Je, Wajua? Mungu Amefanya Jambo Kubwa Miongoni Mwa Binadamu
Enzi ya zamani imepita, na enzi mpya imekuja. Mwaka baada ya mwaka na siku baada ya siku, Mungu amefanya kazi nyingi. Alikuja duniani na kisha Akaondoka. Mzunguko huu umejirudia kupitia vizazi vingi. Leo, Mungu anaendelea, kama awali, kufanya kazi Anayopaswa kufanya, kazi ambayo bado Hajaikamilisha, kwani hadi leo, bado Hajaingia mapumzikoni. Kutoka wakati wa uumbaji hadi leo, Mungu amefanya kazi nyingi. Lakini, je, ulijua kwamba leo Mungu anafanya kazi nyingi zaidi kuliko awali, na mawanda ya kazi Yake ni ya juu zaidi kuliko awali? Hii ndiyo maana Ninasema kwamba Mungu amefanya jambo kubwa miongoni mwa binadamu. Kazi zote za Mungu ni muhimu sana, iwe kwa mwanadamu ama Mungu, kwani kila kipengele cha kazi Yake kina uhusiano na mwanadamu.
Kwa kuwa kazi ya Mungu haiwezi kuonekana wala kuguswa—sembuse kuonwa na ulimwengu—inawezaje kuwa kitu kikubwa? Ni jambo la aina gani hasa ndilo lingechukuliwa kuwa kubwa? Hakika, hakuna anayeweza kukataa kuwa, haijalishi kazi ambayo Mungu anafanya, inaweza kuchukuliwa kuwa kubwa, lakini kwa nini Ninasema hili kuhusu kazi anayofanya Mungu leo? Ninaposema kwamba Mungu amefanya kitu kikubwa, hili bila shaka linahusisha siri nyingi ambazo mwanadamu bado hajazielewa. Acha tuzizungumzie sasa.
Yesu alizaliwa horini katika enzi ambayo haingevumilia kuwepo Kwake, lakini hata hivyo, dunia haikuweza kumzuia, na Aliishi miongoni mwa binadamu kwa miaka thelathini na tatu chini ya utunzaji wa Mungu. Katika miaka hii mingi ya maisha, Alipitia uchungu wa dunia na Akaonja maisha ya taabu duniani. Alijitwika mzigo mzito wa kusulubiwa ili kuwakomboa wanadamu wote. Aliwakomboa wote wenye dhambi walioishi chini ya nguvu za Shetani, na mwishowe, mwili Wake uliofufuka ukarudi mahali Pake pa mapumziko. Sasa kazi mpya ya Mungu imeanza, yaani, enzi mpya imeanza. Mungu anawaleta nyumbani Kwake wale ambao wamekombolewa na Anaanza kazi Yake mpya ya wokovu. Wakati huu, kazi ya wokovu ni kamilifu zaidi kuliko nyakati za nyuma. Si Roho Mtakatifu anayefanya kazi ndani ya mwanadamu kumsababisha abadilike yeye mwenyewe, wala si mwili wa Yesu unaojitokeza miongoni mwa binadamu kufanya kazi hii, na sembuse kazi hii kufanyika kupitia namna nyingine. Badala yake, ni Mungu mwenye mwili anayefanya kazi na kuielekeza Mwenyewe. Anaifanya kwa njia hii ili kumwongoza binadamu kuingia katika kazi mpya. Je, hili si jambo kubwa? Mungu hafanyi kazi hii kupitia baadhi ya wanadamu au kwa njia ya unabii; badala yake, Mungu anaifanya Mwenyewe. Wengine wanaweza kusema kuwa hili si jambo kubwa na kwamba haliwezi kumleta mwanadamu kwa hisia ya upeo wa furaha. Lakini Nitakwambia kwamba kazi ya Mungu siyo hii tu, ila ni kitu kikubwa zaidi na kingi zaidi.
Wakati huu, Mungu haji kufanya kazi kwa mwili wa kiroho, ila kwa ule wa kawaida sana. Zaidi ya hayo, ni mwili wa kupata mwili kwa Mungu mara ya pili, na pia ndio mwili ambao kwao Mungu anarudi katika mwili. Ni mwili wa kawaida sana. Ukimwangalia, huwezi kuona chochote kinachomfanya Aonekane tofauti na wengine, lakini unaweza kupata kutoka Kwake ukweli ambao haujawahi kusikika hapo awali. Mwili huu tu usio na umuhimu ni mfano halisi wa maneno yote ya Mungu ya ukweli, unaobeba kazi ya Mungu katika siku za mwisho, na maonyesho ambayo kwayo mwanadamu anaielewa tabia nzima ya Mungu. Je, hutamani sana kumwona Mungu aliye mbinguni? Je, hutamani sana kumwelewa Mungu aliye mbinguni? Je, hutamani sana kuona hatima ya binadamu? Atakwambia hizi siri zote—siri ambazo hakuna mwanadamu yeyote amewahi kuweza kukuambia—na pia Atakwambia ukweli ambao huelewi. Yeye ndiye lango lako kuingia katika ufalme, na ndiye mwelekezi wako wa kuingia katika enzi mpya. Mwili huu wa kawaida una siri nyingi zisizoweza kueleweka na mwanadamu. Matendo Yake hayafahamiki kwako, lakini lengo zima la kazi Anayofanya linatosha kukuwezesha kuona kwamba Yeye, kama watu wanavyoamini, si mwili wa kawaida tu, kwa sababu Yeye anawakilisha nia za Mungu katika siku za mwisho, na utunzaji wa Mungu kwa wanadamu katika siku za mwisho. Ingawa huwezi kusikia maneno Yake yakionekana kutikisa mbingu na ardhi, ingawa huwezi kuona macho Yake kama mwale wa moto, na ingawa huwezi kupokea adabu ya fimbo Yake ya chuma, hata hivyo unaweza kusikia kutoka katika maneno Yake kwamba Mungu ni mwenye ghadhabu na ujue kwamba Mungu anaonyesha rehema kwa wanadamu, na kuiona tabia ya haki ya Mungu na hekima Yake, na, hata zaidi ya hayo, kuthamini sana jinsi Mungu anavyowajali binadamu wote. Kazi ya Mungu katika siku za mwisho ni kumruhusu mwanadamu amwone duniani Mungu aliye mbinguni akiishi kati ya binadamu, na kumwezesha mwanadamu kumjua, kumtii, kumcha, na kumpenda Mungu. Hii ndiyo maana Amerudi katika mwili kwa mara ya pili. Ingawa kile ambacho mwanadamu anaona wakati huu ni Mungu ambaye ni sawa na mwanadamu, Mungu mwenye pua na macho mawili, na Mungu asiye wa ajabu sana, mwishowe, Mungu atawaonyesha kwamba kama mtu huyu hangekuwepo, mbingu na dunia zingepitia mabadiliko makubwa; kama mtu huyu hangekuwepo, mbingu zingefifia, dunia ingetumbukia katika machafuko, na wanadamu wote wangeishi katikati ya njaa na tauni. Atawaonyesha kwamba iwapo Mungu aliyefanyika mwili wa siku za mwisho hangekuja kuwaokoa, basi Mungu angekuwa amewaangamiza wanadamu wote jahanamu zamani; iwapo mwili huu haungekuwepo, basi ninyi mngekuwa wenye dhambi kubwa milele, na mngekuwa maiti milele. Mnapaswa kujua kwamba iwapo mwili huu haungekuwepo, isingewezekana kwa wanadamu wote kuepuka janga kuu, na isingewezekana kwao kuepuka adhabu kali zaidi ambayo Mungu huwapa wanadamu katika siku za mwisho. Kama mwili huu wa kawaida haungezaliwa, nyote mngekuwa katika hali ambayo mnaomba uzima bila kuweza kuishi na kuomba kifo bila kuweza kufa; kama mwili huu haungekuwepo, basi hamngeweza kupata ukweli na kuja mbele ya kiti cha enzi cha Mungu leo, bali, mngeadhibiwa na Mungu kwa sababu ya dhambi zenu za kusikitisha. Je, mnajua kwamba isingekuwa kwa ajili ya kurudi kwa Mungu katika mwili, kusingekuwa na nafasi ya wokovu kwa yeyote; na kama mwili huu haungekuja, Mungu angekuwa ameshakomesha enzi ya zamani? Hali ikiwa hivi, je, bado mtakataa kupata mwili kwa Mungu mara ya pili? Kwa kuwa mnaweza kupata faida kubwa namna hii kutoka kwa mtu huyu wa kawaida, kwa nini msimkubali kwa furaha?
Kazi ya Mungu ni jambo ambalo huwezi kuelewa. Kama huwezi kufahamu kikamilifu kama chaguo lako ni sahihi, wala huwezi kujua kama kazi ya Mungu inaweza kufaulu, basi mbona usijaribu bahati yako na uone iwapo huyu mtu wa kawaida anaweza kuwa wa msaada mkubwa kwako, na iwapo hakika Mungu amefanya kazi kubwa? Hata hivyo, lazima Nikwambie kuwa wakati wa Nuhu, binadamu alikuwa akila na kunywa, akifunga ndoa na kupeana katika ndoa kufikia hatua ambapo Mungu asingevumilia kushuhudia, hivyo, Aliachilia mafuriko makubwa kuangamiza wanadamu, Akiinusuru tu familia ya Nuhu ya watu wanane na aina zote za ndege na wanyama. Katika siku za mwisho, hata hivyo, wale walionusuriwa na Mungu ni wale wote ambao wamekuwa waaminifu Kwake hadi mwisho. Ingawa enzi zote mbili ni nyakati za upotovu mkubwa ambao ni usiovumilika kwa Mungu kushuhudia, na binadamu katika enzi zote mbili ni mpotovu sana na anakana kwamba Mungu si Bwana wake, Mungu aliwaangamiza tu watu katika wakati wa Nuhu. Binadamu katika enzi zote mbili anamsababishia Mungu dhiki kuu, na bado Mungu bado Amesalia mvumilivu na watu katika siku za mwisho hadi sasa. Mbona hivi? Je, hamjawahi kujuiuliza kwa nini? Kama kweli hamjui, basi acha Niwaambie. Sababu ya Mungu kuweza kuwapa wanadamu neema katika siku za mwisho si kwamba ni wapotovu kwa kiasi kidogo kuliko watu katika wakati wa Nuhu, au kwamba wana nia za kutubu kwa Mungu, sembuse kwamba teknolojia katika siku za mwisho imeendelea sana kiasi kwamba Mungu hawezi kupata moyo wa kuwaangamiza. Badala yake, ni kwamba Mungu ana kazi ya kufanya katika kundi la watu katika siku za mwisho, na kwamba Mungu ananuia kufanya kazi hii Mwenyewe katika mwili Wake. Zaidi ya hayo, Mungu ananuia kuchagua sehemu ya kundi hili kuwa walengwa wa wokovu Wake na tunda la mpango Wake wa usimamizi, na kuwaleta watu hawa katika enzi ifuatayo. Kwa hivyo, bila kujali chochote, gharama hii iliyolipwa na Mungu yote ni kwa ajili ya maandalizi ya kazi ambayo kupata mwili Kwake hufanya katika siku za mwisho. Ukweli kwamba mmefika siku ya leo ni kwa sababu ya huu mwili. Ni kwa sababu Mungu anaishi ndani ya mwili ndiyo mna nafasi ya kuendelea kuishi. Baraka hizi zote zimepatikana kwa sababu ya mtu huyu wa kawaida. Siyo haya tu, lakini mwishowe, mataifa yasiyohesabika yatamwabudu mtu huyu wa kawaida, na vilevile kumpa shukrani na kumtii mtu huyu asiye muhimu, kwa sababu ni ukweli, uzima, na njia Aliyoleta ndivyo vilivyowaokoa wanadamu wote, vikatuliza migogoro kati ya mwanadamu na Mungu, vikafupisha umbali kati yao, na vikafungua kiungo kati ya mawazo ya Mungu na mwanadamu. Pia ni Yeye ambaye Amepata hata utukufu zaidi kwa ajili ya Mungu. Je, mwanadamu wa kawaida kama huyu hastahili uaminifu na ibada yako? Je, mwili wa kawaida kama huu haufai kuitwa Kristo? Je, mtu wa kawaida kama huyu hawezi kuwa onyesho la Mungu kati ya binadamu? Je, mtu kama huyu ambaye amewahurumia wanadamu wasiingie katika maafa hastahili upendo wenu na tamanio lenu la kumshikilia Yeye? Mkiukataa ukweli unaoonyeshwa kutoka katika mdomo Wake na kuchukia kuwepo Kwake miongoni mwenu, basi ni kitu gani kitakachowatendekea mwishowe?
Kazi yote ya Mungu katika siku za mwisho inafanywa kupitia mtu huyu wa kawaida. Yeye atakukirimia kila kitu, na zaidi ya hayo, Anaweza kuamua kila kitu kinachokuhusu. Je, mtu kama huyu anaweza kuwa kama mnavyoamini Yeye kuwa: mtu wa kawaida sana kiasi cha kutostahili kutajwa? Je, ukweli Wake hautoshi kuwaaminisha kabisa? Je, kuona matendo Yake kwa macho yenu wenyewe hakuwezi kuwashawishi? Au ni kwamba njia Anayowaongoza watu kuitembea haistahili kutembewa na nyinyi? Baada ya yote, ni nini kinachowasababisha ninyi kuhisi kuchukizwa na Yeye na kumkataa na kumkwepa? Ni mtu huyu anayeonyesha ukweli, ni mtu huyu anayetoa ukweli, na ni mtu huyu anayewapa njia ya kufuata. Je, inawezekana kuwa bado hamwezi kupata dalili za kazi ya Mungu ndani ya ukweli huu? Bila kazi ya Yesu, mwanadamu hangeweza kushuka chini kutoka msalabani, lakini bila Mungu mwenye mwili wa leo, wale wanaoshuka chini kutoka msalabani hawangewahi kupata kibali cha Mungu ama kuingia katika enzi mpya. Bila kuja kwa mtu huyu wa kawaida, hamngeweza kuwa na fursa ya kuuona uso wa kweli wa Mungu, wala hamngestahili kufanya hivyo, kwani nyinyi nyote ni walengwa ambao wangepaswa kuangamizwa kitambo sana. Kwa sababu ya kuja kwa Mungu mwenye mwili kwa mara ya pili, Mungu amewasamehe na kuwaonyesha huruma. Bila kujali lolote, maneno ambayo lazima Niwaachie mwishowe ni haya: Mtu huyu wa kawaida, ambaye ni Mungu mwenye mwili, ni wa umuhimu sana kwenu. Hili ndilo jambo kubwa ambalo Mungu tayari Amefanya miongoni mwa binadamu.