Utendaji (8)

Ninyi bado hamwelewi vipengele mbalimbali vya ukweli, na bado kuna makosa machache na mikengeuko katika kutenda kwenu; katika mambo mengi mnaishi kulingana na fikira na mawazo yenu, kamwe msiweze kuelewa kanuni za utendaji. Hivyo, bado ni muhimu kuwaongoza watu kuingia kwenye njia sahihi; kwa maneno mengine, ili waweze kudhibiti maisha yao ya binadamu na ya kiroho, waweke vipengele hivyo viwili katika vitendo, na ili kwamba wasihitaji kusaidiwa ama kuelekezwa mara kwa mara. Ni hapo tu ndipo watakapokuwa na kimo cha kweli. Na hata ikiwa hakuna mtu wa kukuelekeza katika siku zijazo, bado utaweza kujipatia uzoefu mwenyewe. Leo, ukielewa ni vipengele vipi vya ukweli ndivyo muhimu na ni vipi visivyo muhimu, katika siku zijazo, utaweza kuingia katika uhalisi. Leo, ninyi mnaelekezwa kwenye njia sahihi, hili likiwaruhusu muelewe ukweli mwingi, na katika siku zijazo mtaweza kuendelea kwa kina zaidi. Inaweza kusemwa kuwa kile ambacho watu wanafanywa kuelewa sasa ni njia safi kabisa. Leo, unapelekwa kwenye njia sahihi—na siku moja, wakati ambapo hakuna mtu yeyote wa kukuelekeza, utatenda na kusonga mbele kwa kina zaidi kulingana na njia hii iliyo safi zaidi kuliko zote. Leo, watu wanafanywa kuelewa ni vitendo vya aina gani ndivyo sahihi na ni vya aina gani vilivyopotoka. Baada ya kuelewa mambo haya, katika siku zijazo, uzoefu wao utakuwa wa kina zaidi. Leo, fikira, mawazo na upotovu katika kutenda kwenu vinageuzwa, na njia ya kutenda na kuingia inafunuliwa kwenu, na baada ya hapo hatua hii ya kazi itakamilika, na ninyi mtaanza kuitembea njia ambayo ninyi wanadamu mnapaswa kuitembea. Kisha, kazi Yangu itakuwa imekamilika, na kutoka wakati huo kuendelea hamtakutana na Mimi tena. Leo, kimo chenu bado ni kidogo. Kuna shida nyingi ambazo hutokana na asili na kiini cha mwanadamu, na kwa hivyo pia, kuna mambo fulani yaliyokita mizizi ambayo bado hayajafukuliwa. Hamwelewi maelezo ya ndani ya kiini na asili ya watu, na bado mnahitaji Mimi niyaonyeshe, la sivyo hamtaweza kuyatambua. Wakati fulani ambapo mambo yaliyo ndani yenu kabisa yamefunuliwa, haya ndiyo yanayojulikana kama kuadibu na hukumu. Ni wakati tu ambapo kazi Yangu imetekelezwa kabisa na kwa ukamilifu ndipo Nitakapoitamatisha. Kadiri viini vyenu potovu vinavyofunuliwa kwa kina zaidi, ndivyo mtakavyokuwa na maarifa zaidi, na hili litakuwa jambo lenye umuhimu mkubwa kwa ushuhuda na kukamilishwa kwenu kwa baadaye. Ni wakati tu ambapo kazi ya kuadibu na hukumu itakapokuwa imetekelezwa kabisa ndipo kazi Yangu itakuwa imekamilika, na nyinyi mtanijua kutokana na kuadibu na hukumu Yangu. Hamtajua tabia na haki Yangu tu, lakini la muhimu zaidi, mtajua kuadibu na hukumu Yangu. Wengi kati yenu wana mawazo makubwa juu ya upya na kiwango cha maelezo ya kazi Yangu. Bila kujali hayo, mnapaswa kuona kwamba kazi Yangu ni mpya na yenye maelezo mengi, na kwamba Ninawafundisha kutenda uso kwa uso, Nikiwashika kwa mkono. Hili tu ndilo lenye faida kwa utendaji wenu na kwa uwezo wenu wa kusimama imara katika siku zijazo; la sivyo, mngekuwa kama majani ya msimu wa kupukutika kwa majani, yaliyonyauka, ya manjano na yaliyokauka, bila hata chembe ya thamani. Mnapaswa kujua kuwa Ninajua kila kitu kilicho ndani ya mioyo na roho zenu; na mnapaswa kujua kuwa kazi Ninayofanya na maneno Ninayonena ni yenye werevu na maana iliyofichika sana. Kwa kutegemea tabia na ubora wenu wa tabia, hivi ndivyo mnavyopaswa kushughulikiwa. Ni kwa njia hii tu ndiyo maarifa yenu kuhusu kuadibu na kuhukumu Kwangu yanaonekana wazi zaidi, na hata ikiwa hujui leo, kesho utajua. Kiumbe yeyote aliyeumbwa ataanguka kati ya maneno Yangu ya kuadibu na hukumu, kwa maana Mimi sivumilii upinzani wa mtu yeyote Kwangu.

Ninyi nyote lazima muweze kuyadhibiti maisha yenu kwa busara. Unaweza kupanga kila siku kwa namna yoyote unayotaka; una uhuru kufanya chochote upendacho; unaweza kusoma maneno ya Mungu, usikilize nyimbo au mahubiri, au kuandika maelezo ya ibada; na ikiwa inakupendeza, unaweza kuandika nyimbo. Je, vyote hivi havijumuishi maisha mazuri? Hivi vyote ni vitu vinavyopaswa kuunda maisha ya mwanadamu. Watu wanapaswa kuishi kwa kawaida; ni wakati tu ambapo wamevuna matunda katika ubinadamu wao wa kawaida na katika maisha yao ya kiroho ndipo wanaweza kuzingatiwa kuwa wameingia katika maisha yanayofaa. Leo, sio tu katika ubinadamu ndiyo unakosa utambuzi na mantiki. Pia kuna maono mengi ambayo yanafaa kujulikana ambayo watu lazima wajiandae nayo, na bila kujali funzo lolote unalokabiliwa nalo, hilo ndilo funzo unalopaswa kujifunza; lazima uweze kuzoea mazingira. Kuboresha kiwango chako cha elimu lazima kufanyike kwa muda mrefu ili kuweze kuzaa matunda. Kuna vitu fulani ambavyo lazima ujiandae navyo ili uwe na maisha yanayofaa ya kibinadamu, na lazima pia uelewe kuingia kwako katika maisha. Leo, umepata kuelewa maneno mengi ya Mungu—kwa kuyasoma tena sasa—ambayo hukuelewa wakati huo, na moyo wako umeimarika zaidi. Haya pia ndiyo matokeo ambayo umepata. Katika siku yoyote ulapo na kunywa maneno ya Mungu na kuna ufahamu kiasi ndani yako, unaweza kuwasiliana kwa karibu na ndugu zako kwa uhuru. Je, haya siyo maisha unayopaswa kuishi? Wakati mwingine, maswali kadhaa huibuliwa, au unatafakari mada fulani, na inakufanya uwe bora zaidi katika kutambua, na inakupa umaizi na busara zaidi, ikikuruhusu uelewe ukweli fulani—na hiki sicho kile kilicho ndani ya maisha ya kiroho yanayozungumziwa leo? Haikubaliki kuweka tu kipengele kimoja cha maisha ya kiroho katika vitendo; kula na kunywa maneno ya Mungu, kuomba, na kuimba nyimbo vyote vinajumuisha maisha ya kiroho, na unapokuwa na maisha ya kiroho, lazima pia uwe na maisha yenye ubinadamu unaofaa. Leo, mengi ya yale yanayosemwa ni kwa ajili ya kuwapa watu mantiki na umaizi, kuwaruhusu wamiliki maisha ya ubinadamu unaofaa. Maana halisi ya kuwa na umaizi; maana halisi ya kuwa na mahusiano yanayofaa kati ya watu wawili; jinsi unavyopaswa kuingiliana na watu—unapaswa kujiandaa na vitu hivi kupitia kula na kunywa maneno ya Mungu, na kile kinachohitajika kutoka kwako kinapatikana kupitia ubinadamu wa kawaida. Jiandae na vitu ambavyo unapaswa kujiandaa navyo, na usizidi kile kinachofaa; watu wengine hutumia maneno na misamiati ya kila aina, na katika hili wanaonyesha uzuri wao. Na kuna wengine ambao husoma vitabu vya kila aina, ambapo wanaendekeza tamaa za mwili. Wao hata huchunguza na kuiga wasifu na nukuu za wale wanaodaiwa kuwa watu maarufu wa ulimwengu, na wanasoma vitabu vya ponografia—hili ni jambo la kuchekesha hata zaidi! Watu kama hawa hawajui njia ya kuingia katika maisha, sembuse kujua kazi ya Mungu leo. Hawajui hata jinsi ya kushinda kila siku. Maisha yao ni matupu hivi! Wao hawajui kabisa kile wanachopaswa kuingia katika. Kile wanachofanya ni kuzungumza na kuwasiliana na wengine, kana kwamba kuzungumza kunakuwa mbadala wa kuingia kwao wenyewe. Je, hawana aibu? Hawa ni watu wasiojua jinsi ya kuishi, na wasioelewa maisha ya binadamu; wao hushinda siku nzima wakila kupita kiasi, na kufanya vitu visivyo vya maana—kuna maana gani ya kuishi kwa namna hii? Nimeona kuwa kwa watu wengi, mbali na kufanya kazi, kula, na kuvaa, wakati wao wa thamani unatumika kwa vitu visivyo vya maana, iwe ni kufanya mzaha na kucheza, kufanya umbeya, au kulala siku nzima. Je, haya ni maisha ya mtakatifu? Je, haya ni maisha ya mtu anayefaa? Je, maisha kama haya yanaweza kukufanya uwe mkamilifu wakati ambapo ni duni, yaliyo nyuma kimaendeleo na yasiyojali? Je, uko tayari sana kujitolea kwa Shetani bure? Wakati maisha ya watu ni rahisi, na hakuna mateso katika mazingira yao, hawawezi kupata uzoefu. Katika mazingira matulivu, ni rahisi kwa watu kuharibika tabia—lakini mazingira magumu hukufanya uombe kwa dharura zaidi, na kufanya hali iwe kwamba huwezi kuthubutu kumwacha Mungu. Kadiri maisha ya watu yalivyo rahisi na yasiyo na furaha zaidi, ndivyo wanavyohisi zaidi kuwa hakuna sababu ya kuishi, na hata wanahisi kuwa ni bora wafe. Hivi ndivyo jinsi miili ya watu wapotovu ilivyo; wao hufaidika tu wakikabiliwa na majaribu.

Hatua hiyo ya kazi ya Yesu ilifanywa huko Yudea na Galilaya, na watu wasio Wayahudi hawakujua kuihusu. Kazi Aliyofanya ilikuwa ya siri sana, na hakuna mataifa mengine mbali na Israeli yaliyojua kuihusu. Ni wakati tu ambapo Yesu alimaliza kazi Yake na ikasababisha vurugu ndipo watu walijua kuihusu, na wakati huo Alikuwa ameondoka. Yesu alikuja kufanya hatua moja ya kazi, Akapata watu kiasi, na Akakamilisha hatua ya kazi. Katika hatua yoyote ya kazi ambayo Mungu hufanya, kuna wengi wanaomfuata. Kama ingetekelezwa na Mungu Mwenyewe pekee yake, haingekuwa na maana; lazima kuwe na watu wa kumfuata Mungu mpaka Atekeleze hatua hiyo ya kazi hadi mwisho kabisa. Ni wakati tu ambapo kazi ya Mungu Mwenyewe imekamilika ndipo watu huanza kutekeleza kazi iliyoagizwa na Mungu, na hapo tu ndipo kazi ya Mungu huanza kuenea. Mungu hufanya tu kazi ya kuikaribisha enzi mpya; kazi ya watu ni kuiendeleza. Kwa hivyo, kazi ya leo haitadumu kwa muda mrefu; maisha Yangu na mwanadamu hayataendelea kwa muda mrefu sana. Ninakamilisha kazi Yangu tu, na kuwaacha ninyi mtekeleze wajibu mnaopaswa kutekeleza, ili kazi hii na injili hii iweze kuenea haraka iwezekanavyo kati ya wasio Wayahudi na nchi nyingine—ni hivyo tu ndivyo mnavyoweza kutimiza wajibu wenu kama wanadamu. Wakati wa sasa ndio muhimu zaidi ya nyakati zote. Ukiupuuza, wewe ni mpumbavu; ukila na kunywa maneno haya na kupitia kazi hii katika mazingira haya, na bado unakosa azimio la kufuatilia ukweli, na hufahamu hata kidogo mzigo—siku zako za baadaye zitakuwaje? Je, mtu kama wewe hastahili kuondolewa?

Iliyotangulia: Utendaji (7)

Inayofuata: Hudumu Jinsi Waisraeli Walivyohudumu

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp