Sura ya 27
Kamwe mienendo ya binadamu haijawahi kuugusa moyo Wangu, wala kuonekana Kwangu kama kitu cha thamani. Machoni mwa mwanadamu, daima Mimi huwa mkali kwake kila wakati, na kila mara Nimemweka chini ya mamlaka kali. Ndani ya matendo yote ya mwanadamu, ni mambo machache sana anayonifanyia Mimi, na mara nyingi hapana kitendo chake kisimamacho imara machoni Pangu. Hatimaye, kila kitu cha mwanadamu kinayumba mbele Yangu bila kunong’ona; ni baada tu ya hapo ndipo Ninapodhihirisha matendo Yangu, na kufanya kila mtu kunijua kupitia kushindwa kwao wenyewe. Hali ya mwanadamu haibadiliki kamwe. Kilicho ndani ya mioyo yao sio kulingana na mapenzi Yangu—sio Ninachohitaji. Ninachochukia zaidi ni ukaidi na ugumu wa mwanadamu, lakini ni nguvu gani inayowachochea wanadamu kuendelea kushindwa kunijua, kuniweka mbali daima, na kutotenda kulingana na mapenzi Yangu mbele Yangu bali kunipinga Mimi nyuma ya mgongo Wangu? Mbona wasitubu dhambi zao na kuzaliwa mara ya pili? Kwa nini watu wako tayari daima kuishi kwenye kinamasi badala ya mahali pasipo na matope? Je, inawezekana kwamba Nimewadhulumu? Je, inaweza kuwa kwamba Nimewaelekeza katika mwelekeo usio sahihi? Je, inaweza kuwa kwamba Ninawaongoza kuzimu? Kila mtu yuko tayari kuishi “kuzimu.” Mwangaza unapotokea, macho yao hupofuka ghafla, kwa kuwa kila chao kinatoka kuzimu. Ilhali watu hawana ufahamu wa mambo haya na wanafurahia tu “raha za motoni.” Wao hata hushikilia kwa nguvu karibu na vifua vyao kama hazina wakihofu kwamba Mimi Nitazinyakua hazina hizi, hivyo kuwaacha bila kiini cha kuwepo kwao. Wanadamu wananiogopa na ndio maana wao hukaa mbali na Mimi na kutokaa karibu Nami Ninapokuja duniani kwa maana “hawapendi kujiletea madhara,” wakiwa na ombi la kuishi maisha ya amani katika familia yao ili wawe na “maisha ya furaha duniani.” Lakini Siwezi kuruhusu wanadamu watende vile wanavyotaka, kwa kuwa lengo Langu hasa ni kuziangamiza familia zao. Kunzia wakati Nifikapo, amani inatoweka katika nyumba zao. Nakusudia kusambaratisha mataifa yote yatawanyike, sembuse familia ya mwanadamu. Ni nani awezaye kuepuka mkono Wangu? Itawezekanaje kuwa wale wanaopokea baraka wataepuka kwa sababu ya kutonuia kwao? Itawezekanaje kamwe kuwa wale walioadibiwa watapata huruma Yangu kwa sababu ya wao kuwa na woga? Katika maneno Yangu yote, wanadamu wameona mapenzi Yangu na kuona matendo Yangu, lakini ni nani awezaye kuondokana na minyororo ya mawazo yake mwenyewe? Ni nani anaweza kupata njia kutoka ndani au nje ya maneno Yangu?
Mwanadamu ameshuhudia upendo Wangu, mwanadamu amenitumikia kwa dhati, na mwanadamu amenitii kwa kweli, akinifanyia kila kitu katika uwepo Wangu. Hata hivyo hili haliwezi kufikiwa na watu leo; hawafanyi lolote ila kulia rohoni mwao kana kwamba wamenyakuliwa na mbwa-mwitu mwenye njaa, na wanaweza tu kunitazama bila msaada, wakinililia bila kukoma. Lakini mwishowe, hawawezi kujiondoa katika matatizo yanayowakumba. Ninakumbuka jinsi ambavyo watu wa kale waliweka ahadi mbele Zangu, wakiapa kwa mbingu na dunia mbele Zangu kulipiza ukarimu Wangu kwa upendo. Walilia kwa uchungu mbele Yangu, na kilio chao kilikuwa cha kuvunja moyo, kigumu kuvumilia. Kwa sababu ya azimio lao, mara nyingi niliwapa watu msaada. Mara nyingi, wanadamu wamekuja mbele Zangu kunitii, mienendo yao ya kupendeza isiyoweza kusahaulika. Mara nyingi, wamenipenda bila kutikisika katika uaminifu wao, bidii yao ikiwa ya kupendeza. Mara nyingi, wamenipenda hadi kiwango cha kuhatarisha maisha yao, wakanipenda Mimi hata zaidi ya wanavyojipenda wenyewe—na kwa vile Nimeona upendo huu ni wa kweli, Nimeukubali. Mara nyingi, wamejitoa kama sadaka mbele Yangu, bila kujali mauti kwa sababu Yangu, na Nimepangusa wasiwasi huo nyusoni mwao, na kwa uangalifu nimekadiria maumbile yao. Kumekuwa na nyakati zisizohesabika ambapo Nimewapenda kama kitu kinachothaminiwa, na kuna wakati mwingine mwingi ambao Nimewachukia kama adui Zangu. Walakini, kile kilicho akilini Mwangu kinasalia nje ya uwezo wa mwanadamu. Watu wanapokuwa na huzuni, Mimi huja kuwafariji, na wanapokuwa dhaifu, Ninakuja kuwasaidia. Wanapopotea njia, Ninawapa mwelekeo. Wanapolia, Mimi hufuta machozi yao. Lakini Ninapohuzunika, ni nani awezaye kunifariji kwa mioyo yao? Ninapopatwa na hofu, ni nani anayejali hisia Zangu? Ninapoona huzuni, ni nani anayeweza kutibu kidonda kilicho moyoni Mwangu? Ninapohitaji mtu karibu Nami, ni nani anayejitolea kushirikiana Mimi? Je, inaweza kuwa kwamba mtazamo wa zamani wa watu Kwangu sasa umepotea, kamwe usiweze kurudi tena? Ni kwa nini kwamba hakuna lolote kati ya haya wanalokumbuka? Inawezekanaje kuwa wanadamu wameyasahau yote haya? Je, haya yote si kwa sababu ya mwanadamu kupotoshwa na adui yake?
Malaika wanapocheza muziki wa kunisifu, hii haiwezi ila kuchochea huruma Yangu kwa mwanadamu. Moyo wangu unajawa na huzuni ghafla, na haiwezekani kujiondoa kwenye hisia hizi za uchungu. Katika furaha na huzuni ya kutengana na kisha kuunganika Kwangu na mwanadamu, hatuwezi kubadilishana mawazo. Kwa sababu tumetengana mbinguni na wanadamu ardhini, nyakati ambapo Mimi na mwanadamu tunaweza kukutana ni nadra sana. Ni nani anayeweza kujitoa katika kuwaza mambo mazuri ya kale? Ni nani anayeweza kuzuia picha hizi za ukumbusho kumwonekania? Ni nani asingetumaini kuendelea kwa hisia hizi nzuri? Ni nani hangetamani kwa hamu kurudi Kwangu? Ni nani ambaye hangetamani kuungana tena Kwangu na mwanadamu? Moyo wangu unafadhaika sana, na roho ya mwanadamu ina wasiwasi mwingi. Licha ya sisi kuwa sawa katika roho, hatuwezi kuwa pamoja mara kwa mara, na mara kwa mara hatuwezi kuonana. Hivyo maisha ya wanadamu wote yamejaa huzuni na kukosa uchangamfu, kwani mwanadamu daima amekuwa akinitamani Mimi. Ni kana kwamba wanadamu walikuwa vitu vilivyoangushwa kutoka mbinguni; wanalilia jina Langu juu ya nchi, wakiinua macho yao Kwangu kutoka ardhini—lakini wanawezaje kuepuka taya za mbwa-mwitu mkali? Je, wanawezaje kujiokoa kutokana na vitisho vyake na vishawishi vyake? Binadamu wanawezaje kukosa kujitolea kwa sababu ya kutii utaratibu wa mpango Wangu? Wanaponisihi kwa sauti, Ninageuza uso Wangu kutoka kwao, kwa maana Sitaki kushuhudia zaidi ya hayo; Lakini, itawezekanaje Nisisikie vilio vya watu hawa? Nitarekebisha udhalimu katika dunia ya mwanadamu. Nitafanya kazi Yangu kwa mikono Yangu mwenyewe ulimwenguni kote, Nikimkomesha Shetani asiwadhuru watu Wangu tena, Nikiwakataza maadui wasifanye kile wapendacho tena. Nitakuwa Mfalme duniani na kukipeleka kiti Changu cha enzi huko, na kuwafanya maadui Wangu wote waanguke chini na kukiri makosa yao mbele Yangu. Katika hali Yangu ya huzuni, hasira imechanganywa, Nitaukanyaga ulimwengu wote sawasawa, bila kumwacha yeyote, na kuwatia maadui Wangu hofu kubwa. Naiangamiza dunia nzima, na kuwafanya maadui Wangu waanguke katika maangamizo hayo, ili kuanzia sasa na kuendelea wasiwapotoshe wanadamu tena. Mpango Wangu tayari umeamuliwa, na hakuna yeyote, haijalishi ni nani, atakayeubadilisha. Ninapotembeatembea kwa fahari kuu ulimwenguni, wanadamu wote watafanywa wapya, na kila kitu kitapewa uhai tena. Mwanadamu hatalia tena, hatanililia tena akitaka msaada. Hapo, moyo Wangu utajawa na furaha tele, na wanadamu Watanirudia kwa shangwe. Ulimwengu mzima, kutoka juu mpaka chini, utabubujikwa na nderemo …
Leo, miongoni mwa mataifa ya ulimwengu, Ninafanya kazi ambayo Nimekusudia kukamilisha. Ninazunguka katikati ya wanadamu, Nikifanya kazi yote ndani ya mpango Wangu, na ubinadamu wote unavunja mataifa mengi kulingana na mapenzi Yangu. Watu walio duniani wameweka mazingatio yao kwenye wanakoelekea, kwani hakika siku inakaribia na Malaika wanapiga tarumbeta zao. Hakutakuwa na ucheleweshaji tena, na viumbe vyote vitaanza kucheza kwa shangwe. Ni nani anayeweza kusogeza siku Yangu kwa mapenzi yake? Inawezekana kiwe kiumbe cha duniani? Au nyota za angani? Au malaika? Ninapotoa tamko la kuanzisha wokovu wa watu wa Israeli, siku Yangu inawasonga wanadamu wote. Kila mwanadamu anahofia kurejea kwa taifa la Israeli. Israeli itakaporejea, hiyo itakuwa siku Yangu ya utukufu, na pia, itakuwa siku ambayo kila kitu kitabadilika na kuwa kipya. Hukumu ya haki inapoukaribia ulimwengu, watu wote watakuwa na woga na hofu, kwa maana ulimwengu wa mwanadamu haufahamu haki. Wakati ambapo Jua la haki litaonekana, Mashariki itaangazwa, kisha litaangaza ulimwenguni kote, likimfikia kila mtu. Iwapo mwanadamu atatenda haki Yangu, ni kitu gani kitakuwa cha kuogopesha. Watu Wangu wote wanangoja siku ya kurudi Kwangu, wanatarajia kwa hamu siku Yangu. Wanangoja Mimi niwaadhibu wanadamu wote na kupanga hatima ya wanadamu katika wajibu Wangu kama Jua la haki. Ufalme Wangu unaenea katika ulimwengu mzima, na kiti Changu cha enzi kimenyakua mioyo ya mamia ya mamilioni nyingi za watu. Kwa usaidizi wa malaika wa mbinguni, utimilifu Wangu mkuu utakamilika hivi karibuni. Wanangu na watu Wangu wote wanangoja kwa hamu kurejea Kwangu, wakitarajia kuunganishwa Kwangu nao, tusije tukatengana tena. Itawezekanaje watu wote wa ufalme Wangu wasikimbie wakifurahiana kwa kuunganika pamoja na Mimi tena? Inawezekana huu uwe muungano usio na gharama yoyote iliyolipwa? Mimi Ninaheshimiwa machoni pa kila mtu, Ninadhihirika katika maneno ya kila mtu. Nitakaporejea, aidha, Nitashinda nguvu zote za adui. Wakati umewadia! Nitaianza kazi Yangu, Nitatawala miongoni mwa wanadamu! Tazama, Ninarejea! Ninaondoka! Hili ndilo kila mmoja anatarajia, ndilo kila mmoja anatumainia. Nitawaruhusu binadamu wote watazame kufika kwa siku Yangu na wote watakaribisha siku Yangu kwa furaha tele!
Aprili 2, 1992