Dibaji
Ingawa watu wengi wanaamini katika Mungu, ni wachache wanaoelewa maana ya imani katika Mungu ni nini, na jinsi wanavyopaswa kufanya hasa ili walingane na nia za Mungu. Hii ni kwa sababu, ingawa watu wanalijua neno “Mungu” na mafungu ya maneno kama “kazi ya Mungu”, hawamjui Mungu, sembuse kuijua kazi ya Mungu. Si ajabu, basi, kwamba wale wote wasiomjua Mungu wamechanganyikiwa katika imani yao Kwake. Watu hawaichukulii imani katika Mungu kwa uzito, na hili kwa ukamilifu ni kwa sababu kumwamini Mungu ni jambo geni sana, jambo lisilofahamika sana kwao. Kwa njia hii, wanapungukiwa sana kufikia matakwa ya Mungu. Kwa maneno mengine, ikiwa watu hawamjui Mungu, na hawaijui kazi Yake, basi hawawezi kuwa wenye kustahili kutumiwa na Mungu, sembuse kuweza kuridhisha nia za Mungu. “Imani katika Mungu” inamaanisha kuamini kwamba kuna Mungu; hii ndiyo dhana rahisi zaidi ya imani katika Mungu. Kueleza kwa urefu zaidi, kuamini kwamba kuna Mungu si sawa na kuamini katika Mungu kwa ukweli; badala yake, ni aina ya imani rahisi yenye mwelekeo mzito wa kidini. Imani ya kweli katika Mungu inamaanisha yafuatayo: Kwa msingi wa imani kwamba Mungu ana mamlaka juu ya vitu vyote, mtu hupitia maneno Yake na kazi Yake, na kwa hivyo hutupa mbali tabia zake potovu, huridhisha nia ya Mungu, na kuja kumjua Mungu. Ni safari ya aina hii pekee ndiyo inayoweza kuitwa “imani katika Mungu.” Hata hivyo, watu mara nyingi huiona imani katika Mungu kama jambo rahisi na la purukushani sana. Watu wanapomwamini Mungu kwa njia hii, hilo hupoteza maana yake, na ingawa wanaweza kuendelea kuamini mpaka mwisho kabisa, hawatapata kamwe kibali cha Mungu, kwa sababu wanatembea katika njia isiyo sahihi. Wale ambao, hadi leo, wanamwamini Mungu katikati ya maneno na mafundisho matupu, bado hawajui kwamba wanakosa kiini cha imani katika Mungu, na kwamba hawawezi kupokea kibali cha Mungu. Bado wanamwomba Mungu awabariki na amani na neema ya kutosha. Hebu tuitulize mioyo yetu na tutafakari kwa kina: Je, yawezekana kuwa kumwamini Mungu ndilo jambo rahisi zaidi duniani? Je, yawezekana kuwa kumwamini Mungu hakuna maana zaidi ya kupokea neema nyingi kutoka kwa Mungu? Je, watu wanaomwamini Mungu bila kumjua au wanaomwamini Mungu na bado wanampinga wanaweza kweli kuridhisha nia za Mungu?
Mungu na mwanadamu hawawezi kuzungumziwa kwa usawa. Kiini Chake na kazi Yake ni vitu visivyoweza kueleweka na kufahamika kabisa kwa mwanadamu. Mungu asipofanya kazi Yake na kunena maneno Yake binafsi miongoni mwa wanadamu, basi, haijalishi chochote, mwanadamu hataweza kuelewa nia za Mungu. Na hivyo, hata wale ambao wamejitolea maisha yao yote kwa Mungu hawangeweza kupokea kibali Chake. Mungu asipoanza kufanya kazi, basi haijalishi mwanadamu atafanya vizuri kiasi gani, yote yatakuwa bure, kwa sababu mawazo ya Mungu daima yatakuwa juu kuliko mawazo ya mwanadamu, na hekima ya Mungu haiwezi kueleweka na mtu yeyote. Na kwa hivyo Ninasema kwamba wale ambao “wanamwelewa kikamilifu” Mungu na kazi Yake ni watu wasiofaa; wote wana kiburi na ni wajinga. Mwanadamu hapaswi kuiwekea mipaka kazi ya Mungu; zaidi ya hayo, mwanadamu hawezi kuiwekea mipaka kazi ya Mungu. Machoni pa Mungu, mwanadamu ni mdogo tu kuliko chungu; kwa hivyo mwanadamu anawezaje kuielewa kazi ya Mungu? Wale ambao daima wanaropoka, “Mungu hafanyi kazi kwa njia hii au ile,” au “Mungu yuko hivi au vile”—je, hawazungumzi kwa kiburi? Sote tunapaswa kujua kwamba mwanadamu, ambaye ni wa mwili, amepotoshwa na Shetani, kwamba asili yake hasa ni kumpinga Mungu, na kwamba hawezi kuwa kwenye kiwango sawa na Mungu, sembuse kutoa ushauri wowote linapokuja suala la kazi ya Mungu. Kuhusiana na jinsi Mungu anavyomwongoza mwanadamu, hii ni kazi ya Mungu Mwenyewe. Ni jambo la kufaa kwamba mwanadamu atii, bila kuwa na mtazamo huu au ule, kwa maana mwanadamu ni mavumbi tu. Kwa kuwa ni nia yetu kumtafuta Mungu, hatupaswi kuweka mawazo yetu kwenye kazi Yake ili Mungu ayazingatie, sembuse kutumia tabia zetu potovu kupinga kazi ya Mungu kwa makusudi na kwa nguvu. Je hili halitatufanya wapinga Kristo? Je, watu kama hawa wanawezaje kusemekana kuwa wanamwamini Mungu hata kidogo? Kwa maana tunaamini kuwa kuna Mungu, na kwa kuwa tunataka kumridhisha na kumwona, tunapaswa kutafuta njia ya ukweli, na njia ya ulinganifu na Mungu. Hatupaswi kuwa katika upinzani sugu Kwake. Ni jambo gani jema linaloweza kutokana na hili?
Leo hii, Mungu amefanya kazi mpya. Unaweza kukosa kuyakubali maneno haya, na yanaweza kuonekana yasiyo ya kawaida kwako, lakini Ningekushauri usifichue uasili wako kwa sasa, kwa maana wale tu walio na njaa na kiu ya haki kweli mbele za Mungu ndio wanaweza kupata ukweli, na wale tu wanaomcha Mungu kwa kweli ndio wanaoweza kutiwa nuru na kuelekezwa na Yeye. Matokeo hupatikana kwa kutafuta ukweli kwa utulivu wa busara, si kwa ugomvi na ubishi. Ninaposema kwamba “leo, Mungu amefanya kazi mpya,” Ninarejelea suala la Mungu kurudi katika mwili. Pengine maneno haya hayakusumbui; pengine unayachukia; au pengine yanakuvutia sana. Katika hali yoyote, Ninatumai kwamba wale wote ambao kwa kweli wanatamani sana Mungu aonekane wanaweza kukabiliana na ukweli huu na kuuchunguza kwa makini, badala ya kukurupuka kuhitimisha kuuhusu; hilo ndilo jambo ambalo mtu mwenye hekima anapaswa kufanya.
Si vigumu kuchunguza jambo kama hilo, lakini linahitaji kila mmoja wetu kwanza ajue ukweli huu mmoja: Yeye ambaye ni Mungu mwenye mwili ana kiini cha Mungu, na Yeye ambaye ni Mungu mwenye mwili ana maonyesho ya Mungu. Kwa kuwa Mungu amepata mwili, Anakuja na kazi Anayokusudia kufanya, na kwa kuwa Yeye ni Mungu mwenye mwili, Anaonyesha kile Alicho, na anaweza kumletea mwanadamu ukweli, kumpa uzima, na kumwonyesha njia. Mwili ambao hauna kiini cha Mungu kwa vyovyote sio Mungu mwenye mwili; hakuna shaka kuhusu jambo hili. Kama mwanadamu anakusudia kuchunguza ikiwa ni mwili wa Mungu mwenye mwili, basi lazima abaini hili kutokana na tabia Anayoonyesha na maneno Anayonena. Yaani, kubaini ikiwa ni mwili wa Mungu mwenye mwili au la, na ikiwa ni njia ya kweli au la, mtu lazima atofautishe kwa msingi wa kiini Chake. Na kwa hivyo, jambo la msingi kuhusiana na kama ni mwili wa Mungu mwenye mwili au la linategemea kiini Chake (kazi Yake, matamko Yake, tabia Yake, na vipengele vingine vingi), badala ya mwonekano wa nje. Ikiwa mwanadamu anachunguza tu mwonekano Wake wa nje, na kama matokeo anapuuza kiini Chake, hili linaonyesha kwamba mwanadamu ni mpumbavu na mjinga. Mwonekano wa nje hauwezi kuamua kiini; zaidi ya hayo, kazi ya Mungu haiwezi kamwe kulingana na fikira za mwanadamu. Je, mwonekano wa nje wa Yesu haukuenda kinyume na mawazo ya mwanadamu? Je, sura na mavazi Yake havikushindwa kuonyesha utambulisho Wake wa kweli? Je, Mafarisayo wakati huo hawakumpinga Yesu hasa kwa sababu walitazama tu mwonekano Wake wa nje, na hawakukubali maneno kutoka kinywani Mwake kwa makini? Ni tumaini Langu kwamba kila ndugu na dada anayetafuta kuonekana kwa Mungu hatarudia mkasa wa historia, na hatakuwa Mfarisayo wa nyakati za kisasa na kumsulubisha Mungu tena. Unapaswa kufikiria kwa makini jinsi ya kukaribisha kurudi kwa Mungu, na unapaswa kuwa na akili iliyo wazi kuhusu jinsi ya kuwa mtu anayetii ukweli. Hili ni jukumu la kila mtu anayemngoja Yesu arudi akiwa juu ya wingu. Tunapaswa kusafisha macho yetu ya kiroho, na tusikwame katika maneno ya njozi. Tunapaswa kufikiria kuhusu kazi halisi ya Mungu, na tuangalie kipengele cha vitendo cha Mungu. Msijisahau au kupotea katika ndoto za mchana, mkitumaini daima kwamba Bwana Yesu atashuka ghafla miongoni mwenu juu ya wingu, na kuwachukua ninyi ambao hamjawahi kumjua au kumwona, na ambao hamjui jinsi ya kufuata mapenzi Yake. Ni bora kufikiria kuhusu mambo yenye uhalisi zaidi!
Unaweza kuwa umefungua kitabu hiki kwa ajili ya utafiti, au ukiwa na nia ya kukubali; haijalishi mtazamo wako, Natumaini kuwa utakisoma mpaka mwisho, na hutakiweka kando kwa urahisi. Pengine, baada ya kuyasoma maneno haya, mtazamo wako utabadilika, lakini hilo linategemea msukumo wako na kiwango chako cha ufahamu. Kunalo jambo moja hata hivyo unalotakiwa kujua: Neno la Mungu haliwezi kuchukuliwa kuwa neno la mwanadamu, na sembuse mtu kulifanya neno la mwanadamu kuwa neno la Mungu. Mtu anayetumiwa na Mungu si Mungu mwenye mwili, na Mungu mwenye mwili si mtu anayetumiwa na Mungu. Katika hili, kuna tofauti ya kiini. Pengine, baada ya kusoma maneno haya, huyakubali kuwa maneno ya Mungu, bali tu kama nuru ambayo mtu amepata. Katika hali hiyo, wewe ni mjinga sana. Maneno ya Mungu yanawezaje kuwa sawa na nuru ambayo mwanadamu amepata? Maneno ya Mungu mwenye mwili yanaanzisha enzi mpya, yanawaongoza wanadamu wote, yanafunua siri, na kumwonyesha mwanadamu mwelekeo anaopaswa kuchukua katika enzi mpya. Nuru aliyopata mwanadamu si chochote ila utendaji fulani rahisi au maarifa. Haiwezi kuwaongoza wanadamu wote kuingia katika enzi mpya au kufunua siri za Mungu Mwenyewe. Hatimaye, Mungu ni Mungu, na mwanadamu ni mwanadamu. Mungu ana kiini cha Mungu, na mwanadamu ana kiini cha mwanadamu. Ikiwa mwanadamu anayaona maneno yaliyonenwa na Mungu kama nuru rahisi ya Roho Mtakatifu, na kuyachukulia maneno ya mitume na manabii kama maneno yaliyonenwa na Mungu binafsi, hilo litakuwa kosa la mwanadamu. Haijalishi chochote, hupaswi kamwe kugeuza nyeusi kuwa nyeupe, au kufanya la juu kuwa la chini, au kuelezea jambo la kina kuwa la kijuujuu; haijalishi chochote, hupaswi kamwe kukanusha kwa makusudi kile unachojua wazi kuwa ukweli. Kila mtu anayeamini kwamba kuna Mungu anapaswa kuchunguza mambo kutoka kwa msimamo sahihi, na kukubali kazi mpya ya Mungu na maneno Yake mapya kutoka kwa nafasi ya kiumbe aliyeumbwa; la sivyo, ataondoshwa na Mungu.
Baada ya kazi ya Yehova, Yesu alipata mwili ili afanye kazi Yake miongoni mwa wanadamu. Kazi Yake haikutekelezwa kivyake, lakini ilijengwa juu ya msingi wa kazi ya Yehova. Ilikuwa kazi ya enzi mpya ambayo Mungu alifanya baada ya Yeye kukamilisha Enzi ya Sheria. Vivyo hivyo, baada ya kazi ya Yesu kukamilika, Mungu aliendelea na kazi Yake ya enzi iliyofuata, kwa sababu usimamizi wote wa Mungu huendelea mbele siku zote. Enzi ya zamani ikipita, itabadilishwa na enzi mpya, na mara tu kazi ya zamani imekamilika, kutakuwa na kazi mpya ya kuendeleza usimamizi wa Mungu. Kupata mwili huku ni kupata mwili kwa Mungu mara ya pili, ambako kunafuatia kazi ya Yesu. Bila shaka, kupata mwili huku hakufanyiki kivyake; ni hatua ya tatu ya kazi baada ya Enzi ya Sheria na Enzi ya Neema. Kila wakati ambapo Mungu anaanzisha hatua mpya ya kazi, kila mara lazima kuwe na mwanzo mpya na kila mara lazima ilete enzi mpya. Vivyo hivyo kuna mabadiliko yanayolingana katika tabia ya Mungu, katika namna ya kufanya Kwake kazi, katika mahali Pake pa kazi, na katika jina Lake. Si ajabu, basi, kwamba ni vigumu kwa mwanadamu kukubali kazi ya Mungu katika enzi mpya. Lakini bila kujali jinsi anavyopingwa na mwanadamu, Mungu anafanya kazi Yake daima, na daima Yeye huwa Akiongoza wanadamu wote kuendelea mbele. Yesu alipokuja katika ulimwengu wa mwanadamu, Aliileta Enzi ya Neema na kuitamatisha Enzi ya Sheria. Wakati wa siku za mwisho, Mungu alipata mwili kwa mara nyingine, na kwa mwili huu, Aliitamatisha Enzi ya Neema na kuianzisha Enzi ya Ufalme. Wale wote wanaoweza kukubali kupata mwili kwa mara ya pili kwa Mungu wataongozwa kuingia katika Enzi ya Ufalme, na zaidi ya hayo wao binafsi wataweza kupokea mwongozo wa Mungu. Hata ingawa Yesu Alikuja miongoni mwa wanadamu na alifanya kazi nyingi, Alimaliza tu kazi ya kuwakomboa wanadamu wote na Akawa kama sadaka ya dhambi ya mwanadamu; Hakumwondolea mwanadamu tabia zake zote potovu. Kumwokoa mwanadamu kikamilifu kutokana na ushawishi wa Shetani hakukuhitaji Yesu tu kuwa sadaka ya dhambi na kubeba dhambi za mwanadamu, lakini pia kulihitaji Mungu afanye kazi kubwa zaidi ili kumwondolea mwanadamu tabia zake zilizopotoshwa na Shetani kikamilifu. Na kwa hivyo, baada ya mwanadamu kusamehewa dhambi zake, Mungu alirudi katika mwili kumwongoza mwanadamu kuingia katika enzi mpya, na akaanza kazi ya kuadibu na hukumu. Kazi hii imemleta binadamu katika ulimwengu wa juu zaidi. Wale wote wanaotii chini ya utawala Wake watafurahia ukweli wa juu zaidi na kupokea baraka kuu zaidi. Wataishi kikweli katika nuru, na watapata ukweli, njia na uzima.
Watu wakibaki wamekwama katika Enzi ya Neema, basi hawatawahi kuondolewa tabia zao potovu, sembuse kujua tabia ya asili ya Mungu. Watu wakiishi daima katikati ya wingi wa neema, lakini wasiwe na njia ya uzima inayowaruhusu kumjua Mungu au kumridhisha Yeye, basi kamwe hawataweza kumpata Yeye kwa kweli katika imani yao Kwake. Imani ya aina hii ni ya kusikitisha kweli. Unapokuwa umemaliza kusoma kitabu hiki, unapokuwa umepitia kila hatua ya kazi ya Mungu mwenye mwili katika Enzi ya Ufalme, utahisi kwamba matamanio ambayo umekuwa nayo kwa miaka mingi hatimaye yamefanikishwa. Utahisi kwamba ni sasa tu ndipo umemwona Mungu ana kwa ana; ni sasa tu ndipo umeutazama uso wa Mungu, umeyasikia matamko Yake mwenyewe, umeifahamu hekima ya kazi Yake, na kuhisi kwa kweli jinsi Alivyo wa vitendo na mwenye uweza. Utahisi kwamba umepata vitu vingi ambavyo watu katika nyakati zilizopita hawakuwahi kuviona wala kuwa navyo. Wakati huu, utajua kwa uhakika ni nini hasa kuamini katika Mungu, na ni nini maana ya kulingana na nia za Mungu. Bila shaka, ukishikilia maoni ya zamani, na ukatae au ukane ukweli wa kupata mwili kwa Mungu mara ya pili, basi utabaki mkono mtupu, hutapata chochote, na mwishowe utatajwa kuwa na hatia ya kumpinga Mungu. Wale wanaoweza kuutii ukweli na kuitii kazi ya Mungu watachukuliwa chini ya jina la Mungu mwenye mwili wa pili—mwenye Uweza. Wataweza kukubali uelekezi wa Mungu mwenyewe, wakipata ukweli zaidi na wa juu zaidi, na vile vile maisha ya kweli. Wataona maono ambayo hayajawahi kuonwa hapo awali na watu wa zamani: “Na nikageuka ili niione ile sauti iliyonena nami. Na nilipogeuka, niliona vinara saba vya taa vilivyokuwa vya dhahabu; Na hapo katikati ya hivyo vinara saba vya taa nilimwona mtu aliyefanana na Mwana wa Adamu, aliyekuwa amevalia nguo iliyofika katika miguu yake, na kifuani alikuwa amefungwa kanda ya dhahabu. Kichwa Chake na nywele Zake zilikuwa nyeupe mithili ya sufu, nyeupe mithili ya theluji; na macho Yake yalikuwa mithili ya ulimi wa moto; Na miguu Yake mithili ya shaba safi, kama kwamba ilikuwa imechomwa ndani ya tanuru; na sauti Yake ilikuwa mithili ya sauti ya maji mengi. Na katika mkono Wake wa kulia Alikuwa na nyota saba: na kinywani Mwake mlitoka upanga mkali wenye makali kuwili: nao uso Wake ulikuwa mithili ya jua liangazavyo kupitia nguvu zake” (Ufunuo 1:12-16). Maono haya ni maonyesho ya tabia nzima ya Mungu, na maonyesho ya tabia Yake nzima pia ndiyo maonyesho ya kazi ya Mungu katika mwili Wake wa sasa. Katika mibubujiko ya kuadibu na hukumu, Mwana wa Adamu anaonyesha tabia Yake ya asili kwa njia ya matamko, Akiwaruhusu wale wote wanaokubali kuadibu Kwake na hukumu wauone uso wa kweli wa Mwana wa Adamu, ambao ni onyesho la kuaminika la uso wa Mwana wa Adamu alivyoonekana na Yohana. (Bila shaka, yote haya hayataonekana kwa wote wasioikubali kazi ya Mungu katika Enzi ya Ufalme.) Uso wa kweli wa Mungu hauwezi kuelezwa kikamilifu kutumia lugha ya mwanadamu, na hivyo Mungu hutumia njia hii ya kuonyesha tabia Yake asili kuuonyesha uso Wake wa kweli kwa mwanadamu. Yaani, wote ambao wameifahamu tabia asili ya Mwana wa Adamu wameuona uso wa kweli wa Mwana wa Adamu, kwa kuwa Mungu ni mkuu kabisa na Hawezi kuelezwa kikamilifu kutumia lugha ya mwanadamu. Mara tu mwanadamu amepitia kila hatua ya kazi ya Mungu katika Enzi ya Ufalme, basi atapata kujua maana halisi ya maneno ya Yohana alipozungumza kuhusu Mwana wa Adamu kati ya vinara vya taa: “Kichwa Chake na nywele zilikuwa nyeupe mithili ya sufu, nyeupe mithili ya theluji; na macho Yake yalikuwa mithili ya ulimi wa moto; Na miguu Yake mithili ya shaba safi, kama kwamba ilikuwa imechomwa ndani ya tanuri; na sauti Yake ilikuwa mithili ya sauti ya maji mengi. Na katika mkono Wake wa kulia Alikuwa na nyota saba: na kinywani Mwake mlitoka upanga mkali wenye makali kuwili: nao uso Wake ulikuwa mithili ya jua liangazavyo kupitia nguvu zake.” Wakati huo, utajua bila shaka yoyote kwamba mwili huu wa kawaida ambao umesema mengi sana bila shaka ni Mungu mwenye mwili wa pili. Zaidi ya hayo, utahisi kwa kweli jinsi ambavyo umebarikiwa, na kujihisi mwenyewe kuwa mwenye bahati kubwa kabisa. Je, wewe hauko radhi kukubali baraka hii?
Sehemu ya kwanza ya kitabu hiki ni “Matamshi ya Kristo Mwanzoni”. Maneno haya yanawakilisha mpito kutoka mwisho wa Enzi ya Neema hadi kwa mwanzo wa Enzi ya Ufalme, na ni ushuhuda wa wazi wa Roho Mtakatifu wa Mwana wa Adamu kwa makanisa. Pia ni utimizo wa maneno katika Ufunuo wa Yohana kwamba “Yeye aliye na sikio, na asikie yale ambayo Roho anayaambia makanisa.” Hii ni kazi ambayo Mungu alianza katika Enzi ya Ufalme. Sehemu ya pili ya kitabu hiki ni maneno ambayo yaliyonenwa binafsi na Mwana wa Adamu baada ya Yeye kujifichua kirasmi. Inajumuisha maudhui kubwa ya matamshi kadhaa tofauti na maneno kama vile unabii, ufunuo wa mafumbo, na njia ya maisha. Kuna utabiri wa siku za usoni ya ufalme, ufunuo wa mafumbo ya mpango wa usimamizi wa Mungu, uchunguzi wa asili ya mwanadamu, ushawishi na maonyo, hukumu kali, maneno ya dhati ya kuliwaza, mazungumzo ya maisha, mazungumzo ya kuingia na kadhalika. Kwa ufupi, kile Mungu Anacho na Alicho, na tabia ya Mungu yote imeonyeshwa ndani ya kazi na maneno Yake. Bila shaka, Mungu Anapopata mwili mara hii, kazi Yake ni kuonyesha tabia Yake, kimsingi kupitia kuadibu na hukumu. Akitumia haya kama msingi, Analeta ukweli zaidi kwa mwanadamu, kuonyesha njia zaidi za matendo, na hivyo Hufikia lengo Lake la kumshinda mwanadamu na kumwokoa mwanadamu kutokana na tabia yake potovu. Hili ndilo liko katika kazi ya Mungu katika Enzi ya Ufalme. Je, unatamani kuingia katika enzi mpya? Je, unatamani kujiondolea tabia yako potovu? Je, unatamani kupata ukweli wa juu? Je, unatamani kuuona uso wa kweli wa Mwana wa Adamu? Je unatamani kuishi maisha yaliyo na thamani? Je, unatamani kufanywa mkamilifu na Mungu? Basi, je, utakaribisha vipi kurudi kwa Yesu?