Njia … (5)
Hapo zamani, hakuna aliyemjua Roho Mtakatifu, sembuse kujua njia iliyotembelewa na Roho Mtakatifu. Hiyo ndiyo sababu watu daima wamejipumbaza mbele za Mungu. Ni sawa kusema kwamba karibu kila mtu anayemwamini Mungu hamjui Roho, na kwamba imani yao imekanganyika na kutatizika. Ni dhahiri kwamba watu hawamwelewi Mungu; na ingawa kwa vinywa vyao wanaweza kusema kwamba wanamwamini, kimsingi, kwa kutegemeza tabia yao, wanajiamini, sio Mungu. Katika yale ambayo kwa kweli Nimeyapitia mwenyewe, Nimeona kwamba Mungu anamshuhudia Mungu mwenye mwili, na kutoka nje inaonekana kuwa watu wamelazimishwa kukiri ushuhuda wa Mungu, kwa kiwango kidogo sana inaweza kusemekana kuwa wanaamini kwamba Roho wa Mungu hana makosa hata kidogo. Hata hivyo, Nasema kwamba kile ambacho watu wanaamini si mtu huyu, sembuse Roho wa Mungu, ila ni hisia zao wenyewe. Je, hawajiamini tu kwa kufanya hilo? Nisemacho ni ukweli. Mimi siwabandiki watu majina, lakini kuna jambo moja ambalo lazima Nieleze wazi: Ili watu waletwe hadi leo, iwe wameelewa ama wamekanganyikiwa, yote ni kwa ajili ya Roho Mtakatifu. Silo jambo ambalo wanadamu wanaweza kulidhibiti. Huu ni mfano wa kile Nilichotaja awali kuhusu Roho Mtakatifu kulazimisha imani ya watu; hii ndiyo njia ambayo Roho Mtakatifu hufanya kazi, na ndiyo njia aliyoichukua Roho Mtakatifu. Bila kujali yule ambaye watu wanamwamini kimsingi, Roho Mtakatifu huwapa watu hisia fulani kwa lazima, Akiwafanya wamwamini Mungu mioyoni mwao. Je, hivyo sivyo unavyoamini? Je, huhisi kwamba imani yako katika Mungu ni jambo la ajabu? Je, hudhani kuwa ni jambo lisilo la kawaida kwamba huwezi kuepuka mkondo huu? Je, hujatia juhudi yoyote katika kulifikiria hili? Je, huu si muujiza na ishara kubwa zaidi kati ya yote? Hata kama umekuwa na hamu kubwa ya kuhepa mara nyingi, daima kuna nishati uhai yenye nguvu inayokuvutia na kukufanya usite kuondoka. Na kila wakati unapojipata katika hali kama hizi, unaanza kulia na kutoa machozi kila wakati, usijue cha kufanya baada ya hapo. Wengine wenu hujaribu kuondoka, lakini unapojaribu kuenda, unahisi uchungu sana, unahisi kana kwamba zimwi fulani wa dunia ameichukua nafsi yako kutoka kwako, akiuacha moyo wako bila utulivu na bila amani. Baada ya hapo, huna budi ila kujikaza na kumrudia Mungu. ... Je, hujapitia hili? Sina shaka kwamba ndugu wadogo, wanaoweza kuifungua mioyo yao watasema: “Ndiyo! Nimepitia hili mara nyingi sana, naaibika kuliwaza!” Katika maisha Yangu mwenyewe ya kila siku, daima Nina furaha kuwachukulia ndugu Zangu kama wandani Wangu, kwa sababu hawana hatia hata kidogo—wao hawana madoa na ni wazuri sana. Wao ni kama marafiki Wangu. Hiyo ndiyo maana daima Natafuta nafasi ya kuwaleta pamoja wandani Wangu wote ili kuzungumzia mawazo yetu na mipango yetu. Mapenzi ya Mungu na yatimike ndani yetu ili sote tuwe ndugu wa karibu, bila vikwazo ama umbali kati yetu. Na sote tumwombe Mungu: “Ee Mungu! Ikiwa ni mapenzi Yako, tunakusihi Utupe mazingira yanayofaa, ili tuweze kutimiza matakwa Yako mioyoni mwetu. Utuhurumie sisi vijana tusio na mantiki, na uturuhusu tutumie nguvu iliyo ndani ya mioyo yetu!” Naamini kwamba haya ni mapenzi ya Mungu, kwani zamani za kale Nilimwomba Mungu na kusema: “Baba! Duniani, tunakulilia bila kikomo, tukitaka mapenzi Yako yaweze kufanyika duniani hivi karibuni. Ningependa kutafuta mapenzi Yako. Na Ufanye utakacho kufanya na Ukamilishe agizo Lako ndani Yangu kwa haraka sana. Hata Niko tayari kwa Wewe kufungua njia mpya miongoni mwetu, ikiwa hili litamaanisha kwamba mapenzi Yako yatatimika karibuni! Naomba tu kwamba kazi Yako iweze kukamilika karibuni, na Naamini kwamba hakuna sheria zinazoweza kuizuia!” Kazi ya Mungu iko hivi leo; je, huoni njia ambayo Roho Mtakatifu anaitembelea? Kila wakati Ninapokutana na ndugu wenye umri mkubwa, Nahisi kukandamizwa sana. Ninapokutana nao, Naona kwamba wanadhihirisha jamii; fikira zao za kidini, uzoefu wao wa kuyashughulikia mambo, namna yao ya kuzungumza, maneno wanayoyatumia, na kadhalika—wote wanaudhi. Wanakisiwa kuwa na “hekima.” Daima huwa Najitenga nao kabisa, kwa sababu Mimi binafsi sijajihami kwa falsafa za kuishi duniani. Kila wakati Nikutanapo na watu hawa, wananiacha Nikiwa nimechoka, kichwa Changu kikijawa jasho; wakati mwingine Nahisi kukandamizwa sana kiasi kwamba Naishiwa na pumzi. Hivyo katika wakati huu wa hatari, Mungu ananipa suluhisho zuri. Huenda ni kuelewa Kwangu vibaya tu. Najali tu kuhusu linalomfaidi Mungu; lililo muhimu zaidi ni kufanya mapenzi ya Mungu. Najitenga kabisa na watu hawa, lakini ikiwa Mungu ananihitaji kukutana nao, bado Natii. Si kwamba wao wanasinya, ila kuwa “hekima,” fikira na falsafa zao za kuishi duniani zinachukiza sana. Niko hapo ili kukamilisha agizo la Mungu, sio kujifunza jinsi wanavyofanya mambo. Nakumbuka jinsi Mungu alivyowahi kuniambia, “Duniani, tafuta tu kufanya mapenzi ya Baba Yako na Ukamilishe agizo Lake. Hakuna jingine linalokuhusu.” Napata amani kidogo Ninapolifikiria hili. Hiyo ni kwa sababu masuala ya binadamu daima hunitatiza sana; Siwezi kuyaelewa, na kamwe Sijui la kufanya. Kwa hivyo nyakati nyingi Nimehangaishwa na hili na Nimewachukia wanadamu; mbona watu lazima wawe wagumu sana? Mbona hawawezi kuwa wa kawaida? Mbona mtu ajaribu kuwa mjanja sana? Nikutanapo na watu, wakati mwingi kunategemezwa kwa agizo la Mungu Kwangu. Kunaweza kuwa na nyakati chache ambapo hali haikuwa hivyo, lakini ni nani ajuaye kilichofichika katika vina vya moyo Wangu?
Mara nyingi Nimewashauri ndugu walio nami kwamba wanapaswa kumwamini Mungu kwa dhati, kwamba hawapaswi kujali masilahi yao wenyewe, ila wayazingatie mapenzi ya Mungu. Mara nyingi Nimelia kwa uchungu mbele za Mungu: Mbona watu hawayazingatii mapenzi ya Mungu? Hakika kazi ya Mungu haiwezi tu kutoweka isionekane tena bila sababu? Wala Sijui mbona—hili limekaribia kuwa fumbo akilini Mwangu—mbona watu hawaitambui njia iliyotembelewa na Roho Mtakatifu kamwe, lakini wanaendelea kuyashikilia mahusiano yasiyo ya kawaida waliyo nayo na wengine? Nachafuka moyo Niwaonapo watu wakiwa namna hii. Badala ya kuitumainia njia ya Roho Mtakatifu, wanalenga matendo ya mwanadamu. Je, Mungu anaweza kuridhishwa na hili? Mara nyingi huwa Nasikitishwa na hili. Limekaribia kuwa mzigo Wangu—na linamsumbua Roho Mtakatifu pia. Je, huhisi lawama yoyote moyoni mwako? Naomba Mungu afungue macho ya roho yako. Mara nyingi Mimi, Ninayewaongoza watu kuingia katika kazi ya Mungu, Nimeomba mbele za Mungu: “Ee Baba! Ningependa mapenzi Yako yawe kiini, Ningependa kutafuta mapenzi Yako, Ningependa kwamba Niwe mwaminifu kwa agizo Lako, ili Uweze kulipata kundi hili la watu. Nakuomba Utupeleke katika nchi ya uhuru, ili tuweze kukugusa kwa roho Zetu, na Naomba Uzindue hisia za kiroho zilizo mioyoni mwetu!” Ningependa kwamba mapenzi ya Mungu yatimike, na kwa hiyo Naomba bila kikomo kwamba Roho Wake aendelee kutupa nuru, kwamba tuweze kuitembea njia inayoongozwa na Roho Mtakatifu—kwani njia Niitembeayo ni njia ya Roho Mtakatifu. Na ni nani mwingine anayeweza kuitembea njia hii badala Yangu? Hili ndilo linaloufanya mzigo Wangu kuwa mzito hata zaidi. Nahisi kana kwamba Ninakaribia kuanguka, lakini Nina imani kwamba Mungu hawezi kamwe kuchelewesha kazi Yake. Huenda tutatengana tu mara agizo Lake litakapokamilishwa. Kwa hiyo labda ni kwa sababu ya matokeo ya Roho wa Mungu ndiyo daima Nimehisi tofauti. Ni kana kwamba kuna kazi ambayo Mungu anataka kufanya, lakini bado Siwezi kuelewa ni ipi. Lakini Naamini kwamba hakuna mtu duniani aliye bora kuliko wandani Wangu, na Naamini kwamba wataniombea mbele za Mungu, na kwa sababu ya hilo Nina shukrani isiyo na kipimo. Ningewataka ndugu Zangu waseme nami: “Ee Mungu! Na mapenzi Yako yadhihirike kikamilifu ndani yetu sisi, watu wa enzi ya mwisho, ili tuweze kubarikiwa na uzima wa roho, na kutazama matendo ya Roho wa Mungu, na kuutazama uso Wake wa kweli!” Punde tunapofikia hatua hii kweli tutakuwa tukiishi chini ya mwongozo wa Roho, na hapo tu ndipo tutaweza kuutazama uso wa kweli wa Mungu. Yaani, watu wataweza kuelewa maana halisi ya ukweli wote, sio kufahamu ama kuelewa kulingana na fikira za binadamu, ila kulingana na nuru ya mapenzi ya Roho wa Mungu. Hii yote ni kazi ya Mungu Mwenyewe, hakuna lolote litokalo katika mawazo ya binadamu ndani yake; ni mpango Wake wa kazi kwa ajili ya matendo Anayotaka kudhihirisha duniani, na ndiyo sehemu ya mwisho ya kazi Yake duniani. Je, ungependa kujiunga na kazi hii? Je, unataka kujihusisha nayo? Je, unatamani kukamilishwa na Roho Mtakatifu na kushiriki katika uzima wa roho?
Kilicho muhimu leo ni kuingia kwa kina zaidi kutoka kwa msingi wetu wa asili. Lazima tuingie kwa kina zaidi katika ukweli, maono, na uzima—lakini kwanza lazima Niwakumbushe ndugu kwamba ili kuiingia hatua hii ya kazi, lazima uachane na fikira zako za awali. Yaani, lazima ubadili jinsi unavyoishi, ufanye mipango mipya, ujirekebishe na kuanza upya. Ikiwa bado unashikilia kile kilichokuwa cha thamani kwako zamani, Roho Mtakatifu hataweza kufanya kazi ndani yako, na Atakimu maisha yako kwa shida. Wale ambao hawafuatilii, ama kuingia, ama kupanga wataachwa kabisa na Roho Mtakatifu—na kwa hivyo wanasemekana kwamba wametelekezwa na enzi. Natumai kwamba ndugu wote wanaweza kuuelewa moyo Wangu, na Natumai kwamba “wanachama wapya” watasimama kushirikiana na Mungu na wakamilishe kazi hii pamoja. Naamini kwamba Mungu atatubariki. Naamini pia kwamba Mungu atanipa wandani wengi zaidi, ili Niweze kutembea kwa kila pembe ya dunia, na kuweza kuwa na upendo mkubwa zaidi kati yetu. Aidha, Naamini kwamba Mungu ataueneza ufalme Wake kwa sababu ya juhudi zetu; Ningependa kwamba hizi juhudi zetu zifike viwango ambavyo havijawahi kufikiwa awali, zikimruhusu Mungu awapate vijana zaidi. Ningependa tutumie muda zaidi tukiombea hili, Ningependa tuombe bila kukoma, ili tuishi maisha yetu yote mbele za Mungu, na tuwe karibu iwezekanavyo na Mungu. Naomba kusiwe na chochote kati yetu tena, na naomba sote tukule kiapo hiki mbele za Mungu: Kufanya kazi pamoja kwa bidii! Kuwa waaminifu hadi mwisho kabisa! Kutowahi kutengana, na kuwa pamoja daima! Natumai kwamba ndugu wote watoe ahadi hii mbele za Mungu, ili mioyo yetu isibadilike kamwe, na azma yetu isiyumbayumbe kamwe! Kwa ajili ya mapenzi ya Mungu, Nasema tena: Tufanye kazi kwa bidii! Tujitahidi kwa uwezo wetu wote! Hakika Mungu atatubariki!