6. Maana ya Mateso na ni Mateso ya Aina Gani Ambayo Waumini wa Mungu Lazima Wastahimili
Maneno Husika ya Mungu:
Leo, watu wengi sana hawana ufahamu huo. Wao huamini kwamba mateso hayana thamani, wao hukanwa na ulimwengu, maisha yao ya nyumbani yamesumbuliwa, wao si wapendwa wa Mungu, na matazamio yao ni matupu. Kuteseka kwa watu wengine hufikia kiwango fulani, na fikira zao hugeukia kifo. Huu si upendo wa kweli kwa Mungu; watu kama hao ni waoga, hawana ustahamilivu, wao ni wadhaifu na wasio na nguvu! Mungu ana hamu ya mwanadamu kumpenda Yeye, lakini kadri mwanadamu anavyompenda Yeye, ndivyo kuteseka kwa mwanadamu huwa kwingi zaidi, na kadri mwanadamu anavyompenda Yeye, ndivyo majaribio ya mwanadamu huwa makubwa zaidi. Ikiwa unampenda Yeye, basi kila aina ya mateso yatakufika—na ikiwa humpendi, basi labda kila kitu kitaendelea kwa urahisi kwako, na kila kitu kinachokuzunguka kitakuwa kitulivu kwako. Unapompenda Mungu, utahisi kwamba mengi kandokando yako hayawezi kushindikana, na kwa sababu kimo chako ni kidogo sana utasafishwa; aidha, huwezi kumridhisha Mungu, na daima utahisi kwamba mapenzi ya Mungu ni ya juu sana, kwamba hayawezi kufikiwa na mwanadamu. Kwa sababu ya haya yote utasafishwa—kwa sababu kuna udhaifu mwingi ndani yako, na mengi yasiyoweza kuridhisha mapenzi ya Mungu, utasafishwa ndani. Lakini lazima muone kwa dhahiri kwamba utakaso hutimizwa tu kupitia usafishaji. Hivyo, katika siku hizi za mwisho lazima muwe na ushuhuda kwa Mungu. Haijalishi mateso yenu ni makubwa vipi, mnapaswa kuendelea hadi mwisho kabisa, na hata wakati wa pumzi yenu ya mwisho, bado lazima muwe waaminifu kwa Mungu, na kudhibitiwa na Mungu; huku pekee ndiko kumpenda Mungu kweli, na huu pekee ndio ushuhuda thabiti na mkubwa sana.
Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Ni kwa Kupitia tu Majaribio ya Kuumiza Ndiyo Mnaweza Kujua Kupendeza kwa Mungu
Usivunjike moyo, usiwe dhaifu, Nitakufichulia. Njia ya kwenda kwa ufalme sio laini hivyo, hakuna kitu kilicho rahisi hivyo! Unataka baraka zije kwa urahisi rahisi, sivyo? Leo kila mtu atakuwa na majaribio machungu ya kukumbana nayo, vinginevyo moyo wa upendo ulio nao Kwangu hautakuwa wenye nguvu zaidi na hutakuwa na upendo wa kweli Kwangu. Hata kama majaribu haya yanajumuisha hali ndogo tu, kila mtu lazima ayapitie; ni kwamba tu ugumu wa majaribu utakuwa tofauti kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Majaribu ni Baraka kutoka Kwangu, na ni wangapi kati yenu ambao huja mbele Yangu na kupiga magoti mkiomba baraka Zangu? Watoto wapumbavu! Wewe daima huhisi kwamba maneno machache ya bahati huhesabika kama baraka Yangu, lakini huhisi kuwa uchungu ni moja ya baraka Zangu. Wale wanaoshiriki katika uchungu Wangu bila shaka watashiriki utamu Wangu. Hiyo ni ahadi Yangu na baraka Zangu kwenu.
Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Matamko ya Kristo Mwanzoni, Sura ya 41
Wakati Mungu anafanya kazi ili kumsafisha mwanadamu, mwanadamu huteseka. Kadiri usafishaji wa mtu ulivyo mkubwa, ndivyo upendo wake kwa Mungu utakavyokuwa mkubwa zaidi na ndivyo nguvu za Mungu zitakavyofichuliwa zaidi kwake. Kinyume chake, kadiri mtu apokeavyo usafishaji mdogo zaidi, ndivyo upendo wake kwa Mungu utakavyokuwa kwa kiwango kidogo zaidi, na ndivyo nguvu za Mungu zitakavyofichuliwa kwake kwa kiwango kidogo zaidi. Kadiri usafishaji na uchungu wa mtu kama huyo ulivyo mkubwa na kadiri anavyopitia mateso mengi zaidi, ndivyo upendo wake kwa Mungu utakavyokuwa, ndivyo imani yake kwa Mungu itakavyokuwa ya kweli zaidi, na ndivyo maarifa yake ya Mungu yatakavyokuwa ya kina zaidi. Katika matukio unayopitia, utawaona watu wanaoteseka sana wanapokuwa wakisafishwa, wanaoshughulikiwa na kufundishwa nidhamu sana, na utaona kwamba ni watu hao ndio walio na upendo mkubwa kwa Mungu na maarifa ya kina na elekevu ya Mungu. Wale ambao hawajapitia kushughulikiwa wanayo maarifa ya juu juu tu, na wao wanaweza tu kusema: “Mungu ni mzuri sana, Yeye huwapa watu neema ili waweze kumfurahia Yeye.” Kama watu wamepitia kushughulikiwa na kufundishwa nidhamu, basi hao wanaweza kuzungumza kuhusu maarifa ya kweli ya Mungu. Hivyo kazi ya Mungu katika mwanadamu ilivyo ya ajabu zaidi, ndivyo ilivyo ya thamani zaidi na ni muhimu zaidi. Kadiri inavyokosa kupenyeza kwako zaidi na kadiri isivyolingana na mawazo yako, ndivyo kazi ya Mungu inavyoweza kukushinda, kukupata, na kukufanya mkamilifu. Umuhimu wa kazi ya Mungu ni mkubwa ulioje! Kama Mungu hangemsafisha mwanadamu kwa njia hii, kama Hangefanya kazi kulingana na njia hii, basi kazi Yake haingekuwa na ufanisi na ingekuwa isiyo na maana. Ilisemwa hapo awali kwamba Mungu angelichagua na kulipata kundi hili na kuwakamilisha katika siku za mwisho; hili lina umuhimu mkubwa sana. Kadiri kazi Anayofanya ndani yenu ilivyo kuu, ndivyo upendo wenu kwa Mungu ulivyo mkubwa na safi. Kadiri kazi ya Mungu ilivyo kuu zaidi, ndivyo mwanadamu anavyoweza kuelewa kitu kuhusu hekima Yake na ndivyo maarifa ya mwanadamu Kwake yalivyo ya kina zaidi.
Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Wale Wanaopaswa Kukamilishwa Lazima Wapitie Usafishaji
Lazima uvumilie mateso kwa ajili ya ukweli, lazima ujitoe kwa ajili ya ukweli, lazima uvumilie udhalilishaji kwa ajili ya ukweli, na kupata ukweli zaidi lazima upate mateso zaidi. Hili ndilo unalopaswa kufanya. Msitupilie mbali ukweli kwa ajili ya maisha ya amani ya familia, na lazima msiipoteze heshima na uadilifu wa maisha kwa ajili ya starehe ya muda mfupi. Unapaswa kufuata yote ambayo ni ya kupendeza na mema, na unapaswa kufuatilia njia katika maisha ambayo ni ya maana zaidi. Kama wewe unaishi maisha ya kishenzi, na wala hufuati malengo yoyote, je, si huko ni kupoteza maisha Yako? Ni nini unachoweza kupata kutoka kwa maisha ya aina hii? Unapaswa kuziacha starehe zote za mwili kwa ajili ya ukweli mmoja, na hupaswi kutupilia mbali ukweli wote kwa ajili ya starehe ya muda mfupi. Watu kama hawa hawana uadilifu au heshima; hakuna maana ya kuwepo kwao!
Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Matukio Aliyopitia Petro: Ufahamu Wake wa Adabu na Hukumu
Wakati ambapo tunapokea hukumu ya maneno ya Mungu, hatupaswi kuogopa mateso, wala hatupaswi kuogopa maumivu; sembuse kuogopa kwamba maneno ya Mungu yataumiza mioyo yetu. Tunapaswa kusoma matamshi Yake zaidi kuhusu jinsi Anavyotuhukumu na kutuadibu na kufichua asili zetu potovu. Lazima tuyasome na kuyafuata na kujilinganisha kwayo mara kwa mara. Usiwalinganishe wengine nayo—tujilinganishe wenyewe dhidi yake maneno hayo. Hatuna upungufu wowote katika vitu hivi vyote; sote tunaweza kulingana nao. Kama huamini hili, nenda ulipitie mwenyewe. … Kwanza lazima tujue kuwa haijalishi ikiwa maneno yoyote Yake yanavutia kuyasikia, ikiwa yanatufanya tuhisi uchungu au utamu—lazima tuyakubali yote. Tunapaswa kuwa na mtazamo huu juu ya maneno ya Mungu. Mtazamo huu ni wa aina gani? Je, ni mtazamo wa kumcha Mungu? Wa uvumilivu? Au, ni mtazamo wa kuteseka? Nitawaambia, si wowote kati ya hii. Katika imani yetu, lazima tusisitize kwa uthabiti kwamba maneno ya Mungu ndiyo ukweli. Kwa kuwa kweli ndiyo ukweli, tunapaswa kuyakubali kwa busara. Bila kujali ikiwa tunaweza kutambua au kukubali au la, mtazamo wetu wa kwanza kuelekea maneno ya Mungu unapaswa kuwa ule wa kukubali kabisa.
Kimetoholewa kutoka katika “Umuhimu wa Kufuatilia Ukweli na Njia ya Kuufuatilia” katika Kumbukumbu za Hotuba za Kristo
Kumpenda Mungu kunahitaji utafutaji wa mapenzi ya Mungu katika mambo yote, na kwamba ujisaili wewe mwenyewe kwa kina jambo lolote likikutokea, kujaribu kujua mapenzi ya Mungu na kujaribu kuona mapenzi ya Mungu ni yapi katika suala hili, Anataka ufanikishe nini, na ni jinsi gani utayajali mapenzi Yake? Kwa mfano: jambo fulani linafanyika linalokutaka uvumilie hali ngumu, wakati huo unapaswa ufahamu ni nini mapenzi ya Mungu, na ni jinsi gani unapaswa kuyajali mapenzi ya Mungu. Usijiridhishe mwenyewe: Jiweke kando kwanza. Hakuna kitu kilicho duni kuliko mwili. Ni lazima udhamirie kumridhisha Mungu, na ni lazima utekeleze wajibu wako. Katika mawazo kama hayo, Mungu atakupa nuru ya kipekee katika jambo hili, na moyo wako pia utapata faraja. Jambo lolote likikutendekea, liwe dogo au kubwa, ni sharti kwanza ujiweke pembeni na kuuona mwili kama kitu duni zaidi kuliko vitu vyote. Kadiri unavyouridhisha mwili zaidi, ndivyo unavyochukua uhuru zaidi; ukiuridhisha mara hii, wakati mwingine utataka zaidi. Hili linapoendelea, watu wanapata kuupenda mwili hata zaidi. Mwili mara zote una tamaa kupita kiasi, mara zote mwili unakutaka uuridhishe, na kwamba uutosheleze kwa ndani, iwe ni katika chakula unachokula, unachokivaa, au kuwa na hasira katika matendo yako, au kuushawishi udhaifu na uzembe wako… Kadiri unavyouridhisha mwili zaidi, ndivyo tamaa yake inaongezeka, na jinsi mwili unavyopotoka zaidi, hadi kufikia kiwango ambacho miili ya watu inahodhi dhana nzito, na kutomtii Mungu, na kujiinua, na kuanza kuishuku kazi ya Mungu. … Hivyo unafaa kuuasi mwili na usiutosheleze: “Mume wangu(mke), watoto, matarajio, ndoa, familia—hakuna hata moja kati ya haya ambalo ni la thamani! Moyoni mwangu mna Mungu pekee na nitajaribu kumridhisha Mungu kadiri ya uwezo wangu, na si kuuridhisha mwili.” Lazima uwe na azimio hili. Daima ukiwa na azimio hili, basi ukiuweka ukweli katika vitendo, na kujiweka kando, utaweza kufanya hivyo kwa juhudi kidogo.
Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Kumpenda Mungu tu Ndiko Kumwamini Mungu Kweli
Iwapo utapata uzima mbele za Mungu, na namna hatima yako itakavyokuwa, inategemea uasi wako dhidi ya mwili utakuwa wa namna gani. Mungu amekuokoa, na kukuteua na kukuamulia kabla, bado ikiwa leo hauko radhi kumridhisha, hauko radhi kuuweka ukweli katika vitendo, hauko radhi kuuasi mwili wako kwa moyo umpendao Mungu kwa dhati, hatimaye utajiangamiza mwenyewe, na kwa hivyo utapitia mateso mengi. Ikiwa mara zote unautosheleza mwili, Shetani atakumeza hatua kwa hatua, na kukuacha bila uzima, au upako wa Roho, hadi siku itafika ambayo ndani utakuwa giza. Ukiishi katika giza, utakuwa umetekwa nyara na Shetani, hutakuwa na Mungu tena moyoni mwako, na wakati ule utaukataa uwepo wa Mungu na kumwacha. Kwa hivyo, ikiwa watu wanataka kumpenda Mungu, ni lazima walipe gharama ya uchungu na kupitia shida. Hakuna haja ya hamasa za nje na shida, kusoma zaidi na kuzungukazunguka zaidi; badala yake, wanafaa kuweka kando vitu vilivyomo ndani yao: mawazo kupita kiasi, maslahi ya kibinafsi, na masuala yao binafsi, fikira, na nia. Hayo ndiyo mapenzi ya Mungu.
Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Kumpenda Mungu tu Ndiko Kumwamini Mungu Kweli
Mungu anawataka watu kuweka ukweli katika matendo kimsingi kushughulikia mambo yaliyo ndani yao, kushughulikiwa fikira zao, na dhana zao ambazo haziufuati moyo wa Mungu. Roho Mtakatifu huwagusa watu ndani ya mioyo yao, na kuwapa nuru na mwangaza. Kwa hivyo katika tukio lolote katika vita: Kila wakati watu wanapoweka ukweli katika vitendo, au kuweka mapenzi ya Mungu katika vitendo, huwa kuna vita vikali, na japokuwa mambo yanaweza kuonekana shwari katika miili yao, ila ndani ya mioyo yao kutakuwa na vita vya kufa na kupona—na ni baada tu ya hivi vita vikali, baada ya kutafakari kwa kina, ndipo ushindi au kushindwa kunaweza kuamuliwa. Mtu anashindwa kujua ama acheke au alie. Kwa sababu motisha nyingi ndani ya watu zina makosa, ama kwa sababu kazi kubwa ya Mungu inakinzana na dhana zao, watu wakiuweka ukweli katika vitendo vita vikali huzuka kisirisiri. Baada ya kuuweka huu ukweli katika vitendo, kisirisiri watu watakuwa wamemwaga machozi mengi sana ya huzuni kabla ya kuamua kumridhisha Mungu. Ni kwa sababu ya vita hivi watu huvumilia shida na usafishaji; huku ni kuteseka kwa kweli. Vita vikikukabili, kama unaweza kusimama kweli upande wa Mungu, utaweza kumridhisha Mungu. Katika harakati ya kutenda ukweli, hakuepukiki kwamba mtu atateseka kwa ndani; ikiwa, wanapoweka ukweli katika vitendo, kila kitu ndani yao kingekuwa sawa, basi wasingehitaji kufanywa wakamilifu na Mungu, na kusingekuwa na vita, na hawangeteseka. Ni kwa sababu kuna mambo mengi ndani ya watu ndipo hawafai kutumiwa na Mungu, na tabia nyingi za uasi wa mwili, ndipo watu wanapaswa kujifunza funzo la kuasi dhidi ya mwili kwa kina zaidi. Huku ndiko Mungu anaita kuteseka ambako Alimtaka mwanadamu kushiriki Naye.
Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Kumpenda Mungu tu Ndiko Kumwamini Mungu Kweli
Katika imani yao kwa Mungu, kile ambacho watu hutafuta ni kupata baraka kwa ajili ya siku zijazo; hili ndilo lengo lao katika imani yao. Watu wote wana kusudi na tumaini hili, lakini upotovu ulio katika asili yao lazima uondolewe kupitia majaribu. Katika hali ambazo bado hujatakaswa, hizi ndizo hali ambamo lazima usafishwe—huu ni mpango wa Mungu. Mungu anakutengenezea mazingira, Akikulazimisha usafishwe hapo ili uweze kujua upotovu wako mwenyewe. Hatimaye, unafika hatua ambapo unaona heri kufa na kuziacha njama na tamaa zako, na kutii mamlaka na mipango ya Mungu. Kwa hiyo, ikiwa watu hawana miaka kadhaa ya usafishaji, wasipovumilia kiwango fulani cha mateso, hataweza kujiondolea vifungo vya upotovu wa mwili katika mawazo na mioyo yake. Katika hali zozote zile ambazo bado ungali mtumwa wa Shetani, na katika hali zozote zile ambazo bado ungali na tamaa zako mwenyewe na matakwa yako mwenyewe, hizi ndizo hali ambamo unapaswa kuteseka. Ni kupitia mateso tu ndiyo mafunzo yanaweza kupatikana, kuweza kupata ukweli, na kuelewa mapenzi ya Mungu. Kwa kweli, ukweli mwingi unafahamika kwa kupitia majaribu makali. Hakuna anayeweza kufahamu mapenzi ya Mungu, kutambua uweza na busara ya Mungu, wala kuiona tabia ya haki ya Mungu anapokuwa katika mazingira ya utulivu na rahisi au wakati hali ni nzuri. Hilo halingewezekana!
Kimetoholewa kutoka katika “Jinsi Mtu Anapaswa Kumridhisha Mungu Katikati ya Majaribu” katika Kumbukumbu za Hotuba za Kristo
Mungu hufanya kazi ndani ya kila mtu, na bila kujali mbinu Yake ni ipi, ni watu, vitu au masuala ya aina gani ambayo Yeye hutumia kufanya huduma, au maneno Yake yana sauti ya aina gani, Ana lengo moja tu la mwisho: kukuokoa. Kabla ya kukuokoa, Anahitaji kukubadili, hivyo utakosaje kuteseka kidogo? Ni lazima upate kuteseka. Kuteseka huku kunaweza kuhusisha mambo mengi. Wakati mwingine Mungu huwainua watu, mambo, na vitu ambavyo viko karibu nawe ili kwamba uweze kujitambua, vinginevyo unaweza kushughulikiwa moja kwa moja, kukupogolewa, na kufunuliwa. Kama vile tu mtu aliye juu ya meza ya upasuaji–lazima upitie maumivu kiasi kwa ajili ya matokeo mazuri. Kama kila wakati Mungu anapokupogoa na kukushughulikia na kila wakati Anaibua watu, mambo, na vitu, hilo huchochea hisia zako na kukuongezea nguvu, basi kupitia hayo kwa njia hii ni sahihi, na utakuwa na kimo na utaingia katika uhalisi wa ukweli. Ikiwa, kila wakati unapopogolewa na kushughulikiwa, na kila wakati Mungu anapoinua mazingira yako, wewe huhisi maumivu au usumbufu wowote, na huhisi chochote kabisa, na kama huji mbele za Mungu kuelewa mapenzi Yake, wala huombi au kutafuta ukweli, basi wewe kweli ni mtu asiyejali kabisa! Watu ambao hawajali kabisa kamwe si hawatambui kiroho; kwa hiyo, Mungu hana njia ya kufanya kazi kwao. Mungu atasema: “Mtu huyu hajali kabisa na amepotoshwa sana. Nimemfanyia mambo mengi, nimetia bidii nyingi, lakini bado Siwezi kuuita moyo wake na Siwezi kuamsha roho yake. Jambo hili ni sumbufu na gumu sana.” Mungu akipanga mazingira, watu, vitu, na mambo fulani kwa ajili yako, Akikupogoa na kukushughulikia na ukijifunza kutokana na hili, ikiwa umejifunza kuja mbele za Mungu kutafuta ukweli, na, bila kujua, umetiwa nuru na kuangaziwa na kupata ukweli, ikiwa umepitia mabadiliko katika mazingira haya, umepata thawabu, na kupiga hatua, ukianza kuwa na ufahamu mdogo kuhusu mapenzi ya Mungu na kuacha kulalamika, basi yote haya yatamaanisha kuwa umesimama imara katikati ya majaribio ya mazingira haya, na umestahimili jaribio. Kwa hiyo, utakuwa umeshinda majaribu haya.
Kimetoholewa kutoka katika “Ili Kupata Ukweli, Lazima Ujifunze Kutoka kwa Watu, Mambo, na Vitu Vinavyokuzunguka” katika Kumbukumbu za Hotuba za Kristo