, na kwa kuonekana, na kwa uangalifu, je, matatizo haya yasingegunduliwa? Je, hitilafu hizi hazingerekebishwa? (Zingerekebishwa.) Viongozi na wafanyakazi wakitembelea makanisa mara kwa mara katika sehemu mbalimbali kukagua hali ya matumizi ya sadaka, wanaweza kugundua matatizo na kuondoshaa aina hii ya ubadhirifu na ufujaji. Iwapo viongozi na wafanyakazi ni wavivu na hawawajibiki, matukio haya ya matumizi yasiyo ya busara na badhirifu na ya ufujaji yataendelea kutokea mara kwa mara—yataendelea kuongezeka upesi. Ni ni husababisha ongezeko hili? Je, halihusiani na viongozi na wafanyakazi kutofanya kazi halisi, na badala yake kujiweka juu ya watu wengine na kuishi kama maafisa wasiofaa? (Ndiyo.) Viongozi na wafanyakazi kama hao hawana dhamiri wala busara, na hawana ubinadamu. Kwa sababu pesa zote zinazotumiwa na kanisa ni mali ya nyumba ya Mungu, na zote ni sadaka za Mungu, na wao wanaamini hazihusiani nao, hawajali wala kuulizia lolote, na huzipuuza. Watu wengi huamini kwamba pesa za nyumba ya Mungu zinapaswa kutumika, kwamba si vibaya kuzitumia kwa namna yoyote, kwamba mradi hawajazipora au kuzibadhiri, basi haijalishi ikiwa zitatatumiwa vibaya, na kwamba ni watu tu wananunua uzoefu na kupanua upeo wao. Viongozi na wafanyakazi hulifumbia hili macho wakisema: “Mtu yeyote anaweza kutumia pesa hizo jinsi atakavyo, na kununua chochote atakacho. Haijalishi ni pesa ngapi zinafujwa—atakayepoteza pesa ndiye atakayeziwajibikia, na kupata adhabu na kuadhibiwa baadaye—mimi hainihusu. Hata hivyo, siyo mimi ninayezitumia, na si pesa zangu.” Je, huo si mtazamo na mwelekeo sawa na ule ambao wasioamini wanao kuhusu matumizi ya fedha za umma? Ni kana kwamba walikuwa wakitumia tu pesa za adui zao. Wasioamini wanapofanya kazi kiwandani, ikiwa uongozi ni wa uzembe, vitu vya pamoja vitaibiwa kila mara na kupelekwa majumbani mwa watu au huharibiwa kiholela; kitu kikiharibika, watasihi kiwanda kinunue kingine kipya. Wanapofanyia kiwanda ununuzi, watanunua tu vitu vizuri na vya gharama kubwa. Kwa vyovyote vile, pesa itatumika kiholela bila mpango. Ikiwa wamwaminio Mungu pia watakuwa na mtazamo kama huo kuhusu sadaka, je, wanaweza kuokolewa? Je, Mungu atalifanyia kazi kundi kama hilo la watu? (Hapana.) Ikiwa watu wana mtazamo wa aina hiyo kuhusu sadaka za Mungu, basi unapaswa kujua Mungu ana mtazamo wa aina gani kuhusu watu kama hao, bila Mimi kukwambia.

Njia ya moja kwa moja kabisa ambayo mtazamo wa mtu kwa Mungu hujidhihirisha ni kupitia mtazamo wake kuhusu sadaka. Mtazamo wako kuhusu sadaka ndio mtazamo wako kumhusu Mungu. Ukichukulia sadaka kama unavyochukulia hesabu zako za akaunti yako ya benki—kwa makini sana, kwa uangalifu, kwa tahadhari, kwa kuwajibika, na kwa umakini sana—basi mtazamo wako kwa Mungu ni karibu sawa na huu. Ikiwa mtazamo wako kuhusu sadaka ni sawa na mtazamo wako kuhusu mali ya umma, kuhusu mboga sokoni—wewe hununua kiholela baadhi ya bidhaa unazohitaji bila hata kuangalia mboga zozote usizozipenda, kuzipuuza bila kujali zimerundikwa wapi, bila kujali kama mtu mwingine atazichukua na kuzitumia, ukijifanya kwamba hujaziona zimedondoka chini na kukanyagwa na mtu, na kuamini kwamba hayo yote hayakuhusu—basi wewe uko taabani. Ikiwa una mtazamo wa aina hiyo dhidi ya sadaka, je, wewe ni mtu wa kuajibika? Je, mtu kama wewe anaweza kutekeleza wajibu wake vizuri? Ni wazi una ubinadamu wa aina gani. Kwa ufupi, katika kazi ya kusimamia sadaka, jukumu kuu la viongozi na wafanyakazi, kando na kuzilinda vizuri, ni kwamba lazima wafuatilie kazi ya baadaye—la muhimu zaidi ni kwamba lazima wakague akaunti mara kwa mara, pamoja na kufuatilia, kuchunguza, na kukagua matumizi ya aina yote, na kufanya uhakiki mkali. Wanapaswa kuondosha kabisa matumizi yasiyo ya busara kabla yasababishe ubadhirifu na uharibifu; na ikiwa matumizi hayo yasiyo ya busara tayari yamesababisha mambo hayo, wanapaswa kuwawajibisha waliohusika, kuwapa onyo, na kuwafanya walipe fidia. Ikiwa huwezi kufanya kazi hii vizuri, harakisha ujiuzulu—usikae kwenye nafasi ya kiongozi au mfanyakazi, kwa sababu huwezi kufanya kazi yoyote kati ya hizi mbili. Ikiwa huwezi hata kusimamia kazi hii na kuifanya vizuri, basi ni kazi gani nyingine unaweza kuifanya? Nieleze kwa utaratibu: Kuna majukumu mangapi, kwa jumla, viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufanya kuhusiana na sadaka? (Ya kwanza ni kuzilinda. Ya pili ni kukagua akaunti. Ya tatu ni kufuatilia, kuchunguza, na kukagua aina zote za matumizi, na kufanya uhakiki mkali; matumizi yasiyo ya busara lazima yaondolewe, na bila kujali ni nani anayesababisha ubadhirifu au uharibifu, lazima awajibishwe na kulipa fidia.) Je, ni rahisi kufanya kazi kwa kufuata hatua hizi? (Ndiyo.) Hii ni njia iliyo wazi na iliyoelezwa kinaganaga ya kufanya kazi. Ikiwa hata huwezi kufanya kazi rahisi kama hii, basi unaweza kufanya nini kama kiongozi au mfanyakazi—kama mtumishi wa nyumba ya Mungu? Kuna visa vya sadaka kuharibiwa na kubadhiriwa mara kwa mara, na, kama kiongozi au mfanyakazi, huna ufahamu juu ya suala hili na huhisi huzuni yoyote kulihusu, basi Mungu yupo moyoni mwako kweli—je, ana nafasi Yake hapo? Hili si hakika. Unasema kwamba moyo wako unaompenda Mungu ni mkubwa na kwamba unamcha Mungu sana, lakini sadaka Zake zinapobadhiriwa na kuharibiwa namna hii, huna ufahamu wowote wala hujuti hata kidogo—je, si hilo linatilia shaka upendo wako na kumcha Mungu? (Ndiyo.) Hata imani yako ina shaka, sembuse upendo wako kwa Mungu na kumcha Mungu. Uchaji na upendo wako kwa Mungu si thabiti—si wa kudumu! Kulinda sadaka vizuri ni wajibu ambao viongozi na wafanyakazi wanapaswa kutimiza, na pia ni jukumu lao lisiloweza kuepukika. Ikiwa sadaka hazitalindwa vizuri, hilo ni kosa la kutowajibika kwa upande wao—inaweza kusemwa kwamba wote wanaolinda sadaka vibaya ni viongozi na wafanyakazi wa uongo.

IV. Kujua Upesi Kuhusu Sadaka Zilipo, Pamoja na Mazingira Mbalimbali ya Walinzi wa Sadaka Hiyo

Mbali na kukagua hali ya matumizi ya sadaka na kukomesha matumizi yasiyo ya busara, viongozi na wafanyakazi wana jukumu lingine muhimu zaidi: Wanapaswa kujua sadaka ziko wapi, pamoja na hali mbalimbali za wale wanaozisimamia. Lengo la jambo hili ni kuwazuia watu waovu, watu wenye mipango ya hila, na watu wenye tamaa katika mioyo yao, wasitumie usimamizi kujipatia sadaka. Watu wengine huona kwamba nyumba ya Mungu ina vitu vingi, na kwamba vingine havina mtu wa kuvilinda au kuviweka katika kumbukumbu, na kwa hivyo wao kila mara huwaza jinsi watakavyovigeuza vitu hivyo kuwa mali yao binafsi, na kuvichukua na kuvitumia wao wenyewe. Kuna watu wa aina hii kila mahali. Watu wengine, usoni, huonekana kana kwamba hawawatumii wengine vibaya, wala hawana tamaa kubwa ya mali au pesa, lakini hiyo ni kwa sababu hali na mazingira hayawaruhusu—kama kweli sadaka zingekabidhiwa mikononi mwao kulindwa, huenda wangejitwalia. Wengine huuliza, “Lakini mtu huyo alikuwa mzuri hapo awali; hakuwa na tamaa na alikuwa mwenye tabia nzuri—kwa nini basi kumkabidhi tu sadaka kidogo kumemfichua?” Hii ni kwa sababu yako kutokaa naye kwa muda mrefu, kutomjua kwa undani, na kutoona kiini chake asilia. Kama ungeelewa mapema kwamba mtu huyo ana asili ya aina hiyo, sadaka zisingeangukia mikononi mwa watu waovu. Kwa hivyo, ili kuzuia sadaka kuangukia mikononi mwa watu waovu, viongozi na wafanyakazi wana jukumu lingine muhimu zaidi: kuchunguza papo hapo mahali ambapo sadaka zipo na kufuatilia hali za wale wanaozisimamia. Tuchukulie kwamba mtu anasimamia mamia au maelfu kiasi kidogo cha yuani, ikiwa ana dhamiri kidogo, hawezi kuzibadhiri—lakini kama ingekuwa ni makumi au mamia ya maelfu, watu wengi wasingeweza kuaminika; hali hiyo ingekuwa hatari, na mioyo yao ingeweza kubadilika. Je, mioyo yao inaweza kubadilika vipi? Kiasi kidogo cha mamia au maelfu hakiwezi kugeuza moyo wa mtu, lakini ifikiapo makumi au mamia ya maelfu, moyo wake unaweza kugeuzwa kwa urahisi. “Haiwezekani kabisa kupata pesa nyingi kiasi hiki hata nifanye kazi muda gani, na sasa ziko mikononi mwangu—laiti zingekuwa zangu, maisha yangu yangekuwa bora kama nini!” Wanazifikiria: “Sihisi hatia kuwa na mawazo haya—je, hivyo, kuna mungu kweli au la? Mungu yupo wapi? Je, si kweli kwamba hakuna anayejua nina mawazo haya? Hakuna anayejua, na sina hisia za hatia wala majuto—je, hii inamaanisha hakuna mungu? Basi nikijipatia hizi pesa, sitapokea adhabu au malipo? Hakutakuwa na madhara yoyote?” Je, si moyo wa mtu huyu upo katika mchakato wa kubadilika? Je, sadaka zilizo mikononi mwake haziko hatarini? (Ziko hatarini.) Zaidi ya hayo, baadhi ya watu wanaosimamia sadaka ni wazuri sana; msingi wa imani yao upo kwa Mungu na ni waaminifu katika matendo yao, na hata ukiwapa makumi au mamia ya maelfu ya yuani wazilinde, wataweza kuyalinda vizuri, na kuna hakikisho kuwa hawatayabadhiri. Lakini kuna wachache ambao sio waumini katika familia zao, na watu hao wakiona pesa, macho yao hugeuka mekundu kama mbwa mwitu anapopeleleza mawindo yake. Acha makumi au mamia ya maelfu—wakiona yuani elfu moja, wataiweka mfukoni. Hawajali ni ya nani; wanaamini kwamba ni ya yule anayeweza kuinyakua kwanza. Ikiwa kuna mbwa mwitu waovu kama hawa karibu na mtu anayesimamia sadaka, je, sadaka hizo haziko hatarini kuchukuliwa mahali popote, wakati wowote? Je, hali kama hiyo inaweza kutokea? (Inaweza kutokea.) Je, si hatari ikiwa viongozi na wafanyakazi watakuwa hawatajali, watakosa kuwajibika, na hata kutotambua hali hiyo wala kufanyia uchunguzi na kufuatilia wakati sadaka ziko katika hali hatari namna hiyo? Jambo linaweza kuharibika mahali popote, wakati wowote. Kuna hali ya aina nyingine: Baadhi ya wasimamizi hulinda pesa na vitu mbalimbali majumbani mwao, na pia huwakaribisha ndugu pamoja na viongozi na wafanyakazi kwao. Hali hii inaweza kuwa salama kwa muda mfupi, lakini je, kuweka sadaka huko kwa muda mrefu kunastahili? (Hapana.) Hata kama mtu anayezilinda sadaka anafaa, mazingira na hali ya mahali hapo hapafai kabisa. Watu wanaokaribishwa kuishi pale wanafaa kuondolewa, au sadaka zihamishwe. Ikiwa viongozi na wafanyakazi hawatachunguza kazi hii wala kutimiza wajibu wao kuhusu jambo hili, mambo yanaweza kuharibika mahali popote, wakati wowote; sadaka zinaweza kupotea na kuishia mikononi mwa pepo waovu wakati wowote, mahali popote. Kuna hali aina nyingine: Makanisa mengine yako katika mazingira ya uhasama ambapo watu hukamatwa mara kwa mara, na kwa sababu hiyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba mahali ambako sadaka zimehifadhiwa zitasalitiwa, na nyumba hizo kuvamiwa na kuporwa na joka kubwa jekundu—sadaka zinaweza kuporwa na pepo waovu wakati wowote. Je, sadaka zinastahili kuhifadhiwa sehemu kama hizo? (Hapana.) Kwa hivyo, kama tayari zimewekwa hapo, unapaswa kufanyaje? Zihamishe mara moja. Baadhi ya viongozi na wafanyakazi hawatimizi jukumu lao wala hawafanyi kazi halisi. Hawawezi kutazamia au kufikiria mambo haya, hawayatambui, na wakati tu ambapo jambo linaharibika na sadaka kunyakuliwa na pepo waovu, ndipo wanapoanza kutafakari, “Tulipaswa kuhamisha hizo sadaka wakati ule,” na kuhisi majuto ya muda mfupi tu kama haya. Lakini kusipokuwa na tatizo, miaka mingine kumi inaweza kupita, bila wao kuhamisha hizo sadaka. Hawawezi kuona ni madhara gani makubwa yanaweza kutokea kutokana na suala hili, na hawawezi kutanguliza mambo kulingana na umuhimu na dharura yake. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuwa na ufahamu wazi wa hali hii wanapokumbana nayo: “Mojawapo ya sehemu ambako sadaka zimehifadhiwa haifai. Mazingira ni hatari sana, na ndugu kadhaa wamekamatwa, wamefuatwa, au kupelelezwa katika eneo hilo la karibu. Tunahitaji kufikiria jinsi ya kuondoa sadaka hizo hapo. Kuzihamisha hadi mahali penye usalama wa kutosha kutakuwa jambo bora zaidi kuliko kuziacha pale na kusubiri zinyakuliwe.” Hali inapotokea tu na wajue kwamba sadaka ziko hatarini, wanapaswa kuzihamisha mara moja ili kuzuia zisitwaliwe na kuliwa kwa ulafi na joka kuu jekundu, ibilisi mwovu. Hii ndiyo njia pekee ya kuhakikisha usalama wa sadaka na kuepuka hatari au makosa yoyote kutokea. Hii ndiyo kazi ambayo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuifanya. Mara panapotokea dalili ndogo sana ya hatari, mara mtu anapokamatwa, au hali yoyote kujitokeza, wazo la kwanza la viongozi na wafanyakazi linapaswa kuwa iwapo sadaka ziko salama, iwapo zinaweza kuanguka mikononi mwa watu waovu, kutwaliwa nao, au kunyakuliwa na pepo waovu, na ikiwa hizo sadaka zimepotea. Wanapaswa kuchukua hatua mara moja kulinda sadaka. Hili ndilo jukumu la viongozi na wafanyakazi. Baadhi ya viongozi na wafanyakazi huenda wakasema, “Kufanya haya mambo kunatuhitaji tuyafanye mambo ya hatari. Je, hatuwezi kuepuka kuyafanya? Si kweli kwamba watu ndio kipaumbele chetu cha kwanza, na ina maana kuwa hakuna haja ya kuzipa sadaka kipaumbele na badala yake watu ndio watangulizwe?” Una wazo lipi kuhusu swali lao? Je, watu hawa wana utu? (Hawana.) Kuzilinda vizuri sadaka, kuzisimamia vizuri, na kuzitunza vizuri—haya ni majukumu ambayo mtumishi mzuri lazima ayatimize. Kwa kusema kwa uzito zaidi, hata kama ni lazima ujitoe mhanga, inastahili, na ndilo jambo unalopaswa kufanya. Ni jukumu lako. Kila mara watu hupiga kelele wakisema, “Kufa kwa ajili ya Mungu ni kifo cha thamani.” Je, watu wako tayari kweli kufa kwa ajili ya Mungu? Huambiwi sasa ufe kwa ajili ya Mungu; unatakiwa tu uchukue jukumu dogo la kulinda sadaka kwa usalama. Je, uko tayari kufanya hivyo? Unapaswa kusema kwa furaha, “Niko tayari!” Kwa nini? Kwa sababu hili ni agizo la Mungu na masharti Yake kwa mwanadamu, ni jukumu lako lisiloepukika, na hupaswi kulikwepa. Kwa kuwa unadai kwamba unaweza kufa kwa ajili ya Mungu, kwa nini basi huwezi kulipa gharama ndogo tu, na kuchukua jukumu dogo tu ili kulinda sadaka? Je, hilo si jambo unalopaswa kufanya? Kama hufanyi jambo lolote halisi, bali unapiga tu kelele kuhusu kufa kwa ajili ya Mungu, je, maneno hayo si ya uongo? Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuwa na ufahamu dhahiri wa kazi ya kulinda sadaka, na wanapaswa kuchukua jukumu hili. Hawapaswi kulikwepa au kuliepuka, na hawapaswi kusita kuhusiana na jukumu lao. Kwa kuwa wewe ni kiongozi au mfanyakazi, kazi hii ni mzigo ambao lazima uubebe. Ni kazi muhimu—je, uko tayari kuifanya, hata kama unafanya mambo kadhaa yanayokuhatarisha, hata kama maisha yako yamo hatarini? Je, unapaswa kuifanya? (Ndiyo.) Unapaswa kuwa tayari kuifanya; hupaswi kamwe kukataa jukumu hili. Haya ndiyo masharti ya Mungu kwa mwanadamu na agizo Lake analompa mwanadamu. Mungu amekwambia sharti na agizo Lake dogo kabisa—ikiwa huko tayari hata kulitekeleza, basi unaweza kufanya nini?

Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufanya kazi ya kulinda na kutumia sadaka kwa uangalifu sana na kwa uthabiti sana iwezekanavyo. Hawapaswi kufanya hivyo kihobelahobela, wala kulichukulia kama jambo lisilowahusu na kukataa jukumu. Viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufanya ukaguzi wao binafsi, kujihusisha, na kuuliza maswali kuhusu mambo haya, na hata kuyashughulikia wao wenyewe, kuwazuia watu waovu na wale wenye ubinadamu duni wasitumie mapengo na kusababisha uharibifu. Kadiri unavyozidi kufanya kazi hii kwa uangalifu, ndivyo watu waovu na wabaya wanavyopata nafasi ndogo zaidi ya kutumia mapengo; kadiri uchunguzi wako unavyozidi kuwa wa kina na usimamizi wako kuwa mkali zaidi, ndivyo kutakavyokuwa na matukio machache ya matumizi yasiyo na busara, ubadhirifu, na uharibifu. Wengine husema, “Je, kufanya hivi kunahusu kuokoa pesa za nyumba ya Mungu? Nyumba ya Mungu imepungukiwa na fedha? Ikiwa imepungukiwa, nitaongeza fedha nyingine.” Je, hilo ndilo linaloendelea? (Hapana.) Hili ndilo jukumu la viongozi na wafanyakazi, ni sharti la Mungu kwa mwanadamu, na ni kanuni ambayo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuifuata wanapofanya kazi hii. Kama muumini wa Mungu, kama mtu ambaye amepewa nafasi ya utumishi katika nyumba ya Mungu, mtazamo wako kuhusu sadaka unapaswa kuwa wa uwajibikaji na wa kufanya uhakiki mkali; la sivyo, hustahili kufanya kazi hii. Ungekuwa muumini wa kawaida asiyethamini uwajibikaji wala kufuatilia ukweli, usingehitajika kufanya mambo haya. Wewe ni kiongozi au mfanyakazi; ikiwa huthamini uwajibikaji, hufai kuwa kiongozi au mfanyakazi, na hata ukihudumu katika nafasi hiyo, wewe ni kiongozi au mfanyakazi bandia asiyewajibika, na siku moja utaondolewa. Wale wote ambao hawathamini uwajibikaji ni watu wasiotetea kabisa kazi ya nyumba ya Mungu—wote hawana dhamiri na mantiki hata kidogo. Watu kama hao wanawezaje kutimiza wajibu? Hao ni watu wapuuzi wasiojali—wanapaswa kuondoka mara moja katika nyumba ya Mungu, na warudi ulimwenguni ambako wanastahili kuwa!

Tusingefanya ushirika wa aina hii kuhusu maarifa ya kawaida yanayohusu sadaka, pamoja na ukweli unaohusiana na kulinda sadaka na kanuni ambazo watu wanapaswa kuzitenda, je, si si mngekosa kuelewa vizuri mambo haya? (Ndiyo.) Watu wanapokosa kuelewa vizuri kuhusu kanuni mahususi, je, wanaweza kutimiza baadhi ya majukumu yao? Je, wamekuwa wakitimiza jukumu lao? Je, watu wengi hawajakuwa wakiishi kwa kufuata nadharia na kanuni za juu juu kabisa za kusema: “Kwa vyovyote vile, sitamani sadaka za Mungu, sizibadhiri wala kuzitumia vibaya, na nazilinda vizuri na siwaruhusu watu wazitumie kiholela—hilo linatosha”? Je, huu ni utendaji wa ukweli? Je, huku ni kutimiza jukumu la mtu? (Hapana.) Ikiwa maarifa ya watu wengi yanakomea hapo, basi mada hii kweli inastahili kufanyiwa ushirika. Kupitia ushirika huu, je, sasa umeelewa na kufahamu zaidi kuhusu jinsi ya kulinda sadaka na mtazamo na ufahamu unaopaswa kuwa nao unapozilinda? (Ndiyo.) Tutamalizia ushirika wetu hapa kuhusu ukweli unaogusia sadaka na kanuni zinazohusiana na jinsi ya kushugulikia na kusimamia sadaka.

Mitazamo na Udhihirisho wa Viongozi wa Uwongo Kuhusiana na Sadaka

I. Kuchukulia Sadaka kama Mali ya Kawaida

Kisha, tutafanya ufichuzi na uchanganuzi rahisi wa viongozi wa uwongo kuhusiana na kipengele cha kumi na moja cha majukumu ya viongozi na wafanyakazi. Tutaangalia ni udhihirisho upi viongozi wa uwongo wanao katika mtazamo wao kuelekea sadaka na katika ulindaji na usimamizi wao wa sadaka. Udhihirisho wa kwanza ni kwamba viongozi wa uwongo wanakosa uelewa sahihi kuhusu sadaka. Wao huamini, “Sadaka hutolewa kwa mungu kwa jina tu, lakini kwa kweli, zinatolewa kwa kanisa. Hatujui mungu yuko wapi, na hawezi kutumia vitu vingi hivyo, hata hivyo. Sadaka hizi zinatolewa kwa mungu kwa jina tu; kwa kweli, zinatolewa kwa kanisa, na kwa nyumba ya Mungu, na hazitolewi waziwazi kwa mtu yeyote maalum. Kanisa na nyumba ya Mungu ni majina mengine ya watu wao wote, na maana ya hili ni kwamba sadaka ni za kila mtu, na kile ambacho ni cha kila mtu ni mali ya umma. Kwa hivyo, sadaka ni mali ya umma ambayo ni ya ndugu wote.” Je, uelewa huu ni sahihi? Ni wazi kabisa kuwa sio. Je, si kunalo tatizo na ubinadamu wa watu walio na uelewa wa aina hiyo? Je, wao si watu wanaotamani sadaka? Watu walio na mioyo ya tamaa na hamu ya kunyakua sadaka hutumia mbinu hii na mtazamo huu linapokuja suala la sadaka. Ni wazi, wanazimezea mate sadaka na wangependa kuzimiliki kwa ajili ya starehe yao wenyewe. Hawa ni viumbe wa aina gani? Je, wao si wa aina moja na Yuda? Hivyo, kiongozi au mfanyakazi wa aina hii huchukulia sadaka za Mungu kuwa mali ya umma ya kanisa. Wao huwa na mtazamo wa aina hii moyoni—hawalindi sadaka kwa dhati, au kuzisimamia kwa busara na kwa uwajibikaji, badala yake, wao hutumia sadaka watakavyo, bila haya, na kwa kwa ujeuri kabisa, wakikosa maadili. Wanamruhusu yeyote azitumie, na yule ambaye “cheo chake rasmi” ni kikubwa zaidi, yule ambaye hadhi yake ni ya juu, yule ambaye ana umaarufu kati ya ndugu, anapewa kipaumbele cha kuzimiliki na kuzitumia. Ni kama tu vile katika makampuni na viwanda katika jamii, ambapo magari ya kampuni na vitu vizuri, vya hali ya juu ni vya kutumiwa na mameneja, wakurugenzi wa viwanda, na wenyeviti. Wanaamini kwamba hivi ndivyo inavyopaswa kuwa kuhusiana na sadaka za Mungu, pia, kwamba yeyote aliye kiongozi au mfanyakazi ana kipaumbele katika kufurahia vitu vya hali ya juu vya nyumba ya Mungu, katika kufurahia sadaka zilizotolewa kwa Mungu. Hivyo, wale wote wanaotumia kuwa kiongozi na mfanyakazi kama kisingizio cha kununua kompyuta za hali ya juu na simu za mkononi, pamoja na viongozi na wafanyakazi wote wanaochukua sadaka kwa ajili yao wenyewe, wanaamini kwamba sadaka ni mali ya umma, na kwamba sadaka zinapaswa kutumiwa na kufujwa wapendavyo. Akina ndugu fulani wanapotoa dhahabu na mapambo ya fedha, mikoba, nguo, na viatu, hawaelezi bayana kwamba wanavitoa kwa Mungu, na hivyo viongozi fulani wa uwongo wanaamini, “Kwa kuwa hawakueleza bayana kwamba vitu hivi vinatolewa kwa Mungu, vinapaswa kuwa kwa ajili ya matumizi ya kanisa. Chochote kinachotolewa kwa kanisa ni mali ya umma, na viongozi na wafanyakazi wanapaswa kuwa na kipaumbele katika kufurahia mali ya umma.” Na hivyo, wanajichukulia vitu hivi kama jambo la kawaida kwao. Vitu vilivyosalia baada ya wao kuchagua vinaweza kutumiwa na yeyote anayetaka na kuchukuliwa na yeyote anayetaka—kila mtu anavichukua kama mgao. Viongozi na wafanyakazi hawa wanaita jambo hili kugawana mali; kwa kuwafuata, watu wanaweza kula na kunywa vizuri, na kujistarehesha kweli. Kila mtu anafurahi, na wanasema, “Shukrani kwa mungu—je, tungeweza kufurahia vitu hivi ikiwa hatungemwamini yeye? Hizi ni sadaka, na sisi hatustahili kuzifurahia!” Wanasema hawastahili, lakini wanavishikilia vitu hivyo na hawawezi kuviachilia. Viongozi na wafanyakazi kama hao hawanyakui tu sadaka na kuzifanya mgao, na kuzifurahia wao wenyewe bila kupata idhini ya mtu yeyote—wanapofanya hivi, wao hupuuza kabisa usimamizi, utumiaji wa pesa, na matumizi ya sadaka, wala hawachagui watu wanaofaa kuzisimamia na kuweka rekodi zake, na sembuse kuzikagua hesabu, au kupitia kwa kina hali ya matumizi ya pesa. Kutojali kwa viongozi wa uwongo kwa usimamizi wa sadaka husababisha vurugu, na sadaka fulani hupotea na kufujwa. Kinachoonekana zaidi katika kazi ya viongozi wa uwongo ni kwamba kila mtu hutenda kwa mapenzi yake mwenyewe. Kile ambacho msimamizi wa timu yoyote anasema, ndicho hufuatwa, na timu yoyote inapohitaji kununua kitu, wanaweza kuamua kufanya hivyo wenyewe, bila kuhitaji kuwasilisha ombi ili liidhinishwe idhini. Mradi kitu kinahitajika kwa ajili ya kazi, wanaweza kukinunua, bila kuwa na wasiwasi kuhusu kinagharimu kiasi gani, kama wanaweza kukitumia, au kama ni muhimu au la—hata hivyo, wanatumia sadaka, sio pesa za mtu yeyote. Viongozi wa uwongo hawasimamii hili au kufanya uhakiki, sembuse kushiriki kuhusu kanuni. Kitu kikiishanunuliwa, viongozi wa uwongo hawajali kabisa kama kuna mtu wa kukilinda, kama kitu kinaweza kuharibika, au kama kinafikia thamani ya pesa zilizotumika. Kwa nini hawajali mambo haya? Ni kwa sababu pesa hizo si zao—wanafikiri kwamba yeyote anaweza kuzitumia, kwani vyovyote vile si pesa zao zinazotumika. Kuna vurugu katika kila kipengele cha usimamizi wa sadaka. Kuna vurugu kiasi gani? Ni kama vile ilivyo katika viwanda vikubwa vinavyomilikiwa na serikali vya nchi za kijamaa, ambapo kila mtu hupata sehemu sawa bila kujali anafanya kazi kiasi gani. Kila mtu hupeleka vitu nyumbani, anakula chakula cha kiwanda na kupata pesa za kiwanda, na kubadhiri vitu vya kiwanda. Ni vurugu tupu. Viongozi wa uwongo hawaweki sheria zozote za matumizi ya pesa katika kununua vifaa au zana yoyote. Nyumba ya Mungu huweka sheria, lakini wao hawapitii kwa kina, kukagua, kufuatilia, au kuchunguza matumizi ya pesa. Hawafanyi kazi yoyote kati ya hizi. Kazi ya viongozi wa uwongo ni ya vurugu tupu, hakuna utaratibu kwa kitu chochote, na kuna dosari kila mahali. Kila uendapo, watu waovu na wale ambao wana nia mbaya wanaruhusiwa kutumia mapengo na kujinufaisha. Sadaka za Mungu zinabadhiriwa na kufujwa kiholela na watu hao, na bado hawaadhibiwi au kuwekewa vikwazo kwa njia yoyote—hawapewi hata onyo. Hawa ni viongozi na wafanyakazi wa aina gani? Je, huku si kuung’ata mkono unaowalisha? Je, wao ni mawakili wa nyumba ya Mungu? Wao ni wezi wasaliti wa nyumba ya Mungu!

Viongozi na wafanyakazi hawa wasiowajibika linapokuja suala la kulinda sadaka wanapaswa kuchukuliwaje? Je, wao si watu wenye tabia duni na wasio na dhamiri na busara? Viongozi hawa wa uwongo huvichukulia vitu vilivyotolewa na ndugu kwa Mungu na kwa kanisa kuwa mali ya nyumba ya Mungu, na husema kwamba zinapaswa kusimamiwa na akina ndugu kama kundi. Na hivyo, matatizo yanapokuwa yamefichuliwa, na Aliye juu anapowawajibisha watu, wao ufanya kila juhudi kujitetea, na hawakiri jinsi lilivyo jambo zito kwao kuiba na kunyakua sadaka za Mungu baada ya kuwa viongozi na kupata hadhi. Je, hawa si watu wenye tabia duni? Wao hawana aibu kabisa! Hawajui kwa nini ndugu wanatoa pesa na vitu, wala hawajui wanavitoa kwa nani. Kama hakungekuwa na Mungu, ni nani ambaye angevitoa vitu anavyovipenda kwa urahisi tu? Hii ni mantiki rahisi sana, na bado hawa wanaoitwa “viongozi” hawaijui au kuelewa. Viongozi hawa wa uwongo wana msemo wa kawaida: “sadaka za nyumba ya Mungu.” Je, msemo huu hauhitaji kurekebishwa? Msemo sahihi unapaswa kuwa upi? “Sadaka” au “sadaka za Mungu.” Ikiwa utaongeza kivumishi, unapaswa kuongeza “Mungu”—sadaka ni za Mungu pekee. Usipoongeza kivumishi, ni “sadaka” tu—watu wanapaswa kujua bado kwamba mmiliki wa sadaka ni Muumba, Mungu, na si mwanadamu. Mwanadamu hastahili kumiliki sadaka, na hata makasisi hawawezi kusema kwamba sadaka ni zao—wanaweza kufurahia sadaka kwa idhini ya Mungu, lakini si mali yao. Kivumishi cha “sadaka” kamwe hakitakuwa mtu yeyote—kinaweza tu kuwa Mungu, na si mwingine yeyote. Ni wazi kabisa, basi, kwamba msemo “sadaka za nyumba ya Mungu” unaosemwa mara nyingi na viongozi wa uwongo ni potofu, na unapaswa kurekebishwa. Hakupaswi kuwa na msemo kama “sadaka za nyumba ya Mungu” au “sadaka za kanisa.” Kuna baadhi ya watu ambao hata husema “sadaka zetu” na “sadaka za nyumba yetu ya Mungu.” Misemo hii yote si sahihi. Sadaka hutolewa kwa Mungu na wanadamu walioumbwa, na wale wanaomfuata Mungu. Mungu pekee ndiye mwenye haki ya kipekee ya kuwa mmiliki, mtumiaji, na mfurahiaji wake. Sadaka si mali ya umma; si mali ya mwanadamu, sembuse mali ya kanisa na nyumba ya Mungu, badala yake, ni mali ya Mungu. Mungu huliruhusu kanisa na nyumba ya Mungu kuzitumia—hili ni agizo Lake. Kwa hiyo, misemo yote kama vile “sadaka za nyumba ya Mungu,” “sadaka za kanisa,” na “sadaka zetu” haina usahihi, na zaidi ya hayo, ni misemo ya watu wenye nia mbaya, imekusudiwa kuwapotosha watu na kuwafanya wawe ganzi, na hata zaidi, kuwaelekeza watu wasivyo. Watu hawa huainisha sadaka kuwa mali ya umma inayomilikiwa na kanisa, au na nyumba ya Mungu, au na ndugu wote. Haya yote yana matatizo na ni makosa na yanapaswa kurekebishwa. Huu ni udhihirisho wa aina moja ya kiongozi wa uwongo. Watu kama hawa huchukulia sadaka kama mali ya umma na kuzitumia wapendavyo; au, wanaamini kwamba wakiwa viongozi, wana haki ya kugawanya vitu hivi, na hivyo wanawagawia watu wanaowapenda au kila mtu kwa usawa. Wanajaribu kutengeneza hali ya aina gani? Hali ambapo kila mtu ni sawa, ambapo kila mtu anaweza kufurahia neema ya Mungu, ambapo kila mtu anashiriki. Wangependa kununua fadhila za watu kwa kuwa wakarimu na rasilimali za nyumba ya Mungu. Je, hilo si jambo la kuchukiza? Hii ni tabia mbaya mno, isiyo na aibu! Watu kama hawa wanapaswa kuainishwaje? Viongozi wa uwongo kama hawa wanatamani sadaka, na ili kuwazuia watu kuwasimamia, kuwafichua, na kuwatambua, wao hugawanya vitu vilivyosalia wasivyovitumia kwa ndugu, wakinunua fadhila yao na kufikia hali ambapo kila mtu ni sawa, na kumwezesha kila mtu kufaidika kwa kuhusiana nao, ili kwamba hakuna mtu atakayewafichua. Kama mngekutana na kiongozi wa aina hii, ambaye angewaruhusu mpate faida fulani na ambaye mngefurahia “mali ya umma” pamoja naye—kama mngekuwa na haki hii na kuchukua faida ya aina hii, je, mngeridhika na hilo? Je, mngeweza kukataa? (Tungeweza.) Kama ninyi ni wenye tamaa, hamna moyo umwogopao Mungu, na hamwogopi Mungu, hamtaweza. Yeyote mwenye uadilifu kidogo, busara kidogo, na moyo umwogopao Mungu kidogo atakataa, na pia atasimama kumkemea kiongozi huyo, kumpogoa, na kumkomesha, akisema: “Jambo la kwanza unalopaswa kufanya kama kiongozi ni kusimamia sadaka vizuri, si kuzibadhiri, sembuse kuamua bila idhini kuzigawanya kwa kila mtu kulingana na mapenzi yako mwenyewe. Huna haki hiyo; hilo si agizo la Mungu kwako. Sadaka ni za Mungu kutumia, na kuna kanuni za matumizi ya kanisa kuzihusu—hakuna mtu aliye na uamuzi wa mwisho juu yake. Unaweza kuwa kiongozi, lakini huna hiyo haki hiyo. Mungu hakukupa haki hiyo. Huna haki ya kutumia vitu vya Mungu—Mungu hakukuagiza ufanye kazi hiyo. Kwa hiyo, fanya hima na uvue dhahabu na mapambo ya fedha ambayo ndugu walimtolea Mungu, na uvue nguo walizomtolea Yeye. Fanya haraka na ulipe fidia kwa vitu ulivyokula ambavyo hukupaswa kula. Ikiwa wewe bado ni mwanadamu na una aibu kidogo, fanya hivi mara moja. Zaidi ya hayo, haijalishi ni nani uliyemtumia sadaka hizi ili kutafuta kibali chake, au ni nani uliyemruhusu azinyakue na kuzifurahia, rudisha sadaka hizo mara moja. Usipofanya hivyo, tutawajulisha akina ndugu wote na tukushughulikie kama Yuda!” Je, mngethubutu kufanya hivi? (Ndiyo.) Kila mtu ana jukumu hili linapokuja suala la sadaka, na anapaswa kuzichukulia kwa dhamiri hii na mtazamo wa aina hii. Bila shaka, pia wana wajibu huu wa kusimamia jinsi wengine wanavyochukulia sadaka, kama wanazilinda vizuri, na kama wanazisimamia kulingana na kanuni. Usifikiri kwamba hili halikuhusu, na kisha usiwajibike, ukisema, “Hata hivyo, mimi si kiongozi au mfanyakazi, hili si jukumu langu. Hata nikiligundua, sihitaji kuhangaika nalo au kusema lolote kulihusu—hilo ni suala la viongozi na wafanyakazi. Yeyote anayetumia pesa kiholela na kubadhiri sadaka, yeye ni Yuda, na Mungu atamwadhibu wakati ukifika. Yeyote anayesababisha matokeo, anawajibika kwayo. Hakuna haja ya mimi kuhangaikia hili. Kuzungumza kwangu kusikofaa kutasaidia nini?” Unamwonaje mtu wa aina hii? (Hana dhamiri.) Ukigundua kwamba, katika sehemu fulani ambazo viongozi na wafanyakazi hawachunguzi, kuna watu wanaofuja na kunyakua sadaka, unapaswa kumuonya muhusika ana kwa ana, na pia kuliripoti tukio hilo mara moja kwa viongozi na wafanyakazi. Unapaswa kusema, “Kiongozi wetu wa timu na kiongozi wetu mara nyingi hujichukulia sadaka wao wenyewe. Pia wanatumia sadaka kiholela, na hawajihusishi katika majadiliano na wengine na wao huamua tu wenyewe kununua hiki na kile. Matumizi yao mengi hayalingani na kanuni. Je, nyumba ya Mungu inaweza kushughulikia hili?” Ni jukumu la watu wateule wa Mungu kuripoti na kutoa taarifa kuhusu matatizo wanayoyagundua. Ushirika wetu uliotangulia umekuwa kuhusu udhihirisho wa aina moja ya kiongozi wa uwongo—mtazamo wao kwa sadaka ni kuzichukulia kama mali ya umma.

II. Kutojali au Kuuliza Kuhusu Matumizi ya Sadaka

Udhihirisho mwingine wa viongozi wa uwongo kuhusiana na kulinda sadaka ni kwamba hawajui jinsi ya kusimamia sadaka. Wanajua tu kwamba sadaka hazipaswi kuguswa, kwamba hazipaswi kutengwa kiholela au kubadhiriwa, kwamba ni takatifu, zimetengwa kama takatifu, na kwamba mtu hawezi kuwa na mawazo yasiyofaa kuzihusu. Lakini linapokuja suala la jinsi, hasa, ya kusimamia sadaka vizuri, jinsi ya kuwa msimamizi mwema katika kuzilinda, hawana njia, hawana kanuni, hawana mipango mahususi au hatua za kazi hii. Kwa hiyo, katika masuala kama vile kusajili, kujumlisha, na kulinda sadaka, pamoja na kukagua hesabu za mapato na matumizi na kukagua matumizi ya pesa, viongozi hawa wa uwongo huwa wasiofanya kitu kabisa. Mtu anapowasilisha kitu ili kiidhinishwe, wao hutia saini. Mtu akiomba kurejeshewa pesa, wanampa. Mtu akiomba pesa kwa ajili ya lengo fulani, wanampa. Hawajui mashine na vifaa mbalimbali vinalindwa vikiwa wapi. Pia hawajui kama mlinzi wa vitu hivyo anafaa, wala jinsi ya kujua kama anafaa; hawawezi kung’amua mioyo ya watu, na hawawezi kung’amua kiini cha watu. Kwa hiyo, ingawa kuna rekodi za sadaka zote zinazotoka chini ya upeo wa usimamizi wa watu hawa, ukiangalia maelezo ya matumizi katika hesabu hizo, matumizi mengi hayana urazini na si ya lazima—mengi ni ya kupita kiasi na ni ubadhirifu. Sadaka hupotea chini ya saini za viongozi na wafanyakazi hawa. Kwa juujuu, wanaonekana kuwa wanafanya kazi mahususi, lakini kwa kweli, hakuna kanuni zozote katika kile wanachofanya. Hawafanyi uhakiki—wanafanya mambo kwa namna isiyo ya dhati, wakifuata sheria na kanuni, basi. Hili halifikii viwango vya kusimamia sadaka kabisa, sembuse kanuni zake. Kwa hiyo, katika kipindi ambacho viongozi wa uwongo wanafanya kazi, kuna matumizi mengi mno yasiyo ya urazini. Ikiwa kuna mtu aliyepo wa kusimamia na kuendesha mambo, matumizi haya yasiyo ya urazini yanatokeaje? Ni kwa sababu viongozi na wafanyakazi hawa hawajukumiki katika kazi yao. Wanafanya mambo kwa namna isiyo ya dhati na kushughulikia mambo kwa kijuujuu tu, na hawatendi kulingana na kanuni. Hawawakwazi wengine, wanatenda kama wenye kutaka kuwafurahisha wengine, na hawafanyi uhakiki unaofaa. Huenda hata kusiwe na mtu mmoja anayewajibika kweli miongoni mwa wale wanaosimamia sadaka, hakuna hata mmoja anayeweza kufanya uhakiki kweli. Viongozi wa uwongo hawajali kama watu wanaolinda sadaka wanafaa, au kama kuna hali zozote za hatari katika makanisa ya watu hao. Kwao, mradi wao wenyewe wako salama, basi kila kitu ni sawa. Hatari inapotokea, jambo la kwanza wanalofikiria ni wapi wanaweza kukimbilia na kama pesa zao wenyewe zitaporwa, ilhali hawachunguzi wala kuuliza kuhusu mahali sadaka zilipo au kama ziko hatarini. Miezi michache au hata nusu mwaka baada ya tukio hilo, wanaweza kuuliza kutokana na dhamiri, na wanapojua kwamba sadaka zingine zimechukuliwa na joka kubwa jekundu, kwamba zingine zimefujwa na watu waovu, na kwamba zingine hazijulikani mahali zilipo, watajisikia vibaya kwa muda—wataomba kidogo, watakiri kosa lao, na huo utakuwa mwisho wake. Hawa ni viumbe wa aina gani? Je, hakuna tatizo kufanya kazi namna hii? Mungu atamtendeaje mtu aliye na mtazamo kama huo kuelekea sadaka? Je, atamwona kama mwumini wa kweli? (La.) Atamwona kama nani, basi? (Kama asiyeamini.) Mungu anapomwona mtu kama asiyeamini, je, mtu huyo anapata hisia yoyote? Anakuwa ganzi na asiyeelewa kwa wepesi rohoni mwake, na anapotenda, hana nuru au mwongozo wa Mungu, au mwanga wowote. Hana ulinzi wa Mungu mambo yanapompata, na mara nyingi yeye ni hasi na dhaifu, akiishi gizani. Ingawa anasikiliza mahubiri mara nyingi, na anaweza kuteseka na kulipa gharama katika kazi yake, hapigi hatua yoyote, na anaonekana wa kusikitisha. Hayo ndiyo “matokeo” yake. Je, hili si jambo gumu zaidi kuvumilia kuliko adhabu? Niambieni, ikiwa haya ndiyo matokeo ya imani ya mtu kwa Mungu, je, hiyo ni sababu ya furaha na kusherehekea au ya huzuni na maombolezo? Si ishara nzuri, kwa maoni Yangu.

Viongozi wa uwongo hawachukulii kazi ya kusimamia sadaka kwa uzito kamwe. Ingawa wao husema, “Watu hawapaswi kugusa sadaka za Mungu; sadaka za Mungu hazipaswi kubadhiriwa na yeyote, na hazipaswi kuanguka mikononi mwa watu wabaya,” na wanapiga kelele wakisema kauli mbiu hizi vizuri kabisa, na maneno yao yanasikika kuwa ya kimaadili na ya adabu sana, lakini hawatendi kama wanadamu. Ingawa hawabadhiri sadaka, na hawana mawazo yasiyofaa kuzihusu, au nia yoyote ya kuzinyakua, na baadhi yao hata hawatumii pesa za nyumba ya Mungu au kugusa sadaka za Mungu kwa ajili ya matumizi yoyote wanayoweza kuwa nayo, na badala yake wanatumia pesa zao wenyewe, kama viongozi na wafanyakazi, hawafanyi kazi yoyote halisi kabisa linapokuja suala la usimamizi wa sadaka. Hawafanyi hata mambo rahisi kama vile kuuliza kuhusu hali ya matumizi ya sadaka au kufanya uhakiki wa matumizi ya sadaka. Hawa, bila shaka, ni viongozi wa uwongo. Mtazamo wao kuelekea sadaka ni huu: “Sizitumii na sizibadhiri, na pia sijishughulishi na jinsi wengine wanavyozitumia au kama wengine wanazibadhiri.” Ninawaambia viongozi hawa wa uwongo kwamba mtazamo huu wako wa vuguvugu ni wa taabu sana. Kutozitumia na kutozibadhiri ndicho kile ambacho watu wanapaswa kufanya, lakini kama kiongozi au mfanyakazi, kile unachopaswa kufanya hata zaidi ni kusimamia sadaka vizuri, na bado umeshindwa kufanya hivi. Huko kunaitwa kupuuza wajibu. Huu ni udhihirisho wa kiongozi wa uwongo. Huenda hukutumia senti moja au kubadhiri sadaka hata moja, lakini kwa sababu hufanyi kazi halisi, na hufanyi kazi yoyote mahususi ya usimamizi kuhusu sadaka, unaainishwa kama kiongozi wa uwongo, na kufanya hivyo ni kwa haki na kunakubalika. Viongozi wengine kamwe huwa hawachukui au kutumia sadaka yoyote kabisa—hata kama viongozi na wafanyakazi wengine wote wanazitumia, wao hawazitumii, na nyumba ya Mungu inapopanga kuwapa kitu, wanakikataa. Wanaonekana kuwa safi kabisa na wasio na tamaa, lakini wanapopangiwa kusimamia sadaka, hawatafanya kazi yoyote mahususi kabisa. Haijalishi ni nani anayetumia sadaka, watatia saini—hawafanyi hata maulizo yoyote, na hawasemi neno zaidi kulihusu hilo. Ingawa watu hawa hawabadhiri hata senti moja ya sadaka, chini ya upeo wa usimamizi wao, sadaka zinachukuliwa na kumilikiwa na watu waovu, na kwa sababu ya kutowajibika kwao na kupuuza kwao wajibu, sadaka zinaweza kufujwa na kupotezwa na yeyote. Je, ufujaji na upotevu huu hauhusiani na usimamizi wao mbaya? Je, hausababishwi na wao kupuuza wajibu wao? (Unasababishwa na hilo.) Je, hawana sehemu katika matendo maovu ya watu hawa? Je, hawajukumikii jambo hilo? Hili ni jukumu kubwa la kubeba, na hawawezi kulikwepa! Wanashikilia tu msimamo wao: “Vyovyote vile, sibadhiri sadaka za Mungu, na sitaki au kupanga kufanya hivyo. Haijalishi ni nani anayetumia sadaka za Mungu, mimi sizitumii; haijalishi ni nani anayezichukua na kuzitumia, mimi sizitumii; haijalishi ni nani anayezifurahia, mimi sizifurahii. Huu ndio mtazamo wangu kuelekea sadaka—unaweza kufanya chochote unachotaka!” Je, kuna watu kama hao? (Wapo.) Wapinga Kristo hutumia sadaka kununua nguo za hali ya juu, bidhaa za anasa, na hata magari. Niambieni, je, kiongozi wa uwongo wa aina hii anaweza kutambua tatizo hili? Yeye mwenyewe habadhiri sadaka, ana mtazamo huu, kwa hivyo, je, haamini kwamba ni vibaya kuzibadhiri? (Anaamini hivyo.) Basi, wapinga Kristo wanapofanya uovu mkubwa namna hiyo, kwa nini anaupuuza na haukomeshi? Kwa nini hauchukulii jambo hilo kwa uzito? (Hataki kuwakwaza watu.) Je, hilo si tendo ovu? (Ni tendo ovu.) Huku si kutimiza jukumu ambalo msimamizi anapaswa kutimiza. Ikiwa, wakati wa usimamizi wako, sadaka zinachukuliwa na kumilikiwa na watu waovu, ikiwa zinafujwa, kupotezwa, na kutumiwa kwa njia isiyo na urazini, ikiwa zinapotea hivi hivi, na bado hufanyi kazi yoyote au hata kusema neno, je, huko si kuacha wajibu? Je, huo si udhihirisho wa kiongozi wa uwongo? Ikiwa husemi unachopaswa kusema, hufanyi kazi unayopaswa kufanya, hutimizi jukumu unalopaswa kutimiza, na ingawa unaelewa kila fundisho, hufanyi tu kazi halisi, basi wewe hakika ni kiongozi wa uwongo. Unaamini, “Hata hivyo, sibadhiri sadaka; wengine wakifanya hivyo, hilo ni shauri lao.” Je, basi wewe si kiongozi wa uwongo? Kutobadhiri sadaka ni shauri lako binafsi, lakini, je, umelinda sadaka vizuri? Je, umetimiza jukumu lako kuhusiana na sadaka? Ikiwa hujatimiza, wewe ni kiongozi wa uwongo. Usijitafutie visingizio, ukisema: “Hata hivyo, sibadhiri sadaka, kwa hiyo mimi si kiongozi wa uwongo!” Kutobadhiri sadaka si sifa ya kigezo cha kupima kama kiongozi au mfanyakazi anafikia kiwango kinachostahili; kigezo cha kweli cha kama anafikia kiwango kinachostahili ni kama anatimiza jukumu lake, anatekeleza kile ambacho mtu anapaswa kufanya, na kutimiza wajibu ambao mtu anapaswa kutimiza, katika mambo aliyokabidhiwa na Mungu—hilo ndilo jambo muhimu zaidi. Kwa hiyo, katika usimamizi wa sadaka, wajibu na jukumu lako ni lipi? Je, umelitekeleza lote? Ni wazi kabisa kwamba hujalitekeleza. Unafanya mambo kwa namna isiyo ya dhati tu; unaogopa kuwakosea watu, lakini huogopi kumkosea Mungu. Unapuuza sadaka kwa sababu unaogopa kuwakosea watu, kuharibu taswira yako nzuri machoni pao—ikiwa una udhihirisho huu, wewe hakika ni kiongozi wa uwongo. Huku si kukubandika jina. Ukweli umewekwa wazi kwa wote kuona: Huwezi hata kutimiza wajibu na jukumu lako—wewe ni mbinafsi sana! Unasimamia vitu vyako mwenyewe, mali yako binafsi, vizuri kabisa, kwa dhamiri, na kwa uangalifu. Huviachii vitu hivyo viharibiwe na hali ya hewa; humruhusu yeyote avibebe, na humruhusu yeyote akutumie vibaya. Lakini inapokuja kwa sadaka, huna hisia ya uwajibikaji kabisa—hutekelezi hata sehemu ya kumi ya jukumu unalotekeleza linapokuja suala la kusimamia vitu vyako mwenyewe. Unawezaje kuchukuliwa kuwa msimamizi mwema? Unawezaje kuchukuliwa kuwa kiongozi au mfanyakazi? Bila shaka wewe ni kiongozi wa uwongo. Huu ni udhihirisho wa aina moja ya kiongozi wa uwongo.

III. Kuzuia Matumizi ya Maana

Kuna aina nyingine ya kiongozi wa uwongo, na wao pia wanachukiza sana. Baada ya watu kama hawa kuwa viongozi, wanaona kwamba mtu ambaye amekuwa akilinda matoleo amekuwa akitumia pesa kwa ubadhirifu na kwa uharibifu sana, kwa hivyo wanamtimua. Kisha wanatamani kupata mtu anayeweza kupanga kwa uangalifu na kupangilia bajeti kwa uangalifu, ambaye anabana matumizi kweli, na anayejua jinsi ya kuendesha nyumba kwa njia ya uekevu. Wanafikiri kwamba huyo ndiye aina ya mtu ambaye atakuwa mtumishi mzuri, na inatokea kwamba hawafikiri kwamba kuna yeyote anayefaa, na wanaishia kulinda matoleo wao wenyewe. Akina ndugu wanaposema kwamba nakala kadhaa za vitabu vya maneno ya Mungu zinahitaji kuchapishwa kwa ajili ya kuhubiri injili, viongozi hawa hawaruhusu hili kufanywa, wakifikiri kwamba inagharimu pesa nyingi sana kuchapisha vitabu; hawajali ikiwa vinahitajika kwa dharura kwa ajili ya kazi—kwao, ni sawa mradi tu waokoe pesa. Hawajui tu ni wapi ambapo kutumia matoleo ya Mungu kunalingana kabisa na nia Yake; wanachojua kufanya ni kulinda matoleo ya Mungu na kutoyaruhusu yaguswe kabisa. Hawatumii kile kinachopaswa kutumiwa—wanatekeleza udhibiti “vizuri” kweli, sawa! Je, kazi inawezaje kuendelea hivi? Je, viongozi hawa wana kanuni katika matendo yao? (La.) Hawaruhusu kazi inayopaswa kufanywa ifanywe, au kuruhusu vitabu vinavyopaswa kuchapishwa vichapishwe, au kuruhusu pesa zinazopaswa kutumika zitumike—hawaruhusu matumizi yoyote yanayofaa. Je, huo ni usimamizi? (La.) Ni nini? Ni ukosefu wa kuelewa kanuni. Watu wasioelewa kanuni hawajui jinsi ya kusimamia matoleo wanapofanya kazi. Wanaamini kwamba lazima waweke ulinzi juu ya pesa na wasiziache zipungue hata kwa senti moja, na kwamba, haijalishi matumizi ni yapi, pesa hazipaswi kuguswa. Je, hili linalingana na nia ya Mungu? (La, halilingani.) Kudhibiti mambo na kutekeleza ulinzi bila kanuni si usimamizi. Matumizi ya kiholela, uharibifu, na ubadhirifu si usimamizi, lakini kutoruhusu senti itumike na kuzuia matumizi yanayofaa kwa sababu ya udhibiti si usimamizi, pia. Hakuna kati ya haya linalolingana na kanuni. Kwa sababu watu wengine hawaelewi kanuni za kutumia, kutenga, na kusimamia matoleo, kila aina ya vituko na kila aina ya vurugu hutokea. Viongozi hawa wanaonekana kwa nje kuwa wenye kuwajibika na waliojitolea sana, lakini kazi wanayofanya ikoje? (Haina maadili.) Na kwa sababu haina maadili, kazi ya injili katika eneo lao inakumbana na kizuizi na vizuio, na kazi fulani za kitaalamu zinazuiwa, pia, kwa sababu ya udhibiti wao mkali kupita kiasi wa matumizi ya matoleo. Kwa juu juu, wanaonekana wenye kufanya kwa makini na kuwajibika sana katika ulinzi wao wa matoleo. Lakini kwa kweli, kwa sababu hawana ufahamu wa kiroho, na wanatenda tu kulingana na mawazo na fikira zao, na hata wanatekeleza udhibiti kwa ajili ya nyumba ya Mungu chini ya kisingizio cha uwekevu kwa ajili ya kanisa, wanaathiri sana maendeleo ya vipengele mbalimbali vya kazi ya kanisa bila hata kujua. Je, watu kama hao wanaweza kuainishwa kama viongozi wa uwongo? (Ndiyo.) Hili linawafanya wastahili kuwa viongozi wa uwongo. Kwa kiwango fulani, tayari wamesababisha vurugu na usumbufu kwa kazi ya injili na kwa kazi ya kanisa. Vurugu na usumbufu huu unasababishwa na ukosefu wao wa kuelewa kanuni, na pia wao kufanya kazi bila kujali kulingana na mapendeleo na mawazo yao wenyewe, na kutotafuta kanuni za ukweli, au kujadili mambo au kushirikiana na wengine. Matoleo hayataharibiwa au kubadhiriwa yakiwa nao, lakini hawawezi kutumia matoleo kwa njia busara kulingana na kanuni, na hawaruhusu yatumike kwa ajili tu ya kuyalinda, na matokeo yake kazi ya kueneza injili inacheleweshwa, na utendaji wa kawaida wa kazi ya nyumba ya Mungu unaathiriwa. Kwa hivyo, kulingana na udhihirisho huu, si kupita kiasi hata kidogo kuwaainisha kama viongozi wa uwongo. Kwa nini watu kama hao pia wanaainishwa kama viongozi wa uwongo? Hawajui jinsi ya kufanya kazi, na ufahamu wao wa jinsi ya kuchukulia matoleo na njia za kuyachukulia umepotoka sana, kwa hivyo, je, wanaweza kufanya kazi nyingine vizuri? Hakika hawawezi. Je, si kunalo tatizo na ufahamu wa watu hawa? (Lipo.) Ufahamu wao umepotoka, wanashikilia sheria, wanajihusisha na kujifanya, na ni wa roho wa bandia. Hawazingatii kazi ya nyumba ya Mungu, na hawatendi kulingana na kanuni—hawawezi kupata kanuni za kutenda, na wanafuata tu ujanja wao mdogo na mapenzi yao wenyewe na kufuata sheria. Hiyo ndiyo sababu kazi yao husababisha vurugu na usumbufu. Njia yao ya kufanya kazi ni ya kipumbavu na isiyo na ustadi—inachukiza. Watu kama hao bila shka ni viongozi wa uwongo. Je, kuna yeyote anayesema, “Ninalinda matoleo vizuri sana, ninafanya kazi hii kwa makini sana, na bado, ninaainishwa kama kiongozi wa uwongo. Basi sitayasimamia tena! Yeyote anayetaka kuyatumia na ayatumie; yeyote anayetaka kuyafanyia kitu na ayafanyie; yeyote anayetaka kuyachukua na ayachukue!”? Je, kuna yeyote aliye na wazo hilo? Basi, lengo letu ni nini katika kufichua hali na madhihirisho tofauti ya aina mbalimbali za viongozi wa uwongo? (Kuwawezesha watu wafahamu kanuni na kuepuka kutembea katika njia ya viongozi wa uwongo.) Hiyo ni sahihi. Ni kuwawezesha watu wafahamu kanuni, waweze kufanya kazi yao vizuri na kutimiza jukumu lao kulingana na kanuni, wasifuate fikira na mawazo, wasiwe na mapenzi ya kibinadamu au kuwa na harara, wasiruhusu nadharia waliyowaza iwe mbadala wa kanuni za ukweli, wasijifanye kuwa wa kiroho, na wasitumie kile wanachoamini kuwa hali ya kiroho kama kitu bandia au mbadala wa kanuni. Watu kama hao wapo miongoni mwa viongozi na wafanyakazi, na inafaa kuwachukulia kama onyo.

IV. Kutwaa na Kufurahia Sadaka

Kuna aina nyingine ya kiongozi wa uwongo, na kazi anayofanya linapokuja suala la kusimamia matoleo ni vurugu hata zaidi. Anaamini kwamba kama kiongozi au mfanyakazi, hawezi kila mara kukaza macho yake kwenye matoleo, au kuwa makini sana linapokuja suala la matoleo. Anafikiri kwa anahitaji tu kufanya kazi ya usimazi wa kanisa vizuri, na kutekeleza kazi ya maisha ya kanisa na ya kuingia katika uzima kwa watu wateule wa Mungu vizuri, na zaidi ya hayo, kuhakikisha kwamba aina mbalimbali za kazi za kitaalamu zinafanywa vizuri. Wanaamini kwamba matoleo ni pesa na vitu ambavyo Mungu hutoa kwa kanisa, na kwamba pesa hizi na vitu hivi vipo ili kukidhi mahitaji ya viongozi na wafanyakazi katika maisha na kazi yao. Maana iliyopo hapa ni kwamba matoleo yanatayarishwa kwa ajili ya viongozi na wafanyakazi, na kwamba punde tu mtu anapochaguliwa kama kiongozi au mfanyakazi, Mungu humruhusu afurahie matoleo haya, na kwamba viongozi na wafanyakazi wanapata kipaumbele katika kuyatenga, kuyafurahia, na kuyatumia—na hivyo, punde mtu anapokuwa kiongozi au mfanyakazi, anakuwa bwana wa matoleo, meneja na mmiliki wa matoleo. Watu wa aina hii wanapokutana na matoleo katika kazi yao, hawayasajili, hawayajumlishi, au kuyalinda, wala hawakagui hesabu za matoleo yanayoingia na kutoka, sembuse kukagua hali ya matumizi na utengaji wake. Badala yake, wanachunguza na kufahamu ni matoleo gani yaliyopo na kama kuna yoyote ambayo viongozi na wafanyakazi wanaweza kufurahia. Hii ndiyo aina ya mtazamo walio nao viongozi na wafanyakazi hawa kuelekea matoleo. Kwa mtazamo wao, matoleo hayahitaji kusajiliwa, kujumlishwa, kulindwa, au kukaguliwa mapato na matumizi yake au hali ya matumizi yake—mambo kama hayo hayawahusu—wanahitaji tu kuyatenga matoleo kwa ajili ya viongozi na wafanyakazi, wakiwapa kipaumbele linapokuja suala la kufurahia matoleo. Kwa mtazamo wao, kile wanachosema viongozi na wafanyakazi ndicho kanuni—ni uamuzi wao jinsi ya kutumia na kutenga matoleo. Wanaamini kwamba kuchaguliwa kama kiongozi au mfanyakazi kunamaanisha kwamba mtu tayari amefanywa kuwa kamili, na kwamba, kama kuhani, wana fursa ya kufurahia matoleo, pamoja na kuwa na kauli ya mwisho, haki ya matumizi, na haki ya kutenga linapokuja suala la matoleo. Katika makanisa fulani, kabla ya vitu ambavyo akina ndugu wanatoa kusajiliwa, kujumlishwa, na kuwekwa ghalani na wafanyakazi wanaofaa, viongozi na wafanyakazi tayari wameviangalia, kuvipepeta, na kuvichuja, wakiweka chochote wanachoweza kutumia, wakila chochote wanachoweza kula, wakivaa chochote wanachoweza kuvaa, na kutenga chochote wasichohitaji moja kwa moja kwa yeyote anayekihitaji, na hivyo kufanya maamuzi badala ya Mungu. Hii ndiyo kanuni yao. Ni nini kinachoendelea hapa? Je, wanafikiri kweli kwamba wao ni makuhani? Je, huku si kukosa busara sana? (Ndiyo.) Kuna viongozi na wafanyakazi wengine wanaoona kwamba familia moja imepungukiwa na viti viwili, kwamba nyingine inakosa jiko, na kwamba mtu fulani ana afya mbaya na anahitaji kutumia virutubisho vya afya, na kisha wanatumia pesa za nyumba ya Mungu kununua vitu hivi vyote. Utengaji, utumiaji, matumizi, na haki ya matumizi ya matoleo yote ni ya viongozi na wafanyakazi hawa—je, hili linaleta maana? Je, mbinu hii haisababishwi na kitu fulani kwenda mrama na utambuzi wao? Wanafanya maamuzi kwa msingi gani? Je, viongozi na wafanyakazi wana haki ya kudhibiti matoleo? (La.) Matoleo ni ya wao kusimamia, si ya wao kudhibiti na kutumia. Hawana haki ya kuyafurahia. Je, viongozi na wafanyakazi ni sawa na makuhani? Je, ni sawa na watu ambao wamefanywa kuwa watimimilifu? Je, wao ni wamiliki wa matoleo? (La.) Basi kwa nini wanaamua kutumia matoleo kuinunulia familia hii na ile vitu bila idhini—kwa nini wana haki hiyo? Nni nani aliyewapa haki hiyo? Je, mipangilio ya kazi inasema: “Jambo la kwanza ambalo viongozi na wafanyakazi wanapaswa kufanya baada ya kuchukua nafasi yao ni kuchukua udhibiti kamili juu ya fedha za nyumba ya Mungu”? (La.) Kwa nini kuna sehemu ya viongozi na wafanyakazi wanaoamini hili, basi? Tatizo ni nini hapo? Ndugu anapotoa vazi la bei ghali na kuna kiongozi au mfanyakazi analivaa siku inayofuata, ni nini kinachoendelea? Kwa nini matoleo yanayotolewa na akina ndugu yanaanguka mikononi mwa mtu binafsi? “Mtu binafsi” hapa linamaanisha kiongozi au mfanyakazi na si mtu mwingine yeyote. Hawashindwi tu kusimamia matoleo vizuri—badala yake, wanaongoza katika kuyanyakua na kuyafurahia kibinafsi. Tatizo ni nini hapa? Tukimtazama kiongozi au mfanyakazi huyu kwa kuzingatia kutofanya kwake kazi halisi linapokuja suala la usimamizi wa matoleo, anaweza basi kuainishwa kama kiongozi wa uwongo—lakini tukimtazama kwa kuzingatia yeye kunyakua na kufurahia matoleo kibinafsi, anaweza kuainishwa kwa asilimia mia moja kama mpinga Kristo. Basi, ni ipi hasa njia ya busara ya kumwainisha mtu anayehusika? (Kama mpinga Kristo.) Yeye ni kiongozi wa uwongo na mpinga Kristo pia. Katika kusimamia matoleo, viongozi wa uwongo huangalia matoleo yote, na kuwaagiza watu wayasimamie. Lakini kabla ya kufanya hivyo, wananyakua sehemu kwa ajili yao wenyewe na kuamua bila idhini kutenga sehemu nyingine. Kuhusu vitu vilivyosalia—ambavyo hawataki, au ambavyo hawatambui lakini hawataki kuvigawa—wanaviweka vitu hivi kando kwa muda. Linapokuja suala la mahali matoleo hayo yalipo, kama kuna mtu anayefaa kuyalinda, kama yanapaswa kukaguliwa mara kwa mara, kama kuna mtu anayaiba, au kama kuna mtu anayanyakua, viongozi wa uwongo kwa umoja hawajishughulishi na mambo haya. Kanuni yao ni hii: “Tayari nimepata mikononi mwangu vitu ninavyopaswa kufurahia na vitu ninavyohitaji. Yeyote anayetaka kuchukua vitu vilivyosalia ambavyo sihitaji anaweza kuvichukua; yeyote anayetaka kuvisimamia anaweza kuvisimamia. Ni vya yeyote anayevinyakua kwanza—yeyote ambaye vinaanguka mikononi mwake anapata faida.” Hii ni kanuni na mantiki ya aina gani? Watu kama hao ni mashetani na wanyama tu!

Wakati mmoja, kiongozi wa uwongo alisema kwamba kulikuwa na vitu vingi sana ghalani, na nikamuuliza kama alikuwa amevisajili. Akasema, “Sijui hata baadhi ya vitu hivyo ni nini, kwa hivyo hakuna njia ya kuvisajili.” Nikasema, “Huo ni upuuzi. Unawezaje kukosa njia ya kuvisajili? Kunapaswa kuwa na kumbukumbu zake tangu vilipoletwa hapa mwanzoni!” “Ilikuwa muda mrefu uliopita, hakuna njia ya kujua.” Haya ni matamshi ya aina gani? Je, anawajibika? (La.) Nikasema, “Kuna nguo kadhaa—angalia ni akina nani kati ya ndugu na dada wanazohitaji, na uwagawie nguo hizo.” “Baadhi yake zimepitwa na wakati. Hakuna anayezitaka.” Nikasema, “Gawa zile ambazo akina ndugu wanahitaji, na ushughulikie wasizohitaji inavyofaa.” Hakutekeleza hili. Je, alikuwa akifanya kazi kwa moyo na bidii? Anapoombwa kufanya kazi fulani, anaendelea kulalamika, akisema maneno hasi na kutaja shida. Asichosema ni kwamba atashughulikia mambo haya vizuri, kulingana na kanuni. Hana nia yoyote ya kutii. Haijalishi ni hitaji lipi ambalo mtu anampa, anaendelea kuzungumzia shida, kana kwamba akimfanya mtu huyo akose la kusema kwa kuendelea hivi, atashinda na kupata ushindi, na kisha amalize kazi yake. Huyu ni mtu wa aina gani? Hukufanywa kuwa kiongozi au mfanyakazi ili usababishe matatizo, au ili utaje ugumu na masuala—ilikuwa ili uweze kutatua matatizo na kushughulikia ugumu. Ikiwa una uwezo kweli katika kazi yako, basi baada ya kuibua masuala na ugumu, ungeendelea kuzungumzia jinsi ambavyo ungeshughulikia na kuyatatua kulingana na kanuni. Viongozi wa uwongo wanaweza tu kupiga mbiu wito, kuhubiri mafundisho, kusema maneno makubwa, na kuzungumzia sababu za uthibitisho na visingizio—hawana uwezo wowote wa kazi halisi, na katika usimamizi wa matoleo, vivyo hivyo hawawezi kutenda kulingana na kanuni au kutimiza jukumu lao. Hivi ndivyo walivyo punguani na wasio na uwezo, lakini bado wanahisi kwamba sasa kwa kuwa wao ni viongozi au wafanyakazi, wana fursa na hadhi, wana utambulisho wa heshima, na ni wamiliki na watumiaji wa matoleo. Kiongozi wa wa uwongo wa aina hii anajua tu jinsi ya kufurahia fursa ya kutumia matoleo—hawezi kuona au kugundua visa vyovyote vya matumizi yasiyo ya busara, ya kiholela ya matoleo, na anaweza hata kuyaona lakini asifanye chochote kuyashughulikia. Kwa nini iwe hivi? Ni kwa sababu wanajua tu kufurahia hisia ya kujiona bora inayokuja na kuwa kiongozi au mfanyakazi—hawana uelewa wowote wa mahitaji ya Mungu kwa viongozi na wafanyakazi au wa kanuni za kufanya kazi ya nyumba ya Mungu. Wao ni nyangarika, ni takataka, na ni punguani. Je, si jambo la kuchukiza kwamba watu waliokanganyika kama hao bado wanataka kufurahia manufaa ya hadhi? Mmeelewa nini kutokana na ufichuzi wetu wa kiongozi wa uongo wa aina hii? Punde tu mtu wa aina hii anapokuwa kiongozi au mfanyakazi, anataka kupanga njama kuhusu matoleo, na macho yao yanakazwa kwenye matoleo. Kwa kutazama tu, mtu anaweza kujua kwamba amekuwa akitamani kwa muda mrefu kutumia pesa kwa ubadhirifu na kubadhiri matoleo. Sasa, hatimaye, ana nafasi yake; anaweza kutumia pesa kiholela kwa namna hiyo, na kutumia toleo la Mungu jinsi atakavyo, akifurahia vitu asivyovifanyia kazi. Sura yake halisi ya ulafi inafichuliwa kikamilifu hivyo. Je, mnawaona watu kama hao miongoni mwa viongozi na wafanyakazi, wa zamani na wa sasa? Kila mara anaeleza vibaya majukumu na ufafanuzi wa viongozi na wafanyakazi, na punde tu anapokuwa kiongozi au mfanyakazi, anajichukulia kuwa bwana wa nyumba ya Mungu, anajiweka miongoni mwa safu ya makuhani, na anajiona kuwa mtu wa heshima. Je, huku si kuwa punguani kidogo? Je, ni kwamba punde tu mtu anapokuwa kiongozi au mfanyakazi, yeye si mwanadamu mpotovu tena? Je, ni kwamba anageuka mara moja kuwa mtu mtakatifu? Punde anapokuwa kiongozi, hajijui yeye ni nani tena, na anafikiri kwamba anapaswa kufurahia matoleo—je, watu kama hao si punguani? Watu kama hao hakika ni punguani, hawana busara ya binadamu wa kawaida. Hata baada ya sisi kushiriki namna hii, bado hawajui wajibu na majukumu ya viongozi na wafanyakazi ni yapi. Hakika wapo viongozi na wafanyakazi kama hao, na udhihirisho wa watu kama hao ni dhahiri sana na yanajitokeza wazi.

Huu hakika ndio udhihirisho wa viongozi wa uwongo wa aina mbalimbali kuhusu kulinda matoleo. Wale walio na matatizo makubwa zaidi hawaingii katika kitengo cha viongozi wa uwongo—wao ni wapinga Kristo. Kwa hivyo, mnahitaji kuelewa vizuri upeo huu. Ikiwa mtu ni kiongozi wa uwongo, yeye ni kiongozi wa uwongo—hawezi kuainishwa kama mpinga Kristo. Wapinga Kristo ni waovu zaidi kuliko viongozi wa uwongo kwa upande wa ubinadamu, matendo, udhihirisho, na kiini. Viongozi wengi wa uwongo wana ubora duni wa tabia, ni punguani, hawana uwezo wa kazi, wamepotoka katika ufahamu wao na hawana ufahamu wa kiroho, sifa zao ni duni, ni wabinafsi na wenye kustahili dharau, na mioyo yao haiko mahali sahihi. Hili linasababisha wasiweze na wasifanye kazi halisi kuhusiana na kulinda matoleo, na inaathiri usimamizi wa busara na ulinzi unaofaa wa matoleo. Hata sehemu ya matoleo huanguka mikononi mwa watu waovu kwa sababu ya viongozi wa uwongo kupuuza majukumu yao, kutofanya kazi halisi, na kutotenda kulingana na kanuni na mahitaji ya nyumba ya Mungu—tatizo la aina hii pia hujitokeza sana. Udhihirisho mbalimbali wa viongozi wa uwongo katika kulinda matoleo kimsingi unafichuliwa hivi: Sifa zao ni duni, ni wabinafsi na wenye kustahili dharau, ufahamu wao umepotoka, wanakosa uwezo wa kazi, ubora wao wa tabia ni duni, hawatafuti kanuni za ukweli hata kidogo, na wako kama watu bubu na punguani. Wengine wanaweza kusema, “Tunakiri udhihirisho mwingine wte ambao Ulifichua, lakini ikiwa wao ni bubu na punguani, waliwezaje kuwa viongozi?” Je, mnakiri kwamba viongozi na wafanyakazi wengine ni bubu na punguani? Je, watu kama hao wapo? Wengine wanaweza kusema, “Unatudharau sana. Sisi sote ni watu wa kisasa, wahitimu wa chuo au shule ya upili—tuna uwezo bora za utambuzi kuhusiana na jamii hii na biadamu. Tungewezaje kumchagua mtu punguani kuwa kiongozi wetu? Hilo halingewezekana!” Kuna nini kisichowezekana kuhusu hilo? Wengi wenu ni punguani, na wenye akili pungufu pia, kwa hivyo ni rahisi sana kwenu kumchagua mtu punguani kuwa kiongozi. Kwa nini Ninasema wengi wenu ni punguani? Kwa sababu wengi wenu, bila kujali mmepitia kiasi gani, hamwezi kuona kiini cha mambo na hamwezi kufahamu kanuni. Mnaweza kuendelea kushika sheria tu kwa miaka na miaka, mkitumia mbinu ileile kwa kurudia bila mabadiliko, mkibaki bila uwezo wa kufahamu kanuni haijalishi ukweli unashirikiwa vipi kwenu. Tatizo ni lipi hapa? Ubora wenu wa tabia ni duni sana. Hamwezi kuona kiini au mzizi wa matatizo, na hamwezi kupata mifumo ya maendeleo ya mambo, sembuse kufuata kanuni zinazopaswa kuwepo katika kufanya mambo—huku kunaitwa kuwa punguani. Inawachukua muda gani nyote kufahamu kanuni za mambo yanayohusiana na wajibu wenu? Kuna watu wengine ambao wamekuwa wakifanya kazi ya maandishi kwa miaka kadhaa, lakini hata sasa, makala na miswada wanayoandika yote bado ni maneno matupu, bado hawawezi kufahamu kanuni, na hawajui uhalisi ni nini, au jinsi ya kusema kitu halisi. Huku ni kuwa na ubora duni sana wa tabia na akili duni sana. Kwa akili mliyo nayo, je, haikuwa rahisi sana kwenu kumchagua mtu punguani kama kiongozi? Na hamkumchagua tu, pia mlimwekea mioyo yenu. Alipokuwa karibu kutimuliwa, hamkutaka hilo litokee. Miaka miwili baadaye, mlipokuwa mmemng’amua na kupata uelewa, hapo ndipo mlikuwa na uwezo wa kutambua kwamba yeye ni kiongozi wa uwongo, lakini wakati huo, haijalishi mliambiwa nini, hamkuruhusu atimuliwe. Je, nyinyi si punguani hata kuliko yeye? Kwa nini Ninasema kwamba viongozi na wafanyakazi wengine wana akili pungufu? Ni kwa sababu wanajua tu jinsi ya kufanya kazi rahisi zaidi. Linapokuja suala la kazi ngumu kidogo zaidi, hawajui jinsi ya kuifanya, wanapokumbana na ugumu kidogo, hawajui jinsi ya kuushughulikia, na wanapopewa kazi ya ziada, hawajui la kufanya. Je, hili si tatizo la akili zao? Je, si viongozi kama hawa wanachaguliwa nyinyi? Na mnasujudu kwa kuwaheshimu: “Wanamwamini Mungu bila kutafuta mpenzi wa kimapenzi, na wamejitumia kwa ajili ya Mungu kwa zaidi ya miaka ishirini. Wana azimio la kuteseka, sawa, na wako makini sana kuhusu kazi yao.” “Je, wanaelewa kanuni katika kazi yao, hata hivyo?” “Kama hawaelewi, basi ni nani anayeelewa?” Na inatokea kwamba kazi yao ni vurugu tupu inapokaguliwa—hawawezi kutekeleza kazi yoyote. Wanaambiwa kanuni za kazi yao, lakini hawajui kamwe jinsi ya kuifanya. Wanaendelea tu kuuliza maswali, na hawajui la kufanya isipokuwa waambiwe moja kwa moja. Kuwaambia kanuni ni sawa na kutosema chochote; hata kama kanuni zimeorodheshwa, moja baada ya nyingine, bado hawatajua jinsi ya kutekeleza kazi. Je, kuna viongozi kama hawa? Haijalishi wanaambiwa kanuni vipi, hawazielewi, na hawawezi kutekeleza kazi. Shiriki nao au uwaagize kuhusu maneno yaleyale au jambo lilelile mara kadhaa, na bado, hawataelewa, na tatizo halitatatuliwa kabisa baadaye—bado watauliza la kufanya, na haitafaa ikiwa mstari mmoja utaachwa. Je, wao si punguani? Je, viongozi hawa punguani hawachaguliwi na nyinyi? (Wanachaguliwa.) Hamwezi kukana hilo, sivyo? Hakika wapo viongozi kama hao.

Udhihirisho mbalimbali wa viongozi wa uwongo ambao tumekuwa tukishiriki leo yanahusiana hasa na kazi ya kusimamia matoleo. Kupitia ufichuzi wetu wa udhihirisho mbalimbali wa viongozi wa uwongo, watu wanapaswa kujua kwamba kusimamia matoleo ni kazi muhimu kwa viongozi na wafanyakazi, na kwamba hawapaswi kuipuuza. Ingawa kazi hii ya mambo ya jumla ni tofauti na kazi nyingine, inahusiana na uendeshaji wa kawaida wa kazi nyingine ya nyumba ya Mungu. Kwa hivyo, kusimamia matoleo ni kazi muhimu sana, na ya kipekee. Je, ni muhimu kivipi? Vitu vinavyolindwa katika kazi ya kusimamia matoleo ni vya Mungu—kusema kwa njia isiyofaa kiasi, vitu hivyo ni mali binafsi ya Mungu, kwa hivyo viongozi na wafanyakazi wanapaswa zaidi kujitolea kwa moyo wote, kuwa wenye dhamiri, na wenye bidii kuhusiana na kazi hii. Tukiitazama kazi hii kwa kuzingatia asili yake, Sidhani kama ni kutia chumvi kuiorodhesha chini ya kazi ya utawala. Sababu inayotufanya tuiorodheshe chini ya kitengo cha kazi ya utawala ni kwamba kufanya kazi hii kunahusiana na mitazamo ya watu kumwelekea Mungu na kuelekea mali Yake. Kwa hivyo, ni muhimu kwa watu kuwa na mtazamo sahihi na kufahamu kanuni sahihi katika kufanya kazi hii. Sababu inayotufanya tuiweke ndani ya kitengo cha kazi ya utawala ni kuwafanya viongozi na wafanyakazi waelewe kwamba ni muhimu sana kufanya kazi hii, na kwamba kazi hii ni agizo zito sana na mzigo mzito sana. Ni kuwafanya waelewe kwamba hawapaswi kuichukulia kana kwamba ni kazi ya kawaida ya mambo ya jumla—kwamba lazima wawe na maarifa sahihi, na ya kina juu ya umuhimu wa kazi hii, na kisha wafikie kuwa wawekevu, wenye dhamiri, na wenye bidii kuhusiana nayo. Watu wanaweza kukosa kuwa makini kuelekea watu wengine—hata makosa yakitokea, si tatizo kubwa. Lakini Ninawasihi watu wasikanganyike, wasifanye mambo kijuujuu, na wasiwe wa kusema tu bila kutenda katika jinsi wanavyomchukulia Mungu. Kufanya kazi ya kusimamia matoleo vizuri ni agizo muhimu kwa viongozi na wafanyakazi kutoka kwa Mungu.

Mei 8, 2021

Iliyotangulia: Majukumu ya Viongozi na Wafanyakazi (11)

Inayofuata: Majukumu ya Viongozi na Wafanyakazi (21)

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp