Mungu Ni Bwana wa Viumbe Wote Walioumbwa

Hatua moja ya kazi ya enzi mbili zilizopita ilifanywa katika Israeli, na moja ilifanywa huko Yudea. Kwa ujumla, hakuna yoyote kati ya hatua hizi mbili iliyovuka mipaka ya Israeli, na kila moja ilifanywa kwa watu wateule wa kwanza. Matokeo yake, Waisraeli wanaamini kwamba Yehova Mungu ni Mungu wa Waisraeli pekee. Kwa sababu Yesu alifanya kazi huko Yudea, ambapo Alikamilisha kazi ya kusulubiwa, Wayahudi wanamwona Yeye kama Mkombozi wa watu wa Kiyahudi. Wanafikiri kwamba Yeye ni Mfalme wa Wayahudi pekee, si wa watu wengine wowote; kwamba Yeye si Bwana anayewakomboa Waingereza, wala Bwana anayewakomboa Waamerika, bali Bwana anayewakomboa Waisraeli; na kwamba ni Wayahudi ndio Aliowakomboa huko Israeli. Kwa uhakika, Mungu ndiye Mtawala wa vitu vyote. Yeye ndiye Mungu wa viumbe wote walioumbwa. Yeye si Mungu wa Waisraeli pekee, wala wa Wayahudi; Yeye ni Mungu wa viumbe wote walioumbwa. Hatua mbili zilizopita za kazi Yake zilifanyika huko Israeli, na watu wamekuza mawazo fulani kutokana na hili. Wanaamini kwamba Yehova alifanya kazi Yake huko Israeli, kwamba Yesu Mwenyewe alitekeleza kazi Yake katika Yudea, na, zaidi ya hayo, kwamba Yesu alifanya kazi hii akiwa amepata mwili. Vyovyote vile, wanafikiri, kazi hii haikuenea nje ya Israeli. Mungu hakufanya kazi kwa Wamisri au Wahindi; Alifanya kazi kwa Waisraeli pekee. Hivyo ndivyo watu huunda mawazo mbalimbali, na kuiwekea mipaka kazi ya Mungu kwa upeo fulani. Wanasema kwamba Mungu anapofanya kazi, ni lazima Afanye hivyo kwa watu wateule, na katika Israeli; kando na Waisraeli, Mungu hafanyi kazi kwa wengine wowote, wala hakuna upeo mkubwa zaidi kwa kazi Yake. Wao ni wakali hasa linapokuja suala la kumdhibiti Mungu mwenye mwili, na hawamruhusu Asonge nje ya mipaka ya Israeli. Je, si haya yote ni mawazo ya binadamu tu? Mungu aliumba mbingu na ardhi na vitu vyote, Aliumba viumbe wote walioumbwa, kwa hivyo Angewezaje kuwekea mipaka kazi Yake katika Israeli pekee? Hali ingekuwa hivyo, kungekuwa na faida gani Kwake kuumba viumbe wote walioumbwa? Aliumba ulimwengu mzima, na Hajautekeleza mpango Wake wa usimamizi wa miaka elfu sita katika Israeli pekee, bali kwa kila mtu katika ulimwengu. Haijalishi wewe ni nani—Mchina, Mwamerika, Mwingereza, Mrusi—kila mtu ni wa uzao wa Adamu; wote wameumbwa na Mungu. Hakuna hata mmoja wao anayeweza kuepuka mipaka ya viumbe walioumbwa, na hakuna hata mmoja wao anayeweza kujitenga na jina la "uzao wa Adamu." Wote ni viumbe walioumbwa, wote ni wa uzao wa Adamu, na pia wote ni dhuria potovu ya Adamu na Hawa. Si Waisraeli pekee ambao ni viumbe walioumbwa, bali watu wote; ni kwamba tu wengine wamelaaniwa, na wengine wamebarikiwa. Kuna sifa nyingi nzuri kuhusu Waisraeli; Mungu alifanya kazi kwao mwanzoni kwa sababu walikuwa watu wenye kiasi kidogo zaidi cha upotovu. Wachina hawawezi kulinganishwa nao; wao ni duni sana. Kwa hivyo, Mungu mwanzoni alifanya kazi miongoni mwa watu wa Israeli, na hatua ya pili ya kazi Yake ilifanywa tu huko Yudea—jambo ambalo limesababisha mawazo na kanuni nyingi miongoni mwa wanadamu. Kwa kweli, kama Mungu angetenda kulingana na mawazo ya binadamu, Yeye angekuwa Mungu wa Waisraeli pekee, na hivyo hangeweza kueneza kazi Yake kwa Mataifa, kwa maana Yeye angekuwa Mungu wa Waisraeli pekee, na si Mungu wa viumbe wote walioumbwa. Unabii ulisema kwamba jina la Yehova lingekuwa kuu miongoni mwa Mataifa, kwamba lingeenea kwa Mataifa. Kwa nini hili lilitabiriwa? Kama Mungu angekuwa Mungu wa Waisraeli pekee, basi Angefanya kazi huko Israeli pekee. Zaidi ya hayo, Hangeeneza kazi hii, na Hangetoa unabii kama huo. Kwa kuwa Alitoa unabii huu, hakika Ataeneza kazi Yake miongoni mwa Mataifa, ndani ya kila nchi na ardhi zote. Kwa kuwa Alisema hili, ni lazima Alifanye; huu ni mpango Wake, kwa maana Yeye ni Bwana aliyeumba mbingu na ardhi na vitu vyote, na Mungu wa viumbe wote walioumbwa. Bila kujali kama Anafanya kazi kwa Waisraeli, au katika Yudea kote, kazi Anayofanya ni kazi ya ulimwengu mzima, na kazi ya wanadamu wote. Kazi Anayofanya leo katika nchi ya joka kuu jekundu—katika nchi ya Mataifa—bado ni kazi ya wanadamu wote. Israeli inaweza kuwa kituo cha kazi Yake duniani; vivyo hivyo, Uchina pia inaweza kuwa kituo cha kazi Yake miongoni mwa Mataifa. Je, sasa si Yeye ametimiza unabii kwamba "jina la Yehova litakuwa kuu miongoni mwa Mataifa"? Hatua ya kwanza ya kazi Yake miongoni mwa Mataifa ni kazi hii, kazi Anayofanya katika nchi ya joka kuu jekundu. Kwamba Mungu mwenye mwili anaweza kufanya kazi katika nchi hii, na kufanya kazi kwa watu hawa waliolaaniwa, linapingana hasa na mawazo ya binadamu; hawa ndio watu wa kiwango cha chini kabisa kati ya wote, hawana thamani, na mwanzoni walitelekezwa na Yehova. Watu wanaweza kutelekezwa na watu wengine, lakini wakitelekezwa na Mungu, basi hakuna aliye na hadhi ya chini zaidi kuliko wao, hakuna aliye na thamani ya chini zaidi. Kwa kiumbe aliyeumbwa, kumilikiwa na Shetani au kutelekezwa na watu ni jambo linaloonekana kuwa chungu sana—lakini kiumbe aliyeumbwa anapotelekezwa na Muumba, inamaanisha kwamba hawezi kuwa na hadhi ya chini zaidi ya hapo. Dhuria ya Moabu walilaaniwa, na walizaliwa katika nchi hii iliyo nyuma; bila shaka, kati ya watu wote walio chini ya ushawishi wa giza, dhuria ya Moabu wana hadhi ya chini kabisa. Kwa sababu watu hawa wamekuwa na hadhi ya chini kabisa hadi sasa, kazi inayofanywa kwao inavunja mawazo ya binadamu zaidi, na pia ina faida zaidi kwa mpango mzima wa usimamizi wa miaka elfu sita wa Mungu. Kufanya kazi kama hiyo kwa watu hawa ndiko kunakoweza kuvunja mawazo ya binadamu zaidi ya yote, na kwa hili Mungu anaanzisha enzi; kwa hili Yeye anavunja mawazo yote ya binadamu; kwa hili Yeye anahitimisha kazi ya Enzi yote ya Neema. Kazi Yake ya kwanza ilitekelezwa Yudea, ndani ya mipaka ya Israeli; miongoni mwa Mataifa, Hakufanya kazi yoyote kuanzisha enzi mpya. Hatua ya mwisho ya kazi haitekelezwi tu kwa watu wa mataifa, bali zaidi sana kwa wale ambao wamelaaniwa. Jambo hili moja ni ushahidi unaoweza kabisa kumfedhehesha Shetani, na hivyo, Mungu "anakuwa" Mungu wa viumbe wote walioumbwa katika ulimwengu, Bwana wa vitu vyote, lengo la ibada kwa kila kitu chenye uhai.

Leo, kuna wale ambao bado hawaelewi ni kazi gani mpya ambayo Mungu ameanza. Miongoni mwa Mataifa, Mungu ameleta mwanzo mpya. Ameanza enzi mpya, na kuanzisha kazi mpya—na Anatekeleza kazi hii kwa dhuria ya Moabu. Je, hii si kazi Yake mpya zaidi? Hakuna mtu katika enzi zote ambaye amewahi kupitia kazi hii hapo awali. Hakuna mtu ambaye hata amewahi kuisikia, sembuse kuielewa. Hekima ya Mungu, maajabu ya Mungu, kutoweza kueleweka kwa Mungu, ukuu wa Mungu, na utakatifu wa Mungu vyote vinafunuliwa kupitia hatua hii ya kazi, kazi ya siku za mwisho. Je, si hii ni kazi mpya, kazi inayovunja mawazo ya kibinadamu? Kuna wale wanaofikiri hivi: "Kwa kuwa Mungu alimlaani Moabu na kusema kwamba Atatelekeza dhuria ya Moabu, Anawezaje kuwaokoa sasa?" Hawa ni watu wa mataifa ambao walilaaniwa na Mungu na kufukuzwa kutoka Israeli; Waisraeli waliwaita "mbwa wa Mataifa." Katika mtazamo wa kila mtu, wao si mbwa wa Mataifa tu, bali hata vibaya zaidi, wana wa maangamizi; yaani, wao si watu wateule wa Mungu. Ingawa walizaliwa ndani ya mipaka ya Israeli mwanzoni, wao si sehemu ya watu wa Israeli, na walifukuzwa hadi katika nchi za Mataifa. Wao ni watu wa hali ya chini kabisa kati ya watu wote. Ni kwa sababu wao ni wa hali ya chini kabisa miongoni mwa wanadamu ndiyo maana Mungu anatekeleza kazi Yake ya kuanzisha enzi mpya kwao, kwa maana wao ni wawakilishi wa wanadamu wapotovu. Kazi ya Mungu si ya kiholela au isiyo na kusudi; kazi Anayofanya kwa watu hawa leo pia ni kazi inayofanywa kwa viumbe walioumbwa. Nuhu alikuwa kiumbe aliyeumbwa, kama ilivyo dhuria yake. Mtu yeyote duniani aliye na damu na nyama ni kiumbe aliyeumbwa. Kazi ya Mungu inaelekezwa kwa viumbe wote walioumbwa; haitegemei kama mtu amelaaniwa baada ya kuumbwa. Kazi Yake ya usimamizi inaelekezwa kwa viumbe wote walioumbwa, si kwa wale watu wateule ambao hawajalaaniwa. Kwa kuwa Mungu anakusudia kutekeleza kazi Yake juu ya viumbe Wake walioumbwa, hakika Ataitekeleza hadi ikamilike kwa mafanikio, na Atafanya kazi juu ya wale watu wenye faida kwa kazi Yake. Kwa hivyo, Yeye anavunja kanuni zote Anapofanya kazi kwa watu; maneno "kulaaniwa," "kuadibiwa" na "kubarikiwa" hayapo Kwake! Watu wa Kiyahudi ni wazuri, kama walivyo watu wateule wa Israeli; wao ni watu wenye ubora wa tabia wa juu na wenye ubinadamu mzuri. Mwanzoni, ni kwao ambapo Yehova alianzisha kazi Yake, na kutekeleza kazi Yake ya mwanzo kabisa—lakini kuwafanya wapokeaji wa kazi ya ushindi leo hakungekuwa na maana. Wao pia wanaweza kuwa sehemu ya viumbe walioumbwa, na kunaweza kuwa na mambo mengi chanya kuwahusu, lakini kutekeleza hatua hii ya kazi kwao hakungekuwa na maana; haingeweza kuwashinda watu, wala haingeweza kuwasadikisha viumbe wote walioumbwa. Hii ndiyo maana hasa ya kuhamishia kazi Yake kwa watu hawa wa nchi ya joka kuu jekundu. Jambo muhimu kabisa hapa ni kuanzisha Kwake enzi, kuvunja Kwake kanuni zote na mawazo yote ya binadamu na kuhitimisha Kwake kazi ya Enzi nzima ya Neema. Kama kazi Yake ya sasa bado ingetekelezwa kwa Waisraeli, kufikia wakati mpango Wake wa usimamizi wa miaka elfu sita unapofikia kikomo, kila mtu angeamini kwamba Mungu ni Mungu wa Waisraeli pekee, kwamba Waisraeli pekee ndio watu wateule wa Mungu, na kwamba Waisraeli pekee ndio wanaostahili kurithi baraka na ahadi ya Mungu. Kupata mwili kwa Mungu katika siku za mwisho katika nchi ya Mataifa, nchi ya joka kuu jekundu, kunatimiza kazi Yake ya kuwa Mungu wa viumbe wote walioumbwa, kunakamilisha kazi Yake nzima ya usimamizi, na kunahitimisha sehemu kuu ya kazi Yake ya usimamizi katika nchi ya joka kuu jekundu. Kiini cha hatua hizi tatu za kazi ni wokovu wa mwanadamu—yaani, kuwafanya viumbe wote walioumbwa wamwabudu Muumba. Hivyo, kuna maana kubwa kwa kila hatua ya kazi; Mungu hafanyi chochote ambacho hakina maana au thamani. Kwa upande mmoja, hatua hii ya kazi inaanzisha enzi mpya na inahitimisha enzi mbili zilizopita; kwa upande mwingine, inavunja mawazo yote ya watu na njia zote za zamani za watu za kuamini na njia za zamani za kuelewa mambo. Kazi ya enzi mbili zilizopita ilitekelezwa kulingana na mawazo tofauti ya binadamu; hata hivyo, hatua hii inaondoa kabisa mawazo ya binadamu, na hivyo kuwashinda wanadamu kikamilifu. Kupitia kuishinda dhuria ya Moabu, kupitia kazi inayotekelezwa kwa dhuria ya Moabu, Mungu atawashinda watu wa ulimwengu mzima. Huu ndio umuhimu wa kina zaidi wa hatua hii ya kazi Yake, na ni kipengele chenye thamani zaidi cha hatua hii ya kazi Yake. Hata kama sasa unajua kwamba nafasi yako mwenyewe ni ya chini na kwamba una thamani ya chini, bado utahisi kwamba umerithi baraka kubwa sana na kupokea ahadi kubwa sana, na kwamba unaweza kusaidia kutimiza kazi hii kuu ya Mungu, kutazama uso wa kweli wa Mungu, kujua tabia asili ya Mungu, na kufuata mapenzi ya Mungu, jambo ambalo unaona kuwa la furaha kuu zaidi. Hatua mbili zilizopita za kazi ya Mungu zilitekelezwa huko Israeli. Kama hatua hii ya kazi Yake katika siku za mwisho ingetekelezwa pia kwa Waisraeli, si tu kwamba viumbe wote walioumbwa wangeamini kwamba Waisraeli pekee ndio waliokuwa watu wateule wa Mungu, bali pia mpango mzima wa usimamizi wa Mungu ungeshindwa kufikia matokeo yake yaliyotarajiwa. Katika kipindi ambacho hatua mbili za kazi Yake zilitekelezwa huko Israeli, hakuna kazi mpya—wala kazi yoyote ya kuanzisha enzi mpya—iliyotekelezwa miongoni mwa Mataifa. Hatua ya kazi ya leo—kazi ya kuanzisha enzi mpya—inatekelezwa kwanza miongoni mwa Mataifa, na, zaidi ya hayo, inatekelezwa mwanzoni juu ya dhuria ya Moabu, na hivyo kuanzisha enzi nzima. Mungu amevunjavunja maarifa yoyote yaliyomo ndani ya mawazo ya binadamu, asiruhusu yoyote kati ya hayo kubaki. Katika kazi Yake ya ushindi, Amevunjavunja mawazo ya kibinadamu, na njia za zamani, za awali za watu za kuelewa mambo. Anawaruhusu watu waone kwamba kwa Mungu hakuna kanuni, kwamba hakuna chochote cha zamani kuhusu Mungu, kwamba kazi Anayofanya haina vizuizi kabisa, ni huru kikamilifu, na kwamba Yuko sahihi katika yote Anayofanya. Ni lazima utii kikamilifu kazi yoyote Anayofanya kwa viumbe walioumbwa. Kazi yote Anayofanya ina maana, na inatekelezwa kulingana na nia na hekima Yake mwenyewe, na si kulingana na chaguzi na mawazo ya binadamu. Ikiwa jambo lina faida kwa kazi Yake, Yeye hulifanya; na ikiwa jambo halina faida kwa kazi Yake, Yeye halifanyi, haijalishi ni zuri kiasi gani! Yeye hufanya kazi na kuchagua walengwa na eneo la kazi Yake kulingana na maana na kusudi la kazi Yake. Yeye hafuati kanuni za zamani Anapofanya kazi, wala Hafuati mifumo ya zamani. Badala yake, Yeye hupanga kazi Yake kulingana na umuhimu wa kazi. Hatimaye, Atafikia matokeo halisi na lengo lililotarajiwa. Iwapo huelewi mambo haya leo, kazi hii haitakuwa na matokeo ndani yako.

Iliyotangulia: Tofauti Kati ya Huduma ya Mungu Mwenye Mwili na Wajibu wa Mwanadamu

Inayofuata: Msimamo Wako Kuhusu Nyaraka Kumi na Tatu ni Upi?

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp