Kujua Hatua Tatu za Kazi ya Mungu Ndiyo Njia ya Kumjua Mungu (Sehemu ya Pili)

Kazi ya Mungu Mwenyewe ni maono ambayo mwanadamu lazima afahamu, kwa kuwa kazi ya Mungu haiwezi kutekelezwa na mwanadamu, wala haimilikiwi na mwanadamu. Hatua tatu za kazi ndizo ukamilifu wa usimamizi wa Mungu, na hakuna ono kuu kuliko hili linalopaswa kufahamika kwa mwanadamu. Kama mwanadamu hafahamu maono haya makuu, basi si rahisi kumjua Mungu, na si rahisi kujua mapenzi ya Mungu, na, zaidi ya hayo, njia ambayo mwanadamu anapitia inazidi kuwa ngumu. Bila maono, mwanadamu hangeweza kufika umbali huu. Ni maono ambayo yamemlinda mwanadamu hadi leo, na ambayo yamempa mwanadamu ulinzi mkuu. Katika siku za usoni, maarifa yenu lazima yawe ya kina, na sharti mfahamu mapenzi Yake yote na umuhimu wa kazi Yake yenye busara katika hatua tatu za kazi. Hiki tu ndicho kimo chenu cha kweli. Hatua ya kazi ya mwisho haisimami peke yake, ila ni sehemu ya yote iliyounganishwa pamoja na hatua mbili za awali, ambayo ni kusema kwamba haiwezekani kukamilisha kazi nzima ya wokovu kwa kufanya kazi ya hatua moja pekee. Ingawa hatua ya mwisho ya kazi inaweza kumwokoa mwanadamu kabisa, hii haimaanishi kwamba ni muhimu tu kutekeleza hatua hii pekee, na kwamba hatua mbili za hapo awali hazihitajiki kumwokoa mwanadamu kutokana na ushawishi wa Shetani. Hakuna hatua moja kati ya zote tatu inayoweza kuwekwa kama maono ya kipekee ambayo lazima yajulishwe mwanadamu, kwa kuwa ukamilifu wa kazi ya wokovu ni hatua tatu za kazi, wala si hatua moja kati ya tatu. Ilimradi kazi ya wokovu bado haijakamilishwa, usimamizi wa Mungu utashindwa kufikia kikomo. Nafsi ya Mungu, tabia, na hekima zimeonyeshwa katika ukamilifu wa kazi ya wokovu, wala hazikufichuliwa kwa mwanadamu hapo mwanzo, lakini zimeonyeshwa hatua kwa hatua katika kazi ya wokovu. Kila hatua ya kazi ya wokovu huonyesha sehemu ya tabia ya Mungu, na sehemu ya nafsi Yake: si kila hatua ya kazi inayoweza moja kwa moja kuonyesha kabisa na kwa ukamilifu nafsi ya Mungu. Kwa hivyo, kazi ya wokovu inaweza tu kuhitimishwa hatua tatu za kazi zitakapokamilika, na kwa hivyo, maarifa ya mwanadamu ya ukamilifu wa Mungu hayawezi kutenganishwa na hatua tatu za kazi ya Mungu. Kile ambacho mwanadamu hupokea kutoka kwa hatua moja ya kazi ni tabia ya Mungu inayoonyeshwa katika sehemu moja ya kazi yake tu. Haiwezi kuwakilisha tabia na nafsi inayoonyeshwa katika hatua ya awali na ijayo. Hii ni kwa sababu kazi ya kumwokoa mwanadamu haiwezi kumalizika mara moja katika kipindi kimoja, ama katika eneo moja, lakini hukuwa kwa kina hatua kwa hatua kulingana na kiwango cha kukua kwa mwanadamu katika wakati na maeneo tofauti. Ni kazi inayofanywa hatua kwa hatua, na haikamilishwi katika hatua moja. Na kwa hiyo, hekima yote ya Mungu imejumuishwa katika hatua tatu, badala ya hatua moja. Nafsi yake yote na hekima yake yote zimewekwa wazi katika hatua hizi tatu, na kila hatua ina nafsi Yake, na ni rekodi ya hekima ya kazi Yake. Mwanadamu anapasa kujua tabia yote ya Mungu iliyoonyeshwa katika hatua hizi tatu. Nafsi hii ya Mungu ndiyo ina maana zaidi kwa wanadamu wote, na ikiwa watu hawana maarifa haya wanapomwabudu Mungu, basi hawana tofauti na wale wanaoabudu Budha. Kazi ya Mungu kati ya wanadamu haijafichiwa mwanadamu, na inapaswa kujulikana na wale wote wanaomwabudu Mungu. Kwa sababu Mungu ametekeleza hatua tatu za kazi ya wokovu kati ya wanadamu, mwanadamu anapaswa kujua maonyesho ya kile Anacho na alicho wakati wa hatua hizi tatu za kazi. Hili ndilo ambalo ni lazima lifanywe na mwanadamu. Kile ambacho Mungu anamfichia mwanadamu ni kile ambacho mwanadamu hawezi kutimiza, na kile ambacho mwanadamu hapaswi kujua, ilhali yale Mungu anayomfunulia mwanadamu ni yale ambayo mwanadamu anapaswa kujua na yale ambayo mwanadamu anapaswa kumiliki. Kila moja ya hatua tatu za kazi huendelea juu ya msingi wa hatua iliyopita; haitekelezwi peke yake, tofauti na kazi ya wokovu. Ingawa kuna tofauti kubwa katika enzi na aina ya kazi ambayo inafanywa, katika kiini chake bado ni wokovu wa mwanadamu, na kila hatua ya kazi ya wokovu ina kina kuliko iliyopita. Kila hatua inaendelea kutoka kwa msingi wa hatua ya mwisho ambayo haiondolewi. Kwa njia hii, katika kazi Yake ambayo daima huwa mpya na kamwe si kuukuu, Mungu mara kwa mara anaonyesha kipengele cha tabia Yake ambayo hayajawahi kuonyeshwa kwa mwanadamu hapo awali, na daima anamfichulia mwanadamu kazi Yake mpya, na nafsi Yake mpya, na hata ikiwa wazoefu wakongwe wa kidini hufanya juu chini kukinzana na hili, na kulipinga waziwazi, Mungu daima hufanya kazi mpya ambayo anakusudia kufanya. Kazi Yake daima hubadilika, na kwa sababu hili, daima inakabiliwa na upinzani wa mwanadamu. Na hivyo, pia, tabia Yake inabadilika daima, na vilevile enzi na wanaopokea kazi Yake. Zaidi ya hayo, kila mara Yeye hufanya kazi ambayo haijawahi kufanywa tena, hata kufanya kazi ambayo huonekana kwa mwanadamu kuhitilafiana na kazi iliyofanywa awali, kuwa kinyume nayo. Mwanadamu anaweza kukubali tu aina moja ya kazi, ama njia moja ya matendo. Ni vigumu kwa wanadamu kukubali kazi ama njia za matendo, ambayo yanakinzana nao, ama yaliyo juu kuwaliko—lakini Roho Mtakatifu daima anafanya kazi mpya, na kwa hivyo kunakuwepo kikundi baada ya kikundi cha wataalamu wa kidini wanaoipinga kazi mpya ya Mungu. Watu hawa wamekuwa wataalamu hasa kwa sababu mwanadamu hana maarifa ya jinsi Mungu huwa mpya wala hazeeki, na zaidi ya hayo, hana maarifa ya kanuni za kazi ya Mungu, na hata zaidi hawana maarifa ya njia nyingi ambazo Mungu humwokoa mwanadamu. Kwa hivyo, mwanadamu kabisa anashindwa kueleza kama ni kazi inayotoka kwa Roho Mtakatifu, au ni kazi ya Mungu Mwenyewe. Watu wengi hushikilia mtazamo ambao, kama inalingana na maneno yanayokuja kabla, basi wanaweza kuikubali, na kama kuna tofauti na kazi ya awali, basi wanaipinga na kuikataa. Leo, je, nyote hamjafuata katika kanuni hizi? Hatua tatu za kazi ya wokovu hazijakuwa na athari kubwa kwenu, na kuna wale wanaoamini kuwa hatua mbili zilizopita za kazi ni mzigo usiohitaji kufahamika. Wanafikiria kuwa hatua hizi hazifai kutangazwa kwa umati na zinafaa kufutwa haraka iwezekanavyo, ili watu wasihisi kwamba wamezidiwa na hatua mbili za awali za zile hatua tatu za kazi. Wengi wanaamini kuwa kupeana ufahamu kuhusu hatua mbili zilizopita ni hatua ya mbali sana, wala haina faida katika kumjua Mungu—hivyo ndivyo mnavyofikiria. Leo, nyote mnaamini kuwa ni haki kutenda vile, lakini siku itawadia ambapo mtagundua umuhimu wa kazi Yangu: Mjue kuwa Sifanyi kazi yoyote ambayo haina umuhimu. Kwa sababu Ninawatangazia hatua tatu za kazi, kwa hivyo lazima ziwe na faida kwenu; kwa sababu hatua hizi tatu za kazi ndizo kiini cha usimamizi mzima wa Mungu, kwa hivyo lazima ziwe lengo la kila mmoja duniani. Siku moja, nyote mtagundua umuhimu wa kazi hii. Fahamuni kuwa mnapinga kazi ya Mungu, ama mnatumia dhana zenu kupima kazi ya leo, kwa sababu hamjui kanuni za kazi ya Mungu, na kwa sababu hamchukulii kazi ya Roho Mtakatifu kwa makini kutosha. Upinzani wenu kwa Mungu na kuzuia kazi ya Roho Mtakatifu kumetokana na dhana zenu na upumbavu wenu wa kiasili. Si kwa sababu kazi ya Mungu si sawa, lakini ni kwa sababu mna tabia ya kiasili ya kutotii. Baada ya kupata imani yao katika Mungu, watu wengine hawawezi hata kusema kwa uhakika mwanadamu alikotoka, ilhali wanathubutu kuzungumza hadharani wakitathmini haki na makosa ya kazi ya Roho Mtakatifu. Na pia wanawakemea mitume ambao wana kazi mpya ya Roho Mtakatifu, wakitoa maoni huku wakizungumza kwa zamu; ubinadamu wao uko chini sana, na hawana hisia zozote. Je, si siku itawadia ambapo watu kama hawa watakataliwa na kazi ya Roho Mtakatifu, na kuchomwa katika moto wa kuzimu? Hawafahamu kazi ya Mungu, lakini badala yake wanakosoa kazi Yake, na pia wanajaribu kumwagiza Mungu jinsi atakavyofanya kazi. Je, ni kwa namna gani watu hawa wasio na busara watamjua Mungu? Mwanadamu huja kumjua Mungu wakati anapomtafuta na anapokuwa na uzoefu naye; si katika kumkosoa kwa ghafla ndipo anapokuja kumjua Mungu kwa kupitia kutiwa nuru na Roho Mtakatifu. Kadiri maarifa ya watu kuhusu Mungu yanavyozidi kuwa sahihi, ndivyo upinzani wao Kwake unavyopungua. Kinyume na hayo, kadri watu wanavyomjua Mungu kwa kiasi kidogo, ndivyo wanavyokuwa na uwezekano wa kumpinga. Dhana zako, ubinadamu wako wa zamani, na utu wako, tabia na maadili ndiyo “mtaji” ambao unampingia Mungu, na kadri unavyokuwa mpotevu, ama ulivyoshushwa heshima na ulivyo duni, ndivyo unavyozidi kuwa adui wa Mungu. Wale waliomilikiwa na dhana kali na wenye tabia ya unafiki wamo hata zaidi katika uadui wa Mungu mwenye mwili, na watu kama hawa ni wapinga Kristo. Ikiwa dhana zako hazitarekebishwa, basi daima zitakuwa kinyume na Mungu; daima hutalingana na Mungu, na daima utakuwa mbali na Yeye.

Ni katika kuweka dhana zako za kale kando tu ndipo utakapoweza kupata maarifa mapya, ilhali maarifa ya zamani si lazima yawe dhana za zamani. “Dhana” inamaanisha vitu vinavyodhaniwa na mwanadamu ambavyo viko mbali na uhalisi. Kama maarifa ya zamani yalikuwa yamepitwa na wakati katika enzi ya kale, na yalimzuia mwanadamu kuingia katika kazi mpya, basi maarifa kama yale pia ni dhana. Ikiwa mwanadamu ataweza kuchukua mwelekeo mzuri kwa maarifa kama yale, na anaweza pata kumjua Mungu kutoka kwa vipengele tofauti, kuunganisha ya zamani na mapya, basi maarifa ya kale yatamsaidia mwanadamu, na yatakuwa msingi wa mwanadamu kuingia katika enzi mpya. Funzo la kumjua Mungu linahitaji kwamba uwe stadi wa kanuni nyingi: jinsi ya kuingia kwenye njia ya kumjua Mungu, ukweli gani unapasa kuelewa ili kumjua Mungu, na jinsi ya kufanya dhana zako na asili yako ya asili kutii mipango yote ya kazi mpya ya Mungu. Ukitumia kanuni hizi kama msingi wa kuingia kwenye somo la kumjua Mungu, basi maarifa yako yatakuwa na kina zaidi na zaidi. Kama una maarifa wazi ya hatua tatu za kazi—ambayo ni kusema kwamba, ya mpango mzima wa usimamizi wa Mungu—na ikiwa utaweza kupatanisha hatua mbili za awali na hatua ya sasa, na unaweza kuona kwamba ni kazi iliyofanywa na Mungu mmoja, basi utakuwa na msingi imara zaidi. Hatua tatu za kazi zilifanywa na Mungu mmoja; haya ndiyo maono makubwa zaidi, na ndiyo njia ya pekee ya kumjua Mungu. Hatua tatu za kazi zingefanywa tu na Mungu Mwenyewe, na hapana mwanadamu yeyote ambaye angeweza kufanya kazi kama hii kwa niaba Yake—ambayo ni kusema kuwa ni Mungu Mwenyewe pekee ambaye angeifanya kazi Yake toka mwanzo hadi leo. Ingawa hatua tatu za kazi ya Mungu zimefanywa katika enzi tofauti na maeneo tofauti, na ingawa kazi ya kila moja ni tofauti, yote ni kazi iliyofanywa na Mungu mmoja. Kati ya maono yote, hili ndilo kuu zaidi ambalo mwanadamu anapaswa kulijua, na ikiwa litaeleweka kabisa na mwanadamu, basi ataweza kusimama imara. Leo, tatizo kuu linalovikumba vikundi kadhaa vya dini ni kwamba havijui kazi ya Roho Mtakatifu, na hayana uwezo wa kutofautisha kati ya kazi ya Roho Mtakatifu na kazi isiyo ya Roho Mtakatifu—na kwa hivyo hawawezi kueleza kama hatua hii ya kazi, kama hatua mbili za awali, pia zimefanywa na Yehova Mungu. Ingawa watu wanamfuata Mungu, wengi hawawezi kueleza kama ni njia sahihi. Mwanadamu anahofia ikiwa hii ndiyo njia inayoongozwa na Mungu Mwenyewe, na kama Mungu kupata mwili ni jambo la hakika, na watu wengi bado hawana dokezo jinsi ya kupambanua ikifikia maneno kama haya. Wale wanaomfuata Mungu hawawezi kujua njia, na kwa hivyo habari zinazozungumzwa zinaathiri sehemu ndogo tu kati ya watu hawa na hayana uwezo wa kufaa kikamilifu, na kwa hivyo, hili basi linaathiri maisha ya watu kama hawa. Ikiwa mwanadamu anaweza kuona katika hatua tatu za kazi kuwa zilitekelezwa na Mungu Mwenyewe wakati tofauti, katika maeneo tofauti, na kwa watu tofauti, basi mwanadamu ataona kuwa[a], ingawa kazi ni tofauti, yote imefanywa na Mungu mmoja. Kwa kuwa ni kazi ambayo imefanywa na Mungu mmoja, basi lazima iwe sawa, na bila dosari, na ingawa halingani na dhana za mwanadamu, hakuna kupinga kuwa ni kazi iliyofanywa na Mungu mmoja. Ikiwa mwanadamu anaweza kusema kwa hakika kuwa ni kazi ya Mungu mmoja, basi dhana zake zitakuwa duni, na ambazo hazifai kutajwa. Kwa sababu maono ya mwanadamu hayako wazi, na mwanadamu anamjua tu Yehova kama Mungu, na Yesu kama Bwana, na ana mitazamo miwili kumhusu Mungu mwenye mwili wa leo, watu wengi wamejitoa kwa ajili ya kazi ya Yehova na Yesu, na wamezingirwa na dhana kuhusu kazi ya leo, watu wengi daima huwa na shaka na hawachukulii kazi ya leo kwa makini. Mwanadamu hana uelewa kuhusu hatua mbili za mwisho, ambazo hazikuonekana. Hili ni kwa sababu mwanadamu haelewi uhalisi wa hatua mbili za mwisho kazi, na wala hakuzishuhudia binafsi. Ni kwa sababu haziwezi kuonekana ndiyo mwanadamu anawaza jinsi anavyopenda; bila kujali atakayodhania, hakuna ukweli wa kudhibitisha, na yeyote wa kurekebisha. Mwanadamu anaruhusu silika yake ya asili itawale, huku akikosa kujali na kuachilia mawazo yake yaende popote, kwa kuwa hakuna ukweli wa kudhibitisha, na kwa hivyo dhana za mwanadamu zinakuwa “ukweli,” bila kujali kama zina dhibitisho. Kwa hivyo mwanadamu anaamini Mungu wake aliyemuwazia akilini mwake, na hamtafuti Mungu wa uhalisi. Ikiwa mtu mmoja ana aina moja ya imani, basi kati ya watu mia moja kuna aina mia moja za imani. Mwanadamu ana imani kama hizi kwa maana hajaona uhalisi wa kazi ya Mungu, kwa sababu amesikia tu kwa masikio yake na hajaona kwa macho yake. Mwanadamu amesikia hekaya na hadithi—lakini amesikia kwa nadra kuhusu maarifa ya ukweli ya kazi ya Mungu. Ni katika dhana zao ndivyo watu ambao wamekuwa waumini kwa mwaka mmoja tu wanaamini Mungu, na hilo ni kweli pia kwa wale ambao wamemwamini Mungu katika maisha yao yote. Wale ambao hawawezi kuona ukweli daima hawawezi kuepuka imani ambayo wana dhana kwazo kumhusu Mungu. Mwanadamu anaamini kuwa amejiweka huru kutokana na vifungo vya dhana zake za kale, na ameingia eneo jipya. Je, mwanadamu hajui kuwa maarifa ya wale wasioweza kuona uso wa kweli wa Mungu kuwa ni dhana na tetesi? Mwanadamu anafikiria kuwa dhana zake ni sawa, na wala hayana kasoro, na hufikiri kuwa hizi dhana zimetoka kwa Mungu. Leo, mwanadamu anaposhuhudia kazi ya Mungu, anaachilia dhana zilizokuwa zimeongezeka kwa miaka mingi. Mawazo na dhana za awali zilikuwa vizuizi vya kazi ya hatua hii, na inakuwa vigumu kwa mwanadamu kuachana na dhana kama hizo na kupinga mawazo kama yale. Dhana kuhusu kazi hii ya hatua kwa hatua ya wengi wa wale wanaomfuata Mungu hadi leo zimekuwa ya kuhuzunisha na watu hawa pole pole wamefanya uadui wa kikaidi na Mungu mwenye mwili hatua kwa hatua, na chanzo cha chuki ni mawazo na dhana za mwanadamu. Ni hasa kwa sababu ukweli haumruhusu mwanadamu kuwa na uhuru wa hiari ya mawazo yake, na, zaidi ya hayo, hauwezi kupingwa na mwanadamu kwa urahisi, na mawazo na dhana za mwanadamu hazistahimili uwepo wa ukweli, na hata zaidi ya hayo, kwa sababu mwanadamu hawezi kufikiria kuhusu usahihi na unyofu wa ukweli, na kwa nia moja tu huachilia mawazo yake, na hutumia dhana yake, kwamba dhana na mawazo ya mwanadamu zimekuwa adui wa kazi ya leo, kazi ambayo haiambatani na dhana za mwanadamu. Hili linaweza kusemwa kuwa kasoro ya dhana za mwanadamu, na wala si dosari ya kazi ya Mungu. Mwanadamu anaweza kufikiria lolote atakalo, lakini hawezi kupinga waziwazi hatua yoyote ya kazi ya Mungu au hata sehemu yoyote; ukweli wa kazi ya Mungu hauwezi kukiukwa na mwanadamu. Unaweza kuruhusu mawazo yako yatawale, na unaweza pia kujumuisha hadithi nzuri kuhusu kazi ya Yehova na Yesu, lakini kamwe huwezi kupinga ukweli wa kila hatua ya kazi ya Yehova na Yesu; hii ni kanuni, na pia ni amri ya utawala, na mnapaswa kuelewa umuhimu wa masuala haya. Mwanadamu anaamini kuwa hatua hii ya kazi hailingani na dhana za mwanadamu, na hivi sivyo katika hatua mbili zilizopita za kazi. Katika mawazo yake, mwanadamu anaamini kuwa kazi ya hatua mbili zilizopita kwa hakika si sawa na kazi ya leo—lakini je, umewahi kufikiria kuwa kanuni zote za kazi ya Mungu ni sawa, na kuwa kazi Yake huwa vitendo daima, na kuwa, bila kujali enzi, daima kutakuwa na halaiki ya watu wanaokataa na kuupinga ukweli wa kazi Yake? Wale wote ambao leo wanakataa na kuipinga hatua hii ya kazi bila shaka wangempinga Mungu wakati uliopita, kwa kuwa watu kama hawa daima watakuwa adui za Mungu. Watu wanaoujua ukweli wa kazi ya Mungu wataona hatua tatu za kazi kama kazi ya Mungu mmoja, na watatupilia mbali dhana zao. Hawa ni watu wanaomjua Mungu, na watu kama hawa ndio kwa kweli humfuata Mungu. Wakati ambapo usimamizi mzima wa Mungu utakaribia kufika mwisho, Mungu ataweka vitu vyote kulingana na aina. Mwanadamu aliumbwa kwa mikono ya Muumba, na mwishowe lazima kabisa Amrudishe mwanadamu chini ya utawala Wake; huu ndio mwisho wa hatua tatu za kazi. Hatua ya kazi ya siku za mwisho, na hatua mbili zilizopitwa katika Israeli na Yudea, ni mpango wa Mungu wa usimamizi katika dunia nzima. Hakuna anayeweza kupinga hili, na ni ukweli wa kazi ya Mungu. Ingawa watu hawajapata uzoefu ama kushuhudia nyingi za kazi hizi, ukweli unabaki kuwa ukweli, na hauwezi kukanwa na mwanadamu yeyote. Watu wanaomwamini Mungu katika nchi zote duniani watakubali hatua tatu za kazi. Kama wajua tu hatua moja ya kazi, na huelewi hatua nyingine mbili za kazi, na huelewi kazi ya Mungu katika wakati uliopita, basi huwezi kuongea ukweli wa mpango mzima wa usimamizi wa Mungu, na maarifa yako ya Mungu yameegemea upande mmoja, kwa kuwa katika imani yako katika Mungu humfahamu, ama kumwelewa, na kwa hivyo hustahili kutoa ushuhuda wa Mungu. Bila kujali kama maarifa yako ya sasa ya mambo haya yana kina kirefu ama cha juujuu tu, mwishowe, lazima muwe na maarifa, na ushawishike kabisa, na watu wote wataona uzima wa kazi ya Mungu na kunyenyekea chini ya utawala wa Mungu. Mwishoni mwa kazi hii, madhehebu yote yatakuwa moja, viumbe wote watarejea chini ya utawala wa Muumba, viumbe wote watamwabudu Mungu mmoja wa kweli, na makundi yote mageni ya kidini yatakuwa bure, na hayataonekana tena.

Mbona mfululizo huu wa marejeo kwa hatua tatu za kazi? Kupita kwa enzi, maendeleo ya kijamii, na uso wa asili unaobadilika yote hufuata mabadiliko katika hatua tatu za kazi. Mwanadamu hubadilika kwa wakati na kazi ya Mungu, na wala hakui peke yake mwenyewe. Kutajwa kwa hatua tatu za kazi ya Mungu ni kwa ajili ya kuleta viumbe wote, na watu kutoka dini zote, chini ya utawala wa Mungu mmoja. Bila kujali wewe ni wa dini gani, mwishowe nyote mtanyenyekea chini ya utawala wa Mungu. Ni Mungu Mwenyewe tu anayeweza kufanya kazi hii; haiwezi kufanywa na kiongozi yeyote wa kidini. Kuna dini kadhaa kuu duniani, na kila moja ina kichwa, ama kiongozi, na wafuasi wameenea katika nchi tofauti tofauti na maeneo yote duniani; kila nchi, iwe ndogo au kubwa, ina dini tofauti tofauti ndani yake. Hata hivyo, bila kujali ni dini ngapi zilizo duniani, watu wote wanaoishi duniani mwishowe wanaishi katika uongozi wa Mungu mmoja, na uwepo wao hauongozwi na viongozi wa kidini au vichwa. Ambayo ni kusema kwamba wanadamu hawaongozwi na kiongozi fulani wa kidini ama kiongozi; badala yake wanadamu wote wanaongozwa na Muumba, aliyeziumba mbingu na nchi, na vitu vyote, na ambaye aliwaumba wanadamu—na huu ni ukweli. Hata ingawa dunia ina dini kadhaa kuu, bila kujali jinsi zilivyo kuu, zote zipo chini ya utawala wa Muumba, na hakuna inayoweza kuzidi wigo wa mamlaka hii. Maendeleo ya wanadamu, maendeleo ya kijamii, maendeleo ya sayansi ya asili—kila moja haitengani na mipango ya Muumba, na kazi hii sio kitu kinachoweza kufanywa na uongozi fulani wa dini. Viongozi wa dini ni viongozi tu wa dini fulani, na hawawezi kuwakilisha Mungu, ama Yule aliyeziumba mbingu na nchi na vitu vyote. Viongozi wa kidini wanaweza kuongoza wale wote walio katika dini yote, lakini hawawezi kuamrisha viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu—huu ni ukweli uliokubalika ulimwenguni. Viongozi wa dini ni viongozi tu, na hawawezi kuwa sawa na Mungu (Muumba). Vitu vyote vi mikononi mwa Muumba, na mwishowe vyote vitarejea mikononi mwa Muumba. Mwanadamu kiasili aliumbwa na Mungu, na haijalishi dini, kila mtu atarejea katika utawala wa Mungu—hili haliwezi kuepukika. Ni Mungu tu Aliye Juu Zaidi kati ya vitu vyote, na mtawala mkuu kati ya viumbe wote lazima pia warejee chini ya utawala Wake. Bila kujali mwanadamu ana hadhi ya juu kiasi gani, hawezi kumfikisha mwanadamu kwenye hatima inayomfaa, wala hakuna anayeweza kuainisha kila kitu kulingana na aina. Yehova mwenyewe alimuumba mwanadamu na kumwainisha kila mmoja kulingana na aina na siku ya mwisho itakapowadia bado Atafanya kazi Yake Mwenyewe, kuanisha kila kitu kulingana na aina—hili haliwezi kufanywa na mwingine isipokuwa Mungu. Hatua tatu za kazi ambazo zilifanywa tangu mwanzo hadi leo zote zilitekelezwa na Mungu Mwenyewe, na zilitekelezwa na Mungu mmoja. Ukweli wa hatua tatu za kazi ni ukweli wa uongozi wa Mungu kwa wanadamu wote, ukweli ambao hakuna anayeweza kuupinga. Mwishoni mwa hatua tatu za kazi, vitu vyote vitaainishwa kulingana na aina na kurejea chini ya utawala wa Mungu, kwa kuwa duniani kote kuna Mungu mmoja tu, na hakuna dini nyingine. Yule asiyeweza kuiumba dunia hataweza kuiangamiza, ilhali Yule aliyeumba dunia hakika ataiangamiza, na kwa hivyo, kama mtu hana uwezo wa kutamatisha enzi na ni wa kumsaidia mwanadamu kukuza akili zake tu, basi hakika hatakuwa Mungu, na hakika hatakuwa Bwana wa mwanadamu. Hataweza kufanya kazi kuu kama hii; kuna mmoja tu anayeweza kufanya kazi kama hii, na wote wasioweza kufanya hii kazi hakika ni adui wala si Mungu. Kama ni madhehebu, basi hawalingani na Mungu, na kama hawaligani na Mungu basi wao ni adui za Mungu. Kazi yote inafanywa na huyu Mungu mmoja wa kweli, na ulimwengu mzima unatawaliwa na huyu Mungu mmoja. Bila kujali kama Anafanya kazi Uchina ama Israeli, bila kujali kama kazi inafanywa na Roho ama mwili, yote hufanywa na Mungu Mwenyewe, na haiwezi kufanywa na mwingine yeyote. Ni kabisa kwa sababu Yeye ni Mungu wa wanadamu wote ndiyo kwamba Yeye hufanya kazi kwa njia ya uhuru, pasipo kuwekewa masharti yoyote—na haya ndiyo maono makuu zaidi. Kama kiumbe wa Mungu, kama ungependa kutekeleza jukumu la kiumbe wa Mungu na kuelewa mapenzi ya Mungu, lazima uelewe kazi ya Mungu, lazima uelewe mapenzi ya Mungu kwa viumbe, lazima uelewe mpango Wake wa usimamizi, na lazima uelewe umuhimu wote wa kazi Anayofanya. Wale wasioelewa hivi hawajahitimu kuwa viumbe wa Mungu! Kama kiumbe wa Mungu, kama huelewi ulikotoka, huelewi historia ya mwanadamu na kazi yote iliyofanywa na Mungu, na, hata zaidi, huelewi jinsi mwanadamu ameendelea hadi leo, na huelewi ni nani anayeamuru wanadamu wote, basi huna uwezo wa kutekeleza wajibu wako. Mungu amemwongoza mwanadamu hadi leo, na tangu alipomuumba mwanadamu duniani Hajawahi kumwacha. Roho Mtakatifu daima haachi kufanya kazi, hajawahi kuacha kumwongoza mwanadamu, na hajawahi kumwacha. Lakini mwanadamu hatambui kuwa kuna Mungu, pia hamjui Mungu, na je, kuna jambo la kufedhehesha zaidi kuliko hili kwa viumbe wote wa Mungu? Mungu binafsi humwongoza mwanadamu, lakini mwanadamu haelewi kazi ya Mungu. Wewe ni kiumbe wa Mungu, ilhali huelewi historia yako mwenyewe, na wala hujui ni nani aliyekuongoza katika safari yako, hutambui kazi iliyofanywa na Mungu, na kwa hivyo huwezi kumjua Mungu. Ikiwa hujui sasa, basi hutawahi kuhitimu kutoa ushuhuda kwa Mungu. Leo, Muumba binafsi huwaongoza watu wote kwa mara nyingine, na kuwafanya watu wote kuona hekima Yake, uweza, wokovu, na kustaajabisha Kwake. Ilhali bado hujatambua au kuelewa—na kwa hivyo, je, si wewe ndiwe utakayekosa kupokea wokovu? Wale walio wa Shetani hawaelewi maneno ya Mungu, na wale walio wa Mungu wanaweza kusikia sauti ya Mungu. Wale wote wanaotambua na kuelewa maneno Ninayozungumza ni wale watakaookolewa, na kumshuhudia Mungu; wote wasioelewa maneno Ninayoyazungumza hawawezi kutoa ushuhuda kwa Mungu, na ni wale watakaoondolewa. Wale wasioyaelewa mapenzi ya Mungu na hawaitambui kazi ya Mungu hawawezi kupata maarifa ya Mungu, na watu kama hawa hawawezi kutoa ushuhuda kwa Mungu. Kama ungependa kumshuhudia Mungu, basi lazima umjue Mungu, na maarifa ya Mungu yanapatikana kwa kupitia kazi ya Mungu. Kwa ufupi, kama ungependa kumjua Mungu, basi lazima ujue kazi ya Mungu: Kufahamu kazi ya Mungu ndilo jambo la umuhimu kabisa. Hatua tatu za kazi zitakapofikia tamati, patafanyika kundi la watu wanaomshuhudia Mungu, kundi la wale wanaomjua Mungu. Watu hawa wote watamjua Mungu na wataweza kuonyesha ukweli kwa matendo. Watakuwa na ubinadamu na hisia, na wote watajua hatua tatu za kazi ya wokovu ya Mungu. Hii ndiyo kazi ambayo itatekelezwa mwishowe, na watu hawa ndio dhihirisho la kazi ya miaka 6,000 ya usimamizi, na ndio ushuhuda wenye nguvu zaidi kwa kushindwa kwa Shetani. Wale wanaoweza kumshuhudia Mungu wataweza kupokea ahadi na baraka za Mungu, na litakuwa ndilo kundi litakalosalia pale mwisho kabisa, lile linalomiliki mamlaka ya Mungu na lililo na ushuhuda wa Mungu. Pengine wale kati yenu wanaweza wote kuwa sehemu ya kundi hili, ama pengine nusu tu, ama wachache tu—inategemea radhi yenu na ufuatiliaji wenu.

Tanbihi:

a. Nakala ya asili imeacha “basi mwanadamu ataona kuwa.”

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp