Utendaji (3)
Lazima muwe na uwezo wa kuishi kwa kujitegemea, wa kula na kunywa maneno ya Mungu ninyi wenyewe, kupitia maneno ya Mungu ninyi wenyewe, na kuishi maisha ya kawaida ya kiroho bila uongozi wa wengine. Lazima muweze kuyategemea maneno ambayo Mungu ananena leo ili muishi, ili muingie katika uzoefu wa kweli, na kupata umaizi wa kweli. Ni kwa kufanya hivi tu ndiyo mtaweza kusimama imara. Leo, watu wengi hawaelewi kikamilifu majonzi na majaribu ya siku za usoni. Katika siku za usoni, watu wengine watapitia majonzi, na wengine watapitia adhabu. Adhabu hii itakuwa kali zaidi; itakuwa ni kuwasili kwa ukweli. Leo, yote unayopitia, kutenda, na kuonyesha yanaweka msingi wa majaribu ya siku za usoni, na kwa kiwango cha chini mno, lazima uweze kuishi kwa kujitegemea. Leo, hali inayohusu wengi kanisani ni kama ifuatayo kwa jumla: Ikiwa kuna viongozi na wafanyakazi wa kufanya kazi hiyo, wao huwa na furaha, na ikiwa hawapo, wao hukosa furaha. Wao hawatilii maanani kazi ya kanisa, wala kwa maisha yao wenyewe ya kiroho, na hawana hata mzigo kidogo kabisa—wao huboronga tu kama ndege wa Hanhao.[a] Kusema kweli, ndani ya watu wengi kazi ambayo Nimefanya ni kazi ya ushindi tu, kwani wengi hawastahili kimsingi kufanywa wakamilifu. Ni sehemu ndogo tu ya watu ndio wanaweza kufanywa wakamilifu. Ikiwa, baada ya kuyasikia maneno haya, unawaza “kwa kuwa kazi inayofanywa na Mungu ni kwa ajili tu ya kuwashinda watu, nitafuata tu kwa uzembe,” mwelekeo wa aina hiyo ungewezaje kukubalika? Ikiwa kweli unamilikiwa na dhamiri, basi lazima uwe na mzigo, na hisia ya kuwajibika. Lazima useme: “Iwe nitashindwa au kufanywa mkamilifu, lazima niwe na hatua hii ya ushuhuda kwa kufaa.” Kama kiumbe wa Mungu, mtu anaweza kushindwa kabisa na Mungu, na hatimaye, mtu anakuwa na uwezo wa kumridhisha Mungu, kulipa upendo wa Mungu kwa moyo wenye upendo kwa Mungu na kwa kujitolea mwenyewe kabisa kwa Mungu. Hili ni jukumu la mwanadamu, ni wajibu unaopaswa kutekelezwa na mwanadamu, na ni mzigo unaopaswa kubebwa na mwanadamu, na mwanadamu lazima atimize agizo hili. Ni wakati huo tu ndipo atakuwa anaamini katika Mungu kwa hakika. Leo, kile unachofanya kanisani ni timizo la wajibu wako? Hili linategemea na kama umebeba mzigo, na inategemea maarifa yako mwenyewe. Katika kuipitia kazi hii, ikiwa mwanadamu anashindwa na ana maarifa ya kweli, basi ataweza kutii bila kujali matarajio au majaliwa yake mwenyewe. Kwa njia hii, kazi kuu ya Mungu itafanywa yote kabisa, kwani ninyi watu hamwezi kufanya lolote zaidi ya hili, na hamwezi kutimiza mahitaji yoyote ya juu zaidi. Ilhali katika siku za usoni, watu wengine watafanywa wakamilifu. Ubora wao wa tabia utakuwa mzuri zaidi, ndani ya roho zao watakuwa na maarifa ya kina zaidi, na maisha yao yatakua.... Ilhali wengine hawawezi kabisa kulitimiza hili, na hivyo hawawezi kuokolewa. Kuna sababu ya Mimi kusema kwamba hawawezi kuokolewa. Katika siku za usoni, wengine watashindwa, wengine wataondoshwa, wengine watafanywa wakamilifu, na wengine watatumiwa—na kwa hiyo wengine watapitia majonzi, wengine watapitia adhabu (majanga ya asilia pamoja na misiba inayosababishwa na mwanadamu), wengine wataondoshwa, na wengine watasalia. Katika hili, kila mmoja ataainishwa kulingana na aina, na kila kikundi kikiwakilisha aina ya mtu. Sio watu wote wataondoshwa, wala watu wote kufanywa wakamilifu. Hili ni kwa sababu ubora wa tabia wa watu wa China ni duni sana, na kuna idadi ndogo tu miongoni mwao walio na aina ya kujitambua ambayo Paulo alikuwa nayo. Miongoni mwenu, wachache wana azimio la kumpenda Mungu sawa na alilokuwa nalo Petro, au imani ya aina sawa na aliyokuwa nayo Ayubu. Kuna wachache sana kati yenu wanaomcha na kumtumikia Yehova kama alivyofanya Daudi, wale walio na kiwango sawa cha uaminifu. Mnasikitisha jinsi gani!
Leo, mazungumzo juu ya kufanywa mkamilifu ni kipengele kimoja tu. Haijalishi kinachofanyika, lazima muwe na hatua hii ya ushuhuda kwa kufaa. Kama mngeulizwa mumhudumie Mungu katika hekalu, mngefanyaje hivyo? Kama hungekuwa kuhani, na hungekuwa na cheo cha wana wazaliwa wa kwanza au wana wa Mungu, bado ungeweza kuwa mwaminifu? Bado ungeweza kutumia juhudi zako katika kazi ya kuupanua ufalme? Bado ungeweza kufanya kazi ya agizo la Mungu inavyofaa? Haijalishi jinsi ambavyo maisha yako yamekua, kazi ya leo itakusababisha uridhishwe kabisa ndani yako, na uweke kando fikira zako zote. Kama kile una kinachohitajika kuyafuatilia maisha au la, kazi ya Mungu itakufanya uridhike kabisa. Watu wengine husema: “Naamini katika Mungu, na sielewi ni nini maana ya kuyafuatilia maisha.” Na wengine husema: “Mimi nimetatanishwa katika imani yangu kwa Mungu. Najua kwamba siwezi kufanywa mkamilifu, kwa hivyo niko tayari kuadibiwa.” Hata watu kama hawa, ambao wako tayari kuadibiwa au kuangamizwa, lazima washurutishwe kukubali kwamba kazi ya leo inafanywa na Mungu. Watu wengine pia husema: “Siombi kufanywa mkamilifu, lakini, leo, niko radhi kukubali mafundisho yote ya Mungu, na niko radhi kuishi kwa kudhihirisha ubinadamu wa kawaida, kuendeleza ubora wa tabia yangu, na kutii mipango yote ya Mungu….” Katika hili, wao pia wameshindwa na kuwa na ushuhuda, ambalo linathibitisha kwamba kuna maarifa fulani kuhusu kazi ya Mungu ndani ya watu hawa. Hatua hii ya kazi imetekelezwa haraka kabisa, na katika siku za usoni, itatekelezwa hata kwa haraka zaidi huko ng’ambo. Leo, watu walio ng’ambo hawawezi kungoja, wote wanakimbilia Uchina—na kwa hiyo ikiwa hamwezi kufanywa wakamilifu, mtakuwa mnawashikilia watu walio ng’ambo. Wakati huo, haijalishi mumeingia vizuri kwa namna gani au jinsi mlivyo, wakati utakapofika kazi Yangu itahitimishwa na kutimizwa. Kazi Yangu haitacheleweshwa na ninyi. Nafanya kazi ya wanadamu wote, na hakuna haja ya Mimi kutumia muda wowote zaidi kwenu! Ninyi ni msio na motisha kabisa, mnaokosa kujitambua kabisa! Hamstahili kufanywa wakamilifu—mna uwezo mdogo sana! Katika siku za usoni, hata watu wakiendelea kuwa wazembe na hobelahobela sana, na kubaki wasioweza kuboresha ubora wao wa tabia, hili halitazuia kazi ya ulimwengu mzima. Wakati ukifika wa kazi ya Mungu kumalizika, itamalizika, na wakati ukifika wa watu kuondoshwa, wataondoshwa. Bila shaka, wale wanaopaswa kufanywa wakamilifu, na wanastahili kufanywa wakamilifu, pia watafanywa wakamilifu—lakini ikiwa hamna tumaini kabisa, basi kazi ya Mungu haitawangoja ninyi! Hatimaye, ukishindwa, hili pia linaweza kufikiriwa kama kuwa na ushuhuda. Kuna mipaka kwa kile ambacho Mungu anahitaji kutoka kwenu; urefu ule wa kimo ambacho mwanadamu anaweza kutimiza ndio, urefu wa ushuhuda unaotakiwa kutoka kwake. Sio kama anavyofikiria mwanadamu kwamba ushuhuda kama huo utafikia mipaka ya juu zaidi na kwamba utakuwa mkubwa sana—hakuna vile ambavyo hili linaweza kutimizwa ndani ya ninyi watu wa China. Nimeshirikiana nanyi kwa wakati huu wote, na ninyi wenyewe mmeona hili: Nimewaambia msipinge, msiwe waasi, msifanye mambo yanayosababisha usumbufu au yanayovuruga bila Mimi kufahamu. Nimewakosoa watu moja kwa moja kuhusu hili mara nyingi, lakini hata hilo halitoshi—punde tu wanapogeuka wao hubadilika, huku wengine hunipinga Mimi kisirisiri, bila majuto yoyote. Unadhani sijui lolote kuhusu hili? Unadhani unaweza kunisababishia Mimi matatizo na hakuna kitakachotokea? Unadhani sijui unapojaribu kubomoa kazi Yangu bila Mimi kufahamu? Unadhani kwamba hila zako ndogo zinaweza kushikilia nafasi ya hulka yako? Wewe kila mara unaonekana kuwa mtiifu lakini wewe ni mdanganyifu kisirisiri, unaficha mawazo mabaya ndani ya moyo wako, na hata kifo si adhabu ya kutosha kwa watu kama wewe! Unadhani kwamba kazi kidogo inayofanywa na Roho Mtakatifu ndani yako inaweza kuchukua nafasi ya uchaji wako Kwangu? Unafikiri ulipata nuru kupitia kwa kuiita Mbinguni? Wewe huna aibu! Wewe huna thamani kabisa! Unafikiria kwamba “matendo yako mema” yalikuwa ya kuigusa Mbinguni sana, na kwamba kwa sababu hiyo Alifanya jambo la pekee na kukupa kiasi kidogo cha vipawa, vilivyokufanya uwe na lugha ya kushawishi, iliyokukubalia kuwadanganya wengine, na kunidanganya Mimi? Wewe ni mpumbavu kweli! Je, wajua mahali ambapo nuru yako inatoka? Je, hujui ulikula chakula cha nani ulipokuwa unakua? Wewe ni wa kupita kiasi kweli! Wengine miongoni mwenu hawajabadilika hata baada ya miaka minne au mitano ya kushughulikiwa na mnaelewa kuhusu mambo haya. Mnapaswa kuelewa asili yenu, na msipinge wakati ambapo, siku moja, mtatelekezwa. Wengine, ambao hudanganya wale walio juu na walio chini yao katika huduma yao, wameshughulikiwa sana; wengine, kwa sababu ni wenye tamaa ya pesa, wameshughulikiwa kwa kiasi kikubwa; wengine, kwa sababu hawaweki mipaka iliyo wazi baina ya wanaume na wanawake, pia wameshughulikiwa mara kwa mara; wengine kwa sababu ni wavivu, wanaofikiria tu juu ya mwili, na hawatendi kulingana na kanuni wanapotenda makanisa, wameshughulikiwa kwa kiasi kikubwa; wengine kwa sababu wao hukosa kuwa na ushuhuda popote waendapo, na hutenda kwa ukaidi na purukushani, na hata kufanya dhambi kwa makusudi, wameonywa mara nyingi kuhusu hili; wengine ambao huzungumza tu kuhusu maneno na mafundisho wakati wa mikutano, wakijiona kuwa wa cheo cha juu kuliko wengine wote, wakikosa uhalisi hata kidogo kabisa wa ukweli, na kupanga njama dhidi ya kina ndugu na kupingana nao—wamefichuliwa mara kwa mara kwa sababu ya hili. Nimezungumza maneno haya kwenu mara nyingi sana, na leo, Sitazungumza tena kuhusu hili—fanyeni mtakalo! Fanyeni uamuzi wenu wenyewe! Watu wengi hawajapitia kushughulikiwa kwa namna hii kwa mwaka mmoja au miwili tu, kwa wengine imekuwa miaka mitatu au minne, huku wengine wamepitia hili kwa zaidi ya muongo mmoja, wakiwa wamepitia kushughulikiwa walikuwa waumini, lakini kufikia sasa kumekuwa na mabadiliko madogo ndani yao. Unasemaje nini, wewe sio kama nguruwe? Inaweza kuwa kwamba Mungu anawaonea? Usifikiri kwamba kazi ya Mungu haitamalizika ikiwa hamwezi kufikia kiwango fulani. Je, Mungu bado atawangoja ikiwa hamwezi kutimiza matakwa Yake? Nawaambia waziwazi—hali si hivyo tena! Usiwe na mtazamo kama huo wa kutia matumaini kuhusu mambo! Kuna kipimo kwa kazi ya leo hii, na Mungu hachezi tu na wewe! Hapo awali, ilipofikia kupitia jaribu la watendaji huduma, watu walifikiri kwamba kwa wao kusimama imara katika ushuhuda wao kwa Mungu na kushindwa na Yeye, walitakiwa kufikia kiwango fulani—walitakiwa kuwa watendaji huduma kwa hiari na kwa furaha, na walitakiwa kumsifu Mungu kila siku, na wasiwe wajeuri au wenye harara hata kidogo. Walifikiri kwamba ni wakati huo tu ndipo wangekuwa watendaji huduma kweli, lakini hali ni hiyo kwa kweli? Wakati huo, watu wa aina mbali mbali walifichuliwa; walionyesha tabia za kila aina. Wengine walitoa malalamiko, wengine walikuwa na fikira, wengine waliacha kuhudhuria mikutano, na wengine hata waligawa pesa za kanisa. Kina ndugu walikuwa wakila njama dhidi ya wengine. Ulikuwa ukombozi mkubwa kweli, lakini kulikuwa na kitu kimoja kizuri kulihusu: Hakuna aliyerudi nyuma. Hii ndiyo iliyokuwa hoja kubwa zaidi. Walikuwa na hatua ya ushuhuda mbele ya Shetani kwa sababu ya hili, na baadaye walipata utambulisho wa watu wa Mungu na wamefaulu hata kufikia leo. Kazi ya Mungu haitekelezwi unavyofikiria, badala yake, muda ukiisha, kazi hiyo itaisha, bila kujali umefikia hatua gani. Watu wengine huenda wakasema: “Kwa kutenda hivi Huwaokoi watu, au kuwapenda—Wewe si Mungu mwenye haki.” Nakwambia waziwazi: Kiini cha kazi Yangu leo ni kukushinda wewe na kukufanya uwe na ushuhuda. Kukuokoa wewe ni nyongeza tu; kama unaweza kuokolewa au la hutegemea ufuatiliaji wako mwenyewe, na hakuhusiani na Mimi. Ilhali lazima Nikushinde wewe; usijaribu kila mara kunidhibiti Mimi—leo Ninakufinyanga na kukuokoa, si vinginevyo!
Leo, kile ambacho mmepata kuelewa ni cha juu zaidi kuliko kile cha mtu yeyote kote katika historia ambaye hakufanywa mkamilifu. Iwe ni ufahamu wenu wa majaribu au imani katika Mungu, vyote ni vya juu zaidi kuliko ya muumini yeyote katika Mungu. Mambo mnayoyafahamu ni yale mnayokuja kujua kabla ya ninyi kupitia majaribu ya mazingira, lakini kimo chenu halisi hakipatani nayo. Kile mnachojua ni cha juu zaidi kuliko kile mnachotia katika vitendo. Ingawa mnasema kwamba watu wanaoamini katika Mungu wanapaswa kumpenda Mungu, na hawapaswi kupania baraka bali kuyaridhisha tu mapenzi ya Mungu, kinachoonekana katika maisha yenu ni tofauti kabisa na hili, na kimewekwa mawaa kabisa. Watu wengi huamini katika Mungu kwa ajili ya amani na manufaa mengine. Isipokuwa kwa manufaa yako, wewe huamini katika Mungu, na ikiwa huwezi kupokea neema za Mungu, wewe huanza kununa. Kile ambacho umesema kingekuwaje kimo chako halisi? Inapofikia matukio ya familia yasiyoepukika kama vile watoto kuwa wagonjwa, wapendwa kulazwa hospitalini, mazao mabaya ya mimea, na kuteswa na watu wa familia, hata mambo haya yanayotokea mara kwa mara, ya kila siku yanakuwa ya kukithiri kwako. Wakati ambapo mambo hayo hufanyika, wewe huingia katika hofu kubwa, hujui la kufanya—na wakati mwingi, wewe hulalamika kuhusu Mungu. Wewe hulalamika kwamba maneno ya Mungu yalikuhadaa, kwamba kazi ya Mungu yalikudhihaki. Je, ninyi hamna mawazo kama haya? Unadhani mambo kama haya hufanyika miongoni mwenu mara chache tu? Mnatumia kila siku kuishi katikati ya matukio kama haya. Hamfikirii hata kidogo sana kuhusu mafanikio ya imani yenu katika Mungu, na namna ya kuyaridhisha mapenzi ya Mungu. Kimo chenu halisi ni kidogo sana, hata kidogo zaidi kuliko cha kifaranga mdogo. Wakati ambapo biashara ya familia zenu hupoteza pesa ninyi hulalamika kuhusu Mungu, wakati ambapo ninyi hujikuta katika mazingira yasiyo na ulinzi wa Mungu ninyi bado hulalamika kuhusu Mungu, na ninyi hulalamika hata wakati ambapo mmoja wa vifaranga wenu hufa au ng’ombe mzee ndani ya zizi anapougua. Ninyi hulalamika kama ni wakati wa wana wenu kufunga ndoa lakini familia yenu haina pesa za kutosha; unataka kutekeleza kazi ya kanisa ya kuwa mwenyeji, lakini huwezi kuimudu, na kisha wewe hulalamika pia. Umejawa na malalamiko, na wakati mwingine huhudhurii mikutano au kula na kunywa maneno ya Mungu kwa sababu ya hili, wakati mwingine wewe huishia kuwa hasi kwa muda mrefu sana. Hakuna chochote kinachokufanyikia leo hii kilicho na uhusiano wowote na matazamio au majaliwa yako; mambo haya yangefanyika pia hata ikiwa hungeamini katika Mungu, ilhali leo hii unampitishia Mungu wajibu wa haya mambo, na kusisitiza kusema kwamba Mungu amekuondosha wewe. Na kuhusu imani yako katika Mungu, je? Umeyatoa maisha yako kwa kweli? Mngepitia majaribu sawa na yale ya Ayubu, hakuna hata mmoja miongoni mwenu anayemfuata Mungu leo hii angeweza kusimama imara, nyote mngeanguka chini. Na kunayo, kawaida kabisa, tofauti kubwa kati ya ninyi na Ayubu. Leo, kama nusu ya mali yenu ingetwaliwa mngethubutu kukana kuwepo kwa Mungu; kama mtoto wenu wa kiume au wa kike angechukuliwa kutoka kwenu, mngekimbia barabarani mkilalamika vikali; kama njia yako ya pekee kupata riziki ingegonga mwamba, ungejaribu kuanza kujadiliana mada hiyo na Mungu; ungeuliza kwa nini Nilisema maneno mengi sana hapo mwanzo kukutisha wewe. Hakuna kitu chochote ambacho hamngethubutu kufanya katika nyakati kama hizi. Hili linaonyesha kwamba hamjapata umaizi wowote wa kweli, na hamna kimo cha kweli. Hivyo, majaribu yaliyo ndani yenu ni makubwa mno, kwani ninyi mnajua mengi sana, lakini kile mnachoelewa kweli si hata sehemu moja kwa elfu ya kile mnachofahamu. Msikome tu kwa ufahamu na maarifa pekee; mngeona vyema kiasi gani mnachoweza kutia katika vitendo kwa kweli, kiasi gani cha nuru na mwangaza wa Roho Mtakatifu kilipatikana kupitia katika jasho la bidii yenu wenyewe, na katika matendo mangapi yenu mmetambua azimio lenu wenyewe. Unapaswa kuchukua kimo chako na kutenda kwa uzito. Katika imani yako kwa Mungu, hupaswi tu kujaribu kufanya mambo kwa namna isiyo ya dhati kwa ajili ya yeyote—kama unaweza hatimaye kupata ukweli na uzima au la hutegemea ufuatiliaji wako mwenyewe.
Tanbihi:
a. Hadithi ya ndege wa Hanhao inafanana sana na hekaya ya Aesop ya mchwa na panzi. Ndege wa Hanhao anapendelea kulala badala ya kujenga kiota wakati hali ya hewa ni ya vuguvugu—licha ya maonyo ya tena na tena kutoka kwa jirani yake, ndege wa jamii ya kunguru. Wakati ambapo majira ya baridi kali hufika, ndege huyo huona baridi sana hadi kufa.