Sura ya 34
Wakati fulani Nilimwalika mwanadamu kama mgeni katika nyumba Yangu, lakini alikimbia huku na kule kwa sababu ya miito Yangu—kana kwamba, badala ya kumwalika kama mgeni, Nilikuwa Nilimleta kwenye uwanja wa kunyongwa. Hivyo, nyumba Yangu iliachwa tupu, kwani mwanadamu kila mara ameepukana na Mimi, na daima alikuwa macho dhidi Yangu. Hili liliniacha bila njia yoyote ya kutekeleza sehemu ya kazi Yangu, ambayo ni kusema, ni kwamba Niliirudisha karamu Niliyomwandalia, kwani mwanadamu hakutaka kufurahia karamu hii na hivyo Sikumlazimisha kufanya hivyo. Ilhali mwanadamu anajikuta ghafla amezingirwa na njaa, kwa hivyo anakuja kugonga mlango Wangu akiomba msaada Wangu—na kumwona akiwa katika hali mbaya sana, Ningewezaje kukosa kumwokoa? Hivyo, kwa mara nyingine tena Ninamwandalia mwanadamu karamu, ili aweze kuifurahia, na ni hapo tu ndipo anahisi jinsi Ninavyopendeka, na hivyo anakuja kunitegemea. Na kwa sababu ya mtazamo Wangu kwake, hatua kwa hatua anakuja kunipenda “bila kusita,” na hashuku tena kwamba Nitampeleka katika “nchi ya uchomaji maiti,” kwani haya si mapenzi Yangu. Na kwa hiyo, ni baada ya kuuona moyo Wangu tu ndipo mwanadamu hunitegemea kweli, ambalo linaonyesha tu jinsi alivyo na “tahadhari”. Lakini Siwi macho kwa mwanadamu kwa sababu ya udanganyifu wake, lakini Husisimua mioyo ya watu kwa kumbatio Langu changamfu. Je, hili silo Nifanyalo sasa? Je, hili silo linalodhihirika ndani ya watu katika hatua ya sasa? Kwa nini wana uwezo wa kufanya mambo kama haya? Kwa nini wana hisia ya moyoni kama hiyo? Je, ni kwa sababu wananijua kwa kweli? Kwa sababu wana upendo usio na mipaka Kwangu kwa kweli? Simlazimishi mtu yeyote kunipenda, lakini Nampa tu uhuru wa kujifanyia uchaguzi wake mwenyewe; katika hili, Siingilii, wala kumsaidia kufanya uchaguzi kuhusu majaliwa yake. Watu waliweka maazimio yao mbele Yangu, waliyaleta mbele Yangu ili Niyakague, na Nilipofungua mfuko uliokuwa na “azimio la mwanadamu,” Niliona mambo yaliyovurugika ndani. Bado mambo yaliyokuwa ndani yalikuwa “mengi,” na watu walinitazama kwa macho yaliyokodoa, wakiogopa sana kwamba Ningeng’oa azimio lao. Lakini kwa sababu ya udhaifu wa mwanadamu, Sikutoa hukumu mwanzoni kabisa, na badala yake Niliufunga mfuko na kuendelea kufanya kazi Niliyopaswa kufanya. Mwanadamu, hata hivyo, haingii katika mwongozo Wangu katika mwamko wa kazi Yangu, lakini anaendelea kujishughulisha na kama azimio lake limesifiwa na Mimi. Nimefanya kazi nyingi sana, Nimenena maneno mengi sana, lakini hadi sasa, mwanadamu bado hawezi kuyaelewa mapenzi Yangu, na hivyo kila kitendo chake cha kushangaza kinaacha “kichwa Changu kikizunguka.” Kwa nini hawezi kuelewa mapenzi Yangu daima, na hufanya mambo kwa haraka kama apendavyo? Je, ubongo wake umepatwa na mshtuko? Inawezekana kuwa haelewi maneno Nisemayo? Kwa nini yeye daima hutenda na macho yake yakiangalia mbele kabisa, lakini hawezi kuunda njia na kuonyesha mfano kwa watu wa baadaye? Je, kulikuwa na mtu yeyote wa kuonyesha mfano kabla ya Petro? Je, si chini ya mwongozo Wangu ndipo Petro akanusurika? Kwa nini watu wa leo hawawezi kufanya hili? Kwa nini, baada ya kuwa na mfano wa kufuata, bado hawawezi kuridhisha mapenzi Yangu? Hili linaonyesha kwamba bado mwanadamu hana imani Kwangu, ambalo ndilo limesababisha hali za leo zenye taabu.
Mimi hufurahia kuwatazama ndege wadogo wakipaa angani. Ingawa hawajaweka azimio lao mbele Yangu, na hawana maneno ya “kunipa” Mimi, wanapata raha katika ulimwengu ambao Nimewapa. Mwanadamu, hata hivyo, haliwezi hili, na uso wake umejaa huzuni—yawezekana kwamba Nina deni lake lisiloweza kulipwa? Kwa nini uso wake daima una michirizi ya machozi? Mimi hustaajabia mayungiyungi yanayochanuka vilimani. Maua na nyasi zinanyooka toka upande mmoja hadi upande mwingine wa miteremko, lakini mayungiyungi yanaongeza mng’aro kwa utukufu Wangu duniani kabla ya kufika kwa majira ya kuchipua—je, mwanadamu anaweza kutimiza kiasi hiki? Je, angeweza kunishuhudia duniani kabla ya kurudi Kwangu? Je, angeweza kujitolea kwa ajili ya jina Langu katika nchi ya joka kubwa jekundu? Ni kana kwamba matamko Yangu yamejaa matakwa kwa mwanadamu—ananichukia sana kwa sababu ya matakwa haya; kwa sababu mwili wake ni dhaifu sana, na hawezi kimsingi kufikia kile Ninachotaka, anaogopa maneno Yangu. Ninapofungua kinywa Changu, Nawaona watu duniani wakikimbia kila upande, kana kwamba wanajaribu kuitoroka njaa. Ninapofunika uso Wangu, wakati Ninapogeuza mwili Wangu, watu ghafla huwa wanaingiwa na hofu, hawajui cha kufanya, kwani wanaogopa kuondoka Kwangu; katika dhana zao, siku Nitakayotoka ndiyo siku ambayo msiba utashuka kutoka mbinguni, siku Nitakayoondoka ndiyo siku ambayo adhabu yao itaanza. Lakini Ninachofanya ni kinyume kabisa na dhana za mwanadamu, Sijawahi kutenda kulingana na dhana za mwanadamu, Sijaruhusu kamwe dhana zake kuwa zenye kupatana na Mimi. Wakati Ninapotenda ni wakati ambapo kwa usahihi mwanadamu anawekwa wazi. Kwa maneno mengine, vitendo Vyangu haviwezi kupimwa na dhana za binadamu. Tangu wakati wa uumbaji mpaka leo, hakuna mtu aliyewahi kugundua “bara mpya” katika mambo ambayo Ninafanya, hakuna mtu aliyewahi kuelewa sheria ambazo kwazo Ninatenda, hakuna mtu aliyewahi kufungua njia mpya. Hivyo, leo, watu bado hawawezi kuingia katika njia sahihi—ambayo ndiyo hasa wanayokosa, na wanayopaswa kuingia ndani yake. Tangu wakati wa uumbaji mpaka leo, Sijawahi kamwe kuanza shughuli kama hiyo hapo awali, Nimeongeza tu vipande vipya kwa kazi Yangu katika siku za mwisho. Lakini hata chini ya hali kama hizo dhahiri, watu bado hawawezi kuelewa mapenzi Yangu—hiki sio kile ambacho wanakosa kabisa?
Baada ya kuingia katika kazi mpya, Nina matakwa mapya kwa mwanadamu. Kwa mwanadamu, ni kana kwamba matakwa ya zamani hayajakuwa na matokeo, ambayo ndiyo sababu anayasahau. Ni njia gani mpya ambayo kwayo Nafanya kazi? Ninataka nini kwa mwanadamu? Watu wenyewe wanaweza kupima kama yale waliyofanya katika siku za nyuma yalifuatana na mapenzi Yangu, ikiwa matendo yao yalikuwa ndani ya mipaka ya kile Nilichotaka. Hakuna haja ya Mimi kukagua kila kitu kimoja kimoja; wanaelewa kimo chao wenyewe, na kwa hiyo katika mawazo yao, wanaelewa wanaweza kutenda hadi kiasi gani, na hakuna haja ya Mimi kuwaambia waziwazi. Ninapozungumza, pengine, watu wengine watajikwaa; hivyo, Nimeepuka kusema sehemu hii ya maneno Yangu ili kuzuia watu kugeuka kuwa wadhaifu kutokana na hilo. Je, hili sio la manufaa makubwa zaidi kwa ufuatiliaji wa mwanadamu? Je, sio la manufaa makubwa zaidi kwa maendeleo ya mwanadamu? Nani hataki kusahau mambo yake ya zamani, na kujitahidi kuendelea mbele? Kwa sababu ya “kutofikiri” Kwangu, Sijui kama watu wanaelewa kuwa njia ambazo kwazo Nanena tayari zimeingia katika eneo jipya. Kwa kuongezea, kwa sababu kazi Yangu ina “shughuli nyingi,” sana, Sijapata wakati wa kuuliza ikiwa watu wanaelewa sauti ambayo kwayo Ninazungumza. Hivyo, Ninataka tu kwamba watu wawe na uelewa zaidi Kwangu. Kwa sababu kazi Yangu ina “shughuli nyingi,” Siwezi kutembelea kibinafsi misingi ya kazi Yangu ili kuwaelekeza watu, na hivyo Nina “ufahamu mdogo” kuwahusu. Kwa jumla, chochote kingine, Nimeanza sasa kumwongoza mwanadamu kuingia rasmi katika mwanzo mpya, na katika mbinu mpya. Katika matamko Yangu yote, watu wameona kwamba kuna kuchekesha, ucheshi, na sauti ya nguvu ya dhihaka hasa katika kile Ninachosema. Hivyo, maelewano kati ya mwanadamu na Mimi huvurugwa bila kujua, na kusababisha kifuniko kizito cha mawingu juu ya nyuso za watu. Mimi, hata hivyo, Sizuiliwi na hili, lakini Naendelea na kazi Yangu, kwani yote ambayo Nasema na kufanya ni sehemu ya lazima ya mpango Wangu, yote yanayonenwa kutoka katika kinywa Changu humsaidia mwanadamu, na hakuna chochote Nifanyacho ni cha upuuzi, lakini cha kuwajenga watu wote. Ni kwa sababu mwanadamu anapungukiwa ndio Naachilia huru na kuendelea kunena. Watu wengine, labda, wananisubiri bila tumaini Nitoe matakwa mapya kwao. Ikiwa ndivyo, basi Naridhisha mahitaji yao. Lakini kuna jambo moja ni lazima Niwakumbushe: Ninapozungumza, Natumai kuwa watu wanapata ufahamu zaidi, Natumai kwamba watakuwa wenye utambuzi zaidi, ili waweze kupata zaidi kutoka kwa maneno Yangu na hivyo kutimiza matakwa Yangu. Hapo awali, katika makanisa, lengo la watu lilikuwa ni kushughulikiwa na kuvunjwa. Kula na kunywa Maneno yangu kulikuwa juu ya msingi wa kuelewa malengo yao na chanzo—lakini leo si kama siku za nyuma, watu hawawezi kabisa kuelewa chanzo cha matamko Yangu, na hivyo hawana nafasi ya kushughulikiwa na kuvunjwa na Mimi, kwa sababu wao wametumia kila kitu walicho nacho kula na kunywa maneno Yangu. Lakini hata katika hali hizi, bado hawawezi kuridhisha matakwa yangu, na hivyo Nafanya madai mapya kwao: Nawataka waingie katika majaribio pamoja nami, kwamba waingie katika kuadibu. Lakini hebu Niwakumbushe jambo moja: Huku si kumwua mwanadamu, lakini kinachohitajika na kazi Yangu, kwa kuwa, katika hatua ya sasa, maneno Yangu hayaeleweki kabisa na mwanadamu, na mwanadamu hawezi kushirikiana na Mimi—hakuna cha kufanya! Naweza tu kumfanya mwanadamu aingie katika utaratibu mpya pamoja nami. Kuna nini kingine cha kufanya? Kwa sababu ya kasoro za mwanadamu, Mimi pia lazima Niingie katika mkondo ambao mwanadamu huingia—je, si Mimi ambaye atawafanya watu wawe kamili? Je, si Mimi Niliyepanga mpango huu? Ingawa matakwa yale mengine si magumu, si ya pili kwa ya kwanza. Kazi Yangu miongoni mwa kundi la watu wa siku za mwisho ni shughuli isiyo na kifani, na hivyo, ili utukufu Wangu ujaze ulimwengu, watu wote lazima wapatie taabu ya mwisho kwa ajili Yangu. Je, unaelewa mapenzi Yangu? Haya ndiyo matakwa ya mwisho ambayo Nataka kutoka kwa mwanadamu, ambalo ni kusema, Natumai kwamba watu wote wanaweza kutoa ushuhuda wenye nguvu, unaovuma Kwangu mbele ya joka kubwa jekundu, kwamba waweze kujitolea wenyewe Kwangu kwa mara ya mwisho, na kutimiza matakwa Yangu kwa mara nyingine ya mwisho. Je, nyinyi mnaweza kufanya hili kweli? Nyinyi hamkuweza kuuridhisha moyo Wangu katika siku zilizopita—je, mnaweza kuvunja mpangilio huu katika mara ya mwisho? Nawapatia watu fursa ya kutafakari, Nawaacha watafakari kwa makini kabla ya kunipa jibu hatimaye—je, ni kosa kufanya hivi? Nasubiri jibu la mwanadamu, Nangoja “barua yake ya kujibu”—je, nyinyi mna imani ya kutimiza matakwa Yangu?
Aprili 20, 1992