Tayarisha Matendo Mema ya Kutosha kwa ajili ya Hatima Yako
Nimefanya kazi nyingi miongoni mwenu na, bila shaka, Nimenena baadhi ya maneno vile vile. Hata hivyo Sina budi kuhisi kwamba maneno Yangu na kazi Yangu havijatimiza kikamilifu lengo la kazi Yangu ya siku za mwisho. Kwa maana katika siku za mwisho, kazi Yangu si kwa ajili ya mtu au watu fulani, bali ili kufunua tabia Yangu ya asili. Lakini kwa sababu zisizohesabika—pengine ukosefu wa muda au shughuli nyingi za kazi—watu hawajapata ufahamu wowote kunihusu Mimi kutokana na tabia Yangu. Kwa hivyo Ninaanza mpango Wangu mpya, kazi Yangu ya mwisho, na Ninafungua ukurasa mpya katika kazi Yangu, ili wale wote wanaoniona Mimi wajipige vifuani na kulia na kuomboleza bila kukoma kwa sababu ya uwepo Wangu. Hii ni kwa sababu Ninaleta mwisho wa binadamu duniani, na kuanzia sasa na kuendelea, Ninaweka wazi tabia Yangu yote mbele ya wanadamu, ili wote wanijuao na wale wote wasionijua waweze kuyafurahisha macho yao na kuona kwamba kweli Nimekuja katika ulimwengu wa binadamu, Nimekuja duniani ambapo vitu vyote vinazidi kuongezeka. Huu ni mpango Wangu, na ndiko “kukiri” Kwangu kwa pekee tangu uumbaji Wangu wa wanadamu. Nawaomba mzingatie kwa makini kila Ninachokifanya, kwa maana kiboko Changu kinawakaribia wanadamu kwa mara nyingine tena, kwa wale wote wanaoenda kinyume na Mimi.
Pamoja na mbingu, Ninaanza kazi ambayo Ninataka kufanya. Na kwa hiyo Ninapenya kati ya misururu ya watu na kupita kati ya mbingu na ardhi. Watu hawajawahi kuitambua miendo Yangu au kuyatilia maanani maneno Yangu. Kwa hivyo, mpango Wangu unaendelea kusonga mbele kwa urahisi. Ni kwamba tu hisia zenu zote zimekufa ganzi kiasi kwamba hamtambui hatua za kazi Yangu. Lakini kwa kweli kuna siku itakuja ambapo mtatambua makusudio Yangu. Leo, Ninaishi pamoja nanyi, na Ninateseka pamoja nanyi, na kwa muda mrefu Nimekuja kuelewa mtazamo ambao wanadamu wanao Kwangu. Nisingependa kuzungumza zaidi kuhusu jambo hili, sembuse kutaka kuwaletea aibu kwa kutoa mifano zaidi ya mada hii inayoumiza. Natumai tu kwamba mtayakumbuka yale yote ambayo mmeyafanya mioyoni mwenu, ili tuweze kulinganisha hesabu zetu siku tutakapokutana tena. Nisingependa kumshutumu yeyote miongoni mwenu kwa njia isiyo ya kweli, kwa sababu daima Nimekuwa nikitenda kwa namna isiyo na upendeleo na kwa namna ya busara, na wazi wazi. Bila shaka, Ninatumai pia kwamba nyinyi mnaweza kuwa wazi na waaminifu, na msifanye lolote lililo kinyume na mbingu na ardhi au na dhamiri yenu wenyewe. Hili ndilo jambo la pekee Ninalowataka mfanye. Watu wengi huhisi kuhangaika na kuona haya kwa sababu wametenda makosa ya kikatili mno, na wengi wanajionea aibu kwa sababu hawajawahi kufanya kitu chochote kizuri. Lakini wapo pia wengi ambao, mbali na kutohisi kufedheheshwa na dhambi zao, wanakuwa wabaya zaidi, wakifichua kabisa sura zao mbaya—ambazo hazikuwa bado zimewekwa wazi kikamilifu—ili kuishawishi tabia Yangu. Sijali kuhusu, wala sitilii maanani hata kidogo matendo ya mtu yeyote mmoja. Badala yake, Mimi hufanya kazi Ninayopaswa kufanya, iwe kukusanya habari, kusafiri katika nchi au kufanya jambo ambalo linanipendeza. Katika nyakati muhimu, Mimi ninaendelea na kazi Yangu miongoni mwa binadamu kama ilivyopangwa awali, bila kuchelewa au kuwa mapema hata kwa sekunde moja, na kwa urahisi na ufupi. Hata hivyo, katika kila hatua ya kazi Yangu, wengine wanatupiliwa mbali, kwa sababu Ninachukia njia zao za kujipendekeza na kujifanya kwao wanyenyekevu. Wale Ninaowaona kuwa wenye kuchukiza sana kwa hakika wataachwa; bila kujali kile wanachofikiri watu, kwa vyovyote vile Nitawafanya wale wote Ninaowachukia wakae mbali sana na Mimi. Ni dhahiri kwamba, Sitawahurumia wale waovu wanaobaki katika nyumba Yangu. Kwa kuwa siku ya adhabu ya mwanadamu inakaribia, Siharahakishi kuzitupa nje zile roho zote zinazochukiza kutoka katika nyumba Yangu, kwa kuwa nina mpango Wangu mwenyewe.
Sasa ndio wakati ambapo Ninaamua matokeo ya kila mtu, si hatua ambamo Nilianza kumfinyanga mwanadamu. Ninaandika katika kitabu Changu cha rekodi, moja baada ya lingine, maneno na matendo ya kila mtu, mchakato wao wa kunifuata, sifa zao za kiasili, na udhihirisho wao wa mwisho. Kwa njia hii, haijalishi yeye ni mtu wa aina gani, hakuna mtu yeyote atakayeepuka mkono Wangu, na wote wataainishwa kulingana na aina yake kulingana na Nilivyopanga. Siamui hatima ya kila mtu kwa msingi wa umri, cheo, au kiwango cha mateso, sembuse kiwango ambacho yeye ni mwenye kutia huruma, bali kulingana na ikiwa ana ukweli. Hakuna chaguo lingine ila hili. Sharti muelewe kwamba wale wote ambao hawafuati mapenzi ya Mungu wataadhibiwa pia bila kumwacha yeyote. Hili ni jambo ambalo hakuna mtu anayeweza kulibadilisha. Kwa hivyo, wale wote wanaoadhibiwa wanaadhibiwa kwa ajili ya haki ya Mungu na kama malipo kwa ajili ya vitendo vyao vingi viovu. Sijafanya mabadiliko yoyote katika mpango Wangu tangu uanzishwe. Ni kwamba tu, kulingana na mwanadamu, wale ambao Ninaelekeza maneno Yangu kwao wanaonekana kupungua kwa idadi, sawa na wale ambao Ninawakubali kwa kweli. Hata hivyo, Ninasisitiza kwamba mpango Wangu haujawahi kubadilika; badala yake, ni imani na upendo wa mwanadamu ambavyo hubadilika daima, kufifia daima, kiasi kwamba kuna uwezekano wa kila mtu kubadilika kutoka kujipendekeza Kwangu hadi kufikia hali ya kuwa baridi kwangu au hata kunitupa nje. Mtazamo Wangu kwenu hautakuwa baridi wala moto, mpaka Nihisi kinyaa na karaha, na hatimaye kutoa adhabu. Hata hivyo, katika siku ya adhabu yenu, bado Nitawaona lakini ninyi hamtaweza kuniona tena. Kwa kuwa namna ya maisha miongoni mwenu imeshakuwa ya kuchosha na yenye uchushi Kwangu, basi, ni wazi kwamba Nimechagua mazingira tofauti ya kuishi, ni afadhali Niepuke kuumizwa na maneno yenu maovu na kwenda mbali na tabia zenu chafu zisizovumilika, ili kwamba msinipumbaze au kunitendea kwa namna isiyo ya dhati tena. Kabla Sijawaacha, lazima bado Ninawahimiza mjiepushe kufanya yale ambayo hayaambatani na ukweli. Badala yake, mnafaa kufanya kile ambacho kinampendeza kila mmoja, kile kilicho na manufaa kwa wote, na kile kinachofaidi hatima yenu wenyewe, la sivyo, yule anayeteseka katika maafa hatakuwa mwingine ila wewe.
Rehema Yangu inaonyeshwa kuelekea wale wanaonipenda Mimi na kujitelekeza wao wenyewe. Adhabu itakayowapata waovu, kwa sasa, ni thibitisho hasa la tabia Yangu ya haki na, hata zaidi, ushuhuda wa ghadhabu Yangu. Maafa yatakapokuja, wale wote wanaonipinga wataomboleza wanapokuwa waathiriwa wa njaa na tauni. Wale ambao wamenifuata Mimi kwa miaka mingi, lakini ambao wametenda kila aina ya matendo maovu, hawataepuka kulipia dhambi zao; wao pia, watatumbukizwa katika maafa, ambayo yameonekana kwa nadra kotekote katika mamilioni ya miaka, na wataishi katika hali ya taharuki na woga daima. Na wale kati ya wafuasi Wangu ambao wameonyesha uaminifu usiogawanyika Kwangu watafurahi na kupiga makofi, wakiisifu nguvu Yangu kuu. Watapitia hali isiyoelezeka ya furaha isiyo na mawazo na kuishi katikati ya furaha ambayo Sijawahi kuwapa wanadamu hapo awali. Kwa sababu Ninathamini matendo mema ya binadamu na kuchukia matendo yake maovu. Tangu Nilipoanza kuwaongoza wanadamu, Nimekuwa nikitamani kwa hamu kupata kundi la watu wenye mawazo sawa na Mimi. Wale ambao si wenye nia moja na Mimi, wakati huo huo, huwa Siwasahau kamwe; huwa Ninawachukia kabisa moyoni Mwangu daima, Nikisubiri nafasi ya kuwafanya walipie matendo yao maovu, jambo ambalo Nitafurahia sana kuona. Sasa siku Yangu imefika hatimaye, na Sihitaji kusubiri zaidi!
Kazi Yangu ya mwisho si kwa ajili ya kumwadhibu mwanadamu tu, bali pia kwa ajili ya kupanga hatima ya mwanadamu. Hata zaidi, ni kwa ajili ya kuwafanya watu wote wayatambue matendo na vitendo Vyangu. Nitamfanya kila mtu aone kwamba yale yote ambayo Nimefanya ni sahihi na ni dhihirisho la tabia Yangu, kwamba si matendo ya mwanadamu, na sembuse si nguvu asili iliyowaumba wanadamu, na badala yake ni Mimi ndiye Ninayerutubisha kila kiumbe anayeishi miongoni mwa vitu vyote. Bila uwepo Wangu, wanadamu wataangamia tu na kusumbuka kutokana na baa la misiba. Hapana mwanadamu atakayeona uzuri wa jua na mwezi, au dunia ya kijani kibichi; binadamu atakumbana tu na usiku wenye giza, wenye baridi na bonde lisiloepukika la uvuli wa mauti. Mimi Ndimi ukombozi wa pekee wa wanadamu. Mimi Ndimi tumaini la pekee la wanadamu, na zaidi ya hayo; Mimi tu Ndimi tegemeo la uwepo wa wanadamu wote. Bila Mimi, binadamu watasimama kabisa mara moja, bila Mimi, wanadamu watakumbana tu na msiba mkuu na kukanyagiwa chini na pepo wa kila aina, ingawa hakuna anayenitilia Mimi maanani. Nimefanya kazi ambayo haiwezi kufanywa na yeyote mwingine, na Ninatumaini tu kwamba mwanadamu anaweza kunilipa kwa kutenda matendo mema kiasi. Ingawa ni wachache tu ambao wameweza kunilipa, bado Nitahitimisha safari Yangu katika dunia ya binadamu na kuanza hatua ifuatayo ya kazi Yangu ambayo iko karibu kutekelezwa, kwa sababu kukimbia Kwangu huku na huko miongoni mwa wanadamu kwa miaka hii mingi kumekuwa na matokeo mazuri, na Nimefurahishwa sana. Ninachojali si idadi ya watu, bali ni matendo yao mema. Kwa hali yoyote ile, Ninatumaini kwamba mtatayarisha matendo mema ya kutosha kwa ajili ya hatima yenu wenyewe. Ni hapo tu ndipo Nitakaporidhika; la sivyo, hakuna yeyote kati yenu anayeweza kuepuka shambulio la maafa. Maafa haya hutoka Kwangu na bila shaka Mimi ndimi Niliyeyapanga. Ikiwa hamwezi kuonekana kuwa wema mbele Yangu, basi hamtaweza kuepuka kupitia maafa. Katikati ya dhiki, matendo yenu hayakufikiriwa kuwa yanafaa kabisa, kwa kuwa imani na upendo wenu vilikuwa vitupu, na mlijionyesha tu kuwa waoga au wenye nguvu. Kuhusu hili, Nitafanya hukumu ya mema au mabaya tu. Kinachonipa wasiwasi bado ni matendo na vitendo na udhihirisho wote, wa kila mmoja wenu, kwa msingi ambao kwao Nitaamua matokeo yenu. Hata hivyo, ni sharti Niseme hili wazi: Kwa wale ambao hawakuwahi kunionyesha uaminifu hata kidogo wakati wa dhiki, Sitakuwa mwenye rehema tena, kwa sababu rehema Yangu ina mipaka. Simpendi yeyote, zaidi ya hayo, yule ambaye amewahi kunisaliti Mimi, sembuse kupenda kujihusisha na wale ambao huyasaliti maslahi ya wenzao. Hii ndiyo tabia Yangu, bila kujali huyo mtu anaweza kuwa nani. Ni lazima Niwaambie hili: Yeyote atakayeuvunja kabisa moyo Wangu hatapokea stahamala kutoka Kwangu mara ya pili, na yeyote ambaye amekuwa mwaminifu Kwangu atadumu moyoni Mwangu milele.
Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?