Utendaji (7)

Ubinadamu wenu umepungukiwa sana, mtindo wenu wa maisha ni duni na wa hadhi ya chini sana, hamna ubinadamu, na mumekosa umaizi. Hiyo ndiyo maana mnahitaji kujitayarisha na vitu vya ubinadamu wa kawaida. Kuwa na dhamiri, mantiki na umaizi; kujua jinsi ya kuzungumza na kuyatazama mambo; kuzingatia usafi; kutenda kama binadamu wa kawaida—hizi zote ni sifa za maarifa ya ubinadamu wa kawaida. Mnapotenda kwa njia inayofaa katika vitu hivi, basi mnachukuliwa kuwa na kiwango kinachokubalika cha ubinadamu. Lazima mjitayarishe pia kwa ajili ya maisha ya kiroho. Lazima mjue kazi yote ya Mungu duniani na myapitie maneno Yake. Unapaswa kujua jinsi ya kutii mipango Yake na jinsi ya kutimiza wajibu wa kiumbe aliyeumbwa. Hivi ndivyo vipengele viwili vya kile unachopaswa kukiingia leo—kujitayarisha kwa maisha ya ubinadamu, na kutenda kwa ajili ya maisha ya mambo ya roho. Vyote ni vya lazima.

Watu wengine ni wa upuuzi: Wanajua tu kujipa sifa za ubinadamu. Hakuna kasoro inayoweza kupatikana katika kuonekana kwao; mambo wanayoyasema na njia yao ya kuzungumza ni ya kufaa, na mavazi yao ni ya heshima na ya kufaa sana. Lakini ni watupu ndani yao; wanaonekana tu kuwa na ubinadamu wa kawaida kwa nje. Kuna wengine wanaolenga tu kile cha kula, kuvaa, na kile cha kusema. Hata kuna wale wanaolenga vitu kama kufagia sakafu, kutandika kitanda na usafi wa jumla pekee. Wanaweza kuwa wamejizoeza vizuri vitu hivi vyote, lakini unapowaomba wazungumze kuhusu maarifa yao ya kazi ya Mungu ya siku za mwisho, ama ya kuadibu na hukumu, ama majaribu na usafishaji, huenda wakaonyesha hawana uzoefu hata kidogo. Unaweza kuwauliza: “Je, una ufahamu wa kazi ya msingi ya Mungu duniani? Je, kazi ya Mungu mwenye mwili leo inatofautiana vipi na kazi ya Yesu? Inatofautiana vipi na kazi ya Yehova? Je, Wao ni Mungu mmoja? Je, Amekuja kutamatisha enzi hii, ama kuwaokoa wanadamu?” Lakini watu kama hawa hawana chochote cha kusema kuhusu masuala haya. Wengine wanajivika mapambo mazuri, lakini ya juujuu: Kina dada wanajivika mapambo mazuri kama maua, na kina ndugu wanavalia kama wana wa wafalme ama wambuji wadogo matajiri. Wanajali tu kuhusu vitu vya nje, kama vitu wanavyokula na kuvalia; ndani yao, wao ni mafukara na hawamfahamu Mungu hata kidogo. Hili lina maana gani? Na kisha kuna wengine wanaovalia kama waombaji maskini—kweli wanaonekana kama watumwa wa Asia Mashariki! Je, kweli hamwelewi Ninachotaka kutoka kwenu? Shirikini kwa karibu: Mmepata nini kweli? Mmemwamini Mungu kwa miaka hii yote, lakini mmevuna hili tu—je, hamna aibu? Je, hamwoni haya? Mmekuwa mkifuatilia kwenye njia ya kweli kwa miaka hii yote, lakini leo kimo chenu bado ni cha chini kuliko cha jurawa! Watazame mabibi wadogo walio miongoni mwenu, warembo kama picha mkiwa mmevalia mavazi na vipodozi vyenu, mkijilinganisha kati yenu—na ni nini mnacholinganisha? Starehe zenu? Matakwa yenu? Je, mnadhani kwamba Nimekuja kuandikisha waonyesha mitindo? Hamna aibu! Maisha yenu yako wapi? Je, kile mnachokifuatilia si tamaa zilizopita kiasi tu? Unadhani kuwa wewe ni mrembo sana, lakini ingawa umevalia kila aina ya umaridadi, kwa kweli wewe si buu anayegaagaa, aliyezaliwa katika rundo la kinyesi? Leo, huna bahati ya kufurahia baraka hizi za mbinguni kwa ajili ya uso wako mrembo, ila kwa sababu Mungu anafanya jambo la kipekee kwa kukuinua. Je, bado huelewi ulikotoka? Maisha yanapotajwa, unafunga mdomo wako na husemi chochote, na unakimya kama sanamu, lakini bado una ujasiri wa kuvalia vizuri! Bado unataka kupaka uso wako rangi nyekundu na poda! Na watazame wambuji walio miongoni mwenu, wanaume waliopotoka wanaoshinda siku kutwa wakitembea huku na kule polepole, wakaidi, na wenye sura tepetevu usoni pao. Je, hivi ndivyo mtu anapaswa kutenda? Je, kila mmoja kati yenu, awe mwamamume ama mwanamke, anazingatia nini siku nzima? Je, mnajua mnamtegemea nani kujilisha? Tazama mavazi yako, tazama kile ulichovuna mikononi mwako, sugua kitambi chako—umefaidika nini kutoka kwa gharama ya damu na jasho ambayo umelipa katika miaka hii yote ya imani? Bado unafikiri kwenda kutalii sehemu maarufu, bado unafikiri kupamba mwili wako unukao—ufuatiliaji usio na maana! Unaombwa uwe mtu wa kawaida, lakini sasa wewe si mtu asiye wa kawaida tu, wewe ni mpotovu. Mtu kama wewe anawezaje kuwa na ujasiri wa kuja mbele Zangu? Ukiwa na ubinadamu kama huu, ukionyesha uzuri wako na kuringa kwa ajili ya mwili wako, ukiishi daima ndani ya tamaa za mwili—je, wewe si mzao wa mashetani wachafu na pepo waovu? Sitamruhusu shetani mchafu kama huyu aendelee kuishi kwa muda mrefu! Na usifikiri kwamba Sijui kile unachofikiri moyoni mwako. Unaweza kudhibiti vikali tamaa na mwili wako, lakini Nawezaje kukosa kujua fikira zilizo moyoni mwako? Nawezaje kukosa kujua tamaa zote za macho yako? Je, ninyi mabibi wadogo hamjirembeshi sana ili kuonyesha miili yenu? Wanaume wana faida gani kwenu? Je, kweli wanaweza kuwaokoa kutoka katika bahari ya mateso? Na kwa wambuji miongoni mwenu, nyote huvalia ili kujifanya muonekane waungwana na wa heshima, lakini, je, hii si hila iliyokusudiwa kuvuta macho kwa sura zenu changamfu? Mnafanya hili kwa sababu ya nani? Wanawake wana faida gani kwenu? Je, wao si chanzo cha dhambi yenu? Enyi wanaume na wanawake, Nimewaambia maneno mengi sana, lakini mmetii machache tu. Masikio yenu hayataki kusikia, macho yenu yamefifia, na mioyo yenu ni migumu kiasi kwamba kuna tamaa tu katika miili yenu, kiasi kwamba mmetegwa nayo, msiweze kutoroka. Ni nani anayetaka kuwakaribia ninyi mabuu, ninyi mnaojifurukuta katika uchafu na masizi? Msisahau kwamba ninyi tu ni wale Niliowatoa kutoka katika rundo la kinyesi, kwamba mwanzoni hamkuwa na ubinadamu wa kawaida. Ninachotaka kutoka kwenu ni ule ubinadamu wa kawaida ambao hamkuwa nao mwanzoni, si kwamba muonyeshe tamaa zenu ama muachilie miili yenu iliyooza, ambayo imeelekezwa na ibilisi kwa miaka mingi sana. Mnapojivisha nguo hivyo, je, hamwogopi kwamba mtategwa kwa kina zaidi? Je, hamjui kwamba mwanzoni mlikuwa wenye dhambi? Je, hamjui kwamba miili yenu imejaa tamaa sana kiasi kwamba hata inavuja kutoka kwa mavazi yenu, ikifichua hali zenu kama mashetani wabaya na wachafu kukithiri? Je, si kweli kwamba mnajua hili vyema zaidi kuliko yeyote mwingine? Mioyo yenu, macho yenu, midomo yenu—je, si vyote vimenajisiwa na mashetani wachafu? Je, hizi sehemu zenu si chafu? Je, unadhani kwamba alimradi hutendi, basi wewe ndiwe mtakatifu kabisa? Je, unadhani kwamba kuvalia mavazi mazuri kunaweza kuficha nafsi zenu duni? Hilo haliwezekani! Nawashauri muwe wenye uhalisi zaidi: Msiwe wadanganyifu na bandia, na msijigambe. Mnaonyeshana tamaa zenu, lakini yote mtakayopata kama malipo ni mateso ya milele na kurudiwa kikatili! Mna haja gani ya kupepeseana macho yenu na kujiingiza katika mapenzi? Je, hiki ndicho kipimo cha uaminifu wenu, kiasi cha uadilifu wenu? Nawachukia kabisa wale miongoni mwenu wanaojihusisha katika uganga na uchawi; Nawachukia sana wale wanaume na wanawake wadogo miongoni mwenu wanaopenda miili yao wenyewe. Ni vyema mjizuie, kwa sababu sasa mnahitajika kuwa na ubinadamu wa kawaida, na hamruhusiwi kuonyesha tamaa zenu—lakini mnachukua kila fursa muwezayo, kwani miili yenu imejaa sana, na tamaa zenu ni kubwa mno!

Kwa nje, maisha yako ya ubinadamu yamepangwa vizuri sana, lakini huna cha kusema unapoambiwa uzungumzie maarifa yako ya maisha; na umepungukiwa sana katika hili. Lazima ujitayarishe na ukweli! Maisha yako ya ubinadamu yamebadilika kuwa bora, na kwa hivyo pia maisha yaliyo ndani yako lazima yabadilike; badili mawazo yako, geuza maoni yako kuhusu imani katika Mungu, badili maarifa na fikira zilizo ndani yako, na ubadili maarifa kumhusu Mungu kama yalivyo ndani ya mawazo yako. Kupitia kushughulikiwa, kupitia ufunuo na ruzuku, badili kwa utaratibu maarifa yako kujihusu, kuhusu maisha ya binadamu, na kuhusu kumwamini Mungu; ufanye ufahamu wako uweze kuwa safi. Kwa njia hii, fikira alizo nazo mwanadamu zinabadilika, jinsi anavyoyaona mambo inabadilika, na mtazamo wake wa kiakili unabadilika. Ni hili tu linaloweza kuitwa mabadiliko katika tabia ya maisha. Huombwi kuyasoma maneno ya Mungu siku nzima ama uoshe nguo na kusafisha. Maisha ya ubinadamu wa kawaida lazima angalau yavumilike kwa kawaida. Aidha, unaposhughulikia masuala ya nje, lazima bado utumie umaizi na mantiki kiasi; lakini kilicho muhimu kabisa ni kwamba ujitayarishe na ukweli wa maisha. Unapojitayarisha kwa ajili ya maisha, lazima ulenge kula na kunywa maneno ya Mungu, lazima uweze kuzungumzia maarifa ya Mungu, maoni yako ya maisha ya binadamu, na hasa, maarifa yako ya kazi iliyofanywa na Mungu wakati wa siku za mwisho. Kwa kuwa unafuatilia uzima, ni lazima ujitayarishe na vitu hivi. Unapokula na kunywa maneno ya Mungu, lazima utathmini uhalisi wa hali yako mwenyewe kulingana na vitu hivi. Yaani, unapogundua dosari zako wakati wa uzoefu wako wa kweli, lazima uweze kupata njia ya kutenda, uweze kupuuza nia na fikira zako zisizo sahihi. Ukijitahidi daima kupata vitu hivi na utake kuvitimiza kwa dhati, basi utakuwa na njia ya kufuata, hutahisi mwenye utupu, na hivyo utaweza kudumisha hali ya kawaida. Ni hapo tu ndipo utakuwa mtu anayebeba mzigo katika maisha yako mwenyewe, aliye na imani. Mbona watu wengine hawawezi kuyaweka maneno ya Mungu katika vitendo baada ya kuyasoma? Je, si kwa sababu hawawezi kuelewa vitu muhimu kabisa? Je, si kwa sababu hawayachukulii maisha kwa uzito? Sasabu ya wao kutoelewa vitu muhimu na kukosa njia ya kutenda ni kuwa wanaposoma maneno ya Mungu, hawawezi kuyahusisha na hali zao wenyewe, wala hawawezi kuwa na ujuzi wa hali zao wenyewe. Watu wengine husema: “Mimi huyasoma maneno ya Mungu na kuyahusisha na hali yangu mwenyewe, na najua kwamba mimi ni mpotovu na mwenye ubora duni wa tabia, lakini siwezi kuyaridhisha mapenzi ya Mungu.” Umeona tu mambo ya nje kabisa; kuna vitu vingi halisi ambavyo huvijui: jinsi ya kuweka kando raha za mwili, jinsi ya kuweka kando kujidai, jinsi ya kujibadili, jinsi ya kuviingia vitu hivi, jinsi ya kuboresha ubora wako wa tabia, na kuanzia kutoka kipengele kipi. Unaelewa tu mambo machache ya nje, na yote unayoyajua ni kwamba kweli umepotoka sana. Unapokutana na ndugu zako, unazungumzia jinsi ulivyopotoka, na inaonekana kwamba unajijua na unabeba mzigo mkubwa kwa ajili ya maisha yako. Kwa kweli, tabia yako potovu haijabadilika, jambo linalothibitisha kwamba hujapata njia ya kutenda. Ikiwa unaongoza kanisa, lazima uweze kuelewa hali za kina ndugu na kuzionyesha. Je, itatosha kusema tu: “Ninyi watu ni wasiotii na wenye maendeleo kidogo mno!” La, lazima uzungumze hasa kuhusu jinsi kutotii kwao na wao kuwa wenye maendeleo kidogo mno kunavyodhihirishwa. Lazima uzungumzie hali zao za kutotii, mienendo yao ya kutotii, na tabia zao za kishetani, na lazima uyazungumzie mambo haya kwa namna ambayo wanashawishika kabisa kuhusu ukweli katika maneno yako. Tumia mambo ya hakika na mifano kutoa hoja zako, na useme hasa jinsi wanavyoweza kujiondoa kwa tabia ya uasi, na uonyeshe njia ya kutenda—hivi ndivyo jinsi ya kuwashawishi watu. Ni wale tu wanaofanya hivi ndio wanaoweza kuwaongoza wengine; ni wao tu walio na uhalisi wa ukweli.

Sasa mmepewa ukweli mwingi kupitia kufanya ushirika, na lazima uutathmini. Unapaswa kuweza kufikia uamuzi kuhusu kuna ukweli ngapi kwa jumla. Punde unapojua na wewe mwenyewe unaweza kutofautisha kati ya vipengele kadhaa vya ubinadamu wa kawaida ambao mtu anapaswa kuwa nao, vipengele vikuu vya mabadiliko ya tabia ya mtu, kuzidishwa kwa maono, na njia zenye makosa za kujua na kupitia ambazo watu wametumia katika enzi zote—ni hapo tu ndipo utakuwa kwenye njia sahihi. Watu wa dini wanaiabudu Biblia kana kwamba ni Mungu; hasa wanazichukulia Injili Nne za Agano Jipya kana kwamba ni nyuso nne tofauti za Yesu na wanazungumzia Utatu wa Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Haya yote ni ya mzaha kabisa, na nyote mnapaswa kuyabaini; zaidi ya hayo, lazima muwe na maarifa ya kiini cha Mungu aliyepata mwili na kazi ya siku za mwisho. Pia kuna mbinu hizo za kale za kutenda, uongo na mikengeuko hiyo inayohusiana na utendaji—kuishi ndani ya roho, kujazwa na Roho Mtakatifu, kukubali yoyote yatakayokuja, kutii mamlaka—ambayo lazima myajue; mnapaswa kujua jinsi watu walivyotenda awali, na jinsi watu wanavyopaswa kutenda leo. Kuhusu jinsi viongozi na wafanyakazi wanapaswa kushirikiana katika makanisa; jinsi ya kuweka kando kujidai na kujionyesha kuwa bora; jinsi ndugu wanavyopaswa kuishi kwa amani; jinsi ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na watu wengine na Mungu; jinsi ya kutimiza ukawaida katika maisha ya binadamu; kile ambacho watu wanapaswa kuwa nacho katika maisha yao ya kiroho; jinsi wanavyopaswa kula na kunywa maneno ya Mungu; ni maneno yapi ya Mungu yanahusiana na maarifa, ni yapi yanayohusu maono, na ni yapi kati yao yanayohusiana na njia ya kutenda—je, haya yote hayajazungumziwa? Maneno haya yako wazi kwa wale wanaofuatilia ukweli, na hakuna mtu anayetendewa kwa upendeleo. Leo, mnapaswa kukuza uwezo wa kuishi kwa kujitegemea, si kutegemea akili ya kutegemeana. Katika siku zijazo, wakati hakuna mtu wa kuwaongoza, mtayafikiria haya maneno Yangu. Katika nyakati za taabu, wakati haiwezekani kuishi maisha ya kanisa, wakati ndugu hawawezi kukutana, wengi wao wakiishi peke yao, wakiweza tu kuwasiliana na watu katika maeneo yao mambo yakiwa mazuri, ni katika nyakati hizi ambapo kwa sababu ya kimo chenu cha sasa, hamwezi kabisa kusimama imara. Wakiwa katikati ya taabu, wengi huona vigumu kusimama imara. Ni wale tu wanaoijua njia ya maisha na wamejitayarisha na ukweli wa kutosha ndio wanaoweza kuendelea kusonga mbele na kufanikisha utakaso na mabadiliko kwa utaratibu. Kupitia taabu si jambo rahisi; ikiwa unafikiri kuwa utazipita kwa siku chache, basi hili linathibitisha jinsi fikira zako zilivyo rahisi! Unafikiri kwamba kwa kuelewa kanuni nyingi, utaweza kusimama imara, lakini hali si hivyo! Ikiwa hufahamu mambo ya maana katika maneno ya Mungu, huwezi kuelewa sifa muhimu za ukweli, na huna njia ya kutenda, basi wakati utakapofika na kitu kikufanyikie, utatumbukia katika vurugu. Hutaweza kuvumilia jaribio la Shetani, wala ujio wa usafishaji. Ikiwa hakuna ukweli ndani yako na huna maono, basi wakati ukifika, hutaweza kujizuia kuanguka. Utakata tamaa kabisa na kusema, “Ni sawa, ikiwa nitakufa liwalo liwe, ni heri niadhibiwe hadi mwisho kabisa! Iwe ni kuadhibiwa ama kurushwa katika ziwa la moto, litimike basi—nitayakabili mambo yanavyonijia!” Mambo yalikuwa hivi wakati wa watendaji huduma: Watu wengine waliamini kwamba walikuwa watendaji huduma kwa vyovyote vile, kwa hivyo hawakufuatilia maisha tena. Walivuta sigara na kunywa pombe, wakafurahisha miili yao, na kufanya kile walichotaka. Wengine walirudi tu duniani kufanya kazi. Mazingira yasiyokalika yako hivi pia; ikiwa huwezi kuyashinda, ukishindwa kujidhibiti hata kidogo, utakata tamaa kabisa. Ikiwa huwezi kushinda ushawishi wa Shetani, utatekwa nyara na Shetani kufumba kufumbua na kuletewa maangamizi tena. Hivyo basi, ni lazima leo ujitayarishe na ukweli; ni lazima uweze kuishi kwa kujitegemea; na unapoyasoma maneno ya Mungu, ni lazima uweze kutafuta njia ya kutenda. Ikiwa hakungekuwa na viongozi ama wafanyakazi wa kukunyunyizia na kukuchunga, unapaswa bado kuweza kupata njia ya kufuata, upate dosari zako mwenyewe, upate ukweli unaopaswa kujitayarisha nao na kutenda. Je, Mungu anaweza kumwandama mwanadamu kila wakati baada ya kuja duniani? Ndani ya fikira zao, watu wengine huamini: “Mungu, usipotufinyanga hadi kwa kiwango fulani, basi kazi Yako haiwezi kuchukuliwa kuwa iliyokamilika, kwa sababu Shetani anakushutumu.” Nakuambia, punde Nitakapomaliza kunena maneno Yangu, basi kazi Yangu itakuwa imekamilika kwa mafanikio. Wakati Sina mengine zaidi ya kusema, basi kazi Yangu itakuwa imekamilika. Mwisho wa kazi Yangu utakuwa thibitisho la kushindwa kwa Shetani, na kwa sababu hiyo, inaweza kusemekana kwamba imemalizwa kwa mafanikio, bila shutuma yoyote kutoka kwa Shetani. Lakini ikiwa bado hakuna mabadiliko ndani yenu wakati kazi Yangu imemalizika, basi watu kama ninyi hamwezi kuokolewa na mtaondolewa. Nitafanya tu kazi inayohitajika. Sitaendeleza kazi Yangu duniani hadi ushindwe kwa kiwango fulani, na nyote muwe na maarifa mazuri ya kila kipengele cha ukweli, na ubora wenu wa tabia uboreke na mnishuhudie kwa undani na nje. Hilo halitawezekana! Leo, kazi Nifanyayo ndani yenu inakusudiwa kuwaongoza hadi katika maisha ya ubinadamu wa kawaida; ni kazi ya kukaribisha enzi mpya na ya kuwaongoza wanadamu katika maisha ya enzi mpya. Kazi hii inatekelezwa na kukuzwa miongoni mwenu hatua kwa hatua na moja kwa moja: Nawafunza ana kwa ana; Nawaongoza moja kwa moja; Nawaambia chochote msichokielewa, Nawapa chochote msicho nacho. Inaweza kusemekana kwamba, kwenu, hii kazi yote ni kwa ajili ya ruzuku yenu ya maisha, kuwaongoza pia katika maisha ya ubinadamu wa kawaida; inakusudiwa hasa kuruzuku maisha ya kundi hili la watu wakati wa siku za mwisho. Kwangu Mimi, hii kazi yote inakusudiwa kukamilisha enzi ya kale na kukaribisha enzi mpya; kumhusu Shetani, Nilipata mwili hasa ili nimshinde. Kazi Nifanyayo miongoni mwenu sasa ni ruzuku yenu ya leo na wokovu wenu wa wakati mzuri, lakini katika miaka hii michache mifupi, Nitawaambia ukweli wote, njia nzima ya maisha, na hata kazi ya siku zijazo; hili litatosha kuwawezesha mpitie mambo kwa njia ya kawaida katika siku zijazo. Nimewaaminia maneno Yangu yote pekee. Sitoi ushawishi mwingine wowote; leo, maneno yote Ninayowazungumzia ni ushawishi Wangu kwenu, kwa sababu leo hamjapitia maneno mengi Ninenayo, na hamwelewi maana yake ya ndani. Siku moja, uzoefu wenu utatimika jinsi tu Nilivyosema leo. Maneno haya ni maono yenu ya leo, na ndiyo mtakayotegemea katika siku zijazo; ni ruzuku ya maisha leo na ushawishi wa siku zijazo, na hakuna ushawishi unaoweza kuwa bora zaidi. Hii ni kwa sababu muda Nilio nao kufanya kazi duniani si mrefu kama muda mlio nao kupitia maneno Yangu; Namaliza kazi Yangu tu, wakati ninyi mnafuatilia maisha, mchakato unaohusisha safari ndefu katika maisha. Ni baada tu ya kupitia mambo mengi ndipo mtaweza kupata njia ya maisha kikamilifu; ni hapo tu ndipo mtaweza kubaini maana ya ndani ya maneno Nizungumzayo leo. Mtakapokuwa na maneno Yangu mikononi mwenu, wakati kila mmoja wenu amepokea maagizo Yangu yote, punde Nitakapowaagizia yote Nipasayo, na wakati kazi ya maneno Yangu imemalizika, basi utekelezaji wa mapenzi ya Mungu pia utakuwa umetimizwa, bila kujali jinsi matokeo makubwa yamefanikishwa. Siyo jinsi unavyodhani, kwamba ni lazima ubadilishwe hadi kiwango fulani; Mungu hatendi kulingana na fikira zako.

Watu hawakui katika maisha yao kwa siku chache tu. Hata wakila na kunywa maneno ya Mungu kila siku, hili halitoshi. Ni lazima wapitie kipindi cha ukuaji katika maisha yao. Mchakato huu ni muhimu. Kwa sababu ya ubora wa tabia wa watu leo, wanaweza kutimiza nini? Mungu hufanya kazi kulingana na mahitaji ya watu, akitoa matakwa yanayofaa kwa kutegemea ubora wao wa kiasili wa tabia. Iwapo kazi hii ingefanywa miongoni mwa kundi la watu wa ubora wa juu wa tabia: Maneno yaliyotamkwa yangekuwa ya fahari zaidi kuliko yale yaliyotamkwa na ninyi, maono yangekuwa ya fahari zaidi, na ukweli ungekuwa wa fahari zaidi. Maneno mengine yangepasa kuwa makali zaidi, yanayoweza zaidi kuruzuku maisha ya wanadamu, yanayoweza zaidi kufichua siri. Akizungumza miongoni mwa watu kama hawa, Mungu angeruzuku kulingana na mahitaji yao. Matakwa yanayotolewa kwenu leo yanaweza kuitwa ya nguvu zaidi; kazi hii ingefanywa kwa watu wenye ubora wa juu zaidi wa tabia, basi matakwa yangekuwa makubwa zaidi bado. Kazi yote ya Mungu inafanywa kulingana na ubora wa kiasili wa tabia ya watu. Kiwango ambacho watu wamebadilishwa na kushindwa leo ni kiwango cha juu kabisa; usitumie fikira zako mwenyewe kupima jinsi hatua hii ya kazi imekuwa yenye kufaa. Mnapaswa kuelewa kile mlicho nacho kiasili, na hampaswi kujiona kuwa bora sana. Mwanzoni, hakuna kati yenu aliyefuatilia uzima, ila mlikuwa waombaji wanaozurura mitaani. Kwa Mungu kuwafinyanga hadi kiwango mnachofikiri, kuwafanya nyote mjisujudu sakafuni, mkiwa mmeshawishika kabisa, kana kwamba mmeona maono makubwa—hilo haliwezekani! Haliwezekani kwa sababu yule ambaye hajaona miujiza ya Mungu hawezi kuamini kikamilifu yote Ninayosema. Hata kama mngechunguza maneno Yangu kwa makini, bado hamngeyaamini kikamilifu; hii ndiyo asili ya mwanadamu. Wale wanaofuatilia ukweli watapitia mabadiliko kiasi, ilhali imani ya awali ambayo wale wasiofuatilia ukweli walikuwa nayo itapunguka na hata inaweza kutoweka. Ugumu mkubwa zaidi nanyi ni kwamba hamwezi kuamini kikamilifu bila kuona kutimika kwa maneno ya Mungu, na hamshawishiki bila kuona miujiza Yake. Bila kuona mambo kama haya, ni nani anayeweza kuwa mwaminifu kabisa kwa Mungu? Na kwa hivyo Nasema kwamba kile mnachokiamini si Mungu, ila miujiza. Sasa Nimezungumza waziwazi kuhusu vipengele mbalimbali vya ukweli; kila kipengele ni kamili, na kuna uhusiano wa karibu sana kati ya vipengele vyote. Umeviona, na sasa ni lazima uviweke katika vitendo. Leo Nakuonyesha njia, na katika siku zijazo, unapaswa kuiweka katika vitendo wewe mwenyewe. Maneno Nisemayo sasa yanatoa matakwa kwa watu kutegemea hali zao halisi, na Ninafanya kazi kulingana na mahitaji yao na vitu vilivyo ndani yao. Mungu wa vitendo amekuja duniani kufanya kazi ya vitendo, kufanya kazi kulingana na hali na mahitaji ya kweli ya watu. Yeye anaelewa. Mungu anapotenda, Hawalazimishi watu. Kwa mfano, ufunge ndoa au la linapaswa kutegemea uhalisi wa hali zako; umezungumziwa ukweli kwa uwazi, na Sikuzuii. Familia za watu wengine huwakandamiza ili wasiweze kumwamini Mungu ila wafunge ndoa. Kwa njia hii, ndoa inawafaidi kwa kinyume. Kwa wengine, ndoa haileti manufaa yoyote ila inawagharimu kile walichokuwa nacho awali. Hali yako mwenyewe lazima iamuliwe na mazingira yako ya kweli na azimio lako mwenyewe. Siko hapa ili Nibuni sheria na kanuni Nitakazotumia kutoa matakwa kwenu. Watu wengi kila wakati wanasema kwa sauti, “Mungu ni wa vitendo; kazi Yake inategemezwa kwa uhalisi, na kwa uhalisi wa hali zetu”—lakini unajua kile kinachoifanya hasa iwe ya kweli? Maneno yako matupu yametosha! Kazi ya Mungu ni ya kweli na imetegemezwa kwa uhalisi; haina kanuni ila ni ya bure kabisa, yote ni wazi na isiyofichwa. Maelezo mahususi ya kanuni hizi chache ni yapi? Je, unaweza kusema ni sehemu zipi za kazi ya Mungu ziko hivi? Lazima uzungumze kwa utondoti, lazima uwe na ushuhuda wa aina mbalimbali wa yale uliyoyapitia, na unapaswa kuwa dhahiri kabisa kuhusu sifa hii ya kazi ya Mungu—lazima uijue, na ni hapo tu ndipo utastahili kuzungumza maneno haya. Je, unaweza kujibu mtu akikuuliza: “Mungu mwenye mwili amefanya kazi ipi duniani katika siku za mwisho? Kwa nini unamwita Mungu wa vitendo? ‘Vitendo’ inamaanisha nini hapa? Je, unaweza kuzungumza kuhusu kazi Yake ya vitendo, kuhusu inajumuisha nini hasa? Yesu ni Mungu aliyepata mwili, na Mungu wa leo pia ni Mungu aliyepata mwili, kwa hivyo tofauti kati Yao ni ipi? Na mifanano ni ipi? Kila mmoja Wao amefanya kazi ipi?” Haya yote yanahusiana na kushuhudia! Usikanganywe kuhusu mambo haya. Kuna wengine wanaosema: “Kazi ya Mungu leo ni ya kweli. Kamwe si onyesho la miujiza na maajabu.” Je, kweli Hatendi miujiza na maajabu? Je, una hakika? Je, unajua kazi Yangu ni gani kweli? Mtu anaweza kusema kwamba Hatendi miujiza na maajabu, lakini si kazi Anayofanya na maneno Anayozungumza yote ni miujiza? Mtu anaweza kusema kwamba Hatendi miujiza na maajabu, lakini hili linategemea jinsi linavyoelezwa na linaelekezwa kwa nani. Bila kuenda kanisani, Amefichua hali za watu, na bila kufanya kazi yoyote kando na kuzungumza, Amewahimiza watu kusonga mbele—je, hii si miujiza? Kwa maneno pekee, Amewashinda watu, na watu wanafuata kwa furaha bila matarajio ama matumaini—je, huu si mwujiza pia? Anapozungumza, maneno Yake yanaibua hali fulani ya moyo ndani ya watu. Ikiwa hawahisi furaha basi wanahisi huzuni; ikiwa hawakabiliwi na usafishaji basi wanakabiliwa na kuadibiwa. Kwa maneno machache makali tu, Anawaadibu watu—je, hili si jambo la mwujiza? Je, wanadamu wanaweza kufanya kitu kama hiki? Umesoma Biblia kwa miaka hii yote, lakini hujaelewa chochote, hujapata umaizi; hukuweza kujitenga na njia hizo za imani zilizopitwa na wakati na za zamani. Huna namna ya kuielewa Biblia. Lakini Yeye anaweza kuielewa Biblia kikamilifu—je, hili si jambo la mwujiza? Ikiwa hakungekuwa na jambo lolote la mwujiza kumhusu Mungu wakati Alipokuja duniani, je, Angeweza kuwashinda? Bila kazi Yake ya ajabu na tukufu, ni nani kati yenu angeshawishika? Machoni pako, inaonekana kana kwamba mtu wa kawaida anafanya kazi na anaishi nanyi—kwa nje, Anaonekana kuwa mtu wa kawaida na wa desturi, unachoona ni sura ya kinafiki ya ubinadamu wa kawaida, lakini kwa kweli, ni uungu unaofanya kazi. Si ubinadamu wa kawaida, ila ni uungu; ni Mungu Mwenyewe anayefanya kazi, kazi Anayofanya kwa kutumia ubinadamu wa kawaida. Kwa hivyo, kazi Yake ni ya kawaida na pia ya mwujiza. Kazi Anayoifanya haiwezi kufanywa na mwanadamu, na kwa kuwa haiwezi kufanywa na watu wa kawaida, inafanywa na kiumbe wa mwujiza. Lakini ni uungu ambao ni wa mwujiza, sio ubinadamu; uungu ni tofauti na ubinadamu. Mtu anayetumiwa na Roho Mtakatifu pia ana ubinadamu wa kawaida na wa desturi, lakini hawezi kufanya kazi hii. Tofauti iko hapa. Unaweza kusema: “Mungu siye Mungu wa mwujiza; Hafanyi chochote cha mwujiza. Mungu wetu anazungumza maneno ambayo ni ya vitendo na halisi. Anakuja kanisani kufanya kazi ya kweli na ya vitendo. Kila siku, Anatuzungumzia ana kwa ana, na Anaonyesha hali zetu ana kwa ana—Mungu wetu ni wa kweli! Anaishi nasi, na kila kitu kumhusu ni cha kawaida kabisa. Hakuna chochote katika sura Yake kinachombainisha kuwa Mungu. Hata kuna nyakati ambapo Anakasirika na tunaona uadhama wa ghadhabu Yake, na wakati mwingine Anatabasamu, na tunaona mwenendo Wake wa kutabasamu. Yeye ni Mungu Mwenyewe aliye na muundo na umbo na, Aliye wa mwili na damu, ambaye ni wa kweli na halisi.” Unaposhuhudia kwa njia hii, ni ushuhuda usio kamili. Utakuwa wa manufaa gani kwa wengine? Ikiwa huwezi kushuhudia maelezo ya ndani na kiini cha kazi ya Mungu Mwenyewe, basi “ushuhuda” wako ni bure kabisa!

Kumshuhudia Mungu hasa ni suala la kuzungumza kuhusu maarifa yako ya kazi ya Mungu, kuhusu jinsi Mungu huwashinda watu, kuhusu jinsi Yeye huwaokoa watu, kuhusu jinsi Yeye huwabadili watu; ni suala la kuzungumza kuhusu jinsi Yeye huwaongoza watu kuingia katika uhalisi wa ukweli, Akiwawezesha washindwe, wakamilishwe na kuokolewa na Yeye. Kushuhudia kunamaanisha kuzungumza kuhusu kazi Yake na yote ambayo umepitia. Ni kazi Yake pekee inayoweza kumwakilisha, na ni kazi Yake pekee inayoweza kumfichua kwa umma, kwa ukamilifu Wake; kazi Yake inamshuhudia. Kazi na matamshi Yake vinamwakilisha Roho moja kwa moja; kazi Anayofanya inatekelezwa na Roho, na maneno Anayonena yanazungumzwa na Roho. Vitu hivi vinaonyeshwa tu kupitia mwili wa Mungu, lakini kwa kweli, ni maonyesho ya Roho. Kazi yote Anayofanya na maneno yote Anayozungumza yanawakilisha kiini Chake. Ikiwa Mungu hangezungumza ama kufanya kazi baada ya kujivika mwili na kuja miongoni mwa wanadamu, na kisha Awatake mjue uhalisi Wake, ukawaida Wake na kudura Yake, je, ungeweza? Je, ungeweza kujua kiini cha Roho? Je, ungeweza kujua sifa za kiasili za mwili Wake ni zipi? Ni kwa sababu tu mmepitia kila hatua ya kazi Yake ndiyo Anawataka mumshuhudie. Ikiwa hamngekuwa na uzoefu kama huu, basi Hangesisitiza kwamba mumshuhudie. Kwa hivyo, unapomshuhudia Mungu, hushuhudii tu kuhusu sura Yake ya nje ya ubinadamu wa kawaida, lakini pia kazi Anayofanya na njia Anayoongoza; unapaswa kushuhudia kuhusu jinsi ulivyoshindwa na Yeye na umekamilishwa katika vipengele vipi. Unapaswa kuwa na ushuhuda wa aina hii. Ikiwa kila uendapo unasema kwa sauti kubwa: “Mungu wetu amekuja kufanya kazi, na kazi Yake kweli ni ya vitendo! Ametupata bila matendo yasiyo ya kawaida, bila miujiza na maajabu yoyote hata kidogo!” Wengine watauliza: “Unamaanisha nini unaposema kwamba Hafanyi miujiza na maajabu? Anawezaje kuwa Amekushinda bila kufanya miujiza na maajabu?” Na unasema: “Anazungumza na bila kuonyesha miujiza ama maajabu yoyote, Ametushinda. Kazi Yake imetushinda.” Hatimaye, ikiwa huwezi kusema chochote cha maana, ikiwa huwezi kuzungumzia mambo maalum, je, huu ni ushuhuda wa kweli? Mungu mwenye mwili anapowashinda watu, ni maneno Yake ya uungu yanayofanya hivyo. Ubinadamu hauwezi kutimiza hili; silo jambo ambalo mtu yeyote anaweza kutimiza, na hata wale wenye ubora wa juu zaidi wa tabia miongoni mwa watu wa kawaida hawawezi kutimiza hili, kwani uungu Wake ni wa juu zaidi kuliko kiumbe yeyote. Hili ni jambo la ajabu kwa watu; hata hivyo Muumba ni wa juu zaidi kuliko kiumbe yeyote. Viumbe hawawezi kuwa wa juu zaidi kuliko Muumba; ungekuwa wa juu zaidi kumliko, Hangeweza kukushinda, na Anaweza tu kukushinda kwa sababu Yeye ni wa juu zaidi kukuliko. Yeye anayeweza kuwashinda wanadamu wote ndiye Muumba, na hakuna mwingine ila Yeye anayeweza kufanya kazi hii. Maneno haya ni “ushuhuda”—aina ya ushuhuda ambayo unapaswa kuwa nayo. Umepitia kuadibiwa, hukumu, usafishaji, majaribu, vipingamizi na majaribio hatua kwa hatua, na umeshindwa; umeweka kando matarajio ya mwili, nia zako binafsi, na maslahi ya ndani ya mwili. Yaani, maneno ya Mungu yameushinda moyo wako kabisa. Ingawa hujakua katika maisha yako kwa kiwango Anachotaka, unayajua mambo haya yote na unashawishika kabisa na kile Anachofanya. Kwa hivyo, hili linaweza kuitwa ushuhuda, ushuhuda ambao ni halisi na wa kweli. Kazi ambayo Mungu amekuja kufanya, kazi ya hukumu na kuadibu, inakusudiwa kumshinda mwanadamu, lakini pia Anahitimisha kazi Yake, akimaliza enzi na kutekeleza kazi ya hitimisho. Anakamilisha enzi nzima, Akiwaokoa wanadamu wote, Akiwakomboa wanadamu kutoka katika dhambi kabisa; Anawapata wanadamu Aliowaomba kikamilifu. Unapaswa kushuhudia haya yote. Umepitia kazi nyingi sana ya Mungu, umeiona kwa macho yako mwenyewe na kuipitia wewe binafsi; wakati umefika mwisho kabisa, ni lazima uweze kutenda kazi inayokupasa uifanye. Litakuwa jambo la kusikitisha kweli usipoweza! Katika siku zijazo, wakati injili inaenezwa, unapaswa kuweza kuzungumzia maarifa yako mwenyewe, ushuhudie yote uliyoyapata moyoni mwako na utumie jitihada yote. Kiumbe aliyeumbwa anapaswa kufanikisha hili. Umuhimu wa kweli wa hatua hii ya kazi ya Mungu ni upi? Athari yake ni ipi? Na ni kiwango chake kipi kinatekelezwa ndani ya mwanadamu? Watu wanapaswa kufanya nini? Unapoweza kuzungumza kwa uwazi kuhusu kazi yote ambayo Mungu mwenye mwili amefanya tangu aje duniani, basi ushuhuda wako utakuwa kamili. Unapoweza kuzungumza kwa uwazi kuhusu vitu hivi vitano: umuhimu wa kazi Yake; maudhui yake; kiini chake; tabia inayowakilisha; na kanuni zake, basi hili litathibitisha kwamba unaweza kumshuhudia Mungu, kwamba kweli una maarifa. Mahitaji yangu kwenu si ya juu sana, na yanaweza kutimizwa na wale wote wanaofuatilia kwa kweli. Ikiwa umeazimia kuwa mmoja wa mashahidi wa Mungu, ni lazima uelewe kile Mungu anachochukia sana na kile Mungu Anachopenda. Umepitia kazi Yake nyingi; kupitia kazi hii, ni lazima upate kujua tabia Yake, uelewe mapenzi Yake na mahitaji Yake kwa wanadamu, na utumie maarifa haya kumshuhudia na kutenda wajibu wako. Unaweza tu kusema: “Tunamjua Mungu. Hukumu na kuadibu Kwake havina huruma hata kidogo. Maneno Yake ni makali sana; ni ya haki na uadhama, na hayawezi kukosewa na mtu yeyote,” lakini maneno haya humkimu mwanadamu hatimaye? Yana athari gani kwa watu? Kweli unajua kwamba kazi hii ya hukumu na kuadibu ni ya manufaa zaidi kwako? Hukumu na kuadibu kwa Mungu vinafichua uasi na upotovu wako, sivyo? Vinaweza kutakasa na kuondoa vile vitu vichafu na vipotovu vilimo ndani yako, sivyo? Kusingekuwa na hukumu na kuadibu, hatima yako ingekuwa ipi? Kweli unafahamu kwamba Shetani amekupotosha kwa kiwango cha juu zaidi? Leo, mnapaswa kujitayarisha kwa vitu hivi na mvijue vyema.

Kumwamini Mungu katika nyakati za sasa siyo imani mnayoweza kudhania—kwamba inatosha kuyasoma maneno ya Mungu, kuomba, kuimba, kudansi, kufanya wajibu wenu na kuishi maisha ya ubinadamu wa kawaida. Kweli imani inaweza kuwa rahisi hivyo? Matokeo ndiyo muhimu. Si idadi ya njia uliyo nayo ya kufanya mambo; badala yake ni jinsi hasa unavyoweza kutimiza matokeo bora zaidi. Unaweza kuyashikilia maneno ya Mungu na kuyaeleza maarifa yako kiasi, lakini unapoyaweka kando, huna chochote cha kusema. Hili linaonyesha kwamba unaweza tu kuzungumzia maandishi na kanuni lakini huna maarifa ya uzoefu. Leo, hutakubalika ukikosa kuelewa kilicho muhimu—hili ni muhimu kabisa kwa kuingia katika uhalisi! Anza kujifunza hivi: Kwanza, yasome maneno ya Mungu, pata kujua vyema maneno ya kiroho yaliyo ndani yake; pata maono muhimu yaliyo ndani yake; tambua sehemu zinazohusu utendaji; viunganishe pamoja vitu hivi, moja baada ya kingine; viingie katikati ya uzoefu wako mwenyewe. Hivi ndivyo vitu muhimu unavyopaswa kuelewa. Utendaji muhimu zaidi wakati wa kula na kunywa maneno ya Mungu ni huu: Baada ya kusoma sura ya maneno ya Mungu, ni lazima uweze kutambua sehemu muhimu zinazohusu maono, na pia ni lazima uweze kutambua sehemu muhimu zinazohusu utendaji; tumia maono kama msingi, na utumie utendaji kama mwongozo wako maishani. Mmepungukiwa na haya zaidi kuliko mengine yote, na ndiyo ugumu wenu mkubwa kabisa; mioyoni mwenu, mnayazingatia kwa nadra. Kwa ujumla, ninyi nyote mpo katika hali ya uvivu, mliokosa motisha, na msiotaka kujitolea ninyi binafsi; ama mnasubiri kwa kukaa tu, na wengine hata hulalamika; hawaelewi nia na umuhimu wa kazi ya Mungu, na ni vigumu kwao kufuatilia ukweli. Watu kama hawa huchukia sana ukweli na hatimaye wataondolewa. Hakuna kati yao anayeweza kukamilishwa, na hakuna anayeweza kusalia. Ikiwa watu hawana azimio kidogo la kupingia nguvu za Shetani, basi hawawezi kuokolewa!

Sasa, iwapo ufuatiliaji wenu umekuwa wa kufaa au la linatathminiwa na kile mlicho nacho sasa. Hiki ndicho kinachotumiwa kuamua matokeo yenu; yaani, matokeo yenu yanafichuliwa katika kujitolea mlikofanya na mambo ambayo mmefanya. Matokeo yenu yatadhihirishwa na ufuatiliaji wenu, imani yenu na mambo ambayo mmefanya. Kati yenu nyote, kuna wengi ambao tayari hawawezi kuokolewa, kwani leo ndiyo siku ya kufichua matokeo ya watu, na Sitakanganyikiwa katika kazi Yangu; Sitawaongoza wale wasioweza kuokolewa kabisa katika enzi ifuatayo. Kutakuwa na wakati ambapo kazi Yangu itakuwa imekamilika. Sitafinyanga maiti hizo ambazo haziwezi kuokolewa hata kidogo; sasa ndizo siku za mwisho za wokovu wa mwanadamu, na Sitafanya kazi isiyo ya maana. Usishutumu Mbingu na dunia—mwisho wa dunia unakuja. Hauepukiki. Mambo yamefika hapa, na hakuna kitu ambacho wewe kama mwanadamu unaweza kufanya kuyasimamisha; huwezi kubadili vitu jinsi utakavyo. Jana, hukulipa gharama ya kufuatilia ukweli na hukuwa mwaminifu; leo, wakati umewadia, huwezi kuokolewa; na kesho, utaondolewa, na hakutakuwa na uhuru wa matendo kwa ajili ya wokovu wako. Hata ingawa moyo wangu ni mpole na Ninafanya kila Niwezalo kukuokoa, usipojitahidi wewe mwenyewe ama kujifikiria hata kidogo, hili linanihusu vipi? Wale wanaofikiria tu miili yao na wanaofurahia faraja, wale wanaoonekana kuamini lakini wasioamini kwa kweli; wale wanaojihusisha katika uganga na uchawi; wale ambao ni wazinzi, walio duni kabisa; wale wanaoiba sadaka za Yehova na mali Yake; wale wanaopenda hongo; wale walio na njozi za kupaa mbinguni; wale ambao ni wenye majivuno na fidhuli, wanaojitahidi tu kwa sababu ya umaarufu na utajiri wa kibinafsi; wale wanaoeneza maneno ya safihi; wale wanaomkufuru Mungu Mwenyewe; wale wanaotoa tu hukumu dhidi ya Mungu Mwenyewe na kumkashifu; wale wanaounda vikundi na kutafuta kujitegemea; wale wanaojitukuza juu ya Mungu, wale wanaume na wanawake wadogo, wa makamo na wakubwa ambao ni wapuuzi na wametegwa katika uasherati; wale wanaume na wanawake wanaofurahia umaarufu na utajiri wa kibinafsi na wanafuatilia hadhi ya kibinafsi miongoni mwa mengine; wale watu wasiotubu walionaswa katika dhambi—je, si wote hawawezi kuokolewa? Uasherati, kutenda dhambi, uganga, uchawi, matusi na maneno ya safihi yote yamejaa kwenu; na ukweli na maneno ya uzima yanakanyagwa miongoni mwenu, na lugha takatifu inachafuliwa miongoni mwenu. Ninyi Mataifa, mliojaa uchafu na uasi! Matokeo yenu ya mwisho yatakuwa yapi? Je, wale wanaopenda mwili, wanaotenda uchawi wa mwili, na waliotegwa katika dhambi ya uasherati wanawezaje kuwa na ujasiri wa kuendelea kuishi! Je, hujui kwamba watu kama ninyi ni mabuu wasioweza kuokolewa? Ni nini kinachowapa haki ya kudai hili na lile? Hadi leo, hakujakuwa na mabadiliko hata kidogo katika wale wasiopenda ukweli na wanapenda tu mwili—watu kama hawa wanawezaje kuokolewa? Wale wasiopenda njia ya uzima, wasiomtukuza Mungu ama kumshuhudia, wanaopanga njama kwa ajili ya hadhi yao wenyewe, wanaojisifu sana—je, si bado wao wako vivyo hivyo, hadi leo? Kuna thamani gani katika kuwaokoa? Iwapo unaweza kuokolewa hakutegemei ukubwa wako ama ni miaka mingapi umekuwa ukifanya kazi, sembuse sifa ambazo umeongeza. Badala yake, kunategemea iwapo ufuatiliaji wako umezaa matunda. Unapaswa kujua kwamba wale waliookolewa ni “miti” inayozaa matunda, siyo miti iliyo na majani yaliyositawi sana na maua mengi lakini ambayo hayazai matunda. Hata kama umeshinda miaka mingi ukizurura mitaani, hilo lina maana gani? Ushuhuda wako uko wapi? Uchaji wako wa Mungu ni kidogo sana kuliko upendo wako kwako mwenyewe na hamu zako zenye tamaa—je, si mtu kama huyu ni mpotovu? Anawezaje kuwa kielelezo na mfano wa wokovu? Asili yako ni isiyorekebishika, wewe ni mwasi sana, huwezi kuokolewa! Je, si watu kama hawa ni wale watakaoondolewa? Je, si wakati ambapo kazi Yangu inakamilika ni wakati wa kufika kwa siku yako ya mwisho? Nimefanya kazi nyingi sana na kuzungumza maneno mengi sana miongoni mwenu—kweli mmeyasikiliza kiasi kipi? Mmewahi kutii kiasi kipi? Kazi Yangu ikamilikapo, huo utakuwa wakati ambapo unakoma kunipinga, wakati ambapo unakoma kusimama dhidi Yangu. Nifanyapo kazi, mnanipinga bila kukoma; kamwe hamyatii maneno Yangu. Nafanya kazi Yangu na wewe unafanya “kazi” yako mwenyewe, ukitengeneza ufalme wako mdogo. Ninyi ni kundi la mbweha na mbwa tu, mnaofanya kila kitu kunipinga! Mnajaribu kila wakati kuwakumbatia wale wanaowapa upendo wao wa dhati—uchaji wenu uko wapi? Kila kitu mfanyacho ni kidanganyifu! Hamna utii wala uchaji, na kila kitu mfanyacho ni kidanganyifu na cha kukufuru! Je, watu kama hawa wanaweza kuokolewa? Wanadamu ambao ni waasherati na wakware daima hutaka kuwavutia makahaba wenye ubembe kwao kwa ajili ya raha zao wenyewe. Sitawaokoa mashetani wa kisherati kama hawa hata kidogo. Nawachukia ninyi mashetani wachafu, na ukware na ubembe wenu utawatumbukiza kuzimuni. Mna nini cha kusema kujihusu? Ninyi mashetani wachafu na pepo waovu ni wa kutia kinyaa! Mnachukiza! Watu ovyo kama ninyi mnawezaje kuokolewa? Je, wale waliotegwa katika dhambi wanaweza kuokolewa bado? Leo, ukweli huu, njia hii, na uzima huu hauwavutii; badala yake mnavutiwa na utendaji dhambi, fedha, hadhi, umaarufu na faida; mnavutiwa na raha za mwili; sura nzuri za wanaume na uzuri wa wanawake. Ni nini kinachowastahiki kuingia katika ufalme Wangu? Sura yenu hata ni ya juu zaidi kuliko ya Mungu, hadhi yenu hata ni ya juu kuliko ya Mungu sembuse fahari yenu kubwa miongoni mwa wanadamu—mmekuwa sanamu ambayo watu wanaabudu. Je, hujageuka kuwa malaika mkuu? Wakati matokeo ya watu yanafichuliwa, ambao pia ndio wakati kazi ya wokovu itakaribia kuisha, wengi kati yenu mtakuwa maiti msioweza kuokolewa na lazima muondolewe. Wakati wa kazi ya wokovu, Mimi ni mwenye huruma na mzuri kwa watu wote. Kazi inapokamilika, matokeo ya watu wa aina tofauti yatafichuliwa, na wakati huo, Sitakuwa mwenye huruma na mzuri tena, kwa kuwa matokeo ya watu yatakuwa yamefichuliwa, na kila mmoja atakuwa ameainishwa kulingana na aina yake, na hakutakuwa na haja ya kufanya kazi zaidi ya wokovu, kwa sababu enzi ya wokovu itakuwa imepita, na kwa sababu imepita, haitarudi.

Iliyotangulia: Utendaji (6)

Inayofuata: Utendaji (8)

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp