Katika Imani Yako katika Mungu Unapaswa Kumtii Mungu

Ni kwa nini hasa unamwamini Mungu? Watu wengi bado wamekanganyika inapokuja kwa swali hili, na daima wao huwa na mitazamo miwili tofauti kabisa kuhusu Mungu wa vitendo na Mungu aliye mbinguni. Inaonyesha kwamba watu wanamwamini Mungu sio kwa ajili ya kumtii, bali ili wapokee manufaa fulani, au ili waepuke mateso ambayo maafa yanaleta; hapo tu ndipo wanakuwa watiifu kwa kiasi fulani. Utiifu wa aina hii una masharti—matarajio yao binafsi ndiyo sharti la mwanzo la utiifu wao; wanatii kwa sababu hawana chaguo lingine. Kwa hiyo, ni kwa nini wewe unamwamini Mungu hasa? Ikiwa ni kwa ajili tu ya matarajio yako na hatima yako, basi ingelikuwa bora usimwamini. Imani ya namna hii ni kujidanganya, kujipa moyo, na kujisifu mwenyewe. Ikiwa imani yako haijajengwa juu ya msingi wa kumtii Mungu, basi mwishowe utapata adhabu kwa kumpinga. Wale wote ambao hawatafuti utii kwa Mungu katika imani yao ni watu wanaompinga Mungu. Mungu anataka kwamba watu watafute ukweli, wawe na kiu ya maneno Yake, wale na kunywa maneno Yake, na wayatie katika vitendo, yote haya ili waweze kufikia utii kwa Mungu. Ikiwa hiyo ndiyo nia yako ya kweli, basi Mungu hakika atakuinua, na hakika atakuwa mwenye fadhili kwako. Hili halina shaka wala halibadiliki. Ikiwa nia yako si kumtii Mungu, na una malengo mengine, basi kila unachosema na kufanya—hata maombi yako mbele za Mungu, na kwenda hata zaidi, kila hatua yako—kitakuwa cha kumpinga Yeye. Hata kama maneno yako ni ya upole na una vitendo vya upole, hata kama kila tendo na mwonekano wako vinaonekana kufaa mbele ya wengine, kana kwamba wewe ni mtu mtiifu, inapokuja kwa nia zako na mitazamo yako kuhusu imani katika Mungu, kila tendo lako ni la kumpinga Mungu; ni kutenda uovu. Watu wanaoonekana kuwa watiifu kama kondoo, lakini ambao mioyo yao imejaa nia ovu, ni mbwa mwitu waliovalia ngozi ya kondoo, na wale wanaomkosea Mungu moja kwa moja. Mungu hatamwacha hata mmoja wao, na Roho Mtakatifu atamfunua kila mmoja wao. Kila mtu ataona kwamba wale wote ambao ni wanafiki hakika watabeuliwa na Roho Mtakatifu. Usiwe na pupa: Mungu atamshughulikia na kumtupa kila mmoja wao mmoja baada ya mwingine.

Ikiwa huwezi kukubali nuru mpya kutoka kwa Mungu, na hutafuti wakati huwezi kuona wazi kile ambacho Mungu anafanya leo, na unakitilia shaka, unakihukumu, au unakichunguza na kukichambua, basi mtu wa namna hiyo hana nia ya kumtii Mungu. Ikiwa, nuru ya wakati wa sasa inapotokea, bado unathamini nuru ya jana na kuipinga kazi mpya ya Mungu, basi wewe si kitu kingine ila mwenye upumbavu—wewe ni mmoja wa wale wanaompinga Mungu kwa makusudi. Jambo muhimu katika kumtii Mungu ni kuichukua nuru mpya zaidi, na kuweza kukubali na kuitia katika vitendo. Huu pekee ndio utii wa kweli. Wale ambao hawana azimio la kumtamani sana Mungu hawawezi kumtii kwa makusudi, bali wanaweza tu kumpinga Mungu kwa sababu wanaridhika na hali ilivyo. Mwanadamu hawezi kumtii Mungu kwa sababu anamilikiwa na yale yaliyotangulia. Vitu vilivyotangulia hapo awali vimezalisha ndani ya mwanadamu kila namna ya dhana na mawazo mbalimbali kumhusu Mungu, na haya yamekuwa mfano wa mungu mawazoni mwake. Kwa hiyo, kile anachoamini ni dhana zake mwenyewe na viwango vya mawazo yake mwenyewe. Ukimpima Mungu anayefanya kazi ya vitendo leo dhidi ya mungu wa mawazo yako mwenyewe, basi imani yako inatoka kwa Shetani na imejengwa juu ya mapendeleo yako mwenyewe—Mungu hataki imani ya aina hii. Bila kujali sifa zao ni za juu kiasi gani, na bila kujali wamejitumia kiasi gani—hata kama wametumia maisha yao yote wakifanya kazi kwa ajili Yake na hata kwenda kujitoa mhanga—Mungu hamkubali mtu yeyote mwenye imani ya namna hii. Anawakirimu tu neema kidogo na kuwaacha waifurahie kwa muda. Watu kama hawa hawawezi kuutia ukweli katika vitendo. Roho Mtakatifu hafanyi kazi ndani yao, na Mungu atamwondosha kila mmoja wao kwa zamu. Wazee kwa vijana sawasawa, wale wasiomtii Mungu katika imani yao na walio na nia zisizo sahihi ndio wanaompinga na kuvuruga, na bila shaka watu kama hawa wataondoshwa na Mungu. Wale wasio na hata chembe ya utii kwa Mungu, wanaolikiri tu jina Lake, na wana hisia fulani za kwamba Mungu ana ukunjufu na anapendeza, lakini hawaendi sambamba na hatua za Roho Mtakatifu, wala hawatii kazi na maneno ya wakati wa sasa ya Roho Mtakatifu—watu kama hao wanaishi katikati ya neema ya Mungu, na hawawezi kupatwa na Mungu wala kufanywa kuwa watimilifu na Yeye. Mungu huwafanya watu kuwa watimilifu kupitia utii wao, kupitia kula, kunywa na kufurahia maneno ya Mungu, na kupitia mateso na usafishaji katika maisha yao. Ni kupitia imani kama hii pekee ndiyo tabia za watu zinaweza kubadilika, na ni hapo tu ndipo wanaweza kuwa na ufahamu wa kweli wa Mungu. Kutotosheka na kuishi katikati ya neema ya Mungu, kutamani na kuutafuta ukweli kwa shauku, na kufuatilia kupatwa na Mungu—hivyo ndivyo ilivyo kumtii Mungu kwa kujua, na hiyo ndiyo hasa aina ya imani Anayoitaka. Watu ambao hawafanyi chochote zaidi ya kuifurahia neema ya Mungu hawawezi kufanywa kuwa watimilifu wala kubadilishwa; wanaweza tu kuwa na utii, uchaji, upendo na uvumilivu wa juujuu tu. Wale wanaofurahia tu neema ya Mungu hawawezi kumjua Mungu kwa kweli, na hata wanapomjua, maarifa yao ni ya juujuu tu, nao husema mambo kama vile, “Mungu anampenda mwanadamu,” au “Mungu ni mwenye rehema kwa mwanadamu.” Haya hayawakilishi maisha ya mwanadamu, wala hayamaanishi kwamba watu wanamjua Mungu kwa kweli. Ikiwa, maneno ya Mungu yanapowasafisha, au majaribu Yake yanapowajia, watu hawawezi kumtii Mungu—ikiwa, badala yake, wanakuwa na mashaka na hata kuanguka—basi hawana hata chembe ya utii. Ndani yao kuna sheria na vizuizi vingi kuhusu imani katika Mungu, na hata uzoefu wa muda mrefu walioupata kutokana na miaka mingi ya imani katika Mungu, au taratibu mbalimbali zinazotumia Biblia kama kanuni yao. Je, watu kama hawa wanaweza kumtii Mungu? Watu hawa wamejaa mambo ya ubinadamu—wanawezaje kumtii Mungu? “Utii” wao unategemea mapendeleo yao kibinafsi—je, Mungu angeutaka utii wa namna hiyo? Huku ni kushika kanuni, si kumtii Mungu; ni kujitosheleza na kujiridhisha wenyewe. Ukisema kwamba huo ni utii kwa Mungu, je, humkufuru Yeye? Wewe ni Farao wa Misri. Unatenda maovu, na unafanya kwa makusudi kazi ya kumpinga Mungu—je, Mungu anataka umtumikie kwa namna hiyo? Afadhali ufanye hima utubu, na ujaribu kutafuta kujitambua. Usipofanya hivyo, afadhali tu urudi nyumbani; hilo litakuwa na faida zaidi kwako kuliko “utumishi kwa Mungu”. Hutavuruga wala kusumbua; utajua nafasi yako na kuishi vizuri—je, hilo halingalikuwa bora zaidi? Na hutampinga Mungu na kuadhibiwa!

Iliyotangulia: Huduma ya Kidini Lazima Ipigwe Marufuku

Inayofuata: Ahadi kwa Wale Wanaofanywa Kuwa Watimilifu

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp