Sura ya 108
Ndani Yangu, wote wanaweza kupata raha na wote wanaweza kuwa huru. Wale walio nje Yangu hawawezi kupata uhuru na furaha kwa sababu Roho Wangu hayuko pamoja na watu hawa. Watu hawa wanaitwa wafu wasio na roho. Nami Nawaita wale walio ndani Yangu watu walio hai wenye roho. Wao ni Wangu, na watarudi kwenye kiti Changu cha enzi. Wale ambao hutoa huduma na wale ambao ni wa ibilisi ni wafu wasio na roho, nao wanapaswa kuangamizwa hadi wawe katika hali ya kutokuwepo. Hii ni siri ya mpango Wangu wa usimamizi, na kitu ambacho wanadamu hawawezi kuelewa kuhusu mpango Wangu wa usimamizi, lakini pia Nimeliweka jambo hili hadharani kwa kila mtu. Wale ambao si Wangu wako kinyume Changu; wale ambao ni Wangu ni wale wanaolingana nami. Bila shaka hii ni kweli, na hii ndiyo kanuni ya hukumu Yangu kwa Shetani. Kila mtu anapaswa kujua kanuni hii ili aweze kuona haki na uadilifu Wangu—wale wote wanaotoka kwa Shetani watahukumiwa na kuchomwa na kugeuzwa majivu. Hii pia ni ghadhabu Yangu, na mtu anaweza kuona tabia Yangu zaidi. Kuanzia sasa na kuendelea, tabia Yangu itatangazwa waziwazi—itafichuliwa hatua kwa hatua kwa watu wote na mataifa yote, kwa dini zote, madhehebu yote, na watu wa kazi na viwango tofauti katika jamii. Hakuna kitu kitakachofichwa. Yote yatafichuliwa. Ni kwa sababu tabia Yangu na kanuni ya utendaji Wangu ni siri zilizofichwa kabisa kwa ajili ya wanadamu ambazo ni lazima Nifanye hivi (kwa namna kwamba wazaliwa wa kwanza hawatazikosea amri Zangu za utawala, na pia ili kutumia tabia Yangu iliyofichuliwa kuwahukumu watu wote na mataifa yote). Huu ni mpango Wangu wa usimamizi, na hizi ni hatua za kazi Yangu. Hakuna mtu atakayebadilisha jambo hilo kwa kupuuza. Tayari Nimeishi kwa kudhihirisha tabia kamili ya uungu Wangu katika ubinadamu Wangu, kwa hiyo Simruhusu mtu yeyote kuukosea ubinadamu Wangu. (Kila kitu Ninachoishi kwa kudhihirisha ni tabia ya uungu—ndiyo maana Nimesema awali, Mimi ni Mungu Mwenyewe aliyeuzidi sana ubinadamu wa kawaida.) Hakika Sitamsamehe yeyote anayenikosea, nami Nitamsababisha aangamie milele! Kumbuka! Haya ndiyo Nimeamua; kwa maneno mengine, hii ni sehemu muhimu ya amri Zangu za utawala. Kila mtu anapaswa kuona hili: Mtu Niliye ni Mungu, na zaidi ya hayo, Mungu Mwenyewe. Lazima jambo hili liwe wazi sasa! Sizungumzi ovyo ovyo. Mimi husema na kuonyesha kila kitu wazi, mpaka uelewe kabisa.
Hali ni yenye wasiwasi mno; si nyumbani Mwangu tu, lakini hata zaidi nje ya nyumba Yangu, Nawasihi kwamba sharti mlishuhudie jina Langu, muishi kwa kunidhihirisha, na kunishuhudia katika hali zote. Kwa sababu hizi sasa ni nyakati za mwisho, kila kitu kiko tayari sasa na kila kitu kinabaki katika umbo lake la asili, na hakitabadilika kamwe. Wale ambao wanapaswa kutupwa watatupwa, na wale ambao wanapaswa kuhifadhiwa watahifadhiwa. Msijaribu kusimama imara kwa nguvu au kujitenga. Msiuvuruge usimamizi Wangu au kuuharibu mpango Wangu. Kwa watu, daima Ninawapenda na kuwahurumia wanadamu, lakini Kwangu, tabia Yangu inatofautishwa kulingana na hatua za kazi Yangu, kwa sababu Mimi ni Mungu wa vitendo Mwenyewe; Mimi ni Mungu wa pekee Mwenyewe! Mimi ni asiyebadilika na anayebadilika milele. Hili ni jambo ambalo hakuna anayeweza kuelewa. Ni wakati tu Nitakapowaambia na wakati Nitakapowaelezea ndipo mtakapoelewa, mtakapofahamu. Kwa wanangu, Mimi ni mwenye upendo, mwenye huruma, mwenye haki, na mwenye kufundisha nidhamu, bali si mwenye kuhukumu (kwa kusema hivyo Ninamaanisha Siwaangamizi wazaliwa wa kwanza). Kwa wale isipokuwa wana Wangu, Ninabadilika wakati wowote kwa kutegemea enzi zinavyobadilika: mwenye upendo, mwenye huruma, mwenye haki, mwadhimu, mwenye kuhukumu, mwenye hasira, mwenye kulaani, mwenye kuchoma, na hatimaye, mwenye kuiangamiza miili yao. Wale ambao wameangamizwa watatoweka pamoja na roho na nafsi zao. Lakini kwa wale ambao hutoa huduma, roho na nafsi zao pekee zitahifadhiwa (kuhusiana na jinsi ya kutia jambo hili katika vitendo hasa, Nitawaambia baadaye, ili mweze kuelewa). Hata hivyo, hawatakuwa na uhuru kamwe na hawataachiliwa huru kamwe, kwa sababu wako chini ya watu Wangu, na wako chini ya udhibiti wa watu Wangu. Sababu ambayo Niliwachukia watendaji huduma sana ni kwamba wote ni vizazi vya joka kuu jekundu, na wale ambao sio watendaji huduma pia ni vizazi vya joka kuu jekundu. Kwa maneno mengine, wale wote ambao si wazaliwa wa kwanza ni vizazi vya joka kuu jekundu. Ninaposema kwamba wale walio katika hali ya kuteseka milele hunipa sifa za milele, Ninamaanisha kwamba watatoa huduma Kwangu milele. Jambo hili ni la hakika kabisa. Watu hao watakuwa watumwa, ng'ombe, na farasi daima. Ninaweza kuwachinja wakati wowote, na Ninaweza kuwatawala Nipendavyo, kwa sababu wao ni vizazi vya joka kuu jekundu na hawana tabia Yangu. Kwa kuwa wao ni vizazi vya joka kuu jekundu, wana tabia yake, yaani, wana tabia ya wanyama. Hii ni ya kweli kabisa, na isiyobadilika milele! Hii ni kwa sababu haya yote yamejaaliwa na Mimi. Hakuna mtu anayeweza kuyabadilisha hili (Ninamaanisha, Sitamruhusu mtu yeyote kutenda kinyume na sheria hii); ukijaribu, Nitakuangusha!
Mnapaswa kuona kutoka kwa siri ambazo Mimi hufichua hatua ambayo mpango Wangu wa usimamizi na kazi Yangu vimeendelea hadi kiwango kipi, kuona kile Ninachofanya katika mikono Yangu, kuona wale ambao hukumu Zangu na ghadhabu Yangu huwafika. Hii ni haki Yangu. Kulingana na siri ambazo Nimefichua, Ninapanga kazi Yangu nami Ninausimamia mpango Wangu. Hakuna mtu anayeweza kubadilisha hili; lazima lifanyike hatua kwa hatua, kufuatana na matamanio Yangu. Siri ni njia ya utendaji wa kazi Yangu, nazo ni ishara kwa ajili ya hatua katika mpango Wangu wa usimamizi. Hakuna mtu atakayeongeza au kuondoa chochote kutoka kwa siri Zangu kwa sababu kama siri si sahihi, njia si sahihi. Kwa nini Ninafichua siri Zangu kwenu sasa? Sababu ni nini? Nani kati yenu anaweza kusema waziwazi? Na Nimesema kuwa siri ni njia, kwa hiyo njia hii inamaanisha nini? Ni mchakato ambao mnapitia kutoka katika nyama hadi mwilini, na hii ni hatua muhimu. Baada ya kufichua siri Zangu, dhana za watu zinaondolewa hatua kwa hatua na mawazo yao yanadhoofishwa hatua kwa hatua. Huu ni mchakato wa kuingia katika ulimwengu wa kiroho. Kwa hiyo Ninasema kuwa kazi Yangu hufanyika katika hatua, nayo si ya mashaka—huu ni ukweli, na hii ndiyo njia Yangu ya kufanya kazi. Hakuna mtu anayeweza kubadilisha hili na hakuna mtu anayeweza kufanya hili kwa sababu mimi ni Mungu wa pekee Mwenyewe! Kazi Yangu inakamilishwa na Mimi mwenyewe. Ulimwengu dunia mzima unadhibitiwa na Mimi peke Yangu, na kupangwa na Mimi peke Yangu. Ni nani anayethubutu kutonisikiliza? (Kwa kusema “Mimi peke Yangu” Namaanisha Mungu Mwenyewe, kwa sababu mtu Niliye ni Mungu Mwenyewe, hivyo usishikilie dhana zako mwenyewe kwa nguvu.) Ni nani anayethubutu kunipinga? Ataadhibiwa vikali! Mmeona matokeo ya joka kuu jekundu! Huo ndio mwisho wake, lakini pia ni jambo lisiloepukika. Lazima kazi ifanywe nami binafsi ili liaibishwe, haliwezi hata kuinuka, na litaangamizwa milele yote! Sasa Ninaanza kufichua siri. (Kumbuka! Siri nyingi ambazo zimefichuliwa ni mambo ambayo mara nyingi ninyi husema kwa vinywa vyenu lakini ambayo hakuna mtu anayeelewa.) Nimesema kuwa mambo yote ambayo watu wanaona kama hayajakamilika yameshakamilika machoni Pangu, na mambo ambayo Mimi naona kama ndiyo yanaanza tu huonekana yameshakamilika kwa watu. Je, hii ni kweli kinzani? Sio. Watu wanafikiri hivyo kwa sababu wana fikira na mawazo yao wenyewe. Mambo ambayo Mimi hupanga hukamilika kupitia kwa maneno Yangu (huanzishwa Ninaposema yaanzishwe na hukamilika Ninaposema yakamilike), lakini haionekani Kwangu kuwa mambo ambayo Nimesema yamekamilika. Hii ni kwa sababu kuna ukomo wa muda kwa mambo Ninayoyafanya, kwa hiyo Nayaona mambo hayo kama yasiyokamilika, lakini katika macho ya kimwili ya watu (kwa sababu ya tofauti katika dhana ya wakati) yameshakamilika. Sasa watu wengi wananitilia shaka kwa sababu ya siri Zangu zilizofichuliwa. Kwa sababu ya mwanzo wa ukweli, kwa sababu nia Zangu hazilingani na fikira za watu, wao ni wenye upinzani kunielekea nao hunikataa. Huyu ni Shetani akijinasa mtegoni katika hila zake mwenyewe. (Wanataka kupokea baraka, lakini hawakufikiri kwamba Mungu hangekubaliana na fikira zao wenyewe kwa kiwango hiki, kwa hivyo wanakimbia.) Hii pia ni athari ya kazi Yangu. Watu wote wanapaswa kunisifu, washangilie kwa ajili Yangu, na wanipe utukufu. Bila shaka kila kitu kiko mikononi Mwangu na kila kitu kiko ndani ya hukumu Yangu. Watu wote wanapotiririka mlimani Kwangu, wazaliwa wa kwanza wanaporudi wakiwa washindi, huo ndio mwisho kwa mpango Wangu wa usimamizi. Ni wakati wa kukamilika kwa miaka Yangu elfu sita ya mpango wa usimamizi. Mimi binafsi Nimepanga yote. Nimeshasema hili mara nyingi. Kwa kuwa bado mnaishi ndani ya mawazo yenu Ninasisitiza hili tena na tena, ili msifanye makosa hapa na kuuharibu mpango Wangu. Watu hawawezi kunisaidia wala hawawezi kushiriki katika usimamizi Wangu, kwa sababu sasa bado ninyi ni wa mwili na damu (ingawa ninyi ni Wangu, bado mnaishi katika mwili). Kwa hiyo Nasema, wale walio wa mwili na damu hawawezi kupokea urithi Wangu. Hii pia ndiyo sababu kuu ya kuwafanya mwingie katika ulimwengu wa kiroho.
Duniani, mitetemeko ya ardhi ni mwanzo wa maafa. Kwanza, Ninaufanya ulimwengu, yaani dunia, ubadilike. Hiyo inafuatwa na mapigo na njaa. Huu ni mpango Wangu, hizi ni hatua Zangu, nami Nitakihamasisha kila kitu kunitumikia, ili kuukamilisha mpango Wangu wa usimamizi. Kwa hiyo ulimwengu dunia wote utaangamizwa, hata bila Mimi kuingilia moja kwa moja. Nilipopata mwili mara ya kwanza na kusulubishwa msalabani, dunia ilitetemeka kwa nguvu sana; itakuwa vivyo hivyo mwishowe. Mitetemeko ya ardhi itaanza wakati huo huo Nitakapoingia katika ulimwengu wa kiroho kutoka katika mwili. Kwa hiyo Nasema, bila shaka wazaliwa wa kwanza hawatapitia maafa. Watu ambao si wazaliwa wa kwanza wataachwa katika maafa na kuteseka. Kwa hiyo, kwa wanadamu, kila mtu yuko tayari kuwa mzaliwa wa kwanza. Katika jakamoyo za watu si kwa ajili ya kufurahia baraka, bali kwa ajili ya kuepuka kupitia maafa. Hii ni hila ya joka kuu jekundu. Lakini Sitaliruhusu litoroke kamwe. Nitalisababisha lipitie adhabu Yangu kali na bado lisimame na kunitolea huduma (hii inamaanisha kuwafanya wana Wangu na watu Wangu kuwa kamili), Niliache lilaghaiwe daima na njama zake lenyewe, likubali hukumu Yangu milele, na likubali uunguzaji Wangu milele. Hii ndiyo maana ya kweli ya kuwafanya watendaji huduma wanisifu (kuwatumia kufichua uwezo Wangu mkubwa). Sitaliruhusu joka kuu jekundu liingie kisirisiri ndani ya ufalme Wangu, na Sitalipa joka kuu jekundu haki ya kunisifu! (Kwa sababu halistahili, halistahili kamwe!) Nitalisababisha tu kutoa huduma Kwangu hadi milele! Nitalisababisha tu linisujudie. (Wale wanaoangamizwa ni bora zaidi kuliko wale walio katika hali ya kuteseka milele. Maangamizi ni adhabu kali ya muda mfupi tu, lakini wale walio katika hali ya kuteseka milele watapitia adhabu kali milele, kwa hiyo Mimi hutumia “kusujudu.” Kwa sababu watu hawa huingia nyumbani Mwangu kisirisiri na kufurahia neema Yangu nyingi nao wana ufahamu fulani kunihusu, Mimi hutumia adhabu kali. Kwa wale walio nje ya nyumba Yangu, unaweza kusema kuwa wasiojua hawatateseka.) Katika fikira za watu, wanadhani kuwa wale ambao wanaangamizwa ni wabaya zaidi kuliko wale ambao wako katika mateso ya milele, lakini badala yake, wale walio katika hali ya kuteseka milele wanapaswa kuhukumiwa kwa ukali milele, na wale wanaoangamizwa watarudia hali ya kutokuwepo milele.