Kazi ya Mungu na Utendaji wa Mwanadamu (Sehemu ya Pili)

Wakati kazi ya Mungu inafikia hatua fulani, na usimamizi Wake kufikia hatua fulani, wale wanaoutafuta moyo Wake wote huwa na uwezo wa kutimiza matakwa yake. Mungu humwekea mwanadamu matakwa kulingana na viwango Vyake mwenyewe, na kulingana na kile ambacho mwanadamu anaweza kufanikisha. Akiwa anazungumzia usimamizi Wake, Yeye humwonyesha njia mwanadamu, na kumpa mwanadamu namna ya kudumu. Usimamizi wa Mungu na vitendo vya mwanadamu vipo katika hatua sawia kikazi, na yote yanafanyika kwa wakati mmoja. Mazungumzo kuhusu usimamizi wa Mungu yanagusia mabadiliko katika tabia ya mwanadamu, na yanazungumzia kuhusu yale yafaayo kufanywa na mwanadamu, na mabadiliko katika tabia ya mwanadamu, hugusia kazi ya Mungu; hakuna wakati ambao haya mawili yanaweza kutenganishwa. Vitendo vya mwanadamu vinabadilika, hatua kwa hatua. Hii ni kwa sababu matakwa ya Mungu kwa mwanadamu yanabadilika na vilevile kwa sababu kazi ya Mungu hubadilika na kusonga mbele kila wakati. Iwapo vitendo vya mwanadamu vitasalia ndani ya mafundisho, hii inathibitisha kwamba amepungukiwa na kazi na mwongozo wa Mungu; ikiwa vitendo vya mwanadamu havitabadilika kamwe au kuwa na kina zaidi, basi hili ni thibitisho kwamba vitendo vya mwanadamu hutendeka kulingana na mapenzi ya mwanadamu, na si vitendo vya ukweli; ikiwa mwanadamu hana njia ya kufuata, basi tayari ameanguka mikononi mwa Shetani, na sasa amedhibitiwa na Shetani, ambayo inamaanisha kwamba amedhibitiwa na roho mchafu. Ikiwa vitendo vya mwanadamu haviendi ndani zaidi, basi kazi ya Mungu haitakua, na kama hakuna mabadiliko katika kazi ya Mungu, basi kuingia kwa mwanadamu kutakwama; hili haliepukiki. Katika kazi nzima ya Mungu, mwanadamu angejifunga katika sheria za Yehova basi kazi ya Mungu isingeendelea na zaidi ingekuwa vigumu kutamatisha enzi nzima. Iwapo mwanadamu angeshikilia msalaba daima na kuishi katika uvumilivu na unyenyekevu, basi kazi ya Mungu isingeendelea. Miaka elfu sita ya usimamizi haiwezi kusitishwa miongoni mwa watu wanaoshikilia tu sheria au kushikilia msalaba na kuishi katika uvumilivu na unyenyekevu tu. Badala yake, kazi nzima ya usimamizi wa Mungu inahitimishwa miongoni mwa watu wa siku za mwisho wanaomfahamu Mungu na ambao wamekombolewa kutoka kwa Shetani na wamejinasua kabisa kutoka katika vishawishi vya Shetani. Huu ni mwelekeo wa kazi ya Mungu usioepukika. Kwa nini inasemekana kwamba vitendo vya walio katika makanisa ya kidini vimepitwa na wakati? Ni kwa kuwa wanayoyaweka katika vitendo ni tofauti na kazi ya leo. Katika Enzi ya Neema, walichotenda kilikuwa sahihi, ila kwa kuwa enzi yenyewe imepita na kazi ya Mungu kubadilika, vitendo vyao hatua kwa hatua vimepitwa na wakati. Vimeachwa nyuma na kazi mpya na mwangaza mpya. Ikiwa imesimama juu ya msingi wake asili, kazi ya Roho Mtakatifu imepiga hatua kadhaa kwa kina. Na bado watu hao wamebaki katika hatua ya asili ya kazi ya Mungu na bado wanapenyeza katikati ya vitendo na mwangaza wa zamani. Kazi ya Mungu yaweza kubadilika pakubwa kwa miaka mitatu au mitano, hivyo si mabadiliko hata makubwa zaidi yaweza kuja kwa kipindi cha miaka zaidi ya 2000? Ikiwa mwanadamu hana vitendo vipya ama mwangaza mpya, inamaanisha hajaenda sawia na kazi ya Roho Mtakatifu. Hili ni anguko la mwanadamu; uwepo wa kazi mpya ya Mungu hauwezi kukanwa kwa sababu, leo hii, wale walio na kazi asili ya Roho Mtakatifu bado wanashikilia vitendo vilivyopitwa na wakati. Kazi ya Roho Mtakatifu daima inasonga mbele, na wote walio katika mkondo wa Roho Mtakatifu wanafaa waendelee mbele na kubadilika, hatua kwa hatua. Hawapaswi kukwama katika hatua moja. Ni wale tu wasioifahamu kazi ya Roho Mtakatifu ndio wanaweza kubaki katika hatua ya kazi ya Mungu ya awali na wasikubali kazi mpya ya Roho Mtakatifu. Ni wale tu walio waasi ndio watakosa uwezo wa kuipokea kazi ya Roho Mtakatifu. Ikiwa vitendo vya mwanadamu haviendani na mwendo wa kazi mpya ya Roho Mtakatifu, basi vitendo vya mwanadamu hakika vimetengana na kazi ya leo na kwa hakika havilingani na kazi ya leo. Watu waliopitwa na wakati kama hawa hawawezi kutimiza mapenzi ya Mungu, na zaidi hawawezi kuwa wale watu wa mwisho ambao watamshuhudia Mungu. Aidha, kazi nzima ya usimamizi haiwezi kutimilika miongoni mwa kundi la watu kama hao. Kwa wale walioshikilia sheria za Yehova kipindi fulani, na wale walioumia wakati fulani chini ya msalaba, ikiwa hawawezi kukubali hatua ya kazi ya siku za mwisho, basi yale yote waliyofanya ni bure na yasiyofaa. Dhihirisho la wazi zaidi wa kazi ya Roho Mtakatifu ni kwa kuyakumbatia ya sasa, sio kushikilia ya zamani. Wale ambao hawajiendelezi na kazi ya leo, na wale ambao wametengwa na utendaji wa leo, ni wale wanaopinga na hawaikubali kazi ya Roho Mtakatifu. Watu kama hao wanaipinga kazi ya Mungu ya sasa. Ijapokuwa wanashikilia nuru ya zamani, hili halimaanishi kwamba inaweza kukanwa kwamba hawajui kazi ya Roho Mtakatifu. Kwa nini kumekuwepo na mjadala huu wote kuhusu mabadiliko katika vitendo vya mwanadamu, kuhusu tofauti za utendaji kati ya zamani na sasa, kuhusu jinsi utendaji ulivyokuwa katika enzi za awali na jinsi ulivyo sasa? Migawanyiko kama hiyo katika vitendo vya mwanadamu hujadiliwa kwa sababu kazi ya Roho Mtakatifu daima inasonga mbele na kwa hivyo vitendo vya mwanadamu vinapaswa kubadilika daima. Ikiwa mwanadamu atasalia amekwama katika hatua moja tu, basi hili linaonyesha kuwa haendi sawia na kazi ya Mungu na mwangaza mpya; haimaanishi kuwa mpango wa usimamizi wa Mungu haujabadilika. Walio nje ya mkondo wa Roho Mtakatifu daima hudhani wako sahihi, lakini kwa hakika, kazi ya Mungu ndani yao ilisita zamani na kazi ya Roho Mtakatifu haimo ndani yao. Kazi ya Mungu imeshahamishiwa kwa kundi jingine la watu, kundi ambalo kwalo Anapania kukamilishia kazi Yake mpya. Kwani walio kwenye dini hawawezi kuikubali kazi mpya ya Mungu, na kushikilia tu kazi kongwe za zamani, hivyo Mungu amewaacha watu hawa na anafanya kazi Yake mpya kwa watu wanaoikubali kazi hii mpya. Hawa ni watu wanaoshiriki katika kazi Yake mpya, na usimamizi Wake utatimilika kwa njia hii tu. Usimamizi wa Mungu daima unasonga mbele na vitendo vya mwanadamu daima vinapanda juu. Mungu daima anafanya kazi na mwanadamu mara zote ni mhitaji ili kwamba wote wanafikia upeo wao, Mungu na mwanadamu wamo katika muungano kikamilifu. Haya ni maonyesho ya kutimilika kwa kazi ya Mungu, na ndiyo matokeo ya mwisho ya kazi nzima ya usimamizi.

Katika kila hatua ya kazi ya Mungu yapo matakwa sawia kwa mwanadamu. Wale wote walio kwenye mkondo wa Roho Mtakatifu wanamilikishwa na uwepo na nidhamu ya Roho Mtakatifu na wasiokuwemo kwenye mkondo wa Roho Mtakatifu wako chini ya utawala wa Shetani na hawana kazi yoyote ya Roho Mtakatifu. Walio kwenye mkondo wa Roho Mtakatifu ni wale walioikubali kazi mpya ya Mungu, wanaoshiriki katika kazi mpya ya Mungu. Iwapo walio ndani ya mkondo huu hawana uwezo wa kushirikiana, na hawawezi kuweka ukweli unaotakiwa na Mungu katika vitendo wakati huu, basi watafundishwa nidhamu, na vibaya zaidi kuachwa na Roho Mtakatifu. Wale ambao wanakubali kazi mpya ya Roho Mtakatifu, wataishi kwenye mkondo wa Roho Mtakatifu, wapokee huduma na ulinzi wa Roho Mtakatifu. Wale ambao wako tayari kuweka ukweli katika vitendo wanapewa nuru na Roho Mtakatifu na wale wasiotaka kuweka ukweli katika vitendo wanafundishwa nidhamu na Roho Mtakatifu na huenda wakaadhibiwa. Bila kujali ni aina gani ya watu, ilimradi tu wamo kwenye mkondo wa Roho Mtakatifu, Mungu atawawajibikia wote wanaoikubali kazi Yake mpya kwa minajili ya jina Lake. Wale wanaolitukuza jina Lake na wako radhi kuweka maneno Yake katika vitendo watapokea baraka Zake; wale wasiomtii na kuyaweka maneno Yake katika vitendo watapokea adhabu Yake. Watu walio kwenye mkondo wa Roho Mtakatifu ni wale wanaoikubali kazi mpya, na kwa sababu wameikubali kazi mpya, wanafaa kuwa na ushirika na Mungu na hawafai kuwa kama waasi wasiofanya wajibu wao. Hili ndilo sharti pekee la Mungu kwa mwanadamu. Sio hivyo na watu wasioikubali kazi mpya: Wako nje ya mkondo wa Roho Mtakatifu, na adhabu na lawama ya Roho Mtakatifu haitumiki kwao. Kila siku hawa watu wanaishi katika mwili, wanaishi katika mitazamo yao, na yote wayafanyayo ni kulingana na mafundisho ya kidini yaliyozalishwa na uchanganuzi pamoja na utafiti wa bongo zao. Si matakwa ya kazi mpya ya Roho Mtakatifu wala sio ushirika na Mungu. Wale wasioikubali kazi mpya ya Mungu wanajinyima uwepo wa Mungu na, zaidi, wanakosa baraka na ulinzi wa Mungu. Mengi ya maneno na matendo yao yanashikilia matakwa ya zamani ya kazi ya Roho Mtakatifu; ni mafundisho ya kidini tu na wala si ukweli. Mafundisho na taratibu kama hizo ni thibitisho la kutosha kuwa kitu cha pekee kinachowaleta pamoja ni dini; si watu walioteuliwa au vyombo vya kazi ya Mungu. Mikutano ya wote walio miongoni mwao haiwezi kuitwa kanisa bali mkutano mkubwa wa watu wa dini. Huu ni ukweli usioweza kubadilishwa. Hawana kazi mpya ya Roho Mtakatifu; wakifanyacho kinanuka dini, wanachodhihirisha katika maisha yao kimejaa dini; hawana uwepo na kazi ya Roho Mtakatifu, na zaidi hawajahitimu kupokea adhabu au kupata nuru ya Roho Mtakatifu. Watu hawa wote ni miili isiyokuwa na uhai, na funza wasiokuwa na mambo ya kiroho. Hawana ufahamu wa uasi na pingamizi wa mwanadamu, hawana ufahamu wa uovu wote wa mwanadamu na hata zaidi, hawaifahamu kazi ya Mungu na mapenzi ya sasa ya Mungu. Wote ni wapumbavu, waovu, ni watu duni wasiostahili kuitwa waumini! Hakuna wafanyacho kinachoambatana na usimamizi wa Mungu, wala hakiwezi kuidhoofisha mipango ya Mungu. Maneno na matendo yao yanaudhi sana, yanasikitisha mno, na hayafai kutajika. Chochote wakifanyacho walio nje ya mkondo wa Roho Mtakatifu hakihusiani na kazi mpya ya Roho Mtakatifu. Kwa sababu hii, haijalishi wanafanya nini, hawana adhabu ya Roho Mtakatifu na zaidi, hawana nuru ya Roho Mtakatifu. Kwani wao ni watu wasiopenda ukweli, na wametokwa na kukataliwa na Roho Mtakatifu. Wanaitwa watenda maovu kwani wanatembea katika mwili, na kufanya chochote kiwafurahishacho kwa kisingizio cha bango la Mungu. Mungu anapofanya kazi, wao wanakuwa maadui kwake kwa makusudi, na kumkimbia Mungu. Kutoshirikiana kwa mwanadamu na Mungu ni uasi wa hali ya juu, bila kutaja kutoroka makusudi kwa watu hawa kutoka kwa Mungu. Basi, je, hawatapokea malipo wanayostahili? Uovu wa hawa watu ukitajwa, baadhi ya watu huwalaani huku Mungu akiwapuuza. Kwa mwanadamu, inaonekana kana kwamba matendo ya watu hawa yanajihusisha na jina la Mungu, ila kwa hakika, kwa Mungu, matendo haya hayana uhusiano wowote na jina Lake au ushuhuda Wake. Bila kujali wanachokifanya hawa watu, hakihusiani na Mungu: hakihusiani na kazi Yake na jina Lake leo. Hawa watu hujiaibisha wenyewe na kumdhihirisha Shetani; ni watenda maovu wanaosubiri siku ya ghadhabu. Sasa, bila kujali matendo yao ni yapi, mradi tu hawazuii usimamizi wa Mungu na hawafanyi chochote kuhusiana na kazi mpya ya Mungu, watu kama hao hawatapata adhabu inayolingana na matendo yao sasa kwa kuwa siku ya ghadhabu bado haijatimia. Yapo mengi ambayo watu wanaamini kuwa Mungu angekuwa ameyashughulikia tayari na kufikiri kuwa wale watenda maovu wanastahili kuadhibiwa haraka iwezekanavyo. Lakini kwa sababu kazi ya usimamizi wa Mungu bado haijafikia kikomo, na siku ya ghadhabu haijatimia, waovu bado wanaendelea kutenda matendo yao maovu. Watu wengine husema kuwa walio ndani ya dini hawana uwepo au Kazi ya Roho Mtakatifu, na kwamba wanaliletea aibu jina la Mungu; basi ni kwa nini Mungu asiwaangamize, badala ya kuendelea kustahimili ufidhuli wao? Watu hawa ambao ni dhihirisho la Shetani na ambao ni wa mwili, ni wapumbavu, wa hali duni, ni watu wasio na busara. Hawataiona ghadhabu ya Mungu kabla ya kuelewa jinsi Mungu anavyofanya kazi Yake miongoni mwa wanadamu, na wakishashindwa kabisa, hao watenda maovu wote watalipwa stahili yao na hamna hata mmoja kati yao atakayeweza kuiepuka siku ya ghadhabu. Sasa si wakati wa adhabu ya mwanadamu, ila ni wakati wa kuendeleza kazi ya ushindi, isipokuwa wawepo wanaoizuia kazi ya usimamizi wa Mungu, ambapo wataadhibiwa kulingana na uzito wa matendo yao. Katika kipindi cha usimamizi wa Mungu kwa wanadamu, wote walio ndani ya mkondo wa Roho Mtakatifu huwa na uhusiano na Mungu. Wale wanaochukiwa na kukataliwa na Roho Mtakatifu huishi katika ushawishi wa Shetani na kile wawekacho katika vitendo hakina uhusiano na Mungu. Wanaoikubali kazi mpya ya Mungu, na wanaoshirikiana na Mungu ndio tu wana uhusiano Naye, kwani kazi ya Mungu inakusudiwa tu kwa watu wanaoikubali wala si watu wote, haijalishi kama wanaikubali au la. Kazi inayofanywa na Mungu daima ina kusudi, na haifanywi bure. Walio na uhusiano na Shetani hawafai kuwa na ushuhuda kwa Mungu, na hata zaidi hawafai kushirikiana na Mungu.

Kila hatua ya kazi ya Roho Mtakatifu inahitaji ushuhuda sawia kutoka kwa mwanadamu. Kila hatua ya kazi ni vita kati ya Mungu na Shetani, na mlengwa katika vita hivi ni Shetani, huku atakayekamilishwa na kazi hii ni mwanadamu. Kazi ya Mungu kuzaa au kutozaa matunda inategemea na jinsi ushuhuda wa mwanadamu ulivyo. Huu ushuhuda ndio Mungu anaohitaji kutoka kwa wale wanaomfuata; ni ushuhuda unaofanywa mbele ya Shetani, na unaothibitisha athari za kazi Yake. Usimamizi mzima wa Mungu umegawika kwa hatua tatu, na katika kila hatua, mahitaji yanayopatana yanatokana na mwanadamu. Aidha, kadri enzi zinavyopita na kuendelea, mahitaji ya Mungu kwa wanadamu huongezeka hata zaidi. Kwa hiyo, hatua kwa hatua, kazi hii ya usimamizi wa Mungu hufikia kilele chake, hadi mwanadamu aamini ukweli wa “kuonekana kwa Neno katika mwili,” na hivyo mahitaji ya mwanadamu huongezeka hata zaidi, na mahitaji ya mwanadamu kutoa ushuhuda huongezeka hata zaidi. Kadiri mwanadamu alivyo na uwezo wa kushirikiana na Mungu kikamilifu, ndivyo anavyozidi kumtukuza Mungu. Ushirikiano wa mwanadamu ndio ushuhuda anaohitajika kuwa nao, na huo ushuhuda ndio matendo ya mwanadamu. Kwa hivyo, kazi ya Mungu iwe au isiwe na athari inayohitajika, au pawepo ama pasiwepo ushuhuda wa kweli, ni mambo ambayo yameunganishwa na ushuhuda wa mwanadamu. Wakati kazi itakapokwisha, yaani, wakati usimamizi wa kazi ya Mungu utakapofikia kikomo, Mwanadamu atahitajika kuwa na ushuhuda wa hali ya juu, na wakati kazi ya Mungu itakapofika mwisho wake, matendo na kuingia kwa mwanadamu vitafikia kilele chake. Wakati wa kale, mwanadamu alihitajika kuzingatia sheria na amri, na alihitajika kuwa mpole na mnyenyekevu. Leo, mwanadamu anahitajika kutii mipango yote ya Mungu na awe na upendo mkuu wa Mungu, na zaidi bado anahitajika kumpenda Mungu katika mateso. Hatua hizi tatu ndizo Mungu anazozitazamia toka kwa mwanadamu, hatua kwa hatua, katika usimamizi Wake wote. Kila hatua ya kazi ya Mungu huzidisha kina kuliko iliyopita, na katika kila hatua, mahitaji ya mwanadamu ni makubwa kuliko yaliyopita, na kwa hali hii, umbo la usimamizi mzima wa Mungu huonekana. Ni hasa kwa sababu mahitaji ya mwanadamu kila mara huwa juu kuliko tabia yake inavyoweza kufikia viwango anavyovihitaji Mungu, na ni hapo ambapo wanadamu wataanza kujiondoa polepole kutoka kwa ushawishi wa Shetani, ndipo kazi ya Mungu itafikia kikomo, wanadamu wote watakuwa wameokolewa kutoka kwa ushawishi wa Shetani. Wakati huo utakapowadia, kazi ya Mungu itakuwa imefika mwisho, na ushirikiano wa mwanadamu na Mungu ili abadilishe tabia zake hautakuwepo, na wanadamu wote wataishi kwenye nuru ya Mungu, na kuanzia hapo kuendelea, hapatakuwa na uasi au upinzani wowote kwa Mungu. Aidha Mungu hatamwekea matakwa mwanadamu, na patakuwepo na ushirikiano mwema zaidi kati ya mwanadamu na Mungu, mojawapo ikiwa maisha ya mwanadamu na Mungu pamoja, maisha ambayo yatafuatia baada ya usimamizi wa Mungu kukamilishwa, na baada ya mwanadamu kuokolewa toka katika mafumbato ya Shetani. Wale ambao hawatafuata kwa ukaribu nyayo za Mungu hawatakuwa na uwezo wa kufikia maisha hayo. Watakuwa wamejishusha ndani ya giza, ambapo watalia na kusaga meno; hao ndio watu wanaoamini katika Mungu lakini hawamfuati Yeye, wanaoamini katika Mungu lakini hawatii kazi Yake yote. Kwa kuwa mwanadamu anamwamini Mungu, ni sharti afuate kwa ukaribu nyayo Zake, hatua kwa hatua; anapaswa “kumfuata Mwanakondoo popote Aendapo.” Hawa tu ndio watu wanaotafuta njia ya kweli, na wao ndio wanafahamu kazi ya Roho Mtakatifu. Watu wanaofuata tu nyaraka na mafundisho ya dini kiutumwa ni wale ambao wameondolewa na kazi ya Roho Mtakatifu. Katika kila kipindi cha wakati, Mungu ataanza kazi mpya, na katika kila kipindi, patakuwepo na mwanzo mpya kwa mwanadamu. Laiti mwanadamu angeshikilia ukweli kwamba “Yehova ni Mungu” na “Yesu ni Kristo,” ukweli ambao unazingatiwa kwa kipindi kimoja, basi mwanadamu hataweza kwenda sambamba na kazi ya Roho Mtakatifu, na daima hataweza kupokea kazi ya Roho Mtakatifu. Bila kujali jinsi Mungu anavyofanya, mwanadamu anafaa kufuata bila shaka lolote, na afuate kwa ukaribu. Kwa jinsi hii basi itakuwaje mwanadamu aondolewe na Roho Mtakatifu? Bila kujali kile anachofanya Mungu, kama mwanadamu ana uhakika ni kazi ya Roho Mtakatifu, na kushirikiana katika kazi ya Roho Mtakatifu bila mashaka yoyote, na kujaribu kufikia mahitaji ya Mungu, basi ataadhibiwaje? Kazi ya Mungu kamwe haijasimama, hatua Zake hazijakwama na kabla kukamilisha kazi Yake ya usimamizi, siku zote Mungu amekuwa mwenye kazi nyingi, na kamwe hajasimama. Lakini mwanadamu ni tofauti: Kutokana na kupata kiwango cha chini cha nguvu za Roho Mtakatifu, yeye huchukulia kwamba hakuna chochote kitakachobadilika; baada ya kupata ufahamu kidogo, hajipi msukumo wa kufuata nyayo za kazi mpya ya Mungu; licha ya kwamba ameona kiasi kazi ya Mungu, yeye anamchukulia Mungu kama kifaa, aina fulani ya umbo la sanamu ya mti, na anaamini kwamba Mungu atasalia kuwa hivyo daima kwani hali imekuwa hii tangu hapo awali na hata katika siku zijazo; akiwa amepata ufahamu wa kijuujuu, mwanadamu ni mwenye kiburi hivi kwamba hujisahau na kuanza kutangaza kwa fujo tabia ya Mungu na hali ya Mungu ambayo haipo; na akiwa amejifunga katika hatua moja ya Roho Mtakatifu, pasi kujali ni mtu wa aina gani ambaye anatangaza kazi mpya ya Mungu, mwanadamu huwa haikubali. Hawa ni watu ambao hawawezi kuikubali kazi mpya ya Roho Mtakatifu; ni watu wenye kushikilia ukale sana, na hawawezi kukubali mambo mapya. Watu kama hawa ni watu wanaomwamini Mungu lakini wakati uo huo wanamkataa Mungu. Mwanadamu anaamini kwamba wana wa Israeli walikosea “tu kumuamini Yehova na kukosa kumuamini Yesu,” huku watu wengi wakiiga jukumu ambapo “humwamini Yehova tu na kumkataa Yesu” na “kusubiri kwa hamu kurejea kwa Masihi lakini wanamkataa Masihi ambaye ni Yesu”. Ndiyo maana, basi, watu wengi bado wanaishi chini ya mamlaka ya Shetani baada ya kukubali hatua moja tu ya Roho Mtakatifu na bado hawapokei baraka za Mungu. Je, si hii ni kutokana na uasi wa mwanadamu? Wakristo ulimwenguni kote ambao hawajazingatia kazi mpya ya sasa wote wameshikilia imani kwamba wao ni wenye bahati na kwamba Mungu atawatimizia kila mojawapo ya malengo yao. Lakini hawawezi kueleza mbona Mungu atawapeleka katika mbingu ya tatu na wala hawafahamu jinsi Yesu atakavyokuja juu ya wingu jeupe na kuwachukua, wala kusema kwa uhakika kamili kama kweli Yesu atawasili akiwa juu ya wingu jeupe siku ambayo wanaiwaza. Wote wana wasiwasi, na kukanganywa; wao wenyewe hata hawafahamu kama Mungu atachukua kila mmoja wao, watu wachache sana, wanaotoka katika madhehebu yote. Kazi ambayo Mungu anafanya kwa sasa, enzi ya sasa, mapenzi ya Mungu—ni vitu ambavyo watu hawavifahamu, na hawana cha kufanya bali kusubiri na kuhesabu siku katika vidole vyao. Ni wale tu wanaofuata nyayo za Mwanakondoo hadi mwisho kabisa ndio wanaoweza kufaidi baraka za mwisho, huku wale “watu werevu,” ambao hawawezi kumfuata hadi mwisho ilhali wanaamini wamepata yote, ndio wasiokuwa na uwezo wa kushuhudia kuonekana kwa Mungu. Wote huamini wao ndio werevu zaidi duniani, na wanasitisha maendeleo ya kazi ya Mungu bila sababu yoyote kabisa, na huonekana kuamini pasi na shaka kwamba Mungu atawachukua mbinguni, wao “wenye uaminifu wa juu zaidi kwa Mungu, humfuata Mungu, na hutii neno la Mungu”. Hata ingawa wana “uaminifu wa hali ya juu” kwa maneno yaliyozungumzwa na Mungu; maneno yao na matendo yao bado hukera kwa sababu wao huipinga kazi ya Roho Mtakatifu, na kufanya uongo na uovu. Wale wasiofuata hadi mwisho kabisa, ambao hawazingatii kazi ya Roho Mtakatifu, na ambao wanashikilia kazi ya zamani hawajakosa tu kupata uaminifu kwa Mungu, bali kwa kinyume, wamekuwa wale wanaompinga Mungu, wamekuwa wale ambao wamekanwa na enzi mpya, na watakaoadhibiwa. Kuna wa kuhurumiwa zaidi kuliko wao? Wengi hata wanaamini kuwa wale wanaokana sheria ya zamani na kukubali kazi mpya hawana dhamiri. Watu hawa, ambao huongea tu kuhusu “dhamiri,” na hawajui kazi ya Roho Mtakatifu, hatimaye watapata kuwa matarajio yao yamekatizwa na dhamiri yao yenyewe. Kazi ya Mungu haizingatii mafundisho, na ingawa ni kazi Yake Mwenyewe, bado Mungu haishikilii. Kile kinachopaswa kukataliwa kinakataliwa, kile kinachopaswa kuondolewa kinaondolewa. Lakini mwanadamu anajiweka kwenye uadui wa Mungu kwa kushikilia sehemu moja ndogo ya kazi ya usimamizi wa Mungu. Si huu ndio upuuzi wa mwanadamu? Si huu ndio ujinga wa mwanadamu? Kadri watu wanakuwa waoga na wenye tahadhari sana kwa sababu wanachelea kutopata baraka za Mungu, ndivyo wanavyopungukiwa zaidi na uwezo wa kupata baraka zaidi, na wa kupata ile baraka ya mwisho. Watu wale wanaoshikilia kiutumwa sheria huwa wanadhihirisha uaminifu wa hali ya juu kwa sheria, na kadri wanavyodhihirisha uaminifu jinsi hiyo kwa sheria, ndivyo wanavyokuwa waasi wanaompinga Mungu. Kwa kuwa sasa ni Enzi ya Ufalme na wala si Enzi ya Sheria, na kazi ya leo haiwezi kulinganishwa na kazi ya zamani wala kazi ya zamani haiwezi kulinganishwa na kazi ya sasa. Kazi ya Mungu imebadilika, na vitendo vya mwanadamu pia vimebadilika; si kushikilia sheria au kuubeba msalaba. Basi, uaminifu wa watu kwa sheria na msalaba hautapata kibali cha Mungu.

Mwanadamu atakamilishwa kabisa katika Enzi ya Ufalme. Baada ya kazi ya ushindi, mwanadamu atapitishwa kwenye mambo magumu ya kusafishwa na taabu. Wale ambao wanaweza kushinda na kushuhudia katika taabu hii ndio hatimaye watakaofanywa wakamilifu; wao ndio washindi. Katika taabu hii, mwanadamu anahitajika kukubali kusafishwa huku, na kusafishwa huku ndio tukio la mwisho la kazi ya Mungu. Itakuwa mara ya mwisho ambapo mwanadamu atasafishwa kabla ya hitimisho la kazi zote za usimamizi wa Mungu, na wale wote wanaomfuata Mungu lazima wakubali jaribio hili la mwisho, lazima wakubali kusafishwa huku kwa mwisho. Wale ambao wamekabiliwa na taabu ni wale wasiokuwa na kazi ya Roho Mtakatifu na uelekezi wa Mungu, lakini wale ambao wameshindwa kwa kweli na wanatafuta mapenzi ya Mungu kwa kweli hatimaye watasimama imara; ndio wale ambao wana ubinadamu, na wanaompenda Mungu kwa kweli. Bila kujali Mungu hufanya nini, hawa washindi hawatapungukiwa na maono, na bado watauweka ukweli katika matendo bila kufeli katika ushuhuda wao. Wao ndio watakaosimama mwishowe kutoka kwenye taabu kubwa. Hata ingawa wale wanaovua samaki katika maji yenye mawimbi mengi bado wanaweza kusaidiwa leo, hakuna yeyote atakayeepuka taabu, na hakuna atakayeepuka jaribio la mwisho. Kwa wale wanaoshinda, taabu ya aina hii ni usafisho mkubwa; lakini wale wanaovua katika maji yenye mawimbi, ni kazi ya kuondolewa kamili. Bila kujali jinsi wanavyojaribiwa, utii wa wale wenye Mungu ndani ya mioyo yao hubaki vile vile; lakini kwa wale wasiokuwa na Mungu ndani ya mioyo yao, wakati kazi ya Mungu hainufaishi miili yao, wanabadilisha mtazamo wao kwa Mungu, na hata kumkimbia Mungu. Hawa ndio wale hawatasimama imara mwishoni, wanaotafuta baraka za Mungu na hawana tamaa ya kujitolea wenyewe kwa Mungu na kujikabidhi wenyewe Kwake. Aina hii ya watu wa msingi watafukuzwa wakati kazi ya Mungu itakapofikia kikomo, na hawafai kuonewa huruma yoyote. Wale wasiokuwa na ubinadamu, hawawezi kumpenda Mungu kwa kweli. Wakati mazingira ni mema na salama, au kama watapata faida, wao ni watiifu kabisa kwa Mungu, lakini wakati walilokuwa wanataka limepatikana au hatimaye kukataliwa, wanageuka mara moja. Hata kama ni kwa muda wa usiku mmoja tu, wao watatoka katika hali ya tabasamu, watu wenye “mioyo mikunjufu” hadi wenye sura mbovu na wauaji wakatili, ghafla wakiwatendea wafadhili wao wa jana kana kwamba ni adui wa milele, bila chanzo wala sababu. Ikiwa mapepo haya hayatarushwa nje, mapepo ambayo yanaweza kuua kwa kufumba na kufumbua jicho, je, hayatakuwa chanzo cha mateso zaidi? Kazi ya kumwokoa mwanadamu haitimizwi kufuatia kazi ya kukamilisha ushindi. Ingawa kazi ya ushindi imefika kikomo, kazi ya kumtakasa mwanadamu haijafika kikomo; kazi hiyo itamalizika tu wakati mwanadamu amesafishwa kikamilifu, wakati wale ambao wamejikabidhi kwa Mungu kikweli wamekamilishwa, na wakati wale wadanganyifu wasiokuwa na Mungu ndani ya mioyo yao wamesafishwa. Wale ambao hawamridhishi Mungu katika hatua ya mwisho ya kazi Yake wataondolewa kabisa, na wale watakaoondolewa kabisa ni wa yule mwovu. Kwa kuwa hawawezi kumtosheleza Mungu, wao ni waasi dhidi ya Mungu, na hata kama watu hawa wanamfuata Mungu leo, hili si thibitisho kwamba wao ndio watakaosalia mwisho. Kwa maneno mengine “wale ambao humfuata Mungu hadi mwisho watapokea wokovu,” maana ya “kufuata” ni kusimama imara katikati ya taabu. Leo, wengi wanaamini kwamba kumfuata Mungu ni rahisi, lakini wakati kazi ya Mungu inakaribia kuisha, utajua maana halisi ya “kufuata.” Kwa sababu tu kwamba unaweza kumfuata Mungu leo baada ya kushindwa, si thibitisho kwamba umo miongoni mwa wale watakaokamilishwa. Wale wasioweza kustahimili majaribu, wale wasioweza kuwa washindi wakiwa kwenye taabu, hatimaye, watashindwa kusimama imara, na basi kushindwa kumfuata Mungu hadi mwisho kabisa. Wale wanaomfuata Mungu kiukweli wana uwezo wa kuhimili majaribu ya kazi yao, ilhali wale wasiomfuata hawawezi kuhimili majaribu yoyote ya Mungu. Karibuni au baadaye watatimuliwa, huku washindi wakisalia kwenye ufalme. Mwanadamu amtafute au asimtafute Mungu kwa ukweli itapimwa kulingana na kazi yake, yaani, kupitia kwa majaribu ya Mungu na hayahusiani na uamuzi wa mwanadamu mwenyewe. Mungu hamkatai mtu yeyote kwa wazo la ghafla; yote ambayo Yeye hufanya ni ili mwanadamu aweze kushawishika mwenyewe. Hafanyi lolote ambalo halionekani kwa mwanadamu ama kazi yoyote ambayo haiwezi kumthibitishia mwanadamu. Iwapo imani ya mwanadamu ni ya ukweli au sio huthibitishwa na ushahidi, na haiwezi kuamuliwa na mwanadamu. Kwamba “ngano haiwezi kufanywa magugu, na magugu hayawezi kufanywa ngano” ni jambo lililo wazi. Wale wote wanaompenda Mungu kwa dhati hatimaye watasalia katika ufalme, na Mungu hatamtesa yeyote ambaye Yeye anampenda kwa kweli. Kwa misingi ya kazi zao na shuhuda zao tofauti, washindi katika ufalme watatumika kama makuhani au wafuasi, na wale wote watakaoshinda taabu watakuwa mwili wa makuhani katika ufalme. Baraza la makuhani litaundwa wakati kazi ya injili ulimwenguni kote itafikia kikomo. Wakati huo ukitimia, yale yanayopaswa kufanywa na mwanadamu yatakuwa jukumu lake ndani ya ufalme wa Mungu, na kuishi kwake pamoja na Mungu katika ufalme. Katika baraza la makuhani, patakuwepo makuhani wakuu na makuhani, na watakaosalia watakuwa wana na watu wa Mungu. Haya yote huamuliwa na ushuhuda wao kwa Mungu wakati wa majaribu; sio nyadhifa zinazopeanwa kwa wazo la ghafla. Wakati hadhi ya mwanadamu itakuwa imeianzishwa, kazi ya Mungu itamalizika, kwa kuwa kila mojawapo imewekwa kulingana na aina yake na kurejeshwa katika hali yake halisia, na hii ndiyo alama ya ukamilisho wa kazi ya Mungu, na haya ndiyo matokeo ya mwisho ya kazi ya Mungu na matendo ya mwanadamu, na ndiko kubainika kwa yale maono ya kazi ya Mungu na ushirikiano wa mwanadamu. Mwishowe, mwanadamu atapata pumziko katika ufalme wa Mungu, na, Mungu pia, atarejea kwenye makazi Yake kupumzika. Haya ndiyo yatakayokuwa matokeo ya miaka 6,000 ya ushirikiano wa mwisho kati ya Mungu na mwanadamu.

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp