Ni kwa Kupitia Majaribu ya Kuumiza Tu Ndiyo Unaweza Kujua Kupendeza kwa Mungu

Unampenda Mungu kiasi gani wakati wa sasa? Na, je, wewe unajua kiasi gani kuhusu yote ambayo Mungu ametenda juu yako? Haya ndiyo mafunzo unayopaswa kujifunza. Mungu anapowasili duniani, yote ambayo Ametenda juu ya mwanadamu na kumruhusu mwanadamu ayaone ni ili kwamba mwanadamu ampende Yeye na amjue Yeye kweli. Kwamba mwanadamu anaweza kuteseka kwa ajili ya Mungu na ameweza kufika umbali huu, kwa upande mmoja, ni kwa sababu ya upendo wa Mungu, na kwa upande mwingine, ni kwa sababu ya wokovu wa Mungu; hata zaidi, ni kwa sababu ya hukumu na kazi ya kuadibu ambayo Mungu ameitekeleza juu ya mwanadamu. Ikiwa ninyi mko bila hukumu, kuadibu, na majaribu ya Mungu, na ikiwa Mungu hajawafanya ninyi mteseke, basi, kusema kweli ninyi hamtampenda Mungu kweli. Kadiri kazi ya Mungu juu ya mwanadamu inavyoongezeka, ndivyo mateso ya mwanadamu yanavyoongezeka, ndivyo inavyozidi kuonyesha jinsi kazi ya Mungu ilivyo na maana kubwa sana, na ndivyo moyo wa mwanadamu unavyoweza kumpenda Mungu kweli zaidi. Funzo la kumpenda Mungu linafikiwaje? Bila dhiki na usafishaji, bila majaribu yenye maumivu—na ikiwa, zaidi ya hayo, yote ambayo Mungu angempa mwanadamu yangekuwa neema, fadhili, na rehema—je, ungeweza kufikia hatua ya kumpenda Mungu kweli? Kwa upande mmoja, wakati wa majaribu ya Mungu mwanadamu huja kujua mapungufu yake na kuona kwamba yeye hana thamani, ni wa kudharauliwa, na duni, kwamba hana chochote na yeye si chochote; kwa upande mwingine, wakati wa majaribu Mungu huandaa mazingira fulani kwa ajili ya mwanadamu ili kwamba ndani ya mazingira hayo, mwanadamu aweze kupitia vyema zaidi kupendeza kwa Mungu. Ingawa maumivu ni makubwa, na wakati mwingine ni magumu sana kuyashinda—hata kufikia kiwango cha huzuni kubwa ya kufisha—baada ya kuyapitia hayo, mwanadamu huona jinsi kazi ambayo Mungu ametenda juu yake inavyopendeza, na ni juu ya msingi huu tu ndiyo huzaliwa ndani ya mwanadamu upendo wa kweli kwa Mungu. Katika wakati wa sasa mwanadamu anaona kwamba kwa neema, fadhili, na rehema za Mungu pekee, hawezi kujijua kweli, sembuse kuweza kujua dutu ya mwanadamu, na kwamba ni kupitia tu hukumu na usafishaji wa Mungu, na wakati wa mchakato wa usafishaji wenyewe, ndipo mwanadamu anaweza kujua mapungufu yake, na kujua kwamba hana chochote. Hivyo, upendo wa mwanadamu kwa Mungu umejengwa juu ya msingi wa usafishaji na hukumu ya Mungu. Ikiwa unafurahia tu neema ya Mungu, ukiwa na amani katika familia au baraka za kimaada, hili halimaanishi kwamba umempata Mungu, wala halimaanishi kwamba umefanikiwa katika imani yako katika Mungu. Mungu tayari ametekeleza hatua moja ya kazi ya neema katika mwili, na kwa kweli amempa mwanadamu baraka za kimaada, lakini mwanadamu hawezi kufanywa kuwa mtimilifu kwa neema, fadhili, na rehema pekee. Katika uzoefu wa mwanadamu, yeye huonja kiasi fulani cha upendo wa Mungu na kuona fadhili na rehema za Mungu, lakini baada ya kupitia kwa kipindi fulani, yeye huona kwamba neema ya Mungu na fadhili na rehema Zake haviwezi kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu, haviwezi kufichua kile kilicho potovu ndani ya mwanadamu, na haviwezi kumwondolea mwanadamu tabia yake potovu, wala haviwezi kuufanya upendo na imani yake kuwa timilifu. Kazi ya neema ya Mungu ilikuwa kazi ya kipindi kimoja, na mwanadamu hawezi kutegemea kufurahia neema ya Mungu ili kumjua Mungu.

Kazi ya Mungu ya kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu inafanikishwa kwa namna gani? Inafanikishwa kupitia tabia Yake ya haki. Tabia ya Mungu hasa inajumuisha haki, ghadhabu, uadhama, hukumu, na laana, na Yeye humfanya mwanadamu kuwa mtimilifu hasa kupitia hukumu Yake. Watu wengine hawaelewi, na huuliza kwa nini Mungu anaweza tu kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu kupitia hukumu na laana. Wanasema, “Ikiwa Mungu angemlaani mwanadamu, je, mwanadamu asingekufa? Ikiwa Mungu angemhukumu mwanadamu, je, mwanadamu asingetiwa hatiani? Basi angewezaje bado kufanywa kuwa mtimilifu?” Hayo ni maneno ya watu wasioijua kazi ya Mungu. Kile ambacho Mungu hulaani ni uasi wa mwanadamu, na kile Anachohukumu ni dhambi za mwanadamu. Ingawa Yeye hunena kwa ukali na bila kujali hisia za mwanadamu hata kidogo, na Yeye hufichua yote yaliyo ndani ya mwanadamu, akifichua kupitia maneno fulani makali kile kilicho cha dutu ndani ya mwanadamu, kupitia hukumu kama hiyo, Yeye humpa mwanadamu maarifa ya kina kuhusu dutu ya mwili, na hivyo mwanadamu hutii mbele za Mungu. Mwili wa mwanadamu ni wa dhambi na wa Shetani, ni wenye uasi, na ndio unaolengwa na kuadibu kwa Mungu. Hivyo, ili kumruhusu mwanadamu kujijua, maneno ya hukumu ya Mungu lazima yamjie na namna zote za usafishaji lazima zitumike; ni hapo tu ndipo kazi ya Mungu inaweza kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Kutokana na maneno yaliyonenwa na Mungu inaweza kuonekana kwamba Yeye tayari ameuhukumu mwili wa mwanadamu. Basi, je, maneno haya si maneno ya laana? Maneno yaliyonenwa na Mungu hufichua hali halisi ya mwanadamu, na kupitia ufichuzi huo yeye huhukumiwa, na anapoona kwamba hawezi kuridhisha nia za Mungu, ndani yake anahisi huzuni na majuto, anahisi kwamba ana deni kubwa sana kwa Mungu, na hawezi kufikia nia za Mungu. Kuna nyakati ambapo Roho Mtakatifu hukutia adabu kwa ndani, na adabu hii inatokana na hukumu ya Mungu; kuna nyakati ambapo Mungu hukukemea na kukuficha uso Wake, ambapo Yeye hakujali na hafanyi kazi juu yako, akikuadibu kimyakimya ili akusafishe. Kazi ya Mungu juu ya mwanadamu hasa ni ili kufunua tabia Yake ya haki. Hatimaye mwanadamu anatoa ushuhuda gani kwa ajili ya Mungu? Mwanadamu anatoa ushuhuda kwamba Mungu ndiye Mungu mwenye haki, kwamba tabia Yake ni haki, ghadhabu, kuadibu, na hukumu; mwanadamu anatoa ushuhuda kwa tabia ya haki ya Mungu. Mungu hutumia hukumu Yake kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu, Amempenda mwanadamu, na amemwokoa mwanadamu—lakini ni mambo mangapi yaliyomo ndani ya upendo Wake? Kuna hukumu, uadhama, ghadhabu, na laana. Ingawa Mungu alimlaani mwanadamu zamani, Yeye hakumtupa mwanadamu kabisa katika shimo lisilo na mwisho, bali alitumia namna hiyo kuisafisha imani ya mwanadamu; Yeye hakumweka mwanadamu katika hali ya hatari ya kufa, bali alitenda ili kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Dutu ya mwili ni ile iliyo ya Shetani—Mungu alisema jambo hilo kwa usahihi kabisa—lakini mambo halisi yanayotekelezwa na Mungu hayatimizwi kulingana na maneno Yake. Yeye hukulaani ili uweze kumpenda Yeye, na ili kwamba uweze kujua dutu ya mwili; Yeye hukuadibu ili uweze kuamshwa, ili akuruhusu kujua mapungufu yaliyo ndani yako, na kujua jinsi mwanadamu alivyo duni na asivyostahili. Hivyo, laana za Mungu, hukumu Yake, na uadhama na ghadhabu Yake—vyote ni ili kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Yote ambayo Mungu anafanya leo, na tabia ya haki Anayofunua kupitia kwenu—vyote ni ili kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Huo ndio upendo wa Mungu.

Katika dhana za kimapokeo za mwanadamu, yeye anaamini kwamba upendo wa Mungu ni neema, rehema, na huruma Yake kwa udhaifu wa mwanadamu. Ingawa mambo haya pia ni upendo wa Mungu, ni ya upande mmoja sana, na si namna ya msingi ambayo kwayo Mungu humfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Watu wengine huanza kumwamini Mungu kwa sababu ya ugonjwa. Ugonjwa huu ni neema ya Mungu kwako; bila ugonjwa huo, usingemwamini Mungu, na kama usingemwamini Mungu basi usingefika umbali huu—na hivyo hata neema hii ni upendo wa Mungu. Katika wakati wa imani katika Yesu, watu walifanya mambo mengi ambayo Mungu hakuyaona kuwa ya kumpendeza kwa sababu hawakuelewa ukweli, lakini Mungu ana rehema na fadhili, na Amewafikisha watu umbali huu na ingawa watu hawaelewi chochote, bado Mungu huwaruhusu watu wamfuate, na, zaidi ya hayo, Amewawongoza watu kufika leo. Je, huu si upendo wa Mungu? Kile kinachodhihirishwa katika tabia ya Mungu ndicho upendo wa Mungu—hili ni sahihi kabisa! Wakati ujenzi wa kanisa ulipofikia kilele chake, Mungu alifanya hatua ya kazi ya watoa huduma na akamtupa mwanadamu katika shimo lisilo na mwisho. Maneno ya wakati wa watoa huduma yote yalikuwa laana: laana za mwili wako, laana za tabia yako potovu ya kishetani, na laana za mambo yanayokuhusu ambayo hayaridhishi nia za Mungu. Kile ambacho Mungu alionyesha katika hatua hiyo ya kazi Yake kilikuwa uadhama, na punde baadaye Alitekeleza hatua ya kazi ya kuadibu, na hapo kukaja jaribu la kifo. Katika kazi kama hiyo, mwanadamu aliona ghadhabu, uadhama, hukumu, na kuadibu kwa Mungu, lakini pia aliona neema ya Mungu, fadhili Zake, na rehema Zake. Yote ambayo Mungu alifanya, na tabia Aliyoidhihirisha, vilikuwa upendo wa Mungu kwa mwanadamu, na yote ambayo Mungu alifanya yaliweza kukidhi mahitaji ya mwanadamu. Yeye alifanya hivyo ili kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu, na Yeye alimkimu mwanadamu kulingana na kimo chake. Kama Mungu asingefanya hili, mwanadamu angeendelea kutokuwa na uwezo wa kuja mbele za Mungu na asingekuwa na namna ya kujua jinsi Mungu alivyo kwa kweli. Tangu wakati ambapo mwanadamu alianza kumwamini Mungu kwa mara ya kwanza hadi leo, Mungu amemkimu mwanadamu hatua kwa hatua kulingana na kimo cha mwanadamu, ili kwamba, ndani yake, mwanadamu aje kumjua Yeye hatua kwa hatua. Ni baada tu ya kufika leo ndipo mwanadamu anatambua jinsi hukumu ya Mungu ilivyo ya ajabu. Hatua ya kazi ya watoa huduma ilikuwa tukio la kwanza la kazi ya kulaani tangu wakati wa uumbaji hadi leo. Mungu alimlaani mwanadamu atupwe katika shimo lisilo na mwisho. Mungu asingefanya hivyo, leo mwanadamu asingekuwa na maarifa ya kweli kumhusu Mungu; ilikuwa tu kupitia laana ya Mungu ndiyo mwanadamu alikumbana rasmi na tabia Yake. Mwanadamu alifichuliwa kupitia jaribu la watoa huduma. Aliona kwamba uaminifu wake ulikuwa na upungufu, kwamba kimo chake kilikuwa kidogo sana, kwamba hakuwa na uwezo wa kuridhisha nia za Mungu, na kwamba alisema tu kwa maneno kwamba lazima amridhishe Mungu nyakati zote. Ingawa Mungu alimlaani mwanadamu katika hatua ya kazi ya watoa huduma, tukiangalia nyuma sasa, hatua hiyo ya kazi ya Mungu ilikuwa ya ajabu: Ilimletea mwanadamu mgeuko mkubwa sana, na kusababisha badiliko kubwa katika tabia ya uzima wake. Kabla ya wakati wa watoa huduma, mwanadamu hakuelewa chochote kuhusu ufuatiliaji wa uzima, maana ya kumwamini Mungu, au hekima ya kazi ya Mungu, wala hakuelewa kwamba Mungu anaweza kumjaribu mwanadamu katika kazi Yake. Tangu wakati wa watoa huduma hadi leo, mwanadamu huona jinsi kazi ya Mungu ilivyo ya ajabu, akiiona kuwa isiyoweza kueleweka, na huona kwamba hawezi kufikiria kwa akili yake jinsi Mungu anavyofanya kazi. Yeye pia huona jinsi kimo chake kilivyo kidogo, na kwamba mambo mengi sana kumhusu ni ya uasi. Mungu alipomlaani mwanadamu, ilikuwa ili afikie matokeo, na Yeye hakumfanya afe. Ingawa Alimlaani mwanadamu, Alifanya hivyo kupitia maneno; hakuna kilichompata mwanadamu kwa kweli, kwa maana kile ambacho Mungu alikilaani kilikuwa uasi wa mwanadamu, na hivyo maneno ya laana Zake pia yalinenwa ili kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Iwe Mungu anamhukumu mwanadamu au anamlaani, yote mawili humfanya mwanadamu kuwa mtimilifu: Yote mawili yanafanywa ili kukifanya kuwa timilifu kile ambacho kina mchanganyiko ndani ya mwanadamu. Kupitia namna hii mwanadamu husafishwa, na kile ambacho kinakosekana ndani ya mwanadamu kinafanywa kuwa timilifu kupitia maneno na kazi Yake. Kila hatua ya kazi ya Mungu—iwe ni maneno makali, au hukumu, au kuadibu—humfanya mwanadamu kuwa mtimilifu, na inafaa kabisa. Katika enzi na vizazi vyote Mungu hajawahi kufanya kazi kama hii kamwe; leo, Yeye hufanya kazi ndani yenu na kuwafanya ninyi mthamini hekima Yake. Ingawa ninyi mmepitia mateso fulani kwa ndani, mioyo yenu daima inahisi kuwa imetulia na yenye amani; ukweli kwamba ninyi mnaweza kufurahia hatua hii ya kazi ya Mungu ni bahati yenu njema. Bila kujali kile mnachoweza kupata katika siku sijazo, mnaona kwamba kazi yote ya Mungu juu yenu leo ni upendo. Ikiwa mwanadamu hapitii hukumu na usafishaji wa Mungu, akifanya mambo kwa nje tu na kuonyesha bidii ya nje, huku tabia yake haibadiliki kamwe, je, hili linaweza kuhesabiwa kama kupatwa na Mungu? Leo, ingawa bado kuna mambo mengi ndani ya mwanadamu ambayo ni ya kiburi, tabia ya mwanadamu ni thabiti zaidi kuliko hapo awali. Mungu kukupogoa wewe kunafanywa ili kukuokoa, na ingawa unaweza kuhisi maumivu kiasi wakati huo, siku itakapofika ambapo tabia yako inabadilika, utaangalia nyuma na uone jinsi kazi ya Mungu ilivyo ya hekima, na wakati huo ndipo utaweza kuelewa kweli nia ya Mungu. Leo, kuna baadhi ya watu wanaosema kwamba wanaelewa nia ya Mungu, lakini hilo si jambo halisi. Wanasema mambo ya uwongo. Hii ni kwa sababu, katika wakati wa sasa, bado hawajafikia kutambua iwapo nia ya Mungu ni kumwokoa mwanadamu au kumlaani mwanadamu. Pengine huwezi kuliona jambo hili waziwazi sasa, lakini siku itakapofika ambapo utaona kwamba siku ambayo Mungu anapata utukufu imewadia, na utaona jinsi ilivyo na maana kumpenda Mungu—kwa kuwa kunakuwezesha kujua maisha ya binadamu, na kunawezesha mwili wako kuishi katika ulimwengu wa kumpenda Mungu, huku roho yako ikipata uhuru, maisha yako yakiwa yamejaa furaha, na wewe daima ukimkaribia Mungu na kumtazamia Yeye—ndipo utajua kweli jinsi kazi ambayo Mungu anafanya sasa ilivyo na thamani kubwa sana.

Leo, watu wengi hawana maarifa hayo. Wanaamini kwamba kuteseka hakuna thamani, na kwamba dunia inawakataa, maisha yao ya nyumbani yana matatizo, Mungu hawaoni kuwa wa kumpendeza, na matarajio yao hayana matumaini. Watu wengine hata wanataka kufa wanapoteseka kwa kiwango fulani. Huu si upendo wa kweli kwa Mungu; watu kama hao ni waoga, hawana ustahimilivu, ni wanyonge na hawana uwezo! Mungu anatamani mwanadamu ampende Yeye, lakini kadiri mwanadamu anavyompenda Yeye zaidi, ndivyo mateso ya mwanadamu yanavyokuwa makubwa zaidi, na kadiri mwanadamu anavyompenda Yeye zaidi, ndivyo majaribu ya mwanadamu yanavyokuwa makubwa zaidi. Ikiwa unampenda Yeye, basi mateso ya kila aina yatakujia—na ikiwa humpendi, basi huenda kila kitu kitakuendea vizuri na kila kitu kinachokuzunguka kitakuwa na amani. Unapompenda Mungu, daima utahisi kwamba mambo mengi yanayokuzunguka ni magumu sana kuyashinda. Na kwa sababu kimo chako ni kidogo sana, utasafishwa, na hutakuwa na uwezo wa kumridhisha Mungu—daima utahisi kwamba nia za Mungu ni za juu sana, kwamba ziko mbali na uwezo wa mwanadamu. Kwa sababu ya haya yote utasafishwa—kwa sababu kuna udhaifu mwingi ndani yako, na wewe, katika mambo mengi, huna uwezo wa kuridhisha nia za Mungu, utasafishwa kwa ndani. Hata hivyo ninyi lazima mwone waziwazi kwamba utakaso unafikiwa tu kupitia usafishaji. Hivyo, wakati wa siku hizi za mwisho ninyi lazima mtoe ushuhuda kwa ajili ya Mungu. Haijalishi mateso yenu ni makubwa kiasi gani, mnapaswa kuendelea hadi mwisho kabisa, na hata katika pumzi yenu ya mwisho, lazima muwe waaminifu kwa Mungu na mjiweke chini ya mpango wa Mungu; huku tu ndiko kumpenda Mungu kwa kweli, na huu tu ndio ushuhuda thabiti na wenye kishindo. Unaposhawishiwa na Shetani, unapaswa kusema, “Moyo wangu ni wa Mungu, na Mungu tayari amenipata. Siwezi kukuridhisha—lazima nimridhishe Mungu ipasavyo.” Kadiri unavyomridhisha Mungu zaidi, ndivyo Mungu atakavyokubariki zaidi, na ndivyo msukumo wako wa kumpenda Mungu utakavyoongezeka; utakuwa pia na imani na azimio, na utahisi kwamba maisha ya kumpenda Mungu ndiyo maisha yenye thamani na maana zaidi. Inaweza kusemwa kwamba punde tu unapompenda Mungu, hutakuwa tena na huzuni. Ingawa kuna nyakati ambapo mwili wako ni dhaifu na una matatizo mengi halisi, ikiwa katika nyakati hizi unamtegemea Mungu kwa kweli, utafarijiwa na ndani ya roho yako utahisi utulivu na kutegemezwa. Kwa namna hii, utaweza kushinda hali nyingi, na hutalalamika kuhusu Mungu kwa sababu ya mateso unayostahimili. Badala yake, utataka kuimba nyimbo za sifa, kucheza, na kuomba, kukusanyika na kushiriki, na kumfikiria Mungu, na utahisi kwamba watu, matukio, na vitu vyote vinavyokuzunguka ambavyo Mungu amevipanga vinafaa. Usipompenda Mungu, kila kitu unachokiangalia hakitakuwa kama unavyotaka na hakuna chochote kitakachopendeza machoni pako; hutapata kuachiliwa na utakandamizwa ndani ya roho yako, na daima utaweka moyoni malalamiko kumhusu Mungu, na daima utahisi kwamba mateso unayostahimili ni makubwa sana, na kwamba umetendewa isivyo haki sana. Ikiwa hufuatilii kwa ajili ya furaha, bali ili umridhishe Mungu na usishutumiwe na Shetani, basi ufuatiliaji kama huo utakupa msukumo mkubwa wa kumpenda Mungu. Unapoweza kutenda yote yaliyonenwa na Mungu, na yote unayofanya yanaweza kumridhisha Mungu, huku kunaitwa kuwa na uhalisi. Kufuatilia kumridhisha Mungu ni kutumia moyo wako umpendao Mungu kuyatia maneno Yake katika vitendo. Haijalishi ni wakati gani, daima una moyo umpendao Mungu ndani yako, hata wengine wanapoishiwa nguvu, na unamtamani Mungu kwa kina na unamfikiria kutoka katika kina cha moyo wako. Hiki ndicho kimo halisi. Ukubwa wa kimo chako unategemea jinsi moyo umpendao Mungu ulivyo mkubwa, iwapo unaweza kusimama imara unapojaribiwa, iwapo wewe ni dhaifu wakati hali fulani inapokujia, na iwapo unaweza kushikilia msimamo wako wakati ndugu na dada zako wanakukataa; kufika kwa mambo halisi kutaonyesha hasa jinsi moyo wako umpendao Mungu ulivyo. Inaweza kuonekana kutokana na kazi nyingi ya Mungu kwamba Mungu kwa kweli anampenda mwanadamu sana. Ni kwamba tu macho ya kiroho ya mwanadamu bado hayajafumbuliwa kikamilifu na hawezi kuona waziwazi kazi nyingi ya Mungu na nia Zake, wala mambo mengi ambayo ni ya kupendeza kumhusu Mungu; mwanadamu ana kiasi kidogo sana cha upendo wa kweli kwa Mungu. Umemwamini Mungu kwa wakati huu wote, na leo Mungu amefunga njia zote za kutoroka. Kusema kweli, huna budi ila kuifuata njia iliyo sahihi, na ni hukumu kali na wokovu mkuu wa Mungu ndio unaokuongoza kwenye njia hii iliyo sahihi. Ni baada tu ya kupitia dhiki na usafishaji ndipo mwanadamu anajua kwamba Mungu anapendeza. Baada ya kupitia hadi leo, inaweza kusemwa kwamba mwanadamu amekuja kujua sehemu ya kupendeza kwa Mungu, lakini hili bado halitoshi, kwa sababu mwanadamu ana upungufu mwingi sana. Mwanadamu lazima apitie kazi nyingi zaidi za ajabu za Mungu, na usafishaji mgumu zaidi ambao Mungu amepanga kwa ajili yake. Ni hapo tu ndipo tabia ya uzima ya mwanadamu inaweza kubadilishwa.

Iliyotangulia: Wale Wanaopaswa Kukamilishwa Lazima Wapitie Usafishaji

Inayofuata: Kumpenda Mungu tu Ndiko Kumwamini Mungu Kweli

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp